Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Charles John Mwijage (7 total)

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nichukue fursa hii kumuuliza swali dogo Mheshimiwa Waziri wa Jeshi la Ulinzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo la Jeshi la Kambi ya Kaboya katika Vijiji vya Mayondwe na Bugasha uhakiki ulishafanyika na kwa sababu wakati wowote Waziri anategemea kupata pesa kutoka Wizara ya Fedha, anaweza kuwahakikishia wananchi hao kwamba baada ya kulipa Kilwa sasa ni zamu ya Kaboya kabla ya mwezi Juni?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwijage, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali ni maeneo mengi ambayo tunastahili kulipa fidia na baadhi uhakiki umeshafanyika kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge. Natambua kwamba eneo la Kaboya linastahili fidia na uhakiki umekamilika tunachosubiri ni fedha. Kwa maana hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zilizotengwa katika bajeti endapo zitapatikana kabla ya mwisho wa mwaka huu basi Kaboya nayo tutaijumuisha katika maeneo yatakayolipwa fidia.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuwa umekamilisha kumlipa mtu fidia unapoweka pesa kwenye akaunti yake. Kwa nini sasa Serikali isiwalipe wananchi wa Kyamkwikwi kwa kuhakikisha pesa zinaingia kwenye akaunti zao kabla ya mwisho wa mwezi huu ili jibu la Mheshimiwa Waziri liweze kuwa sahihi? Hawa watu hawajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tunapozungumza Bandari ya Kyamkwikwi tunamaanisha huduma kwa Visiwa vya Bumbile, Makibwa, Nyaburo, Kerebe na Gooziba. Sasa kwa nini Serikali isichukue maoni ya wananchi waliyoyatoa kwa Kepteni Mwita wa MV Clarias juu ya chombo muafaka cha kuweza kwenda katika hivyo visiwa nilivyovirejea? Kwa sababu unapozungumzia MV Chato, MV Chato haiwezi kupita kwenye mkondo wa Makibwa kuelekea Kerebe.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI(MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuelekeze Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi atumie wataalam wake atueleze status ya fidia ya wananchi hawa, itakapofika Bunge la jioni Mheshimiwa Mbunge atapewa majibu sahihi ni lini wananchi wake watalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anasema ni kwa nini tusichukue maoni ya wananchi waliyotoa kwa Kepteni Mwita kama alivyotaja, ili yaweze kufanyiwa kazi kwa lengo kubwa la kuboresha huduma ya usafiri katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuyapokee maoni haya tuyafanyie kazi, yapitiwe na wataalam wetu tupate ushauri sanifu ili tuweze kutekeleza kama ambavyo tunapaswa kukidhi mahitaji ya wananchi. Kwa sababu lengo la Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhudumia wananchi, tena wananchi wale ambao wana uhitaji mkubwa hasa wa pale Muleba Kusini na Kaskazini.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kuanzisha block farming kwenye maeneo aliyoyataja kama kwetu Kigoma, maeneo yanayotengwa yanauzwa kwa watu kwamba hekari Tano njoo utoe pesa, lakini mojawapo ya lengo la block farming ni kuwagawia wale wananchi ambao ndio walikuwa wazalishaji wakubwa kwamba Serikali muwabebe halafu mkiwabeba kwa gharama za Serikali ile pesa mliowekeza wananchi watairudisha unapouza.

Kwa nini Serikali sasa msijiandae mkafungua maeneo makubwa mukawatoa Watanzania kwenye nusu heka kwa kaya mkawapeleka heka tano na mkavumilia tunapouza kwa sababu haya mazao ya kimkakati, tutakapouza tukaweza kurudisha hizo pesa kwenye Mfuko wa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwijage kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, dhana ya block farming kama alivyoieleza ina njia mbili, aidha Halmashauri ikitenga eneo watu wenye uwezo waweze kununua kuwekeza na kumilikishwa eneo hilo, lakini njia nyingine ni eneo ambalo ardhi inakuwa ni mali ya Halmashauri halafu Wawekezaji wanakuja kuwekeza kwa kupewa long term leasing ambayo wao wanawekeza.

Kwa hiyo, nilitaka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba kama Wizara tuko tayari kukutana na Halmashauri yoyote ambayo itakuwa tayari kujadiliana na sisi tutengeneze module ambayo ita attract watu wengi kuweza kuwekeza katika eneo hilo na hilo ni wazo ambalo tunalipokea na tuko tayari kuweza kujadiliana kuweza kufanikisha jambo hilo.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba, sasa Tanzania ni soko la chakula, naomba Serikali itueleze kasi ya Serikali katika kuwekeza kwenye umwagiliaji kwa kutumia sekta binafsi katika mito ambayo ina maji yasiyokauka, mito kama mabonde ya Kagera, basin ya Viktoria, Ruvuma na maziwa yetu? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Katika maelezo ya hizo hekta 95,000 zinazozungumzwa naomba Serikali inihakikishie hekta 11,000 za Mto Ngono na zenyewe zimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, katika Jedwali la Sita katika Kitabu cha Bajeti iliyosomwa na Waziri wa Kilimo limeelezea mabonde 22 ambayo Serikali imeamua kuyafanyia upembuzi yakinifu na usanifu ili mwisho wa siku nchi yetu kuanzia Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini yote tufanye kilimo cha umwagiliaji. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mpaka hivi sasa ninavyozungumza tayari kazi hii imekamilika na tuko katika hatua za kuwapata Wakandarasi kwa ajili ya kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika maeneo yote hayo mabonde yale makubwa, yaani kuanzia Bonde la Ziwa Viktoria, Malagarasi, Mto Manonga, Ifakara, Idete, Mto Songwe, Rufiji Basin Kwenda mpaka Mkoazi maeneo yote haya tutayagusa. Lengo letu ni kufanya kilimo cha umwagiliaji na mwisho wa siku tufikie malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Mto Ngono, kwenye hili la Mto Ngono nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ambaye amekuwa akilisimamia sana jambo hili, katika yale mabonde 22 ambayo tunayafanyia upembuzi yakinifu na usanifu, Mto Ngono pia upo. Kwa hiyo, ekari zile 11,000 zitakuwepo kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge suala la Mto Ngono tumelichukulia katika umakini mkubwa sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mwaka jana Oktoba, Bibi yangu Ndugu Juliana Leo Gaesha, aliitwa kituo cha Polisi na kupelekwa Mahakama Kamachumu, Hakimu alimueleza mlalamikaji kwamba Bibi huyu apandishwe pikipiki na mlalamikaji akalipa fedha, Bibi yangu na watu wawili wakafungwa mshikaki kwenye pikipiki wakaenda Muleba, kufungwa Muleba magereza. Sasa kwa majibu yako Waziri ni lini mamlaka yako Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Sheria na TAMISEMI, mtatengeneza Tume ya Kitaifa, yaani ngazi ya Taifa muende mpeleleze tukio hili la Juliana Gaesha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tukio hili lililotokea Muleba, kwa kweli hatuhitajiki kuunda Tume, badala yake wale ambao wako kule wanaosimamia utekelezaji wa sheria wazingatie sheria, labda kama jambo lingekuwa limepitiliza sana hiyo ipo haja ya kufanya hivyo. Lakini kwa kiwango hiki ninaamini wasaidizi wetu walioko ngazi hizo watazingatia na kuanza kutekeleza. Kama linaigusa Mahakama, wenzangu wa Mahakama wapo wamesikia litatekelezwa Mheshimiwa. Ahsante sana.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE : Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, gati la kuegesha meli katika Kisiwa cha Godzba baada ya maji kushuka ya Ziwa Victoria, kuegesha meli za Songoro Marine na hiyo Clarias imekuwa ni shida. Serikali mnaonaje haraka mtujengee gati lile liweze kuhimili kupokea meli zetu maji yanapopanda na kupwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza; visiwa vya Ikuza bandari ya Magarini, Mazinga, Bumbile Kerebe havijahusishwa kwenye mpango wa Serikali ulioutaja. Je, ni lini Serikali itaangalia gati za visiwa hivyo na kuweza kuzitekeleza kusudi Muleba nzima iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika gati hili la Godzba kuna changamoto ya maji kushuka na hivyo kusababisha gati hilo kutotumika ipasavyo na meli hizi. Kwa maana hiyo, Serikali inatoa maelekezo kwanza kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini kutuma timu ya wataalam ili kulirekebisha gati hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa hatua za awali kwa kuwa wenzetu wa MSCL wana-floating dock tatu (tishari), nataka moja ije eneo hili la Godzba ili lianze kufanyakazi wakati meli hii inafanya kazi eneo hili na tishari nyingine itaenda katika kisiwa cha Gana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anataka kujua ni lini tutapeleka huduma katika visiwa vya Kerebe Bumbile, Kyamkwikwi, Godzba na maeneo mengine. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa meli hii ya MV Clarias tayari tumeshakamilisha matengenezo yake jana na tunategemea ndani ya wiki hii, namuelekeza mkurugenzi wa TASAC atume timu yake ya wataalamu ili wakajiridhishe na hatimaye meli hii ianze kufanya kazi. Kwa maeneo ya visiwa ambavyo umevitamka Mheshimiwa Mbunge nako tutaanza kupeleka huduma kama ambayo inafanya sasa maeneo mengine. Ahsante.
MHE. CHARLES JOHN P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nisikitike kwa majibu ya Serikali. Serikali imegawa ambulance lakini sisi Wilaya ya Muleba ambayo 70% ni maji na kuna visiwa 38 hatuna kifaa sio dharura yaani ndiyo maisha yetu visiwa 38 vinahitaji vesal realiable vesal ya ku-move. Serikali hamuoni kwamba mchukue jitihada za Mheshimiwa Rais ku-copy ile vesal mliyopeleka Mafia na sisi mtununulie kama hiyo kusudi wananchi waweze kufika katika sehemu za huduma kwa sababu eneo hilo lina watu wengi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba tu nimuhakikishie Mheshimiwa Mwijage kwamba Serikali ya awamu ya Sita inatia kipaumbele cha hali ya juu sana katika maeneo ambayo hayafikiki kuhakikisha kwamba huduma za rufaa zinatekelezwa ipasavyo. Ndiyo maana sasa imeandaa mpango makakati wa kuainisha maeneo yote ambayo ni magumu kufikika yale ambayo yanahitaji boat ambulance ikiwemo Halmashauri ya Muleba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tayari tupo hatua nzuri na mwaka ujao wa Fedha 2024/2025 tunaanza kutenga fedha kwa ajili ya kupata hizo boat ambulance.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.