Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Francis Isack Mtinga (24 total)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona naomba niulize swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa changamoto zilizoko Namtumbo zinafanana kabisa na changamoto zilizoko Mkalama hasa Kata ya Mwanga ambayo haikuwahi kupata umeme kabisa katika awamu zote. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kata hii ambayo imekuwa ikiutizama tu umeme huu wa REA katika kata nyingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mkalama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika,kama tulivyokwishasema kwamba katika Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili wa REA, tutapeleka umeme katika vijiji vyote Tanzania vilivyobaki bila kupata umeme ambavyo hesabu yake ilikuwa ni 2,150. Kazi hiyo itaanza mwezi huu wa pili na tunahakikisha kwamba kufika mwezi Septemba, 2022 vijiji vyote vilivyopo nchini Tanzania vitakuwa vimepata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee kwamba tunapopeleka umeme vijijini, kimsingi tunapeleka kwenye Mkoa, Wilaya, Kata, vijiji halafu Vitongoji. Kwa hiyo, kuna vitongoji ambavyo pia vitanufaika na awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa upelekaji wa umeme kwenye mradi huo ambao utaanza mwezi huu na kukamilika kufikia mwezi Septemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Mkalama kwamba vijiji hivyo vilivyopo katika kata hiyo, vitapatiwa umeme kwa uhakika.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imepeleka vifaa vya maabara kwenye shule 18 kati ya 19: Je, sasa wana kauli gani kuhusu kupeleka walimu wa kutosha wa sayansi katika huu mgao unaokuja wa walimu ili vifaa hivi viweze kuwatendea haki wanafunzi wetu wa Mkalama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa Wilaya ya Mkalama ina High School moja tu na ambayo iko kwenye mchepuo wa Sanaa: Je, Serikali ina mpango gani kuhusu kuongeza hostel katika Sekondari ya Gunda ambayo sasa wana hostel moja ili angalau sasa tuweze kuanzisha mchepuo wa sayansi katika sekondari hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tunapokea pongezi ambazo amezitoa kwa sababu, Serikali imefanya kazi nzuri katika jimbo lake na Halmashauri yake ya Mkalama kwa kupeleka vifaa vya maabara katika sekondari 18 kati ya 19 za jimbo lake. Swali lake la msingi ambalo ameiliza ameuliza tu ni lini Serikali itapeleka Walimu wa Sayansi wa kutosha katika shule hizo zenye maabara, ili angalau sasa pamoja na vifaa basi pawepo na basi pawepo na Walimu wa kutosha kwenye huo mgawo unafuatia. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea ombi lake na tutazingatia wakati wa mgawanyo ambao tutautoa hivi karibuni kabla ya mwisho wa mwezi Juni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameomba tujenge hostel ya Sekondari ya Dunga ili angalau na wao waweze kupata kidato cha tano na cha sita. Niseme tu ombi lake limepokelewa na tutalifanyia kazi kulingana na mahitaji ya jimbo lake.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba jina langu ni Francis Isack Mtinga, sio Mtenga, Mtenga ni Wachaga, Mtinga ni Wanyiramba.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya waziri ya kukiri mgogoro lakini nakiri sijaridhishwa kabisa na jibu walilolitoa. Na hivyo nitauliza swali moja tu la nyongeza ili nitoe na maelezo kidogo.

Mheshimiwa Spika, mpaka huu ni wa mkoa; mpaka kati ya Hanang’ na Mbulu na Wilaya ya Mkalama ni mpaka wa Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Singida na amekiri kwamba tatizo hili ni la muda mrefu sana lakini majibu aliyoyatoa kwamba ni kupima, kupima hakutatui tatizo la mgogoro. Na tatizo hili limekuwa kubwa sasa kule Kijiji cha Eshkeshi, Wilaya ya Mbulu wameingia kilometa mbili katika Kijiji cha Ulamoto kule...

SPIKA: Uliza swali!

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naomba Waziri aniambie kwamba lini tutakwenda naye akafanye mkutano na wataalam kwa vijiji hivi ili kutambua mipaka ili kuondoa mgogoro huu na wananchi wafanye kazi za utawala vizuri, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Isaack.

Mheshimiwa Spika, suala la kutambua migogoro katika mpaka sio kufanya mikutano tu, kinachotakiwa pale ni kwenda na GN zinazohusika na kufanya tafsiri ya GN kuangalia zile coordinates katika yale maeneo. Naomba nimuhidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tukimaliza tutampa wapima watakwenda wakiwa na zile GN zinazotaja mipaka ya Wilaya zote mbili ili waweze kutambua na kuweza kubainisha mipaka. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri sana yanayotia moyo ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa kilimo cha mkataba ni kilimo ambacho kinahitaji mahitaji muhimu sana na mengi ili kifanikiwe mojawapo kubwa ni mbegu bora. Je, Wizara imejipangaje kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Singida na hasa Mkalama wanapata mbegu bora na kwa bei rahisi?

Swali la pili, kwa kuwa viwanda vingi vya alizeti Mkoa wa Singida vinafanyakazi kwa miezi mitatu tu kwa sababu ya ukosefu wa mbegu, Wizara imejipangaje kuhakikisha kwamba tatizo hili linatatuliwa Serikali inapata mapato na inatatua tatizo kubwa la mafuta ya mboga nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Francis Isack kama ifuatavyo:-

Kwanza nitumie Bunge lako Tukufu kuwaalika Wabunge wa maeneo ya Singida, Dodoma na Manyara katika mkutano utakaoongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu siku ya tarehe 13 Juni unaohusiana na suala la alizeti na mazao ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tunayoichukua ya kwanza Wizara sasa hivi inafanya tathmini ya mahitaji ya mbegu zitakazochakatwa na viwanda ili kuweza kuondoa gap ya mafuta. Hatua ya pili tuta-subsidize mbegu kupitia maviwanda badala ya mbegu ya high sun kununuliwa kwa shilingi 30,000 Serikali inafanya tathmini sasa hivi tuta-subsidize kwa kiwango kisichopungua asilimia 50 ya bei hiyo ili wakulima waweze kupata mbegu hizi kwa bei rahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua ya tatu tunayochukua gap mahitaji yetu ya mbegu kwa ajili ya kuzalisha alizeti zitakazotosheleza viwanda vyote kwa msimu wa mwaka mzima ni metric tans 3,900 na sisi kama Serikali uwezo wetu wa uzalishaji wa ndani ni metric tans zisizozidi 700. Wizara sasa hivi inafanya mchakato wa kuagiza mbegu metric tans 3,000 ambazo zitakuwa subsidize na hizo tutazigawa kwa wakulima kwa bei rahisi ili viwanda viweze kupata alizeti ya kutosha katika msimu ujao.

Kwa hiyo, kwa misimu ya miaka miwili tutaagiza gap na msimu wa tatu kwa fedha mlizotupitishia mwaka huu katika bajeti kwa ajili ya ASA tutakuwa na uwezo wa kuzalisha mbegu zote za alizeti ndani ya nchi yetu na hatutokuwa na gap. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa kuwa barabara hii ya Mkwiti – Amkeni inayounganisha mkoa wa Lindi na Mtwara tatizo lake linafanana kabisa na barabara ya Singida Simiyu inayoanzia Iguguno na kwa kuwa Serikali imevunja nyumba za wananchi wa Iguguno hivi karibuni.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi barabara hii hasa kuanzia Iguguno mpaka Nduguti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ni barabara ambazo zitajengwa katika kipindi hiki cha miaka mitano na itategemea na upatikanaji wa fedha hatuwezi leo tukaahidi kwamba itaanza mwaka ujao kwa sababu haijaingia kwenye mpango. Lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika miaka inayokuja ya bajeti itaingizwa kwenye mpango ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni kuanzia na upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na hatimaye kujenga kwa kiwango cha lami ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mkalama ni wilaya mpya na ina mapato madogo sana. Naomba tu niseme Wizara itakuwa tayari kulipokea boma hili kama sisi Halmashauri ya Mkalama tutaamua kuwakabidhi ili walikarabati liweze kuleta manufaa kwa nchi na kwa jamii ya Mkalama; swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Naibu Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge twende naye mpaka Mkalama ili akaone hali halisi ya boma hili na aone umuhimu wake ili aharakishe mchakato wa kulichukua kama tutawakabidhi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Francis Mtinga, amekuwa ni mfuatiliaji sana kwenye eneo hili la kuboresha malikale likiwemo hili boma la historia lililoko katika Wilaya ya Mkalama. Nimpongeze sana na pia niwapongeze wananchi wa Mkalama Iramba Mashariki kwa kuwa na Mbunge mahiri anayefuatilia maeneo haya ya kihistoria ambayo ni mojawapo ya chanzo cha mapato katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa haya maeneo ni maeneo muhimu kwa ajili ya kuhamasisha utalii lakini pia kuongeza mapato katika sekta zetu hizi, nimuahidi kwamba tutaenda kulitembelea lakini pia kama Halmashauri itashindwa kulikarabati boma hili basi Wizara iko tayari kulipokea na kulikarabati na liwe eneo mojawapo ya chanzo cha mapato katika Serikali, ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali ya Mama Samia kupitia Wizara hii, baada ya kilio cha muda mrefu hatimaye wananchi wangu wa Tumuli walilipwa fedha hizo. Pamoja na shukurani hizo naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi wetu wadogo wa Tumuli, ambao walihamishwa pale katika lile eneo na kwenda kuanzisha maeneo mengine hasa kwa kupelekewa umeme na barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili Serikali ina mpango gani pia kwa kuwasaidia hao wachimbaji wadogo vifaa vya uchimbaji kwa mkopo nafuu haswa hao wa Tumuli, Langida na Ibaga ambao ni wachimbaji wadogo wanaokuza uchumi katika nchi yetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wachimbaji hawa wadogo wa Kata ya Tumuli wanapaswa kuingia katika vikundi, ili watakapokuwa wamekuwa katika vikundi halafu waweze kujisajili na wakishakuwa wamesajiliwa wakatambulika rasmi kama kikundi kilichosajiliwa, basi baada ya hapo taratibu za kuwawekea mazingira bora zinaweza zikaanza ikiwa ni pamoja na kuwapa leseni.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba panapokuwa na uchimbaji wenye tija katika maeneo ya wachimbaji wadogo, tunawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Nishati. Kwamba, kama machimbo hayo yana tija basi waweze pia kupelekewa nishati ya umeme kama ambavyo tumefanya katika machimbo baadhi ya wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, na hili suala la vifaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo tumekuwa siku za karibuni tukiwasiliana na mabenki yetu ya ndani, kuona kwamba yanaweza yakaanza kukopesha vifaa kuliko hata fedha zenyewe na katika suala hili pia tumefikia mahali pazuri na hivyo nimpe tu tija Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaenda tena kuwaona wachimbaji wake kama wameji-organize katika vikundi tutawasajili na baada ya hapo, tutawaunganisha na mabenki yetu ili kwamba waweze kusaidiwa kama ambavyo wengine pia wanasaidiwa hapa nchini. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja tu la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mpaka sasa Halmashauri ya Mkalama ndio wanaotunza shamba hili; na kwa kuwa, hatuna ugomvi na Wizara na tunajali sana maslahi ya umma: Je, Wizara ipo tayari sasa kukaa meza moja na Halmashauri ya Mkalama ili tuweze kukaa na kujadili matumizi bora zaidi ya eneo hili kuliko kuendelea kuwa shambapori kama ambavyo lilivyo sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Isack Francis Mtinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, milango ya Wizara iko wazi. Tunawakaribisha viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, wakiongozwa na Mheshimiwa Mbunge makini, waweze kuja tukae mezani kuzungumza na kuona hatima njema ya eneo lile na hususan katika kuboresha mifugo yetu na huduma nyingine. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; kwa kuwa barabara ya Iguguno kupitia Nduguti mpaka daraja la Sibiti inaunganisha Mkoa wa Singida na Simiyu na inapita makao makuu ya Wilaya.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga kipande cha kilometa 42 kutoka Iguguno mpaka makao makuu ya Wilaya kwa mtindo wa build and design? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga barabara hii lakini daraja alilolisema tunajenga daraja la msingi na hili daraja ambalo amelisema, liko kwenye mpango wa kufanyiwa usanifu ili liweze kujengwa kwa kiwango cha zege.

Kwa hiyo, naomba baada ya hapa tukutane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuelekezana zaidi jinsi kazi hii itakavyofanyika. Ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa jicho lako kuniona. Naomba katika Halmashauri yangu ya Mkalama, Kata ya Matongo Kijiji cha Mnung’una yuko mwananchi mmoja ambaye amechukua ardhi ya wananchi karibu ekari 400; na hata baada ya matumizi bora ya ardhi ameendelea kukaidi: Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kama yuko tayari kufuatana nami ili kwenda kuondoa tatizo hili ambalo ni kubwa sana kwa wananchi wangu wa Matongo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Francis kwamba niko tayari kuongozana naye kwenda kuzungumza juu ya mgogoro huu ambao unakabili vijiji vyake katika eneo hilo la Kata ya Matongo.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Mkalama pamoja na kuwa Kituo hicho kimekuwa gofu muda mrefu lakini pia Askari ni wachache sana, katika Kata zote 17 ambazo zinamtawanyiko mkubwa, sehemu kubwa tunatumia mgambo. Serikali inatuambia nini kuhusu kutupatia Askari wapya katika mgao unaokuja. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Mtinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya nyingi hasa ambazo hazikuwa na Vituo vya Polisi, wamekuwa na Askari kulingana na uwezo wa vituo vilivyopo kuwabeba. Tunashukuru baada ya kupata ajira ya zaidi ya Askari 4,200 waliotoka kwenye mafunzo mwanzoni mwa mwaka huu, wameweza kugawiwa kwenye vituo hivi, vikiwemo mpaka ngazi za Kata. Naamini Mheshimiwa Francis anafahamu kwamba sasa hivi tunao Askari Kata ngazi ya Cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kwa ajili ya kusimamia usalama katika ngazi hizo. Kwa hiyo, naamini atakuwa amepata Askari hao kwenye Jimbo lake la Mkalama. Nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba kujua ni lini Wizara itajenga minara katika Kata ya Kikonda, Kinampundu na Mwangeza, ukizingatia Mwangeza wanavamiwa na tembo kila wakati, kwa hiyo wanahitaji mawasiliano kwa ajili ya kuomba msaada? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema hapa awali katika majibu yangu ya msingi ni kwamba kuna miradi mbalimbali inayoendelea. Niwaombe Wabunge, kuna miradi 763 ambayo imeshaletwa Bungeni, lakini pia tuna hayo maeneo ambayo ni 216 ambayo yameshafanyiwa tathmini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe Bunge lako Tukufu, wajaribu kupitia katika ile miradi pale ambapo Mheshimiwa Mbunge atagundua kwamba maeneo anayoyasema bado hayajaingizwa katika mpango wa utekelezaji, basi Serikali tutayapokea kwa ajili ya kufanya hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri sana ya Serikali yanayotia moyo, naomba naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Katika Kata ya Iguguno kuna Mahakama ya Mwanzo ya kisasa kabisa na ya kidigitali. Je, Serikali sasa haioni haja ya kuanza Mahakama ya Wilaya kwa muda katika Kata hii, kwani wanachi wanapa shida sana kwenda Wilaya ya Iramba kwenda kufuata Mahakama ya Mwanzo?

Swali la pili, iwapo Serikali itaridhia kutumia Mahakama hii; je, itakuwa tayari sasa kutumia mahabusu ya Singida Mjini badala ya kwenda Kiomboi kwani uhakika wa usafiri wa Singida Mjini ni rahisi na ni karibu zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kimsingi maoni yake yote tunayachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi kuona Je, kuna uwezekano wa kuanza kutumia huduma zote hizi mbili ambazo Mheshimiwa Mbunge amependekeza. Ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, naomba nimtake Waziri, pamoja na kwamba wataalamu wamefanya mambo haya, lakini Wakuu wa Wilaya walipaswa Kwenda kufanya mkutano pale kwa pande zote mbili na kuonesha beacon, lakini jambo hilo halijafanyika.

Je, uko tayari sasa kuwataka Wakuu wa Wilaya kwa muda maalum kwenda kutekelza agizo hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jimbo langu linapakana pia na Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Manyara na tatizo hili mipaka limekuwa kubwa.

Je, agizo hilo pia utamwagiza pia Mkuu wa Mkoa wa Singida na Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwenda kufanya mambo haya haya ili tatizo hili liweze kuisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki ama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe rai kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya hizi na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, kama ambavyo maelekezo ya Serikali siku zote yamekuwa yakitolewa kwamba ni muhimu na ni lazima kufika katika maeneo yenye migogoro ya mipaka kati ya kijiji na kijiji, kata na kata lakini kati ya wilaya na wilaya na mkoa na mkoa, ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za mipaka kwa kutumia njia shirikishi na kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naelekeza Wakuu wa Wilaya hizi na Mikoa ya Manyara lakini na Singida kuhakikisha kwamba wanatekelza haya maelekezo ya Serikali, ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali katika suala la mgawanyo, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri katika mgawanyo uliopita wa Walimu ajira zilizopita, Halmashauri yangu ya Mkalama ilipata walimu 12 tu ikilinganisha na Halmashauri zingine ambazo zilipata zaidi ya walimu 40.

Je, unatuambia nini katika mgawanyo huu unaokuja kuhusu Halmashauri yangu ya Mkalama kwani tuna upungufu wa Walimu zaidi ya 800 katika Halmashauri yangu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuzingatia vigezo vya kupeleka Walimu ambao watapata nafasi hiyo katika Halmashauri zote nchini kulingana na mahitaji. Tunatambua kwamba changamoto bado ni kubwa na mahitaji ya walimu bado ni makubwa lakini kwenye hizi tutaendelea kutenda haki. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaleta kulingana na idadi na mahitaji ya eneo husika. Kwa hiyo, siyo wote 800 lakini ni wale ambao watatosheleza kwa wakati wa sasa. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali yanayojaribu kuwafariji wananchi wa Kinyangiri na Mkalama nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Kinyangiri ni cha enzi ya ukoloni, ni kituo cha siku nyingi sana na kinahudumia Tarafa nzima, kilipelekea mpaka kiongozi mkubwa wa chama kinachounda Ilani kuwaahidi wananchi wa Kinyangiri kwamba ifikapo Disemba kama hawajapata majengo waandamane ofisini kwake. Serikali na Wizara ina kauli gani kuhusu kauli hii nzito ya Kiongozi mkubwa wa chama kinachounda Ilani?

Swali la pili; Kituo cha Afya Mkalama pia ni cha wakati wa ukoloni hakina uwezo hata wa kufunga P.O.P kama mtu amevunjika mkono au mguu, hivyo wananchi wanateseka na kinahudumia wananchi takribani 15,000. Serikali ina- commitment gani kuhusiana na bajeti hii inayokuja kuhusiana na Kituo hiki cha Afya cha Mkalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Kinyangiri ni kituo chakavu na kituo kongwe, Serikali imeshaweka mpango wa kutafuta fedha ili kwenda kukikarabati pia kuongeza majengo ambayo yanapungua. Nimhakikishie kwamba Serikali hii kwa sababu inatekeleza Ilani cha Chama cha Mapinduzi na Kiongozi wetu alifika pale na kutoa maelekezo hayo, tunachukua maelekezo hayo na tunaanza kuyafanyia kazi kuhakikisha tunapata fedha kwa ajili ya kituo cha Kinyangiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pili; kuhusiana na kituo cha afya cha Mkalama ambacho nacho ni chakavu tutaendelea kutenga fedha kwa awamu ili tuweze kuvikarabati vituo kama hivi pia kuongeza miundombinu ambayo inakosekana. Ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Manispaa ya Singida ipo katikati ya nchi na malori kutoka upande wa nchi yanapita pale; je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuwahisha ujenzi wa bypass hii ili kuondoa msongamano unaokua kwa kasi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wakati wenzetu wanaongelea Bypass, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama haina hata mita moja ya lami; na kwa kuwa, upembuzi yakinifu wa barabara ya Simiyu – Singida umekamilika: Serikali haioni haja katika bajeti hii kutenga walau kilometa 20 Makao Makuu ya Halmashauri ya Mkalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Mtinga, Mbunge wa Mkalama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Singida kuna traffic kubwa. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba tumekamilisha mwaka 2022 kufanya usanifu na tunavyoongea sasa hivi, tayari tumeshafanya tathmini ya wale watakaofidiwa kupisha barabara; na Serikali inaandaa malipo kwa ajili ya kuwafidia hawa watu watakaopisha barabara. Kwa hiyo, tunataka tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida kwamba, Serikali imedhamiria kwa dhati kujenga hiyo bypass.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua kwamba barabara aliyoitaja ni muhimu sana ambayo pia ni kutoka Singida kwenda Sibiti hadi Bariadi. Naomba pia, avute Subira, tuone kwenye bajeti hii inayokuja tumetenga nini? Ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara hii inaangalia sana suala la maslahi ya wasanii na michezo kwa ujumla; ni lini Serikali itapitia upya makato inayokata katika mambo ya michezo? Kwa mfano juzi Simba wamepata milioni 180 katika 450; ni lini itapitia makato haya ambayo ni kandamizi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na swali la Mheshimiwa Mbunge Isack kuwa liko pembeni kabisa ya swali la msingi, lakini kimsingi tunaangalia utaratibu ambao utawezesha vilabu vyetu viweze kuendelea kufaidika zaidi. Lakini kuna gharama kubwa za uendeshaji wa michezo inayotajwa na taasisi zetu zinaingia gharama kubwa ambayo inatoka mifukoni kwao kuweza kuifanya michezo hii ifanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo pamoja na lengo letu la kuhakikisha timu zetu zinafaidika, lakini kuna gharama kubwa ambazo taasisi zetu zitashindwa kujiendesha kama tutazizuia moja kwa moja kukata makato yale, ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri sana ya Serikali yanayotia moyo; hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Mkalama inategemea sana vitunguu kwa mapato yake ya ndani.

Je, Serikali haioni haja ya kwamba mpango huu mzuri ufanyike kwa mtindo wa build and design ili uweze kwenda kwa haraka zaidi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa pale Mwangeza kuna mradi wa ASDP two ambao ulibomoka;

Je, Serikali haioni sasa haja ya kuukarabati mradi huo haraka ili wananchi wa pale mwangeza waendelee kupata umwagiliaji wakati wakisubiri hili bonde la vitunguu kufanyiwa design?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi yote ya umwagiliaji ambayo tumeipita nchi nzima utaratibu unaofanyika hivi sasa ni kuhakikisha kwanza tunaanza na upembuzi yakinifu na baadaye ndipo unakuja usanifu wa kina na kisha twende kwenye ujenzi. Hii ni kwa sababu tulipata changamoto ya miradi mingi sana ya miaka iliyopita ambayo haikupitia hatua hii na hivyo imekuwa ikibomoka kwa haraka sana. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa endelevu na ya kudumu ili wakulima waweze kunufaika. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge wavumilie taratibu hizi zikamilike mradi huu utajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la kuhusu Mwangeza. Katika kiambatisho cha saba katika jedwali lile la bajeti yetu eneo la Mwangeza ni kati ya maeneo ambayo yanakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu na baadaye pia tutajenga skimu na kukarabati ili wakulima waweze kupata fursa ya kushiriki katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo ni eneo ambalo lipo ndani katika mipango ya Serikali tayari.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kituo hiki kilikuwa na plan ya kuwa Kituo A na kilishajengwa msingi kwa ajili ya ghorofa na ghorofa hilo lingekuwa na nyumba juu kwa ajili ya OCD. Sasa kwa sababu wamebadilisha na kuwa Kituo B, Serikali sasa ina mpango gani wa kepeleka fedha kwa ajili ya kujenga nyumba pembeni kwa sababu, sasa nyumba haitakuwepo tena juu?

Swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kupeleka gari la Polisi kwa sababu tuna shida kubwa ya magari katika Halmashauri ya Mkalama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba kwa ajili ya Askari au Mkuu wa Kituo ni kweli kwamba, awali ilikuwa kiwe Daraja A, lakini Sera ya Jeshi la Polisi inatambua Kituo cha Polisi Daraja A ni kituo kikubwa akinachostahili kujengwa kwenye ngazi ya Mkoa kwa maana ya kuwa chini ya Regional Police Commander (RPC), lakini hivi vinavyotokea ngazi ya Wilaya vinapaswa viwe Daraja B. Kwa hivyo, nyumba ile itatengwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kutoka kwenye mfuko wetu wa tuzo na tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gari la Polisi, juzi nilijibu hapa kwamba, tumetenga bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya Polisi, magari haya yatakapopatikana, Wilaya ya Mkalama ni moja ya Wilaya itakayopelekewa gari na pikipiki kuwezesha shughuli za ulinzi na usalama wa raia. Nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Ni lini Serikali itaigawa Kata ya Mwangeza ambayo ina idadi ya watu 32,000 na hivyo huduma ni ngumu sana kwa wananchi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtinga ni kwamba, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha maeneo yale ambayo tayari yameshagawanywa, kwa sababu tutapogawanya Kata mpya maana yake itabidi kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa sekondari nyingine, ambapo nyinyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge humu ndani, kwa sasa Serikali inapeleka fedha katika kila Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari na hivyo tunaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi tukimaliza kupeleka vitu vya msingi katika Kata zilizopo ambazo ni mpya zilianzishwa mwaka 2010 na nyingine zilianzishwa mwaka 2015 Serikali ikikamilisha katika kuweka mazingira bora katika maeneo hayo tutaangalia vilevile katika Kata ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali ninamaswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa mfumo wetu wa bajeti niwakutumia kadri unavyokusanya. Je, na kwa sababu kituo hiki ni cha Wilaya na ni chamuhimu sana Waziri ananiambiaje kuhusu kunipa kipaumbele katika fedha za maendeleo za kwanza tu zitakazopelekwa katika bajeti inayoanza Julai? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa upya wa Wilaya ya Mkalama tuna askari 83 tu, tuna upungufu wa askari 57. Je, Waziri ananipa commitment gani kuhusu vijana askari wanaomaliza kozi muda mfupi ujao kupeleka katika Wilaya yangu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja; tunamuhakikishia kwamba fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha ujao shilingi milioni 992 tutahakikisha kwamba zinapelekwa katika jimbo lake ili kukamilisha kituo hicho kama kipaumbele miongoni mwa vipaumbele vilivyotajwa na Waziri wakati wa kuwasilisha bajeti yake.

Mheshimiwa Spika, pili; tunatambua kwamba wanao askari 84 na katika mgao wa askari wanaotarajia kumaliza mafunzo zaidi ya 4000 waliopo vyuoni Wilaya ya Iramba ni moja ya maeneo ambayo yatazingatiwa ili kuhakikisha kwamba wanapata askari wa kutosha, ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kata ya Kikonda, Kinampundu na maeneo ya Kata ya Ilunda yana shida sana ya mtandao. Ni lini Serikali inaenda kujenga mnara katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, changamoto katika jimbo lake ilikuwa kubwa sana, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo tunayaingiza kwenye utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, lakini katika kata hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja, naomba niipokee ili tukaiingize katika utaratibu wa hatua zinazofuata kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo nina maswali mawili ya nyongeza. Kituo cha Afya Mkalama ni kituo chakavu sana kinazidiwa hata hadhi na baadhi ya zahanati. Je, Serikali haioni haja sasa ya kutamka kabisa rasmi kwamba ni lini watakwenda kufanya ukarabati kwenye kituo hiki ambacho kinahudumia tarafa kubwa sana yenye watu wengi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kituo cha Afya Kinyangiri Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi alipita pale na kutoa ahadi na akaweka na dead line kwamba mwezi wa 12 mwaka huu kitakuwa kimeshafanyiwa upanuzi na ukarabati. Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania akakazia ahadi hiyo juzi alivyokuja Singida. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kutamka rasmi kwamba wanakwenda kufanya ukarabati kwenye kituo hiki kwa kuzingatia kauli za wakubwa wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga Mbunge wa Jimbo la Irambva Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Kituo cha Afya hilki cha Mkalama ambacho ni chakavu sana Serikali imekwisha kiainisha kama nilivyotangulia kusema. Hivi sasa tuko kwenye utaratibu wa kutafuta fedha na fedha ikipatikana mapema iwezekanavyo itapelekwa Halmashauri ya Mkalama kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Mkalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mkalama kwamba Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Afya. Inatafuta fedha na mapema iwezekanavyo fedha ikipatikana tutahakikisha kinakarabatiwa na kuwa hadhi ya kituo cha afya kama vilivyo vituo vya afya vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kinyangiri ni kweli ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kipaumbele na natoa kauli rasmi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba tunakwenda kutekeleza ahadi ya Rais. Tunakwenda kutekeleza ahadi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi mapema iwezekanavyo, ahsante.