Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rwegasira Mukasa Oscar (23 total)

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na takwimu nzuri za Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu matukio ya uporaji kwa watu wanaotoka kuchukua fedha tasilimu benki, ni miongoni mwa matukio mengi yanayotokea hivi sasa na kwa kuwa kuna imani na minong‟ono miongoni mwa wananchi kwamba watumishi na wafanyakazi wa benki kwa namna fulani wanahusika na kuwezesha uhalifu huu. Serikali inatoa kauli gani kuhusu imani hiyo na minong‟ono ya Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa baadhi ya matukio ya uporaji wa pesa, watu wanavyotoka kuchukua pesa tasilimu benki yanahusisha matumizi ya pikipiki na kwa kuwa pikipiki zinatoa ajira halali kwa vijana wa bodaboda, lakini wachache wanatumia kuichafua na kuumiza Watanzania. Serikali inasema nini kuhusu kushindwa kwake kuwadhibiti hao wachache ambao wanatumia vibaya vyombo vya usafiri ambavyo vinatoa ajira na masilahi mengine kwa Watanzania katika kudhibiti hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na wizi wa benki ni kweli kumetokea na wimbi la kuiba benki katika kipindi cha karibuni, lakini wananchi wamechukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kufanya kazi karibu kabisa na benki hizo ili kuona kwamba kama kuna miongoni mwa wafanyakazi ambao sio waaminifu waweze kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile siyo tu miongoni mwa wafanyakazi ambao siyo waaminifu, lakini pia wale ambao wana kawaida ya kuchukua fedha nyingi, ni vizuri kabisa wakafanya utaratibu wa kuweza kuwasiliana na polisi ili waweze kuwapa ulinzi. Wakati mwingine taarifa hizi zinatoka miongoni mwa sehemu au makampuni ambayo yanajihusisha ya biashara mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kutoa wito kwa makampuni yote au wafanyabiashara wote ambao wanaweza kusafirisha fedha nyingi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, walitaarifu Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi litatoa ulinzi ili kudhibiti hali kama hiyo, wakati huo huo Jeshi la Polisi likiwa linafanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba, linawatia mikononi na kuweza kuwapeleka katika vyombo vya sheria wale wote ambao wanahusika kwa njia moja ua nyingine na limeshaanza kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na suala la pikipiki. Polisi haijashindwa kuwadhibiti hawa watu wachache ambao wanatumia vibaya fursa hii ya vijana ambao wana pikipiki, siyo tu bodaboda hata pikipiki za kawaida zimekuwa zikitumika katika uhalifu mbalimbali. Ndio maana sasa hivi kuna mazoezi mbalimbali yanaendelea nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba wanazikagua pikipiki hizi ili kuweza kubaini uhalali wake, lakini pia uhalali wa wale ambao wanaendesha pikipiki hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kipindi hiki ambapo Polisi inaendesha zoezi la kuweza kuhakiki pikipiki hizi ili kuweza kuhakikisha kwamba, sheria zinafuatwa na waendesha pikipiki hizi iwe kwa utaratibu wa wafanya biashara kwa maana ya boda boda au utaratibu wa kutumia pikipiki kwa matumizi ya kawaida.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri yenye kuakisi nia ya Wizara na Serikali kushirikiana nasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la msingi, imeelezwa vizuri kabisa kwamba uvunjifu wa amani ni moja ya matokeo hasi ya kukosekana kwa fursa hizi za wananchi wa Mavota kushiriki kwenye uchumi uliowazunguka. Kwa sababu suala la uvunjifu wa amani si suala la kusuburi, ni la haraka, je, Serikali na Wizara iko tayari kutoa kauli inayothibitisha uharaka wao katika kuja kuzungumza na wananchi wa Mavota?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua ambazo Serikali imechukua kupitia Wizara yetu ni pamoja na kuhakikisha kwamba uchimbaji salama na makini unafanyika kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo, ofisi yetu iko tayari kwenda kuzumgumza na wananchi kuwahakikishia amani zaidi kwenye shughuli za uchimbaji eneo la Mavota.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa wakandarasi wa REA wanalalamika hawajalipwa pesa mpaka juzi na hili linaweza kuathiri uanzaji wa Awamu ya III kwa sababu shughuli ya Awamu ya II haijakamilika, Serikali inatoa kauli gani?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nipate ufafanuzi vizuri, tunataka tuwatambue wakandarasi wote wanaolalamika kwamba hawajalipwa pesa ili tujue wanalalamikia nini, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inawezekana kukawa na malalamiko kwamba baadhi ya wakandarasi hawajalipwa pesa lakini kwa takwimu tulizonazo wakandarasi kwa mara ya mwisho, miezi miwili iliyopita tumewalipa pesa kwa ajili ya kuanza kazi. Inawezekana kuna baadhi ya wakandarasi nao wanaweka pia subcontractors, inawezekana wanaolalamika ni wale subcontractors. Napenda nimhakikishie kwamba suala hili tutalifanyia kazi. Nimelichukua, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge tuone ni mkandarasi gani analalamika tuanze kulifanyia kazi mara moja.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ipo ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati akiomba kura kwa wananchi wa Biharamuro ya kujenga barabara kilometa 4 - 5 kwa kiwango cha lami kwenye Mji wa Biharamuro. Naomba kufahamu kutoka Serikalini kwamba utekelezaji wa ahadi hiyo umefikia wapi? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Biharamuro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi anayoongelea ni kweli ilitolewa na Mheshimiwa Rais na kwa kweli ahadi hiyo ilianzia kutoka Serikali ya Awamu ya Nne na ni kwa ajili ya eneo hilo lakini vilevile eneo jirani ambalo Mheshimiwa Dkt. Kalemani anatoka, ahadi hizo zote tutazitekeleza. Lini, itategemea na upatikanaji wa fedha kwa sababu utekelezaji wa ahadi hizo unahitaji rasilimali fedha. Kwa hiyo, naomba nikuahidi ahadi hizo tutazitekeleza na nikuahidi miaka mitano hii ambayo ndiyo tumepewa hii dhamana ya kuwajengea Watanzania miundombinu na kutekeleza ahadi zote ambazo viongozi wetu walizitoa nikuhahikikishie tutazitekeleza.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa idadi ya karibu vifo 12,000 vilivyosababishwa na ajali za barabarani kwa miaka hiyo mitatu vinaweza kulinganishwa na mauaji ya kimbari, mauaji ya halaiki, na majeruhi 44,444 ni sawa na kiwanda cha kutengeneza Watanzania kupata ulemavu wa viungo mbalimbali. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu kuja na suluhisho lenye mashiko na kutatua tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ajali za barabarani hasa za mabasi ya abiria zinashiriki sana kwenye kutengeneza vifo na majeruhi, tena kwa kiwango kikubwa kwa mara moja, Je, Serikali ina mkakati gani pia kudhibiti ajali za barabarani zinazohusisha mabasi ya abiria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kama ifuatavyo:-
Kwanza, tunajaribu kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Pia Jeshi la Polisi kupitia Askari wa Usalama Barabarani wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara na ukaguzi ili kuweza kuwabaini na kuwakamata wale ambao wanavunja sheria. Pia kumekuwa na utaratibu wa kutumia zile kamera za tochi ambazo zinabaini wale ambao wanakiuka taratibu za usalama barabarani ikiwemo kuongeza kiwango cha speed zaidi ya kilichowekwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa pia tukiangalia mchakato wa kuangalia utaratibu wa utoaji leseni vile vile ili kudhihirisha kwamba kwa kushirikiana na mamlaka nyingine watu wote ambao wanaendesha vyombo vya moto barabarani basi wawe ni ambao wana leseni zilizopo kisheria na isiwe kuzipata kinyemela. Pia kuna utaratibu wa kuchukua hatua stahiki kwa wanaovunja sheria siyo tu wale ambao wanaendesha vyombo hivi, hata wasimamizi wa sheria hizi mara moja inapotokea kutaka kulitia madoa Jeshi la Polisi basi hatua zimekuwa zikichukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mifumo ambayo tumejaribu kuanza nayo sasa hivi, mifumo ya matumizi ya point ambayo bado haijaanza ipo katika utaratibu mzuri, nadhani muda siyo mrefu sana tutaweza kutumia ili kuwafanya sasa watu wawe na hofu zaidi ya kuvunja sheria hizo za barabarani. Pia kuna utaratibu wa tozo za papo kwa papo na hii imesaidia sana kiasi fulani kudhibiti ajali hizo. Tuna utaratibu wa kutumia TEHAMA kwa ajili ya kudhibiti ajali za barabarani. Pia tuna mipango, maana alitaka mipango ya sasa hivi na baadaye, tunayo mipango ya matumizi ya kamera ambayo nayo vile vile ipo katika michakato na ukaguzi wa lazima kwa magari yote. Kwa hiyo, hizo ni baadhi ya hatua ambazo Serikali imekuwa ikichukua katika Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Polisi cha Usalama Barabarani kudhibiti hali ya ajali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi fulani imepungua, na ndiyo maana ukiangalia kwenye takwimu nilizozisoma kwenye swali la msingi utakuta ajali za barabarani zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inashiriki kwenye mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Taifa, lakini iko haja ya kutafuta namna ambavyo Wilaya na Halmashauri ambazo zinapakana na nchi jirani zinazoshiriki kwenye Jumuiya hii kuzitumia fursa ambazo wigo wake unaishia kwenye Wilaya zinazopakana na nchi hizo.
Kwa kuwa Biharamulo inapakana na Rwanda kijiografia na kimiundombinu; na kwa kuwa wananchi wa Biharamulo kwa kushirikiana na Mbunge wao wameshazitambua fursa lakini wanahitaji nguvu ya kidiplomasia ya ngazi ya kitaifa kuhakikisha tunazichukua; je, Waziri yuko tayari kuleta nguvu ya uchumi wa kidiplomasia Biharamulo kuzungumza nasi ili tuzitumie?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi akiwa pamoja na wataalamu wa diplomasia ya uchumi kutoka Wizara yake ili tukae na wataalam wa Biharamulo tuzitumie fursa hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Wilaya na jamii ambazo zipo mipakani zina nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika fursa zinazopatikana kwa mtangamano wa Afrika Mashariki na ni kweli kabisa nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara iko tayari kabisa kuangalia ni namna gani inasaidia jamii na Wilaya zinazopakana na nchi za jirani ili kuweza kutumia fursa hizo. Naomba nimweleze tu kwamba, hilo siyo kwamba ndiyo linaanza sasa, ni kwamba kama nilivyoeleza katika swali la msingi, tayari Wizara inatoa elimu na ufahamu kwa wananchi kutambua fursa zilizopo ili waweze kuzitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu Wizara kuandamana naye ili kufika Jimboni na kuangalia hizo fursa, naomba nilichukue hili, nitamshauri Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ili waangalie namna ya yeye au Naibu Waziri na timu yake waweze kwenda kwa Mheshimiwa Mbunge ili waweze kuangalia namna ya kutumia hizo fursa kwa ukaribu zaidi.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kazi ya kuboresha miundombinu ya maji kwenye Mji wa Biharamulo imefikia kwenye upembuzi yakinifu kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini hatua ya kupata fedha bado iko mbali; na kwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji ni dharura sasa hivi Biharamulo, wananchi wanapata maji kwa wiki moja katika wiki nne. Kwa hiyo wiki moja yanapatikana wiki tatu hayapatikani. Je, Naibu Waziri au Waziri wako tayari kuambatana na mimi twende kufanya tathmini ili kuona namna ya kutatua hali ya dharura wakati tunasubiri mradi mkubwa ufikie wakati wake?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, Mheshimiwa Mbunge Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017, Wilaya ya Biharamulo imetengewa Sh. 2,267,018, 000/= kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji. Kwa hiyo, namwomba sana, kwenye Vikao vya Madiwani, auekeze Uongozi wa Halmashauri ya Biharamulo wajaribu kuangalia matumizi ya hizi fedha ambazo tumezitenga kwa kufanya utafiti kama ni kuchimba visima, kama kujenga mabwawa au kama kuna maeneo ambayo yanaweza yakawa na maji ya mtiririko ili kuweza kutekeleza miradi kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama fedha hazitatosha, basi tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili kuona ni jinsi gani sasa tutashirikiana pamoja kuhakikisha kwamba, wananchi hawa wa Biharamulo, ambao wanapata shida ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu hasa kwa kuzingatia kwamba, mradi huu utakaoleta ufumbuzi wa kudumu bado usanifu haujakamilika. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kusikia pia kauli ya Serikali kuhusu pia wachimbaji wadogo wa Biharamulo wakiwemo wa Busiri, Kalukwete, Mavota, Kalenge na wale Nyanchimba Wilaya Chato kwa sababu nao wanapenda kusikia kauli ya kutengewa hekta kadhaa 500, 600 kama ilivyofanyika kwenye maeneo ya Geita.
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema na nitumie nafasi hii nikushukuru sana rafiki yangu Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo kwa sababu ni jirani yangu, maeneo ya Biharamulo mwaka jana tumetenga hekta 1332 kwa Mheshimiwa Oscar, lakini Mheshimiwa Oscar bado tunakutengea eneo pale kwenye Mgodi wa Tulawaka, pale Mavota tunafanya mazungumzo. Tumeshakaa na wewe na Mbunge wa Bukombe tumeainisha mahektari kama hekta 2100 tuzitenge kwa ajili ya wananchi wako, lakini bado nikushukuru sana kwa sababu umependa pia nizungumzie kwangu kule Chato. Kule Chato Kampuni ya Wakawaka
imeachia eneo takribani ya hekta mbili ambako wananchi wako wa Biharamulo na wangu tutawagawia kwa utaratibu huo huo.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwanza ni amani yangu kwamba wataalamu waliopelekwa kutoa ushauri wa kupelekwa Wilayani Chato ila wamepeleka Wilayani Biharamulo.
Pili maelezo kidogo tatizo hili limekuwepo kwa miaka mingi na tumekuwa tunapata majibu mara nyingi kutoka Serikalini ambayo kwa kweli hayajaweza kukidhi kulingana na ukubwa wa tatizo. Tulisikia swali la kisera kuelekea kwa Waziri Mkuu mwezi wa saba likapelekea kiti chako Mheshimiwa Naibu Spika kutoa maelekezo kwamba Serikali ichukue hatua na ilete majibu hapa.
Sasa swali langu kwa sababu hali halisi inaonesha kabisa kwamba tatizo hili ili likabiliwe kuna mambo matatu lazima yafanyike la kwanza utafiti ili kuja tatizo ni nini ambalo tayari...
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kufanya kikao maalum na Wabunge wa Mkoa wa Kagera ili tuone namna gani tunaweka mikakati ya kutafuta utashi wa kisiasa wa kukabili tatizo hili, lakini namna ya kutafuta na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi na hata private sector ndani ya Tanzania ili tukabiliane na tatizo hili? Kama uko tayari, upo tayari kwa muda wa karibuni, muda wa kati au muda wa mbali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilipotaja Chato nilisahau Biharamulo, lakini mimi ndiyo sijasoma kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Biharamulo nayo imo.
Kuhusu ombi lake la kufanya mkutano, tayari nimeshawasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ameahidi kwamba tukitoka kwenye Bunge hili atafanya mkutano na Wabunge wanaotoka Mkoa wa Mwanza vilevile Mkoa wa Kagera ili kuangalia namna ya kuweza kushughulikia tatizo hili, kwa hiyo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge tayari tumepokea na tutafanya haraka tuweze kukutana nao. (Makofi)
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Upo ushahidi wa matumizi yasiyo sahihi ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa viongozi wa Serikali na miongoni mwetu Wabunge. Kwa sababu Bunge na viongozi wa Serikali ni miongoni mwa makundi ya jamii na taasisi zenye wajibu wa juu kabisa wa kulinda lugha hii na kwamba inaashiria tatizo hili haliko kwenye vyombo vya habari tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inasema nini kuhusu upana wa tatizo hili hasa kwa wakati huu ambapo inatengeneza sera hiyo?
Pili, kwa sababu matumizi, kwa mfano ya neno “hichi” badala ya “hiki,” “nyimbo hii” badala ya “wimbo huu,” uchanganyaji wa lugha ya Kiingereza kwa kiwango kilichokithiri kwenye sentensi za Kiswahili, vinakera. Tunaomba kujua ni lini sera hii inakuja kudhibiti hali hii inayoendelea? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Oscar Mukasa, Mbunge wa Biharamulo kwa jinsi ambavyo amejitahidi kuonesha ukinara katika kuikuza lugha ya Kiswahili. Naomba kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na matumizi ambayo siyo sahihi ya lugha yetu ya Kiswahili na wengi tumekuwa tukishuhudia kwa mfano “hiki kikao” wengine husema “hichi kikao,” “hiki kitu”, “hichi kitu” na pengine kama alivyosema katika maelezo yake kwenye swali lake la msingi, ni kwamba hata watoto kwa sasa ukifuatilia utaona, “hiki kitu” kwa sababu tunatumia “hichi kitu,” sasa na wao wameanza kusema “hiko kitu.” Wameibadilisha, badala ya “hiki kitu,” sasa wanasema “hiko kitu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile siyo katika Kiswahili tu, watu wamekuwa wakichanganya Kiingereza, lakini hata lugha zetu za asili vilevile wamekuwa wakichanganya Kiingereza. Kwa mfano, unaweza kumsikia mtu anasema “infact kwa kweli angambila nshomile.” Haya ni maneno ambayo yamekuwa yakichanganywa katika lugha za asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wito wa Serikali ni kwamba tulinde Kiswahili na pia tulinde lugha zetu za asili kwa sababu zile lugha za asili ndipo tunapoweza kupata maneno ya kuongeza kwenye Kiswahili pale ambapo tutakuwa hatuna maneno mbadala ya Kiingereza. Kwa hiyo, tulinde lugha zetu zote, lugha ya Kiswahili na pia lugha ya asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea tu ni kwamba Serikali ipo tayari kupitia BAKITA kuja kutoa semina katika Bunge hili ili kusudi tuweze wote kwa pamoja kufuatilia na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha. Nalisema hili kutokana na kwamba kuna visababishi ambavyo vinapelekea matumizi yasiyo sahihi au visababishi ambavyo vinaweza kumwezesha mtu atumie lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika nchi za Afrika Mashariki wanaotumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili ni watu wapatao milioni mbili hadi milioni 15 kwa mujibu wa takwimu. Lakini wengi wao kuanzia milioni 50 hadi milioni 150, wengi wanatumia Kiswahili kama lugha ya pili. Kwa hiyo, wakati mwingine inatokea tafsiri ya lugha zile za asili kwa Kiswahili.
Vilevile kuna kisababishi kingine ambacho ni jinsi gani ile lugha ya asili inashabihiana na lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, Kiswahili kina „r‟ na kina “l” lakini zipo lugha ambazo hazina „r‟ na hazina „l‟. Kwa mfano, kuna lugha moja ya asili isiyokuwa na „r‟, akitaka kusema „anataka kula‟ anasema „nataka kura‟ na mwingine akisema naomba kura anasema „naomba kula.‟ Kwa hiyo, hivi ni visababishi ambavyo vinapelekea matumizi sahihi au yasiyo sahihi kwa lugha ya Kiswahili.
Jambo lingine ni dhamira ya mtu ya kutaka kuwa kinara katika kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, tunavyomwona Mheshimiwa Rwegasira, yeye ana dhamira ya kutakakuwa kinara. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na viongozi tuwe na hii dhamira.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ile tabia ya kujisomea vitabu vya Kiswahili, magazeti, kamusi pamoja na kutumia miongozo mbalimbali. Hivi vyote hupelekea mtu kuweza kuongea Kiswahili kwa ufasaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linahusiana na Sera ya Lugha…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naomba ufupishe kidogo jibu linalofuata.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu inaendelea kukusanya maoni ya wadau kuhusiana na Sera ya Lugha ili kusudi kuweza kupata changamoto ambazo zinaikabili lugha yetu ya Kiswahili, lakini vile vile kujua ni jinsi gani tutazingatia masuala mbalimbali katika Sera ya Lugha na hivyo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2016/2017 tunatarajia kwamba rasimu ya kwanza ya Sera ya Lugha itakuwa imekamilika na hivyo tuipeleke katika hatua za juu kwa ajili ya maamuzi.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa mujibu wa takwimu tulizopewa kwenye majibu na Mheshimiwa Waziri, asilimia 80 ya waendesha bodaboda hawana leseni, jambo ambalo linawafanya waishi kwenye mzunguko wa kukimbizana na polisi badala ya kuzalisha mali kwa ajili kujenga uchumi wao na uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, Serikali iko tayari kuwasaidia kwa kuwawekea ruzuku ya kupunguza walau kwa mara moja kodi ya kulipia leseni angalau kwa nusu ili waweze kupata leseni kama hatua ya kwanza ya kuwasaidia ili tuweze kushirikiana nao kuongelea habari ya kuwahamisha kuwapeleka kwenye ushirika wa SACCOS na mambo mengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi twende Biharamulo kuziona fursa nyingine zaidi ya kuwaomba tu wajiunge kwenye SACCOS ambazo Serikali Kuu ikishirikiana na sisi tunaweza kuzitumia kuwatoa kwenye yale waliyonayo ili Biharamulo iwe mfano wa kusambaza hatua kama hiyo maeneo mengine ili kundi kubwa la bodaboda nchini tulisaidie liwe la ujasiriamali kweli kweli? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZAA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Mbunge kama ikiwezekana Serikali ifanye uwezeshaji, naomba nikiri wazi kwamba hatuwezi kusema kama Serikali tufanye uwezeshaji kwa watu wote, lakini tunakuwa na mikakati mbalimbali ya kufanya uwezeshaji. Mimi niwapongeze Wabunge wengi humu ndani ambao wamefanya initiatives katika Majimbo yao kuhakikisha vikundi mbalimbali vinahamasishwa na wao wanasaidia ku-chip in humo kwa ajili ya kuwasaidia vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mimi ninajua wazi kwamba kuna baadhi ya Halmashauri nyingine zina mipango mbalimbali yenye lengo la kuwasidia hawa vijana ili hatimaye, kama ulivyofanya Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lako ambapo na sisi tume-recognise shughuli na juhudi kubwa unazofanya katika Jimbo lako, nadhani tukifanya uhamasishaji sisi wengine tutafanya kwa kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yetu na hivyo tutaweza kuwasaidia hao vijana kwasababu lengo letu ni kwamba vijana waweze kukomboka katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kikubwa zaidi kama hatufahamu; bahati nzuri Ofisi ya Mama Jenista Mhagama katika Baraza la Taifa la Uwezeshaji, hata jana nadhani walikuwa wanafunga mafunzo yao, wameona kwamba jinsi vijana wengi wanavyokosa fursa hizi kwa kutokuwa na ufahamu wa kutosha na ndiyo maana wamesema sasa hivi wanataka kuzifanya programu zao kupitia maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu ya pili naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi nipo radhi, nilifika Biharamulo mara ya kwanza, lakini kama kuna jambo lingine mahususi tutakwenda tena ili kuwasaidia vijana wetu waweze kufika mbele katika suala zima la maendeleo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo kwa majibu yake mazuri kwenye swali hili la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaka kuiuliza Serikali ni kwa kiasi gani inaweza ikajipanga kupeleka juhudi za ziada ili kuhakikisha kwamba vijana wa Tanzania, hasa vijana wa kule Biharamulo wanaweza kufaidika na mikopo mbalimbali na kuweza kuwaboreshea shughuli za ujasiriamali wakiwemo vijana wa bodaboda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie kwamba, Mheshimiwa Mbunge ni kati ya Wabunge ambao walihudhuria maonyesho ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, na tumeshakubaliana na Mheshimia Mbunge kwamba baada ya shughuli hizi za Bunge kukamilika, Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na timu ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na yeye Mheshimiwa Mbunge watakuwa na ziara maalum kule Biharamulo ili kuangalia Serikali inaweza ikafanya nini kwa ajili ya maendeleo ya vijana na sekta nyingine.
Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, tumefunga maonesho ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, tunaomba sana tuendelee kuwasiliana ili fursa zilizopo ndani ya Serikali ziweze kuwafikia Watanzania wengi hasa wakipato cha chini na kipato cha kati wakiwemo vijana na kuweza kuwainua kiuchumi. Nakushukuru
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba kufahamu kwamba kwa maelekezo hayo ambayo Serikali imeyatoa kwa waajiri kutekeleza upandishwaji wa madaraja hayo.
Je, Serikali iko tayari sasa kuratibu suala hilo ili kuhakikisha kwamba tunafanya uhakiki wa walimu wote wenye malalamiko haya ili yapatiwe utatuzi.
Swali la pili, kwa sababu pia yako malalamiko kutoka kwenye Halmashauri zetu kwamba Walimu wanapokwenda kujiendeleza unatokea upungufu wa Walimu kwenye shule wanazotoka.
Je, Serikali iko tayari kutumia vizuri fursa ya Chuo Kikuu Huria ili yenyewe kwa ngazi ya Serikali Kuu iratibu namna ya kuwasaidia Walimu wajiendeleze kwa kupitia Chuo Kikuu Huria bila kuathiri uwepo wao kwenye shule zao? Ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hoja ya Mheshimiwa Oscar ni kwamba kufanya tathmini ya kuratibu vizuri mchakato huu, naomba tulipokee hili kwa sababu lengo kubwa ni kwamba kama Serikali tuna haja ya watumishi mbalimbali ambao malalamiko yao yapo yaweze kufanyiwa kazi kwa sababu tunajua yakifanyiwa kazi vizuri ndiyo wataweza kufanya kazi vizuri wanapokuwa ofisini mwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mukasa nadhani hii ni hoja ya mapendekezo na sisi tutaangalia jinsi gani tuweze kuratibu vizuri ili haki ya mfanyakazi iweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika eneo la pili ni kwamba jinsi gani tufanye kwamba tutoe maelekezo ya watumishi wote kada ya ualimu kutumia Chuo Kikuu Huria. Nadhani tuweke hili dirisha wazi kwa sababu kila mwalimu ana preference yake na kitu gani anachokihitaji, isipokuwa jambo la misngi ni lazima tuweke mipango mizuri lengo ni kwamba walimu watakapoenda kujiendeleza basi tusiwe na mapungufu makubwa katika maeneo yetu. Tunajua kwamba tatizo hili limekabili maeneo mbalimbali lakini hoja hii ni hoja ya msingi nadhani hili sasa katika mamlaka ya Serikali za Mitaa tutatoa maelekezo mahsusi ya kiutawala/kiofisi kwamba nini kifanyike kama walimu wangapi wanatakiwa wakiondoka wengine wabaki, ili watoto wasiathirike.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika mchakato wetu ambao tunaufanya hivi sasa lengo kubwa ni kuajiri walimu wapya tunajua kwamba tukiongeza idadi ya Walimu tutaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo hili ambalo liko hivi sasa katika Halmashauri zetu. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nataka kuweka msisitizo tu kwamba msimamo wa Serikali kuhusu wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu ni kwamba mwanafunzi anachagua mwenyewe mahali ambapo anataka kusoma, kwa hiyo utaratibu huo unawahusu watarajiwa wote wa vyuo vikuu ikiwa ni pamoja na walimu. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuweka tu mazingira mazuri ili wanafunzi waweze kuendelea kuwa na fursa ya kwenda mahali wanapotaka lakini Serikali haiwezi ikampangia mtu kinyume na matakwa yake. (Makofi)
HE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naishukuru Serikali kwa majibu yake, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja natambua jitihada za Serikali za kuweka mfumo kwa ajili ya kuwafikia walemavu, lakini suala la mfumo ni moja na suala la kufikisha huduma wanazohitaji kwa maana ya kuwafanyia upendeleo chanya (positive discrimination) ni lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni kwa namna gani Serikali sasa imeweza kuwafikishia rasilimali fedha na rasilimali mafunzo watu wenye ulemavu kwenye vikundi vyao, tofauti na kuwajumuisha kwenye vikundi vingine ambapo mahitaji yao mahususi hayawezi kutimizwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa namna gani na kwa kiwango gani Serikali inadhani inaweza kuwapatia nafuu kwenye yale mambo ya msingi kwa mfano Bima ya Afya. Tuchukulie mfano mlemavu wa ngozi akipata ruzuku kwenye bima ya afya una uhakika wa kuhakikisha anakingwa kwa bima, kitu ambacho anakihitaji kama Watanzania wengine lakini yeye anakihitaji zaidi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia na kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linauliza ni jinsi gani Serikali imeweza kuwapatia vikundi vya watu wenye ulemavu fedha. Niki-refer kwamba swali lake lilikuwa linauliza kwa habari ya vijana; kuna mfuko wa maendeleo ya vijana ambao mfuko huu unawawezesha vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee kidogo kwamba kinachotakiwa kufanyika ni kwamba vijana wanatakiwa wajiunge kwenye vikundi, wakishajiunga kwenye vikundi mbalimbali, kwenye maeneo yalipo wanatakiwa pia kuwe na SACCOS. Kwa hiyo, kama Serikali tunapeleka hela kwenye zile SACCOS halafu baada ya kupeleka hela kwenye zile SACCOS vile vikundi vinapewa kupitia zile SACCOS.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo kikubwa ambacho kinapatikana kwenye hivi vikundi ni kwamba wakati ule wa kurejesha wanatakiwa warejeshe riba ya asilimia 10. Katika hiyo riba ya asilimia 10, asilimia tano inabaki kwenye kikundi husika, asilimia mbili inabaki kwenye Halmashauri na asilimia tatu inaenda Serikalini. Kwa hiyo, hiyo ni njia mojawapo ambayo kama Serikali tunavipatia hivi vikundi fedha lakini pia kuna hii mifuko ya uwezeshaji kiuchumi wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kikubwa ambacho ninapenda niongelee hapa, nitoe wito kwa Halmashauri mbalimbali wawahamasishe watu wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi, kwa sababu hizi hazitolewi kwa matu mmoja mmoja. Wawahamasishe watu wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi, yakiwepo makundi ya vijana lakini pia na makundi mengine ambayo sio ya vijana ili waweze kunufaika na hizi fedha ambazo zinatolewa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameongelea kwa upande wa afya, kwa upande wa afya ametolea mfano wa watu wenye ualbino. Kwa upande wa watu wenye ualbino tayari Serikali imekwisha kuziagiza Halmashauri kwamba zinapoagiza dawa kutoka MSD zihakikishe zinajumuisha mafuta ya watu wenye ualbino katika madawa ambayo wanaagiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jingine la pili ameongelea kwamba kwanini Serikali haitoi bima ya afya kwa watu wenye ulemavu. Niseme wazi kwamba Serikali, hicho ni kitu ambacho kama Serikali tunakichukua, hatuna specific kwamba hii ni bima ya afya kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Lakini watu wenye ulemavu wasiokuwa na uwezo wanatibiwa baada ya kutambulika kwamba hawa watu hawana uwezo wa kugharamia mahitaji yao. (Makofi)
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja; eneo la Karukwete lina wachimbaji wadogo na lipo jirani kabisa na Kijiji cha Busiri kinachazungumziwa kwenye swali la msingi. Waziri yupo tayari kulijumuisha kwenye mkakati wa kuwawezesha kielimu na uwezeshaji?
Swali la pili; naomba kujua orodha ya mambo ya kiuwezeshaji yatakayofanyika kwa wananchi wa Karukwete na Busiri na lini tutawenda kuzungumza nao kuwafahamisha? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mukasa kwamba eneo la Karukwete nalo litaongezwa kwenye maeneo ya kufikiriwa kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la pili kwenye orodha ya huduma zitakazotolewa kwa msaada huu ni pamoja na kuwapatia ruzuku wachimbaji wadogo. Mwaka huu kwenye bajeti yetu mtaona tumetenga takribani shilingi milioni tisa za Tanzania pamoja na dola bilioni nne kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Pia tutaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuwa na uchimbaji wenye tija.
Pamoja na hayo bado Wizara yetu itatuma wataalam wa GST iyafanyie tathmini maeneo yote yatakayotengwa ili wachimbaji wawe na uhakika wa uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuongeza kwa manufaa ya wengine kwamba maeneo ambayo tutayatenga yapo mengi tunategemea kutenga eneo la Kasubwiya hekta 495, eneo la Nyaluyeye hekta 658, eneo la Matabe hekta 659 na maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutaendelea kuwawezesha.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ipo ahadi pia ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mji wa Biharamulo ya kuweka kilometa nne za lami wakati akituomba kura. Kwa kuwa sisi habari ya kilometa nne haina mambo makubwa yanayojumuisha mpaka habari ya vivuko kwenye Ziwa Victoria, Naibu Waziri anatuambia nini kuhusu utekelezaji wa haraka na wa siku za karibuni wa ujenzi huo wa ahadi ya Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwape pole watu wa Kagera kwa msiba mkubwa uliotupata na najua sio hilo tu, maana yake maeneo mbalimbali kule yatakuwa yameathirika hasa miundombinu ya barabara. Naomba nimhakikishie, kwa sababu ahadi hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na ndiyo maana Mheshimiwa Rais amejielekeza katika ukusanyaji wa mapato ili mradi kuhakikisha ahadi zake zimetekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu, kama mwenyewe anavyosema na kama Serikali yake inavyoonesha jinsi gani ukusanyaji wa mapato ulivyo, tutahakikisha barabara hii inatengenezwa, lakini sitaki kukwambia commitment ya tarehe, kwamba lini tutafanya hivyo, lakini katika kipindi hiki naamini itatengenezeka kwa sababu nguvu kubwa inaelekezwa kuhakikisha ahadi za Rais na utekelezaji wa ilani unatekelezeka katika kipindi hiki.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kwa kuwa Nyakanazi ni eneo lililokaa kimkakati kwa maana ni njia panda ya kuelekea Kigoma, Kahama na nchi za jirani za Rwanda na Burundi na kwa kuwa hivi karibuni kulingana na mipango ya Serikali iliyopo, kutakuwa na reli inatoka Isaka kwenda Rwanda.
Je, Naibu Waziri haoni kwamba sambamba na mchakato unaopaswa kufanywa na kijiji kupitia Halmashauri na Mkoa, Serikali Kuu nayo ina wajibu wa kuingia kwenye mchakato huo ili nguvu hizo zikutane kupaboresha zaidi kwa sababu panaendelea kuwa sehemu ya mkakati ikiwekwa reli?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuambatana nami atakapopata fursa ili twende kuona kwa pamoja na kufanya maandalizi ya kifikra kabla hata mchakato wa vikao haujaanza? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niungane na Mheshimiwa Mbunge kwamba pale Nyakanazi ukiangalia kijiografia, ndiyo unapata njia ya kwenda Kakonko kule, lakini inaondoka Rwanda na huku tena inaenda Bukoba yaani ni junction pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kweli ukuaji wake ni mkubwa sana, ndiyo maana hata mwaka huu katika usajili wa watoto peke yake, inaonekana darasa la kwanza tumesajili zaidi ya wanafunzi 1,000 na kitu katika shule ya Nyakanazi. Kwa hiyo, mahitaji ni makubwa, lakini baada ya kuongea na viongozi pale, kuna mpango mkakati kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge siku nilivyofika pale, ni kwamba wanataka kuifanya kuwa hub fulani ya kibiashara kubwa sana kwa ajili ya kufanya mji ule kuwa chemchem.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kuungana na wananchi wa pale, kama Serikali Kuu tumesema kwamba kama hilo litafanyika vizuri na Waziri mwenye dhamana hapa kuhusu Maliasili na Utalii watakapoona jambo hilo na kuangalia assessment pale hali ikoje, nadhani Serikali itafanya maamuzi sahihi kutokana na taratibu zinavyokwenda. Kwa hiyo, hilo naomba Mheshimiwa Oscar aondoe hofu kuhusu ushiriki wa Serikali Kuu katika jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuambatana, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tulikubaliana kuna mambo na changamoto mbalimbali kwamba mara baada ya Bunge la Bajeti tutapanga ratiba maalum kwa ajili ya kufika Biharamulo. Vilevile licha ya changamoto ya pale Nyakanazi, kuna mambo mengine ya msingi uliyazungumza katika siku za nyuma tutakuja kuyajadili pamoja katika Jimbo lako la Biharamulo Magharibi.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ni miaka miwili na miezi minne sasa toka Serikali imetamka hilo ililolitamka kuhusu maeneo yaliyopoteza sifa mpaka leo na bado habari ya tathmini inazungumzwa mpaka leo, naomba Kauli ya Serikali kuhusu dhamira ya kukamilisha kazi hii ili tupeleke maendeleo kwa pamoja utalii, kilimo na mifugo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, asilimia 54 ya eneo la Wilaya ya Biharamulo ni maeneo yaliyohifadhiwa. Naomba kujua kutoka kwa Serikali, miongoni mwa maeneo yanayoonesha dalili za kupoteza sifa, yako yale yaliyozunguka Wilaya ya Biharamulo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Oscar kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kuwatetea wananchi wa Jimbo lake, hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kweli tathmini ilishakamilika katika hayo mapori tengefu 12 na tulishamaliza kazi. Kazi iliyobaki sasa ni kuhaulisha. Tararatibu za kisheria za kufuta yale maeneo lazima zizingatiwe. Kwa hiyo, huo ndio mchakato ambao bado unaendelea kwa hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu maeneo ambayo yanahusika katika Jimbo la Biharamulo; kwanza, kuna Masasi River, Biharamulo ambalo lina ukubwa wa kilometa 180 lipo kwenye orodha ya hayo mapori tengefu ambayo tunayaangalia. Lakini pia, kuna eneo lingine, Inchwakima nalo ni eneo ambalo bado tunaliangalia katika lile Jimbo la Biharamulo. Kwa hiyo, maeneo haya mawaili ndio yale ambayo yako katika mapori ya akiba ambayo tunayafanyia kazi, ili yaweze kurudishwa kwa wananchi pale ambapo utaratibu utakamilika.
Kwa hiyo, baada ya hapo naamini Mheshimiwa Mbunge utafurahi na wananchi wako watayatumia maeneo hayo vizuri na ipasavyo.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa Serikali imeonesha nia ya kufanyia kazi wazo hili na kwa kuwa Biharamulo tuko tayari, Mheshimiwa Waziri uko tayari kwa hivi karibuni tuje mimi na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwa ajili ya kuanza mazungumzo na wataalam wako wa Jeshi la Kujenga Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri uko tayari kututembelea ili kabla ya maongezi haya hayajaanza uone fursa zilizopo ili maongezi yawe yamesheheni ushahidi na mambo ambayo tumeyaona kwa pamoja?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutembelea niko tayari kufanya ziara katika eneo hilo ili kutambua fursa ambazo zinaweza zikashughulikiwa ili kutoa ajira kwa vijana hao.
Kuhusu mazungumzo na wataalamu wake nina shauri nipate fursa kwanza ya kujadiliana suala hili na wataalam wa JKT ili kuona uwezekano wake na watakapokuwa wao tayari kuja basi wenzao hawa wawe tayari kwa ajili ya mazungumzo haya.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu lakini naomba nipeleke pongezi kwa wananchi wa Kijiji cha Luganza na Ntumagu kwa sababu ni nguvu zao za wananchi za ujenzi wa kituo hicho ambazo ndio zimesababisha utulivu, nina maswali mawili.
Ni lini Serikali Wizara itajenga nyumba za askari kwasababu hivi tunavyozungumza askari wanne na familia zao wanaishi ndani ya kituo, kwa hiyo, kuna muingiliano wa minong’ono na mazungumzo baina ya familia za askari na mahabusu hasa nyakati za usiku? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni lini Serikali itatoa usafiri walau pikipiki kwasababu eneo hili kijiografia limekaa kwa namna ambayo askari wale wanahitaji usaidizi zaidi wa namna ya kufika kwenye maeneo wanayohudumia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la nyumba kama ambavyo nimekuwa nikijibu katika siku za karibuni kwamba kuna jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika ambazo zinahusisha pia Mkoa wa Kagera kwa ujumla pamoja na Wilaya ya Biharamulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Kagera tunakumbuka kwamba kuna nyumba ambazo zimefikia takribani asilimia 75 kukamilika pale Buekera ambazo katika bajeti ya mwaka huu tunatarajia kuzikamilisha, lakini sambamba na hilo katika fedha ambazo Mheshimiwa Rais ametupatia hivi karibuni za ujenzi wa nyumba 400 basi maeneo hayo yatahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la gari ni kweli kuana changamoto ya usafiri lakini tumefanya jitihada kupeleka magari nadhani kama ni manne sasa hivi kwa mkoa wa Kagera kwa ujumla na kipaumbele chetu kimeelekea zaidi katika maeneo ambayo yako mpakani ili kudhibiti uhalifu hasa kwa wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia na kufanya uhalifu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue changamoto hii katika eneo lake ambapo tuna magari katika kituo hiki ambacho nimekitaja cha Nyakanazi tuna gari mbili zinasaidia kufanya doria katika maeneo ya kituo hiko, hata hivyo tunakubaliana na ombi la Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya kuongeza pale ambapo magari yatapatikana tutaongeza vilevile kulingana na changamoto ya hali ya mahitaji mengine nchi nzima.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tumeshuhudia namna ambavyo Naibu Waziri anasisitiza kwa ukali kabisa kuchukuliwa hatua watu wanaoingiza mifugo hifadhini jambo ambalo ni sawa. Lakini anaongea kwa sauti ya chini na unyonge inapofikia kufidia mwananchi anayeharibiwa mazao na wanyama. Sasa kwa sababu Biharamulo asilimia 50 karibu ya eneo ni hifadhi na kwa sababu vijiji zaidi ya 15 kila mara wanaharibiwa mazao yao, yuko tayari twende tutathimini? Inawezekana akiona hali ile atajua namna Serikali ikae kutafuta namna ya kubadilisha approach ili tuwafidie wananchi badala ya kuwapa kifuta jasho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika maeneo yale ya Biharamulo sehemu kubwa ni hifadhi na kumekuwa na changamoto mbalimbali hasa zikiwemo hizo za mifugo pamoja na uharibifu na uvamizi katika maeneo haya ya vijiji. Naomba nimhakikishie tu kwamba niko tayari wakati wowote tupange twende tukaangalie tuone ni maeneo gani na tuone mikakati gani tunaweza tukaifanya kwa kushirikiana na Serikali tuone hatua za kuchukua. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa Biharamulo kijiografia inafursa ya kufanya biashara na nchi na Congo, Rwanda na Burundi na inafanya hivyo lakini kwa namna ambayo haina tija ya kutosha na kwa kuwa Halmashauri ya Biharamulo imetenga eneo la hekari 61 kwa ajili ya kuanzisha eneo la Agro Processing Zone.

Je, Wizara iko tayari kuja kuzungumza nasi wakisindikizana na TAN-TRADE kwa ajili ya kuchukua hizo fursa za nchi ambazo zimetuzunguka?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza tunamshukuru na kumpongeza sana kwa jitihada kubwa anazofanya za kusaidia Wizara yetu kuhakikisha kwamba anasaidia kuonesha fursa zilizopo nimuhakikishie kwamba ningependa sana kuambatana naye na kuweza kufanya hivyo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza nipende kupongeza majibu mazuri ya Mheshimiwa Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Viwanda, lakini kipekee sana kupongeza Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kwa namna ambavyo wanatekeleza muongozo wa kuanzisha viwanda katika ngazi ya Serikali ya Mtaa na kwa maeneo zaidi ya matatu ambayo wameyatenga katika eneo la Usahunga pamoja na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, lakini niendelee kutoa rai kwa halmashauri zingine kuhakikisha kwamba wanaweka kipaumbele katika kutenga maeneo ya uwekezaji lakini zaidi kuhakikisha kwamba wanaweka miundombinu muhimu ili kuweza kuvutia wawekezaji wengi zaidi na niwahakikishie kwamba tutaendelea kuvutia wawekezaji ikiwemo Biharamulo na sehemu zingine muhimu tu tuendelee kupeana ushirikiano. Nashukuru sana.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti ilishafanya utafiti Wilayani Biharamulo ikiwemo eneo la Busiri na ripoti ipo; na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema STAMICO imenunua mtambo utakaosaidia wachimbaji kuongeza uzalishaji, je, Serikali iko tayari sasa kupeleka mtambo huo sambamba na kwenda na Waziri ili tukaweke mipango vizuri pale ili tuanze shughuli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri amesema Vituo vya Umahiri vinaanzishwa na kwenye Mkoa wa Kagera ni mmojawapo lakini bahati mbaya siyo Biharamuro ambapo ndiko reserved kubwa ya madini ya dhahabu ipo. Je, Serikali inaweza ikatuambia ni kwa nini Kituo hicho cha Umahiri hakikuwekwa Biharamulo? Kwa sababu kuweka kiwanda cha korosho Bukoba au kiwanda cha kupaki senene Mtwara ni jambo ambalo linaweza lisiwe na tija.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na STAMICO tuko tayari kabisa kupeleka mtambo huo katika maeneo hayo kwa ajili ya utafiti. Walete maombi na sisi tupo tayari kupeleka mtambo huo kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa amehoji kwa nini Kituo cha Umahiri tumekiweka sehemu nyingine na wala si Biharamuro. Kwa kweli kituo hicho tumekiweka katika Mji wa Bukoba na kitaendesha mafunzo yake katika Mji wa Bukoba kwa sababu tumeangalia sehemu ambayo ni center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni mkubwa, tuna uchimbaji mwingine mfano wa tin kutoka Kyerwa, dhahabu kutoka Biharamuro na maeneo mengine. Kwa hiyo, pale ni center ambapo wachimbaji watakutana na ni rahisi kufika Bukoba. Kama ilivyokuwa katika huduma zingine za kimkoa kutoka wilaya mbalimbali wanakusanyika pale Bukoba. Kwa hiyo, tuliamua hivyo kwa sababu pale ni center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nimhakikishie tu Mheshimiwa Oscar kwamba tupo pamoja na yeye na tutakwenda na tutashirikiana naye na tufanya kazi pamoja kuwasaidia wapigakura wake. Ahsante sana.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana ni kwa nini Kituo cha Afya Nemba ambacho ni kipya na ujenzi umekamilika hakianzi kutoa huduma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba kule kwake kulikuwa na changamoto kubwa sana na ndio maana tulianza na ujenzi wa kituo kile cha afya cha Yakanazi lakini kazi kubwa inaendelea ujenzi wa hospitali sasa wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tumejenga vituo vya afya 352 na vituo hivi tumeshaanza kuwakilisha kwamba vingine vinapata vifaa na hivi sasa tunawasiliana na wenzetu MSD katika vile vituo vyote ambavyo vimekamilisha vifaa viweze kupatikana na kupeleka wataalam wetu, na lengo kubwa ni vituo hivi viweze kufunguliwa. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Oscar wala usiwe na hofu kituo kile kitafanya kazi vizuri kama ulivyopigania humu Bungeni na wananchi wako watapata huduma vizuri bila mashaka ahsante sana.