Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe (14 total)

MHE.DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Kata ya Mamba, Majimoto, Chamalema na Mwamapuli zitapatiwa maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua tatizo la maji katika Kata ya Mamba, Serikali imetenga shilingi milioni 24.2 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu katika Kijiji cha Ntaswa ambacho hakina maji, kati ya vijiji nane vilivyopo. Aidha, kwenye Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji Awamu ya Pili, zimetengwa shilingi milioni 650 ili kupanua mradi mserereko kutoka Kilida hadi Ntaswa na Kisansa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo havijapata huduma ya maji katika Kata ya Majimoto ni Luchima na Ikulwe ambavyo vimetengewa shilingi milioni 48.4 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya kuchimba visima virefu katika kila kijiji. Vijiji vilivyobaki vinapata maji kupitia mradi uliogharimu shilingi milioni 526,8 na umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, zimetengwa milioni 48.4 kwa ajili ya kuchimba visima viwili katika Vijiji vya Chamalendi na Mkwajuni, vilivyopo Kata ya Chamalendi ili kutatua tatizo la maji kwa wananchi maeneo hayo. Katika Kata ya Mwamapuli Vijiji vyenye matatizo ya maji ni Mwamapuli Ukigwaminzi na Lunguya ambavyo vimetengewa shilingi milioni 77.4 ambapo vitachimbwa visima virefu vitatu vya maji.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Halmashauri ya Kavuu ni mpya na mapato yake yako chini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa inawapatia wananchi mawasiliano ya barabara japo kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mtandao wa barabara za changarawe katika Halmashauri mpya ya Mpingwe ni kilomita 37.7, sawa na asilimia 19 ikilinganishwa na kilomita 202.5 kwa Wilaya nzima. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imepanga kufanya matengenezo ya kilometa 42 kwa kiwango cha changarawe ambapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo ni shilingi milioni 246.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017, ni kufanya matengenezo ya kilometa nyingine 49.8 kwa kiwango cha changarawe pamoja na matengenezo ya sehemu korofi na matengenezo ya kawaida katika barabara za Halmashauri. Jumla ya shilingi milioni 324 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali ya Watu wa Jamhuri ya China wasichangie huduma za afya kwa wananchi wanaopata ajali zinazotokana na waendesha bodaboda?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO ajilibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa kumekuwepo na ongezeko la ajali nyingi za bodoboda ambazo zinaongeza gharama za matibabu. Ongezeko la ajali hizi limekuwa likichangiwa na sababu mbali mbali ikiwemo vifaa hivi kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, madereva kukosa umakini, ulevi, uzoefu na miundombinu chakavu.
Mheshimiwa Spika, vyombo hivi vinapoingia nchini kuna mamlaka mbalimbali ambazo zinasimamia uingiaji wake. Mamlaka hizi ni pamoja na ile ya udhibiti wa ubora yaani TBS na Mamlaka ya Mapato (TRA) ambapo hulipiwa ushuru kabla havijaingia sokoni.
Aidha, kabla mtumiaji hajaanza kutumia kwa biashara inamlazimu kukata leseni ambayo pia hukusanywa na Serikali. Sanjari na hilo ni vyema kufahamu kwamba pikipiki zinazoingizwa nchini zinatoka nchi mbalimbali na si China peke yake.
Mheshimiwa Spika, katika Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo ninatarajia kuiwasilisha hapa Bungeni, nimependekeza kuwa kila mwananchi awe na kadi ya bima ya afya ili e ndapo atapata ajali aweze kupata matibabu bila kiwazo chochote.
Mheshimiwa Spika, hata kama watu wote watakuwa na bima, suala hili la ajali za bodaboda halikubaliki na halivumiliki. Ninaomba wote tukemee vitendo vya uendeshaji mbaya wa bodaboda ili kulinda uhai wa wananchi wetu. Aidha, ninaliomba Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani kuendelea kulisimamia suala hili ili kupunguza ajali za barabarani zinazoweza kuepukika.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhana ya ugatuaji madaraka kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo, hususan katika sekta za afya na elimu:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu mfumo huo kutokuwa na tija endelevu katika sekta hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dhana ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi (Decentralisation by Devolution) inatokana na Ibara ya 145 na Ibara 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Madhumuni ya kupeleka madaraka kwa umma yakiwemo madaraka ya kisiasa, kifedha na kiutawala ni kusogeza madaraka ya kufanya maamuzi kwa wananchi ili kuboresha, kuimarisha utoaji wa huduma kulingana na matakwa yao ya kuboresha maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kupata mafanikio katika sekta ya afya na elimu kwa kuwashirikisha wananchi katika kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi na Sekondari (MMEM na MMES) na Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM). Kupitia utekelezaji wa hiyo fursa ya elimu ya msingi na sekondari zimeweza kuongezeka kutokana na ujenzi wa miundombinu ya elimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Vilevile huduma za afya zimeimarishwa kwa kuratibiwa kwa karibu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ugatuaji wa madaraka kwa wananchi bado ni dhana muhimu kwa nchi yetu kwani ndio mfumo unaotoa fursa kwa wananchi kuweza kushiriki katika maamuzi na utekelezaji wa vipaumbele vyao katika mchakato mzima wa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda ilikuwa ya bweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, lakini sasa imekuwa ya kidato cha tano na sita tu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuirejesha shule hiyo kama ilivyokuwa awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda ilisajiliwa kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita pekee ili kukidhi malengo ya kuwa na shule za kutosha za Kitaifa katika Mkoa wa Katavi. Shule hii ni miongoni mwa shule saba za sekondari zenye kidato cha tano na sita kati ya shule 38 za sekondari zilizopo Mkoani Katavi. Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa shule za sekondari za kutwa za kidato cha kwanza hadi cha nne, Serikali imeona umuhimu wa kuongeza shule ya kidato cha tano na sita ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mpanda.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Tarafa inakuwa na sekondari ya kidato cha tano na sita. Serikali inatambua nia njema ya Mheshimiwa Mbunge kwa watoto wa eneo hilo. Hata hivyo, kama kuna ulazima wa kufanya hivyo, inahitajika maombi yafanyike kupitia taratibu husika za usajili wa shule. Serikali inaendelea kuboresha shule za kata zilizoko Mkoani Katavi ili kupunguza msongamano na kutoa elimu bora.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Bunge lilipitisha tozo ya kodi ya majengo ya shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na shilingi 50,000 kwa nyumba za ghorofa, lakini Manispaa na Halmashauri mbalimbali nchini zimekuwa zikitoza kodi hiyo zadi ya kiasi hicho.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, kifungu cha 64 kimebainisha kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania itakusanya kodi ya majengo kwenye maeneo ya Majiji, Mji na Miji Midogo yote nchini, badala ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majengo mengi hayajafanyiwa uthamini, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya uamuzi wa kuweka kiwango maalum cha shilingi 10,000 kwa majengo ya kawaida na shilingi 50,000 kwa majengo ya ghorofa kwa kila ghorofa. Viwango hivi ni vya mpito wakati Serikali inakamilisha zoezi la uthamini kwa majengo yote yanayostahili kulipiwa kodi ya majengo.
Aidha, majengo yote yaliyofanyiwa uthamini yanalipiwa viwango stahiki kulingana na uthamini. Kwa hiyo, mwenye nyumba yeyote akiona amepelekewa bili ya zaidi ya shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na zaidi ya shilingi 50,000 kwa nyumba ya ghorofa afahamu kwamba nyumba yake imefanyiwa uthamini.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Hitaji la kuni limekuwa kubwa kwa matumizi kama nishati ya kupikia na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira:-
Je, Serikali itawezesha vipi wananchi kupata nishati mbadala kwa matumizi ya kupikia majumbani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha Uendelezaji na Usambazaji wa Teknolojia za Kilimo Vijijini (CAMARTEC) inaendelea na ujenzi wa mitambo ya bayogesi nchini kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine majumbani, taasisi za Serikali zikiwemo shule, hospitali na Magereza. Hadi sasa mitambo ya bayogesi iliyojengwa inafikia 20,000. Lengo la kituo ni kujenga jumla ya mitambo 22,000 kwa nchi nzima ifikapo mwaka 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009 Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ilianza kutekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kupitia mradi wa mfano (Pilot Project) kwa ajili ya kupikia majumbani. Hadi sasa hoteli tatu, gereza moja, nyumba 70 na viwanda 36 vinatumia gesi asilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, TPDC imekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Miradi ya usambazaji wa gesi asili katika mikoa hiyo utaanza mwaka 2018 na kukamilika mwaka wa 2020/2021 kwa kuwafikishia gesi wateja wapatao 50,410. Miradi hii itagharimu jumla ya dola za Marekani milioni 126.959.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Julai, 2017, Serikali kupitia TPDC itaanza kutekeleza mpango wa kupeleka gesi majumbani katika mikoa mingine ya Tanzania Bara ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma hii.
MHE. ANDREW J. CHENGE (K.n.y. MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati Bungeni ili ziweze kupitiwa upya ziendane na wakati uliopo hasa zikiwemo Sheria za Usalama Barabarani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinakidhi mahitaji ya wakati, Serikali imekuwa ikifanya mapitio ya sheria ya kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania iliyopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Spika, Tume hii imekuwa ikifanya mapitio na tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa ni msingi wa marekebisho ya sheria au kutungwa kwa sheria mpya hapa nchini. Kazi ya mapitio ya sheria ni endelevu na Serikali itaendelea kuwasilisha Bungeni miswada ya sheria ambayo inalenga kurekebisha sheria za nchi au kutunga sheria mpya ili kukidhi matakwa ya wakati.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiwahimiza wananchi wajiunge kwenye vikundi ili waweze kupata mikopo ya kuwasaidia kuendesha shughuli zao:-
Je, Serikali haoni kuwa sharti hilo linawakosesha fursa baadhi ya wananchi ambao pengine wanahitaji huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wake Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017 ambayo itawezesha kuchochea maendeleo stahiki na ubunifu wa huduma ndogo za kifedha ili kukidhi mahitaji halisi ya wananchi wa kipato cha chini na hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini. Pia Serikali inalenga kutatua changamoto inayowapata wananchi juu ya mtazamo wa mifumo ya ukopeshaji kwa vikundi au mtu mmoja mmoja. Sera hii itapelekea kutungwa kwa sheria itakayoweka utaratibu mzuri wa huduma ndogo ya fedha.
Mheshimiwa Spika, utoaji mikopo kwa kutumia vikundi ni mfumo ambao hutumika kutoa mikopo midogo midogo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali. Mfumo huu hutumika kutoa mikopo kwa watu ambao uwezo wao wa kiuchumi ni mdogo, hasa kwa wakopaji ambao hawana dhamana. Pia mfumo huu husaidia kuweka dhamana mbadala ya usalama wa mikopo inayotolewa kwa kuwafanya wanakikundi kuwa na uwajibikaji wa pamoja juu ya mkopo huo.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu umekuwa ukitumiwa na taasisi nyingi za kifedha ambazo zimekuwa zikitoa mikopo kwa watu wenye kipato cha chini ikiwepo mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inayomilikiwa na Serikali kutokana na faida yake katika kuhakikisha kuwa usalama wa mikopo hasa kwa wakopaji wasio na dhamana. Mfumo huu pia husaidia kurahisisha ufuatiliaji wa kuwajengea uwezo wanakikundi kupitia mafunzo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mfumo huu kutumika lakini ni pia mwananchi mmoja mmoja wamepatiwa fursa za uwezeshaji kupitia benki na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji kama vile Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali, Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi na Mfuko wa Wajasiriamali wadogo wadogo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Katika Bunge lililopita la 2010 – 2015 Serikali iliongelea kuhusu mpango wa kuwekeza umeme unaotumia chemchemi ya maji ya moto yanayopatikana katika Kata ta Maji Moto:-
a) Je, mpango huo umefikia wapi?
b) Je, ni lini sasa Jimbo la Kavuu litapata umeme kwa maendeleo ya wananchi wa eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi ni moja ya mikoa inayopitiwa na Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, hivyo kuwepo na uwezekano wa kuwa na hifadhi kubwa ya joto ardhi. Serikali inaendelea kufanya tathmini ya rasilimali ya nishati ya joto ardhi ili kujiridhisha na uwepo wa rasilimali ya kutosha kabla ya kuchoronga visima vya majaribio. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali kupitia Tanzania Geothermal Development Company imepanga kufanya utafiti wa kina katika maeneo zaidi ya 50 yenye viashiria vya joto ardhi likiwemo eneo la Maji Moto.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Jimbo la Kavuu vya Kibaoni, Usevya, Ilalangulu na Manga, vinapata umeme kutoka Sumbawanga, Mkoani Rukwa kupitia Mji wa Namanyere, Wilayani Nkasi. Aidha, vijiji vingine vya Jimbo la Kavuu ikiwa ni pamoja na Maji Moto, Mbende, Chamalangi, Mkwajuni, Ikuba, Mamba na Kasansa vitapatiwa umeme kupitia mzunguko wa kwanza wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupatikana kwa suluhisho la kudumu la umeme katika Jimbo la Kavuu, Serikali imeanza hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme wa gridi, kV 400 kutoka Mbeya – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma hadi Nyakanazi. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza Machi, 2019 na kukamilika mwaka 2021. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza-:-

Je, Serikali itakamilisha lini ujenzi wa barabara ya kutoka Kibaoni kupitia Majimoto mpaka Inyonga kwa kiwango cha lami ukizingatia kuwa daraja la Kavuu limekwishakamilika ili barabara hiyo ianze kutumika?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:--

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibaoni-Majimoto- Inyonga ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 152 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi. Barabara hii ni ya changarawe na inapitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza zabuni kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Zabuni kwa ajili ya kazi hiyo zinatarajiwa kufunguliwa taehe 11 Februari, 2019.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali imeanza kujenga sehemu ya barabara hii kwa awamu kwa kiwango cha lami kuanzia Mji wa Inyonga ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya kilometa 1.7 zilijengwa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 mkandarasi wa kujenga kilometa 2.5 amepatikana na yupo katika hatua za maandalizi ya kuleta vifaa na wataalam katika eneo la mradi ili kuanza kazi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itachukua hatua za kimkakati kuhakikisha kwamba migogoro kati ya wafugaji na wananchi wanaoishi pembezoni mwa mbuga za wanyama inakwisha kabisa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuwepo kwa migogoro mingi baina ya wafugaji na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa agizo la kutoviondoa vijiji 396 vilivyoainishwa kuwa na migogoro katika maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mheshimiwa Rais kutoa agizo hilo kamati maalum iliundwa kwa lengo la kumshauri juu ya namna bora ya kutekeleza agizo hilo. Kamati hiyo iliongozwa na Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara zingine zilizohusika ilikuwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Ofisi ya Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Kilimo na Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imekamilisha utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo ya Serikali kuhusu suala hilo yatatolewa na kwa wananchi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-

Je, Serikali inasema nini juu ya ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu na mbolea ambazo huwasababishia wakulima hasara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, upungufu wa mbolea nchini umechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupatikana kwa mahitaji kutoka kwa makampuni ya mbolea hapa nchini; kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutokana na bei nzuri ya mazao kwa msimu wa 2018/2019; kuongezeka kwa kilimo cha kibiashara baada ya Serikali kuwahakikishia wakulima kuwa haitafunga mipaka na kuingilia upangaji wa bei za mazao ya kilimo; na kuwepo kwa mvua nyingi ambazo zimesababisha kuongezeka kwa viwango vya matumizi ya mbolea kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2019/2020 upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbegu bora hadi kufikia Desemba, 2019 ni tani 71,155.13. Kati ya hizo, tani 58,509.9 zimezalishwa nchini, tani 5,175.79 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 7,469.44 ni bakaa ya msimu 2018/2019. Aidha, upatikanaji wa mbolea hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020 ni tani 410,499 zikijumuisha tani 92,328 za UREA na tani 84,311 za DAP. Kati ya hizo, tani 225,417 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 16,685 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 168,397 ni bakaa ya msimu wa 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa upungufu wa pembejeo nchini, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wingi ili kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi. Hatua hizo ni pamoja na kutoa vibali kwa wasambazaji wakubwa wa mbolea kuagiza nje ya mfumo wa BPS kutokana na mahitaji ya wakulima na soko ambapo tani 200,000 zimeagizwa na hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020; kutoa kibali cha kuagiza tani 45,000 kwa Umoja wa wasambazaji na wauzaji wa pembejeo za kilimo; na kuagiza mbolea tani 43,000 kwa kutumia mfumo wa BPS ambapo mbolea hiyo imeanza kuingia nchini na kusambazwa nchini tangu tarehe 28 Januari, 2020. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji, uthibiti na usambazaji wa pembejeo nchini ambapo sekta ya umma na binafsi zitashirikishwa na kuhamasishwa kuzalisha pembejeo nchini ili kukidhi mahitaji.
MHE. ANDREW J. CHENGE (K.n.y. MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE) aliuliza:-

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akikemea sana baadhi ya kodi ambazo zimekuwa ni kero kwa wananchi:-

Je, ni kwa nini baadhi ya Halmashauri zimekuwa zikikaidi agizo hilo la Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kodi kero zilifutwa na Serikali kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 mwaka 2017. Hivyo, Halmashauri yoyote inayoendelea kuwatoza wananchi kodi ambazo zilifutwa na Serikali kwa mujibu wa sheria ni kukiuka maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuziagiza Halmashauri kuacha kutoza kodi ambazo zimefutwa kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Rais, TAMISEMI haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa Halmashauri ambayo itabainika kuwatoza wananchi kodi ambazo zimefutwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, endapo Mheshimiwa Mbunge anazo taarifa za Halmashauri inayotoza kodi zilizofutwa, tunaomba taarifa hizo ili Seriali iweze kuchukua hatua. Ahsante.