Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Daniel Baran Sillo (16 total)

MHE. SILLO D. BARAN Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya mipaka kati ya Hifadhi ya Tarangire na Vijiji vya Gijedabung, Ayamango, Gedamar na Mwada katika Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilihakiki mpaka wa Hifadhi ya Taifa Tarangire mwaka 2004 kwa kutumia Tangazo la Serikali Na. 160 la tarehe 19 Juni, 1970 ambapo alama za mipaka ziliwekwa ardhini. Kazi hiyo ilifanywa na wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Spika, uhakiki huo ulibainisha kuwa: (i) hifadhi ilikuwa imechukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Mwikantsi (Hekta 1,014) na Sangaiwe, Kata ya Mwada (Hekta 536), hivyo maeneo haya yalirejeshwa kwa wananchi. (ii) wananchi pia, walichukua maeneo ya hifadhi katika Vijiji vya Ayamango (Hekta 2,986.3), Gedamar ( Hekta 2,185.1), Gijedabung (Hekta 1,328.2), Quash (Hekta 1,587.9) na Orng’andida (Hekta 930.6) ambavyo vimerejeshwa.

Mheshimiwa Spika, katika Vijiji vya Quash na Orng’ndida maeneo yaliyoangukia ndani ya mpaka wa hifadhi hayakuwa na watu, hivyo ilikuwa rahisi kuyarejesha hifadhini. Upande wa maeneo ya Vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gijedabung uthamini wa mali za wananchi ambao walikuwa ndani ya mpaka wa hifadhi ulifanyika. Jumla ya kiasi cha shilingi za Kitanzania 175,050,924 zililipwa kwa wananchi hao kama fidia ya mali, posho ya usumbufu, posho ya makazi na posho ya usafiri kwa wote waliotakiwa kuhama. Malipo hayo ya fidia yalifanyika kama ilivyokuwa imepangwa na wananchi waliondoka ndani ya hifadhi.
MHE. SILLO D. BARAN aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet – Dongobesh kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Dareda – Bashnet hadi Dongobesh yenye urefu wa kilometa 54 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania- TANROADS ambapo kilometa 10 zimejengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 44 ni za changarawe. Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet hadi Dongobeshi kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilifanywa na Mhandisi Mshauri Luptan Consults Ltd kwa kushirikiana na Mhandisi Consultancy Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 398. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 513.594 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Bashnet baada ya Serikali ya Kijiji kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mpango wa kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuendelea na ujenzi wa vituo vya afya nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Babati. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Babati kupitia mapato yake ya ndani imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Bashnet katika eneo lenye ukubwa wa ekari 12.6 lililotengwa na Serikali ya Kijiji.

Mhjeshimiwa Spika, Ujenzi huo utaanza katika mwaka wa fedha 2021/2022 kama ilivyopangwa.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza upembuzi yakinifu na ujenzi wa miundombinu ya maji katika Ziwa Madunga ili kutatua tatizo sugu la maji katika Kata ambazo hazina maji Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa Babati Vijijini ni asilimia 74. Kwa lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Serikali inaendelea na utafiti wa ubora na uwingi wa maji katika chanzo cha Ziwa Madunga. Utafiti huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2021 na usanifu wa miundombinu ya maji utakamilika katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. REGINA N. QWARAY K.n.y. MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu na Vjiji vya Olacity na Minjingu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro kati ya Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu na Vijiji vya Olacity na Minjingu ulitokana na vijiji kutokutambua mipaka halisi kati ya vijiji hivyo na kiwanda, hivyo kusababisha wananchi kutoka katika vijiji hivyo kuingia na kufanya maendeleo katika eneo la kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwezi Januari, 2021 Serikali ilifanya uhakiki wa mpaka wa Kiwanda cha Minjingu na vijiji vinavyozunguka kiwanda hicho na kubaini kuwa kuna jumla ya kaya 83 ndani ya eneo la kiwanda ambapo kaya kutoka Vijiji vya Olacity na Minjingu ni miongoni mwa vijiji hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kaya hizo, kaya 40 za wahanga wa mafuriko ambazo ziliombewa na Kijiji cha Minjingu makazi ya muda ndani ya eneo la kiwanda, lakini baada ya muda wa makubaliano kuisha, kaya hizo zimegoma kuondoka katika eneo la kiwanda, hivyo kusababisha kuwepo kwa mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Manyara kukutana na pande zote mbili zinazohusika ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo ifikapo Desemba, 2021.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasaidia ujenzi wa Kituo cha Polisi Galapo Tarafa ya Babati ambacho kinajengwa kwa nguvu za Wananchi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake na nimwahidi kuwa sitamwangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mhesimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na kuthamini michango na jitihada zinazofanywa na wananchi, Wabunge na Viongozi wengine katika kuchangia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao. Kituo cha Polisi cha Galapo kimejengwa kwa nguvu za wananchi na kwa sasa kimeshapauliwa na kazi iliyobaki ni kuweka milango, madirisha, kupiga plasta, kuweka sakafu pamoja na kupaka rangi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapongeza sana wananchi wa Galapo pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zao zilizowezesha ujenzi huo. Kwa njia ya kuunga mkono jitihada hizo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itatumia fedha kutoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo katika mwaka wa fedha 2022/2023 ili kukamilisha ujenzi huo.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya Gidas?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji mkubwa uliopo wa magari ya kubebea wagonjwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 imefanya manunuzi ya magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Babati.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasaidia ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Gidas?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilipeleka shilingi bilioni 1.04 kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri, Kituo cha Afya, Nyumba ya Mtumishi na ukamilishaji wa zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uhitaji wa wodi ya mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Gidas.

Mheshimiwa Naibu Spika, kituo hiki kimeombewa fedha Hazina na ujenzi utaanza mara fedha zitakapotolewa.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza Mradi wa Maji wa Darakuta hadi Minjingu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Darakuta - Magugu ndio unaoendelezwa mpaka Minjingu ambapo utagharimu shilingi bilioni 5.672 na kazi zinazoendelea kufanyika ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu kwenye umbali wa kilometa 46, ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji umbali wa kilometa 66, ujenzi wa tanki la lita 250,000 na ufungaji wa pampu. Utekelezaji wa mradi huu umeanza mwezi Septemba, 2022 na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo wananchi wapatao 23,000 wa Kata za Mwada na Nkati watanufaika.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu, yenye urefu wa kilomita 50 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, lini Serikali itapunguza tatizo la upungufu wa walimu katika Shule za Sekondari Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza kupunguza tatizo la upungufu wa Walimu u katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, walimu 50 walipelekwa katika shule zilizopo Babati Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetangaza nafasi 13,390 za ajira kwa walimu ambapo baadhi ya walimu hao watapangiwa katika Shule zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri walimu na kuwapeleka katika shule zote nchini hususan katika maeneo yenye uhitaji kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Babati Galapo hadi Orkesumeti kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS, imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami mwezi Februari, 2023. Kwa sasa Serikali inaendelea na zoezi la kufanya uthamini wa mali za wananchi watakaoathirika na mradi lililoanza tarehe 5 Juni, 2023 na inatarajiwa kukamilika tarehe 5 Julai, 2023. Baada ya zoezi la uthamini kukamilika na waathirika kulipwa fidia, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kupandisha hadhi Mji wa Magugu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uanzishaji wa Mamlaka za Miji Midogo hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Mwongozo wa Uanzishaji wa Maeneo ya Utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 ambapo umeanishwa utaratibu na vigezo vinavyopaswa kufuatwa.

Mheshimiwa Spika, kusudio la kupandisha hadhi Mji wa Magugu lipo katika hatua za upangaji wa Mji ikiwemo uandaaji wa mpango wa jumla na mpango kina ambapo ikikamilika itatangazwa kupitia gazeti la Serikali.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa katika Kata za Qameyu, Madunga na Kiru Babati Vijijini?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Sillo Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Qameyu ina jumla ya vijiji vinne ambavyo ni Endaw, Qameyu, Gawal na Merri. Kati ya vijiji hivyo, vijiji vitatu vya Endaw, Qameyu na Gawal tayari vimepatiwa umeme. Kijiji kimoja cha Merri ndio hakijapata umeme na kipo kwenye mradi wa REA III Mzunguko wa Pili ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya kuchimba mashimo na kusimika nguzo katika kijiji hicho. Kazi za mradi katika Kijiji hicho cha Merri zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2022.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Madunga ina vijiji vitatu ambavyo ni Madunga, Utwari na Gidng’war. Vijiji vyote vitatu tayari vimeshafikiwa na huduma ya umeme. Kata ya Kiru ina jumla ya vijiji sita ambapo kijiji kimoja cha Kiru Six tayari kimeshapata huduma ya umeme. Vijiji vyote vitano visivyokuwa na umeme vya Kiru Dick, Kimara, Kokomay, Kiru Ndogo na Erri vinapatiwa umeme katika mradi wa REA III Mzunguko wa Pili unaoendelea. Mkandarasi anaendelea na kazi za kuchimba mashimo na kusimika nguzo katika vijiji hivyo. Kazi za mradi zinatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2022.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Vilima Vitatu, Mwada na Ngolee dhidi ya Hifadhi ya Tarangire?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Sillo Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto za migogoro katika Hifadhi ya Taifa Tarangire na baadhi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tutatuma wataalam kwenda kufafanua au kutafsiri mipaka ili wananchi wajue maeneo ya vijiji na kuheshimu mipaka ya hifadhi.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, lini Serikali itatekeleza mradi wa maji wa Darakuta – Magugu - Mwada hadi Minjingu – Babati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji Darakuta-Magugu ndiyo unaoendelezwa kwa awamu ya pili mpaka Minjingu ambapo utagharimu shilingi bilioni 5.672 na kazi zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu umbali wa Kilometa 46, ujenzi wa tenki la lita 250,000 na ufungaji wa pampu za kusukuma maji. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Juni, 2022 chini ya Mzabuni Plasco Limited na kazi hiyo ilitarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 3 Julai, 2023, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA) ilivunja Mkataba na Plasco Limited baada ya kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati. Kwa sasa, Serikali imeanza ununuzi wa mabomba kupita mfumo mpya wa Ununuzi wa NEST, na ifikapo mwezi Desemba 2023, Mzabuni wa mabomba atakuwa ameshapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi sita na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2024 na utanufaisha wananchi zaidi ya 23,000 wa Kata za Mwada na Nkaiti.