Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mariam Madalu Nyoka (7 total)

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Je, lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa kwenye majengo mengine yaliyo chakavu zaidi katika Hospitali hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; uchakavu wa majengo ya hospitali hiyo yanakwenda sambamba pamoja na uchakavu wa vifaa tiba, ikiwemo ultra sound, Mashine ya kufulia na vifaa vingine. Je, Serikali haioni umuhimu wa kununua vifaa hivyo katika hospitali hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nilikuwa naongea na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ananiambia alimtembelea juzi kabla ya kuja Bungeni. Kama alivyotembea amejionea yeye mwenyewe kwanza jengo ambalo limejengwa hilo la magonjwa ya dharura, lakini alijionea ukarabati mzuri uliofanyika kwa mapato ya ndani kwenye magonjwa yanayoambukiza ambayo sasa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua wamelazwa mle ndani na Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo mengine kwa mtindo ambao sasa jengo ambalo linamalizika mwezi Oktoba umefanyika.

Mheshimiwa Spika, pia akumbuke kwamba pamoja na hilo kwa juhudi za Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mheshimiwa Jenista Mhagama, walianzisha mchakato wa kupata hospitali mpya kabisa ya mkoa, ambapo kule Mwenge - Mshindo wameweza kupata heka 276 kwa ajili ya kujenga hospitali mpya ya mkoa. Waziri wa Afya alituma watu wa kwenda kuangalia eneo, lakini ikaonekana kuna watu sita walitakiwa kufidiwa na ikafanyika tathmini ikaonekana inatakiwa milioni 700 kwa ajili ya kufidia. Sasa Waziri wa Afya ameagiza hebu tuhakiki hiyo milioni 700 kwa watu sita kwa nyumba za udongo ni nini. Kwa hiyo, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuangalia tujihakikishie hilo ili sasa tuanze michakato ya kupata Hospitali mpya kabisa ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu vifaa tiba; Mheshimiwa Mbunge atakumbuka, Bunge lililopita alikuja akilalamika kuhusu x-ray yao iliyoharibika ambayo ilikuwa ina shida ya battery na ilikuwa imeagizwa nje na imeshafika sasa na x-ray inafanya kazi. Tunampongeza sana Mbunge kwa juhudi zake hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshapeleka milioni 348 MSD, zipo cash pale ambazo ni fedha, tukimaliza hapa tukutane mimi na Mheshimiwa Mbunge ili tuwasiliane na Uongozi wa Hospitali na Mkoa ili tuweze kupanga kulingana na mahitaji anayoyasema…

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, lakini Rais wetu amepeleka direct kwenye akaunti yao milioni 110, nayo hiyo haijapangiwa chochote, kwa hiyo tunaweza vilevile kupanga kuelekeza kwenye maeneo anayoyasema.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru ahsante.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, pia kuna milioni 130 kwa ajili ya Kiwanda cha Majitiba, kwa hiyo kazi inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na Mungu akubariki.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize swali langu lingine la nyongeza.

Kwa kuwa mazingira ya nje ya majengo ya hospitali hii ya Mkoa wa Ruvuma sio rafiki hasa kwa watumishi na wagonjwa kwa kipindi cha mvua; je, Serikali ina mpango gani wa kuweka paving pamoja na kujenga mifereji ya maji ya mvua katika hospitali hii?
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka kwa swali lake zuri, lakini kwa kufatilia maendeleo ya utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Spika, nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuboresha hospitali zote za rufaa za mikoa kwa kuwa ni kiungo muhimu cha utoaji huduma kati ya ngazi ya msingi na huduma za rufaa za juu. Kwa hiyo, tumepokea changamoto ya mazingira ya nje ambayo hayavutii na nikuahidi kwamba najua pia kuna suala la barabara tutawasiliana na TARURA ili pia kuweza kuweka lami katika barabara ambayo inaelekea kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, suala la tent hilo ni jambo ambalo tutalifanyia kazi.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Majengo, Ruvuma, Subira kwenda Mpitimbi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Nyoka, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya kazi ya usanifu wa kina ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, je, lini Serikali itajenga barabara ya Mbinga – Mpepai – Mtuha - Lipalamba kwenda Mpepa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina Serikali itatafuta fedha kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimia Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nyingine.

Mheshimiwa Spika, hospitali za Wilaya za Mkoa wa Ruvuma pamoja na vituo vyake vya afya vina changamoto kubwa ya magari ya kubebea wagonjwa, kutoka kwenye vituo vya afya kwenda kwenye hospitali za Wilaya au kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari ya kubebea wagonjwa katika vituo hivi vya afya au hospitali zake za Wilaya Mkoa wa Ruvuma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mhehsimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwamba anafuatilia vizuri sana masuala yanayoendelea kwenye Wilaya zao kwa kushirikiana na Wabunge.

Mheshimiwa Spika, unaona kwamba kuna magari ya kubebea wagonjwa zaidi ya 727 maana yake ni kwamba hakuna Wilaya ambayo itakosa gari. Tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kuyatizama yale maeneo specific yenye uhitaji maalum ambayo yanahitaji kupewa magari zaidi ya moja na nadhani eneo lake la Mkoa wa Rukwa ni mojawapo ya hiyo mikoa Lindi, Mtwara, Kigoma na sehemu zingine ili tuone ni namna gani tunatatua hilo tatizo kwa wakati ambao tumeusema hapa.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika kutokana na ahadi mbalimbali za viongozi wa Serikali, tangu Serikali ya Awamu ya Tatu, yaani mika 23 mpaka sasa uthamini wa maeneo hayo tayari umeshafanyika zaidi ya mara tatu. Sasa naombe nijue;

Je, ni lini wananchi wa maeneo haya watalipwa fidia ili waweze kupisha ujenzi wa barabara hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali jingine, kulingana na uwingi wa malori kulazimika kupita katikati ya mji wa songea hivyo kulazimisha msongamano ajari na uchafuzi wa mazingira.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara ile ili kuweza kupunguza adha inayowakuta wananchi wa Mkoa wa Ruvuma hususani wakazi wa Songea Mjini, kuzingatia kwamba bajeti ya Serikali ya Wizara hii bado haijapitishwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tathmini tumekwisha kufanya mara tatu, na hii ni kutokana na sheria ya tathmini; kwamba inapofika baada ya miezi sita na kama hakuna malipo yamefanyika inatakiwa tathmini ile iweze kufanyika tena, vinginevyo ilipwe kwa fidia.

Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi ambao wataathirika katika ujenzi huu ni kwamba tayari sasa tathmini imekamilika, hii ya mwisho, na daftari lipo kwa Mthamini Mkuu wa Serikali ili aweze kusaini na hatimaye Serikali itafute fedha kwa ajili ya kulipa fidia hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli tunatambua umuhimu wa barabara hii na ndiyo maana kwa kushirikiana na Benki ya Dunia Serikali imepata mkopo kwa ajili ya ujenzi katika kipande hiki cha Songea - Lutukila na tupo katika hatua za manunuzi.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, mara baada ya manunuzi kukamilika tunaanza kujenga, na iko ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watumishi waliolipwa mafao pungufu hasa walimu; na wanapofuatilia wanaambiwa walipe gharama kwa ajili ya ufuatiliaji Dodoma? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Nyoka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa wastaafu ambao michango yao haikupelekwa, kwanza ni kosa kisheria, kwa sababu sheria zetu zinamtaka mwajiri kuwasilisha michango ya mwanachama kila mwezi, lakini pia kama kuna changamoto za hao wastaafu ambao wanaambiwa tena pia waanze kupeleka michango yao wenyewe, hilo naomba nilichukue na ni jambo serious nahitaji nilifanyie kazi siku ya leo, nikitoka hapa niongee na Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya hatua zaidi.