Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare (7 total)

MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Kufuatia taarifa zilizotolewa na vyombo vya Serikali vinavyohusika na masuala ya utafiti na takwimu, Mkoa wa Kagera ulikuwa miongoni mwa mikoa mitano maskini ya mwisho Kitaifa.
(a) Je, ni mambo gani yametumika kama vigezo vya kuingiza Mkoa wa Kagera katika orodha ya mikoa mitano maskini Kitaifa?
(b) Je, ni jitihada gani za makusudi zinazochukuliwa na Serikali kuunusuru Mkoa wa Kagera na umaskini huo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vilivyotumika katika kubainisha Mikoa na Wilaya maskini ni uwezo wa kaya kukidhi mahitaji ya msingi kama vile chakula chenye kiwango cha kilo kalori 2,200 kwa siku, mavazi na malazi. Kwa kutumia vigezo hivi uchambuzi wa kina wa takwimu zilizotokana na utafiti wa mapato na matumizi katika kaya wa mwaka 2011/2012 na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ulibaini kuwa Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha umaskini wa asilimia 39.3.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kunusuru Mkoa wa Kagera na umaskini, Serikali inafanya jitihada na kuchukua hatua mbalimbali kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama ifuatavyo:-
(i) Kuendeleza maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda kwa kujenga miundombinu ya msingi ili kuwezesha uwekezaji na ukuaji wa viwanda vidogovidogo na vya kati katika Mkoa wa Kagera.
(ii) Kuendelea kuhamasisha wananchi wote ikiwemo Mkoa wa Kagera kutumia fursa na rasilimali mbalimbali zilizopo katika mikoa husika.
(iii) Kuendeleza Sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo, utafiti, na masoko ya mazao.
(iv) Kukuza sekta ya viwanda, hususan vya kusindika mazao ya maliasili, kilimo na uvuvi.
(v) Kuendeleza viwanda vya nyama vilivyopo Kanda ya Ziwa ikiwemo Mkoa wa Kagera, viwanda hivyo vitasaidia kuendeleza ufugaji utakaoinua kipato cha mtu mmojammoja pamoja na kuendeleza uchumi wa mkoa husika.
(vi) Uendelezaji wa viwanda vya nguo katika mikoa inayozalisha pamba ambapo Kagera huzalisha kwa asilimia 2 ya pamba yote katika Ukanda wa Magharibi.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-

Kingo za Ziwa Victoria katika mwambao wa Manispaa ya Bukoba katika maeneo ya Kalobela Bandarini, Hoteli ya Spice, Kiroyela, Nyamukazi na Kifungwa zimelika na maji na mawimbi ya maji kusogea kiasi cha kuingia kwenye nyumba zilizoko kandokando mwa ziwa hilo na kuhatarisha maisha ya watu:-
(a)Je, Serikali inachukuliaje hali hii na inawatolea tamko gani wakazi wa maeneo hayo?
(b)Je, Serikali iko tayari kutafuta mfadhili au kuchukua hatua za kujenga ukuta imara wa kuzuia maji kusogea jambo linalooneka kuhatarisha ofisi za Makao Makuu ya Mkoa, nyumba ya Mkuu wa Mkoa na majengo ya Mahakama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa mmomonyoko katika fukwe za Ziwa Victoria mwambao wa Manispaa ya Bukoba hali inayohatarisha baadhi ya majengo na miundombinu iliyojengwa karibu na maeneo hayo. Hali hii inawezekana kuwa imesababishwa na kuongezeka kwa kina cha maji na kasi ya mawimbi katika Ziwa Victoria kutokana na matukio ya vimbunga, upepo mkali na mvua nyingi yanayohusishwa na mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, hali hii pia yaweza kuwa inasababishwa na uharibifu wa mazingira kando ya ziwa na mito inayoingiza maji ziwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa tamko kwa wakazi wa maeneo ya fukwe za Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini kuacha kufanya shughuli za kudumu za kibinadamu zenye athari kwa mazingira ndani ya eneo la mita 60 kutoka kwenye kingo za ziwa kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004. Hatua hii itasaidia kuzuia uharibifu wa mazingira na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mmomonyoko wa kingo za Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafanya tathmini ya kina ili kutambua chanzo na ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki za kuhimili athari hizo mara baada ya tathmini kufanyika. Ufadhili unaweza kutokana na vyanzo vya ndani, mifuko mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kama vile Adaptation Fund, Least Developed Countries Fund, Green Climate Fund na wadau wengine wa maendeleo.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Mji wa Manispaa ya Bukoba una vijiji ambavyo havina umeme kabisa na havikuingizwa katika mpango wa REA wa kusambaza umeme.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia umeme vijiji vya kata za Nyanga, Ijuganyondo na Kahororo ambavyo mazingira na hali ya kiuchumi haitofautiani na vijiji vilivyosambaziwa umeme katika wilaya nyingine vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Muganyizi Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu umeanza rasmi nchi nzima mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele vya mradi vitatu vya Densification, Grid Extension na Off-Grid Renewable. Mradi huu unalenga kusambaza umeme katika vijiji vyote nchi nzima, vitongoji vyote, taasisi zote za umma na maeneo yote ya pembezoni, ikiwa ni pamoja na visiwa. Mradi wa REA Awamu ya Tatu utakamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO inaendelea na usambazaji wa umeme katika maeneo ya mijini ambayo hayajapata umeme, vikiwemo vijiji vya Kata za Ijuganyundo, Kahororo, Nyanga pamoja na Jimbo zima la Bukoba Mjini. Kazi hii inafanyika mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwa gharama ya shilingi bilioni 22.96.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengine ikiwemo kata ya Nyanga na vijiji vya Hyolo, Kyakailabwa pamoja na Vijiji vingine vya Rubumba, vitapatiwa umeme kupitia umeme wa Urban Electrification Program chini ya TANESCO. Mradi huu unatarajiwa pia kuanza mwaka 2018. Upembuzi yakinifu wa mradi huo umeshakamilika. Mradi utafikisha umeme kwa wateja wote wa awali 469 na utagharimu shilingi bilioni 782.6.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali imepanga kuwalipa fidia Wakazi wa eneo la Kifungwa, Kata ya Kahororo, Manispaa ya Bukoba, ambao ardhi zao na mali iliyomo vilichukuliwa na Serikali miaka miwili iliyopita (12/07/2014) kupisha mradi wa maji taka wa BUWASA?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini. Katika utekelezaji wa miradi hiyo kuna wananchi ambao walitoa maeneo yao ili kupisha miradi ya maji ikiwemo Mradi wa Maji Bukoba. Kabla ya kuanza ujenzi wa mradi Serikali imeweka utaratibu wa kuwalipa fidia kwa mujibu wa Sheria wamiliki wote wa ardhi na mali nyinginezo zitakazoathiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mradi wa Maji Taka Bukoba Serikali kupitia Wizara ya Maji imetuma fedha za fidia katika Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka na Usafi wa Mazingira Bukoba, jumla ya Sh.1,960,000,000/= kwa ajili ya malipo ya fidia katika eneo la Kifungwa, Kata ya Kahororo ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba, 2016 wadai wote 194 walilipwa fedha zao.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Serikali imeamua kuhamisha tozo la kodi ya umiliki wa nyumba kutoka Serikali za Mitaa kwenda TRA na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa mapato na bajeti za Halmashauri nyingi nchini zilizokwishapendekezwa na kupitishwa na vikao vya Halmashauri:-
• Je, Serikali inazipa Halmashauri ushauri gani wa kitaalam wa hatua za kuchukua ili kuziba pengo hilo la kibajeti?
• Kwa kuzingatia uwezo mdogo uliooneshwa na TRA katika kukusanya kodi mbalimbali ambazo wamekuwa wakikusanya kwa mujibu wa sheria. Je, Serikali haioni kwamba uamuzi huu ni kuzidi kuipa TRA mzigo mkubwa ambao hawatauweza?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma na maendeleo kwa wananchi. Hata hivyo, hatua ya Serikali kukasimu jukumu la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa TRA haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali ni kuimarisha ukusanyaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa kwenye ukusanyaji wa kodi ya majengo kwenye Halmashauri zetu. Changamoto hizi zipo pia kwa upande wa matumizi ya mapato hayo yanatokana na kodi ya majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ufanisi katika ukusanyaji na matumizi ya kodi zote zinazokusanywa ndani ya Taifa letu. Aidha, Halmashauri zote zinapata mgawo wa fedha kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yaliyokuwa yakisimamiwa na TRA yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.28 mwaka 2015/2016, hadi bilioni 34.09 kwa mwaka 2016/2017, kipindi ambacho TRA ilianza kukusanya kodi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.6 ya makusanyo halisi yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ongezeko hili la makusanyo linadhihirisha kuwa TRA imefanya vizuri zaidi katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa na Halmashauri hizo 30 katika mwaka wa 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018, TRA ilipangiwa kukusanya kodi ya majengo ya kiasi cha shilingi bilioni 11.9. Hadi kufikia 30 Septemba, 2017, TRA ilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 13.2 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 111. Kwa mwenendo huu wa makusanyo ni wazi kwamba TRA imefanya vizuri kwa sababu ya uzoefu walionao katika kukusanya mapato pamoja na kuwa na mifumo ya kisasa ya kukusanya mapato ikilinganishwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Kufuatia kuzama kwa Meli ya MV Bukoba, kuharibika kwa Meli za MV Victoria na MV Serengeti ambazo zilikuwa zikitoa huduma ya usafirishaji abiria na mizigo kati ya Mwanza na Bukoba kwa gharama nafuu katika Mkoa wa Kagera:-
(a) Je, ni lini Meli za MV Victoria na MV Serengeti zitamalizika kufanyiwa matengenezo yenye viwango vya uhakika ili zianze kutoa huduma?
(b) Je, ni lini ahadi ambazo zilianza kutolewa na Serikali ya Awamu ya Tatu tangu kuzama kwa MV Bukoba za kununuliwa kwa meli mpya zitatelekezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng.ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Muganyizi Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua adha ya usafiri kwa njia ya maji wanayoipata wananchi wa Mwambao wa Ziwa Victoria, hususani wakazi wa Mwanza na Bukoba kutokana na Meli za MV Victoria na MV Serengeti kusitisha kutoa huduma kwa maeneo hayo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uchakavu hasa kwa Meli ya MV Victoria na hitilafu ya mitambo kwa MV Serengeti ilivyovipata vyombo hivyo vya usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilitenga fedha katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ya shilingi bilioni 24.496 kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya mbili na ukarabati wa meli tano za Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) ikiwemo Meli za MV Victoria na MV Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa Meli za MV Victoria na MV Butiama, unatarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya KTMI kutoka nchini Korea ikishirikiana na Yuko’s Enterprises Company Limited wakati wowote kuanzia sasa baada ya kusainiwa kwa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo. Matengenezo haya yanatarajiwa kuchukua miezi kumi tangu kusainiwa kwa mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, zabuni ya ukarabati wa MV Serengeti ilitangazwa tarehe 25 Aprili, 2018 na inatarajiwa kufunguliwa tarehe 24 Mei, 2018. Uchambuzi wa kina utafuata mara baada ya ufunguzi wa zabuni hiyo ili tuweze kumpata mzabuni sahihi mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa meli moja mpya katika Ziwa Victoria, zabuni za kumpata Mkandarasi wa kujenga meli hiyo ziligawanywa kwa makampuni makubwa mbalimbali ya ujenzi wa meli duniani ambapo kampuni zenye uwezo zilionesha nia ya kujenga meli katika Ziwa Victoria kwa vigezo vya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchakato wa kumpata mzabuni, tarehe 10 Aprili, 2018, Kampuni ya STX Engine Company Limited na STX Offshore & Shipbuilding Company Limited Joint Venture zilishinda zabuni ya ujenzi wa meli hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, Serikali na kampuni hizi hazikufikia makubaliano ya mwisho na hivyo kushindwa kutia saini mkataba wa utekelezaji wa mradi na hivyo kulazimika kusitisha zabuni hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitangaza tena zabuni hiyo tarehe 24 Aprili, 2018 na inatarajiwa kufunguliwa tarehe 24 Mei, 2018.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI - (K.n.y MHE. WILFRED M. LWAKATARE) aliuliza:-
Kukua kwa elimu ya uraia na ufahamu wa mambo ya kisiasa kumefanya wananchi wengi kuupokea mfumo wa vyama vingi na kuchagua wawakilishi wengi wa Vyama vya Upinzani kuongoza Kamati za Maendeleo za Kata, Halmashauri za Miji, Miji Midogo, Wilaya, Manispaa, Majiji na Majimbo ya Ubunge na Udiwani:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza kanuni, utaratibu na mfumo wa kutoa elimu na maelekezo kwa watendaji na viongozi wa Kiserikali kuyakubali na kupata ufahamu wa mabadiliko ya kisiasa yanayokua kwa kasi ili kuepusha migogoro na migongano ya usimamizi wa kazi baina ya watendaji wa Serikali na wawakilishi wa wananchi?
(b) Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuwa na uchaguzi huru na haki kama vile Tume Huru ya Uchaguzi na chombo huru cha kusimamia chaguzi za vitongoji, vijiji na mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kwanza uniruhusu nimsahihishe kidogo Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali kwa niaba, huyu Mheshimiwa haitwi Alfred Lwakatare anaitwa Wilfred Lwakatare. Naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji na viongozi wa Serikali wanafanya kazi kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo iliyopo. Ni wajibu wa viongozi na watumishi wote katika ngazi zote za Serikali kuzifahamu nyenzo hizo za kazi ili kuepusha migogoro na migongano baina yao. Serikali imekuwa ikiwaongezea uwezo wa kiutendaji na uongozi watendaji na viongozi wao kupitia mafunzo ya mara kwa mara na vikao vya kazi ili wawahudumie wananchi vizuri na kwa tija zaidi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa husimamia uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa ambao hufanyika ukiwa huru na haki kila baada ya miaka mitano kwa kushirikisha wadau wote wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa ambao hutoa maoni yao kunzia kwenye maandalizi ya uchaguzi.