Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Richard Phillip Mbogo (32 total)

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Miradi mingi ya maendeleo imekuwa haifanyiki, sababu kubwa pia ni kutokana na baadhi ya gharama za uendeshaji na Halmashauri zetu kutokupelekewa fedha, kwa mfano gharama za kusimamia mitihani. Je, Serikali inajipangaje kulipa madeni hayo kabla mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 haujaisha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na katika jibu la swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula, Serikali imejipanga vizuri, mapato yanaongezeka na miradi yote itapelekewa pesa ili iweze kukamilika kwa wakati.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Kwa kuwa, tatizo lililoko Halmashauri ya Nzega linafanana kabisa na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, haina Sekondari ya kidato cha tano na sita. Kwa kuwa, Serikali ilitupa ukomo wa bajeti bilioni 14 na tumeshindwa, tumekatwa fedha nyingi za maendeleo.
Je, Ofisi ya Rais TAMISEMI, iko tayari kututafutia fedha kwenye vyanzo vingine ili tuweze kujenga sekondari ya kidato cha tano na sita katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Nsimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli najua kwamba, mwaka huu kulikuwa na suala zima la ukomo wa bajeti lakini ndiyo mwaka pekee ambao bajeti yake imevuka tumeenda karibuni kutoka bajeti ya maendeleo ya asilimia 27 mpaka asilimia 40, kwa hiyo kuna kazi kubwa imefanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa siwezi kusema kwamba, mwaka huu kuna fedha zingine zitaingia kwa sababu mchakato wa bajeti umeshapita. Lengo kubwa ni nini! Nina imani kwamba, katika mwaka mwingine wa fedha unaokuja hii itakuwa ni kipaumbele kwa sababu tunajua wazi kwamba, tumejenga shule nyingi za Kata vijana wengi wanafaulu. Kwa mfano, mwaka huu tuna vijana karibuni zaidi ya elfu tisini, lakini ukiangalia capacity yetu inaenda karibuni vijana zaidi ya elfu hamsini, maana yake inaonekana tuna tatizo kubwa sana la kuhakikisha tunaweka miundombinu kuwa-accommodate vijana wa form five na form six.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Richard Mbogo katika mchakato wa bajeti wa mwakani tuweze kuliangalia kwa pamoja zaidi. Hata ikiwezekana kwa sababu mambo haya tumesema kwamba, hata shule zingine za Kata ambazo ziko vizuri tunaweza tukazi-upgrade zile baadhi ya shule kuziongezea miundombinu kuweza kuwa shule za form five na form six.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo katika mwaka wa fedha unaokuja tutaangalia kwa pamoja ni jinsi gani tutatanya Nsimbo tupate high school moja kwa ajili ya vijana wetu.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kupata taarifa za wafanyabiashara ili waweze kulinganisha na maandalizi ya kumbukumbu zao za hesabu. Sasa katika uhasibu kuna marekebisho ya kiuhasibu, inatokea mtu anatoa kitu kinaitwa credit note au debit note ili kufanya masahihisho. Lakini kwa sasa mfumo huu wa electronic signature device hauchukui marekebisho ya kiuhasibu. Je, ili kuondoa hali ya sintofahamu na kulinganisha kumbukumbu za TRA na wafanyabiashara, Serikali ipo tayari kubadilisha mfumo wake na kuingiza hizi credit note au debit note katika marekebisho ya kiuhasibu ili ziweze kusomeka katika mtambo wa TRA na kurahisisha kazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi; lengo la mashine hizi ilikuwa ni kupata taarifa na kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara na mauzo yao, lakini kama kuna jambo lolote ambalo litaweza kuboreshwa zaidi Serikali yetu iko wazi kabisa, naomba tushirikiane ili tuweze kuhakikisha kumbukumbu zote zinaingia katika mfumo huo. Kwa sasa, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba tumeanza na hizo kumbukumbu za mauzo na mapato ya wafanyabiashara ila haya mengine yote pia tunaendelea kuboresha mfumo wetu, nina imani kubwa yote yataingizwa kwenye mfumo huu.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa tatizo la Masasi linafanana na Jimbo la Nsimbo na sasa hivi taasisi nyingi za Serikali zina masalia ya fedha, mojawapo ikiwa ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi imerudisha shilingi bilioni 12. Je, Serikali ina mpango gani wa hizi fedha zinazobakia katika bajeti hii ya 2015/2016 katika moja ya Majimbo kutuletea kujenga vituo vya afya na zahanati kama Jimbo la Nsimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa Serikali kuhusu pesa zinazobakia, kwanza naomba nimjulishe kwamba hizi pesa kubakia ni kutokana na uongozi mzuri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa mara ya kwanza tunaona fedha zinarudishwa Serikalini kutatua matatizo ya wananchi. Naomba nilipongeze na Bunge lako hili kuhakikisha zile pesa zinarudi Serikalini na sisi Wabunge wote tutapata madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kusema kwamba pesa zilizorudi zitaenda Nsimbo, isipokuwa kwa mtazamo mpana wa Mheshimiwa Rais ataangalia jinsi gani ya kutatua changamoto za wananchi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika ajenda kubwa ya kubana matumizi na kuwapelekea wananchi huduma ya msingi. Kwa hiyo, nadhani tunaangalia kwa ukubwa wake, lakini Rais ataelekeza vizuri nini cha kufanya katika nchi yetu, kipaumbele ni nini ili wananchi wapate huduma bora.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Serikali imekuwa ikijali sana wanafunzi wa vyuo kwa kuwapa mikopo na allowance mbalimbali, lakini hivi karibuni kumekuwa na fununu za kucheleweshwa kwa hizi fedha. Sasa je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba fedha zinaenda kwa wakati na kama zinachelewa taarifa inaenda kwa viongozi husika, ili kuondoa hali ya sintofahamu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakati mwingine huwa kunakuwa na ucheleweshaji wa fedha, lakini lazima niregiste kwamba, kazi kubwa wanayofanya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuwe wakweli, wakati mwingine unasema kwamba, kuna mtu anazungumza jambo lakini hatekelezi. Wabunge hawa unaowaona humu ni waadilifu wa hali ya juu, siku zote wanalia suala la wanafunzi wanaokosa mikopo. Lakini wengine wanasema wanafunzi wanakosa mikopo ilimradi watengeneze umaarufu wa kisiasa tu, ikiletwa bajeti hapa kupitisha wanasema hapana. Lakini Wabunge hawa wanajadili kuhakikisha kwamba bajeti hizo kila mwaka zinapita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie, waliweza ku-raise budget kuanzia shilingi bilioni 56 mwaka 2006 mpaka 2007, leo hii tunazungumzia bajeti ya shilingi 480,000,000,073 watoto wanapata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tukiri kwamba, kuna kazi kubwa imefanywa na Wabunge hawa kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wanapata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini isitoshe ni kweli wakati mwingine changamoto zinajitokeza. Na juzi-juzi nimesikia kwamba, Chuo cha Dar es Salaam kuna wanafunzi walitaka kugoma. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha pesa zinapelekwa na pesa zimeshapelekwa katika vyuo mbalimbali. Kuna baadhi ya vyuo vichache ambavyo bado uhakiki unafanyika, especially Chuo cha UDOM na baadhi ya vyuo vingine. Na uhakiki huu unafanyika kwa sababu imebainika kuna wanafunzi wengine ni wanafunzi hewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba ndugu zangu tuwe na subira kidogo ni kwamba, mchakato huu unafanyika katika baadhi ya vyuo, vyuo vingine tayari ilitokea mpaka jana nafanya analysis, baadhi ya vyuo vingine wameshapelekewa cheque zao jana, wengine wamepelekewa cheque zao juzi kwa ajili ya vyakula vya wanafunzi. Jukumu letu kubwa kama Serikali ni kuwahudumia wanafunzi hao kwa sababu, tunajua kwamba kuweka bajeti ya shilingi karibuni bilioni mia nne na zaidi kwa ajili ya wanafunzi sio jambo dogo ni jambo ambalo lina utashi wa kisiasa.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tuendelee. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa anajibu kwa niaba. Tunaendelea, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, sasa aulize swali lake.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 145(a) na (b), yeyote ambaye anaingia katika maeneo ya Bunge au ukumbini ni lazima akaguliwe. Kwa utaratibu huo huo, magari ya Mawaziri na ya Wabunge wakati mwingine hukaguliwa kwa kutumia mbwa. Unapotumia mbwa kukagua magari wakati mwingine hudondosha mate na yale mate ni najisi tunaita muhalladha na najisi ile haiondoki mpaka uoshe mara saba na mara moja uhakikishe unatia mchanga. Je, hakuna utaratibu mwingine mzuri wa ku-check magari haya hasa kwa wale waislamu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Bunge lililopita tulishuhudia Mbunge mwenzetu akivamiwa katika maeneo anayoishi na kuharibiwa gari lake. Je, Bunge lina utaratibu gani kuhakikisha kwamba Wabunge hawa wanapata ulinzi au usalama wao unalindwaje kwenye maeneo yao wakiwa katika Bunge hili?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rashid Abdallah kwa observation yake ya msingi kabisa ambayo ni ya kiimani. Kwa kuwa ameuliza hakuna utaratibu mwingine na sisi kama Serikali pamoja na Bunge tuseme tumepokea ushauri ili tuli-digest jambo hilo huku tukiangalia maslahi mapana kwani imani inatuhusu na ulinzi unatuhusu. Kwa hiyo, ni jambo ambalo sote tutaliangalia tufikie muafaka mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili kuhusu Mbunge kuvamiwa, taarifa zake tunazo na tunachofanya ni kuimarisha ulinzi katika mazingira ya Wabunge wetu ili kuhakikisha kwamba wako katika maeneo salama. Niwahakikishie tu Wabunge kwamba wako mikono salama na kwa kuwa mnafanya kazi vizuri na sisi tunahakikisha kwamba wanakuwa salama. Niwatangazie tu Watanzania kwamba Wabunge hawa wanachapa kazi na jana wamechapa kazi mpaka saa sita usiku, wameunganisha kikao hiki. Kwa hiyo, wanapokutana nao huko uraiani watambue kwamba Wabunge hawa ni wachapakazi. Niwaambie vijana wangu kwamba hata wanapokuwa barabarani hawa Wabunge wakiona wako speed wawaambieni tu tunawahitaji lakini watambue ni kutokana na uchapakazi wao wanawahi mikutano.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na matatizo ya askari ambayo yameelezwa, lakini kuna matatizo yaliyoko kwa Askari wetu wa Kikosi cha Reli ambao huwa wanasindikiza hizi treni katika maeneo mbalimbali kama vile Mpanda, Kigoma na Mwanza. Sasa kuna utaratibu wa wao kulipwa allowance katika hizo kazi wanazofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Askari wa Kikosi cha upande wa Kata ya Katumba na Ugala wana madai yao tangu mwaka 2013 mpaka sasa hawajalipwa. Sasa je, Waziri yuko tayari kuhakikisha kwamba Shirika la Reli linalipa mafao yao ili waondokane na tatizo la usumbufu kwa sababu imepelekea mpaka wamefungua kesi Mahakamani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo malalamiko ya madai mbalimbali ya askari yakiwemo hayo ya askari wale wanaofanya kazi upande wa TAZARA. Kilichokuwa kinafanyika ilikuwa ni uhakiki wa madai hayo na Wizara yangu tayari imeshawasiliana na Wizara ya Fedha ili punde ambapo uhakiki huo utakuwa umekamilika wa madai mbalimbali yakiwemo ya askari hao aliowataja Mheshimiwa Mbunge, malipo hayo yaweze kufanyika na kuweza kuondoa kero hiyo ambayo imekuwa ikijitokeza kwa askari wetu wanaofanya kazi nzuri.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, napenda tu kuiambia Serikali kwamba Halmashauri ya Nsimbo ni moja ya Halmashauri katika nchi yetu ya Tanzania ambayo wananchi kwa kiwango cha chini kabisa wanapata maji safi na salama. Ni asilimia 34 tu. Sasa katika hii bajeti ya milioni 757, kuna miradi ya Kijiji cha Katesunga na Kijiji cha Nduwi ambayo itafadhiliwa na World Bank kama shilingi milioni 273: Je, ni lini fedha hizi zitapatikana ili miradi hii iweze kuanza?
Swali la pili, kutokana na majibu ya Serikali kwamba Mto Ugalla una maji machache kwa kipindi cha kiangazi, lakini wananchi wa pale wamekuwa wakitumia mto ule kwa ajili ya maji kipindi chote na kuna mamba ambao wanahatarisha sana maisha yao: Je, kwa nini Serikali wakati mpango wa muda mrefu; maji kutoa Ziwa Tanganyika ukiwa unafanyika, isitenge fedha ili wananchi wa Kata ya Ugalla na jirani ya Litapunga waweze kupata maji kutoka Mto Ugalla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza kwamba lini fedha zitapatikana; mpango wa upatikanaji wa fedha ni katika mwaka huu wa fedha katika bajeti hii. Ndio maana juzi hapa katika Maswali kwa Waziri Mkuu siku ya Alhamisi, Waziri Mkuu aliongelea suala zima la mtiririko wa fedha na akalihakikishia Bunge hili kwamba kipindi siyo kirefu sana tutaanza kuziona fedha katika Halmashauri zetu; fedha za maendeleo na fedha za OC. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tuwe na imani kwamba katika mchakato huu wa sasa hivi kabla muda haujapita sana, bajeti hizi zitaanza kutoka ili mradi iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuhusu Mto Ugalla kwamba kwa nini usitumike kwa sasa, kwa sababu mpango uliokuwepo ni wa muda mrefu? Naomba nikiri wazi kwamba Mheshimiwa Richard Mbogo ni Mbunge ambaye nilikuwa naye Jimboni kwake Nsimbo na miongoni mwa miradi tuliyoikagua ni miradi ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri wazi kwamba nilivyotembelea Jimbo la Nsimbo, ni kweli shida ya maji imekuwa ni kubwa sana. Kwa hiyo, nadhani hili ni wazo jema. Tutalichukua lakini tutawashirikisha na wenzetu kule katika Halmashauri na katika Mkoa, kuona kama ule mradi mkubwa kutoka Ziwa Tanganyika, huenda una gharama kubwa sana, tujue ni kiasi gani, tuweze kuja na mpango mwingine mbadala kusaidia katika Kata hizi ili tusisubiri muda mrefu sana miaka miwili, mitatu au minne kwa wananchi kuendelea kupata shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Richard Mbogo kwamba jambo hili sasa tutalichukua, tuone ni jinsi gani tutafanya ili kama katika hizo Kata mbili kuna mradi mwingine mbadala tuweze kuufanya. Nadhani jambo hili ni jambo shirikishi sana kwetu Serikali na Halmashauri ya Wilaya. Tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua anafuatilia sana ili wananchi katika zile kata mbili wapate fursa ya maendeleo ya maji.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Tunaipongeza Serikali kwa kukusanya kodi kwa kiwango ambacho ni cha juu sana, lakini wafanyabiashara wanatakiwa wajikisie makisio yao na ndio walipe kodi kutokana na vipengele ambavyo wameweka kwenye makisio.
Je, Serikali ina kauli gani juu ya malalamiko yaliyoko sasa hivi kwamba watumishi wa TRA wanakisia zaidi ya yale makisio ambayo wao ndio wanatarajia kufanya mauzo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko hayo kuhusu watumishi wetu wa TRA na tumekuwa tukifanya vikao kuhusu suala hili. Naomba kuliharifu Bunge lako tukufu kwamba pia
kumekuwa na tatizo la wafanyabiashara zetu kuleta taarifa ambazo sio sahihi ndio maana inapelekea kupata mvutano kati ya wafanyakazi wetu wa TRA na wafanyabiashara. Lakini kama Serikali tunasimamia uadilifu na kwa uhakika kabisa kinachotendeka ndani ya TRA ni kitu ambacho kinasimamiwa kwa maadili, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
MHE. RICHARD P.MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina swali dogo kuhusiana na makazi ya Katumba, yaliyokuwa makazi ya wakimbizi. Makazi haya ya Katumba yana barabara takribani nne ambazo zinaingia kwenye eneo hilo. Tuna barabara kuu ya kijiji cha Msaginya ambako kuna geti ambalo limekuwa ni usumbufu mkubwa kwa wananchi wa Katumba hususani kuanzia saa 12.00 jioni kutokana na sheria za wakimbizi. Sasa kwa kuwa wananchi wa eneo hilo takribani asilimia 90 wameshapewa uraia na wengine hawaishi ndani ya eneo hilo.
Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kwa lile geti la Msaginya kuendolewa au muda kuongezwa hata ikawa saa 24?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake tumelichukua na tutalitafakari tuone jinsi gani tutalifanyia kazi.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, naomba tu niipe taarifa Serikali kwamba hiyo fedha imetengwa sh.milioni 220 siyo sahihi ni fedha ambayo ipo kwenye maombi maalum, kwa sababu binafsi nilipitia bajeti ya Halmashauri yote, CDG tulipewa shilingi bilioni 1.24; allocation ya gari la wagonjwa haikuwepo kutokana na fedha kuwa ndogo na mahitaji ya Jimbo la Nsimbo kwa upande wa elimu, afya, na maeneo mengine kuwa na uhitaji zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo gari moja lililopo ni msaada ambao Jimbo la Nsimbo lilipata kutoka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), tunashukuru kwa mgao huo, kutokana na Jimbo kuwa na makazi ya wakimbizi kwenye Kata ya Katumba.
Je, Serikali haioni ule mpango tuliouleta wa maombi maalum wakachukua kile kipengele tu cha gari la wagonjwa, watuidhinishie ile Halmashauri yetu tuweze kupata gari hilo au laa, hatuna wasiwasi na utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali kuhusiana na kujali afya za wananchi wake kwa kutoa magari ya wagonjwa, kama hivi juzi Mheshimiwa Rais ametoa mgari matatu je, Serikali haioni tena kuna umuhimu wa Jimbo la Nsimbo na lenyewe likaangaliwa kupata gari la wagonjwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema kwamba kwanza tumewashukuru wenzetu wa Nsimbo na Mheshimiwa Mbunge naomba nikushukuru sana kwa kuonesha commitment yenu kwamba kulikuwa na hili hitaji ya gari. Ndiyo maana naomba niseme kwamba, kwa kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, Mheshimiwa Rais na Serikali yake amejipanga sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri umesuhudia hapa kwamba, juzi Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Ally Kessy Mohamed na wenzie Mheshimiwa Rais alitoa magari matatu personally pale, lakini kuna magari mengine 50 yaliweza kupelekwa katika maeneo mbalimbali. Hii yote ni jukumu la Serikali kuwahudumia wananchi. Hivyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Richard Mbogo kwamba tutaangalia kile kinachowezekana ili kulisaidia Jimbo lako ambalo liko mpakani kabisa ili suala hili la gari la wagonjwa na yale mambo mengine ya msingi likiwemo suala zima la ujenzi wa kituo cha afya, kufanya ukarabati katika eneo lako tutalifanya. Serikali ya Awamu ya Tano lengo kubwa ni kuwapunguzia adha akina mama na watoto.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia wafanyabiashara nchini iliweza kuahidi kugawa hizi mashine bure ili kurahisisha ufanyaji wa hii miamala. Je, zoezi hili limefanyika kwa kiwango gani na Serikali ina mpango gani wa kukamilisha?(Makofi)
Swali la pili dogo, sasa hivi tunafanya miamala kielektroniki kwa mfano kulipa gharama mbalimbali kama vile umeme, muda wa maongezi wa simu, ving’amuzi, kupitia kampuni za simu. Serikali itakubaliana na maelezo ya wafanyabiashara wanaoandaa mahesabu kwamba tulifanya malipo hayo kwa njia ya kimiamala?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza ni kweli Serikali iliahidi kugawa mashine hizi na kwa sasa tumefikia hatua nzuri, maana yake tulisitisha zoezi ili tufanye tathmini ya zile mashine tulizozigawa ili sasa kuweza kugundua changamoto na fursa nyingine katika utekelezaji wa suala hili na uthamini huu unakaribia kukamilika na muda siyo mrefu tutaendelea kuzigawa mashine hizi kwa wafanyabiashara wote ambao wako registered kwa ajili ya VAT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malipo ya kielektroniki ni sahihi yanafanyika katika miamala ya simu kulipia malipo mbalimbali na sisi tunashirikiana na tayari tumeisha saini Memorandum of Understanding at TCRA ili malipo yote yanayofanyika kupitia simu au e-payment yoyote ile tuweze kui-truck na kuhakikisha document zote na kumbukumbu zote zinaweza kupatikana kwa ajili ya kufanya uthamini kwa ajili ya kodi. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu imerithi Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizaraya Afya. Je, kwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Msaginya kilichoko Jimbo la Nsimbo, Mkoa wa Katavi, kuna mkandarasi miaka miwili amesimama kazi anaidai Serikali. Je, Serikali ina mpango gani wa kumlipa ili kukamilisha ukarabati wa majengo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkandarasi anadai, kimsingi kama ambavyo mnafahamu vyuo hivi vimeletwa kwenye Wizara yetu katika kipindi cha mwaka huu wa fedha unaoishia. Tunachofanya ni kwanza kuvitembelea na kuweza kuviangalia viko katika hali gani, kama kuna Mkandarasi alikuwa anafanya kazi eneo hilo na hakulipwa, Wizara tunao wajibu wa kumlipa lakini baada ya kufanya uhakiki na kujua kwamba kazi aliyoifanya inafanana na uhalisia na aweze kulipwa kwa kadri ya kazi yake.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Badala ya kuwa na fao la kupoteza ajira, kwa nini Serikali isilete sheria na kuibadilisha katika mafao ya mtu apewe angalau theluthi moja ya mafao yake baada ya kuwa amepoteza ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirejee tu maneno yangu ambayo nimeyasema pale awali katika jibu la msingi ya kwamba Serikali tutaleta mapendekezo yetu na Bunge hili litakuwa na nafasi ya kuweza kutushauri vema. Mimi nafikiri katika hali hii ambayo tumefikia hivi sasa, Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie na msubiri muone mapendekezo ya Serikali na baada ya hapo mtatushauri tuone namna bora ya kuweza kulifanya jambo hili tuondoe matatizo kwa wafanyakazi wetu. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Pamoja na majibu ya Serikali, ningependa niikumbushe Serikali kwamba wakati Halmashauri ya Wilaya Mpanda inafanya mpango wa matumizi bora ya ardhi ilizingatia mahitaji ya wananchi pamoja na maendeleo yao kwa wakati huo, kwa sasa hivi tunavyozungumza Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi idadi yake ya wananchi imeongezeka. Haya matangazo ya Serikali, Tangazo Na. 447 ya mwaka 1954 Na. 296 ya mwaka 1949 hayaendani na uhalisia na hali ilivyo chini kutokana na ramani hizi kuidhinishwa na Wizara ya Ardhi mwaka 2008 na zilianza kuidhinishwa na ngazi ya Mkoa mpaka na Wizara ya Ardhi kwa Kamishna wa Upimaji na Ramani. Kwa sasa hivi tunaenda kwenye nchi ya viwanda na maeneo mengi yanahitaji wakulima kwa ajili ya kulima mazao mbalimbali na Mkoa wa Katavi tuna mkakati wa kuanzisha zao la korosho. Kulingana na matangazo ya Serikali yanatofautiana na ramani zilivyo, uhalisia na mahitaji ya wananchi. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari hii Kamati ya Ushauri ya Taifa juu ya Misitu iambatane na Mbunge wa Jimbo la Nsimbo baada ya Mkutano huu wa Tisa kwenda kuangalia hali halisi ili waweze kumshauri Waziri na waweze kubadilisha mipaka kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Misitu ya mwaka 2002?
Swali la pili, kutokana na uhitaji mkubwa wananchi kwa maeneo haya na masika tayari imekwishaanza na tunajua Waziri wa Maliasili na Utalii kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 yeye ndiye mwenye dhamana ya kutoa kauli. Je, yuko tayari kuwaruhusu wananchi katika Kijiji cha Matandarani na Igongwe Kata ya Isalike waweze kupata maeneo ya kujihifadhi kwa kulima, wakati Kamati ya ushauri ikiendelea kupitia maeneo na kuweza kumshauri Waziri?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuko tayari baada ya Mkutano huu wa Tisa kumalizika Kamati ya Ushauri itapita maeneo yote ambayo yana migogoro nchi nzima ili iweze kumshauri Mheshimiwa Waziri na aweze kutoa maamuzi sahihi.
Swali la pili, kuhusu kulima ni kweli wananchi wale nimefika katika lile eneo wana matatizo mengi, lakini ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tulipokaa na Mheshimiwa DC pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri walikubali kwamba wametenga eneo la ekari zaidi ya 700 ambalo sasa linatolewa kwa wananchi wale ili waweze kuendelea na hizo shughuli. Kwa hiyo, hatutaweza kuruhusu kwa sasa hivi waendelee na shughuli hizo kwa sababu tayari wameshaondolewa na ukiwaruhusu kupanda zao la korosho ambalo ni la muda mrefu mpaka lije lianze kuvunwa itakuwa ni muda mrefu sana, kwa hiyo tutakachokifanya ni kuwapeleka katika hayo maeneo ambayo tayari yameshatengwa na Serikali ili waendelee na shughuli zao zile ambazo zipo.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, kwanza niipongeze Serikali kwa mwaka wa fedha tuliopo kwa kuweza kupunguza hizo tozo 10 ambazo sasa zinaweza kusaidia kwa kiasi fulani wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi tozo zilizopunguzwa tozo tano zinahusiana na makampuni ambayo hayaja washawishi katika kuboresha bei ya ununuzi wa tumbaku, na tukizingatia kwamba wanaendelea kushusha kiwango cha kununua toka tani 60,000 mpaka tani 55,000 na imepelekea wakulima wanazalisha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na tumbaku ya ziada ambayo ilizalishwa na ikapelekea Serikali kuwa na maongezi na makampuni bei ya dola 1.25 kwa grade ya juu. Lakini kwa sasa hivi tunavyozungumza wananunua tumbaku hiyo mpaka senti 64 kwa kilo. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wakulima wa tumbaku wanafaidika katika suala la bei kuliko na matatizo ambayo yametokea mwaka jana na tumbaku imekuwa sasa hivi inanunuliwa kwenye grade ambayo iko ya chini kwa kukaa muda mrefu kupata unyevu nyevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Swali la pili, Chama cha Wakulima wa Tumbaku Mkoa wa Katavi (RATCO) kutokana na masawazisho ya bei ya pembejeo ilipelekea kuwa na madeni ya zaidi kudai vyama vingine/mikoa mingine zaidi ya dola 400,000 na ambazo kuna vyama vingine vimekufa na vingine bado viko hai.
Sasa Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Katavi ili waweze kulipwa madeni yao kutokana na masawazisho ya bei ya pembejeo ambayo ilitokana na usafirishaji wa hizo pembejeo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza na ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbogo kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana katika zao zima hili la tumbaku na jinsi wakulima wanavyopata shida katika eneo lake la Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ya (a) na (b) naomba nijibu; la kwanza naomba niseme tu kwamba kwa upande wa wakulima wa tumbaku zao la tumbaku, kunakuwa na makubaliano ya bei za kuzalisha kila mwaka, kwa mfano sasa hivi tuko katika mwaka wa 2018 unakuta kwamba tangu Septemba, 2017 wakulima hao walikuwa wameshajadiliana ni bei gani watazalisha kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mfano mwaka huu, tayari tutakapokuwa tunazalisha lile zao la tumbaku, tumeshajua ni shilingi ngapi wale wakulima watanunua. Lakini nikija katika swali lake la bei, kuhusu bei ya zao la tumbaku kwa maana amezungumzia dola 1.25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa wakulima wote wa tumbaku kwamba kwanza wazalishe tumbaku kwa kiwango cha ubora, lakini vilevile ninaomba ntoe siku saba kwa Mrajisi wangu kutokana na lile deni ambalo anasema wananchi wakulima wa Katavi wamekuwa wakiwadai kutokana na mambo ya WETCO hawajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema yale siyo madeni, wakulima wa tumbaku wana tabia ya kufidiana na kuchangiana katika zao la tumbaku bila kujali eneo, bila kujali umbali, bila kujali bei. Lakini kwa sababu ya Mheshimiwa Mbunge ameli-raise hili na mimi ninampa Mrajisi siku saba awe ameshashughulikia kuhakikisha kwamba wananchi wa Katavi wanapata haki yao ya malipo yao.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kwanza naomba niseme, mimi nikiwa ni Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, nina masikitiko makubwa sana kuhusiana na uongozi wa Wilaya na Mkoa kwamba katika kutekeleza majukumu yao, hawaangalii haki za msingi. Tarehe 24 wamefanya operation ya kuondoa watu kwenye Hifadhi ya Kijiji ambao walipewa na uongozi wa Kijiji kwa kuwachomea nyumba, mvua zinanyesha, wanakosa pa kulala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii imekuwa ni tofauti na kauli ya Mheshimiwa Makamu wa Rais aliyotoa mwaka 2016 kwamba endapo watu wako katika maeneo ya hifadhi, wanatakiwa watafutiwe maeneo mengine na ndiyo wapelekwe. Kutokana na hilo, naomba kuuliza, je, Wizara husika iko tayari kuwafuta machozi wananchi wa Kitongoji cha Kamini, Kaumba katika Kijiji cha Katambike, Kata ya Ugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ilitolewa taarifa hapa kwamba imeundwa tume ambayo inashirikisha Wizara karibu tatu kushughulikia kero za migogoro ya ardhi. Sasa tunaomba majibu ya hiyo tume, yamefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa ilifanya uchomaji wa nyumba kwa sababu hii taarifa kwetu sisi ni mpya, ni ngeni, naomba tulichukue hili kwanza kwa ujumla wake kwa sababu jambo hili maana yake ni haki za binadamu ambao saa nyingine wameathirika. Kwa hiyo, kama Ofisi ya TAMISEMI tunasema kwamba habari hii kwanza tumeipata, tutaifanyia kazi kwanza, lakini suala zima la ulipaji wa fidia kwa wale walioathirika kwa Wizara yenye dhamana kwa sababu jambo hili, sijajua, ni jambo mtambuka. Je, iliyohusika ni Wizara ya Maliasili na Utalii au Ofisi ya Rais - TAMISEMI?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema jambo hili kwanza lazima lifanyiwe tafiti ya kina kujua nini kilichojiri kule katika eneo hilo. Pia kuna suala zima la kikosi kazi kilichoundwa na Wizara takriban nne, je, kimefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kazi ile inaendelea hivi sasa, tukijua kwamba tuna changamoto kubwa sana nchini mwetu. Leo hii mikoa mbalimbali, ukiangalia Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani na karibu katika maeneo yote kuna tatizo hilo kubwa sana. Ninaamini kabisa kikosi hicho kinaendelea na kazi hiyo na pindi taarifa hiyo itakapokuwa imekamilika ambapo aliyehitaji jambo hilo lifanyike ni Waziri Mkuu mwenyewe, basi tutapata taarifa rasmi ya Kiserikali kuhusiana na jambo hili linavyoshughulikiwa katika maeneo mbalimbali, lakini kujua ukubwa wake maana yake tunataka kuokoa Taifa hili kwa sababu sasa hivi janga la mauaji limekuwa kubwa sana, na huu ndiyo suluhu ya jambo hili kwa sababu kila eneo sasa hivi lina shida kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Richard Mbogo naomba tuvute subira tu, taarifa hii ikikamilika itatolewa rasmi hapa katika Bunge letu.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu yake mazuri, lakini nilipenda tu kuongeza jibu kwa hoja ya msingi aliyokuwa ameuliza kwenye swali la nyongeza kwamba ile Kamati iliyoundwa mpaka sasa hivi imefanya kazi wapi na wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ile Kamati mpaka sasa imeshakwenda mikoa minne; imekwenda Geita, Kagera, Morogoro na Tabora. Wakimaliza hapo, wanaelekea Kaskazini. Kwa hiyo, ile Kamati tayari imeshaanza kazi yake, lakini pia sisi ndani ya Wizara tumeshaanza kazi hiyo katika kufuatilia. Ni juzi tu nilikuwa Kusini na Waziri wangu alikuwa Kaskazini. Kwa hiyo, tunaendelea na kazi hiyo.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nifanye masahihisho kidogo ni Kata ya Katumba siyo Mtumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maeneo ambayo ilikuwa ni makazi ya wakimbizi yalikuwa yanapata ufadhili wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) katika huduma mbalimbali za jamii ikiwemo elimu, maji na barabara. Ningependa kujua Serikali ina mpango gani wa kuhusisha UNHCR kwa kuwa makambi yanaenda kuvunjwa, msaada gani ambao watautoa ili kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo sasa hivi imekuwa ni hafifu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale awali kwamba maeneo haya uchaguzi bado haujafanyika, japo uchaguzi haujafanyika jukumu kubwa la Serikali ni kuhakikisha katika maeneo hayo, wanaendelea kupata huduma za kijamii kwa ufanisi kama kawaida. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI jambo hilo tunaliangalia kwa karibu zaidi na kwa kuanza changamoto yetu kubwa ni kuisukuma bajeti hii ambayo sasa hivi imepitishwa kuhakikisha kwamba Halmashauri hii inafanya uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni kuhakikisha kwamba, kwanza tunajua katika maeneo hayo huduma za kijamii nyingi zilikuwa zinatolewa na Shirika la Wakimbizi Duniani, sasa hivi ni jukumu la Serikali. Hili ni jukumu letu kubwa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapeana ushirikiano wa kutosha ili wananchi wa pale waweze kupata huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo miundombinu ya barabara, huduma ya elimu, huduma ya afya na ifike muda na wao wajione kwamba ni wananchi kama wananchi wengine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Asilimia 67 ya Watanzania wako kwenye ajra ya kilimo na kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuna mikopo inayotolewa na ndani ya Halmashauri tunatenga asilimia tano kwa ajili ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua upande wa Serikali ni lini watabadilisha hiyo sheria ili ukomo wa umri kwa vijana katika kukopa usiwepo kwa sababu, kumekuwa na changamoto, wengine wamefikia miaka 45 miaka 50, lakini bado wanahitaji mikopo, lakini wanakwamishwa na suala la umri. Ni lini Serikali itabadilisha hiyo sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kuhusu lini tutabadilisha umri, hili ni suala la kisera. Siwezi kulisema hapa moja kwa moja, lakini definition ya kijana si ya Tanzania peke yake ni definition ya kidunia na sisi tunakwenda katika definition ambayo inazungumzwa na ILO, lakini kama kuna mahitaji hayo nafikiri baadae, kupitia sera na mahitaji mbalimbali, jambo hilo linaweza likaangaliwa upya, lakini kwa sasa bado tunabaki kuwa na umri huo kuanzia miaka 15 mpaka 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uwezeshaji; kwenye uwezeshaji ukiacha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao ndio una-limit umri, mifuko mingine bado iko zaidi ya mifuko 19 ya uwezeshaji ambayo yenyewe haiangalii umri. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Mbunge uendelee tu kuwapa elimu wananchi waelewe mifuko mingine ya uwezeshaji ili waweze kuitumia kwa ajili ya kuweza kujiwezesha. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia wafanyabiashara nchini iliweza kuahidi kugawa hizi mashine bure ili kurahisisha ufanyaji wa hii miamala. Je, zoezi hili limefanyika kwa kiwango gani na Serikali ina mpango gani wa kukamilisha?(Makofi)
Swali la pili dogo, sasa hivi tunafanya miamala kielektroniki kwa mfano kulipa gharama mbalimbali kama vile umeme, muda wa maongezi wa simu, ving’amuzi, kupitia kampuni za simu. Serikali itakubaliana na maelezo ya wafanyabiashara wanaoandaa mahesabu kwamba tulifanya malipo hayo kwa njia ya kimiamala?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza ni kweli Serikali iliahidi kugawa mashine hizi na kwa sasa tumefikia hatua nzuri, maana yake tulisitisha zoezi ili tufanye tathmini ya zile mashine tulizozigawa ili sasa kuweza kugundua changamoto na fursa nyingine katika utekelezaji wa suala hili na uthamini huu unakaribia kukamilika na muda siyo mrefu tutaendelea kuzigawa mashine hizi kwa wafanyabiashara wote ambao wako registered kwa ajili ya VAT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malipo ya kielektroniki ni sahihi yanafanyika katika miamala ya simu kulipia malipo mbalimbali na sisi tunashirikiana na tayari tumeisha saini Memorandum of Understanding at TCRA ili malipo yote yanayofanyika kupitia simu au e-payment yoyote ile tuweze kui-truck na kuhakikisha document zote na kumbukumbu zote zinaweza kupatikana kwa ajili ya kufanya uthamini kwa ajili ya kodi. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika mapato yanayotokana na uwindaji katika hivi vitalu halmashauri zetu ambazo ziko na maeneo haya zinapata asilimia 25 ya mapato, lakini katika hiyo asilimia 25 ni baada ya kutoa zile gharama za uendeshaji. Sasa kumekuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa haya makusanyo na kiwango hiki kinachotolewa bado ni kidogo na ukizingatia kwamba halmashauri ndizo ambazo zinasimamia kwa ukaribu maeneo haya. Sasa je, Serikali iko tayari kuongeza kiwango toka asilimia 25 mpaka 30 ili tuweze kukidhi gharama za operesheni katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika majibu ya Serikali wameeleza namna bora za kudhibiti hizi nyara za Serikali na tunatambua juhudi ambazo Wizara imefanya kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama, kuboresha kanuni na kuvihusisha kwenye kulinda maliasili hizi za Serikali. Hata hivyo, kuna udhaifu waa kibinadamu, yaani watumishi katika hizi kampuni. Je, Serikali itafanya mkakati gani kuhakikisha kwamba watumishi wa hizi kampuni hawachangii katika udhaifu wa kupoteza nyara za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Richard Mbogo kwa swali zuri na kwa jinsi ambavyo amekuwa akifanya kazi katika kutetea wananchi wake wa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zinavyoelekeza ni kwamba 25% inayotokana na mapato yote ya uwindaji wa kitalii ndio yanakuwa-calculated na yanaenda kwenye halmashauri, si baada ya kutoa gharama. Hivi sasa tunafanya mapitio ya sheria zote zinazohusu uhifadhi na wanyamapori. Baada ya hizo sheria kukamilika kanuni husika pia zitapitiwa tutaangalia kama hilo walilopendekeza litawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu watumishi ambao wanajihusisha na upotevu wa nyara za Serikali; ni kwamba hivi sasa ofisi yangu tumeunda Kamati ndogo ambayo inapita katika maeneo mbalimbali kubaini makampuni pamoja na watumishi wa ofisi zetu, wale ambao wanakuwa wanahusika na upotevu wa nyara za Taifa. Baada ya Kamati hiyo kukamilisha na mapendekezo kuletwa, hatua stahiki zitachukuliwa kwa watumishi wote wa namna hiyo, kwa sababu tunataka mtumishi afanye kazi yake kwa weledi, kwa kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya kazi yake.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kanzidata zinatunzwa na hizi kampuni za simu na sio sisi wamiliki wa hizi kampuni na kwa kuwa inaweza ikatokea simu ikapotea au ikaibwa na kumbukumbu mtu asiwe nayo. Sasa je, Serikali iko tayari kupokea maelezo ambayo yatakuwa yameandikwa kwenye vocha ya malipo ambapo mfanyabiashara ameweka tu ile reference number, je Serikali itakuwa tayari kuikubali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tulivyoanzisha mifumo ya electronic devices (electronic signature device, electronic fiscal device na electronic tax register) wafanyabiashara wakubwa (large tax payers) walipewa bure kwa maana ya kwamba waliweza ku-claim kutoka kwenye uandaaji wa VAT return. Sasa kwa mpango huo ambao ulifanyika kwa wafanyabiashara wakubwa, je, Serikali haioni haja sasa ikatoa hizi EFD bure kwa wafanyabiashara wadogo au ikaweka ruzuku ambapo itawawezesha…
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwenye majibu yangu ya msingi nimesema kifungu cha 35(3) kinamtaka mlipa kodi mwenyewe kutunza kumbukumbu zake kwa miaka mitano mfululizo. Kifungu hiki kinaweka utaratibu wa kwamba unapokuja kukaguliwa na watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wanakutaka uwe na hizi kumbukumbu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe tu walipa kodi wetu wajitahidi kuwa na hizi kumbukumbu kama sheria inavyotuelekeza lakini kwa jitihada za Serikali yetu ya Awamu ya Tano makampuni yote ya simu yametakiwa kupitisha miamala yao katika kanzidata yetu pale Kinondoni. Kwa hiyo, kama mlipa kodi atakuwa amepoteza kumbukumbu zake ni rahisi zaidi kuzipata taarifa zake pale katika kituo chetu cha Kinondoni.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, napenda kulihakikisha Bunge lako tukufu kwamba ni sahihi tuligawa mashine hizi kwa wafanyabiashara hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam na sasa tunaandaa utaratibu wa kuwafikia wafanyabishara wetu wote, lakini sio kwa kuwapa bure kwa sababu hata wale wa mwanzo hawakupewa bure, kilichofanyika anapewa mashine ya EFD halafu anakatwa kwenye kodi yake ambayo alitakiwa kuilipa Serikalini.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea na mfumo huo na kuanzia tarehe 1 Julai, Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanza yenyewe kugawa mashine hizi badala ya kutumia mawakala ambao wametuingiza gharama zisizo za msingi kwa wafanyabiashara wetu na tuna uhakika tunapolichukua jambo hili hata gharama za mashine hizi zitakuwa ndogo kwa wafanyabiashara wetu.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Changamoto iliyopo Wilaya ya Kyela inafanana kabisa na Wilaya ya Mpanda katika barabara ya Stalike – Misunkumilo, bado wananchi wanadai fidia na ni miaka mitano sasa. Je, ni lini Serikali itawalpa fidia wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbogo anafuatilia sana juu ya wananchi hawa ambao wanastahili kulipwa au wana madai yao na amenipa barua ambayo inahusiana na madai haya.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba sheria inaangalia pande zote; inaangalia upande wa wale wahusika ambao wana madai yao lakini pia inatazama kwa sisi Serikali wakati tunafanya malipo ya madai ya wananchi. Kwa maana hiyo, malipo yote yanafanyika kwa kufuata sheria.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Sheria ya Barabara Namba 13 ya 2007, hasa section 16 inaonesha utaratibu unaotakiwa utumike kulipa fidia. Hii ni pamoja na kuitazama Sheria hii ya Utwaaji wa Ardhi (Land Acquisition Act), Sheria ya Ardhi yenyewe na Sheria ya Ardhi ya Vijiji pamoja na sheria nyingine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati tunaendelea kutazama uhalali wa fidia hizo baada ya hapo wananchi hawa wataweza kupata haki zao. Kwa hiyo, nimtoe hofu lakini niwatoe hofu wananchi wa Nsimbo kwamba suala lao liko mikononi mwetu na tunaendelea kulishughulikia, haki za watazipata.
MHE.RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mito inapeleka mpaka Mbuga ya Katavi lakini kwa mujibu wa sheria watu wote wana haki. Sasa niombe ni lini sasa Serikali itakamilisha kandarasi hiyo upembuzi yakinifu ili katika bajeti ya mwaka 2019/2020 tuweze kutengewa fedha kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna mradi wa umwagiliaji uliopo kwenye kata ya Ugala ambapo una miaka mingi haujakamilika na mifereji bado na unasimamia na Mamlaka ya Bonde makao makuu yaliyoko Mbeya. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha ili kukamilisha mradi huu ili uweze kutumika na wananchi katika uzalishaji na kuinua maeneo yao ya kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri na namna anavyofuatilia changamoto za wananchi wake. Kubwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji kutokana na changamoto hiyo katika umwagiliaji, tumeona haja sasa ya kufanya upembuzi wa haraka. Kubwa ambalo nataka nimhakikishie, tutafanya usimamizi wa haraka ili mwisho wa siku hili jambo liweze kukamilika na ujenzi ule uweze ujengwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la ukamilishaji wa mradi aliouelezea, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Wizara yetu ya Maji tumeainisha miradi ambayo haijakamilika. Tumeona tumekuwa na miradi zaidi ya 1,967 ambayo haijakamilika. Kwa hiyo, wajibu wetu ni kuhakikisha tunaikamilisha ili mwisho wa siku iwe na mchango mkubwa sana katika uchumi wetu wa kati. Tunajua kabisa umwagiliaji ni kilimo cha mbadala ambacho kina mchango mkubwa kabisa katika suala zima la uchumi kwa maana ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalisimamia hili jambo mradi wao ukamilike ili uweze kuwa na tija kwa wananchi wake. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Changamoto zilizopo maeneo ya Serengeti na kwingine, zinafanana kabisa na Mbuga yetu ya Katavi ambayo inakosa watalii kutokana na miundombinu mibovu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ndani ya Mbuga ya Katavi ili kuvutia watalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba tunayo hifadhi kubwa ya Katavi ambayo ina wanyama wa kila aina.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Setikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba kwanza tunaboresha miundombinu iliyopo ndani ya ile hifadhi ili tuweze kuwavutia watalii wengi kutoka maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ni kwa sababu ule uwanja wa Ndege wa Katavi umekuwa mzuri kabisa na tunaamini katika hizi jitihada ambazo Serikali imechukua za kuongeza ndege, basi safari za ndege zikianza kutumia uwanja ule wa Katavi basi ina maana watalii wataongezeka sana katika lile eneo na hivyo miundombinu ikiwa inapitika, watalii wengi sana wataweza kuvutiwa na kutembelea katika ile mbuga ya Katavi.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Changamoto zilizoko kwenye zao la tumbaku ni nyingi sana na kwa Mkoa wa Katavi Wilaya ya Mpanda Kampuni ya TLTC iliiandikia barua Bodi ya Tumbaku kwamba ina kusudio la kuacha kununua tumbaku katika Wilaya ya Mpanda. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili kwa sababu mpaka sasa wakulima hawana uhakika wa kuuza tumbaku yao kwa msimu ujao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zao la tumbaku mara nyingi wakulima wote wa tumbaku wanalima kilimo cha mkataba. Kampuni hizi ambazo zinaingia mikataba na wakulima wale kawaida ile mikataba huwa wanasaini kabla ya msimu kuanza. Niitake Kampuni ya TLTC kuhakikisha kwamba pamoja na wale wananchi wa Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ule mkataba wao kama unasema alitakiwa kununua kiwango hiki cha tumbaku, basi mkataba ule lazima uheshimiwe na lazima wanunue kiwango kile kinachotakiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi pamoja na majibu ambayo yametolewa na Serikali niishukuru kwamba Serikali imekuwa ikiongeza bajeti tulikuwa shilingi milioni 500, shilingi milioni 800 na mmefika shilingi bilioni 1.4. Lakini swali la msingi lilikuwa ni kwamba tunapandisha vipi kiwango ha upatikanaji maji safi na salama kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo na tupate angalau bilioni tatu.

Sasa je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuwa na mjadala na Mbunge pamoja na watendaji wake wa Wizara ili kuona namna gani kiwango kinaongezeka kutoka shilingi bulioni 1.4 angalau tuwe na reasonable amount ambayo itaweza kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya. Lakini kikubwa tunatambua kabisa maji ni uhai na jukumu la Wizara yetu ya Maji ni kuhakikisha watanzania na wana Nsimbo wanapata maji safi, salama na yenye kutosheleza. Sasa katika kuhakikisha tunalinda uhai wa wana Nsimbo sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kufanya mjadala na Mheshimiwa Mbunge nadhani baada ya Bunge hili tukutane tuweze kukutana na watendaji wetu ili tuweze kujadiliana ni namnaa gani tunaweza tukatatua tatizo la mji Nsimbo kwa haraka. Ahsante sana.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu ya Serikali, tunajua ongezeko la mapato. Tuna Halmashauri 185 lakini zinatofautiana kati ya Halmashauri na Halmashauri. Kwa hiyo, pamoja na ongezeko la kibajeti, bado Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imeathirika na mabadiliko ya Sheria hii. Sasa je, Serikali iko tayari kuongeza ruzuku toka hii ambayo tumeipata ya shilingi milioni 250 ambapo tumeweza kumalizia maboma ya shule mbalimbali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tuna changamoto pia upande wa huduma za kiafya. Kata ya Itenka pamoja na Kata ya Ugara ziko mbali sana na upatikanaji wa huduma: Je, Serikali iko tayari kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya katika Kata hizi mbili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali iko tayari kuendelea kukamilisha maboma ya afya na elimu na ndiyo maana Mwezi wa Pili tumepeleka fedha zaidi ya shilingi bilioni 29.9 katika Majimbo mbalimbali likiwepo na hili la Nsimbo kukamilisha maboma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimesema, Serikali itaendelea kupeleka fedha ya ruzuku ya miradi ya maendeleo mbalimbali kadri ambavyo fedha itapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anaulizia kuwa na vituo vya afya. Ni nia njema ya Serikali kuendelea kuimarisha huduma za afya na tumefanya hivyo, vimejengwa vituo 352. Kwenye bajeti hii ambayo tunaendelea na mjadala kwenye Bunge lako Tukufu tunavyo vituo 52 vingine, hospitali 27, ukiongeza zile 67 zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufanya kazi hii ya kutoa huduma ya afya kwa wananchi wake kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali juu ya majibu ya tumbaku, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, katika jibu la (b) kuhusiana na tozo (Produce cess) kwa kweli Serikali ilipunguza kutoka asilimia tatu mpaka tano. Ukiangalia discount hii ilikuwa ni karibuni asilimia 40 na mkulima hajafaidika. Kuhusiana na tathmini, binafsi kwenye halmashauri zetu tumekwishafanya tathmini mapato yameshuka. Sasa Je, Serikali iko tayari katika mabadiliko ya sheria yanayoletwa sasa hivi Mwezi Juni kwenye Finance Bill kurudisha hii produce cess kuwa asilimia tano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili dogo; Kampuni ya Premium ambayo inanunua tumbaku nchini ikiwemo Katavi, Chunya pamoja na Ruvuma mpaka sasa haijalipa tozo za halmashauri pamoja na kwenye vyama vya msingi kwa sababu kwamba wana madai yao Serikalini ya marejesho ya kodi la ongezeko la thamani (VAT refund) na tangu mwaka jana tunafuatilia na mpaka sasa Serikali haijailipa hii kampuni na wanadai takribani bilioni 12. Sasa Je, Serikali haioni kwamba kutolipwa kwa wakati fedha hizi inachelewesha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbogo kwa namna anavyofuatilia zao la tumbaku kwa manufaa ya wakulima wa tumbaku nchini.

Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbogo anauliza kama tuko tayari kurudisha produce cess kutoka asilimia tatu kurudi kwenye asilimia tano. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Mheshimiwa Mbogo ana hoja nzuri lakini kama nilivyojibu ni mapema kwa sababu tuko kwenye fiscal year ya kwanza katika utekelezaji wa hii sheria na Serikali tumesema hatutasita baada ya kufanya tathmini na kuona kuna haja ya kurudisha hiyo produce cess. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira angalau twende kwenye fiscal year kama mbili, tatu halafu baada ya hapo tutafanya tathmini na kuona namna ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mbogo, anasema kutolipwa kwa VAT refunds kwa muda kunaathiri malipo kwenda kwenye halmashauri na vyama vya ushirika. Kwa vile suala hili linahusu VAT claims basi nimwahidi Mheshimiwa Mbogo tutakaa na wenzetu Wizara ya Fedha na kuangalia namna ya ku-expedites ili Kamouni hii iweze kulipa madeni ya halmashauri na AMCOS.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, tunajua Muungano wa Kikanda au wa Kimataifa kama vile SADC una faida kubwa nzuri sana kwa vijana hususan kwenye kupata ujuzi pamoja na mafunzo. Je, huu mkutano uliopita hivi karibuni nini vijana watafaidika na SADC?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuna maazimio gani ambayo tayari yaliyopo aidha kwenye EU umoja mwingine wa Kimataifa ambayo yatasaidia vijana zaidi kwenye suala lile la mikopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, kwanza kwenye Mkutano wa SADC uliomalizika hivi karibuni tuchukue fursa hii kuwashukuru sana Wakuu wote wa nchi pamoja na Mwenyekiti wetu wa SADC kwa azma na kauli yao thabiti ya kuhakikisha kwamba vijana wanashiriki katiak sekta ya uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano uliomalizika agenda kubwa ilikuwa ni kuwashirikisha vijana katika uchumi wa viwanda na kwa Tanzania vijana walipata fursa ya kutembelea na kuona fursa mbalimbali na kujifunza kupitia Mataifa mengine na tunaamini kabisa kupitia Mkutano huu liko jambo ambalo limeongezeka katika fikra za vijana hasa katika kwenda kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda. Kwa hiyo ni Mkutano ambao ulikuwa na tija na vijana wamehamasika na tunaamini kutokea hapo vijana wengi zaidi watashiriki katika uchumi wa viwanda, moja kwa moja au isivyo moja kwa moja.

Mhehsimiwa Spika, swali lake la pili alitaka kujua Maazimio ya Kikanda kupitia AU. Katika Azimio la 601 la mwaka 2017 katika moja ya nguzo iliyosemwa ni uwezeshwaji wa vijana na Serikali ya Tanzania tunayafanya hayo kupitia Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji wa Vijana na kuwajengea vijana uwezo hasa katika kuwajengea ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali ya Awamu ya Tano inayafanya hayo kuzingatia maamuzi yaliyofikiwa na Wakuu wa nchi katika Umoja wa Afrika.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini pia naomba nipongeze Serikali wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais mwaka jana mwezi wa kumi Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Ummy aliweza kukagua Hospitali tunayojenga ya Mkoa na kuongeza fedha za ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa kupata majibu ya Serikali je, ni lini tena ujenzi wa Hospitali yetu ya Mkoa wataongeza fedha ili kuweza kuikamilisha kwa wakati na huduma ziweze kupatikana kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ili kuipunguzia mzigo Hospitali yetu ya Mkoa ambayo inajengwa na kwa msingi tunahitaji Ujenzi wa Vituo vya Afya viongezeke kwa maeneo ya mbali ili kusogeza huduma kwa wananchi wetu hususani Kata ya Ugala ambayo ni km 80 kutoka Mpanda Mjini.

Je, ni lini Serikali tena itatuongezea fedha ili tuweze kufanya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Ugala? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mbogo Mbunge wa Nsimbo, swali la kwanza ni lini tutakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa!

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie Mheshimiwa Mbogo lakini na Wabunge wote wa kutoka Katavi mwezi huu tumeongeza shilingi bilioni nukta moja kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Katavi na timu yangu ilikuwa kule Katavi Mpanda na ni matarajio yetu kabla ya mwezi wa sita tutakuwa tumemaliza Jengo la OPD, Jengo la Maternity pamoja na maabara ili tuweze kutoa huduma kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu ujenzi wa Kituo cha Afya ni Sera yetu ya Afya kuhakikisha kwamba tunajenga Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali za Halmashauri. Lakini tunataka kubadilisha kidogo Sera, Sera ya Afya ambayo tunaiandika sasa hivi tunasema Serikali itajenga Miundombinu ya kutoa huduma za Afya katika ngazi zote kwa kuzingatia vigezo vikubwa vitatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kigezo cha kwanza Jiografia ya eneo husika, kigezo cha pili, idadi ya watu na kigezo cha tatu ni mzigo wa magonjwa katika eneo husika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbogo nakubaliana na wewe Kituo cha Afya kwa sababu eneo lako liko mbali na Kituo cha Afya ambacho kipo kwa hiyo tutakuweka katika vipaumbele vyetu kuhakikisha tunajenga Kituo cha Afya kwa kushirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa kuangalia na kutoa ruzuku kwenye Halmashauri zetu, hususan ambazo zina vipato vya chini. Swali la kwanza; kwa kiwango hiki ambacho Serikali imetoa, bado kulingana na uhitaji kwenye Halmshauri ya Wilaya ya Nsimbo ni kidogo. Je, wako tayari kutuongezea ili tuweze kukidhi ukamilishaji wa maboma na uhitajikwenye upande wa elimu pamoja na afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika upande wa mahitaji haya je, Naibu Waziri yupo tayari kurejea ziara yake atembelee Halmashauri ya Nsimbo kujionea na aweze kuona namna bora ya kuiwezesha Halmashauri ya Nsimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nipokee pongezi hizi za Mheshimiwa Mbunge, na hii pia imezingatia sana kwamba amekuwa akilisemea sana eneo lake hili ili kuweza kuondoa kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza kama Serikali ipo tayari kuongeza fedha. Naomba nimhakikishie yeye na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali nia yake kubwa ni kuhakikisha kwamba inaondoa changamoto ya miundombinu ya elimu na afya na kazi hiyo itakuwa inaendelea kufanyika kadri ya upatikanaji wa fedha kwa Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ananiuliza kama nitarejea ziara katika eneo hili. Ni kweli nimeshapanga ziara karibu mara mbili ikikaribia kwenda kule eneo la Katavi na Rukwa, ziara hii imekuwa ikiahirishwa. Naomba nimhakikishie ratiba nimeshaipanga, tukiahirisha Bunge hili Mheshimiwa Mbunge nitakuja Katavi na Rukwa na ntatembelea majimbo yote ya ukanda ule. Ahsante sana.