Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Innocent Lugha Bashungwa (7 total)

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Kwa miaka mingi sasa Tanzania Investment Bank na TADB imekuwepo ila mchango wake katika kupunguza umaskini haufahamiki zaidi hata kwa Waheshimiwa Wabunge. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Benki za TIB na TADB zinajielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa sababu ndiyo mkataba wa mpango kazi wa maendeleo ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa Benki ya TIB na TADB kama benki za maendeleo ni kutoa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu kwa lengo la kufadhili miradi ya kimkakati. Katika kutimiza azma ya kufadhili miradi ya kimkakati ya kufungua fursa za kiuchumi na kupunguza umaskini, TIB imetoa mikopo katika maeneo yafuatayo:
Mradi wa Maendeleo ya Makazi (Temeke na Kinondoni); Mradi wa Maendeleo ya Miji kupitia NHC; Viwanda vya Kubangua Korosho; maghala; mabomba ya maji; sukari na kilimo cha miwa; kukoboa na kusindika kahawa; kusindika matunda; mifuko ya kuhifadhia mazao; nyaya za umeme; vinu vya pamba na uzalishaji wa mafuta yatokanayo na mbegu za pamba; na mahoteli. TIB umewekeza katika mashirika ya umma kama vile Shirika la Reli (TRL), imeiwezesha TPDC katika mradi wa gesi na kuipatia TANESCO mkopo kwa ajili ya fidia kwa wananchi ili kuweka njia mpya ya kusafirisha umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mwaka jana (2015), TIB imewawezesha Watanzania wengi kupambana na umaskini kwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 550 katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Katika sekta ya kilimo, TIB imewasaidia wananchi wengi kwa kusimamia mikopo iliyotolewa na Serikali kupitia Dirisha la Kilimo inayofikia shilingi bilioni 58.8 hadi mwishoni mwa mwaka 2015. Mikopo hii ilitolewa kupitia makampuni binafsi yapatayo 121, taasisi ndogo ndogo za fedha zipatazo 11 na SACCOs 78.
Mheshimiwa Naibu Spika, TIB pia imetoa mkopo wa shilingi bilioni 489.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 181 ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA na kaya 257,000 zimenufaika na mradi huo. Aidha, vikundi 17 vya wachimbaji wadogo wadogo vimenufaika na mikopo ya jumla ya shilingi bilioni nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya TIB kwa sekta na taasisi mbalimbali imesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira mpya na kuendeleza zilizopo. Pia mikopo ya TIB imetumika kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje kama vile maua, kahawa na dhahabu. Pamoja na Benki ya Kilimo kuchelewa kuanza kutoa mikopo ni wazi kabisa kuwa Benki ya TIB imejielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kama vile Dira ya Taifa (2025), Mpango wa Pili wa Maendeleo na Maendeleo Endelevu 2020 pamoja na Ajenda ya Afrika 2063.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) aliuliza:-
Mpango wa NSSF kutoa mkopo kwa bei nafuu kwa Vyama vya Ushirika ili navyo viweze kutoa mikopo kwa bei nafuu kwa wananchi wa Karagwe ulikuwa mzuri lakini umekabiliwa na changamoto na kero kubwa kwa wananchi waliotozwa sh. 280,000/= kama kigezo cha kupata mikopo hiyo, lakini mpaka sasa wananchi hawajapata mikopo hiyo na Serikai haijatoa maelekezo yoyote juu ya hali hiyo:-
Je, ni nini msimamo wa Serikali kuhusiana na jambo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilianzisha mpango wa kuongeza idadi ya wanachama kutoka sekta isiyo rasmi hasa wakulima ili kuhakikisha wanajiunga na Hifadhi za Jamii. NSSF ilifanya uhamasishaji na wakulima ikiwa ni pamoja na Karagwe wakajiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa hiari na kutakiwa kuchangia kiasi kisichopungua sh. 20,000 kila mwezi na kuweza kupata mafao yanayotolewa na shirika kama vile matibabu, uzazi na hata pensheni ya uzee. Aidha, wakulima walihamasika na kujinga na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuendelea kuchangia kwenye Mfuko hadi kufikisha viwango tofauti kuanzia sh. 120,000 hadi 280,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika NSSF ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanachama wake kama njia mojawapo ya kuwahamasisha wanachama kujiunga na NSSF. Masharti ya kupata mkopo huo ni pamoja na wanachama kuchangia kuanzia miezi sita na kuendelea, kuanzisha SACCOS chini ya Vyama vya Ushirika vilivyosajiliwa na mkopo kutolewa kwa wanachama wa NSSF, Chama cha Ushirika kiwe kimefanyiwa ukaguzi wa hesabu zake na COASCO, uthibitisho wa Mrajisi kuhusu ukomo wa madeni na mkopo uridhiwe na Bodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Vyama vya Ushirika ambavyo vilitimiza masharti haya na kupewa mikopo ni Nkwenda Rural Primary Cooperative Society (RPCS), Kakanja (RPCS), Kikakanya SACCOS, Karongo Agriculture Marketing Cooperative Society (AMCOs) UVIKASA SACCOS, Nguvumali SACCOS. Kwa wanachama ambao wapo kwenye Vyama vya Ushirika ambavyo vilishindwa kutimiza masharti, hawakupewa mikopo, lakini nafasi bado ipo wakitimiza masharti wataendelea kupewa mikopo.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya M. Kikwete aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Karagwe kuwa Mradi wa Maji wa Lwakajunju ambao haukujengwa kama ulivyoahidiwa, lakini Mheshimiwa Rais John P. Magufuli naye aliahidi kwamba mradi huo utatekelezwa:-
Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Maji (Water Sector Development Program), na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) iko katika hatua ya kusanifu mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa Mji wa Karagwe kwa kutumia chanzo cha Ziwa Lwakajunju. Usanifu huu unahusisha pia miradi ya maji kwa miji mingine ya Kyaka, Biharamulo, Chato, Muleba na Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imemwajiri Mhandisi Mshauri, Basler and Hoffman kwa kushirikiana na WILALEX na RWB kwa ajili ya kusanifu miradi ya maji safi katika miji hii. Kazi hii ilianza Januari, 2014 na ilitarajiwa kuwa imekamilika Januari, 2015. Kuchelewa kukamilika kwa usanifu huo, kumetokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati. Kwa sasa, Mhandisi Mshauri, tayari amewasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu na hivi sasa yuko katika hatua ya usanifu wa kina na matajario ni kuwa, kufikia mwishoni mwa mwezi huu tulionao, Juni, 2016 kazi hii itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni kutatuwezesha kujua gharama za utekelezaji wa mradi huu ili kuwezesha taratibu za kutafuta fedha za utekelezaji kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imewasilisha andiko la mradi kwenda Serikali ya India kwa ajili ya kupata mkopo nafuu wa kutekeleza mradi wa ujenzi katika miji 17 ikiwemo mradi wa maji wa Mji wa Kayanga na Umulushaka kutoka Ziwa Lwakajuju.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Wilaya ya Karagwe ina walimu ambao bado wanadai malimbikizo ya mishahara, walimu hawa hupandishwa madaraja bila ya kurekebishiwa mishahara yao kitu ambacho kimekuwa ni kero kubwa kwa walimu wa Karagwe na maeneo mengine nchini.
(a) Je, Serikali inawaambia nini walimu hawa na imefikia wapi kutatua kero zao?
(b) Je, Serikali imefikia wapi katika kuhakikisha Teachers Service Commission (TSC) inapata rasilimali watu na fedha ili iweze kutetea maslahi ya walimu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikilipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya walimu kila mwezi kupitia akaunti zao za benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 30/6/2017 Serikali imelipa kiasi cha shilingi bilioni 14.236 kwa walimu 18,865 kati ya shilingi bilioni 69.461 ilizokuwa ikidaiwa hadi kipindi cha 2015/2016 ambapo walimu 12,284 ni wa shule za msingi na 6,581 ni wa shule za sekondari wakiwemo walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe 105 waliolipwa jumla ya shilingi 110,555,836.70. Serikali itaendelea kuongeza kiasi inacholipa kwa mwezi ili kumaliza kabisa deni hili kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TSC, Serikali imeendelea kuimarisha Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa kuipatia Ofisi za Makao Makuu, Ofisi za Wilaya pamoja na kuipatia samani na watumishi katika ofisi hizo. Kwa mfano, Ofisi ya TSC Wilaya ya Karagwe yupo Katibu wa Wilaya na Maofisa wawili. Katika mwaka huu 2017/2018 TSC imepewa kibali cha nafasi za ajira mpya 26 na mwaka ujao 2018/2019 nafasi 43 endapo Bunge litaridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kukamilisha ikama iliyoidhinishwa inayohitaji watumishi wasiopungua sita na wasiozidi nane kwa kila Wilaya. Hadi Desemba, 2017 TSC imepewa shilingi bilioni 1.247 za matumizi mengine ukiacha mishahara kati ya shilingi bilioni 4.622 zilizotengwa mwaka huu 2017/2018. Bajeti ya mishahara ikijumlishwa na hiyo Bajeti ya Matumizi Mengineyp (OC), TSC kwa mwaka 2017/2018 imetengewa jumla ya shilingi 12,422,291,495.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Kwa muda mrefu wananchi wa Karagwe wamekuwa wakiahidiwa kujengewa Hospitali ya Wilaya na taratibu zote zimekuwa zikifuatwa kupitia Vikao vya Baraza la Madiwani na RCC lakini maombi haya hutupiliwa mbali na TAMISEMI.
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa hospitali hii ambayo pia ipo kwenye ahadi za Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imetenga eneo la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria ili kutekeleza shughuli ya ujenzi. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 imetengwa shilingi milioni 70 kutoka kwenye fedha za mapato ya ndani na shilingi milioni 60 kutoka kwenye ruzuku ya miradi ya maendeleo (CDG).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeweka kipaumbele na kutenga shilingi milioni mia moja ili kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo endapo Bunge litaridhia maombi hayo. Chanzo cha fedha hizo ni mapato ya ndani shilingi milioni 50 na shilingi milioni 50 zitatokana na ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
NSSF ilikuwa na mpango wa kutoa mikopo kwa Vyama vya Ushirika ili viweze kukopesha wanachama wake. Kwa upande wa Karagwe wananchi walitozwa michango ya kujiunga na NSSF lakini hawajapata mikopo hiyo.
(a) Je, ni lini NSSF itatoa hiyo mikopo nafuu?
(b) Je, ni kwa nini wananchi wanailalamikia NSSF kwa muda mrefu lakini hakuna majibu yanayotolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilianzisha Mpango wa NSSF Hiari kwa ajili ya kuwawezesha wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Wakulima (AMCOS) na Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) kujiunga na hifadhi ya jamii. Mpango huu ulilenga kila mwanachama kuchangia kiasi cha shilingi 20,000 kwa mwezi ili aweze kupata mafao ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kuvutia wanachama kujiunga na mpango huu, shirika lilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa mwanachama aliyechangia mizei sita na kuendelea kupitia SACCOS na AMCOS zao. Utaratibu huu haukuwa endelevu kutokana na wanachama kutokurejesha mikopo, kutokuendelea kuchangia na vyama vya ushirika kutokidhi matakwa ya kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limepitia upya utaratibu wa kutoa mikopo kupitia Vyama vya Ushirika na kuja na utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo utakaoshirikisha Benki ya Azania. Utaratibu huu utaanza rasmi tarehe 1 Julai, 2017 ambapo wanachama kupitia Vyama vyao vya Ushirika vitakavyokidhi vigezo watapata mikopo kupitia Benki ya Azania.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa juu ya mpango huu wa kujiunga NSSF Hiari na suala zima la mikopo kupitia Vyama vya Ushirika zimekuwa zikitolewa mara kwa mara kupitia ofisi zetu zilizopo nchi nzima ikiwemo Karagwe. Aidha, wanachama kupitia Vyama vya Ushirika watataarifiwa juu ya utaratibu huu mpya wa kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu.
MHE. INNOCENT L. BUSHUNGWA aliuliza:-
Wananchi wa Bushagaro wamekuwa wakitengwa na maeneo mengine wakati wa vipindi vya mvua kwa sababu ya ubovu wa barabara ya Nyakahanga-Chamchuzi, na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 aliahidi ujenzi wa barabara hiyo kwa lami na kuweka kivuko eneo la Chamchuzi:-
(a) Je, ni lini barabara hiyo itatengenezwa na kuwekwa kivuko?
(b) Je, ni lini ahadi ya kujengwa kwa lami kilomita 5 ya kianzio kwa ajili ya kutengeneza eneo korofi la Kajuna Nketo itaanza kama Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alivyoahidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nyakahanga – Chamchuzi (km 97) inahusisha barabara ya Kajura – Nkeito (km 5) na barabara ya Nyakahanga – Nyabionza – Nyakakika (km 92), ambazo ni barabara za Wilaya zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA). Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitenga shilingi milioni 150 kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ili kufanya matengenezo sehemu korofi na kujenga makaravati. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga shilingi milioni 150 ili kuendelea kuifanyia ukarabati barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zake pamoja na ahadi za Viongozi Wakuu wa Taifa zilizotolewa katika nyakati mbalimbali. Utekelezaji wa ahadi hizo unazingatia sera na vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ambavyo ni pamoja na kukamilisha kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa, kuunganisha Tanzania na nchi jirani kwa barabara za lami na ujenzi wa barabara nyingine muhimu, ikiwemo barabara ya Nyakahanga – Chamchuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwekaji wa kivuko eneo la Chamchuzi, Serikali kupitia Wizara yangu itapeleka wataalam eneo la Chamchuzi ili kutafiti katika eneo hilo kuona uwezekano wa kuweka kivuko. Utafiti huo pamoja na mambo mengine, utahusisha kutambua kina cha maji ya mto iwapo kinatosha kuweka kivuko ambacho kitaelea kipindi chote cha mwaka. Mahitaji ya miundombinu yote katika eneo hilo kama vile barabara unganishi na maegesho ya kivuko (ramps) katika pande zote mbili za mto. Uamuzi wa kuweka kivuko katika eneo hilo utategemea matokeo ya utafiti huo.