Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare (19 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. WIFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Unapozungumzia suala la reli ya kati, reli ya kati kwa Kagera haiishii Mwanza. Reli ya kati inaishia katika bandari ya Kemondo ambapo siku za nyuma wakati bado reli inafanya kazi vizuri reli ya kati, tulikuwa na meli ambayo ilikuwa inapakia mabehewa na kuna njia ya reli ambayo inaishia bandari ya Kemondo. Tunapozungumzia reli wananchi wa Kagera, Mheshimiwa Lugola amezungumzia kwa upande wake namna gani ambavyo bidhaa zinavyosafirishwa kwa njia ya barabara zinavyokuwa na bei kubwa zinapofika katika eneo lake. Sasa nazungumza kwake ni tisa, kumi ni Kagera, sisi ndiyo tuliopo pembezoni mwa nchi hii. Cement ni shilingi elfu ishirini na mbili kufikishwa pale Bukoba Mjini na bei hii naamini ni kwa sababu bidhaa ya cement na bidhaa nyinginezo zinasafirishwa kwa njia ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwetu sisi kukosekana kwa reli ya kati kwa wananchi wa Kagera na hususani Bukoba mjini, ni kwamba mipango hii inayopangwa bila kuzingatia kuweka reli, wananchi wa Kagera mnataka waendelee kuwa maskini. Na mimi niseme hivi, umaskini huu unakwenda mpaka kusababisha bei ya kahawa kushuka, kipindi cha nyuma kahawa ilikuwa inasafirishwa kwa reli, yale mabehewa yalikuwa yanayokwenda mpaka Bukoba kupeleka bidhaa pale Kemondo, yanarejesha bidhaa ya kahawa mpaka kwenye bandari zetu tayari kusafirishwa kwenda nchi za nje, kwenye masoko.Usafiri wa barabara wa kusafirisha kahawa umechangia pamoja na sababu nyingine umechangia kushusha bei ya kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe, tunapopanga mipango hii Waheshimiwa, tujitahidi kuangalia kina na kiini cha ni namna gani watu mipango mnayoipanga inashindwa kuwaondoa ndani ya umaskini. Niseme kwa wananchi wa Kagera na Bukoba in particular, tukumbushane hata ahadi zinazofanyika mziweke katika mipango na zitekelezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mkapa katuahidi meli baada ya Mv. Bukoba kuzama; Mheshimiwa Kikwete katuahidi meli, Mheshimiwa Magufuli naye wakati akiomba kura ameahidi meli. Sasa huko mbele tunapokwenda leteni mipango kanyaboya, leteni mipango ambayo haioneshi ahadi zilizopita.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Taarifa!..
MHE. WIFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ili roho yake ipone pamoja na kwamba na yeye amemwita Magufuli basi Rais Magufuli, furahi basi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi, nilikuwa nazungumzia suala la ahadi, tuliahidiwa meli, meli haijaja. Sasa katika uchunguzi wangu tatizo linalotupata katika mipango inayopangwa na Serikali, suala la kutoleta sheria inayopaswa kwenda sambamba na mipango inayoletwa. Matokeo yake hakuna nidhamu ya utekelezaji wa mipango hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata ndani ya Bunge hili, kulikuwa na utaratibu wa kuunda Kamati ya Governance Assurance Commitee, Kamati ya Ahadi za Serikali, hii Kamati naamini ingeweza kusaidia katika suala la kuishinikiza na kuisimamia Serikali kwa ahadi zinazotolewa Ndani ya Bunge hili. Matokeo yake hakuna Kamati hizi. Kwa hiyo, mipango inayopangwa na naamini hata hii mipango inayopangwa, kwa kuwa hatuna sheria, hatuna Kamati inayosimamia hii mipango, huenda hizi ahadi na mipango ikawa hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sheria hizi hazipo na mimi hapa ndiyo maana namuunga mkono Mheshimiwa Warioba katika Katiba ya Warioba ambayo ilikuwa inahitaji Mawaziri wasiwe Wabunge. Kwa sababu tatizo la nchi hii kutokana na kwamba hatusimamiwi na sheria, kila mmoja anayepata nafasi ya kuwa Rais, kuwa Waziri Mkuu, kuwa Waziri, wote wanaanza kukimbilia kuangalia kwao kunahitajika nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ajabu tukaanza kusikia hata mipango mingine zaidi ya Bagamoyo, zaidi ya viwanja vya ndege, zaidi ya kupeleka mabomba ni kwa sababu watu hawasimamiwi, watu mipango inapangwa kufuatana na nani yuko wapi na ana-influence gani na Hazina. That is the problem! Kwa hiyo, niombe sambamba na mipango hii sheria itungwe lakini ile Governance Assurance Committee ifanye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nipo Chuo Kikuu Walimu wangu akiwemo Profesa Baregu, Profesa Mutahaba, Marehemu Profesa Liviga waliwahi kuniambia na kunifundisha kwamba mahala ambapo hakuna good governance hakuna true democracy. Mipango yoyote haiwezi kuenda. Mheshimiwa Mpango naamini na wewe ni msomi unaamini kabisa, najua unaamini kwamba mipango yote unayoipanga kama itakuwa na sokomoko la kutuingiza tena katika mgogoro wa miaka yote mitano kuingia sakata lililokuwepo mwaka 2000 mpaka 2005 kule Zanzibar hakuna mipango itakayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme ndugu zangu sikio lililokufa halisikii dawa. Hawa CCM, kwanza niwashukuru wananchi wa Bukoba Manispaa, waliuthibitishia ulimwengu na Taifa hili na wakathibitishia wengine waliosema wana ushahidi ndani ya dunia hii na mbinguni kwamba Lwakatare ni gaidi. Malipo ya wananchi wa Bukoba waliyoyatoa ni kuhakikisha Lwakatare anashinda kwa kishindo na anakabidhiwa Halmashauri kuja Bungeni hapa. (Makofi)
Sasa niwaambie Makamanda hizi nyimbo, miongozo, taarifa mnaopigwa iwape nguvu ya kukanyaga mafuta ndani ya Bunge. Nilipokuwa likizo nje ya Bunge nilikuwa naona mlikuwa mnaanzia hapo mpaka hapa. Leo tumewasukuma, tumekwenda mpaka pale nawahakikishia Bunge linalokuja mtasogea hivi na wengine watapita njia hii. (Makofi)
Makamanda nilikuwa likizo nje ya Bunge, wananchi huko nje ya Bunge wanatuelewa. Wananchi nje ya Bunge sisi uwanja wetu wa kucheza na watu wanaotushangilia wako nje, hapa wacha washangiliane wenyewe kwa wenyewe. Nawahakikishia Makamanda msirudi nyuma. Mapigo mliyopiga akina Msigwa ndiyo yamezaa leo Halmashauri za kutosha, imezaa Wabunge wa kutosha na 2020 Wallahi na Mtume nawaambia tunachukua Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la Zanzibar CCM mumshukuru Maalim Seif. Maalim Seif uzuri wenyewe anapenda Ikulu lakina ni mtu mfaidhina, ni mtu anaswali swala tano ndiyo bahati yenu, angekuwa kama akina a.k.a Nkurunzinza wallahi pangechimbika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami pia nitumie fursa hii kushukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wote, Mheshimiwa Spika, niwashukuru Wabunge wa CHADEMA na UKAWA pia Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na pia Chama changu na hususan Mjumbe wa Kamati Kuu, Mheshimiwa Lowassa. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Abdallah Bulembo wa CCM, pia taasisi za ndani na nje ya nchi, makampuni mbalimbali, Mabalozi na watu binafsi ambao kwa kweli walitukimbilia katika Mkoa wetu wa Kagera kuweza kutoa misaada mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Waziri Mkuu, pamoja na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ndani ya Bunge, Mwenyekiti wa NCCR pamoja na Mawaziri mbalimbali wa Wizara nyingi ambao walitukimbilia katika Mkoa wetu kwa ajili ya kuangalia kwa karibu lile janga lililotupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako na kupitia kwa Baraza la Mawaziri, Mawaziri waliopo hapa na hususan Waziri Mkuu niombe wamfikishie ujumbe Mheshimiwa Rais kwamba kutofika kwake katika Mkoa wetu na kuangalia majanga na kuhudhuria msiba ambao kimsingi unamhusu sana, niseme kabisa bado haijaingia akilini kwa wananchi wa Kagera. Wengi wanatoa tafsiri nyingi, nyingine huenda ni za kweli, nyingine huenda ni za uwongo, lakini ili kumaliza biashara hiyo na kuweza kuweka wigo vizuri, mimi binafsi nawasilisha kilio hicho cha wananchi wa Kagera, ni vema angefika. Kwa sababu kutofika kwake watu wengine wanafikiri yale majanga ni mepesi, kufika kwa Rais kutaweza kufunua macho watu wengine ambao wanataka kutusaidia sisi kama Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme majanga yale ya Mkoa wa Kagera yaliyotokea ya tetemeko, kama mtu hajafika kule hawezi kujua ukubwa wa tetemeko lile. Ndiyo maana katika mpango huu ninapozungumza hapa kwa niaba ya watu wa Bukoba Town na Mkoa wa Kagera kwa ujumla na hususan niliposoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba yatakayozingatiwa katika kukamilisha mpango na mwongozo ni pamoja na: nachukua kipengele cha kwanza: “Kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango na miradi ya maendeleo”. Kipengele pia cha nne: “Kuchagua miradi michache ya kipaumbele kwa kuzingatia uwezo wa kibajeti.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huo mambo niliyojifunza katika janga la tetemeko la Kagera, ni kwamba kwa kweli mipango yetu haijajiandaa katika kukabiliana na majanga au maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatia aibu kwamba majanga yanatokea kama lile tetemeko halafu Kitengo cha Maafa hakina hata senti tano, kinaanza kutegemea hela ya kuchangiwa na kutembeza kapu, matokeo yake shida haina mwenyewe, haingojei, ni kwamba watu wanatakiwa kupata msaada wa haraka hawapati. Kwa hiyo, ningeomba katika mpango huu nilichojifunza kwa tetemeko la Kagera ni kwamba Serikali ilikuwa haijajipanga na bado haijajipanga kwa sababu matatizo bado ni makubwa kweli. Tuone kwamba janga hili linaweza likatokea wakati wowote na kwa bahati mbaya kama nilivyowahi kueleza huko nyuma na Naibu Waziri wa Fedha akanijibu Mkoa wa Kagera majanga makubwa ya Kimataifa na ya Kitaifa yamekuwa yanaanzia kule, sasa funga kazi imekuja kwenye hili la tetemeko!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Naibu Waziri wa Fedha alikiri kwamba Kagera ina matatizo na ile kuwa maskini kati ya mikoa mitano kuna sababu za kihistoria na tumezijata hapa. Sasa kumeongezeka tetemeko, kwa hiyo hapa kwa kweli hebu jaribuni kusaidia na mpango uje mahsusi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri yeye alinihakikishia kwamba watatuweka kwenye Big Result Now (BRN), Big Result Now ianze kuonekana kwenye mpango wa kutunusuru hili janga la tetemeko. Kwa wataalam ambao wamefika pale na namshukuru Mheshimiwa Mbatia alisema kabisa ili kurudisha uchumi wa Kagera katika mstari wake baada ya janga la tetemeko kunahitajika si chini ya shilingi trilioni mbili, sasa shilingi trilioni mbili siyo hela ya mchezo bila kuiweka katika mpango mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imeelezwa na wataalam kwamba lile janga litachukua zaidi ya miaka 10 kurudi kwenye mstari kama kweli Serikali itakuwa ina mpango mahsusi. Naomba wakati anapo-windup au wakati unapopanga mipango ya kuelekea huko mbele, basi Mkoa wa Kagera uainishiwe kabisa hatua za makusudi ambazo zitachukuliwa ili kutunusu katika umaskini ule uliopita kwa sababu zilizotajwa na hili janga la tetemeko ambalo limetupata hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningeomba kuzungumza ni kwamba, lile tetemeko linahitaji mipango ya short term, medium term na long term. Sasa short term ni hii ambayo imeanza kufanyika ingawa nayo haichukuliwi hatua kwa umakini. Hata hivyo, nianzie kusema kwamba, kuna mambo mengine ambayo nimejifunza yanayoleta matatizo. Kuna matamko yanayokinzana ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali baada ya kuzidiwa na suala la kuwahudumia watu walitoa tamko kwamba michango mingi ambayo ilikuwa inakusanywa chini ya Kamati ya Maafa, walieleza kwamba ile michango itaelekezwa zaidi kukarabati na kurejesha miundombinu pamoja na kukarabati taasisi za umma na wakatoa tamko na clip ninazo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba wakasema watu waanze kusaidiana wenyewe katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali haitakuwa na uwezo, tukalipokea. Baada ya siku mbili nyumbani kwangu kulijaa watu wanamlilia Mbunge, kwamba Mbunge wewe ndiyo mtu wa kwanza kutusaidia zile kura walizonipa zaidi ya 25, 000 si mchezo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge kwa umakini wake akaweka mipango ya kuanza kuwasaidia watu wake nikaandika barua na naiweka kwenye table naomba ije ichukuliwe iwasilishwe, nikaandikia marafiki zangu na sehemu ya wale walionichagua wanisaidie; nashukuru baadhi yao walionisaidia licha ya wapiga kura hata Wabunge bila kujali vyama vyao, hata wa CCM wakaanza kunisaidia na kwa kuogopa hela mimi nisizishike mkononi nikawaelekeza wanunue vitu vinavyohitajika, maturubai ambayo Serikali ilishindwa kuwapa watu wananyeshewa mvua, wanapigwa na baridi, nikawaomba wawape watu wangu mablanketi, wawanunulie kwenye maduka, wanipe vifaa
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu nilichojifunza watendaji wenu mmewatia nidhamu ya woga, watu wana woga sijawahi kuona na nakala ya barua hiyo nikampelekea Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Mkuu wa Mkoa kwa kumweleza utaratibu wangu mimi kama Mbunge ambaye nimeapishwa hapa ndani ya Bunge, kwamba utaratibu wangu wa kuwasaidia watu ni huu, marafiki zangu wanataka kunisaidia, lakini nilishangaa barua hii ikawa ni kigezo eti napelekwa Polisi Lwakatare atafutwe eti ananzisha utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mbunge ambaye nimeapishwa ndani ya jengo hili kwa Katiba, Rais ameapishwa pale uwanja wa Taifa wote kwa Katiba, hivi kama siwezi kuaminika na kukimbiliwa na wananchi wangu nani awakimbilie? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kinacholeta matatizo ni watendaji wenu mmewajaza woga, mnawatumbua bila utaratibu matokeo yake wanashindwa kusimamia hata kazi mnazowapa matokeo yake tunakimbizana huku na huko. Sasa na mipango hii tunayoipanga hapa tusipowaondolea watendaji wetu woga, mipango ya Mheshimiwa Waziri itapwaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuleta maombi maalum kwenye mipango ambayo itapangwa na hili naomba niliwasilishe kupitia hapa, kwanza niseme kabisa nimeombwa na wananchi wangu niliwasilishe hili la kwanza tunaomba sisi kama Kagera tupewe tax holiday kwa kipindi maalum (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni miaka mitano, miaka kumi kwamba bidhaa za ujenzi zipunguzwe bei. Hili jambo si la kwanza, tunakumbuka enzi za Mwalimu wakati tukianza kujenga Makao Makuu Dodoma uliwekwa utaratibu kuwashawishi wafanyabiashara waweze kuja kuwekeza Dodoma na cement ikawa imepunguzwa bei, vifaa vya ujenzi vikapunguzwa bei ili watu wajenge. Katika hili ili kuweka utaratibu mzuri na watu wasichakachue viwanda vilielekezwa kuwekwa alama maalum, nembo maalum. Sasa wananchi wa Kagera tunajua Serikali haiwezi kutujengea sisi wote na janga ni kubwa, tunaomba iwekwe tax holiday kwa bidhaa za ujenzi ili wananchi wajijengee badala ya kubaki ombaomba, hili ni janga kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili wafanyabiashara wameniomba, kuna wafanyabiashara wanaidai Serikali zaidi ya bilioni moja, wamewakopa wametoa huduma mbalimbali za ku-supply hawajalipwa zaidi ya miaka minne. Hawa ndiyo matajiri wetu wa Mji wa Bukoba, ndiyo wenye majumba yaliyoanguka, hawakopesheki tena na kwa bahati mbaya nyumba wanasema haziwekewi bima kwa suala la tetemeko, kwa sababu ni natural disaster. Sasa wamenituma katika suala la kulipa kwenye majanga na wafanyabiashara hao muwaweke kwenye package ya kuwalipa ili hawa watu warudi kwenye reli, vinginevyo wamefilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu kuna watu walikopa kwa kutumia nyumba ambazo zimeteketea tunaomba Mheshimiwa Waziri katika mpango wake alitolee tamko kuzielekeza taasisi na mabenki yaliyokuwa yanawadai wananchi wa Bukoba na Kagera kwa ujumla waliopata janga, nyumba walizoweka kama security zimebomoka, zimeanguka wanafanyaje au mnataka wajinyonge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la misaada inayotolewa, tunaomba misaada inayotolewa kama Serikali imeamua misaada yote kuweka kapuni, hili suala linajaribu kuwazuia na kuwa na walakini kwa wachangiaji wengine, pale mnapochanga kwa mgongo wa waathirika lakini kapu lote linaelekezwa kwenye kujenga taasisi za umma bila kwenda kuwasaidia waathirika wenyewe. Kama mmeamua kufanya hivyo basi watu wasiendelee kujitoa na kuingia mitini kutuchangia tuweke makapu mawili wanaochangia Serikali na wale wanaotangaza kuchangia waathirika wachangie waathirika kuliko kuweka kapu moja vinginevyo watu wanaona mmetumia matetemeko kama chanzo cha mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, tunaomba bajeti ya maafa ieleweke, katika mpango wa Mheshimiwa Waziri suala la maafa ajaribu kulitengea fedha zinazoeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la sita, wananchi wa Kagera wamenituma na bahati nzuri hili suala nilishafika hata kwa Waziri Lukuvi, wanasema mwaka kesho pale Luguruni kuna makampuni mbalimbali toka duniani kote yanakuja kuonesha nyumba za bei nafuu na ambazo ni earthquake proof, nyumba ambazo hazizidi milioni nne mpaka milioni tano.
Tunaomba zoezi hili lianzie Kagera ambako nyumba zaidi ya 3000 zimekwisha, tunaomba nyumba hizi zije na iwekwe mipango mahsusi ambayo inaweza ikazi-attract hizi taasisi mbalimbali kuweza kuanzisha mpango huu ukaonekane Kagera ambako zaidi ya nyumba 4000 zote zimeteketea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya suala la mwisho kabisa, ni kuhusu suala la njaa, Mheshimiwa Bashungwa amezungumzia suala la njaa; Karagwe wanalima na Kyerwa, Muleba wanalima na mikoa mingine wanalima, wanaonunua ni watoto wa Bukoba Town bidhaa zote zinaingia mjini sisi ndio wanunuzi, sasa huko wote wamepigwa na njaa tutanunua nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bukoba kuna njaa na Mkoa mzima wa Kagera una njaa, ukame unatumaliza. Tunaomba Mheshimiwa Waziri katika mipango yake na Waziri wa Kilimo nilisikitika alikwenda Karagwe tu, lakini janga la njaa liko mkoa mzima, tunaomba mipango kabisa ipangwe kabla ya wananchi hawajateketea na bahati mbaya wananchi wa Bukoba Mjini huwaga hatupendi kulialia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kupongeza hotuba nzuri sana aliyotoa Msemaji wa Kambi ya Upinzani, ambayo kusema kweli kama tuna Serikali sikivu, inapaswa itoke hapo kwamba imepata somo na iende iwatendee Watanzania haki. Imekuwa ni mazoea kuchukulia michango ya wapinzani kama mzaha, lakini mwisho wa yote tunaona dublication ya mambo yale yale ambayo tayari yamekuwa yametolewa tahadhari na upande wa Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, akisema sasa zoezi la kubaini watumishi hewa kila mtumishi kuanzia Waziri mpaka chini hakuna shughuli nyingine ni kutafuta watendaji hewa. Tutaendesha hii Serikali kwa decree mpaka lini? Hapa ndiyo umuhimu wa instrument unapokuja.
Mheshimiwa Spika, tulikuwa Dar es Salaam katika ofisi ndogo za Bunge, wakaja wasomi ambao walikuwa wanajaribu kutupa orientation ya namna ya ku-scrutinize bajeti na namna ya kupanga bajeti, niliwauliza kitu kimoja, niliwaambia nchi hii uchumi wake unafanana na uchumi ulioanza kule kwenye nchi za Taiwani, Kuwait, Botswana, Vietnam, Rwanda, Singapore, Malaysia, Hong Kong na nchi nyingine, lakini leo hii hata Vietnam walikuja kuchukua mbegu ya korosho huku sasa hivi ni mzalishaji wa korosho dunia nzima. Nikawauliza hawa wasomi niambie muwe wakweli, hivi tatizo la mipango yenu tangu mwaka 1961 mpaka leo mwaka 2016, mipango yenu hakuna unaotekelezeka kutupa uchumi ambao ni endelevu wenye mashiko. Matatizo ni usomi wenu, vyuo mnavyosoma, walimu wanaowafundisha au matatizo ni yapi?
Mheshimiwa Spika, wale mabwana waliniambia Mheshimiwa Lwakatare wewe yaache tu hayo bwana. Lakini ninachofahamu tatizo ni mfumo, mfumo wa kiutawala hata angekuja malaika mwenye mipango mizuri ya uchumi ukamtumbukiza kwenye Chama cha Mapinduzi, wallah yote inakuwa mguu chini, mguu pande, mna matatizo! CCM ndiyo tatizo, mnawapotosha watu wa mipango yetu, mnawapotosha hata wanasheria.
Mheshimiwa Spika, najua huyu siyo Mwakyembe halali tunayemjua wa Chuo Kikuu, huyu ni wa kutengenezwa, amechongwa kutokana na mfumo uliopo, hawezi kutetea, huwezi kukurupuka, hawezi kuchomoka, hata AG hawezi, CCM is a problem, angekuwa bado babu yupo kule Loliondo tungewapeleka mkapate kikombe cha babu.(Kicheko/Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Lwakatare malizia.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa ikiridhia mikataba na tumekuwa tunaletewa mikataba ya kuridhia na najua itaendelea kuletwa, ningeomba basi tunapoletewa mikataba, tuwe na political will, tuwe na utashi ambao ni wa dhati, na ambao unanuia kuwasaidia Watanzania pindi mikataba hiyo inaporidhiwa.
Mheshimiwa Wenje akiwa Bungeni hapa, aliitanabaisha Serikali madudu gani alikuwa anayafanya Ndugu Kabwe kule Mwanza, ninyi mkaona tu kwamba ni mchezo wa kuigiza, lakini juzi tu Makonda akampandia mtu yule yule na akalalamika kwa Rais na Rais akamfukuzia mtu kwenye jukwaa la shughuli nyingine kabisa ya kuzindua daraja. Jamani kuweni serious na hoja zinazotolewa na Upinzani.
Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu ninaomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, msomi Mwakyembe na AG, kweli mpo pale kwa ajili ya kumsaidia Rais kama wasomi wazuri wa sheria ambao Taifa hili limewaamini mmeteuliwa kwa usomi wenu, mnakaa katika Baraza la Mawaziri kumshauri Rais kwa mambo yanayohusiana na sheria? Inapokuja kutoka kitu ambacho amekizungumza kwa kina Mheshimiwa Lissu ni aibu! Huo ndiyo ukweli maana yake kuna mtu tumbo limemletea shida barabarani akachepuka aende pembeni akaanza kujisitiri kidogo ili tumbo liwe released kidogo, sasa kwa kuwa watu wanapita anajifunika uso anafikiri hawamwoni kumbe mwili wote uko nje.
Mheshimiwa Spika, mambo haya ninaamini ukweli mnaujua, lakini pamoja na usomi wenu mnapotosha mambo maksudi kwa sababu ya hulka za kisiasa. Matokeo yake Rais mnamuweka katika matatizo makubwa, mnamweka katika tension ya ajabu, mpaka juzi, kwenye sherehe za walimu anasema anajuta kwa nini alivuta fomu, matokeo ni haya! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kama Serikali inaendeshwa, bila instrument, Rais anajikuta maskini anafanya kila kitu. Kuagiza sukari yeye, kuipanga sukari yeye, wakati kuna Waziri mhusika wa shughuli hii, ni kwa sababu watu aliowateua wote kama yeye amejikuta katika mfumo huo, anakwenda kwa decree, ikizungumzwa majipu, kuanzia juu kwa Rais, Waziri Mkuu nani wote, majipu kila mmoja yuko kwenye majipu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mikataba ambayo imewahi kuridhiwa, kuna Mkataba wa nchi za SADC wa Utawala Bora na Uchaguzi wa Kidemokrasia ambao kimsingi pamoja na kusainiwa na viongozi wetu haujawahi kuletwa hapa ndani ya Bunge kuridhiwa.
Mheshimiwa Spika, ninaomba wakati Mheshimiwa Waziri na AG anatoa ufafanuzi, ni lini mnaleta mkataba huu uridhiwe? Najua hamtaki huu mkataba unayozungumzia masuala ya utawala bora na kuchungana katika demokrasia kupiga kura na uchaguzi hamtaki, ndiyo maana mwendelezo wa kuiba kura umeendelea, ndiyo maana matendo yanayofanyika Zanzibar wala hamuoni haya, mnayafanya makusudi kwa sababu ya kisingizio kwamba hamjaridhia mikataba ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaeleze ukweli siyo kwamba Watanzania pamoja na kutowaonesha live nini tunachoongea siyo kwamba hawajui, ninawapongeza Wabunge wote ambao sasa wameamua kutafuta njia mbadala. Sasa hivi ma-group yote yanapata live, mambo yanayoendelea humu, hata CCM kuna ma-group ambayo tunaona na wao wana-post hotuba zao ili watu wajue wanasema nini, huo ndiyo unafiki uliopo humu.
Kwa hiyo, suala la kuzuia habari msifikiri kuzuia live coverage ya tv Watanzania hawapati taarifa!
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Lema Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, kwa kutoa ndani ya roho yake na ndani ya nafsi yake maudhui aliyekuwa ameyatayarisha kwa ajili ya kuwakilisha kambi. Nizungumze suala moja, mimi binafsi sitaki kuunga hoja na napinga kwa nguvu zangu zote mafungu ambayo yameelekezwa kwa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu ya Jeshi la Polisi kutumiwa vibaya wakati wa kipindi cha uchaguzi. Wakati wa uchaguzi Jeshi la Polisi kasoro tu hawavai nguo za green wanavaa kombati za polisi lakini asilimia 100 wanakuwa wametayarishwa kusaidia Chama cha Mapinduzi kushinda uchaguzi, huo ndio ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hiyo kwa mifano hai. Mwaka 2005 nikiwa nagombea pale Bukoba Mjini, Jeshi la Polisi lilitumika kunizuia kukusanya matokeo chini ya mtutu wa bunduki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 Jeshi la Polisi limetumika kusimamia uharamia na kubaka demokrasia ya watu kupiga kura kadri wanavyotaka. Nachukua mfano hai wa kwangu, nimewapa taarifa polisi kwamba Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi amebaka uchaguzi kwa kunyofoa karatasi ndani ya vitabu vya kupigia kura na anazisambaza kwa ajili ya kuhakikisha yule mpinzani wangu anashinda na pia wagombea wa CCM wanashinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini polisi wakakataa kufuatilia suala, lakini vijana makamanda walikuwa wamejipanga tukazifuma hizo kura zilivyokuwa zimepangwa. Nashukuru vituo vya ITV vilifanya kazi nzuri lakini hata mimi na makamanda tuliweza kuzizingira kura zaidi ya 2000 zikiwa zimetayarishwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye masanduku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kubwa ya kura hizo niliziwasilisha mpaka kwa msimamizi wa uchaguzi. Nilitoa taarifa kwa makamanda wa Jeshi la Polisi wote wakazikimbia, lakini msimamizi wa uchaguzi nilihakikisha kwamba nampelekea sehemu ya kura hizo na nikaandika waraka kwenda mpaka Tume. Mpaka leo ninapozungumza Tume haijawahi kuchukua hatua yoyote na hiyo imeonesha jinsi gani wenzetu wa upande wa pili wanashinda uchaguzi, wananyofoa kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wasimamizi wa uchaguzi wanakuwa ndiyo marefa, lakini kumbe ni wachezaji pia. Polisi inajifanya kusimamia lakini na wenyewe wanaongeza namba, wanacheza namba mpaka wachezaji 16 upande mmoja. Kwa kuthibitisha hilo, sehemu ya kura ambazo sikuzikabidhi ni hizi hapa, wasiwe wanatambatamba kwamba, wanashinda uchaguzi wakati kura bandia zipo tuliziteka, hizi hapa zimepigwa tick, mgombea CCM wa Urais na Makamu wake mkizihitaji nitapeleka mezani njoo mchukue. (Makofi/Vigelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa nyingine namuuliza Mkurugenzi, hizi zimetokaje katika mfumo wake? Anakimbia, anakimbia hana maelezo. Kwa hiyo, makamanda ninachowaambia kwa jeshi tulilonalo ,kwa chama tawala tulichonacho wameshazoea vya kunyonga, vya kuchinja hawaviwezi, tutapiga kelele hapa, tutaimbiana ngonjera hawa watu sikio la kufa halisikii dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwaeleza ukweli lililopo makamanda ni kujipanga upya kukabiliana na ngoma inayokuja mwaka 2020. Watakuja vingine hawa kwa wizi wa style nyingine, wanasema wana-style 86. Kwa hiyo, ninachowaomba makamanda hapa ni kutwanga maji kwenye kinu, hawa watu wameshazoea vya kunyonga, vya kuchinja hawaviwezi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona wakati wa uchaguzi, tulikuwa na vituo vyetu vya kuweza ku-tally matokeo katika maeneo mbalimbali, chama kilikuwa kimeandaa vijana wa IT wa kuweza kusema matokeo CCM wakiwa Milimani City na sisi vijana wetu wakiwa katika maeneo mengine, vituo tulivyokuwa tumeviandaa, lakini Jeshi la Polisi limetumika kuwavamia vijana wetu katika maeneo walipokuwa wana-tally kura za uchaguzi, lakini CCM wakaachwa bwelele wakafanya jinsi wanavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu nafikiri huko mbele tunapoelekea hili Jeshi la Polisi ukweli wenyewe tunapopitisha mafungu hapa tunakwenda kuongeza nguvu kuwaelekeza na kupata mafunzo namna ya kubaka demokrasia ya kweli. Hiyo siko tayari kuacha pesa ziende kufanya haramu, Jeshi la Polisi tulilonalo ndugu yangu Kitwanga namfahamu vizuri sana, tena bahati nzuri nilimwona na Shekhe Yahya Simba hawa walikuwa inside brothers kwenye club moja tukiwa Chuo Kikuu, walikuwa vijana safi, wametulia, wenye maadili, naomba maadili hayo basi hebu ajaribu kurekebisha na kunyoosha Jeshi la Polisi, tuwe na jeshi ambalo linajiita polisi jamii lisiwe polisi...?
Polisi CCM. Tunaomba, tunaomba suala hili kama jeshi haliwezi kujirekebisha ni vyema tuanze kujenga hoja, tuanze kukusanya sahihi za Watanzania na tuombe ulimwengu, tuombe Taasisi za Kimataifa zije kusimamia uchaguzi mwaka 2020 badala ya jeshi la namna hii ambalo limebeba sura na taswira ya kubaka demokrasia ni hilo siwezi kukubaliana nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ambalo nataka kuzungumza ni suala la kubambikiana kesi. Makamanda, sisi wengine tunatembea kama wafungwa watarajiwa, kwa sababu ya Jeshi la Polisi kubambikiza kesi, lakini hata hivyo nawashukuru wengine tumejengewa historia ya kusindikizwa na ving’ora kama Rais jambo ambalo hatukulitarajia. Tumejenga dhana, lakini nataka kuomba Jeshi la Polisi lijerekebishe vinginevyo msiufikishe umma, msiwafikishe Watanzania wakaanza kuwa na fikra za kuona wanajipangaje katika majeshi yasiyokuwa rasmi kwa ajili ya kulinda haki yao ya kura wanazozipiga. Hilo litafanyika watalifanya kwa kulazimishwa na hali ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze vijana wa Bukoba wakati namaliza, pamoja na mbinu zote hizo zilizokuwa zimepangwa kuleta Mbunge wa kuchonga lakini vijana walikaba mpaka penalty, vijana wa Bukoba walikaba mpaka penalty na wala hizo dhuluma, hazikuweza kupenya. Makamanda na Watanzania wote nawapa rai, hawa jamaa ni wepesi, ni wepesi kuliko nyama ya utumbo, kama unajipanga hawa jamaa ni wepesi kwelikweli, lakini nawaomba na nyie polisi basi, polisi Mheshimiwa Rais aliwahi kusema kwamba, ukielezwa na wewe changanya...?
Na za kwako, hebu msitumike, msitumike kwa sababu hawa jamaa huko tunakokwenda naamini ICC inakwenda kufanya kazi The Hague, angalia na wewe usiwe miongoni mwa list ambayo itapelekwa The Hague.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo. Naamini kabisa kwamba, katika historia ya bajeti ya Nishati na Madini na hususan katika Mafungu ya Maendeleo Wizara hii imevunja rekodi kwa safari hii. Wamepewa fedha za kutosha, japo kuandikwa katika vitabu ni suala moja, sasa tungojee wakati wa kugawa mafungu haya kwa Wizara hii husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ni kipindi kifupi kilichopita alitembelea Mkoa wetu wa Kagera na sehemu mojawapo alitembelea Manispaa ya Bukoba Town, mojawapo ya kazi ambayo tuliifanya baada ya kuongea naye ni suala la kufikiria kuweza kutupa umeme katika vijiji mji vya Mji wa Bukoba ambavyo kimsingi haviko katika programu ya REA. Naamini Mheshimiwa Waziri anatambua kabisa nyaraka husika zimeshafika kwenye ofisi yake kama alivyohitaji, tunaomba vijiji vya Nyanga, Kitendagulo, Ijuganyondo, Buhembe, Kibeta, Kagondo pamoja na visiwa ambavyo kule Bukoba tunaviita Pemba na Unguja ndogo, bila shaka tunaamini Waziri atatimiza ile azma na matumaini aliyowaachia wananchi wa Bukoba Town kwamba vijiji mji hivi atavitafutia fursa ya kuviingiza katika mpango wa REA. Vijiji hivi pamoja na kuwa katika eneo la mji ni vijiji ambavyo kwa kweli maisha yao ya kila siku ni sawasawa na maeneo mengine ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni suala la mpango mzima wa nishati na vyanzo vyake. Ukisoma kitabu cha bajeti ya Wizara hii kuna vikolokolo vingi ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya kuwa vyanzo vya umeme. Kwa mtizamo wangu, kama walivyokuwa wametangulia kuzungumza wenzangu, Tanzania ina bahati ya kuwa na vyanzo vingi vya nishati, nashauri ni vema tukafikia mahali kama Taifa tukaamua ni chanzo gani tuingize nguvu zetu zote ili tuweze ku-utilize nguvu hiyo kuweza kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaamua kuingia kwenye upande wa umeme unaotokana na makaa ya mawe, basi tuelekeze nguvu na investiment kubwa ielekezwe huko, lakini hii ya kutawanya tawanya nguvu kwenda kwenye vyanzo vingi pamoja na kwamba tunavyo, tunatawanya man power, tunatawanya a concentration ya human resource tuliyonayo katika Wizara hii japo ni chache, kwa hiyo, unakuta Makamishna wanabaki kuzunguka sehemu nyingi na matokeo yake tija inakuwa ni ndogo. Kwa kweli, tufike mahali ambako concentration tunaweza tukaiweka ikawa kubwa kwenye mradi mmoja mkubwa ninajua tunavyo vyanzo ambavyo vinaweza vikatoa umeme wa kutosha kama ni gesi, kama ni makaa ya mawe, kama ni vyanzo vya maji, mimi naamini tuchague badala ya kutawanyatawanya resources na matokeo yake tunabaki tunahangaika na hatupati umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu ni ushauri kwa ndugu zangu wa TANESCO. Kama tumefika mahali ambapo makampuni mengi yana-out source services, nafikiri TANESCO nao kidogo wangechukua ushauri huu kwamba sidhani kama ni mahesabu ya kiuchumi, kama inapigwa simu kutoka Katoro kilomita 60 kutoka Bukoba Town labda kuna hitilafu ndogo imetokea kwenye nguzo kwenye transfoma, hata kwenye nyumba ya mtu, unakuta kikosi cha TANESCO kwa sababu hakijui nini tatizo limetokea wanahama mji mzima na mafundi wake wote wanajazana kwenye gari wanakwenda kilometa 60, kumbe unakuta ni fuse ni kitu kidogo tu kimeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya sekta ambayo tuna watu wamebobea na hawana kazi wana makampuni ambayo yanaweza kujikita katika suala la kuingia katika sekta ya kutoa huduma ya kurekebisha hata shughuli ndogo ndogo basi TANESCO iweze kuwa na authorized agents ambao wanaweza kufanya shughuli ndogo ndogo sawa na makampuni yanavyofanya, kwa mfano, Vodacom kwa M-Pesa, unaweza ukatawanya kwa maajenti wakafanya kazi nzuri tu, tajiri anakaa Afrika ya Kusini au huko Ulaya anakula hela tu, ana-outsource hizi services kwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa nne na ninaamini utakuwa wa mwisho ni kwamba kama nilivyosema Wizara hii imetengewa fedha za kutosha, lakini inanitia wasiwasi binafsi kwamba unapotoa shilingi 1,56,350,669,000 lakini ukatenga OC kwa maana ya ku-supervise hizi pesa shilingi 66,220,848,000 kwamba hii asilimia sita iende ku-supervise asilimia 98 ya bajeti hapa ni mgogoro. Ni sawa na kutaka kupika kilo 1000 za mchele kwa gunia moja la mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunatoa fursa ya kuendelea kutendeka mambo tuliyoyakuta Njombe, nina-declare kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati hii bahati nzuri, kwamba mkandarasi yuko kule kwenye Mradi wa REA, anafanya vitu vya ajabu, anafunga matransfoma ambayo ni mabovu yanalipuka kila siku, anafunga transfoma na anawaambia wanakijiji kwamba hawaruhusiwi kufunga mashine ya unga zaidi ya moja, tunamuuliza supervisor wa TANESCO na bosi wake wa Mkoa anaanza kutueleza alikuwa hajaenda wala hajui kinachoendelea, alikwenda siku Kamati imekwenda, ndiyo na yeye mara ya kwanza anakwenda kule kukagua mradi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maskini yule bwana hawezi kuzungumza ukweli, lakini kwa mafungu ya OC kama hayapo na hii nazungumzia kwa miradi hata mingine ambayo inatengewa mafungu makubwa ya maendeleo, kama fedha za supervision kwa misingi ya OC kwamba anahitaji mafuta, anahitaji gari, gari inaharibika, inahitaji vipuri hawa wakandarasi wataogelea katika kutufanyia mambo ya ajabu kwa fedha hizi chungu mzima mlizozitenga kwa ajili ya maendeleo, hata kama makandarasi watafanya kazi, hawa supervisors wetu kuna uwezekano wa kuwa vibarua wa makandarasi. Wakati wa kwenda kuwasupervised mkandarasi anaweza akamwambia supervisor wake ambaye anatokana na TANESCO hata Wizara anampitia na anamlipia nauli kwenda kum-supervise ili asaini certificate. Hii biashara ina convince rushwa, mazingira haya yana convince hawa watu ku-collaborate hata kufanya hujuma ya aina yoyote. Kwa hiyo, suala la OC ni vizuri pamoja na kwamba najua kuna watu wameshapewa yellow card wakithubutu kuomba OC watapigwa red card. Naomba suala la OC lipatiwe tafsiri sahihi. Tunakubali kwamba kuna wakati linakuwa misused na ubadhilifu unapitia hapo, lakini katika maana halisi wa ku-supervise projects na kusimamia ipasavyo OC ina umaana wake, tusije tukajikuta tumetenga fungu kubwa lisilokuwa na usimamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nilipata bahati ya kwenda Merereni na sikuishia juu tu peke yake, lakini niliingia chini kabisa kwenye mgodi zaidi ya mita 700 na kitu kushuhudia ili nisisimuliwe.
Waheshimiwa Wabunge, kama ni kuibiwa pale Tanzanite sisi tumefungua milango tuibiwe. Mambo yanayofanyika pale, huyu anayejiita mwekezaji ambaye naamini hakuna kitu ambacho ameshawekeza tangu akabidhiwe huo mgodi ni kwamba tutaendelea kuibiwa na kuibiwa na kuibiwa, na hata hawa wawekezaji wazalendo waliowekwa pale inaonekana wale watu ni watu wa deal tu. Wale ni third part wanategeategea kuchukua mzigo. Mbaya zaidi kama nilivyowaeleza suala la kutokuwa na fedha ya ku- supervise, niliwakuta kule chini wale vijana wa TMAA wanaopaswa kufanya kazi ya auditing ya madini yanayochimbwa kule, naamini ni njaa ya kutopelekewa hela ya kuishi, wale unawaona moja kwa moja wana njaa na wamechoka kuliko kawaida. Sasa unaanza kujiuliza…..
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nitumie fursa hii pamoja na majanga na madhara yote ambayo tumeyapa Mkoa wa Kagera lakini niupongeze Mkoa wa Kagera na hususani Walimu wetu wa Mkoa wa Kagera wa shule za sekondari kwa Mkoa wa Kagera kujitokeza kuwa Mkoa wa tatu kwa matokeo mazuri Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, niipongeze Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ikiongozwa na kijana wa mvuto na mnato Chief Kalumuna kama Mstahiki Meya kwa kuongoza Baraza, Halmashauri, Walimu na shule za sekondari kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ninapotoka mimi ku-appear kama namba moja Kitaifa katika matokeo ya form four. Naomba ushirikiano ambao tunao pale Bukoba Mjini bila kujali itikadi zetu za kisiasa, sisi tukipiga mzigo tunapiga mzigo kweli kweli na matokeo yake tumeyaona kwa matokeo ya mwaka huu, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, katika Mpango wa Maendeleo ulioletwa mwaka jana hapa, nilizungumza kwa kina kabisa matatizo ya Mkoa wetu wa Kagera na majanga ambayo tumeyapata na ya kihistoria ambayo yanasababisha mkoa ule kuwekwa katika orodha ya mikoa maskini. Japo matukio hayo ambayo yanatuathiri wananchi wa Mkoa wa Kagera yamegeuzwa sasa kama utani na majina mengine kutumika kama kututania japo ni majina ya kihistoria tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali kama Serikali na kupitia katika bajeti na mipango ambayo inaletwa na imesomwa hapa na Kamati, ni kazi ya Serikali kusimamia…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lwakatare majina gani umesema?
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Majina?
MWENYEKITI: Ndiyo.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Haya. Mwenyekiti ametaka kujua majina ambayo ni ya kihistoria na nafikiri watu wamekuwa wanayatumia vibaya majina kama Mto Ngono, Katerero, hayo ni majina tu ambayo yana historia yake. Kwa hiyo, naomba watu wanayoyatumia wanione niwaeleze umaana wake wasiyatumie vinginevyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi ya Serikali kuangalia ustawi wa watu wake. Sisi wananchi wa Kagera na hususani Bukoba Manispaa ninapotoka Mwenyezi Mungu alipotuweka kule kijiografia na tukaumbwa kukaa katika nchi ya Tanzania badala ya Uganda hatukukaa kule kwa bahati mbaya. Serikali inapaswa itambue umbali wa kutoka kwenye centre ya maamuzi na sehemu kubwa ya kiuchumi kama Dar es Salaam na tukawa Bukoba, Serikali inapopanga mipango yake lazima izingatie suala la cost and price standardization katika baadhi ya mambo ambayo yanaweza yakatusaidia sisi kama Watanzania na kama Watanzania wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kwamba baada ya tetemeko kumejitokeza tatizo la watu kupata malazi na kujenga upya nyumba, ni suala ambalo Serikali inapaswa ilizingatie katika mipango yake. Mama Ghasia na Kamati nzima kwa ujumla nawaomba tunapokwenda kwenye bajeti ya mwaka huu bila kuli-address suala la Kagera na matatizo ambayo tumeyapata na nimesikitika pamoja na kwamba tumekuwa tunalizungumza na Mheshimiwa Conchesta na jana amezungumza, inapokuja wakati wa majumuisho sijasikia mtu anayelizungumza hili lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi wa Kagera hatutaacha kulizungumza kwa sababu tetemeko limeacha limetusambaratisha, uchumi umeparaganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria mtu ambaye wamechangishana wakajenga nyumba kwa miaka saba anaishi na familia yake, leo tetemeko la sekunde tatu linasambaratisha kila kitu maana yake ni kusambaratisha uchumi wa familia na ukoo kwa ujumla. Sasa tunapokuja kutaniana na naomba Mheshimiwa Msigwa ambaye ni Mwandishi Mkuu wa Mheshimiwa Rais pale Ikulu awe anatusaidia kutoa matamko kwamba safari hii Rais alikuwa anatania au safari hii Rais yuko serious. Hata leo nilisikia Rais wa Chama cha Wanasheria akihojiwa akasema aah, aah Rais alipowaeleza Majaji na Mawakili kwamba kuna Majaji ambao wanatetea wahalifu alikuwa anatania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba labda kuwe kunatolewa matamko kwamba Rais hapa anatania, hapa yuko serious kwa sababu mahali pengine utani mwingine unakuwa wa ukweli. Mfano pale alipotamka kwamba magari na pikipiki zikipita kwenye barabara ya mwendokasi zing‟olewe matairi na Mapolisi wakaamka wameng‟oa matairi ya pikipiki zote. Hata tulipoelezwa akina Lwakatare twende tukajenge Kiwanda cha Mabati ili tukauze mabati kwa Sh.1000, sijui Rais alikuwa anatania au alikuwa serious? Kwa hiyo, kama Rais alikuwa hatanii katika mipango ya bajeti tuanze na suala hili la cost and price standardization kwa vifaa vya ujenzi vinavyokwenda Kagera kama imeshindikana katika kuangalia policy na taxation kupunguza bei ya vifaa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari inalimwa Kagera lakini inauzwa Sh. 2,000, Sh. 2,200 hata pale pale Bukoba pamoja na kuwa kiwanda kipo kilometa 20 kutoka Bukoba Mjini lakini bei ni ile ile inayouzwa sukari Singida au Kahama ni kwa sababu ya standardization ya price. Vilevile TBL wanauza bia Sh. 2,500, Sh. 2,000 au Sh.1,500 hapa Dodoma na bei hiyo hiyo unaikuta Bukoba, kwa nini suala la cement, nondo, mabati ishindikane? Kwa nini Serikali kupitia kwenye bajeti na mipango thabiti isiliangalie suala hili ili wananchi wa Kagera kama ambavyo ni Watanzania wenzenu tukaweza kurudisha uchumi wa Wanakagera na makazi, tukajenga nyumba zetu kwani sasa hivi hali ni mbaya, nalieleza hili lieleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtakapokuwa mnajumuisha na hasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba asipotezee kama ambavyo mmekuwa mnapotezea hamtujibu watu wa Kagera, mnatusadiaje suala hili katika mipango ya bajeti kwa sababu hali ni mbaya. Nalieleza hili na nitaendelea kulieleza kusudi lieleweke na hiyo ni sehemu ya kazi ya Serikali kuangalia wananchi wake wanapata malazi, chakula na mavazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tetemeko kutokana na uchumi kuparaganyika, Mkoa wa Kagera unategemea kupata njaa ndani ya mwezi Machi, hili tunalizungumza kwa uwazi, kutakuwepo na njaa. Natoa ilani hiyo acheni kutuletea takwimu ambazo ni za imaginations. Waheshimiwa njaa haina bouncer, tunaomba kabisa kabla janga hili halijaukumba Mkoa wa Kagera na hususani wananchi wa Bukoba Mjini ambao tunanunua ndizi kutoka Karagwe kwa Mheshimiwa Innocent, ndizi Mheshimiwa Innocent atawaambia, hakuna ndizi Muleba, hakuna ndizi Karagwe, wananchi wa Bukoba Mjini ambao sisi huwa tunatembeza mchuzi kununua ndizi, tuko katika hatari ya njaa na sasa hivi bei za vyakula zinapanda kama vile hazina akili nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba mtakapokuwa mnajumuisha hapa hebu toeni tamko mmejipangaje kutusaidia wananchi wa Kagera katika suala hili na hasa katika kuhuisha mfumo utakaowawezesha watu wapate vifaa kwa bei ya chini kwa sababu hali ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kagera nafikiri watanisikia Lwakatare hapa jembe lao nazungumza tena kwamba hali ni mbaya. Serikali itusikilize, iache kuja kututania mambo ya Katerero, mambo ya ngono hayatusaidii, sisi tuna shida. Wanaotaka Katerero waje tutawafundisha kijiji kipo, huo utaalam tutawafundisha. Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Kwanza kabisa nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi wa Mkoa wa Kagera na hususan Bukoba Town ambao majuzi usiku wa kuamkia tarehe 30 Aprili waliweza kupata tena mshutuko wa tetemeko ambalo tunamshukuru Mungu kwamba tetemeko hilo halikuweza kuleta athari kubwa zaidi ya kuongeza nyufa katika nyumba ambazo zilikwishapata nyufa pamoja na kuangusha kuta ambazo watu waliambiwa waanze kujenga wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichoweza kuwaombia ni kwamba nawaomba wawe watulivu na kuondoa hofu huku wakisubiri ripoti ya wataalam ambao tumeahidiwa kwamba watakwenda huko na hasa baada ya hoja yangu humu ndani ya Bunge na Mheshimiwa Waziri Muhongo kuweka kalenda kwamba timu hiyo itakwenda kule tarehe 17 kuweza kuwasilisha ripoti, pamoja na hayo amefanya uugwana ametanguliza advance party ya kufanya maandalizi na kuwaondoa watu hofu katika Mji wa Bukoba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tetemeko ambalo lilitupiga mnamo tarehe 9 Oktoba, 2016 liliacha athari kubwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake watambue kabisa kwamba zahanati nne pamoja na vituo vya afya viwili vilisambaratishwa kabisa. Baada ya Mheshimiwa Rais kutembelea Mkoa wetu na mji wetu na akavunja ile Kamati akitumia usemi kwamba hata kamati za harusi huwa zikakuwa na mwisho wake, jukumu la kuendelea kupokea michango na kuendeleza kazi zilizokuwa zinaendelea liliachwa kwenye kitengo cha maafa husika ambacho kiko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo shughuli nzima za Kamati ya Maafa zinasitishwa tayari vituo hivi kamati ilikuwa imeitengea shilingi milioni 380 kwa ajili ya ukarabati, tayari kwa zahanati za Buhembe pamoja na Rwamishenye tayari matofali yalishasombwa na kuwekwa pale, lakini tangu Rais alivyotoa maagizo yake na Kamati ile ikasitishwa kazi yake na shughuli zikarudishwa kwenye kitengo husika, ni kwamba zaidi ya matofali hakuna ambacho kimeendelea hadi hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati hizo pamoja na kituo cha afya bado viko katika hali ile ile, nitaomba Mheshimiwa Waziri aliangalile hili ili wananchi wa Bukoba Mjini waweze kutendewa haki na Serikali yao. Jamani hatujiombei maafa hili naomba litambulike, ni tatizo tu la kuwa katika mkondo wa majanga ya Kimataifa ndiyo kitu kinachotuletea matatizo. (Makofi)

Kwa hiyo, tutaomba kabisa Mheshimiwa Waziri unapohitimisha ulijue hilo na kama unatenga mafungu yaende yakasaidie kwa kazi ambayo haikuweza kukamilika mtusaidie wananchi wa Bukoba. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, pili natambua kabisa ni utaratibu na sera ya Serikali na hasa na mwenzangu alizungumza hii ni Ilani la Chama cha Mapinduzi kwamba kila Wilaya inapaswa kuwa na hospitali ambayo ni ya ngazi ya Wilaya.

Katika Mji wa Bukoba tayari hospitali hii ilishaanza kujengwa jengo kubwa la ghorofa moja, lakini jengo hilo limeendelea kutumika kama OPD kwa sababu hospitali hii ya Manispaa haina theatre, haina pharmacy, haina jengo la utawala wala haina majengo ya madaktari; yaani ni jengo hilo moja tu. Huko nyuma kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika bajeti, tulielekezwa kuwasilisha maombi maalum ambayo tuliahidiwa kupewa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuendelea kuimarisha hospitali hii ya Wilaya. Nasikitika kuzungumza kwamba mpaka dakika hii fedha hizo hazijawahi kuletwa.(Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, mwaka huu nimeona kabisa katika mafungu ambayo yananuiwa kuelekezwa huko ni bilioni mbili tena. Naomba safari hii Serikali itutimizie haki hiyo ituletee fedha hizo na ikiwezekana iongeze fungu ili jamani wananchi wa Bukoba Mjini muwaangalie kwa jicho la huruma kabisa. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Mkoa wa Kagera na Hospitali yetu ya Mkoa kwa utaratibu unaoeleweka ndani ya Wizara ile ni Hospitali ya Rufaa. Nitaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie na Watanzania wote wajue kupitia hili, hivi hospitali inapoitwa Hospitali ya Rufaa tunaomba kujua ipaswa kuwa na sifa zipi? Maneno tu ya kuita Hospitali ya Rufaa isiwe ni kigezo ya kuwa rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka huko nyuma hata Serikali iliwahi kuingia kwenye mtego huo kila taasisi ikawa inageuzwa Chuo Kikuu, lakini baadaye Serikali ilikuja kujitafakari zaidi ikaondoa utaratibu huo.

Mheshimwa Mwenyekiti, nafikiri suala hili la Hospitali ya Rufaa inabidi tulitendee haki sawa na huduma inayopaswa kutolewa kama hospitali za rufaa. Sidhani kama suluhisho la timu kuifunga timu nyingine ni kupanua magoli, nafikiri suluhisho huwa ni kufundisha soko ndiyo unapata magoli kupanua magoli sidhani kama ndiyo solution ya kujua kama timu inaweza kucheza mpira. (Makofi/Kicheko)

Mheshimwa Mwenyekiti, ninaomba wakati wa maafa ya tetemeko yalipotokea kupitia kwa Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya kamati ya maafa na wananchi wa Mkoa wa Kagera, aliomba at least CT-Scan kwa sababu wakati wa athari za tetemeko wagonjwa wengi waliopata athari ilibidi wapelekwe Bugando, Mwanza, kwa sababu ya kukosa baadhi ya vipimo. Tunaomba hiyo ahadi tuliyoahidiwa kwamba Hospitali ya Mkoa italetewa CT-Scan kwa njia ya dharura, nitaomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hotuba yako usingoje tuende kwenye mafungu kuzibiana mishahara, hii ahadi ya CT-Scan mnatuletea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi umeona tena tetemeko lingine, hivi mnataka tuwe wageni wa nani kama Serikali inatuahidi, haitekelezi kile ambacho imekuwa imetuahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wakati unahitimisha hotuba yako hili suala ulizungumzie ili wananchi wa Kagera na Mji wa Bukoba kwa ujumla waweze kupata hope na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa lisemwalo lipo kama halipo linakuja. Mheshimiwa Waziri akina mama wanaojifungua wameanza kuwa na wasiwasi kwa baadhi ya matukio yanayotokea bila Wizara au Mamlaka husika kutoa taarifa za haraka au kutoa statements.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Temeke inasemekana kuna mama mmoja alijifungua mapacha halafu pacha mmoja akayeyuka kinamna namna, mambo haya yamewahi kuwa reported kwamba kuna vitendo vya kuiba watoto. Kuna wafanyakzi wanafanya deal la kuiba watoto wanaozaliwa. Tutaomba kupitia kwako hebu waondoe akina mama wasiwasi wanaojifungua, warudishe imani na hospitali zetu, waache kujifungulia vichochoroni kwa sababu ya kukwepa kwamba wataibiwa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napongeza hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Komu, Waziri wetu Kivuli, lakini pia napongeza hotuba au mchango uliotolewa na dada yangu, Mheshimiwa Riziki pamoja na Mheshimiwa Mwaifunga pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Kivuli, Mheshimiwa Cecil Mwambe.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwelekeza ndugu yangu, Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Kingu, ajaribu kuchukua hotuba ya Upinzani ukurasa wa 42 na 43 atajua namna gani brain ya Oppostion ilivyo. Hili ndilo tatizo, kwamba watu wengine wanasoma hivi vitabu kwa kutumia miwani ya mbao. Hilo ndilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba watu wote wenye vitabu vya rangi hii; na kaka yangu Mheshimiwa Mwijage, asome vizuri hotuba ya Upinzani pamoja na Kamati ya Viwanda na Biashara, zitamusaidia sana. Acha maneno ya sound hizi nyingine zinazotoka kwingine…

KUHUSU UTARATIBU. . .

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naamini bado dakika zangu tisa zilizokuwa zimebaki, ziko palepale. Matatizo yote haya nafikiri ambulance zitatoa watu roho hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua wazi kabisa, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage, Waziri wa Wizara hii; Wizara hii ndiyo mlezi wa wafanyabiashara, ni mlezi wa watu wanaotaka kufanya biashara, ni mlezi wa watu wanaotaka kukuza biashara, ni mlezi wa watu wanaotaka kuweka mitaji katika biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mahali huwa najiuliza kwamba wakati wa vikao vya cabinet kama kweli Mawaziri mnamsaidia Mheshimiwa Rais inavyopasa. Kwa sababu pale inapokuja kutokea kila Wizara kuendesha operesheni zake kivyake vyake bila coordination kuonekana kama Serikali inafanya kazi, mimi huwa nachanganyikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunapozungumza, wafanyabiashara wakijua fika kwamba Wizara hii ndiyo mlezi, wanakamatiwa mali, wengine wanakamatiwa magari yakiwa barabarani, eti kwa sababu kuna gari ambayo imesimama miaka sita haijalipa road license.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kituko kimemgusa Msukuma mmoja alikuwa amepakia samaki anatoka Mwanza anakwenda Dar es Salaam, akasimamishwa na Maaskari gari likapelekwa kituoni. Msukuma akalia akasema kwamba pesa niliyonayo yote imemalizika katika kusafirisha; niko tayari kulipa faini pindi nitakapofikisha mzigo wangu mahali unapokwenda, lakini walimng’ang’ania na samaki wakaoza akaenda kupaki hiyo gari katika kituo. Hii ukiangalia kwa undani ni kukosa busara na akili ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Wizara kama mlezi mama wa wafanyabiashara, naomba ichukue jukumu lake kama mlezi wa wafanyabiashara. Hivi sasa mazingira siyo rafiki kwa wafanyabiashara. Policies zinabadilika badilika, haieleweki! Yaani siku hizi watu wanakaa kwenye TV na redio, hawajui kiongozi akiwa kwenye ziara atazungumza kitu gani. Lolote linaweza likabadilika! Policies zinabadilika! Wafanyabiashara hawako tayari kuwekeza kwenye mazingira ambayo hayaeleweki kwamba leo na kesho itakwendaje? Naomba hili mliangalie sana. Play role ya kulea wafanyabiashara, mazingira yawe rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Bukoba, wafanyabiashara, wajasiriamali waliowekeza kwenye mashine za unga, TFDA wamekwenda pale na kufunga biashara ya kusaga unga kwa sababu tu wanataka watu wajenge ma-godown au wajenge nyumba kubwa za kuweka mashine kwa kutumia matofali.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli hiyo imesababisha Bukoba Mjini unga umepanda bei kwa sababu ya maamuzi ya mtu mmoja tu. Ukienda Halmashauri, wale wafanyabiashara wanashindwa kujenga hayo ma-godown kwa sababu hawajapata vibali toka Halmashauri ambayo ni owner wa eneo hilo. Sasa unakuta maamuzi ya mtu mmoja tu yanakuwa tatizo kwa watu wengi na mazingira yanakuwa siyo rafiki kwa wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Mwijage, watu wangu wa Kashai, Soko Kuu, Rwamishenye, pale sokoni Kibeta Uswahilini wanataka awaeleze, pesa iko wapi? Pesa imekwenda wapi? Mzunguko wa pesa mbona mbaya? Mtu anapanga nyanya mshumaa, ntongo, yaani inaanza ikiwa Azam, inabadilika rangi inakuwa Yanga, mwisho inakuwa Simba na matokeo yake hakuna anayeinunua ntongo tena. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanataka kujua pesa inakwenda wapi, mbona kodi wanalipa? Nitaomba kwa lugha nyepesi awaeleze wafanyabiashara pesa imekwenda wapi? Inafungiwa wapi? Kufuli gani hili? Ni kubwa kiasi gani linafungia hela? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yupo kiongozi mmoja aliwahi kusema kweli kwamba jero itaitwa mia tano; buku itaitwa 1,000; na mtu mwenye kifua cha kukaa Dar es Salaam kama atavuka mwezi wa Saba, basi huyo ni mwanaume. Nafikiri huko ndiko tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, benki sasa hivi zinashindwa hata kukopesha, hata uwe na nyumba yenye hati, kwa sababu hata zile watu walizokopesha kwa kutumia collateral za nyumba, haziuziki; benki zinashindwa hata kuziuza. Pesa haizunguki! Pesa haipo!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwijage, akija hapo mbele atueleze, pesa iko wapi? Watu wafanyaje? Waipatie wapi? Waifukuzie wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wa Bukoba walio-supply taasisi za Serikali wanadai mpaka sasa hivi zaidi ya shilingi milioni 900 kuelekea shilingi bilioni moja; na kwa bahati mbaya wafanyabiashara hawa, wengi ndiyo wale waliokuwa na nyumba zilizopigwa na tetemeko. Sasa walitarajia hata kale kadogo kalikochangwa na wadau angalau wangekatiwa kidogo. Sasa hivi ni maskini, hawawezi kukopa kwa sababu hawana collateral, nyumba zina nyufa lakini pia hawawezi kukopeshana kwa sababu hela iko mikononi mwa taasisi za Serikali, hazijawalipa, wanafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, pia atambue Bukoba imepigwa tetemeko la mwezi wa Kumi; juzi hapa limepiga lingine, mafuriko yamepita! Nashukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo atakwenda Bukoba na wataalam wake kuweza kutoa ripoti ya athari ya tetemeko na aina ya miamba, uchunguzi wao. Hiyo itakuwa ni taarifa ya kuhusu tabia za miamba ili tuweze ku-project watu wa Bukoba kwamba wanaweza kujenga nyumba za namna gani? Tuletewe michoro ya Japan, ya Australia, ya Paris ili tupewe ushauri wa nyumba za namna gani zinazoweza kuhimili matetemeko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, huyo ni Mheshimiwa Profesa Muhongo, nampongeza sana. Kwa upande wa Mheshimiwa Mwijage, hizi athari za wafanyabiashara ambao sasa, yaani kwanza Bukoba imeshakuwa dangerous zone… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kushiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lwakatare, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hatuwezi kuendelea kukaa hapa tunaambiwa Wizara inakusanya, watu wanafungiwa maduka kwa kudaiwa kodi, watu wanafunga biashara kwa kulemewa mizigo, wanataka kukamuliwa huku hakuna mashudu, maziwa sijui yatoke wapi, wakati Waziri na Timu zake na vyombo vyake wanakusanyia kwenye pakacha linalovuja. Ukweli wenyewe tunapigwa mno, tunakusanyia kwenye pakacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi juzi inaripotiwa kwamba kuna mtumishi wa TAKUKURU amepiga ile mbaya, hebu Waheshimiwa Wabunge fikirieni vyombo ambavyo Mheshimiwa Rais amezungumza kwamba sasa anaviamini, vyombo vya ulinzi na usalama ndiyo vimsaidie kudhibiti mapato na mianya ya rushwa, TAKUKURU anakuwa ndiyo mpigaji mkubwa, hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri anapokuja hapa kuhitimisha atueleze yeye na timu yake sasa kwa awamu hii wamejipangaje kuzuia pakacha hili linavyovuja vinginevyo watu wanakatishwa tamaa na wanapata hofu, tunawaonea watu kwa kuwatoza kodi inayokwenda kuvuja, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kila Kamati ya Bunge iliyokuja hapa na Mawaziri wengi waliokuja hapa wanalalamika bajeti haitoshi yaani kwa maana nyingine Mheshimiwa Mpango na Naibu wake shemeji yangu, kwa lugha nyepesi ya Mheshimiwa Rais wanatuletea bajeti hewa, hizi ni bajeti hewa yaani watu wanapewa eight percent ya bajeti yao ambayo sisi kama Wabunge tunakuja kukaa hapa Madaktari, Profesa na watu wa kada mbalimbali mnakuja mnapitisha 100 kwa 100, mwisho wa siku ripoti inakuja kwamba mnapitisha eight percent maana yake ni kwamba hata performance ya Serikali ni eight percent katika eneo hilo husika, tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa akija hapa atueleze tunamalizianaje, hizi bajeti hewa, bajeti hewa ya safari hii iwe ya mwisho, hatutaki tena bajeti hewa. Tunataka apange mambo machache yanayoendana na kile anachokusanya, asijipangie mambo mengi akawapa watu kiu kumbe wanaishia kunawa kula hawali, hilo haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumza kwamba wawape pesa kwa muda mchache uliobaki, ukitoa pesa mwishoni ni sawa na una gari la V8 unaweka mafuta ukiongeza speed ikaanza 200 ujue valve zimefunguka zinakunywa mafuta ile mbaya, sasa hii pesa ya kutolewa mwishoni, zinapigwa hatutaki mchezo huo. Pesa zitoke kwa ratiba ambayo imepangwa na kwa muda husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wafanyabiashara wa Bukoba Town, nimekuwa napiga kelele hapa, Mheshimiwa tutataka Marshall Plan ya Bukoba – Kagera, tumeumia sana na shemeji yangu amekuwa anakuja ukweni unapendelea watu waendelee kulala maturubai? Tunataka
Marshall Plan ya Bukoba Town, wafanyabiashara wana madeni hamuwalipi, walipeni basi madeni yao ya ku-supply huduma Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni road license, wadau wanaomba hii road license ya kutoza gari ambalo liko under grounded miaka saba au nane na mbaya zaidi unakamata gari linalotembea lipo kwenye biashara eti mpaka lile deni la gari ambalo lipo garage liligongwa au lilianguka lilipiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba utaratibu huo ubadilishwe hata kama ni kuweka kwenye mafuta bora road license iwekwe kwenye mafuta, kwa njia hiyo hutalipata gari linalotembea kwa sababu limekwenda kunywa mafuta na tutakuwa tumemalizana kuliko kuwaonea watu, watu wanakamatiwa vyombo vyao, watu wanashindwa kuelewa na imekuwa ni chanzo cha rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sitaki kugongewa kengele, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Kwanza niseme kabisa natambua Jimbo langu la Bukoba Mjini pamoja na pale Kyerwa angalau kupewa fedha za kupanua hospitali yetu 1.5 billion shillings, inabidi nitambue hilo na ninalipongeza. Najua hatua hii itapunguza idadi kubwa ya wagonjwa ambao wanatibiwa kwenye Hospitali ya Rufaa pale Bukoba Mjini, sasa angalau itapatikana alternative.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye ukurasa wa 103 kifungu namba 179 cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amezungumzia huduma na malezi kwa ajili ya watoto wachanga na zile care centres. Sasa niseme, lipo tatizo la vituo hivi na siyo kwa Jimbo langu, nafikiri ni kwa Tanzania nzima, kwa utaratibu uliopo hivi sasa na kwa Bukoba Town, ni kwamba wale Maafisa wa Ustawi wa Jamii walitoa barua ambayo ilivifunga vile vituo. Ile barua kwa sababu waliandika kwa shinikizo baada ya kutiwa ndani na vyombo vya dola, waliamua vituo vifungwe siku hiyo hiyo wakati waliposhinikizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati wakivifunga wanarejea sheria ambayo kimsingi ipo, kwamba ili kufungua hizi centres lazima uwe umepata usajili kutoka kwa Kamishna. Tunatambua hiyo sheria, ipo, je, ni kweli inaendana na mazingira halisi ya hivi sasa na watoto tulionao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Waziri katika hotuba yake ametoa takwimu za vituo vilivyopo kwamba mwaka 2017/2018 wamesajili vituo 139; mwaka 2016/2017 vilisajiliwa vituo 270 na hadi sasa viko vituo 1,046 kwa Tanzania nzima. Sasa hii hali haiendani na ukweli kutokana na nini kinachoendelea katika mazingira yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nieleze kwa ufupi. Ni kwamba vituo hivi kwa mujibu wa sheria ili visajiliwe inabidi viwe na walezi wasiopungua 20; mlezi mmoja kwa ratio ya watoto 20, kuwe na first aid kit, kuwe na fire extinguisher, kuwe na vyoo vya mashimo matatu, kuwe na jiko la kupikia uji, kuwe na uzio uliozungushwa kwenye kituo kizima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubali kwamba sheria hii inaweza ika-apply Oysterbay au Mikocheni, lakini kwa mwananchi ambaye yuko Katatolowanzi Bukoba Town, aliyeko Kaororo, aliyeko Nshambia, mimi nasema hiki kitu hakiwezi ku-apply kwa sababu hakiendani na mazingira ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba pamoja na sheria hii, iko sheria inayotambua kabisa kwamba kwenye sehemu ya 12, kwenye masharti mengineyo, kifungu cha 155 kinatambua kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa inaweza kushauriana na Waziri wa masuala ya Ustawi wa Jamii kutoa sheria ndogo ya miongozo kwa kuzingatia mazingira ya eneo lenyewe, lakini maafisa wetu wamekuwa hawajikiti katika masharti haya, wao wanafunga vituo kwa kutegemea kwamba vyote visajiliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nataka kutamka tena kwamba jambo hili kwa size ya nchi yetu na kwa jinsi mwamko ulivyopatikana kwa watu kuanzisha vituo vyao kwa maeneo mbalimbali, hata kwenye Kijiji cha Nkasi vituo vinafunguliwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwa kuipongeza hotuba iliyowasilishwa na Kambi ya Upinzani hapa Bungeni. Kwa bahati mbaya Mheshimiwa Waziri hata leo hayupo na wakati hotuba ile inawasilishwa hakuwepo lakini bahati nzuri kipindi chote Naibu Waziri amekuwepo. Kwa manufaa ya Taifa hili, naomba hiyo hotuba pamoja na kwamba ina kurasa nyingi hebu wajaribuni kuisoma, itawasaidia sana na itasaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujisema mimi mwenyewe kwamba miaka ya 2000 niliwahi kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ndani ya Bunge hili nikiongoza vyama vitano. Kwa hiyo, bajeti zote ambazo zilipita wakati wa kipindi changu nikiwa Kiongozi (KUB) ni bajeti ambazo hata tukienda kutafuta kwenye Hansard, hakuna bajeti hata moja ambayo Wabunge wa CCM hawakuipitisha mia kwa mia, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata nilipokuwa gerezani kwenye kesi feki ya ugaidi kwa kipindi cha miezi kama minne hivi, nampongeza Kamishna wa Magereza aliruhusu nika-own radio nikiwa gerezani na kipindi cha bajeti zilipitishwa kwa maneno matamu kweli na Wabunge wa CCM. Yale maneno haijawahi kutokea, hii ni bajeti ya kihistoria, hii ni bajeti ya kizazi kipya, kwangu mimi ambaye nina experience na Bunge hili chini ya Chama cha Mapinduzi na Serikali yake ni maneno ambayo mimi nayaona ni swaga za kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nadanganya twende tu huko mbele, hakuchi, kutakucha hata hii bajeti utasikia inapigwa mapiku hata bajeti zingine zijazo. Kwa hiyo, kwangu mimi nafikiri mvinyo ni ule ule kinachobadilika ni chupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri atakapokuja ku-wind up na najua atatanguliwa na baadhi ya Mawaziri ambao wako Serikalini kujibu katika maeneo yao, hebu tuambieni wananchi wa Kagera, Bukoba, Kanda ya Ziwa meli ambayo tumekuwa tunaahidiwa tangu MV Bukoba izame na watu wengine bado wamo humo humo ndani ya meli hiyo mpaka leo, inaonekana wapi katika nyaraka hizi, hotuba hii na bajeti hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametaja meli za Nyasa, viwanja vya ndege ambavyo vimekuja baada ya tukio la MV Bukoba na hata lugha ya kuizungumziazungumzia hii meli mpya ambayo tumekuwa tunaahidiwa na Awamu zote za uongozi wa nchi hii chini ya Chama cha Mapinduzi inaanza kueleaelea au kufutikafutika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, badala ya kuelezwa kijuujuu tuelezeni maandalizi ya hiyo meli yako wapi, inakuwa designed wapi, nchi gani na imetengewa hela kutoka wapi? Taarifa hizi zitasaidia wananchi wa Kagera, Bukoba na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kufahamu moja nini kinachoendelea. Kama wametupotezea tu kijuujuu ni bora wakatamka bayana kwamba hamna hela na wala hamna nia ya kutupa meli mpya. Sasa hivi dunia ni kijiji, mimi naamini kuna watu wako nchi nyingine wanaweza kujitolea kutuletea meli wananchi wa Kagera, Bukoba ambao wanatambua mateso tunayoyapata kuliko kuendelea kuuziwa mbuzi kwenye gunia (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kahawa, tumesikia hapa kodi zimeondolewa. Nataka Waziri atakapokuja ku- wind up na kwa kuwa nafahamu hata Waziri wa Kilimo anaweza akachangia katika ku-wind up kwa upande wa Serikali atueleze maana sehemu kubwa ya kodi zilizoondolewa zinawazungumzia watu wa kati na wale ma- processor. Watu wa Kagera na Bukoba Town ambao tuna vijiji vinavyolima kahawa pale greenbelt vijiji vya Kata za Kibete, Kitendagulo, Iduganyongo, Nyanga wanauza kahawa, wawaeleze kilo moja kwa kodi hizi zilizopungua inakwenda kupanda kwa kiasi gani? Hicho ndicho mkulima anachohitaji siyo maneno maneno haya ya jumla jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nakubaliana na nawaunga mkono Waheshimiwa Wabunge waliochangia sana hapa kwamba katika suala la madini na vita ya rasilimali inayoendelea inahitaji uzalendo na mshikamano wetu wote. Hilo naliunga mkono na naweza nikalipigania mimi kama Lwakatare. Hata hivyo, uzalendo ni lazima utengenezewe mazingira. Huwezi kutoka hewani unazungumzia tuwe wazalendo, tuwe na mshikamano, lazima tutengeneze mazingira ambayo yatawezesha, kwanza tuheshimiane humu ndani, tutambuane umuhimu na tuheshimu hoja ambazo ni kinzani kwa nia ya kujifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi maana natoka Kagera mimi Mlangira mimi, sili chakula ambacho ni half cooked, ni kwamba mambo ya kubebeshana maiti ambapo hatujui marehemu kafia wapi tunakuja kubebeshana tu, mimi siko tayari kuibeba hiyo maiti. Tungetaka kutokea kwa viongozi wetu wakuu wawe consistency maana kiongozi anakwenda mahali fulani anasema mimi kwa capacity yangu siwezi kumteua Mpinzani kwenye Serikali yangu, haijapita kipindi anateua Wapinzani. Jamani dunia ni kijiji kuna wenzetu wanatushangaa kwa matamko tunayoyatoa. Hiyo inafanya tunashindwa kuwa na consistency ya matamko ya viongozi wetu na dunia wanashindwa kuelewa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kumalizia nalo, naomba bajeti hii Mheshimiwa Waziri leo yuko Naibu Waziri lakini Serikali iko pale pale, wamwongezee pesa Msajili wa Vyama vya Siasa na iende purposely kwa ajili ya kujenga capacity kwenye vyama vyetu, vyama vinapaswa kujengewa capacity. Chama cha kwanza ambacho kwa kweli kutokana na michango na yale yanayoendelea naona kijengewe capacity ni Chama cha Mapinduzi. Haiwezekani kwa miaka 56 ya Uhuru tunaendesha Serikali kwa individual capacity badala ya taasisi. Matokeo yake Mheshimiwa Rais wamemuachia mzigo ndiye anaendesha Serikali wakati tuna Baraza la Mawaziri hewa, viongozi wa taasisi hewa, Wakurugenzi hewa kwa sababu wote wanakwenda kwa mtindo wa ndiyo mzee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani yanayoonekana sasa hivi na mimi namkubalia Ndugu yangu Mheshimiwa Bwege alisema sasa hivi inayoendesha Serikali ni Serikali ya Magufuli aliyoisema yeye mwenyewe, Watanzania chagueni Serikali ya Magufuli, hakuna Serikali ya CCM hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya hili inazaa suala la watu kujipendekeza, kila mmoja anajipendekeza kwa mtu mmoja anayeendesha Serikali. Msajili akijengee Chama cha Mapinduzi capacity ya kuendesha Serikali kitaasisi. Matokeo yake huyu Rais jamani tutamuua bure, kubeba mizigo ya Wizara zote, taasisi zote, makontena ya madini anatembelea yeye, yeye ndiyo anapanga bajeti, akiamua sijui… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na ningependa kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ndani ya Bunge lako tukufu na niseme tu kwanza awali niwapongeze Waheshimiwa Madiwani wote kwa ujumla wao bila kujali itikadi zao wa Manispaa ya Bukoba kwa kufanya jambo la kihistoria siku ya juzi kwa kupitisha kwa kauli moja, wakapingana na kauli na njama ambazo zimekuwa zinafanywa na Mwenyekiti wa chama tawala, wa CCM kwa kutaka kudumaza mradi kujenga stand ya Bukoba kwa sababu ambazo hazina msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo ambalo ni la kihistoria kwamba sisi Bukoba kwa awamu hii tuliamua kwamba tunaweka siasa pembeni, tunapiga mzigo, wananchi wa Bukoba wanatoka katika historia za malumbano, wanataka mabadiliko ya Bukoba Town. Kwa hiyo, nawapongeza kabisa, kabisa na hususana Mwenyekiti wa caucas ya Madiwani wa CCM Mheshimiwa Richard, Mungu ambariki kwa kuonyesha kwamba sasa Bukoba imebadilika. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nitoe pole kwa vijana wa bodaboda wawili wa Kata ya Kashai ambao wanatokea maeneo ya Kisindi na Kashenye ambao wameuawa kinyama kwa kupigwa visu na mapanga na hivi sasa tunapozungumza hata wahusika hawajakamatwa, suala hili limewarejesha katika kumbukumbu za watu kutolewa koromeo kwa sababu vijana hao wameuawa, pikipiki haikuchukuliwa, pesa hazikuchukuliwa, helmet haikuchukuliwa. Ni jambo ambalo hivi sasa limewafanya vijana kuanza kulala saa mbili na kwamba hivi sasa ikifika saa mbili usiku Bukoba hakuna usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitoe pole kwa familia ya Mzee Kahigi ambaye ameondokewa na mtoto wake ambaye amepigwa risasi na watu wanaojidai kwamba wanaendesha programu au shughuli ya operesheni ya uvuvi haramu, yaani amepigwa risasi na matukio hayo mpaka sasa hivi polisi hawataki kutoa statement rasmi. Sasa masuala kama haya nakumbuka kwa Wizara zilizopita, watu wamezungumzia suala la amani na utulivu lakini Serikali imekuwa inapata kigugumizi kutaka kukubali hata kuleta Scotland squad waje watuambie tatizo liko wapi kwa sababu vyombo vyetu inaonekana vimeshindwa kung’amua matatizo yako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mheshimiwa Mwijage nimelizungumza hili ili na Mheshimiwa Mwigulu alijue, mazingira ambayo ni mema ya kuwekeza yanategemea amani ya mazingira yenyewe, sio kukata leseni peke yake. Pale ambapo Maafisa wa Ubalozi wanatekwa na kunyang’anywa kile walichonacho na kuumizwa ujue taswira mbaya inakwenda kwenye nchi za wenzetu na kwa wawekezaji kwa ujumla wao kiasi kwamba hata wawekezaji wataogopa kuwekeza Tanzania kwa sababu hakuna amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nataka kuzungumzia senene. Senene ni watamu kuliko nyama na ni kitoweo ambacho hivi sasa ni international, ukienda Dubai, London na Washington, sasa hivi senene zinakatiza, wanaliwa na watu wengi, ukienda Tanzania hii kila Mji Mkuu wa Wilaya wa Mkoa machinga hawezi kutengeneza hela kama hajafanya biashara ya senene. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwijage, nimetumwa na wanaumoja wa wauza senene Bukoba Mjini, wanasema hivi; wao hii biashara walianza tangu mwaka 2000 nilipokuwa Mbunge ya kuanza kuuza senene kwamba ni zao, niliwaelekeza kama ni fursa. Ikaanza kuuza Dar es Salaam kwenye mataa na nini sasa imevuka mipaka. Sasa wanasema, wanaomba uwaunganishe na TBS, TFDA, Sokoine University hata na wenzetu wa Ubalozi wa Canada ambao tumeona katika kitabu chako umesema kuna taasisi zinasaidia wajasiriamali wachanga, ili senene sasa kwanza zitangazwe kama ni zao ambalo lina ladha inayolika Tanzania nzima na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili wanataka sasa kuwa na senene ambazo ni standardized ambao wana ladha inayofanana ambayo mtu wa Washington akiwala basi wanafanana na yule aliyeila South Africa.

Kwa hiyo, kwa maneno mengine hizo Taasisi zilizoombwa tunaomba ziende ziwasaidie hawa wajasiriamali wa senene kwamba sasa hili zao wafundishwe namna ya processing, wasaidiwe namna ya packaging kimataifa ili zao hili liendelee kuwa fursa kwa wananchi wa Bukoba na wengine kwenye mikoa ambao wanakuja hawajui namna ya kuwakamata basi watu wa Bukoba watakwenda na kufunga mitambo ya kienyeji iliyoko Bukoba hivi sasa. Sasa viwanda vile vilivyoko Bukoba tunataka mwekezaji apatikane kwa njia yoyote ili aende kwa local industry ambayo imeanzishwa na iboreshwe tuweze kupata viwanda vya kisasa, vya ku-process, ku-pack senene vizuri ili tuanze ku-export kwenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi, watu wanaofanya biashara ya senene, wanajenga, wanasomesha, yaani senene ni product ambayo ni bora kuliko hata kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwijage umekuwa maarufu sana kwa hapa ndani ya Bunge kwa kauli zako kwamba mtu yeyote anayehitaji mwekezaji muonane nje ya Bunge umkabidhi mwekezaji aondoke naye kwenda jimboni. Sasa mimi siondoki kwenye Bunge hili, nitakuomba unipe mwekezaji, awe wa Kichina, wa Kijapani, mimi niende naye tuangalie mikakati ya kukamata senene. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa pointi hiyo usemi wa Kireno unaosema batakusiima kwiluka ukalabauliembo mwanyu. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo maana yake ni kwamba usisifiwe kufanya kazi sana kabla hujaangalia mazingira ambayo yanakuzunguka. Hiyo ndiyo tafsiri, nafikiri ameelewa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. WILFRED M. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, wataalam na Serikali nzima ya Chama cha Mapinduzi kwamba wanapopanga miradi ya kutekelezwa ni vema wakaanza kuchukua dira tofauti na kuangalia dira ya uchaguzi. Miradi mingi inapangwa kwa ku-focus uchaguzi 2020, 2019 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, matokeo yake wanakuwa over ambitious, wanapanga miradi ambayo kiukweli haiwezi kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini nimezunguka katika miradi mbalimbali. Ukimsikiliza Mheshimiwa Waziri humu ndani, lugha anazoongea na wakati akijibu maswali wanazungumzia lugha ya kwamba kila kijiji lazima kiwekewe umeme kwa sera ya REA lakini kwa watu tuliotembea, tuliokwenda kwenye maeneo kukagua miradi unakuta kwenye kijiji ni kitongoji kimoja ndiyo kina umeme na kitongoji chenyewe unakuta ni watu watatu, ni kaya nne au tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningemuomba Mheshimiwa Waziri, ili kutowaweka Wabunge katika sakata baya sana ifikapo wakati wa uchaguzi, wataulizwa maswali huo umeme uko wapi kwa kila kaya, badala yake ningemshauri hii lugha ya kila kijiji ibadilike na kuwa kwamba mahali ambako kutapitishwa umeme au kwenye centre ya maeneo fulani, ili wananchi tuanze kuchukua sera mpya, wananchi waanze kuwekewa mpango wa kuvuta wao wenyewe umeme kutoka sehemu mnazoweka umeme. Hii lugha ya kila kijiji haipo, haitekelezeki, kutokana na kutolewa mafungu machache hiki kitu hakitekelezeki, ni uwongo uliokubuhu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la ulipaji wa wakandarasi. Naipongeza taarifa ya Kamati ya Bunge imezungumza ukweli kwamba, wakandarasi kwa mfano wa Phase III, tangu mwezi Oktoba mpaka leo watu hawajalipwa pesa. Matokeo yake hawa watu wamesaini mikataba ambayo kimsingi baada ya miaka miwili wanapaswa wawe wamemaliza mikataba hii. Tutaomba Mheshimiwa Waziri atueleze ukweli kutokana na ucheleweshwaji wa hawa wakandarasi Serikali inaingia hasara kiasi gani ili tujue upande wa pili wa shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna mdudu huyu ambaye ameingia, mimi namuona kama mdudu. Hili suala linaloitwa uhakiki, malipo mengi ndani ya Serikali yanachelewa kutokana na kuambiwa kuna suala la uhakiki. Hili suala la uhakiki linaanzia REA wanahakiki kivyao, inakuja Wizara inahakiki na Hazina wanahakiki, hivi Serikali gani ambayo hamuaminiani? Kwa nini hamuaminiani? Kwa nini kusiwe na centre moja, kama ni uhakiki ufanyike katika centre moja badala ya centre tatu, matokeo yake miradi inachelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni compensation kwa wananchi. Kwa mfano, katika mradi wa KV 400 wa Singida - Arusha mpaka Namanga, wananchi wamezuiwa kuendeleza maeneo yao kwa sababu pale kutapitishwa mradi, tunajua sheria inazungumzia miezi sita, hawa wananchi sasa hivi ni miaka miwili. Mheshimiwa Waziri tutaomba uwaelezee Wabunge na wananchi wasikie hatima yao ya kulipwa compensation ni nini? Kama miaka imepita, miezi sita imepita, je, watalipwa interest kwa kucheleweshwa au vinginevyo izungumzwe wazi hapa, wananchi waruhusiwe kuendeleza maeneo yao kwa sababu Serikali imeshindwa kufanya compensation na hawajui hatima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni umeme katika vijiji mji. Nashukuru huu mradi umeanza uko Kigamboni na unategemewa kutekelezwa. Naomba kujua katika Vijiji vya Ijuganyondo, Buhembe, Kahororo, Kibeta nini hatima yeke katika suala hili. Mnajua sisi wananchi wa Mjini (Bukoba Town) umeme ni deal, hatuulizii stakabadhi ghalani, hatuulizi pembejeo sisi umeme ndiyo mahala pake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa wale ambao hawanifahamu vizuri, niliwahi kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ndani ya Bunge hili. Nikiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, nilipata bahati kwa miaka mitano kusimamia bajeti mbadala ya Kambi lakini pia kuzisikiliza bajeti mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na Mawaziri wa Fedha na Mipango. Sikuwahi kusikia Waheshimiwa Wabunge na hasa wa upande wa Chama Tawala kwamba kuna Kambi ambayo haikupewa mashadidio kushadidiwa maana siku zote wamekuwa wakisema hii bajeti ni kiboko, haijawahi kutokea, ni funga kazi, ni mwarobaini wa matatizo mpaka bajeti ya mwaka huu wanasema haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mtu kama mimi mzoefu ambaye niliwahi kuwa ndani ya Bunge hili, ni kati ya ma-veteran wachache ambao nilichukua likizo kidogo kwenda kuchungulia wananchi wanaendeleaje halafu nikarudi, maneno haya huwa nayasikiliza kama swaga. Kwa hiyo, hayanipi matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea maneno ya Mheshimiwa Spika juzi juzi hapa wakati hotuba iliposomwa, Mheshimiwa Spika, akasema angetaka maelezo fasaha kutoka kwa Mheshimiwa Mpango kwamba kwa nini bajeti ya Kenya pamoja na idadi ndogo ya watu inakuwa karibu mara mbili ya bajeti yetu? Ni bajeti ambayo uki-combine ya Uganda, Tanzania na Rwanda na vichokochoko vingine, ndio bajeti ya Kenya?

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ni mepesi. Tatizo letu sisi tunafanya business as usual. Halafu naingiwa na wasiwasi, kwa capacity ya watu wetu; capacity ya wataalam, Mawaziri wetu, watu wanaomshauri Mheshimiwa Rais na siyo kwa awamu hii ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ni awamu zote tangu siku za nyuma. Ukiangalia bajeti za miaka ya nyuma, bajeti imekuwa inapanda lakini matatizo kwa nini ni yale yale? Huwa nafika mahali najiuliza, hawa wataalam wetu wanasoma shule gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimewahi kusoma mahali, kuna Profesa mmoja wa nchi ya Norway; nitakapokumbuka citation nitaitafuta, anasema vijana na wasomi wa Kitanzania wanajua sana kukariri vitu ambavyo sometimes siyo lazima wavi-apply, kwa hiyo, ni watu ambao wamebobea kwenye theory. Nilipokuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kulikuwa na mwanafunzi mmoja, ukienda library utakuta amepanga vitabu vinamzidi hata urefu, vingi tu, lakini ukija mtihani akijitahidi sana anaambulia karai. Yule bwana alikuwa anasifika, halafu anabeba vitabu kweli kweli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa mahali ninakokaa, nikajaribu kupanga vitabu ambavyo nimepewa hapa Bungeni, yaani mimi ni mrefu, sasa hivi vimenifika kwenye bega. Watanzania tunajua kuandika, mipango iko kwenye makaratasi, lakini unapokuja kwenye ku-practise pale ndipo tunatofautiana na wenzetu wa Kenya. Hapa tunazungumza mno vitu ambavyo vingine hata yule anayevisema haviamini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa nasikiliza sana, japo huwa sina bahati ya kupata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na huenda nitahama hapa ninapokaa. Huwa nasikiliza linapigwa swali pale unakuja kusikiliza majibu; samahani, kwa mtu kama mimi naona hili jibu ni bora twende, kwamba leo lipite tukutane kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huo, kwa staili hii tunayokwenda nayo, mfumo huu tunaokwenda nao wa kibajeti, kwa sababu ni mfumo ambao unaweza ukau- refer kuanzia miaka ya nyuma, wala siyo awamu hii tu, tunakuwa na bajeti ambazo hazitekelezeki. Tunakuwa na maneno ambayo ni matamu kuyasikiliza, lakini unapokuja kwenye practise hayapo, huwezi ukayapata yote kiasi kwamba nasema hata Mheshimiwa Dkt. Mpango tungekuwa na uwezo wa kumpitishia bajeti ya shilingi trilioni 200, haki ya Mungu kwa utaratibu na mfumo huu, nchi hii hatubadiliki, hatutoki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kenya mtu kuja kuwa Waziri, anachujwa na vitu vingi mno. Kwanza capacity yake yeye mwenyewe, yeye vipi? Mambo aliyonayo kichwani, je, anayaamini? Je, anaweza akayaweka katika vitendo na utekelezaji? Ndipo unampata mtu kweli anayeweza kusimama na maneno ambayo anayazungumza humu. Wengi hapa huwa wakijibu maswali, wakitoa mipango mbalimbali, wakisoma matamko unamwona kabisa huyu mtu ni mwongo yaani unamsoma kabisa ni mwongo yaani hata kile anachokizungumza hakiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba tubadilike, tuanzie hapo, tubadilike. Tuwe na mapinduzi ya kifikra na mapinduzi ya Bunge jipya ambalo linakwenda na hiyo three line whip kwamba ni dhamira ya mtu mwenyewe na ndiyo capacity yake na mitizamo yake na mtazamo wa Chama chake na Taifa lake. Hapa over 95% unakuta ni dhamira ya kichama, that is a major problem, kiasi kwamba mtu anaweza akawa na nondo zake, ni Profesa, Doctor, ana Masters, lakini unamwona kabisa kwa sababu ya dhamira moja kubeba 95% inamsababishia azungumze kitu ambacho hata yeye hakiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza na wananchi wangu wa Bukoba. Kule Bukoba Town tuna ile mialo ya Bakoba, Kahororo na Custom, watu wamezoea miaka yote tangu nizaliwe wanakwenda kuvua samaki kwa kutumia ndoano. Kuna kijana mmoja akanipigia simu jana, akasema Mheshimiwa Lwakatare, hebu tuambie nikiweka ndoana kule niweke na bango kwamba kama huna sentimita 25 usiguse? Nimekosa jibu la kumjibu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tunalolipata, tunapotunga sheria, kwanza naamini sheria nyingi tuna-copy na ku-paste, ni matakwa ya Wazungu. Kwa sababu, Wazungu kwenye viwanda vyao wanataka samaki awe na sentimita 25 au sentimita ngapi, tukija hapa hatutumii hata loophole ya nguvu tulizopewa za kanuni. Naamini kama Mheshimiwa Waziri anaona sheria ni ya jumla sana na haitekelezeki katika mazingira yetu, basi atumie loophole ya Kanuni aweke na vigezo ambavyo vinaendana na maisha yetu ya kila siku na maisha ya watu wetu, lakini tukienda tu, yaani ni gari linakwenda lakini halijui kwamba kuna reverse na kona, haki ya Mungu wataumia wengi. Huu mtindo wa mzigo ufike, punda asife, tuache kuutumia tunawaumiza watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Marehemu Mwalimu Nyerere, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, aliwahi kusema kwamba mtu akikuletea vichupa vilivyosagwa vinang’aa akakwambia kwamba hii ni almasi na anataka uamini kuwa ni almasi, wewe utakuwa ni zuzu yaani ukikubali anaokuona wewe ni zuzu. Mimi huwa ni mtu wa mwisho kutoamini kitu ambacho unaona kabisa dhahiri hakipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Dkt. Mpango weka vitu ambavyo vinatekelezeka kwa elimu yako uliyonayo, usisikilize watu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nitoe pole kwa familia ya Marehemu Mheshimiwa Bilago kwa kuondokewa na mpendwa wao. Pia pole kwa Waheshimiwa Wabunge wote hususan Chama cha CHADEMA. Pia namwomba Mwenyezi Mungu aweze kumsimamia na kuweka mkono wake kwenye operation ya Mheshimiwa Lissu ambayo inasemekana ni ya mwisho ili iweze kufanyika vyema na aweze kupona na kuweza kuungana nasi pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja zangu ni mbili ambazo nimetumwa na wananchi wa Bukoba Town, ambazo kimsingi zinawagusa Watanzania wote kwa ujumla wao. La kwanza ni suala la property tax. Siku chache zilizopita, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye ni shemeji yangu, alitoa ufafanuzi mzuri sana kuhusiana na nyumba ambazo zinapaswa kulipa property tax na categories ambazo zimepangwa.

Mheshimiwa Spika, kuna nyumba ambazo kimsingi, kiutaratibu zilipangiwa kulipa Sh.10,000/= ambazo ni nyumba zilizopo kwenye squatters ambazo ni unsurveyed na nyumba za ghorofa ambazo zipo katika maeneo hayo. Nyumba hizi za squatters ni Sh.10,000/= na nyumba za ghorofa ambazo zipo kwenye sehemu ambazo haziko surveyed na wala hazijafanyiwa evaluation ni Sh.50,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ninayoileta hapa, wananchi wa Bukoba wanaamini wanatapeliwa na TRA, kwa sababu hivi sasa TRA inatoza karibu almost nyumba zaidi ya asilimia 70 za ndani ya Mji wakidai kwamba zimefanyiwa evaluation; wakati utaratibu uliotumika kuzungumzia hicho kiwango ambacho kinasemekana kilifanyiwa evaluation ni kwamba taratibu za Sheria ya Uthamini hazikufuatwa.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba ni watu wameunda kikundi wakawaendea wataalam ndani ya Halmashauri husika. Wanakwenda kwenye nyumba mbalimbali, wao wana-dictate terms wana-dictate zile rates kwamba hii nyumba thamani yake shilingi milioni 50, hii ni
shilingi milioni 100 bila kufuata Sheria ya Uthamini. Kwa hiyo, hivi sasa ni disaster na naamini iko katika maeneo mbalimbali ya miji mbalimbali hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wamebambikiwa rates ambazo siyo sawasawa na thamani ya nyumba; na nyumba zenyewe ziko vichochoroni. Mbaya zaidi tunajua Sheria ya Uthamini lazima iwe shirikishi, aidha na Uongozi ulioko katika eneo hilo la mitaa, eneo ambalo watu wenyewe, wahusika wenye nyumba hizo, wanapaswa washirikishwe, wanapaswa wataarifiwe. Sasa watu wamekuwa wanakutana na bili za TRA wakishangaa zinatoka wapi, kwa sababu wakati wa zoezi la evaluation hawakushirikishwa wala hawajui lilifanyika lini? Kwa hiyo, huu mimi naweza nikausema ni utapeli wa hali ya juu na kwa kweli wananchi wa Bukoba Town wamenituma kwamba wanataka maelezo yenye misingi iliyosimamiwa na Sheria ya Tathmini.

Mheshimiwa Spika, vinginevyo, kwa kuwa kule kuna watafiti wengi, hivi sasa zoezi tunalolifanya, tunakusanya data za nyumba ambazo evaluation imefanyika kinyemela na baada ya kukusanya hizo data tutatafuta ushauri wa hatua gani ya kuchukua na hata ikibidi kuipeleka TRA Mahakamani, kusimamisha zoezi hili mara moja kwa sababu halikufuata utaratibu wa kufanya tathmini.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa nyumba zinazotozwa hela, unakuta mtu ni mzee kabisa amestaafu, anaambiwa ile nyumba ambayo masikini ameijenga katika mazingira magumu kwa hela ya pensheni mtu anaambiwa atoe Sh.150,000/= kwa mwaka, atazitoa wapi? Kuna nyumba watu wengine wamerithi kutoka kwa wazazi wao ambao wameshafariki, unakuta amebaki mjane, wote hao wanatozwa hela kwa rates ambazo kwa kweli ni unaffordable, hawana uwezo wa kuzilipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, namshukuru alitoa majibu ambayo yamesimama vizuri, lakini kwa mazingira ya Bukoba Town ni kwamba lile zoezi la evaluation ambalo wanadai ndiyo linasimamia rates ambazo zinatozwa na TRA, zoezi halikufanyika katika taratibu za kisheria. Namwomba Mheshimiwa Waziri anapo-wind-up azungumzie Bukoba, tutakwenda hivyo au twende na route ya kutafuta haki mbele ya vyombo vingine.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo kimsingi nalo linalalia huko huko, ni kwamba Mheshimiwa Waziri amekuwa katika takwimu zake na katika vyombo vya Habari na taarifa zinazotolewa na TRA kwamba wanakusanya vizuri, hongera kwa hilo. Kwa mtu anayekusanya vizuri, vilevile kuwepo na vielelezo na taswira na mazingira ya kuonesha anakusanya vizuri lakini pia analipa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwa katika bajeti ya Wizara kwa kuwa nimo ndani ya Kamati, kwa nini fedha hazitoki? Mbona Wakandarasi wengi wanadai? Mbona Wakandarasi wanasaini mikataba nje ya wakati? Naomba kabisa Mheshimiwa Mpango, asione haya, pesa inakwenda wapi? Nieleze linalozungumzwa, mimi sina minong’ono, wanasema yeye anabana mno, mpaka penalty. Pesa hazitoki. Zina mlango mmoja wa kuingia, lakini wa kutoka ni mwembamba kama ule tunaoambiwa wa kwenda Mbinguni. Kwa nini pesa haitoki? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifikiria labda hapa tukiwa pamoja na Kambi ya Upinzani na wenzetu wa CCM, kama anatuonea haya, hebu wakiwa kwenye caucus huko wazungumze, wanong’one, kwa nini pesa haitoki? Kwa hiyo, maendeleo ambayo tutaendelea kuyazungumza kimsingi yanakuwa ni maendeleo ya vitu, siyo ya watu. Watu wamechacha ile mbaya, maisha hayatamaniki.

Mheshimiwa Spika, kuna watu wanakula mlo mmoja pamoja na kwamba wengine hawakufunga Ramadhani, lakini inabidi wafunge kwa sababu hela haiko katika mzunguko. Watu wa Bukoba wanauliza hela iko wapi? Hela nyingi inayokusanywa, inakwenda wapi? Naomba atupe majibu hapa. Kama ataona hapa kuna soo, wakikutana huko, najua caucus watakutana, hebu awaeleze Wabunge wenzetu wa CCM hela inakwenda wapi? Mbona matatizo! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili sambamba na hilo kuhusu madeni, nawazungumzia wapiga kura…

TAARIFA . . .

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, nimepokea na kukupongeza kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, nazungumzia specifically madeni ya Wakandarasi wa Mji wa Bukoba na Mkoa wa Kagera ambao wamenituma. Tunazungumzia kwa mfano, Wakandarasi wa Mradi wa REA ambao tunaambiwa mpaka leo wanadai. Kimsingi, bahati nzuri wale Wakandarasi wakubwa wana watu wa kuwazungumzia. Nataka kuzungumzia kwenye local content, niite local content basi ya miradi hii, kwamba kuna ma-supplier wadogo wadogo ambao wanakuwa wanawa-supply hawa Wakandarasi wanaowadai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina ma-supplier zaidi ya 20 hapa ambao wamem-supply contractor aliyekuwa anasimamia na kuendesha mradi wa REA katika Mkoa wa Kagera. Hawa watu wanadai zaidi ya Sh.1,300,000,000/= hawajalipwa. Wengine majuzi Benki zimetangaza kuwafilisi na kunadisha nyumba zao. Kuna mama mmoja alikuwa ana-supply vyakula kwa wafanyakazi wa Kampuni hii, yule mama ameukimbia mkoa kwa sababu ya madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka watueleze haya madeni yanalipwa lini? Kwa sababu yasipolipwa yana-affect hata wengine ambao wapo chini wanao-supply vitu mbalimbali kwa hawa Wakandarasi. Kuna bwana mmoja ambaye mpaka katika kituo chake cha mafuta ameshindwa kununua mafuta mengine kwa sababu alikuwa supplier wa huyu Mkandarasi, anadai mamilioni ya hela.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anapo-wind-up atueleze kwa sababu haya madeni hayawa- affect hawa Wakandarasi wakubwa tu, yanawa-affect hata ma-supplier wadogo ambao kimsingi ndio wapo wengi kule chini. Ndiyo maana circulation ya hela inakuwa haipo na watu wanaishia kwenye umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu ambalo naomba Mheshimiwa alifafanue, ni hiki kitu ambacho kinaitwa uhakiki. Nashangaa na nitaomba kwa kweli nipewe tuition kidogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru, kwanza kabisa katika mchango wangu niungane na watanzania wote na IPP Media kutoa pole kwa kuondokewa na mwekezaji makini na mahiri bwana Dkt. Reginald Mengi, naamini tunapozungumzia pengo, Dkt. Mengi ameacha pengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika historia nafikiri tukichimbua historia ni mtanzania ambaye ameacha rekodi ambayo haijawekwa na mtanzania tangu nchi hii iumbwe katika rekodi tulizonazo. Ni mojawapo ya matajiri, wapo matajiri wanaomzidi fedha lakini moyo wake na nafsi yake imefanya mengi kama jina lake lilivyo. Nathubutu kusema hata kama kuna mabaya ambayo anayo kama binadamu lakini mazuri yanafunika mara mia tano mara elfu moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nipende kupongeza bayana hotuba ya Kambi ya Upinzani na pia hotuba ya Kamati Huduma ya Jamii. Naamini Mheshimiwa Waziri na Msaidizi wake na watendaji wao wakizisoma vizuri hotuba hizi na ushauri uliotolewa nafikiri tutapiga hatua moja kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, napenda tutambue kabisa unapozungumzia afya, unapozungumzia ustawi wa jamii ndio msingi wa shughuli zingine zozote ambazo zinafanywa ndani ya nchi. Ni kama mtu ambaye ninaamini hawezi kuanza kununua tairi kabla hajanunua gari, kununua spear tairi inakuja baada ya kununua gari. Mambo yote yanayofanyika bila Wizara hii bila idara ya Wizara hii kupewa bajeti kadri tunavyozipitisha ndani ya Bunge hili tutakuwa hatuwatendei haki watanzania tunao wawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kila Mbunge anayesimama hapa ambaye amezungumza mapungufu mengi yaliyopo. Hotuba zote mbili za Upinzani pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii zimeeleza hali halisi iliyopo huko. Lakini pia tunaponzungumzia ukosefu wa fedha inasikitisha inapokwenda au inapopelekea kwamba hata pesa zinazopitishwa ndani ya Bunge hili, sasa zinapolewa pungufu kwa kweli inaonekana sisi wenyewe wasimamizi tunaosimamia Serikali au wapishi wetu ambao ndio waliokabidhiwa dhamana ya kuweza kusimamia hii mifuko na hazina fedha ya nchi hii kuna matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukosefu wa bajeti au kutotimilisha bajeti maana yake ni kutotimiza huduma zilizotarajiwa kwa wananchi wetu. Ninaamini huenda na hili ndiyo tatizo ambalo hata ndani ya Manispaa yangu ya Bukoba katika bajeti hii tunayoelekea kuimaliza tulipangiwa 1.5 bilioni kwa ajili ya hospitali yetu inayotakiwa kuwa hospitali ya wilaya ambayo mpaka sasa hivi ina jengo moja tu linalohudumia watu wa OPD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa tunashindwa kuiita hospitali ya wilaya au kituo cha afya, nashindwa kuelewa, sasa kwa kuwa labda imebakia miezi kama miwili hivi, nafikiri Mheshimiwa Ummy atakapokuja na Msaidizi wake mtaniambia labda miezi miwili hii fedha itatoka ili tuwe na hospitali ya Wilaya. Na katika hili nafikiri ifike mahala nchi yetu uwekwe utaratibu kitu gani kinapelekea hospitali iitwe hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Mkoa, Hospitali ya Rufaa, Zahanati, kituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiriki tuchukue hatua tuweke category kama tunataka hospitali iitwe ya Wilaya au ya Rufaa basi iwe imetimiza masharti fulani, iwe na vifaa vya aina fulani, iwe na capacity ya aina fulani isiwe ni majengo tu, kukuta bango ndio hospitali ya Mkoa, hospitali Rufaa X-ray hamna MRI hamna, madaktari hamna. Kwa kweli nafikiri ni ushauri wangu kama yanayofanyika kwenye hoteli, unapojua unakwenda five star unajua utakuta huduma ya aina gani sasa hili lipelekwe hata kwenye hospital zetu vinginevyo tutakuwa tunadanganyana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine niseme kabisa nimnufaika wa NHIF na ninawapongeza sana taasisi hii kwa afya yangu wamekuwa wadau muhimu kwa kuendelea kuwa na afya njema nawapongeza sana wamenihudumia sana. Nimekuwa nahudumiwa vizuri bila shaka kwa sababu bima yangu ni kubwa. Ambayo inaniruhusu kupata matibabu yoyote na weza nikapata madawa yoyote naweza nikapata vipimo vyoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kuwa nimekuwa nahudhuria katika matibabu pia nimegundua wananchi wa kawaida wanavyo kufa. Watu wana kufa si kwa sababu ya kile ambacho tunaambiwa kwamba bwana ametoa na bwana ametwaa. Nafikiri Bwana anatoa lakini wapanga mipango wanatwaa kwa sababu naamini asilimia 95 ya magonjwa yameshafanyiwa research namna ya kutibiwa. Sasa watu wanakufa kwa utapia mlo, watu wana kufa kwa sababu utumbo umejikunja kwa kweli naamini bwana akweli anatoa tunashukuru na tutakuwa jina halihimidiwi bali tunadhihaki jina la Mwenyenzi Mungu tukienda namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya watumishi nafikiri kuna haja ya hata kuweka category tunapojumuisha kwamba watumishi wote wasipandishwe mishahara, watumishi wote wasilipwe pesheni. Lakini naamini kuna kila sababu ya kuwaangalia watumishi wetu wa idara hii, kuna kila sababu tukianzia watu wote, nafikiri mlikwenda shule. Katika shule zetu na vyuo vyetu watu wanaominika kuchimba sana na kubundi ni madaktari, na wanasoma kwa miaka mingi tukiwapeleka jumla jumla na watumishi wengine hatuwatendei haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza watumishi wa Idara ya Afya, miongoni mwa watu wanaokwenda sambamba na kiapo chao ni watu wa sekta hii. Ni watu ambao hata wafanyiwe vituko gani wanakomaa wanatimiza viapo vyao. Hebu fikiria kuna idara, kuna sekta ambayo anaweza akaenda akachakachua cement, kwenye kujenga daraja, lakini hakuna daktari au nesi ambaye ameambiwa akupige dawa ya kiwango fulani akakudunga sindano ambayo inazidi kiwango kile ili ufe au daktari pamoja na uwezo wake wakati wa kufanya operation au kukupiga nusu kaputi ile anaweza akakumaliza. Lakini pamoja na kwamba hajalipwa mshahara, hajalipwa mapunjo anakomaa anaamua kutimiza kiapo chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tufike mahali tuwaangalie watu hawa ili tuweze kuwatimizia haki sambamba na huduma na aina ya commitment ambayo wanakuwa nayo katika kazi yao.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Kama haiwezekani nafikiri yale masharti ambayo yaliwekwa ya watu kutofanya kazi za ziada, naomba daktari aruhusiwe kuweza kutafuta kipato cha ziada cha kufidia pato dogo mnalomlipa. Nafikiri ipo haja kubadilisha utaratibu hawa watu wakapata fursa ya kujiongezea kipato kama mmeshindwa kuwalipa sawa sawa na haki yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiaria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lwakatare kengele ya pili ililia.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mchango wangu utajielekeza kwenye mambo mawili, kwa haraka haraka. Jambo la kwanza Mheshimiwa muwasilisha hoja na msaidizi wake na hasa msaidizi wake (Naibu) wanatambua kabisa kwamba takwimu ambazo zimekuwa zinatolewa zimekuwa zinaonesha Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa maskini. Binafsi naamini Kagera haina sababu ya kuwa maskini au kutambulikana kuwa maskini. Nachoamini ni kwamba Mkoa wa Kagera haujatengenezewa mipango ambayo ingeweza kutumia fursa za geographical position ya mkoa pamoja na fursa nyingine kuwa mkoa ambao unachangia pato la Taifa na watu wake kwa matajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kupitia Mpango huu naomba upelekee kuwepo mipango ambayo inaweza ikachochea uwekezaji wa kibiashara pamoja na uwekezaji utakaoshindana au utakaokuwa kwenye nafasi ya kushindana na biashara zilizoko katika nchi jirani. Mkoa wa Kagera ni mkoa ambao una advantage kuliko mikoa karibu yote ya Tanzania kwa kupakana na nchi nne ambayo ni mipaka ya moja kwa moja lakini pia inapakana na nchi mbili japo siyo moja kwa moja lakini nchi hizo mbili una uwezo wa kuendesha gari kwenda mpaka kwenye makao makuu ya nchi hizo na ukarejea katika mji wa Bukoba, nchi za South Sudan pamoja na DRC Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sasa kwamba uwepo mpango maalum wa upendeleo, taratibu za kikanuni, za kisheria zisaidie mpango huo wa kuifanya Kagera kuwa na mipango maalum ya kiuwekezaji na hata ikibidi mpango huo uwe wa upendeleo wa kipindi maalum, kama ambavyo imewahi kufanyika kwenye baadhi ya mikoa ikiwemo Dodoma wakati tunajenga Makao Makuu ili Kagera isiendelee kuhesabika kama mkoa maskini kwa sababu tu ya mipango ambayo ni mibovu. Mheshimiwa Mpango na hasa Naibu wake ambaye naamini amefika Mtukura, Lulongo, Rusumo, Kabanga anaweza akawa shahidi yeye mwenyewe jinsi upande wa pili biashara zinavyochanganya lakini ukiangalia upande wa Tanzania ni wakiwa. Mimi nafikiri ni suala la mpango ili kwa kweli Kagera iwe ni gate la nchi za Afrika Mashariki pamoja na nchi za Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na suala hili, tunakumbuka katika kampeni za mwaka 2015, Mheshimiwa Rais wakati akijinadi miongoni mwa ahadi alizozitoa katika Mkoa wa Kagera ni kuifanya Kagera kuwa sehemu maalum ya kiuwekezaji. Sasa naona kipindi kinayoyoma sijui huu mpango tunaoujadili sasa nafikiri unaweza ukanusuru na ahadi ya Mheshimiwa Rais ikatekelezeka. Pia katika kuweka kiki kubwa zaidi katika kikao cha RCC cha juzi ambacho kimefanyika pale mjini Bukoba na nafikiri Mheshimiwa Mwijage ni shahidi alihudhuria hicho kikao ni kwamba mkoa umepitisha suala hili kama azimio na naamini tayari limeshafikishwa katika ofisi husika ili Mheshimiwa Mpango hili suala aliweke katika mpango wake kwa sababu ni jambo ambalo limeridhiwa na limepitishwa katika vikao vyetu vya RCC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili, naamini mpango huu na ndivyo ilivyo kwamba ndiyo utakaozaa bajeti ya mwaka 2020/2021 na hiyo bajeti itasheheni mabilioni ya kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020. Experience ya chaguzi ndogo za Madiwani, chaguzi ndogo za Majimbo na hata uchaguzi unaoendelea hivi sasa wa mchakato wa Serikali za Mitaa, hautoi picha nzuri kwa taifa letu kama kweli tuko serious na mfumo wa vyama vingi. Mbaya zaidi tumekuwa tunaonekana tunapoteapotea, mipango ya kiuchaguzi tunaonekana hatujawa wazoefu badala ya kuwa uchaguzi inaonekana unakuwa uchafuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hatupaswi kuwa na mipango na kupanga bajeti kubwa kwa chaguzi ambazo zinaacha watu wamepigwa, vilema, watu wamefungana na zaidi watu wameongezeana chuki, hawasalimiani na wanafungana. Kwa kweli huo hautakuwa ni uchaguzi wa kuweza kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati Mwalimu akiwa mojawapo ya watu walioshadidia na kupitisha mfumo wa vyama vingi japo watu waliopiga kura asilimia ilikuwa ndogo, Mwalimu alikuwa na matumaini makubwa na mfumo wa vyama vingi kwamba itakuwa kitovu cha watu kuchakata mawazo ya watu tofauti na kujenga mipango ya kuweza kujenga uchumi endelevu kwa faida ya watanzania, ndiyo ilikuwa vision ya Mwalimu. Pia, mtakumbuka kwamba Mwalimu wakati alipoona kwamba hatujawa tayari katika suala la kuchimba madini, alifanya maamuzi ya makusudi kuweza kuahirisha kwamba tusihusike katika suala la madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitamke kabisa, nilikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF kwa muda mrefu sana tu. Nilishuhudia mambo yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2001 ambayo ilisababishwa na dalili ninazoziona hata hivi sasa kwa Tanzania Bara. Tukifanya mchezo tunakwenda kuchafua nchi yetu kwa sababu za kiuchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mambo yako hivi, mimi ningeshauri, kuliko kuendelea chaguzi kuwa sehemu ya kutesa watu wetu, basi tuunde mfumo tofauti na huu tulionao, iletwe sheria, ifanyike research tuwe na mfumo tofauti wa kupambana hivi na hivi na hivi ili uchukue nafasi ya mfumo tulionao sasa hivi ambao kwa kweli siyo endelevu. Kwa kweli wananchi wao walikuwa na utashi, wameonesha kuupenda mfumo wa vyama vingi lakini watu wenye ubinafsi mimi naona hawaupendi mfumo huu kwa sababu zao binafsi. Kipimo pekee cha kuonesha watu kwamba wana utashi, huu uchaguzi wa Mitaa umefanyika baada ya miaka minne yote hakuna mikutano ya vyama vingi, hakuna mikutano ya kisiasa lakini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lwakatare naona bado dakika mbili.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Sawa.

MWENYEKITI: Unaweza ukachangia Mpango sasa.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo mpango wenyewe, mimi nataka kupinga huu Mpango utakaotuletea fedha ya bajeti ya uchaguzi utakaoharibika na kutochagua viongozi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi, kitendo cha wananchi kujitokeza kwa wingi baada ya kuzuiwa kufanya mikutano, zaidi ya 92% na ndiyo takwimu sahihi, nafasi 92 ziligombewa, halafu unakuja kuwaondoa inabaki 12% kwa takwimu tulizonazo, haitupi matumaini mema huko mbele. Mimi naamini CCM walipaswa kutumia fursa hii kuzipima project ambazo CCM wanazitaja kwamba zimefanyika kuwaachia watu ambao wanagombea waende kuzinadi ili wachaguliwe kwa sababu ya project nzuri zilizofanyika wapate kura lakini hiki kitengo cha kutumia mlango wa nyumba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lwakatare, ni kengele ya pili.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Naam.

MWENYEKITI: Ni kengele ya pili.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru lakini Mheshimiwa Mpango ningeomba bajeti na mpango wa ku-provide fedha kwa uchaguzi ambao ni uchafuzi bora hiyo fedha isitolewe na tuwe na mfumo mwingine, kama CCM wabaki wenyewe basi waendelee wenyewe kuliko kuwa na uchaguzi wa kuwaumiza watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Kwanza nipongeze hotuba ya Kambi ya Upinzani ambayo imejaribu kurejea mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Wizara hii ili waweze kuyafanyia kazi mambo ambayo yametolewa kama ushauri na mambo ambayo wameweza kuyaainisha kama sehemu zenye kasoro ndani ya Idara mbalimbali za Wizara hii. Pia nipongeze hotuba ya Kamati ambayo pia imeainisha mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Wizara hii ambayo bajeti yake tunaijadili.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kwa ufupi kabisa kutoa pole kwa wananchi wa Manispaa ya Bukoba ambao wamepatwa na dhahma ya mafuriko na ambapo mpaka sasa hawajaweza kukaa sawa. Ninaamini kwamba Wizara hii itajaribu kurudisha kwa kasi sana miundombinu ambayo ya umeme ambayo imeharibiwa na mafuriko haya ili watu waweze kurejea katika hali iliyo salama na kuendelea kutumia nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, Katika tamko la Serikali ambalo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa aliainisha bayana kwamba Serikali inatoa ushauri na msukumo wananchi waanze kuhama katika maeneo mengi ya Mji wa Bukoba kwenda katika maeneo ya Vijiji Mji, ambavyo ni Nyanga, Kahololo, kuna Vijiji vya Ijuga Nyondo, Kibeta na Kagondo. Vijiji hivi, kama ambavyo nimekuwa nikieleza huko siku za nyuma, na Mheshimiwa Waziri anajua, sehemu nyingi hazina umeme. Sasa kama alternatively ya kukimbia mafuriko imekuwa kwenda kwenye vijiji hivi naomba huu mpango wa kuweka umeme kwenye Vijiji Mji uweze kufanyika kwa haraka katika Mji wa Bukoba ili watu waweze kupata huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Pamoja na mambo mbalimbali ambayo yameshauriwa katika hotuba ya Kambi ya Upinzani na Kamati ya Nishati ningeomba kutoa ushauri kwa mambo mbalimbali yafuatayo.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa REA ni miongoni mwa Miradi ambayo inapata fedha, au ina vyanzo vya uhakika vya kupata fedha. Lakini pamoja na uhakika wa vyanzo hivi tumeona kupitia katika hotuba hususani ya Kambi Rasmi ya Upinzani figisu zinazojitokeza hasa za matumizi mabaya au usimamizi mbaya wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimejikita zaidi kuangalia tatizo linaweza likawa nini. Mimi binafsi sikubaliani na mfumo wa usimamizi wa fedha unaotumika ndani ya REA. Kuifanya TANESCO kuwa mshauri au kuwa consultant wa hii Miradi ya REA ni jambo kidogo ambalo mimi nafikiri linakosesha transparency inayopaswa kufanyika kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ni vyema REA ikawa na ma- consultant, ikatangazwa nafasi ya consultant, kazi za consultant, ili TANESCO ambayo kimsingi nayo unakuta kuna wakati inakuwa ni Kampuni shindani kwenye baadhi ya Miradi, lakini pia ni Kampuni ambayo inakuja kurithi Miradi ya REA; unapomfanya ni consultant mimi naamini unatoa nafasi ya baadhi ya mambo kufukiwa ndani kwa ndani na hata kufanya kazi ya trace, hata kama pesa imekuwa misused inakuwa ni kazi ngumu kwa sababu msimamizi ni yule yule, huyo huyo anachukua contract na anashindana na Kampuni nyingine. Hata wakati mwingine tumnapata taarifa kwamba nguzo ambazo TANESCO kama consultant anazikataa wakandarasi wasizitumie yeye anapokuja kufanya kazi yeye anatumia nguzo hizo hizo wakati ambapo anakuwa amezikataa kwa wakandarasi binafsi; hii ni double standard. Mimi ushauri wangu ni huo; kwamba kwa kweli ifike mahala hizi kazi wapewe ma-consultant ili TANESCO naye asimamiwe badala ya kuwasimamia watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu ni suala ambalo limezungumzwa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambapo mara nyingi Wizara au taarifa mbalimbali zinazotolewa na Kampuni za TANESCO, REA wamekuwa wanatumia kigezo cha kijiji usambazaji wa umeme kwa kigezo cha vijiji. Kama Kambi ilivyo shauri, ni vyema tukaanza kutumia kaya, Maana katika maeneo mengi tunaambiwa vijiji kadhaa vimepewa umeme au vimesambaziwa umeme lakini ukienda kwa uhakika unakuta kuna vitongoji vingi mno, vinakuwa havijapewa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakuta kwenye kijiji ziko kaya kama 30, 40 lakini maeneo mengine ya vijiji, tukija hapa Bungeni tunaambiwa takwimu chungu nzima ya vijiji kwamba vimepata umeme; hii tunakuwa tunajitekenya na kucheka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imekuwa inaomba sana kukutana na wakandarasi ili waeleze maeneo wanayokwama, lakini imekuwa kizungumkuti, sasa nitaomba kujua kupitia kwa Waziri wakati ana-windup; tatizo liko wapi kwa Kamati kukutana na Wakandarasi? Kunafichwa nini la kutukutanisha na Wakandarasi hawa? Maana kukutana nao kutatupa picha wanakwama wapi au wanakwamishwa wapi na Serikali. Hata hivyo na wakandarasi wenyewe nasikia nao wanatishwa juu ya suala la kukutana na Kamati, wengine wanaogopa hata kukutana na Kamati kwasababu wanahisi wanaweza wakakosa hata tenda pindi wakija kuomba. Sasa ili tuwe wawazi mimi nafikiri mchakato wa kukutana na Wakandarasi ufanyike.

Mheshimiwa Spika, Suala la tano, gharama za kuunganisha umeme. Tulipokuwa kwenye Kamati, Waziri alizungumza bayana kabisa, kwamba kuunganisha umeme wa REA pamoja na ile miradi inayorithiwa na TANESCO unapaswa kutozwa 27,000, ndicho kiwango kinachopaswa kutolewa. Ili kuweka mambo bayana mezani tulimuomba Waziri na akaahidi kwamba utatolewa waraka ambao utagawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wote kipindi hiki cha bajeti waondoke nao kwenda kuwaelewesha na kuwafahamisha wananchi kwamba wasitozwe pesa zaidi ya 27,000. Mheshimiwa Waziri tutaomba waraka huo utoke kwa sababu ni ahadi yako, ili watu tuondoke nao twende nao huko na kuufahamisha Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwisho ni Kuhusu Miradi Mikubwa. Ifike mahala Bunge linapokuwa linajadili mambo tuweke binding ya kutopindua maneno yetu. Nilikwenda library kusoma Hansard ya mwaka 2013/2014 baadhi ya Wabunge walioko humu ndio walishadadia gesi, kwamba gesi sasa tumepata biashara imekwisha mkombozi wetu ni gesi, na baadhi ya Wabunge wako humu, akiwemo na kaka yangu Mwijage. Leo hii wamehama wanakuja kwenye Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mimi naomba Bunge lijiwekee utaratibu wa kuweka binding ya maneno ambayo tunakuwa tumepitisha na kushadadia badala ya kuwa tunaokota huku tunakuja huku, kesho kutwa tunaokota hili tunakuja hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwanza nipongeze hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyotolewa hapa na nishauri Serikali chini ya Mawaziri wake wote wawili na washauri wao ni vyema wakachukua ushauri ambao umetolewa na Kambi ya Upinzani kwa manufaa ya bajeti nzuri kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili; Waheshimiwa nizungumze kauli ambayo nimewahi kuitoa hata tangu nikiwa kiongozi wa Kambi ya Upinzani huko nyuma na sasa nairudia kwamba vipindi mfululizo ambavyo tumekuwa ndani ya Bunge hili na mpaka leo hii sijawahi kuona upande wa pili ukisema hii bajeti ni mbaya na kwamba siyo bajeti ya wanyonge, bajeti zote tunaambiwa ni bajeti za wanyonge pamoja na kwamba zinakua kwa kiasi mwaka baada ya mwaka lakini matatizo yanabaki vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi nakwenda mbele zaidi ya kuhoji capacity ya wataalam wetu na watu wanaotutengenezea bajeti hizi, kwamba nashauri Researchers wetu, wataalam wetu, taasisi zinazojenga capacity na hata taasisi zinazosaidia capacity building ya sisi Wabunge, wajaribu kuangalia tatizo letu la msingi liko wapi; kwa nini tunatengeneza bajeti ambazo miaka nenda, miaka rudi hazioneshi effectiveness kwa kuondoa umaskini ule unaolengwa wa kipato kwa watu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna masikio, tuna macho, tuna mikono, tunasafiri na leo nilikuwa naangalia kwenye ma-group, naangalia watu waliokwenda Egypt wanatuonesha mahali walipo, wanakopita. Kwangu mimi kinachokuja ni kwamba mambo yote tunayoyaona kwenye runinga au ukienda kwenda geographical ile TV ukaona mambo watu wanayofanya, ile ni brain, brain ndiyo inayofanya mambo yote hayo. Sasa na mimi najiuliza, brain ya sisi Watanzania na wataalam wetu ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli Mheshimiwa Dkt. Mpango, Naibu Waziri, Mawaziri wetu, Wabunge; huko tunakotoka vijijini tunapozungumzia suala la umaskini wa watu wetu, kweli tunahitaji Wazungu ndio waje watuoneshe umaskini wa watu wetu? Hivi mtu atoke hapa aende kilometa 20 tu kutoka ndani ya Dodoma, aone kama hajui umaskini unafananaje, aende aone; hivi tunaridhika na hizi bajeti tunazotengeza kwamba kweli zinajielekeza kubadili hali ya watu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kabisa, kuna nchi ambazo early 50s kuja mpaka 90s, Nchi kama Indonesia, Malaysia, Philippines, Thailand, Vietnam na sasa Botswana, hata Rwanda hapa jirani ambao tulikuwa tunalingana na wengine wako nyuma ya uchumi wetu wakati tunapata uhuru, wamefanya maajabu gani mbona wana vichwa kama vyetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, mbona akina Mheshimiwa Dkt. Mpango ndio wanakwenda katika nchi kule, tena Watanzania wanasifika sana wakienda kwenye mitihani au kuandika thesis wanapata A nyingi, lakini inapokuja kwenye kutafsiri elimu wanayoipata kuja kwenye matendo tunapotelea wapi, mbona mambo hayabadiliki? Naomba hilo tujielekeze tuangalie matatizo yetu kimsingi yako wapi. Tulete Researchers wajaribu kutafiti vichwa vyetu vinaharibikiwa wapi, kutuhamisha akili tulizonazo kwenda kwenye vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango wakati tukieleka Jumanne kupiga kura, nataka aniridhishe na kitu kimoja ambacho hapa katikati kinaweza kunipa ushauri wa kupiga kura; aniridhishe kwamba bajeti hii inakwenda kufanya maajabu gani, anakwenda kufanya maajabu gani tofauti na experience ambayo tumeipata katika bajeti hii inayokwenda kumalizika mwisho wa mwezi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa na maana gani; kwamba bajeti iliyopita kwa mapato ya kodi kwamba tuliambiwa kwamba kila mwezi wanapata average ya 1.2 pamoja ni nje ya trilioni 17 ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anazizungumzia. Sasa ukija kwenye average tumekuwa tunaelezwa wanajaribu kupata 1.2 trillion kila mwezi. Kwa bajeti hii inaonekana lazima tutakwenda katika average ya kutaka kukusanya at least 1.4 – 5 trillion kwa kila mwezi kama tutakuwa tumekwenda vizuri, ili tupate ile 19 ya mapato ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa experience iliyoonekana hapa kupata hata hiyo 1.2 ni kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango na wasaidizi wake na TRA na taasisi nyingine wametumia mitulinga isiyo ya kawaida. Maana yake wame-pull forces zote kadri walivyoweza; maana yake pale polisi wameshiriki, mgambo wameshiriki, TISS imeshiriki, wajasiriamali nao na vitambulisho wameshiriki, yaani kuna watu wengine hata mpaka wakawekwa ndani na wengine wakawekewa hata kesi za money laundering, yaani hata kwa forces zote hizo lakini amepata average ya 1.2 trillion. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati tukielekea tena kwenye hii bajeti naiita bajeti ya uchaguzi, yaani kupata 1.5 trillion, kama kule alikuwa anatumia viboko nafikiri safari hii atatumia rungu au inabidi atumie SMG kabisa mtaani na vinginevyo mimi naitafsiri kwamba inaweza ikawa bajeti ya mateso na maumivu kwa wananchi wetu na wafanyabiashara. Maana yake tusidanganyane; wananchi watarajie hilo. Vinginevyo kama ni tofauti napo anieleze anakwenda kufanya maajabu gani ili kuwaepusha watu na mambo ambayo mimi nayaota kwamba yatatokea. Kama wafanyabiashara walikuwa wanakimbizana na TRA sasa watahama hata nchi kabisa kwa sababu hali kusema kweli haivutii.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ambalo nataka kumaliza nalo; mimi natoka Bukoba Town na kwa Bukoba Town na wananchi wa Kagera sisi meli, unapomwambia mwananchi wa Kagera meli wameijua tangu wakati wa Mkoloni, kumekuwepo na Mei MV Victoria ile ililetwa tangu wakati wa Mwingereza. Kwa hiyo kwa mwananchi wa Kagera meli ni maisha, meli ni uchumi. Kwa sababu leo mwananchi wa Kagera njia pekee ambayo anapata huduma na kuwa supplied na vitu mbalimbali ni kutumia barabara. Ukitumia barabara tunajua expenses za ku-transport mizigo kwenda mpaka Kagera kwa njia ya barabara, kwamba ni very expensive.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi naomba, tuliona bajeti iliyopita, kwenye upande wa huduma za meli ni kwamba zilikuwa zimetengwa 20 billion, lakini zilizotoka mpaka mwezi wa Nne ni only three billion. Na mwaka huu nimeona zimetengwa 70 billion. Sasa ile 20 ilishindikana na zikatolewa tatu kwa bajeti ya kutafuta kwa mitulinga, sasa hii ya sasa 70 billion sijui zitapatikana wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalizungumza kabisa. Bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Mpango ni Muha na Waha ni wajukuu zetu maana yake ile ya Wahaya babu zao, sisi tunaitwa Wahaya tulipoona mjukuu asilingane na babu tukaondoa ya ikabaki Waha. Hata Mheshimiwa Engineer Nditiye nafikiri anatoka kule na shemeji yangu, Naibu Waziri, sisi Bukoba tunataka meli. Kama meli mpya imeshindikana watupe Victoria yetu aliyoacha Mwingereza, hebu wajaribu kuikarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu meli sisi wakati inafanya kazi mfuko wa simenti ulikuwa 17,000, 16,000, lakini sasa hivi kwa barabara simenti 20,000. Sisi Kagera wamekuwa wepesi kutuambia sisi ni mkoa maskini sasa hivi. Ni lazima tutafute tuliharibikia wapi Kagera, Kagera ulikuwa ni mkoa ambao unasifika dunia nzima. Ule mkoa hata wakati tunapata uhuru Mwalimu Nyerere aliwekewa guarantee gari la kwanza kutoka kiwandani na BCU (Chama cha Ushirika cha Kagera). Kwa hiyo huu umaskini wa Kagera mimi nafikiri umetengenezwa tunahitaji Marshall Plan ya Kagera ili mkoa urudi katika nafasi yake, wasianze kutuambia ninyi ni watu wa matatizo, sijui mafuriko huko, matetemeko huko. Sasa turudi katika kuutengeneza huo mkoa ili urudi mahali pake. (Makofi)