Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Alex Raphael Gashaza (42 total)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Naitwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Jimbo la Ngara.
Kwa kuwa barabara ya Murugarama – Rulenge – Nyakahura yenye kilometa 85 ni barabara ambayo iliahidiwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2008 kwamba itaweza kujengwa kwa kiwango cha lami na miaka miwili iliyopita wananchi wa Jimbo la Ngara walikuwa wakielezwa kwamba tayari upembuzi yakinifu wa barabara hii umeanza.
Naomba kumuuliza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ni lini mkandarasi atakuwepo site kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata taarifa kutoka kwa Waziri mwenyewe wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juu ya upatikanaji wa fedha za kulipa madeni ya wakandarasi, kama jana mlimsikia alisema ni karibu shilingi bilioni 419 zimeshatolewa. Kwa hiyo, katika lile deni la shilingi trilioni 1.268 sasa tumeshuka tuko kwenye shilingi bilioni 800 na zaidi. Naomba kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mara fedha zitakapopatikana kwa mradi huo, barabara yake itashughulikiwa kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Napenda kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa umwagiliajii wa Bonde la Bigombo ambao ulianza 2012 na ulitakiwa kukamilika 2013, ulifadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya ASDP, mpaka sasa mradi huo haujakamilika. Mradi huu ilikuwa ni tegemeo kwa wananchi wa Jimbo la Ngara hususani wananchi wa Kata ya Rulenge, Keza na Nyakisasa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Ni lini sasa mradi huu utaweza kukamilika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilisema kwamba miradi yote ya umwagiliaji inasimamiwa na Tume ya Umwagiliaji. Nikasema katika bajeti ya mwaka huu wa 2015/2016, tumepanga fedha kiasi cha shilingi bilioni 53 katika kuendeleza sekta hii ya umwagiliaji. Miradi hii ilikuwa imeanzishwa chini ya programu ya ASDP ambapo wafadhili ni African Development Bank na mingi ilikuwa haijakamilika. Kwa sababu tumeunda Tume, tutakwenda kufuatilia tuone tunaweza kukamilisha kwa namna gani mradi ambao tayari ulikuwa umeshaanza.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, barabara ya Mrugarama – Rulenge kwenda mpaka Mzani iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini kwa mwaka wa fedha 2016/2017 haiko kwenye bajeti, badala yake ni Kilometa tatu na nusu tu ambazo zimewekwa kwenye bajeti kwa ajili ya kiwango cha changarawe chini ya TANROAD; na barabara hii imekuwa mbaya sana kwa kipindi kilichopita cha mvua na mwaka mzima maana yake hakuna bajeti nyingine itakayotengeneza barabara hii:-
Je, Waziri haoni umuhimu wa kuongeza fungu ili kwa kipindi cha mwaka wa 2016/2017, barabara hii iweze kupitika kwa wepesi japo itakuwa imetengenezwa kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wa kuongeza bajeti sina kwa sababu nina uhakika huu mwaka ndiyo tumemaliza, mmetupa kazi, mmepitisha bajeti yatu na tunawahakikishia sisi tutaisimamia kwa nguvu zetu zote. Kitu ambacho ninamhakikishia, tutahakikisha hii barabara aliyoiongelea, inapitika mwaka mzima. Kama itatokea mahitaji makubwa ya fedha kutokana labda na kuharibika kwa kiwango ambacho hakitegemewi, namhakikishia kwamba tutatafuta fungu la dharura ili kuweza kurudisha mawasilino kama yatakatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mawasiliano yatakuwepo katika kipindi chote cha mwaka wakati tukijiandaa na bajeti ya miaka inayokuja.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa mgogoro uliopo katika Pori la Kagera Nkanda unataka kufanana na matatizo yaliyopo katika Pori la Burigi na Kimisi hususan maeneo yaliyopo katika Jimbo la Ngara; kama ambavyo tangu mkutano wa pili wa Bunge niliweza kueleza na hata katika mchango wangu wa bajeti ya maliasili; kwamba tangu mwaka 1959 mrahaba ule wa asilimia 25 ambao unatakiwa kurudishwa kwenye Halmashauri kutokana na vitalu vya uwindaji haijawahi kupelekwa kwenye Jimbo la Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Waziri wa Maliasili na Utalii anaweza kuwaeleza wananchi wa Jimbo la Ngara na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, ni lini pesa hizo zitapelekwa, ambazo tangu mwaka 1959 mpaka leo hazijapelekwa?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la mrabaha likilinganishwa na swali la msingi ambalo nimelijibu ni mahususi kidogo na bila shaka linahitaji takwimu na linahitaji taarifa ambayo ni mahususi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuahidi Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki cha asubuhi, mchana awasiliane na mimi nitaweza kumpa jibu sahihi kwa swali lake ambalo ni mahususi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Alex Raphael Gashaza, ni Mbunge wa Jimbo la Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa barabara ya Murugarama Lulenge mpaka Mzani kilomita 85 iliahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2012, lakini barabara hiyo imeahidiwa tena na Rais wa Awamu ya Tano wakati wa Kampeni mwaka 2015 na ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, lakini katika bajeti hii ya 2016/2017 haipo kwenye bajeti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge tumeongea naye kwa muda mrefu, tulikutana na Waziri wa Ujenzi na baadaye tukaomba twende tukakutane na Katibu Mkuu. Kwa kweli anafuatilia sana ujenzi wa hii barabara. Namshukuru sana na naomba aendelee na juhudi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho tulikuwa tumemwambia na naomba kurudia ni kwamba ahadi zote za Mheshimiwa Rais na ahadi za Viongozi wengine wote zilizotolewa na zile ambazo zimewekwa katika Kitabu cha Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa mwaka 2015 hadi 2020, Serikali hii ya Awamu ya Tano itazitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotekea, kwa nini mwaka huu fedha hazikutengwa, ni kwa sababu tu tulitoa kipaumbele kwa zile barabara ambazo zilishaanza kujengwa na Wakandarasi wako site na Serikali inapoteza fedha kuwalipa watu ambao hawafanyi kazi. Tulitaka barabara hizi kwanza zikamilike, halafu kuanzia mwaka ujao wa fedha tutaanza kuingia katika maeneo mapya ambayo viongozi wetu wakuu waliahidi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ni majibu ya Serikali. Lakini kwa kuzingatia kwamba Ngara ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Kagera, Wilaya inayopakana na nchi mbili, Rwanda na Burundi imekuwa ni waathirika wakubwa sana wa hali ya usalama katika eneo hilo. Sasa swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanzisha Kanda Maalum ya kipolisi kwa Wilaya hii ya Ngara ambayo kwa muda mrefu wamekuwa ni waathirika wa hali ya usalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa tukiangalia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana za kiusalama nchini mwetu na maamuzi ya kuongeza Wilaya katika maeneo hayo yanatokana na wingi wa matukio ya uhalifu. Ngara ni moja kati ya sehemu ambayo kuna matukio ya uhalifu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, hasa kutokana na kupakana na nchi jirani. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge atuachie hili tunalifanyia kazi na baadaye pale ambapo hatua itakapofikiwa, tutamjulisha.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ambayo yamejielekeza kwenye sehemu ndogo tu ya swali langu la msingi; kwa sababu ameelezea juu ya mpango wa maji kwenye miji sita ya Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kwamba Wilaya yangu ya Ngara, takriban asilimia 50 ya maeneo ya vijijini kuna tatizo kubwa hili la maji; na bahati nzuri tarehe 30 mwezi Desemba mwaka jana, 2016, Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo alifika akaona mito hiyo na mlima huo ninaousema; na kwa kutumia vyanzo hivi maana yake ni kwamba tutaondoa kabisa kero ya maji katika vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara na hizi nyingine ambazo nimezitaja; na huu ndiyo utakuwa ni mwarobaini:-
Sasa swali langu namba moja: Je, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wako tayari kutuma wataalam ili waweze kufika maeneo yale na kuweza kuweka mkakati wa kuandaa mradi mkubwa ambao unaweza ukaondoa kero hii ya maji kwenye Vijiji vya Wilaya ya Ngara, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo na Chato kama ilivyoelezwa kwenye swali la msingi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka 2016 mwezi wa Pili Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara ilipeleka barua kwenye Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kuomba mitambo miwili ya kusukuma maji kwenye eneo la K9 ambapo kuna taasisi za Serikali na wananchi kwa maana Kambi ya Jeshi, Shule mbili za Sekondari na wananchi wa Kijiji cha Kasharazi; na pampu ya pili kwenye eneo la Mamlaka ya Mji wa Ngara Mjini, ambayo pamoja mamlaka kushugulikia usambazaji wa maji mjini, bado kulingana na umuhimu wa taasisi zilizopo pembezoni kama Shule ya Sekondari Ishunga walikuwa wakipeleka maji kule, lakini baada ya mtambo kuharibika uliokuwa unasukuma maji, imekuwa ni tatizo.
Je, Wizara kwa sababu tayari ilishaji-commit tangu tarehe 25 mwezi wa Pili kwamba itapeleka pampu hizi mbili mwaka jana…
SPIKA: Mheshimiwa Gashaza, sasa si uulize swali!
Mheshimiwa Spika, swali langu je, ni lini sasa Wizara itapeleka fedha hizi ambazo ni takriban shilingi milioni 50 kwa ajili ya kununua pampu hizi za kusukuma maji katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Gashaza amezungumzia matatizo ya maji ya Ngara na Wilaya zote Mkoa wa Kagera akihusisha pia na vijiji vya wilaya hizo; na ameomba kwamba tupeleke wataalam.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa yupo mtaalam mshauri ambaye anaangalia uwezekano wa kutumia mito hiyo miwili ambayo ni mikubwa ili kuweza kupeleka maji kwa wananchi. Miradi hii ambayo itatekelezwa chini ya Wizara ya Maji, itahakikisha inapeleka maji kwenye miji mikuu ya hizo Wilaya na vijiji vinavyopitiwa na bomba kuu kuelekea kwenye hizo Wilaya.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Vijijini, katika bajeti ya mwaka huu tumehakikisha kwamba kila Wilaya imepewa bajeti ili waweze kushughulikia kupeleka maji kwenye Kata na Vijiji vinavyozunguka hizo Halmashauri. Mheshimiwa Waziri ametoka kuzungumza sasa hivi kwamba tayari baada ya kuona kwamba utekelezaji unasuasua tuliamua kuandika mwongozo kupeleka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maji kupitia bajeti ambayo imetengwa na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, pia nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari na tumekuwa tunafanya hivyo. Kama Halmashauri zinahitaji wataalam, basi tunaweza tukashirikiana kutoa wataalam ili kwenda kuangalia hilo tatizo kwa pamoja tuone jinsi ya kulishughulikia.
Mheshimiwa Spika, nikiri katika swali lake la pili, ni kweli na mimi mwenyewe waliniambia na aliniletea nakala ya barua kuhusiana na maombi ya pampu kwa ajili ya kufufua zile pampu ambazo zimeharibika.
Mheshimiwa Spika, nizungumze suala moja. Waheshimiwa Wabunge, ikishakuwa Mamlaka, maana yake, inajitegemea kwenye running. Serikali inasaidia katika uwekezaji. Sasa inawezekana barua hizo baada ya kwenda kule kwenye Wizara zilikutana na tatizo hilo. Mara nyingi kwenye uwekezaji ndiyo tunasaidia mamlaka, lakini kwenye yale matumizi ya kila siku huwa tuaachia wao wenyewe wafanye kazi hiyo kwa kutumia mapato yao. Inategemea sasa, Mamlaka kama ipo chini ya Wilaya, kama kuna matatizo inabidi waripoti kwenye Wilaya. Mamlaka zilizopo chini ya Mikoa, kama kuna tatizo, wanaripoti kwenye Mikoa.
Mheshimiwa Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala kwa sababu nalifahamu, nitajaribu kuwasiliana na Wizara kuona limefikia wapi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyetambua kwamba mabadiliko ya tabianchi ni janga la kitaifa na kimataifa. Kwa kutambua hilo binafsi kama Mbunge wa Jimbo la Ngara kwa kushirikiana na wataalam wangu katika Halmashauri yangu ya Ngara tumejipanga kuanzisha programu ya kuwa na vikosi kazi vya kupambana na moto kama kisababishi kikuu cha uharibifu wa mazingira. Programu hiyo ambayo tutaiita Community Fire Brigade kuanzia kwenye ngazi ya vijiji na kata.
Sasa swali, Serikali kupitia Wizara ya Muungano na Mazingira wako tayari ku-support programu hii kwa kutoa fedha kwa sababu lengo ni kuanzisha vitalu, kupanda miti katika maeneo ambayo yameathirika na moto lakini pia
kuanzisha miradi ambayo ni rafiki wa mazingira kwa maana ufugaji wa nyuki kwa malengo matatu, moja, kulinda mazingira; lakini pili, kuinua kipato cha wananchi na tatu, kutoa ajira.
MWENYEKITI: Naomba swali kwa ufupi Mheshimiwa.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Tayari nimeshauliza swali…Serikali ipo tayari…
MWENYEKITI: Basi naomba ukae upate majibu!
MHE. ALEX R. GASHAZA: Haya!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuanzisha mkakati huo katika Jimbo lake na Wabunge wengine waige mfano wa Wabunge kama mtazamo alionao Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kabisa kwamba ofisi yangu haina tatizo lolote, tunaomba huo mkakati wake atuandikie ili tuweze kuona jinsi ya kuuingiza katika mipango ya Serikali tuweze ku-support mpango huo ili kuweze kuhakikisha kwamba mazingira yanalindwa kwa gharama zote kuhakikisha kwamba mazingira yako salama lakini tunapambana nahii hali ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kweli inahitaji wadau mbalimbali wote wa Tanzania wote kwa ujumla kuunga mkono jitihada hizi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ngara yapo mabonde matano ambayo Serikali iliyaainisha kwa ajili ya kuanzisha skimu ya umwagiliaji. Upo mradi katika Bonde la Vigombo ambao mradi huo ulianza kutekelezwa na ulitakiwa ukamilike mwaka 2014, lakini mpaka sasa haujakamilika. Haitoshi, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga takribani shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kutekeleza
miradi katika mabonde mawili, Bonde la Mngozi, Kata ya Nyakisasa na Bonde la Muhongo katika Kata ya Bukiliro, lakini mpaka dakika hii tuko quarter ya nne hakuna hata senti moja ambayo ilishapelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini kauli ya Mheshimiwa Waziri kwa wananchi wa Jimbo la Ngara kuhusu upelekaji wa fedha na ili kuweza kutekeleza miradi hii kama ilivyopangwa katika bajeti?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, kwanza ni kweli kuna miradi ambayo
inaendelea kwenye mabonde hayo anayoyaelezea. Lakini kwa sababu wanataka kujua lini ni vizuri hata mimi nikapata nafasi ya kuingia kuuangalia mradi maana siwezi kujua miradi yote lini itakamilika. Lakini lengo la Serikali ni kwamba, miradi yote tutaikamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, na suala la kupeleka fedha; fedha hatuzipeleki tunalipa certificate. Tumeshafanya mambo ya kupeleka fedha halafu unakuta fedha zinakaa hazishughuliki vyovyote. Tunataka matokeo kwa hiyo, fedha tutapeleka kulingana na utekelezaji wa mradi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Dar es Salaam – Isaka – Rusumo, inayojulikana kama central corridor ni barabara inayohudumia nchi takriban nne ambazo zipo kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, lakini kipo kipande cha kilometa 150 kutoka Lusahunga kutoka Rusumo; Nyakasanza kwenda Kobelo mpaka Bujumbura. Kipande hiki kimekuwa ni kero kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana ambao ndiyo
huu tunamalizia 2016/2017 barabara hii ilitengewa shilingi bilioni tano, lakini mpaka sasa hivi ukarabati unaofanyika ni mdogo na kwa bajeti hii ya 2017/2018 tumetengewa shilingi bilioni 1.19 tu kiasi kwamba haiwezi kufanya ukarabati unaoridhisha. Je, ni lini Serikali sasa itaweza kutenga fedha za kutosha ili kukarabati kipande hiki ambacho ni kero kwa Watanzania wanaotumia barabara hii na wageni wanaotoka kwenye nchi za Burudi na Rwanda, Kongo na Uganda ili barabara hii iweze kukidhi viwango na kukidhi mahitaji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Gashaza kwa sababu anapita hii barabara, anafahamu kazi kubwa inayofanywa kuirekebisha hiyo barabara kuanzia Isaka na kuendelea. Tunakwenda kwa hatua; mimi mwenyewe nimeona ukarabati ulioanzia Rusahunga kuelekea Rusumo. Nimeiona, nimepita hiyo barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge, aridhike na hiki kinachofanyika na kwa vyovyote vile, baada ya kukamilisha hii, tutakwenda kukamilisha kipande kilichobakia. Suala siyo rahisi kupata fedha zote za kutosha kuikamilisha barabara yote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuikarabati barabara hii mpaka ikamilike. Tutafika Rusumo, tutafika hii njia inayokwenda Burundi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali kuhusu uhamisho wa watumishi, Halmashauri mbalimbali ikiwemo Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara wameendelea kufanya uhamisho huo bila kulipa stahiki za uhamisho za watumishi hao na hivyo kuzalisha madeni. Je, Serikali inachukua hatua gani juu ya watendaji hawa ambao hawazingatii maelekezo wala mwongozo wa Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza tumekuwa tukitoa maelekezo katika nyakati mbalimbali lakini nimefanya reference ya maelekezo ya mwisho ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 1 Mei, 2017. Tumekuwa tukichukua hatua na mifano ya karibuni tu ni katika Halmashauri ya Kilombero na Bagamoyo ambapo wale ambao hawakuzingatia taratibu hizi waliweza kuchukuliwa hatua mbalimbali za kiutumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuwaeleza Wakurugenzi wetu na Mamlaka za Ajira wazingatie maelekezo haya. Ni lazima pindi wanapofanya uhamisho wawe wametenga fedha katika ikama, lakini vilevile wahakikishe kwamba lengo la uhamisho huo lina manufaa kwa umma na ni katika kuboresha ikama katika Halmashauri zetu.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na ambayo yanatia matumaini. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kutambua kwamba kuna vivutio hivyo katika Jimbo la Ngara, kama maporomoko hayo, lakini bado hifadhi hizo za Burigi na Kimisi na bado kuna vivutio vingine kama pango lililokuwa linasafirisha watumwa kutoka Burundi kupitia Tanzania, pango la Kenza Kazingati, kuna mlima mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera, kuna mito miwili ambayo unaweza ukafanya boat riding na ili vivutio hivi kufanya kazi na kupata watalii ni lazima kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, sasa tuna uwanja wa ndege wa Luganzo. Je, Wizara iko tayari kuboresha uwanja huu wa ndege wa Luganzo ambao unaweza ukasaidia kuleta watalii na wakafanya utalii katika eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ilitegemea kupata gawio la asilimia 25 kutokana na utalii wa uwindaji katika Hifadhi za Burigi na Kimisi. Hata hivyo, takribani miaka 30 iliyopita tangu Hifadhi ya Burigi imeanzishwa na miaka takribani 12 tangu Hifadhi ya Kimisi imeanzishwa ni mwaka jana tu ambapo tumeweza kupata gawio la shilingi milioni 7, gawio ambalo ni dogo. Sasa nahitaji nipate ufafanuzi kwamba shilingi milioni 7 hizi zilitokana na mapato ya kiasi gani na ni wanyama kiasi gani waliowindwa katika hifadhi hizi mbili? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Gashaza kwa ufuatiliaji wake wa karibu na mawazo mazuri katika kuendeleza na kuboresha maeneo haya kama maeneo yanayovutia watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna uwanja wa ndege ambao umekuwa unatumiwa na wawindaji katika eneo lile ambao urefu wake ni mita 1,700. Tutatuma wataalam wetu wanaoshughulika na masuala ya uwindaji ili washirikiane na TAA katika kuboresha uwanja huu ili kuhakikisha kwamba vivutio hivi vinaweza kufikiwa kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uwindaji, Wizara yangu itafuatilia zaidi malipo ambayo yamefanywa ili kuona ni namna gani tunaweza kuboresha ushirikiano kati ya wawindaji, Wizara na wananchi wa Ngara, ili kuboresha hali ya uwindaji katika eneo hilo.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Pamoja na jitihada za Serikali kudhibiti taasisi ambazo zinatoa elimu na mafunzo ambazo hazijakidhi vigezo kwa maana ya kusajiliwa bado kuna taasisi ambazo zinaendelea kufanya hivyo, kwa mfano ni Chuo kimoja ambacho kinaitwa Dodoma College of Business Management ambacho kiko hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe au niseme Mheshimiwa Waziri anaweza kufuatilia na kujiridhisha kuona kwamba Chuo hiki cha Dodoma College of Business Management hakijasajiliwa? Kwa sababu kinasababisha hasara kwa watoto, kwa miaka minne mfululizo chuo hiki kimekuwa kikitoa vyeti ambavyo havitambuliwi na NACTE wala VETA yuko tayari kufuatilia na kujiridhisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kusema kwamba ni marufuku Chuo ambacho hakijasajiliwa rasmi kuanza kutoa mafunzo na kuanza kukusanya ada kwa wazazi kiasi cha kusababisha usumbufu baadaye. Vilevile kwa hicho chuo ambacho unakizungumzia nitaomba nipate taarifa ili tuweze kukifuatilia.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Sambamba na hilo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na miradi ya vijiji kumi ambayo imechukua muda mrefu bila kukamilika. Kwa mfano, mradi wa Kijiji cha Mbuba, Munjegwe, Kanazi, Kabarenzi na Mkibogoye, je, ni lini miradi hii itakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kwamba tumepata shilingi milioni 24 kwa ajili ya pampu ya K9, lakini kwa namna ya kipekee nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 20 alipokuwa Ngara alitupatia shilingi milioni 13 kwa ajili ya kununua pampu ya maji ili kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Ngara. Imeshafungwa na maboresho yamefanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na ahadi yake ni pamoja na kuanzisha mradi ambao unaweza ukawa suluhisho kwa Vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara na Wilaya ya jirani kwa kutumia mradi wa vyanzo vya maji, Mto Kagera, Mto Luvubu na Mlima Shunga na akaahidi kwamba ataagiza Waziri na watendaji kufika kwa ajili ya kuangalia namna ya kufanya usanifu wa mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Waziri na timu yake ya wataalam yupo tayari baada ya Bunge hili kuambatana nami kwenda Ngara ili kuona uwezekano wa kusanifu mradi huu ambao utakuwa ni suluhisho kwa vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara na Wilaya jirani? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia huduma ya maji katika Wilaya yake ya Ngara na hasa Mji wa Ngara ambapo Mheshimiwa Rais alipatembelea na akaweza kutoa fedha za kutengneza pampu ili wananchi wa pale waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maswali yake ya nyongeza, Mheshimiwa Mbunge ameulizia baadhi ya Vijiji ambavyo anasema havijakamilika. Nitoe tu taarifa kwamba Serikali imetenga shilingi 1,500,000,000 katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018 kwa maana ya kuendelea kukamilisha miradi hiyo inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kama nipo tayari kwenda naye Ngara, mimi nipo tayari na nimepanga baada ya Bunge hili nitakwenda Ngara kuangalia huduma ya maji katika Mkoa mzima wa Kagera. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na kwa jitihada ambazo wanazifanya, natambua jitihada hizo; niombe kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Ngara kuna maeneo ambapo kuna mifugo mingi zaidi kuliko maeneo haya yaliyotajwa kuwekwa miradi hii. Kwa mfano kwenye kata za Keza, Nyamagoma, Mnusagamba katika kijiji cha Mnusagamba na Ntanga. Sasa, je, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya kupeleka huduma hii ya malambo katika maeneo hayo kwa sababu ndiyo maeneo yenye mifugo mingi zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye sekta hii ya mifugo, ikiwa ni pamoja na Jimbo la Ngara, hususan baada ya mifugo mingi kutoka maporini kwenye hifadhi kurudi vijijini, kuna tatizo kubwa la migogoro kwa maana ya wakulima na wafugaji, lakini Serikali iliunda Kamati kutoka kwenye Wizara sita ili kupitia mchakato kuona ni namna gani ambavyo wanaweza wakatoa suluhisho la kudumu.
Je, ni lini Kamati hii iliyoundwa ya Wizara sita itakuja na mpango au pengine ku-implement matumzi bora ya ardhi kama suluhisho la kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Alex Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ameuliza juu ya lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya maeneo hayo yenye mifugo mingi. Jambo hili linapaswa yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge na wenzake katika Halmashauri waliibue na sisi Serikali tuko tayari kuhakikisha ya kwamba tunawaunga mkono ili kuweza kuondoa kero hiyo ya ukosefu wa maji kwa ajili ya mifugo katika Wilaya ya Ngara na maeneo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ameuliza juu ya Kamati iliyoundwa na Serikali kupitia Wizara sita kuondoa matatizo ya wakulima na wafugaji, ndiyo maana nilieleza katika jibu letu la msingi ya kwamba maeneo ya Ngara yanalo tatizo kubwa la kuvamiwa na mifugo kutoka nchi jirani na ndiyo maana sisi katika Serikali tumejielekeza ya kwamba hatutarudi nyuma, tutahakikisha mifugo yote iliyotoka nchi jirani kuingia Tanzania kutufanya kuwa sisi ni eneo la malisho tutaitoa kwa namna yoyote ile ama kuikamata na kuhakikisha tunaitaifisha kwa Sheria Na. 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003. Lakini vilevile kwa sheria ya mwaka 2010 inayohusu rasilimali malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na juu ya task force hii iliyoundwa jitihada nyingi zimeshafanyika katika maeneo haya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba maeneo yetu ambayo tulikuwa tumeyahifadhi kama vile Mwisa II yanakwenda kugawanywa kwa ajili ya wafugaji waweze kupata maeneo ya kufanyia shughuli zao za ufugaji kwa nafasi. Naomba sasa Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine watupe ushirikiano kuhakikisha jambo hili linafanikiwa.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mto Kagera, pamoja na Mto Ruvugu ni mito ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kuondoa kero ya maji kwa Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Geita; na kwa kuwa tayari mwaka 2017 Mheshimiwa Rais alipokuja Jimbo la Ngara wananchi wa Jimbo la Ngara kupitia Mbunge wao tulimwomba kuanzisha mradi huu mkubwa wa maji kwa ajili ya kutatua kero ya maji Wilaya za Ngara, Biharamulo, Karagwe, Bukombe, Mbogwe na Chato kwa kutumia fursa ya kijiografia Wilaya ya Ngara.
Ni lini mradi huu sasa utaanza kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu ili kuondoa kero kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na Kagera? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Kamala linahusu pia Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ambapo huyu mkandarasi ambaye anamalizia usanifu wa kina, anahusisha miji sita kama alivyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunarajia kwamba kwa vile tayari upembuzi yakinifu tunao, tunamalizia usanifu wa kina, tunarajia kupanga bajeti kwenye mwaka ujao wa fedha na kuanzia mwezi wa tisa tutaanza kutangaza tenda ambayo itahusha pia na Mji wa Ngara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie pamoja na wananchi wako wa Ngara kwamba tunatekeleza hiyo miradi ili uweze kupata huduma ya maji. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa
kupongeza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano wanaonipa kuhakikisha kwamba tunapata zao jipya Tanzania, zao linaloitwa stevia kupitia Jimbo langu la Ngara.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi tayari wameshatoa kibali cha kuingiza mbegu ya zao la stevier zao ambalo ni sukari ambayo ni anti-diabetes, antipressure lakini zao ambalo ni zao la kuinua kipato cha Watanzania. Pamoja na kutoa kibali hicho kwa sababu ni
zao geni tunahitaji kufanya utafiti kwanza na tayari Wizara imeelekeza Kituo cha Utafiti Maruku ambacho kiko Mkoa wa Kagera kushirikiana na Kampuni ya East African Stevier and Agro-Investment kufanya utafiti wa zao hilo lakini tatizo ni fedha za kufanyia utafiti. Je, Wizara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi wako tayari kutenga pesa ili kuwezesha kituo cha utafiti Maruku kushirikiana na Kampuni ya East Africa Stevier kutoa pesa ili kuweza kufanya utafiti huu na hatimae zao hilo liweze kuanzishwa katika nchi yetu ya Tanzania na kuleta mabadiliko ya uchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Gashaza kwa jitihada na ubunifu ambao ameufanya Jimboni kwake katika kutafuta mazao ambayo yana tija kwa wakulima. Kimsingi tumekuwa tukishirikiana naye kama Wizara ili kuangalia namna ya kuleta nchini zao la stevier
ambalo huko maeneo mengine linakolimwa lina tija kubwa sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo tayari tumeshashirikiana naye katika hatua za kusajili hilo zao, Wizara iko tayari vilevile kushirikiana naye na wananchi wake katika kufanya utafiti katika kituo chetu cha Maruku ili zao hilo liweze kuanza kulimwa nchini na Wizara iko tayari kutenga bajeti ya kawaida ya utafiti kwa kituo hicho ili utafiti huo uweze kufanyika.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa uchafuzi wa mazingira ni pamoja na uchomaji misitu hovyo unaosababisha uzalishaji hewa ya ukaa, na kwa kuwa tayari Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kupitia Mbunge wao tulishandaa andiko la mradi kwa ajili ya kupambana na uchomaji moto Mradi unaoitwa Participatory Community Based bush Fire Management and Livelihood Improvement na tukawasilisha Wizara ya Muungano na Mazingira kwa ajili ya kuanza na vijiji 15 kati ya vijiji 75.
Je, ni lini Wizara yenye dhamana itawezesha ili Halmashauri tuweze kutekeleza mradi huu ambao unaonekana kuwa na tija, kwa sababu tutapanda miti ni macadamia na ufugaji wa nyuki vitakavyopelekea kutoa ajira lakini na kudhibiti mazingira, ni lini Wizara yenye dhamana itawezesha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Alex Gashaza amekuwa akifuatilia sana juu ya andiko lake katika ofisi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakikishie Waheshimiwa Wabunge na nitoe wito kwa Watanzania wote na hasa ambao wanamiliki viwanda, suala la hewa ya ukaa ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumzia ambalo ndio msingi na chimbuko la andiko lake, mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatokea sasa yanaanza kuandama nchi yetu, ni kutokana na hewa ya ukaa inayozalishwa kwenye nchi zilizoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika nchi yetu tumeanza kuwa na maendeleo ya viwanda, kwa hiyo viwanda vihakikishe vinadhibiti hewa ya ukaa isije na vyenyewe vikaendelea kuongeza ukubwa wa tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Gashaza hewa ya ukaa, pamoja na kwamba upandaji wa miti utasaidia sana kwa sababu mchana miti inavuta hewa ya ukaa, kwa hiyo, ni kweli kwamba tukipanda miti kwa wingi tutaweza kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hewa ya ukaa ni bidhaa ambayo ni adimu sana inauzwa kupitia Mfuko wa Mazingira Duniani. Ukiwa na hewa ya ukaa ukaivuna takwimu zile ukizipeleka kule ni fedha nyingi sana.
Kwa hiyo andiko lako Mheshimiwa Gashaza, Ofisi yetu inaendelea kulifanyia kazi, ili kuhakikisha maandiko ambayo tumeomba fedha kwenye mifuko ya Mazingira Duniani itakapopatikana basi andiko lako ambalo wataalam wetu wameliona ni zuri sana tutakwenda kulitekeza. Ahsante sana.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya mwezi Desemba, 2017 kuhusu barabara ya Nyakahura - Murugarama ilieleza kwamba iko kwenye hatua ya mchakato wa manunuzi, ni lini sasa mchakato huo wa manunuzi utakamilika ili barabara hii yenye urefu wa kilometa 85 iweze kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kumpata mkandarasi shughuli za ujenzi wa kipande hicho cha barabara zitaanza mara moja.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna kituo kidogo cha forodha katika eneo la Murusagamba Kusini mwa Wilaya ya Ngara kwenye mpaka wa Tanzania na Burundi, kituo hiki kimekuwa maarufu tangu miaka ya 1970 lakini kwa muda mrefu mpaka sasa kinahudumiwa na watumishi kutoka kituo kikubwa cha Kabanga.
Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kupandisha hadhi kituo hiki ili kiweze kujitegemea kwa sababu kuna ofisi nzuri ya TRA, kuna kituo cha Polisi ni Makao Makuu ya Tarafa ya Murusagamba eneo ambalo ni strategic kwa ajili ya maendeleo. Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kupandisha kituo hiki kuwa kituo cha forodha kinachojitegemea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inafanya tathimini ya vituo vyake vyote vya forodha na vituo vya mamlaka vilivyopo katika ofisi zetu zote ili kutambua uhitaji wa ofisi zote hizo na kwamba tutaweza kubadilisha ofisi zetu hizi. Ni dhamira ya Serikali yetu na ndio maana tumeanza kufanya tathimini na uhakiki wa nini kinachohitajika. Lakini kwa kituo alichokitaja Mheshimiwa Gashaza kuhudumiwa na watumishi kutoka kituo kingine, Serikali ndani ya mwaka huu imetoa tayari nafasi za kuajiri watumishi 52,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya watumishi 52,000 wataajiriwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ili tuweze kuwapeleka katika ofisi zetu zote hasa ofisi zetu za forodha zilizo katika mipaka ya Taifa letu.(Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi, ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa miongoni mwa Retention License zilizofutwa ni pamoja na Retention License No. 0001/2009 ambayo ilikuwa inamilikiwa na Kabanga Nikel Company Limited. Kwa kuwa sababu zilizokuwa zimesababisha Kabanga Nikel wasiweze kuanza kuchimba ni kutokana na bei ya nikel kushuka lakini pia miundombinu ya usafirishaji kwa maana ya reli na Ngara kutokuwa na umeme wa uhakika. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Tanzania na hususan wananchi wa Jimbo la Ngara, ambao walikuwa wanategemea mgodi huu kama ungeanza wangeweza kupata ajira na kuinua kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Alex Gashaza, Mbunge wa Ngara. Kabla sijajibu, niseme tu kwamba, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Alex Gashaza kwa ufuatiliaji wake kwenye mradi huu wa Kabanga Nikel, kwa kweli, amekuwa mtu ambaye kila mara anataka kujua nini kinchoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo jana Naibu Waziri wa Madini, Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Waziri walivyojibu, walieleza juu ya ufutwaji wa leseni zote za retention. Nataka niendelee kumwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba leseni hizi zote za retention zimefutwa kwa mujibu wa sheria na Serikali sasa inaangalia namna bora ya kuzisimamia leseni hizo ambazo zimerudishwa Serikalini.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ni miongoni mwa Halmashauri ambazo ziliendelea kuruhusiwa kukusanya kodi ya majengo lakini Mkurugenzi wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara amekuwa akienda tofauti na kinyume na kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana ilielekezwa kwamba majengo yote itakuwa ni flat rate Sh.10,000, ghorofa Sh.50,000 kwa floor, lakini katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rulenge sasa hivi kuna mtafaruku mkubwa, nyumba ambazo hazijakamilika…

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi kuna nyumba za tope zinatozwa kodi, kuna nyumba za wazee wa zaidi ya miaka 70 zinatozwa Sh.200,000 mpaka Sh.300,000. Naomba Serikali itoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara kwa sababu ni usumbufu na anawatishia kwamba atawapeleka Mahakamani wakati anakiuka sheria na kanuni ya makusanyo ya fedha hizo za property tax. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa maelekezo ya Serikali na sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ilikuwa kwamba majengo yote ambayo hayajafanyiwa tathmini yatatozwa flat rate ya Sh.10,000 kwa majengo ya kawaida na kila ghorofa litatozwa Sh.50,000, kama tu halijafanyiwa tathmini. Kwa majengo yanayotozwa zaidi ya pesa hiyo ni majengo yaliyofanyiwa tathmini, ndiyo sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu inavyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri tajwa kwamba kama anakwenda kinyume na hivyo, anatakiwa kuwashirikisha wananchi wake kwamba tathmini imeshafanyika na kinachotozwa ni kodi stahiki. Kama tathmini haijafanyika, hatakiwi kutoza kodi hiyo anayoitoza. Pia sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu, iliainisha ni nyumba za aina gani. Kwa hiyo, namwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri husika aweze kufuata sheria na taratibu.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa, Mwenyekiti, pamoja na kwamba…
Mheshimiwa Oliver Semuguruka ameuliza swali hilo lakini nataka kusema kwamba Ngara ni sehemu ambayo ni special zone, ni mpakani. Tuna vituo viwili vya forodha vya pamoja, one stop border post kwenye mpaka wa Burundi na Tanzania na mpaka wa Rwanda na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajali iliyotokea ya moto ya tarehe 19 mwezi wa jana ni ajali kubwa, gari sita zikaungua, dereva akafa, kwa hiyo tunaiomba Serikali iweze kuchukua nafasi na iweze kuchukua hatua ili tuweze kupata gari kwenye vituo hivi ambavyo sasa kumekuweko na msongamano mkubwa. Tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikwisha andika barua tangu tarehe 18 Mei, kwa hiyo tunaomba ichukue hatua ya dharura kwa ajili ya maeneo haya (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni ya msingi na tunaichukulia kwa uzito unaostahili. Tunatambua changamoto na location ya ile wilaya yake, Wilaya ya Ngara ama jimbo lake lilivyo, kuna umuhimu wa kuwepo kwa gari la polisi pale kwa sababu Mkoa wa Kagera tuna gari nadhani hazizidi nne ambazo zinasaidia kutoa huduma ikiwemo maeneo ya Ngara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa hilo jambo na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalichukulia uzito unaostahili.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kwanza niipongeze Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya chini ya Waziri mwenye dhamana Naibu Waziri na watendaji wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la ardhi limekuwa na changamoto kubwa hususan katika kutatua migogoro kutokana na uchache wa watumishi kwenye Mabaraza ya Ardhi hususan Mabaraza ya Wilaya. Kwa mfano Wilaya yangu ya Ngara Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya anahudumia zaidi ya Wilaya mbili, na hivyo kupelekea kesi kukaa muda mrefu bila kukamilika, na wananchi wanatoka maeneo mbalimbali na kutumia gharama kubwa hata kuweza kukata tamaa.
Ni lini Serikali itaweza uajiri Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Ngara ili kuondoa usumbufu huu atakaekuwa yuko stationed katika Wilaya hiyo ya Ngara?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Gashaza ametaka kujua ni lini Wizara itapanga Mwenyekiti wa Baraza katika eneo lao, napenda tu nitoe taarifa kwamba upangaji wa Wenyeviti wa Mabaraza kutokana na uchache wa Wenyeviti tulionao unapangwa kutegemeana na wingi wa mashauri katika eneo lile. Lakini kwa habari tu nzuri kwenu ni kwamba sasa hivi tayari tumetangaza nafasi 20 tumepewa, kwa ajili ya kuajiri Wenyeviti watakaokwendakatika Mabaraza.
Kwa hiyo, kitakachofanyika ni tathimini kujua ni Wilaya ipi ina mashauri mengi na inahitaji kuongezewa nguvu na Wilaya zipi ambazo zinakwenda kuanzishwa ili kuweza kupewa Wenyeviti kama Wilaya ya Mbulu ambao huwenda wakapata Mwenyekiti kwa sababu ya shughuri hizo. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi tu kwamba tutalifanyia kazi na kuweza kujua kama watahitaji kuongezewa mtu mwingine.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi. Niipongeze Serikali kwanza kwa kazi nzuri iliyofanyika kwenye mapori ya hifadhi ya wanyamapori Kimisi, Burigi na Biharamlo kwa kuondoa mifugo na sasa hifadhi hizo zimepanda hadhi kuwa National Parks. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna tatizo hususani kwa Maafisa ya Wanyamapori ambao siyo waaminifu ambao sasa wanaenda vijijini na kuswaga mifugo kuingiza kwenye pori la hifadhi kwa lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa. Serikali inachukua hatua gani kwa maafisa hawa ambao sio waamini? Hili limetokea Ngara na ushahidi upo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza na ni kweli kabisa kwamba Serikali imepandisha mapori matano katika eneo lile kuwa sasa ni Hifadhi ya Taifa. Naomba nitumie nafasi hii kumjulisha tu kwamba baada ya kupandisha hayo mapori sasa hakuna shughuli yoyote ya kibinadamu au uwindaji wowote unaoruhusiwa katika maeneo hayo kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa. Kwa hiyo naomba tu tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba hayo hayatokei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba wafanyakazi wetu wanakamata mifugo na kuiingiza kwenye hifadhi halafu ndiyo wanaomba rushwa, naomba nitumie fursa hii kusema kwamba kwanza wafanyakazi hawaruhusiwi kufanya hivyo na pale ambapo inabainika wafanyakazi wetu wanakiuka maadili ya kiutumishi basi tunaomba taarifa wananchi watusaidie kututajia kwamba kuna mfanyakazi huyu na huyu anaomba rushwa nasi tutachukua hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, katika maeneo yote ya mapori nchini hairuhusiwi mifugo wala kilimo kuingia katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwaombeni hakuna mwananchi yeyote anayeruhusiwa kuingiza mifugo ikiingizwa itataifishwa na hivyo ndiyo sheria inavyoelekeza. Kwa hiyo, naomba ushirikiano na wananchi wote.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Ngara Mjini - Nyamiaga - Murukulazo - Lusumo yenye urefu ya kilomita 24 ni barabara muhimu ambayo ipo chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS) lakini ni barabaara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya na nchi jirani ya Rwanda na kuna mradi mkubwa wa umeme unaoshirikisha nchi tatu, je, Serikali iko tayari kupandisha barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni pamoja na kujenga daraja kwenye Mto Ruvubu ambapo kwa sasa tunatumia ferry? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Kumwendo - Kigarama - Mururama - Bukiriro ni barabara inayounganisha kata tatu, Kata ya Kabanga (kijiji cha Juligwa); Kata ya Mbuba na Kata ya Bukiriro. Kipo kipande cha Mkajagali ambacho kiko karibu na mto lakini barabara hii wakati wa mvua haipitiki inatakiwa kujengwa daraja na tayari Meneja wa TARURA alishapeleka maombi maalum ili kujenga box culvert mbili zenye kipenyo cha mita 2.5 kwa ajili ya kuunganisha kata hizi…
Mheshimiwa Spika, nauliza, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya kujenga daraja hili ili kurahisisha mawasiliano kwa kata hizi tatu, fedha zisizozidi shilingi milioni 300? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hizi naweza kuzifahamu kwa sababu tumezungumza naye mara nyingi sana. Nimpongeze wakati akizungumza imenipa nafasi ya kuzifahamu vema barabara hizi lakini pia kuona changamoto zilizokuwepo tuweze kuzishughulikia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza, hii barabara ambayo inatoka Rusumo inapita ng’ambo kwenda Ngara ina urefu kama kilometa 24 hivi, najua kuna kivuko pale lakini barabara hii ni muhimu kwa sababu ujenzi wa barabara hii utatufanya sisi tutekeleze sera ambayo inataka mikoa yetu tuweze kuiunga na nchi za jirani na maeneo haya yanaunga upande ule wa Rwanda. Kwa hiyo, hiyo hii barabara itafupisha safari kwa wasafiri wanaotoa Rusumo kwenda Ngara. Ziko kata mbili hizi, niseme tu kwa maeneo hayo ya Murukuruzo na Nyamiyaga ni muhimu na pia tutaweka kivuko kwenye upande mwingine ambapo tunahamisha kile kivuko baada ya kujenga daraja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hili ili kutoa hiki kivuko ambacho tutakiweka tutakifanyia kazi. Nimuombe tu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera atazame eneo hili tuone uwezekano wa kuweka daraja. Kadri tunavyofanya improvement kubwa katika maeneo mbalimbali kwetu sisi ni fursa ili kuja na hatua zingine za kuendelea kutibu maeneo ambayo ni korofi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, eneo hili la Rulenge ni kweli yapo madaraja ya chini na ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo haya yanapitika. Kuna wakati mwingine tunapata mvua nyingi inalazimika wananchi wa maeneo haya kutopita kwa muda kupisha maji yapite na hivyo kuwa na usumbufu kidogo wakati wa mvua nyingi. Kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba wamewasilisha maombi maalum, tutayazungumza ili tuone hili ombi maalum linashughulikiwaje ili hiki kiasi cha takriban shilingi milioni 300 kiweze kutumika kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maeneo mengi nchini kunapokuwa na drift hizi ni kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapita maeneo haya wakati wowote. Kila wakati tunaendelea kufanya maboresho ya barabara zetu lakini tunaanza kutengeneza madaraja ili wananchi waweze kupita. Kwa hiyo, nimtoe hofu yeye pamoja na wananchi wa Ngara na hususan wa maeneo haya ya Rulenge kwamba eneo hili tutalitazama ili Kata hii ya Kabanga pamoja na kata mbili jirani zake ziweze kuunganika vizuri.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapema mwaka 2017 niliwasilisha andiko la mradi ujulikanao kama Commitment Bush Fire Management and Livehood Improvement kwa lengo la kudhibiti uchomaji moto ovyo. Ni lini Wizara yenye dhamana itaweza kuwezesha mradi huu kwa kutoa fedha ili tuweze kutekeleza kikamilifu kwa kuanzisha zao ambalo ni rafiki na mazingira lakini pia na ufugaji wa nyuki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, mapema katika Mkutano uliopita Mheshimiwa Gashaza aliuliza swali la nyongeza kuhusiana na mradi wake huu.
Napenda nimhakikishie kwamba sasa hivi Ofisi ya Makamu wa Rais inaandaa maandiko mbalimbali kwa ajili ya kuomba fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunahamasisha Halmashauri za Wilaya waweze kuandika maandiko ambayo watayaleta Ofisi ya Makamu wa Rais ili tuweze kuwatafutia fedha katika kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Gashaza, andiko lake tumelipitia ni muhimu sana. Pia aliweza kuwahusisha wananchi wa Jimboni kwake kupitia michezo wakiwa na kauli mbiu ya kwamba mazingira ni uchumi ili waweze kucheza ligi ile na kauli mbiu hiyo waweze kuhakikisha kwamba wanajihusisha na ufugaji wa nyuki pamoja na kilimo ili wasiendelee kuchoma misitu ambayo inaendeleza uharibu wa mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Gashaza kwamba hata hiyo ligi yake, baada ya kupata fedha mimi mwenyewe nitaenda kumsaidia kuizindua ili iwe kichocheo kwa nchi nzima ili wananchi wengine nao wafanye hivyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitaomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ngara kimejengwa tangu enzi za ukoloni na majengo yake yamechakaa pamoja na nyumba za watumishi kwa maana nyumba za askari wetu. Sasa ni lini Serikali itaweza kukarabati kituo hiki cha polisi na nyumba za askari wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Jimbo la Ngara wameathirika kwa kiasi kikubwa sana na operesheni zinazoendelea hususani za Uhamiaji. Maeneo mengi Dar es Salaam, Kahama, Arusha, Ngara kwenyewe wananchi hawa wanapokamatwa kwa kuhisiwa na kueleza kwamba wanatokea Ngara moja kwa moja wanachukuliwa kwamba ni wahamiaji haramu. Wamekuwa wakipigwa na kuumizwa na baadaye baada ya kujiridhisha inaonekana kwamba ni Watanzania halisi. (Makofi)
Sasa je, Serikali iko tayari pale inapobainika kwamba wananchi hawa wamehisiwa, wakadhalilishwa, wakapigwa wako tayari kulipa fidia kwa hawa wananchi wanaokuwa wamedhalilishwa na kupigwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua kuhusiana na uwezekano wa kukarabati Kituo cha Polisi Ngara pamoja na nyumba za polisi. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba dhamira hiyo kwa Serikali ipo na pale tu ambapo hali ya kifedha itaruhusu tutakarabati kituo hicho cha Ngara na nyumba za polisi pamoja na maeneo mengine nchini ambako kuna changamoto kubwa za uchakavu wa vituo na nyumba za polisi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wananchi ambao wamepigwa na kuonekana kwamba wamedhaniwa kwamba si Watanzania. Kwanza si utaratibu wa Jeshi la Polisi kupiga raia ama hata wageni. Kuna utaratibu wa kisheria ambao ikiwa mgeni ama raia amevunja sheria unatakiwa uchukuliwe kwa mujibu wa sheria. Nadhani suala hili labda Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili tukae tuone jinsi gani tunaweza kulichunguza ili tujue hatua za kuchukuliwa baada ya hapo kama kutakuwa kuna ukiukwaji wa sheria, sheria iweze kufuata mkondo wake.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa ipo zahanati ya Kijiji cha Kigarama ambayo jengo la OPD limejengwa kwa nguvu ya wananchi mpaka kukamilika, lakini zahanati hiyo takribani miaka miwili haijaweza kufanya kazi kwa sababu hakuna nyumba ya watumishi na choo hakijakamilika. Upo uwezekano wa kupata nyumba ya kupanga kwenye center hiyo ya karibu ambapo ni rahisi Mganga kuweza kuhudumia akitokea hapo. Je, Wizara iko tayari kutoa kibali ili zahanati hiyo iweze kufunguliwa kuondoa adha ya akinamama wanaokwenda kujifungua kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 30 wakati tayari wameshatoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa kauli yako naomba nimwagize Mganga Mkuu wetu wa Mkoa wa Kagera aende akafanye ufuatiliaji wa zahanati hiyo, kama imekamilika kweli lazima wahakikishe nguvu za wananchi ambao lengo lao wapate huduma kuhakikisha kwamba wanaipata. Kwa hiyo namwagiza Mganga wetu Mkuu wa Mkoa wetu wa Kagera aende akafanye kazi ili na Mheshimiwa Mbunge apate kibali na wananachi wapate huduma.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa upo mradi wa maji ambao tunautegemea sana katika Wilaya ya Ngara, mradi ambao tayari umeshapata kibali cha Serikali; na mwaka huu unaoishia kwenye bajeti zilikuwa zimetengwa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanza usanifu wa mradi huu.

Ni lini Mhandisi Mshauri atakuwepo site tayari kwa ajili ya kuanza usanifu wa mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, binafsi nilipata nafasi ya katika Jimbo lake la Ngara na tumeona chanzo cha Mto Ruvubu ni chanzo cha uhakika na kina maji mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama viongozi wa Wizara ndiyo maana tukamtuma mtaalam wetu. Kwa hiyo, kubwa tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha Mhandisi Mshauri anapatikana kwa haraka ili kazi iweze kuanza mara moja na wananchi wake waweze kupata mradi huo.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mhandisi Mshauri yupo site kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Nyakahura - Lulenge – Mulugarama; na kwa kuwa barabara hii ni ya muda mrefu.

Ni lini sasa ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Gashaza, ni kwa muda mrefu sana amekuwa akifuatilia hii barabara ambayo naomba niitamke kwa ladha yake; inaitwa Nyakahuura – Kumubuga, inapatia Murusangamba - Lulenge mpaka Murugarama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri anakiri kwamba Mshauri Mwelekezi yupo pale kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na baada ya kumaliza zoezi hilo atafanya usanifu wa awali kisha usanifu wa kina kupata michoro kwa ajili kutambua gharama za ujenzi. Hatua zinakwenda vizuri mpaka sasa hivi. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo. Tukishapata nyaraka zote hizo husika, hiyo barabara itaanza kurekebishwa tena kwa kiwango cha lami.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa katika Jimbo la Ngara hakuna maeneo yaliyotengwa kwa maana hakuna blocks kwa ajili ya malisho ya mifugo, sasa Serikali kupitia Wakala wake wa Mafunzo ya Mifugo Nchini LITA, wako tayari kuanzisha kituo hiki cha Incubation Youth Center katika Wilaya ya Ngara ambako kuna mifugo mingi zaidi ya Ng’ombe 75,000 ili kuweza sasa kuwawezesha vijana kuanzisha mashamba darasa ili waweze kujikimu kiuchumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa upo mnada ambao Serikali iliweka fedha nyingi, mradi wa Mursagamba uliojengwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, natambua kwamba Serikali imepeleka fedha sasa kwa ajili ya kukarabati ili uweze kuanza kutoa huduma, ni lini sasa mnada huu utafunguliwa ili uanze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Alex Gashaza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba Chuo chetu cha LITA kilichopo pale Mkoani Kagera, katika Wilaya ya Karagwe katika ranch yetu kubwa ya Kikurura complex tutakitumia kwenda kufanya mafunzo ya hii program maalum ya Incubation Youth Center kwa ajili ya kuwanufaisha watu wa Wilaya ya Ngara, vijana mahususi kwa ajili ya kuweza kutumia fursa ya mifugo iliyokuwa mingi kuzalisha na kupata ajira na kuinua kipato chao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni juu ya mnada wa Mursagamba; ni kweli katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali na Wizara yetu ya Mifugo tulitenga pesa kwa ajili ya kuweza kuufanyia marekebisho mnada wa Mursagamba na hivi ninavyozungumza, utaratibu wa kuweza kukamilisha hatua hiyo unaendelea na mara tu baada ya kukamilishwa kwa hatua hiyo tutakwenda kuufungua na tutamkaribisha Mheshimiwa Mbunge Gashaza ambae ailipigia debe sana kuhakikisha mnada huu unafunguliwa ili na yeye aweze kushiriki kikamilifu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu na Wilaya ya Ngara kwa ujumla wake.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niliulize swali dogo la nyongeza. Hospitali ya Nyamiaga ni Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ambayo ilipatiwa hadhi kutoka kituo cha afya mwaka 2013, lakini mpaka sasa hivi hakuna maboresho ya miundombinu katika hospitali hiyo. Kwa hiyo kuna upungufu wa jengo la utawala, jengo la upasuaji, jengo la X-Ray, mortuary na labor Ward:-

Ni lini Serikali itaweza kutenga fedha kwa ajili kuboresha hospitali hiyo ukizingatia kwamba hatuna hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gashaza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba maeneo mengi ambayo vilikuwa aidha vituo vya afya au ilikuwa zahanati ikapandihswa hadhi; kwanza tumekuwa na changamoto ya eneo, hata pale ambapo tumepandisha hadhi kituo cha afya kuwa hospitali ya Wilaya inakuwa haina hadhi ya kulingana na hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba Serikali katika utaratibu mziwa wa kuboresha na kujenga Hospitali za Wilaya zile za mwanzo zinaanza kuonekana kwamba zimeanza kuwa outdated. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri ambavyo tumeanza na hosptali 67, zikaongezeka 27 kwa kadri bajeti itakavyoruhusu hakika na wao hatutawasahau ili wale na Hosptali ya Wilaya yenye hadhi ya kulingana na Hospitali za Wilaya za Halmashauri nyingine.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Wiki tatu zilizopita niliuliza swali kuhusu Zahanati ya Kigarama ambayo wananchi wamejenga kwa nguvu zao, miaka miwili wamekamilisha OPD, lakini kuna upungufu wa choo na nyumba ya Mganga na haiwezi kufunguliwa kabla ya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itaweza kukamilisha majengo hayo yanayopungua ili Kituo hiki kiweze kutoa huduma kwa wananchi ambao wanahangaika muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jambo hili tunalifahamu na kama nilivyojibu tangu wiki iliyopita ni kwamba tupo kwenye mchakato wa kupeleka fedha za kumalizia maboma ya Zahanati na Vituo vya Afya na naomba jambo hili tulichukue kwa uzito, tutalifanyia kazi, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi. Ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Ngara ni sehemu ya Mkoa wa Kagera na ni Wilaya inayopakana na nchi mbili kwenye Mpaka wa Rusumo kwa maana kupakana na nchi ya Rwanda na mpaka wa Kabanga kupakana na nchi ya Burundi. Kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, kwenye mipaka hii kuna vituo vya pamoja vya forodha, lakini ipo fursa ya masoko ambayo hatunayo sasa na hivyo kupelekea wananchi wetu washindwe kufanya biashara katika maeneo haya ya mipakani.

Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kujenga masoko maeneo hayo ikiwezekana shopping malls ili kunufaika na fursa hii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Halima Bulembo na swali lingine la Mheshimiwa Gashaza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali la Mheshimiwa Halima Bulembo kuhusu kujenga kituo kikubwa cha biashara cha Afrika Mashariki katika Mkoa wa Kagera, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Serikali yetu ipo katika mpango mkakati wa kujenga kituo kikubwa cha kibiashara pale katika eneo la Nyakanazi ambapo soko hili litaweza kufikiwa na wananchi wetu wa mikoa inayozunguka Kagera, lakini pia nchi za DRC, Burundi, Rwanda na Uganda wote watakuwa na fursa ya kufika pale Nyakanazi kwenye kituo kikubwa hiki ambacho Serikali yetu kwa kushirikiana na Halmashauri zetu imeanga kukijenga kuanzia sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye swali la Mheshimiwa Gashaza kuhusu Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kujenga masoko haya pale Rusumo na Kabanga, nilifika pale Kabanga na kuona hali halisi ilivyo na tayari upo mradi ambao unaendelea wa ujenzi wa soko la kimataifa pale Kabanga ambapo naamini ndani ya miaka miwili litakuwa limekamilika na wananchi wetu watakuwa wamefikiwa ili waweze kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo, kule Rusumo pia Serikali ipo kwenye mpango wa kuhakikisha tunaanzisha soko ili kuhakikisha sasa wananchi wetu wa Kagera wananufaika na jiografia yao ya kupakana na nchi zilizozunguka.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, napongeza viongozi wote wa Wizara hii ya Madini, Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na matokeo yake tunayaona.

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwamba tayari katika mchakato huu na katika ombi hili wameshatekeleza kwa sehemu kwa kuwapa kibali wachimbaji hawa kwa kuanza na tani 500, nashukuru na kuipongeza Serikali kupitia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa lipo soko kubwa la madini haya ya manganese nje ya nchi; Uturuki, India, Afrika Kusini na tayari wachimbaji hawa wadogo wameunganishwa kwenye masoko hayo lakini uchimbaji wa madini hayo unahitaji mtaji mkubwa kwa maana mitambo pia ya kisasa, Serikali iko tayari kuwawezesha wachimbaji hawa wadogo wadogo ili waweze kupata mitambo kama excavator, tipping trucks ili waweze ku-meet uhitaji wa soko na kuongeza kipato kwa Serikali yetu na kwao binafsi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa vile miongoni mwa madini yanayopatikana katika Jimbo la Ngara ni pamoja na Nickel na kwa muda mrefu tumekuwa tukisubiria kuona mradi huu wa Kabanga Nickel unaanza ili kutoa ajira, kuongeza kipato kwa wananchi wa Jimbo la Ngara na Watanzania kwa ujumla, ni lini mgodi huu utaanza ili kuweza kuleta tija kwa wananchi na kwa Taifa pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli soko la Manganese lipo ndani ya nchi na lipo nje ya nchi, na wachimbaji wadogo wamekutana sana na changamoto ya kuwa na upungufu wa mitaji kwa maana ya kununua vifaa vya uchimbaji, Serikali kupitia ule mradi wa SMRP ambao ulikuwa unafadhiliwa na World Bank kupitia katika Wizara yetu ya Madini ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini ruzuku hizo hazikutumika vema inavyostahili ndipo tuliposimamisha utoaji wa ruzuku hizo na sasa hivi tunatoa elimu kwa wachimbaji, tunatoa taarifa za uchimbaji kwa maana ya geological information na hizi taarifa tunazipendekeza kuzipeleka, au tunazipeleka na kuwashauri watu wa mabenki mbalimbali waweze kuzitambua taarifa hizi na kuweza kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo ili wachimbaji hao waweze kukopa na kununua vifaa mbalimbali ambavyo vinaweza vikatumika katika uchimbaji na kuongeza tija katika uchimbaji huo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na mgodi wa Kabanga Nickel ni kweli kabisa nickel hapo kipindi cha nyuma katika soko la dunia ilikuwa na bei ya chini sana ambapo uchimbaji wake ulikuwa hauna tija, kwa sababu bei ya nickel katika soko la Dunia ilikuwa chini ya dola 3.5 kwa pawn moja, lakini sasa hivi, bei ya pawn moja ya nickel imepanda kwenda hadi dola Sita katika soko la Dunia ambapo Wawekezaji sasa wameanza kuona kwamba wakiwekeza kwenye nickel itaweza kuwa na faida, katika ule mradi wa Kabanga moja ya leseni ambayo ilikuwa ni retention license ilifutwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya mabadiliko ya sheria mwaka 2017 hapa tulipo ni kwamba ile retention license ipo na sasa hivi tunaifanyia mchakato wa kutafuta Mwekezaji ambaye tunaona yuko serious anaweza akawekeza, sasa hivi tuko tayari kutoa leseni hiyo kwa mtu yeyote ambaye tunaona anaweza akafanya shughuli hiyo, mpaka sasa hivi tuna mchakato unaoendelea ndani ya Wizara yetu kuona namna ya kuweza kumpa Mwekezaji ambaye tunaona anaweza akawekeza kwa faida na mradi huo uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni wakati wowote watu wa Kabanga wataona mradi huo unaanza na ninapongeza Serikali kwa juhudi zake za kupeleka umeme eneo hilo pamoja na miundombinu ya reli na barabara ambayo sasa itakuwa ni miundombinu muhimu katika utekelezaji wa mradi huu wa Kabanga Nickel.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara, lakini kipo kipande cha barabara kutoka eneo la Rusaunga kuelekea Rusumo mpakani barabara inayoelekea Rwanda kimeharibika kuna mashimo utafikiri ni mahandaki, hii inapelekea magari kuharibika na kusababisha ajali zisizo za lazima. Magari sasa yanachepuka kupitia barabara ya Rusaunga, Rurenge, Mrugarama ambayo ni ya vumbi na hivyo kuendelea kusababisha uharibifu kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa kwa kiwango kinachostahili ukizingatia kwamba ni barabara ya kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii kutoka Rusaunga kwenda Rusumo kilomita 92 ni barabara ambayo imechoka imechakaa ina mashimo, ina mahandaki na imekuwepo kwa miaka mingi sana ni zaidi ya miaka 34 na Serikali imekuwa ikifanya juhudi ya kuiboresha barabara hii kwa sababu imejengwa muda mrefu kutoka Isaka kwenda Rusumo, kwa sehemu kubwa ya barabara hii matengenezo yamekuwa yakifanyika tumebakiza hizo kilomita 92.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote katika Mkoa huu wa Kagera kwamba tumetenga fedha kwenye Bunge hili la kuifanyia matengenezo upya barabara hii, lakini kwa hatua za awali kuboresha haya mahandaki ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaita kuna fedha tayari Serikali imeshatoa na tulikuwa tunakamilisha hatua za manunuzi, mkandarasi ameshapatikana tutaanza kwanza kuboresha ili kuyapunguza haya mashimo Mheshimiwa Mbunge, tutayapunguza wakati harakati zile za kuanza mradi mkubwa wa kuboresha barabara hii haya mashimo tutakuwa tumeyaondoa.(Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, takribani watoto 115 waliomaliza darasa la saba mwaka jana na kufanya mtihani kutoka Jimbo la Ngara katika Shule ya Msingi Kumnazi walifutiwa mtihani na wazazi wa watoto hao kwa umoja wao walimwandikia Katibu Mkuu Baraza la Mitihani barua ya tarehe 10 Desemba lakini mpaka sasa hivi hawajapata majibu. Watoto na wazazi wamechanganyikiwa ukizingatia ni watoto yatima na wengi wao ni watoto wa maskini. Nini kauli ya Serikali kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwanza swali hili halina uhusiano na swali la msingi ambalo nilikuwa najibu lakini naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barua ambao wazazi wale wameandika kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani, naomba nifuatilie nijue barua hiyo majibu yake yanatoka lini. Hata hivyo, ifahamike tu kwa umma na kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba ni kosa kujihusisha na uhalifu wa mitihani. Kwa hiyo, pale mtuhumiwa atapobainika kwamba kweli amehusika hatua stahiki zinachukuliwa na hatua hizo inakuwa ni pamoja na kumfutia mtihani na matokeo. Kwa hiyo, ifahamike tu kwamba kwa kweli ni kosa lakini nitaenda kufuatilia halafu nitampa jibu.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mbali na Kituo cha Kabanga, kuna Kituo kidogo cha Forodha cha Murusagamba ambacho kinalelewa na Kituo cha Kabanga. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupandisha hadhi Kituo hiki cha Murusagamba ili kiweze kuwa kituo kamili hasa kwamba upo mkakati wa kuunganisha barabara ya lami kutoka Nyakahura – Murusagamba - Burundi route ambayo pia itaendelea kuwa karibu? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa hivi ina Vituo vya Forodha vipatavyo 97 na upandishwaji wa Vituo vya Forodha kutoka kuwa vituo vidogo kuwa vituo kamili vya forodha huwa vina criteria yake ambayo na Kituo cha Murusabanga nacho tutaendelea kukifanyia kazi na tathmini. Kikikidhi vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa kituo kamili cha forodha kutokana na shuguli nyingi za kiuchumi zinazofanyika maeneo yale, Serikali haina shaka kukipandisha kituo hicho na Mheshimiwa Mbunge wa Ngara tuko tayari kufika tuweze kufanya tathmini hiyo.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa matukio haya yamekuwa yanajitokeza mara kwa mara hususan katika Kijiji hicho cha Kabukome; na kwa kuwa Serikali imetoa maelekezo kwa Halmashauri kwamba wananchi hawa waweze kuwasilisha madai yao ili waweze kulipwa kifuta jasho: Je, Naibu Waziri pengine baada ya Bunge hili kufika katika eneo hilo ili kuweza kushauriana pia na wananchi wa eneo hilo kuona ni namna gani ya kuweza kuzuia tukio hili lisiweze kuwa endelevu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Kijiji hiki cha Kabukome kinavyoathirika inafanana sana na baadhi ya vijiji katika Jimbo la Ngara vinayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato, Kijiji cha Gwakalemela Kata ya Kasulu na Kijiji cha Rusumo Kata ya Rusumo kwa sababu matukio haya yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara, anaweza akafika pia katika maeneo hayo kwa ajili ya kushauriana na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo namna gani ya kuweza kuendelea kudhibiti uvamizi wa wanyama hawa hasa tembo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Alex Gashaza kwa kuwa mshiriki mzuri katika uhifadhi, amekuwa pia akitusaidia sana kurejesha mahusiano kati yetu na wananchi katika maeneo yanayozunguka pori la Burigi - Chato. Pia namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Oscar Mukasa kwa sababu amekuwa akifuatilia sana haki za wananchi wake katika eneo hili ambalo wamepata mgogoro wa wanyama.

Mheshimiwa Spika, taratibu za kulipa fidia ndiyo zinazosumbua kwenye maeneo mengi. Inatakiwa mwananchi anapopata tatizo la kuliwa kwa mazao yake au kushambuliwa na wanyama, ndani ya siku tatu, kama ni shamba awe ametoa taarifa kwenye Serikali ya Kijiji; na Afisa wa Kilimo amekagua na kuwasilisha kwa Afisa Wanyamapori wa Wilaya. Afisa Wanyamapori au Afisa wa Kilimo wa Wilaya ndiye anayeleta taarifa hizi kwenye Wizara yetu nasi tunashughulikia.

Mheshimiwa Spika, kama ni shamblio la mauaji, Afisa wa Kijiji anatoa taarifa Polisi na Polisi na Daktari wanafanya postmortem na baadaye taarifa hizi zinafika kwenye Wizara yetu nasi tunaweza kulipa. Hata hivyo, sehemu nyingi taarifa hizi zinachelewa kufika, zinafanyika baada ya tukio kupita muda mrefu, kwa hiyo, wanapokwenda watu wa kufanya tathmini, wanakuta shamba lilishapata uoto mwingine wa asili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi Wizara yetu iko tayari kutoa kifuta jasho na kifuta machozi mara tu tukio hili linaporipotiwa ndani ya muda.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, anaomba mimi Waziri nipate nafasi kwenda Jimboni kuweza kushirikiana kutoa elimu katika vijiji vya Benako, Kalemela na Kasulo, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari na nitafanya hivyo baada ya Bunge hili. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Ngara tumehamasisha vijana wanaosoma vyuo vikuu nchi nzima wanaotoka Wilaya ya Ngara kwa ajili ya kuweka umoja na ushirika na miaka miwili mfululizo wamekuwa wakija kujitolea wakati wa likizo ndefu kufundisha kwenye shule zetu za sekondari na tayari wamesajili shirika lao linaitwa Mzalendo Education Organisation (MEO). Serikali iko tayari kuwashika mkono ili kusudi waweze kuendelea kutengeneza mazingira ya ajira kwa vijana wenzao kwa sababu tayari Halmashauri imeshawapatia ekari 10 kwa ajili ya kuanza miradi ya mfano.

Je, Serikali wako tayari kuweza kuwashika mkono ili vijana hawa wawe mfano kwa vijana wenzao nchi nzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuunganisha vijana katika eneo lake na kuwapa mawazo haya ambayo ni mawazo mema kweli kweli. Ni kweli, tupo tayari na utayari wetu umeshaanza kutekelezwa. Naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara na Afisa Elimu pale waende katika eneo hili wakutane na vikundi hivi vya vijana, wazungumze nao halafu walete maoni ni kitu gani hasa wanataka kusaidiwa ili waweze kufanya kazi hii nzuri ambayo imeanza. Ahsante sana.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na sasa naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa bado kuna vijiji ambavyo havijaweza kupata minara ya mawasiliano kama vile Kijiji cha Kititiza, Kikoi, Mkalinza Kata ya Mabawe na maeneo mengine ya Jimbo la Ngara, ni lini Serikali itaweza kuwezesha ujenzi wa minara katika maeneo hayo yaliyobaki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, baadhi ya maeneo hususan katika Kata za mipakani kama vile Kata ya Kabanga, Mabawe, Rusumo, Kata ya Kasulu, Kata za Mipakani zinazotokana na nchi ya Burundi na Rwanda, usikivu umekuwa ni hafifu na hata kuwepo na mwingiliano wa mitandao ya nchi jirani. Je, Serikali ina mkakati gani kumaliza tatizo hili la mwingiliano wa mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Gashaza kwa ajinsi anavyofanya bidii kubwa sana kushughulikia wananchi wake kupata mawasiliano. Nikianza na swali lake la kwanza Vijiji vya Mabawe, Kititiza na Kigoi tunategemea kuviingiza kwenye mpango wa vijiji 811 ambavyo tunategemea kuvitangaza hivi karibuni kwa ajili ya kupatiwa huduma ya mawasiliano kabla ya mwezi wa tatu mwakani. Kwa hiyo, namuomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira vijiji hivyo vitapatiwa mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli kwamba bado tuna changamoto kubwa kwenye maeneo ya mipakani ambapo mawasiliano yamekuwa yakiingiliana kati ya nchi jirani na nchi yetu. Hata hivyo, tumechukua hatua za dharura kwa kuwaelekeza TCRA washirikiane na mamlaka za mawasiliano za nchi jirani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mwingiliano huo unapunguzwa au kuondolewa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huo umefanyika Mjini Arusha mwezi wa Nne kupitia kikao chao cha East African Communication (EACO) ambapo umeshaweka mkakati na kwa kuanzia maeneo ya mikoa ya Moshi na Kagera Vodacom wameshaanza kurekebisha mwingiliano wa mawasiliano ili kuhakikisha kwamba kila nchi inapata mawasiliano ambayo anahusika nayo badala ya kufanya roaming.