Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. David Mwakiposa Kihenzile (30 total)

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, lakini pia swali hilo linafanana na hali ya kule Mufindi. Kwa kuwa Mufindi ni kitovu cha viwanda nchini na zaidi ya viwanda tisa viko pale na miundombinu imekuwa ni mibovu sana; na kwa kuwa barabara ya Nyololo - Mtwango na Mafinga - Mgololo zimeahidiwa kuanzia wakati wa Mwalimu Nyerere, pamoja na Rais Magufuli, zimeahidiwa na Mawaziri Wakuu, Mzee Pinda na Mzee Kassim Majaliwa, zimetajwa kwenye Ilani ya CCM karibu mara tatu…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuingiza kwenye bajeti barabara hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara zote alizozitaja zinakwenda kwenye maeneo ya uzalishaji mkubwa sana ambao yanachangia fedha nyingi sana kwenye Mfuko wa Serikali na kama alivyosema barabara hizo zimeahidiwa na viongozi wengi wa Kitaifa, lakini pia barabara hizo zimetajwa kwenye Ilani, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizo kwa sababu ya umuhimu wake, kuanzia bajeti inayokuja zitaanza kutengewa fedha ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kwa kuwa Serikali inatambua jambo hili ambalo nimesema nataka kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini Serikali itamaliza kero ya maji katika ukanda huu wa baridi ambapo kuna vyanzo hivyo na hivyo kufanya tatizo la maji kuwa historia katika maeneo ya Kata za Migohole, Kasanga, Mninga, Mtwango, Idete pamoja na maeneo mengine ya Makungu, Kiyowela na Mtambula?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza, kwa kuwa suala la maji ni mtambuka na ni muhimu sana, katika eneo hilo la Mufindi Kusini kulikuwa na mradi ulikuwa unaitwa Imani, ni lini Serikali itakwenda kuufufua kwa kuboresha miundombinu ili wananchi waliokuwa wananufaika waweze kunufaika especially kwenye Kata za Ihoanza, Malangali, Idunda, Mbalamaziwa, Nyololo, Maduma na Itandula?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge David Kihenzile kwa namna ambavyo amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa matatizo ya maji katika Jimbo lake. Hii ni kawaida yake kwa sababu pia amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza tatizo la maji litakoma lini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama Ilani ya CCM inavyotutaka Serikali kuhakikisha kufika mwaka 2025 tuweze kukamilisha maji vijijini kwa 95%, kwa maeneo ya Mufindi tutahakikisha mwaka ujao wa fedha tunakuja kuweka nguvu ya kutosha ili libaki kuwa historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la kufufua miundombinu, katika maeneo mbalimbali suala hili linaendelea kutekelezwa. Katika eneo la Mufindi, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha tutakuwa tumeshafanya kwa sehemu kubwa kuona miundombinu chakavu tunaitoa na tunaweka miundombinu ambayo inaendana na matumizi ya sasa.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa majibu ambayo yametolewa kwa kuzingatia kwamba barabara hizi tumezipigia kelele kwa muda mrefu na tunategemea zitusaidie kutuvusha kwenda uchumi wa kati wa juu, kwa sababu ndizo zinakusanya viwanda vyote kule ambapo tunakusanya zaidi bilioni 40 kwa mwaka na pengine kwa miaka kumi ni nusu trilioni. Fedha hizi zote zinakwenda kujenga maeneo mengine, pale wananchi wakitaabika na hivi ninavyozungumza magari hayapatiki.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la nyongeza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alisema hapa Bungeni mwezi Februari, zingeingizwa kwenye mwaka wa fedha huu 2021/ 2022; na kwa kuwa amezungumza pia usanifu umekamilika wa barabara hii moja. Kwa nini sasa hii iliyokamilika ya kilomita 40 ya kutoka Nyololo mpaka Mtwango isianze kujengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; hii ya pili ambayo amesema usanifu unakamilika ni ipi commitment ya Serikali sasa, itaanza lini na itakamilika lini? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa amesikiliza jibu la msingi, tunatambua kwamba mbao zote karibu tunazoziona zinatoka eneo la Mafinga zinapita huko, magogo ni mengi. Ndio maana katika jibu langu la msingi nimesema mwaka 2022/2023, Serikali inatoa commitment kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sababu ni barabara ambayo sasa zimekuwa ni changamoto kwetu kutokana na uzito mkubwa kwamba kwa uwezo wa changarawe barabara zinashindwa kuhimili uzito wa magari yanayopita hapo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mufindi Kusini kwamba commitment ya Serikali ni kama tulivyosema kwenye jibu la Msingi tutaanza kujenga 2022/2023. Ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nataka niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, hospitali hiyo iko mbali na makazi ya watu, ni upi mpango wa Serikali sasa katika kujenga makazi kwa ajili ya watumishi wa hospitali hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, ni upi mpango wa Serikali katika kutatua kero kubwa ya wataalam wa sekta ya afya katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika Jimbo letu la Mufindi Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa David Kihenzile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza hapa ni lini Serikali itajenga makazi kwa ajili ya watumishi wa afya wa Hospitali ya Halmashauri ya Mufindi. Nimueleze tu kwamba katika jitihada za Serikali, moja ya jitihada kubwa ni kama tulivyoeleza katika jibu letu la msingi tumekuwa tukiongeza fedha kuhakikisha tunaboresha hospitali hiyo na kila mwaka tumekuwa tukitenga fedha. Kwa hiyo, nimueleze tu kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo kuanzia wodi, OPD pamoja na nyumba za watumishi kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi, Serikali ina nia njema kwenye suala hili na tutalifanyia kazi ombi lake na siyo tu kwa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi bali kwa nchi nzima katika vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusiana na kero ya wataalam, Serikali inaendelea na ajira na katika kipindi hiki Serikali itaajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya zaidi ya 2,600. Katika mgawanyo huo, sehemu ya watumishi hao tutawapeleka katika Halmshauri ya Wilaya ya Mufindi kwa ajili ya kupangwa kwenye vituo vyake vya afya. Ahsante sana.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anisaidie kujibu, hicho kituo cha afya kipo mbali sana, kimejitenga ndio kila siku napigia kelele habari za barabara. Atuambie ni lini sasa Serikali itapatia kituo cha afya pale gari ya kubebea wagonjwa kwa sababu ipo mbali sana, ni tofauti na maeneo mengine anayosema?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kituo cha afya ambacho gari hilo linatoa huduma kipo mbali na kituo hiki ambacho kinahitaji gari lingine la nyongeza kwa ajili ya kusaidia gari dogo lililopo. Kwa kutambua hilo, Serikali imeona ni busara gari lile liwe standby wakati wowote kusaidia ikitokea kuna dharura pamoja na umbali wakati tunaendelea kutafuta fedha, Serikali kwa kushirikiana na wadau ili tuweze kupata gari kwa ajili ya kuhakikisha linapelekwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge jukumu ambalo limechukuliwa na Serikali ni la muda mfupi la kuondoa changamoto ya kukosa magari ya wagonjwa, lakini mpango ni kutafuta fedha na nikuhakikishie kwamba fedha zikipatikana, tukipata magari ya wagonjwa tutakupa kipaumbele katika Jimbo la Mufindi Kusini.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anisaidie kujibu, hicho kituo cha afya kipo mbali sana, kimejitenga ndio kila siku napigia kelele habari za barabara. Atuambie ni lini sasa Serikali itapatia kituo cha afya pale gari ya kubebea wagonjwa kwa sababu ipo mbali sana, ni tofauti na maeneo mengine anayosema?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kituo cha afya ambacho gari hilo linatoa huduma kipo mbali na kituo hiki ambacho kinahitaji gari lingine la nyongeza kwa ajili ya kusaidia gari dogo lililopo. Kwa kutambua hilo, Serikali imeona ni busara gari lile liwe standby wakati wowote kusaidia ikitokea kuna dharura pamoja na umbali wakati tunaendelea kutafuta fedha, Serikali kwa kushirikiana na wadau ili tuweze kupata gari kwa ajili ya kuhakikisha linapelekwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge jukumu ambalo limechukuliwa na Serikali ni la muda mfupi la kuondoa changamoto ya kukosa magari ya wagonjwa, lakini mpango ni kutafuta fedha na nikuhakikishie kwamba fedha zikipatikana, tukipata magari ya wagonjwa tutakupa kipaumbele katika Jimbo la Mufindi Kusini.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili la hali ya Mufindi linafanana pia na hapa mtangulizi amezungumza lakini tofauti ni kwamba asilimia 70 ya nguzo katika nchi hii zinatoka pale kwenye Jimbo letu, sasa ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye maeneo ambayo ni ya giza pamoja na kwamba nguzo zinatoka pale, especial maeneo la Idete, Maduma pamoja na Idunda na vijiji vya Kisasa na maeneo mengine ambayo hayana umeme kabisa na wanashuhudia nguzo zikipita kila siku mbele yao. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimwa Kihenzile Mbunge wa Mufindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunakiri kuna maeneo bado hayana umeme mpaka sasa, Mufindi ni eneo mojawapo ambalo mkandarasi wa REA III round II tayari amepatikana MS Servicies na tayari ameenda kufanya survey kwenye maeneo husika, tunamhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utuatiliaji wake ambao amekuwa akiufanya mara kwa mara utazaa matunda na tutapeleka umeme katika vijiji vyote alivyovisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo lazima lipewe kipaumbele na heshima kwa sababu ndiyo linalisha na maeneo mengine yanayotumia nguzo za miti, kwa hiyo kweli katika hali ya kawaida siyo kitu cha kufurahisha kuona unatoa bidhaa halafu wewe haunufaiki nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla ya mwaka 2022 kukamilika tutakuwa tayari tumefikisha umeme katika maeneo yote ambayo hayana umeme. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu dhamira ya Rais wetu aliyoionesha kwenye eneo la michezo, na tarehe 15 Juni, 2021 alipokuwa anazungumza na vijana wa nchi hii pale Mwanza alizungumzia eneo hili la msamaha wa kodi. Na katika maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wataanza kufanya practice kwenye upande wa majijii na halmashauri za manispaa, na wakifanya vizuri watahamia kwenye Wilaya.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ina maana wanamaanisha kwa mfano kama Dodoma Mjini wakipewa hayo majaribio waki under perform basi ina maana Kongwa hawatapewa kwenye phase two.

Mheshimiwa Spika, hii nadhani si sawa. Ni vyema kama wanakwenda kufanya majaribio wafanye kote kwenye halmashauri za manispaa, majiji na kule kwingine.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ili kurahisisha utekelezaji wa jambo hili Je, Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla haioni sasa umefika wakati wa kuanzisha wakala wa vifaa vya michezo nchini ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya michezo kirahisi kuanzia kwenye shule zetu hata kwa Wabunge wenyewe ambao kimsingi kila mwaka wamekuwa wakiagiza vifaa vya michezo kwa wananchi wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakiposa Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali kuanza na majiji na halmashauri hayakuwa na maana ya kuangalia mapungufu ambayo yanaweza kusababisha maeneo mengine yasipate sipokuwa yalikuwa yana lengo la kuangalia mapungufu ili yatakapopelekwa maeneo mengine mapungufu yale yasijitokeze. Kwa mfano katika matumizi ya nyasi hizi bandia yamekuwa yakitumika katika shughuli mbalimbali wakati mwingine unaweza ukaenda hata kwenye bar ukakuta hizi nyasi bandia zipo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie kwamba Serikali inadhibiti matumizi mabaya ya fursa hii njema iliyowekwa na kwa dhamira njema ya Serikali ni vyema tungeanza hatua kwa kwa hatua. Kwa hiyo elimu ambayo tumeipata katika utekelezaji katika awamu ya halmashauri na majiji itatusaidia tunapopanua wigo katika maeneo mengine mengi zaidi kuweza kufahamu ni mapungufu yapi na tukayoweza kuyadhibiti kirahisi ili kuepuka madhara na hasara kwa Serikali; hiyo ndiyo iliyokuwa dhamira. Malengo ni kuhakikisha kwamba tunasambaza huduma hizi katika maeneo yote nchini hatua kwa hatua na awamu kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wazo lake la pili, ni jambo jema sana na Mheshimiwa Mwakiposa amekuwa kwakweli ni mpambanaji sana wa suala hili. Mara nyingi amekuwa akija akituulizia kuhusiana na utekelezaji, na kwamba angependa kuona mabadiliko na maboresho makubwa katika eneo hili. Kwa hiyo kuhusiana na hoja hii ya pili nadhani ni hoja ya msingi. Mheshimiwa Waziri wa Michezo na Mheshimiwa Naibu wake hapa wapo, wamesikia na ninahakika watalitafakari na kama wataona kuna tija basi watalitekeleza. Hili lipo katika Wizara ya Michezo na Serikali hapa ipo, tumelisikia.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, parachichi ni moja ya mazao saba ya kimkakati ambayo Serikali imeyatangaza, zao la pili kwa Mufindi Kusini ni chai.

Mheshimiwa Spika, naomba kufahamu commitment ya Serikali katika kusaidia wakulima ambao majani yao yanamwagwa wanakosa soko na viwanda havichukui.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ziko tetesi kwamba kiwanda hicho kimeuzwa atatusaidia Mheshimiwa Naibu Waziri kama atakuwa na majibu ipi commitment ya Serikali juu ya maslahi ya wafanyakazi kama kweli kiwanda hicho kimeuzwa Mufindi ya Kusini?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru na nimpongeze Mbunge mwenzangu kutoka Mufindi ambaye anafuatilia sana maendeleo ya wilaya hiyo.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema nia ya Serikali Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na hasa tukizingatia kuwa sekta binafsi iwe kiongozi kwa ajili ya kufikia uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, moja ya mikakati ya kukwamua maendeleo katika sekta ya viwanda ni kuhakikisha viwanda vilivyopo vinaendelea, lakini pia kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanda vya parachichi; viko viwanda viwili katika mkoa wa Iringa; Kibidula Avocado Packiging Industry ambayo inafanyakazi vizuri, lakini pia na Kiwanda cha GBRI, Kampuni ya GBRI pale Iringa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Unilever kwa maana ya Kampuni ya Chai, sisi kama Wizara tumeshapata notice ya kuuzwa kwa kampuni hiyo na taarifa hizi ziliifikia Tume ya Ushindani mwaka jana mwezi Desemba kwa maana ya tarehe 17 Desemba, 2021 na hatua zinazochukuliwa kwa kampuni ambayo inauzwa huwa kwanza ni kutangaza notice ya siku 14 kwa wale ambao ni wadau au wanahusika katika mchakato wa kuuza. Kwa hiyo siku zile 14 ziliisha na hakukuwa na mtu yeyote mwenye maoni au malalamiko.

Mheshimiwa Spika, lakini pili sisi kama Serikali kupitia Tume ya Ushindani tunaendelea sasa kufuatilia hatua stahiki za uuzwaji wa kampuni hiyo. Kwa ruhusa yako labda nifafanue kidogo kama utaruhusu kampuni ya Unilever ina kampuni tanzu ya Ekaterra ambayo ndiyo inasimamia sekta ya chai, sasa wanauza kwa Kampuni ya Puchin Bidco ambayo yenyewe itachukua eneo hilo. Kwa hiyo, kwa sasa tumeshaiagiza FCC waendelee kufuatilia na kama kuna watu wenye malalamiko kuhusiana na mauziano haya walete maoni au malalamiko kwenye Tume ya Ushindani.

Mheshimiwa Spika, lakini tatu kuna masuala ya maendeleo ya wafanyakazi nayo yatazingatiwa katika mchakato huo, nakushukuru.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana Mheshimiwa kwa majibu mazuri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, moja, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Mtambula, Luhunga na Mninga kule Mufindi Kusini?

Mheshimiwa Spika, pili, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya maji ya Malangali, Nambalamaziwa na Igohole ambayo tayari Serikali imeshaanza kutenga fedha?
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza, Serikali imejipanga hivi sasa katika kata zile tatu alizozitaja inafanya utafiti wa kupata vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, la pili, tayari taratibu za manunuzi zimekwisha kukamilika na mnano mwezi Desemba utekelezaji wa mradi utaanza.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Tarafa ya Malangali hususan Kata za Nyololo, Maduma, Ihoanza, Idunda mpaka Mbalamaziwa wanafuatilia kwa umakini sana pengine kufahamu commitment ya Serikali, ni lini sasa kwa maana kama ni mwezi au kama ni mwaka wa fedha watapata matumaini ya kupata huu mradi wa umwagiliaji kutokana na changamoto kubwa sana ya ukame kwenye maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji na Serikali pia inatambua kwamba eneo la Mufindi ni kati ya maeneo ambayo kuna wakulima wengi na uzalishaji wake utaongeza tija kwenye kilimo cha nchi yetu ya Tanzania. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayokuja kwa maana kuanzia mwezi Julai tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba uhakiki huo unakamilika, tukisha-establish mahitaji baada ya hapo sasa tutakwenda kwenye hatua inayofuata ambayo itakuwa ni hatua ya ujenzi kutokana na mahitaji.

Mheshimiwa Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge na kwamba zoezi hilo litaanza mapema mwezi wa Saba ambapo uhakiki huu utafanyika na baadaye tutaenda katika hatua ya ku-establish mahitaji.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru; kwenye Wizara hiyo hiyo ya Ujenzi na Uchukuzi tuna changamoto kubwa sana ya barabara ya Mafinga – Mgololo na Nyororo – Mtangwo ambazo zimeahidiwa kuanzia Serikali Awamu ya Nne mpaka Awamu ya Tano, na tarehe 26 Aprili, 2021 Serikali Awamu ya Sita imetoa commitment letter kuanza kujenga barabara hizo.

Nataka kujua ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi hii ya kuwajengea barabara wananchi Mufindi Kusini ili waweze kunufaika na barabara hizo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliamuahidi Mheshimiwa Mbunge na ni ahadi ya viongozi wa Kitaifa tangu Awamu ya Kwanza kwamba barabara hii ambayo ni barabara kuu lakini ni barabara kimkakati kwamba tutaijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge endapo bajeti ambayo tunaenda kuipitisha itapitishwa bila mabadiliko, barabara hii imeweza kuwekwa kwenye mpango ili iweze kujengwa kwa kiwango lami hasa tukizingatia kwamba sehemu kubwa ya mazao ya mbao tunayoyaona Tanzania yanatoka katika eneo hilo.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana ya maji kwenye Kata ya Mtambula katika Jimbo la Mufindi Kusini; je, Serikali haioni wakati umefika sasa kuwapelekea maji sasa wananchi wa kata hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari tumeona umuhimu na tupo katika taratibu za kuhakikisha hayo maeneo uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, tunayaletea maji safi na salama yakiwa bombani.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na kupitisha kwenye mfumo wa EPC katika zile barabara saba, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Mafinga - Mgololo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara tajwa ipo kwenye evaluation, Mgololo - Mafinga.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi wanayofanya ya kuhamasisha VETA katika nchi yetu.

Nataka kufahamu tu kwa ufupi ni lini Serikali inakwenda kutekeleza ujenzi wa VETA pale Mufindi, ikizingatiwa kwamba sasa tarehe 29 Aprili, Baraza la Madiwani limeamua VETA ikajengwe Nyololo, lini utekelezaji wake unafanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kihenzile, alikuwa anafuatilia suala hili kwa karibu. Mheshimiwa Kihenzile wewe mwenyewe ni shahidi nadhani tumeshawahi kuonana siyo mara moja, siyo mara mbili na umeshawahi kuja ofisi zaidi ya mara moja kwa ajili ya suala hili. Kwa vile tayari mmeshapitisha kwenye Baraza lenu la Madiwani ambalo ndilo lenye mamlaka ya kupanga wapi chuo hiki kijengwe. Nikuondoe wasiwasi iwapo Serikali itapata fedha, kipaumbele kitakuwepo katika maeneo haya ya Mufindi kwa sababu tunajua kule kuna shughuli nyingi sana ambazo zinahitaji masuala haya ya ufundi kuweza kuzingitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nikuondoe wasiwasi nalo hili tunalifahamu tutalitilia mkazo kwa karibu zaidi. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na kupitisha kwenye bajeti hii inayoendelea lakini bado barabara ya Mafinga – Mgololo na Mgololo – Mtwango hazijaanza kujengwa. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Kihenzile Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilipangiwa bajeti. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini kwamba tayari mkandarasi alishapatikana na kinachomsumbua pia kuanza hii kazi ni kwa sababu tu ya hali ya hewa na Mheshimiwa Mbunge nilishamuhakikishia yeye mwenyewe kwamba tayari tumeisha mpata mkandarasi na tayari ameishaandaa vifaa lakini hawezi kuanza kwa kweli ujenzi kwa mazingira ya Jimbo lake lina mvua nyingi sana lakini mara tu mvua itakapokatika mkandarasi ataanza kujenga kwa kiwango cha lami kwa bajeti ambayo tulikuwa tumeipanga kwa mwaka huu unaoendelea, ahsante sana.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali iliahidi kuanza kujenga barabara ya Mafinga – Mgololo ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu. Tunashukuru kwa sababu, tayari wamesema itaanza kujengwa: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ni: Je, ni lini mchakato wa EPC + F utakamilika ili barabara ya Mafinga – Mgololo ianze kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mafinga kwenda Mgololo imeingizwa kwenye Mpango wa EPC + F. Kama Wizara, upande wa ufundi kwa maana ya engineering, yaani Engingeering Procurement na Construction, tumeshakamilisha, na sasa ziko zinachakatwa na Wizara ya Fedha, na baada ya hapo basi taratibu zinazofuata za manunuzi zitaanza, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kuna changamoto kubwa sana kwenye ukanda wa joto wa Mufundi kwenye zile kata Saba nadhani unazifahamu Mheshimiwa Naibu Waziri, Nyororo, Maduma, mbalamaziwa, Ihoanza, Itandula pamoja na Idunda;

Je, ni lini sasa Serikali watatuletea scheme za umwagiliaji ili wananchi wa pale waweze kulima kipindi chote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika,napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja kati ya kazi kubwa ambayo tutaifanya katika mwaka wa fedha ujao ni kuhakikisha scheme zote za umwagiliaji tunazozijenga zinakuwa na chanzo cha maji ili wakulima waweze kulima mwaka mzima. Mheshimiwa Mbunge katika bajeti inayokuja maeneo uliyo yataja tutachimba mabwawa kwa ajili kuanza scheme za umwagiliaji ili wananchi wetu waweze kulima mwaka mzima.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ya kuahidi kuleta magari mawili kwenye hivi vituo viwili cha Mtwango pamoja na cha Mgololo. Swali langu la nyongeza ni moja.

Je, kwa kuwa wananchi katika maeneo haya wameonesha jitihada kubwa za kuanza kujenga vituo hivyo vya afya, Serikali iko tayari kuleta fedha ili vikamilike mara moja kutokana na uhitaji mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge amewasilisha hoja hizi za Vituo vya Afya vya Mtwango na Mgololo. Niwapongeze wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini kwa kuanza kujitolea nguvu zao. Nawahakikishia kwamba Serikali imeshaweka kwenye mpango wa kupeleka fedha ili kukamilisha vituo hivi vianze kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa. Kutoka Makambako mpaka unaingia Mafinga hali ya usalama sio nzuri kwa sababu hakuna Kituo cha Polisi na tayari jitihada zimekwishaanza kufanywa na wananchi kwa kutenga eneo na hata mimi mwenyewe Mbunge kupeleka cement. Je, Wizara iko tayari kupeleka fedha kuhakikisha kwamba Kituo cha Polisi cha Nyololo kinakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, kwa jitihada ambazo zimekwishafanywa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake wizara itamuunga mkono kukamilisha kituo hicho, nashukuru.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mufindi Kampuni ya Ekaterra imeinunua Kampuni ya UNILEVER jambo ambalo limeacha malalamiko makubwa ya wananchi kukosa stahiki zao. Je, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu haioni umuhimu wa kuwasaidia wananchi hawa kumaliza malalamiko yao, ikiwa ni pamoja na kufika pale ili waendelee kunufaika na Taifa lao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwamba suala hili Mheshimiwa Kihenzile amekuwa analifuatilia kwa muda mrefu la kampuni hiyo ya UNILEVER baada ya kuingia mkataba wa kwamba sasa kampuni inakuwa winded up na kuchukuliwa na kampuni nyingine. Utaratibu uliopo kampuni inaponunuliwa au inapoenda kufilisika wajibu wa kwanza ni kuhakikisha wametambua madeni lakini pia kwa maana ya liabilities pamoja na assets zilizopo. Kwa wafanyakazai hatua ya pili itakuwa sasa ni kulipa madeni ikiwemo madeni ya wafanyakazi kwenye kampuni husika, hata kama kuna transfer ya umiliki, jambo la kulipa madeni ambayo ni liabilities ni la msingi na ni la kuzingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwenye eneo hili la kesi ya UNILEVER Mheshimiwa Mbunge nimueleze tu kwamba kuna hatua mbili ambazo Ofisi ya Waziri Mkuu ilichukua. Hatua ya kwanza Kamishna wa Kazi alikutana na wafanyakazi hao na kuchukua malalamiko yao. Wapo ambao walifukuzwa kazi wakati huo bila kufuata utaratibu wa retrenchment tuliagiza warudishwe kazini. Pia lipo kundi la pili la wafanyakazi ambao walilipwa walikuwa zaidi ya 500 na hatua ya tatu kundi la tatu kwenye wafanyakazi hao ni wale ambao bado maslahi yao yalikuwa hayajaelezeka vizuri, wapo ambao walikuwa wana mikataba na wasiokuwa na mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambayo tumeichukua tuliwaelekeza waende CMA ambapo shauri linaendelea mpaka sasa katika Mahakama ya Kazi na hatua ya tatu ambayo tunaenda kuichukua ni kuhakikisha baada ya maamuzi ya CMA na wale ambao walikuwa bado hawajaainishwa kwamba wako kwenye eneo gani la vipengele vya mikataba, wakutane na Kamishna wa Kazi ili haki zao ziweze kulindwa. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kule Mufindi Kusini kuna Mabwawa ya Nzivi, Ngwazi pamoja na Kihanga; na mabwawa mengine kama yale ya Ihoanza ambayo yanachimbwa. Changamoto kubwa ambayo ilikuwepo pale ni mambo mawili; suala la vifaranga takribani milioni tano na zana za uvuvi: Je, Serikali iko tayari kupeleka vifaranga takribani milioni tano pamoja na mikopo ya vifaa vya uvuvi vya kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Uzuri ni kwamba, jambo hili ambalo amelizungumza Mheshimiwa Kihenzile, alishafika mpaka ofisini kwetu na tulizungumzanaye mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri na wataalamu wetu. Tulishamuahidi kwa sababu, kwa sasa tuna vifaranga kama milioni 15 na tuliahidi katika jimbo lake kupeleka minimum ya vifaranga milioni nne. Kwa hiyo, hilo lipo katika mpango, ikiwemo zana za kisasa kulingana na tutakavyovipata katika mwaka wa fedha unaokuja, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliongeza zao la parachichi kama zao la kimkakati na katika kutimiza ajenda hiyo, iliamua kuanza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata parachichi kilichopo Nyololo Mufindi ili isaidie mikoa yote ya Nyanda za juu Kusini. Hata hivyo mpaka sasa hivi ujenzi haujaanza.

Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya mradi huu muhimu sana kwa wananchi wa Mufindi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika bajeti yetu ya mwaka 2022, 2023 tuliweka mpango wa kujenga common use facilities mbili. Moja itajenga Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro na moja inajengwa nyololo Jimboni kwa Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa njema Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekamilisha taratibu zote za awali na muda si mrefu mkandarasi atapatikana na kazi ya ujenzi wa common use facilities itaanza. Kazi hii ikianza itawapa nafasi wakulima wote wa parachichi kukusanya maparachichi yao sehemu moja, tukafanya collection, tukafanya grading na sorting na baadaye packaging ili maparachichi yetu ya Tanzania ionekane duniani kwamba ni produce of Tanzania kuliko hivi sasa ambapo maparachichi mengi yanakwenda katika nchi za jirani. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Moja; kwa kuwa wananchi wa Mufindi Kusini wameamua kuwa na shughuli mbalimbali mbadala ili wasikate miti na kuharibu vyanzo vya maji. Je, Serikali iko tayari sasa kuwaunga mkono na itaanza lini kuchimba mabwawa ili waweze kufanya shughuli zingine mbadala kama za uvuvi katika eneo la Mufindi Kusini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuzingatia unyeti na uzito na umuhimu mkubwa wa Mto Ruaha kwenye Taifa letu. Je, Serikali iko tayari kufanya elimu kwenye Mamlaka za Serikali Mitaa ili itoe fursa kwa wananchi kujua pengine umuhimu wa kuhifadhi mto huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Kihenzile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uchimbaji wa mabwawa katika maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. Kwanza nimpongeze kwa sababu alishiriki katika hili kuona kwamba tafiti inakamilika na kupita Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, tafiti ile Mheshimiwa Mbunge imeshakamilika na tunatarajia mwaka ujao wa fedha tuweze kuchimba mabwawa maeneo yale ambayo tunaona yatakuwa ni msaada kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa suala la fedha kwa ajili ya kuendeleza semina mbalimbali kutoa elimu kwa jamii; kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, tayari sisi kama Wizara tumeanza kutoa elimu kwa hasa viongozi wa vyombo vya watumia maji, lakini sasa hivi tutakwenda zaidi kwa viongozi na makundi mbalimbali na jukumu hili litatekelezwa na Bonde la Rufiji.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Iliwahi kuahidiwa hapa Bungeni juu ya kutupatia minara kwenye Kata za Maduma, Kitasengwa, Kasanga na Makungu na Kasanga kuna kituo cha afya: Je, lini Serikali itatimiza ahadi hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa David Kihenzile, ameshaleta changamoto hii na tunafahamu kwamba eneo la Kasanga kuna kituo cha afya, na ili kuhakikisha kwamba kituo kile kinafanya kazi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, ni lazima tufikishe huduma ya mawasiliano. Maeneo haya ya Maduma, Makungu pamoja na Kasanga tumeshaingiza kuhakikisha kwamba yanatekelezwa ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma ya mawasiliano, ahsante sana.

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa hiyo. Kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kukubali kuanza kusaini kesho barabara karibu nane kwa mfumo wa EPC and F, maana Bungeni hapa imezungumzwa muda mrefu kuhusu hilo suala; je, mara baada ya kutangaza habari ya kusaini hiyo kesho, ni lini ujenzi utaanza kwa barabara hizo ikiwemo Mafinga – Mgololo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niseme, barabara ambazo tunategemea kutia sahihi ni barabara saba. Pengine tu nilijulishe Bunge hili kwamba kazi kubwa ambayo tulikuwa Mheshimiwa Rais anakwenda kuifanya ni kusaini mikataba ya hizi barabara zote saba ambazo tumeziongelea sana hapa za EPC + F na kazi hiyo itafanyika kesho hapa Dodoma Jakaya Kikwete. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu pengine Wabunge wengine hawajapata taarifa, tungetamani pia Wabunge wote ambao hizo barabara zinapita waweze kushuhudia kitu kikubwa ambacho kinafanyika kuanza kujenga hizo kilometa 2,035 kwa mpigo. Muda ungetosha ningeweza kuwakumbusha zile barabara lakini kwa sababu ya muda, ni hizo barabara zote saba ambazo kwa ruhusa yako labda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge ni barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Ifakara – Lupilo – Malinyi – Kilosa – Kwa Mpepo hadi Lumecha Namtumbo, nyingine ni barabara ya Igawa – Mbeya Mjini – Songwe hadi Tunduma, barabara ya Kongwa – Kibaya – Orkesumet – Rosinyai hadi Arusha, barabara ya kutoka Karatu - Mbulu – Hydom – Sibiti – Lalago hadi Maswa na mwisho ni barabara ya Mafinga – Mtwango – Mgololo, ahsante. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani Jimbo la Mufindi Kusini haikujengewa kituo cha afya hata kimoja, wakati maeneo mengine yamepata fursa hiyo. Wananchi wa Mufindi Kusini wana uhitaji mkubwa.

Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya cha Mtwango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kujenga kituo cha afya Mtwango. Kwa hatua za mwanzo naomba nimuelekeze Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa kutuma timu kwenye eneo la Mtwango na kufanya tathmini na kuona mahitaji ambayo yako katika Kata ile, baada ya kufanya tathmini hiyo aiwasilishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Ili tuweze kuona ni namna gani tunapeleka fedha.

Mheshimiwa Spika, nimtoe mashaka Mheshimiwa Kihenzile Serikali hii ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha kujenga vituo vya afya kwenye maeneo yote ya kimkakati nchini ikiwemo kule Kata ya Mtwango Jimboni kwake.

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Niishukuru kwanza Wizara kwa kazi kubwa sana ambayo wameifanya, wamekwishaanza. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; kwenye Kata ya Kasanga ndiyo Makao Makuu ya Tarafa yetu na ndipo kilipo kituo cha afya ambapo wanatibiwa wananchi wengi, hakuna mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani kuweza kusaidia wananchi wetu ili hata mtu akiwa hospitali aweze kuwasiliana na ndugu zake?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni upi mkakati wa Serikali ili kupunguza multiplicity ya minara kila sehemu? Kwamba, tuwe na mnara mmoja pengine na networks nyingine waweze ku-hire pale, ni upi mkakati wa Serikali katika jambo hili? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakiposa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tunapokea ombi la Kata ya Kasanga ambayo, kama alivyoeleza mahitaji yake ni makubwa na kwa sababu ya huduma ambazo ziko pale. Nimuahidi kwamba, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tunazo kata na tunayo maeneo ambayo tutayapelekea huduma maalum. Nalichukua hili eneo na tutawaagiza watu wa UCSAF kwenda kufanya tathmini na kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, tutajenga mnara kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ni kweli kwamba, si jambo zuri kuwa na minara mingi katika mazingira tuliyonayo. Sisi Serikali kupitia Sheria ya EPOCA tunawahamasisha na kuwashawishi watoa huduma wachangie minara badala ya kila mtoa huduma kuwa na mnara wake. Changamoto iliyopo ni kwamba, baadhi ya maeneo na hasa ya vijijini ambayo watumiaji wa mtandao ni wachache, kiuchumi kuna changamoto ya ku-share mnara badala yake wana-opt kuachiana maeneo ili watoe huduma wasigawane wale watumia huduma wachache.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali tuko katika mchakato wa kuliwezesha Shirika letu la Mawasiliano - TTCL kumiliki minara na kwa sababu ni shirika la Serikali ni rahisi kuwabana wakawavutia wawekezaji watoa huduma wengine wakapanga kwenye minara ya TTCL badala ya ile ambayo inaendeshwa na watoa huduma ambayo kwa kweli, inaendeshwa kibiashara na inakuwa ngumu kwa maeneo ya vijijini ku-share kwa sababu ya gharama za uendeshaji. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbeya kwenda mpaka Dar es Salaam eneo la changarawe maarufu kama Jinja wakati wote limekuwa likisababisha ajali na kuuwa Watanzania walio wengi; na hivi majuzi Watanzania takribani 20 walifariki. Serikali ina mkakati gani kufanya tathmini hata ikibidi matengenezo kuhakikisha kwamba eneo lile haliendelei kuchukua roho za watu ambao hawana hatia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kutoa pole kwa wananchi wengi ambao siku za karibuni tumesikia wamepoteza maisha katika eneo hilo la Majinja katika Wilaya ya Mufindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukweli kwamba eneo hili limeendelea kusababisha ajali nyingi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeshawaagiza makao makuu TANROADS pamoja na TANROADS Mkoa wa Iringa kuunda timu ambayo itakwenda kufanya study kujua tatizo ni nini ambalo limeendelea kusababisha ajali katika eneo hilo, ili kama ni suala la utaalamu kwa maana ya miundombinu ya barabara timu hiyo iweze kuishauri Serikali nini kifanyike ili kuondokana na ajali kama zinasababishwa na namna yoyote ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa hatua za haraka tumewaagiza TANROADS Mkoa wa Iringa waweze kuweka alama nyingi za kutoa tahadhari kwamba eneo hili ni hatari ikiwa ni kuona pia uwezekano kama wanaweza kuongeza matuta ili kupunguza ajali ikiwa hiyo ni hatua za muda mfupi, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Mufindi kwa ujumla makao yake makuu iko kwenye Kata ya Mtwango, lakini eneo hilo mpaka sasa pamoja na kwamba imehamishiwa makao makuu Mafinga Kata ya Mtwango yenye population kubwa haina kituo cha afya; je, ni lini Serikali sasa itapeleka kituo cha afya pale kwa ajili kuhudumia kata hiyo na kata jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kata hii ya Mtwango ni kata kubwa na ina wananchi wengi na Mheshimiwa Mbunge ameisemea mara nyingi na tumekubaliana tunatafuta fedha kwenda kujenga kituo cha afya katika kata hiyo, ahsante.