Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mariam Madalu Nyoka (5 total)

MHE. MARIAM M. NYOKA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia ukarabati mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa ni ya muda mrefu na majengo yake yamechakaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariamu Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo chakavu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kubomoa majengo chakavu manne; jengo la Masjala ya zamani, choo cha nje cha wagonjwa, jengo la viungo bandia na jengo la zamani la huduma za kifua kikuu, kwa ajili ya kujenga jengo la kisasa la wagonjwa wa dharura ambalo limefikia asilimia 95. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi 630,340,507.00, ambapo hadi sasa fedha hiyo imetolewa yote. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2021. Ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha jengo la hosteli ya madaktari watarajali katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma lililoanza kujengwa mwaka 2014/2015?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la hosteli ya madaktari watarajali (interns) katika Hospitali ya Mkoa Ruvuma.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa hosteli hii utaendelea mara tu fedha hizi zitakapokuwa zimetolewa na tunatarajia ujenzi huu utakamilika ifikapo Juni, 2023.
MHE. JONAS W. MBUNDA K.n.y. MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Songea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariamu Madalu Nyoka Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Songea imepokea Shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Jumla ya majengo 14 yamejengwa kwenye Hospitali hiyo ambapo majengo saba yamekamilika na majengo mengine saba ujenzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kununua gari la utawala na gari la Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mhehsimiwa Spika, Serikali imenunua magari 727 kwa ajili ya kubebea wagonjwa na magari 146 kwa shughuli za kiutawala. Hadi sasa magari 20 yamepokelewa na magari 117 yapo njiani kutoka kwa mtengenezaji.

Mheshimiwa Spika, magari yote yanatarajiwa kuwasili nchini na kukabidhiwa katika vituo vya kutolea huduma kabla ya mwezi Juni 2023. Aidha, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Hospitali zitakazopata mgao wa magari hayo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Barabara ya Mletele - Msamala – Mkuzo hadi Namanditi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Barabara ya Mletele – Msamala – Mkuzo hadi Namanditi (Songea Bypass) yenye urefu wa kilometa 14 umejumuishwa katika mradi wa ujenzi wa Barabara ya Makambako hadi Songea yenye urefu wa kilometa 280. Sehemu ya kutoka Songea – Rutikira (km 97) ambao unagharamiwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia chini ya mradi wa Tanzania Transport Integration Project (TanTIP). Maandalizi kwa ajili ya kutangaza zabuni za kumpata mkandarasi wa ujenzi yanaendelea, ahsante.