Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (25 total)

MHE. ZITTO Z. R. KABWE: Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitoa taarifa ya upotevu wa shilingi bilioni 28 za wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, aliyekuwa Rais katika Serikali wa Awamu ya Nne, alikwenda Tabora akaagiza viongozi wa Ushirika wa WETCU na wahusika wote wa ubadhirifu ule wakamatwe mara moja na kufikishwa Mahakamani. Mpaka leo hii hakuna ambaye amekamatwa wala kufikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, wakulima kwa kupitia vyama vyao vya msingi inabidi walipe fedha zile shilingi bilioni 28. Serikali ya Awamu ya Tano inachukua hatua gani dhidi ya watu hawa ambao wamewaibia wakulima wa tumbaku na kuwafanya waendelee kuwa maskini licha ya kwamba wanajitahidi kulima mwaka hadi mwaka? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea tayari ninayo ile ripoti ya Mkaguzi na naipitia mstari kwa mstari na ninategemea baada ya Bunge hili nitapitia katika maeneo hayo yanayolima tumbaku hasa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kwenda kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa.
Mheshimiwa Spika, siyo tu kwenye tumbaku, tunafuatilia malalamiko ya maeneo mengine yote kwenye mazao mengine yote kuhakikisha wakulima hawaibiwi na watu wasio waaminifu wanaokuwa kwenye vyama hivyo.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe wiki iliyopita tu Mheshimiwa Spika nilikuwa Iringa nikakuta Vyama vya Msingi vimekopa matrekta kutoka CRDB na wamesainiana mikataba na wamekatwa kutokana na michango yao na kutokana na mazao yao, lakini baadhi ya wajanja wameweka utaratibu kwamba baada ya makato kwisha yale matrekta yawe ya kwao.
Mheshimiwa Spika, niliyarudisha kwa Vyama vya Msingi na niliagiza CRDB iandike hati zile kwa Vyama vya Msingi na nikaagiza mamlaka zinazohusika wachukue hatua za kisheria kwa wale ambao wamefanya utapeli.
Kwa hiyo, tutalifanya na wale waliohusika ambao walibainika kupitia Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, hakuna uchunguzi juu ya uchunguzi. Naagiza vyombo vinavyohusika vichukue hatua kwa sababu tayari mtu aliyepewa dhamana ya kukagua alishakagua na kubainisha wale walioiba. Kwa hiyo, nitaenda kufuatilia kujua ni wangapi wameshafikishwa Mahakamani kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2014 zao la korosho lilivunja rekodi ya uzalishaji mpaka tani laki mbili kwa mwaka, lakini zao la pamba lilishuka uzalishaji wake kwa takribani asilimia 40, na bado nchi yetu inauza korosho nje kama korosho ghafi, ilihali kulikuwa na viwanda vingi ambavyo vilijengwa na Baba wa Taifa takribani viwanda 12, na baadhi ya viwanda sasa hivi vimegeuka kuwa ni ma-godown kwa ajili ya stakabadhi ghalani.
Serikali inachukua hatua gani ya kuhakikisha kwamba korosho zote ambazo zinazalishwa nchini zinabanguliwa kwanza hapahapa nchini kabla ya kupelekwa nje na kutungeneza ajira nje? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba nitoe jibu kwa Mheshimiwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa na kugeuzwa maghala, Treasury Registrar ametoa malekezo na wito wote wajisalimishe kwao waeleze kwa nini wamekiuka misingi ya mauziano. Misingi ya mauziano ilikuwa ni kwamba walipe pesa kidogo kusudi viwanda vile waendelee kuvitumia kwa kubangua korosho na kutoa ajira. Kwa hiyo, tangazo limetolewa na muda wake umeishakwisha kwa hiyo asiyeenda anakiuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ubanguaji wa korosho. Ubanguaji wa korosho ndiyo msimamo wetu na wiki iliyopita niliongea na Balozi wa India anasema wao hawana matatizo. India wamefungua dirisha kwa mazao ya Tanzania yapatayo 480 anasema hana tatizo, na taarifa yako Mheshimiwa Zito na watu wa Kanda ya Korosho, kuna kampuni imeishaanza mchakato wa kujenga viwanda vipya katika ukanda wa korosho na wanasema korosho yote iliyopo haitoshelezi viwanda vyao wakianza kazi, na wameniomba niwape hata kibali cha kuagiza korosho nyingine kutoka nje ya nchi nimesema hapana, wasaidieni wananchi wetu kulima zaidi ili mbangue na muuze huko duniani.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kati ya mwaka 2011/2012 mpaka mwaka 2015/2016, jumla ya fedha amba zo Serikali ilizikopa nje kwa mfumo wa namna hii ni shilingi trilioni 6.8. Katika taarifa ya hukumu ambayo Mheshimiwa Waziri amei-refer kwenye statements of facts ukurasa wa 17 aya ya 113 inaonesha kwamba mtindo huu wa kutumia vikampuni kwa ajili ya kuweza kupata mikopo umekuwa ukitumika na benki nyingi za biashara hapa nchini.
Serikali haioni kwamba imefikia wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aweze kufanya ukaguzi maalum wa mikopo yote ya kibiashara ambayo Serikali imeichukua kati ya 2011/2012 mpaka 2015/2016 ili kuweza kujua kama pia kulikuwa kuna aina za rushwa za namna hii ambazo zilikuwa zinafanyika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwamba DFA ambayo ndiyo hiyo hukumu ya Uingereza ilikuwa ina lengo la kuilinda Benki ya Uingereza ambayo ndiyo iliyotoa hongo kwa maafisa wetu ili iweze kupata biashara. Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa Serikali ifungue kesi dhidi ya benki hii ya Uingereza ili iwe ni fundisho kwa makampuni ya nje yanayohonga kupata biashara katika nchi za Kiafrika?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwanza, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anayo majukumu ya Kikatiba ya kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo, naomba kushauri tu kwamba hili ni jukumu lake anaweza akalitekeleza wakati wowote ili kujiridhisha kama mikopo hii ambayo imekuwa ikipatikana imekuwa ikipatikana kwa namna ambayo inaifanya nchi iingie kwenye hasara.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili nirejee tu pia kwenye jibu zuri la Naibu Waziri wa Fedha, kwamba kama Mheshimiwa anazo taarifa zozote zinazoweza kutusaidia sisi, ama kufungua shauri la madai au kufungua shauri la jinai, basi ashirikiane na vyombo vinavyofanya. Kwa mfano, hili shauri la madai sisi tukiletewa litaletwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tutaliangalia tuone kama linakidhi sifa na sheria na kwa kuzingatia pia mahusiano tuliyonayo na nchi kama ya Uingereza tuone kama tunaweza, moja, kufungua kesi ya jinai au pili, tulifanye kwa namna ambayo tunaweza tukafungua kesi ya madai. Lakini mpaka sasa kilichopo ni kwamba hii benki iliingia makubaliano na Serious Fraud Office ya Uingereza kwa kitu kinachoitwa deferred prosecution agreement, ambayo pamoja na mengine walitakiwa walipe hizi dola kama Naibu Waziri wa Fedha alivyosema. Wakishindwa Serikali ya Uingereza itawachukulia hatua ya kesi ya jinai hii benki na sisi huku kama alivyosema Naibu Waziri wa Fedha, Benki Kuu imewataka Stanbic Tanzania nao walipe hiyo faini na muda huu ambao walipaswa wawe wametoa jibu ilikuwa ni tarehe thelathini. Kwa hiyo, tuupokee tu ushauri wa Mheshimiwa Zitto, Serikali itaufanyia kazi kwa kuzingatia sheria za ndani ya nchi na mahusiano yetu ya kisheria katika Jumuiya ya Kimataifa. Ahsante sana.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, alichokiuliza Mheshimiwa Sabreena ni kwa nini Serikali haitumii mawakala. Mawakala hawana gharama ni kama leo unaposema kwamba TANESCO iuze LUKU yenyewe badala ya kutumia ma-agent wa LUKU. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri na Mkurugenzi Mkuu wa TRL wakae, kwa sababu mimi na Mkurugenzi Mkuu wa TRL na Waziri tumekutana Kigoma, tumekwenda Stesheni, tumeona hali ilivyo na tumekubaliana kwamba the best way ni kuruhusu mawakala kuuza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtu yupo Ilagala, yupo Kibondo, yupo Kasulu, kama alivyosema Mheshimiwa Sabreena, mawakala wauze, tunakuwa tunajua idadi ya mabehewa yatakayokuja Kigoma, abiria watakaoondoka, tiketi zitolewe ziweze kuuzwa. Nashindwa kuelewa Mheshimiwa Naibu Waziri anazungumzia gharama gani hapa, sielewi kabisa, inabidi ujifunze kwa watu wa Nishati na Madini, TANESCO wanafanyaje kwenye LUKU.
Mheshimiwa Waziri tunaomba umsaidie Naibu wako bwana!
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikwenda pamoja na Mheshimiwa Zitto kule Kigoma na tuliona hali halisi na kupitia kampuni yetu ya TRL tuliamua kuanzia sasa hivi tunakwenda kufanya mfumo wa elektroniki ambao watu wanaweza kununua tiketi kwa simu popote pale walipo Tanzania. Tunaanzia na trial ya kwanza kuanzia Mpanda mpaka Tabora wakati wowote kuanzia sasa hivi, halafu tunakwenda Kigoma na Tabora. Ahsante sana.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba, moja ya gharama kubwa sana ya miradi ya maji ni gharama za kusukuma maji, pampu za maji na kwa mujibu wa mradi huu tunategemea kutumia pampu za umeme wa mafuta kwa kuweka jenereta na kununua umeme kutoka TANESCO ambapo gharama zitakuwa ni kubwa zaidi kwa wananchi katika kuyalipia hayo maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri haoni kwamba, itakuwa ni jambo la busara na economical kutumia hizi liquidated damages ambazo wamempa Mkandarasi kufunga solar pumps, ili ziweze kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi kupelekea wananchi waweze kupata maji kwa gharama nafuu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi huu kwa usanifu wake tumesanifu kutumia pump kwa kutumia nishati ya umeme. Naomba nipokee ushauri wake kwamba, tuweze kuangalia uwezekano wa kubadilisha. Tukishakuwa tumekabidhiwa huu mradi Serikali tunaweza tukabadilisha sasa pampu zile tutumie solar kwa maana ya kutaka kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi ule.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo Naibu Waziri ameyajibu amesema kwamba Benki Kuu haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya dhahabu. Nadhani swali la msingi hapa ni kuweka akiba (reserve) kama dhahabu, siyo kufanya biashara ya dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, Waziri atakuwa anakumbuka huko nyuma Tanzania ilikuwa inaweka reserve hii kwenye dhahabu. Kwa hiyo, uzoefu wa kuweka hivyo tunao na swali la msingi hapa ni kwamba kwa nini tusitumie na baadhi ya migodi tunaimiliki wenyewe, tusitumie sehemu ya uzalishaji kutunza kwa sababu bei ya dhahabu hata iwe nini bado huwa ni stable zaidi kuliko bei ya dola au fedha zingine za kigeni ambazo tunawekea akiba zetu.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Na baadae imepanda.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kuhusu uwezo wa Benki Kuu ya Tanzania ni kweli miaka ya 1980 tulikuwa na utaratibu huo lakini tulipigwa kweli, maana wakati ule bei ya dhahabu iliporomoka kutoka dola za Kimarekani 700 kwa ounce zikaporomoka chini mpaka kufikia dola 235 kwa ounce moja. Hiyo ndiyo ilifanya Serikali iamue kuuza hata ile dhahabu iliyobaki baada ya kupata hasara kubwa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Baadae imepanda ni sawa.
Lakini sasa uzoefu tunaouzungumzia ni pamoja na uwezo wenyewe wa pale Benki Kuu kusema hii ni dhahabu kweli na hii siyo…
Waheshimiwa Wabunge, tuelewane Mheshimiwa Spika amenipa nafasi.
Kwa hiyo, ni muhimu sana ule uwezo wenyewe uweze kujengwa ndani ya Benki Kuu, siyo tu kuitambua ile dhahabu yenyewe iliyo halali na sivyo, lakini na biashara yenyewe na kufuatilia mwenendo unavyoenenda duniani.
Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ni kwamba Serikali inalifanyia kazi ili kuangalia tena uwezekano wa kuweka akiba yetu katika dhahabu au madini mengine ya vito ambayo tunayo hapa nchini.
vya Majimaji ni Mahenge ambako takribani Watanzania wakati ule Watanganyika 30,000 waliuawa kwa njaa kwa sababu wanajeshi wa Ujerumani walichoma chakula cha Watanzania ili wasiweze kuishi na kufa jambo ambalo kwa tafsiri za kivita ni sawasawa na genocide.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari Serikali ya Ujerumani imeomba radhi na kulipa fidia kwenye Vita ya Namaqua na Herero Namibia, Serikali sasa katika mapendekezo ambayo imeyakubali kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge itapeleka kwa Serikali ya Ujerumani pamoja na ombi la kuomba radhi rasmi kwa mauaji ambayo wanajeshi wake waliyafanya Tanzania?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwamba mifano ya nchi zilizoomba fidia kwa vita vilivyotokea kipindi cha ukoloni ni mingi, hapa tumetajiwa Kenya, lakini sasa tunaambiwa Namibia. Kwa hivyo, nitawaomba wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wanataka kuanza rasmi taratibu hizi ili tuweze kupata hiyo fidia basi wawasiliane na nchi hizi ili kujua wameanzaje na hatimaye tuweze kupeleka hilo ombi rasmi. Wakati huohuo nataka nikubaliane na Mheshimiwa Zitto kwamba, pamoja na fidia, kama itathibitika kwamba kulikuwa kuna mambo yaliyofanyika ambayo yanaashiria genocide, basi Serikali hiyo iweze kuomba msamaha vilevile.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika,
changamoto kubwa ya umaskini Tanzania ni kwamba idadi kubwa ya watu ama wako chini kidogo ya mstari wa umaskini au juu kidogo ya mstari wa umaskini. Kwa hiyo, hata wakipata fedha hizi za TASAF wakipata shock yoyote ya
kimaisha wanarudi chini kwenye mstari wa umaskini na wanakuwa maskini, kwa hiyo, juhudi zote hizi zinakuwa hazijaleta manufaa anayotakiwa. Serikali haioni kwamba umefikia wakati muafaka katika fedha hizi za TASAF kuwe na component ya social protection ili kuhakikisha kwamba baadhi ya watu hawa wanaingizwa kwenye hifadhi ya jamii, wanaweka akiba, wanaweza kupata mikopo midogo midogo ya kuendesha biashara zao, wanaweza wakapata bima ya afya, ili watakapopata shock wasirudi tena kwenye mstari wa umaskini? Haoni kuna haja ya kufanya hivyo sasa hivi kwenye TASAF inayoendelea?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru maana ni hoja ambayo amekuwa akiifuatilia mara kwa mara. Tulipofanya semina katika Bunge hili ambayo iliendeshwa na TASAF pia aliweza kuhoji swali kama hili.
Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema kwamba,
lengo la conditional cash transfers kokote duniani ni kuhakikisha kwamba mwisho wa siku ni kuwa na social protection moja ambayo inaunganisha kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Sisi kama TASAF tumeanza na sasa watoto wenye miaka sifuri mpaka tano, mpaka sasa hivi watu wazima
walau kuna hizo component tatu kwenye miradi ya ujira, tunatoa pia ajira za muda, tunatoa miradi ya miundombinu, tuna targeted infrastructure pamoja na mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kusema,tunaiona hoja yake lakini kwa sasa ngoja tumalizie awamu ya kwanza ya awamu ya tatu. Tutakapokuja kusanifu sasa awamu ya pili itakayoanza mwaka 2019/2020 tutaweza kuona ni kwa namna gani swala hili linaweza kuzingatiwa.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 Serikali iliingia mkataba au ilikubaliana na Kampuni ya Total ya Ufaransa kwa ajili ya utafutaji wa mafuta katika Lake Tanganyika North Block baadae mazungumzo yakafa, mwaka 2014 Kampuni nyingine ya Ras Al Khaimah nayo pia ikawa imepewa zabuni ya utafutaji wa mafuta wa kitalu cha Kaskazini cha Lake Tanganyika, lakini mpaka sasa na kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri hakuna maelezo yoyote kuhusiana na hilo, kuna maelezo ya block ya Kusini peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 TPDC ilifanya survey katika eneo lote la ziwa na katika majibu ya Waziri hakuna matokeo yoyote ya utafiti kama jinsi ambavyo Mheshimiwa Nsanzugwanko alikuwa anataka kupatiwa taarifa.
Swali la kwanza, Serikali inaeleza nini status ya sasa hivi ya utafutaji wa mafuta katika eneo la Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika ambapo Waziri hujalitolea maelezo kabisa?
Swali la pili, nini status ya umeme wa maporomoko ya Mto Malagarasi ambao ni tegemeo kubwa sana la uzalishaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zitto, nakumbuka tangu wakati wa uwekezaji katika Mto Malagarasi, wakati wa uwekezaji na ufadhili wa MCC alikuwa mbele sana kufuatilia umeme wa Kigoma, kwa hiyo nakupongeza sana kwa niaba ya wananchi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana wananchi pia na Wabunge wa Kigoma wote Mheshimiwa Serukamba Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa mshikamano wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye maswali mawili ya Mheshimiwa Zitto, status ya utafiti ikoje katika Ziwa Tanganyika. Kwanza kabisa pamoja na maswali ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Zitto, kama alivyosema mwaka 2011 kampuni ya Total ilianza kufanya utafiti, lakini kulingana na gharama za uwekezaji ilishindwa na haikuendelea. Hata hivyo, taarifa zake zilitusaidia sana katika utafiti unaoendelea kwa sababu katika taarifa ambazo tulizipata, kampuni kwa kushirikiana na TPDC waliweza kuchora ramani za urefu wa kilometa 20,024 chini ya Ziwa Tanganyika ambazo zinatupa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili walitathmini taarifa za utafiti za Total za miaka 80 iliyofanyiwa utafiti na makampuni ya nyuma, kwa hiyo, Kampuni ya Total iliacha lakini ilituachia taarifa Mheshimiwa Zitto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo status ikoje, ni kwamba baada ya utafiti huo TPDC mwaka 2014/2015 ilifanya geo-survey katika maeneo ya Ziwa Tanganyika na kwa kweli pesa kubwa sana zilitumika shilingi bilioni 6.96 kwa ajili ya utafiti huo na matokeo yake kwa kweli matarajio ya kupata mafuta katika Ziwa Tanganyika yapo. Hiyo ndiyo status Mheshimiwa Zitto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mradi wa Malagarasi ni kati ya miradi muhimu sana katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, maeneo ya Kigoma na maeneo ya jirani kwa sababu kwa sasa Mheshimiwa Zitto tumekamilisha upembuzi yakinifu na tumeshaanza majadiliano na wawekezaji pamoja na wafadhili wetu, tumepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na mradi ule utagharimu dola milioni 149.5. Kwa hiyo, shughuli zitaanza mwezi wa saba mwakani na zitakamilika mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. ZITTO Z. R. KABWE: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji tuliamua kutumia sehemu ya ushuru ambao manispaa inakusanya kwa ajili ya kuongeza fedha za kuwalipa watu hawa, Wenyeviti wa Mitaa pamoja na kuwalipia Bima ya Afya. Hata hivyo, kutokana na hatua ambayo Serikali Kuu imechukua, mmechukua kodi ya majengo, ushuru wa mabango, haya maelekezo mnayoyatoa kwamba halmashauri ziwalipe hawa watu hizi 20 percent zitatoka wapi wakati ushuru wote, mapato yote Serikali Kuu inayachukua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasema hiyo ni the best practice ambayo mmeifanya na tunataka innovative idea kama hizo wakati mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, suala la kuchukua fedha Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Waziri wa Fedha alizungumza wazi, kwamba kinachofanywa na Serikali Kuu ni kukusanya baadaye inarudisha katika halmashauri husika; hii ilikuwa ni wazi kabisa, utaratibu wote ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha alizungumza, kutokana na hamasa nzuri, ndiyo maana leo hii tunaona jinsi ambavyo watu wanapanga foleni TRA kwenda kulipa kodi ya majengo. Kwa hiyo kikubwa zaidi naomba tukubaliane na Serikali, lengo la Serikali ni kusukuma mambo yaende vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokihitaji ni kwamba tufike Taifa ambalo linaweza kuamua kufanya mambo vizuri zaidi. Kwa hiyo, tutachukua zile best practice ambazo sehemu mbalimbali zipo. Hata hivyo niseme kwamba Serikali haikuwa na nia ya kunyang’anya authority ya halmashauri katika kuchukua mapato, isipokuwa ni utaratibu tu unawekwa halafu baadaye tutaona nini faida ya jambo hili ambalo ni jipya, lakini ambalo kwetu lina msingi mkubwa sana.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2016 mikopo ya benki kwenda kwenye sekta binafsi imeporomoko kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha inachukua hatua gani madhubuti ya kuhakikisha kwamba wajasiliamali na hasa viwanda na wafanyabiashara wanaendelea kupata mikopo benki kwa kuboresha hali ya uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba hali ya uchumi wa Taifa letu bado iko imara na iko vizuri na si kwamba kutokupewa mikopo kwa sekta binafsi kunaashiria kuporomoka kwa uchumi, hilo naomba niliweke vizuri hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwambie kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha mikopo hii kwa sekta binafsi inaendelea kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba, benki zetu zimekaa vizuri sasa katika kuhakikisha zinadhibiti mikopo chechefu ambayo imekuwa ikizisumbua miaka mingi iliyopika. Kwa hiyo ni usimamizi madhubuti uliowekwa na Benki Kuu kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, na tunaendelea kusimamia kuhakikisha kwamba kabla ya benki na taasisi za kifedha hazijatoa mikopo wahakikishe mtu wanaempa mikopo ni nani na ana uhakika gani wa kurejesha mikopo ambayo ipo.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kufikia hatua hii kuna juhudi kubwa ambazo zimefanywa na ninapenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watu wa Tume ya Umwagiliaji kuweza kuhakikisha kwamba tunafikia hatua hii. Lakini kumekuwa na tabia ya miradi ambayo tayari inakubaliwa na wafadhili lakini hatua za kuchukua mpaka kupata hiyo miradi inakuwa ni ya muda mrefu sana mfano wa mradi huu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali. Kwa hiyo, kwa mfano mradi huu toka mwaka 2015 tumepewa haya masharti na sasa hivi ndiyo kwanza tunakwenda kwenye hatua za manunuzi ya mtalaamu mwelekezi.
Sasa Waziri anaweza kutufahamisha hatua hizi za kukamilisha detailed design na hii feasibility study zitakamilika lini ili kuweza kuona mradi wenyewe utaanza kutekelezwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kwa upande wa Serikali ni hatua gani zitachukuliwa katika kuhakikisha kwamba miradi ambayo tunakuwa tumeahidiwa na imeshakubalika tunapunguza muda ambao tunauchukua kuikamilisha ili hii miradi isiende nchi nyingine? Kwa sababu sasa hivi miradi mingi inaenda Kenya na Mozambique kwa sababu ya kuchelewa kwetu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameonesha concern yake kwamba wafadhili wanatoa fedha lakini pengine taratibu zinachukua muda mrefu. Nikuhakikishie Mheshimiwa Kabwe kwamba ni utaratibu wa kawaida, kunapokuwa na mradi ni lazima ufanye feasibility study ili uweze kuonesha economic viability ya mradi ule na huwezi ku-rush, lazima uende uweze kupata taarifa za uhakika zinazotakiwa. Baada ya hapo unaingia kwenye hatua nyingine sasa ya detailed design. Information hii tunayoifanya Mheshimiwa Mbunge kama haikukaa vizuri haiwezi kupitishwa kule tunakopeleka. Kwa hiyo, tunachokifanya ni utaratibu wa kawaida kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, Serikali inaitaka hiyo fedha, haiwezi kuiacha na ndiyo maana Hazina wanaendelea kufanya mawasiliano na hii Falme ya Kuwait ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kututunzia hiyo fedha na taarifa tayari zipo. Sasa hivi tunafanya manunuzi ya kumpata mtaalamu mshauri na huyo ndiye atakaye-define, kwa sababu tunapoweka ile proposal ya kwa wale ma-consultant ndipo tunawapa muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kutokana na complexity ya ile site tunaweza tukasema mfanye kwa miezi sita wakasema haitawezekana tukafanye miezi nane kulingana na hali yenyewe ya eneo wanalofanyia kazi. Hatuwezi kutoa muda kwa sasa, ngoja kwanza tusaini mikataba ya consultant ambayo itaonyesha period watakayotumia na wao ndio watakaotushauri muda tutakaouanza suala la ujenzi; baada ya hapo Mheshimiwa Mbunge tutakupa taarifa.
MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ambayo Serikali imeitoa ya nchi za Hungary na Russia, nchi hizi ni miongoni mwa nchi ambazo duniani zinatuhumiwa kwa kuendeshwa bila misingi ya kidemokrasia na kidikteta. Ni aibu sana kwamba nchi yetu inaweza ikaiga nchi ambazo tayari zinaonyesha kabisa kwamba hazifuati misingi ya kidemokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukwaa haya ya kimataifa yanatengeneza ushawishi wa nchi kwenye mataifa. Leo hii Mwenyekiti wa OGP ni nchi ya Canada, juzi Rais ame…
Ndio swali langu la kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Rais amesema kwamba amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Canada kuhusiana na suala la Bombardier. Je, Serikali haioni kwamba iwapo Tanzania ingekuwa imeendelea kuwa mwananchama wa OGP na Canada ndio Mwenyekiti wa OGP. Ombi hili la Rais lingeshughulikiwa kwa uzito zaidi kwa sababu ya mahusiano yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa Miji 15 duniani ambayo inashiriki katika OGP kwa uhuru kabisa na haizingatiwi kama nchi iko kwenye OGP au la. Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na ushiriki si tu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo inafaidika sana kwenye OGP lakini pia na Miji mingine ya Tanzania ambayo inataka kuingia kwenye OGP, Serikali inatoa kauli gani kuhusu hili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto ametoa mfano wa nchi zailizojitoa kwamba zinaendeshwa kwa udikteta na nini na nini. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanzania ilipofanya maamuzi haya, imefanya kwa kupima vigezo kwa Tanzania ilivyoona inafaa, hatujamuiga mtu. Sisi ni Taifa huru, linalojitawala, linalofanya maamuzi yake yenyewe bila kushurutishwa na Taifa lolote, liwe kubwa ama dogo duniani. Kwa hiyo, kwamba nchi yetu imeiga mawazo hayo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema kwamba Rais wetu amemwandikia Rais wa Canada na kwamba Canada ni Mwenyekiti wa hili, mahusiano yetu pengine jambo lingekuwa hili. Nataka nimweleze ndugu yangu Zitto Kabwe, sisi na Canada ni wanachama wa Jumuiya ya Madola, sisi tuna ubalozi Canada, with or without OGP yaani kuwepo ama bila kuwepo OGP mawasiliano yetu na Canada haiwezi kuwa tatizo. Na juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu walikuwa kule Canada. Kwa hiyo mambo haya ya Bombardier na OGP wala sijui yanaendaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefurahi kweli, swali lako la pili nimefurahi sana Ndugu Zitto Kabwe anataka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya ushiriki wa Kigoma Ujiji. Andiko lile la mradi ule linasema nchi ikijitoa, washirika wake wote waliomo ndani ya ile nchi na wao uanachama wao shughuli zao zinakoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo taarifa kwamba Manispaa ya Kigoma Ujiji mpaka sasa wanawasiliana na OGP na OGP wamemuandikia Waziri wa Mambo ya Nje kwamba wana nia ya kuendelea kushirikiana na ninyi. Sasa nataka kupitia Bunge lako Tukufu kuionya Manispaa ya Kigoma Ujiji, nchi inayozingatia utawala bora, haiwezi Serikali Kuu ifanye maamuzi Baraza la Madiwani wakasema sisi hatuta-comply, haijatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nionye Manispaa ya Kigoma waache mara moja, watekeleze maamuzi ya Serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama wanavyofanya sasa Serikali itachukua hatua kali zaidi. Na ninyi mnajua Serikali kwenye Manispaa sheria kali kuliko zote ni kuvunja Baraza la Madiwani na kuweka Tume ya Manispaa. (Makofi)
Nawaomba huko mliko Waheshimiwa Madiwani wa Kigoma na ndugu yangu Zitto Kabwe, msiifikishe Serikali huko. (Makofi)
MHE. ZITO Z. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mchakato wa bajeti mpya ya Serikali ya Mwaka 2018/2019 unaendelea, kumekuwa na taarifa kwamba Serikali sasa inajiondoa katika mfumo wa conditional cash transfer, yaani kwenda kuwapa fedha wananchi na inaanzisha mfumo tofauti. Baadhi ya mikataba ambayo Wizara ya Fedha ilikuwa iingie na baadhi ya nchi wafadhili ikiwemo Benki ya Dunia, Wizara ya Fedha imesitisha kusaini kwa sababu Serikali haitaki tena kuendelea kutoa hizi conditional cash transfer. Tunaomba taarifa rasmi ya Serikali ndani ya Bunge kuhusiana na jambo hili.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya TASAF sina taarifa ya Serikali sasa hivi kujiondoa katika kuwapelekea hizi fedha. Taarifa nilizonazo ni kwamba sasa hivi tunafanya utafiti wa hizi fedha. Badala ya watu kwenda kupanga foleni pale wilayani kila siku tunaangalia uwezekano wa kupekea fedha zao kwa njia ya simu ili kuwaondolea usumbufu wa kwenda wilayani. Hilo ambalo anasema Mheshimiwa Zitto Kabwe kama analisema liko njiani, lakini halijafika mezani kwa Waziri mwenye dhamana ya TASAF. (Makofi)
MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza wavuvi wa Kanda ya Ziwa hasa Soko la Mwaloni Mwanza hawana uwezo wa kuuza mazao yao ya samaki popote pale Tanzania. Akitaka kupeleka Mtwara, Kigoma, Morogoro, Dodoma, Serikali inamtaka alipe export royalty pale Mwanza kwa mazao ambayo anayauza ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara ya Mifugo na Uvuvi inanyanyasa wavuvi wa Kanda ya Ziwa na sasa nasikia kwamba wataelekea mpaka wavuvi wa Kigoma na Mbeya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano, haina nia ya kumnyanyasa mvuvi wa Tanzania. Nia yetu ni katika kuhakikisha kwamba mosi, tunalinda rasilimali za nchi yetu. Tunahakikisha kwamba mianya yote ya upotevu wa mapato yatokanayo na rasilimali za nchi yetu, ni lazima tudhibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wetu umetuonesha, anayoyasema Mheshimiwa Zitto ni mazao ya samaki kule Kanda ya Ziwa maarufu kama kayabo. Utafiti wetu kayabo kwa kiasi kikubwa haziliwi Tanzania, Kanda ya Ziwa yote hakuna walaji wakubwa wa kayabo. Imethibitishika kupitia tafiti zetu kayabo inaliwa zaidi nje ya mipaka ya nchi yetu na kwa kiasi kidogo sana katika Mikoa ya pembezoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi nia yetu sio kuwanyima wafanyabiashara na wadau wa uvuvi kufanya shughuli za uvuvi bali ni kuhakikisha mapato yetu hayawezi kupotea. Ndiyo maana tumewaomba wahakikishe kwamba wanalipia export royalty kwa sababu tulikwenda katika mipaka ya Ngara na kwingineko ambapo wananchi wenyewe kwa utafiti mdogo tulioufanya wametuthibitishia kwamba pale Ngara mathalani ulaji wa kayabo ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, samaki wale wengi wanakwenda nje ya mipaka yetu. Wavuvi wale na wafanyabiashara wasio kuwa na nia njema na mapato ya nchi yetu wanatumia fursa hiyo kudanganya kwamba wanapeleka Ngara, Songwe Tunduma na kwingineko mipakani mwetu, hali ikiwa si hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tuungane mkono katika wakati huu ambapo tunajaribu kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi yetu zinainufaisha nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa samaki mchango wake kwa Wizara, Halmashauri na Serikali Kuu haizidi shilingi bilioni 10 kwa mwaka, sisi tunataka tutoke katika shilingi bilioni 10 twende kwenye shilingi bilioni 200. Uwezo huo tunao, sababu hizo tunazo, tunaomba mtuunge mkono ili tuweze kufika mahala hapo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZITTO R. Z. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la changamoto za Bandari ya Bagamoyo, Bandari ya Nyamisati ni changamoto zinazofanana kabisa na miradi minne ya Bandari ya Kigoma. Uboreshaji wa Bandari ya Kigoma, Bandari kavu ya Katosho, Bandari ya Ujiji na Bandari ya Kibirizi; lakini tu ni kwamba fedha zimetengwa toka mwaka 2016/2017 na tayari Mamlaka ya Bandari imekwishaweka utaratibu wa manunuzi. Wizara imezuia Mamlaka ya Bandari kutangaza zabuni hizo za Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ilieleze Bunge hapa, ni kwa nini haijaidhinisha zabuni hizo kutangazwa ili wananchi wa Mkoa wa Kigoma waweze kupata faida ya uchumi wa jiografia kwa kuboresha Bandari ya Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba Serikali imezuia; unajua ujenzi una hatua zake, Mheshimiwa Zitto anafahamu. Ziko hatua, ndiyo maana tunaanza kwenye usanifu, tunaanza kuweka fedha na mijadala iko mingi kama kunajitokeza jambo ambalo linahitaji labda wakati mwingine kupata muda kuli-clear kwamba kama kuna risk inajitokeza lazima Serikali ichukue hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi na asubiri. Mheshimiwa Waziri wakati akijibu katika hotuba ya Waziri Mkuu alisema hapa Bungeni na alijaribu kusema kwa ufupi na akasema tusubiri wakati wa bajeti Mheshimiwa Zitto ataona namna tulivyojipanga ili kuhakikisha Bandari zote kwa upande wa Kigoma, kwa upande wa Ziwa Victoria, kwa upande wa Ziwa Nyasa na maeneo mengine. Kwa hiyo, niseme tu kwamba maeneo yote ambayo Mheshimiwa Zitto anataja kwa maana ya Katosho na Kibirizi tumeonesha vizuri katika mapendekezo ya bajeti ambayo ni Jumatatu tu tutaanza kuizungumza bajeti ya Wizara hii.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ilipitisha Sheria Ndogo ya Nyongeza ya Tozo mbalimbali katika Halmashauri na sheria ile ikasainiwa na Waziri mwenye dhamana wa TAMISEMI. Katika hali ya kushangaza, Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi alikuja Kigoma Machi, 2018 na kutangaza kwamba sheria ile isitekelezwe. Mpaka sasa watendaji wa halmashauri wanaogopa kukusanya ushuru kwa sababu ya agizo la Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi. Serikali inasema nini kuhusu jambo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ambazo tunazo katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni kwamba Baraza la Madiwani lilipitisha viwango vya tozo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, hizo taarifa ndizo tulizonazo na hata Mkuu wa Wilaya ya Kigoma anazo taarifa hio na ametuarifu. Kwa hiyo, hizi taarifa ambazo Mheshimiwa Zitto amezileta ni mpya na yeye ni rafiki yangu, hajawahi hata kuja ofisini kuniambia. Kwa hiyo, tutafuatilia baada ya kuwa amezitoa hapa ili tuone zina ukweli kiasi gani.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Februari, 2017, Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kigoma RCC ilipitisha mkakati wa kuendeleza zao la michikichi. Mpaka leo toka barua imepelekwa Wizara ya Kilimo hata kujibu kwamba imepokea barua ile kutoka Mkoa wa Kigoma haijajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yote yanayotolewa hapa kuhusiana na tissue culture Mikocheni, utafiti pale Tabora si ya kweli kwa sababu Kigoma ndiyo imepeleka mbegu Mikocheni na wala si Serikali. Je, Serikali haitaki kututhibitishia kwamba imeshikwa na wafanyabiashara wanaoagiza mawese ghafi kutoka Indonesia na Malaysia na ndiyo maana haitaki hata kujibu barua ya Mkoa wa Kigoma ya kuendeleza zao la michikichi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la kaka yangu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake ni zuri na kwa sababu Serikali hii ya Awamu ya Tano ni ya Hapa Kazi tu basi ningemwomba sana, sana, sana Mheshimiwa Mbunge kaka yangu kwa heshima na taadhima atuletee nakala ya hiyo barua sisi tuko tayari kuifuatilia na kuhakikisha kwamba tunaifanyia kazi.
MHE. ZITTO R. Z. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Serikali za Mitaa ni pamoja na sheria zinazohusiana na mabadiliko ya Sheria Ndogo za Tozo na Ushuru mbalimbali. Mpaka hapo tunapozungumza, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji haikusanyi ushuru, watendaji wamegoma kwa sababu ya amri ya Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi. Mara ya mwisho nilivyouliza Waziri alisema hana taarifa na nina uhakika sasa ana taarifa. Anatuambia nini kuhusiana na kutotekelezwa kwa sheria ambayo imetungwa na Baraza la Madiwani na imepitishwa na Waziri mwenye dhamana ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA - (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hoja ambayo ameileza Bunge lako tukufu kwa sasa naielewa vizuri sana baada ya kuwa ameigusia wiki iliyopita. Niseme tu kwamba Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kigoma ambalo linaongozwa na ACT lilipandisha ushuru kutoka Sh.15,000 mpaka Sh.50,000 kama tozo kwa wafanyabiashara na hizo ni tozo halali ambazo zinatakiwa kukusanywa na sisi tulimuagiza Mkuu wa Wilaya asimamie tozo hizo ziendelee kukusanywa kama zilivyopitishwa na Baraza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wananchi wa Kigoma wamekuwa wakilalamika na malalamiko yao mengine wameyapeleka kwa viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumetuma timu ya watalaam kwenda Kigoma kuangalia kinachoendelea na taarifa yao hawajatuletea. Kwa hiyo, naamini wakituletea taarifa yao Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe tutampa majibu sahihi zaidi.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme Kigoma ni wingi wa umeme na bahati mbaya sana Kigoma bado haijaunganishwa na Gridi ya Taifa na hata mpango ambao ulisainiwa kwa msaada wa Serikali ya Korea ambao Waziri wa Fedha alisaini takribani mwaka na nusu uliopita bado kabisa kuanza kutekelezwa. Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Mto Malagarasi, Igamba III ambao ndio jawabu la kudumu la umeme katika Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe sahihisho kidogo sio Malagarasi Igamba III; ni Malagarasi Igamba II. Baada ya kusema hayo sasa ni kweli kabisa mradi wa Malagarasi ilikuwa kwanza utekelezwe wakati wa mradi wa MCC mwaka 2008, lakini ikaonekana kwamba kulikuwa kuna matatizo ya REA species.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe taarifa katika Bunge lako tukufu ni kweli kabisa mradi huu sasa utaanza kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha na tumeshatenga fedha na juzi Mheshimiwa Zitto nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge tulikuwa nao wakati tunakamilisha majadiliano ya Benki ya Maendeleo ya Dunia kwa ajili ya kufadhili mradi huo na zinahitaji dola milioni 149.5 kwa ajili ya kuutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Mbunge mradi huu unakwenda kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KABWE R. Z. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali itafanya utafiti iweze kutoa kanuni za kuwezesha uvuvi wa kisasa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi katika Mkoa wa Kigoma kuweza kufanyika? Lini utafiti huo utaweza kufanyika kwa sababu sio wajibu wa wananchi ni wajibu wa Serikali kufanya huo utafiti na miaka 21 imepita bila huo utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sasa hivi kumekuwa na leseni nyingi sana za uvuvi. Mvuvi mmoja yaani kwa chombo kimoja kinahitaji leseni takribani tisa na hivyo kuongeza gharama kubwa sana kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika. Vilevile gharama za kuuza mazao ya uvuvi nje zimeongezeka kutoka senti 0.5 ya dola ya Marekani mpaka dola 1.5 kitu ambacho kinatufanya wavuvi wa Mkoa wa Kigoma kutokushindana vizuri na wenzetu wa Burundi na Congo kwa sababu wao hawana tozo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itahusianisha hizo tozo na kuzishusha ili tueweze kuendeleza export tunayoifanya sasa hivi ya mazao yetu kutoka Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali linalouliza kuwa ni lini Serikali itafanya utafiti. Kupita taasisi yetu ya TAFIRI tumeanza hatua za awali za kufanya utafiti katika maji yetu ya Ziwa Victoria, lakini vile vile tunacho kituo cha TAFIRI pale Kigoma. Kwa hivyo hatua za mwanzo za utafiti huu kwa kushirikiana na nchi zinazozunguka Ziwa hili Tanganyika kupitia taasisi inayotuunganisha tutafanya utafiti pia wa kujiridhisha ya stock assessment na hatua za kuweza kuwaruhusu wawekezaji wakubwa, wakati na wadogo ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la ni juu ya leseni nyingi zilizopo. Uwepo wa leseni katika tasnia ya uvuvi
ni jambo la matakwa la kisheria lakini vilevile ya kitaalam. Kwa sababu inatusaidia hata kujua idadi ya wavuvi tulionao.

Naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge juu ya tozo tunazozitoza kuonekana kuwa ni nyingi na kubwa na kutufanya tusiwe na ushindaji sahihi na wenzetu. Jambo hili ndani ya mamlaka yetu, tupo tayari kukaa na wadau kuweza kushaurina ili kuweza kufanya tasnia ya uvuvi iweze kuwa na manufaa kwa Taifa letu.
MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Segerea utakuta idadi ya mahabusu ni wengi zaidi kuliko watu ambao wameshahukumiwa na hii inatokana na sheria kandamizi ambazo zinanyima watu dhamana kama zilivyonyima dhamana Wabunge wetu wawili; Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Matiko na Sheria ya Anti Money Laundering ambayo makosa yanawekwa tu ili kuweza kuwaweka ndani watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba imefikia wakati kwa watu ambao umri wao ni kuanzia miaka 75 na kuendelea kama ilivyokuwa kwa Mheshimiwa William Shelukindo ambaye aliwekwa kwenye Gereza la Maweni kwa kukosa dhamana tu, kuweka utaratibu watu hawa wawe wanafungwa kifungo cha nyumbani kwao badala ya kuwajaza magerezani bila sababu kutokana na umri wao kama ambavyo nchi nchi nyingine wanafanya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto amezungumza vitu viwili kwa pamoja suala la mahabusu na wafungwa. Suala la wafungwa siku zote nimekuwa nikieleza mikakati ya Serikali ya jinsi ya kupunguza msongamano kwenye magereza kupitia njia mbalimbali. Tumeona Mheshimiwa Rais akitoa msamaha kwa wafungwa, tuna sheria za parole, sheria za huduma za jamii na nyinginezo. Pia tunafanya jitihada ya kujenga magereza ili kupunguza ule msongamano. Kwa hiyo, kimsingi kwa wafungwa huo ndiyo mkakati wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mahabusu ni suala la kisheria zaidi, kumchukua mahabusu na kumpa kifungo cha nje anakuwa bado hajahukumiwa. Kwa hiyo, cha msingi ni kufuata sheria za dhamana ili aweze kupata dhamana wakati huo huo sisi tukifanya jitihada za kuboresha mahabusu zetu ili kuepusha msongamano na madhara yanayoweza kujitokeza.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa halmashauri ambazo zinalima korosho maamuzi yanayohusiana na ununuzi wa korosho ndiyo yaliyopelekea wao kupoteza mapato. Kuna halmashauri ambazo makusanyo yake sasa hivi ni 6% tu kwa sababu fedha zake zote walikuwa wanategemea korosho, Serikali haioni ni busara kufanya compensation ya fedha hizi ili halmashauri hizi ziweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida ikiwemo kuwalipa Madiwani?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nadhani jambo hili kila halmashauri inapanga mipango yao na kilichofanyika na Serikali ni kwamba ilikuwa ni lazima tuchukue hatua kuwawezesha watu wetu waweze kuuza korosho zao, lakini halmashauri zenyewe maelekezo ya Serikali ni kwamba kwa kuwa hiki kilikuwa ni kipindi cha mpito tunaamini kwamba msimu ujao watajipanga vizuri waweze kukusanya kwa kuzingatia Sheria na miongozo yao. Kwa sasa suala la compensation halitakuwepo kwa sababu hiyo bajeti hatuna, ahsante.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako Tukufu kila mwaka linatenga jumla ya shilingi elfu 10 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi. Katika fedha hizo shilingi elfu sita zinapaswa kwenda moja kwa moja kwenye mashule na shilingi elfu nne zinakwenda TAMISEMI kwa ajili ya ununuzi wa vitabu, lakini Serikali inafahamu kwamba katika mpango wa GEP, Serikali ilipata zaidi ya shilingi bilioni 45 kwa ajili ya kununua vitabu, na kwa jumla ya idadi ya wanafunzi waliopo nchini wa shule za msingi, kuna zaidi ya shilingi bilioni 144 zilipaswa zinunue vitabu na shule hazina vitabu na kuna vitabu ambavyo viliondolewa, Serikali….

NAIBU SPIKA: Uliza swali.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni kwamba, ni muafaka sasa kufanya ukaguzi maalum ili kuweza kutambua jumla ya fedha hizi shilingi bilioni 190 zimetumika namna gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika uchunguzi uliofanywa kwenye jumla ya halmashauri za wilaya 12 hapa nchini, katika shilingi elfu sita inayopaswa kwenda kwenye mashule kwa kila mtoto, fedha inayofika, kwenye hii sample ya wilaya 12 ni shilingi elfu 4200 tu. Serikali haioni haja ya kufanya ukaguzi maalum ili kuweza kufahamu hii shilingi 1200 ambayo haifiki kwenye shule inakwenda wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza si kweli kwamba TAMISEMI tunanunua vitabu, tumegawana kazi, suala la vitabu na kiwango chake na ubora wake linafanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa kuwa ameuliza swali la kitakwimu na Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu yupo hapa, basi unaweza ona namna ya kutenda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la kujibu hapa ni kwamba, Mheshimiwa Zitto, anasema halmashauri zimekaguliwa, sisi kama Serikali hatuna taarifa ambayo anaizungumzia hapa Mheshimiwa Zitto, kwamba fedha
hazifiki katika shule zetu, na Mheshimiwa Zitto Kabwe, bahati nzuri kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ya LAAC, Halmashauri ya Kigoma Ujiji ambayo ni Halmashauri ya chama chake cha ACT, ndiyo halmashauri ambayo imekuwa na hati chafu miaka minne mfululizo, lakini vilevile miradi ya elimu iliyopo pale, ina hali mbaya kweli kweli. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna halmashauri imekaguliwa tuna takwimu za kutosha ni halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge. Jibu ni kwamba, hakuna taarifa ambazo anazitoa, siyo za kweli, hakuna ukaguzi uliofanyika mahususi na hakuna malalamiko ambayo yameletwa kwamba Serikali tufanye ukaguzi maalum, tukipata taarifa hizo na maombi hayo, Serikali itachukua hatua kufanya ukaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi wa fedha ya elimu na miradi ya Serikali inafanyika kila wakati, kuna Kamati za Bunge, imeenda TAMISEMI, imeenda watu wa Ustawi wa Jamii wamekagua na taarifa zipo. Kila wakati tunachukua hatua kabla ya bajeti na baada ya bajeti hii ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zitto kasema kwamba fedha za Global Partners for Education dola milioni 46 zinatumika kwa ajili ya vitabu. Naomba nimfahamishe kwamba, fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu kwa ujumla na siyo specific kwa ajili ya vitabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba nimhakikishie kwamba, fedha zote ambazo zinakwenda kwenye vitabu, zimeenda kwenye Taasisi yetu ya Elimu na kwa sasa tumefikia sehemu ambayo karibia vitabu vyote vinapatikana. Kuna vitabu ambavyo tunaendelea kuvichapisha lakini kwa sehemu kubwa vitabu vinapatikana sasa isipokuwa kama kuna changamoto kwenye halmashauri moja moja, inakuwa ni kesi ambayo ni specific lakini kwa ujumla kwa sasa tumeshaondokana na shida ya vitabu, tulichapisha vitabu vipya na tena vitabu ambavyo havina makosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi, ninaweza nikakutana na Mheshimiwa Zitto nimueleweshe zaidi kwa sababu takwimu yeye ndiyo kaja nazo ambazo ziyo takwimu za Serikali, kwa hiyo, akitaka ufahamu zaidi anaweza akakutana na mimi nikamfahamisha.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya juhudi kadhaa ambazo zimefanywa lakini bado unyanyasaji wa watu Maafisa Uhamiaji kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, na hasa Manispaa ya Kigoma Ujiji kwenye masuala ya Uraia bado ni mkubwa, sasa Serikali haioni kwamba inge-priortise watu kupewa vitambulisho vya Uraia kwa haraka, ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaondoa hili tatizo la watu kila wakati kukisiwa kwamba sio raia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie Mheshimiwa Zitto, kwamba, malalamiko ambayo yeye pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma ambayo walikuwa wanayatoa kipindi cha nyuma kuhusiana na unyanyasaji wa wananchi tuliyafanyia kazi na kipindi ambacho tulikwenda kwenye ziara nikiwa nimeambatana na Mheshimiwa Waziri Mkuu na yeye alikuwepo nadhani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulilithibisha hilo kwamba sasa hali siyo kama ilivyokuwa, hata hivyo nimpongeze kwa rai yake na nimuhakikishie kwamba rai ambayo amezungumza ndio rai ya Serikali na ndiyo maana katika Bajeti yetu iliyopita tulieleza kwa mapana kuhusu malengo ya Serikali ya kuhakikisha kwamba tunafikia yale malengo tuliyoyapanga ili wananchi waweze kupata Vitambulisho hivi na hatimaye iweze kurahisisha mambo mbalimbali ikiwemo hayo ambayo yamezungumzwa, lakini na mambo mengine mengi ambayo yanatokana na faida za kuwa na kitambulisho hiki cha uraia.