Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Albert Ntabaliba Obama (14 total)

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y. MHE. ALBERT O. NTABALIBA) aliuliza:-
Mwaka 2011/2012 tuliweka Mkataba kati ya Halmashauri ya Buhigwe na Hospitali ya Heri Mission, Biharu Hospitali na Mulera Dispensary juu ya kutoa huduma ya matibabu kwa wazee, watoto na akinamama bure na Serikali imetoa fedha hizo na wananchi wamenufaika na huduma hizo lakini tangu Disemba, 2015 hadi sasa fedha hazitolewi tena:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali imeacha kutoa fedha ilizokuwa ikitoa?
(b) Je, ni lini sasa fedha hizo zitaanza tena kutolewa ili huduma hizo ziendelee?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Ntabaliba Obama, Mbunge wa Buhigwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe inatakiwa kuchangia 15% ya fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya katika Hospitali Teule ya Heri Mission, Kituo cha Afya Biharu na Zahanati ya Mulera. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, robo ya kwanza na ya pili hadi Disemba, 2015 tayari zimepelekwa shilingi milioni 27.5 katika Hospitali Teule ya Heri Mission, shilingi milioni 8.0 zimepelekwa katika Kituo cha Afya cha Biharu na shilingi milioni 8.0 zimepelekwa Zahanati ya Mulera. Fedha ambazo hazijapelekwa ni za robo tatu (Januari – Machi, 2016) na robo ya nne (Aprili – Juni, 2016) kutokana na kutopokelewa kwa fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya kutoka Hazina.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, fedha ambazo hazijapelekwa katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya ni za robo ya tatu na robo ya nne ambazo zitapelekwa baada ya Halmashauri kupokea fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Busket Fund) kutoka Hazina. Napenda kutoa wito kwa Halmashauri kuimarisha usimamizi kwa kushirikiana na wamiliki binafsi wa hospitali ili makundi yanayotakiwa kutibiwa bure waweze kupata huduma hiyo.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya Mnanila – Kasulu yenye urefu wa kilometa 42 kwa lami.
(a) Je, lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
(b) Zile kilometa nne ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba zingeanza kujengwa kwa kiwango cha lami katika Makao Makuu ya Wilaya ya Buhigwe utaanza lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Ntabaliba Obama, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mnanila – Kasulu yenye urefu wa kilometa 48 ni barabara ya mkoa chini ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na inaunganisha Wilaya tatu za Kasulu, Buhigwe, Kigoma na nchi jirani ya Burundi. Barabara hii ni sehemu ya barabara ya Kibondo – Kasulu – Manyovu yenye urefu wa kilometa 250 ambayo kazi ya usanifu wa kina inaendelea ikiwa ni hatua muhimu katika ujenzi kwa kiwango cha lami. Utekelezaji utafanyika kupitia wahisani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) chini ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baada ya kukamilika kwa usanifu, taratibu za ujenzi kwa kiwango cha lami zitafuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa kipande cha barabara kilometa mbili katika makao makuu ya Wilaya ya Buhigwe, Halmashauri imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ambao utasaidia kujua gharama za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Kukamilika kwa hatua hiyo, kutawezesha Serikali kuweka katika mpango na kutenga bajeti ili kuanza ujenzi.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Mradi wa Maji wa Mnanila, Mwayaya na Mkatanga utaanza kutoa maji kwa kuzingatia ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli?
(b) Je, kwa nini Serikali haitoi fedha ili kumaliza miradi ya maji ya Munzenze, Kirungu na Nyamugali ambayo sasa imekuwa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Ntabaliba Obama, Mbunge, wa Jimbo la Buhigwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Mnanila, Mwayaya na Mkatanga ni mradi wa zamani uliyotekelezwa katika miaka 1970. Mradi huu kwa sasa umechakaa, na haufanyi kazi. Kutokana na ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Serikali ilituma fedha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kiasi cha shilingi 10,000,000 kwa ajili ya kufanya usanifu wa mradi na kuhamasisha jamii kushiriki katika ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha andiko la ukurabati la mradi huu linaonesha mradi utagharimu shilingi bilioni moja nukta sifuri nane. Utekelezaji wa mradi huu utaanza katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji ya Munzenze, Kirungu, na Nyamugali ni miongoni mwa miradi ya vijiji kumi inayotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Vijijini ambapo utekelezaji umefikia asilimia 86 kwa mradi wa Munzenze, asilimia 65 kwa mradi wa Kirungu na asilimia 50 kwa mradi wa Nyamugali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.28 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe. Serikali itaendelea kutuma fedha ili kukamilisha miradi kwa kadri zinavyopatikana.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. ALBERT O. NTABALIBA) aliuliza:-
Wilaya ya Buhigwe ni Wilaya ambayo upandaji miti haujafanyika vya kutosha.
Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuweka bajeti juu ya zoezi hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya wilaya ikiwemo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma kutokufanya vizuri katika zoezi la kupanda miti. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa mbegu, miche na aina ya miti inayofaa kupandwa kwa kila wilaya. Aidha, suala la ukame, upatikanaji wa maeneo na ardhi ya kupanda miti, usimamizi dhaifu wa viongozi na watendaji na mwitikio mdogo wa jamii navyo huchangia kukwamisha zoezi la upandaji miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya zoezi la kupanda miti na kwa kutambua hilo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 imetenga shilingi bilioni mbili katika Mfuko wa Mazingira ambazo zitatumika kwa ajili ya zoezi la upandaji miti nchini. Aidha, tunahimiza Halmashauri zote nchini na taasisi za umma na binafsi kutenga fedha kwa ajili ya kupanda miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitumie fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kushiriki katika upandaji miti na utunzaji wa miti. Aidha, ni matumaini yangu ya kuwa Waheshimiwa Wabunge watakuwa mstari wa mbele katika kushiriki na kuhamasisha wananchi kupanda na kutunza miti ili kuifanya Tanzania iwe ya kijani.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami baraba Mnanila – Manyovu – Kasulu ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 48.7 ni barabara ya kiwango cha changarawe na inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kasulu hadi Manyovu ni sehemu ya mradi wa kikanda wa Barabara ya Kibondo - Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 250 inayofanyiwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kupitia mpango wa NEPAD yaani New Partnership for Africa’s Development kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Soko la Kimataifa la Mnanila – Buhigwe lilikuwa kwenye mpango wa kujengwa mwaka 2012/2013, lakini hadi sasa soko hilo halijajengwa. Je, ni lini soko hilo litajengwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba nitangulie kumjibu Mheshimiwa Albert Obama na nichukue fursa hii kutambua na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge huyo kwa juhudi zake za kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa Soko la Mnanila– Buhigwe. Mheshimiwa Obama pia aliwahi kuuliza swali kama hili ambalo lilijibiwa Juni, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokuwa nimeeleza katika jibu langu la awali, Serikali kupitia Mradi wa Uwekezaji wa Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agriculture Sector Investments Project - DASIP) ilipanga kujenga masoko saba ya mpakani katika maeneo ya Mnanila - Buhigwe, Mutukula - Misenyi, Kabanga - Ngara, Nkwenda - Kyerwa na Muronga - Kyerwa, Remagwe - Tarime na Busoka - Kahama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ujenzi wa masoko mawili ya Mnanila na Mutukula haukuingia katika mpango wa ujenzi wa masoko hayo kutokana na kucheleweshwa kwa taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi. Mradi wa DASIP ulihitimishwa mwaka 2013/2014 na masoko matano yaliyokuwa yanajengwa yalikamilika kwa kiwango cha kati ya asilimia 40 mpaka 60. Wizara ya Kilimo ambayo ndio ilikuwa inasimamia mradi wa DASIP inaendelea na juhudi za kukamilisha ujenzi wa masoko hayo kwa kutumia vyanzo vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Mradi wa DASIP kufikia ukomo Serikali inaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kuingiza ujenzi wa soko hilo katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ili kufanikisha ujenzi wa soko hilo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itaendelea kutafuta wahisani wa maendeleo, ili kujenga soko la mpakani eneo la Mnanila.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA (K.n.y. MHE. ALBERT O. NTABALIBA) aliuliza:-
Katika jimbo la Buhigwe hususan eneo la Munzeze, soko la tangawizi limekuwa la shida sana na tangawizi huuzwa bei ya chini sana.
Je, Serikali inasaidiaje upatikanaji wa masoko ili wananchi wauze kwa bei ambayo itawafaidisha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la tangawizi ni miongoni mwa viungo vyenye thamani kubwa na linalimwa kwa wingi katika Mikoa ya Kigoma, Ruvuma, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga, Njombe, Songwe na Mbeya. Kama alivyosema Mheshimiwa Ntabaliba, zao hili limekuwa na tatizo la upatikanaji wa soko zuri na la uhakika. Ili kutatua tatizo hili, Wizara kupitia Mamlaka ya maendeleo ya biashara Tanzania Tantrade imeratibu jitihada za kupata soko katika nchi za Ulaya na Marekani. Wateja wa awali wamefurahia ubora wa tangawizi za Tanzania na wameomba watumiwe tani 25 kama sampuli ya kujaribu soko (market testing). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninashauri Mheshimiwa Ntabaliba na wananchi wenye fursa ya kulima tangawizi katika maeneo yao wawasiliane na Wizara yangu au Taasisi ya SIDO pamoja na Mamlaka ya Tantrade. Soko la Ulaya na Marekani ambalo limevutiwa na ubora wa tangawizi yetu linahitaji takribani tani 750,000 za viungo kwa mwaka kama tukikidhi vigezo.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Akina mama na vijana wa Jimbo la Buhigwe wanajituma sana katika kilimo na uwekezaji.
(a) Je, ni lini Serikali itawasaidia kimtaji ili waweze kujikomboa?
(b) Je, ni kiasi gani kimetolewa kuwawezesha akina mama na vijana katika miaka ya 2010 hadi 2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuwahamasisha vijana wa Mkoa wa Kigoma kuanzisha vikundi vingi vya wajasiriamali ambavyo ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya wanawake, vijana na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwasaidia wanawake na vijana kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Vijana. Mikopo hii imelenga kuwasaidia kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi hivyo kujiongezea kipato na kukuza uchumi.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe imeanza kufanya kazi Januari, 2013 hivyo taarifa zilizopo ni kuanzia mwaka huo. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ilitoa jumla ya shilingi 25,377,057 kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya wanawake na vijana. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia Mei, 2018 jumla ya shilingi 10,500,000 zimetolewa katika vikundi vya wanawake na vijana. Aidha, kupitia Mfuko wa Jimbo Mheshimiwa Mbunge alitoa shilingi 10,500,000 kwa vikundi saba vya bodaboda na kikundi kimoja cha mafundi seremala.
Mheshimiwa Spika, jumla ya shilingi 20,200,000 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa wakulima 435 wa kahawa waliodhulumiwa katika Jimbo la Buhigwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabalika, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2011/2012, Kikundi cha Wakulima wa Kahawa cha Kalinzi Organic kilipeleka jumla ya tani 15.8 za kahawa yenye thamani ya Dola za Kimarekani 74,397.24 kwa Kampuni ya Tanganyika Coffee Curing Co.Ltd kwa ajili ya kukobolewa na baadaye kuuzwa mnadani. Hata hivyo, baada ya kukoboa kampuni ya TCCCo Limited ilitambulisha kimakosa kahawa ya Kikundi cha Kalinzi Organic kuwa ni kahawa ya Kikundi cha Kalinzi Coffee Farmers kwa maana ya (KACOFA) na hivyo Bodi ya Kahawa Tanzania kukilipa fedha za mauzo ya kahawa kikundi cha KACOFA badala ya Kikundi cha Kalinzi Organic.
Mheshimiwa Spika, baada ya kugundulika mkanganyiko huo, taratibu za usuluhishi zilifanyika na maamuzi yalitolewa ambapo kikundi cha KACOFA kilikubali kurejesha fedha hizo kwa Kikundi cha Kalinzi Organic kupitia mauzo ya kahawa yao ya msimu ule wa 2012/2013. Hata hivyo, katika msimu wa 2012/2013 na 2013/2014 Kikundi cha KACOFA hakikupeleka kahawa ya kuuza kwenye soko la mnada hivyo fedha hizo hazikuweza kurejeshwa kwa Kikundi cha Kalinzi Organic kama ilivyoamuliwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya mashauriano kati ya uongozi wa kiwanda, Bodi ya Kahawa, Wizara ya Kilimo na viongozi wa Mikoa ya Kilimanjaro na Kigoma iliamuliwa kuwa suala hilo liwasilishwe kwenye vyombo vya usalama kwa ajili ya uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, upelelezi wa suala hilo umekamilika na jalada la shauri hilo lipo kwa Mwanasheria wa Serikali ili atoe uamuzi na mapendekezo ya hatua za kuchukua kwa kikundi cha KACOFA. Aidha, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba haki ya Kikundi cha Kalinzi Organic itapatikana. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya mpya ya Buhigwe na kutoa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto za miundombinu Kijiografia pamoja na nyinginezo zinazoikabili pamoja na mikoa mipya hapa nchini. Changamoto hizi ni pamoja na uhaba wa Ofisi na nyumba za kuishi watumishi. Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika Wilaya mpya ya Buhigwe limeshatenga eneo kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Kituo cha Polisi cha Wilaya chenye ukubwa wa ekari tano. Pia zimetengwa ekari 20 kwa ajili ya nyumba za makazi ya Askari Polisi. Aidha, kwa sasa huduma za kipolisi katika maeneo ya Buhigwe hutolewa kupitia kituo kidogo cha Polisi cha Buhigwe na Manyovu.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya vituo vya polisi pamoja na nyumba za makazi ya askari nchini ni makubwa na yanahitaji fedha nyingi. Haya hivyo, Jeshi la Polisi limeweka vipaumbele katika Mikoa na Wilaya mpya, Miji inayokuwa kwa kasi pamoja na maeneo yenye viashiria na matishio ya kiusalama ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA Wilayani Buhigwe unasuasua sana.
Je, ni lini vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Buhigwe ina kata 20, vijiji 44 na vitongoji 190. Kupitia Miradi ya REA Awamu ya Pili vijiji 14 vilipatiwa umeme, vijiji hivyo ni Kasumo, Kalege, Nyanga, Biharu, Kigege, Bulimanyi, Nyamugali, Songambele, Kavomo, Buhigwe, Mulera, Munanila, Manyovu na Mwayaya. Aidha, katika awamu hiyo taasisi mbalimbali za umma zilipatiwa umeme ikiwamo Shule ya Msingi ya Kalege, Kituo cha Afya cha Muyama, Zahanati ya Buhigwe, Kituo cha Polisi cha Buhigwe, pamoja na Ofisi ya Uhamiaji ya Munanila nayo ilipatiwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vipatavyo 22 vya Wilaya ya Buhigwe vimejumuishwa katika Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Mwezi Mei, 2018 katika Wilaya za Buhigwe, Kasulu, Kigoma na Uvinza. Utekelezaji wa mradi huu umechelewa kuanza katika Wilaya hizo kutokana na mmoja wa wakandarasi walioomba kazi hiyo kuilalamikia kampuni iliyokusudiwa kupewa kazi hiyo mahakamani. Vijiji vitakavyopelekewa umeme ni pamoja na Nyakimwe, Mkatanga, Rusaba, Nyaruboza, Muhinda, Kibande, Kajana, Bweranka, Kigogwe, Kibwigwa, Kinazi, Kitambuka, Munzese, Bukuba, Nyankoronko, Migongo, Mubanga, Mugera, Kirungu, Katundu, Munyegera na Nsagara. Kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilometa 103.64 za njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 na kilometa 142 za njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma 71 na uunganishwaji wa wateja wa awali 3,011. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 8.53.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vyote na vitongoji vyake pamoja na taasisi za umma zitapelekewa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu baada ya taratibu zote zinazoendelea kukamilika. Vijiji nane vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao unatarajiwa kuanza Novemba, 2019 na kukamilika Juni, 2021, ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-

Walimu wa hesabu na sayansi ni changamoto kubwa ndani ya Wilaya ya Buhigwe:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu katika wilaya hiyo na waliopo sasa ni wangapi?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika shule za Buhigwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo.

(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ina jumla ya shule 19 zenye wanafunzi 6,622. Jumla ya Walimu waliopo wa hisabati na sayansi ni 83 sawa na asilimia 54 ya Walimu 155 wanaohitajika. Mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri Walimu wa masomo hayo kwa awamu na kwa sasa kibali cha kuajiri Walimu 4,549 kimekwishatolewa ambapo kati ya hao, 1,374 ni wa Masomo ya Sayansi na Hisabati. Utaratibu wa kuajiri Walimu hao unaendelea na watapangwa kwenye halmashauri zenye upungufu mkubwa ikiwemo Halmashauri ya Buhigwe.

(b) Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, Halmashauri ya Buhigwe ilipokea vifaa vya maabara kwa shule mbili za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara. Vilevile katika Mwaka 2018/2019 Serikali inatarajia kununua na kusambaza vifaa vya maabara kwenye shule za sekondari 1,250 zikiwemo shule za sekondari katika Halmashauri ya Buhigwe zilizokamilisha vyumba vya maabara.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutumia Kituo cha Forodha Manyovu ili kupitisha mizigo kwenda Burundi kwa kiwango cha kutosha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Forodha Manyovu kinatoa huduma za forodha mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Mkoa wa Kigoma. Kituo hicho kinatoa huduma kidogo ikilinganishwa na uwezo wake kwa sababu ya changamoto ya umbali wa transit route ya Dar-es-Salaam hadi Burundi kupitia Manyovu.

Mheshimiwa Spika, umbali wa transit route ya Dar-es- Salaam – Isaka – Nyakanazi hadi Manyovu ni kilometa 1457 wakati transit route ya Dar-es-Salaam – Isaka – Nyakanazi hadi Kabanga ni kilometa 1330. Tofauti ya umbali kati ya transit route ya Kabanga na Manyovu ni kilometa 127. Aidha, transit route ya Dar-es-Salaam – Manyoni – Tabora hadi Manyovu ni kilometa 1273, lakini route hii pia inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa sehemu ya barabara ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto ya umbali wa transit route ya Dar-es-Salaam - Isaka – Nyakanazi - Manyovu pamoja na ubovu wa sehemu ya barabara ya transit route ya Dar-es-Salaam – Manyoni – Tabora - Manyovu wafanyabiashara wengi hutumia Kituo cha Forodha Kabanga ili kuokoa sehemu ya gharama ya usafiri na usafirishaji.

Aidha, pamoja na changamoto hizi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Kituo cha Forodha Manyovu kimeunganishwa na Mfumo wa Forodha wa Uthaminishaji Mizigo wa TANCIS na kina uwezo wa kutoa huduma za kiforodha kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu. Vilevile, taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Uhamiaji, Polisi na Wizara ya Kilimo zimeanzisha Ofisi katika kituo hicho kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiforodha.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio ya Serikali kwamba huduma za forodha katika Kituo cha Forodha Manyovu zitaimarika zaidi baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa vipande vya barabara ya Manyoni – Tabora – Uvinza; ujenzi wa barabara ya Kasulu – Manyovu na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa, pamoja na mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-

Ni lini Serikali itavipatia maji vijiji vya Rusaba, Kilelema, Migongo, Nyaruboza na Kibwigwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya hali ya huduma ya maji inayoikabili Halmashauri ya Buhigwe kwa vijiji vya Rusaba, Kilelema, Migongo, Nyaruboza na Kibwigwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika vijiji vya Kilelema na Migongo mkandarasi wa kujenga miundombinu ya miradi ya maji katika vijiji hivyo amepatikana. Aidha, mabomba yatakayolazwa katika mradi huo tayari yameagizwa na mara yatakapoasili yatalazwa katika mtandao wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika vijiji vya Rusaba, Nyaruboza na Kibwigwa, vimewekwa katika Mpango wa Utekelezaji katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maji ambapo vitatekelezwa katika mwaka 2020/21.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 Halmashauri ya Buhigwe imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.15 ili kuhakikisha miradi ya maji inakamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.