Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 4 Sitting 3 Questions to Prime Minister Maswali kwa Waziri Mkuu 2 2021-09-02

Name

Halima James Mdee

Gender

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu kama yalivyo maeneo mengine duniani, tupo kwenye wimbi la Covid awamu ya tatu, natambua kazi ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwanza kutambua uwepo wa ugonjwa, lakini pili kuleta kinga ambayo mtu anaweza akaamua ajikinge ama la kutokana na uamuzi wake binafsi. Hata hivyo, bado kuna changamoto nyingi sana, wananchi wetu wengi wanakufa ama kwa kukosa maarifa ama kwa hospitali zetu kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha ama kwa Madaktari wetu na wahudumu wa afya kutokuwa motivated kwa sababu wanafanya kazi wanachoka kupita kiasi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa kwa kuzingatia kwamba changamoto hii inapoteza maisha ya Watanzania wengi sana, hapa Mbunge mmoja mmoja ukimuuliza amepoteza ndugu au Wanajimbo ni wengi sana. Nataka tu nijue Serikali ina mikakati gani ya ziada kuweza kutatua ama kukabiliana na hii changamoto kwa mazingira ya ziada tofauti na mazingira yaliyopo sasa?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Watanzania tunajua kwamba dunia nzima imekubwa na ugonjwa huu na toka tumeanza kuukabili ugonjwa huu, kila nchi imekuwa ikitafuta namna nzuri ya kuokoa wananchi wake kwa kuwahusisha wataalam katika kutoa elimu ya namna ya kujikinga ugonjwa huu. Nikubaliane naye kwamba tumepoteza ndugu zetu wale ambao wanapata tatizo hili na bado wapo wengine wanaugua wapo kwenye maeneo ya utolewaji huduma, lakini pia maambukizi bado yapo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nini ambacho Serikali inakifanya sasa ni kutoa elimu kwanza ya kujua namna ya kujikinga na ugonjwa huu; lakini pia kuimarisha utoaji huduma kwenye maeneo yetu yote ya kutolea huduma kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya, Hospitali za Wilaya, Mikoa; lakini pia na kupeleka madawa yale ambayo yanahusu lakini na vifaa vya kusaidia kutibu ugonjwa huu. Zoezi hili linaendelea nchini kote huku pia wataalam wetu wakiendelea kushauri namna nzuri ya kukabiliana na ugonjwa huu kwa ngazi ya Serikali na sisi pia tunatumia njia hiyo kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari ili tuweze kukabiliana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, uzuri ugonjwa huu sasa tunashirikiana na Shirika la Afya Duniani, lakini pia tunapata uzoefu namna ambavyo wenzetu wanakabiliana nalo ili kuhakikisha kwamba kwanza tunapunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa maambukizi; lakini mbili wale ambao wanapata tatizo wanahudumiwa vizuri kwenye hospitali zetu; na kuhakikisha kwamba nchi hii haiendelei kupata ugonjwa huu na kuusambaza maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, inawezekana pia kwamba hatua hii bado sio sahihi sana au haitoshelezi mahitaji ya kukabiliana na ugonjwa huu, bado Serikali inaendelea kushirikisha wataalam wetu wa ndani kutafuta mbinu mbalimbali, lakini pia tunahamasisha pia hata tiba za asili kama nazo zinasaidia. Tumewahi kufanya hayo na tumefanikiwa, lakini sisi tunaendelea pia kumwamini Mwenyezi Mungu, tunaomba na dua pia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunajaribu kutafuta mbinu zote, tunajitahidi kutafuta mbinu zote ili mradi tunakabiliana na hili. Tunaendelea kuhamasisha wananchi wetu pia kushiriki kikamilifu katika namna yote inayoweza kusaidia kupunguza maambukizi kama hivyo kuvaa barakoa pale ambapo unaona upo eneo hatarishi lakini pia kutumia vitakasa mikono, maji tiririka pamoja na sabuni; ni mambo ambayo tunahamasisha.

Mheshimiwa Spika, Madaktari wameenda mbali zaidi wanatuhamasisha lishe bora ambayo itatusaidia kuongeza virutubisho mwilini na kufanya mazoezi, kuuweka mwili imara kwa wale ambao wana uwezo wa kimwili. Kwa hiyo, tunajitahidi kutafuta mbinu mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Watanzania tuendelee kushiriki pamoja katika kupambana na ugonjwa huu. Tumeona nchi mbalimbali nazo pia zinachanja na tumeona pia kuna umuhimu wa kuchanja kwa sababu chanjo inaimarisha pia kuweka virutubisho ndani ya mwili. Najua, kuna vipingamizi, watu wengine wanapinga lakini ni kwa kutoelewa na wale ambao wanapinga ni wale tu ambao hawajaguswa na tatizo hili ndani ya familia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viongozi wa nchi hii toka ugonjwa huu ulipoingia walieleza wazi kabisa kwa Watanzania kwamba huu ugonjwa ni hatari, lakini mbinu mbalimbali zinatumika, Madaktari wanashauri pamoja na chanjo lakini tutajiridhisha kila aina ya tiba ili na sisi tuweze kuingia hapo. Nataka niwaambie Watanzania tumetumia Madaktari/ wataalam wetu wa ndani kwenda kufanya uchunguzi wa aina hizi za chanjo kama zinafaa na sisi pia kushiriki na wamefanya hivyo, wameshiriki na tuliowatumia hawa ni Madaktari ambao ni ndugu zetu, kaka zetu, dada zetu ambao wamebobea kwenye Sekta ya Afya na wanaaminika pia hata huko nje. Kwa kweli ushauri wao na sisi tumejiridhisha kwa sababu hatuamini kwamba Daktari huyu Mtanzania aliyezaliwa hapa. ana ndugu kaka, dada akamshauri achanje chanjo ambayo itakuja kumpotezea maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile wote mnajua kiongozi wa nchi, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametangulia mbele, pamoja na nyadhifa alizonazo, dhamana aliyoibeba katika nchi hii ya kuwalinda na kuwahifadhi Watanzania yeye amekuwa mstari wa mbele kuchanja na kutuhamasisha tuchanje, lakini amesema chanjo sio lazima lakini ni muhimu. Chanjo sio lazima lakini muhimu kwa sababu inaongeza kinga mwilini. Kwa hiyo, Watanzania tumeanza kuona wanajitokeza na niendelee kuwahamasisha Watanzania wajitokeze kwenda kuchanja ili tuweze kujikinga. Hizi zote ni njia za kupambana na ugonjwa huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kwamba Serikali tutaendelea kushirikiana na Mataifa ambayo tunajua yana nia njema na sisi na yanatumia njia mbalimbali katika kujikinga, lakini pia kwa kuwatumia wataalam wetu kujiridhisha na hatua hizo kama zinafaa na sisi pia kushiriki kwa namna hiyo. Ahsante sana. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister