Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Humphrey Herson Polepole (6 total)

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mojawapo ya mazao yanayoagizwa kwa kiasi kikubwa sana Uchina ni soy beans (maharage ya soya); na kwa mwaka Uchina wanatumia zaidi ya dola bilioni 40 na kuna nchi 12 tu ambazo zinaruhusiwa kupeleka maharage hayo kule Uchina. Tanzania ni nchi ya hivi karibuni ya 12 imeingia katika nchi hizo 12 na ndio ambayo iko karibu zaidi na Uchina ukilinganisha na zile nchi nyingine 11. Uzalishaji wetu ni mdogo sana na tumeshaingia mkataba wa kupeleka tani laki nne. Uzalishaji wetu kwa mwaka unaonekana kuwa kwenye tani 14,000 hivi.

Je, Serikali imejipanga vipi kutumia soko hili kubwa litakaloleta tija kwa wakulima hapa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Polepole kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, hivi karibuni tumeingia makubaliano na Serikali ya China kwa ajili
ya kuwauzia soya. Nataka nitumie Bunge hili kuwataarifu Watanzania kwamba, consignment ya kwanza ya kupeleka soya tani 140 imesafirishwa mwezi Machi. Hatua tunazochukua za kwanza sasa hivi Taasisi yetu ya TARI na ASA tumewapa jukumu la kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu, hilo ni jambo la kwanza. Bajeti itakapokuja mwaka huu, mtaona tumetenga fedha kwa ajili ya kuyawezesha mashamba yote 13 ya ASA na kuyawekea mifumo ya umwagiliaji ili yaweze kuzalisha mbegu za kutosha za mazao mbalimbali na soya ikiwa mojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hatua ya awali, hatua ambayo tumechukua ili kuli-maintain soko hili, tumeamua kuondoa mifumo ya ukiritimba ya kuwasajili wafanyabiashara kwa ajili ya export. Kwa kuwa soko lipo na wafanyabiashara wapo, wakulima wenyewe wataongeza uzalishaji watakapopata mbegu za uhakika ambazo Wizara tunaanza kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumefungua mlango wa re-export; tumewaruhusu wafanyabishara wa Tanzania, kwa kuwa, zao la soya pamoja na sisi kuwa tunazalisha, lakini linapatikana katika baadhi ya nchi zinazotuzunguka. Kwa hiyo, tumewaruhusu kwa mwaka huu wa kwanza, wakati tunajenga uwezo wa upatikanaji wa mbegu ya kutosha, waweze ku-import na waweze ku-re-export kwa sababu, bila ya hivyo tunaweza kulipoteza soko hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga pia kuanzia mwakani mbegu zitakuwa za kutosha na tutawahamasisha wakulima waingie mikataba moja kwa moja na makampuni yote yanayosajiliwa, bure bila gharama yoyote, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi naomba kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa Wilaya za Kilombero, Majimbo ya Kilombero, Mlimba, Wilaya ya Ulanga pamoja na Malinyi unategemea sana barabara ya kutoka Kidatu mpaka Ifakara kukamilika kwa ujenzi wa lami. Nakumbuka mkandarasi alishafanya mobilization, lakini kwa sababu ya changamoto za mgogoro wa kikodi limesimama.

Ni lini sasa Serikali inawahakikishia wananchi wa maeneo hayo kwamba tutaanza kujenga barabara hiyo kwa lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Humphrey Polepole, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ya Mikumi – Ifakara ni barabara ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi anayeitwa Reynolds.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema, kulikuwa na changamoto za kikodi lakini pande zote zimeshakaa kwa maana ya Wizara, Wizara ya Fedha na mkandarasi na kwamba zile changamoto zilizokuwepo zimeondolewa na tunaamini muda sio mrefu barabara hii itaanza kujengwa na kwa maana ya kukamilika kwa barabara hii itakuwa imerahisisha sana wafanyabiashara na wananchi wa Wilaya alizotaja za Malinyi, Ulanga, Kilombero, Mlimba na hata Ifakara yenyewe.

Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto zilizokuwepo tayari Serikali na mkandarasi imeshakaa pamoja na imeziondoa na tuna hakika ujenzi utaanza mara moja ambao ulikuwa umesimama. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani; na ni lini itaanza kuwezesha majaribio ya kitabibu au kwa Kiingereza wanaita clinical trials kwa bidhaa za mimea dawa ambazo zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na mbadala na tayari
zinatumika kwa uhiyari wa wagonjwa kama over the counter drugs na zimeonyesha ufanisi mkubwa katika kutibu magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mfumo wa upumuaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri. Labda nimwambie tu siyo kwamba ni lini itaenda kuanza, imekuwa ikifanya hivyo; na taasisi yetu ya NIMR na kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakumbuka kwenye fedha hizi ambazo zimetoka, shilingi trilioni 1.3, katika fedha hizo, shilingi bilioni 6.1 zilitengwa kwa ajili ya eneo hilo la tafiti ikiwepo na suala la tiba asili. Kama mnakumbuka hapa Bungeni, niliwahi kusema kwamba kuna kipindi Mheshimiwa Rais wetu alipeleka shilingi bilioni 1.2 pale NIMR kwa ajili ya kufanya mambo kama hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaulizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Rais wetu ameielekeza Wizara kwamba tuwekeze nguvu nyingi sana kwenye eneo hili la kufanya tafiti za madawa yetu ya asili kwa sababu yametusaidia sana kipindi kile ambapo tunapitia wakati mgumu kwenye Corona wakati hakuna anayejua suluhu ni nini kwenye tatizo hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tanzania ni mojawapo ya nchi mbili Ulimwenguni ambazo zimepewa baraka na Mungu ya kuzalisha organic phosphate. Organic phosphate ni mojawapo ya madini muhimu yanayotumika kutengeneza mbolea. Organic phosphate ulimwenguni inapatikana Tanzania na Australia peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia ku-export organic phosphate kama ambavyo inaendelea kufanyika sasa hivi, ili ibaki hapa nchini na kuendelea kuzalisha mbolea ili wakulima wetu wapate mbolea hapa na pasipo na kuhangaika kutoka maeneo mengine? Natambua kiwanda kinakuja Dodoma lakini kuna tamaa kubwa sana ya ku-export organic phosphate kwa sababu ni nchi mbili tu ulimwenguni ambazo zinatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Polepole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nchi tunakuwa guided na WTO Regulation za Trade. Kwa hiyo, ku-declare openly tunazuia export au biashara yoyote sidhani kama katika misingi ya kibiashara ni jambo jema. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili sisi kama Serikali tumeshafanya comprehensive analysis kuangalia deposit yetu ya phosphate iliyopo katika nchi yetu. Tunazo taratibu za kuruhusu mahitaji yanapohitajika kwenda nje tunazo guidance zinazotu-guide. Haturuhusu export ya holela katika phosphate. Hilo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu kwa kuwa tumeshapata Mwekezaji ambaye anawekeza na atatumia phosphate katika Kiwanda cha Mbolea, kinachojengwa hapa Dodoma ambacho kinazalisha tani 600,000 na kitaanza mwaka kesho mwezi wa pili kuanza kuzalisha. Nataka niwahakikishie tu wakulima kwamba tuta-regulate matumizi ya rasilimali hii kwa maslahi ya Watanzania bila kuathiri mahusiano yetu ya kibiashara na nchi zingine. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za Kitafiti zinasema kila mwaka tani milioni tatu za udongo zinaingia katika Ziwa Victoria na kulipunguzia Ziwa hilo kina cha maji. Serikali ina mpango gani na iko katika hatua ipi ya kutekeleza National Water Grid au mtandao wa maji wa kitaifa kutoka Kusini, Kaskazini, Magharibi ili kuweza kupunguza pressure katika Ziwa Victoria? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Polepole kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna hii changamoto ya matope kuingia katika vyanzo vyetu vya maji na sisi kama Wizara tuna ofisi zetu za mabonde zinazoshughulika na kazi hizi na tayari Mheshimiwa Waziri amewaagiza. Hivyo, tayari hili linafanyiwa kazi kuona kwamba tunaendelea kutunza na kuvilinda vyanzo vyetu vya maji. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nchi za Uingereza, Denmark, Sweden na Norway zimeamua kuachana kabisa na masharti kichefuchefu dhidi ya ugonjwa wa Corona; na kuamua kuishi na ugonjwa wa Corona kama magonjwa mengine. Nini kauli ya Serikali kuhusu mwelekeo huu mpya Kimataifa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali, ninachokiona ni kwamba Sweden na nchi zilizotajwa zimeamua kusimama kwenye msimamo wa Tanzania toka mwanzo. Kauli ya Tanzania ni moja tu kwamba sisi kama Tanzania tutaendelea kuhakikisha tunakuwa makini katika kufuata zile taratibu zote ambazo WHO wamezielekeza. Pia tutaendelea kufuata zile taratibu ambazo ni local, zinazotokana na watu wetu na nchi yetu ambazo tulishazifuata toka mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo tutaendelea kulinda mipaka yetu na kuwapima watu wanaoingia na wanaotoka kuhakikisha watu wetu ndani ni salama. Pia tuwahakikishie usalama wenzetu waliopo huko duniani wakija kwetu, nasi tukienda kwao ili tuweze kuitengeneza dunia salama kwa kufanya kazi kwa pamoja. Kwa sababu tukiwa wote salama, wote tutakuwa salama; mmoja asipokuwa salama, wote hatutakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, lakini niseme, dunia siku moja itafika mahali ikubali mwelekeo wa Tanzania toka mwanzo ulikuwa ni sahihi. Ahsante sana. (Makofi)