Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 49 Finance and Planning Maswali kwa Waziri Mkuu 2 2016-06-23

Name

Hamida Mohamedi Abdallah

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini sasa nielekeze swali langu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza lengo lake la sera za fedha na sheria kwa kupeleka maendeleo vijijini na hasa kwa kuwapelekea fedha za miradi ya maendeleo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo, zinafika katika Halmashauri kwa wakati ili kuhakikisha wanatekeleza shughuli za maendeleo?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka nia ya dhati ya kupeleka fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu, Wizara na Taasisi za Umma ili kufanya kazi za maendeleo. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mwaka huu kupitia bajeti yetu hii ambayo sasa tunaendelea nayo, tumefanya mabadiliko makubwa ya kutenga na kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo kutoka asilimia 27 mpaka asilimia 40.
Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba miradi yote ya maendeleo, yale yote ambayo tunahitaji yafanyiwe maboresho, yanatekelezwa kama ambavyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mikakati kadhaa, moja ni kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato, lakini pia tunadhibiti mianya ya ukwepaji kodi ili kuweza kujiongezea pato zaidi, lakini kubwa zaidi ni kusimamia fedha hizi ambazo tunazipeleka kwenye Taasisi za Umma kwamba zinatumika kama ilivyokusudiwa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali bado tunaendelea kuwataka watumishi, pindi fedha hizi zitakapokusanywa na baada ya Bunge hili, tutaanza kupeleka fedha kwenye mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na Taasisi na Wizara.
Nataka nitumie nafasi hii kuwaambia Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kupokea fedha na kusimamia matumizi, kuhakikisha kwamba fedha hii iliyotengwa inatumika kama ambavyo imekusudiwa; na kwamba hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote ambaye atathibitika kupoteza fedha hizi nje ya matumizi ambayo tumeyakadiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni mkakati wetu pia kuhakikisha kwamba baada ya makusanyo tuzipeleke fedha zote. Wajibu mwingine ni kuhakikisha kwamba miradi inayotekelezwa inakuwa na thamani ya fedha iliyopelekwa kwa ajili ya matumizi ya maeneo hayo. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itasimamia jambo hili, lakini pia tushirikiane Wabunge wote, nyie pia ni Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani kwenye maeneo yenu. Kwa hiyo, tusaidiane tukishirikiana, mkakati wa Serikali wa kupeleka fedha kwa wakati na mkakati wa Serikali wa kutaka
kuongeza fedha ili kupeleka kwenye maendeleo uweze kufikiwa na hatimaye Watanzania waweze kuiona tija.

Additional Question(s) to Prime Minister

Name

Hamida Mohamedi Abdallah

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Question 1

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH:
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa majibu yake mazuri, lakini ningependa kujua sasa, eneo hili la watumishi kupitia Halmashauri zetu, wamejipangaje kwa suala zima la mapo
keo haya ya mabadiliko ya kuendelea kutaka kuleta maendeleo zaidi? Kwa sababu kuna maeneo mengine tuna Makaimu Wakurugenzi na Makaimu Watendaji mbalimbali. Sasa napenda kujua Serikali imejipanga vipi katika eneo hili la Watendaji wetu? Ahsante.

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa namna gani tumejipanga kuhakikisha fedha hizi zinapokelewa na watu stahiki, kwa maana wenye
mamlaka kamili; kama ambavyo mnajua, Mheshimiwa Rais anaendelea kuunda Serikali kwa kuteua watumishi mbalimbali katika kada mbalimbali.
Najua hatua iliyobaki sasa ni ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wenye dhamana. Wakurugenzi watashirikiana na Wakuu wa Idara na watumishi wote kwenye Halmashauri zetu.
Kwa hiyo, moja kati ya mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapeleka
fedha kwa wahusika ni kwa kukamilisha uundaji wa Serikali kwenye ngazi ya mamlaka ya Serikali za Mitaa na Halmashauri za Wilaya jambo ambalo litatokea pindi Mheshimiwa Rais atakapofanya maamuzi ya kusoma orodha ya Wakuu wa Wilaya na Wakarugenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu zaidi, ni kwamba mtumishi yeyote
atakayekuwa kwenye eneo hilo na fedha zimefika na anawajibika kuzipokea ili aende kuzisimamia, anao wajibu wa kuzisimamia. Kwa sababu jukumu hili la kila mtumishi wa mamlaka ya Serikali za Mitaa, inaweza kuwa Mkurugenzi au Mkuu wa Idara na Mkuu wa Idara huyo kwa idara yake, anawajibika kupeleka fedha kwenye ngazi ya vijiji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi anawajibika kufanya hilo na Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote ambaye atahusika kwa ubadhirifu wa fedha ambazo tutazipeleka kwenye shughuli za maendeleo kwenye ngazi zetu za Vijiji na Kata.