Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joshua Samwel Nassari (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ukisoma maandiko, Biblia Yeremia 33 mstari wa tatu, inasema, “niite nami nitakuitikia, nami nitakuonesha mambo makubwa na magumu usiyoyajua.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wamelia na wamemwomba Mungu, wamemwita naye amewasikia na sasa hivi yameanza kujidhihirisha, matokeo yake ndiyo haya, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, wanakuja Bungeni kuomba sanamu ya Mashujaa iondoke iwekwe ya Diamond. Matokeo yake wengine wanaongea kwenye Bunge hili, wanasema wana uchungu sana, hawataki Bunge lionekane live, halafu siku moja baadaye anakwenda kuomba exclusive interview ya Ayo TV ili aonekane yeye kwenye TV.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile maombi haya ambayo Watanzania wameomba Mungu, yameonekana leo hii, ndiyo maana Mheshimiwa Rais anafanya vetting ya Mawaziri kwa zaidi ya mwezi mmoja, badala yake anatuletea Mawaziri walevi wanaokunywa viroba asubuhi. Hili ndilo tatizo la kukosa sukari kwenye nchi na uongozi thabiti. Ndiyo maana naona Mawaziri wanakunywa viroba. Sasa kama Mawaziri wanalewa, sijui madereva wa bodaboda kule mtaani watafanya namna gani? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kwenye uchangiaji wa leo kwenye Wizara ya Ardhi. Mwaka 1952, Mtanganyika wa kwanza aliyekwenda Umoja wa Mataifa miaka tisa kabla ya uhuru, alikuwa anaitwa Japhet Kirilo Ngura Ayo, akiwa ni mwananchi wa Meru, baada ya hapo, kilichompeleka UN Marekani 1952, New York, ilikuwa ni suala la ardhi na akianzia Meru, kwa sababu ya mgogoro uliokuwepo wa ardhi ndani ya iliyokuwa inaitwa Wilaya ya Arusha Meru miaka hiyo na Kiriro huyo akaja kuwa Mbunge wa kwanza. Wakati wa harakati za uhuru Mwalimu Nyerere amelala sana pale Meru nyumbani kwa Kiriro, alikuwa anakuja kutafuta ushauri, kwa sababu mwezake alikwishafika kabla yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka tisa kabla ya uhuru Kiriro ametumwa UN, New York, kwa fedha ambazo zilichangwa barabarani kwenye vyungu ambavyo watu wa Meru waliweka zikamsaidia kwenda yeye pamoja na Mwanasheria United Nations, 1952.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata uhuru, ameingia Nyerere, Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na Awamu ya Tano, bado ardhi ya Meru imeendelea kizungumkuti. Halafu matokeo yake, mnavyotuona sisi kule tunaamua kuchukua sheria mkononi sasa, tukija Bungeni mnaanza kutuambia Mheshimiwa Mbunge unatakiwa utulie, uwe kiongozi, uvae suti vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nivae suti? Kiriro alivaa suti mwaka 1952, mpaka leo ardhi haijarudi. Tumepata uhuru over 50 years, bado kilio ni kile kile! Matatizo ni yale yale! Ndiyo maana tunasema Serikali hii kwa kweli imechoka. You guys are sick and tired!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize kwa mfano, amekuja Mheshimiwa Simbachawene Meru mwaka 2014 kama siyo 13, akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Tumeongozana kwenda kwenye shamba la ACU la Valesca, Serikali ikakubali kutoa ekari 1500 kwenda kwa wananchi, leo hii ni mwaka 2016, bado zoezi halijawahi kufikia mwisho, bado ni mgogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Mheshimiwa Ole-Medeye akiwa Naibu Waziri wa Ardhi kabla yake 2012, tumekwenda kwenye shamba la Karamu, mimi na yeye mguu kwa mguu mwaka 2012. Leo ni mwaka 2016, we are crying a very same, we are singing a very same song. Kila siku hadithi ni zile zile. Tufanyeje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaishia hapo, Tanzania Plantation; na mimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kikubwa kweli! Mheshimiwa Waziri nakushukuru leo umetupa begi kubwa, nafikiri hili begi nitapeleka nyumbani, litatusaidia kufanya kazi za nyumbani. Kwenye kitabu hiki ukurasa wako wa 39 ambao umeonesha hali ya migogoro ya ardhi kwenye nchi, umetaja hapa mashamba yaliyoko Arumeru, umeyataja mengi; Lusi, Dolly Agakhan sijui nini Tanzania Plantation na mengine na ukasema chanzo cha mgogoro ni wananchi kuingiza mifugo kwa nguvu bila idhini katika mashamba ya wakulima wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa mkononi ninalo Gazeti la Serikali (Government Gazette), ambalo limesainiwa na kutolewa mwezi Agosti, 1993 kabla mimi sijaanza Darasa la Kwanza, ambalo linaonesha kabisa kwamba kulikuwa na nia ya Rais ku-revoke. Baada ya hapo ikafutwa na likatwaliwa. Leo hii ni mwaka 2016 tangu mwaka 1993, leo unatuambia wananchi wanaingiza mifugo kwenye shamba la mwekezaji mkubwa, eti ndiyo maana kuna mgogoro. Hivi ni nani ambaye amevamia hapa? Ni wananchi au Mhindi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi inawekewa mfukoni Mhindi mmoja mwenye uraia wa Uingereza, anaishi Tanzania, anamiliki ardhi, ardhi imefutwa na Rais, leo anaendelea kuimiliki, amegawa, ameuza na anaendelea kuuza. Who is powerfull in this country? A business person au the Government itself? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, nina nyaraka nyingi hapa mkononi na Mheshimiwa Waziri, anajua vizuri kwa sababu kwake mimi nimekuwa ni mgeni wa kila siku. Nimemwomba pengine aje Arumeru akae hata wiki moja au mbili; kama hana sehemu ya kukaa mimi nitam-host kama ni chakula mimi nitampa. Aje kwa gharama zangu, siyo kwa gharama ya Ofisi ya Mbunge, tufanye kazi tumalize. Leo naomba nimpe tu list ya mashamba ambayo kuna nyaraka zake ziko hapa na nitaziwasilisha mezani kwa Mwenyekiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ambayo ni kizungumkuti ni Shamba la Valesca ekari 1500, shamba la Karamu, shamba la Tanzania Plantation, shamba la Madira ambalo lilitwaliwa na wenyewe na lilipaswa kurudi kwa wananchi na nyaraka zipo hapa nitakupa badala yake tumepewa ekari 200, nyingine akapewa ekari 50 Mbunge mmoja wa Chama cha Mapinduzi alikuwa wa Vunjo anaitwa Aloyce Kimaro. Wakati huo amekwenda nje huko akadanganya anakuja kujenga hoteli, asaidie ku-host Mkutano wa Sullivan, leo ni miaka karibu 10 baada ya Mkutano wa Sullivan, hakuna hoteli wala nini, ardhi bado imehodhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, achia mbali shamba la Madira, kuna shamba la kwa Hidaya. Mzungu mmiliki hayuko Tanzania, miaka zaidi ya nane, nimekwenda kumtatufa, hayupo. Limeachwa, limekuwa pori hapo, sijui yupo nchi gani huko, tunaangalia. Shamba la kwa Ugoro, mpaka na kesi Mahakamani wananchi walishinda, lakini halirudishwi kwa wananchi. Shamba la kwa Oscar, badala yake linakodishiwa wananchi au watu mpaka leo; nimekuja na risiti ninazo nitaziwasilisha kwako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe hii barua mojawapo hapa, imeandikwa mwaka 2001 na ikasainiwa na mtu anayeitwa T. J. Nkya, Msajili wa Hati Msaidizi, Kanda ya Kaskazini na anaonesha kabisa kwamba shamba la Arusha Ex Coffee Farm limekuwa revoked. Kwenye barua yake kwenda kwa Kamishina wa Ardhi anasema kabisa kwamba napenda kuthibitisha kwamba hati tajwa hapo juu ilitwaliwa; kwenye mabano ikaandikwa (revoked) na Mheshimiwa Rais, tangu tarehe 27 Februari, 1990, revocation kusajiliwa tarehe 3 Januari, 1991; chini ya waraka namba 6156. Mpaka leo hii tunavyozungumza lile shamba linamilikiwa na Wazungu na wameuza, wamegawa na wamepata hati, wamefanya subdivision Serikali imelala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina nyaraka nyingine tena kwa mtu anayeitwa N. J. Masuwa, Kamishina wa Ardhi, alizungumzia suala hilo hilo na akasema kwamba utaratibu wake ulikwisha, anamwambia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru awagawie wananchi. Mpaka leo hii hakuna kitu. Matokeo yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake sasa ni kwamba wananchi wanapojaribu kuingia kwenye shamba hilo kwa nyaraka hizi, wananchi wa Kijiji cha Maksoru mwaka 2015 wakashikwa wakafunguliwa kesi, tena wakapewa kesi ya armed robbery. Mimi Mbunge ndiyo nilihangaika mpaka kesi ikabadilishwa wakatoka wako nje leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu mwezi wa Tatu, Arumeru Magharibi kwa Mheshimiwa Gibson hapo, wananchi wengine kwenye lile lile shamba la Tanzania Plantation ambalo nimesoma taarifa yake ambayo imekuwa gazetted kwenye gazeti la Serikali hapa, wamefunguliwa kesi mwaka huu mwezi wa Tatu wakapewa armed robbery. Wengine tena upande wa huku kwangu mwaka 2015 akapewa kesi ya mauaji, kisa tu au chokochoko anadai ardhi. Nataka niulize, Serikali hii mtaweza nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikija hapa sijawahi kuomba kwamba eti naomba kule kwangu sijui kuna shule haina choo au madawati. Kama mnashindwa kusimamia nyaraka, mtaweza kusaidia wananchi wapate madawati nyie! Mtaweza kujenga matundu ya vyoo kwenye shule? Mtaweza kununua ndege? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda na nimeshagongewa kengele ya kwanza, Mheshimiwa Waziri hizi nyaraka zote na nyingine nimeshazifikisha kwake na leo nimekuja nazo nitapeleka kwa Mwenyekiti. Wakati akihitimisha hotuba yake leo, kama asipozungumzia masuala hayo, kwa kweli naomba niweke nia kabisa kwamba nitatoa shilingi. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili na la mwisho ambalo naomba niliguse kabla ya kengele kulia, Mheshimiwa…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Nashukuru, lakini ujumbe umefika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwa kuanza, sincerely kabisa nimpongeze sana Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi la Taifa pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. Pamoja na changamoto ndogo ndogo ambazo bado zipo, lakini nyingi tunajua zinasababishwa na financial constraints na tukizingatia kwamba makusanyo yote yanayokusanywa na TANAPA yanakwenda kwanza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, kwa kweli nimpongeze na ni matumaini yangu kwamba, yale madogo madogo ambayo bado hayajafanyiwa kazi na yenyewe yatafanyiwa kazi kadiri muda unavyokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwazungumzia ma-guides ambao ndiyo wanafanya kazi za kuwa na watalii tangu wanapoingia nchini mpaka wanapoondoka. Makampuni ya utalii yanatengeneza fedha kupitia biashara ya utalii, lakini ukiangalia mtu ambaye ana-deal na utalii tangu mtalii anapotua airport mpaka siku ya mwisho anaporuka ni guide, lakini ukiangalia maisha yao, ukiangalia namna gani ambavyo wanakuwa mistreated, kwa kweli inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii kumwomba ndugu yangu Profesa Jumanne Maghembe pamoja na Mhandisi Ramo Makani kwamba sasa waielekeze Wizara au hao Maafisa ambao wapo kwenye Wizara yao waangalie ni namna gani ya kukaa chini na vyama vya hawa waongoza utalii kwa maana ya guides ili wazungumze nao na waangalie changamoto ambazo wamekuwa nazo na waangalie ni kwa namna gani wanakuwa mistreated na kampuni na ni namna gani ambavyo kampuni zinaamua tu ku-hire and fire leo ama kesho. Vile vile guides wengi wamekuwa hawapati ajira za kudumu kwenye kampuni zao, bado wanafanya kazi kama vibarua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiachilia mbali hawa guides vile vile wapo watu ambao wanaitwa porters ambao wanabeba mizigo na kusindikiza wageni kupanda mlimani. Siku za nyuma Serikali iliagiza kwamba kila porter ambaye anakwenda na mgeni milimani kwa siku moja alipwe fedha ambazo siyo chini ya dola 10 za Kimarekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka tunavyozungumza leo hii bado wapandisha wageni mlimani wapo ambao mpaka leo hii wanalipwa sh. 6,000/= mpaka sh. 5,000/= kwa siku; na kazi wanayoifanya ni kubwa kupindukia kwa sababu wakati mwingine watalii wanaugua wakiwa njiani na wengine wanazidiwa wakiwa wanapanda mlima. Pia hawa watu kazi yao si tu kubeba mizigo peke yake kuna wakati mwingine unakuta mpaka kuwabeba watalii wakati wakizidiwa wanapougua huko njiani na wanaofanya ile kazi ni porters.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawahi kuona porters wakisafirisha watalii ambao wamejiharishia kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, kuzidiwa wakiwa mlimani, lakini ukiangalia pesa wanayolipwa mtu analipwa sh. 6,000/- kwa siku na anapanda mlima kwenye high altitude. Kwa kweli inasikitisha. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atoe maelekezo upya kwamba wanaopandisha wageni mlimani wanapaswa kulipwa shilingi ngapi na kampuni ambazo haziwapi ile dola 10 ambayo Wizara ilielekeza tujue wanachukuliwa hatua gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo, niongelee suala moja ambalo limezungumzwa pia kwenye hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu kampuni inayoitwa Green Mile Safari Limited. Kampuni hii na naamini kwamba ofisi ya umma (The Public office) is an institution. Anapoamua Waziri mmoja kumnyanganya mtu leseni kwa sababu amekosa sifa za uwindaji na ushahidi upo wa nyaraka, picha za video na picha za mnato, halafu mwaka mmoja au miwili baadaye anakuja Waziri anamrudishia tena mtu yule yule leseni ya kurudi kuendelea kuwinda kwenye kitalu. Halafu unamnyang‟anya kampuni nyingine kama wanavyonyang‟anywa hao Winget Window safaris.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tufahamu, hivi ni kwamba maamuzi yaliyofanyika miaka miwili iliyopita hayakuwa maamuzi sahihi? Hizi zile picha za video na picha za mnato ambazo zilionyesha namna gani hawa watu walikuwa wanawinda jike wadogo ambao hawaruhusiwi kuwindwa kwa mujibu wa taratibu leo hii wamekuwa watakatifu tena?. Ndiyo maana inasemwa mtaani kwamba kampuni hii ilikuwa ina backup kutoka State House.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sina uhakika lakini mtanifanya niamini hivyo kwa sababu kama imenyanganywa leseni kwa kutokufuata taratibu halafu leo hii mnairudishia bila kufuata taratibu tena, tunapata mashaka kidogo. Mheshimiwa Maghembe tusije tukapata wasiwasi na yeye na utendaji wake wa ofisi, naomba alizungumze wakati anahitimisha, vinginevyo tutafanya vile ambavyo huwa tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine niongelee kuhusu TFS. Sisi kule Meru kwa mfano lipo shamba la miti na wanaotunza mashamba yale ni wananchi wa vijiji vinavyozunguka, kama Vijiji vya Kilinga, Mulala, Songolo, Sakila na vijiji vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa juzi baada ya kuvuna miti; wakati TFS wanapanda miti mingine wananchi huwa wanapewa zile plot wanalima huku wanatunza miti. Lakini badala yake tumeona kwa miaka ya hapo nyuma na hususan mwaka 2014; kwamba badala ya kuwapa wananchi ambao wanazunguka yale mashamba, wanapewa watu wengine kutoka nje, wanapewa watu kutoka Jeshi la Polisi, anapewa OCD wa Wilaya ili waki-backfire awasaidie kuzuia wananchi. Sasa tunaomba tu kujua hivi nini maana ya dhana ya ujirani mwema? Hivi hawa wananchi siku moja akaamka tu mwananchi kichaa akachukua dawa akaenda akapiga ile miti si itakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba hawa watu wa TFS wahakikishe wanaboresha mahusiano na vijiji vinavyozunguka na mojawapo ya namna ya kuboresha mahusiano ni ikiwepo kuhakikisha wanaopata zile plots za kulima ni wa vijiji vinavyozunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni habari ya hoteli za kitalii na masuala ya service levy kwenye Halmashauri zetu. Kwa mfano tu kwa Halmashauri yangu ya Meru peke yake, kwa takwimu za mwaka mmoja wa fedha peke yake, nitasoma baadhi ya hoteli tu hapa. Hoteli ya Dik Dik peke yake tumeshindwa kupata mapato kwa mwaka mmoja shilingi milioni tisa na laki tisa. Hoteli ya Kigongoni shilingi milioni mbili laki nane; hoteli ya Arumeru River Lodge shilingi milioni tatu na laki nne; hoteli ya Hatari Lodge shilingi milioni kumi na laki moja; hoteli ya Mountain Village shilingi milioni thelathini na laki tisa; kampuni ya Macho Porini Tours zaidi ya shilingi milioni mbili na laki tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijumlisha kwa mwaka mmoja wa fedha kwa haya makampuni sita niliyoyataja hapa peke yake Halmashauri tume-loose zaidi ya shilingi milioni 59. Sasa milioni 59 kwa hoteli sita peke yake kwa Halmashauri moja maana yake it’s a lot of money kwa miaka mitano ambazo zingeweza kusaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tungeomba kujua ni kwa namna gani hawa watu wanakwepa? Wengine wanajisajili kwenye EPZ ili waweze kupata grace ya kodi? Kwa hiyo, ningeomba Mheshimiwa Waziri hili nalo akija alizungumzie ili tusije tuka-suffocate Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na muhimu sana, ni Operation Tokomeza. Nilikuwepo kwenye Bunge lililopita na tulizungumza kuhusu habari ya Operation Tokomeza na Bunge hili lilielekeza Serikali kwamba ifanye nini na maazimio tuliyapitisha hapa ndani ya Bunge lako Tukufu. Badala yake leo hii ni miaka miwili ama mitatu baadaye bado maazimio ya Bunge hayajatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani tusisahau kwenye Operation Tokomeza tunao wananchi ambao wamepoteza maisha, ambao walilazimishwa mpaka kufanya mapenzi na miti, tunao watu ambao walilazimishwa kufanya mapenzi mbele ya watoto wao wakiwa wanaona, tunao watu ambao walinyanganywa ya mbao mpaka leo wameingizwa kwenye umaskini, tunataka kujua fidia zao ni lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maazimio ambayo yaliazimiwa ndani ya Bunge hili Tukufu ni lini yanakwenda kutekelezwa. Kwa sababu tunajua kuna baadhi ya watu wamesafishwa lakini mimi ninao wananchi mpaka leo wanaripoti polisi, ninao wananchi mpaka leo wamenyang‟anywa silaha zao halali ambazo wamemilikishwa kihalali zipo polisi mpaka leo hawajarudishiwa. Tunao watu ambao wameingizwa kwenye umaskini baada ya Operation Tokomeza na kwa kweli hatujui ni kwa namna gani wanakwenda kufidiwa, hatujui ni kwa namna gani tunaenda kugusa ile trauma ambayo waliipata kupitia Operation Tokomeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni hii ha bari ya ufugaji, uhifadhi pamoja na ukulima. Ndugu zangu katika hili niseme wazi kwamba, viongozi lazima tuangalie tusije tukaligawa Taifa vipande vipande. La pili, vile vile niulize hivi ni lini ng‟ombe wamewahi kula miti, hivi ni lini ng‟ombe wamewahi kuchoma mkaa, kwa sababu leo hii tunasema kwamba wafugaji tuwaondoe kabisa kama vile hawapo kwenye ramani ya hili Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba baadhi yetu tumekuwa Wabunge, tumekuwa Mawaziri, tumesoma kwa sababu ya ng‟ombe. Naomba nioneshwe leo hii nani Waziri hapa ambaye amewahi kusoma kwa sababu ya utalii peke yake? Ni mwananchi gani Mtanzania ambaye anaguswa moja kwa moja na impact ya utalii kwenye nchi ukilinganisha na impact ya ufugaji kwenye Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakosea viongozi na baada ya hapo tunakwenda kuwatesa wananchi. Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, nilimsikia kauli yake aliyoisema, anapaswa kuwaomba radhi Watanzania na hususani wafugaji wa Taifa hili. Narudia akitaka abaki salama kwenye kiti chake na nilifikiri pengine angekuwa Waziri wa kwanza kuja kutumbuliwa kwa ile kauli, kwa bahati mbaya Kitwanga ametangulia, nimwombe anapaswa kuwaomba radhi Watanzania baada ya hapo akaw chini na Waziri wa Ardhi na Waziri wa Mifugo wazungumze waangalie ni kwa namna gani tunaweza ku-strike a balance. Tunahitaji mifugo, tunahitaji conservation at the same time tunawahitaji wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawezi tu kuwafanya wafugaji ni kama vile ni jamii ambayo imekuwa neglected, ni watu ambao wamekuwa vulnerable kwa miaka mingi, at the same time na yeye Minister anasimama anaanza kusema kama vile kwanza hatufugi, hatuhitaji ng‟ombe kwenye nchi, hatuhitaji nyama wakati nimemwona leo akila nyama canteen. Sasa nashindwa kuelewa, hawa ng‟ombe anaowakataa mbona leo alikuwa anawala kwa nini asingekula msitu pale canteen leo, kwa nini asingekula nyama ya simba pale canteen! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tunapokuwa viongozi tuangalie namna ya kuliunganisha Taifa na siyo kuligawa Taifa, tunawahitaji wafugaji, tunahitaji uhifadhi, tunawahitaji wakulima ili Taifa liweze kusonga mbele...
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kipekee, kwanza kabisa kabla ya kuzungumza, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Arumeru ambao wamenivumila kwa kipindi chote ambacho nilikuwa masomoni nchini Uingereza mpaka sasa
ambapo nimerejea kuja kuendelea na kazi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia inazunguka kwa kasi sana. Kwa nini nasema hivyo? Leo kwenye Bunge hili, Mawaziri wanatuambia tusizungumze habari ya kugusa wala kujadili habari ya Usalama wa Taifa letu. Kwenye mkono huu, ninayo barua hapa yenye kurasa saba iliyoandikwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, leo hii ni Waziri wa Habari, Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe. Barua hii
imeandikwa tarehe 9 Februari, 2011. Kwenye barua hii Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alikuwa anatuhumu baadhi ya watu wakiwemo watu wa Utumishi wa Usalama wa Taifa kutaka kuchukua maisha yake; kutaka kumteka ama vitendo ambavyo vimekuwa vikiendelea kwenye Taifa hili.
Usipoguswa, huyasikii maumivu; ukiguswa unayasikia maumivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu umesema tusizungumzie habari ya Usalama wa Taifa nitaiacha ila nitaendelea kujadili hotuba hii nikizingatia utaratibu uliofanywa na watu ambao ni wakubwa kwenye Serikali yetu akiwepo mwalimu wangu Mheshimiwa Dkt. Harison
Mwakyembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari ya usalama naiweka pembeni, lakini kuonesha namna gani dunia inakwenda kwa kasi, ni Mheshimiwa Dkt. Harisson Mwakyembe huyu huyu Waziri wa leo; mwaka 2008 aliongoza Kamati Teule ya Bunge hili Tukufu ambayo ilijadili suala la Richmond. Katika suala lile hakusikiliza upande wa pili kwa maana ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Lowassa, akasikiliza upande mmoja akatoa ripoti kwenye Bunge hili ambayo ilipelekea Mheshimiwa Lowassa kuachia ngazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwakyembe huyu leo amepokea ripoti ya aliyekuwa Waziri kwenye Wizara yake Mheshimiwa Nape yupo hapa; upande wa pili kwa maana ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyekataa kuhojiwa, akakimbia kwa mlango wa mbele wakati
amewatuma watu kwa mlango wa nyuma. Leo Mwakyembe anasema ripoti hii haija-balance stori kwa hiyo siwezi kuifanyia kazi. Mwakyembe hiyo balancing of the story ya Mheshimiwa Lowassa na kuachia ngazi uliitoa wapi? Hukumsikiliza Lowassa alikuwa Waziri Mkuu hapa.
Taarifa...
Namheshimu sana mwalimu wangu Dkt. Mwakyembe lakini naomba nimkumbushe pia kwamba taarifa yake siipokei kwa sababu zifuatazo:- Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwanza; ni Profesa ama Dkt. wa kwanza wa PhD kwenye nchi hii ambae aliandika thesis yake ya PhD iliyoonesha ili taifa hili liende mbele lazima kuwe na Serikali tatu na tena wakati wa Bunge la Katiba alikataa thesis yake mwenye hapa ndani ya Bunge hili; mimi nilikuwa Mbunge hapa, huyo hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru lakini naomba tu niweke upepo sawa; sina shida na mwalimu wangu Dkt. Harrison Mwakyembe napenda sana amenitoa kwenye ujinga; lakini ukweli ni kwamba nilikuwa naikataa taarifa ya Dkt. Harrison Mkwakyembe kwa kutumia reference and the kind of reference I used was his own thesis. Sasa kama mimi natumia reference ya andiko ambalo ameliandika yeye mwenyewe kwa miaka; ninyi mnataka mtu atumie reference gani jamani, mnataka nitumie Mwanahalisi ya Kubenea, Mwananchi au Tanzania Daima? Natumia reference ya alichokiandika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnapeleka wapi Bunge ninyi watu? Muda wangu tafadhali.
Mheshimiwa NaibuSpika, mimi nimepata nafasi ya kusoma ya kwenye nchi za Magharibi, nchi za Amerika, Ulaya na nchi za Asia, zilizoendelea. Katika kipindi cha miezi tisa iliyopita nimekaa nje ya siasa za Kitanzania, siasa za Kibunge kwa hiyo nimezitazama nikiwa niko nje ya siasa za nchi hii. Nimeona siasa zinatia kichefu chefu; ukiongea ukweli kama huu unakandamizwa. Leo wewe asubuhi ameongea Mzee
Bulembo hapa, kwenye mchango wake hapa amemsema Mbunge wa Siha Dkt. Mollel wa CHADEMA mbona hamjamzuia?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimepewa taarifa nakataa taarifa with a reference wewe ni mwalimu wa sheria unajua huyu ni mwalimu mwenzako wa sheria kwa nini unaikataa taarifa yangu kukataa taarifa yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuthibitishie kwamba nilipoziangalia siasa za nchi yetu kutoka nje niliona ujinga ufuatao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza; ni mara ya kwanza kwenye historia ya siasa za dunia unamuona mtu mwenye cheo kama cha Ukuu wa Mkoa anavamia kwenye media house tena si media house anaingia kwenye production room akiwa yupo full armed. Mahali pekee kwenye dunia unaona kiongozi mkubwa wa ngazi hiyo anaingia kwenye media house tena production room akiwa na watu wapo full armed na silaha. Kuna mambo mawili; la kwanza ni jaribio la Mapinduzi na la pili ni Mapinduzi yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa liko kimya, watu wamezungumza hapa; ni mara ya kwanza tunakuta maiti zipo Mto Ruvu watu saba wameuawa zimefungwa kwenye viroba halafu mnasema Bunge lisijadili, mnatetea akina nani kwenye nchi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mara ya kwanza kwenye nchi Mbunge anawekwa ndani miezi minne mfululizo. Mimi nimeondoka Arusha nimemuacha Lema yupo magereza; mwezi wa Kumi na Moja nimekuja kumtembelea. Nimeondoka nimerudi, nimemaliza masters yangu;
nimemaliza semester mbili namkuta Mbunge bado yupo ndani kwa sababu Hakimu amefungwa mikono ya kutoa masharti ya dhamana, si dhamana. And you want us to stay quiet?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Tanzania pekee ambayo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Shija Lutoja Alexander Pastory Mnyeti ameingia, Madiwani wametengeneza Bajeti ya Halmashauri kwa mujibu wa sheria, wameipitisha. Bajeti ya Halmashauri inajadiliwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na inaamua kupeleka bajeti mbadala; mmewahi kuona wapi ninyi? Ni mara ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimempokea Waziri Mkuu; nipo masomoni Uingereza tunatumiana email anakuja Mkoani kwetu muungwana, Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa huyu. Nimekuja kumpokea nimepanda ndege kwa gharama zangu sijalipiwa na Bunge kuja kumpokea; namwambia issues za wananchi ananiuliza tufanye nini Mheshimiwa Nassari? Namwambia ni hili la ardhi na hili na hili; ametoa maelekezo Waziri wa Ardhi aje Jimboni, nikampongeza, mnakumbuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Ardhi amekuja tunakwenda kwenye mkutano wa hadhara wenye matatizo ya wananchi; wananchi waje na mabango na makaratasi, Lukuvi ameagiza. Wanakuja Mkuu wa Wilaya anaongea jukwaani baada ya kuongea hatambui uwepo wa Mbunge, anamuita Waziri jukwaani. Namshukuru ndugu yangu Lukuvi alikataa, he refused. Alisema hapana, hili Jimbo linaye mwakilishi wa wananchi; azungumze kwanza mimi Serikali nitajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora uko wapi? Yaani bajeti ya Halmashauri inajadiliwa kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama; wale wanajeshi wanajuaje wanajuaje kwamba wananchi wa kata 25 za Jimbo langu hawana vyoo, how do they know? Tunaongea, wanatoa miongozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara ya kwanza kwenye nchi, first time in the history of this country, Bunge linafanya kazi likiwa limeingiziwa hofu. First time in the history of this country, Bunge linatukanwa halafu unataka nikae kimya? Walisema waliotangulia Bunge linapaswa kulindwa kwa wivu wa hali ya juu. Leo unatoa mwongozo hapa kwamba Wabunge wasiguse Usalama wa Taifa; ni kweli sitaugusa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nikukumbushe mwalimu wangu wa sheria; ulimfundisha mke wangu sheria. Nchi hii ina mihimili mitatu; mhimili wa Bunge unasimamia mhimili wa Serikali; Kitengo cha Usalama wa Taifa nchi hii kipo chini ya executive, kinasimamiwa na Bunge.
Vitu ambavyo hatuwezi kujadili kwenye Bunge hili ni nchi ina mizinga mingapi, ina vifaru vimekaaje na vimeangalia kushoto au kulia, lakini habari ya kujadili Waziri kama Nape anatolewa bastola mbele ya kamera za waandishi wa habari, we cannot stay quiet, are you kidding us?
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa linafika hatua vituo vya redio vinavamiwa usiku saa sita na unataka Wabunge tukae kimya? Leo Mfuko wa Jimbo wa Mbunge unaingiliwa na Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ndiye nayeamua kwamba miradi gani ipewe pesa wakati Sheria ya Mfuko wa Jimbo imesema an MP keeps records.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo asubuhi, nimeumia sana hapa ndani. Kwa historia za Kiafrika mtu mwenye uchungu na watoto, mtu mwenye uchungu na mtu yeyote; kwa sababu kila aliyekaa hapa ndani ni mtoto wa mama, kila aliyekaa hapa ndani ni mtoto wa mwanamke, yeyote, awe na miaka 90 au miaka 80; wenye uchungu na watoto ni akinamama, ni wanawake, bila kujali vyama vyao. Leo asubuhi hapa mama anaongea habari ya watu kutekwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa yale mliyofanikiwa ndani ya Wizara lakini pia nawapa pole kwa yale ambayo yamekwama kwa namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, one thing, wananchi kwenye maeneo ya milimani waliokuwa wanalima zao haramu la bangi kama zao la biashara na hivi ndivyo ambavyo wameweza kusomesha watoto na kujikimu kimaisha. Serikali kupitia Bodi ya Pareto waliahidi kuanzisha zao hili kama zao mbadala na iliahidiwa kuwa elimu ingetolewa na miche ingetolewa mapema mara tu mvua za masika zitakapoanza. Mvua zilianza mwanzoni na katikati ya mwezi Machi lakini mpaka mwezi wa nne bado hakukuwa na lolote. Tafadhali naomba kauli ya Wizara katika hili ukizingatia kilimo cha bangi kilikuwa kwa sababu za kibiashara hususan kwenye nchi jirani na walikuwa wakitegemea kilimo hiki kwa
livelihood yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise, all the best.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nawashukuru waliotangulia kuchangia Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Millya angalau wamegusa kidogo masuala yetu na hili suala la KIA na wananchi wa vijiji vinavyozunguka nashukuru leo limesemewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa hiyo nina uhakika limechukuliwa kwa uzito mkubwa zaidi kuliko ningelisema mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliongea sana hapa Bungeni, nililia sana, Mheshimiwa Lukuvi unakumbuka ombi langu kubwa kwako lilikuwa ni kama ikiwezekana uje Meru nikuambie nini cha kufanya kwenye mashamba yaliyoko Meru ambayo yaliachwa tangu enzi za walowezi waliokuwepo Meru kwa wale mnaojua historia, nilisema hapa mwaka 1952 watu wa Meru walimtuma Umoja wa Mataifa Ndugu Kiliro Japhet Ngura Ayo, miaka tisa kabla ya Uhuru alikuwa ni Mtanganyika wa kwanza aliyekwenda Umoja wa Mataifa kwa sababu ya kudai ardhi la Meru, Meru land case.

Sasa nishukuru tu kwa Waziri Mkuu kwanza, pili kwa Waziri wa Ardhi ambao wote mlikuja kwa pamoja na Waziri Mkuu alitoa yale maelekezo na Waziri ukaja na tukafanya kazi nzuri sana kwa pamoja, kwa kweli nikushukuru mno na niseme tu kwamba unapokuwa mpinzani siyo unapinga kila kitu kinapofanyika kitu kizuri huwa tunasema na leo mmeona kwa Waziri Lukuvi hapa amesifiwa mpaka na Kiongozi wa Upinzani, kwa wale Mawaziri wengine ambao mna-ego, huwa mnajisikia na huwa hamsikii, jifunzeni kwa Mheshimiwa Lukuvi, nafikiri mtaweza kutengeneza Serikali nzuri sana, na niliwakumbusha nikasema nikasema kuwa hii dunia inazunguka leo Mheshimiwa Profesa Muhongo naye anauliza maswali ya nyongeza humu ndani, juzi alikuwa huko.

Kwa hivyo ego siyo kitu kizuri sikilizeni Wabunge wanaleta vilio gani kwenu, halafu muende kusikiliza msaidie Watanzania, kwa sababu dunia inazunguka kwa kasi niliwahi kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, niseme tu baada ile baada ya ziara yako Mheshimiwa Waziri kule Meru, tulikubaliana kwamba Baraza la Madiwani na hususani Kamati, tufanye ziara kwenye mashamba yote na kujionea halafu tuandike mapendekezo ambayo yatakuwa na consensus ili yaweze kupita Mkoani kuja kwako ili uweze kufanyia kazi. It is very unfortunate na nilikuambia siku ile nikiwa jukwaani pale nikasema kunaweza kuwa na mashaka kwamba kusitokee consensus au siasa za kipuuzi ambazo zimekuwa zikiendelea kwenye Wilaya nyingi nchi hii, zikafanyika na pale Meru zimefanyika kwenye ziara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mapendekezo ambayo yamekuja kwako nashukuru Mungu yamerudishwa nyuma kuja kuanza upya hayakuwa na consensus hata kidogo na yatakayoletwa tena nakuomba ufanye verification utuulize wawakilishi wa wananchi, uwaulize Madiwani uwaulize Wenyeviti wa Vijiji, kwamba haya mapendekezo yamekuwa na consensus au yametoka kwenye ofisi moja pale Wilaya kuja moja kwa moja kwenye ofisi yako bila kuzingatia nini wawakilishi wa wananchi kwa maana ya Madiwani walichokipindekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo ripoti ya kwanza iliyokuja kwako utaona ndani yake, vile vilio ambavyo nimekuwa nikiongea hapa ndani havijasikilizwa, havijaainishwa ndani yake kabisa, utaona kabisa inaandikwa ripoti ya kuja kumnyang’anya mtu shamba heka 10, heka 18, Meru hatulilii heka 10 na 18 tunalilia thousands of acres, hundred of acres. Mashamba ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Walowezi ambayo yalipata kibali cha Rais pia miaka ya mwanzo ya tisini kufutwa, lakini usajili haukufanyika ambapo imerudi kwenye mikono ya baadhi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nilikukumbusha nafikiri unafahamu vizuri kwa mfano, shamba la Tanzania Plantation kwanza nikushukuru kwamba ulikubali kutoa hata fedha kutoka Wizarani kwako kwa ajili ya upimaji na yule mtu alikuwa ameshakubali, mkakubaliana kwamba anabaki na kiasi gani na kiasi gani kiende kwa wananchi, it is very unfortunate kwamba amekwenda Mahakamani kufunga mikono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya watumishi wa ardhi kwenye Mkoa wetu Arusha siyo watu wazuri kwako naomba nikuambie na ndiyo wanaokwenda kuwashawishi hawa Wazungu kwamba nendeni mkafungue kesi Mahakamani mfunge Wizara mikono, mfunge Halmashauri mikono, hakuna kinachoweza kufanyika. Ukweli ni kwamba huyu Mhindi wa Tanzania Plantation na sijui polisi wetu wa Interpol wanafanya kazi gani hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huyu bwana ana passport mbili, ana passport ya Tanzania na ana passport ya Uingereza, na nchi hii haijaruhusu Dual Citizenship, tumefanya uchunguzi kabisa mara nyingi akiondoka nchini huwa anakwenda Nairobi anaruka na passport yake ya Uingereza, na huyu amekufunga mikono Mahakamani, naomba watu wa Mambo ya Ndani wakusaidie. It is very easy kum-capture huyu bwana, kwa sababu unaangalia rekodi zake za safari na unaangalia kwenye passport yake ziligongwa mihuri lini na lini na tarehe gani kwa sababu kuna tarehe ambazo ameondoka ambapo passport yake ya Tanzania haina hiyo mihuri kabisa, kwa hiyo huyu bwana anatuibia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Waziri anakumbuka kwenye ile list tuliweka hiyo list ambayo imekuja kwako ambayo nimesema haikuwa na consensus liliandikwa na shamba la Karamu, shamba la Karamu tumefanya mazungumzo na Halmashauri pamoja na mmiliki tumembana na amekubali kuingia kwenye terms ambazo Halmashauri kwa maana wananchi wa Meru wanafaidika, vijiji vinavyozunguka kwa maana vijiji vya Ndato na Mkwaranga wanapata share yao na Halmashauri inapanga ule Mji na ule ni Mji ambao ukiangalia master plan ambayo unakuja kuizundua mwezi wa Agosti Arusha, imependekeza lile eneo liwe ni eneo la residential, low density na hilo ndilo lengo letu tunakoelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tulete kwako ufute atakwenda Mahakamani atakufunga mikono tena tutafanya nini, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninaomba tu kwamba hilo liweke kwenye kumbukumbu zako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia kengele niseme tu mengine nitayaleta kwenye maandishi ikiwemo mgogoro wetu ikiwemo na wa Hifadhi ya Arusha na vijiji vinavyozunguka na Momela na mingine pia na issue ambayo ameiongea Mheshimiwa Mbowe lile shamba la Valeska tuende kwa staili aliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kabla sijaanza, ni-declare kabisa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nitazungumzia mambo matatu. La kwanza, migogoro kati ya wananchi, vijiji na hifadhi za Taifa. Vilevile nitagusia sekta nzima ya utalii kama ilivyo na mwisho nitagusia kidogo habari ya Stiegler’s Gorge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na migogoro kati ya wananchi na hifadhi zetu. Waheshimiwa Wabunge ambao tunakaa ndani ya Bunge hili kama kweli tunataka kuitendea haki nchi hii, kama kweli tunataka kuwatendea haki wapiga kura waliotuchagua kuja ndani ya Bunge hili leo tunaitwa Waheshimiwa, ukizunguka kwenye nchi hii wafanyabiashara wanalia, wakulima wanalia, wafugaji wanalia na wavuvi wanalia, whom are we serving? Tunamhudumia nani? Sasa leo hifadhi zetu baraka ambayo tulipewa na Mungu badala ya kuwa baraka kwetu imegeuka kuwa laana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, to be specific, mimi natoka Meru. Mwaka 1949,1950 mpaka 1951, Watanzania ama Watanganyika kutoka jamii ya watu wa Meru walichomewa nyumba na wakafukuzwa kwenye makazi yao na waliokuwa wakoloni kwa maana ya walowezi wakati ule na hiki ndicho kinachoitwa The Meru Land Case, kwa wale ambao wameipitia wanaifahamu vizuri. Watu walikuwa displaced, wakafukuzwa kwenye maeneo yao, wakachomewa nyumba, wakaenda kuanza maisha mapya sehemu nyingine kabisa. Mwaka 1952, watu wa Meru walichanga fedha kwenye vyungu barabarani, haikuibiwa senti hata moja, mwaka 1952 alikwenda Umoja wa Mataifa, Mtanganyika wa kwanza kwenda Umoja wa Mataifa, UNO wakati ule aliitwa Ndugu Japhet Kirilo Ngura Ayo na alikuwa Mbunge wa kwanza wa jamii yetu ndani ya Bunge hili. Amekwenda UNO mwaka 1952 kwa sababu ya ardhi ya watu wa Meru, watu wa Ngarenanyuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mwaka 2018, miaka mingi na uhuru umepatikana na tumesonga mbele, watu wa Meru wamekwenda kufukuzwa kwenye ardhi yao ile ile ya Ngarenanyuki. Sasa, who is better? Mkoloni ambaye alichoma tu nyumba au leo ambaye anafukuza watu, anawapiga na risasi, anapiga rasilimali zao risasi, anawapiga na mabomu, wanawaachia vidonda, who is better?

Mheshimiwa Mwenyekiti, with due respect, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla is a good friend of mine and he knows na urafiki wetu it’s personal, lakini katika hili Mheshimiwa Waziri tunahitaji msaada wako. Where is the supremacy of this Parliament? Mwaka jana nimeongea ndani hapa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hii akakubali kuondoka hapa kwenda Meru kusaidiana ku-solve mgogoro wa watu wa Momela na Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa masomoni Uingereza, nikamuomba Mheshimiwa Mbatia hapa anisaidie ku-handle this case nikijua uwezo wake na heshima ambayo anayo na namna gani anaweza ku-handle vizuri suala lile. Akakubaliana na Waziri hapa, wameondoka wamekwenda Arusha, Mheshimiwa Mbatia ametangulia Momela kukaa kwa niaba ya Mbunge Nassari, Waziri amechoma mafuta kafika Arumeru, amezuiwa wilayani akaambiwa mgogoro huu umekwisha, hakuna kinachoendelea, hakuna tatizo, akalazimishwa kuondoka. Mheshimiwa Mbatia akapigiwa simu akaambiwa nimepata dharura bwana ondoka, rudi zako Moshi, kisa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya aliyeondoka kwenda kuweka vigingi yeye na askari wa TANAPA kwenye hifadhi ya Taifa ya Arusha kwenye namba 40 na 41 akiitwa Alexander Mnyeti, bila kushirikisha mwananchi hata mmoja wa Momela, hata mmoja. Vigingi vimewekwa siku ya Jumapili watu wako Kanisani, wanatoka wanakuta vigingi vinawekwa. Mnatutonesha vidonda. Yale tuliyofanyiwa na wakoloni mnakuja kutufanyia leo, mnatonesha vidonda vya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ninayokuonesha hapa, hizi ni risasi za moto na mabomu waliyopigwa wananchi wa Momela. I will table this, nitaweka kwako hapo. Siyo hivyo tu, hizi ni picha na ng’ombe waliopigwa risasi pale Momela shamba 40 na 41 ambalo wakoloni walinyang’anya watu wa Meru wameondoka wamewaachia leo hii 2018, linakuwa claimed kwamba ni sehemu ya hifadhi, hifadhi imeanza miaka 60, watu wa Meru tumeishi hapo kabla, tumenyang’anywa mwaka 51, tumerudi leo hii mnatunyang’anya, twende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono maoni ya Kamati yaliyosomwa na Mheshimiwa Nape hapa leo, kwamba zoezi la uwekaji wa vigingi lisimame. Leo hii ukienda Rukwa, Shule ya Msingi aliyosoma Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, shule ya msingi aliyosoma Waziri aliyeko hapa ndani leo anaitwa Mheshimiwa Kamwelwe, leo imeambiwa ni sehemu ya hifadhi lakini Waziri Mkuu alisoma hapo, are we serious? Shule aliyesoma Nsa Kaisi leo inaambiwa iko ndani ya hifadhi, are we serious? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, with due respect Mheshimiwa Waziri, tafadhali na Naibu Waziri alishakubali tuondoke hapa twende Meru. Naomba maoni ya Kamati yaheshimiwe, zoezi lisimame, ushirikishwaji ufanyike. Leo unaenda kuweka kigingi kwenye kitanda cha mtu anaishi hapo, hivi kweli, nani mwenye thamani nchi hii tembo au raia wa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wananyanyaswa kwenye nchi hii, ng’ombe waliochukuliwa wakaenda kuhifadhiwa na ANAPA hawa hapa wamekaa zaidi ya mwezi mmoja kule ndani, angalia walivyodhoofu. Wamekuja kuachiliwa, achilia mbali waliopigwa risasi, over 75 percent of them wamekufa kwa sababu ya kudhoofu. Wale wanyama walikuwa wanatumika kwenye kilimo wakati wa masika watu hawakulima kwa sababu wanyama wameshikiiwa, wengine walikuwa ni ng’ombe ambao wana ndama, ndama wamebaki ndani wakafa. Msitutie umaskini nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Meru kwenye kata 26, kwenye Kata ya Ngarenanyuki ambapo Momela ndiyo kata pekee ambayo Chama cha Mapinduzi mlichaguliwa mkapata Diwani mmoja, ndiko mmekwenda kuwapiga risasi, mtawaambia nini 2020? Mtawaambia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, utalii kama sekta. Kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania Economic Update ya World Bank Tanzania tuna uwezo wa ku-earn over 27 trillion per year kama kweli tukiweza kuwekeza vizuri kwenye sekta ya utalii. Southern Circuit peke yake ni eight billion USD. Leo tunavyozungumza, tunakwenda kujenga Stiegler’s Gorge, Selous, world heritage, dunia inatushangaa, tunatafuta megawatt 2100, hivi tuko serious? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikusomee kwa sababu ya muda niende haraka tu. Wote tunahitaji umeme na mimi nahitaji umeme sana kule kwangu lakini kwa miradi ifuatayo ambayo ni upstream bila kwenda kuhangaika na Selous na kuharibu miti milioni 2, bila kuchukua eneo ambalo ni kubwa usawa wa Dar es Salaam ndani ya hifadhi ya Selous, tuna uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawatt 2196, leo tunatafuta megawatt 2100 Selous, uwekezaji hela hatuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikiliza, megawatt 180 peke yake tunaweza kupata Kihansi ambayo tayari imeshafanyika, megawatt 165 Mwanga, megawatt 685 Ruhuji, megawatt 485 Mnyera, megawatt 87 Iringa, megawatt 130 Lukose na megawatt 464 Kilombero. Bomba la gesi tumetumia six percent peke yake, tuna megawatt 800 kwenye miradi ya Kinyerezi. Tukitumia asilimia 25 ya bomba la gesi ambalo leo
Watanzania tunawalipa Wachina waliotukopesha, tuna uwezo wa kupata over 3000 megawatts, are we thinking right? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nawauliza ndugu zangu wa CCM mnapata wapi hela ya kujenga huu mradi wa Stiegler’s Gorge? Wamarekani hawawapi shilingi kwa sababu UNESCO wamekataa na mashirika yote ya dunia yamepinga. Ulaya hamtapata shilingi hata moja, mnasema mtakwenda China, China wamebaki kwenye Paris Agreement as we are speaking today, China ndiyo wame- burn meno ya tembo wanajaribu kuji-brand duniani kwamba wanapigania uhifadhi, where are you getting the money? Tunahitaji umeme lakini siyo kwa namna hii. Naomba Wabunge tuitendee haki nchi yetu. Tulitendee haki Taifa letu, tutendee haki nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya utalii nilizungumza kidogo. Wanaotangaza utalii leo nchini ni tour operators. Tour operators ndiyo wanakwenda kwenye trade fairs, ndiyo wanakwenda Indaba, WTM, ITB, Vegas, leo Waziri wa Maliasili na Utalii tangu ameingia madarakani kama Waziri hajawahi kushiriki kwenye trade fair hata moja. Tumsaidie Waziri asafiri akaitangaze nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni Wakenya wanafanya kitu gani, nyie mmeweka VAT tulikubaliana kwenye mkutano wa East African Community baada ya kukubaliana mmegeuka, Wakenya wakaondoka, sisi tumeweka. Leo hii ukichukua miaka minne mfululizo tangu mwaka wa fedha 2012 -2016 growth rate ya utalii nchi hii kwa maana ya watalii waliokuwa wanakuja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)