Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 22 Questions to Prime Minister Maswali kwa Waziri Mkuu 1 2017-05-11

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Gender

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kumuuliza Waziri Mkuu swali.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, Bunge kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63(2), ndicho chombo kikuu chenye mamlaka na wajibu wa kuisimamia na kuishauri Serikali. Katika Bunge hili, Bunge la Kumi na Mabunge mengine kadhaa, Bunge limekuwa linatoa Maazimio kadhaa kuitaka Serikali itoe taarifa na Serikali imekuwa inaahidi kutoa taarifa, lakini taarifa nyingi ambazo ni Maazimio ya Bunge yamekuwa hayatekelezwi na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna Maazimio ya Bunge kuhusiana na Tokomeza mpaka leo Serikali haijaleta majibu. Kuna Maazimio ya Bunge kuhusiana na ESCROW na IPTL, Serikali mpaka leo haijatoa majibu. Kuna Maazimio ya Bunge kuhusu mabilioni ya Uswis, Serikali mpaka leo haijatoa majibu na Maazimio mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri Mkuu unaliambia nini Bunge na unaliambia nini Taifa. Wewe kama Kiongozi wa Serikali Bungeni, utapenda kusema kwamba Serikali inalidharau Bunge ama Serikali haina majibu ya kutoa?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikuhakikishie kwamba Serikali inaheshimu sana Mhimili wa Bunge na inathamini sana maamuzi ya Mhimili huu wa Bunge na tutaendelea kushirikiana na Mhimili wa Bunge katika kupata ushauri na namna nzuri ya kuendesha Serikali kwa mapendekezo ambayo yanatolewa na Waheshimiwa Wabunge kupitia chombo cha Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua vikao kadhaa huko awali kumekuwa na Maazimio yanayoitaka Serikali ilete maelezo, lakini baadhi ya maeneo ambayo yanatakiwa kuletwa hapa ni yale ambayo yanahitaji uchunguzi wa kina na uchunguzi huu unapokamilika ndipo unapoweza kuletwa Bungeni.

Sasa yapo ambayo tunaona upo umuhimu wa kuyaleta ni pamoja na hayo uliyoyasema, nataka nikuahidi kwamba haya ambayo umeyatamka kwenye maeneo yanayogusa Wizara kadhaa ambazo zinatakiwa kuleta taarifa nitafanya ufuatiliaji, pale ambapo tutakuwa tumekamilisha uchunguzi wetu, nitayaleta kwa utaratibu ambao Bunge utakuwa umetoa maelekezo yake. Ahsante sana.

Additional Question(s) to Prime Minister

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Gender

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Question 1

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu yake, ni ukweli usiopingika kwamba pale muda unapotumika au unapopita sana bila majibu hata status kutolewa katika Bunge, hoja hiyo huonekana kwamba imefifia umuhimu na ulazima wake.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na kwamba umetoa ahadi ya kwamba Wizara zitashughulikia, unaweza ukatoa a firm commitment kwamba katika Bunge hili, kabla Bunge hili la Bajeti halijaisha, Serikali itapitia Hansard na kumbukumbu zote zinazohusiana na Maazimio yaliyopita ya Bunge halafu Serikali itoe status report na naomba itambulike hapa kwamba status report siyo lazima ndiyo iwe ripoti ya uchunguzi ya mwisho, angalau ituambie jambo hili limefikia hapa, limefanyiwa kazi moja, mbili, tatu, bado tutaletewa katika hatua ya baadae.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalau Bunge lipewe status ya Maazimio kadhaa ambayo ni mengi kwa kweli, ambayo yameshaazimiwa na Bunge hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu ya hiyo nia njema ya Serikali, unaweza ukatoa commitment hiyo?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza awali kwamba masuala yote haya yanagusa maeneo mengi sana ambayo yanatakiwa ufuatiliaji wa kina na baadae nilieleza kwamba kila tukio linagusa Wizara kadhaa, kwa hiyo siwezi kusema kwamba katika Bunge hili nitakuja kuleta taarifa hiyo mpaka pale ambako nitakutana na Wizara, nijue wamefikia hatua gani, pia tutakutana na Mheshimiwa Spika ili tujue utaratibu mzima wa namna ya kupata hizo Hansard na kufanya mapitio. Tukijiridhisha na tukiona kwamba jambo hilo sasa linafaa kuletwa Bungeni na kwa kuwa liliazimiwa na Bunge, basi tutafanya maamuzi ya pamoja ya kuleta Taarifa hiyo Bungeni.