Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Innocent Sebba Bilakwate (72 total)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri lakini sijaridhika na majibu yake. Niliuliza ni lini masoko haya yatafufuliwa kwa sababu haya masoko ni muhimu kwa ajili ya wananchi wa Kyerwa na Waziri mwenyewe anajua wananchi wa Kyerwa wanapata shida hawana mahali pa kupeleka mazao yao. Naomba anieleze ni lini masoko haya yatafufuliwa yaanze kujengwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba Naibu Waziri awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa na Watanzania ambao wananufaika na masoko haya, je, Serikali imetenga pesa kwenye Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya masoko haya kukamilika?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Innocent Bilakwate ameuliza nijibu ni lini? Nimemweleza, DASIP I ilikoma, nimewasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwamba Mpango wa DASIP II haujaanza, utakapoanza tuwaweke watu wa Karagwe na Kyerwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina maslahi na sehemu hizi, napenda niseme ukweli, msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. Katika bajeti sijaweka lolote kwa ajili ya masoko haya ya Nkwenda na Murongo, lakini kwa ajili ya Nkwenda na Murongo tumeandaa utaratibu ambapo wakulima wa mazao wa Karagwe, hasa maharage tutawaunganisha moja kwa moja na wanunuzi wa Oman na Innocent Bashungwa nimemteua aratibu shughuli hiyo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati yupo kwenye kampeni aliahidi kuondoa tozo mbalimbali ambazo zinamdidimiza mkulima wa kahawa. Mpaka sasa Serikali bado haijaondoa hizo tozo. Je, Serikali ipo tayari kuwaruhusu wananchi wale wanaolima kahawa waweze kuuza kahawa sehemu nyingine ambapo watapata bei nzuri?
shimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi Watanzania kwamba huu msururu wa kodi utatafutiwa utaratibu wa kuziondoa zile ambazo hazistahili kutozwa au zenye kuleta kero kwa wananchi. Pamoja na nia hiyo nzuri ya Mheshimiwa Rais bado mazao haya tunayahitaji hapa nchini. Serikali hii imeweka kipaumbele cha kuwa nchi ya viwanda na hivi viwanda vitahitaji malighafi ipatikane hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, halitakuwa jambo la busara leo tukisema kwa sababu tuna tatizo hili la kodi ndogo ndogo zenye kero, basi tuachie malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu ianze kuuzwa nje. Utaratibu tunaoufanya ni kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kwamba bei zinakuwa nzuri na masoko yanakuwa mazuri ili kutowapa shida wananchi wakati wa kuuza mazao yao.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hizi pesa ni za wananchi ambao ni maskini na zimekaa muda mrefu bila kupata hiyo mikopo. Je, Serikali iko tayari kurejesha hizo pesa au kuongeza riba kwa sababu hizi pesa zimekaa muda mrefu na hawa wananchi hawajapata jibu na hili tatizo limekuwepo Karagwe pamoja na Kyerwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, dhana nzima ya kwanza kabisa ya makusudio ilikuwa ni kuwafanya wakulima hawa kuingia katika Hifadhi ya Jamii lakini mkulima aliingia katika mfumo huu baada ya kuchangia kipindi cha miezi sita mfululizo alikuwa anapata sifa ya kuweza kukopesheka kupitia SACCOS katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii tu kumwomba Mheshimiwa Mbunge kama bado kuna matatizo haya katika maeneo yao na kwamba wako wakulima ambao walikwisha kutoa fedha hizi wametimiza masharti na hawajapata mikopo mpaka leo, basi wawasiliane na ofisi yetu ili tuweze kuwasaidia katika upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya wakulima hawa. Vilevile nimtoe hofu tu ya kwamba fedha ile ambayo ilikuwa inachangiwa ni fedha ambayo ilikuwa ni ya mkulima mwenyewe kujiwekea kinga ya kijamii na ambayo ingemsaidia katika mafao tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama bado wana mawazo tofauti, Ofisi yetu iko wazi kwa ajili ya mashauriano na kuweza kuwasaidia katika kutatua changamoto hii ambayo inawakabili wananchi hawa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza sijaridhika na majibu ambayo amenipa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu kusema hii barabara inapitika kila wakati si kweli! Barabara hii mwaka wa jana mzima ilikuwa ni barabara mbovu imejaa mashimo, magari yote yanayopita barabara ile yanaharibika sana. Kwa hiyo, kuna taarifa ambazo wamekuwa wakiletewa ambazo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza; je, yuko tayari yeye mwenyewe binafsi kwenda kuitembelea barabara ile na kuiona ili aone umuhimu wake kwa sababu taarifa ambazo wamekuwa wanaletewa sio za kweli?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Rais akiwa pale Nkwenda kwenye kampeni aliiona barabara ile ikiwa na umuhimu kwa kuwa barabara hii inapita katikati ya Wilaya. Aliahidi kutupa kilometa 20 akiingia tu madarakani. Hizo kilometa 20 zinaanza kujengwa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri kwamba miongoni mwa Wabunge ambao wanakuja ofisini kila wakati kufuatilia ni pamoja na Mheshimiwa Bilakwate. Mheshimiwa Bilakwate ameifuatilia barabara hii na tumekuwa tukijaribu kuangalia katika hizi barabara mbili zote zinaanzia karibu sehemu moja kuishia karibu sehemu moja. Suala ni ipi kati ya hizi mbili ni muhimu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kilichopita kama ambavyo tumeongea ofisini, ni kwamba uongozi wa Mkoa pamoja na Mbunge aliyepita waliona kwamba hii barabara ya kupitia Kigarama ndiyo ipewe umuhimu wa kwanza na hii ya kupitia Omurushaka nayo wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa kule aliipa kipaumbele. Kwa hiyo, barabara zote mbili sisi kama Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tumezichukua kwa umuhimu wake. Tutaanza na hii ambayo tumeshaanza kufanya kazi, tukiimaliza hii tutakuja kukamilisha hii nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tunasubiri kuanza hii ya pili ambayo ndiyo anayoifuatilia kwa umakini sana Mheshimiwa, tunamwomba sana akubali kwamba ile kazi tunayoifanya kwanza ya kuimarisha ule mlima maana tatizo kubwa liko pale mlimani hasa. Ombi lake la kwanza nalikubali, nitakuwepo naye huko, tukaongee na wananchi kuthibitisha ahadi ya kiongozi wetu mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo afahamu mazingira tuliyonayo kutokana na hizi barabara mbili ambazo zote zinaonekana zina kipaumbele lakini viongozi wa Mkoa na Mbunge aliyepita inaonekana hiyo nyingine ndiyo waliitanguliza zaidi. Sasa ni suala la kutafuta namna gani zote mbili twende nazo kwa sababu zote zina umuhimu wa pekee na zinatoa huduma kubwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mheshimiwa Waziri naomba nikuulize swali; barabara ya Mgakolongo kwenda Kigarama mpaka Mlongo upembuzi ulishafanyika muda mrefu na wananchi wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwasababu walishawekewa “X”. Barabara hii ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Bilakwate kwa namna anavyofuatilia ujenzi wa barabara zote mbili zinazopita katika Jimbo lake; moja upande wa Kaskazini na nyingine Kusini n nikubaliane na yeye kwamba hii ya Kusini inapita katika maeneo makubwa, ingawa hapa hajayasema lakini ameyaongea katika Ofisi yangu. Naomba nimhakikishie kwamba fedha zimetengwa kwenye mwaka huu wa fedha wa mwaka 2016/2017; nimuhakikishie tutajenga kabla ya tarehe 30 Juni, 2017.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la maji katika Jimbo la Kyerwa ni kubwa sana na wananchi wake hawapati maji, hata asilimia 20 haifiki: Je, Serikali inawaahidi wananchi wa Jimbo la Kyerwa kama alivyojibu, “upembuzi yakinifu unaoendelea utakapokamilika mwaka 2017/2018;” Serikali inaahidi kutenga pesa ya kutosha kwa ajili ya kukamilisha mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ili miradi hii iweze kusimamiwa vizuri, ni vizuri tukawa na wataalam. Wilaya yangu ya Kyerwa hatuna wataalam wa kutosha, lakini wataalam wenyewe hao waliopo hawana vitendea kazi kama gari na vifaa vingine. Je, Serikali ipo tayari kutuletea wataalam wa kutosha na vitendea kazi ili kazi isimamiwe vizuri?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza alitaka kujua kama katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tungeweza kuweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu ambao unaendelea kufanyiwa usanifu. Namwahidi kwamba kazi hiyo tutaifanya ili wananchi wetu kule waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la pili, kwamba Wilaya yake ina wataalam wachache; ni kweli wilaya nyingi hazina Wahandisi wala vifaa. Katika Program ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili, tumeweka bajeti kwa ajili ya kununua magari na vifaa muhimu, lakini pia tumeomba vibali kwa ajili ya kuajiri Wahandisi wa kutosha ili tuweze kuwapeleka kwenye wilaya mbalimbali.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lilivyo swali la msingi, kwa zao la kahawa na migomba kuna ugonjwa uitwao mnyauko kwa jina lingine unaitwa ugonjwa wa manjano. Ugonjwa huu umeshambulia migomba pamoja na kahawa. Je, Serikali imefanya utafiti upi ili kulipatia ufumbuzi zao hili lisije likapotea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kati ya magonjwa ambayo yameleta changamoto katika zao la migomba na kahawa ni ugonjwa wa mnyauko na kwa kipindi fulani umeleta matatizo makubwa sana katika Mkoa wa Kagera. Serikali ilichukua hatua mahsusi za kutafuta namna ya kuzuia ugonjwa huo na tayari kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kampeni kubwa iliyofanyika kuudhibiti, Serikali ilishaudhibiti na sasa hali siyo mbaya sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya katika utendaji wao wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Lwakajunju, imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana zaidi ya miaka 15. Kwa maana hiyo tumewaahidi sana akina mama wa Karagwe na wananchi kuwatua ndoo kichwani kwa muda mrefu sana. Kama unavyojua akina mama ule muda ambao wanautumia kwenda kuchota maji umbali mrefu ndio muda huo huo ungeutumia kufanya kazi za maendeleo. Sasa swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri naomba unipe comfort, je,huu mradi wa Lwakajunju utatekelezwa lini? Ni lini wananchi wa Karagwe watapata hii huduma ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za kibajeti za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, je, Wizara ipo tayari kushirikianan na Halmashauri kuhakikisha fedha ambapo tunahitaji kwa ajili ya kuchimba mabwawa katika Kata za Kanoni, Igulwa Ihanda, Chonyonyo na Nyakahanga zinapatikana ili wananchi wapate huduma ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusiana na Mradi wa Lwakajunju, ameomba apate confort na wananchi wake pia. Comfort ya kwanza ni kwamba mradi huu umetengewa dola milioni 30 kutokana na mkopo wa India, ni mkopo wenye uhakika na sasa hivi tupo kwenye taratibu za kukamilisha usanifu ili tutangaze tender. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba mradi huu unatekelezwa kwasababu tayari una fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili linalohusiana na ushirikiano na Halmashauri, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba tutaendelea kushiriakana na Halmashauri zote kuhakikisha kwamba miradi ya maji inatekelezwa, mabwawa, mserereko, visima na mingine ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Kuhusu suala la fedha upungufu wa fedha tutaenda nalo sabamba, lakini suala la msingi ni kuhakikishe kwamba wananchi wanapata maji.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kweli nasikitika sana kuona majibu ambayo ametoa Mheshimiwa Waziri. Hii ni mara yangu ya pili namwuliza hili swali. Mara ya kwanza alinijibu hapahapa Bungeni, akasema kabla ya mwezi wa Sita barabara hii itakuwa imeanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, anapotujibu siyo kuwajibu Wabunge kuwafurahisha, haya ni majibu ambayo tunakuja kuuliza kwa ajili ya wananchi wetu. Naomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu ambayo ni ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; ni lini barabara hii ujenzi utaanza? Kwa sababu hii barabara ni ya muda mrefu tangu kipindi cha Mheshimiwa Rais Mkapa amestaafu; amekuja Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, sasa anakuja Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018, je, imetengwa pesa kwa ajili ya ujenzi huu kuanza na wananchi wapewe fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie, tunapojibu hapa kwanza tunaonesha dhamira lakini pili, tunaonesha mipango ambayo ipo mbioni. Hatuwezi kuanza ujenzi wa barabara hii kabla ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika. Hakuna aina hiyo ya ujenzi ya barabara kuu na muhimu kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge atupe fursa tukamilishe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa mwaka huu tunakamilisha kazi hizo mbili. Kwa hiyo, hatujatenga fedha za kuweza kujenga, tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi hizo mbili. Nimhakikishie kwamba mara baada ya kazi hizo mbili kukamilika, ujenzi utaanza, Serikali hii ya Awamu ya Tano inachosema inakusudia kukitekeleza na huwa inakitekeleza.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti ya mwaka huu hakutupatia pesa kwa ajili ya mradi mkubwa ambao uko kwenye usanifu. Naomba awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa, mradi huu utakapokuwa umekamilika kwa ajili ya usanifu.
Je, yuko tayari kuhakikisha anawapatia wananchi wa Jimbo la Kyerwa maji safi na salama kwa sababu maji ni tatizo Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Mheshimiwa Bilakwate ilipata shilingi milioni 200 na fedha hizo tayari zimeshatumika kuboresha chanzo cha maji kwenye kijiji kimoja eneo la mjini na tayari maji yanapatikana. Pia, kupitia vyanzo vingine vya Wizara yetu ya Maji na Umwagiliaji, tayari tumesaini mkataba wa usanifu ambao ukikamilika, umelenga kuvipatia vijiji zaidi 57 maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kesho tunawasilisha bajeti kwenye Bunge hili na katika bajeti hiyo tayari utaona wewe mwenyewe ni nini tumetenga ambacho kitahakikisha kwamba baada ya kukamilisha mradi wa usanifu, basi ujenzi utaanza bila wasiwasi wa aina yoyote.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa Redio ya Taifa haisikiki katika Wilaya ya Kyerwa na wananchi hao wanapofungua redio wanapata Redio ya Rwanda na Uganda kitu ambacho kimewafanya wananchi hawa kuonekana kama wametengwa kwa sababu hawawezi kupata taarifa ambazo ni muhimu zinazohusu Taifa lao.
Je Serikali haioni kuwa wananchi hawa wamekosa haki yao ya msingi ya kupata habari za Serikali hasa hasa kutoka kwa viongozi wao kama Mheshimiwa Rais anapokuwa anaongea na viongozi wengine? Hata mimi Mheshimiwa Mbunge ninapokuwa Bungeni nawawakilisha, hawa wananchi hawapati taarifa yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za dharura ili wananchi hawa waweze kupata taarifa ya Redio ya Taifa kwa sababu wanakosa hii haki ya msingi? Laini hata Televisheni ya Taifa haisikiki wala haionekani vizuri. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Innocent kwa maswali yake mawili mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba unipe ridhaa ya kuelezea suala hili kwa kirefu kidogo kwa sababu tuna Wilaya karibu 84 ambazo hazina usikivu wa redio katika nchi hii na suala hili limesababisha Wabunge wengi mara kwa mara kuuliza maswali yanayohusiana na usikivu wa redio yao ya Taifa. Kwa hiyo, naomba nitoe ufafanuzi kidogo ili kusudi tuweze kusaidiana kwa pamoja na kuhakikisha kwamba tatizo hili linapata ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kwanza ametaka kujua kwamba Serikali haioni kwamba wananchi wanakosa haki yao ya msingi ya kusikiliza redio yao ya Taifa. Nitoe tu maelezo kwa kifupi kwamba kuna matatizo ambayo yanasababisha au tuseme kuna factors ambazo zinasababisha kuathiri usikivu wa redio katika maeneo mbali mbali. Kwanza, ukirudi nyuma tulikuwa tunatumia mitambo ya medium wave ambayo ilikuwa inaenea katika nchi nzima lakini kutokana na uchakavu wa mitambo hii na gharama kubwa ya kuinunua au kuikarabati imebidi sasa tuweke mitambo ya FM katika kila mkoa. Kwa hiyo, kila mkoa una mtambo wa FM.
Mheshimiwa Spika, sasa masuala ambayo yanaathiri usikivu kwanza ni capacity ya ule mtambo wenyewe lakini pia uwepo wa milima katika maeneo husika kwa mfano kama eneo la Mheshimiwa Innocent kuna milima mirefu ambayo mitambo hii inashindwa kuufikia. Suala lingine ambalo linaathiri usikivu ni ule uharibifu wa baadhi ya vifaa kama power amplifier ambao unatokana na matatizo mbalimbali kama vile radi au kukatika kwa umeme. Katika eneo la Mheshimiwa Innocent, kule Bukoba upo mtambo ambao kuna kifaa kimeharibika – MOSFET imeharibika na imekufa kabisa, kwa hiyo, usikivu umeathirika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, hatua za haraka ambazo tumeamua kufanya, kwanza nimeshatoa maagizo ili kusudi wataalam waende katika maeneo yake, katika Wilaya ya Kyerwa ili kuweza kuona jinsi gani ya kutatua tatizo hili kwa sababu kwanza uwezekano upo wa kuweka booster, lakini pia waone kama wanaweza wakanunua kifaa kile ambacho kimeharibika.
Vilevile kuna utaratibu ambao sasa hivi TBC inafanya kuubadilisha mfumo wa satellite uplink ambayo iko Mikocheni, tunaamini kabisa kwamba hii satellite uplink ikirekebishwa ikawa ya kisasa zaidi tutaboresha usikivu kwa asilimia takribani 15 hivi.
Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao maeneo yao hayana usikivu, kufikia mwisho wa mwaka huu tunaamini kabisa hii satellite uplink inaweza ikawa imerekebishwa, kwa hiyo, usikivu utakapokuwa umeboreka katika maeneo yao watupe taarifa. Vilevile, kutokana na uharibifu wa vifaa katika vile vituo vyenyewe, yale maeneo ambayo yana usikivu wakati wowote watakapoona usikivu umesita katika maeneo yale watupe taarifa mapema ili kusudi wataalam wetu waweze kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tunafanya kwa sasa hivi ni huu utaratibu wa kuweka mitambo ya FM yaani kuongeza transmitter katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, nimetoa maagizo tayari kwamba wataalam wapite katika maeneo ya mipakani waone ni wapi panapostahili kuwekwa boosters lakini ni wapi pia ambao panastahili kuwekwa transmitters mpya. Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu miradi hii ni ya muda mrefu na miundombinu yake inazidi kuharibika kama vile vifaa ambayo viko pale kuna kama nondo na vifaa vingine vinazidi kuharibika, kwa sababu Serikali imeshatenga pesa kwenye bajeti ya 2017/2018, kwa nini Serikali isichukue hatua za dharura kupeleka pesa hii ili iweze kukamilisha miradi hii kwa sababu ya umuhimu wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale kwenye miradi ile kuna walinzi ambao walikuwa wamewekwa pale, walinzi hao wametelekezwa muda mrefu na imefikia wakati hao walinzi wameondoka, pale hakuna walinzi. Serikali haioni pasipokuwa na walinzi inaweza ikasababisha vifaa vingine kuibiwa na kuharibu miundombinu ya mahali pale?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amezungumza kwamba miradi hii ni ya muda mrefu, lakini ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, nimuahidi tu kwamba nitafuatilia kuona kwamba kama tunaweza tukapata fedha hizo zilizotengwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na walinzi, niiombe Halmashauri ya Kyerwa kuhakikisha kwamba hata kwa kutumia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ni vema kuendelea kulinda miundombinu hii ambayo tayari ipo wakati tukiendelea kupata fedha kwa ajli ya kukamilisha miradi hiyo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kama lilivyo swali la msingi, kwenye Jimbo langu la Kyerwa, wananchi wameanzisha vituo ambavyo wameshaanza ujenzi, wamefika kwenye kumalizia boma. Kwa mfano, kama Kata yangu ya Kimuri, kuna wananchi ambao wamejenga boma limefikia kwenye lenta na wameweza kujenga maboma zaidi ya kumi. Maboma haya yamekaa karibu miaka saba. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha maboma haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nikupe taarifa, Mheshimiwa Bilakwate anapoishi kwake pale wakati mwingine ninapofika pale hata mtandao wa simu anapata nchi ya Rwanda. Bahati mbaya hana Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya suala hili la maboma, kutokana na ombi lake tumeamua kujenga theater sasa na sehemu ya kupasulia wagonjwa pamoja na kupata huduma nyingine katika Kituo chake cha Afya cha Mulongo. Tumefanya hivi ili eneo lake liweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumefanya assessment ya maboma yote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jinsi gani tutayamalizia, yale ya Vituo vya Afya na Zahanati, takriban shilingi bilioni 950 zinahitajika. Katika mwaka huu wa bajeti tumeshatenga karibu shilingi bilioni takriban 95. Lengo kubwa ni kuhakikisha tunamalizia hivi viporo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Local Government Capital Development Grant, tumetenga karibu shilingi bilioni 251, karibu one third ya fedha hizo zinakwenda katika suala zima la umaliziaji wa maboma. Kwa hiyo, nawaagiza Wakurugenzi wote wakiwemo na wa Halmashauri yake; inapofika ile fedha, naomba tuweke mgawanyo mzuri wa jinsi gani tutakavyomalizia maboma haya na siyo ya afya peke yake, hata katika Sekta ya Elimu. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake kuhakikisha inaboresha zao la kahawa.
Mheshimiwa Spika, kwenye zao la kahawa kulikuwa na kodi nyingi na Serikali imejitahidi kuondoa kodi 17, lakini hizi kodi hazimnufaishi mkulima moja kwa moja zinawalenga wafanyabiasha. Je, Serikali imejipanga vipi kuondoa hizi kodi ambazo zinamgusa moja kwa moja mkulima ili aweze kupata bei nzuri ya kahawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi mkulima anapoanza kulima, kupalilia mpaka kuvuna hasaidiwi kitu chochote, mwisho anaanza kukatwa kodi na mambo mengine. Je, Serikali imejipanga vipi kumsaidia huyu mkulima ili iweke miundombinu mizuri kuanzia anapolima akiwa shambani mpaka kwenye mnada? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana zao hili la kahawa ambalo linalimwa pia kwa wingi katika Jimbo lake lile la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, katika swali lake la kwanza, ni kweli kwamba Serikali tumeliona hili na ndiyo maana tumeanzisha ule utaratibu wa kuuza kahawa mnadani moja kwa moja kupitia Vyama vyetu vya Ushirika. Vilevile Serikali tumepunguza tozo ya mauzo ya mazao kupitia cess au farm gate price kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3.
Mheshimiwa Spika, swali lake lile la pili ni kwamba zao la kahawa linategemea sana na muonjo ule wa kahawa. Kwa maana hiyo, katika kuweka ubora wa miundombinu pia na ubora wa zao lenyewe, ni kwamba kulekule shambani wakulima wanapaswa kutumia zile CPU kwa ajili ya kuchakata zile kahawa kwa sababu kahawa mbichi hairuhusiwi, hivyo iweze kuanikwa na kusafishwa vizuri, kabla haijapelekwa kukobolewa kule kwenye curing.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Sasa hivi ni kipindi cha msimu wa kahawa. Vyama vya Ushirika vimeshindwa kuwahudumia wananchi kupata maturubai ya kuvunia Kahawa na hii kahawa inaendelea kukaukia Mashambani, wananchi wamekosa msaada. Hata hivyo, hata wale ambao wamepata maturubai, maturubai haya hayana viwango yanachanika hovyo. Ni hatua zipi za dharura ambazo zitachukuliwa ili kunusuru zao hili na mkulima aweze kulifaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na matatizo sana katika suala zima la Vyama vyetu vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika na ndiyo maana kama Serikali tunasema kwamba, tuko katika mikakati ya kuhakikisha tunafufua, tunaimarisha na kuboresha Vyama vya Ushirika.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo kutokana na swali lake hili la msingi katika Jimbo lake la Kyerwa, kwamba mpaka sasa hivi kunasuasua, naomba nichukue fursa hii kuagiza Chama Kikuu cha Ushirika cha Kyerwa kuanzia leo wahakikishe kabisa kwamba, zoezi zima la mazao ya kahawa katika Jimbo la Kyerwa wanafanya kazi yao kwa ubunifu, wanafanya kazi yao kwa utii, wanafanyakazi yao kwa weledi, wanafanyakazi yao kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, lakini na mimi kama Naibu Waziri nikitoka hapa Bungeni ninaahidi kuwapigia Vyama Vikuu vya Ushirika vile AMCOS pale Kyerwa nikishirikiana na Mrajisi wangu kuhakikisha kwamba jambo hili halijirudii na linaweza kufanikiwa kwa uhakika. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya umeme kwa Kyerwa ni makubwa sana, yako maeneo mengi ambayo hayafikiwa kabisa kama Kata ya Bugomola, Kibale, Businde na Bugara na maeneo mengine mengi hayajafikiwa. Ni kwa nini Wizara isiruhusu TANESCO, REA wanapomaliza kupitisha line kuu, Wizara isiruhusu TANESCO wakaanza kuwafungia umeme wananchi ambao wanahitaji umeme?
Swali la pili, REA Awamu ya Pili ambayo kwetu Kyerwa ni REA Awamu ya Kwanza kwa sababu ndipo umeme ulipopelekwa huyu Mkandarasi amesuasua sana mpaka sasa ameshindwa maeneo mengi, wako wananchi wengi ambao wamelipia mpaka sasa hawajafungiwa miaka miwili.
Je, ni hatua zipi zinachukuliwa kwa Mkandarasi huyu ambaye inaonekana ameshindwa kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate naye pia nimpongeze kwa namna ambavyo amefuatilia masuala la nishati katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza lilijielekeza kwenye mahitaji ya umeme, kwa nini TANESCO isiendelee kuwaunganisha wananchi wa maeneo hayo wanaopenda umeme. Napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli katika Mkoa wa Kagera, Mkoa ambao pia ulikuwa haujaunganishwa kwenye gridi ya Taifa tumeunganisha Wilaya za Ngara mpaka Muleba na tunatarajia kukamilisha mpaka Bukoba Mjini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uunganishwaji wa gridi ya Taifa katika maeneo hayo kumejitokeza mahitaji na tumeendelea kuwapa maelekezo TANESCO kwamba inapotokea fursa siyo lazima kusubiri miradi ya REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, kama kweli wapo wananchi wa Wilaya ya Kyerwa wanahitaji umeme na wao hoja siyo kusubiri umeme wa REA ambapo una bei nafuu wako tayari kulipia hata gharama za kuunganishwa umeme na TANESCO, naielekeza TANESCO ifanye upembuzi yakinifu na iwapelekee umeme wananchi hao kwasababu wao kwao umeme hawaangalii hoja kwamba ni wa REA au ni umeme kupitia TANESCO.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, natambua Kata alizozitaja Mheshimiwa na ni kweli mpaka sasa hivi hazijasambaziwa umeme. Natambua uwepo wa Mkandarasi Makuroi katika Mkoa wa Kagera, lakini ni ukweli nakiri kwamba katika Wilaya zingine mkandarasi yule hajafanya vizuri, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulimuita Makuroi kwa sababu anafanya pia na Mkoa wa Rukwa, na mimi nilipata fursa ya kutembelea Mkoa wa Rukwa nikaona ni namna gani anavyolegalega lakini kwa sasa ameshaagiza magari na nimeyathibitisha ana magari mengi tu ya kusambaza nguzo na tulithibisha order ambazo amezitoa katika viwanda mbalimbali vya nguzo vya Mkoa wa Iringa, kwa sasa hivi kwa kweli tumemuelekeza na wakandarasi wote wa miradi hii kwamba lazima kila Wilaya kuwe na genge lake na wasijielekeze sehemu moja.
Kwa hiyo, naomba nimthibitishe Mheshimiwa Mbunge baada ya jibu au baada ya kikao hiki tukutane ili tuendelee na mikakati yakuwasimamia wakandarasi wote. Ahsante.
MHE. INNOCENT L. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa kuleta maji kwenye Mji wa Lubwera pale Makao Makuu ya Wilaya, lakini maji yale yaliyoletwa hayawatoshelezi wananchi. Naiuliza Serikali,ni lini itapanua ule mradi ili uweze kuwatosheleza wananchi kwa sababu ule mji unapanuka sana? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi anavyofuatilia matatizo ya maji katika jimbo lake, jimbo ambalo lina vyanzo vingi vya maji, lakini lilikuwa halina maji ambayo yalikuwa yamewafikia wananchi; na jana alikuja ofisini kwangu kuendelea kufuatilia huo mradi wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo Lubwela tulichimba visima viwili, lakini mtandao umekuwa mkubwa, maji hayatoshi. Namwongezea kisima kimoja, tutaanza kuchimba mwezi huu pamoja na kujenga tenki, lakini hiyo ni sambamba na kupitia sasa huo mradi mkubwa ambao tayari usanifu wake unakamilika ambao utapeleka maji kwenye vijiji 57 katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu wananchi wa Mheshimiwa Mbunge kwamba, yeye yuko makini, atahakikisha kwamba, wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, barabara inayotoka Mgakorongo – Kigalama – Bugomola - Mlongo ni barabara muhimu na inaunganisha nchi jirani pamoja na Wilaya jirani ya Karagwe. Barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne, lakini na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi itajengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini barabara hii itajengwa na wananchi wakalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, maarufu kama Mchungaji, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Mgakorongo – Kigalama – Mlongo ni barabara ambayo inaunganisha nchi yetu na Uganda na inahudumiwa na Wakala wetu wa Barabara TANROADS. Katika sera ni kati ya barabara ambazo zina kipaumbele katika kutengenezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo tumeongelea hizi barabara, sijafika Kagera kwa ziara lakini nazitambua kwa sababu tumekuwa tukibadilishana mawazo. Niwapongeze sana wananchi wa Kyerwa kwa kweli hawakukosea kumchagua Mheshimiwa Bilakwate kwa sababu kazi nzuri anaifanya. Jukumu ambalo wamempa analifanya kisawasawa na sisi kama Serikali tunaendelea kushirikiana naye kuhakikisha kwamba hatuwaangushi wananchi wa Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu barabara hii urefu wake ni takribani kilometa 79 hivi, ambapo itakwenda kuungana na barabara kubwa ambayo inakwenda kuunganisha nchi yetu pia na upande ule wa Mtukula. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu wa barabara hii, inapita maeneo yenye uzalishaji mkubwa na itakuwa na mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ipo kwenye mpango kwa kweli, labda Mheshimiwa Bilakwate baada ya hapa tukae tuzungumze ili tuangalie kwa upana kwenye strategic plan tumepanga namna gani hatua kwa hatua kuikamilisha barabara hii. Pia tumetenga fedha kuhakikisha kwamba barabara hii inaimarishwa ili dhana nzima ya kuhakikisha tunatekeleza sera yetu ya kuunganisha mikoa yetu na nchi za jirani inakamilika na wananchi wanapata huduma na kwa kweli inachangia pia katika uchumi wa nchi yetu.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wamekuwa wakishiriki huduma za afya kwa kujenga maboma. Kwenye Kata yangu ya Kimuri, wananchi wameweza kujenga vyumba zaidi ya 20 lakini vyumba hivi vimekaa zaidi ya miaka 10 Serikali haijaweza kukamilisha. Je, Mheshimiwa Waziri wako tayari kukamilisha hivyo vyumba ili wananchi waweze kupatiwa huduma bora ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo Serikali tunaenda kujenga vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya ni pamoja na Mkoa wa Kagera. Naamini Mheshimiwa Mbunge naye ni miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge wanufaika katika Serikali ya Awamu ya Tano ambao wanaenda kupata huduma hii ambayo haikuwepo kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la kukamilisha hivyo vyumba 20 ambavyo anavisema, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, wanasema kuona ni kusadiki. Ni vizuri pale ambapo tutapata nafasi ya kwenda kutazama ili tujue uhalisia na bajeti kiasi gani itahitajika kumalizia huo ujenzi ili nguvu ya wananchi isije ikapotea, kama Serikali tutakuwa tupo tayari.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka jana kwenye msimu wa kahawa, Serikali ilitangaza bei elekezi Sh.1,400 lakini wakulima wamelipwa Sh.1,106. Ni kwa nini wamelipwa hiyo badala ya bei elekezi iliyoelekezwa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafsi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kupitia Bodi ya Kahawa, mwezi Julai mwaka jana ilitangaza bei elekezi ya Sh.1,400 ya kahawa. Bei elekezi ni bei ya chini anayotakiwa kulipa mkulima maana yake kama tungeruhusu wafanyabiashara binafsi kununua, lakini kahawa hii haikununuliwa na wafanyabiashara binafsi, ni wakulima wenyewe kupitia Vyama vyao vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika waliamua kwenda kuuza kahawa yao kule mnadani Moshi. Kwa hiyo kama wakulima wenyewe kupitia vyama vyao ndiyo waliamua kwenda kuuza kule baada ya kukusanya kahawa yao, kwa hiyo wanakwenda kulipwa kutokana na bei waliyouza kwenye mnada, siyo bei iliyotangazwa ile elekezi kwa sababu hakuna mfanyabiashara binafsi aliyenunua kwa wakulima kule Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hivi Vyama vya Ushirika siyo wafanyabiashara bali wanakusanya kwa niaba ya wanachama wenzao, kwa niaba ya wakulima wenzao baadaye wanakwenda kuuza kwa pamoja kule Moshi na ndiyo maana kwamba sasa hivi kutokana na myumbo wa bei mwaka jana, bei ilishuka kwenye soko la dunia na ikaathiri mnadani pale Moshi na ndiyo maana sasa bei hiyo wanakwenda kulipwa kwa kuzingatia bei iliyouzwa hiyo kahawa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kututengea hizi pesa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya, lakini kipekee nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Jafo kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikimsumbua kuhusiana na Vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, kulingana na jiografia ya Wilaya yangu, ninaomba kuuliza swali. Kwa kuwa tuna vituo vitatu kwenye Tarafa nne na kwenye Kata 24: Serikali iko tayari kututengea kituo kingine kimoja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kyerwa tuna upungufu mkubwa wa watumishi. Kwenye kituo kingine unakuta kuna watumishi wawili kwenye Zahanati moja: Je, Serikali iko tayari kututengea watumishi wa kutosha ili wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge. Katika hali ya kawaida, mtu anayeshukuru tafsiri yake ni kwamba anaomba kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga Vituo vya Afya kwa kadiri nafasi ya kibajeti itakavyoruhusu. Jiografia ya Kyerwa hakika ni jiografia ambayo ina utata mkubwa, Jimbo ni kubwa. Naomba aendelee kuiamini Serikali, kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu na tutakavyokuwa tunaendelea kujenga Vituo vya Afya, naye tutamkumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna swali lake la pili; anaomba kuongeza idadi ya watumishi ili waweze kutoa huduma ambayo inastahili kwa wananchi wake. Sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba kibali cha kuweza kupata nafasi za kuajiri. Kwa kadiri nafasi zitakavyokuwa zimepatikana, hakika katika usambazaji tutahakikisha maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa yanazingatiwa. Naamini na eneo lake ni miongoni mwa maeneo hayo. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, ninaomba kutoa maelezo ya nyongeza kuhusu uhaba wa watumishi, hasa afya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali inafanya jitihada za kujenga Vituo vya Afya na Zahanati nchi nzima. Tunakiri kwamba watumishi hawatoshi, ndiyo maana kwa kushirikiana na TAMISEMI tunafanya utaratibu wa kuongeza. Nimesimama hapa kueleza kwamba, sisi upande wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora tutaweka kwanza kipaumbele katika Zahanati na Vituo vya Afya vipya ambavyo havijaanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Viongozi wa Mikoa, Waheshimiwa Wabunge mkiwasimamia, kuhakikisha wanapoleta maombi watuletee kwamba Zahanati mpya inahitaji watumishi kadhaa, Kituo cha Afya kipya kinahitaji watumishi kadhaa. Pamoja na uhaba uliopo, lengo ni kwamba Vituo vyote vya Afya na Zahanati zote mpya zifunguliwe mara moja, ndiyo tutawapa kipaumbele, kwa sababu sehemu nyingine huduma bado zitaendelea kutolewa japo kwa upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda kwa ruhusa yako pia, nijibu suala la uhaba wa Walimu. Sasa hivi baada ya kufungua mwaka mpya huu wa masomo, Walimu wengi wamestaafu mwaka 2018, wengine wamefariki. Sisi upande wa Utumishi tutaanza kwanza kujaza idadi ya Walimu waliostaafu mwaka 2018, ili tuwe na kiwango cha Walimu kama waliokuwepo mwaka 2018, baada ya hapo tutaendelea na zoezi la kuajiri Walimu wapya.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa hatua ambayo imefikia kwenye usanifu, lakini niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa sababu ya hali ngumu kwa wananchi wa Jimbo la Kyerwa hasa hasa kwenye vijiji ambavyo vinaguswa na mradi huu, je, Serikali iko tayari kwenye bajeti ya 2019/2020 kutenga angalau kiasi kidogo ili mradi huu uweze kuanza wakati Serikali inaendelea kutafuta hela kubwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna miradi ambayo iko katika Kata ya Mabira, Lukulaijo na kwenye Kijiji cha Kageni miradi hii imeshaanza lakini wakandarasi wamekuwa wakienda kwa kusuasua kwa sababu bado certificate zao hazijalipwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa wakandarasi hawa ili waweze kukamilisha hii miradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Bilakwate, mimi binafsi nilipata nafasi ya kwenda katika jimbo lake, nimeona kazi kubwa anayoifanya katika jimbo lake pamoja na wananchi wake. Sasa nataka nimhakikishie sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo kwa wananchi wa Kyerwa kupata maji safi salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Spika, tumefanya tathmini ule mradi ni fedha nyingi sana, lakini tunatambua maji ni uhai na hayana mbadala. Sasa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ukikosa ziwa la mama, la ngombe unanyonya, sisi tupo tayari kufanya njia mbadala katika kuhakikisha wananchi wake wa Kyerwa wanapata maji safi na salama ili waweze kuishi katika eneo lake. Kikubwa na cha msingi kabisa nimwombe kutokana na kuna miradi ambayo inaendelea katika jimbo lake, tukutane baada ya saa saba ili tuangalie ni namna gani tunamsaidia katika kuhakikisha fedha zile tunazilipa wananchi wake waweze kupata maji safi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, lakini zao hili limekuwa kila mwaka linapungua uzalishaji. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa kahawa ili zao hili muhimu lisiweze kufutika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naamini miongoni mwa sababu zinazosababisha zao za kahawa kushuka ni kwa sababu tunapeleka kahawa ghafi kwenye soko la dunia. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuanzisha viwanda ili tupeleke kahawa ambayo iko tayari kutumika kuliko kupeleka kahawa ghafi ambayo bei yake inakuwa chini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Seba Bilakwate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kujua mikakati ya Serikali kuhusu kuongeza uzalishaji. Mkakati wetu wa kwanza ni kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo hasa kupitia Maafisa Ugani wetu na Maafisa Kilimo ili watumie mbinu za kisasa kwa ajili ya kuongeza tija ambayo ndio tatizo sugu kwa kilimo cha Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika zao la kahawa hilo hilo, ni kuendelea kuzalisha. Tuna mkakati na program ya miaka mitano ya kuzalisha miche milioni 10 na kuisambaza katika mikoa yote inayolima kahawa. Mkakati huo unaanza mwaka huu 2019/2020 na utaisha 2024/2025. Pia tunaendelea kupanua mikoa, tunaendelea kulitambulisha zao hili la kahawa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu mkakati wa Serikali katika uimarishaji wa viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani. Sisi kama Serikali tulishaanza kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza kwenye sekta hii ya kahawa. Nichukue nafasi hii kuwapongeza kampuni ya ndani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, jibu kwa kifupi sana.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda viwili mpaka sasa Kiwanda cha Chanika kule Bukoba pamoja na Kiwanda cha Amir Hamza ambavyo vinazalisha zaidi ya tani 6000 za kahawa iliyoongezewa thamani, lakini changamoto kubwa tuliyonayo matumizi ya ndani ni madogo. Nitoe wito kwa sisi Wabunge na wananchi kwa ujumla tuweze kupenda vyetu tutumie bidhaa zinazozalishwa ndani, ili kuunga uchumi wa Taifa letu na kuleta moyo kwa hawa waliowekeza viwanda hapa nchini.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, lakini zao hili bei yake imekuwa ikisuasua kila mwaka; na ukilinganisha uzalishaji wa zao hili kwa mkulima gharama zinakuwa kubwa:-

Nini mkakati wa Serikali ili kuweza kuongeza bei ya kahawa ili mkulima aweze kuendeleza zao hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Spika, kwanza mkakati wa Serikali ni kutambua gharama halisi za uzalishaji za wakulima. Wizara ya Kilimo chini ya Naibu Katibu wa Mkuu Prof. Tumbo, sasa hivi tumeanza program ya kuanza kufanya evaluation ya mazao yote kujua mkulima anatumia shilingi ngapi.

Mheshimia Spika, kuhusu zao la kahawa, kama nilivyosema wakati namjibu Mheshimiwa Shangazi, ni kweli linakumbana na changamoto nyingi. Changamoto ya bei ya ni matokeo ya mfumo ambao umekuwepo muda mrefu ambao umemnyonya mkulima. Sasa hivi tunatumia Benki ya TADB ambayo imeanza kuzipa fedha taasisi za ushirika zilizopo katika Mkoa wa Kagera ili waanze kuchukua mazao ya wakulima kwa bei maalum na wakati huo huo tukitafuta masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge watupe muda kama Wizara, mazao yote haya tutayabadilisha mfumo wake na kuruhusu sekta binafsi iwe competitive wakati huo huo tukipunguza gharama za uzalishaji kama Serikali ili mkulima awezi kupata faida.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwanza niipongeze Serikali kwa juhudi ambazo zinaendelea kuwapatia wananchi wa Jimbo la Kyerwa maji na napongeza kwa ajili ya mradi wa Rutunguru, Kaisho na Isingiro ambao mkandarasi alisimamishwa lakini mradi huu umeanza, naipongeza Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Waziri alipofika Kyerwa tulikaa na kukubaliana mradi huu utakapoanza uweze kwenda kwenye Kijiji cha Kagenyi ambacho tumejenga hospitali ya wilaya, lakini kwenye vijiji ambavyo mmevieleza Kijiji cha Kagenyi hakipo. Ninaomba Mheshimiwa Waziri unihakikishie hospitali yetu ya wilaya ambayo iko kwenye Kijiji cha Kagenyi itapelekewa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuna mradi unaoendelea kwenye Kata ya Mabera lakini kumekuwepo na ucheleweshwaji wa kulipwa mkandarasi na sasa hivi anadai zaidi ya milioni 150. Mheshimiwa Waziri ni lini mkandarasi huyo atalipwa ili mradi huu uweze kukamilika na wananchi wa Kata ya Mabera waweze kupata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kiukweli naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa Wabunge ambao ni wachapakazi na ni wapiganaji hususan maendeleo ya wananchi wake. Kikubwa binafsi nimekwenda na Mheshimiwa Waziri amekwenda kuhusu suala la huu utekelezaji wa mradi huu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa nachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kutokana na jitihada kubwa ambazo amezifanya ujenzi wa hospitali ile kubwa sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo, namhakikishia kijiji kile tutakipelekea huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali lake la pili tuna mrai ambao tunautekeleza katika Kata ya Mabira, mradi takribani milioni 586, upo asilimia 80 ambao unatekelezwa na mkandarasi ambaye anaitwa Vumwe Company Ltd anadai takribani milioni 137. Nataka nimhakikishie ndani ya mwezi huu tutalipa fedha ile ili mradi ukamilike na wananchi waweze kupata huduma ya maji na mimi nipo tayari kwenda kuufungua kuambatana na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa mradi wa vijiji 56 unaoendelea kule Kyerwa usanifu umekamilika. Sasa swali kuna kata ambazo zina hali ngumu sana kama Kata ya Bugomola, Kata ya Kibale, Kata ya Businde na Kata ya Bugala.

Je, Serikali wakati tunaendelea kusubiria huu mradi uanze wako tayari kuwachimbia wananchi visima ili waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru lakini nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya nataka nimuhakikishie sisi tupo tayari na tunalishukuru Bunge lako tukufu limetuidhinishia sisi Wizara ya Maji zaidi ya shilingi bilioni 610 katika kuhakikisha tunatekeleza miradi ya maji bila shaka tutampa nafasi hiyo katika kuhakikisha tunamsaidia visima.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nisikitike sana kwa majibu ambayo yametolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, uthaminishaji wa maeneo yale umefanyika zaidi ya miakakaribia miaka minne, na kwa mujibu wa sheria inabidi warudi tena kufanya uthaminishaji upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama wameshindwa huu wa kwanza kulipa, watawezaje kufanya uthaminishaji wa awamu ya pili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, mko tayari kuwatangazia wananchi wa Rwenkorongo pale Kyerwa kuwa mmeshindwa kuwalipa ili waweze kuendeleza maeneo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu inaonesha moja kwa moja mmeshindwa kuwalipa wananchi, mko tayari kuongea na Halmashauri ili iwatafutie maeneo mengine ambayo hayatahitaji fidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijashindwa kulipa fidia wananchi na Serikali ina nia ya kulipa fidia wananchi. Kama ambavyo nimezungumza katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba fidia hizi, maeneo haya ni mengi ambayo yanahitaji kulipwa fidia na suala hili haliwezi likafanyika kwa wakati mmoja.

Kwa hiyo, ninalirudia jibu langu la msingi ambalo nimejibu kwamba fidia za eneo hili ambalo lilichukuliwa kwa ajili ya magereza na maeneo mengine, najua kuna Waheshimiwa Wabunge ambao maeneo yao mengine vilevile yanahitaji kulipwa fidia, zitalipwa kwa awamu kadri hali ya kifedha na kibajeti itakavyoruhusu.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama lilivyo swali la msingi, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwenye Wilaya ya Kyerwa tuna kata 24 lakini tuna vituo vya afya vitatu; Serikali ina mpango gani wa kuongeza vituo vya afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kituo cha Afya Nkwenda ni kituo ambacho tumeanzisha jengo la mama na mtoto ambalo bado halijakamilishwa. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Kituo cha Afya Nkwenda kwenye jengo la mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Halmashauri ya Kyerwa kuwa na kata 24 na vituo vya afya vitatu tu na Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba halmashauri hiyo inapata vituo vya afya kadri ya maelekezo na sera. Kama ambavyo nimetangulia kusema kwenye jibu la msingi, Serikali imedhamiria kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuunga mkono ujenzi wa vituo vya afya katika kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa utekelezaji wa miradi hii ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata ni endelevu na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 27.75 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo 555. Pia katika mwaka wa fedha ujao tutatenga bajeti kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo hivyo. Halmashauri ya Kyerwa na kata zake ni sehemu ya halmashauri na kata ambazo zitanufaika katika mradi huu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili litafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kituo cha afya kuwa na jengo la wazazi na Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha jengo hilo linakamilika na kutoa huduma. Hilo ni jambo la muhimu sana katika kusogeza huduma kwa wananchi. Kwa sababu Serikali inatambua na ina dhamira ya dhati ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga, kipaumbele ni pamoja na kutenga fedha kadri zinavyopatikana kwa ajili ya kukamilisha majengo kama haya. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba pia jengo hilo litakuwa sehemu ya mpango huu ili liweze kukamilishwa na kutoa huduma zinazokusudiwa kwa wananchi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa juhudi za kuwapatia wananchi wa Kyerwa maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza maswali, kwenye majibu aliyotujibu, kuna sehemu ambayo haiko sahihi. Vijiji vya Kibale, Nyamiaga na Magoma hakuna kisima ambacho kimechimbwa. Kwa hiyo, hiyo taarifa aliyonipa siyo sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, huu mradi ni muhimu sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Mheshimiwa Waziri ananihakikishia kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 atatenga fedha kwa ajili ya mradi huu ili uweze kutekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ziko Kata ambazo haziko kwenye huu mradi, Kata za Bugomora, Kibale, Murongo pamoja na Businde. Serikali ina mpango gani wa kuzipatia maji Kata hizi ili nao watoke kwenye adha wanayoipata? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kuhusu kutengwa fedha kwa mwaka wa fedha ujao kwa mradi huu mkubwa, azma ya Serikali ni kuhakikisha miradi hii yote tunaitekeleza kwa wakati. Hivyo, katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022 mradi huu utapatiwa fedha kwa awamu na utekelezaji wake utaanza mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge, napenda tu kusema kwamba tutahakikisha maeneo yote yenye matatizo ya maji, maji yanapatikana. Kwa mradi huu mkubwa ambapo bomba kubwa litapita, michepuo ya maji pia itazingatiwa; na kwa maeneo ambayo michepuo haitafika kwa urahisi, basi uchimbaji na ujenzi wa visima utazingatiwa katika mwaka wa fedha ujao.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri ya Jimbo la Kyerwa, tunalo jengo la halmashauri. Jengo hili limechukua muda mrefu na halijakamilishwa. Nini ahadi ya Serikali kukamilisha lile jengo la halmashauri katika Wilaya ya Kyerwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ndiyo inayojenga majengo yote ya halmashauri katika nchi yetu likiwemo jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa. Hivyo basi, kutokana na mahitaji na malengo ya Serikali ambayo imejiwekea na bajeti ambayo tumeitenga, tutalikamilisha lile jengo kadri bajeti yetu tulivyoiweka. Ahsante sana.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya Mgakolongo kwenda Kigalama mpaka Mlongo inayounganisha na nchi ya Uganda, usanifu wake umeshakamilika muda mrefu. Ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye Ilani na nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira tuone bajeti ambayo tunaiandaa hiyo barabara itashughulikiwaje. Kwa sasa siwezi nikasema chochote maana ndiyo tuko kwenye kipindi cha bajeti, kwa hiyo, naomba awe na subira aone kama barabara yake itajengwa lakini tunatambua ni barabara muhimu sana. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kinipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa juhudi zinazoendelea kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Ibanda na Rumayika.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwenye awamu iliyopita ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alitoa maelekezo kuwekwa mipaka maeneo ambayo yalikuwa yamevamiwa na wananchi na akaelekeza maeneo haya yawekewe mipaka ili wananchi wasiendelee kuvamia yale maeneo, na Serikali ilileta wataalam wakaja kupitia maeneo yale. Baada ya kupitia, Serikali bado haijaweka mipaka kwenye maeneo hayo ya hifadhi na wananchi wameendelea kubugudhiwa. Je, ni lini Serikali itaweka mipaka inayotambulika ili wananchi hawa wasiendelee kusumbuliwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye hifadhi hizi pamoja na kutengwa sisi tunashukuru sana Serikali, lakini bado hatujaona juhudi za Serikali za kuweka vivutio ambavyo vitawavutia watalii. Ni lini Serikali italeta vivutio katika Hifadhi ya Ibanda na Rumanyika ili kuvutia watalii waje katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Swali lako la pili halijaeleweka Mheshimiwa Bilakwate; Serikali ilete vivutio tena wakati hifadhi zenyewe ndiyo vivutio?

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, samahani, kwenye hizo hifadhi hakuna wanyama, yaani hakuna vile vivutio ambavyo vinaweza kuwavutia watalii kuja kuangalia.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye kipengele (a) na (b), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze na mipaka. Ni kweli Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikiainisha maeneo mbalimbali yanayohusiana na hifadhi kwa kuweka mipaka katika maeneo ambayo yanahusiana na uhifadhi. Katika Hifadhi ya Ibanda – Kyerwa na Rumanyika tulifanya tathmini baada ya wataalam wetu kwenda kuainisha mipaka na utekelezaji wake tunaendelea kuandaa mazingira ya kupeleka wataalam kwa ajili ya gharama za uthamini ikiwemo kuainisha maeneo yenye changamoto hizi za uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, lakini tunatoa maelekezo kwenye upande wa maeneo haya ambayo tayari yamesha ainishwa, kwamba wananchi ambao wanazunguka maeneo haya wasiendelee kubugudhiwa mpaka pale ambapo wataonyeshwa eneo ambalo linahitajika kwaajili ya uhifadhi na maeneo ambayo wataachiwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upande wa vivutio. Serikali inatambua kwenye hifadhi hizi ambazo ni mpya ambazo tayari zimeshatangazwa, zina wanyama lakini baadhi hawapo, hasa vivutio vya wanyama wakali kama simba na tembo. Serikali ina mpango wa kupeleka mbegu za wanyama hawa ili kuimarisha maeneo yenye uhifadhi katika maeneo hayo ili kuendelea kuongeza idadi ya Wanyama katika hifadhi hizi, lakini pia vivutio mbalimbali vinavyohusiana na mambo ya mali kale na mambo mengine ambayo yanahusiana na vivutio. Naomba kuwasilisha.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Changamoto iliyopo Nkasi ndiyo changamoto iliyopo Kyerwa. Kyerwa tuna kata 24 lakini vituo vya afya vinavyotoa huduma ni viwili na kipo Kituo cha Afya Nkwenda ambacho jengo la mama na mtoto halijakamilika. Lini Serikali itakamilisha kituo hiki ili kiweze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kutoa ufafanuzi, kwamba dhamira na malengo ya Serikali na katika mipango yote ambayo Serikali inaandaa, ni pamoja na kuhakikisha inachangia nguvu za wananchi katika kukamilisha maboma ya zahanati, vituo vya afya na kupanua hospitali za halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo hili la Kyerwa ambapo kuna vituo vya afya viwili na Kituo cha Afya cha Nkwenda ambacho kimeshajengewa jengo la RCH na halijakamilika, ni miongoni mwa vituo ambavyo vitaendelea kupewa kipaumbele katika bajeti za Serikali ili viweze kukamilishwa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba katika mwaka ujao wa fedha, Mheshimiwa Waziri akija kuwasilisha bajeti hapa, tuna vituo takribani 121 ambavyo tunatarajia kwenda kujenga kwa fedha za Serikali Kuu na fedha za mapato ya ndani ya halmashauri. Kwa hiyo kwa kupitia mpango huo tutaendelea kusogeza zaidi huduma ikiwemo katika Jimbo hili la Kyerwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa inayosababisha wakulima wasipate bei nzuri ya kahawa ni kupeleka kahawa ghafi nje. Serikali ina mpango gani wa kuanzisha viwanda vikubwa ambavyo vitachakata hii kahawa ili kuongeza thamani mkulima aweze kupata bei nzuri ya kahawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza tunayoichukua specifically kwa Mkoa wa Kagera, sasa hivi kiwanda ambacho kinamilikiwa na wakulima wa Mkoa wa Kagera cha TANICA, installed capacity yao ni tani 3,000. Sasa hivi tunavyoendelea walikuwa wanadaiwa madeni mengi, tumeshachukua hatua ya kwanza kuhakikisha kwamba TADB inafanya intervention kuweza kuyaondoa yale madeni na kuyachukua wao kwa sababu madeni yale walikuwa wanaidawa na benki za kibiashara ambazo zilikuwa zinachaji riba kubwa.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili, tunakifanyia sasa hivi kiwanda cha TANICA feasibility study ili tuweze ku-expand uwezo wake wa kuchakata kahawa ya wakulima wa Kagera ili kupitia kiwanda chao cha TANICA waweze ku-process na kuuza kahawa iliyochakatwa kama finished product. Vilevile tunafanya maongozi na wafanyabiashara kikiwepo kiwanda kikubwa kilichopo Kagera ambacho kina matatizo na Tanzania Investment Bank ili tuweze kukisaidia kuki-bail out kiwanda kile kiweze na chenyewe kuchakata kahawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mwelekeo wa Serikali cha kwanza ni ku-perfect mfumo wa soko kuhakikisha wakulima wanalipwa kwanza malipo yao vizuri. Hatua ya pili ni expansion ya TANICA ili Mkoa wa Kagera waweze kuuza kahawa yao ikiwa processed.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zinazoendelea za kuwapatia maji wananchi wa Jimbo la Kyerwa kwenye Mradi wa Vijiji 57.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ziko kata ambazo haziko kwenye Mradi wa Vijiji 57, kama Kata ya Bugara, Kibale, Businde pamoja na Mlongo. Nini juhudi za Serikali kuwapatia wananchi hawa maji?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana sana kaka yangu Mheshimiwa Bilakwate kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Kyerwa. Kubwa ambalo nataka kusema, sisi kama Wizara ya Maji, tumejipanga na zaidi ya miradi 1,527 tunakwenda kuitekeleza katika maeneo ya vijijini katika kuhakikisha wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishe maeneo ambayo hayana maji, sisi kama Wizara tumejipanga kuhakikisha tunawafikishia hii huduma ya maji safi na salama.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nisikitike kwa kusema majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri sijaridhika nayo kwa sababu yeye anasema Serikali inaelekeza wananchi walipwe baada ya siku tatu, hili jambo si sawa wananchi wamekuwa wakikaa zaidi ya miezi mtatu hawajalipwa. Kwa hiyo, mnapoleta majibu kwanza myafanyie utafiti, swali la kwanza, Je, Serikali kama msimamizi mkuu wa Ushirika ipo tayari kushirikiana pamoja na vyama vikuu vya Ushirika ili wanapokwenda kuomba hii mikopo Benki waweze kupewa haraka ili kuondoa adha ambayo wanaipata wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Serikali baada ya kuruhusu wanunuzi binafsi je, ni utaratibu upi ambao imeuweka ili huyu mnunuzi binafsi kahawa yake aipate ikiwa salama lakini pia huyu mkulima apate fedha yake kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bilakwate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu mikopo ambayo tumekuwa tukisaidia katika vyama vya Ushirika ambavyo vimesaidiwa na Serikali kwa kipindi cha miaka miwili, mitatu mfululizo ni vyama vya KDCU ambapo Mheshimiwa Mbunge anatoka, Serikali ilikichukua chama hiki kikiwa kina deni la zaidi ya bilioni saba Serikali ika-develop a bailout system na kukifanya chama hiki sasa hakidaiwi hata shilingi moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mikopo tunawasaidia na ni vyama vya KCU na KDCU tumewasaidia kupitia Tanzania Agricultural development Bank na msimu uliopita wamepata jumla ya bilioni 23 kwa ajili ya ku- aggregate kahawa kutoka kwa wakulima na wamepata kwa interest ya asilimia 9. Ndio vyama pekee ambavyo katika ukanda ule, pamoja na matatizo ya korona wakulima wa Kagera walipata bei bora zaidi ya kahawa yenye maganda kuliko kahawa ya wakulima wa nchi ambazo zimekuwa jirani na sisi. Wakati wenzetu wakipata wastani wa Shilingi 700 hadi 800 kahawa ya Kagera ilinunuliwa kwa shilingi 1,200 kwa usimamizi wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu na nitumie Bunge hili kuwaambiwa Waheshimiwa Wabunge wa Kagera wiki iliyopita tumekaa na vyama vikuu vya Ushirika vya KDCU, KCU na makampuni binafsi. Mpaka sasa ni makampuni saba yameonyesha interest ya kununua kahawa katika vyama vya Msingi, na ninarudia hatutowaruhusu kwenda kwa mkulima mmoja mmoja wataenda kwenye vyama vya msingi na sasa mikataba itakuwa tripartite itasainiwa na Chama cha Msingi, itasainiwa na Mkulima, itasainiwa na Chama Kikuu lakini chini ya usimamizi wa Bodi ya Kahawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu mnunuzi anataja bei anayonunulia na kiwango anachohitaji na atakapochukua kahawa kutoka kwenye chama cha Msingi nilazima alipe ndani ya muda usiozidi masaa 72 hayo ndio maelekezo ya Serikali.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali kwa kazi inayofanyika kwa upande wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kyerwa ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina vipindi virefu vya mvua, barabara zake zinatengenezwa kwa udongo, sasa Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti ili barabara hizi ambazo hazipitiki kipindi cha mvua ziweze kutengewa bajeti ya changarawe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; niishukuru Serikali kwa ombi langu lla kujenga lami katika Mji wa Nkwenda, kazi ambayo tayari imekamilika lakini nilileta ombi kwa sababu ya umuhimu wa ule Mji wa Nkwenda kuweka taa pale. Je, Serikali imefikia wapi ombi ambalo nimelileta kwenu kuweka lami katika Mji wa Nkwenda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKLIA ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anaomba tu, amejaribu ni ombi vilevile ni ushauri, upi ni mpango wa Serikali wa kuongeza bajeti. Nafikiri baada ya Wabunge wengi kuzungumza ndani, Serikali katika bajeti kuu imekuja na mpango wa kuongeza fedha kwa TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuseme tu kwa ongezeko hilo la fedha ambalo Bunge lako Tukufu likiwapendeza wakapitisha, basi tutaongeza bajeti katika halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Kyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; ameshukuru kwamba Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami katika eneo la Mji wa Nkwenda na hiyo lami imeshakamilika lakini sasa hivi alileta ombi Serikalini na nimhakikishie tu kwamba ombi lake linatekelezwa na Serikali kwa sababu mkandarasi ameshapatikana, yupo site na taa zitawekwa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kawaambie wananchi wa Kyerwa katika Mji wa Nkenda kwamba ombi ulilolileta basi linaanza kutekelezwa; hivi niavyozungumza mkandarasi amekwenda site, ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye Wilaya ya Kyerwa, Kata ya Bugomora, Kata ya Mlongo, Kata ya Kimuli na Kata ya Kyerwa Kagenyi, kuna miradi ambayo usanifu wake umekamilika, lakini mpaka sasa hivi Serikali bado haijatoa fedha ili miradi hii ianze. Lini Serikali itatoa fedha miradi hii ianze? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa hiyo compliment. Kwa swali la Mheshimiwa Mbunge kutoka Jimbo la Kyerwa, eneo hili pia Serikali tumeendelea kulipa jicho la kipekee. Wizara kupitia RUWASA na mamlaka pale Mji wa Kyerwa wataendelea kushirikiana kuhakikisha miradi hii yote ambayo haijakamilika iweze kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na Serikali ya Awamu ya Sita.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Murushaka kwenda mpaka Mrongo ni barabara ya kiuchumi kwa Mkoa wa Kagera, lakini pia ni barabara muhimu inayounganisha nchi ya Tanzania na Uganda; na kwa umuhimu wake Mheshimiwa Hayati Pombe Magufuli aliahidi ijengwe kilometa 50 za haraka. Ni lini kilometa 50 hizi zitajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara ya Mrongo yenye urefu wa kilomita 112 aliyoitaja Mheshimiwa Bilakwate ni kweli iliahidiwa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, barabara hii imeingizwa kwenye mpango na fedha imetengwa kwa ajili ya kuanza mwaka wa fedha ujao kwa kiwango cha lami. Nadhani tumetenga kama siyo chini ya shilingi bilioni tatu kwa kuanzia. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa wa Kyerwa na wananchi wa Kyerwa, ahadi ya Mheshimiwa Rais Hayati itaanza kutelekezwa mara tutakapoanza utekelezaji wa bajeti ambayo Bunge lako imelipitisha. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye Wilaya ya Kyerwa kuna mradi wa vijiji 57, mradi huu Serikali imesema utajengwa kwa awamu, lakini kwenye bajeti kuna Kata ya Kikukulu, Kata ya Songembele, Kichwechwemkula na Rukaija havikuwekwa bajeti. Nini kauli ya Serikali juu ya kata hizi ambazo hazikuwekwa kwenye bajeti? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Bilakwate kwa namna anavyopigania jimbo lake la Kyerwa, kubwa ambalo nataka nimuhakikishie mkakati wa Wizara yetu ya Maji ni kuhakikisha tunatumia vyanzo toshelevu ikiwemo Mto Kagera.

Sasa moja ya vijiji ambavyo vingi tunakwenda kutatua tatizo la maji zaidi ya 50. Tumesema mradi huu tunakwenda kuutekeleza kwa awamu, kata ambazo hazipo katika bajeti hii tutahakikisha bajeti ijayo tunaziweka ili kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaweza kupata huduma hii muhimu ya maji. Ahsante sana.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali ikiwemo afya pamoja na shule, yamekuwa yakivamiwa na watu ambao hawana nia njema: -

Serikali ina mpango gani maeneo haya yote ili yaweze kupimwa kuondoa hii adha ambayo imekuwa ikijitokeza? (Makofi)

Swali la pili; tunayo miji midogo kama Nkwenda, Nsingiro, Mrongo na Mabira. Maeneo haya yanakua kwa kasi: Serikali ina mpango gani wa kupima haya maeneo ili baadaye wasije wakaanza kuwavunjia wananchi nyumba zao? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Naomba nijibu mawali mawili ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli uvamizi ni mkubwa sana katika maeneo mbalimbali, lakini nilitaka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji, Mamlaka ya Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri za Wilaya. Maana yake ni kwamba ukipanga unapaswa kusimamia, wanaopanga master plan. Wanaopanga mipango flani flani ya utekeleaji wa master plan ndani ya sheria za nchi hii ni Halmashauri ndiyo wanaohitaji na ndiyo wanaojua kwamba ardhi yao itumike namna gani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwa Halmashauri zote, zisimamie na zilinde maeneo kama yalivyopangwa na mamlaka zao. Maeneo yote ya wazi hayapaswi kutumika kwa shughuli nyingine na nimeelekeza wenzangu kwamba maeneo yote ya Umma kama yanaangukia kwenye sekta fulani, basi sekta hiyo iyalinde, ichukue hati na iweke mipaka inayoonekana/alama zinazoonekana, kama ni maeneo ya shule wayalinde wachukue hati, nasi tulisema hatutawadai kodi ya ardhi ya kila mwaka. Kama ni maeneo ya afya, basi yalindwe, yapimwe yachukuliwe hati na yawekewe alama zinazonekana ili wananchi waweze kujua. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuyalinda.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kweli kutokana na ustaarabu na utekelezaji ulio mzuri wa sera za CCM na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, leo tuna umeme kila kijiji. Umeme unaleta ustaarabu na unabadilisha maisha. Kwa hiyo, imetokea kwamba baadhi ya vijiji vingi sasa vimeanza tabia ya kimji. Sheria inaelekeza kwamba maeneo hayo, Halmashauri myawahi mapema. Maeneo ambayo mnajua yameanza kuchipukia na maisha yanakuwa ya kimji, pelekeni na mjadili kwanza muainishe maeneo hayo hata kama ni ya vijiji, mpelekeeni Waziri wa Ardhi ayatangaze kama town planning areas ili maeneo hayo ya vijiji yanayochipukia kuwa na maisha ya kimji, Waziri ayatangaze ili yapangwe kimji na Halmashauri zipime na watu wapewe viwanja na hati kama za mjini. Kwa namna hiyo tunaweza tukalinda, baadaye kukawa hakuna squatter katika mji yetu. Kwa hiyo, ni jukumu letu Mheshimiwa Mbunge Halmashauri na sisi kama Wajumbe tusimamie katika kupanga na kusimamia ardhi yetu.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nipongeze Wizara ya Maji kwa juhudi zinazoendelea za kuwapatia wananchi wa Jimbo la Kyerwa maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kyerwa tunao Mradi wa Vijiji 57, lakini mradi huu tumekubaliana utajengwa kwa awamu. Hata hivyo, zipo Kata kama Businde, Songa Mbele, Kikukuru, Kitochenkula; kata hizi haziko kwenye awamu hii ya kwanza. Je, Serikali iko tayari angalau hata kuchimba visima ili hawa wananchi ambao wanapata wakati mgumu waweze kupatiwa maji safi na salama wakati wanasubiria mradi mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna mradi mzuri sana pale kwenye Jimbo la Kyerwa na Mheshimiwa Innocent amekuwa bega kwa bega na Wizara. Tumekuwa tukishirikiana naye sana Mheshimiwa Mbunge. Kwa visima kuchimbwa kwa dharura wakati miradi mikubwa ikiendelea na utekelezaji, hii ni moja ya jitihada za Wizara na tumetenga zaidi ya visima 500 kuona kwamba tunavichimba katika maeneo ambayo miradi yake inachukua muda mrefu. Hivyo, kwa kata hizi ambazo ziko pembezoni kwenye Jimbo la Kyerwa nalo tutalifikiria kuona visima vinachimbwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa nafasi ambayo amekuwa akinipa kujadili miradi ya Wilaya ya Kyerwa.

Swali langu la nyongeza, tunao mradi wa vijiji 57 na mradi huu Mheshimiwa Waziri tumekubaliana unajengwa kwa awamu. Lakini kuna mradi unaotoka Kyerwa, Nyaruzumbula, Nyakatuntu mpaka Kamuli. Mradi huu umechukua muda mrefu ni lini mradi huu utaanza? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote dhati ya moyo nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Kyerwa kwa kazi kubwa na nzuri, ambayo anaifanya na amekuwa msumbufu sana kuhusu suala zima la Jimbo lake liweze kupatiwa huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuhakikishie utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan sisi Wizara yetu anatupatia fedha kila mwezi kupitia Mfuko wa Maji na tumetengewa zaidi ya shilingi bilioni 459.2 kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji vijijini. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ahadi ambazo tuliziahidi kama Wizara ya Maji tutakwenda kuzitekeleza kwa sababu ya upatikanaji wa fedha ambazo tunapewa na Mheshimiwa Rais. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambapo REA wamepeleka umeme wamepitisha laini kuu na pale chini kwa wananchi wa kawaida hakuna umeme. Kwa mfano nimueleze Mheshimiwa Waziri, nina vitongoji 610, vitongoji ambavyo havijafikiwa ni 503 na ukija kuangalia wanasema vijiji karibu asilimia zaidi ya 75 vimeshapata umeme, lakini ukiangalia wananchi wengi hawana umeme na mahitaji ni makubwa. Ni lini hivi vitongoji vitapelekewa umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninamshukuru kaka yangu, Mheshimiwa Bilakwate, kwa swali zuri kabisa, na mimi Kyerwa ninapafahamu. Lakini ninaomba Mheshimiwa Bilakwate achukue tu na kuamini maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, kwamba tunafahamu kwamba vitongoji vingi sana havina umeme na plan na mkakati mkubwa sana wa Serikali wa kufikisha umeme katika vitongoji hivyo vyote ndani ya miaka minne upo na unaendelea na utakapokuwa tayari vitongoji vyote 37,000 nchini ambavyo havina umeme vitapatiwa umeme.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Murushaka kwenda mpaka Murongo, ahadi ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kilometa 50, imeshatangazwa muda mrefu lakini mpaka sasa hivi haijaanza ujenzi; nini tatizo lake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara haina shida, nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tulishatangaza, mzabuni (mkandarasi) alishapatikana na tunategemea muda wowote ataoneshwa site ili aanze kutekeleza hiyo kazi, kilometa 50, kama zilivyoahidiwa na kama tunavyotegemea mkandarasi aanze kuifanya hiyo kazi. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kyerwa tuna Vitongoji 670, Vitongoji ambavyo vina umeme ni vitongoji 170, vitongoji 500 vyote havina umeme sawa sawa na asilimia zaidi ya 75.

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupelekea vitongoji vingine ambavyo havina umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la Pili; Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa Mikoa ambayo tunapata adha kutokana na umeme unaokatika mara kwa mara. Je, nini mkakati wa Serikali wa haraka kuunganisha Mkoa wa Kagera na gridi ya Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme katika maeneo ya vitongoji ni katika maeneo matatu. Kwanza ndiyo hii ambayo tunaifanya saa hizi ya REA III Round II, ambayo inafikisha umeme katika vijiji lakini katika vitongoji pia. Kama tulivyosema kwenye jibu la misingi Vitongoji 33 vitapata umeme.

Mheshimwa Spika, kuna mkakati wa pili ambao unafanyika wa umeme jazilizi (densification) na Mkoa wa Kagera kwenye eneo lake la Kyerwa densification katika two B na C zimo na kuanzia Januari tutaongeza wigo wa kupeleka kwenye maeneo hayo.

Mheshimwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta pesa sasa nyingi zaidi kwa ajili ya kumaliza vitongoji vyote nchini takribani kama elfu 30 na zaidi ambavyo havijapata umeme, inahitajika karibia Trilioni Sita na Bilioni Mia Tano kuweza kukamilisha eneo hili lote na jitihada za Serikali kutafuta hizo pesa zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, mwezi huu, Mheshimiwa Rais amezindua kituo cha kupooza umeme cha pale Nyakanazi ambacho ndiyo sasa kimeingiza Gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma na katika Wilaya mbili za Mkoa wa Kagera ambapo ni Ngara na Biharamulo. Jitahada za kuhakikisha kwamba Mkoa mzima wa Kagera unapata umeme kutoka katika chanzo hicho unaendelea na tayari mradi wa kuanza kupeleka umeme kutoka Benako kwenda Kyaka umeshatangazwa na Mkandarasi anatafutwa ili sasa Mkoa wa Kagera na wenyewe uweze kuingia katika Gridi ya Taifa hivi karibuni.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na uharibifu huo uliojitokeza wananchi hawa walihamishwa kwenye vitongoji vile kwa sababu ya uharibifu wa wale tembo. Mpaka sasa hivi wananchi wale wanaendelea kupata shida hakuna walicholipwa. Je, ni nini mpango wa Serikali angalau wa kuwapa fidia hawa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwenye Kata ya Businde, Kata ya Bugara pamoja Kikwechenkura, tembo wanaendelea kufanya uharibifu mkubwa, taarifa zinaendelea kutolewa lakini hakuna chochote ambacho Serikali inafanya. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kudumu kuweza kuwahamisha wanyama hao waharibifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitoe pole kwa wananchi wote ambao wamekuwa wakikutwa na kadhia hii ya changamoto ya wanyama wakali na waharibifu. Serikali inatambua changamoto hizi na ndio maana tumeanza ujenzi wa vituo vya askari ili kusogeza huduma hii kwa ukaribu zaidi na wananchi waweze kutoa changamoto zao na huduma hii iweze kutolewa kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tumeanza kufundisha vijana kwenye maeneo husika hususan vijana wa kwenye maeneo ya vijijini kama VGS ambao watashirikiana na askari kuhakikisha kwamba, wanyama wanaposogea katika maeneo ya shughuli za kibinadamu, basi iwe rahisi kuwaondoa.

Mheshimiwa Spika, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inachukua hatua na suala la kifuta machozi na kifuta jasho, tayari tumeshaanza kufanya tathmini na utekelezaji wake utafanyika hivi punde. Ahsante.
MHE. INNOCENT. S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali kwa juhudi za kuendelea kuwapatia maji wananchi wa Jimbo la Kyerwa lakini tunao mradi wa Kyelwa, Nyaruzumbura, Nyakatuntu mpaka Kamuli, mradi huu tumeupitisha kwenye bajeti iliyopita lakini mpaka sasa mradi huu haujaanza, je, ni lini utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii yote ambayo mtaji wake ni ukubwa bado tunaendelea kuona kwamba tunapata fedha na kwenda kuitekeleza. Hivyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge Bilakwate tunakwenda kuutekeleza huu mradi na si kwa kuona kwamba tunatekeleza tu wajibu wetu, bali tunazingatia pia uhai kwa sababu maji ni uhai.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mgakorongo kwenda mpaka Mrongo ni barabara muhimu ya kiuchumi kwa Mkoa wa Kagera lakini pia inaunganisha nchi jirani ya Uganda. Barabara hii ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni barabara kuu inayounganisha Tanzania na Uganda kupitia mpaka wa Murongo ambayo inaanzia Umugakarongo - Kigarama hadi Murongo.

Mheshimiwa Spika, tunavyoongea sasa hivi, taratibu za manunuzi zinaendelea na ikiwezekana barabara hii itatangazwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa maelezo ambayo ameyaeleza Mheshimiwa Waziri inaonesha Ofisi ya NIDA imeshindwa kuwapatia Wanakyerwa vitambulisho, kwa sababu wananchi waliojitokeza ni 112,518. Wananchi waliopatiwa vitambulisho ni 31,897 ambayo ni asilimia 28. Kwa hiyo asilimia 71.7 bado hawajapatiwa vitambulisho.

Je, nani ambaye atalaumiwa kwa sababu wananchi hawa kutopatiwa vitambulisho hawawezi kusajili simu zao, wananchi hawa hawawezi kusajili hata kampuni, ni nani wa kulaumiwa katika hili?

Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili kwa sababu inaonesha NIDA wameshindwa kutoa vitambulisho, kwa nini zoezi hili la NIDA lisisitishwe nchi nzima ili wakajipanga upya kuja kuwahudumia wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja; wa kulaumiwa nani? Nadhani hilo tumeshapata suluhisho Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeridhia kutoa fedha ambazo zilikwamisha kwa muda mrefu kutomlipa mzabuni zaidi ya bilioni 17. Baada ya kumlipa mzabuni mkataba umehuishwa na uzalishaji wa vitambulisho unaendelea. Na tuishukuru Wizara ya Fedha imeanza kutoa katika bajeti fedha iliyopitishwa katika bajeti bilioni 42 imeshatoa zaidi ya bilioni 10 ili kumlipa mkandarasi aanze kuzalisha vitambulisho hivyo. Kwa mwenendo huu nina uhakika wananchi wote watapata vitambulisho kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, ili suala la kwamba wameshindwa sasa tusitishe; sasa tuko kwenye mkataba na Serikali imeshaji- commit kutoa fedha sasa unasitisha ili u-achieve nini wakati vitambulisho bado ni muhimu. Jambo la msingi watekelezaji wetu wa Serikali maeneo mbalimbali kama mtu ana namba ya utambulisho tumeshatoa mwongozo kwamba namba ile itumike kama kitambulisho, kama kuna mahali mtu anakwamisha tupeane taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa, nashukuru.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na Serikali kuongeza bajeti kwa Wilaya ya Kyerwa, lakini tulileta ombi maalum kwa ajili ya barabara ya Kibingo kwenda Rwesinga, Barabara ya Mabira kwenda Nyamiri- Makamuri, barabara ya Kikukuru -Mkunyu - Lwele, barabara ya Kakanya - Lwele pamoja Bushongore. Ombi hili ni lini litatekelezwa ili kuondoa changamoto iliyopo Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Bilakwate kwa namna ambavyo anaendelea kuwapambania wananchi wa Jimbo la Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, pia nimhakikishie ni kweli ameleta maombi maalum ya barabara zenye urefu wa takribani kilomita 55 ambazo amezitaja. Tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMi tumepokea na tutaanza utekelezaji mwaka ujao wa fedha kuhakikisha barabara zote zinapitika vizuri. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na nishukuru kwa hatua ambazo Serikali imefikia kwa ujenzi wa barabara hii. Pia naomba kujua barabara ya Murushaka kwenda mpaka Murongo, ambayo walishatangaza tender, wamefikia wapi, ili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Swali la pili; tunayo barabara inayotoka Kyerwa, Makao Makuu ya Wilaya, Nyakatuntu, Kamuli, Kitwe, Mabira mpaka inaunganisha Karagwe; nataka kujua, barabara hii ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wetu na ndiyo kuna uzalishaji mkubwa, lakini imekuwa ikijengwa kwa kiwango ambacho siyo kizuri: Ni lini Serikali itaweka barabara hii yote iweze kujengwa kwa changarawe ipitike wakati wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Omurushaka – Nkwenda - Kyerwa hadi Murongo itaanzwa kujengwa kilometa 50 kati ya Kyerwa kuja Omurushaka kilometa 50. Utaratibu utakaotumika ni kusanifu na kujenga. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii tayari tender ilishatangazwa na mwisho wa kupokea tender ni tarehe 10 mwezi huu wa Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; nampongeza sana Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kwa ufuatiliaji. Kwenye suala hili alilouliza la pili, amekuja ofisini mara kadhaa; na tumekwambia kwamba baada ya kutoa haya maelezo, tumetoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera ili akaangalie barabara hiyo ili iweze kutengenezwa yote kwa kiwango cha changarawe. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kyerwa kwamba kazi hiyo itafanyika katika bajeti ya mwaka unaokuja. Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

REA awamu ya kwanza Wilayani Kyerwa ilipita laini kuu na wakapeleka umeme kwenye maeneo ya center. Kwa hiyo vijiji vingi pamoja na vitongoji havijafikiwa na umeme.

Ni lini Serikali itapeleka umeme kwa wale wananchi ambao walipitiwa na laini kuu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali kwamba vijiji vyote vimeingizwa katika mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili na iwapo kuna maeneo ya vijiji ambayo hayajaingizwa basi tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba yanaingizwa na kuhakikisha kwamba vijiji hivyo vinapata Mkandarasi ambaye atafanya na kumaliza kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vitongoji ipo program mpya ambayo inaandaliwa ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote. Ningependa pia kuongeza kwamba wiki moja kabla ya bajeti yetu ya Wizara ya Nishati hapa katika viwanja vya Bunge kwa ridhaa ya Mheshimiwa Spika, tutawaleta Wakandarasi wote nchi nzima na mameneja wote wa TANESCO nchi nzima na waratibu wote wa REA nchi nzima, watakuwepo hapa kwa muda wa siku nne katika viwanja vya Bunge, ambapo Waheshimiwa Wabunge watapata fursa ya kupata majibu ya moja kwa moja kwa Wakandarasi hao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kwamba Serikali imeamua kuajiri waratibu wa miradi ya REA kwa kila Jimbo. Kama inafahamika REA haina watumishi kwenye wilaya kutokana na changamoto za maswali mengi kuhusu maendeleo ya miradi ya REA tumeamua kwamba kila Jimbo kutakuwa na mtu mahsusi wa REA ambaye atakuwa ni kiungo kati ya Wabunge, Wizara, TANESCO na Mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya ajira hiyo yapo Ofisi ya Rais Utumishi, imani yetu ni kwamba kibali kikitoka mapema kabla ya bajeti yetu basi hao watu watakuwepo wakati wa bajeti yetu ili tuwaunganishe na Wabunge, kila Mbunge awe na mtu wake anayemjua ambaye atakuwa anamtuma wakati wowote au anampa taarifa Mheshimiwa Mbunge kuhusu maendeleo ya miradi ya REA na pale panapokwama basi huyo awe kiungo kati ya Wabunge, Halmashauri, REA, TANESCO na Wizara. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Omulushaka Kwenda mpaka Mlongo mkandarasi ameshapatikana tangu mwaka jana, lakini mapaka leo mkataba bado haujasainiwa. Tatizo liko wapi ili mkataba uweze kusainiwa na mkandarasi aweze kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Olumushaka kwenda hadi Mlongo tayari mkandarasi alishapatikana, na hatua ambayo imebaki sasa ni hatua ya kusaini mkataba ili mkandarasi aweze kukabidhiwa site; na tutaanza kujenga kilomita 50, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafsi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi wa Lunyinya – Chanya na Mradi wa Kilela – Rutungu – Lusungiro, miradi hii imesimama kwa muda mrefu kwa sababu mkandarasi hajalipwa. Ni lini mkandarasi atalipwa ili miradi hii iweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi vyote alivyovitaja vina miradi miwili, hii miradi ni kweli tayari imeanza kufanyiwa kazi na malipo yanaendelea kufanyiwa kazi. Tayari fedha zimepatikana wiki iliyopita, baadhi ya wakandarasi tunaanza kuwapunguza, kuwalipa. Hivyo, mkandarasi huyu pia tunatarajia aweze kulipwa fedha yake.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; zao la kahawa limevamiwa na ugonjwa wa mnyauko ambao unaweza ukasababisha zao hili kutoweka zao hili muhimu: -

Je, Serikali imechukua hatua gani za haraka ili kulinda zao hili muhimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; zao la kahawa ni zao la kimkakati lakini bado halijaweza kumnufaisha mkulima ipasavyo: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka masoko mazuri ambayo yatamnufaisha mkulima apate bei nzuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la kwanza, kahawa inaathiriwa na magonjwa makubwa matatu chulebuni, kutu ya majani pamoja na mnyauko fuzari. Mnyauko fuzari ndio umekuwa ni changamoto kubwa sana. Hatua ambazo tumezichukua, kituo chetu cha utafiti wa zao la kahawa TaCRI hivi sasa kinakuja na variety mpya ambayo itakuwa ni himilivu katika magonjwa, hasa ugonjwa huu wa mnyauko fuzari. Pia tumeendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya kufanya palizi ; kwa sababu moja ya changamoto kubwa ni mashamba kuwa machafu, vilevile kung’oa miche yenye changamoto na isipandwe kabla ya miezi sita ndio elimu tumekuwa tukizitoa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mradi wa Kilela, Lutunguru na Isingiro, mradi huu unajengwa kwa awamu mbili, mkandarasi anakaribia kukamilisha awamu ya kwanza. Ni lini Serikali itatangaza awamu ya pili ili mradi huu uweze kukamililka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wataalamu walifika kwenye Kata ya Businde, Bugala, Kibale pamoja na Kikukuru wakapima vijiji vichache ili wananchi waweze kupatiwa maji lakini adha ni kubwa wananchi wanayoipata. Je, Serikali iko tayari kupima vijiji vyote vya kata hizo ili wananchi hawa waweze kupatiwa maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi ule wa kwanza alioutaja unaopita kwenye vijiji vya Kilela, Lutunguru ni kweli awamu ya kwanza umeshakamilika na sasa tunaelekea kwenye usambazaji na tunatarajia mwezi Mei kuweza kuutangaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la pili, maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge ni kweli vijiji vilishapimwa na tayari tunaendelea na utaratibu wa kuona kwamba maeneo haya yote ambayo miundombinu ya maji kuyapitia iko mbali basi tuweze kuchimba visima na tayari tumshukuru Mheshimiwa Rais ile mashine ambayo ilipaswa kufika Mkoa wa Kagera sasa inatarajiwa kutoka Karagwe na kuelekea Kyerwa lakini vile vile vijiji ambavyo havikupimwa tunavitarajia navyo vipimwe viingie kwenye mpango wa kupata maji safi na salama.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya Nkwenda na Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa ina upungufu mkubwa wa watumishi. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi na vifaa tiba ili kuondoa adha wanayoipata wananchi wa Jimbo la Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, katika hawa watumishi 8,070 ambao Serikali itaajiri hivi punde, tutahakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa nayo inapata watumishi hawa. Kwenye vifaa tiba, Serikali ilikuwa imeshatoa shilingi bilioni 34 nchi nzima katika kuhakikisha hospitali hizi za Wilaya zinapata vifaa tiba na tutaangalia pia kama hospitali ya Wilaya ya Kyerwa imo na kama haimo, basi itaingia katika mwaka wa fedha ambao unafuata.
MHE. INNOCENT M. BILAKATWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Zao la kahawa limevamiwa na ugonjwa wa mnyauko.

Je, Serikali iko tayari kuongeza miche yenye ubora ili zao hili muhimu lisije likafutika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa; na katika bajeti yetu ya mwaka 2023/2024 tumeongeza miche kufikia miche milioni 20 ili wakulima waweze kupata miche bora ambayo pia itakuwa na ukinzani wa magonjwa ambayo yanaathiri zao la kahawa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kuendelea kuongeza bajeti kwenye barabara za TARURA Wilayani Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kasoni kwenye Kata ya Nyakatuntu kwenda mpaka Mkuyu Kata ya Kikukuru niliiombea fedha na fedha imeshapatikana.

Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Spika, barabara hii ya Kasoni – Nyakatuntu – Mkuyu kwa maana imetengewa fedha kwenye bajeti hii ambayo tunaanza kuitekeleza tarehe 1 Julai mwaka huu, tutahakikisha kwamba barabara hii inapatiwa mkandarasi haraka ili iweze kuanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, ninapongeza jitihada za Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Bilakwate, kwa maana amekuwa akiifuatilia sana barabara hii na kuhakikisha kwamba inatekelezwa kwa wakati. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tarafa ya Nkwenda ina kituo cha afya kimoja na kituo hiki kimezidiwa na wagonjwa wengi;

Je, ni lini Serikali itajenga kituo ha afya kwenye kata ya Songambele ambako tayari tulishaleta maombi?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Bilakwate linalohusiana na Tarafa ya Nkwenda kuzidiwa; ni adhma ya Serikali kuhakikisha inajenga vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini ikiwemo Jimbo lake lile la Kyerwa. Tutaangalia katika bajeti ya 2023/2024 kama imetengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Kama haikutengwa tutatenga fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025 kadri ambavyo fedha itapatikana.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante; Barabara ya Mugakorongo – Kigalama mpaka Mrongo mkandarasi alishapatikana; ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara ambazo zilitangazwa kwamba zitakuwa zimesainiwa, barabara anayoisema tayari mkandarasi alishapatikana na taratibu zinafanyika kwa ajili ya barabara hiyo, kuanzia upande wa Mrongo. Tunachosubiri sasa hivi ni kufanya signing na kumkabidhi mkandarasi site ili aanze kijenga. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali langu la kwanza, kwenye Wilaya ya Kyerwa tunayo maboma ambayo yanazidi ya miaka 10 mpaka 15. Kwa mfano Kata ya Kimuli kuna boma ambalo linazaidi ya miaka 15 halijakamilishwa na ni nguvu ya wananchi. Kata ya Kikukuru kuna Zahanati ya Omkutembe na yenyewe haijakamilika zaidi ya miaka 10. Je, ni lini Serikali itakamilisha maboma haya ili wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukamililishaji wa maboma ambayo yameanza kujengwa kwa nguvu za wananchi nchini kote na mpaka mwezi Juni mwaka huu jumla maboma elfu moja na sitini na sita Serikali ilikuwa imepeleka fedha yamekamilishwa ujenzi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili linaendelea kwa awamu. Kwa hiyo, ni mhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba maboma haya ya zahanati yenye umri mrefu wa miaka 10 na zaidi yatapewa kipaumbele kwenye bajeti za Serikali. Pia naelekeza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, kwamba Halmashauri hii ya kyerwa watenge pia mapato ya ndani kuhakikisha wanakamilisha majengo haya kwa huduma za wananchi, ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naishukuru Serikali kwa majibu angalau yenye matumaini.

Swali langu la kwanza; barabara ya Rulama -Kanyantama - Ruita mpaka Mabira barabara hii inaunganisha kata nne; Kata ya Kibale, Businde, Kamuli mpaka Mabira na inaunganisha Tarafa mbili na ni muhimu sana kuna wakulima wengi. Ni lini barabara hii itatengewa fedha iweze kutengenezwa ili iweze kupitika kipindi chote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini barabara ya Nkwenda mpaka Mabira itapandishwa hadhi iwe chini ya TANROADS kwa sababu inahitaji fedha nyingi na ni muhimu sana kwa wananchi wa Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bilakwate, kwanza nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako tukufu kumwarifu Mheshimiwa Bilakwate kwamba ombi lake kama mwakilishi wa Wanakyerwa la fedha kwa ajili ya barabara ya Kasoni - Mkuyu tayari pesa hiyo imepatikana na muda si mrefu Mheshimiwa Mbunge mkandarasi atapatikana ili kuingia site na kuanza ujenzi wa barabara hii kama alivyokuwa ameiomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye maswali yake; hii barabara ya Ruhama – Kanywaa – Ntama - Ruhita ambayo inaunga kata nyingine na Kata ya Mabira tayari andiko lilikuwa limewasilishwa na Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera lilishawasilishwa Makao Makuu ya TARURA na walikuwa wameomba shilingi milioni 700 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri ya upatikanaji wa fedha TARURA itapeleka fedha katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili barabara ya Nkwenda inayokwenda Mabira kupandishwa hadhi na kuwa barabara ya TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kisheria ziko wazi, ni lazima wao wenyewe katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa waanze na vikao vyao ikiwemo DCC ikitoka DCC waipeleke katika RCC halafu kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa na baada ya Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wanawasilisha ombi lile kwenda kwa Waziri mwenye dhamana ya barabara yaani Waziri wa Ujenzi ndipo barabara hiyo iweze kupandishwa hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naomba niwaase waanze mchakato huo kwa ajili ya kuwasilisha kwenda kwa Waziri wa Ujenzi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mrushaka kwenda mpaka Mrongo ilikuwa isainiwe tarehe 24 Agosti, lakini haikusainiwa ni lini barabara hii itasainiwa kwa umuhimu wa wananchi wa Kyerwa na Karagwe? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, wajina wangu na jirani yangu kule Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mara tu Mheshimiwa Rais, aliponiamini na kunileta Wizara hii, moja ya simu niliyoipata ilikuwa ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate akiulizia barabara hii. Nikamwahidi kwamba naomba awe na subira, niape kwanza halafu nitakapokuja ofisini basi tuangalie cha kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge na kwa vile hii barabara inapita Jimbo la Karagwe, nimegundua kwa Waheshimiwa Wabunge wengi ipo mikataba ambayo inasubiria kusainiwa kama hii ya Mheshimiwa Bilakwate, kwa hiyo, hatutowachelewesha. Nimeshamwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kufanya haraka iwezekanavyo ili mikataba hii isainiwe, Wakandarasi waanze hatua za ujenzi wa barabara hizi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba wakulima wanapata soko la uhakika. Lakini inapofika kipindi cha mavuno ya kahawa kumekuwepo na vitendo vya kuwakamata wakulima wanaotoka kata A kwenda kata B kuvuna kahawa kwa kuwanyang’anya kahawa na kutaifisha ile kahawa;
Je, ni nini tamko la Serikali juu ya vitendo hivi ambavyo havifai?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mibuni mingi mkoani Kagera imekauka kwa sababu ya ugonjwa wa mnyauko. Tumeangalia kwenye bajeti tumetengewa mibuni (miche ya kahawa) michache;

Je, Serikali iko tayari kuongeza miche mingine ya kahawai li kukidhi mahitaji ya wakulima wa Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikubaliki na hairuhusiwi kumkamata mkulima mwenye mazao yake anayoyatoa sehemu moja Kwenda sehemu nyingine ndani ya Wilaya husika, isipokuwa kama mkulima anayatoa shambani kupeleka kwenye AMCOS kwa ajili ya Kwenda kufanya aggregation hapo ni makosa kumkamata. Vile vile kama kuna mfanyabiashara ambaye pia na yeye anatoa mazao hayo kutoka kwenye AMCOS kupeleka kwenye viwanda lazima tuhakikishe awe ana nyaraka ambayo inamruhusu ili kuondokana na usumbufu. Lakini katika ujumla wake Serikali haiwezi kuwa sehemu ya kuzuia maendeleo ya mkulima; na ninatoa maelekezo katika uongozi wa maeneo husika kuhakikisha kwamba wanawalinda wakulima na wasiwanyanyase wakulima katika mazao ambayo wanayalima wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kuhusu mibuni. Ni kweli mibuni mingi hivi sasa imeshatimiza zaidi ya miaka 25 na kimsingi imezeeka na inapunguza sana uzalishaji. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa maana ya TaCRI pamoja na Bodi ya Kahawa tunaendelea na uzalishaji wa miche ya kahawa. Mwaka huu tumeendelea kuzalisha miche 20,000,000. Vilevile tutaongeza uzalishaji wa kahawa kupitia teknolojia ya chupa ili kuongeza wigo mpana zaidi na wakulima waweze kupata miche mingi na kwa uharaka zaidi ili kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nishukuru Serikali kwa majibu yake. Wilaya ya Kyerwa tunayo mapungufu ya watumishi kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya.

Je, lini Serikali itaongeza watumishi kwenye sekta hizo ambazo nimezitaja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuna watumishi 18 ambao wamestaafu mwaka 2018 wakiwemo watendaji wa kata, watumishi hawa mpaka sasa hivi bado hawajalipwa mafao yao. Nini tamko la Serikali juu ya watumishi hawa kulipwa mafao yao ili na wao waweze kufurahia utumishi ambao wametumikia Taifa hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba Serikali imeendelea kupandisha madaraja watumishi wake pia imeendelea kuajiri watumishi katika maeneo ambayo yanahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapungufu aliyoyaeleza Mheshimiwa Mbunge nataka nimwahidi kwamba Serikali imeendelea kuyashughulikia na kwa mfano katika bajeti iliyopita ya mwaka 2022/2023 vibali vya ajira 30,000 vilitolewa na watumishi wote hawa waliajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka unaofuta wa fedha ambao Bunge lako limetupitishia bajeti yetu tunatarajia kuajiri wafanyakazi au watumishi 45,000. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba Serikali itaendelea kukabiliana na upungufu wa watumishi katika sekta zote zilizomo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anataka kujua juu ya watumishi 18 ambao hawajalipwa mafao. Nataka nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba watumishi hao kama hawajaleta barua katika Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi basi barua zao zifike haraka na kama wameshazileta baada ya hapa naomba nipate taarifa zaidi ili niweze kuyafatilia.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Wizara tayari imeanza kutumia Mto Kagera kuwapatia wananchi wa Kyerwa maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali, Mradi wa Maji wa Kata ya Kimuli ambao unapeleka kwenye vijiji vitatu tayari umeanza, lakini mkanadarasi haendi vizuri kwa sababu bado hajalipwa pesa ya certificate ya kwanza; je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi huyu ili wananchi wa Kata ya Kimuli waanze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongezi kwa sababu kazi inayofanyika ni kwa sababu ya ufuatiliaji wake makini, na kuhusiana na malipo ya mkadarasi Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara tunaendelea na michakato ya kuona wakandarasi wote tunakwenda kuwalipa kwa sababu ni wengi wako kwenye maandalizi ya malipo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kata ya Itela ina zahanati mbili; Itera pamoja na Chanya. Zahanati hizi zimekamilika kila kitu lakini bado hazijasajiliwa. Ni lini zitasajiliwa ili wananchi waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Tarafa ya Nkwenda ina kata saba na ina kituo kimoja cha afya na ina zaidi ya wakazi 150,000; na msongamano umekuwa mkubwa katika kituo kile cha afya, lakini tulileta ombi Wizarani la kujenga kituo kingine cha afya katika Kata ya Songambele: Je, ni lini Serikali italeta pesa ili tuweze kujenga kituo cha afya ili kuondoa msongamano uliopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hizo zahanati mbili ambazo zimekamilika katika eneo la Itera ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliainisha, nimwakikishie tu kwamba zipo katika mchakato wa usajili na usajili utakapokamilika manake na sisi tutapeleka wahudumu ili zianze kutoa huduma. Kwa hiyo, nimwondoe shaka kwenye hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuhusu Tarafa ya Ikwenda ambayo walileta maombi ya kuongezewa kituo cha afya kingine, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba jukumu la kwanza la Serikali ilikuwa ni kuhakikisha tarafa zote tunazipelekea vituo cha afya. Jambo hilo tumelifanya na sasa hivi ujenzi unaendelea. Jukumu la pili la Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye uhitaji kulingana na umbali na ukubwa wa maeneo tutapeleka vilevile vituo vya afya ikiwemo katika Tarafa yake ya Ikwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye bajeti iliyopita tulitengewa fedha kwa ajili ya kujenga Mahakama ya Wilaya ya Kyerwa lakini mpaka sasa Mahakama hiyo haijaanza kujengwa. Ni lini Serikali itaanza ujenzi ili kuondoa adha wanayoipata wananchi wa Wilaya ya Kyerwa.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nipende kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika mpangokazi wa Wizara yangu tulipanga kuanzisha ujenzi wa Mahakama hii, iko kwenye mpango wa 2021/2022. Ninapenda tu kumuahidi kwanza Mheshimiwa Mbunge kwamba baada kikao hiki tutawasiliana kuona kama kuna uhakika wowote mradi huo haujaanza kwa sababu ofisi yangu haijapokea taarifa za kutoanza kwa mradi huu. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye Wilaya Kyerwa mwaka 2020/2021 kwenye bajeti tulitengewa minara saba na Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Kyerwa ukatuahidi minara hiyo itajengwa lakini mpaka leo minara hiyo haijajengwa na wananchi wanaendelea kupata adha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate Mbunge wa Kyerwa Kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nilifika katika kata hizo na katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Vilevile labda nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tunapotangaza tender na mtoa huduma akapatikana maana yake yeye anaingia sasa kwenye kutafuta mkandarasi ambaye anaenda kumjengea minara hiyo. Na sasa tayari watoa huduma washatujulisha kwamba wako katika mchakato wa kuhakikisha kwamba mkandarasi anapatikana kwa ajili ya kwenda kujenga ile minara. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo lakini utekelezaji wa Serikali pale inapoahidi ni lazima ahadi yake itatimizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye bajeti iliyopita tulitengewa fedha kwa ajili ya kujenga Mahakama ya Wilaya ya Kyerwa lakini mpaka sasa Mahakama hiyo haijaanza kujengwa. Ni lini Serikali itaanza ujenzi ili kuondoa adha wanayoipata wananchi wa Wilaya ya Kyerwa.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nipende kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika mpangokazi wa Wizara yangu tulipanga kuanzisha ujenzi wa Mahakama hii, iko kwenye mpango wa 2021/2022. Ninapenda tu kumuahidi kwanza Mheshimiwa Mbunge kwamba baada kikao hiki tutawasiliana kuona kama kuna uhakika wowote mradi huo haujaanza kwa sababu ofisi yangu haijapokea taarifa za kutoanza kwa mradi huu. Ahsante.