Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima (20 total)

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nitake tu kumhakikishia kuwa eneo hilo la ekari 10,760 na hizo ekari 5,760 ambazo yeye amezitolea majibu kwamba zinatumika kwa ajili ya mifugo na kilimo, nimhakikishie tu kwamba eneo kubwa halijaendelezwa kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zadi ya ekari 4,500 hazijaendelezwa kwenye kitu chochote. Gereza hawajalima wala hawana mifugo. Wananchi wa vijiji vitatu, kijiji cha Kabeba, Ilagala na Sambala hawana maeneo ya kulima na historia inaonesha walichukua zaidi ya ekari 4,000 bila makubaliano na vijiji hivi vitatu.
Swali langu je, ni kwanini Mheshimiwa Waziri asielekeze gereza litoe angalau ekari 1,500 ili na hawa wananchi wa Jijiji vitatu wapate maeneo ya kulima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kumekuwa na tabia ya baadhi ya Maafisa Magereza kuwakamata wananchi wa vijiji hivi vitatu kuwapiga, kuwanyang‟anya zana zao za kilimo, lakini pia kuwafungulia kesi na kuwapeleka mahakamani. Je, Mheshimiwa Waziri, kama Serikali anatoa tamko gani kwa wananchi wa vijiji hivyo vitatu ambao wamekuwa harassed na Maafisa wa Gereza la Ilagala? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Hasna Mwilima kwa jinsi anavyofuatilia mambo ambayo wananchi wake wamemtuma na kwa kweli yeye ni Mbunge makini, hata juzi nilipita kule wakasema hata uchaguzi ungefanyika leo, angeshinda kwa kiwango kikubwa kuliko kilichopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwenye suala hili alilolisemea, ni kweli kuna ekari ambazo hazijaendelezwa, lakini kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, zile zilizoachwa ni zile ambazo zimewekwa kwa sababu ziko kwenye chanzo cha maji ambayo yanatumika siyo tu kwa gereza, yanatumika hata kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu wa malengo mapana ya taasisi zetu hizi za magereza ni hasara kuwa na wafungwa wanaolishwa kwa kodi za walipakodi halafu wakawa hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo, hicho tunachosema hata eneo lile lililopo halijatosheleza tunamaanisha malengo marefu ya kuweza kuwatumia wafungwa wanaoweza kufanya kazi ikiwa ni sehemu ya kuwarekebisha ili magereza yetu yaweze kujiendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu tamko la Serikali kwa wale wananchi ambao wananyang‟anywa vifaa; moja niseme Serikali ya Wilaya ambako ndiko na Jimbo lilipo ni vizuri wakapanga matumizi bora ya ardhi na wanaweza hata wakawasiliana na Wizara ya Ardhi ili kuwatafutia wananchi maeneo mbadala ya kufanya kazi hizo ili wasiingie bila ruhusa katika maeneo ya Magereza na hivyo kusababisha mgongano huu ambao unasababisha wao kukamatwa. Lakini maeneo yote ambayo yana Magereza, tunaendelea kuhimiza mahusiano bora kati ya Taasisi hizo za Serikali pamoja na wananchi wanaozunguka maeneo husika.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tarehe 16 Desemba 2016, wadau wote wa zao la tumbaku walikuwa na mkutano Morogoro na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Dkt. Tizeba. Katika mkutano huo vyama vililalamika kuhusiana na kuwa na madeni ya muda mrefu yanayowasababishia kukosa mikopo ya pembejeo kwenye mabenki. Mheshimiwa Waziri alitoa tamko kwenye mkutano huo hapo Morogoro kwamba mabenki sasa wachukue yale madeni ya muda mrefu badala ya kuvibebesha mizigo vyama vya msingi yapelekwe moja kwa moja kwa mwanachama au mkulima mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kwa msimu huu, mabenki hayajatekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri kutaka madeni yale yaelekezwe kwa mtu mmoja mmoja badala ya vyama. Je, nini kauli ya Serikali kwa wakulima wa vyama vya msingi kwenye zao hili la tumbaku waliokosa mkopo wa pembejeo kwenye msimu huu wa 2016? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kilimo cha tumbaku kinahitaji utunzaji wa mazingira na kwa mujibu wa kanuni ya zao hili kila mkulima anatakiwa kwenye hekta moja anayopanda tumbaku apande miti 150 na miti 200 apande kwenye mashamba yanayomilikiwa na vyama vya msingi. Kwenye Halmashauri yetu ya Uvinza vyama vya msingi tulivyonavyo vinahitaji jumla ya hekta 240 sawa na hekari 600. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvisaidia vyama vya msingi vya zao la tumbaku kupata maeneo ya kupanda miti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyoeleza kwamba mwaka jana Mheshimiwa Waziri alitoa kauli ya kuelekeza namna bora ya kulipa madeni ya muda mrefu yanayovikabili vyama vya msingi na alielekeza kwamba ufanyike utaratibu ili madeni yale yaweze vilevile kulipwa na wale wanaodaiwa moja kwa moja badala ya kuleta mzigo kwenye chama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado huu ndiyo msimamo wa Serikali. Serikali itaendelea kufuatilia kwamba kwa nini hili halijatokea kama ilivyotakiwa kwa sababu tunaamini kuendelea kuvibebesha vyama vya msingi mzigo ndiyo chanzo cha vyama hivyo kuporomoka na hatimaye zao la tumbaku kuanguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utunzaji wa mazingira, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ana uelewa mzuri sana kuhusu namna zao la tumbaku linavyotakiwa kuendeshwa kwamba ili uweze kuzalisha tumbaku ambayo ina vigezo vya kimataifa lazima iwe environmentally compliant (ikidhi vigezo vya mazingira) na ndiyo maana kuna hitaji la kupanda miti. Nitaongea na Mheshimiwa Mbunge ili niangalie namna ya kuongea na Halmashauri za Mkoa wake kuhusu namna ya kupata ardhi kwa ajili ya kupanda miti hiyo ambayo inatakiwa kwa ajili ya zao la tumbaku.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nina masikitiko makubwa sana, itabidi Naibu Waziri anipe uhakika wa hao wafanyakazi 389 walilipwa lini na wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapoongea hivi nina ushahidi, suala hili hata Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali analifahamu. Lilifanyiwa uhakiki, watu walitumwa kutoka Hazina wakaja Uvinza wakafanya uhakiki, wakaona kweli wafanyakazi hawa wana haki hawakulipwa mshahara wao wa mwisho na hawakulipwa nauli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumefanyiwa uhakiki Mwanasheria Mkuu wa Serikali analifahamu bahati mbaya leo hayupo hapa, lakini analifahamu, alihakikisha na akatoa ushauri kwamba hawa wafanyakazi walipwe, wanadai zaidi ya shilingi milioni 320.9; je, Waziri yupo tayari kuniletea ushahidi kwamba walilipwa lini na nani, kwa sababu ninavyofahamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayo haya madai juu ya meza yake?
Swali langu la pili, Kiwanda cha Chumvi hivi tunavyoongea wamiliki wameuza kila kitu, wameuza vifaa vyote, wameuza vyuma, wameuza magari, wameuza matofali, kila kitu. Tunajua kabisa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha viwanda, vilivyopo na kufufua vingine na kuhamasisha vingine ili viweze kujengwa. Swali langu ni kwa nini, kama dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendeleza viwanda, leo tunaachia kiwanda kama kile cha chumvi ambacho wananchi wa Uvinza akina mama.....
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu kwa nini wanaachia wamiliki wanaoendesha kiwanda hiki kufunga kiwanda kinyume na utaratibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu kuleta orodha, jambo ambalo linaweza kufanyika hapa ambalo ni rahisi la kuweza kuwasaidia wafanyakazi wetu, katika majibu yangu ya msingi nilisema kama wako wale ambao wanahisi kwamba madai yao hayakulipwa ipasavyo na bado wana malalamiko, mimi na Mheshimiwa Mbunge tunaweza kuchukua hizi taarifa zote mbili tukazioanisha ili tupate muafaka wa kuweza kuwasaidia wafanyakazi hawa wa Kiwanda cha Chumvi.
Kwa hiyo, nimuondoe hofu tu Dada yangu Mheshimiwa Mwilima kwamba nalichukua jambo lako kwa uzito mkubwa sana, na kwa namna alivyozungumza kwa masikitiko makubwa, na mimi niungane nae kwamba tutakwenda pamoja wote kuangalia arodha hii ili kama bado kuna mapungufu tutafanya kazi ya kushughulikia pamoja na taasisi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusu kufunga viwanda na wakati tunasema nchi yetu ni ya uchumi na viwanda. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hata hili nalo pia linahitaji kuweza kufahamu hasa changamoto ambazo zimepelekea jambo hili kutokea, lakini nimuahidi tu kwamba chini ya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tunashughulikia masuala ya kazi na ajira na mategemeo yetu na matazamio yetu makubwa ni kuona kwamba viwanda vingi vinakuwepo, uwepo wa viwanda ndipo ajira zinatengenezwa.
Mheshimiwa Mbunge hata katika taarifa ya ILO ya mwaka 2014 ya The Global Employment Trend inasema ya kwamba ili kuendelea kuongeza nafasi za ajira hasa kwa vijana ni vema tuwe na viwanda vingi zaidi. Ninakachokisema hapa ni kwamba, nakwenda kufuatilia kufahamu changamoto na tatizo ambalo limepelekea kiwanda hiki kufungwa ili tuweze kupata suluhisho la kudumu, vijana wa Kigoma waweze kupata ajira.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naomba pia niulize swali; kwa kuwa Jimbo la Kigoma Kusini kwenye Ukanda wa Ziwa Tanganyika tunatumia meli ya Liemba, lakini kwa bahati mbaya gati karibu tano kwa muda mrefu sasa hazijajengwa na wala hazijakamilika.
Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri; je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwapunguzia adha wananchi wanaotumia meli ya Liemba kwa kujenga Gati ya Kirando, Mgambo, Sibwesa na Gati ya Kalia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi gati anazoziongelea katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ni gati muhimu sana kwa sababu tuna vilevile tatizo la barabara. Kwa hiyo, usafiri wa ile meli ni muhimu sana kabla hatujafungua usafiri wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishawaagiza Tanzania Ports Authority kwamba katika mwaka huu wa fedha lazima ahadi ambazo viongozi wetu walizitoa kuanzia Serikali ya Awamu Nne na hii Serikali ya Awamu ya Tano, ni lazima tulitekeleze katika eneo hili kwa sababu mateso yaliyoko katika eneo hilo kwa kweli ni makubwa.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia mwaka huu wa fedha na katika miaka hii mitano ikikamilika ahadi zile tutakuwa tumezikamilisha, ikiwa ni pamoja na kuimarisha gati ya Kirado, Simbwesa na hizo zingine ambazo Mheshimiwa Mbungu amezitaja.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Posho ya Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kwenye Halmashauri zingine hawalipwi kabisa. Sasa nataka niulize tu swali kwa nini Wizara ya TAMISEMI isitoe Waraka Maalum kwenda chini kwa Wakurugenzi wote kuwaelekeza kwamba katika own source za Halmashauri wawe wanatoa kiasi fulani kwa ajili ya Wenyeviti wa Vijiji huku tukijua hao ndiyo wanaotusaidia kufanya kazi kubwa za maendeleo kwa niaba ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) : Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, huo Waraka ambao Mheshimiwa Mbunge anaupendekeza ulitolewa mwaka 2003, lakini kwa sababu umekuwa ni wa muda mrefu pengine labda baadhi ya wenzetu wanaanza kuusahau, basi tutachukua ushauri wake ili tutoe maelekezo tena.
Mheshimiwa Spika, msisitizo ni kwamba lazima Halmashauri zote zifanye mapitio ya vyanzo vyao vya mapato, waongeze mbinu za ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kusudi wawe na uwezo mzuri wa kuweza kulipa. Hii ni kwa sababu hata taarifa za CAG zinaonesha kwamba ile asilimia 20 katika baadhi ya Halmashauri imekuwa hairudi kule kwenye vijiji kwa sababu tu ya malalamiko kwamba wamekusanya kidogo sana. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Kwa kuwa Bandari Ndogo za Kirando, Lukoma, Mgambo na Sibwesa hazijakamilika na kwa vile wafanyabiashara wa Jimbo langu la Kigoma Kusini kwenye kata zinazopakana na nchi za DRC, Burundi na Zambia hufanya biashara zao na kupitishia mizigo kwenye Bandari hii ya Kigoma. Swali langu; kwa kuwa wafanyabiashara hawa hutumia magari makubwa na wanapitia kwenye kivuko cha Ilagala na kivuko hiki hakina uwezo wa kubeba magari makubwa, je, kwa nini sasa tenda ya kutangazwa ujenzi wa Daraja la Ilagala haijatangazwa mpaka leo ilhali tumepitisha pesa kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) inayo mpango wa kujenga Bandari ndogo katika eneo la Kilando na Sibwesa. Mpaka sasa hivi Bandari ya Sibwesa imeshakamilika kwa asilimia 93, tunasubiri tu taratibu mbalimbali za kikandarasi na za kiufundi kwa ajili ya kwenda kuifungua hiyo Bandari ya Sibwesa ianze kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Kilando utaratibu wa kumpata mkandarasi unaendelea, tayari watu wameshafanya design; tunasubiri tu taratibu zikikamilika tutangaza tenda kwa ajili ya kumpata mtu wa kufanya ukarabati na ujenzi wa Bandari hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa Daraja la Ilagala nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari taratibu za mwanzo zimeshaanza za upembuzi yakinifu. Baada ya hapo tutafanya usanifu wa kina ili kupata gharama tutangaze tenda kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Jimbo la Kigoma Kusini tunapakana na nchi ya Congo kwenye vijiji 27 na niliona juzi/hivi karibuni wakati Mheshimiwa Waziri anatoa tamko la kupata ugonjwa huu, ukawa unaweza kuingia nchini, tuliona Kigoma kuna mtu mmoja tu ambaye alioneshwa kwenye tv kwamba yupo peke yake na kifaa anachotumia ni kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangaliza kwa mazingira ya Mkoa wa Kigoma, Jimbo hili la Kigoma Kusini ndilo ambalo lina vijiji vingi vinavyopakana na nchi ya Congo kwa maana ya ukanda wote wa Kalemi. Hadi leo nilikuwa nawasiliana na DMO, hakuna kituo hata kimoja ambacho kimewekewa mashine ya kuwapima Wakongo wanaotumia maboti kuingia nchini kwetu.
Je, Wizara imejipangaje kuisaidia Halmashauri ya Uvinza, wananchi wake wasiathirike na huu na ilhali wameingiliana kwa kiwango kikubwa sana na nchi ya Congo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kusisitiza kwamba sisi kama Serikali tumeendelea kujipanga, siyo tu katika sekta za afya, tunashirikiana na mamlaka nyingine za Kamati za Ulinzi na Usalama na zimepewa elimu hii kuhakikisha kwamba katika maeneo ambayo tuna mipaka, tunaweka ufuatiliaji wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, timu yetu ya Wizara kupitia Mganga Mkuu wa Serikali, hivi tu juzi ametoka tena Kigoma kwenda kukaa na kufuatilia kuhakikisha haya tunayoyasema wakiwa pamoja na Shirika la Afya Duniani kwenda kuangalia jitihada na juhudi ambazo tunaendelea kuvifanya. Niseme tu kwamba mipaka yetu iko salama, tutaendelea kuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja yake nyingine ambayo ameisema Mheshimiwa Mbunge, kuhusiana na kuweka huduma za ufuatiliaji wa wagonjwa katika Vituo vyetu na Zahanati, hatuwezi tukaweka katika maeneo yale. Ugonjwa huu ndugu zangu ni hatari sana. Sio kila mtu anayeruhusiwa kumgusa wala kumtibu mgonjwa huyo. Pale anapobainika, watoa huduma wetu wamepewa maelekezo jinsi gani ya kum-handle na kum-isolate yule mgonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ambazo zina uwezo zaidi ambazo ni zile Isolation Centers zetu na maabara zile ambazo tumezitenga, ndiyo ziweze kuchukua majukumu ya kumtibu yule mgonjwa. Sio kila mtu ana uwezo wa kuwatibu wagonjwa hao. Kwa hiyo, nilitaka nimhakikishie tu kwamba mipaka yetu iko salama, na sisi kama Serikali, tumejipanga vizuri.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini tumekuwa na tatizo kubwa la wakandarasi hawa, kwa mfano, Mradi wa Nguruka Mheshimiwa Rais alifanya ziara tarehe 23 Julai, 2017 akatoa tamko hadi Desemba. 2017 Mradi wa Nguruka uwe umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa zinaletwa na Serikali wakandarasi hawa hawakamilishi miradi hii na mradi wa Nguruka wananchi wanaona pesa zinaingia lakini hawapati maji. Mradi wa Uvinza pesa zinaletwa lakini wakandarasi hawakamilishi ili wananchi wapate maji. Mradi wa Kandaga Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi tarehe 17 Julai, 2018 tulifanya ziara pale ukampa mkandarasi wiki mbili lakini hadi leo hii hakuna maji yanayotoka pale. Swali langu la kwanza, je, Serikali ina kauli gani kwa hawa wakandarasi ambao wanalipwa pesa lakini hawakamilishi miradi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tarehe 29 Julai, 2018, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye Kijiji cha Mwakizega na wananchi wakamlilia kwamba tunahitaji maji na tamko tukaambiwa tuandae taarifa ya mradi wa maji ili tuweze kuwasilisha Wizarani. Hivi navyoongea Injinia wa Maji Halmashauri ya Uvinza yuko hapa Dodoma ameshawasilisha andiko hilo la mradi ambalo linagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.9. Je, ni lini sasa Wizara itatuletea pesa ili tuanze kutekeleza huu mradi mpya wa Mwakizega? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kwamba Serikali inachukua hatua gani kwa wakandarasi ambao wanashindwa kukamilisha kazi kwa wakati. Kuna taratibu mbalimbali Serikali inachukua kama mkandarasi anashindwa kukamilisha kazi kwa wakati. Hatua ya kwanza, kama mkandarasi anachelewesha kazi tunampiga faini kutokana na ucheleweshaji na kila siku mkandarasi huyo analipa faini inategemeana na mradi wenyewe na kiasi cha gharama za mradi. Hatua ya pili ambayo kama mkandarasi atashindwa kutelekeza kazi kwa wakati tunaweza kumfutia usajili na mwisho wake hatoweza kufanya kazi yoyote ya ukandarasi kwenye sekta zote za ujenzi pamoja maji na sekta zote hapa nchini. Tutawasimamia wakandarasi wote tuhakikishe kwamba wanafanya kazi kwa wakati na wanazimaliza kwa wakati ili Watanzania ambao wamesubiri maji kwa muda mrefu waweze kupata maji na salama kwa muda unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kuhusu andiko, andiko tumelipokea na kama kawaida andiko lolote lazima lipitie michakato mbalimbali. Mara litakapokamilika tutaweza kutoa fedha ili mradi huo uweze kutekelezwa. (Makofi)
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye swali langu la (a) amejibu kitu tofauti kabisa na swali ambavyo nilivyoliuliza. Pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; hivi karibuni tumemwona Mheshimiwa Rais wetu akitoa maelekezo kwenye Wizara hii ya Maliasili kugawa baadhi ya maeneo ya Hifadhi kwa ajili ya wakulima na wafugaji, kwa mfano Kagera Nkanda, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa wananchi wa Kagera Nkanda, Wilaya ya Kasulu wapewe eneo ndani ya hifadhi kwa ajili ya kulima na kufuga. Kwa nini sasa Mheshimiwa Waziri asitoe maelekezo yale yale yaliyotumika kuwagawia wananchi wa Kagera Nkanda awagawie sasa na wananchi wanaouzunguka maeneo ya Pakunda, Pachambi na maeneo ya Ipuguru?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa tunafahamu kwamba utaratibu wa uwekaji wa vigingi unatakiwa ufuate sheria. Kijiji cha Kalilani na Kijiji cha Sigwesa kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria. Je, Mheshimiwa Waziri akija akigundua kwamba GN hivi vigingi vilivyowekwa kwenye Kijiji cha Kalilani na Kijiji cha Sigwesa hakikufuata taratibu atakuwa yuko tayari kuondosha vile vigingi na kuviweka nyuma ili kupunguza migogoro iliyopo baina ya Vijiji vya Sigwesa na kijiji cha Kalilani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza kwa jinsi ambavyo ameeleza, inawezekana kweli labda maeneo mengine majibu tuliyoyatoa hayajafikia, hayajawa katika kile kiwango alichokusudia, nimuahidi tu kwamba mimi nitapata nafasi ya kwenda kutembelea katika eneo hilo, ili niende kutembelea kijiji hadi kijiji na kitongoji hadi kitongoji kusudi tuweze kubaini kama kweli kuna upungufu wa namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwagawia maeneo ya hifadhi naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza utaratibu wa kugawa hifadhi kwa sasa jinsi ulivyo, kwa kweli kuna kazi kubwa sana. Hata hivyo, kama pale ikionekana kweli wananchi wa Jimbo husika wana matatizo ya ardhi na hawana mahali pa kulima, hawana mahali pa kufugia mifugo yao na mambo mengine, basi namuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri aangalie, afanye mchakato na awasiliane na Wizara ya Maliasili na Utalii ili tuangalie katika yale maeneo ambayo yanahifadhiwa chini ya Serikali za Vijiji, kama yanaweza yakamegwa na wananchi wakaweza kupatiwa hilo eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusu kuondoa vigingi pale ambapo itaonekana kuna makosa. Tuko tayari kabisa pale ambapo itaonekana vigingi vimewekwa katika maeneo ambayo siyo sahihi, tuko tayari kabisa kwamba tutaviondoa na tutaviweka katika maeneo ambayo yanastahili pale ambapo mipaka kisheria inatakiwa kuwekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna matatizo hayo Nchi nzima, na ndiyo maana tuliahidi mbele ya Bunge hili tutakwenda kila eneo kuhakikisha kwamba vigingi vinawekwa katika maeneo yale yanayotakiwa. (Makofi)
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Kigamboni shida waliyokuwa wanaipata kabla ya kujengwa daraja lile la Nyerere ilikuwa ni kubwa sana. Pia wananchi wangu wa Kata ya Ilagala na kata zingine za Ukanda wa Lake Tanganyika wanapata shida kubwa sana kwa Kivuko kilichopo pale, kila siku ajali za magari yanaingia kwenye Mto Malagarasi. Je, kwa nini Serikali sasa isiwajengee Daraja la Ilagala na wanajua kabisa waliahidi kujenga daraja hili tangu 2008?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali inaendelea kuboresha mawasiliano ya usafiri katika maeneo ya Mheshimiwa Mbunge ambayo anatoka na natambua kwamba uko usanifu wa kuunganisha barabara kupita kwenye daraja ambalo analizungumza kwa hiyo Mheshimiwa Mwilima nafikiri baadaye tunaweza tukazungumza ili aone mpango mahususi tuliokuwa nao kuhakikisha daraja hili linaweza kutengenezwa ili tuweze kuunganisha maeneo haya na maeneo mengine ya Kanyani kule tukiwa tuaelekea kule Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tulizungumze ili aone namna tulivyojipanga kwa ajili ya kutoa hii adha na najua na suala la kivuko kulikuwa na shida pia ya kuvuka usiku katika eneo hili, yote haya tunayashughulikia ili wananchi hawa wasipate adha ambayo ilikuwepo katika eneo hili.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni timu ikiongozwa na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma walienda Tarafa ya Nguruka kukagua vijiji vyote vitakavyopatiwa umeme REA III lakini hadi leo hii tunavyoongea, mkandarasi alikuwa afike tarehe 2 Juni, 2018 hajakanyaga kwenye vijiji hivyo ambavyo vinatakiwa vipate umeme kwenye Tarafa yangu ya Nguruka. Je, ni lini sasa mkandarasi atafika na kuanza kazi kuingiza umeme kwenye vijiji vyangu vya Tarafa ya Nguruka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namjibu Mheshimiwa Nsanzugwanko nimesema, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia maeneo hayo. Jumatano ijayo mkandarasi kwa Mkoa wa Kigoma tunamkabidhi site nasi tutafuatilia utekelezaji wake. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Uvinza, eneo la Nguruka litakuwemo kwenye mpango huu pamoja na eneo la Ilagala na maeneo mengine. Kwa hiyo, Jumatano ijayo Mheshimiwa Mbunge wa Uvinza mkandarasi pia atafika na maeneo yake yataanza kupelekewa umeme kwa wakati mmoja.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wagonjwa wa figo wako pia kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini. Kwa vile wanapokuwa na matatizo hayo wanatakiwa waende hospitali ya wilaya ili waweze kupata referral ya kwenda Hospitali ya Muhimbili. Je, ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Jimbo la Kigoma Kusini ili wagonjwa wangu wa vijijini wenye ugonjwa wa figo waweze kupata eneo la kutibiwa na kupata referral ya kwenda Muhimbili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunaendelea kuboresha mifumo yetu ya rufaa na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na za magonjwa haya ya figo. Sasa hivi huduma hizi kwa kiasi kikubwa sana tumeweza kuzisambaza sehemu mbalimbali za nchi, tunazijengea uwezo hospitali zetu za rufaa za mikoa vilevile tunazijengea uwezo hospitali zetu za wilaya kuweza kutambua dalili za awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, magonjwa haya ya figo yanasababishwa sana na magonjwa makubwa mawili ya kisukari na shinikizo la damu ambayo kama hatutaweza kuyadhibiti vizuri na kupata matibabu yaliyo sahihi yanapelekea mtu kupata ugonjwa wa figo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba swali la msingi la Mheshimiwa Hasna Mwilima alikuwa anaulizia ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya katika Jimbo lake la Kigoma Kusini ili wananchi wake waweze kupata huduma hii. Katika bajeti hii ya mwaka huu Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za wilaya. Naamini hospitali ya wilaya hii itakuwa ni moja kati ya hospitali hizo zitakazojengwa.
MHE. HASNA MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Kwenye Vijiji vyangu vya Mwakizega, Kabeba na Lilagala tangu Awamu ya II ya REA nguzo zimeshawekwa na taratibu zote zimekamilika. Mradi ule ulitakiwa uzinduliwe mwezi wa pili mwaka jana 2017 lakini kwa masikitiko yangu makubwa Mheshimiwa Waziri umeshakuja Kigoma umepita umeenda Kibondo, wananchi wanauliza maswali, tumewekewa nguzo na transfoma tuizone? Ni lini umeme wa Kata hizi mbili za Mwakizega na Ilagala utawashwa rasmi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mwilima kweli nilitembea naye katika maeneo yake. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge huyu kwa sababu kwanza tulienda eneo la Nguruka lililokuwa na shida kubwa tukawasha umeme Nguruka tukiwa pamoja, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo ambayo ameyataja eneo la Ilagala pamoja na Nguruka huyu mkandarasi wa REA Awamu ya Tatu anyekuja kufanya kazi ni kati ya maeneo ambayo ataanzia kuyafanyia kazi na kuyawashia umeme. Kwa hiyo, nimpe tu pongezi Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira wakati…
...mkandarasi tunampata katika mwezi huu kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza, tarehe 5 Mei ataanza kazi katika maeneo hayo na maeneo yatakayowashwa ni pamoja na Ilagala pamoja na Nguruka maeneo yaliyobaki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira tutafanya kazi pamoja.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Natambua kwamba Jimbo la Kigoma Kusini linakidhi vigezo vyote vya kugawanywa na kuwa majimbo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu kwa mfano, Mkoa wa Katavi una kilometa za mraba 45,000 population 564,000. Jimbo hili la Kigoma Kusini lina vigezo vyote na tayari tulishafanya vikao kuanzia kwenye Vijiji, Kata, Baraza la Madiwani, DCC, vikao vikaenda mpaka kikao cha Mkoa kwa maana ya RCC na tayari tulipeleka Wizara ya TAMISEMI. Tume ya Uchaguzi mwaka 2015 waliliweka kwenye website yao kuonesha kwamba wako tayari sasa kuligawa, kama taratibu zote zilishafanyika na tulishawasilisha kwenye Wizara ya TAMISEMI, kwa nini walipotangaza majimbo mengine 2015 hawakuligawa jimbo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nguruka ilishafuata taratibu zote za kisheria na vigezo vyote inavyo kwa maana tuna kata nne na vigezo vya kisheria vinasema lazima tuwe na kata tatu. Je, kwa nini sasa Wizara ya TAMISEMI wasiamue tu rasmi kutangaza kwamba Mamlaka ya Mji wa Ngaruka sasa tayari inaweza kuanzishwa rasmi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, nina wasiwasi aliposema kwamba ana uhakika Jimbo la Kigoma Kusini limekidhi vigezo vyote, lakini nilipokuwa najibu swali la msingi nilizungumza kigezo kimojawapo ni ukubwa wa ukumbi wa Bunge. Sasa sijaelewa kama kigezo hicho nacho tayari kimefikiwa kwa kuangalia ukubwa na viti vilivyomo ndani ya Bunge kama kweli vinaweza vikakidhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimhakikishie tu kwamba kwa mawasiliano zaidi na kuwapa uhakika wananchi wa Kigoma Kusini tutapeleka barua Tume ya Taifa Uchaguzi ili kusudi watupe mrejesho mzuri zaidi wa hatua ambayo imefikiwa mpaka sasa hivi. Nina uhakika 2020 bado iko mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu Nguruka kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo, naomba sana arejee jibu langu la msingi nimesema kwamba vikao vinatakiwa vianzie kwenye Serikali ya Kijiji, Halmashauri ya Kijiji ikae ipeleke kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji upitishe, upeleke kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata iende kwenye Halmashauri, iende Mkoani ndio ije kwetu kwa ajili ya kumshauri Waziri mwenye dhamana na Waziri mwenye dhamana ni Rais. Kwa hiyo, itakapofika kwetu tutatoa ushauri, naomba sana awe na subira.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri ametuhamasisha Waheshimiwa Wabunge tuwahamasishe wananchi ili waweze kujenga shule za sekondari kwenye Kata ambazo hazina sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini tunazo shule mbili za sekondari; tunayo Shule ya Basanza na Shule ya Mwakizega, lakini kinachosikitisha ni kwamba tangu hizi shule wananchi wamejenga wameweka madarasa kumi, ofisi za walimu na sasa hivi wanakimbizana na maabara. REO Mkoa wa Kigoma na Ukaguzi hawataki kabisa kuzisajili hizi shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini TAMISEMI na Wizara ya Elimu hawakai pamoja na kuona ni jinsi gani shule ambazo mnatuhamasisha tuwaambie wananchi wajenge muwe pia mnazipa kipaumbele katika usajili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimhakikishie dada yangu, Mheshimiwa Hasna kwamba TAMISEMI na Wizara ya Elimu tunafanya kazi kwa vizuri zaidi, ndiyo maana mimi na pacha wangu, Mheshimiwa Profesa Ndalichako tunakwenda vizuri, lakini hata hivyo naomba niwahakikishie kwamba tumefanya hamasa kubwa sana watu wajenge hizi shule kwa ajili ya kupunguza umbali wa watoto kusafiri na hasa kesi ya mimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na inawezekana kuna maeneo mengine kuna case by case, naomba niichukulie kesi hii ya Mkoa wa Kigoma, Uvinza kuona kuna nini kinachoendelea. Lakini hata hivyo, naomba nitumie fursa hii kumuagiza Mkurugenzi wangu wa Elimu pale Ofisi ya Rais, TAMISEMI kufuatilia jambo hilo haraka iwezekanavyo ili mradi kwamba kama vigezo vyote vimekamilika kuweka mchakato wa haraka kuhakikisha shule hizo zinasaidiwa haraka iwezekanavyo.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa na nimesimama hapa kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara yangu ndiyo inayohusika na usajili wa shule na hakuna urasimu wowote katika kusajili shule. Kinachotakiwa ni kwamba wanapoomba usajili vigezo na masharti viwe vimekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule ambazo Mheshimiwa Mbunge, dada yangu, amezisema, bahati nzuri hizo shule nazifahamu na ukaguzi ulishafanyika. Kuna mapungufu ambayo yameonekana na hatua iliyopo sasa hivi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza ameshaji- commit kwamba ndani ya miezi mitatu, ifikapo Disemba, 2018 atakuwa amekamilisha mapugufu yaliyopo na timu yangu itarudi kukagua na kama viko vizuri usajili utatolewa kwa sababu tuko hapa kwa ajili ya kuwezesha juhudi za wananchi watoto wakasome.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, natambua kazi nzuri wanayoifanya. Ni kweli kabisa kwamba, Nguruka pale tulitoa ekari 30 kwa ajili ya ujenzi wa hiyo substation, lakini Meneja wa TANESCO alienda, hadi leo utekelezaji haujaonekana. Sambamba na hilo mwaka jana mwezi wa Nane mkandarasi alifanya survey katika Kata ya Nguruka, Kata ya Mtego wa Noti, Kata ya Itebula, Kata ya Mganza, Kata ya Sunuka, sambamba na vijiji ambavyo vilisahaulika kwenye Mradi wa REA awamu ya pili. Swali langu. Je, Wizara hii mnawaambia nini wananchi wa kata hizi, ni lini mkandarasi atapeleka materials ili sasa utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu uweze kuanza rasmi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, natambua kwamba, kuna mazungumzo baina ya mwekezaji kutoka Marekani pamoja na Wizara ya Nishati kufua umeme kwenye Mto Ruwegere uliopo kwenye Kijiji cha Mgambazi, Kata ya Igalula. Sasa wananchi wa Kata ya Buhingu, Kata ya Herembe, Kata ya Sigunga na Kata ya Igalula yenyewe wanataka kusikia Kauli ya Serikali. Ni lini sasa mkandarasi huyu ataanza rasmi kutekeleza uzalishaji wa kufua umeme kwenye Mto Ruwegere, megawati tano? Nataka majibu ya Serikali.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi wa swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge kwa vile ambavyo amelieleza. Napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya nishati kwa wananchi wa Uvinza. Baada ya kusema hayo napenda sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mbunge wa Maeneo ya Uvinza, Jimbo la Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa mkandarasi alipata kazi dakika za mwisho ukilinganisha na mikoa mingine. Hata hivyo, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge na jinsi anavyofuatilia, hivi sasa mkandarasi ameshaanza ku-order materials na ataanza kupeleka materials kwenye eneo la Uvinza kuanzia tarehe 22 mwezi huu. Maeneo yatakayopelekewa ni pamoja na Kazuramimba, Ilagala, Kajeje kuelekea Sunuka, lakini pia maeneo ya Nguruka na katika maeneo mengine ya Uvinza ambayo hayajapelekewa nishati ya umeme. Maeneo yote 27 ya kwa Mheshimiwa Mbunge yatapelekewa umeme ndani ya miezi tisa ijayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nimpe tu uhakika kwa wananchi wa Uvinza kwamba, mkandarasi amesha-mobilise material na kuanzia tarehe 22 mwezi huu ujenzi utaanza rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili, ni kweli kulikuwa na mkandarasi aliyetarajia kufanya survey kwa ajili ya kuzalisha umeme megawati nane katika Mto Rwegere, lakini taarifa za awali baada ya kupewa kazi na baada ya kufanya tathmini za awali inaonesha Mto Rwegere unaweza kutupatia megawati tano kutokana na maporomoko ya maji ya Mto Rwegere.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kazi inayofanyika mara baada ya kuleta taarifa mkandarasi amefanya mapitio na wataalam wetu, ni matumaini yetu kwamba, mwezi ujao atatuletea taarifa za mwisho, ili kuona kama mradi huo utakuwa na tija na kuzalisha megawati tano. Kwa hiyo, nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwamba, hiyo kazi inatushirikisha sana, inaendelea vizuri na tunaweza tukapata megawati tano mbali na megawati 45 za Mto Malagarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, samahani kidogo niongeze kwenye mradi muhimu sana kwa Kigoma, ujenzi wa transmission line kutoka Tabora kupita Urambo kwenda mpaka Nguruka hadi Kidahwe umeshaanza. Tunatarajia mkandarasi atakamilisha kazi Februari mwakani ili wananchi wa Kigoma waweze kupata umeme wa gridi nao kutoka umeme wa gridi unaotoka Tabora wa kilovoti 120. Nimeona nilifafanue kwa sababu, sasa hivi clearance ya major substation inafanyika Urambo na wiki inayokuja itafanyika Nguruka na Kidahwe wanamalizia mwezi ujao. Hiyo ni taarifa kwa ajili ya umeme wa wananchi wa Kigoma. Ahsante sana.
MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri na ninaishukuru pia Serikali kwa hiyo fedha ambayo imetuletea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kweli kwamba tunazo hizo High School mbili kwa maana ya Lugufu Boys na Lugufu Girls. Shule hizi kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, zimeanzishwa kwenye majengo chakavu yaliyokuwa yakitumika na wakimbizi. Hali ya hizo shule ni mbaya sana na hata hiyo shilingi milioni 150 waliyoleta, yaani inakuwa haionekani imefanya nini kutokana na mazingira halisi tuliyonayo pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata umeme na maji kwenye hizi shule, hakuna. Sasa swali langu kwa Naibu Waziri: Je, ni lini sasa Serikali itaweza kutatua changamoto ya miundombinu iliyoko Lugufu Boys na Lugufu Girls sambamba na kuwapelekea umeme na maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kweli kabisa kwamba Halmashauri inaangalia uwezekano wa kuanzisha Kidato cha Tano na cha Sita kwenye Sekondari zetu za Buhingu na Sekondari ya Sunuka. Kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameonyesha kwamba Halmashauri inatumia pesa zake za ndani. Sisi wote ni mashahidi, hali ya kipato cha Halmashauri sasa hivi ni mbaya sana. Kwa hiyo, naiomba Wizara; swali langu ni: Je, Wizara haioni sasa ni vyema ituletee fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu kwenye Shule ya Sekondari ya Sunuka na Shule ya Sekondari ya Buhingu ili tuweze kuwa na Kidato cha Tano na cha Sita?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, hawa ni miongoni mwa Wabunge jembe wanawake wa Majimbo ambao wanafanya kazi kubwa sana kuwatetea Watanzania wenzao na hasa katika suala zima la elimu na unaona anazungumza habari ya wanawake ili na wao wafikie hatua kama yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua ni namna gari Serikali imejipanga kuboresha majengo ya shule hasa ambazo amezitaja ambazo ni chakavu. Ni utaratibu wa Serikali kuboresha majengo haya na bahati nzuri kwenye Bunge hili Tukufu ambalo linaendelea tumeishapitisha bajeti ya TAMISEMI na tuna fedha mle karibu shilingi bilioni 90 ambayo itakwenda kufanyakazi EP4R. Kwa hiyo, tutagawa fedha katika maeneo yale na ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutazingatia hili katika kupeleka fedha kwenye eneo hilo kwa shughuli ambayo ameitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, amezungumza habari ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita. Siyo kwamba Serikali imejitoa kushiriki. Tunachosema ni kwamba Halmashauri lazima ianze. Kuna mambo ya msingi kwa mfano ardhi, iwe na umiliki hatuna fedha ya kulipa fidia, lakini wachangie kupitia mapato yao ya ndani, nasi kama Wizara tunaongezea pale na kuboresha pamoja na kupeleka wataalam na maabara nyingine. Kwa hiyo, tutachangia jambo hili ila walianzishe. Kipaumbele ni kwamba kila Tarafa angalau iwe na High School moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema kwamba ni muhimu tungeomba kuhimiza, pamoja na kuanzisha Shule za Kidato cha Tano na cha Sita, ukweli ni kwamba hizi shule ni za Kitaifa, zikianzishwa maana yake utapeleka watoto kutoka nchi nzima. Kwa hiyo, unaweza kubadilisha miundombinu mingine ili watoto wa eneo lile kama ni Uvinza, utaenda kuwasaidia Nguruka. Ni muhimu kuhimiza elimu ya msingi, sekondari, halafu wengine tunaenda huko mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika timu hiyo ya Mawaziri saba ambayo Mheshimiwa Rais aliunda, walipata pia fursa ya kutembelea Jimbo la Kigoma Kusini kwenye Kata ya Buhingu, Kijiji cha Kalilani. Tangu wamekuja kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kuhusiana na migogoro ya ardhi, mpaka leo wananchi hawajapata majibu kuhusu hatima ya maamuzi ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri leo hii aweze kuwaambia wananchi wa Kijiji cha Kalilani na wananchi wa Kijiji cha Sibwesa, kwa sababu wanaishi kwa mashaka hawajui watatolewa kwenye ardhi yao au wataendelea kubaki: Je, ni lini? Maamuzi ya Serikali yanasema nini kuhusiana na timu ile iliyoundwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimetoka kujibu swali la nyongeza hapa la Mheshimiwa Umbulla kwamba hii kazi ya kuondoa migogoro na kupanua baadhi ya maeneo ili wakulima wetu na wafugaji wapate maeneo na kupunguza migogoro, ni kazi ambayo Mheshimiwa Rais kwa ukarimu wake yeye mwenyewe aliamua kuunda timu ya Waheshimiwa Mawaziri na akawatuma, wamezunguka nchi nzima. Namaomba Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote, Mheshimiwa Rais ameona tatizo, amechukua hatua, mambo haya yanahitaji mambo mbalimbali ya kiutaratibu yafanyike na kila sekta ijiridhishe na kuangalia sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpe nafasi Mheshimiwa Rais nia yake njema itimie. Mgogoro huu utaisha Mheshimiwa Mbunge na wananchi wako wa Kigoma Kusini wataendelea kuwa na amani, kwa sababu Rais mwenyewe ameshika mpini na ameamua migogoro ipunguzwe. Jambo jema ni kwamba hata maeneo ambayo yalikuwa na malalamiko, ameelekeza watu wengine wasivunjiwe kuna uwezekano wa kuongeza maeneo au kupunguza maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamwamini Mheshimiwa Rais, ana nia njema. Jambo hili litafika mahali pazuri sana. Ahsante.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Halmashuri ya Uvinza ni halmashauri ambyao kijiografia na kimuundo imekaa katika mazingira magumu sana. Lakini kwenye mgao wa bajeti Halmashauri ya Uvinza imekuwa ikipata pesa dogo, na huku inashindwa kutekeleza miradi ya kimaendeleo katika halmashauri yake. Mheshimiwa Waziri ni shahidi aliona ukubwa wa jimbo na mazingira jinsi yalivyo na alituahidi kutuongezea fedha katika mgao wa bajeti.

Je, Mheshimiwa Waziri katika bajeti ya 2019/2020 umezingatia kuongeza pesa za maendeleo katika Halmashauri ya Uvinza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nami nilikuwepo Uvinza mara kadhaa na juzi juzi nilikuwanae Mheshimiwa Mbunge. Na ni kweli ukitoka makao Makuu ya uvinza mpaka unafika kule kalya karibu kilomita 300 na jimbo kweli ni kubwa, kwa hiyo, jukumu la Serikali tutafanya kila liwezekanalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana katika bajeti ya mwaka huu kuna fedha kidogo tumeiongeza Mheshimiwa Mbunge na hata katika kipaumbele tukaona hata pale mjini kidogo japo angalau tuongeze na tabaka la lami.

Kwa hiyo, kuna bajeti ya kuweka tabaka lami pale mjini lakini hata hivyo tunajua kwamba changamoto kubwa ipo katika Uvinza kwa siku za usoni tutaendelea kwa kuifanyia kazi eneo hili kwa sababu kasungura kenyewe kadogo tutajitahidi kufanya kila liwezekano lengo kubwa ni kuimarisha Uvinza iende vizuri.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini, sambasamba na majibu yake ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tunatambua kwamba bodaboda baadhi yao ni kweli huwa wanafanya makosa barabarani na wanapofanya makosa barabarani wanatozwa faini ya Sh.30,000, lakini hata magari pia wanapofanya makosa barabarani ambako ni matairi manne pia hutozwa faini ya Sh.30,000. Sasa kwa kuwa tozo hizi zinatokana na Kanuni na Mheshimiwa Waziri anayo mamlaka ya kubadilisha Kanuni wakati wowote, swali langu, kwa nini sasa Waziri asibadilishe Kanuni ili bodaboda yenye matairi mawili pamoja bajaji yenye matairi matatu waweze kupunguziwa tozo hii ya Sh.30,000 na hatimaye ishuke chini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, tunafahamu kwamba SUMATRA huwa wanatoza tozo ya Sh.22,000 kwa bodaboda, lakini Sh.25,000 kwa hiace na Sh.120,000 kwa mabasi. Ada hii imekuwa ni kubwa sana kwa watu wa bodaboda ukigawanya 25,000 kwa hiace abiria wako 15, ukigawanya hiyo unaipata kila abiria mmoja wa hiace analipa 1,666 lakini kwa bodaboda wanalipa 22,000, ukiigawanya kwa dereva na abiria inakuwa analipa 11,000 sasa swali langu, ni kama hili la kwanza, kwa nini sasa hizi Kanuni zisibadilike ili SUMATRA waweze kuwatoza angalau 10,000 kwa mwaka badala ya 22,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili muhimu ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nichukue nafasi hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu na umma kwa ujumla kwamba tupo katika hatua za mwisho katika Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani na tunatarajia mchakato huo utakapokuwa umekamilika sheria hiyo italetwa hapa Bungeni ili Waheshimiwa Wabunge tuweze kuijadili na hatimaye kuipitisha na sheria hiyo itakapokuwa imekamilika itapelekea vilevile kutoa fursa kwa Mheshimiwa Waziri kufanya mabadiliko ya Kanuni kulingana na Sheria itakavyokuwa imepitishwa na Bunge. Katika mambo ambayo tumeona kwamba ni muhimu kuyabadilisha katika Sheria ya Usalama Barabarani, moja, tumeona kwamba Sheria iliyopo sasa hivi inachangia ama inakwaza mapambano dhidi ya kupunguza ajali za barabarani nchini na moja katika jambo ambalo tuliona kwamba tutalipendekeza katika sheria hiyo ni juu yenu Waheshimiwa Wabunge kuona kama linafaa au halifai ni kuziangalia hizi tozo ambazo zinatozwa kwa hawa watu ambao wanafanya makosa ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, kama wataona kwamba tozo zilizopo sasa hivi ni ndogo na hivyo zinapaswa kuongezwa na kufanya hivyo pengine itasaidia kuwafanya waendesha vyombo hivi waogope, basi ni juu ya Waheshimiwa Wabunge na huo ndiyo mtazamo ambao nauona ni sahihi. Kwa mtazamo wangu mimi, nahisi kwamba baadhi ya waendesha vyombo vya moto wamekuwa wakifanya makosa kwa sababu wanaona wanaweza wakalipa hizi faini kwa kuwa ni kidogo na wanaweza wakalipa mara moja na wakaendelea na shughuli zao. kwa hiyo hili niseme kwamba kwa kuwa litakuja hapa Bungeni, tulipatie muda.

Mheshimiwa Spika, hili linakwenda sambasamba vilevile na swali lake la pili ambalo lilikuwa linazungumzia vilevile masuala ya tozo, ingawa hili la pili linahusiana na masuala ya SUMATRA ambayo kwa kuwa Serikali ni moja, basi nina hakika tutakaa pamoja na Wizara ya Uchukuzi ili kuona kwamba mambo haya mawili tutakwenda nayo vipi kwa pamoja.