Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daniel Baran Sillo (35 total)

MHE. SILLO D. BARAN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa bado mgogoro huu unafurukuta katika vijiji nilivyovitaja, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufanya ziara ili wananchi wapate kutatua migogoro hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili…

SPIKA: Kwa nini Waheshimiwa mnamgombea Mheshimiwa Waziri kama mpira wa kona aje majimboni kwenu?

Endelea Mheshimiwa swali la pili.

MHE. SILLO D. BARAN: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 2019 ulitokea uharibifu wa mazao ya wananchi katika vijiji nilivyovitaja ambao ulisababishwa na wanyama hasa tembo, je, ni lini Serikali itawalipa kifuta jasho wananchi hawa ambao mashamba yao yameathirika?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Sillo juu ya kuongozana na mimi maana ni majukumu yangu ya kazi, hivyo hilo niko tayari baada ya Bunge lako hili Tukufu tutaenda naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza ambalo ameuliza juu ya uharibifu wa wanyama wakali; Serikali inawajali sana wananchi wake na inatambua kwamba kuna uharibifu wa wanyama wakali ambao wamekuwa wakiwasumbua wananchi hasa wale ambao wanakuwa wamepanda mazao yao na wanyama wakali hususan tembo huenda katika maeneo hayo na kuharibu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua hilo ilianzisha Mfuko ambao huwa tunalipa kifuta jasho au kifuta machozi. Kifuta machozi au kifuta jasho ni kwa ajili ya kuwapoza wale ambao wanakuwa wameathirika na changamoto hii ya wanyama wakali. Hivyo, hadi Machi, 2020, Serikali ilikuwa imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya kifuta machozi au kifuta jasho kwa wananchi hawa ambao wamekuwa wakiathirika na changamoto ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kuhakiki madai yote ambayo wananchi wameathirika na changamoto hii ya wanyama wakali na itaendelea kulipa kadri inavyopata taarifa.
MHE. SILLO D. BARAN Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pamoja na majibu hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika, je, ujenzi wa barabara hii unaweza ukaanza kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2021/2022? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pilli, kwa kuwa barabara hii inafanana na barabara ya Magugu kwenda Mbuyu wa Ujerumani kupitia Daraja la Magara ambalo limejengwa na Serikali kwa thamani ya shilingi bilioni 13 hadi Mbulu; je, Serikali ipo tayari kuanza ujenzi wa barabara hii pia ili kuchochea maendeleo katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sillo Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Dareda hadi Dongobesh yenye urefu wa kilometa 54 kwenye maeneo ya escarpment ambayo tulijua yana changamoto yameshajengwa kilometa 10. Pia tumekamilisha usanifu wa kina mwaka huu, kwa hiyo, tusubiri bajeti; siwezi nikasema sasa hivi lakini nadhani litajitokeza kwenye bajeti lakini kwa maana ya kukamilisha usanifu wa kina maana yake tuna mpango wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na hiyo tu ni hatua za kuelekea huko.

Mheshimiwa Spika, ameuliza barabara inayoanzia Mbuyu wa Mjerumani hadi Daraja la Magara. Barabara hii pia ipo kwenye mpango na itakamilika kufanyiwa usanifu wa kina Septemba mwaka huu. Kwa hiyo, tayari pia ipo kwenye mpango kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya upungufu wa watumishi iliyoko Wilaya ya Korogwe ni sawa sawa kabisa na iliyoko Jimbo la Babati Vijijini hasa Sekta za Afya na Elimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili la watumishi hawa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tuna upungufu wa watumishi lakini kama ambavyo nimetangulia kusema kwenye jibu la msingi, Serikali imeendelea kutenga ikama kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kuandaa na kuomba vibali vya ajira kila Mwaka wa Fedha ili kuendelea kuongeza idadi ya watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hivyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Baran kwamba katika Wilaya ya Babati pia tutahakikisha tunaipa kipaumbele katika ajira za Mwaka wa Fedha ujao ili angalau tuendelee kuboresha idadi ya watumishi katika halmashauri hiyo.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo, lakini naomba niulize swali moja tu dogo la nyongeza.

Je, Serikali ipo tayari kuongeza wataalam wa afya katika Kituo cha Afya cha Ufana ambacho kipo jirani na Bashnet ili wananchi wa Bashnet wapate huduma ya afya wakati wanasubiri kujengewa kituo cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kuongeza watumishi katika kituo cha afya katika ajira hizi za watumishi 2,726 zilizotangazwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo kwa Mheshimiwa Waziri.

Je, Serikali ina mpango gani wa kumailizia Kituo cha Afya cha Gidas ambacho kinahudumia si tu wananchi wa Kata ya Gidas ila pamoja na wananchi wa mipakani mwa Kondoa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati njema wiki iliyopita tulikuwa kwenye ziara jimboni kwake na tulipita katika maeneo haya ikiwepo katika Kituo cha Afya cha Gidas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie, kama tulivyokubaliana kwamba kituo kile ni cha kimkakati, tutakwenda kutafuta fedha ili kukikamilisha ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri yanayotia moyo hasa pale ambapo wananchi wamejitolea kufanya kazi kubwa na Serikali inapounga mkono. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; kwa kuwa kituo hiki kinahudumia siyo tu Kata ya Galapo, lakini Tarafa nzima ya Babati ikiwemo Kata ya Kashmamire, pamoja na vijiji vya Jirani vya Wilaya za Kondoa na Kiteto: Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kituo hiki kupatiwa gari? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili: Je, Waziri yupo tayari sasa kuelekeza kwamba kituo hiki kifanye kazi masaa 24 kuliko ilivyo sasa hivi ambapo kinafungwa saa 12.00 jioni? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kituo hiki kuwa na gari hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tutaweza kupata gari za kutosha, tutazingatia maombi yake ya kupeleka gari katika kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba hatuoni sasa kuna umuhimu wa kituo hicho kufanya kazi masaa 24; hili nimelichukua. Tutaangalia hali halisi ya kituo kilivyo kama kinaruhusu kuweza kutoa huduma kwa masaa 24, basi tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa magari yaliyonunuliwa ni 195 na halmashauri ziko 184 nchini; je, kati ya haya magari yaliyobaki moja litakwenda kwenye Kituo cha Afya cha Gidas?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mahitaji ya wahudumu wa afya katika kituo hicho ni 32 na waliopo sasa ni nane tu; je, Serikali iko tayari kuongeza wahudumu wa afya ili kuboresha huduma za afya kwenye kituo hicho? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba magari yatakayonunuliwa ni 195 lakini tuna halmashauri 184 na tutazama zile halmashauri au vituo ambavyo viko mbali zaidi maeneo ambayo ni hard to reach tutawapa kipaumbele kuwapa gari zaidi ya moja katika halmashauri hizo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hoja ya Kituo cha Afya cha Gidas amesema kwa muda mrefu, tutakwenda kuona uwezekano wa kuwatafutia gari ili tuweze kuondoa changamoto ya wananchi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, kuhusiana na watumishi ni kweli tunachangamoto ya upungufu wa watumishi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo ameona Serikali imeendelea kuajiri watumishi na kuwapeleka kwenye vituo vya afya, tutahakikisha tunaendelea hivyo kwa awamu na tutatoa kipaumbele cha afya hicho cha Gidas. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mbuyu wa Mjerumani kupitia Magala hadi Mbulu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbuyu wa Mjerumani kwenda Mbulu ni barabara ambayo ndiyo tumekamilisha usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ipo kwenye mpango, tulichokuwa tunafanya ni kukamilisha usanifu na tukishakamilisha Serikali itaendelea kutafuta fedha ili kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliahidi kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Galapo katika mwaka wa fedha 2022/2023. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili kazi hiyo iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Sillo kwamba mpango wa ukamilishaji wa vituo vya Polisi kwa kweli inategemea upatikanaji wa fedha. Ninafahamu wakati wa bajeti yetu iliyosomwa mwaka huu, Waziri aliainisha maeneo mbalimbali ambayo yatapelekewa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo. Ninamuomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, miongoni mwa maeneo ambayo yatapewa kipaumbele ni haya ambayo yana matukio mengi ya uhalifu ikiwemo eneo la Galapo ambalo limekuwa ni kituo kikubwa cha kibiashara na tutakipa pia kipaumbele. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itamalizia Kituo cha Polisi cha Galapo ambacho iliahidi kwamba itatekeleza katika mwaka huu wa fedha 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumeshazungumza juu ya jambo hili na Mheshimiwa Sillo, nimeahidi baada ya Bunge hili kutembelea eneo lile la Galapo kwa sababu ni eneo ambalo ni kubwa sana kibiashara linahitaji Kituo cha Polisi. Tumeingiza kwenye mpango wa kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma za usalama wa raia na mali zao.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali moja. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Babati, Galapo hadi Orkesumet kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijiji, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ni barabara muhimu ambayo tayari imeshakamilishwa kufanyiwa usanifu wa kina na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, mara Serikali itakapopata fedha, barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza: Kwa kuwa mahitaji ya wahudumu wa afya katika Kituo cha Afya Gidas ni 52 na waliopo sasa ni watano tu: Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wahudumu wa afya ili kuwasaidia wananchi hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa kituo cha afya kiko mbali na hospitali ya wilaya: Je, Serikali ipo tayari kupeleka gari la kubebea wagonjwa ili kuwasaidia wananchi wetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upungufu wa wahudumu wa afya, Serikali inatambua upungufu wa wahudumu wa afya katika maeneo mbalimbali ya vituo vyetu vya huduma na ndio maana wiki iliyopita, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi alitoa taarifa katika Bunge lako kwamba Serikali imeweka mpango wa kutoa vibali na kuanza kutoa ajira; na katika ajira hizo watumishi wa sekta ya afya watakuwemo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanya mkakati na mara watakapoajiriwa, tutahakikisha kituo hicho kinapata watumishi ili kuboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na gari la wagonjwa, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu ya msingi, magari ya wagonjwa 195 yatanunuliwa katika mwaka huu wa fedha na yatapelekwa kwenye Halmashauri zote ikiwepo Halmashauri ya Babati Vijijini. Kwa hiyo, kituo hicho pia kitapata gari la wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Manyara ambao eneo lilishatengwa eneo la Mwada?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu zinaendelea za kutwaa eneo ambalo uwanja huu utajengwa na baada ya taratibu hizo kukamilika uwanja huu utaanza kujengwa.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninaomba Mheshimiwa Naibu Waziri afanye mawasiliano na wataalam wake wa maji wanaohusika na eneo husika, kwa sababu taarifa anazosema nadhani haziko sahihi na ambazo ninazo. Amesema kazi zinazofanyika labda angesema kazi zitakazofanyika kwa sababu mradi huo kwa sasa umeishia Kata ya Magugu.

Mheshimiwa Spika, la pili; miradi yetu ya maji mingi inachelewa kwa kuwa na utaratibu wa manunuzi ambao huchukua muda mrefu sana.

Sasa Wizara ina mpango gani wa kuboresha kitengo hicho cha manunuzi ili mradi uweze kukamilika kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kuwasiliana na watendaji naomba nilipokee na nitalifanyia kazi kwa karibu sana kuhakikisha kazi zote zinafanyika kwa wakati kama ambavyo inapaswa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu uboreshwaji wa hatua za manunuzi, Kiwizara tunaendele kuhakikisha tunatumia taratibu ambazo hazitachelewesha miradi na pale itakapobidi basi ushauri tunapokea na tutafanyia kazi. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Jimbo la Babati Vijijini kwenye Kata za Gidas na Ufana na kuahidi kwamba, ataleta minara ya mawasiliano. Je, ni lini ahadi hii itatimizwa ili wananchi wapate mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa nimeshafika katika Jimbo la Babati Vijijini na katika Kata ambazo Mheshimiwa Sillo ameziongelea, tayari zimeingizwa kwenye mradi wa Tanzania kidijitali, tenda hiyo ilifunguliwa Tarehe 31 Januari, hivyo tunasubiri majibu ili tujue kwamba, ni Mkandarasi gani anapatikana kwa ajili ya vijiji hivyo. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, ni lini Serikali hii itapeleka vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Bashnet na Madunga katika Jimbo la Babati Vijijini ambavyo viko tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na Kituo hiki cha Afya cha Bashnet, lakini na vituo vingine vya afya ambavyo vimekamilika katika Jimbo la Babati Vijijini Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 69.95 katika mwaka huu wa fedha na tayari vifaa tiba vimeanza kupelekwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele pia katika kituo hiki cha afya ili kiweze kupata vifaa tiba hivyo, ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, Serikali itaanza lini ujenzi wa Barabara ya Dareda - Bashnet mpaka Dongobesh kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii iko kwenye mpango na naomba tu tusubiri bajeti kwamba barabara hii Dareda - Dongobesh Serikali ina mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, ninataka kujua, Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mizani katika Wilaya ya Babati - Kondoa hadi Dodoma.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii amekuwa akiifuatilia sana Mheshimiwa Mbunge, nataka nimhakikishie kwamba kama tunavyomwelekeza na kumweleza kwamba Serikali ina mpango wa kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kulingana na patikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza naipongeza Serikali kwa ujenzi wa barabara ya Dodoma – Kondoa hadi Babati. Lakini ni lini Serikali itajenga mizani katika barabara hii ili isiharibike ndani ya muda mfupi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ya Dodoma – Kondoa hadi Babati haina mizani, na ni kwa sababu wakati stadi inafanyika hapakuonekana kama kutakuwa na traffic kubwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi tunafanya mipango ya kutafuta eneo kujenga mizani ili kuilinda hii barabara ikiwa ni pamoja na barabara ya kutoka hapa kwenda Iringa ambapo napo hapakuwa na lami, tayari tumeshaanza kujenga mizani. Kwa hiyo, Serikali imeshaliona hilo na tuko mbioni kujenga mizani ili kuilinda hiyo barabara. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza.

Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo Desemba mwaka huu Vijiji vyote vya nchi hii ikiwepo Babati Vijijini vinapata umeme. Lakini kwa kasi hii ndogo ya kusuasua ya Wakandarasi je, mpango huu bado upo au umebadilika? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto hiyo niliyoieleza awali ya bei na upatikanaji wa vifaa vya umeme. Katika makubaliano mapya ambayo tutaingia na Wakandarasi wa REA kutakuwa na program mpya ya kazi ambayo itakuwa na maelekezo ya kuharakisha utekelezaji wa kazi hizi, kwa sababu pale ambapo mikataba itarekebishwa, itarekebishwa kwenye bei lakini tunaamini kwamba ratiba ya kazi itakuwa pale pale, bado nia yetu ni kukamilisha miradi hii kabla ya Desemba, 2022.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna changamoto kubwa sana ya mawasiliano katika Jimbo la Babati Vijijini hasa Tarafa za Bashnet na Goroa na pia Mheshimiwa Naibu Waziri alishafika. Je, ni lini Serilkali itaanza kujenga minara ili wananchi wetu waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Sillo kwa sababu nilifanya ziara katika jimbo lake na tulitembea wote na tulijionea hali halisi, lakini habari njema kwa ajili ya wananchi wa Babati ni kwamba kata ambazo amezitaja tayari zipo kwenye mpango wa utekelezaji wetu. Hivyo basi, wananchi wa Babati wasubiri tu hatua za manunuzi zikamilike. Hatua hizo zikishakamilika basi nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanatupa maeneo ambayo hayana migogoro kiasi kwamba tukiweka minara yetu isiingie kwenye migogoro ya ardhi. Ahsante sana.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara ya Dareda – Dongobesh – Usariva usanifu wa kina umeishafanyika na zabuni kutangazwa Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo Mbunge wa Babati Vijijini kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara imeishatangazwa na ipo kwenye hatua ya manunuzi kwa hiyo, sasa hivi kuna majadiliano yanayoendelea na mkandarasi ambazo ni taratibu za kawaida za manunuzi. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara hii mara tutakapokamilisha hayo majadiliano mkandarasi tukishakubaliana atakabidhiwa site ili aendelee na ujenzi, ahsante.
MHE. DANIEL S. BARAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Gallapo kinahudumia Tarafa nzima ya Babati ikiwemo Kata za Endakiso, Mamire, Qash na Gallapo. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba ya Mama na Mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nilifanya ziara Babati Vijijini, tulishirikiana sana na Mheshimiwa Mbunge tulifika Kituo cha Afya cha Gallapo, ni kweli kinahitaji muindombinu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeweka mpango wa kutafuta fedha kupeleka Gallapo ili kianze ujenzi wa majengo ya Mama na Mtoto na majengo ambayo yanapungua, ahsante sana.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili. Swali la kwanza; je, Serikali iko tayari sasa kuongeza fedha 2023/2024, walau kuanza kilometa 10 za barabara hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kilometa nane kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Dareda – Dongobesh imetangaza zabuni mwezi Machi, sasa ni lini kazi hii itaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara hii ya kutoka Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu tumeshaanza kuijenga kwa kiwango cha lami kwenye maeneo ya escarpment na tutaendelea. Tumeshajenga kilometa nne lakini pia tumetenga fedha ili kuendelea kujenga eneo hilo la muinuko mkali kwa kiwango cha lami wakati Serikali sasa inaendelea kutafuta fedha kuijenga barabara yote ya Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Barabara ya Dareda – Dongobesh, tulitangaza tenda wakandarasi wakakosa sifa. Tumetangaza tena na sasa hivi tupo kwenye evaluation. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa ahsante, zabuni ya ujenzi wa kilometa nane za awali kwa Barabara ya Dareda – Dongobesh imetangazwa zaidi ya mara mbili. Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo itaanza kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni kweli tulishatangaza lakini tumeitangaza tena nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba barabara hii kilomita zote zilizotangazwa kilomita 8 tutaijenga katika kipindi hiki shida ilikuwa tu baada ya kutangaza hatukumpata mkandarasi sahihi. Kwa hiyo, mpango upo na tayari tumeishaitangaza upya na tuko kwenye mazungumzo na mkandarasi ambaye ataijenga. Kwa hiyo, tutakapokuwa tumeikamilisha hayo mazungumzo barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa wako walimu wanaojitolea kwa muda mrefu katika Shule ya Sekondari ya Wilaya ya Babati: Je, katika ajira mpya, Serikali iko tayari kuwapa kipaumbele hao wanaojitolea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kati ya shule 38, kuna shule sita ambazo zina mwalimu mmoja mmoja wa kike wa Shule za Sekondari ya Taraget, Burunge, Nar, Kameri, Ndeku na Endamanang’; je, Serikali iko tayari kuongeza walimu wa kike katika shule hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la kwanza la Mheshimiwa Sillo la wale ambao wanajitolea; katika ajira hizi ambazo nimezitaja, Serikali imetoa 13,390, tutakwenda kwa kuangalia vigezo, kwa sababu ajira hutolewa kwa usawa.

Hao wanaojitolewa kama wameomba ajira hizi na wanakidhi vigezo vilivyowekwa katika tangazo la ajira, basi nao pia watapata, lakini hakutakuwa na upendeleo maalum ambao utatolewa kwa wale tu wanaojitolea kwa sababu wanajitolea, ili kutoa fursa sawa kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali la pili la upungufu wa walimu wa kike katika shule ambazo Mheshimiwa Sillo amezitaja, hili agizo lilishatolewa kwa Makatibu Tawala wote wa Mikoa Tanzania kuhakikisha wanafanya msawazo wa walimu katika mikoa yao. Sasa katika ajira mpya hizi zinazokuja, kuna walimu wa kike nao wataajiriwa, wakifika mikoani kule wapangiwe katika shule zenye upungufu wa walimu wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena hapa kuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara kuhakikisha anafanya msawazo katika shule ambazo amezitaja Mheshimiwa Sillo kupeleka walimu wa kike kutoka ndani ya Mkoa wake.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, wananchi wa Kata ya Bashnet tayari wametenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi; je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kituo hiki kidogo cha Polisi cha Kata ya Bashnet ni kituo cha ngazi ya Daraja C. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge kupitia juhudi alizozifanya kama tulivyofungua kituo kipya hivi karibuni, alifanya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, waanze ujenzi kwenye eneo lao la Bashnet then Wizara kupitia Jeshi la Polisi itakamilisha mtakapokuwa mmefikia stage ya umaliziaji hasa lenta na uwekaji wa samani, nashukuru.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa mahitaji ya Walimu wa shule za msingi katika Jimbo la Babati Vijijini ni 1,956 na waliopo ni 1,226 na hivyo kuwa na upungufu wa Walimu 730. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Walimu wanaopatikana katika shule za msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishasema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inaendelea kuweka kipaumbele cha kuajiri Walimu na hasa katika shule za msingi kuhakikisha inapeleka Walimu wa kutosha kwenye maeneo yenye upungufu ikiwemo kule Jimboni kwa Mheshimiwa Sillo. Katika hao 13,130 tutaangalia ni mgao kiasi gani ambao Mheshimiwa Sillo amepata kule katika Halmashauri yake na nitakaa naye kumpa hiyo orodha.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali iko tayari kutenga fedha katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ni lini Serikali itasaini mkataba na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kilomita nane za barabara ya lami ya Dareda Center kwenda Dareda Mission ikiwa sehemu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Dareda kwenda Dongobesh? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ndiyo inayounganisha Makao Makuu ya Mji wa Manyara, Babati na Wilaya mbili ya Kiteto na Simanjiro. Kwa hiyo, ni wazi kama tulivyosema kwenye mpango wetu kwamba tutaziunganisha hizo barabara kwa kiwango cha lami, kwa hiyo, naamini kwa mwaka wa fedha utakaokuja, hizi barabara zitaingia kwenye mpango na ndiyo maana sasa hivi tunakamilisha usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Dareda – Dongobesh ambayo tutaijenga kwa kuanza na kilomita nane, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu za manunuzi zimekamilika na tunategemea pengine kabla ya tarehe 22 kama taratibu zitakwenda kama tulivyopanga, mkandarasi awe ameonyeshwa site kuanza ujenzi wa hizo kilomita nane, ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Wananchi wa Babati Vijijini wanatumia sana zao la mbaazi kama zao lao la biashara: Ni nini mkakati wa Serikali wa kutafuta soko la zao hili la mbaazi kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi ya wananchi wa Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kutafuta soko la uhakika la mbaazi na hasa kwa kuishirikisha Serikali ya India, ikiwa ni mmoja kati ya wanunuzi wakubwa. Wiki moja iliyopita, tulimtuma Naibu Katibu Mkuu wetu wa Wizara ya Kilimo, kwenda India kwa ajili ya kufuatilia yale makubaliano ya awali yaliyokuwepo ya soko la mbaazi na majadiliano yanakwenda vizuri ili tuweze kuwahakikishia wakulima wetu masoko ya uhakika, hasa ya mbaazi ambapo India wamekuwa wanunuzi wakubwa.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Babati Vijijini wamekamilisha ujenzi wa zahanati za Guse, Hayamango na Yasanda, lakini zahanati hizo zimeshindwa kufunguliwa kwa sababu ya upungufu wa watumishi wa afya: Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuwapeleka watumishi ili zahanti hizo ziweze kufunguliwa na kuhudumia wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba kuna zahanati nyingi hazijafunguliwa kwa sababu ya kukosa watumishi, nasi kama Serikali tunalijua hilo na katika watumishi ambao tutawapeleka, tutawaagiza Wakurugenzi wawapangie katika zile zahanati ambazo zimekamilika ili ziweze kutoa huduma, ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa Mji wa Bashnet ambao ni Makao Makuu ya Tarafa hauna kituo cha polisi na badala yake polisi hutoka Mji wa Babati ambao ni kilometa 60 na kurudi jioni.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Mji wa Bashnet ambao ni Makao Makuu ya Tarafa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua baadhi ya maeneo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ana uhaba wa vituo umbali wa kilometa 60 ni umbali mkubwa na haukubaliki. Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaweka kipaumbele kwenye eneo lake ili kuweza kuanza ujenzi wa Kituo hicho cha Polisi, nashukuru.

MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa barabara ya Dareda - Dongobesh usanifu wa kina umeshakamilika; je, ni lini zabuni zitatangazwa ili ujenzi huu uanze mara moja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara ya Dareda - Dongobesh imeshakamilika kwa kufanyiwa usanifu wa kina. Kwa hiyo, kwa sasa Serikali ipo kwenye hatua za kutafuta fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa migogoro kati ya Hifadhi ya Tarangire na vijiji vya Gijedangu, Hayamango, Vilimavitatu na Salama ni vya muda mrefu.

Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuonesha kwamba migogoro hii inafika mwisho ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu ya nyongeza kwamba, maeneo yote ambayo yamezungukwa na hifadhi, Serikali itahakikisha wananchi wanafaidika na uhifadhi. Tunatambua kwamba hawa wananchi kwa asilimia kubwa wanatusaidia kusimamia maeneo haya. Sisi tuko huku makao makuu na pamoja na kuwa tuna wataumishi wetu walioko kwenye maeneo ya hifadhi, lakini askari peke yake hawawezi kulinda haya maeneo bila kushikirisha wananchi ambao ndiyo hasa wenye uchungu wa haya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba CSR ni moja ya priority ya Wizara ama Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanajisikia kwamba ni sehemu ya hifadhi. Hivyo, tutahakikisha kwamba wananchi wa jimbo lake wanaona umuhimu wa uhifadhi ili waendelee kutusaidia kusimamia maeneo haya yanayozunguka hifadhi ya Tarangire. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ya kujenga barabara ya Mbuyu wa Mjerumani kupitia Magara hadi Mbulu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ilitolewa wakati anazindua barabara ya Magara na tayari tumeshaanza kufanya usanifu kama alivyoagiza ikiwa ni maandalizi kuijenga barabara hiyo ya kutoka Mbuyu wa Mjerumani - Magara hadi Mbulu kwa kiwango cha lami.