Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tarimba Gulam Abbas (35 total)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nakushukuru. Napenda kuiuliza Serikali kuhusiana na Kituo cha Afya pale Kigogo ambacho kinahudumia Wilaya tatu za Ubungo, Ilala na Kinondoni yenyewe, lakini tuna shida kubwa ya jokofu la kuhifadhia maiti. Tayari Serikali imeshatupatia jokofu lile, lakini limekaa bila ya kuwekwa katika sehemu husika.

Ni lini Serikali itatujengea eneo ambalo tutahifadhia jogofu lile kwa madhumuni ya kuweza kuwahifadhi wenzetu ambao wanatangulia mbele za haki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Kigogo ni kituo muhimu sana na niseme kwa bahati nzuri, mwanzo wa ujenzi mpaka kinakamilika nilikuwa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni. Kwa hiyo, nakifahamu vizuri sana kituo kile kwamba ni muhimu na kinahudumia wananchi wengi sana katika Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie katika Halmashauri ambazo zina mapato mazuri na juzi tulipokuwa na Kamati ya LAAC katika Manispaa ya Kinondoni, sehemu muhimu ambayo tuliona ni mfano wa kuigwa katika nchi yetu ni uwekezaji mkubwa wa fedha za mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kwa uwezo wa makusanyo ya ndani ya Manispaa ya Kinondoni, kazi ya ujenzi wa chumba za kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya cha Kigogo ni jambo linalowezekana. Naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni waweke mpango wa haraka ili waweze kujenga chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya cha Kigogo. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naona kijembe kimeingia sawasawa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nami niwapongeze kwa sababu Simba Sports Club wameisadia Tanzania kuonekana vizuri. Pia ule utaratibu wa kuitangaza Tanzania, “Visit Tanzania”, kusema kweli ni jambo ambalo linafaa kuigwa hata na wenzetu wa Young Africans pindi watakapopata nafasi ya kuingia katika mashindano haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu ni jepesi sana kuhusiana na bodaboda. Ni dhahiri kabisa biashara…

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, umesikia maoni ya Mheshimiwa; muige mambo mazuri tunayofanya. Mheshimiwa endelea. (Kicheko)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, biashara ya bodaboda ni nzuri sana kwa vijana wetu. Pale Dar es Salaam bodaboda wanafanya vitu ambavyo vinasababisha abiria ambao ni raia wa Tanzania, ni very innocent, wapate ajali, kupoteza miguu, mikono na wengine maisha yao kwa kupita kwenye alama za taa nyekundu bila kujali, kupita no entry bila kujali, kupita katika barabara za mwendokasi bila kujali na mambo haya yanafanyika mbele ya askari wa usalama wa barabarani. Je, ni lini Serikali itasimamia kidete kuhakikisha kwamba biashara hii inaendeshwa kwa utaratibu wa kisheria ili kupunguza na kuondoa ajali ambazo zinawafika watu wetu?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hawa madereva wa bodaboda kwa kweli ni shughuli kubwa kuwasimamia. Sheria hairuhusu ku-overtake kushoto lakini ukiangalia wote utadhani wana chuo walichojifunza ambapo wamefundishwa ku-overtake kushoto. Nafahamu kwa nini wanafanya hivyo; wanafanya hivyo kwa sababu ku-overtake kulia wanakuwa kati ya gari moja na nyingine, si salama zaidi kwao. Madereva wa magari mtu aki-overtake kushoto jicho lako linakuwa kulia zaidi, ni rahisi kama unakwenda kushoto ukaingia bila kutazama, ndiyo ajali nyingi zinatokea kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Spika, niseme tu, bado tuna kazi kubwa. Nami niwaagize tu Jeshi la Polisi Kitengo cha Traffic kuhakikisha kwamba madarasa yanafanyika ili kutoa elimu kwa sababu watu hawa tunawahitaji. Kuna graduates wanaendesha bodaboda, kuna watu wa masters wanaendesha bodaboda, kwa hiyo, siyo industry ya kuidharau, ni industry inayofanywa na watu wanapata riziki yao, lakini tuwaombe sana kwamba wazingatie sheria kwa sababu wanazifahamu lakini wanafanya kusudi. Jeshi la Polisi upande wa traffic wahakikishe wanatoa elimu kama tunavyofanya katika utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwenye vituo vya bodaboda, wafundishwe namna ya kutumia chombo cha moto.

Mheshimiwa Spika, jambo hili nadhani liwe concern ya sisi sote kwa sababu kundi hili ni kubwa, askari wetu ni wachache, hawawezi wakafanya kwa kila mahali. Matajiri wa hizi bodaboda wako na humu ndani, kila mmoja akitekeleza wajibu wake tunaweza angalau kupunguza vifo vya hawa vijana, nguvu kazi kubwa ya Taifa inapotea. Ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru ahsante.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii niipongeze na kuishukuru Serikali ya CCM ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuweza kukubali mradi huu ambao wananchi wa maeneo haya wameteseka kwa miaka mingi sana. Siyo tu kwamba mradi huu unakwenda kupata suluhisho la mafariko kwa watu wa Kigogo, Hananasifu, Magomeni na Mzimuni, lakini pia makazi yao yanakwenda kuboreshwa na uoto wa asili unakwenda kurudi, nina maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, pale Kigogo kuna mito mingine miwili midogo ambayo inaitwa Tenge na mwingine Kibangu, mito hii sambamba na mto Msimbazi wakati wa mvua maji yanakuwa ni mengi sana na wananchi wanataabika sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa tuko katika hatua za awali za upembuzi wa jinsi gani Mto Msimbazi unakwenda kujengwa; Je, Serikali inakubaliana na mimi ni wakati sasa wa kwenda kupeleka wataalam ili wakausanifu Mto Kibangu uchepushwe maji yake yahamie kwenye Mto Msimbazi ili kuwanusuru wananchi wa maeneo hayo na adha hiyo ya mafuriko?

Swali langu la pili, kwa kuwa katika Kikao cha Tatu cha Mkutano wa Bunge lililofanyika tarehe 29 Aprili mwaka huu, Serikali ilikubali kumpeleka Mheshimiwa Naibu Waziri kwenda kujionea mwenyewe maeneo yale. Je, sasa Serikali iko tayari kuniambia ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri nitakwenda naye kule Kinondoni akajionee mwenyewe changamoto hizi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge amelileta kama ombi kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama tuko tayari kupeleka wataalamu wakafanye tathmini juu ya mito midogo ambayo inapeleka maji ikiwemo Mto Kibangu na Tenge, niseme tu kwamba jambo hili tumelipokea na tutatuma wataalam wakafanye tathimini waone namna ambavyo lile eneo limeathirika jinsi hiyo mito itakavyoleta maji tuone na gharama jinsi zitakavyokuwa na mwisho wa siku, baada ya hapo maana yake tutatoa taarifa kama litafanyika kwa wakati gani kulingana na bajeti itakavyopatikana kulingana na tathimini ambayo tutakuwa tumeifanya.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ameomba tuongozane kwenda Kinondoni nafikiri mara ya Bunge hili kuisha tutakwenda tutafanya ziara katika eneo la Kinondoni pamoja na maeneo yete ya Dar es Salaam, kwa hilo niko tayari kwenda kujionea hizi athari zote zinazotokea. Ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa juhudi wanazozifanya katika kutafuta majawabu ya eneo hili. Lakini vilevile nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Msimbazi sasa hivi umepoteza kina kutokana na kujaa michanga mingi sana kiasi kwamba tupo katika kipindi cha mvua, kipindi ambacho maji hutapakaa na wananchi wa maeneo ya Kigogo Jaba, Kigogo Kati, Kata ya Mzimuni, Daraja la Magomeni na hata Kata ya Magomeni yenyewe, pale wanapata athari kubwa sana ya mafuriko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba commitment ya Serikali kwamba wasaidie juhudi za wananchi katika maeneo hayo, juhudi ambazo zinaongozwa na Madiwani wangu Mheshimiwa Richard Mgana, Mheshimiwa Loto na Mheshimiwa Nurdin katika kuondoa mchanga katika maeneo yale ili mvua hizi zisilete athari tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, changamoto hii pia…

NAIBU SPIKA: Hilo swali la pili nenda moja kwa moja kwenye swali.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningemuomba Mheshimiwa Waziri aambatane nami kutembelea Kata za Tandale, Magomeni, Ndugumbi, Makumbusho, Kijitonyama, Mwananyamala na Hananasif ili kwenda kuona athari za mto Ng’ombe kutokana na mafuriko vilevile ili aweze kusaidia juhudi za Serikali ambazo zimeshaanza kuujenga mto huo. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Abbas Tarimba Gulam kwa juhudi yake ambayo anaifanya katika jimbo lake la Kinondoni. Lakini pili kuwa ni Mwenyekiti wa Bunge Sports Club kwa awamu ya pili nadhani. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba. Swali la kwanza, kwa kuwa juhudi imeshafanyika kwa wananchi wa Jimbo la Kinondoni katika kuhami, kuokoa mafuriko ambayo yanatokea katika Mto Msimbazi, basi Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa ajili ya kuondoa mchanga huo kuongeza kina cha maji, kuongeza kina cha mto ili maji yaweze kupita kwa usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la pili, niko tayari Mheshimiwa Abbas kufuatana na wewe kwenda katika sehemu inayohusika. Ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza na hili linahusu rushwa. Weekend iliyopita timu ya Prisons ilicheza na mabigwa wa kihistoria Young Africans kule Katavi na katika mchezo ule baada ya kumalizika na mabigwa hawa kupata ushindi kiongozi wa Prisons alisimama na kusema kwamba na amenukuliwa katika vyombo vya habari kwamba timu yake ilikua iko katika kuhongwa shilingi milioni 40 ili iweze kuachia mchezo ule.

Je, Serikali haioni sasa kwamba taarifa kama hizi ndizo za kuanzia kufanya kazi na kuwahoji watu kama hawa ili tuweze kupata ukweli? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tabia ya viongozi wa timu mbalimbali hapa nchini hasa wanapofungwa na Young Africans kwa halali kabisa, kutoa kauli za kwamba waliogwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike wakati sasa viongozi wa timu hizi na timu hizi na Watanzania kwa ujumla kwamba wakubali kwamba Young Africans, Yanga moja ndiyo timu bigwa hapa Tanzania na tibu bora hapa Afrika, kwa hiyo, wanapofungwa wakubaliane na matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Deo Ndejembi kwa kujibu maswali vizuri, hongera sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, ningependa kuwahakikishia kwamba Serikali kupitia Wizara ya Michezo ninayoiongoza tunapambana na rushwa kwenye michezo kwa nguvu zote na tunashirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalaam kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ya michezo nchini kukua bila kuwepo na mazingira ya rushwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa kuwapa uhakika Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania kwamba Serikali hii haitafumbia macho timu au mshirika yoyote katika michezo ambaye anatumia rushwa ili kuweza kujipatia ushindi ahsante sana. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa changamoto zilizoko katika swali la msingi ni sawa na zilizoko katika Jimbo langu la Kinondoni katika Kata ya Makumbusho ambako kuna dispensary ilianza kujengwa tangu mwaka 2019 na ilikuwa imalizike Aprili, 2020, sasa hivi ni mwaka mmoja haijamalizika.

Pamoja na juhudi za Manispaa kusimamia ujenzi ule na Mfuko wa Jimbo, je, Serikali haiwezi ikatia mkono sasa kuhakikisha kwamba dispensary ile inamalizika ili wananchi wa Kata ya Makumbusho, Jimbo la Kinondoni waweze kupata huduma? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameiomba Serikali kuweka mkono katika Kata ya Makumbusho kwenye eneo ambalo limejengwa dispensary ambayo ilikuwa imepaswa kumalizika Aprili, 2020. Tunatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Halmashauri ya Kinondoni hususan katika sekta ya afya, tunatambua kazi kubwa anayofanya Mbunge katika Jimbo la Kinondoni na tunatambua kazi nzuri inayofanywa na Serikali kuboresha sekta ya afya nchini.

Kwa hiyo, tumelipokea ombi lake lakini tutaendelea kusisitiza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni sisi pamoja na wao kwa pamoja tuimalize dispensary hii ili wananchi waanze kupata huduma za afya.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pale katika Jimbo la Kinondoni tuna shule za sekondari tisa zenye wanafunzi zaidi ya 11,000 na pass rate pale pamoja na wale wanaokwenda kidato cha tano na sita ni zaidi ya asilimia 80. Hata hivyo, hawa ni watu wa hali ya chini sana, wanapelekwa shule za mbali. Kwa kuwa hatuna high school, naiomba Serikali ikubaliane na mimi kwamba itujengee hata day school ya high school ambayo itaweza kuwasaidia wananchi wa vipato vya kawaida kabisa katika jimbo lile badala ya kuwapeleka mbali wanafunzi wetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba moja ya maelekezo moja ya maelekezo aliyotoa Waziri wa Nchi katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Kinondoni ambazo zina mapato mengi na haya maelekezo tumewaagiza Wakurugenzi kuhakikisha wanatenga fedha kupitia fedha zao za ndani kujenga shule za sekondari ikiwemo kumalizia madarasa katika maeneo ambayo hakuna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ambalo wameliomba hapa namwagiza Mkurugenzi wa Kinondoni kuhakikisha hili linatekelezeka nami nitakwenda kufuatilia kuhakikisha hii ahadi ambayo nimeiahidi hapa Bungeni inafanya kazi, Kinondoni wana huo uwezo wa kutekeleza kwa kutumia mapato yao ya ndani. Ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwezi wa nane mwaka huu nikiwa na Kamati ya Bajeti tulipata nafasi ya kutembelea border post ya Namanga. Lakini katika jambo ambalo lilitushangaza ni kwamba border post ile haikuwa na Cargo scanner; na katika kuuliza tukaambiwa kuna border post nyingine vilevile hazina cargo scanner, jambo ambalo linahatarisha mapato ya Serikali vilevile kuchelewesha upitishaji wa mizigo.

Mheshimiwa Spika, ningeomba Serikali itueleze ni nini msimamo wa Serikali katika kuhakikisha border post zote kubwa zinapata cargo scanners ili kuweza kuondokana na matatizo yaliyopo? Ahsante, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko katika mpango wa miaka mitano kuanzia mwaka 2020/2021 mpaka mwaka 2024/2025, ambapo mpango huu unalenga pamoja na mambo mengine kuimarisha ama kuboresha utendaji kazi wa vituo vyetu vyote tisa vya one stop border kote nchini; ikiwemo kuweza kuipatia vifaa, watumishi, kuwajengea uwezo watumishi, kuweza kuviimarisha kwa njia mbalimbali. Kwa hiyo mpango huu utakapokuwa umekamilika hii changamoto za scanner na changamoto za vitendea kazi vingine pamoja na mifumo ya TEHAMA kwa ujumla wake, maabara nakadhalika na nyingine ambazo nimezitaja zitakuwa zimepatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, nimwombe avute subra wakati kipindi cha utekelezaji wa mkakati huu utakapokamilika ni imani yangu kwamba tatizo la scanner Namanga na maeneo mengine litakuwa imepatiwa ufumbuzi.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jitihada za kunijibu ingawa swali langu la msingi niliuliza ni lini sasa Serikali itakwenda mitaani, itashuka chini kwa maana ya TRA kuweza kuwabaini wafanyabiashara hawa waweze kuandikishwa na hatimaye waweze kupata tax clearance?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu tunaona kwamba, Serikali inasema kuna kampeni ya mlango kwa mlango, nataka nikiri, sijaiona kampeni hiyo na kwa hali hiyo kama utaratibu huo upo maana yake ni kwamba, utachelewesha sana kuweza kulifanya zoezi hili: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; kwa kuwa, Serikali imeweza kufanikisha kuwepo kwa Maafisa kwenye kila kata, kwa mfano Maafisa wa Elimu, Maafisa Afya, Maafisa Kilimo, na kadhalika; ni kwa nini sasa Serikali isifikirie kuwa na Maafisa Kodi kwenye kila kata ili waweze kufanya kazi ambayo ni ya kuwafikia kwa urahisi wafanyabiashara ambao kila siku wanalalamikia masuala ya tax clearance na license? Kule Kinondoni shida ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; ili kuweza kuwabaini wafanyabiashara hasa hawa wadogowadogo katika maeneo yetu, je, Serikali haioni busara kama inaweza ikaanzisha madaftari katika kila mtaa kuweza kuwabaini wafanyabiashara ndogondogo ili matatizo yao ya elimu ya ulipaji wa kodi na masuala mengine yakatatuliwa kwa urahisi, badala ya kuzungumzia elimu ambayo inatolewa na mamlaka kupitia kwenye ofisi za kodi kiasi kwamba, si rahisi jambo hilo kuweza kutekelezeka zaidi ya nadharia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Abbas, Mbunge wa Kinondoni, kwa namna anavyowapigania na kuleta maendeleo katika Jimbo lake la Kinondoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Abbas, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la kushuka chini ni kama ambavyo tumezungumza katika swali la mwanzo la Mheshimiwa Agnesta. Serikali yetu iko tayari kushuka chini kwenda hadi Serikali za Mitaa kwa ajili ya ukusanyaji wa kodi, lakini la kuanzisha maafisa ndani ya Serikali za Mitaa, hili tutachukua kama ni wazo na ushauri na tutautekeleza baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Abbas kwamba, kampeni ya mlango kwa mlango ipo na pengine tu kutokana na majuku yake mengi hajashuhudia. Hii ni kwa sababu, tayari mpaka kufikia tarehe 31 mwezi jana, basi walipakodi 432,323 ndani ya Kinondoni peke yake tumewasajili tayari na wafanyabiashara kati ya hao ni 171,973 kwa hiyo, suala hili la mlango kwa mlango liko Mheshimiwa Abbas. Ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini la pili, nikupongeze wewe pamoja na Wabunge wote wapenzi wa Simba Sports Club kwa kuonja ushindi angalau jana; matarajio yetu mtaendelea na utaratibu huo ambao mmeuanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; naomba nipate kauli ya Serikali juu ya matumizi ya barabara wanazozijenga Serikali, hasa barabara ya mwendokasi pale Dar es Salaam na hususan katika Jimbo langu la Kinondoni. Matumizi ya barabara zile yamekuwa mabaya sana, pikipiki zinapita, magari binafsi yanapita, magari ya Serikali yanapita, hali ambayo inasababisha ajali nyingi sana.

Ni nini kauli ya Serikali pamoja na vyombo vyake kuhakikisha kwamba tabia hii ya kutumia vibaya barabara zinazojengwa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba umeshaeleweka; Mheshimiwa Waziri.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, lakini na la kwanza umenielewa Mheshimiwa, la pongezi. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alichokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwa na kutokutumia vizuri barabara hizi za mwendokasi na inawezekana ni kwa sababu tu hizi barabara kwetu ni mpya. Lakini naomba nitumie nafasi hii kuwajulisha wananchi wa Tanzania kwamba zile barabara zimewekewa alama na zina matumizi yake. Barabara ya mwendokasi ni ya mwendokasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nitumie nafasi hii kuhakikisha kwamba watumiaji wote wa barabara hizi za Dar es Salaam ambapo mwendokasi unapita basi wazingatie sheria ili tusisababishe ajali na matatizo mbalimbali kwa watumiaji wa barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ni kweli kuna haja ya kuweza kuifanyia marekebisho sheria hii ya mwaka 1973, lakini kama ilivyo sheria hii, bado ina nguvu ya kuweza kusimamia matatizo ya usalama barabarani kama askari wa polisi wa usalama barabarani watakuwa wanafanya kazi yao inavyostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bodaboda zinapita taa nyekundu, zinapita no entry, zinapita barabara za mwendokasi; ni nini kauli ya Serikali wakati tunasubiri kwenda kurekebisha sheria kwenye suala hili linalohusiana na matumizi mabaya ya barabara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye, kwamba sheria ilivyo bado inaweza ikadhibiti usalama barabarani ikisimamiwa ipasavyo. Lakini hawa vijana wetu wanaoendesha bodaboda matendo wanayofanya ni hatarishi, siyo kwao tu, bali hata wale abiria wanaowabeba kama wataendelea kutumia barabara kama wanavyofanya inavyozungumzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie Bunge lako Tukufu kuviomba vyombo vyote vya dola vishirikiane na hawa polisi wa usalama barabarani kuwadhibiti vijana hawa, lakini pia kutumia nafasi hii kuwaelimisha wazingatie Sheria ya Usalama Barabarani kama ambavyo imeanza kufanyika kwenye maeneo mengine. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; mwaka 2017 Kampuni ya SportPesa ilikarabati uwanja wa Benjamin Mkapa kwa thamani ya shilingi bilioni moja na nusu na mwaka 2019 machinery zote tulizotumia kwa ajili ya ukarabati wa uwanja ule ikiwemo seeding tractors, tractors pamoja na special grass cutting machines.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutumia machine zile kupeleka katika viwanja vyenye uhitaji ili waweze kutumia machine zile? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Wizara hatuna kizuizi chochote pale ambapo tunapata ombi la kuboresha viwanja vya michezo. Mheshimiwa Mbunge utakapotuletea pia tuta-consider ombi lako. Ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri anasema moja ya kigezo cha wachezaji kuteuliwa katika timu ya Taifa ni kupata muda wa kutosha kwa maana ya play time katika ligi za juu kwa maana ya premier na first division. Wachezaji wa Tanzania wanapata vipi nafasi kiasi hicho wakati ligi zetu zimejaa wageni walio wengi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kunipa nafasi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba Abbas kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba hili ni la msingi, lakini sisi tuna limitation ya usajili wa wachezaji wa nje katika timu. Hata wanapocheza wanapoingia uwanjani kocha anazingatia pia kuna uwakilishi wa vijana wetu katika mechi hiyo ya siku hiyo. Tutaendelea kulizingatia na tutaendelee kushauri TFF wahakikishe pamoja na kwamba wamesajili wachezaji kutoka nje kwa limit ile ambayo tumewapa kupitia BMT vijana wetu wanapata nafasi wacheze waoneshe vipaji vyao, ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, kwanza kutokana na majibu haya naomba nimpongeze Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Suleman Hamza ambapo mwaka jana yeye amefanikisha kupeleka mikopo ya asilimia mia moja ya shilingi bilioni 3.1 kwa watu wa Kinondoni, nimpongeze kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, swali langu, kwa kuwa marejesho yanaonekana hayakuwa asilimia mia moja kuna asilimia 31 ya fedha za mikopo hazijarejeshwa. Je, Serikali ipo tayari kufanya performance audit ili kuweza kujua kama fedha hizi kweli ziliwafikia walengwa na sababu ya kutokurudishwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali iko tayari kufanya utafiti kujua kwamba fedha hizi zinapopelekwa kwa walengwa hakika zinawafikia na zinabadilisha Maisha yao kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano marejesho yalikuwa asilimia 69.32 na Serikali ilifanya performance audit kwa kuhakikisha kwamba tunaita halmashauri zote 184 na kuona mtiririko wa mikopo kwa miaka yote mitano.

Mheshimiwa Spika, maelekezo tuliyoyatoa Serikali ni kuhakikisha tunabainisha vikundi vyote ambavyo vilikopeshwa na vilikuwa havikurejesha marejesho hayo na virejeshe marejesho hayo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari marejesho yanakwenda vizuri, kwa vikundi vyote ambavyo vilikopa na vilikuwa havijarejesha.

Mheshimiwa Spika, pili, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tumeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kikopeshaji wa mikopo wa asilimia kumi, na halmashauri zote zimelekezwa kuingiza vikundi vyote vilivyokopeshwa na ambavyo havijarejesha kwenye mfumo wa kielektroniki ambao tutaufutilia kila siku na kuona kila hatua ya marejesho ya fedha hizo. Kwa hiyo, mpango huu wa asilimia kumi umeboreshwa kwa kiasi kikubwa na marejesho yanakwenda vizuri. Ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri, na kwa changamoto za matumizi ya barabara kwa bodaboda kuongezeka na kuhatarisha Maisha kila siku; sasa Serikali haioni leo kutoa tamko kwamba bodaboda wote wanaopita kwenye taa nyekundu, no entries pamoja na kupakia mishikaki wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ni kosa kubwa sana si bodaboda tu hata magari kukatisha wakati taa nyekundu zimewaka, zikawazuia kwenda wao wakapita; kwa sababu wakati taa nyekundu zimekuzuia wewe za kijana zimeruhusu gari nyingine kupita. Kwa hiyo, unapojaribu kukatisha kwa kweli unajiweka kwenye hatari kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba polisi wetu wa usalama barabarni huchukua hatua, lakini mara nyingine imekuwa changamoto kwa upande wa viongozi wa kisiasa kuwatetea vijana hawa. Kwa hiyo, niombe tushirikiane sote. Elimu tunatoa, sheria huchukuliwa, lakini wote tuwe na utashi wa kisiasa, kwa maana ya mabaraza ya madiwani, ngazi zetu sisi Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya ili wote tuzungumze lugha moja kuhusu usalama wa barabarani, hususan hawa vijana wa boda boda nashukuru sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Jimbo la Kinondoni lina watu wengi sana na mahitaji ya usalama wa watu hao pamoja na mali zao ni mkubwa, hasa ikitiliwa maanani nyumba ziko karibu karibu sana: -

Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka kuruhusu vituo vidogo vya Polisi vinavyofungwa saa 12 vifanye kazi masaa 24 ili kuweza kusaidia usalama katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua wingi wa watu kwa wananchi wa Kinondoni na umuhimu wa kuwa na vituo vidogo vya Polisi katika maeneo mbalimbali. Tutatathmini kwa sababu ili Kituo Kidogo cha Polisi kiweze kufanyakazi saa 24, vinahitaji rasilimaliwatu; na muundo wa kituo kile kuweza kuhifadhi silaha na mambo kama hayo. Kwa hiyo, tutatathmini kuona mahitaji, tutashauriana na Mheshimiwa Abbas kuona namna gani tuvifanye viweze kutoa huduma saa 24. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru Serikali kwa majibu yake lakini nikiangalia majibu haya naona kana kwamba yanakinzana na azma ya blue print ambayo inataka wafanyabiashara kwa maana ya walipa kodi waweze kufanya biashara zao wa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Siku zote ukaguzi husababisha interest na penalties kitu ambacho kinafanya ulipaji wa kodi ule unakuwa mgumu. Kuna ukakasi gani kwa Serikali kuweza kuleta mabadiliko kwamba tax audit sasa zifanyike kila mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuchelewesha hizi tax audit wafanyabiashara wanabambikiziwa makodi makubwa sana kiasi kwamba wanakimbilia kwenda mahakamani, fedha za Serikali hazikusanywi inavyopaswa na kwa wakati. CAG anazungumza trillions of moneys zimekwama kule katika mahakama. Hivi Serikali haioni kwamba ni wakati sasa kurahisisha shughuli za ukokotoaji wa kodi ili fedha za Serikali ziweze zikapatikana kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza tunalichukua kama ushauri, Serikali itaenda kufanya utafiti tukiona kwamba umuhimu wa kuwekwa sheria hiyo basi Bunge lako tukufu tutapeleka mapendekezo yetu na kutunga sheria nyingine ambayo tufanye ukaguzi wa kila mwaka kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili pia nalo tunaenda kulifanyia ukaguzi na utafiti kama kweli fedha zinapotea basi atatusaidia na Wabunge wenzangu atatusaidia namna gani ya kuweza kudhibiti na kukusanya fedha hizo kwa wakati stahiki. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, pale Muhimbili miaka ya nyuma katika bustani (gardens) zinazozunguka na zingine zilizo ndani kulikuwa na street lights lakini vilevile kulikuwa na sehemu za kupumzika kwa wagonjwa; badala ya kukaa kwenye wodi muda wote huwa wanatoka kupata fresh air huduma zile hazipo.

Je, ni lini Serikali inatarajia kuzirudisha huduma zile?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, bado naendelea kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge, hizo sehemu zipo na sasa zinafanyiwa renovation ambayo ndio inayoleta shida ambazo wabunge wa Dar es Salaam wanaziona. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge avumilie kwa muda mfupi sana, renovation inayoendelea itakamilika, na hata hayo ya nje yatakuwa yameongezeka zile sehemu za kupumzikia.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea majibu ya Serikali lakini sheria ilivyo sasa inaelekeza kwamba ujenzi au uendelezaji uanze ndani ya miaka mitatu lakini sheria hiyo haitoi ukomo ni lini majengo hayo yamalizike kujengwa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuleta sheria ambayo itaweka ukomo katika uendelezaji wa majengo na wale ambao watakaidi waweze kupata adhabu kwa kuchelewesha ujenzi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pil, ni nini kauli ya Serikali hasa katika uendelezaji wa majengo ya miradi ya taasisi za umma kama vile NSSF, PSSSF na National Housing ikiwemo suala la majengo yale ambayo yametelekezwa kama vile Hotel Embassy, Motel Ajib kule Dar es Salaam na mengineyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na sheria inazungumza vipi juu ya yale majengo ambayo hayajaendelezwa; kwanza nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya sheria ya Ardhi inayohusu uendelezaji, inamtaka muendelezaji au mtu anayepewa milki aendeleze ndani ya miaka mitatu, ni kweli lakini wako baadhi ya watu wamekuwa wanafanya kazi ya kuanzisha ujenzi ndani ya miaka mitatu na kwa sababu sheria hiyo imetoa ombwe katika lini anatakiwa amalize.

Mheshimiwa Spika, ushauri wako ulioutoa tunauchukua Mheshimiwa Mbunge na ndani ya Wizara tumeendelea kufanyia kazi na itakapofika punde tutakuja kuwasilisha mbele ya Bunge lako ili Waheshimiwa Wabunge, wapate kujua sasa ni kipande gani au mwaka gani mtu anatakiwa kumaliza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, juu ya Serikali inaendelezaje majengo yaliyosimama, maelekezo ya Serikali ni kwamba majengo yote ambayo hayajaendelezwa yaendelezwe ili yaweze kukamilika yasije yakatumika kwa matumizi yasiyofaa. Juu ya Shirika la National Housing, hasa in particular, Serikali imekwishaelekeza juu ya shirika hilo liweze kukopa na mwanzo lilikopa shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya uendelezaji na sasa tupo katika mazungumzo na wenzetu wa Hazina ili tuweze kukopa katika kipande kilichobakia ili tuweze kumalizia sehemu iliyobakia katika majengo mengine.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ya 141 kati ya 190 kwa ugumu wa ufanyaji biashara. Majibu ya Mheshimiwa Waziri yananipa mashaka juu ya commitment ya Serikali juu ya kutumiza haja ya reforms katika regulations zetu. Hivi ni kwa nini hiyo taarifa ya utekelezaji msiilete Bungeni ili tuweze kuijadili, badala ya kuipeleka kwenye Kamati peke yake, tuleteeni Bungeni hapa tuijadili, tuna usongo na hali hii sisi, tunataka tumalize haya matatizo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ni moja ya Kamati ambazo zimetungwa na Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo namini kwa utaratibu ule ule kwamba Kamati hizo zinawasilisha Bunge hili na kwa maelekezo yenu nadhani inawezekana kama kutatakiwa kuleta hapa, basi ni maelekezo ya Bunge lako Tukufu ili tuweze kufanya hivyo.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Moja ya vichocheo vikubwa vya udhalilishaji wa wanawake na watoto ni picha za ngono zilizoko katika mitandao, nchi za Uarabuni zimefanikiwa kuzuia kitu wanachoita Uniform Resource Locators (URL) ili picha za ngono zisionekane katika nchi ile.

Je, Serikali haichukui hatua sasa kuzuia picha za ngono kuonekana katika mitandao yetu ya simu ili kuokoa vijana wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa ajili ya kujikinga na vitendo vya ukatili kwa watoto wote kupitia vijarida mbalimbali na pia Serikali inakataza kutoa picha za ngono katika mitandao. Mtu yeyote ambaye atafanya vitendo hivyo na akagundulika, basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA
HABARI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niongezee maelezo kidogo kwenye swali lililoulizwa na Ndugu Tarimba Abbas, Mbunge wa Kinondoni.

Mheshimiwa Spika, katika maendeleo ya TEHAMA, moja ya changamoto kubwa tunayoipata ni udhibiti huo wa baadhi ya taarifa ambazo kwa kweli zinamomonyoa utamaduni na maadili ya nchi yetu, lakini kupitia TCRA tumeongeza uwekezaji mkubwa na sasa tuko katika hatua za mwisho za kuongeza nguvu ya kudhibiti movement ya picha kama hizo kwa kuweka gateways. Uwekezaji huu ukikamilika na ufungaji wa mifumo hii ukikamilika, hili jambo tutakuwa tumelidhibiti kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilithibitishie Bunge lako, tunao uwezo mpaka sasa wa kufuatilia na kujua nani anasambaza picha chafu. (Makofi)

Kwa hiyo, nitoe tahadhari kwa watu ambao wanatumiwa picha, njia rahisi ukitumiwa picha chafu usimtumie mtu, ni bora ukaifuata kwa sababu ukimtumia mtu mamlaka zina uwezo wa kujua nani kamtumia nani.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mahiri kabisa kwamba ninaamini kabisa kwamba anafahamu changamoto hizi zilivyo. Kwa kuwa mradi huu wa Bonde la Mto Msimbazi ni hoja kuu ya Jimbo la Kinondoni, na kwa kuwa sasa Serikali inakwenda kuanza mradi huu Julai, 2022. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa mpango wa utekelezaji, kwa maana ya program and planning of action, ili wananchi wale wa mto Msimbazi waweze wakajua ni lini wanatakiwa wanaondoke na ni lini kabisa watatakiwa waweze kupata fidia zao pale itakapobidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Abbas kwa kuwa Jimbo lake na yeye ni moja ya miongoni mwa Majimbo yaliyopita katika Mto Msimbazi lakini anafanya kazi kubwa ya kutusaidia kama Serikali kwa kuwaelewesha wananchi. Namwambia Mheshimiwa Tarimba Abbas kwamba aende akawaambie wananchi kwamba tathmini inaendelea. Imeshaanza kama miezi mitatu iliyopita na kwa kuwa inaendelea matokeo lazima wananchi tutawaambia. Kwa hiy,o naomba akawaambie wananchi wa Kata za Kinondoni, Kata za Mzimuni, Kata ya Magomeni, Kata ya Kigogo na maeneo mengine yaliyopita mto huu kwamba tathmini itakapotoka majibu watapewa na lazima tuwaambie kabla ili tusije tukawavamia tukaja tukatengeneza mivutano baina ya wananchi na Serikali. Nakushukuru.(Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, natambua juhudi za Serikali katika kuendea suala zima la uwekaji mifumo ambayo itakuwa ni rahisi lakini utekelezaji ni mdogo sana na unachelewa sana. Andiko la Blue Print linaelekeza kwamba kutakuwa na mchanganuo wa jinsi gani ya kutekeleza na time frame.

Mheshimiwa Spika, swali langu, Je, Serikali iko tayari kuleta Bungeni mchanganuo wa jinsi gani changamoto hizi zinakwenda kutekelezwa na muda wake kwa maana ya time frame?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Serikali ilidhamiria kujipima yenyewe kwa kutengeneza kitu kinachoitwa National Ease of Doing Business Report pamoja na kitu kinachoitwa Organizational Performance Index.

Je, Serikali imefikia wapi katika kutekeleza utaratibu huo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo wawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba Abbas, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayofanya katika kuhakikisha biashara na mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini yanakua.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Blue Print utekelezaji wake ambao tulianza mwaka 2018 tunaenda vizuri lakini bado changamoto chache ambazo ni endelevu. Nakubaliana na yeye kwamba lazima tuhuishe kwa sababu changamoto zilizokuwepo wakati ule na sasa ziko tofauti. Kwa hiyo, tunahuisha time frame ya kuendelea kutatua changamoto za utekelezaji wa Blue Print kila mwaka na tutafanya taratibu hizo kuona Wabunge wote wanapata time frame hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kuwa na National Ease of Doing Business, Wizara tumeanza kutekeleza hilo na hivi karibuni tutakuwa na vitengo katika Mamlaka za Halmashauri ambavyo vitakuwa vina Watalaam wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambao watashirikiana na Mamlaka ili kuhakikisha tunaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge ambao pia ni Madiwani tuendelee kushirikiana kwa sababu sisi ni sehemu ya Mabaraza ya Madiwani, tunapotunga zile Kanuni Ndogo (By Laws) basi tuangalie zisije zikawa nazo ni sehemu ya kuweka vikwazo vipya au kero mpya katika kutekeleza blue print. Nakushukuru.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana. Pale katika Jimbo la Kinondoni kwenye Kata ya Kigogo Serikali ilituletea jokofu la kuhifadhia maiti lakini limekaa zaidi ya miaka mitatu sasa bila ya kuweza kujengewa eneo lake ilhali tathmini imeshafanyika;

Je, sasa Serikali imepanga kutoa lini fedha ili nyumba zilizokaribu pale ziweze kufidiwa na jengo lile likaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Kigogo kilipelekewa jokofu lakini Serikali ilielekeza mara vifaa tiba vinavyofikishwa katika vituo vyetu vianze kutumika mapema iwezekanavyo. Kwa hiyo kwanza nitumie fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kwa ajili ya kujenga jengo la kuhifadhia maiti na kuingiza jokofu ili lianze kufanya kazi ya kuhudumia wananchi kama inavyotarajiwa, ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa mradi huu unapita katika Kata za Kigogo, Mzimuni, Magomeni, na Hananasifu. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa Tarehe au muda lini mapitio hayo yataenda kufanyika ili wananchi wa maeneo yale waweze kufahamu?

Swali langu la pili, ningependa kama ikiwezekana Serikali itoe tangazo mapema ili wananchi wale wote waweze kuwepo wakati tathmini hizo zikifanyika. Ahsante sana.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Tarimba Abbas kwa maswali yake mawili.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimfahamishe kwamba katika mradi ambao unaendelea sasa pamoja na Kata alizozitaja mpaka sasa wananchi waliofikiwa ni 2,217 kati ya 2,432 ambao watafikiwa. Katika hao ambao wamefikiwa sasa katika ule mradi, asilimia 92 ni wananchi 2,057 wameshakubali wamefanyiwa uhakiki na kati yao ni 160 tu ambao hawajafikiwa. Kwa hiyo, kaya ambazo hazijafikiwa ni
215 na nadhani zipo katika yale maeneo ambayo umeyasema, hivyo wakifikiwa nadhani nao pia watapata huduma ile ile ambayo wamepatiwa wengine.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu kutoa tangazo, inawezekana likatoka, lakini huwezi ukalitoa kwa sasa kwa sababu procedure hiyo bado inaendelea. Kampuni iliyopewa kufanya kazi hiyo bado ipo uwandani inafanya kazi. Kwa hiyo, pale itakapokuwa imefikia kwenye hatua ambayo ni ya mwisho, kwa sababu maeneo yanayotwaliwa yote yanafahamika, basi wataambiwa wananchi, lakini kwa sasa huwezi kutoa tangazo kwa sababu bado pia tupo kwenye utaratibu wa kukamilisha.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwa kuwa Serikali imekubali maombi ya wananchi na wakazi wa Magomeni Quarter, familia 644 kuwauzia nyumba hizo na kuwapunguzia bei ya ununuzi na vilevile kuwaongezea muda wa kulipa kutoka miaka 15 hadi 30. Swali langu: Je, Serikali iko tayari kupokea shukrani zangu za dhati pamoja na wananchi wa Magomeni Quarter kwa uamuzi wa Serikali kuwauzia nyumba hizo na kuboresha familia zao, kitendo ambacho kinaonekana ni kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania? Shukrani hizi zimwendee Mheshimiwa Rais na Mtendaji Mkuu wa TBA Bwana Kondoro. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani alizotoa Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba nizipokee shukrani hizo ambapo ni kazi kubwa imefanyika, na kweli amejali wananchi waliokuwa wanaishi hapo, ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa mujibu wa swali hili ni kwamba maji pia hutuama katika barabara za lami ambazo nyingi zinakuwa na mashimo na hata zikitengenezwa mashimo yanajirudia pale pale.

Je, Serikali haioni kwamba sasa ni muhimu kuwa na kitengo katika moja ya halmashauri za Jiji za Dar es Salaam kusimamia utengenezaji wa mashimo yale badala ya kutegemea kandarasi ambazo zikifanya kazi bado mashimo yanatokea tena? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ina kitengo tayari cha usimamizi wa matengenezo ya mara kwa mara ya barabara zetu, yakiwemo haya mashimo ambayo yanasababisha maji kutuama. Vitengo hivyo ni Idara za Wakuu wa Idara, kwanza tuna TARURA kila halmashauri ya wilaya, pia tuna ngazi ya mkoa lakini pia kwenye halmashauri kuna ma-engineer. Kwa hiyo, wale ndio wataalamu na vitengo vile ni sahihi kusimamia.

Mheshimiwa Spika, kinachokosekana mara nyingine ni uthabiti na umakini wa usimamizi kwa vile vitengo ambavyo vina ma-engineer tayari. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutaendelea kusimamia kwa karibu na kuchukua hatua kwa wale ma-engineer ambao hawatimizi majukumu yao ipasavyo, ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Niipongeze Serikali kwa kujenga vituo 234 vya afya nchini kikiwemo kituo cha kisasa kabisa pale katika Kata ya Kinondoni ambacho tayari kimeanza kufanya kazi. Tatizo ni uhaba wa madaktari na wauguzi;

Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuhakikisha vituo hivi vipya ambavyo vimejengwa vinapata na kuondolewa tatizo la kuwa na madaktari na wauguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba la kupata madaktari na wauguzi katika kituo cha afya Kinondoni. Jitihada za Serikali ya Awamu hii ya Sita katika kuhakikisha vituo vya Afya vyote vilivyojengwa na vilivyopo vinapata watumishi wa kutosha imefanyika kubwa katika mwaka wa fedha huu 2022/2023 kwa kuajiri watumishi wa afya 8070. Tayari watumishi hao wameanza kupangiwa maeneo yao ya kazi ikiwemo Halmashauri ya Kinondoni. Hivyo basi nimtake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha kati ya wale ajira mpya atakao wapokea aweze kuwapangia katika vituo hivi vya afya ambavyo vimejengwa kwa fedha nyingi iliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ikiwa haya ndiyo majibu ya Serikali.

Je, Serikali iko tayari sasa kutengeneza kitu kinachoitwa Program and Plan of Action kikionesha tarehe na miezi na mwaka kuelekea kuanzishwa kwa mradi huu badala ya kusema tu majadiliano yanaendelea? Watupe commitment ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kama nilivyosema ni kweli tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu na sababu kubwa ilikuwa ni upande wa pili kwa maana ya huyu mwekezaji ambaye kidogo alikuwa haji kwenye majadiliano kwenye vikao. Sasa kama nilivyosema, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaweka mahusiano mazuri na nje wanakotoka wenzetu wawekezaji hawa. Kwa hiyo tunaamini sasa kwa sababu wameshaanza kuja maana yake tutafikia muafaka karibuni, halafu tutatoa hiyo programu kwamba schedule ya utekelezaji wa mradi huu itakuwaje, nakushukuru.

MHE. ABBAS G. TARIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda niiulize Serikali, kwenye upande wa kuhamasisha na kuleta wawekezaji wakubwa katika ukulima mkubwa kwa maana ya large scale farming hasa katika ngano. Ni nini mtazamo wa Serikali katika zao hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha tunakuza kilimo cha nchi yetu ya Tanzania na ni ukweli ulio dhahiri kwamba ili kukuza kilimo chetu lazima tukubali kwamba dunia ya leo inahitaji uwekezaji mkubwa. Kwa sasa mlango uko wazi kwa ajili ya majadiliano na kuwakaribisha wawekezaji na Mheshimiwa Mbunge yeyote ambaye anaona kuna wawekezaji wanakuja kuwekeza nchini na kuna tija, tuko tayari kuwasikiliza na kuweza kuwasaidia ili jambo hili liweze kukamilika.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matatizo ya kukatikakatika kwa umeme mara kwa mara katika Jimbo la Kinondoni na mara nyingi sana bila hata taarifa kutoka TANESCO.

Ni nini kauli ya Serikali katika kuondoa tatizo hili ili wananchi wa Kinondoni waweze kuishi kwa amani na kupata huduma hii?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kabisa jitihada kubwa zimefanyika katika siku chache zilizopita na imepunguza sana kukatikakatika kwa umeme katika maeneo mengi sana nchi. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayokuja, Serikali imetenga pesa ya kutosha kwa ajili ya kurekebisha vituo vya kupoza umeme, kuongeza ukubwa wa transfoma tulizonazo, kurekebisha miundombinu ya umeme kama nyaya na nguzo na hivyo tuna uhakika kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha ujao matatizo ya kukatika kwa umeme yatakuwa kama siyo kuisha, yamepungua kwa asilimia kubwa kabisa.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi; pale kwenye Kata ya Tandale Jimbo la Kinondoni kuna kituo cha afya ambacho kinahudumia zaidi ya watu 1,000 kwa siku na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, lakini kituo kile hakina gari la wagonjwa nafahamu mtaleta magari hayo ambayo mmeyataja lakini kwa Kinondoni mahitaji ni makubwa.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuipelekea gari kituo cha Afya cha Tandale ili kuweza kuondoa matatizo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye majibu yangu ya msingi tunakwenda kununua magari 195 lakini tutaongeza magari mengine kwa sababu kwa utaratibu ambao tunanunua magari haya kupitia UNICEF tutapata saving ambayo tuna uhakika magari yataongezeka na kigezo cha kugawa magari haya itakuwa ni vitu vyenye idadi kubwa ya wagonjwa kama Tandale na maeneo mengine, lakini umbali kutoka kituo kile kwenda hospitali ya halmashauri.

Kwa hiyo, nimhakikishiwa Mheshimiwa Mbunge tutafanya tathimini ya uhitaji huo na pale ambapo vigezo vitafikiwa tutaleta gari pia katika vituo hivyo. Ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pale Jimbo la Kinondoni, kwa kupitia fedha za mfuko wa Jimbo tumejenga jengo la mionzi kwa maana ya (Radiology).

Je, Serikali iko tayari sasa kutupatia vifaa tiba kama vile x-ray, ultrasound pamoja na wafanyakazi ili kituo kile kiweze kuanza kazi? Nakushukuru
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kutenga fedha kupitia Mfuko wa Jimbo na kujenga Jengo la mionzi na nafahamu amekuwa akifuatilia mara kwa mara. Nimhakikishie kwamba Serikali itashirikiana na halmashauri ya Kinondoni kupitia mapato ya ndani ili waweze kununua baadhi vifaa tiba ambavyo viko ndani ya uwezo wao kama ultrasound, wakati Serikali kuu inaangalia uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya x-ray ili wananchi wapate huduma bora, ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni nini, kauli ya Serikali katika kuipanua barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma kutokana na ufinyu wake na matumizi makubwa ya barabara hii.

Je, Serikali haioni haja ya kuipanua barabara hii na kuifanya njia nne?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa ufatiliaji wake, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na Dar es Salaam ndiyo Commercial City ya nchi yetu, kwa hiyo, ni vizuri tukaviunganisha kwa mawasiliano ya barabara ya uhakika. Bahati nzuri kama nilivyosema juzi, kwenye hoja za Kamati ya Miundombinu, tunapanga kujenga barabara hii ya kutoka Kibaha inapoishia njia nane, Chalinze, Morogoro mpaka Dodoma kutumia utaratibu wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari wapo wabia ambao wamejitokeza tunaendelea na mazungumzo nao, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Tarimba pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wote tunahitaji barabara hii kuunganisha Dar es Salaam pamoja na Dodoma, tuko mbioni kuijenga barabara ya Express Way Dar es Salaam – Dodoma kwa njia ya PPP, ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni nini, kauli ya Serikali katika kuipanua barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma kutokana na ufinyu wake na matumizi makubwa ya barabara hii.

Je, Serikali haioni haja ya kuipanua barabara hii na kuifanya njia nne?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa ufatiliaji wake, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na Dar es Salaam ndiyo Commercial City ya nchi yetu, kwa hiyo, ni vizuri tukaviunganisha kwa mawasiliano ya barabara ya uhakika. Bahati nzuri kama nilivyosema juzi, kwenye hoja za Kamati ya Miundombinu, tunapanga kujenga barabara hii ya kutoka Kibaha inapoishia njia nane, Chalinze, Morogoro mpaka Dodoma kutumia utaratibu wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari wapo wabia ambao wamejitokeza tunaendelea na mazungumzo nao, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Tarimba pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wote tunahitaji barabara hii kuunganisha Dar es Salaam pamoja na Dodoma, tuko mbioni kuijenga barabara ya Express Way Dar es Salaam – Dodoma kwa njia ya PPP, ahsante Sana.