Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe (140 total)

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Urambo imebahatika kuwa na Mto Ugalla unaopita Kusini kwake kuelekea Mto Malagarasi ukiwa na maji ya kutosha.

Je, kwa nini Serikali isianzishe mradi wa kuvuta maji ya Mto Ugalla kupeleka Mji wa Urambo ambao unakuwa kwa haraka na wananchi wake wamekuwa wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mji wa Urambo unakuwa kwa haraka na wananchi wake wanakabiliwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu. Katika kutatua tatizo la maji kwa Mji wa Urambo, Serikali imepanga kuupatia Mji huu maji kutoka chanzo cha Mto Ugalla.

Katika kutekeleza azma hii ya kutoa maji kutoka Mto Ugalla, Serikali imeendelea na upembuzi yakinifu ili kutathimini wingi wa maji na pia ili kupata muafaka na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kuhusiana na kutekeleza Mradi ndani ya Hifadhi ya Ugalla.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imepanga kuanzisha mradi mwingine wa kutoa maji Mto Malagarasi kwa ajili ya kuleta maji Miji ya Urambo, Kaliua, Mji mdogo wa Nguruka, baadhi ya vijiji vilivyopo Wilayani Uvinza na maeneo mengine ya Wilaya ya Uyui, Manispaa ya Tabora na vijiji vitakavyokuwa umbali wa kilomita 12 kando kando ya bomba kuu. Mradi huu utasaidia kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wengi zaidi kwa kuwa Mto Malagarasi una maji mengi yanayotiririka wakati wote wa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mhandisi Mshauri anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, pamoja na uandaaji wa makabrasha ya zabuni. Kazi hii ilianza mwezi Julai, 2015 na inategemewa kukamilika mwezi Februari, 2016. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2015/2016, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kazi ya usanifu wa mradi mkubwa na utekelezaji wa mradi mkubwa na utekelezaji wa miradi ya muda mfupi ya kuboresha huduma ya maji katika Miji ya Urambo na Kaliua.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Pamoja na Mkoa wa Simiyu kuzungukwa na Ziwa Victoria, bado una tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.
(a) Je, wakazi wa Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima na Busenga watanufaika lini na uwepo wa maji ya Ziwa Victoria?
(b) Je, Serikali itaacha lini kutoa ahadi zisizotekelezeka kwa wananchi?
(c) Je, Serikali ya Awamu ya Tano inatoa ahadi gani katika kutekeleza mipango ya kuwapatia wananchi huduma ya maji?
NAIBU WAZIR WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba Mbunge wa Viti Maalum lenye vipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza utekelezaji wa mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu kwa Miji Mikuu ya Wilaya za Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima na Busega na vijiji vilivyopo umbali wa kilomita 12 Kambi ya Mbomba Kuu.
Mheshimiwa Spika, mtaalamu mshauri aliwasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu mwezi Oktoba, 2015 na hivi sasa anaendelea na usanifu wa mradi. Gharama za utekelezaji wa mradi mzima unakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 747.8, sawa na Euro milioni 313.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kupitia Mashirika na wadau mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ahadi zinazotekelezeka, utekelezaji wa ahadi hizo huchelewa kutokana na upatikanaji wa rasilimali fedha kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi la (b) nitaomba uniruhusu kutoa maelezo ya ziada.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, baada ya kukamilisha Sera ya Maji ya mwaka 2002 ilianzisha programu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima. Katika programu hiyo kulikuwa na miradi 1855. Miradi ambayo imekamilika hadi sasa ni miradi 1143, miradi inayoendelea ni miradi 454 na miradi ambayo inatarajiwa kuanza wakati wowote ni miradi 258.
Mheshimiwa Spika, lakini Mkoa wa Simiyu ni mkoa mpya na una matatizo ya maji na ni mkoa ambao unahesabika katika mikoa yenye ukame.
Kupitia programu hii kumekuwa na miradi ya Vijiji Kumi ambayo imetekelezwa katika Halmashauri zote za Wilaya, Wilaya ya Busega, Wilaya ya Itilima, Wilaya ya Meatu, Wilaya ya Maswa pamoja na Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu yaani Bariadi.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza miradi ya maji ambayo lengo lake ni kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 95 ya wakazi wa miji na asilimia 85 ya wakazi wa vijijini, ifikapo mwaka 2020. Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na Mradi wa Maji Safi kutoka Ziwa Victoria kwenda Miji ya Igunga, Nzega, Tabora na Sikonge. Mradi wa Maji Safi Magu, Misungwi na Lamadi na Mradi wa Maji Safi Urambo kuelekea Kaliua.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako:-
Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kupita awamu ya kwanza ya programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (Water Sector Development Program - WSDP) imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa maji wa Makambako. Kazi zitakazotekelezwa katika mradi huu ni pamoja na ujenzi wa bwawa la Tagamenda, uchimbaji wa visima virefu vya Idofi na chemichemi ya Bwawani, ujenzi wa bomba kuu na mfumo wa usambazaji wa maji na matanki makubwa ya kuhifadhi maji. Mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha wastani wa shilingi za Kitanzania bilioni 70.3 sawa na dola za Marekani milioni 32.39 na unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 155,233.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Mradi wa Maji Makambako utatekelezwa katika awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) katika mwaka wa fedha 2016/2017. Hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za kupata mkopo wa gharama nafuu kutoka Serikali ya India kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga shilingi bilioni moja ili kuboresha hali ya huduma ya maji katika Mji wa Makambako. Wakati mradi mkubwa unasubiriwa na pindi fedha zikipatikana kabla ya mwaka kumalizika fedha hizo zitatumwa.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Bwawa la Kalemawe lilijengwa mwaka 1959 na kumekuwepo na makubaliano baina ya Serikali, UNCDF na wadau wengine juu ya ukarabati wa Bwawa hili.
Je, kazi ya ukarabati itaaza lini ili Wafugaji na Wakulima waondokane na shida ya uchakavu wa bwawa hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimwa Spika, ni kweli bwawa la Kalemawe lilijengwa mwaka 1959, lengo la ujenzi wa bwawa hilo lilikuwa ni kwa ajili ya utunzaji wa maji ya kunywa, mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Same ina mpango wa kukarabati bwawa la Kalemawe kwa kuondoa udongo ambao umejaa kwenye bwawa hilo ili kuongeza ujazo wa ukubwa wa maji kwa ajili ya mifugo na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia fedha kutoka Mfuko wa Kimataifa wa United Nations Capital Development Fund.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ukarabati wa bwawa hilo, scheme ya Kalamba yenye jumla ya hekta 350 pia itakarabatiwa kupitia mpango huo. Maji ya umwagiliaji ya scheme ya Kalamba yatatoka katika bwawa la Kalemawe. Kazi inayoendelea hivi sasa ni ya kumpata Mtaalam Mshauri (Consultant) ili aweze kufanya kazi ya usanifu na kujua gharama za ukarabati. Pindi mtaalam mshauri atakapokamilisha kazi yake kazi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa bwawa na scheme itaanza.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu na Watanzania zaidi ya 75% wanategemea kilimo kama ajira ya kuendesha maisha yao:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha miradi mikubwa ya kuhifadhi maji (water reserves) ili kuwa na scheme itakayowezesha wakazi wa Kata za Mnazi, Lunguza na Mng‟aro kuendesha shughuli zao za kilimo msimu mzima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, Serikali inayo mikakati ya kujenga na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, Serikali ilishajenga skimu ya umwagiliaji ya Kitivo yenye eneo la hekta 500 kwenye miaka ya 1990. Vilevile mwaka 2013, Serikali ilijenga banio kwa ajili ya skimu ya Kwemgiriti yenye jumla ya hekta 800 na Kituani Mwezae yenye jumla ya hekta 600.
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu hizi zinanufaisha wananchi wa maeneo ya Kata za Mng‟aro, Lunguza na vijiji vinavyozunguka Kata hizo. Chanzo cha maji ya umwagiliaji katika skimu hizo ni Mto Umba ukiunganishwa na Mto Mninga. Taarifa iliyopo kwa sasa inaonesha kuwa wingi wa maji katika Mto Umba umepungua kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea katika maeneo ya vyanzo vya mito pamoja na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Mnazi kuna skimu ya Kwemkazu yenye eneo la hekta 150 ambayo ilifanyiwa maboresho ya miundombinu mbalimbali kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2013. Skimu hii inapata maji kutoka Mto Mbarama. Tatizo ambalo limejitokeza kwa sasa, mto huu unakuja na mchanga mwingi sana unaoathiri ufanisi wa banio. Tatizo hili linasababishwa na shughuli za kibinadamu na uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya mto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha wingi wa maji katika skimu zilizotajwa hapo juu, Serikali itafanya uchunguzi wa awali katika maeneo husika ili kuangalia kama kuna maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mapya.
Aidha, namshauri Mheshimiwa Mbunge kushirikiana kwa karibu na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuangalia namna bora inayoweza kufanywa kuhifadhi mazingira katika vyanzo vya mito ili kuiwezesha kutiririsha maji vizuri na kupunguza tatizo la mchanga.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, Serikali itakamilisha lini ukarabati wa Mradi wa Maji wa Ntomoko ili kuwaondolea wananchi adha ya ukosefu wa maji kwenye vijiji vya Sambwa, Kirikima, Churuku, Jangalo, Jinjo, Hamai, Songolo na Madaha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa Mradi wa Maji wa Ntomoko ulianza kutekelezwa mwezi Februari, 2014 na mkataba wa kazi hii ulikuwa ni wa miezi sita. Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha, kazi zilizopangwa kutekelezwa hazikuweza kukamilika katika kipindi cha miezi sita. Gharama ya mradi huo ni shilingi bilioni 2.87.
Utekelezaji wa mradi unaendelea na hadi sasa Mkandarasi amekwishalipwa jumla ya shilingi milioni 841.5 mwezi Agosti, 2015. Wizara ilituma shilingi milioni 600, mwezi Januari kwa ajili ya kuendelea na kazi. Aidha, Wizara itatuma shilingi milioni 728.7 mwezi Februari, 2016 na itaendelea kutuma fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo. Wizara imejipanga kukamilisha mradi huo mwezi Aprili, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo utakapokamilika wananchi wa vijiji vya Makirinya, Hamai, Songolo, Kirikima, Lusangi, Madaha, Churuku, Jinjo, Kilele cha Ng‟ombe na Jangalo watanufaika na huduma ya maji.
MHE. DUA W. NKURUA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi Mkoani Mtwara ya kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Mangaka kwa kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma, mradi ambao pia ungeweza kutatua tatizo la maji katika vijiji zaidi ya 12 vitakavyopitiwa na bomba kuu la mradi huo:-
Je, utekelezaji wa ahadi hiyo umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliyoitoa Mkoani Mtwara ya kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Mangaka pamoja na vijiji zaidi ya 12 kwa kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma. Wizara imeajiri Mhandisi Mshauri na anaendelea na kazi za kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na kuandaa makabrasha ya zabuni ambayo kazi hiyo inategemewa kukamilika mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo itakapokamilika itatoa idadi halisi ya vijiji ambavyo viko ndani ya kilomita kumi na mbili kila upande wa bomba litakapopita na gharama ya utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa mradi unaanza mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Vijiji vya Ngiresi, Sokoni II na Oldadai Kata ya Sokoni II Jimbo la Arumeru Magharibi vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji ya bomba, kwa muda mrefu licha ya kwamba vijiji hivyo kuna vyanzo vingi vya maji na mabomba yanayopeleka maji Arusha Mjini:-
(a) Je, Mamlaka ya Maji Jiji la Arusha inashindwa kutekeleza maombi ya wananchi wa vijiji hivyo ya kupatiwa maji kutoka kwenye mabomba kwa utaratibu wa kulipia?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza na kuboresha vyanzo vya maji katika Jiji la Arusha na Halmashauri zake kutokana na ongezeko kubwa la wakazi wake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Saidi Kabomgo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuondoa tatizo la maji Jiji la Arusha, imepata mkopo wa dola za Kimarekani milioni 210.96 kutoka Benki ya Maendeo ya Afrika (AfDB) ili kutekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao maji safi na maji taka sambamba na kuboresha vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu mkubwa utawezesha Jiji la Arusha pamoja na viunga vyake, ikiwa ni pamoja na vijiji vyote vilivyopo umbali wa kilometa 12 kando kando ya bomba kuu, vikiwemo vijiji vya Ngilesi, Sokoni II na Oldadai ili kupata huduma ya majisafi na majitaka. Jumla ya gharama za ujenzi ni dola za Marekani milioni 233.92 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 476.44.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa mkopo huu nafuu umesainiwa na Mamlaka ya Maji Arusha, kwa sasa inaendelea na taratibu za kupata Mhandisi Mshauri wa kusimamia mradi pamoja na Wakandarasi wa Ujenzi. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017 na kukamilika mwaka 2019/2020. Mradi huu ukikamilika utaboresha vyanzo vya maji na utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Arusha na Halmashauri zake ambazo zimekumbwa na ongezeko kubwa la wakazi.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa ujenzi wa bomba la maji ya Ziwa Victoria kutoka Magu - Sumve - Malya utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inatekeleza miradi ya maji safi na maji taka kwa Jiji la Mwanza pamoja miradi ya maji safi katika miji mitatu ya Magu, Misungwi na Lamadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mji wa Magu mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha Euro milioni 5.3 na Mkandarasi anatarajiwa kuanza ujenzi wa mradi ifikapo mwezi Julai, 2016. Idadi ya wananchi watakaonufaika na mradi huu inakadiriwa kuwa wananchi 73,363 ifikapo mwaka 2040.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miji ya Sumve na Malya, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini gharama za eneo la kupitisha mradi. Kazi ya upimaji pamoja na usanifu itakamalika mwezi Aprili, 2016 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali kupitia Benki ya Dunia ilianzisha mradi wa maji katika Miji ya Haydom, Masieda, Tumati Arri na Bwawa la Dongobesh lakini mpaka sasa mradi huo haujakamilika baada ya fedha kusitishwa:-
Je, Serikali imejipangaje kumaliza miradi hii ili wananchi wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ya Hydom, Masieda, Tumati Arri na Bwawa la Dongobesh ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama ifuatavyo:-
(i) Mradi wa maji wa Hydom umefikia asilimia arobaini na tano. Mradi huu utapokamilika utahudumia wakazi wapatao 16,737.
(ii) Mradi wa Maji wa Masieda umefikia asilimia tisini na tisa na wananchi wapatao 3,137 wanapata huduma ya maji.
(iii) Mradi wa maji wa Mongahay - Tumati umefikia asilimia kumi na sita. Hata hivyo, mkataba umevunjwa kutokana na mkandarasi kushindwa kutekeleza mkataba. Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu inaendelea na taratibu za kupata mkandarasi mwingine. Mradi huu utakapokamilika utahudumia wakazi wapatao 8,679.
(iv) Mradi wa Arri utahudumia wananchi wapatao 17,580. Ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia arobaini na tano.
(v) Ujenzi wa tuta la bwawa la umwagiliaji la Dongobesh umekamilika kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii imechelewa kukamilika kutokana na kukosekana kwa fedha za kuwalipa wakandarasi. Serikali itaendelea kutoa fedha kila zinapopatikana ili kukamilisha miradi hiyo.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Tatizo la maji limeendelea kuwa kubwa Morogoro Mjini pamoja na Mji wa Gairo ambapo wanawake wanapata shida sana kutafuta maji:-
Je, ni lini tatizo hili la maji litaisha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Changamoto za Mileniamu, kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani (MCC) imekamilisha mradi wa maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 24,000 kwa siku hadi kufikia mita za ujazo 34,000 kwa siku kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hilo limeiwezesha Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kupanua mtandao wa usambazaji maji hadi kwenye maeneo ya Nanenane, Tubuyu, Mfuluni, Tungi, Mgudeni, Mjimwema, Tushikamane, Tuelewane, Majengo Mapya, Jakaranda, Kihonda Kaskazini pamoja na Azimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mji wa Gairo, Serikali inakamilisha mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Gairo. Ujenzi wa mradi umefikia asilimia 87 na utakamilika mwezi Juni, 2016. Mradi huu utazalisha mita za ujazo 1,279 kwa siku. Aidha, Serikali ilitekeleza mradi wa uchimbaji wa visima virefu vitatu na uchimbaji ulikamilika mwezi Agosti, 2015. Visima hivyo vimeongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 328 hadi 678. Miradi hii yote kwa pamoja itafikisha uzalishaji wa mita za ujazo 1,957 kwa siku Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kuendelea kuboresha upatikanaji wa maji kwa Mji wa Gairo, Mamlaka ya Majisafi MORUWASA imetuma wataalam wake kwenda Gairo kutafiti na kuainisha maneno ambayo yatachimbwa visima vingine vitatu katika vitongoji vya Mnjilili na Malimbika. Wataalam hao wapo katika hatua ya mwisho ya kutafiti upatikanaji wa maji na uchimbaji visima ambao utakamilika Machi, 2016.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ili usambaze maji katika vijiji vyote vya Jimbo la Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Safi wa Masasi – Nachingwea kutoka chanzo cha Mbwinji unahudumia wakazi wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya Vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Nachingwea na Ruangwa. Jumla ya wakazi wapatao 188,250 wanahudumiwa. Mradi huo uliojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 40 na kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 24 Julai, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma za maji katika Wilaya ya Masasi, Mradi wa Masasi – Nachingwea unakusudiwa kuendelea kufanyiwa upanuzi wa miundombinu ili kuunganisha vijiji vingi zaidi na huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Masasi inaendelea na kazi ya kuunganisha maji katika vijiji vilivyo katika Jimbo la Masasi ambavyo viko mbali na bomba kuu linalopeleka maji katika Mji wa Masasi ili kuongeza upatikanaji wa maji kupitia mradi wa Masasi – Nachingwea. Kwa sasa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa miundombinu ya maji katika Vijiji vya Nangaya, Nangose, Temeke na Marokopareni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwenye Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ili vijiji vingi zaidi ya Jimbo la Masasi vipate maji.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Je, ni kwa nini Mkoa wa Pwani usiwe na Mamlaka yake ya Maji kuliko ilivyo sasa kuwa chini ya DAWASCO ambapo hakuna huduma ya uondoaji maji machafu na bei ya maji iko juu kuliko ile ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Pwani huduma ya maji safi na usafi wa mazingira inatolewa na Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo isipokuwa kwa Miji ya Kibaha na Bagamoyo ambayo inahudumiwa na DAWASA kwa kupitia Shirika la Usambazaji Maji la DAWASCO. Muundo huu ni kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Miji ya Kibaha na Bagamoyo imewekwa chini ya DAWASA kwa sababu za kijiografia na kiuendeshaji. Vyanzo vikuu vya maji yanayotumika kwa Kibaha, Bagamoyo na Dar es Salaam viko Wilaya za Kibaha (Ruvu Juu) na Bagamoyo (Ruvu Chini). Aidha, wakati mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini inajengwa, Miji ya Kibaha na Bagamoyo haikuwa na watu wengi wanaokidhi kuanzishwa kwa Mamlaka inayojitegemea.
Mheshimiwa Spika, bei ya maji kwa wananchi wa Kibaha na Bagamoyo ni sawa na ile inayotumika Dar es Salaam. Hakuna huduma ya uondoaji majitaka katika miji ya Kibaha na Bagamoyo hivyo wananchi hawalipii huduma hiyo. Kwa sasa DAWASA imepangiwa na EWURA kutoza bei ya majisafi kwa Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo, Mkoa wa Pwani kiasi cha Sh. 1,663 kwa lita 1,000 na bei ya majitaka kwa Jiji la Dar es Salaam ni Sh.386 kwa lita 1,000. Hivyo kwa mteja aliyeunganishiwa mtandao wa majitaka na majisafi Jiji la Dar es Salaam analipa jumla ya Sh.2,049 kwa lita 1,000 za majisafi na majitaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa uondoaji majitaka kwa Miji ya Kibaha na Bagamoyo. Utaratibu wa kumpata Mhandisi Mshauri atakayesanifu mradi huo umekamilika na usanifu unatarajiwa kuanza Mei, 2016 na kukamilika Oktoba, 2016. Mshauri atatayarisha mpango kazi pamoja na nyaraka za zabuni zitakazotumika kutangaza zabuni ya ujenzi.
MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:-
Maji ni tatizo kubwa kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishaanza utatuzi wa tatizo la maji katika Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia miradi ya maji inayotekelezwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Utekelezaji wa miradi hiyo umefikia hatua mbalimbali kama ifuatavyo:-
Mradi wa Maji wa Nyarubanda, Kagongo na Nkungwe inayohudumia wananchi wapatao 13,757 imekamilika. Taratibu za kumpata Mkandarasi atakayejenga mradi wa maji wa Kalinzi zimekamilika. Fedha zikipatikana Mkataba utasainiwa ili mkandarasi aanze kazi mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha Serikali inaendelea kutatua kero ya maji katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Halmashauri ya Kigoma imepanga kutekeleza miradi mbalimbali katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017. Vijiji vilivyowekwa kwenye mpango huo ni Mwandiga, Kibingo, Kiganza, Kaseke, Nyamoli, Mkigo, Matendo, Pamila, Matyazo, Mkabogo, Kiziba, Kidahwe, Kigalye, Kalinzi, Kalalangabo, Mtanga, Bugamba, Nyamhoza, Kizenga, Mgaraganza, Mahembe, Samwa, Bubango, Chankele, Kagunga, Zashe, Bitale, Mwamgongo, Machazo na Mkongoro.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Serikali imetoa ahadi nyingi za kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam lakini sasa ni takribani miaka sita tangu Serikali itoe ahadi hizo na tatizo hilo bado liko pale pale:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kumaliza tatizo hilo la maji?
(b) Je, ni kwa nini Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kuwapatia wananchi wake maji wakati haina uwezo wa kutekeleza ahadi zake hizo?
(c) Je, ni nini kimesababisha kutokamilika kwa mpango wa kusambaza maji toka Ruvu ambao ulitarajiwa kuwa ungemaliza tatizo la maji katika maeneo mengi ya Jiji hasa Jimbo la Ubungo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, lenye vipengele (a), (b), (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza ahadi zote ilizoahidi kuhusu kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam. Tayari ahadi ya kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini na ulazaji wa bomba kubwa lenye kipenyo cha milimita 1800 kutoka Ruvu Chini hadi Jijini lenye urefu wa kilomita 56 imekamilika. Mtambo wa Ruvu Chini umeanza kuzalisha lita milioni 270 kutoka lita milioni 180 za awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu umekamilika na sasa una uwezo wa kutoa maji lita milioni 196 kutoka lita milioni 82 za awali kwa siku. Kazi za ulazaji wa mabomba mawili kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa tenki jipya la maji la Kibamba na ukarabati wa matenki ya Kimara zimefikia wastani wa asilimia 98. Uendeshaji wa majaribio umeanza mwezi Aprili, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea kutekeleza mradi wa Kimbiji na Mpera ambapo hadi sasa Mkandarasi amekamilisha uchimbaji wa visima tisa kati ya visima 20 vilivyopangwa, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2016. Visima hivyo vyote vikikamilika vitatoa lita milioni 260 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa ujenzi wa mabomba ya kusambaza maji Jijini Dar es Salaam ulisainiwa tarehe 11/12/2015 na Mkandarasi yuko kazini akiendelea kutambua njia za mabomba na maeneo ya kujenga matanki na kuchukua vipimo yaani survey. Matarajio ni kuanza ujenzi mwezi Mei, 2016 kazi hii itakamilika June, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa umefikia lita milioni 390 kwa siku, ukilinganisha na mahitaji ya maji lita milioni 450 kwa siku za sasa. Miradi yote ikikamilika uzalishaji wa maji Jijini Dar es Salaam utafuikia lita milioni 750 ambapo yatakidhi mahitaji hadi kufikia mwaka 2032.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-
(a) Je, Serikali imefikia wapi katika ujenzi wa bomba la maji la kwenda Tabora- Igunga kupitia Nzega?
(b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kusambaza maji hayo katika Tarafa za Simbo na Choma kupitia Ziba kama Mheshimiwa Makamu wa Rais alivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa … Samahani!
NAIBU SPIKA: Anaitwa Seif Khamis Gulamali!
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza mchakato wa kupata Wakandarasi watakaotekeleza kazi za ujenzi wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na Vijiji 89 vilivyo umbali wa kilomita 12 kutoka bomba kuu. Zabuni ya ujenzi ilitangazwa mwezi Disemba, 2015 ambapo mpaka sasa mchujo wa awali (prequalification) umekamilika na Wakandarasi wanategemewa kuanza kazi katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa za Simbo na Choma zipo zaidi ya kilomita 30 kutoka bomba kuu linalotajarajiwa kujengwa kwenda Igunga kutoka Nzega hivyo kuwa nje ya kilomita 12 zilizosanifiwa kwa mradi huu. Katika kuboresha huduma ya maji katika Tarafa hizi, Serikali inatafuta chanzo mbadala cha maji ili kupunguza tatizo la maji katika Tarafa hizo. Aidha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ili kuendelea kuboresha huduma ya maji.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Ujenzi wa bwawa la Mwanjoro lililopo Wilaya ya Meatu ulianza mwaka 2009 lakini hadi sasa ujenzi wa bwawa hilo haujakamilika:-
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa bwawa hilo ili liweze kutumika kwa ajili ya wananchi na mifugo katika Vijiji vya Jinamo, Mwanjoro, Itaba, Nkoma na Paji?
(b) Je, ni lini Serikali italeta fedha za miradi ya aina hii kwenye Halmashauri ili Halmashauri ziweze kutafuta Mkandarasi kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa karibu na hatimaye kuondoa usumbufu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bwawa la Mwanjoro ulisimama baada ya Mkandarasi kuondoka eneo la mradi bila ridhaa ya mtaalam mshauri wala mwajiri. Hadi wakati shughuli za ujenzi zinasimama utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 78. Serikali itafanya tathmini ya bwawa hilo mwezi Mei, 2016, baada ya mvua zinazonyesha hivi sasa kupungua ili kujua ubora wa tuta lililojengwa, viwango vya kazi zilizobaki, kazi zinazohitajika kuboreshwa, kuandaa michoro ya kuendeleza ujenzi na kuandaa kabrasha la zabuni kwa ajili ya kutafuta Mkandarasi mwingine. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kufanyika mwaka wa fedha 2016/2017
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa usumbufu wa huduma ya maji kwa wananchi, Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo ya kujenga mabwawa na kutenga bajeti ya ujenzi wa bwawa angalau moja kila mwaka. Aidha, Serikali itaendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JOYCE J. MUKYA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la maji katika Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce John Mukya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kutatua tatizo la maji Jiji la Arusha imepata mkopo wa Dola za Marekani milioni 210.96 sawa na shilingi bilioni 462.37 kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AFDB-African Development Bank) ili kutekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji safi na maji taka sambamba na kuboresha vyanzo vya maji. Mradi huu mkubwa utawezesha Jiji la Arusha pamoja na viunga vyake ikiwa ni pamoja na vijiji vyote vilivyopo umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu kupata huduma ya maji safi na maji taka. Jumla ya gharama za ujenzi ni Dola za Marekani milioni 233.92 sawa na shilingi bilioni 512.69.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha, imeshapata Mhandisi Mshauri wa kupitia usanifu ikiwa ni pamoja na kuandaa makabrasha ya zabuni. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2006/2007 hadi 2025, Serikali itatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji yenye lengo la kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama. Katika mpango wa miradi ya maji ya Vijiji 10, Mkoa wa Arusha unatekeleza jumla ya miradi 71 katika halmashauri zote saba ambapo miradi 19 imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wakazi wapatao 112,412. Miradi 52 iko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maji ambao utasaidia kuondoa tatizo la upatikanaji wa fedha na hivyo miradi itatekelezwa kama ilivyopangwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha miradi yote inayotekelezwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma ya maji safi.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Nanyamba kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida ya ukosefu wa maji safi na salama:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi hao wanapata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalumu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kufanya upanuzi wa mradi wa maji wa Kitaifa wa Makonde kutokea katika Kijiji cha Chikunda kupitia Kijiji cha Nyundo hadi Dihamba. Wakazi wapatao 49,206 waishio katika Vijiji 49 vya Halmashauri ya Nyanyamba na Vijiji saba vya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara watanufaika na mradi huo utakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na tathmini ya awali, upanuzi wa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 11.4. Utekelezaji wa mradi huo unategemea upatikanaji wa fedha zitakazotengwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Halmashauri ya Nanyamba ina mpango wa kufanya ukarabati wa miundombinu ya bomba katika miradi ya maji iliyojengwa kwa ufadhili wa AMREF ipatayo 17 inayotumia nishati ya nguvu za jua. Ukarabati huo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 719 na unakadiriwa kuwanufaisha wakazi wapatao 15,433 waishio katika Jimbo la Nanyamba na hivyo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Mtwara Vijijini inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya Mbembelo - Mwang‟anga na Nanyamba - Maranje. Miradi hii itanufaisha Vijiji vya Mwang‟anga, Mbembaleo, Mwamko, Maranje, Mtimbwilimbwi, Mtopwa, Mtiniko, Shaba, Mbambakofi na Mnivata vyenye wakazi wapatao 20,166. Miradi hii itakapokamilika upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya Nanyamba utaongezeka kutoka asilimia 43 hadi asilimia 80.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Kijiji cha Manzase ulishalipiwa nusu ya gharama za mradi na Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne.
(a) Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina Mpango gani kuukamilisha ili wananchi wa Kijiji hicho wapate huduma ya maji safi na salama;
(b) Kijiji cha Chinoje kilipata Mradi wa World Bank na kuchimbwa visima 10 lakini maji hayakupatikana. Je, Serikali ina Mpango gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Miradi ya Maji ya Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri, Halmashauri ya Chamwino inatekeleza miradi kwenye vijiji saba ambapo miradi katika Vijiji vitano vya Mvumi Makulu, Itiso, Mvumi Mission, Chamuhumba na Membe imekamilika na wananchi wapatao 49,000 wanapata huduma ya maji. Mradi wa Wilunze unaendelea kutekelezwa na upo asilimia 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Manzase umefikia asilimia 40. Kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba ya mashine na ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 80,000. Gharama ya ujenzi wa mradi ni shilingi milioni 355, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 71 kimeshapelekwa kwenye Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Serikali itaendelea kupeleka fedha ili kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji katika Kijiji cha Chinoje ni kati ya miradi iliyokosa chanzo cha maji wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Program ya Maendeleo ya Maji. Utafiti wa chanzo kingine cha maji unafanyika na ujenzi wa mradi utafanyika katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MPAKATE D. IDDI aliuliza:-
Katika Wilaya ya Tunduru kuna miradi mingi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo imesimama kwa muda mrefu bila kukamilishwa na wakandarasi kwa sababu ya ukosefu wa fedha:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kumalizia miradi hiyo ambayo wananchi wanajua kuwa fedha zilitolewa na Benki ya Dunia lakini hazijulikani zilikwenda wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mpakate Daimu Iddi, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo ugharamiaji wa maji chini ya programu hii hutokana na fedha za Serikali na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia. Hivyo, upelekaji wa fedha kwenye halmashauri hutegemea upatikanaji wa fedha kutokana na bajeti ya Serikali na fedha za wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hii, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilipanga kutekeleza jumla ya miradi 11. Hadi sasa jumla ya miradi miwili katika Vijiji vya Nandembo na Nalasi imekamilika na inahudumia wananchi 21,224. Miradi minne ya Vijiji vya Lukumbule, Amani, Mtina na Matemanga ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mradi wa maji katika Kijiji cha Mbesa umesimama kutokana na mkandarasi kukiuka masharti ya mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, mpaka kufikia Februari 2016, Wizara imeshatuma kiasi cha shilingi milioni 537.2 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi hiyo. Aidha, miradi minne katika Vijiji vya Majimaji, Muhuwesi, Nakapanya na Mchoteka haijaanza kutekelezwa kutokana na kukosa vyanzo vyenye maji ya kutosheleza. Miradi hii itatafutiwa vyanzo mbadala katika utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji kwenye Jimbo la Kibiti kwenye maeneo ya Delta kama Nyamisati, Mchinga, Mfisini, Kiomboi, Masala, Kiongoroni, Naparoni na Mbunchi.
Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Delta yanakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 25,780; ambapo wakazi wapatao 12,942 sawa na asilimia 50.2 wanapata huduma ya maji kwa sasa. Hivyo ninakubalianana ipo changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua changamoto hiyo Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 iliidhinisha shilingi milioni 403 na tayari zimepokelewa shilingi milioni 272.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji kumi. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imetenga shilingi milioni 83.2 kwaajili ya ujenzi wa mfumo wa maji ya bomba katika kijiji cha Nyamisati.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo yaliyobaki kadri rasilimali fedha zitakavyo patikana.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji ya mradi wa Mbwinji kwenye Vijiji vyote vinavyozunguka mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Maji safi wa Msasi-Nachingwea kutoka chanzo cha Mbwinji unahudumia wakazi wapatao 188,250 wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya Halmashauri za Wilaya ya Masasi, kama vile Nachingwea na Ruangwa. Zaidi ya shilingi bilioni 40 zimetumika katika ujenzi wa mradi huo ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Julai, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya za Masasi, Ruangwa na Nachingwea, Mamlaka ya mradi wa Kitaifa wa Masasi - Nachingwea (MANAWASA), inakusudia kufanya upanuzi wa miundombinu ili kuunganisha vijiji vingi vikiwemo vijiji vya Mtepeche, Naipanga, Chemchem, Mailisita, Mkotokuyana na Nampemba vya Wilaya ya Nachingwea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kutekeleza miradi ya upanuzi wa miundombinu ya usambazaji maji kupitia katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea na itaendelea kutenga fedha zaidi ili kupanua huduma ya upatikanaji wa maji katika Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na vijiji vyake.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Mji wa Kasulu ni Mji wa siku nyingi sana tangu enzi za Wajerumani lakini hauna mtandao wa maji unaokidhi mahitaji ya wakazi wa mji huo:-
(a) Je, ni lini Serikali itakarabati vyanzo vya maji vilivyopo ili maji yafike katika mitaa ya Kata za Mrusi, Mwilavya na Kidyama?
(b) Je, ni kwanini Serikali haitoi fedha ili kujenga tenki la kusafisha maji kwa sababu maji yaliyopo ni machafu?
(c) Je, ni kwanini Serikali haitoi pesa ili chanzo kingine kilichoainishwa kijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lenye sehemu(a) (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya mtandao wa maji inayoukabili Mji wa Kasulu. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kupanua mfumo wa usambazaji maji katika Mji huo. Fedha hizi zitatumika kwa ajili ya kuboresha hali ya huduma ya maji ikiwemo kuongeza mtandao wa maji Mjini Kasulu ambapo pia Kata za Mrusi, Mwilavya na Kidyama zitapata huduma ya maji safi na salama.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa maji safi Mjini Kasulu. Usanifu huo pia umehusisha chujio la kutibu maji katika Mji wa Kasulu. Kwa sasa andiko la mradi limewasilishwa Tume ya Mipango kwa ajili ya kuombea ufadhili kutoka Serikali ya India. Gharama za mradi huo ni kiasi cha Dola za Marekani shilingi milioni 9.89.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika kipengele (b) hapo juu, Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa mradi huo kupitia ufadhili au mkopo nafuu kutoka Serikali ya India. Fedha hizi zikipatikana, ujenzi wa chanzo kingine utafanyika.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:-
Mji wa Mbinga ni miongoni mwa Miji inayokua kwa kasi hapa nchini, hali inayopekekea ongezeko la hitaji kubwa la huduma ya maji safi na salama:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta mradi wa uhakika wa maji safi na salama utakooweza kuwahudumia wananchi wa Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Raphael Mapunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la maji kwa muda mrefu kwa mji wa Mbinga, Serikali imeweka mji huo katika mpango wa utekelezaji wa Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili. Lengo ni kusambaza maji safi na salama kwa wakazi wote wa Mji wa Mbinga pamoja na kujenga Kituo cha Kutibu Majitaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu, mabomba ya usambazaji, ujenzi wa Kituo cha Kutibu na Kusafisha Maji, jengo la kuhifadhi madawa, ukarabati wa mantanki yaliyopo, ujenzi wa matanki mapya na ujenzi wa Kituo cha Kutibu Majitaka. Mhandisi mshauri amekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni. Utekelezaji wa mradi huu utagharimu Dola za Marekani shilingi milioni 11.86.
Mheheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Kwa sasa Serikali imewasilisha andiko la mradi huo, BADEA kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (K.n.y. MHE. STEPHEN J. MASELE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha vijiji vilivyo ndani ya kilomita tano kutoka bomba kuu la maji ya Mradi wa KASHWASA vinapatiwa maji vikiwemo vijiji vya Kolandonto, Ibadakuli na Kuzumbi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetekeleza mradi wa maji safi kutoka Ziwa Viktoria kwenda Manispaa ya Shinyanga kupitia bomba kuu la KASHWASA. Katika kuhakikisha vijiji vilivyopo umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu vinapatiwa maji, Serikali inaendelea kuunganisha maji kutoka bomba hilo hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Hadi sasa jumla ya vijiji 12 tayari vimeunganishwa kati ya vijiji 40 vilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa kupeleka maji katika Mji wa Kishapu Mkoani Shinyanga. Kupitia mradi huo kijiji cha Kolandoto kinatarajiwa kupata huduma ya maji. Kwa sasa kazi ya ulazaji bomba kuu unaendelea na tayari kilometa 22 zimelazwa. Vijiji vya Ibadakuli na Kizumbi vinapata huduma ya maji safi kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira SHUWASA. Kwa sasa mtandao wa maji uliopo haujafika vijiji vyote ambapo Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambao wameonesha nia ya kusaidia fedha za ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji katika maeneo hayo.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Mji wa Mombo ni mji unaokua kwa kasi kubwa na kuna mradi mkubwa wa maji unaotoka Vuga – Bumbuli kwenda Mombo katika Kitongoji cha Mlembule na mradi huo utagharimu shilingi 900,000,000.
(a) Je, ni lini mradi huo utakamilika?
(b) Kwa kuwa mradi huo unapita katikati ya Mji wa Mombo, je, Mji wa Mombo utafaidikaje na mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Kijiji cha Mlembule ambacho kwa sasa ni mtaa ndani ya Mji Mdogo wa Mombo ni Mradi wa Maji ya Mtiririko ambao ulianza kujengwa mwezi Desemba mwaka 2013 chini ya mpango wa vijiji 10 kwa kila halmashauri. Mradi huu ulikusudiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 913.5. Mradi huu ulishindwa kukamilika kwa wakati kutokana na wananchi wa vijiji vya Kishewa, Kihitu na Kidundai kumzuia mkandarasi asijenge chanzo cha maji hadi wao pia wapatiwe huduma yao kwani chanzo cha maji kipo kwenye kijiji chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa utekelezaji unahusisha jamii, Serikali imeridhia mradi huo uendelee kwa kujenga chanzo kipya kitakachokuwa na maji ya kutosha ili kuwahudumia pia wakazi wa vijiji vya Kishewa, Kihitu, Kidundai pamoja na Mji wa Mombo. Kwa sasa Mhandisi Mshauri yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha usanifu ikihusisha chanzo kipya cha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri ya Korogwe imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kukamilisha miradi inayoendelea ukiwemo mradi huo.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Miradi ya Maji Manga pamoja na Kijiji cha Mutulingara inasuasua tu mpaka sasa.
Je, ni lini miradi hii itapatiwa fedha ili iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya Maji ya Manga na Mutulingara, ni miongoni mwa miradi ya Vijiji 10 inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Makambako. Kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Manga inaendelea na hadi kufikia mwezi Machi, 2016, utekelezaji wake ulifikia asilimia 90. Serikali tayari imemlipa mkandarasi kiasi cha shilingi milioni 235.08 kati ya shilingi milioni 491.9 anazodai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Mradi wa Mutulingara, bado haujaanza kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi huu katika awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 992.8 kwa ajili ya miradi ya maji katika Halmashauri ya Mji wa Makambako.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-
Je ni lini mradi mkubwa wa maji Wilayani Longido utaanza rasmi, ambao utakuwa ni mkombozi kwa wananchi wote wa Wilaya ya Longido.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi mkubwa wa Maji Wilayani Longido ambao chanzo chake ni Mto Simba uliopo ndani ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, ulifanyiwa usanifu wa kina na kazi hiyo ilikamilika mwezi Machi mwaka 2015. Mradi umekisiwa kugharimu sh. 13,998,791,270.40 na utaweza kuhudumia watu 21,666. Serikali imepanga kujenga mradi huu na kuukamilisha katika awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.61 kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi ya Vijiji 10 katika Halmashauri ya Longido. Pia imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Longido.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Mji wa Mpwapwa wenye wakazi zaidi ya 41,000 unakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji, ambapo wananchi wanapata shida kubwa sana kutembea mwendo mrefu zaidi ya kilometa tano kufuata huduma ya maji; na kuna baadhi ya mitambo imeharibika na Mamlaka ya Maji Safi na Salama hawana fedha za kukarabati mitambo hiyo. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja kubwa ya kusaidia ukarabati wa mitambo hiyo ili wananchi wa Mji wa Mpwapwa na vitongoji vyake waweze kupata huduma ya maji karibu na makazi yao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya ukarabati wa mitambo ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya Mpwapwa, kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni 24.5. Kazi zilizotekelezwa ni ununuzi na ufungaji wa mota mbili, pamoja na control panel ambazo zimebadili kutoka mfumo wa star delta starter, kwenda soft starter, kwa ajili ya kuendesha mota hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa kazi hiyo mwezi Aprili mwaka 2016, kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka asilimia 59 hadi kufika asilimia 71, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuondoa tatizo la kuungua mara kwa mara kwa mota za mitambo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara, ili kuhakikisha huduma ya maji katika Mji wa Mpwapwa inakuwa endelevu.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Bonde la Mto Ruhuhu lililopo katika Kata ya Ruhuhu Wilaya ya Ludewa ni eneo muhimu sana, linaweza kuzalisha mazao mengi na kupunguza uhaba wa chakula Tanzania:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza bonde hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Francis Ngalawa, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Ruhuhu linalojumuisha Kata ya Manda, Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe na Kata ya Lituhi Wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma kwa kilimo cha mazao ya aina mbalimbali yakiwemo mpunga, mahindi, mihugo na mboga mboga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maandalizi ya uendelezaji wa bonde hilo, upembuzi wa awali ulifanyika kati ya mwaka 2013 na 2014 na kubaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa katika eneo la Kikonge kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kudhibiti mafuriko katika Bonde la Mto Ruhuhu, kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa eneo la takriban hekta 4,000 na kufua umeme mkubwa utakaounganishwa kwenye Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa eneo hili pamoja na kuweka miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. HUSSEIN M. BASHE (K.n.y. MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU) aliuliza:-
Mji wa Igunga unakabiliwa na tatizo kubwa la maji kutokana na kupanuka kwa kasi wakati miundombinu ya maji ni ile ile na pia imechakaa sana na haitoshelezi mahitaji ya maji kwa wakazi wake:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Mji wa Igunga maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya maji ili kupunguza tatizo la maji katika Mji wa Igunga ambapo kwa sasa hali ya huduma inayotolewa ni asilimia 60 ya wakazi wote. Mahitaji ni lita za ujazo milioni 3.5 wakati huduma inayotolewa ni lita za ujazo milioni 2.5. Hii ni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mtambo wa kusafisha na kutibu maji mwezi Januari, 2013. Hata hivyo Serikali inakusudia kuboresha hali ya huduma ya maji kwa mji huo na imeshaanza mchakato wa kutoa maji Ziwa Viktoria kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo umbali wa kilometa 12 kila upande kutoka bomba kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kupata Wakandarasi wa ujenzi wa mradi huu zinaendelea ambapo mradi unategemewa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu, ujenzi wa matenki mapya kwa Vijiji na Mji wa Igunga, ulazaji wa mabomba mapya ya usambazaji na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji. Hivyo, kukamilika kwa mradi huu kutaongeza huduma ya maji kufikia asilimia mia moja.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Miundombinu ya maji Mtwara na mikoa yote ya Kusini mwa Tanzania ni hafifu na wakazi wengi wa miji ya Kusini na vijijini hawapati maji safi na salama.
Je, Serikali iko tayari kujenga bomba la kuvuta maji toka Mto Ruvuma ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu bila mafanikio?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara pamoja na vijiji 25 vitakavyopitiwa na bomba kuu ndani ya kilometa 12 kila upande, kazi hiyo imekamilika mwezi Julai, 2015.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadilinao na Serikali ya China kwa ajili ya kupata mkopo nafuu wa utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo, mtambo wa kutibu maji, bomba kuu la kupeleka maji Mtwara Mikindani, matanaki pamoja na mabomba ya kusambazia maji.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 za awamu ya kwanza kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Endagaw na mradi huo kwa ujumla unagharimu shilingi milioni 800:-
Je, ni lini Serikali itamalizia kiasi cha fedha kilichobaki ili kukamilisha mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Endagaw ina jumla ya eneo la hekta 256 linalofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa sasa eneo linalomwagiliwa ni hekta 200. Wananchi wa Skimu ya Endagaw kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang waliibua miradi wa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang iliwasilisha maombi ya kupatiwa fedha yenye jumla ya shilingi milioni 800 kutoka Mfuko wa DIDF kwa ajili ya kuboresha mfumo wa umwagiliaji. Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi milioni 410 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa skimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kujenga mfereji mkuu wa upande wa kushoto wa kijito cha Endagaw kwa kuusakafia ili kudhibiti upotevu wa maji ardhini kwa urefu wa meta 3,000 na maumbo sita ya kudhibiti mwenendo wa maji ya umwagiliaji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga kuendelea na ukamilishaji mfereji mkuu wa upande wa pili wa kijito wenye urefu wa meta 3,000.
MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza:-
Tatizo la maji ni changamoto kubwa sana katika Mkoa wa Songwe na Wilaya zake zote:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea adha ya maji wanawake wa Mkoa huu hususan Mji Mdogo wa Tunduma ambako hali ni tete zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua adha kubwa ya tatizo la maji inayowakabili wananchi wa Mkoa wa Songwe hususan wanawake. Katika mpango wa muda mrefu wa uboreshaji wa huduma ya majisafi Mkoa wa Songwe, Serikali imekamilisha usanifu na uandaaji wa vitabu vya zabuni kwa ajili ya kuboresha huduma ya majisafi katika Miji ya Mkoa wa Songwe ikiwemo Vwawa ambako ni Makao Makuu ya Mkoa, Itumba, Isongole pamoja na Tunduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za kutekeleza mradi huo kutoka kwa wafadhili mbalimbali. Kwa sasa Serikali imewasilisha maombi katika Benki ya Maendeleo ya Ufaransa ya kupata mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa majisafi Mjini Tunduma. Pia Serikali imewasilisha maandiko ya miradi ya majisafi kwa Miji ya Vwawa na Tunduma kwenda Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa ajili ya kutafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji kwa Miji ya Vwawa na Tunduma, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika miji hiyo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Bwawa la maji la Kijiji cha Mwamihanza limejaa mchanga hivyo kukauka mapema hasa ifikapo nyakati za kiangazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kulikarabati bwawa hilo pamoja na miundombinu inayopeleka maji kwa wananchi wa Kijiji cha Mwamihanza na vijiji jirani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la maji katika Kijiji cha Mwamihanza, Wilayani Maswa lilijengwa na Serikali mwaka 1970 kwa lengo la kutoa huduma ya maji kwa wananchi na mifugo katika Kijiji cha Mwamihanza na vijiji vya jirani, na limekuwa likihudumia wakazi 1,518 na mifugo 3,578. Bwawa hili limejaa mchanga kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo shughuli za kilimo na mifugo eneo la catchment baada ya mradi wa maji kusimama kwa muda mrefu bila kufanya kazi kwa kushindwa kuendeshwa na wananchi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bwawa la Mwamihanza ni chanzo muhimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mwamihanza na vijiji vya jirani, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imeweka ukabarati wa bwawa pamoja na miundombinu katika mpango wa bajeti wa miaka mitatu ambapo ukarabati utafanyika kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 kupitia vyanzo vya fedha za ndani za Halmashauri na fedha za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ya Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali ina mpango wa kubadilisha mitambo ya kusukuma maji, inayotumia diesel, ili itumie nishati ya jua kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji kwa wananchi na kufanya mradi uwe endelevu. Aidha, Serikali imeanza kuvijengea uwezo vyombo vya watumia maji, ili viweze kudumu kuendesha miradi ya maji na kuifanya kuwa endelevu.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imepata USD 17 milioni katika mgao wa USD 500 milioni zilizotolewa na Serikali ya India kusaidia miradi ya maji kwa bajeti ya 2016/2017.
Je, ni lini fedha hizo zitaanza kupelekwa katika Halmashauri husika ikizingatiwa kuwa shida ya maji imezidi kuwatesa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kwingineko katika nchi yetu kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwezi Julai, 2016, Serikali ya Tanzania na Serikali ya India zilifikia makubaliano ambapo Serikali ya India imekubali kuikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya maji. Mkopo huu utatekeleza miradi katika Miji 17 ikiwemo Mji wa Manyoni.
Mheshimiwa Spika, Miji mingine itakayofaidika na mkopo huu ni pamoja na Muheza, Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Wanging‟ombe, Makambako, Kayanga, Karagwe, Songea, Zanzibar, Mradi wa Maji wa Kitaifa wa HTM, Njombe, Mugumu, Kilwa Masoko, Geita, Chunya, Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Makonde, Sikonge, Kasulu na Rujewa.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi ya maji chini ya mkopo huu itaanza mara baada ya kukamilisha taratibu za mkopo. Aidha, miradi hii itatekelezwa moja kwa moja na Wizara hivyo fedha hazitatumwa kwenye Miji au Halmashauri husika.
MHE. CAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Makonde ulijengwa mapema miaka ya 1950 kwa lengo la kuondoa kero ya maji katika uwanda wa Makonde wenye Wilaya za Newala, Tandahimba na sasa Mtwara Vijijini; lakini mradi huu mitambo yake imechakaa na watumiaji wameongezeka ambapo upatikanaji wa maji kwa Wilaya ya Newala ni 31% tu.
Je, Serikali inalifahamu tatizo hilo na inachukua hatua gani kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo mengi hapa nchini likiwemo eneo linalohudumiwa na Mradi wa Maji ya Kitaifa wa Makonde.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mfupi mwaka 2015/2016 Serikali kwa kushirikiana na shirika la DFID kutoka Uingereza ilikamilisha ukarabati wa visima virefu sita eneo la Mitema na kufunga pampu katika visima hivyo. Kukamilika kwa kazi hizo kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 7.4 hadi lita milioni 14.8 kwa siku, hivyo kuongeza huduma ya maji katika baadhi ya maeneo yanayohudumiwa na Mradi wa Makonde.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa Mradi wa Kitaifa wa Makonde na kugundua kuwa chanzo cha Mitema katika Bonde la Mambi kina maji ya kutosha ya kuweza kuhudumia wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Nanyamba, Tandahimba pamoja na Newala.
Mheshimiwa Spika, kupitia mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya India, Mradi wa Makonde umetengewa dola za Marekani milioni 87.41 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa mradi huo. Aidha, wakati mradi mkubwa ukisubiriwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mradi wa Kitaifa wa Makonde.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui haina maji chini ya ardhi na hivyo wananchi hawawezi kupata maji kwa kuchimba visima. Wananchi wanaipongeza Serikali kwa kubuni mradi wa kuleta maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga, Kahama, Nzega mpaka Isikizya na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi huo ili wananchi wa jimbo la Tabora Kaskazini katika vijiji vya Isikizya, Upuge, Majengo na Kanyenye wapate huduma ya maji?
(b) Kwa kuwa bomba hilo la maji litatoa maji kwa umbali wa kilometa 25 kuwafikia wananchi wachache. Je, Serikali haioni kuna sababu ya kuanzisha mradi wa kuchimba mabwawa na kukinga maji ya mvua kama chanzo kingine cha maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naona baada ya kupitisha bajeti jana watu wameridhika na maji.
Kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliai naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo ndani ya kilometa 12 kwa kila upende kutoka bomba kuu, vikiwemo vijiji vya Isikizya, Upuge na Majengo. Kwa sasa taratibu za kupata wakandarasi wa ujenzi mradi huo zinaendelea ambapo ujenzi wa mradi unategemewa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, kijiji cha Kanyenye utekelezaji wake utajumuishwa katika mipango ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma ya maji Serikali itaendele akutenga fedha pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa na kuweka utaratibu kupitia Halmashauri husika kuvuna maji ya mvua kwa maeneo yote ambayo hayatapitiwa na mradi pamoja na yale yenye shida kubwa ya maji.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-
Napongeza jitihada za Serikali kwa kuanzisha mradi wa maji katika kijiji cha Mingumbi ambao utakapokamilika wananchi katika vijiji vya Mingumbi, Kilelima, Naipuli, Njia Nne, Tingi, Mtandago na Miteja kuondokana na tatizo la maji. Hata hivyo, tatizo la maji bado ni kero kubwa katika maeneo mengi ya Jimbo la Kilwa Kaskazini na Wilaya ya Kilwa kwa ujumla.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mradi mkubwa wa maji kutoka katika Mto Rufiji ambao upo jirani na Wilaya ya Kilwa kwa madhumuni ya kumaliza kabisa kero sugu ya maji inayowakabili wananchi wa Wilaya ya Kilwa.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ambapo ujenzi wa miradi umekamilika katika vijiji sita vya Kandawale, Mtandi, Ngea, Njinjo, Nanjilinji na Hanga. Ujenzi katika vijiji vya Mtandango na Mingumbi unaendelea na upo katika hatua mbali mbali, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha shilingi 785,924,000 kwa ajili ya kufanya utafiti, wa vyanzo vingine vya maji katika vijiji vya Lihimaliao, na Nainokwe ambavyo hapo awali vilikosa vyanzo, pamoja na kukamilisha miradi inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, wa kumaliza kabisa kero ya maji, inayowakabili wananchi waishio maeneo yanayozungukwa na Mto Rufiji, ikiwemo Wilaya ya Kilwa. Serikali kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji ambao umeanza mwezi Januari, 2016 itaangalia uwezekano wa kufanya utafiti wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kupeleka maeneo yote yanayozungukwa na mto huo, vikiwemo vijiji vya Wilaya ya Kilwa Kaskazini. (
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Moja ya Changamoto alizokutana nazo Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika Wilaya ya Kilindi ni tatizo la maji hususan maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya, Kata za Saunyi, Mabaranga na kadhalika na Serikali ina Mradi wa Maji wa HTM ambao unatarajia kuwapatia jirani zetu wa Wilaya ya Handeni huduma ya maji ambapo utekelezaji huo utafanyika mwaka huu:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya extension katika Wilaya ya Kilindi ili nayo ifaidike na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa HTM umepangwa kutekelezwa katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha upanuzi wa chanzo cha maji kilichopo, kuongeza uwezo wa mtambo wa kusafisha maji, kukarabati mfumo wa kusukuma maji, kusafirisha maji pamoja na matenki ya kuhifadhi maji. Awamu ya pili itahusisha kuunganisha vijiji vyote vilivyopo umbali wa kilometa 12 kila upande kutoka bomba kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Songe, Wilaya ya kilindi uko mbali, wastani wa kilometa 120 kutoka Handeni linapoishia bomba kuu la Mradi wa Maji wa HTM; hivyo gharama ya kufanya upanuzi wa mradi ni kubwa na ikizingatiwa linapoishia bomba kuu hakutakuwa na maji ya kutosheleza kufikisha katika Mji wa Songe pamoja na vijiji vilivyo jirani. Hata hivyo, Kata ya Saunyi kuna mradi wa maji unaoendelea ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 25, na Kata ya Mabaranga mradi wake wa maji utekelezaji katika awamu ya pili ya programu ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani nitarudia hapo. Hata hivyo Kata ya Saunyi kuna mradi wa maji unaoendelea ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 25. Kata ya Mabaranga mradi wake wa maji utatekelezwa katika awamu ya pili ya programu ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini (Water Sector Development Program II)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) imeanza kazi ya uchimbaji wa visima katika Mji wa Songe ambapo hadi sasa visima viwili vimeshachimbwa. Kazi ya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya maji itafanyika baada ya kazi hiyo kukamilika.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya M. Kikwete aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Karagwe kuwa Mradi wa Maji wa Lwakajunju ambao haukujengwa kama ulivyoahidiwa, lakini Mheshimiwa Rais John P. Magufuli naye aliahidi kwamba mradi huo utatekelezwa:-
Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Maji (Water Sector Development Program), na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) iko katika hatua ya kusanifu mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa Mji wa Karagwe kwa kutumia chanzo cha Ziwa Lwakajunju. Usanifu huu unahusisha pia miradi ya maji kwa miji mingine ya Kyaka, Biharamulo, Chato, Muleba na Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imemwajiri Mhandisi Mshauri, Basler and Hoffman kwa kushirikiana na WILALEX na RWB kwa ajili ya kusanifu miradi ya maji safi katika miji hii. Kazi hii ilianza Januari, 2014 na ilitarajiwa kuwa imekamilika Januari, 2015. Kuchelewa kukamilika kwa usanifu huo, kumetokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati. Kwa sasa, Mhandisi Mshauri, tayari amewasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu na hivi sasa yuko katika hatua ya usanifu wa kina na matajario ni kuwa, kufikia mwishoni mwa mwezi huu tulionao, Juni, 2016 kazi hii itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni kutatuwezesha kujua gharama za utekelezaji wa mradi huu ili kuwezesha taratibu za kutafuta fedha za utekelezaji kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imewasilisha andiko la mradi kwenda Serikali ya India kwa ajili ya kupata mkopo nafuu wa kutekeleza mradi wa ujenzi katika miji 17 ikiwemo mradi wa maji wa Mji wa Kayanga na Umulushaka kutoka Ziwa Lwakajuju.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. JAMES K. MILLYA) aliuliza:-
Tangu kuanzishwa kwake Wilaya ya Simanjiro haijawahi kupata maji ya uhakika licha ya ahadi mbalimbali ikiwemo ile ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kuwa Simanjiro itatengewa shilingi bilioni 30 ili kuleta maji kutoka Mto Ruvu hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Orkesumet.
Je, Serikali itatekeleza lini ahadi hiyo ili kuwakomboa wananchi wa Simanjiro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Kinyasi Millya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, huyo ni Mbunge wa Simanjiro siyo Mbunge wa Viti Maalum. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, naomba nirudie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Kinyasi Millya, Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) na Mfuko wa Nchi Zinazozalisha Mafuta (OFID) inatekeleza mradi wa maji safi utakaohudumia Mji wa Orkesumet ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Simanjiro. Mradi huu utagharimu dola za Marekani milioni 18.4 ambapo BADEA watatoa dola za Marekani milioni nane, OFID watatoa dola za Marekani milioni nane na mchango wa Serikali kwa mradi huo ni dola za Marekani milioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu umepangwa kutekelezwa katika vipande viwili, yaani lots mbili. Kipande cha kwanza kitahusu ujenzi wa chanzo cha maji kutoka Mto Pangani eneo la Ruvu, mtambo wa kusafisha maji pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka. Makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha kwanza yamewasilishwa BADEA kwa ajili ya kupata kibali yaani no objection cha kutangaza zabuni. Kipande cha pili kinahusu ujenzi wa bomba kuu, matanki ya kuhifadhi maji na mabomba ya usambazaji maji. Kibali cha kutangaza zabuni kimepatikana na taratibu za kutafuta mkandarasi zimekamilika na Wizara inasubiri kibali kwa ajili ya kuanza ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo. Mradi huo utakapokamilika, utahudumia wakazi wapatao 52,000.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Miradi ya kuboresha huduma ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Kiarabu (BADEA), Shirika la Mafuta Ulimwenguni (OFID) na Serikali ya Tanzania katika Kijiji cha Mwankoko na Kisaki katika eneo la Irao inaleta changamoto kubwa.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kulipa fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo ambapo tayari uthamini ulishafanyika kwa mara ya pili ambapo Mwankoko wanadai shilingi 1,510,427,634 na uthamini ulifanyika tarehe 13 Machi, 2014 na mradi wa Irao shilingi 2,932,001,058/=?
(b) Mradi wa maji wa Irao katika visima vyake vyote viwili vinapoteza uwezo wa kutoa maji kutoka Q250-170 kwa saa na kisima cha pili ni Q150-70 kwa saa. Je, Serikali ina mpango gani juu ya kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha uhakiki wa fidia kwa eneo la Mwankoko na imetuma kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa fidia ya eneo hilo. Kwa upande wa Irao inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 2.9 zitahitajika kulipia fidia katika eneo hilo. Serikali inaendelea na tathmini ya uhakiki wa gharama za fidia hiyo na uhakiki huo ukikamilika fidia hizo zitalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa mradi wa maji safi Mjini Singida, kumejitokeza tatizo la kushuka kwa viwango vya uzalishaji maji katika visima viwili vya Irao. Kutokana na tatizo hilo, Serikali imechukua hatua za haraka ikiwemo kusafisha visima hivyo, kushusha pampu za visima vyote ili kuongeza kina cha kuchota maji. Baada ya jitihada hizo, imeonekana uwezo wa visima kutoa maji uliongezeka kwa kiasi. Aidha, Serikali imepanga kubadilisha pampu hizo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma ya maji, Serikali imepanga kufunga pampu kwenye visima vitatu vya akiba vilivyochimbwa awali wakati wa utekelezaji wa mradi mkubwa katika Manispaa ya Singida. Kazi hii itatekelezwa pamoja na shughuli ya ulazaji wa mabomba kutoka kwenye visima hivyo vitatu hadi kwenye tanki dogo la kukusanya maji yanayovutwa na kusukumwa kwenda kwenye matenki makubwa katika eneo la karakana.
MHE. MARTIN M. MSUHA (K.n.y. MHE. SUSAN L. KIWANGA) aliuliza:-
Pamoja na Jimbo la Mlimba kuwa na vyanzo vingi vya maji ikiwemo mito mikubwa, wananchi bado wanakumbwa na uhaba mkubwa na maji safi na salama.
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha mpango wa usambazaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mlimba?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha skimu za umwagiliaji ili kuvipa tija vyanzo vya maji vilivyopo katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri zote nchini. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero inatekeleza miradi 14, kati ya miradi hiyo miradi nane ipo katika Jimbo la Mlimba. Ujenzi wa miradi mitano katika vijiji vya Mlimba A, Mlimba B, Viwanja Sitini, Kamwene na Masagati umekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 24,632. Miradi mitatu ya Idete, Namwawala na Matema ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Lengo la Serikali ni kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ili wananchi waweze kupata huduma ya maji kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Skimu ya Umwagiliaji ya Njage yenye eneo la hekta 325 kupitia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Umwagiliaji (DIDF) na hivi sasa skimu hii imeingizwa katika mradi wa Expanded Rice Production Project ili kukamilisha ujenzi wa skimu hiyo.
Aidha, Serikali kupitia Gereza la Idete, inajenga skimu ya umwagiliaji yenye jumla ya eneo la hekta 1,000. Vilevile shamba la Kilombero Plantation Limited (KPL) lenye eneo la hekta 4,000 litaendelea kuzalisha mazao na liko katika hatua ya uendelezwaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, kupitia Mfuko wa Feed the Future inafanya upembuzi yakinifu katika maeneo yaliyoainishwa katika mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2002 ya Kisegese, Udagaji na Mpanga – Ngalimila. Maeneo yatakayofaa yataingizwa kwenye hatua ya usanifu wa kina.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Mradi wa Maji wa Mnanila, Mwayaya na Mkatanga utaanza kutoa maji kwa kuzingatia ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli?
(b) Je, kwa nini Serikali haitoi fedha ili kumaliza miradi ya maji ya Munzenze, Kirungu na Nyamugali ambayo sasa imekuwa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Ntabaliba Obama, Mbunge, wa Jimbo la Buhigwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Mnanila, Mwayaya na Mkatanga ni mradi wa zamani uliyotekelezwa katika miaka 1970. Mradi huu kwa sasa umechakaa, na haufanyi kazi. Kutokana na ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Serikali ilituma fedha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kiasi cha shilingi 10,000,000 kwa ajili ya kufanya usanifu wa mradi na kuhamasisha jamii kushiriki katika ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha andiko la ukurabati la mradi huu linaonesha mradi utagharimu shilingi bilioni moja nukta sifuri nane. Utekelezaji wa mradi huu utaanza katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji ya Munzenze, Kirungu, na Nyamugali ni miongoni mwa miradi ya vijiji kumi inayotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Vijijini ambapo utekelezaji umefikia asilimia 86 kwa mradi wa Munzenze, asilimia 65 kwa mradi wa Kirungu na asilimia 50 kwa mradi wa Nyamugali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.28 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe. Serikali itaendelea kutuma fedha ili kukamilisha miradi kwa kadri zinavyopatikana.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Serikali ina mkakati wake wa kupata maji kutoka Mto Ugala ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji katika Wilaya ya Urambo.
(a) Je, ni hatua gani zimechukuliwa hadi sasa katika kutekeleza ahadi hiyo na kiasi gani cha fedha kitatumika?
(b) Je, kiasi gani kimetengewa kwa mwaka mpya wa fedha?
(c) Je, ni lini mradi huu utafikisha maji Urambo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margatet Simwanza Sitta Mbunge wa Jimbo la Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Urambo kwamba wamechagua jembe. Mila za Kiafrika tunajua kwamba akina mama ndio wanaochota maji na huyu mama anahangaika sana na hadi leo asubuhi amekuja ofisini, hakunikuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la maji kwa Mji wa Urambo Serikali ilipanga kupatia mji huu maji kutoka chanzo cha Mto Ugala. Katika hatua za awali za upembuzi yakinifu wa mradi, ulionekana Mto Ugala hukauka wakati wa kiangazi kati ya Juni na Oktoba. Kutokana na changamoto zilizotajwa, mpango wa Serikali wa kupeleka maji Urambo ni kutoka Mto Malagarasi na siyo Mto Ugala. Mradi huu unatarajiwa kugharimu kiasi cha dola za Marekeni 332.91.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya kukamilisha usanifu wa mradi. Aidha, Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Ufaransa AfD kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo mkubwa utagawanywa katika lot nne ili kuharakisha utekelezaji wake. Kwa kufanya hivyo mradi unatarajiwa kufikisha maji Urambo katika kipindi cha Miaka miwili mara baada ya fedha kupatikana.
MHE. ALLY K. MOHAMED aliuliza:-
Serikali imekwishatumia zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya Mradi wa Skimu ya Lwafi, lakini mradi huu haujawanufaisha kabisa wakulima zaidi ya 4000 kwa sababu haujakamilika:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha mradi huo ili uwe wa msaada kwa wakulima wa mpunga zaidi ya elfu nne?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Keissy, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wa Tarafa ya Kilando kuhusu uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Lwafi, ilianza kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu husika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Mnamo mwaka 2012, banio lilijengwa na mfereji mkuu wa urefu wa kilomita 1.6 ulichimbwa na kusakafiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mkopo kutoka Serikali ya Japan, Serikali inategemea kupeleka fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mwezi huu Juni, 2016. Fedha hizo zitatumika kuchimba sehemu ya mfereji mkuu wenye urefu wa kilomita 16 na kusakafia na kujenga maumbo ya maji ndani ya mfereji huo. Hatua hiyo itawezesha wakulima wa mpunga katika skimu hiyo kunufaika.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu unaanzia Wilaya ya Busega na tayari mipango pamoja na fedha ya kuanza kutekeleza mradi imeshapatikana:-
Je, lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huo muhimu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu katika Miji Mikuu ya Wilaya za Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima na Busega pamoja na vijiji vilivyopo umbali wa kilomita 12, kando ya bomba kuu. Tayari Mtaalam Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa mkabrasha ya zabuni ameajiriwa. Gharama za utekelezaji wa mradi mzima zinakadiriwa kuwa kiasi cha Euro milioni 313 na mradi huu utatekelezwa katika awamu mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza itagharimu kiasi cha Euro milioni 105 na itahusisha kufikisha maji katika miji mikuu ya Wilaya za Bariadi, Itilima na Busega pamoja na vijiji vilivyo kando ya bomba kuu. Hadi hivi sasa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KFW imechangia kiasi cha Euro milioni 25 na kiasi kilichobaki cha Euro milioni 80 kinatarajiwa kupatikana kutoka Mfuko wa Green Climate Fund.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka 2016/2017 na utachukua miaka miwili hadi kukamilika. Kwa sasa mtaalam mshauri anaendelea kufanya usanifu wa tathmini ya athari za kimazingira na kijamii katika maeneo ya mradi huo. Kazi hiyo itakamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili ya mradi itafikisha maji katika Miji ya Mwanhuzi na Maswa kwa gharama ya Euro milioni 208. Fedha hizi pia zinatarajiwa kutoka Green Climate Fund. Miradi hii ikikamilika, inatarajiwa kunufaisha watu zaidi ya 834,204.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Morogoro Mjini bado ina kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya Manispaa kama vile Kata ya Tungi, Mkundi, Kiegea A na B, Kihonda, Kisanga na Ngerengere:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kero hii ya maji katika Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Azizi Abood Mbunge wa Morogoro Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) inaendelea kutatua kero ya maji iliyoko katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro. Katika mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji, kazi zilizopangwa ni upanuzi wa mtandao wa bomba katika maeneo yasiyo na mtandao, ufungaji wa mita za maji, ubadilishaji wa bomba chakavu na uzibaji wa mivujo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kufunga pampu eneo la mizani na bomba kuu la kupandisha maji kwenye tanki lililopo Kilima cha Kilimanjaro ambalo litahudumia eneo la Kiegea A na B na Kata ya Mkundi. Aidha, eneo la Kasanga, Kata ya Mindu kuna mradi mpya unaojengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambao ukikamilika utaondoa kero ya maji kwa wakazi wa Kasanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imeanza kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa maji, ambapo hatua za kumpata mtaalam mshauri atakayepitia usanifu wa vitabu vya zabuni inaendelea. Ujenzi utaanza mara baada ya kukamilika kwa mapitio hayo. Kukamilika kwa ujenzi wa mradi kutamaliza kero ya maji kwa kiasi kikubwa na kukidhi mahitaji hadi itakapofika mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za kutekeleza mradi zitachangiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Ufaransa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ufaransa EFD ambao wameahidi kuchangia Euro milioni 40. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MBONI M. MHITA (K. n. y. MHE. SHABAN O. SHEKILINDI) aliuliza:-
Jimbo la Lushoto linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hususan katika maeneo ya Umiri, Makanya, Kwemashai, Gare, Mlola, Mbwei, Malibwi na Kilole:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi hao maji safi na salama ili waondokane na adha hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omar Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la maji Halmashauri ya Lushoto, inatekeleza mradi wa maji wa Mlola ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 50, mradi wa maji wa Malibwi umefikia asilimia 85 wakati miradi ya maji katika maeneo ya Kwemashai na Ngulu umefikia asilimia 15.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji Ubiri ulijengwa mwaka 1972 na unahudumia watu 2,013. Hata hivyo, huduma ya maji inayotolewa haitoshelezi mahitaji, hivyo Halmashauri ina mpango wa kutoa maji kutoka Kijiji cha Ngulu pindi mradi wa Ngulu utakapokuwa umekamilika bila kuathiri malengo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha miradi katika Vijiji vya Makanya, Kilole na Mbwei imewekwa katika mpango wa utekelezaji wa program ya maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili. Mradi wa Gare ambao unahitaji kufanyiwa upanuzi na kuongeza idadi ya vituo vya kuchotea maji utaingizwa katika mipango ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.4 ili kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa.
MHE. ALMASI A. MAIGE aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui halina maji chini ya ardhi na hivyo wananchi hawawezi kupata maji kwa kuchimba visima, hivyo Serikali ikabuni mradi wa kuleta maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga, Kahama, Nzega mpaka Isikizya na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi huo ili wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini katika vijiji vya Isikizya, Upuge, Majengo na Kanyenye wapate huduma ya maji?
(b) Kwa kuwa bomba hilo la maji litatoa maji umbali wa kilometa 25 kushoto na kulia na kuwafikia wananchi wachache; je, Serikali haioni kuna sababu ya kuanzisha mradi wa kuchimba mabwawa na kukinga maji ya mvua kama chanzo kingine cha maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo ndani ya kilometa 12 kwa kila upande kutoka bomba kuu. Kwa sasa taratibu za kupata wakandarasi wa ujenzi wa mradi huo zinaendelea ambapo ujenzi wa mradi unategemewa kuanza mwezi Disemba, mwaka huu wa 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, bomba kuu la kutoa maji Ziwa Victoria litahudumia vijiji vilivyopo ndani ya kilometa 12 kila upande. Aidha, Serikali itaendelea kubuni vyanzo vingine vya maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya uvunaji maji ya mvua na uchimbaji wa visima virefu ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga kiasi cha shilingi milioni 754.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Halmashauri ya Uyui.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-
Upo mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Mpwayungu kwa jina maarufu Mgangalenga wa muda mrefu na Serikali imegharamia fedha nyingi sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha mradi huo ili wananchi waweze kunufaika nao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, Mbunge wa Mtera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, scheme ya umwagiliaji ya Mpwayungu ilijengwa kupitia Mradi Shirikishi wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji (PIDP) mwaka 2005/2006. Ujenzi wa scheme hii ulihusisha ujenzi wa banio na kuchimba mifereji ya kufikisha maji mashambani. Scheme hii ina eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lenye hekta 160. Eneo lililoendelezwa kwa kufikiwa na mifereji ya udongo linafika hekta 140 ambalo ni kwa ajili ya kilimo cha mpunga lakini kwa sasa eneo linalotumika ni chini ya hekta 25. Kwa sasa Serikali inaendelea na juhudi za kuhamasisha wakulima kulitumia eneo hilo ambalo limeshaendelezwa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Umwagiliaji itafanya mapitio ya usanifu wa mradi huu katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa nia ya kuongeza ufanisi wake.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Miradi ya Maji ya Benki ya Dunia nchini imekuwa ikisuasua sana na hata ile iliyokamilika maji yamekuwa yakitoka wakati wa mvua tu.
Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi inayosuasua ikiwemo ile ya Wilaya ya Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza programu ya maendeleo ya sekta ya maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi katika Jimbo la Tunduru kama ilivyo pia katika maeneo mengine nchini ilitokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha pamoja na kutopatikana kwa vyanzo vya maji vya uhakika katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo Sekta ya Maji, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilipanga kutekeleza jumla ya miradi kumi na moja, kati ya hiyo, miradi minne ya vijiji vya Nandembo, Nalasi, Lukumbule na Amani ujenzi wake unaendelea na miradi minne katika vijiji vya Majimaji, Muhuwesi, Nakapanya na Mchoteka haikupata vyanzo. Aidha, mradi wa Mbesa umesimama baada ya Halmashauri kuvunja mkataba wa mkandarasi kutokana na kutokishi taratibu za kimkataba na tayari taratibu zinaendelea kumpata mkandarasi mwingine.
Mheshimiwa Spika, miradi yote ambayo haikupata vyanzo itapewa kipaumbele katika Awamu ya Pili ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyoanza mwezi Januari, 2016.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, mwezi Agosti, 2016 Wizara imetuma kiasi cha shilingi milioni 147.4 kwa Halmashauri ya Tunduru na Serikali itaendelea kutuma fedha kwa kadri zitakavyopatikana. Upungufu wa maji kwenye miradi iliyokamilika hususan wakati wa kiangazi umesababishwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu. Wizara inashauri tuendelee kuihamasisha jamii katika uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Mradi wa umwagiliaji Lupilo umesimama na haujulikani ni lini utaendelea kujengwa:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Jimbo la Ulanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechagua skimu za kimkakati katika maeneo ya uwekezaji wa kilimo ikiwemo Bonde la Mto Rufiji na Kilombero. Skimu hizo ni pamoja na eneo la Lupilo Ulanga, eneo la Sonjo Kilombero na eneo la Itete Malinyi. Ili kuendeleza skimu hizi Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa skimu za Lupilo na Sonjo pamoja na ujenzi wa skimu ya Itete.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza skimu ya umwagiliaji ya Lupilo, Serikali imefanya upembuzi yakinifu wa skimu ya Lupilo yenye eneo la hekta 4000. Kazi zilizofanyika ni pamoja na uchunguzi wa udongo, uchunguzi wa athari za mazingira, upimaji, uchunguzi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii, uchunguzi wa rasilimali maji, usanifu wa awali na makisio ya gharama za ujenzi wa skimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa na gharama za ujenzi wa skimu ya Lupilo Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuendeleza skimu hii.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Katika mpango wa Serikali wa kuchimba visima katika vijiji 10 vya kila Halmashauri, katika Mji Mdogo wa Makongorosi maji hayakupatikana kwenye kisima kilichochimbwa na kuwa mji huo unakua kwa kasi sana na kero ya maji ni kubwa sana:-
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Makongorosi ni moja ya miradi ya awali iliyopewa kipaumbele kutekelezwa kwenye mpango wa vijiji 10 kwa kila Halmashauri. Baada ya maji kukosekana kwenye kisima kilichochimbwa, mradi huu haukuweza kuendelea kutekelezwa na jitihada za kutafuta chanzo kingine zinaendelea.
Mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Makongorosi umepangwa kutekelezwa upya kwenye Awamu hii ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Chunya imepangiwa bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 561.5 na kazi zilizopangwa kufanyika ni kutafuta chanzo kingine kufanya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya mradi.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji katika Mto Rufiji ili kuongeza ajira na chakula?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mto Rufiji umepita katika maeneo mengi ambayo yanafaa sana kwa kilimo cha umwagiliaji ingawa maeneo mengi huwa yanakumbwa na changamoto ya mafuriko wakati wa kipindi cha mvua.
Mheshimiwa Spika, mpango kabambe wa umwagiliaji (National Irrigation Master Plan) wa mwaka 2002 uliahinisha maeneo yanayofaa kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo ya Mto Rufiji yakiwemo maeneo ya Segeni, Nyamweke, Ngorongo na Ruwe.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaanza kuendeleza scheme ya umwagiliaji ya Segeni, Wilayani Rufiji ambapo hekta 60 zilishaendelezwa na kuna mpango wa kuongeza hekta 60 zaidi. Aidha, Serikali imetuma shilingi milioni 358 kwa ajili ya scheme ya Nyamweke ambayo ina hekta 300 iliyopo Wilayani Rufiji kupitia mradi wa kuendeleza scheme ndogo za umwagiliaji kupitia ufadhili wa Serikali ya Japan.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliainisha pia mashamba ya makubwa ya uwekezaji kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya miwa na mpunga. Baadhi ya mashamba yaliyoainishwa ni pamoja na Lukulilo hekta 8,000 kwa ajili ya kilomo cha mpunga, Mkongo hekta 10,551 kwa ajili ya kilimo cha miwa, Muhoro hekta 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa, na Tawi/Utunge hekta 15,924 kwa ajili ya kilimo cha miwa. Aidha, taratibu za kuwapa wawekezaji katika maeneo hayo zinaendelea kupitia Tanzania Investment Centre.
MHE. SALOME W. MAKAMBA aliuliza:-
Serikali kupitia Mawakala wake wa Maji katika Mkoa wa Shinyanga imepandisha bei ya maji kwa takribani asilimia 100 kwa unit na service charge.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza bei ya huduma ya maji ili wananchi waweze kumudu gharama za huduma hiyo na pia kuwavutia zaidi wawekezaji viwandani ili waendelee na uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA) imepandisha bei ya maji mwezi Septemba, 2015 kwa matumizi mbalimbali kwenye Manispaa hiyo.
Mamlaka hiyo ilipandisha bei hizo baada ya kupata kibali cha kufanya hivyo toka Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA). Bei hizo zimepandishwa kutoka shilingi 790 hadi shilingi 1,000 kwa ujazo wa lita 1,000 kwa matumizi ya majumbani ambayo ni sawa na asilimia 26 na shilingi 1,370 hadi shilingi 2,000 kwa ujazo wa lita 1,000 kwa matumizi ya viwandani ambayo ni sawa na asilimia 46.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuongeza bei za maji ni wa kawaida na ni wa kisheria. Kabla ya kupandisha bei za maji mamlaka husika hulazimika kuomba kibali cha kufanya hivyo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) wakionesha sababu za kusudio la kupandisha bei hizo ambazo hujumuisha gharama za uendeshaji pamoja na sehemu ya uwekezaji wa miundombinu. EWURA kwa kuzingatia sheria, kanuni na ushirikishaji wa wataalam mbalimbali katika eneo au mji unaohudumiwa na mamlaka hiyo huendesha uchunguzi na mchakato wa kujiridhisha na uhalisia wa kupandisha bei hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kupunguza bei za maji pale inapogundua gharama za umeme kwa ajili ya uzalishaji wa umeme utatumia gesi ya asili ambayo ina gharama nafuu kuliko ukizalisha kwa kutumia dizeli. Kwa maeneo ya vijijini gharama za uzalishaji zitapungua maeneo mengi kwani Serikali ina mpango wa kubadilisha mifumo ya mitambo ya maji kwa kutumia nishati ya jua.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Wilaya ya Hanang ni moja ya Wilaya ambazo ziko katika Bonde la Ufa na hivyo upatikanaji wa maji ni wa shida sana. Suluhisho la kudumu ni kuchimba visima virefu na kujenga mabwawa.
(a) Je, ni lini Serikali itajenga bwawa la maji katika Kijiji cha Gidahababiegh ambalo lilibomoka kutokana na mvua?
(b) Je, ni lini Serikali itarudia kuchimba visima katika Vijiji vya Hirbadamu, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela ambavyo awali vilipata ufadhili kupitia Mradi wa Benki ya Dunia lakini maji hayakupatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Jimbo la Hanang, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Bwawa la Gidahababieg ni bwawa kwa ajili ya umwagiliaji na lilibomoka kutokana na athari za mvua za mwaka 2006. Makisio ya gharama ya ujenzi wa bwawa hilo ilikuwa ni shilingi bilioni 1.09 na yaliwasilishwa kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu – TAMISEMI tarehe 18/02/2013 kwa ajili ya kuomba fedha za ujenzi wa bwawa hilo. Ukarabati wa bwawa hilo haukuweza kufanyika kwa wakati huo kwa sababu ya kukosa fedha.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji itatuma wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa bwawa hilo katika robo ya tatu ya mwaka 2016/2017. Aidha, katika bajeti ya 2017/2018, Serikali itatenga fedha ili kuanza ujenzi wa Bwawa la Gidahababeigh ili liweze kutoa huduma kwa wananchi.
(b) Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mradi wa Maji Vijijini kupitia Mpango wa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri, Halmashauri ya Hanang ilikamilisha miradi saba na miradi mitatu ya Wandela, Dajameda na Hirbadawa ilikosa vyanzo vya maji. Vilevile miradi ya Mwanga, Gidika na Lalaji iliyofadhiliwa na wadau wengine ilikosa vyanzo vya maji. Vijiji vyote vilivyokosa vyanzo vya maji vimepewa kipaumbele katika Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ili viweze kutafutiwa vyanzo vingine vya maji na hatimaye wananchi waweze kupata huduma ya maji kama ilivyokusudiwa.
MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mto Ruaha Mkuu unatiririsha maji yake katika Bwawa la Mtera na Kidatu kwa mwaka mzima kama ilivyokuwa miaka iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Saidi Kabongo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mto Ruaha Mkuu ni kati ya mito mikuu minne inayounda Bonde la Rufiji ambayo ni Mto Kilombero, Mto Luwegu, Mto Ruaha Mkuu na Mto Rufiji wenyewe. Maji ya Mto Ruaha Mkuu hutokana na mito inayotiririka kutoka safu za Milima ya Livingstone kule Mbeya. Mito hiyo huingiza maji yake kwenye eneo oevu la Usangu (Ihefu) ambalo likishajaa maji hutoka hapo kama Mto Ruaha Mkuu.
Mheshimiwa Spika, upungufu wa maji kwenye mto huu kwa kiasi kikubwa unachangiwa na shughuli za kijamii na kiuchumi ambazo zinasababishwa na ongezeko la watu. Shughuli hizo ni pamoja na kupanuka kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo miundombinu yake haijasanifiwa na kuboreshwa. Vilevile uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti, kilimo kisichokuwa bora, ongezeko la mifugo na mabadiliko ya tabia nchi vinachangia upungufu huo wa maji.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hii, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika Bonde la Rufiji imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kwa lengo la kuongeza mtiririko wa maji kwenye mto huo. Jitihada hizo ni pamoja na mpango wa ujenzi wa Bwawa la Lugoda katika Mto Ndembela ambapo lengo kuu la mradi ni kuongeza mtiririko wa maji wakati wa kiangazi katika Mto Ruaha Mkuu unaopita katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yakiwemo Mabwawa ya Mtera na Kidatu.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta mradi wa maji Ziwa Tanganyika ili maji yaweze kuvutwa mpaka Mpanda na Mkoa wa jirani wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto za upatikanaji wa maji nchini. Hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto ya maji katika Mikoa ya Rukwa na Katavi zimegawanyika katika mipango ya muda mfupi na muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mfupi, Serikali imekamilisha usanifu na uandaaji wa kabrasha za zabuni kwa ajili ya mradi wa maji kwa Mji wa Inyonga Mkoa wa Katavi, Miji ya Chala, Laela, Namanyere na Matai katika Mkoa wa Rukwa.
Katika usanifu huo, vyanzo mbalimbali vimeainishwa vikiwemo mabwawa, chemchemi na visima virefu. Aidha, kwa Mji wa Mpanda, Serikali imetekeleza mradi wa maji wa Ikolongo wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuboresha hali ya huduma ya maji Mjini Mpanda. Mradi huu umekamilika mwezi Julai mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imejielekeza katika kutumia vyanzo vya maji vya Ziwa Tanganyika na mito mikubwa kwa ajili ya kuhudumia Miji ya Mpanda na Sumbawanga, Miji mingine pamoja na vijiji vitakavyokuwa kando kando ya Bomba kuu. Hivyo Wizara imeziagiza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpanda na Sumbawanga kufanya tathmini ya awali na kuiwasilisha Wizarani ili kuweza kuajiri wataalam washauri watakaofanya usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Majisafi Sumbawanga wameshaandaa andiko hilo na Mamlaka ya Majisafi Mpanda pia nao wameandaa andiko hilo ambalo linawasilishwa mwezi Februari mwaka 2017. Kazi ya usanifu itaanza wakati wa utekelezaji wa programu ya maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Pili iliyoanza Julai, 2016.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji safi na salama katika Mji Mkongwe wa Bagamoyo katika Kata za Magomeni na Dunda:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Mji Mkongwe Bagamoyo maji kwa kiwango cha kuridhisha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mji Mkongwe wa Bagamoyo katika Kata ya Magomeni na Dunda wanapata huduma ya maji ya mgao kutoka katika chanzo cha Ruvu Chini.
Tangu tarehe 23 Machi, 2016 Serikali ilikamilisha upanuzi wa chanzo hicho na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki yaliyoko Makongo eneo la Chuo cha Ardhi, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kuwezesha wananchi hao kupata huduma ya maji kwa uhakika, Serikali tayari imemwajiri Mkandarasi anayejulikana kwa jina la Jain Irrigation System kwa kazi ya kujenga tanki kubwa Bagamoyo Mjini. Ataweka mabomba ya kutoa maji kutoka bomba kuu na kuyaleta kwenye Tanki na atalaza Mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na Kata ya Magomeni na Dunda. Kazi hii imeanza mwezi Machi, 2016 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2017.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Jimbo la Kawe ni miongoni mwa Majimbo ambayo (baadhi ya maeneo) yamekuwa yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi kirefu ambayo ni Kata ya Mabwepande (Mtaa wa Mbopo, Mabwepande na Kinondo), Kata ya Makongo (Mtaa wa Changanyikeni na baadhi ya maeneo ya Mtaa wa Makongo Juu), Kata ya Wazo, Mbweni na Mbezi Juu; na changamoto hii sugu ilitarajiwa kupungua na kumalizika kabisa baada ya mradi mkubwa wa maji wa Ruvu chini kukamilika ambao kwa sasa tayari umeshakamilika:-
(a) Je, mikakati ya usambazaji maji pamoja na Mabomba (katika maeneo ambayo hayana mtandao wa mabomba) ikoje ili kutatua kero husika?
(b) Je, ni miradi gani inayotarajiwa kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Chini umekamilika na umeanza kutumika rasmi tarehe 23 mwezi Machi, 2016. Mradi huu ulihusu upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa Bomba kuu kutoka Ruvu Chini kwenda Dar es Salaam. Hivi sasa uzalishaji wa maji kutoka Ruvu Chini ni mita za ujazo milioni 270 kwa siku ikiwa ni ongezeko la mita za ujazo milioni 90 kwa siku. Kutokana na kukamilika kwa mradi huu, kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa hayapati maji licha ya kuwa na mabomba ya DAWASCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Kwanza, Serikali inatekeleza mradi wa uboreshaji na usambazaji wa maji unaogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 32.772 kutoka Benki ya Exim-India. Katika Jimbo la Kawe la Mheshimiwa Mbunge, mradi huu utatekelezwa katika maeneo ya Changanyikeni, Makongo, Salasala, Wazo, Tegeta, Ununio, Bunju na Mabwepande. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukumia maji katika Kata ya Mabwepande na matanki ya kuhifadhia maji katika Kata za Makongo na Wazo pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Katika Mto Malagarasi iko miradi mikubwa mitatu ambayo ni mradi wa kutoa maji Mto Malagarasi kwenda katika vijiji 69 vilivyopo Wilaya ya Urambo, uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji wa miwa na mradi wa uzalishaji wa umeme wa megawati 44.5.
(a) Je, Mto Malagarasi una ujazo gani wakati wa masika na kiangazi?
(b) Je, maji ya mto huo yanatosheleza mahitaji ya miradi hiyo mitatu?
(c) Je, Serikali imefanya utafiti wa kiufundi kujua bajeti ya maji katika mto huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia Mto Malagarasi, ikiwemo mradi wa maji kwa ajili ya Miji ya Urambo na Kaliua, kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji umeme wa megawati 44.5. Wakati wa masika mto huu unakuwa na maji yanayotiririka kwa mita za ujazo 55 kwa sekunde; na wakati wa kiangazi unakuwa na mita za ujazo 40 kwa sekunde.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza imekamilisha mipango ya pamoja ya uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji katika Bonde la Ziwa Tanganyika ambako Mto Malagarasi unapatikana. Hii ni sehemu ya utafiti wa kiufundi wa kujua wingi na ubora wa maji pamoja na mgawanyo sawia wa matumizi ya maji katika Bonde dogo la Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utafiti huo, umeonesha ya kuwa Mto Malagarasi una maji ya kutosha kwa miradi mbalimbali itakayoibuliwa ikiwemo miradi mitatu iliyotajwa na bado yatabaki kuelekea yakitiririka kwenda Ziwa Tanganyika.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza:-
Mradi wa Masoko Group Water Scheme umeshughulikiwa kidogo na
miundombinu tayari imeshaharibika.
Je, ni lini mradi huu utamaliziwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na
Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa
Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Masoko Wilayani Rungwe
unatarajiwa kuhudumia jumla ya vijiji 15. Mradi huu ni miongoni mwa miradi
inayojengwa chini ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji kwa fedha za
ndani. Mradi huu ulisimama baada ya Halmashauri kuvunja mkataba na
Mkandarasi ajulikanaye kwa jina la Osaka Store.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa sasa umeanza tena kutekelezwa
na Mkandarasi Multi Professional Limited, aliyeanza kazi mwezi Februari, 2016
ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa chanzo cha Mbaka, ujenzi wa
tenki la kuhifadhi maji Kijiji cha Lufumbi, kulaza mabomba yenye urefu wa
kilomita 12.6 na kujenga vituo vitano vya kuchotea maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe tayari mwezi
Disemba, 2016 ilitangaza zabuni ya kuwapata wakandarasi watakaotekeleza
ujenzi wa awamu ya pili utakaohusisha ulazaji wa bomba kilomita 92.1 na ujenzi
wa vituo 135 vya kuchotea maji. Mradi huu ukikamilika utagharimu jumla ya
shilingi bilioni 5.3 na utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika Vijiji vya
Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa,
Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
MHE. AZZA H. HAMAD (K.n.y. MHE. AHMED ALLY SALUM) aliuliza:-
Miradi ya maji ya World Bank katika Jimbo la Solwa imesimama kwa
sababu ya Wakandarasi kutokulipwa fedha zao kwa muda mrefu sasa:-
Je, ni lini Serikali itawalipa Wakandarasi fedha zao ili miradi hiyo ikamilike.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la
Solwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi mingi ya maji ikiwemo miradi ya
Jimbo la Solwa ilisimama kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji mpaka sasa imeshatuma fedha
kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kiasi cha shilingi bilioni 1.17 kwa ajili
ya kuwalipa Wakandarasi kulingana na hati zao za madai walizowasilisha. Kwa
sasa wakandarasi wote wanaojenga miradi ya maji katika Halmashauri ya
Shinyanga Jimbo la Solwa wanaendelea na kazi katika Vijiji vya Mendo,
Nyashimbi, Mwanamadilana na Mwakitolyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutuma fedha katika
Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Shinyanga kwa kadri fedha
zitakavyopatikana ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ilivyokusudiwa.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Mwalushu ulianza kutekelezwa tarehe 19 Januari, 2014 na vituo vyote 28 vimejengwa, mabomba yamelazwa na matenki mawili yamekamilika, lakini mradi huo hautoi maji mpaka sasa kutokana na Mkandarasi kutolipwa fedha zake:-
Je, ni lini Serikali itatoa pesa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Mradi wa Maji wa Mwalushu ulianza kujengwa mwaka 2014 na kwa sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji. Mradi huu unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.2 na umelenga kuwahudumia jumla ya watu 2,051 kwa kutumia vituo 29 vya kuchotea maji. Kwa sasa kazi zilizobakia ni ufungaji wa umeme, ujenzi wa tenki la chini ya ardhi na ununuzi wa pampu.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Januari, 2017 Mkandarasi wa mradi huu tayari amekwishalipwa jumla ya shilingi milioni 701. Wizara itaendelea kumlipa Mkandarasi madai yake kadri atakavyowasilisha kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Itilima. Aidha, Mkandarasi anatarajia kukamilisha kazi zilizobaki ifikapo mwezi Aprili, 2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED aliuliza:-
Serikali imekwishatumia zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya Mradi wa Skimu ya Lwafi, lakini mradi huo haujawanufaisha kabisa wakulima zaidi ya 4,000 kwa sababu haujakamilika:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha mradi huo na kuwa msaada kwa wakulima wa mpunga zaidi ya 4,000?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Keissy, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wa Tarafa ya Kirando inaendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Lwafi. Hadi sasa eneo la Awamu ya Kwanza la hekta 300 linaweza kumwagiliwa kati ya hekta 2,500 zilizokuwa zimetengwa. Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha eneo lote la hekta 2,500 zilizopimwa na kusanifiwa mwaka wa 2012/2013 zimejengewa miundombinu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha eneo lote la hekta 2,500 zilizopimwa na kusanifiwa zinajengwa miundombinu, Serikali ilifanya marudio ya usanifu uliokamilika mwezi Septemba, 2016. Usanifu huo wa mapitio ulifanyika kulingana na hali ya sasa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza awamu ya pili ya utekelezaji wa skimu hiyo kwa kupata fedha za mkopo kutoka Serikali ya Japan, ambapo jumla ya shilingi milioni 580 zimepelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuchimba mifereji ya kati yenye urefu wa mita 16,000, kujenga kivushamaji chenye urefu wa mita 200 kwa kuvuka mto Lwafi na kujenga vigawa maji 28 katika mifereji ya kati.
Mheshimiwa Spika, kazi hizo zitakapokamilika, eneo litakalomwagiliwa litafika hekta 800 kati ya hekta 2,500 zilizosanifiwa. Serikali itaendelea kutafuta fedha kupitia vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba eneo lote la hekta 2,500 linajengewa miundombinu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za kuwapata Wakandarasi wa Ujenzi wa miundombinu iliyopangwa; na makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuwapata Wakandarasi hao, yamekamilika.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-
Jimbo la Ngara ni miongoni mwa Majimbo tisa ya Mkoa wa Kagera yenye tatizo kubwa la maji safi na salama katika vijiji vyake vingi; na Jimbo hili lina utajiri mkubwa wa vyanzo vya maji vikiwemo Mto Kagera na Mto Ruvubu pamoja na mlima mrefu kuliko yote ya Mkoa wa Kagera (Mlima Shunga) ambao kitako chake kinagusa hii mito yote miwili kiasi kwamba yakijengwa matenki makubwa kwenye kilele cha mlima huu, maji yanaweza kusambazwa kwa mtiririko Vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara, Biharamulo, Karagwe, Kyelwa na Chato:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia mito hii miwili ili kumaliza kabisa tatizo la maji katika maeneo yote tajwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mji wa Ngara una uhaba wa maji kama ilivyokuwa miji mingine iliyoko ndani ya Mkoa wa Kagera. Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba, imemwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni katika miji mitano iliyopo katika Mkoa wa Kagera na mji mmoja katika Mkoa wa Geita. Miji hiyo ni Ngara, Biharamulo, Kayanga/Omurashaka, Kyaka/Bunazi, Muleba katika Mkoa wa Kagera na Chato katika Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa ya upembuzi yakinifu uliofanywa na Mhandisi Mshauri huyo, Mto Kagera na Mto Rubuvu itakuwa ni mojawapo ya vyanzo vya maji vitakavyotumika katika Mji wa Ngara. Miji mingine itapata maji kutoka katika vyanzo vyenye uhakika vilivyopo katika Wilaya hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mhandisi Mshauri anaendelea na kazi ya usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2017. Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Serikali itatenga fedha za ujenzi kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili ambayo imeanza kutekelezwa Julai, 2016.
MHE. SHALLY J. RAYMOND (K. n. y MHE. DKT. DAVID M. DAVID) aliuliza:-
Je, mradi wa maji tambarare ya Mwanga na Same hadi Korogwe umefikia hatua gani na wananchi wategemee utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kupeleka maji katika Miji ya Mwanga na Same pamoja na Vijiji vya Wilaya ya Mwanga, Same na Korogwe vilivyopo kandokando ya bomba kuu. Mradi huu utakapokamilika unatarajia kuhudumia watu 456,931. Ujenzi wa mradi huo umegawanywa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, mitambo ya kusafisha maji na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza maji katika miji ya Mwanga na Same. Awamu ya pili inahusisha ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika vijiji 38 vilivyo kandokando ya bomba kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza imepangwa katika loti tatu. Utekelezaji wa loti ya kwanza unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji na kulaza bomba la urefu wa kilomita 12.8 kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matanki ya kituo cha kusukuma maji Kisangara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, loti ya pili inahusu ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika Mji wa Mwanga ambao upo katika hatua ya manunuzi. Tayari zabuni zimetangazwa ili kumpata mkandarasi mwenye sifa. Aidha, fungu la tatu la ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika Mji wa Same utekelezaji wake unaendelea na mkandarasi yupo katika hatua ya maandalizi ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi wa Same - Mwanga - Korogwe awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Disemba, 2019. Ujenzi wa awamu ya pili ambayo inahusisha kupeleka maji katika vijiji vilivyo kandokando ya bomba kuu haujaanza kutokana na ukosefu wa fedha. Serikali inaendelea kutafuta fedha za utekelezaji wa awamu hiyo.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa yenye ukame hapa nchini; ukame huo unasababisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo mengi Mkoani Singida:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Singida inapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuwasaidia wananchi hususan wanawake kushiriki kwenye shughuli nyingine za uzalishaji mali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Singida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa iliyo chini ya wastani wa kitaifa wa utoaji huduma ya maji. Hadi kufikia mwezi Juni, 2016 wananchi waliokuwa wanapata huduma ya maji katika mkoa huo ni asilimia 51.2 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 71.3 kwa maeneo ya mijini. Katika Mkoa huo hakuna mito inayotiririsha maji kwa mwaka mzima. Vyanzo vingine vya maji juu ya ardhi kama maziwa na mabwawa ya asili maji yake yana chumvi nyingi isiyofaa kwa matumizi ya binadamu. Kwa msingi huo, vyanzo vinavyotegemewa kwa huduma ya maji safi ni maji ya ardhini kupitia visima virefu na visima vifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa Mkoa wa Singida inapatiwa ufumbuzi, Serikali imekamilisha kujenga mradi wa maji safi katika Manispaa ya Singida ambapo kwa sasa huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama imeongezeka. Aidha, mkakati wa Serikali ni kuendelea kupanua mtandao wa maji na kufunga pampu katika visima vya ziada ambavyo vilichimbwa kwenye mradi huo uliokamilika.
Vilevile kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika Mji wa Manyoni na Kiomboi ambapo hadi sasa zabuni za ujenzi zimetangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maji vijijini, Serikali inatekeleza miradi ya maji katika vijiji 66. Kati ya hivyo, vijiji 47 vimekamilika na vijiji vingine vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 6,750 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida zikiwemo Halmashauri za Manyoni na Singida Vijijini. Aidha, katika juhudi za kukabiliana na hali ya ukame, Wizara imetoa agizo katika Ofisi ya Mkoa kuhakikisha kila Halmashauri inaainisha maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa madogo na kutenga fedha katika bajeti zao za ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza kujenga mradi wa maji wa Sawala, Mtwango, Rufuna na Kibao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Sawala - Kibao ambao utahudumia vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufuna na Kibao vilivyopo katika Kata ya Mtwango ulianza kutekelezwa tarehe 01/06/2015 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 01/06/2016 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huo ulipangwa kufanyika kwa awamu tatu ambazo ni kujenga intake na kupeleka maji kijiji cha Sawala, kujenga mfumo wa bomba kuu kutoka kijiji cha Sawala hadi Kibao na kujenga mtandao wa kusambaza maji katika vijiji vya Mtwango, Rufuna na Kibao. Awamu ya kwanza utekelezaji umefanyika katika kijiji cha Sawala kwa mkataba wa gharama ya shilingi milioni 644.21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, jumla ya shilingi milioni 261.64 zimetumika kwenye mradi. Kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa intake, sump well, pump house, ulazaji wa bomba kuu, ujenzi wa tenki la mita za ujazo 200, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 16 na sehemu ya mabomba ya usambazaji kilometa 3.4; kwa wastani kazi iliyofanyika imefikia asilimia 50 kwa kijiji cha Sawala tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo haukuweza kukamilika kwa wakati kutokana na mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba. Mwezi Novemba, 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ilivunja mkataba na mkandarasi huyo, na kuamua kuutangaza upya tarehe 07/02/2017 ili kuweza kupata mkandarasii mwingine wa kumalizia kazi zilizobaki. Mkandarasi anatarajiwa kupatikana mwezi Juni, 2017 na kazi itakamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A.
GHASIA) Aliuliza:-
Wananchi wa Kitere na Bonde la Mto Ruvuma wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha mpunga kwa miaka mingi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima hao kuwa na kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Umwagiliaji wa Kitere ulianza kutekelezwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo shughuli zilihusisha ujenzi wa bwawa, mifereji na vigawa maji mashambani. Ujenzi huu ulifanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na kukamilika Disemba, 2015. Mradi una jumla ya eneo la hekta 270 na wananchi wanaonufaika ni takribani 3,300 ambao kwa sasa wanajihusisha na kilimo cha mpunga na mbogamboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya Bonde la Mto Ruvuma, mwaka 2012 Serikali kwa kushirikiana na SADC iliajiri mtaalam mshauri Kampuni ya SWECO toka Sweden aliyepewa kazi ya kuainisha matumizi mbalimbali ya Bonde la Mto Ruvuma ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme, umwagiliaji na uhifadhi wa mazingira. Kazi hii tayari imekwishafanyika na taarifa ya mtaalamu mshauri imeainisha maeneo yote ambayo yatafanyiwa upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Umwagiliaji wa Kitere na ile iliyopo katika Bonde la Mto Ruvuma tayari imekwisha ingizwa katika Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ambao hivi sasa unafanyiwa mapitio ili uendane na hali halisi ya sasa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara yangu imeyaweka maeneo hayo katika bajeti kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kuendeleza maeneo hayo.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA Aliuliza:-
Wilaya ya Same ni miongoni mwa Wilaya zinazokumbwa na baa la njaa mara kwa mara na Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kupeleka chakula cha msaada; na kwa kuwa Wilaya ya Same ina mito mikubwa na maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji:-
(a) Je, Serikali inasema nini juu ya maombi ya muda mrefu yaliyowasilishwa Wizarani ya kujenga Bwawa la Yongoma ili maji yatumike kwa ajili ya umwagiliaji kwenye mashamba yaliyoko katika Kata za Maore, Ndungu, Kihurio na Bendera;
(b) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga bwawa hilo ili kuokoa maisha ya wananchi na fedha nyingi za Serikali zinazotumika kununua chakula cha msaada mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, nchi yetu imekuwa inakumbwa na upungufu wa chakula katika maeneo machache. Ili kuondokana na hali hiyo, hivi sasa Wizara yangu inafanya mapitio ya mpango kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002.
Mheshimiwa Spika, bwawa la Yongoma ni bwawa ambalo litakuwa na ukubwa wa kati na litahudumia Kata za Maore na Ndungu. Serikali inashauri bwawa hilo lipewe kipaumbele na Halmashauri husika kama hatua muhimu ya kukabiliana na suala zima la mabadiliko ya tabianchi. Aidha, bwawa la Kalimawe ambalo linahudumia Kata za Kihurio, Bendera, Kalimawe na Ndungu, Wizara inashauri lifanyiwe ukarabati na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inahusika na ujenzi wa mabwawa makubwa ya kimkakati ambayo yanaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali zikiwemo matumizi ya maji ya kawaida ya majumbani, umwagiliaji na uzalishaji umeme. Kwa sasa, Wizara inatekeleza miradi ya mabwawa ya Farkwa (Dodoma), Lugoda (Iringa) na Kidunda (Morogoro Vijijini). Aidha, Wizara imekuwa ikitoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kuweka kwenye mipango yake utaratibu wa kujenga mabwawa ya ukubwa wa kati na madogo. Wizara ipo tayari kutoa msaada wa kitaalam utakapohitajika.
MHE. JOSEPH L. HAULE Aliuliza:-
Mradi wa maji Madibira ulianzishwa mwaka 1975 na sasa miundombinu yake imechakaa sana na banio (intake) lake imekuwa dogo sana wakati idadi ya watu imeongezeka sana.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukarabati miundombinu hiyo ili kuwaokoa wananchi wa Mikumi na taabu ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikwishabaini changamoto zinazoukabili mradi wa maji wa Madibira unaotumiwa na wananchi wa Mikumi. Changamoto hizo kwa sehemu kubwa zinachangiwa na uchakavu wa miundombinu ya mradi pamoja na ongezeko la watu, hivyo kusababisha kiasi cha maji kinachozalishwa kutokidhi mahitaji ya maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali imechukua hatua za kutatua changamoto ya maji katika eneo la Mikumi, ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji chini ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji inatekeleza ujenzi wa mradi mpya wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 809.4, hadi kufikia Machi, 2017 mradi huo umekamilika kwa wastani wa asilimia 86 na unatarajiwa kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi Mei, 2017 kukamilika kwa mradi huo, kutaboresha hali ya huduma ya maji katika Mji wa Mikumi. Baada ya kukamilika kwa mradi huo mpya, Serikali itaanza pia kufanya ukarabati wa mradi wa maji wa Madibira ili kuuwezesha uendelee kutoa huduma ya maji katika Mji wa Mikumi.
MHE. PAULINE P. GEKUL Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya miradi ya maji ya visima kumi katika vijiji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ilifanya tathmini ya awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji mwaka 2015 ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Serikali ilipanga kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Mutuka, Chemchem, Kiongozi, Malangi, Managhat, Halla, Himti, Haraa, Nakwa na Imbilili. Ujenzi umekamilika katika vijiji vinne vya Mutuka, Himti, Chemchem na Managhat ambapo wananchi wanapata huduma za maji. Ujenzi wa miradi mingine katika vijiji sita unaendelea na umefikia hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itahakikisha inazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika kutekeleza awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Baadhi ya changamoto hizo ni kuchelewesha manunuzi ya miradi, upungufu wa wataalam wa maji, kukosa wataalam wabobezi wa taaluma za kifedha pamoja na baadhi ya maeneo yaliyokusudiwa kuchimba visima kukosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Halmashauri zote zinaendelea kupewa mafunzo ili kujenga uwezo wa kusimamia miradi, kusajili na kuunda vyombo na kuimarisha usimamizi wa mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za miradi ya maji vijijini ili kuwa na takwimu sahihi.
MHE. OMARY T. MGUMBA Aliuliza:
Mto Ruvu ndiyo chanzo kikuu cha maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za kutunza mazingira katika vyanzo vya maji ambavyo viko katika hatari ya kukauka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za kibinadamu?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwashirikisha wataalam wa SUA katika utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa miaka mitano wa kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji ambao utekelezaji wake ulianza mwaka wa fedha 2014/2015. Wizara yangu inatenga fedha za utekelezaji wa mpango huu katika bajeti yake kila mwaka. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kilitengwa kwa ajili ya mpango huo.
Mheshimiwa Spika, suala la utunzaji wa vyanzo vya maji ni mtambuka, ambalo linahitaji ushirikishwaji wa wadau ikiwa ni pamoja na wataalam kutoka sekta mbalimbali zikiwemo sekta za kilimo, madini, viwanda, mazingira na misitu. Mkoa wa Morogoro uko kwenye Bonde la Wami/Ruvu na wataalam na wadau wengine wanashirikishwa katika utekelezaji wake. Mpango huu pamoja na mambo mengine umeainisha maeneo ya vyanzo vya maji na kuweka mikakati ya jinsi ya kutunza na kuhifadhi maeneo hayo ili vyanzo hivyo visiharibike. Aidha, kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu wataalam wamekuwa wakishirikishwa katika kufanya utafiti na ukusanyaji wa takwimu na taarifa mbalimbali muhimu ili zitumike katika kutoa maamuzi sahihi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
MHE. MARY D. MURO Aliuliza:-
Maji ni mahitaji muhimu kwa wanadamu na viumbe vyote lakini gharama za maji ni kubwa sana.
Je, ni lini Serikali itawasambazia maji wananchi waishio pembezoni mwa bomba kuu la Ruvu Juu Mlandizi - DSM katika maeneo ya Pangani, Lumumba, Kidimu na Zogowale ikizingatiwa kuwa maeneo hayo yapo karibu na bomba hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa mradi maeneo mengi ndani ya kilometa 12 ya pembezoni mwa bomba kuu la Ruvu Juu yameanza kupata huduma ya maji.
Hata hivyo, maeneo ambayo bado hayajaanza kupata huduma ya maji yatapata huduma hiyo baada ya utekelezaji wa miradi mipya ya kujenga mtandao wa mabomba ya kusambaza maji katika maeneo yote ambayo hayana huduma hiyo. Miradi hii itatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa kuanzia, tayari tunaye mkandarasi anayejulikana kwa jina la M/S Jain Irrigation System Limited ameanza kazi ya ujenzi wa mabomba ya usambazaji katika maeneo ya Malamba Mawili, Msigani, Mbezi Luis, Msakuzi, Kibamba, Kiluvya, Mloganzila na Mailimoja na atakamilisha kazi hiyo mwaka huu 2017. Maeneo ambayo yanapata maji kutoka Bomba la Ruvu Juu ni pamoja na Mlandizi na vitongoji vyake, Visiga, Misugusugu, Soga, Korogwe, Picha ya Ndege, Kwa Mathias, Tumbi, Mailimoja, Pangani, Kiluvya, Kibamba, Mloganzila, Mbezi kwa Yusufu, Mbezi Mwisho, Kimara, Kilungule, Mavurunza, Baruti, Kibo, Kibangu, Tabata, Segerea, Kinyerezi na Karakata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za usambazaji maji katika bajeti 2017/2018 ili maeneo yote ya pembezoni mwa bomba kuu la Ruvu Juu, toka Mlandizi hadi Dar es Salaam umbali wa kilomita 12 yakiwemo maeneo ya Pangani, Lumumbana, Kidumu na Zugowale yapate huduma ya maji.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Vyanzo vingi vya maji vinavyojaza Bwawa la Kihansi vinatoka Wilaya ya Kilolo.
Je, Wilaya hii inanufaika vipi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methusalah Mwamoto, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vyanzo vingi vya maji vinavyojaza Bwawa la Kihansi vinatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa Bwawa la Kihansi unategemea sana vyanzo hivyo muhimu ambapo Taifa linanufaika kutokana na shughuli kubwa inayofanyika katika bwawa hilo ya kufua umeme. Uhifadhi wa Bwawa la Kihansi unatokana na vijiji 22; kutoka Wilaya za Mufindi vijiji nane, Wilaya ya Kilolo vijiji nane na Kilombero vijiji nane ambapo kwa sasa kuna mradi maalum unaosimamiwa na Baraza la Mazingira la Taifa kwa ajili ya uhifadhi mzima wa Bonde la Mto Kihansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo inanufaika na bwawa hilo kwa kupata umeme ambao umesambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika maeneo mengi ya vijijini ambapo katika Wilaya ya Kilolo vijiji vilivyonufaika ni pamoja na Masisiwe, Boma la Ng’ombe, Mwatasi, Ng’ingula na Wangama. Pia uwepo wa Bwawa la Kihansi umesababisha mashirika mbalimbali kuanzishwa kwa lengo la kusaidia jamii katika mambo mbalimbali kama vile upandaji wa miti kwa lengo la kuhifadhi mazingira, ufugaji wa nguruwe, mbuzi pamoja na ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wananchi wa Halmashauri ya Kilolo wameendelea kupata huduma ya maji kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa chini ya mpango wa miradi ya vijiji kumi, ambapo jumla ya miradi saba ya Irindi, Ihimbo, Mwatasi, Kipaduka, Vitono, Ikuka na Ilamba imekamilika na miradi mingine ipo katika hatua mbalimabli za utekelezaji.
MHE.SILVESTRY F. KOKA aliuza:-
Kazi kubwa ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Maji kutoka Ruvu Juu kupitia Kibaha Mkoani Pwani hadi Kimara Jijini Dar es Salaam, imeshafanyika.
Je, ni lini mradi huo kwa upande wa Kibaha Mjini utakamilika na wananchi waweze kupata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji
na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutumia mkopo
wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India, imetekeleza mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ulazaji wa bomba kuu la kutoka Mlandizi hadi Kimara na ujenzi wa tanki jipya la Kibamba. Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu uliogharimu Dola za Marekani milioni 39.7 umeongeza uwezo wa mtambo wa kuzalisha maji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na Ujenzi wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara kumeongeza uwezo wa kuzalisha maji ya kutosha na hivyo maeneo yenye mtandao wa mabomba ya usambazaji ya Mlandizi, Kibaha na Kiluvya pamoja na maeneo ya Kibamba, Mlonganzila, Mbezi kwa Yusufu, Mbezi mwisho, Kimara, Kilungule, Mavurunza, Baruti, Kibo, Kibangu, Tabata, Segerea, Kinyerezi, Vingunguti, Kipawa, Airport na Karakata yameanza kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, DAWASCO wako katika kampeni ya siku 90 ya kuunganisha wateja wote wanaohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu chini. Kwa upande wa Kibaha, DAWASCO wamepanga kuwaunganishia maji wateja wapya elfu 30. Ombi langu kwa wananchi, wapeleke maombi ya kuunganishiwa maji katika Ofisi za DAWASCO iliyoko katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara yangu itaendelea kutenga fedha kwenye programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Pili, ili kupanua mtandao wa mabomba ya kusambaza maji na kuweza kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Miradi ya maji inayojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika vijiji vya Lilondo na Maweso imekwama kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, licha ya miradi hiyo kutumia fedha nyingi na nguvu kubwa za wananchi:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha miradi hiyo?
(b) Je, ni lini miradi hiyo itakamilika ili kutatua kero za maji kwa wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ya Maweso na Lilondo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ni kati ya miradi iliyoibuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika mpango wa vijiji kumi kwa kila Halmashauri chini ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini. Aidha, utekelezaji wa miradi hii imekuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutokana na kuwa illibuliwa na kuanza kutekelezwa wakati Madaba ikiwa ni sehemu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Maweso kwa mujibu wa mkataba una gharama ya shilingi 546,792,163.2. Jumla ya shilingi 109,771,259 zimetumika kumlipa mkandarasi. Vilevile, mradi wa Lilondo kwa mujibu wa mkataba una gharama ya shilingi 1,048,875,254 na jumla ya shilingi 224, 491,637.25 zimetumika kumlipa mkandarasi. Hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Songea imewasilisha hati ya madai ya wakandarasi wa miradi hiyo na Wizara imetuma jumla ya shilingi 101,444,072 ili kuwalipa wakandarasi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima kuu ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivyo, Serikali kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa itahakikisha inapeleka fedha kwa kadri zinavyopatikana katika miradi hii kulingana na hati za madai zilizohakikiwa na Halmashauri, Sekretarieti ya Mkoa na Wizara ili iweze kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2017.
MHE. HASSANI S. KAUNJE aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Ng’apa ambao upo Manispaa ya Lindi ulikusudiwa kuwahudumia wakazi wa Lindi Mjini tangu mwezi Mei, 2015, lakini mpaka sasa mradi huo haujakamilika. Je, ni lini mradi huo utakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Ng’apa unagharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya kupitia Benki ya Maendeleo ya KfW kwa gharama ya Euro milioni 11.56. Ujenzi wa mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi ajulikanaye kwa jina la Overseas Infrastructure Alliance kutoka nchini India. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ufungaji wa pampu katika visima ambavyo vimeshachimbwa na vina uwezo wa kutoa maji mita za ujazo 7,500 kwa siku; ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji; ujenzi wa mtambo wa kutibu maji; ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhi maji; ujenzi wa nyumba ya wafanyakazi, karakana, ghala, nyumba ya walinzi; ujenzi wa mabwawa ya kusafisha maji na ununuzi wa gari moja la majitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa mradi huu ulitegemewa kukamilika mwezi Mei, 2015. Sababu kuu zilizosababisha kutokamilika kwa mradi huu ni kutolipwa kwa wakati kwa fidia na kasi ndogo ya mkandarasi katika ujenzi wa mradi. Hadi sasa Serikali imefanikiwa kuwalipa waathirika wote wa mradi waliokuwa wamefanyiwa tathmini. Kwa upande wa mkandarasi, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kulingana na masharti ya mkataba, ikiwemo kumkata fedha za adhabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua mbalimbali zilizochukuliwa zimewezesha utekelezaji wa mradi kufikia asilimia 85 kwa sasa na mradi unategemea kukamilika mwezi Julai, 2017.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Maeneo mengi ya Jimbo la Kilwa Kaskazini bado hayajapata huduma ya mawasiliano ya simu kama vile kata za Kibata, Kinyumbi, Kandawale na vijiji vya Nandete na Mkarango.
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hii katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya kata za Kibata, Kinyumbi, pamoja na vijiji vya Nandete na Mkarango kutoka katika kata ya Kipatimu, Jimbo la Kilwa Kaskazini vitafikishiwa huduma ya mawasiliano ya Kampuni ya Simu ya Viettel kupitia utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi unaotegemewa kukamilika ifikapo Novemba, 2017. Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, itaainisha vijiji vya kata ya Mandawale na kuviingiza katika orodha ya miradi kwa ajili ya zabuni za siku za usoni kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA aliuliza:-
Tatizo la Maji Mkoa wa Tanga ni kubwa licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji, viongozi wa Serikali kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoa ahadi mbalimbali lakini hakuna hatua za makusudi za kutatua tatizo la maji:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka maji kupitia mradi wa Manga/Magoroto ambao ulianza tangu mwaka 1970?
(b) Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya uchakavu wa miundombinu hasa mabomba na mipira katika mradi wa Kicheba na Kwemhosi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yosepher Ferdinand Komba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji Magoroto ulijengwa mwaka 1977 na ulilenga kuhudumia wakazi wapatao 8,000 katika Mji wa Muheza na maeneo yanayozunguka Mji wa Muheza. Hivi sasa mradi huu unahudumia wakazi wapatao 30,834 walioko katika Mji wa Muheza; idadi hii ni kutokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu mradi huu hautoshelezi mahitaji katika Mji wa Muheza. Ili kuondoa tatizo, mradi wa dharura utakaogharimu shilingi bilioni 2.6 unaendelea kutekelezwa kwa kutoa maji eneo la Pongwe. Taratibu za kumpata Mkandarasi zinaendelea na kazi inatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji katika Kijiji cha Kwemhosi ulitekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 225 na ulikamilika mwezi Juni, 2013. Mradi huu unafanya kazi kama ulivyosanifiwa, ila kwa sasa mradi huo umeharibiwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Aidha, Mradi wa maji wa Kicheba ulijengwa mwaka 1999 na Kanisa Katoliki ambapo hivi sasa miundombinu yake imechoka. Mradi huu utaendelea kukarabatiwa na Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya watumiaji maji katika eneo la Kicheba, kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali hutumia gharama kubwa katika utafiti wa maji na ujenzi wa miundombinu ya maji, lakini baadhi ya miradi inayokabidhiwa kwa mamlaka za maji za mji na jumuiya ya watumia maji (COWUSA) zinasuasua na kutonufaisha jamii kama ilivyokusudiwa:-
Je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha miradi ya maji inanufaisha jamii kama iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiaha Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini. Katika kuhakikisha miradi hiyo inanufaisha jamii kama ilivyokusudiwa Wizara imeandaa na inatekeleza uundaji, usajili wa vyombo vya watumia maji na kuvijengea uwezo kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi. Katika kuhakikisha mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira zinatoa huduma endelevu mamlaka hizo zinasimamiwa na bodi ambazo zinajumuisha wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utekelezaji huo kumekuwa na changamoto mbalimbali katika miradi hiyo ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya maji, wizi wa vifaa vya maji pamoja na watumiaji maji kutolipia huduma hiyo zikiwemo taasisi za Serikali. Hali hiyo ya baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa madeni yao kumepelekea mamlaka nyingi kushindwa kugharamia matengenezo ya miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na wizi wa maji pamoja na uchakavu wa miundombinu Wizara inaendelea kurekebisha Sheria za Maji ili ziweze kutoa adhabu kali kwa wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji. Vilevile mamlaka za maji na usafi wa mazingira mijini zinaendelea kukarabati miundombinu ya maji iliyochakaa, kufunga dira za maji kwa wateja wote ili kubaini matumizi yao halisi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji. Aidha, Wizara imeanza kuchukua hatua za kutumia nishati ya jua kwenye mitambo ya maji hususani vijijini kwa ajili ya kupunguza gharama za uendeshaji.
MHE. OMARY T. MGUMBA (K.n.y. MHE. DKT. HADJI H. MPONDA) aliuliza:-
Vijiji vya Ngoheranga na Tanga katika miradi ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (Phase II World Bank Project), vimepangiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya maji; zoezi hili limeishia tu kwa uchimbaji wa visima virefu nane na mradi kusitishwa.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha utekelezaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba kama ilivyo katika vijiji vingine vinavyofadhiliwa na Benki ya Dunia?
(b) Je, ni lini Serikali itapelekea maji katika vijiji vilivyosahaulika vya Mtimbira, Majiji, Kiswago na Ihowanja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali Mheshimiwa Dkt. Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Ngoheranga na Tanga ni kati ya vijiji kumi ambavyo vilifanyiwa usanifu mwaka 2008 na mwaka 2010 vilichimbwa visima vitatu ili vitumike kwa ajili ya usambazaji wa maji ya bomba. Kati ya visima hivyo visima viwili vilikosa maji kabisa na kitongoji kimoja cha Mkanga kilipata maji kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 wataalam wa Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge walishauri vichimbwe visima virefu na kufungwa pampu za mkono kwa kila kitongoji ikiwa ni mbadala wa maji ya bomba. Ushauri huu ulizingatiwa na visima 13 vilichimbwa ambapo visima vinane vilipata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha uwekaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba katika visima vinane vilivyopata maji kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo imeanza kutekelezwa mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, vijiji vya Mtimbira, Majiji, Kiswago na Ihowanja havijasahaulika kwani Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji hivyo kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Halmashauri inaendelea kukamilisha taratibu za utekelezaji wa miradi katika vijiji hivyo ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya maji.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Naibu Waziri wa Maji alipotembelea Mji wa Maswa alipata nafasi ya kutembelea bwawa lililobomoka la Sola na kuahidi kutoa fedha ya ukarabati wa bwawa hilo kiasi cha shilingi milioni 900.
(a) Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambalo ni muhimu kwa wakazi wa Mji wa Maswa?
(b) Kuna mabwawa 35 katika Wilaya ya Maswa, je, ni lini Serikali itatoa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 ambazo zilikadiriwa kwa ajili ya kukarabatiwa mabwawa hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la New Sola lina uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 4,200,000 na maji hayo ndiyo yanayotumika kuhudumia Mji wa Maswa na vijiji 11 vinavyozunguka mji. Bwawa lililobomoka ambalo ni la Old Sola liko kwenye dakio lilelile la bwawa la New Sola na liko upande wa juu (upstream). Kwa hivyo, ukarabati wake utapunguza maji katika bwawa la New Sola ambalo tayari lina miundombinu ya kusambaza maji. Wizara itafanya uchunguzi zaidi kuhusu faida za ukarabati wa Bwawa la Old Sola.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mabwawa manne na malambo 31 yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa. Aidha, mpango mkakati wamiaka mitano umeandaliwa kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mabwawa ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa vyanzo vya maji katika Halmashauri zote nchini. Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini imeanza zoezi la kuainisha mabwawa (inventory) ambayo yatakidhi viwango vya kiufundi, hatimaye kufanyiwa tathmini ili kujua idadi na gharama halisi ya ukarabati wa mabwawa hayo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Maeneo mengi ya Mkoa wa Simiyu na Mikoa mingine kama vile Dodoma, Singida, Shinyanga na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tabora na Mwanza yanapata mvua za masika hafifu sana, hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo katika Mikoa hiyo:-
Je, Serikali ina mpango gani mkubwa wa kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ilikwishaainisha maeneo yote nchini yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kuandaa mpango kabambe wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wa mwaka 2002. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya ardhi, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Japan inafanya mapitio ya mpango huo ili uhusishe ujenzi wa mabwawa madogo, ya kati na makubwa kwa nchi nzima yakiwemo maeneo yanayopata mvua hafifu za masika. Vilevile mpango huo utahusisha matumizi ya maji ya maziwa makuu, ikiwemo Ziwa Viktoria, kwa ajili ya umwagiliaji wa kutumia teknolojia zinazotumia maji kwa ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupitia mpango huo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018. Kukamilika kwa mpango huo kutawezesha kufanyika kwa usanifu wa miradi ya mabwawa kwenye maeneo yenye mvua hafifu yaliyotajwa pamoja na maeneo mengine yenye uhaba wa mvua. Katika mpango huo Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaanza ujenzi wa mabwawa makubwa ya kimkakati ya Kidunda, Ndembela na Farkwa.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali imepanga kuwalipa fidia Wakazi wa eneo la Kifungwa, Kata ya Kahororo, Manispaa ya Bukoba, ambao ardhi zao na mali iliyomo vilichukuliwa na Serikali miaka miwili iliyopita (12/07/2014) kupisha mradi wa maji taka wa BUWASA?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini. Katika utekelezaji wa miradi hiyo kuna wananchi ambao walitoa maeneo yao ili kupisha miradi ya maji ikiwemo Mradi wa Maji Bukoba. Kabla ya kuanza ujenzi wa mradi Serikali imeweka utaratibu wa kuwalipa fidia kwa mujibu wa Sheria wamiliki wote wa ardhi na mali nyinginezo zitakazoathiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mradi wa Maji Taka Bukoba Serikali kupitia Wizara ya Maji imetuma fedha za fidia katika Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka na Usafi wa Mazingira Bukoba, jumla ya Sh.1,960,000,000/= kwa ajili ya malipo ya fidia katika eneo la Kifungwa, Kata ya Kahororo ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba, 2016 wadai wote 194 walilipwa fedha zao.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Pamoja na jitihada nyingi zinazofanyika, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeendelea kuwa na tatizo la maji kila siku:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha na kukarabati Bwawa la Mindu ili kusaidia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kupata maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Mji wa Morogoro. Serikali kwa sasa imefanikiwa kupata fedha kiasi cha Euro milioni 70 kutoka Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo (AfD) kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji safi na maji taka katika Manispaa hiyo. Mtaalam Mshauri atakayefanya mapitio ya taarifa zilizokuwepo za uboreshaji wa huduma ya maji safi amepatikana na alianza kazi mwishoni mwa mwezi Februari, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huo, kazi kubwa zitazotekelezwa ni uboreshaji wa Bwawa la Mindu kwa kuongeza kina cha tuta kwa mita 2.5 ili liweze kuhifadhi maji mengi zaidi. Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji eneo la Mafiga, upanuzi wa miundombinu ya kusambaza maji na ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia kiasi cha mita za ujazo 61,000 kwa siku kutoka mita za ujazo 33,000 kwa siku za sasa na utakidhi mahitaji ya maji katika mahitaji ya maji katika Manispaa ya Morogoro hadi mwaka 2025 na ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Miradi ya maji ya Mugeta/Nyang’aranga na Nyamuswa ambayo inadhaminiwa na Benki ya Dunia imeshindwa kumalizika tangu mwaka 2013 hadi leo.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi hii kwa ufanisi na kukabidhi kwa watumiaji?
(b) Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya ahadi ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Makala akiwa Bungeni ya ukaguzi wa miradi hii hususan mradi wa Mugeta ambao una bajeti mbili kwa mradi mmoja?
NAIBU WA WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza miradi ya maji chini ya Programu ya Maendeleo ya Maji (WSDP) ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inatekeleza Miradi kwenye Vijiji 10 vikiwemo Vijiji vya Mugeta/Nyang’aranga na Nyamuswa. Jumla ya miradi mitano ya Karukekere, Mumagunga, Kung’ombe, Mugeta na Ligamba imekamilika. Miradi ya Nyamuswa, Nyamatoke, Kibara, Bulamba na Kinyambwiga ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mugeta umekamilika na hivi sasa wananchi wanapata huduma ya maji isipokuwa Kitongoji kimoja cha Manyangale ambacho kitapata maji kutoka chanzo kingine baada ya kufanyiwa usanifu mwezi Agosti, 2016. Ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Nyang’aranga umekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa kuwa mradi huu ulikuwa unatumia bajeti mbili, tayari Mkoa wa Mara umechukua hatua kwa kuunda timu ya wataalam kukagua na kuchunguza jambo hilo. Pindi ripoti hiyo itakapotufikia, basi hatua stahiki zitachukuliwa.
MHE. CATHERINE N. RUGE (K.n.y. MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Wilaya ya Tarime imepakana na Ziwa Victoria na Mto Mara ambao sehemu yake kubwa uko ndani ya Wilaya ya Tarime, licha ya kuwa karibu sana na vyanzo vya maji, wananchi wa Tarime Mjini kwa muda mrefu wamekuwa wanatumia maji ya Bwawa la Kenya Manyori lililojengwa na Mjerumani ambalo halijawahi kufanyiwa usafi tangu kuchimbwa kwake na kupelekea wananchi watumie maji yasiyo safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji ndani ya Mji wa Tarime kutoka Ziwa Victoria na Mto Mara kama ilivyowahi kuyapeleka Shinyanga?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta wataalam kusimamia na kuendeleza chanzo cha maji kilichopo japo hakikidhi mahitaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Mji wa Tarime. Usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni ya mradi huo ulikamilika mwaka 2012 na kwa sasa Serikali inafanya mapitio ya usanifu wa mradi huo (design review) na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2017. Baada ya mapitio ya usanifu wa mradi kukamilika na gharama za ujenzi kufahamika, Wizara itatafuta fedha kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje, kadri hali itakavyoruhusu ili mradi uweze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imeandaa mradi wa kuboresha chanzo cha sasa cha Mto Nyandurumo ili kiweze kuzalisha maji mengi zaidi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa choteo la maji (water intake) ili liweze kuingiza maji mengi zaidi.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Mwaka 2014 Rais wa Awamu ya Nne alipokuja Makambako aliahidi kutoa Sh.600,000,000/= ili zisaidie kuboresha au kuchimba bwawa la maji Makambako litakalotoa huduma ya maji kwa wananchi wa mji huo:- Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili zifanye kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa maji Makambako. Mradi huu utahusisha ujenzi wa bwawa eneo la Tagamenda, chujio la kutibu maji, matanki ya kuhifadhi maji na ulazaji wa bomba kuu na mabomba ya kusambaza maji. Mradi huu unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 38. Serikali imepata mkopo wa gharama nafuu kutoka Serikali ya India kwa ajii ya utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali wakati inasubiri utekelezaji wa mradi huo mkubwa imechukua hatua za dharura za kuboresha hali ya huduma ya maji mjini Makambako kufuatia ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Mji wa Makambako. Mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 654. Kazi zitakazotekelezwa kwa mradi huu ni pamoja na ujenzi wa kitekeo, tanki, bomba kuu, pampu ya maji na nyumba ya pampu. Kiasi cha shilingi bilioni mbili kimetengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 na zabuni imetangazwa tarehe 4/1/2017 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. AZZA H. HAMAD) aliuliza:-
Je ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya kuchimba Bwawa la Mradi wa Umwagiliaji Masengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya umwagiliaji ya Masengwa ambayo ilijengwa kati ya mwaka 2004 na 2006 chini ya Programu Shirikishi ya Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji, ina eneo lililoboreshwa lipatalo hekta 325. Hata hivyo, eneo linalolimwa linafikia hekta 800. Aidha, kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, tumeshuhudia ukame hali ambayo imewafanya wakulima wawe na hitaji la kujengewa bwawa kwa ajili ya kutunza maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hitaji hilo, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Mwanza, imetenga fedha kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kutoa gharama halisi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo. Aidha, Wizara ilikwishaainisha maeneo yote nchini yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kuandaa mpango kabambe wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wa mwaka 2002 (National Irrigation Master Plan). Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, hivi sasa Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Japan inaendelea na mapitio ya mpango huo ambao utahusisha ujenzi wa mabwawa madogo, ya kati na makubwa kwa nchi nzima.
MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI aliuliza:-
PPRA na TEMESA vimekuwa vyombo vinavyoisababishia Halmashauri zetu hasara kubwa katika utekelezaji wa miradi katika utengenezaji magari na mitambo badala ya kusaidia Serikali katika kutimiza majukumu yake kwa bei nafuu:-
Je, Serikali haioni umefika wakati wa kuvifuta vyombo hivyo au kuvibadilishia utaratibu wake wa kufanya kazi ili viweze kuwa na tija kwa Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Blasius Ole-Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umeanzishwa chini ya Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 ya Wakala. TEMESA ina majukumu ya kusimamia matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali, matengenezo ya mifumo ya umeme, elektroniki na viyoyozi kwenye majengo ya Serikali pamoja na kutoa huduma ya uendeshaji vivuko vya Serikali na ukodishaji wa mitambo. Aidha, TEMESA hutoa huduma za ushauri wa kitaalam kwa Serikali kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013, TEMESA ina jukumu la kutoa huduma zake kwa Serikali. Katika kuboresha utendaji wa TEMESA, Serikali kila mwaka imekuwa ikiwekeza katika kuboresha karakana za TEMESA, ikiwemo kuongeza vitendea kazi vya kisiasa na kuajiri wataalam wenye ujuzi wa magari na mitambo ya kisasa. Kwa sasa TEMESA ina jumla ya Wahandisi 78 na mafundi 344. Serikali pia imebadilisha Menejimenti ya TEMESA kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali itahakikisha kuwa huduma za TEMESA zinaboreshwa na kutolewa kwa ufanisi bila urasimu wowote kwa kufuata Mkataba wa Huduma kwa Wateja na Mwongozo wa Matengenezo ya Magari ya Serikali. Vilevile, Serikali itaendelea kusimamia TEMESA ili kuhakikisha kuwa kuna usimamizi wa karibu wa ubora wa matengenezo ya magari na karakana zake zinatumia vipuri halisi katika matengenezo ya magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa inayoikabili TEMESA ni madeni makubwa ambayo wakala unadai Wizara, Taasisi za Serikali na Halmashauri. Mpaka sasa TEMESA inazidai taasisi hizo zaidi ya shilingi bilioni 11. Kuchelewa kulipwa madeni haya kunaipunguzia TEMESA uwezo wa kutoa huduma. Napenda kutumia fursa hii kuzitaka Wizara, Taasisi za Serikali pamoja na Halmashauri zote zinazodaiwa na TEMESA kulipa madeni yao haraka kabla Serikali haijachukua hatua stahiki.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Barabara mpya ya Mwenge - Tegeta kwa kiwango fulani imesaidia kupunguza tatizo la foleni ingawa ina changamoto kadhaa kama kukosekana kwa taa za kuongoza magari kunakosababisha ajali za mara kwa mara; nyakati za mvua barabara hujaa maji sababu ya udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua hususan eneo la Makonde - Mbuyuni hali inayohatarisha uhai wa wananchi na barabara yenyewe; kuna maeneo hatarishi sana ambayo Serikali inatakiwa ama kuweka matuta au vivuko vya waenda kwa miguu ili kuzuia ajali, miongoni mwa maeneo hayo ni eneo la Bondeni (Jeshini Kata ya Mbezi Juu) karibu na njia panda ya kwenda Kawe:- Je, ni lini changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara zetu ili kusaidia kupunguza ajali hususan barabara ya Mwenge -Tegeta. Mkandarasi wa ujenzi wa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya Afrikana tayari amepatikana na anatarajia kuanza kazi wakati wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua yanayosababisha kero katika eneo la Makonde hadi Mbuyuni, Serikali inakamilisha taratibu za kusaini mkataba wa ujenzi wa mtaro mkubwa eneo la Mbezi Samaki Wabichi ambao utatatua kero ya barabara kujaa maji nyakati za mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Kawe Bondeni hadi Jeshini, Kata ya Mbezi Juu na Kawe tayari limeshapatiwa ufumbuzi. Serikali itajenga daraja la juu kwa ajili ya kivuko cha waenda kwa miguu (Over- Head Pedestrian Bridge) eneo la Kawe Bondeni. Kwa sasa mkandarasi wa kujenga daraja hilo yupo kwenye hatua za maandalizi (mobilization) kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa sana la ukosefu wa maji safi na salama katika Mkoa wa Simiyu pamoja na Wilaya zake ambao ni Bariadi, Itilima, Busega, Maswa na Meatu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji wananchi wa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza utekelezaji wa mradi wa majisafi kutoka Ziwa Victoria katika Mkoa wa Simiyu kwa miji mikuu ya Wilaya za Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima, Busega na vijiji 253 vilivyopo umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu. Tayari Mtaalam Mshauri anakamilisha upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni. Gharama za utekelezaji wa mradi mzima zinakadiriwa kuwa kiasi cha Euro milioni 313. Mradi huu utawanufaisha wakazi wapatao 834,204 na unatarajiwa kutekelezwa katika awamu mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza itahusisha kufikisha maji katika Wilaya ya Bariadi, Itilima na Busega pamoja na vijiji vilivyopo kando kando ya bomba kuu ambapo Benki ya Maendeleo ya Ujerumani imeahidi kutoa Euro milioni 25 na tayari mkataba wa fedha (financial agreement) umesainiwa. Fedha zingine kiasi cha Euro milioni 80 zitatolewa na Global Climate Fund na ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018 na utachukua miaka miwili hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya mradi itafikisha maji katika Wilaya za Meatu, Mji wa Mwanhuzi na Maswa kwa gharama ya Euro milioni 208. Fedha hizi pia zinatarajiwa kutoka katika Global Climate Fund.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa hotuba ya bajeti 2016/2017 Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilionesha kuwa Serikali ya India imesaidia kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya uimarishaji wa huduma ya maji nchini.
Je, Serikali inaweza kutueleza juu ya utekelezaji wa jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Jimbo la Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara yangu ilitoa taarifa ya mchango mkubwa inaoupata kutoka Serikali ya India ili kuboresha huduma ya maji nchini. Kwa kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India, awamu ya kwanza Serikali ya Tanzania ilipata dola za Kimarekani millioni 178.125.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zilizotekelezwa katika awamu ya kwanza ni mradi mkubwa wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ujenzi wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa mradi wa Chalinze-Wami awamu ya tatu. Utekekelezaji wa kazi ya upanuzi wa ruvu juu na ulazaji wa bomba kutoka Mlandizi hadi Kimara umekamilika na miradi ya ujenzi wa mfumo wa usambazji maji kwa Jiji la Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa mradi wa Chalinze-Wami awamu ya tatu inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya pili, Serikali ya India itatoa fedha dola za Marekani milioni 268.35 kwa ajili ya mradi mkubwa wa kutoa maji katika mradi wa KASHWASA kutoka kijiji cha Solwa kwenda katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Tinde na Uyui pamoja na vijiji 89 vinavyopitiwa na bomba kuu umbali wa kilometa 12 kila upande, wakandarasi wa kutekeleza mradi huo wamepatikana na wapo katika hatua ya maandalizi ya utekelezaji (mobilization).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya tatu Serikali ya India imeahidi kutoa fedha kiasi cha dola milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 16 ya Tanzania Bara pamoja na miradi ya maji upande wa Zanzibar. Hatua inayoendelea kwa sasa ni kufanya manunuzi ya Mhandisi Mshauri atakayefanya mapitio ya usanifu wa miradi na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi, kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda lililopo katika kata ya Serembala, Morogoro Kusini umesababisha matatizo makubwa kwa wananchi wa kata ya Serembala, Magogoni na vijiji jirani kutokana na fidia kidogo kwa kupisha ujenzi wa mradi huo ikilinganishwa na mali walizoziachia yaani mashamba, nyumba zao na mali nyingine zilizo kwenye maeneo makubwa ya ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya mradi huo.
(a) Je, Serikali iko tayari kurudia zoezi la tathmini ya mali za wanavijiji wote walioathirika kwa kutoa nyumba na mashamba yao ili kupisha mradi wa bwawa la Kidunda na kuwalipa fidia wanayostahili?
(b) Je, Serikali iko tayari kwenye bajeti hii kumalizia malipo ya takribani shilingi bilioni 3.7 kuwafidia wananchi hao kulingana na tathmini iliyofanyika?
(c) Je, Serikali itakuwa tayari kuwawekea miundombinu ya uanzishwaji wa mashamba ya umwagiliaji na viwanda vidogo vidogo kwenye kata ya Serembala kwa ajili ya kutoa ajira kwa wananchi Serembala Magogoni, Mvuna na Kkata za jirani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaandaa malipo ya fidia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 ambayo inaelekeza pia kuwa endapo malipo ya fidia yatachelewa kulipwa kwa zaidi ya miezi sita tangu kupitishwa, mlipaji anapaswa kufanya mapitio na kulipa nyongeza kutokana na muda uliozidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 7.4 kwa familia 2,603 kama fidia ya kupisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2017/2018, kwa ajili ya fidia kulingana na tathmini iliyofanyika. Malipo yamekuwa yanafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Kidunda linajengwa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi maji ya matumizi ya majumbani kwa wakazi wa Kibaha, Bagamoyo na Dar es Salaam. Bwawa hilo halitahusu kilimo kikubwa cha umwagiliaji. Serikali itaangalia uwezekano mwingine wa kuweka miundombinu wezeshi ya kilimo cha umwagiliaji kulingana na maeneo husika.(Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Serikali imekamilisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Mji wa Ngudu na vijiji vilivyo karibu na Mji huo Wilayani Kwimba, mradi huu unatoa maji ya uhakika kuliko miradi ya visima vifupi ambavyo ni vya msimu, lakini Mji Mdogo wa Malampaka na vijiji vingine vya karibu kama Jihu, Bukigi, Muhida, Lali, Nyabubinza na Mwang’horoli ambavyo vipo karibu na Mji wa Ngudu havijaunganishwa kwenye mradi huo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha Mji Mdogo wa Malampka na vijiji vya Jihu, Bukigi, Muhida, Lali, Nyababinza na Mwang’horoli katika mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetekeleza mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Mji wa Ngudu na vijiji vilivyopo kandokando ya bomba linalopeleka maji katika Mji wa Ngudu. Vijiji hivyo ni Runele, Ngatuli, Nyang’onge, Damhi na Chibuji. Mradi huu ulihusu ulazaji wa bomba kilomita 25 na sehemu nyingine ya bomba lilitumika bomba la zamani la mradi wa visima uliojengwa miaka ya 70. Bomba hilo ni la kipenyo cha inchi nane na kulingana na usanifu halitoshi kupeleka maji kwenda Malampaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inatekeleza miradi ya maji Malampaka, Sayusayu, Mwasayi, Njiapanda na Sangamwalugesha, ambapo miradi hii imekamillika na wananchi wanapata maji.
Aidha, miradi ya maji ya Lalagomandang’ombe na Jija inaendelea kujengwa na ujenzi umefikia asilimia 50. Serikali pia imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa miradi ya maji ya Mwabulimbu, Mwamanenge, na Badi ambao utahudumia vijiji vitatu vya Muhiba, Jihu na Badi yenyewe. Ujenzi wa miradi hii utafanyika katika awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda kwenye Miji ya Sumve, Malampka na Mallya. Hadi sasa taratibu za kumpata mtaalamu mshauri atayefanya usanifu wa mradi huo zianendelea. Hivyo, baadhi ya vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge vitajumuishwa katika mradi huo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huo.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mwezi Juni, 2015 Serikali ya Falme ya Kuwait kupitia Wakfu ya Kuwait iliijulisha Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kuwa wapo tayari kufadhili mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Delta ya Mto Luiche.
Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi huo ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini, kujenga viwanda vidogo vya mazao ya kilimo na kuondoa umaskini kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kilimo cha umwagiliaji unaopendekezwa katika Bonde la Mto Luiche, Manispaa ya Kigoma Ujiji una wastani wa eneo la hekta 3,000 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga. Mnamo mwaka 2015 Serikali iliwasilisha ombi kwa Serikali ya Falme ya Kuwait kuhusu uendelezaji wa mradi huo ambapo Serikali ya Falme ya Kuwait ilikubali kwa masharti ya kupewa taarifa ya upembuzi yakinifu (feasibility study report) na maoni kutoka kwa nchi zinazotumia maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma hii, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu wa awali mwaka 2015. Hivi sasa Serikali ipo katika hatua ya manunuzi ya mtaalamu mshauri kwa ajili ya kazi ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi hii ikikamilika Serikali itawasilisha taarifa ya kina ya kiwango cha maji kinachohitajika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
MHE. OMARI M. KIGUA alijibu:-
Moja ya changamoto kubwa inayokabili maeneo mbalimbali nchini ni huduma ya maji safi na salama. Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kitaifa kama Benki ya Dunia wamekuwa wakitoa ahadi za kuwezesha miradi mikubwa ya maji nchini lakini mara nyingi wamekuwa hawatekelezi ahadi zao.
Je, Serikali haioni sasa imefika wakati wa kuweka mikakati ya dhati ya kutenga bajeti kwa kutumia mapato ya ndani ili kutoathiri miradi ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NAUMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia wameendelea kutoa ahadi na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji safi na salama hapa nchini. Kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha ya 2006/2007 hadi Julai 2017 Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilianzisha Mpango wa Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo jumla ya miradi 1,810 iliibuliwa na tayari miradi 1,333 imekamilika na miradi 477 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha fedha za ndani zinazotengwa na zinatekeleza miradi ya maji nchini kote, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maji ambao umeimarisha upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maji kwa wakati na fedha na hizo za mfuko zimetoa kipaumbele kwa miradi ya maji vijijini. Serikali itaendelea kubuni vyanzo vingine vya fedha za ndani ili miradi mingi ya maji itekelezwe kwa wakati na wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutumia mapato ya ndani pamoja na uanzishaji wa mfuko wa maji inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya miradi ya maji mfano mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 690 ambayo ni sawa na asilimia 75 ni fedha za ndani na mwaka wa fedha 2017/ 2018 shilingi bilioni 408.6 sawa na asilimia 66 ya bajeti yote ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
MHE. LAZARO S. NYALANDU aliuliza:-
Vijiji vyote vya Tarafa ya Ilongero, Mtinko na Mgori bado vinahitaji mfumo wa usambazaji maji kutoka visima virefu vilivyopo kwenye baadhi ya vijiji na tarafa hizo tatu zinahitaji kuongezewa visima virefu na mabwawa ya kuhifadhia maji ya mvua.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanikisha mradi huo ili kuwaondolea adha wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Samuel Nyalandu, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Singida inaendelea kushirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana. Hadi sasa wananchi wanaopata huduma ya maji kwa Halmashauri ni asilimia 53 sawa na wakazi 130,908.
Mheshimiwa Spika, katika Tarafa ya Ilongero kuna miradi 24, Tarafa ya Mtinko kuna miradi 14 na Tarafa ya Mgori kuna miradi kumi iliyokamilika na inatoa huduma ya maji. Miradi mingi kati ya hii inatumia nguvu ya nishati ya jua kuendesha mitambo ambayo imeunganishwa moja kwa moja kwenye chanzo au kisima na kujengewa kituo kimoja cha kuchotea maji.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri imeanza kufanya upanuzi wa miundombinu ya maji katika kijiji cha Pohama, Tarafa ya Mgori, ambao umefikia asilimia 90 ya utekelezaji. Halmashauri inaendelea kufanya usanifu wa miradi ya maji kwa ajili ya ujenzi wa mitandao ya mabomba kutoka kwenye visima katika vijiji vya Mtinko na Ghalunyangu, Tarafa ya Mtinko na Ngamu, Tarafa ya Ilongero. Aidha, ujenzi wa miradi hiyo unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Halmashauri imepanga kuchimba visima virefu na kujenga mitandao ya mabomba katika vijiji 11 na vijiji hivyo ni pamoja na Merya, Mughamo, Mughunga, Msange, Itaja, Mudida, Ughandi, Kijota, Mwasauya, Mtinko na Mwakiti. Pia kufanya ukarabati na upanuzi wa miradi katika Vijiji vya Msange, Ghalunyangu, Ngimu, Mdilu, Mwasauya, Pohama, Nkwae, Msisi na Sagara.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Ulumi kilichopo Kata ya Ulumi ambao ulianza kujengwa mwaka 2010 haujakamilika mpaka sasa.
(a) Je, ni sababu zipi zimefanya mradi huo kutokamilika mpaka sasa na ni lini utakamilika?
(b) Je, Serikali ilitenga kiasi gani cha fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 ili kukamilisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji Ulumi ulianza kujengwa mwaka 2012 kwa kujenga banio lenye gharama ya shilingi milioni 213,279,000 kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Msaada wa Chakula baina ya Serikali ya Tanzania na Japan bila kuhusisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji mashambani ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.3 zinahitajika kukamilisha kazi zote. Aidha, Wizara yangu hivi sasa inafanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa lengo la kuihuisha ili uendane na hali ya sasa. Kazi hii inatarajia kukamilika mwezi Septemba mwaka 2018 na kupitia mpango huu Mradi wa Ulumi ni miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbele kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji kwa manufaa ya wananchi wa Ulumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa mradi huu kwa wananchi wa Kalambo, Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2018/2019 itaingiza mradi huu katika bajeti kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili mradi huu uweze kuanza utekelezaji.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Matatizo ya mipaka kati ya hifadhi na wanakijiji wanaopakana na maeneo ya Hifadhi ya Bwawa la Igombe katika Jimbo la Tabora Mjini ni ya muda mrefu hususani katika Kata za Kabila, Ikomwa na Misha.
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo wa mipaka ambao ni wa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bwawa la Igombe ambalo ni chanzo cha sasa cha maji katika Mji wa Tabora lilijengwa na kukamilika mwaka 1958 chini ya Serikali mkoloni Mwingereza. Bwawa hilo lina eneo la hifadhi lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 12,000. Sehemu ya eneo hilo linalohifadhi maji ni Kilometa za mraba 4,144 ndani ya hifadhi ya msitu wa Igombe, hivyo sehemu ya bwawa inazungukwa na hifadhi msitu wa Igombe na mipaka yake ipo kisheria na imekuwa ikilindwa na kuheshimiwa hata wakati wa operation vijiji ya mwaka 1974.
Mheshimiwa Spika, tatizo la msingi lililopo hapa ni kwamba baadhi ya wananchi wanaozungula Msitu wa Bwawa la Igombe wanataka uhalali wa kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kutumia kama malisho ya mifugo, kukata miti kwa ajili ya mbao na nishati ya mkaa, kulima bustani kando kando ya bwawa kwa kutumia maji ya bwawa hususani nyakati za kiangazi, utafutaji wa madini na baadhi ya wananchi kudiriki hata kuanzisha makazi ndani ya ene hilo.
Mheshimiwa Spika, mipaka ya Hifadhi ya Msitu wa Igombe iliainishwa vizuri na Ofisi ya Bonde la Ziwa Tanganyika na Wizara ya Maliasili na Utalii hivyo Serikali itaendelea kulinda mipaka hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa kata zinazoizunguka hifadhi hiyo ili kuhakikisha kuwa bwawa hilo na hifadhi yote inakuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
MHE. RADHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Skimu ya Umwagilaji ya Mng’aro imekuwa haina ufanisi mzuri tangu kuanzishwa kwake.
(a) Je, ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya skimu hiyo ili kuleta tija?
(b) Je, ni lini skimu hiyo itakaguliwa ili kuondoa malalamiko ya ubadhirifu wa mali za ushirika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagilaji Mng’aro (Kitivo) ipo katika Kijiji cha Mng’aro Wilaya ya Lushoto na iliibuliwa na wananchi miaka ya 1980 kwa ajili ya kuzalisha mazao ya mpunga, mahindi, maharagwe na mboga mboga. Uzalishaji wa mazao katika skimu hiyo haukuwa na tija kwa kuwa wakulima hawakuwa na miundombinu bora ya umwagiliaji ambayo ilikuwa inasababisha upotevu mkubwa wa rasilimali maji na wakati mwingine kukosa kabisa mavuno kutokana na mafuriko au ukame.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, Serikali iliboresha skimu hiyo kati ya mwaka 1988 na 1995 kupitia fedha kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa kwa kujenga banio kuu la kuchepusha maji kutoka Mto Umba, kuchimba na kusakafia mifereji mikuu ya kupeleka maji mashambani, kujenga vigawa maji na vivuko vya mifereji, kuchimba mifereji ya matupio ambayo ni mifereji ya kutolea maji ya ziada mashambani na kujenga barabra za kupeleka pembejeo na kutolea mazao mashambani.
Mhesmiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali itaingiza skimu hii kwa lengo la kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ili wannachi waendelee kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi za Serikali, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kushirikiana na Serikali kuhamasisha wafaidika wakulima wa skimu hiyo ili waweze kuchangia mfuko wao wa uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya umwagiliaji iliyokwishajengwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, itatuma wakaguzi kukagua nyaraka mbalimvbali cha Chama cha Ushirika cha Skimu ya Mng’aro (Kitivo) Kijiji cha Mng’aro ili kuona kama kuna ukweli juu ya tuhuma za ubadhirifu wa mali za ushirika na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kufanya ubadhirifu.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne iliahidi kupeleka maji katika vijiji vya Nkata, Ntemba, Kitosi, Ntuchi, Isale hadi Msilihofu kupitia mradi uliokuwa na thamani ya shilingi bilioni 2.8 na vilevile ahadi hiyo imetolewa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Je, mradi huo umefikia hatua gani?
Je, ni lini hasa wananchi wategemee kutatuliwa kwa kero yao ya ukosefu wa maji safi kupitia mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa maji wa Isale ulisanifiwa mwaka 2013 katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kupitia mpango wa vijiji kumi kwa kila Halmashauri. Mradi huu ulilenga kukipatia maji Kijiji cha Isale kutoka Mto Nzuma. Mwaka 2014 utekelezaji wa mradi huu ulisimama kwa muda ili kufanya mapitio ya usanifu wa mradi utakaojumuisha pia mahitaji ya huduma ya maji kwa wananchi wa vijiji vya Ntuchi, Nkata, Mtemba na Msilihofu.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya awali ya usanifu iliwaislishwa na Mtaalam Mshauri na kujadiliwa kwa pamoja na Halmashauri na Mkoa ambapo Mtaalam Mshauri ameelekezwa kufanya marekebisho ili kukidhi mahitaji halisi ya vijiji vyote. Mapitio ya usanifu yatakamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2017 na mradi utatekelezwa katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyoanza kutekelezwa mwezi Julai, 2016 na utakapokamilika utatatua kero ya ukosefu wa maji safi kwa wananchi wa Nkasi Kusini.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya maji.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya maji ya Kata za Chanika, Kipunguni na Majohe ili wananchi wa Kata hizo na maeneo ya jirani wapate maji ya uhakika?
(b) Je, ni lini Serikali itachimba bwawa kubwa katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu ili ng’ombe wanaouzwa hapo wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kukamilisha miradi ya maji katika Kata za Chanika, Kipunguni na Majohe. Miradi mingi imekamilika na inahudumia wananchi na mingine ipo katika hatua za mwisho za ujenzi. Miradi iliyokamilika ni pamoja na Kipunguni B, Kwa Mkolemba, Chanika Shuleni, Majohe, Nyang’andu na Msongola. Miradi inayoendelea kujengwa ni bomba mbili za Kipunguni B, ambao unatekelezwa na Manispaa ya Ilala. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kuleta maji katika maeneo ya Pugu kutoka katika mradi mkubwa wa visima virefu vilivyopo Mpera katika Wilaya ya Mkuranga. Kazi ya uchimbaji wa visima hivi inaendelea na matarajio ni kukamilisha uchimbaji mwaka huu wa fedha na baada ya hapo Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha maji hayo hadi Pugu na kuyasambaza maeneo yote ya Pugu, Chanika, Ukonga, Gongolamboto, Kinyerezi, Kitunda, Kipawa, Yombo na maeneo ya barabara ya Nyerere kuanzia Pugu hadi TAZARA.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Wananchi wa Kisiwa kidogo cha Jibondo – Wilayani Mafia wamekuwa na shida kubwa ya maji.
Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa muda mrefu wa kuvusha maji kutoka Kisiwa Kikuu eneo la Kiegeani kwenda Kisiwani Jibondo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutatua tatizo la maji katika Kisiwa cha Jibondo kwa awamu ambapo kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitumia kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa kisima, ujenzi wa nyumba ya pampu na kukiunganisha na umeme kituo cha kusukuma maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya mradi itaanza mwanzoni mwa mwezi Juni, 2017 na kazi zitakazotekelezwa ni usanifu, uandaaji wa nyaraka za zabuni, kumpata Mkandarasi na ujenzi wa kuunganisha bomba la maji safi chini ya bahari eneo la kutoka Kiegeani kwenda katika Kisiwa cha Jibondo. Ujenzi wa mradi huo utaanza mwaka wa fedha 2017/2018 na utanufaisha wananchi wapatao 3,000.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaunganisha Jimbo la Ulyankulu katika miradi ya maji toka Ziwa Victoria na maji toka Mto Malagarasi?
(b) Je, Serikali iko tayari kuyakinga maji ya Mto Igombe ili kuwa na bwawa kubwa ambalo litapunguza shida ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza utekelezaji wa mradi kutoa maji kutoka Mto Malagarasi kwa ajili ya kuleta maji katika Miji ya Urambo, Kaliua, Nguruka na Usoke. Mradi huu pia utahudumia baadhi ya vijiji vilivyopo Wilayani Uvinza na maeneo mengine ya Wilaya ya Uyui, Manispaa ya Tabora na vijiji vitakavyokuwa umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu. Mradi huu utasaidia kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wengi zaidi kwa kuwa Mto Malagarasi unayo maji mengi yanayotiririka wakati wote wa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jimbo la Ulyankulu, Serikali imemuagiza Mhandisi Mshauri katika usanifu unaoendelea kuweka matoleo kwa ajili ya upanuzi wa mradi kwa awamu zitakazofuata ili wananchi wengi zaidi wakiwemo wa Ulyankulu waweze kufaidika na mradi huo. Usanifu wa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni, 2017.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la kukinga maji ya Mto Igombe kwa ajili ya kujenga bwawa kubwa linahitaji kufanyiwa utafiti na usanifu wa kina ii kulinganisha gharama za uwekezaji na manufaa ya mradi huo. Mipango ya Serikali katika kuendeleza hifadhi ya vyanzo vya maji ni pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa. Aidha, kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji Serikali imetoa wito katika Halmashauri zote nchini kuanza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa madogo ambayo yatasaidia kutatua shida ya maji kwa wananchi, mifugo pamoja na umwagiliaji. Kwa sasa Ulyankulu inapata maji kutoka kwenye visima virefu.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi sana kuanzisha miradi mikubwa na midogo ya maji.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza ni miradi gani mikubwa na midogo iliyokamilika na isiyokamilika katika Jimbo la Nyang’hwele?
(b) Je, kama kuna miradi ambayo haijakamilika mpaka hapo ilipofikia imetumia fedha kiasi gani?
(c) Je, ni lini sasa miradi hiyo itakamilika katika Jimbo la Ngang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Nyang’hwele inatekeleza mradi mkubwa mmoja wa Nyamtukuza kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Mradi huu utahudumia jumla ya vijiji tisa vya Nyamtukuza, Nyarubele, Kakora, Kitongo, Ikangala, Kharumwe, Izunywa, Kayenze na Bukwimba ambavyo vinaendelea na ujenzi. Miradi ya maji iliyokamilika katika Halmashauri ya Nyang’hwale ni Kanyenze, kakora, Ikangala, Nyamtukuza na Kharumwa.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Nyamtukuza unaotuma chanzo cha Ziwa Victoria unatekelezwa kwa jumla ya fedha shilingi bilioni 15 na mpaka sasa Serikali imepeleka fedha shilingi bilioni 3.78 za kutekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Serikali ni kutuma fedha kwa Halmashauri zote zinazoendelea na ujenzi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote iliyoanza inakamilika kabla ya kuanza kwa miradi mipya.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Mji wa Liwale unakuwa kwa kasi lakini una chanzo kimoja cha maji ambacho kwa sasa hakiwezi kukidhi mahitaji hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa maji.
• Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji wa maji?
• Je, mradi wa kumwagilia wa Ngongowele utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha huduma ya maji ili kuwaondolea adha wananchi wa Mji wa Liwale, Serikali katika mpango wa muda mfupi imepanga kukarabati na kupanua mtandao wa majisafi, kununua na kufunga dira za maji kwa wateja, kukarabati chanzo cha maji na kukarabati matenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hizo zinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2017/2018. Kiasi cha shilingi milioni 300 kimetengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kazi hizo.Taratibu za kumpata mkandarasi atakayetekeleza kazi hiyo zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.5 katika bajeti wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni katika Miji Mikuu ya Wilaya nchini ikiwemo na Mji wa Liwale. Taratibu za kumpata mtaalam mshauri atakayetekeleza kazi hizo zinaendelea. Kukamilika kwa upembuzi na usanifu wa kina kutatoa gharama halisi ya utekelezaji wa mradi mkubwa katika Mji wa Liwale pia idadi ya Kata zitakazonufaika na mradi huo wa maji zitajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya umwagiliaji ya Ngongowele iliyopo Kata ya Ngongowele, Wilayani Liwale iliibuliwa mwaka 2008. Ujenzi wa skimu hii ulifanyika kwa awamu tatu kati ya mwaka 2009 na 2012 kwa kujenga banio, vigawa maji, kivusha maji, vivuko vya watembea kwa miguu, pamoja na kuchimba mifereji miwili yenye urefu wa jumla wa mita 4,800 ambapo mita 1,080 tayari zimesakafiwa. Aidha, kwa miaka miwili mfululizo 2010/2011 na 2011/2012 skimu hii ilikumbwa na mafuriko makubwa na kusababisha uharibifu wa baadhi ya miundombinu ambayo hata hivyo baadhi imefanyiwa marekebisho ili kudhibiti uharibifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na mapitio ya miradi yote ya umwagiliaji hapa nchini ili kubaini mahitaji na gharama za ukarabati ama kujengwa upya. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jimbo la Nyamagana lina ukubwa wa kilometa za mraba 256, kati ya hizo kilometa za mraba 71.56 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria lakini bado wananchi wake hawapati maji ya uhakika ya bomba hasa kwa zile Kata zilizoko nje ya Mji.
Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa wananchi wa Nyamagana wanapata maji ya uhakika hasa ikizingatiwa kuwa wamezungukwa na Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya maji katika Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza inatolewa kwa asilimia 90 ya wakazi wote wa Wilaya hiyo. Hata hivyo baadhi ya wakazi ambao wanaishi sehemu za mwinuko pamoja na wanaoishi pembezoni mwa Jiji wanakosa huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua hilo imepata mkopo wa masharti nafuu kutoka European Investment Bank (EIB)kiasi cha Euro milioni 54 sawa na shilingi bilioni 110 ili kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Mwanza kwa kuhusisha Wilaya za Nyamagana na Ilemela. Mkandarasi wa utekelezaji wa mradi huo amepatikana na ujenzi umeanza. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na kuboresha huduma ya majisafi katika maeneo ya milimani hususani yaliyo juu ya matenki ya maji ambayo hayapati huduma kwa sasa, kubadilisha mabomba ya zamani yaliyochakaa na kuongeza mtandao wa mabomba pamoja na upanuzi na kuboresha miundombinu ya majitaka na mabwawa ya kutibu majitaka. (Makofi)
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-
Miradi mbalimbali ya maji katika Jimbo la Kalenga imesimama kutokana na wakandarasi kutolipwa licha ya wananchi kukabiliwa na tatizo la maji.
Je, ni lini Wakandarasi hao watalipwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imeendelea kutekeleza miradi mitano ya maji katika Vijiji vya Igangidung’u, Kikombwe, Weru, Mfyome, Magunga - Isupilo
- Itengulinyi - Lumuli kuanzia mwezi Juni, 2012. Gharama ya miradi yote ni shilingi 4,060,691,054 ambapo hadi mwezi Machi, 2017 kiasi cha fedha zilizokuwa zimelipwa kwa wakandarasi waliofanya kazi ni shilingi 3,027,831,071 sawa na asilimia 74.56. Hadi sasa miradi minne ya Vijiji vya Igangidung’u, Weru, Mfyome na Kikombwe imekamilika na inatoa huduma ya maji. Miradi hii ilikuwa na gharama ya shilingi 1,862,549,397 na kiasi cha shilingi 1,716,002,352 kimelipwa na kilichobaki kitalipwa baada ya kipindi cha matazamio (defects liability period) kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Magunga - Isupilo
– Itengulinyi – Lumuli wenye mkataba wa gharama ya shilingi 2,198,141,657 ulisimama mwezi Julai mwaka 2015 wakati mkandarasi akiwa amelipwa shilingi 1,311,828,719 na utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 45. Kutokana na kuchelewa kwa malipo, mkandarasi alifungua kesi ya madai (Adjudication na Arbitration NCC) ya kulipwa riba kwa kucheleweshewa malipo ya interest pamoja na standby cost zinazofikia shilingi 939,276,170. Halmashauri haikukubaliana na madai hayo, hivyo, mkandarasi (RJR Construction Co. Ltd) akafungua shauri la madai (arbitration NCC) na shauri limeshasikilizwa tunasubiri uamuzi wa arbitrator ili tujue hatma ya madai hayo. Ni azma ya Serikali kuendelea na ujenzi wa mradi ili ukamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuleta fedha ili kuwalipa Wakandarasi kulingana na kazi zilizofanyika na kuhakikiwa. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Kwa mujibu wa Sera ya Usambazaji wa Maji kutoka bomba kuu litakalotoa maji ya Ziwa Victoria kutoka Kahama hadi Tabora Mjini, ni kwamba vijiji vyote vilivyo ndani ya kilometa 12 toka bomba kuu vitaunganishwa na maji.
Je, ni vijiji vingapi vya Jimbo la Bukene ambavyo vimo ndani ya kilometa 12 vitaunganishwa maji kutoka bomba kuu hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa naiba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupitia Kahama una lenga kuwapatia huduma ya maji wakazi wa Miji ya Tabora, Uyui, Nzega na Tinde pamoja na vijiji 89 vilivyopo ndani ya eneo la kilomita 12 kila upande wa bomba kuu la Mradi wa KASHWASA. Mradi huu ni wa malengo ya muda mrefu ya kuwapatia huduma ya maji ya uhakika wananchi wapatao milioni 1.1 wa maeneo hayo. Ujenzi wa mradi umegawanyika katika Awamu Mbili. Awamu ya Kwanza itahusisha kupeleka maji katika Miji ya Tabora, Igunga, Uyui, Nzega na Tinde. Kazi zitakazotekelezwa katika awamu hiyo ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu kutoka Kijiji cha Solwa, ulazaji wa mabomba na ukarabati wa mitandano ya usambazaji maji katika miji hiyo. Awamu ya Pili mradi itahusu kupeleka maji katika Mji wa Sikonge kutoka Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo la Bukene lililopo katika Halmashauri ya Nzega Vijijini, jumla ya vijiji vitatu vya Iboja, Ilagaja na Chamipulu vitapata huduma ya maji kupitia bomba kuu la kutoa maji Ziwa Victoria kutoka Kijiji cha Solwa kwenda Nzega. Kwa vijiji vingine ambavyo vipo umbali zaidi ya kilometa 12, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji hivyo kwa kutumia vyanzo vingine vya maji. Kazi hii itaendelea kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya kazi hiyo. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Wakulima wa Wilaya ya Mbozi wamekuwa wakitegemea mvua za msimu zisizotabirika katika kilimo chao.
Je, Serikali haioni kwamba huu ni wakati muafaka wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya hivi karibuni, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeanza kuathirika na vipindi vya ukame hata wakati wa msimu wa mvua, tofauti na ilivyokuwa miaka ya huko nyuma. Kutokana na hali hiyo, halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilikwishaanza kutekeleza mipango ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika wilaya hiyo kupitia mipango ya kuendeleza kilimo cha wilaya. Kupitia mipango hiyo, Skimu za Umwagiliaji za Sasenga (hekta 540), Iyula (hekta 180), Songwe (hekta 250), Bara (hekta 300), Mbulu Mlowo (hekta 100), Mkombozi (hekta 150), Ikumbilo Chitete (hekta 60), Ruanda Mbulu (hekta 52) na Wasa (hekta 45) ziliainishwa na kuanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ina mpango wa kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo yanayofaa kujengwa mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa maji ya umwagiliaji kwa ajili ya Skimu za Nambizo, Msia na Hamwelo katika Halmashauri hiyo.
Aidha, kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Halmashauri zote zinazotekeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Serikali ilianzisha mradi wa kupeleka maji kwenye Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Dodoma toka Ziwa Victoria Mkoani Mwanza; mradi huu ulisaidia upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na shughuli za kilimo.
Je, kwa nini Serikali isianzishe mradi kama huu kutoa maji kwenye Mito ya Ruvuma na Rufiji kwa ajili ya wakazi wa Lindi na mikoa jirani ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji na kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza miradi miwili mikubwa ya kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara/ Mikindani na Miji ya Mangaka. Kwa upande wa Manispaa ya Mtwara/Mikindani, Wizara imekamilisha taratibu zote za manunuzi hadi kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara/Mikindani pamoja na vijiji 26. Kwa sasa kinachosubiriwa ni kusaini mkataba wa kifedha baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kupitia Benki ya Exim.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mji wa Mangaka upembuzi yakinifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka katika mji huo pamoja na vijiji 26 umekamilika mwezi Oktoba, mwaka 2016. Kwa sasa kazi ya usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uanzishwaji wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji, Wizara itaendelea kutafuta fedha za kufanya utafiti ili kuwa na michoro na thathmini ya kiutaalam ili kutayarisha andiko litakalosaidia kutafutwa fedha za utekelezaji wa mradi huo kutoka vyanzo vya ndani na nje ya Serikali. Malengo ya miradi hii yote ni kutoa huduma ya maji safi na salama. Pia Serikali itaangalia uwezekano wa kuanzisha miradi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Lindi na mikoa jirani.
MHE. MARY P. CHATANDA (K.n. y. MHE. STEPHEN H. NGONYANI) aliuliza:-
Serikali ilitenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi lakini baadaye Serikali ilihamishia fedha hizo Mkoa mwingine.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha pesa hiyo ili Bwawa lililokusudiwa lijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2003 na 2004 wananchi wa kijiji cha Manga Mkocheni, kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe walionesha hitaji la mradi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga katika Bonde la Mkomazi. Aidha, mwaka wa fedha 2006/2007 Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa wakati huo kupitia Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanyika upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ambapo walibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni kumi na tatu zingehitajika kuendeleza Bonde la Mkomazi ikiwemo ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo, usanifu huo ulibaini kuwa bwawa hilo lingezamisha Ziwa Manga lililopo katika Kijiji cha Manga, ambalo lina maji ya chumvi ambayo yangeathiri kilimo cha zao la mpunga. Kutokana na changamoto hii mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilianza kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu kwa kuepuka kuzamisha Ziwa Manga na kubaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufikia azma hii Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016 ilitenga jumla ya shilingi milioni mia nane kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi. Hata hivyo bajeti ya maendeleo kwa fedha za ndani iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji ikiwemo Bwawa la Mkomazi haikutolewa na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezwa. Sambamba na fedha hizo kutotolewa bado kuna baadhi ya wananchi ambao walikuwa wanaukataa mradi kwa sababu ya maeneo yao kuzamishwa ndani ya maji na hivyo kufanya mazingira ya kutekeleza mradi huo kutokuwa rafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi walio wengi wa Kata ya Mkomazi kupitia Mheshimiwa Mbunge bado wanaona umuhimu wa mradi huo na hasa katika hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji italiingiza bwawa hili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza utekelezaji ili hatimaye lengo la Serikali na wananchi wa Mkomazi waweze kuwa na kilimo cha uhakika na hivyo kuwa na usalama wa chakula na kujiongezea kipato kupitia zao la mpunga.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Mji wa Songea ni kati ya Miji yenye matatizo makubwa ya maji katika nchi yetu na katika utoaji wa maji, Halmashauri ya Mji wa Songea inategemea visima virefu na vifupi na maji ya mtiririko. Mji huo una jumla ya vituo 187 ambavyo havitoi maji ambapo kila kituo kinagharimu wastani wa shilingi milioni tatu (3) kwa ajili ya ukarabati, gharama zote ni jumla ya shilingi milioni 561.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kumaliza tatizo hilo?
(b) Je, Serikali haioni kuwa ikondoa tatizo hilo itakuwa imemaliza kero kubwa kwa wananchi zaidi ya 30,000 ambapo kila kituo kitakuwa kinahudumia watu 250?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Manispaa Songea una wastani wa watu wapatao 230,000, ambapo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea inatoa huduma katika maeneo ya mji yanayokadiriwa kuwa na jumla ya wananchi 194,000 na pembezoni mwa mji kuna wastani wa wakazi wapatao 36,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya pembezoni mwa mji kuna vituo vya kuchotea maji 187 vilivyogawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni visima vifupi 89 na kundi la pili ni vituo vya kuchotea maji kutoka katika mradi wa maji wa mtiririko.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikwishaona umuhimu wa kumaliza tatizo la maji katika Manispaa ya Songea na kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha fedha shilingi milioni 314 kilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa visima vifupi 89 ambavyo ufanisi wake umepungua. Taratibu za kumpata mzabuni wa kufanya kazi hiyo zimekamilika na tayari mkataba umesainiwa mwezi Mei 2017 na Mkandarasi ataanza kuleta pampu hizo mwishoni mwa mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali itakarabati vituo vingine 98 vilivyobaki, hivyo huduma ya maji itakuwa imeboreshwa na wananchi zaidi ya 30,000 waishio pembezoni mwa Mji wa Songea watapata huduma ya maji. Vilevile Serikali imetenga Dola za Marekani milioni 50.89 zitakazopatikana toka mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 toka India ili kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Songea.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Jimbo la Kibamba linapaswa kuhudumiwa kwa sehemu kubwa na maji ya kutoka mtambo wa Ruvu Juu:-
(a) Je, ni maeneo gani mpaka sasa yana shida kubwa ya maji na lini maeneo hayo yatapata huduma kamili ya maji?
(b) Je, ni kwa nini miradi mikubwa ya maji imechelewa kukamilika kinyume na ratiba iliyotolewa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu ni pamoja na Mlandizi, Visiga, Misugusugu, Kongowe, Picha ya Ndege, Tumbi, Pangani, Kibaha, Maili Moja, Kiluvya, Kibamba, Kwa Yusufu, Mbezi, Makabe, Msakuzi, Malamba Mawili, Msigani, Matosa, Kimara, Kibangu, Makuburi, Tabata, Segerea, Kinyerezi na Kipawa. Maeneo yote haya yataanza kupata maji baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusambaza maji ambao unaendelea kutekelezwa na kampuni ya Jain Irrigation Systems Limited. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine mikubwa inachelewa kukamilika kutokana na sababu mbalimbali ambazo ni pamoja na kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za ujenzi, ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa miradi, changamoto za kiufundi na kuchelewa kuwasili kwa mitambo na vifaa kutoka nje ya nchi kwa miradi yenye kuhitaji mitambo hiyo. Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo. Kwa sasa utekelezaji wa miradi mingi mikubwa unaenda vizuri.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Hitaji la kuni limekuwa kubwa kwa matumizi kama nishati ya kupikia na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira:-
Je, Serikali itawezesha vipi wananchi kupata nishati mbadala kwa matumizi ya kupikia majumbani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha Uendelezaji na Usambazaji wa Teknolojia za Kilimo Vijijini (CAMARTEC) inaendelea na ujenzi wa mitambo ya bayogesi nchini kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine majumbani, taasisi za Serikali zikiwemo shule, hospitali na Magereza. Hadi sasa mitambo ya bayogesi iliyojengwa inafikia 20,000. Lengo la kituo ni kujenga jumla ya mitambo 22,000 kwa nchi nzima ifikapo mwaka 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009 Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ilianza kutekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kupitia mradi wa mfano (Pilot Project) kwa ajili ya kupikia majumbani. Hadi sasa hoteli tatu, gereza moja, nyumba 70 na viwanda 36 vinatumia gesi asilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, TPDC imekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Miradi ya usambazaji wa gesi asili katika mikoa hiyo utaanza mwaka 2018 na kukamilika mwaka wa 2020/2021 kwa kuwafikishia gesi wateja wapatao 50,410. Miradi hii itagharimu jumla ya dola za Marekani milioni 126.959.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Julai, 2017, Serikali kupitia TPDC itaanza kutekeleza mpango wa kupeleka gesi majumbani katika mikoa mingine ya Tanzania Bara ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma hii.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata za Mtambula, Idunda, Itandula, Kiyowela, Idete, Maduma na Nyololo Shuleni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza kwa nchi nzima tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele-mradi vitatu vya Densification, Grid Extension na Off-Grid Renewable ambayo inalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji na vitongoji ambavyo havikufikiwa na miundombinu ya umeme. Kata za Idete, Idunda, Itandula, Kiyowela, Mtambula, Maduma pamoja na Kata nyingine za Wilaya ya Mufindi zimejumuishwa katika utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu wa Grid Extension utakaokamilika mwaka wa fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vya kata hizo itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 153.65; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4, yenye urefu wa kilometa 233; ufungaji wa transfoma 92, pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,225. Gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 14.1. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE (K.n.y. MHE. SALOME W. MAKAMBA) aliuliza:-
Zaidi ya Kaya 800 za wananchi wa Mitaa ya Bukondamoyo na Muhunguala katika Kata ya Muhunguala, Jimbo la Kahama Mjini wamezuiliwa kupatiwa huduma muhimu za kijamii kwa madai kwamba wanaishi kando ya Bwawa la Nyihogo, ilihali wananchi hao wanaishi umbali wa zaidi ya mita 700 kutoka katika bwawa hilo:-
Je, ni kwa nini Serikali inawanyima wananchi hao huduma za kijamii wakati wako umbali wa mita 60 zilizowekwa kisheria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Nyihongo ndiyo chanzo pekee mbadala cha maji katika Mji wa Kahama, ambapo bwawa hilo lilisanifiwa mwaka 1948, lenye eneo la zaidi ya ekari 145. Mipaka ya bwawa hilo ilitangazwa katika Gazeti la Serikali, Namba 72, mwaka 1963.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi wamevamia kwenye hifadhi ya eneo tengefu la bwawa hilo, hasa katika sehemu za kidakio cha maji na wengine wapo kwenye eneo hatarishi, linalopitisha maji baada ya bwawa kujaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Maji Kahama kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Kahama na Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa ujumla umetoa ilani ya kusitisha shughuli zote za kibinadamu kufanyika ndani ya hifadhi ya bwawa na kidakio cha maji. Kutokana na hilo Serikali inaandaa mpango wa kuwaondoa wananchi hao katika maeneo hayo na kuendelea kuzuia shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa huduma kwa kaya zote ambazo ziko nje ya mpaka wa hifadhi ya bwawa kwa kuwapatia huduma ya maji safi na inawashauri wananchi ambao wapo ndani ya hifadhi ya bwawa hilo kuhama ili kulinda chanzo hicho kwa manufaa yao wenyewe.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuza:-
Kwa muda mrefu sasa Mji wa Kibondo hauna maji baada ya chanzo cha maji kuharibiwa na shughuli za kibinadamu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mradi mwingine wa maji toka chanzo kingine (hasa Mto Malagarasi) ili Kata za Busunzu, Busagara, Lusohoko, Kitahana, Kumwambu, Kibondo Mjini na Miserezo zipate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba la Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo Sekta ya Maji awamu ya pili, Serikali imepanga kuboresha huduma ya Maji safi katika Mji wa Kibondo kwa kufanya usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni ili kupata gharama ya ujenzi wa mradi mkubwa ambao utapita katika Kata saba zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge kwa kutumia chanzo cha Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtaalam Mshauri anaendelea na usanifu wa kina pamoja na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni unaotarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2017. Vilevile taratibu za kumpata Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii zinaendelea na anatarajiwa kupatikana mwezi Julai, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa Mji wa Kibondo. Taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zinaendelea na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 21017/2018. Kazi zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na upanuzi wa mtandao umbali wa kilomita saba na ukarabati wa bomba la maji urefu wa kilomita nne, ununuzi dira 850 na ufungaji wa pampu na mota.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Wilayani Kibondo wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeitengea kiasi cha shilingi milioni 826.8 Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya vijijini.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Kumekuwa na upungufu mkubwa wa maji safi na salama kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu nchini na mpaka sasa nchi yetu bado inategemea maji kutoka vyanzo vichache kama mabwawa, mito, maji ya mvua na kadhalika.
Je, Serikali ina mkakati gani maalum wa kubadilisha matumizi ya maji ya bahari kwa ajili ya matumizi ya kawaida ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nchi yetu kwa sasa kulingana na takwimu zilizopo ina maji juu ya ardhi na chini ya ardhi yanayofaa kwa matumizi mbalimbali kiasi cha kilomita za ujazo elfu 96.27, ambapo kila mwananchi ana uwezo wa kupata maji wastani wa mita za ujazo 1,800 kila mwaka hadi mwaka 2035 iwapo hatua madhubuti zitachukuliwa za kusimamia rasilimali za maji. Kiwango hicho cha maji kwa kila mtu kwa mwaka ni kikubwa ukilinganisha na kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kinachokubalika kimataifa cha mita za ujazo 1,700 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa rasilimali za maji ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa uvunaji maji ya mvua ili nchi yetu isifike kiwango kikubwa cha uhaba wa maji na kusababisha athari kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maji yaliyopo yanatosha, na gharama za uwekezaji katika maji ya bahari kwa matumizi ya kawaida ni kubwa Serikali itaendelea kutumia vyanzo vingine vilivyopo, na endapo itabainika vyanzo hivyo vimepungua maji Serikali itajielekeza kuwekeza katika maji ya bahari kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Kumekuwa na mlundikano wa viwanda vingi vya aina moja katika kanda moja, kwa mfano kumekuwa na viwanda vingi vya saruji (cement) katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo hilo ili kuondoa changamoto za madhara ya athari kwa binadamu wanaoishi maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa wapi kiwanda kijengwe kwa kiasi kikubwa hutegemea uwepo wa soko la bidhaa itakayozalishwa na/au upatikanaji wa malighafi na/ au teknolojia.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Ukanda wa Pwani kuanzia Tanga mpaka Mtwara wanayo faida ya kuwa na malighafi nyingi na yenye ubora wa hali ya juu wa utengenezaji wa saruji. Lakini pia inapotokea malighafi hiyo inaagizwa kutoka nje ya nchi, viwanda vilivyoko Pwani vinakuwa na faida katika unafuu wa gharama za usafirishaji. Vile vile kihistoria soko kubwa la saruji na hata bidhaa nyingine ni Ukanda wa Pwani na hasa Dar es Salaam, si kwa nia mbaya viwanda kulundikana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuondoa changamoto za madhara ya shughuli za viwanda kuwa ndani ya makazi ya watu wanaoishi maeneo ya karibu kupitia Sera ya Mazingira, ambapo kwanza kabla ya kiwanda kujengwa katika eneo husika, Tathmini ya Athari za Mazingira (Environmental Impact Assessment) hufanywa. Zoezi hili hufanywa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara inayosimamia.
Mheshimiwa Spika, pili, baada ya kiwanda kuanza kufanya kazi Ukaguzi wa Athari za Mazingira (Environmental Auditing) hufanyika kila baada ya mwaka mmoja. Tatu, Serikali huhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Kwa mfano matumizi ya Electrostatic precipitator, west scraper ili kuzuia vumbi kusambaa hewani na kwenye makazi ya watu. Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inaendelea kutoa mafunzo na kusimamia Sheria ya Mazingira ili kuepusha madhara yatokanayo na shughuli za viwanda nchini.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Mkoa wa Katavi hauna umeme wa Gridi ya Taifa. Je, ni lini Mkoa huo utapatiwa umeme wa Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Mikoa ya Kusini Magharibi ikiwemo Katavi, Kigoma na Rukwa kuunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa. Serikali kupitia TANESCO imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa Gridi Msongo wa kilowati 400 yenye urefu wa kilometa 1,080 kutoka Mbeya – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma hadi Nyakanazi.
Mheshimiwa Spika, mtaalam mshauri amekamilisha kazi ya kudurusu taarifa ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuhuisha mradi kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 400. Utekelezaji wa ujenzi wa mradi huu utaanza mwezi Desemba, 2017 na kukamilika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Mkoa wa Katavi utaanza kupata umeme wa Gridi ya Taifa. Gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 664.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna ongezeko la bidhaa bandia na zisizo na viwango zinazoingizwa nchini, miongoni mwa bidhaa hizo ni pembejeo za kilimo, madawa ya mifugo, dawa za binadamu, vyakula, vinjwaji, vifaa vya nyumbani na kadhalika.
(a) Je, ni hasara gani imepatikana kwa mwaka mmoja uliopita kutokana na bidhaa hizo kuingizwa nchini na kutumiwa na wananchi?
(b) Je, ni hatua gani zinachukuliwa kukomesha bidhaa hizo kuingia nchini hasa maeneo ya vijijini ambako uelewa wa watumiaji ni mdogo na maafisa wadhibiti ni wachache?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Ushindani (FCC) na kwa kushirikiana na wamiliki wa nembo za biashara, inaendelea kudhibiti bidhaa bandia zisiingie nchini ili kuhakikisha ushindani wa haki katika biashara. Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2016 Tume ya Ushindani ilikamata bidhaa bandia zenye thamani ya shilingi bilioni 18.67. Bidhaa hizo zilikamatwa kwenye kaguzi za bandarini, vitengo vya makontena (ICDs) na katika masoko.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Machi, 2017, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Taasisi nyingine waliteketeza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Bidhaa hizo ni pamoja na nguo, nyama na sausage, vilainishi vya injini, battery za magari na za solar 1,430.
Mheshimiwa Spika, shirika pia lilifanya ukaguzi wa mabati na kutekeleza mabati 84,000 ambayo hayakukidhi viwango. Aidha, takriban lita 94,869 za vilainishi vya injini, na katoni 200 za bendera za Taifa zilirudishwa nchi zilikotoka. Vilevile aina 11 za pombe kali katoni 123,942 zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki vilizuiliwa kuingia sokoni na kurudishwa katika nchi zilikotoka.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Ushindani na TBS zinafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kudhibiti bidhaa zinazopitia katika mipaka na nchi jirani, kufuatilia ubora wa bidhaa hafifu na bandia na kuziondoa katika soko. Ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi hizi, Serikali inongeza ajira za watumishi, kufungua vituo vya ukaguzi wa bidhaa katika mipaka yote na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama vile luninga, redio na magazeti na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalma kuzuia magendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote tushirikiane kupambana na bidhaa bandia na zisizokidhi viwango. Adui namba moja wa viwanda ni bidhaa bandia na zile zisizokidhi viwango.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa maporomoko ya Ntomoko Wilayani Kondoa?
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Ntomoko ulilenga kutoa huduma katika vijiji 18 vya Wilaya ya Kondoa na Chemba lakini kutokana na uwezo mdogo wa chanzo kumesababisha kutokidhi mahitaji ya huduma ya maji katika vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Novemba 2017 Wiraza kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliunda timu ya pamoja ya Wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa kina wa mradi huo pamoja na kutafuta chanzo kingine mbadala ili kuongeza wingi wa maji utakaokidhi mahitaji ya wananchi katika vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mapitio ya usanifu wa kina timu hiyo ilibaini kuwa chanzo cha Ntomoko hakina tena uwezo wa kuhudumia vijiji hivyo. Ili kukidhi mahitaji ya maji kwa vijiji hivyo, Serikali imepanga kukarabati miundombinu iliyoko pamoja na kujenga bwawa lenye mita za ujazo milioni 2.8 kwenye eneo la Kisangali katika kijiji cha Mwisanga litakalotoa huduma kwa vijiji vyote 18. Usanifu wa bwawa hilo pamoja na bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi makutano ya kijiji cha Lusangi umeshafanyika. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto zilizojitokea awali juu ya ukarabati wa miundombinu ya mradi huo, Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) kutekeleza ukarabati wa mradi huo badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Tatizo la maji katika vijiji vya Mlibansi, Mazwe, Mgamsamansi, Ilangu, Kapemba na Busongola ni kubwa sana.
Je, ni lini Serikali itakarabati visima vilivyochimbwa na UNHCR ili viweze kutatua tatizo la maji katika vijiji hivyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini kote. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.302 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini inayohusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji. Kupitia fedha hizo zilizotengwa Serikali itakarabati miradi mbalimbali ya maji katika Halmashauri ya Mpanda ikiwemo visima vilivyochimbwa na UNHCR vilivyopo katika Vijiji vya Mlimbasi, Mazwe, Mgamsamansi, Ilangu, Kapemba na Busongola.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Halmashauri wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020 wa usambazaji wa maji safi na usafi wa mazingira, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imepanga kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi mikubwa ya usambazaji maji katika kijiji cha Busongola. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga miradi ya maji nchini kulingana na upatikanaji wa fedha ili iweze kutatua kero ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Mfumo wa mabomba ya maji kwenye maeneo mengi nchini ni chakavu hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa maji:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kubadilisha mabomba yote chakavu katika nchi ili kuokoa maji yanayopotea kutokana na uchakavu huo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sekta ya maji imekuwa inakabiliwa na changamoto ya upotevu wa maji kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyojengwa miaka mingi iliyopita. Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeendelea na jitihada za uwekezaji katika ukarabati wa miundombinu chakavu maeneo mbalimbali ya mijini ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Singida pamoja na ukarabati wa miradi ya kitaifa ya Makonde, Wanging’ombe, Maswa, HTM, Mugango Kiabakari na Chalinze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Miradi ya Maji Vijijini, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuimarisha Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa kutumia Mfumo wa Malipo ya kwa Matokeo (Payment for Results -PforR na Payment by Results – PbR) ambapo kwa pamoja zinalenga kuhakikisha kasi ya uendeshaji, matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya miradi ya maji vijijini inakuwa endelevu na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada hizo kwa pamoja zitasaidia kupunguza hali ya upotevu wa maji katika miradi ya maji mijini na vijijini.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
(a) Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu miradi ya maji ya Kali, Rukoma, Ilagala, Kandego, Uvinza na Nguruka ambayo wakandarasi wamesimama kwa ukosefu wa fedha?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza chini ya Mpango wa Vijiji 10 kwa kila halmashauri, Miradi ya Maji ya Rukoma na Kandaga ilitekelezwa katika Halmashauri ya Kigoma na miradi ya maji katika vijiji vya Kalya, Ilagala, Uvinza na Nguruka ilitekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakandarasi wa miradi hiyo walikuwa wamesimama kutokana na changamoto ya kifedha. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018, Serikali tulitumia kiasi cha shilingi bilioni 1.01 katika Halmashauri ya Uvinza kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi ya maji ambayo haijakamilika ikiwemo miradi ya Kayla, Ilagala, Uvinza na Nguruka. Aidha, Halmashauri ya Kigoma ilitumia jumla ya shilingi bilioni 581.2 kuendelea kukamilisha miradi ya maji vijijini ikiwemo Rukoma na Kandaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.8 na shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya Halmashauri za Wilaya ya Uvinza na Kigoma mtawalia ili kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji. Aidha, halmashauri zote nchini zimeshauriwa kuwasilisha kwa wakati hati za madai ya wakandarasi wanaojenga miradi ili ziweze kulipwa mapema iwezekanavyo.
MHE. FELISTER A. BURA (K.n.y. MHE. EDWIN M. SANNDA) aliuliza:-
Mtandao wa miundombinu ya usambazaji wa maji toka chanzo kikuu cha maji ya chemchem katika Jimbo la Kondoa Mjini ni ya zamani na chakavu. Katika ziara yake mwaka jana, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi kutupatia fedha za ukarabati wa miundombinu hiyo:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Sannda, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uchakavu wa miundombinu ya usambazaji maji katika chanzo kikuu cha maji ya chemchem katika Jimbo la Kondoa Mjini. Serikali imekwishafanya tathmini ya awali ya ukarabati wa chanzo hicho unaokadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.1. Ukarabati wa chanzo hicho unatarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Kondoa ilikamilisha uchimbaji wa visima vinne vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 2.6 kwa siku. Ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa maji kutoka kwenye visima hivyo unaendelea. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 9.912, ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 30.172 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 33. Kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi wapatao 13,191 wa maeneo ya mitaa ya Kwapakacha, Bicha, Kilimani, Kichangani na Tura.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
(a) Je, mradi wa Tanzania na Malawi wa kujenga mabwawa matatu makubwa kandokando ya Mto Songwe umefikia wapi?
(b) Mradi huo ulikuwa uanze kwa awamu tatu, na ya kwanza ilikuwa iwe Ileje lakini unaanzia Kyela kisha uende Malawi na kumalizia awamu ya tatu Ileje, je, ni nini kilifanya utaratibu wa awali ubadilishwe?
(c) Wananchi wa Kata za Bubigu na Ileje walishaambiwa wasifanye shughuli zozote katika eneo hilo ili kupisha mradi huo, je, kuna mpango gani wa kuwalipa fidia au kuwaruhusu waendelee na shughuli zao?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Jimbo la Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa matatu katika Bonde la Mto Songwe. Kwa sasa utekelezaji huo upo katika awamu ya tatu inayohusisha ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini litakalotumika kwa ajili ya kuzuia mafuriko, kuzalisha umeme pamoja na shughuli za umwagiliaji. Makubaliano ya utekelezaji wa awamu hii ya tatu pamoja na mkataba wa uanzishwaji wa Kamisheni ya Kudumu ya Bonde la Mto Songwe yalitiwa saini katika kongamano la wawekezaji lililofanyika tarehe 18 Mei, 2017 nchini Malawi. Mkataba huo uliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 7 Septemba, 2017 Jijini Dodoma. Kwa sasa Serikali hizi mbili zinatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utekelezaji wa miradi haujabadilishwa. Ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini utaanza baada ya kupatikana kwa fedha za ujenzi. Mabwawa mengine ya Songwe Kati na Songwe Juu, usanifu kina na ujenzi wake utaanza baadaye. Taratibu za kuwahamisha wananchi wa Kata ya Bubigu kutakakojengwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa ya Songwe Juu na Songwe Kati zitafanyika kwa mujibu wa sheria. Kwa sasa wanaruhusiwa kuendelea na shughuli zao hadi itakapotangazwa vinginevyo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna miradi ya umwagiliaji iliyogharimu fedha nyingi kuijenga lakini inatumika chini ya uwezo na usanifu (below designed capacity) kwa sababu mbalimbali.
a) Je, ni Halmashauri ngapi zina fursa ya kilimo cha umwagiliaji na zimewekeza kwa kiwango cha kutosha kwenye miundombinu ya umwagiliaji?
b) Je, kuna mpango wowote unaotekelezwa wa kuwapata wataalam wa umwagiliaji katika muda mfupi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zote nchini zina fursa ya kilimo cha umwagiliaji na Halmashauri hizo zimeweka katika mipango yake ya maendeleo miradi inayofaa kuendelezwa kuwa kufuata vipaumbele. Skimu za umwagiliaji zimejengwa katika Halmashauri mbalimbali nchini, lakini kutokana na kukosekana kwa fedha baadhi ya skimu hizo ujenzi wake haukukamilika. Kwa sasa Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) imefanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Taifa ulioandaliwa mwaka 2002. Mapitio hayo yataainisha maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji katika kila Halmashauri na mikoa yote nchini. Mapitio hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata kibali cha kuajiri wataalam wa kutosha katika fani ya umwagiliaji. Pamoja na hayo, Halmashauri ambazo hazina wataalam wa umwagiliaji zinashauriwa kuajiri wataalam wa fani hizo.
MHE. NURU A. BAFADHILI (K. n. y. MHE. SONIA J. MAGOGO) aliuliza:-
Tatizo la maji limekuwa sugu sana Wilayani Handeni:-
Je, Serikali imefikia wapi katika kutatua tatizo hili la kunusuru maisha ya wananchi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, ambapo kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018, ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 921 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya maji nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatekeleza ujenzi wa Mabwawa ya Kwandugwa, Mkata na Manga ambayo hadi sasa wakandarasi wapo katika maeneo ya kazi. Serikali inaendelea na usanifu wa miundombinu ya miradi ya maji katika Kijiji cha Pozo na kufanya utafiti wa kuchimba visima katika Vijiji vya Msirwa na Mkata Komnara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inatekeleza mradi wa kitaifa wa Handeni ambao utahudumia vijiji 70 vya Wilaya ya handeni. Serikali imepata fedha za mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi wa kitaifa wa Handeni. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha mitambo ya kusafisha maji, ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji na ulazaji wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji. Ujenzi wa mradi huo utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la maji kwenye Halmashauri ya Handeni na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2018/2019. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO (K.n.y. MHE. ZAINAB M. BAKAR) aliuliza:-
Maji ni muhimu katika maisha ya mwanadamu na bila maji safi na salama afya za wananchi zinaweza kuwa hatarini:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kwa vijiji ambavyo havina vyanzo vya maji, hasa ikizingatiwa kuwa, bila maji safi na salama ni kuhatarisha afya na maisha ya wananchi hao?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar, Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyoanza mwaka 2006 na awamu ya kwanza ilikamilika mwezi Juni, 2016. Kwa sasa Wizara inatekeleza awamu ya pili ya programu hiyo iliyoanza mwezi Julai, 2016 ambayo inatekelezwa kwa miaka mitano. Mpaka sasa jumla ya miradi 1,469, kati ya miradi 1,810 imekamilika na miradi mingine iliyobaki inaendelea kujengwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika halmashauri zilizokamilisha ujenzi wa miradi ya awamu ya kwanza tayari ujenzi wa miradi ya awamu ya pili unaendelea. Aidha, Serikali inatekeleza miradi ya kimkakati katika maeneo mbalimbali yenye lengo la kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi ili kufikia malengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika maeneo ambayo ujenzi wa miradi haukukamilika kwenye awamu ya kwanza na maeneo ambayo miradi haikutekelezwa kutokana na kukosa vyanzo vya maji vya uhakika. Serikali inaendelea kutoa elimu ya utunzaji wavyanzo vya maji, ili kuhakikisha vyanzo vilivyopo vinahifadhiwa ili kutoa huduma endelevu, ikiwa ni pamoja na elimu juu ya uvunaji wa maji ya mvua, hasa kwenye maeneo yenye uhaba wa vyanzo vya maji.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Same – Kisiwani hadi Mkomazi ambayo inaunganisha Majimbo matano ya Same Magharibi, Same Mashariki, Mlalo, Mkinga na Korogwe Vijijini?

(b) Je, ni fedha kiasi gani zimetumika kuanzia mwaka 2015/2016 – 2019/2020 kwa ajili ya kukarabati barabara hiyo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu kwa pamoja swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Same – Kisiwani – Mkomazi imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka. Aidha, kuanzia Mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi 2019/2020, kiasi cha Sh.3,299.365 kimetumika kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo. Kufuatia kufanyika na kukamilika kwa upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa kina kwa kilometa zote za barabara hiyo kilometa 100.5, Serikali kupitia Wizara yangu imetenga kiasi cha shilingi bilioni tano (Shilingi milioni 5,000.00) katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 ili kitumike kuanza ujenzi kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-

Baadhi ya minara ya simu ya Vodacom, Airtel, Tigo na Halotel katika Kata za Kipili, Kilumbi, Kiloli, Kitunda, Kisanga, Mole, Kiloleli na Ipole haifanyi kazi vizuri kwani mtandao katika Kata hizo ni mdogo sana na hivyo wananchi hawapati huduma nzuri ya mawasiliano licha ya uwepo wa minara hiyo. Aidha, katika Kata za Nyahua, Igigwa na Ngonjwa hakuna kabisa mawasiliano ya simu:-

(a) Je, ni lini Serikali itawapatia mawasiliano ya uhakika wakazi wa Sikonge wanaoishi kwenye Kata zenye minara ya simu lakini isiyokamata mtando vizuri?

(b) Je, Serikali itawapatia lini mawasiliano ya simu wananchi wa Sikonge ambao wanaishi kwenye Kata ambazo hazina kabisa minara ya mawasiliano ya simu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika Wilaya ya Sikonge katika Kata za Kiloli, Igigwa, Kipanga, Kipili na Kitunda kwa kushirikiana na TTCL na VODACOM kupitia miradi ya mawasiliano ya awamu ya kwanza na awamu ya tatu.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Igigwa, Serikali kupitia Mfuko ilitangaza zabuni na kupata mtoa huduma TTCL ambaye ameanza maandalizi ya ujenzi wa mnara katika kata hiyo. Kwa upande wa Kata za Nyahua na Ngonjwa, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itazijumuisha kata hizi katika Mradi wa Mawasiliano Vijijini awamu ya tano ndani ya mwaka wa fedha 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itafanya ukaguzi wa ubora wa huduma za mawasiliano kwa kushirikiana na watoa huduma kulingana na viwango vya ubora vilivyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Ubora ili kuhakikisha wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika kwa maeneo yenye usikivu hafifu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mbulu mpaka Haydom kilometa 50 kama ilivyopitishwa kwenye bajeti ya 2019/2020?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mbulu – Haydom kilometa 50 ni sehemu ya barabara ya Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti, Lalago – Maswa kilomita 389 ijulikanayo kama Serengeti Southern Bypass. Barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida na Simiyu. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa mradi wa Serengeti Southern Bypass iko katika hatua za mwisho. Mara baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kukamilika hatua itakayofuata ni usanifu wa kina wa maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mradi huu unahusisha barabara ndefu yenye urefu wa kilometa 389, ili kurahisisha utekelezaji wake wakati wa ujenzi, mradi huu umegawanywa katika sehemu saba ambazo ni Karatu – Mbulu kilometa 79; Mbulu - Haydom kilometa 70.5; Haydom - Chemichemi kilometa 67; Chemichemi - Mwanhuzi kilometa 80; Mwanhuzi – Lalago - Maswa kilometa 83; Haydom - Kadash kilometa 67 na Lalago - Kolandoto kilometa 62.

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza baada ya kukamilisha usanifu wa kina.