Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Venance Methusalah Mwamoto (83 total)

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa kuna umuhimu wa kuunganisha barabara za mikoa na wilaya na kwa kuwa barabara inayounganisha barabara ya Iringa na Morogoro inapitia kwenye milima Kitonga na kwa kuwa linapotokea tatizo katika milima hiyo inakulazimu upite Dodoma, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha kuunganisha barabara nyingine ambayo ni fupi inayoanzia Kidabaga – Idete – Itonya - Mhanga ambayo inaenda kutokea Mbingu kule Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hili eneo la Kitonga likiwa na matatizo wasafiri wa upande wa barabara hii wanayoitumia kutoka Dar es Salaam – Mbeya na kwenda Tunduma wanapata matatizo sana na wakati mwingine wanalazimika kupitia njia ambazo ni ndefu zaidi. Ni kweli vilevile hii barabara iliyoongelewa na Mheshimiwa Mwamoto inayoanzia Kidabaga na kuingia Morogoro ni barabara fupi sana na sehemu ya kuunganisha ni kilometa zisizozidi 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutahakikisha eneo hili tunalifanyia kazi kwa haraka ili azma ya halmashauri zilizokuwa zinafungua barabara pande zote za kutoka upande wa Morogoro na upande ule wa Iringa iweze kukamilika kwa kumalizia hicho kipande kidogo kilichobakia cha kuunganisha mikoa hiyo miwili.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri. Niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kilichopelekea kuunda Tume hii mpaka kwenda Zurich ilikuwa ni swali ambalo liliulizwa hapa ndani na Mheshimiwa Hafidh Ali na imekuwaje Serikali imeshindwa kutoa jibu mapema mpaka leo baada ya kuuliza swali ndiyo majibu yamekuja?
Swali la pili, kwa kuwa kutotambuliwa kwa ZFA na FIFA kutapelekea bado kuwa na timu ya Taifa moja na kwa kuwa TFF na ZFA zinaposhiriki Kimataifa zinapata tatizo la ukosefu wa fedha na hivyo kupelekea timu zetu za Taifa kufanya vibaya, je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kuzichukua timu za Taifa wakati zinaposhiriki kwenye mashindano ya Kimataifa ili tusiendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwamoto kwa mchango wake mkubwa kwa michezo ya nchi yetu, hasa kwa michezo ya hapa Bungeni kila asubuhi namkuta uwanjani anafanya kazi nzuri, namshukuru sana.
(a) Ni kweli kwamba suala hili la mvutano kati ya ZFA na TFF limechukua muda mrefu sana. Limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu pamoja na magizo ya Serikali kwamba jambo hili liwe limemalizika, moja ya sababu pamekuwa na mivutano na tumeshuhudia mivutano mikubwa kwenye ZFA kwa maana ya uongozi, lakini juzi wamefanya uchaguzi na tunaamini sasa hali ya ZFA imetulia na Serikali tutaweka juhudi za kutosha kuhakikisha kwamba ZFA na TFF wanakaa chini na kusaini makubaliano. Lakini sababu ya pili, walipokaa mara ya kwanza wakatengeneza makubaliano, upande mmoja wa pande hizi mbili ulisita kusaini hayo makubaliano mpaka leo. Kwa hiyo, tutakachofanya tutaweka nguvu kuhakikisha pande hizi mbili zinakuja pamoja, zinasaini makubaliano na utekelezaji wa makubaliano yale unaanza kutekelezwa.

(b) Sehemu ya pili ya swali lake ameuliza kama Serikali sasa iko tayari kufadhili timu ya Taifa. Kwa kweli nchi yetu ina michezo mingi na haiwezekani Serikali ikatenga pesa kwa ajili ya michezo yote. Tunachofanya ni kuviwezesha vyama vya michezo nchini kwanza viwe na vyanzo vya mapato vya kutosha kufadhili na kuendesha michezo, lakini pia kuhamasisha sekta binafsi na wafadhili wengine waweze kusaidia kazi hii ya kufadhili michezo nchini na wako ambao wamekuwa wakifanya vizuri, ndiyo mana ligi zetu nyingi zinakwenda vizuri.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jibu lako zuri, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa moja ya usumbufu mkubwa wanaopata wakulima ni suala la usambazaji wa pembejeo ambao haufiki kwa wakati. Lakini tatizo kubwa ambalo linasababisha hilo ni mawakala kutokufikisha kwa wakati na mawakala wamekuwa wakilalamika kwamba hawalipwi pesa za usambazaji. Mpaka leo ninavyozungumza kuna baadhi ya mawakala waliosambaza mwaka jana ambao walikuwa wanafanya kazi hiyo kwa niaba ya makampuni makubwa, kama TFC na MINJINGU, hawajalipwa. Sasa Serikali haioni kwamba tutaendelea na hili zoezi la kuwasaidia wananchi na kutowasaidia wengine wanaosambaza ni makosa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba kumekuwa na ucheleweshwaji wa malipo kwa mawakala wanaotoa huduma za ruzuku. Nimuhakikishie tu kwamba tatizo hilo linashughulikiwa sasa na Wizara inaandaa malipo ili utaratibu wa kuwalipa uweze kuanza bila kuchukua tena muda. Lakini nimueleze kwamba kama nilivyosema nilipokuwa najibu swali la nyongeza la
Mheshimiwa Gama ni kwamba utaratibu mzima unaotumika kwa sasa ni mbovu ndio umetuleta hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu ambao hauwanufaisha walengwa, watu ambao wamenufaika sana na mfumo tulionao sasa wa pembejeo ni wajanja wachache. Mara nyingi pembejeo hizo hazifiki kwa wananchi, lakini hata pale zinapofika zinachelewa, kwa hiyo nilichosema ni kwamba Wizara yangu iko katika hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu mpya ambao ni tofauti na huu ili kuweza kuondoa changamoto hii. Pembejeo ziweze kufika kwa wakati na kwa bei ambayo wananchi wanamudu, lakini vilevile kusiwe tena na malalamiko haya ya ucheleweshwaji wa mawakala kulipwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa barabara iliyotajwa ya kuunganisha Mbeya na Makete bado imechukua muda mrefu na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ana mpango wa kwenda Mkoa wa Njombe, haoni sasa kuna sababu kubwa ya kupita na kuangalia, kutokana na majibu aliyojibu kuona kama kweli itajengwa kwa wakati ambao ameahidi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hizi zipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ikiwemo hii ya kuunganisha Wilaya ya Kilolo na Iringa Mjini. Je, haoni sasa ni muda muafaka wa kufika na kutembelea barabara ambayo inaanzia Ipogolo – Ndiwili - Kilolo ambayo kwa miaka saba imejengwa kilometa saba na kilometa zilizobaki ni 28, haoni kwamba itachukua miaka 28 pia kumalizia hicho kipande kilichobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nitakagua kama ambavyo amependekeza ili kuthibitisha kwamba eneo hilo tunalokusudia kulijenga kweli litajengwa.
Pili, kuhusu barabara ya kutokea Kilolo hadi Iringa, ni barabara ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020 na hata hiyo barabara nyingine nayo ni sehemu ya Ilani. Namhakikishia, barabara zote zilizopo ndani ya kitabu cha Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tutazishughulikia na kuzikamilisha kwa awamu kadri tutakavyokuwa tunapata uwezo mwaka hadi mwaka.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la msingi lilikuwa linahusu kuhusu kupandisha vituo vya afya; na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo toka ilipoanzishwa mwaka 2000 haijawahi kuwa na hospitali ya Wilaya, imekuwa na Kituo cha Afya cha Dabaga na hivyo imepelekea ili wananachi kufuata huduma za hospitali inabidi waende Ilula kilometa zaidi ya 120.
Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu wa kupandisha hadhi kituo hicho cha Dabaga kuwa hospitali ya wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwamoto, Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba tupokee huo mtazamo kwamba Kilolo hakuna Hospitali ya Wilaya kwa hiyo ina maana lazima watu waende Ilula kwa ajili ya kupata matibabu. Nilieleza hapa katika vipindi tofauti kwamba mchakato wa kupandisha ama Zahanati kuwa Kituo cha Afya au Kituo cha Afya kuwa Hospitali ya Wilaya kuna utaratibu wake muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wake unaanzia kwenye WDC kwa maana ya Mabaraza ya Madiwani mwisho wa siku unafika Wizara ya Afya ambao ndiyo wenye dhamana. Wizara wakishafanya uhakiki kwamba kituo hicho kimekidhi kuwa hospitali ya wilaya basi inapandishwa moja kwa moja kama nilivyozungumzia katika suala la wenzetu wa Nanyumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo haya, naomba nimuelekeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua yupo makini sana katika Kamati ya TAMISEMI, ahakikishe kwamba ule mchakato wa awali unaenda na kuangalia vigezo vinafikiwa mwisho wa siku na sisi TAMISEMI tutaweka nguvu na Wizara ya Afya wataangalia vigezo vikikubalika kituo hicho cha afya kitapandishwa hadhi lengo kubwa likiwa ni kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi. Ni kweli haiwezekani wala haiingii akilini mwananchi kutembea kilometa 100, ni umbali mkubwa sana.
Kwa hiyo, hili ni jambo la msingi na naomba mchakato uendelee kwa kufuata utaratibu unaoelekezwa, nadhani Serikali italiangalia kwa jicho la karibu zaidi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu zuri. Swali langu ni kwamba, kuna maeneo ya Wilaya ambayo hata Hospitali za Wilaya hakuna. Je, Serikali inasemaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kufika maeneo kama ya Kilolo, kuja kuona anafanyaje ili kuhakikisha angalau vile Vituo vya Afya na Zahanati ambazo zimeanzishwa na wananchi, kuzipa msukumo ili angalau wapate matibabu na wao wajue kwamba ilani yao wanaitekeleza vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba niko tayari na bahati nzuri Mheshimiwa Mwamoto Jimboni kwake wanakuja hapa Ihula karibu kilometa 100. Kwa hiyo, wana changamoto kubwa na matatizo haya tunayafahamu vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi, Mheshimiwa Mwamoto kwamba tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo. Tutafika, tukiangalia tutapata jawabu kwa pamoja. Kama kuna Vituo vya Afya ambavyo vime-advance vizuri zaidi, tutaangalia jinsi gani tuvipe nguvu vile Vituo vya Afya, ili mradi wataalam kutoka Wizara ya Afya wakija kukagua, vituo vile viweze kupanda, basi viweze kutoa huduma kwa wananchi kwa hadhi ya Hospitali; kwa kadri itakavyoonekana kama mahitaji ya kuwahamisha kutoka katika Kituo cha Afya, kwenda Hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mwamoto naomba nikiri wazi, nitafika Jimboni kwakE tutabadilishana mawazo na wananchi wakE, lengo ni kuboresha huduma ya afya katika nchi yetu.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa sasa hivi suala la michezo Tanzania ni sawasawa na mgonjwa na unapokuwa na mgonjwa aidha umpeleke kwenye maombi, hospitali au kwa mganga wa kienyeji.
Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri na anajua tatizo hilo na tatizo kubwa limekuwa ni kwamba Serikali imeshindwa kuwekeza kutoka chini kwa maana ya kwenye shule za msingi, UMISHUMTA, UMISETA na michezo mingine na kuifuta, sasa Serikali inasemaje kuhusu kufufua michezo hiyo kwa nguvu zote na kupanga bajeti ya kutosha? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa michezo ni ajira na Serikali ilikiri yenyewe kwamba itahakikisha inapeleka ajira kwa vijana kupitia michezo; na michezo inaleta pato la Taifa kwa mfano nchi kama Nigeria, Cameroon na Ghana imekuwa ni pato, sasa Serikali kwa nini imesahau kwamba hiyo itakuwa ni pato kubwa kwa nchi yetu na kuitelekeza michezo? Naomba jibu. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza Serikali haijafuta michezo ya UMISHUMTA, UMISETA kama ambavyo imekuwa ikikaririwa, isipokuwa mwaka huu kilichotokea ni kwamba michezo hii iliahirishwa kwa muda, kwa sababu ya kuwa na maandalizi ambayo hayakuwa yanaridhisha na hivyo tukasema ni vizuri tujipange upya ili michezo hii iwe na maana.Kwa muda mrefu sasa michezo ya UMISHUMTA, UMISETA imekuwa ikifanyikakama matamasha ikifikia kilele mwishoni hakuna matokeo yanayoendelezwa baada ya michezo ile.
Mheshimiwa Spika, Serikali inajipanga kuhakikisha kwamba, michezo hii sasa inapofikia kilele chake wale wanaofanya vizuri wanapelekwa kwenye shule maalum zitakozotengwa kwenye Mikoa na Wilaya kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao badala ya kutokea kama ambavyo imekuwa ikitokea, michezo ile ikimalizika watoto wanarudi kwenye shule zao na vile vipaji vinapotea.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwamba suala la uwekezaji kwenye michezo. Ni kweli michezo inahitaji uwekezaji mkubwa, kwa uwekezaji mdogo hatutapata matokeo ya kutosha. Serikali haijatelekeza michezo kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kwenye bajeti zake, lakini na kuangalia vyanzo vingine ambavyo hata wenzetu wamekuwa wakivitumia kuendeleza michezo. Vyanzo vingine ni pamoja na pesa zinazotokana na Bahati Nasibu za Taifa. Duniani kote Michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa ndio ambayo imekuwa ikifadhili michezo badala ya kutegemea hii bajeti ndogo.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kusaidiana katika kuwekeza katika michezo, tumeona sasa tunakoelekea michezo itakuwa ni biashara kubwa, italipa na hivyo natoa wito kwa wadau mbalimbali kuwekeza katika michezo wakishirikiana na Serikali na tukifanya hivyo tunaamini tutapata matokeo mazuri.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ni Wizara ambazo zinashabihiana katika utekelezaji kwenye maeneo ya Wilaya yetu; na kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo hakuna barabara wala hakuna mawasiliano. Kwa mfano, Kata ya Mahenge katika Kijiji cha Ilindi Namagana, Kata ya Ruaha Mbuyuni katika Kijiji cha Ikula na Kata ya Nyanzwa katika Kijiji cha Nyanzwa hakuna mawasiliano, hakuna barabara, sasa Serikali inasemaje kuboresha maeneo hayo ili wale wananchi nao wahisi kwamba wapo Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, analozungumzia Mheshimiwa Mwamoto ni jambo la msingi, na kama Serikali naomba niseme kwamba ni haki ya Serikali kusikiliza kwanza, nikijua kwamba ujenzi wa barabara una vipaumbele vyake kutokana na Sera za Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengine wanaweza wakashangaa kwa nini barabara kutoka Airport kila wakati inakarabatiwa ni kwa sababu barabara ikiwa bora lazima ikarabatiwe kwanza, lakini barabara ikiwa korofi inawekwa kipaumbele cha mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo haijafunguliwa maana yake inakuwa kipaumbele cha mwisho kabisa. Kwa hiyo jambo la msingi ukiangalia hata Mfuko wa Barabara maana yake hautoelekeza katika kufungua hizo barabara mpya. Ni lazima tubuni mipango mikakati mingine jinsi gani tutafungua barabara hii.
Mheshimiwa Mwamoto najua kwamba tarehe 18 Julai, nitakuwa Jimboni kwako kutembelea, naomba tufike maeneo hayo tubainishe kwa pamoja. Katika ziara yangu naanzia Mkoa wa Iringa katika Jimbo la Kilolo, tutakaa pamoja kama nilivyokuahidi, tutatembelea kubaini nini tufanye kwa pamoja, ni mkakati gani tutafanya ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma inayokusudiwa, na kwamba wakiri kwamba Mwamoto aliyekuwa DC sasa ni Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Kilolo anafanyakazi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Kibondo ni Wilaya ambayo ilikaliwa na wakimbizi na kwa kuwa kuna majengo ambayo yamekaa kwa muda mrefu ya IOM ambayo Serikali ya Wilaya na Mkoa ilisharidhia kwamba yatumike kwa ajili ya chuo hicho. Je, Waziri haoni sasa ili kubana matumizi ya Serikali afike na kutoa ushauri ili yale majengo yatumike kwa ajili hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti swali la pili, kwa kuwa makampuni mengi ya ujenzi baada ya kujenga barabara yamekuwa yakiacha miundombinu ya majengo mazuri. Sasa haoni ni wakati muafaka wa kupunguza upungufu wa wauguzi zikiwepo Wilaya nyingi pamoja na Kilolo kwa kuweza kuyatumia yale majengo vizuri ili Serikali iweze kupata manufaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwamba nifike Kibondo ili nikashauriane na Serikali ya Mkoa ambao wameshapitisha azimio la kutaka kutumia majengo yaliyoachwa na IOM namwahidi nitafika mara baada ya Bunge la Bajeti kukamilika ili nishirikiane na Serikali ya Mkoa nione kwa ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo wana dhamana ya mali na maeneo yote ya wakimbizi, ni nini Serikali itafanya ili kuwezesha azimio lao hilo mkoani kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na majengo yaliyoachwa na miradi mbalimbali ya ujenzi; taratibu kwa kweli zimekuwa ni hivyo kama anavyopendekeza Mheshimiwa Mbunge. Hivyo, wafuate taratibu za kuzungumza ndani ya vikao vyao vya kufanya maamuzi kwenye halmashauri husika, ili walete mapendekezo Serikali Kuu tuone kama yanaweza yakapitishwa na wanaohusika na mradi huo kutumika kwa ajili ya shughuli ambazo wanazipendekeza.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la ulinzi na usalama ni tatizo na sasa hivi ukichukulia kumetokea mauaji ya mara kwa mara nchi hii, na watu wamelalamika kwamba hawasikilizwi wanapokwenda kwenye vituo vya polisi na mahakama na kwa hivyo kujichukulia sheria mkononi. Serikali haioni sasa inabidi ifanyie kazi suala hili ili kupunguza haya mauaji ambayo yamekuwa ni kero na shida katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jambo ambalo ni la muhimu sana wananchi wakalifahamu mauaji ni kweli yanatokea, lakini siyo sahihi kwamba hali ya mauaji haya imekuwa kubwa na inaongezeka zaidi ya ilivyokuwa. Ninasema hivyo kwa uthibitisho wa kitakwimu ambapo takwimu za haraka ukiangalia kwa mfano katika kipindi cha Januari mpaka Aprili, 2016 jumla ya matukio yaliripotiwa yalikuwa ni 1,030 na idadi ya watu waliouawa ni 1,060 ukilinganisha na watu 1,173 katika kipindi kama hicho ambayo ilikuwa kwa matukio 1,153 kwa mwaka uliopita.
Kwa hiyo, inaonekana kuna upungufu wa matukio kama 123 ambayo ni sawa na asilimia 10.7. Hata hivyo punguzo hilo halimaanishi kwamba hatuyachukulii uzito matukio ambayo yanatokea hasa katika kipindi hiki cha karibuni tumeona kulikuwa na matukio yameshamiri kidogo ya mauaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze Bunge lako Tukufu pamoja na kujibu swali la Mheshimiwa Mwamoto kwamba nataka niwatoe wasiwasi wananchi na Wabunge, kimsingi matukio haya ya mauaji yanasababishwa na vyanzo tofauti, kwa mfano kwa haraka haraka nizungumze najua muda ni mfupi lakini asilimia 33 ya matukio ya mauaji ambayo yamejitokeza kipindi cha karibuni ni yanatokana na wizi, 11.6 yanayotokana na ugomvi wa kifamilia, imani za kishirikina asilimia 10.3, wivu wa mapenzi asilimia 7.6, risasi asilimia 6.5, ugomvi wa ardhi asilimia 6.2 na nyinginezo asilimia 24 nukta kadhaa.
Kwa hiyo, utaona kwamba matukio haya ingelikuwa yanatokana na tukio moja tu tungesema kwamba kuna mtandao hatari labda wa jambo fulani. Hata hivyo Serikali lazima ichukulie kwa uzito kupotea kwa maisha ya raia mmoja iwe kwa chanzo chochote kile. Na ndiyo maana sasa Jeshi la Polisi likafanya kwa mafahikio makubwa kwa haraka sana kuweza kuwakamata watuhumiwa mpaka sasa hivi matukio hayo yaliyotokezea aliyoyazungumza Mheshimiwa Mwamoto kwa karibuni watuhumiwa 72, mpaka sasa hivi ambao wanatupa dalili nzuri ya kuwashughulikia na wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee na hiyo kazi na naamini kabisa kazi hiyo ya Jeshi la Polisi itaifanya kwa mafanikio na Waheshimiwa Wabunge na wananchi msiwe na wasiwasi watu wote ambao wamejihusisha katika matukio haya ya mauaji iwe kwa sababu yoyote. Iwe kwa wivu wa mapenzi, iwe kwa ujambazi, iwe kwa ugomvi wa ardhi, iwe kwa kifamilia watatafutwa popote walipo na watachukuliwa hatua za kisheria.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo inafanana kabisa na matatizo ambayo yako hapo, na ni katika Majimbo makubwa, takriban lina kilometa za mraba takribani 21,000; na kwa kuzingatia hilo, Serikali iliamua kutoa Mji Mdogo wa Ilula, sasa ni muda mrefu.
Je, haioni sasa ni muda muafaka wa kupewa hadhi ya kuwa Halmashauri kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika kumbukumbu zangu pale kuna barua ya tarehe 2 Juni, 2015 imetoka Kilolo iliyokuwa ikiomba uanzishaji wa Halmashauri hii. Katika maeneo ambayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaenda kufanya uhakiki, eneo la Kilolo litakuwa mojawapo. Kwa hiyo, tufanye subira katika hilo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa nafasi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu Wilaya zipo kisheria na zipo ndani ya Katiba, Serikali inasemaje kwa baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa vikiwapuuza, vikiwadharau na kutotii amri zao pale wanapotakiwa kufanya hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba yetu na sheria mbalimbali zimeunda nafasi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Katika utaratibu wa Katiba yetu ukisoma katika Ibara ya 64 inaelekeza wazi kabisa kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ni wawakilishi wa Serikali katika eneo husika kwa maana ya Rais. Kwa hiyo, wako pale kwa niaba ya Serikali na ndiyo maana kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanasimamia na kuelekeza yale matakwa na mambo yote ambayo Serikali imekuwa ikiyataka yafanyike katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa mujibu wa Sheria ya Utawala wa Mikoa, Sura ya 97, katika kifungu kile cha 14(1)-(3) imeelezea wazi pia kazi ya Wakuu wa Wilaya. Kwa hiyo, niwaombe tu wanasiasa wenzangu ikifika masuala ya utendaji, viongozi hawa wako kwa mujibu wa sheria na Katiba hawajajiweka wenyewe. Kwa hiyo, amri zao, maelekezo yao ni lazima yazingatiwe kwa sababu wako pale kwa niaba ya Mheshimiwa Rais na kwa niaba ya Serikali.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningependa niulize swali langu moja.
Kwa kuwa fedha ambazo zinatolewa kwa hawa akina mama lishe na kufanya biashara ni fedha za Serikali ambao walio wengi zinatoka TASAF, ni fedha za kuondo umasikini. Na kwa kuwa sasa Watendaji wengi sana wa Vijiji hawajaajiriwa kwa hiyo wanafanya zile kazi kama kukomoa. Je, sasa Serikali inasemaje kuhusu hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba maeneo mengi vijijini Watendaji wa Vijiji na hata wa Kata, hawajaajiriwa kwa ajira rasmi na Halmashauri husika, na hii inapelekea utekelezaji wa shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na uwajibikaji kuwa katika kiwango cha chini kwa sababu mtu anaona mimi sijaajiriwa kwa hiyo nikifanya lolote lile ni sawa tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekubaliana na tulipitisha hapa utaratibu kuanzia mwaka jana, tumeruhusu kwamba kada fulani za chini zinaweza zikatolewa ajira hizo na mamlaka husika kutegemeana tu bajeti zao walizozitenga. Nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinatoa ajira za Watendaji wa Vijiji ambao kwa sifa na kwa utaratibu tulioweka wanaruhusiwa kuzitoa wao ili waweze kuwa wamekamilisha idadi ya vijiji na watendaji wote wakamilike wale walioajiriwa na Serikali itakuwa tayari kupokea isipokuwa tu wazingatie sifa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vyuo ambavyo vinatoa watu waliosomea masuala ya mamlaka ya Serikali za Mitaa na mifumo ya Serikali za Mitaa Tanzania, Chuo cha Hombolo ambacho kina wataalam wazuri sana tunacho Chuo cha Mipango, Dodoma ambacho nao wamefundishwa masuala haya ya mipango vijijini ni vizuri watu wanaoajiriwa wakawa wanatoka kwenye vyuo hivi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Simanjiro, naomba niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikia kilio chetu, lakini sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa swali la msingi lilikuwa linahusu ahadi za viongozi; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alipopita kwenye maeneo mbalimbali alitoa ahadi kuhusu maji ikiwepo Wilaya ya Kilolo maeneo ya Ilula na aliahidi kwamba suala la maji litakuwa ni historia kwa Wilaya ile. Je, Serikali inasemaje na mwaka huu imetenga fedha kwa ajili ya wananchi wa Ilula?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo la maji linatatuliwa kwa ujenzi wa mabwawa na kwa kuwa kuna mabwawa yaliyojengwa sehemu za Nyanzwa, Ilindi, Ruaha Mbuyuni na Mahenge na wakati yanajengwa wananchi walikuwa wachache, sasa wameongezeka kwa hiyo maji yale hayatoshi. Serikali itakuwa tayari kuongeza fedha ili wananchi wale waweze kupata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza suala la ahadi, ahadi zote zimeishaainishwa. Wizara ya Maji tuna ahadi zaidi ya 60 ambazo Mheshimiwa Rais wetu Magufuli wakati anapiga kampeni aliwaahidi wananchi. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba tunatekeleza ahadi za viongozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ilula nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari mazungumzo yanaendelea na Serikali ya Australia na mradi huu wa Ilula utagharimu dola milioni tisa, kwa hiyo, tunaufanyia kazi. Pia katika mwaka huu wa fedha kwenye bajeti tumemtengea shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mabwawa, hii ni ahadi yetu, kama tumejenga mabwawa, sasa hivi wananchi wameongezeka, tutakachofanya moja ama ni kulipanua bwawa lile kama lina uwezekano wa kupanuliwa lakini pili ni kuongeza bwawa jipya. Kwa sasa tumeshaagiza Wakurugenzi wote wajaribu kufanya utafiti, waainishe maeneo yote ya kujenga mabwawa na walete ili tuweze kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli hiyo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo Wizara hii imefanya sasa naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, kuna baadhi ya Vijiji vikiwemo Ng‟ang‟ange, Pomelini, Masege, Mwatasi, Kesamgagao, Masisilo, Ukumbi na vijiji vingine umeme tayari umeshafungwa na umefika, sasa tatizo ni kuwasha! Ni lini utawashwa ili wananchi sasa waendelee kuishi kwa matumaini na mategemeo makubwa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, yeye suala lake ni kuwasha tu, lakini miundombinu yote ipo. Nimeshaongea na Meneja, wiki ijayo Jumanne atamwashia Mheshimiwa Mwamoto katika vijiji vyake vyote. Kwa hiyo, kwake umeme utawaka bila wasiwasi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilolo ni majimbo yanayopakana. Kwa kuwa vijiji vingi ambavyo vinapakana na hifadhi huwa haviruhusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi lakini tembo wamekuwa kero kwenye vijiji hivyo, kwa mfano, Kata ya Ruaha Mbuyuni, Mahenge na Nyanzo hivi ninavyozungumza uharibifu mkubwa wa mazao umefanyika. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutoa tamko lolote leo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wanyama waharibifu kuvamia mashamba, ni kweli Serikali inazo taarifa kutoka katika vijiji mbalimbali vinavyopakana na hifadhi juu ya usumbufu wa wanyamapori wanaoharibu mazao ya wananchi. Siku za nyuma tulikuwa tukijikita zaidi katika kutumia vikosi vya Askari wa Wanyamapori kupambana na wanyama hao, lakini pale inapotokea wameshafanya uharibifu tulikuwa na ule utaratibu wa vifuta jasho.
Hata hivyo, Serikali imeshaona kwamba kutumia vikosi tu vya Askari wa Wanyamapori nguvu hiyo haitoshi lakini pia kusubiri mpaka wanyama wawe wameshafanya uharibifu ndipo tulipe vifuta jasho nao pia siyo mkakati mzuri kwa sababu siyo endelevu wakati mwingine gharama zinakuwa kubwa kuliko bajeti ya Serikali. Kwa hiyo, kuanzia sasa Serikali imejipanga upya kubadilisha ulinzi ule wa kutegemea tu Askari wa Wanyamapori na kwenda kwenye ulinzi shirikishi au kufanya uhifadhi shirikishi. Vijiji vyote vinavyopakana na hifadhi kutapatikana askari ambao watawezeshwa kwa kupewa elimu na silaha kwa utaratibu ambao utaonekana unafaa ili ulinzi sasa ufanyike kwa njia ambayo ni pana zaidi ili kuweza kuzuia zaidi kuliko kusubiri kutibu baada ya kutoa vifuta jasho
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize swali moja la nyongeza.
Pamoja na kufanya kazi nzuri ya kupatikana kwa wafanyakazi hewa ambao takribani wataokoa zaidi ya shilingi bilioni kumi na Serikali inapaswa ijazie hizo nafasi kutokana na watumishi wengine. Lakini walio wengi ni wale wanavyuo ambao sasa wanakwenda kuanza vyuo, lakini mpaka leo tunavyozungumza hawajapata mikopo wanahangaika. Je, kuendelea kutokuwapa mikopo hatuoni kwamba tunaweza tukazalisha hewa nyingine zaidi? Sasa Serikali iseme mpango mzima kwa nini mpaka leo mikopo ya wanafunzi baadhi hawajapata?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa katika nyakati tofauti tofauti ni kwamba kimsingi fedha kwa ajili ya mikopo kwa awamu hii zilishatolewa jumla ya shilingi bilioni 80 na tayari bajeti yake ipo sawa. Suala lililokuwa limetuchelewesha lilikuwa ni suala la uhakiki kwa misingi kwamba watu wanaohitaji mikopo sio wote watakaoweza kupata kwa sababu fedha ambayo inatolewa ni kwa ajili ya watu wale ambao hasa wana uhitaji wa kupita wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo nina maana kwamba tumeangalia mikopo tu, lakini Serikali kupitia Wizara ina majukumu mengine makubwa sana ya kuangalia mfano tumeona vijana wetu wengi walikuwa wanakaa katika maeneo ambayo walikuwa wakijipangia wenyewe, mabweni yalikuwa yanakuwa hayapo, vitendea kazi vingine vilikuwa viepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyoangalia katika utoaji wa elimu tunaangalia Nyanja zote na haswa katika kuona kwamba elimu inatolewa kwa kiwango kinachostahili na kwa haki inayostahili mwanafunzi kuipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo wale wote ambao wanastahili kupata mikopo kutokana na uhitaji uliopimwa, mikopo yao itapatikana, lakini hata hivyo lazima tuzingatie kwamba mikopo hiyo inamfikia mlengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini ndani ya wiki hii tutakuwa tumefikia mahali pazuri zaidi. Ahsante
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la maji pale Ilula, Wilaya ya Kilolo ni kubwa na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba anataka kuwatua akinamama ndoo kichwani, ni la muda mrefu. Je, Waziri anaweza akatoa majibu mazuri ambayo yatawafanya wananchi wa Ilula wapate moyo na kuacha sasa kuniita mimi Mwamaji badala ya Mwamoto?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kwamba Serikali itapeleka maji ya uhakika kwa wananchi wa Ilula. Serikali bado inaendelea kushughulika kuweza kutafuta fedha za kugharamia mradi huo na tupo kwenye hatua nzuri. Serikali ya Austria imeonesha nia ya kusaidia mradi ule, bado hatujakamilisha tu makubaliano ya fedha ambazo tutaweza kugharamia mradi huo, lakini mazungumzo yanaendelea vizuri. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge hutaendelea kuitwa Mwamoto utaitwa Mwamamaji ili kusudi wananchi wa Ilula waweze kupata maji.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa walengwa ni wakina mama ambao wengi wao bado wako Vijijini kama muuliza swali alivyosema. Lakini ukiangalia riba wanatozwa ni sawa sawa na wafanyabiashara wa kawaida na wao wanategemea kilimo. Sasa je, benki hii ili wafikie akina mama wakulima walipo maeneo tofauti na kule Kilolo inaonaje sasa ikiwapa mkopo uwe wa muda mrefu badala ya kuwapa kama wafanyabiashara ndogo ndogo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la riba ni suala ambalo linazingatia masharti yanayotolewa na regulator ambaye ni Benki Kuu na kutokana na masharti hayo benki yetu haiwezi kukiuka masharti ambayo yanawekwa na Benki Kuu ili tu kuwafikia akina mama na ndiyo maana Waziri wa Afya aliagiza tutengeneze scheme maalum kwa ajili ya kuwafikia akina mama wa vijijini na akina mama wajasiriamali wadogo wadogo ili riba itakayotolewa na benki hii iwe ni mahususi na iwafikie akina mama hawa waweze kupata mikopo nafuu zaidi kuliko ilivyo sasa. Kwa hiyo, suala hili tunaliangalia.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hali ya Wilaya ya Tarime kule Rorya inafahamika, kesi ni nyingi na zinachukua muda mrefu kuamuliwa na hivyo, kuwatia hasira watu wa Rorya, kama ambavyo tunajua.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuongeza watumishi wengi zaidi ili kesi ziende haraka? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyoko Rorya yanafanana kabisa na yaliyoko Kilolo na kwa kuwa Kilolo ni Wilaya ambayo imeanzishwa toka mwaka 2000, lakini haina Mahakama yoyote.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wa kuanzisha Mahakama ya Wilaya kwa kuwa kesi nyingi za Wilaya ya Kilolo mnajua hasira zao huwa zinaishia wapi ili waanzishe haraka?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu wa kuongeza watumishi katika mahakama zetu mbalimbali ili kesi ziweze kwenda haraka. Pia niweze tu kutoa tahadhali vilevile kwamba hata kama kuna watumishi wapo wa kutosha, bado kesi ambazo zinachukuwa muda mrefu ni kesi za jinai ambazo zinahitaji kwa kweli uangalifu wa kutosha hasa upande wa upelelezi na vilevile katika kuchambua ushahidi ambao unajitokeza.
Mheshimiwa Spika, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa upande wa mahakama tutajitahidi kuongeza watumishi kama nilivyosema kwa upende wa Wilaya hiyo ya Rorya na tutajitahidi vilevile kuharakisha usikilizaji wa kesi nchini. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mahakama imejipanga kwamba, baada ya mwezi Disemba mwaka huu, kuanzia mwaka kesho Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu zitahakikisha hazina kesi za zamani zilizozidi umri wa miezi 24 yaani miaka miwili. Vilevile Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi hazitazidi mwaka mmoja na Mahakama za Mwanzo hazitakuwa na kesi za zamani za miezi sita.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba Kilolo haina Mahakama ya Wilaya, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge, hizo Wilaya tunazihitaji, lakini ujenge na hoja tuletee kwa maandishi, vilevile tuhakikishie una eneo lenye nyaraka stahili tuweze kuingiza katika mpango wa ujenzi wa mwaka ujao wa fedha.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa fedha hizi ambazo zimekuwa zikipelekwa katika Halmashauri ni kidogo sana kiasi kwamba hata hazitoi msaada mkubwa kwa wale vijana. Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna ubaya gani kama vijana hawa ambao walio wengi hawana ajira hasa wale wanaotoka kwenye vyuo vikuu na sehemu nyingine wakaanzishiwa Benki ya Vijana ambayo itakuwa rahisi kui-control na kuwapata wale wahitaji ambao kwa kweli wanataka kutumia hizo fedha vizuri hasa sehemu kama za Kilolo na hasa hapa kwake Dodoma, je, atakuwa tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuelekea katika uanzishwaji wa Benki ya Mendeleo ya Vijana lakini kabla hatujafikia hatua hiyo tukasema ni vyema kwanza tuwaanzishie vijana SACCOS mbalimbali ili tuanze kuwakopesha kupitia SACCOS hizo, wajifunze nidhamu ya fedha na matumizi yake na baadaye tutaenda kufikia katika uanzishwaji wa Benki ya Maendeleo ya Vijana wakati tayari tumeshaandaa kundi letu kubwa hili la vijana kwenda kushiriki katika masuala ya fedha. Vinginevyo, usipoanza na utaratibu huu wa kuwazoesha mwisho wa siku fedha ile ya mikopo inaweza kutumika katika mambo tofauti na ikawa haijamsaidia kijana huyu. Kwa hiyo, tumeanza katika SACCOS baadaye tutakwenda mpaka kwenye uanzishwaji wa Benki ya Maendeleo ya Vijana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Kilolo imeanza toka mwaka 2002 takribani sasa ni miaka 15, lakini kwa muda mrefu OCD amekuwa akikaa tarafa nyingine na makao makuu yako Tarafa nyingine na inabidi kuwasafirisha mahabusu kwani wako kule anakokaa OCD zaidi ya kilomita 100 kuwapeleka katika tarafa nyingine ya Kilolo. Kama Serikali yenyewe bado haijajiweka vizuri, kwa nini isitumie National Housing au NSSF kujenga nyumba pale Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumekuwa tukieleza kila siku na leo vilevile, mipango ya ujenzi wa nyumba upo njiani. Kwa hiyo, hakuna haja ya kufikiria kwamba labda suala la OCD wa Kilolo kutokuwa na nyumba halijatiliwa maanani. Namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, pale ambapo mipangilio yetu itakapokamilika na mikataba itakapokuwa imesainiwa, basi ujenzi huo utaanza na tatizo ambalo linamkumba OCD wetu huyo wa Kilolo na Ma-OCD wengine popote nchini litakuwa limepata ufumbuzi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali langu dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, katika Wilaya ya Kilolo kilimo cha mvua ni kilimo ambacho hakitegemewi; sasa hivi kilimo cha uhakika ni umwagiliaji; na kwa kuwa, katika Wilaya ya Kilolo kuna maeneo ambayo tayari mabwawa yalishachimbwa kwa muda mrefu, lakini yanashindwa kusaidia wananchi kwa sababu ya ongezeko la watu; sehemu za Nyanzwa, Ruaha Mbuyuni na Mahenge. Je, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa, ni ahadi ya muda mrefu ya kuboresha mabwawa hayo, atakuwa tayari kufika na kuona ili katika bajeti hii aweze kutenga fedha ili kuboresha mabwawa hayo ili yaweze kulisha wananchi wengi wa Tanzania tuondokane na njaa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme niko tayari kwenda kuangalia hayo mabwawa. Katika orodha tuliyonayo kwa sasa ya mabwawa, tumeainisha pamoja na bwawa hili kulifanyia usanifu upya ili kuyakarabati yaweze kutoa huduma iliyokuwa inatarajiwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa naamini kabisa wapo watu kutoka EPZ ambao walikuwa wanafuatilia jambo hili na kwa mara ya mwisho shamba hili lilifutwa miaka mitano iliyopita, kwa hiyo jambo hili lilikufa. Lakini kutokana na jitihada za Mkuu wetu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi limefufuliwa. Sasa Mheshimiwa huoni kuna haja sasa ya wewe mwenyewe kufika na kujionea; kwasababu, katika Mkoa wa Iringa sehemu pekee ambayo tumeitenga ni sehemu ambayo wananchi waliitoa au tulinyang‟anya mashamba kutoka kwa watu wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawayatumii. Sasa huoni kuna haja yaw ewe Mheshimiwa Waziri, na kwa kuwa, umesoma Tosa Maganga, ukafika ukaona hili jambo? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, kiashiria kimojawapo cha ujio wa viwanda ni pamoja na EPZ na mambo mengine, na ili viwanda viendelee, ili upate viwanda ambavyo unaimba kila siku na kuvizungumzia vizuri unahitaji uwe na miundombinu ya barabara, maji na umeme; na ukichukulia kwamba katika Mkoa wa Iringa sehemu pekee ni Kilolo ambayo ina sifa hizo, lakini haina miundombinu ya barabara, maji wala haina umeme wa kutosha. Sasa je, huoni kuna haja ya wewe na Mawaziri wenzio mkakaa mkaangalia uwezekano wa kuboresha miundombinu, hasa katika Wilaya ya Kilolo katika barabara za Rang‟ang‟ange, Kidabaga, Mwatasi na sehemu nyingine?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari na nilishazungumza hata Mheshimiwa Ritta, kuna viwanda vya maji vinatengenezwa. Niko tayari sana, nakwenda, na nimeeleza kwenye jibu la msingi kwamba, inatengenezwa master plan ambayo itaonesha miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi. Miundombinu wezeshi na saidizi ndio inawahusu Mawaziri wengine. Ngoja mimi nisafishe njia, Mawaziri wengine watakuja, nakwenda Kilolo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo Wizara hii inafanya, naomba niulize swali dogo tu la nyongeza. Niliwahi kuuliza hili swali kwamba kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ndiyo wilaya pekee ambayo maji mengi yanayojaza Kihansi yanatoka kule ambayo ndiyo yanasaidia kupelekea kuleta umeme nchi hii. Je, Kilolo inanufaikaje sasa? Naomba kwa nafasi hii atueleze hapa wananchi wa Kilolo watanufaika vipi ili kuhakikisha wanapata umeme.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa eneo la Kilolo linatupatia maporomoko ya maji ambayo yanatusaidia sana kuingiza kwenye Gridi ya Taifa. Lakini wananchi wa Kilolo pamoja na hasa wananchi wa Kihesa Mgagao watanufaika sana na umeme huu na nitaje tu Mheshimiwa Mwamoto, hivi sasa katika Mkoa wa Iringa, REA Awamu ya Tatu imeshaingia na eneo mojawapo ambalo linapelekewa umeme ni pamoja na Kihesa Mgagao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa Kilolo wataendelea kunufaika na miradi ya umeme.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyokiri Mheshimiwa Waziri, sheria hii ni ya muda mrefu lakini imekuwa ikikinzana
sana na baadhi ya mila, desturi za makabila na baadhi ya sheria za dini ambazo baadhi ya makabila na sheria za dini zinatambua mtoto wa kike hata akiwa na miaka kumi akishavunja ungo ni mtu mzima. Hivyo, haioni sasa hiyo pia ilikuwa ni kichocheo kikubwa cha watoto wadogo kuolewa kabla ya wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sheria hii ya ndoa imechelewa na kusababisha ongezeko kubwa
la ndoa nyingi kuvunjika na kusababisha watoto wa mitaani kuongezeka, sasa Serikali haioni kwa kuwa Katiba bado itachukua muda, sheria hiyo iletwe hapa ili tuifanyie marekebisho?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Moja, kuhusu suala la umri wa msichana au mvulana kuoa pamoja na suala la imani, dini na desturi. Kwa wale
ambao wametabahari (wame-specialize) katika eneo hili la Sheria za Ndoa watafahamu kwamba hili ni moja ya maeneo ambayo yanahitaji umakini mkubwa sana ili kufikia muafaka wa nini kifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bara la Afrika Tanzania ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kufanikiwa kutunga Sheria ya
Ndoa. Uganda toka mwaka 1966 chini ya Ripoti ya Kalema mpaka leo wameshindwa kuwa na Sheria ya Ndoa, kwa sababu ya mambo hayo ya mila, desturi na imani. Kenya ambao mwaka 1968 waliunda Tume ya Spry, wameweza kutunga sheria mpya ya ndoa ambayo haifanani na ya kwetu kwa maana ya kwetu ni bora zaidi baada ya Katiba yao mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ya ndoa ilipotungwa mwaka 1971 ili kuweza kuvuka, yalikuwepo maarugu (rationale). Maarugu hayo yaliyosababisha baadhi ya vipengele ambavyo leo vina upungufu, ndiyo yaliyowezesha sheria hii kupita na moja lilikuwa ni umri wa mtoto kuolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka wa Serikali Na.1 wa mwaka 1969, Ibara ya 7 inaeleza kinagaubaga kwamba huo ndiyo ulikuwa umri pia uliopitishwa na Umoja wa Mataifa.
Sasa kwa kuzingatia muktadha wa leo, mazingira ya leo, ni dhahiri kabisa kwamba eneo hilo linahitaji kufanyiwa
marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwa mtoto wa kike; ukisoma kifungu cha 15(2) kinaruhusu mtoto wa kike lakini
hata mtoto wa kiume kuoa chini ya umri wa miaka 14 na hiyo ilikuwa kukubaliana na mazingira ya wakati ule, kwa
sababu makundi mawili mwaka 1971 yaliikataa Sheria ya Ndoa, ilikuwa ni Baraza la Maaskofi Katoliki na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania na ilikuwa ni vyema baadhi ya maoni hayo kuyachukua ili tuvuke, lakini baadhi ya mambo hayo sasa kwa muktadha wa leo yamebadilika, tutayafanyia kazi na yanahitaji uangalifu mkubwa ili tusikwame kama
walivyokwama Uganda na Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masuala yanayohitaji afua
mbalimbali (interventions) ili kuweza kuyavusha.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini swali langu hasa lilikuwa linahusu upande wa umeme. Naomba niulize maswali mawili madogo, kwa kuwa Waziri wa Nishati yuko hapa kama ataona anaweza kumsaidia basi anaweza akajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ambalonalielekeza Wizara ya Maji; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Kilolo kuna vyanzo vingi vya maji, lakini sasa hivi wakulima walio wengi walikuwa wanategemea sana vilimo vya mabondeni, kwa lugha ya kwetu tunaita vinyungu ambavyo ndiyo vimewapelekea kuwasomesha watoto zao na kuendesha maisha ya kila siku lakini sasa hivi wamezuiwa. Kwa kuwa Serikali ilipokuwa inazuia ukataji wa miti ilihamasisha watu watumie umeme na kupunguza bei ya gesi sasa Serikali imezuia watu wasilime kwenye vyanzo vya maji, Wizara imejipangaje ili kuhakikisha wale wananchi wanaendelea kupata fedha kwa kutumia kilimo cha vinyungu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nilitegemea ningejibiwa na watu wa umeme, kwamba kwa kuwa vyanzo vingi vimekwenda Kihansi na Kihansi ndiyo inatoa maji wananchi wa Kilolo wananufaika vipi kwa sababu wametumia muda mwingi kutunza vyanzo vile? Naomba maswali yangu yajibiwe.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi wa kwanza ni hivi, sio wananchi wa Kilolo peke yake ni suala la dunia nzima, unahitaji maji kuzalisha umeme, lakini unahitaji maji kwa ajili ya umwagiliaji. Huu ni mjadala ambao dunia nzima wataalam wa maji na wa umeme wanaendelea kujadiliana. Kwa hiyo, siyo kitu cha ajabu kwa kwetu hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la umwagiliaji tulivyoenda huko vijijini kusema ukweli zile mbinu wanazozitumia ni za kizamani, mtu anakuja anajenga yale mataruma kwa zege, wakati wa mvua anamwagilia, wakati wa kiangazi anamwagilia. Kwa hiyo, nadhani Serikali imefanya utafiti hasa watu wa Kilimo kwamba kuna njia bora za umwagiliaji. Cha kwanza ni kutumia njia bora za umwagiliaji, lakini wote wawili wanahitaji maji, wakulima na watu wa kuzalisha umeme, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la wanafaidikaje, tuna mradi mmoja katika miradi ya REA III ambayo tutakuja kuieleza kwenye bajeti yetu kuna mradi wa kuwapatia watu umeme walio kwenye mkuza mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Iringa - Dodoma mpaka Shinyanga kama ambavyo tulivyofanya kuwapatia watu umeme walioko kwenye mkuza wa bomba kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam, huo mradi tayari unatekelezwa.
Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Mwamoto afahamu kwamba ndani ya REA III huo ni mradi mmojawapo, wanaotutunzia vyanzo vya maji watapata umeme ule wa jogoo wawili shilingi 27,000, ahsante.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa tatizo ambalo lipo kule Mufindi linafanana kabisa na kule Kilolo; barabara nyingi za Kilolo zimekuwa zikiahidiwa na hasa na Mheshimiwa Waziri. Sasa je, ni hatua gani ambazo inapaswa tuchukue endapo Mheshimiwa Waziri ameahidi kwa upande wa Serikali lakini utekelezaji haujafanyika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ni dhamira, kwa hiyo tunapotoa ahadi tunaonesha dhamira ya kutaka kutekeleza hicho kitu. Hatua inayofuata baada ya kuwa na hiyo dhamira ni kutafuta fedha na mara fedha zitakapopatikana hii ahadi yetu tutaitekeleza.
MHE.VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nimpe pongezi kubwa kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia pale Kilolo kwa ujenzi wa hospitali, ni kilio cha muda mrefu. Pamoja na hayo, bado shida ipo, tuna tatizo kubwa sana la wagonjwa ambao inabidi waende kutibiwa kwenye Kituo cha Kidabaga lakini kituo kile kiko mbali na kata kama Idete, Masisiwe, Boma la Ng’ombe na Kata nyingine. Tatizo ni kwamba hakipo sawasawa kwa sababu hakuna daktari, hakuna chumba cha upasuaji, hakuna wodi ya akina mama wala hakuna ambulance. Sasa kwa wakati huu tunaposubiria ile hospitali, unasemaje?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Halmashauri ya Kilolo, kwanza walikuwa hawana Hospitali ya Wilaya, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, tulipofika pale tulifanya initiatives za kutosha na walipata karibu shilingi bilioni 2.2. Wao ni miongoni mwa watu wanaojenga hospitali ya kisasa sasa hivi, nawapongeza sana kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo najua kwamba kutoka pale kwenda Kidabaga ni mbali sana na ndiyo maana Serikali katika kipindi cha sasa tutaenda kufanya ule ujenzi. Nilishamweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa Kidabaga wawe na amani, kituo chao ni miongoni mwa vituo tunaenda kufanyia uboreshaji mkubwa kwa sababu kijiografia eneo lile lina changamoto kubwa sana. Time frame yetu tuliyoweka ni kwamba kabla ya mwezi wa Disemba kituo kile kitakuwa kimekamilika na facilities zake zote. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali.
Kwa kuwa ukiangalia shule nyingi zilizoungua, chanzo kikuu huwa ni vibatari au mshumaa, hii ni kwa sababu ya kukosekana kwa umeme; kwa kuwa Serikali imeshatoa maelekezo kwamba kila sehemu yenye taasisi kama shule na sehemu nyingine muhimu umeme upite, lakini mpaka leo baadhi ya sehemu wamekosa haki hiyo ya kupelekewa umeme. Je, Serikali inasemaje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba shule zote katika Halmashauri zote kwa nchi nzima tumeshaanza sasa kuchukua stock taking kuona shule za msingi na sekondari ambazo zimekamilika ili zipelekewe umeme kupitia mradi wa REA ambao umeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na nimhakikishie kwamba Halmashauri zote kwa kutumia nafasi hii, Wakurugenzi wote ambao hawajafanya hivyo niwaagize wafanye hivyo ili mradi utakapofika waweze kupitishiwa umeme haraka sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji kwenye Wilaya ya Kilolo ni kubwa na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ina utajiri mkubwa wa mito na vyanzo vya maji; na kwa kuwa tayari kuna utekelezaji mkubwa wa mradi wa maji ambao uliahidiwa na Mheshimiwa Rais ambao Wizara hii inafanya; je, kwa maeneo yale mengine ambayo tumekuwa tukipigia kelele kwa mfano Ruaha Mbunyuni, Wambingeto na sehemu nyingine, Waziri anasemaje? Ni pamoja na kuja kutembelea miradi hiyo ambacho ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi; Serikali inasemaje?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Jimbo lake ni miongoni mwa Majimbo ambayo yaliahidiwa kupata msaada kutoka Austria. Mpango huo unaendelea lakini kwa kuona kwamba unachelewa, sasa tumeanza utekelezaji kwa kutumia fedha za ndani. Mfano, Ilula sasa hivi tumepata chanzo cha maji kizuri kutoka Mkombozi na mradi umeanza ambao unatekelezwa na Mamlaka yetu ya Maji ya Iringa (IRUWASA) na pale ni kilometa 14, kilometa mbili zinatekelezwa na tutakuongezea shilingi bilioni tano kuhakikisha kwamba sasa maji yanafika mpaka Mji wa Ilula; na mipango mingine yote uliyoomba Mheshimiwa Mbunge tunaifanyia kazi ikiwemo Ruaha Mbuyuni, lakini pamoja na kuchukua maji Mto Mtitu kupeleka kwenye Makao Makuu ya Wilaya pale Kilolo, tunaendelea kuifanyia kazi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali ambalo nimeshawahi kuliuza leo ni mara ya tatu, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nilishawahi kuishauri Serikali kwamba moja ya sababu kubwa ambayo inasababisha timu yetu ya Taifa kutokufanya vizuri ni utitiri wa wachezaji wa kigeni kwenye nchi yetu na tulipoanza kwanza walikuwa wanaruhusiwa wachezaji watatu, baadae wakaongeza wakwa watano, leo ni saba. Sasa tunategemea Taifa Stars itafanya vizuri? Ningeshauri Serikali wapunguze idadi ya wachezaji wa kigeni abaki moja au wawili kwa sababu sisi tuna wachezaji wetu. (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Bunge lilishawahi kutunga sheria ya kutenga fedha kutoka kwenye michezo ya kubahatisha kwenda kusaidia michezo ni kwa nini basi hizo fedha zimekuwa hazipelekwi ili kusaidia michezo maana sasa hivi ni sawasawa unakwenda benki kuchukua fedha wakati hujaweka pesa, usitegemee kama utapata. Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameonesha kwamba sababu mojawapo ya kushindwa kimichezo hasa mchezo wa soka ni utitiri wa wachezaji wa kigeni na kwamba pengine tupunguze idadi.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimtaarifu tu Mheshimiwa Venance kwamba ni kweli wapo wachezaji wa nje takribani 40 katika timu zetu, lakini wachezaji wetu kwenda nje wako 14 tu. Kulingana na concern yake aliyoionesha ni kwamba sasa hivi tuko katika mchakato wa kupitia upya Sera ya Michezo ambapo maoni yanatolewa na wadau wengi na tunalichukulia hili kama ni maoni ya wadau akiwa mdau mmojawapo mzuri sana wa michezo. Kwa hiyo, katika kupitia sera hiyo ambayo iko katika hatua nzuri ambapo tunaiandaa sasa iende katika ngazi za juu zaidi, tutayachukua maoni yote kulingana na suala lake ambalo amelionesha ili tuweze kulifanyia kazi vilevile.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusu kutenga fedha za michezo ya kubahatisha ni kweli kipindi cha nyuma hili suala lilikuwa halifanyiwi kazi japo linatakiwa kisheria, lakini kwa bahati nzuri napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kuanzia mwezi wa saba fedha hizi zimetoka rasmi na zimekwenda BMT na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia sasa BMT itakuwa ikipata fedha za Bahati Nasibu ya Taifa. Lakini sio hivyo tu, tunalifanyia kazi ili kusudi michezo yote ya kubahatisha itoe kiasi cha fedha kwenda BMT ili kusaidia maendeleo ya michezo.
Mheshimiwa Spika, kabla sijamalizia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Venance Mwamoto kwa jinsi alivyokuwa mdau wetu mzuri wa ukweli katika sekta ya michezo kwa jinsi alivyoshiriki, ameshirikiana na BMT kutatua mgogoro wa timu ya Lipuli ambayo sasa baada ya mgogoro huo kutatuliwa inaendelea vizuri na anifikishie salamu zangu kwa Serikali ya Mkoa vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze Waheshimiwa Wabunge ambao wameshiriki katika kuendesha ligi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na yeye Mheshimiwa Venance Mwamoto nawapongeza sana, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wetu, Mheshimiwa Flatei G. Massay, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Silvestry Koka na Waheshimiwa Wabunge wengine na niwaombe tuige mfano huu lakini kuna wengine ambao bado hawajajitokeza kutuambia lakini wanafanya zoezi hili. Nakushukuru sana.(Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watu wa Rufiji na sehemu nyingine ambapo gesi hiyo itapita ni watu ambao wanasubiria kwa hamu jambo hilo. Bado hawajapata elimu ya kutosha kujua umuhimu wa jambo hilo kwenye maeneo yao. Sasa Serikali itakuwa tayari kupita kutoa elimu ya kutosha, hasa mashuleni, ili wananchi kazi hiyo itakapoanza ya kupitisha gesi waone kwamba ile ni rasilimali yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi sasa walio wengi wanategemea gesi ikianza kutoka kwa wingi na tumepewa taarifa kwamba, kuna gesi ambayo inaweza ikatumika kwenye magari. Anatuambiaje Mheshimiwa tujue kwamba unafuu wa kutumia gesi ama petroli kutakuwa kuna tofauti kubwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwamoto kwa kuuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji na Waheshimiwa Wabunge hawa wanafanya kazi nzuri sana kwenye majimbo yao. Ni matarajio yao kwamba wananchi wanawasikia vema.
Mheshimiwa Spika, elimu ambayo tumetoa mpaka sasa, nitoe tu taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji na Mheshimiwa Mwamoto, tumeshatoa elimu katika vijiji vya Mwaseni, vijiji vya Ngarambe, kijiji cha Korongo pamoja na Kotongo, lakini tunakwenda sasa kutoa mwezi wa 10 na wa 11 elimu katika maeneo ya Jaribu Magharibi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, tutaendelea kutoa elimu kwa ajili ya manufaa ya miradi hii ili wananchi wa Rufiji nzima waweze kuipata kwa hiyo, tunaendelea na utaratibu wa elimu kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusiana na gesi kwenye magari, ni kweli kabisa ule mradi wa kutengeneza gesi kwa ajili ya matumizi ya kwenye magari na majumbani ulishaanza tangu mwaka 2016 na hivi sasa mwakani mradi huo utaendelea. Tulishaanza katika Vituo viwili vya DIT pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mpaka sasa magari 16 yameshaunganishwa kwa kutumia gesi badala ya petroli. Na unafuu wake ni kwamba, unapunguza asilimia 40 ya matumizi ya kawaida ya petroli unapotumia gesi.
Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa niaba ya Watanzania wote, utaanza mwaka 2018 hadi 2020 kwa kwenda katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara pamoja na Lindi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa REA III tayari umeanza na vijiji vingi vimepimwa, lakini sasa hivi kuna baadhi ya vijiji ambavyo vilisahaulika na baadaye tukaleta kuomba tena viingizwe.
Sasa Serikali inatuambiaje hasa katika Wilaya ya Kilolo, je, vijiji ambavyo vilisahaulika vitaongezwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema, mradi wa REA una awamu mbili, na lengo lake ni kuvifikia vijiji 7,823. Awamu ya kwanza vijiji 3,559 na awamu ya pili vijiji 4,313. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote vitafikiwa umeme ifikapo mwaka 2020/2021. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ambayo yanatofautiana na swali langu, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimkumbushe kidogo Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Milima ya Uluguru wanakaa Waluguru, Milima ya Usambaa wanakaa Wasambaa wanaotoka Tanga na Milima ya Udzungwa wanakaa Wadzungwa na Udzungwa iko Wilaya ya Kilolo kwa asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu nililopewa hapa, inaonekana kwamba Kilolo wanapewa kama hisani, siyo haki yao. Kwa hiyo, ninachoomba kwa kuwa tayari yalikuwepo makubaliano ya kuhamisha Makao Makuu ya Udzungwa kwenye Kilolo Udekwa, lifanyike ili wananchi wale wanufaike kwamba ile Udzungwa ni ya Wadzungwa siyo ya Waluguru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mara nyingi yamekuwa yakitokea maafa, kwa mfano vijiji vya Msosa, Ikula, Ruaha Mbuyuni, Mahenge na Mtandika wananchi wanauawa na tembo bila kulipwa fidia; na fidia ambayo wanalipwa ni fedha ndogo sana, ni pamoja na uharibufu wa mazao yao.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutunga au kuja kuleta hapa tubadilishe sheria ili wananchi hawa wawe na thamani zaidi ya wanyama ambao ndiyo wanawaua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akifanya katika Jimbo lake. Amekuwa akifuatilia sana na amekuwa akiwatetea sana wananchi wa Jimbo la Kilolo. Kwa kweli hongera sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala la kuhamisha Makao Makuu, tutalishughulikia. Yapo mambo mengi ya kuzingatia tunapotaka kuhamisha makao makuu na jitihada sasa hivi zinafanywa katika kuangalia miundombinu kama itawezekana kwenda kufikika katika hayo maeneo ambayo yalikuwa yamekubalika pale awali. Baada ya hilo kukamilika, basi tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu fidia ya wananchi ambao wanakuwa wameadhirika na wanyamapori hususan tembo na wanyama wengine, hili suala lipo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa tararibu zetu. Ni kweli kabisa taratibu ambazo zipo zinabainisha ni aina gani ya kifuta machozi ambacho kinatolewa kwa wananchi wanaokuwa wameathirika na haya matatizo. Sasa namuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba katika hao wananchi ambao amewasema, hiki kiasi japo ni kidogo, hakilingani na thamani ya binadamu anayekuwa amepotea, lakini bado tutaendelea kutoa kwa wakati, nitaomba tuwasiliane nipate hayo majina ili niweze kuyafanyia kazi mara moja. Hilo nitalishughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimhakikishie kwamba tuko kwenye harakati ya kuweza kupitia upya sera yetu pamoja na sheria ili tuakikishe kwamba tunahuisha na kuweka viwango vile ambavyo vitakuwa vinatosheleza na vinasaidia katika kupunguza haya matatizo. Nashukuru.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ni Wilaya ambayo ina matatizo makubwa sana ya miundombinu na kupelekea usafiri wa magari usiwepo, kwa hiyo, mawasiliano pekee tuliyokuwa tunategemea, ni simu.
Sasa kuna vijiji ambavyo havina kabisa mawasiliano na hivyo kupelekea watu kupata shida na hata kupoteza maisha. Kwa mfano, Masisiwe, Ilambo, Magana, Mdaila, Kising’a, Masege na Uruti, hakuna kabisa. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu unawaambiaje watu wa Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Serikali ilitambua kata zenye uhitaji wa mawasiliano 443.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya kata hizo, tayari tumeshapeleka huduma za mawasiliano kupitia mkataba wa Serikali ya Viatel, ambao ndiyo wanatoa huduma za Halotel.
Pia mtambue kwamba Kata 75 ambazo zina vijiji 154 zinatakiwa ziongezwe kwa ajili ya kufikishia mawasiliano itakapofika Juni, 2018 .
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja kati ya kata hizo na vijiji alivyovitaja, vitakuwemo kwenye mpango wa kupelekewa huduma za simu itakapofika Juni, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Venance Mwamoto, kama ana mashaka niko tayari kwenda naye Jimboni kwake kwa ajili ya kuendelea kuhakikisha kwamba wananchi wa Kilolo ambako bahati nzuri nimeshafika, tena zaidi nilifika kwenye kijiji chake cha Masege, wanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri, kumekuwana kisingizio kikubwa cha sababu ya ucheleweshaji wa fedha kwa kutokukamilika kwa miradi mingi na kupelekea wakandarasi kudai kwamba wanalipwa kidogo kidogo. Kwa mfano, miradi ya maji ambayo iko katika Kijiji cha Ipalamwa, Kitoho, Ilamba na sehemu nyingine. Sasa Serikali inasemaje, nani wa kuchukuliwa hatua, ni Halmashauri husika au Mkandarasi ambaye ameshindwa kumaliza mradi kwa wakati na ubora?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zinapelekwa kulingana na certificate ambayo mkandarasi ameiwasilisha Halmashauri na imefanyiwa tathmini na imewasilishwa Wizara ya Maji ndiyo tunapeleka fedha kulingana na kiwango cha uzalishaji ambacho Mkandarasi amezalisha. Kwa hiyo hapo, Wakurugenzi wanaagizwa kuwasukuma wakandarasi waweze kuzalisha zaidi ili Serikali iweze kutoa fedha zaidi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa kiwango hicho ni kidogo ambacho kinapelekea hata nauli; kwa mfano, hata katika mabasi ya mwendo kasi ukipiga hesabu hayamtoshelezi huyu mfanyakazi; hawaoni sasa wafanyakazi hawatafanya kazi kwa moyo na tija kwa sababu ya mshahara mdogo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna wenzetu wawekeza wa nje hasa Wachina wameingia, wanafanya kazi ambazo Watanzania wanazifanya, tena kwa bei nafuu; sasa Serikali haioni ni wakati wa kuwabana kuhakikisha kwamba zile shughuli zinazoweza kufanywa na Watanzania zifanywe na Watanzania badala ya wawekezaji wanaouza mpaka vocha ambao wameshaingia nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA, NA WENYE ULEMAVU – MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge amehoji juu ya viwango hivyo kwamba ni vidogo na katika jibu langu la msingi nimeeleza vyema ya kwamba, Serikali kila baada ya miaka mitatu kupitia Waziri mwenye dhamana, amekuwa akitoa kitu kinaitwa wage order. Wage order ndiyo mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wage order ya mwaka wa mwisho ilikuwa ni ya mwaka 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hivi tayari Mheshimiwa Waziri ameshaunda Bodi ya watu 17 ambao wanaanza kushughulikia suala hilo la mshahara wa kima cha chini. Bodi hii itafanya uchunguzi kutoka na sekta husika na wataangalia maisha ya leo jinsi yalivyo na gharama zilivyo na baadaye sasa watapendekeza kwa Mheshimiwa Waziri kima kingine cha chini cha mshahara kutokana na sekta.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu zoezi hili ndio linaendelea sasa na Mheshimiwa Waziri ameshakamilisha kazi yake, tunasubiri mapendekezo kutoka kwenye Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Waajiri pamoja na Serikali ili baadaye Mheshimiwa Waziri aweze kutoa amri kwa maana ya order.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukuwe fursa hii kuwasisitiza wenzetu wa Vyama vya Wafanyakazi kuhakikisha kwamba wanasimamia majukumu yao ipasavyo ili waendelee kufanya vikao na waajiri ili katika yale ambayo bado wanaweza wakazungumza na waajiri katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi, basi wafanye hivyo kwa niaba ya wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge aliuliza kwamba wako wafanyakazi wengi sana wa kigeni ambao wanaendelea kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 Bunge hili lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira kwa Wageni na ninyi wenyewe ni mashahidi, Serikali kupitia Wizara ya Kazi, tumekuwa tukisimamia sana sheria hii kuhakikisha kwamba zile kazi zote ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania na ambazo zina ujuzi ndani ya nchi hii ziweze kufanywa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Wizara, tutaendelea kuimarisha kaguzi mbalimbali ili kuwabaini watu wote ambao wanafanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania ambapo kwa namna moja ama nyingine kumekuwa kuna tatizo kubwa sana la udanganyifu kwa maana ya kwamba, watu wakiomba vibali wanadanganya nafasi anayokuwa, lakini baadaye unakuta amechukua nafasi ambazo zinaweza zikafanywa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Serikali tutahakikisha kwamba tunaimarisha ukaguzi ili jambo hili lisiendelee kuwepo na tumekuwa tukichukuwa hatua stahiki pale inapobainika.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa
Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nianze kwanza kwa kuishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha
watu wa Kilolo kwa ujenzi wa hospitali. Pamoja na hiyo, Mheshimiwa Waziri, itachukua muda mrefu hiyo hospitali kuweza kuisha. Lakini tatizo ambalo lipo ni kwamba Wagonjwa inabidi wapelekwe Kituo cha Afya Kidabaga ambacho hakijakamilika, hakina wodi ya watoto, wodi ya wazazi wala upasuaji, lakini inabidi sasa wasafirishwe waende
kwenye hospitali ambayo iko zaidi ya kilometa 120. Tatizo hakuna gari Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hiyo utatusaidiaje ilituweze either kukarabatiwa vizuri kituo cha Kidabaga au tupate gari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu tulifanya ziara pamoja na tukakuta hospitali yao ya Wilaya pale iko taabani. Tukafanya mawazo ya pamoja, na bahati nzuri ndani ya muda mfupi wakapaa shilingi bilioni 1.2. Lakini, kama hiyo haitoshi niwapongeze; kwasababu wameshafanya harakati na ujenzi unaendelea kule site na Mungu akitujaalia ndani ya wiki mbili hizi wakati tuko Bungeni nitakwenda kutembelea ili kuona ni jinsi gani ujenzi unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kituo cha Afya cha Kidabaga nadhani unafahamu kwamba Serikali tutaweza kuweka nguvu kubwa pale kwa sababu tukiangalia jiografia yake ni tata sana, tutaangalia namna ya kufanya. Tutapeleka fedha kwa ajili ya kujenga theatre ikiwezekana na wodi ya wazazi. Lengo kubwa wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma bora.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza nianze kuwapa pole wananchi wa Kilolo ambao wameunguliwa na shule ya wazazi kule Ukumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize swali langu moja, kwa kuwa wananchi wa Kilolo moja ya zao kubwa wanalolitegemea ni misitu, tumehamasisha na inasaidia kutunza mazingira. Pia kwa njia ya misitu wanapata mbao ambazo zimesaidia kwa kiwango kikubwa sana kujenga majengo ambayo yamesababisha ofisi nyingi kuhamia Dodoma haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo lipo sasa ni kwamba wale wananchi wameanza kunyanyasika kusafirisha mbao, watu wa TFS (Wakala wa Misitu) wanawasumbua, TRA wanawasumbua kiasi kwamba wananchi sasa wako tayari kuacha kupasua mbao. Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kwenda kukaa na watu wa TRA kule ili tatizo hili liishe na wananchi wa Kilolo waendelee kufanya biashara zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa zao la misitu ni la muhimu sana na limekuwa likitoa mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi yetu, na wananchi wa Kilolo ni mojawapo ambao wmaekuwa wakijishughulisha sana na hili zao, kwa kweli hongera sana kwa kuhamasisha jinsi wanavyojishughulisha na hili suala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumeweka utaratibu kwamba mwananchi yeyote mwenye misitu ambaye anataka kujishughulisha na hili zao lazima apate kibali kutoka kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) pamoja na TRA ili ahakikishe kwamba anasafirisha kwa kufuata utaratibu. Na niombe tu kusema kwamba niko tayari kwenda kukaa na TRA pamoja na TFS kuhakikisha kwamba utaratibu mzima unafuatwa pale ambapo wananchi wa Kilolo wanataka kusafirisha mbazo zao.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuuliza swali. Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa askari katika baadhi ya sehemu na askari wengi sana kwa maana ya traffic wako barabaran, je, Serikali sasa haioni imefikia wakati wa kuweza kupata kamera au teknolojia nyingine badala ya kutumia askari ambao kwa kweli utendaji wao hauna tija. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mwamoto kwa jambo hilo alilolitoa. Ni kweli kuna uhitaji mkubwa sana wa kuhamia kwenye teknolojia, nchi nyingi zilizoendelea ndio utaratibu unaotumika. Sisi kama Serikali wataalam wanaendelea kufanyia kazi jambo hilo ikiwepo na kufanya upembuzi yakinifu ili kuweza kujua mahitaji pamoja na maeneo ambayo tunaweza tukaanza nayo ili kuweza kupunguza adha inayojitokeza; kwa sababu kwanza tu kukaa kwenye jua kukaa kwenye mvua pamoja na uchache wa askari inasababisha ufanisi kupungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo lake hilo tunalifanyia kazi na nimpongeze sana kwa kuleta hoja hiyo makini, lakini nimpe pole tu kwa yeye ni ndugu yangu kwa yale yaliyotokea Jumamosi, yaliyotokea tarehe moja. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda naomba usikilize vizuri kwa sababu ni kiwanda hicho. Kwa kuwa ligi bora duniani ni Uingereza na ndiyo ligi yenye wachezaji wengi wa kigeni kuliko ligi nyingine lakini timu ya Taifa ya Uingereza ni moja ya timu mbovu ambazo zinashindwa kufanya vizuri kwa kuwa ina wageni wengi. Ligi bora katika Afrika Mashariki ni Tanzania, lakini kwa kuwa inawachezaji wengi wa kigeni timu ya Taifa imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu. Kwa kuwa mwaka 2000 wakati tukiwa hatuna wachezaji wengi wa kigeni timu yetu ilifikia rank ya kimataifa ya 65 na leo tumeongeza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni tumefikia kwenye rank ya 139. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuendelea kuruhusu wachezaji wengi wa kigeni ni kuua timu yetu ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanuni za TTF ziko wazi ili timu ishiriki Ligi Kuu lazima iwe na kiwanja, ikate bima kwa ajili ya wachezaji wake na iwe na timu ya under 20 vyote hivyo vinakiukwa. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siwezi kupingana naye kwamba ongezeko kubwa la wachezaji wa nje linaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya soka ndani ya nchi. Katika jibu langu kwa swali la msingi nimesema kati ya mwaka 2010 mpaka 2015 tulikuwa tunaruhusu wachezaji watano wa nje na baadaye ndipo tumeruhusu wachezaji saba. Ukiangalia wenzetu Kenya wao walianza na saba na sasa hivi wanaruhusu watano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini uzoefu tulioupata katika msimu huu ni kwamba tulikuwa na timu 16 kwenye Ligi Kuu na timu zote kikanuni zinaruhusiwa kusajili wachezaji 30 na kati ya hao saba wanaweza kuwa wanatoka nje. Wadau wanasema kwa kweli hii saba ni ukomo tu na mara nyingi ukomo huo hatuufikii.
Vilevile kwa nchi ambayo tayari imekubali professional football huo wigo wa saba siyo mbaya hata kidogo. Ni kweli timu zote hizo 16 zingesajili wachezaji saba kwa mfano tungekuwa na wachezaji wa kulipwa nchini 112 lakini mwaka huu ni wachezaji 35 tu ambao ni asilimia saba ya wachezaji wote. Kwa sababu timu 16 mara wachezaji 30 kama 480 kwa hiyo ni asilimia saba tu ndiyo ambao waliweza kuajiriwa kutoka nje. Kwa hiyo, ni ukomo tu na usitutie wasiwasi hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, timu zilizofanya vizuri sana katika ligi hii Mheshimiwa Mwamoto unaelewa zilikuwa hazina wachezaji kutoka nje. Chukulia timu ya Kagera Sugar ambayo ilikuwa ya tatu ilikuwa haina mchezaji kutoka nje, chukulia Mtibwa ilikuwa namba tano ilikuwa haina mchezaji yeyote kutoka nje. Vilevile mimi mwenyewe nimehusika katika utoaji zawadi kwa ajili ya wachezaji waliokuwepo kwenye Vodacom Premier League, wachezaji waliofunga magoli kwa kiwango cha juu na kupata zawadi walikuwa ni wawili mmoja kutoka Ruvu Shooting Stars (Abdulrahman) na mwingine kutoka Yanga (Msuva) wote ni Watanzania, hakuna mchezaji wa nje. Kwa hiyo, nimshawishi Mheshimiwa Mwamoto akubali tu kuwa na wigo wa wachezaji saba ila tu tusiongeze wakawa wachezaji kumi na kuendelea huko, lakini hii idadi inatosha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, umeongelea kuhusu timu zinazoshiriki kwenye ligi yetu kuu kwamba zingine nadhani hazina vigezo kwa mfano kuwa na vijana wa under 20 na zingine hazina viwanja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kwamba timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu sharti lao lazima ziwe na timu za vijana chini ya umri wa miaka 18 siyo under 20 actually. Kwa sababu hawa wanaosajiliwa 30 ni umri wa miaka 18 na kuendelea lakini lazima uwe na timu ya vijana ya miaka 18 ambapo tunaruhusu vijana watano kushiriki kwenye Ligi Kuu. Vilevile naomba tu baadaye aniambie ni timu gani ambayo haina kiwanja inachezea barabarani kufanya mazoezi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nia kubwa ya kugawa maeneo ni kusogeza huduma kwa wananchi na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri baada ya sisi wananchi wa Kilolo kupige kelele kutokana na ukubwa wa Wilaya yetu, uliridhia na kutupa Halmashauri ya Mji Mdogo sasa ni muda mrefu na ulifika na kuona kwamba sasa tunastahili kupata Halmashauri kamili. Je, ni lini sasa Mheshimiwa? Hebu tupe jibu ili wananchi wakusikie.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli. Mwaka jana tulikwenda na Mbunge tukafika mpaka jimbo lake, tukatembea. Kijiografia jimbo lile ni kubwa sana, linapakana na ndugu yangu Profesa Jay, linapakana na Waziri wangu Simbachawene huku Kibwakwe, ni jimbo ambalo liko tata kweli kweli. Hata hivyo tulivyofika pale Ilula tumekutana na wananchi wa Ilula ambao mapendekezo yao yametufikia, na bahati nzuri baada ya ile ziara nikatuma timu kwenda kufanya verification.
Mheshimiwa Mwenyekiti, verification imeshafanyika na hivi sasa tuko katika mchakato wa kufanya maamuzi ambapo kwa jambo hili mwenye kufanya maamuzi ni Mheshimiwa Rais mwenyewe mwenye dhamana katika eneo hilo, atakaporidhia basi Mheshimiwa Mwamoto naomba usiwe na hofu, ni kweli Serikali imefanya process zote na sasa tuko katika final stage katika kufanya maamuzi. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Pamoja na Serikali kufanya jitihada kubwa katika kuhimiza ujenzi wa Vituo vya Afya, kumetokea tatizo kubwa sasa hivi ambalo linakabili vituo ambavyo vimekwisha; ni upungufu wa watoa dawa za usingizi. Kwa hiyo, nataka nijue tu, kwa kuwa Vituo vya Afya vingi vitajengwa katika nchi yetu, Serikali
imejipangaje?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mwamoto kwa swali lake zuri. Ni kweli tunategemea mpaka mwisho wa mwezi Desemba, takriban Vituo vya Afya 100 vitaweza kufanya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni. Kwa hiyo, tayari tumeshaongea na Chuo Kikuu cha KCMC kwa ajili ya kuendelea kutoa kozi mahususi za wataalam wa usingizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muda huu pia, wale ambao wako tayari katika maeneo ya kazi, tumeandaa mpango wa kuweza kupewa mafunzo ya haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tahadhari, wataalam wangu wanasema tusifanye mafunzo ya haraka, matokeo yake badala ya kuwaokoa akinamama wajawazito tukawaua. Kwa hiyo, tuna-negotiate muda wa mafunzo haya uwe angalau miezi 9 au 12. Wataalam wamekataa muda usiwe chini ya miezi sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo suala tunalifanyia kazi na naamini Mheshimiwa Waziri wa Utumishi yuko hapa, kwa hiyo, pia atatusaidia katika kuajiri wataalam hawa wa usingizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji katika Wilaya ya Kilolo hasa sehemu za Ilula Mheshimiwa Waziri analifahamu na ameahidi mara nyingi kufika pale, sasa hivi mradi umeanza kwa sababu ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Je, atuambie leo ni lini atakwenda pale kuona ule mradi ambao ni ahadi ya Mheshimiwa Rais unaendelea vizuri na unakwisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba nimepanga ziara ya mikoa 15 baada ya Bunge hili la Bajeti ikiwemo Iringa. Nitafika pamoja na kwenda kuangalia Mto Lukosi una maji mengi sana mwaka mzima ili tuone ni jinsi gani tutashusha maji pale Ilula, lakini pia huo mradi nitakwenda kuukagua Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa naomba niulize swali moja. Kwa kuwa, miradi ya maji imekuwa ikisumbua sehemu nyingi hata Wilaya ya Kilolo imekuwa haiishi vizuri na kwa kuwa kuna watu wanaitwa Wakandarasi Washauri wamekuwa wakilipwa pesa kwa ajiili ya kushauri miradi yetu ili iende vizuri pale inapokuwa imeharibika wanachukuliwa hatua gani hawa Wakandarasi Washauri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba huyu Mkandarasi Mshauri au Consultant kwenye usajili wake akipata kazi yoyote ya Serikali kuna kitu kinaitwa Design Liability Insurance. Insurance hiyo inalinda performance ya kazi yake na kama hakufanya vizuri kupitia kwenye ile insurance au kupitia kwenye ile bond basi anatakiwa arudishe hela kama mradi haukufanyika vizuri. Kwa hiyo, kama haujafanyika vizuri kwenye eneo lake naomba sana Mheshimiwa Mbunge awasiliane na TAMISEMI au na Wizara ya Maji ili tuweze kumwajibisha huyo Mhandisi Mshauri. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara inayounganisha Mkoa wa Iringa na Morogoro ni moja tu inapitia Kitonga; na kwa kuwa hoja hii nilishawahi kuileta kwamba siku itakapotokea barabara ya Kitonga imefunga kwenda Zambia na Afrika ya Kusini itabidi watu wazunguke Dodoma. Kwa kuwa wananchi wa Kilolo wa Kata ya Muhanga, Masisiwe, Idete, Itonya, Kimala wameanza kwa makusudi kabisa kupasua barabara ambayo Serikali ilishaahidi kuunganisha Mkoa wa Morogoro na kutokea kwa Mheshimiwa Susan Kiwanga, wamefanya jitihada kubwa, je, Mheshimiwa Waziri atakubali kuitembelea na kutuunga mkono ili wananchi waweze kupata nguvu na kuimalizia barabara hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, nilivyofika katika Halmashauri na Jimbo la Kilolo, Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kilolo walizungumzia concern ya barabara hiyo. Kwa sababu jukumu letu kama Serikali ni kubwa ni kutoa huduma kwa wananchi, nami nilieleza wazi kwamba ni jukumu la Serikali kushughulikia barabara hii. Kwa sababu barabara hii itadondokea kwa wenzetu wa TANROARD, lakini ni Serikali yetu yote kwa ujumla, tutaangalia nini cha kufanya kwa ajili ya kuipa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia siku ile wananchi walisema endapo barabara ile ikijifunga watashindwa kusafiri lakini hatuwezi kutoa ahadi ya moja kwa moja hapa. Niseme Serikali tumelichukua kwa ujumla wake na kuliweka miongoni mwa mipango mikakati ili siku za usoni barabara ile ikiwezekana tuiboreshe kwa huduma pana ya wananchi wa Tanzania lakini hata nchi jirani.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa linauliza habari ya ahadi za viongozi. Mheshimiwa Rais aliahidi pale Ilula, Kilolo kwamba suala la maji litakuwa ni historia. Nataka nijue Mheshimiwa Waziri ni lini mkataba ule utasainiwa ili wananchi wa Kilolo, Ilula tatizo la maji liwe historia kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu ujenzi wa mfumo wa maji Kilolo. Tulikuwa tunatarajia kwamba fedha ambazo zingetumika ilikuwa ni fedha kutoka Austria, lakini baada ya kuona kwamba fedha za Austria zinachelewa Serikali kwa kutumia makusanyo ya ndani imefanya mchakato imekamilisha na tarehe 30 Aprili, Jumatatu ijayo tunakwenda kutia saini mkataba ili sasa utekelezaji uanze wananchi wa Kilolo wapate maji. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ukiangalia majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba waliokopeshwa kwa kutumia hatimiliki za kimila takribani ni shilingi bilioni 59, lakini ukiangalia idadi ya wanaomiliki hati hizo miliki za kijiji wako wengi, sasa hii inaonesha kwamba kuna tatizo katika wakopeshaji.
Sasa je, Waziri atakubali kulifuatilia jambo hili ili kuhakikisha kwamba wale wanyonge ambao hasa ndiyo wanalengwa kwa sasa wanapata mikopo bila usumbufu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Sheria Namba Nne na Namba Tano ya mwaka 1999 ya Ardhi ya Vijiji iko wazi na inatakiwa marekebisho kwa sababu wanaokwenda kutoa haki inapotokea matatizo ya ardhi vijijini ni mabaraza ya kata. Lakini kwa kuwa kuna tatizo pale.
Je, Waziri atakuwa tayari kukutana na Waziri wa TAMISEMI na yeye Waziri wa Ardhi ili kurekebisha kwa sababu haki haitendeki kama ambavyo inatakikana?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema imeonekana ni wazi kwamba wahitaji wa mikopo ni wengi, lakini wanaokopeshwa ni wachache. Hapa kuna mambo mawili kuna either watu kuogopa kwenda kuchukua mikopo au benki kutokubali zile hatimiliki za kimila.
Napenda nimthibitishie tu kwa sababu elimu inayotolewa wanapopewa zile hati za haki miliki za kimila wanaambiwa zina sifa sawa sawa na hati zingine na ndiyo maana benki 11 zimeweza kutoa hizo shilingi bilioni tisa na ninawapongeza sana watu wa Mbozi ambao ndiyo wanaongoza kwa kutoa mikopo kwa kutumia hati miliki za kimila. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili ambalo amelizungumzia naomba tu niseme kwamba kweli tunayo changamoto hiyo na hasa ya uelewa, kwa maana katika maeneo mengi tunahitaji kuwa na watu ambao ni waajiriwa wanaoweza kufanya kazi hiyo ya kusimamia Mabaraza ya Ardhi. Sasa kama hilo linaonekana ni tatizo nadhani bado tunaweza tukaliangalia. Ni kweli kuna shida na maeneo mengi Mabaraza ya Ardhi ya Kata hayafanyi kazi yake vizuri pengine kutokana uelewa mdogo au kutokuwa na manpower ya kutosha, kwa hiyo, hili tunalichukua tutalifanyia kazi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa natambua uwepo wa Simba hapa ndani, lakini pia niwaombe watoe tofauti zao na zetu ili waweze kuwaombea Yanga waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linasema hivi, kwa kuwa kuna skimu kubwa ya umwagiliaji kule Mahenge, Mgambilenga, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea mradi ule kwa sababu ni muda mrefu sasa haujafanyiwa kazi kwa sababu fedha nyingi zilikuwa zinatoka nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari na nadhani katika ziara nitakayokwenda Mufindi nitapita katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Kata Ruaha Mbuyuni iko Kilolo - Iringa, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahi kupita pale na kutoa ahadi, lakini baadaye Waziri husika alifika mwaka 2017 tarehe 28 Desemba akatoa ahadi kwamba Halmashauri ifanye designing na ipeleke mradi ule Wizarani ili yeye atoe kibali cha kutangaza. Sasa hivi imeshachukua muda mrefu na wananchi wanaendelea kusubiri.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri naye anasemaje ili wananchi wa Ruaha Mbuyuni waweze kupata uhakika kwamba sasa watapata maji safi na salama ili kipindupindu ambacho kimekuwa kikiwaua kwa muda mrefu kiache kuwaua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua maji ni huduma muhimu sana kwa wananchi na kwa kuwa hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, sisi tunatambua kabisa ahadi ni deni. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo tutaietekeleza ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi salama na yenye kutosheleza.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo anazifanya. Kwa kuwa wananchi wa Kilolo bado hawajaanza kupata athari yoyote ya minara hii sasa naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu nimekuwa nikiulizia swali la kupata mawasiliano ambayo hayapo kabisa katika vijiji vya Imalutwa, Mazombe, Isele, Kising’a, Mahenge, Maganailindi na Ilambo. Je, Serikali sasa safari hii itakuwa tayari hasa Mheshimiwa Waziri na ulitoa ahadi kwamba utafika ili wananchi hawa waweze kupata mawasiliano ili waendane na sera ya viwanda kwenye nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Venance kwa jinsi anavyofuatilia sana suala la wananchi wake kupata mawasiliano katika shughuli zao, kwa kweli amefuatilia sana na katika awamu hii ambapo tumetenga kata 173 za kupelekewa mawasiliano kuna Kata zake nafikiri tatu ambazo tayari tumeshazitengea kwenda kupata mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi tu kwamba hizo kata nyingine ambazo hazijapatiwa mwisho wa mwezi huu kuna kata nyingine 205 ambazo tunategemea zitaingizwa kwenye mpango wa kupelekewa mawasiliano ya simu. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kilolo kuna barabara ambayo inaunganisha na Mkoa wa Morogoro, swali hili nimeshaliuliza zaidi ya mara tatu na ahadi ya Serikali ilikuwepo. Hivi leo ninavyozungumza wananchi wa Kimala, Itonya, Muhanga, Idete na Idunda wanafanya kazi kwa mikono, na mimi kama Mbunge nimechangia na wananchi wengine wamechangia.
Je, sasa Serikali itakuwa tayari na yenyewe kuchangia ili wale wananchi wa Kilolo kwa nguvu zao waweze kupasua barabara kuelekea Morogoro ambako naunganishwa na Jimbo la Mheshimiwa Susan Kiwanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZU NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa kuunganisha Mikoa. Kwa Mkoa wa Iringa tunao mpango wa kuunganisha eneo hili la Kilolo kuja Mkoa wa Morogoro kupitia Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimpongeze tu Mheshimiwa Mwamoto kwa sababu amekuwa mfuatiliaji mzuri na mwenyewe anafahamu hii barabara kutoka Iringa kuja Kilolo na sehemu ambayo ilikuwa inasumbua kwa maana ule mpango wa Halmashauri kufanya marekebisho ya maana alignment ya ile barabara; tumetoa maelekezo ili waweze kurekebisha ili wananchi ambao walikuwa wamepata usumbufu tatizo lao litakuwa limeondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hii eneo hili tunalolizungumza ni kilomita chache sana, lakini kwa sababu ya nature ya eneo tunalifanyia kazi ili tuweze kukuunganisha na eneo la Mlimba.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Naibu Waziri pamoja na Waziri husika kwa kazi nzuri ambayo mnafanya ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika baadhi ya vijiji kikiwemo Kijiji cha Kihesa Mgagao na umeme tayari umeshafika. Naomba awaondoe wasiwasi wananchi wa sehemu umeme umefika hasa vitongoji kwamba umeme watapata au hawatapata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kata za Ukwega, Kising’a, Nyanzwa, Udekwa na Winome hawajapata umeme haujapimwa kabisa. Naomba niulize ni lini wataenda kupimiwa ili nao wawe na uhakika wa kuingia kwenye nchi mpya ya viwanda?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kweli mradi wa REA III unaendelea vizuri na umeshaanza katika mikoa yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwamoto, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mwamoto anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake la Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilifika katika Jimbo la Mheshimiwa Mwamoto na kijiji cha Nghuruwe pamoja na Kihesa Mgagao kulikuwa na changamoto kubwa sana. Kijiji cha Nghuruwe kilishapata umeme na sasa wanaendelea kupeleka umeme katika Kijiji cha Kihesa Mgagao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kabla ya mwezi huu kuisha vitongoji vyote vya Kijiji cha Kihesa Mgagao vitakuwa vimeshawashwa umeme. Kadhalika bado vitongoji vyake saba katika maeneo ya karibu na Kihesa Mgagao, navyo tutavitembelea wiki ijayo namhakikishia kwamba na vyenyewe vitapata umeme kabla ya mwisho wa mwezi ujao. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya kufikisha maji pale Ilula kwa ahadi za Mheshimiwa Rais naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nia na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtua ndoo mama kichwani, na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo eneo kubwa ni eneo ambalo lina miundombinu mibaya kwa maana barabara hazipitiki. Sasa, je, Serikali itakuwa radhi kuweza kutoa fedha ambazo tumeshaleta maandiko katika Vijiji ambavyo vinapata shida vya Idete, Ndengisivili, Kihesa Mgagao na Winome? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa chanzo kikubwa cha maji kiko pale Ilula ambapo Serikali imetoa zaidi ya bilioni tano na sasa hivi mradi unaendelea; je, Serikali itakuwa tayari sasa kuhakikisha yale maji yanafika Mlafu, Ikokoto, Image na Wambingeto? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mwamoto kwa jinsi ambavyo analitetea Jimbo lake na jinsi ambavyo anafuatilia miradi ya maji katika Jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza Idete; Mheshimiwa Mwamoto yeye mwenyewe ni shahidi, Mheshimiwa Rais wetu tarehe 10 Mei, alielekeza sasa muundo mpya wa utekelezaji wa miradi ya maji. Nimwombe tu, kwamba asiwahishe shughuli leo saa sita mchana tutatoa press release na Mheshimiwa Jafo kuhusiana na utekelezaji wa miradi kuanzia sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika utekelezaji huo tutahakikisha vijiji vyote alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, ikiwemo Idete na vinginevyo tunahakikisha vinapata maji kwa sababu kazi yetu ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo tuliwaahidi wananchi na wananchi wakaamini Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Ilula Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ni mashahidi tayari Serikali imetoa bilioni tano, mkataba umeshasainiwa, utekelezaji unaendelea vizuri na maeneo mengine yaliyo jirani na Ilula ikiwemo Image na Image nilienda mwenyewe nikaelekeza lazima bomba lifike Image na maeneo mengine yote ya jirani ili yaweze kunufaika na huu mradi wa Ilula. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utatuzi wa migogoro katika sekta ya michezo bado ni changamoto kubwa sana; je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuanzisha chombo ambacho kitakuwa chini ya BMT ili kuweza kusaidia kutatua migogoro badala ya kuacha watu wanaenda mpaka FIFA kwenda kufuata haki zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza suala la uimarishaji na ujenzi wa viwanda na michezo ni moja ya kiwanda kikubwa; je, Serikali sasa itakuwa tayari kuandaa kongamano la Waheshimiwa Wabunge wanamichezo na wadau ili kujitathmini tulikotoka, tulipo na tunakokwenda?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mpaka sasa sijaona kama utaratibu tuliouweka chini ya Baraza la Michezo Tanzania na chini ya Mashirikisho yanayohusika ya michezo kwamba umeshindikana kiasi cha kuunda chombo kingine kipya. Sisi kama Wizara tuko tayari kupokea maoni kutoka kwa wanamichezo kama Mheshimiwa Mwamoto, tuweze kuelewa umuhimu wa kuunda chombo kipya sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu kuandaa kongamano, namwomba Mheshimiwa Mwamoto, yeye mwenyewe anaweza kuanzisha hilo, na sisi tutamuunga mkono kwa sababu suala la kongamano ni kujadiliana tuweze kusonga mbele katika michezo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Najua nia ya Serikali ya kuanzisha vyuo hivi ni pamoja na kukuza utalii na kuingiza pato la letu la ndani na nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tembo wametoka kwenye Hifadhi ya Udzungwa National Park wameshambulia katika Vijiji vya Mailindi, Maghana kwenye Kata ya Mahenge, wananchi wako kwenye hali mbaya na jambo hili limekuwa likijitokeza kila mwaka. Naomba tu Mheshimiwa Waziri aende akaone hali jinsi ilivyo lakini pia ahakikishe kwamba kituo kidogo cha askari wa wanyamapori kinafunguliwa pale. Tatizo hili ni la kila mwaka, namwomba sana Mheshimiwa Waziri.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Balozi Venance Mwamboto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwamoto, amekuwa akifuatilia sana hili suala na tumekuwa tukizungumza ni hatua gani ambazo tunaweza kuzichukua. Naomba nimhakikishie kwamba nitakuwa tayari kwenda kuangalia hali halisi katika Kata hiyo ya Mahenge ili kuona ni hatua gani zichukuliwe na Serikali. Moja ya hatua ambazo tunategema kuzichukua ni pamoja na kujenga out post katika lile eneo ili wasaidiane na wananchi na Halmashauri ile katika kudhibiti hao tembo ambao wamekuwa wakizagaa katika maeneo mbalimbali.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nashukuru kwa kutupa matumaini kwamba kuna siku mshahara utapanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niulize swali dogo kwamba watakapokuwa wanapandisha mishahara, je, watakuwa tayari kuzingatia watu wenye ulemavu hasa wa macho ambao wenyewe huhitaji msaidizi? Wanapolipwa mshahara sawa na wengine wao wanakuwa wanapata mshahara kidogo kwa sababu hauwatoshi. Je, Serikali itakuwa tayari kuwapa motisha au kuwapa kitu cha ziada ili iwasaidie? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa mtetezi na mpigania haki wa watu wenye ulemavu. Katika hili, kwa sababu mshahara na stahiki na haki za wafanyakazi zinaongozwa kwa mujibu wa sheria, niseme tu kwamba kwa hivi sasa sheria ambayo imewekwa ndiyo utaratibu wake utaendelea kufuatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama unavyofahamu pia kuna Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ambayo inalinda haki zao na kwa namna moja ama nyingine pia kumekuwepo na incentives mbalimbali za kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata haki kama watu wengine. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inajali watu wenye ulemavu lakini katika hili la mishahara kwa mujibu wa sheria; sheria yetu inatuongoza katika utaratibu ambao umewekwa hivi sasa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais mwezi Mei alifika Iringa katika Wilaya ya Kilolo na akatoa ahadi kwamba barabara ile ya kutoka Ipogolo - Kilolo ambayo inaitwa sasa barabara ya Mfugale ianze kujengwa mara moja. Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa ili ahadi ile ya Rais aliyotoa kwa wananchi iweze kutimia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwamoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa sababu tumezungumza sana juu ya barabara hii hata kabla ya ahadi ya Mheshimiwa Rais. Kwa vile Mheshimiwa Rais ametoa ahadi kuitengeneza barabara hii, tulikubaliana kwamba baada ya Bunge hili nitatembelea huko ili tuweze kuweka msisitizo kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi natambua kwamba barabara hii ilishasanifiwa. Kwa hiyo, harakati za ujenzi wa barabara hii, napenda wananchi wa Kilolo wajue ujenzi ulishaanza kwa sababu hatua za awali tumeshaanza, sasa ni zoezi la kupata fedha ili barabara ijengwe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwamoto asiwe na wasiwasi barabara hii itajengwa na kwa msisitizo wa Mheshimiwa Rais tutakwenda kuijenga barabara hii. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alifika Kilolo, tena Kijiji cha Kihesa Mgagao, Kata ya Ng’uruwe, na kuwaahidi vizuri wananchi wa Kilolo kuhusu umeme; na kwa kuwa sasa baadhi ya vijana wameshatenga maeneo kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo. Je, ni nani haswa anayepaswa kusogeza umeme kwenye maeneo ambayo vijana tayari wameshatengewa maeneo, ni gharama za nani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukushukuru sana kwa namna ambavyo umetambua mahitaji ya nishati na kuwapa fursa Waheshimiwa Wabunge kuuliza maswali mengi. Umenipa fursa ya kujibu maswali ya Mheshimiwa Njeza, Mheshimiwa Mwamoto pamoja na Mheshimiwa Frank.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Njeza na Mheshimiwa Mwamoto maswali yao yanalingana kwa sababu yamehusisha masuala ya umeme vijijini. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Njeza, tulifanya ziara Mbeya, pamoja na kwamba Jimbo lake ni Mbeya Vijijini, hapa amezisemea kata ambazo zipo ndani ya Jiji la Mbeya, na kama nilivyosema, Serikali imetambua ukuaji wa maeneo katika Miji, Manispaa na Majiji na ndiyo maana tumekuja na mradi huu unaoitwa Peri-Urban. Niliombe Bunge lako tukufu, tutakapowasilisha bajeti yetu ya mwaka 2018/2019 ituunge mkono katika miradi mbalimbali ukiwemo Mradi huu wa Peri- Urban kuupitisha kwa kishindo kisha tufanye kazi ya kupeleka umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, Mheshimiwa Mwamoto, ni kweli tulifanya ziara tena kwa mara ya kwanza Mawaziri wawili, Mheshimiwa Waziri mwenyewe na mimi Naibu Waziri tulikuwa kwenye kata hiyo aliyoitaja. Nataka niseme sisi lengo letu ni kupeleka nishati kwenye maeneo yenye uhitaji ikiwemo mojawapo ya maeneo ambayo kweli yanahitaji nishati ni eneo la viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwapongeze Mheshimiwa Mbunge na vijana hao kwa kutenga eneo la viwanda vidogo vidogo na kwa gharama za Serikali umeme utafika katika maeneo hayo na nitoe rai tu wao waendelee kujipanga kuunganisha lakini umeme utafika kama ambavyo tumeahidi katika ule mkutano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la mwisho la Mheshimiwa Frank, ni kweli Mji wa Tunduma ni mji ambao umekuwa na upo mpakani. Nataka niseme Mji wa Tunduma upo katika Mkoa mpya wa Songwe na wakati huo umeme katika Mkoa wa Songwe ulikuwa unatoka katika njia ya kusafirisha umeme ni ndefu kutoka Mbeya. Serikali ina mpango wa kujenga sub-station palepale Tunduma kwa ajili ya kuufanya Mkoa mzima wa Songwe upate nishati ya uhakika na wakati wote. Kwa hiyo, nimthibitishe Mjumbe kwa kuwa yeye Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Kamati yetu ya Nishati na yeye pia atuunge mkono katika bajeti yetu ili mradi huu wa ujenzi wa sub-station pamoja na line ambayo inatoka Mbeya inayoenda Sumbawanga - Mpanda – Kigoma - Nyakanazi ya KV 400 ambayo yote kwa pamoja itachangia kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika. Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Kakunda, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, atakuwa tayari kufika katika Wilaya ya Same ili kwenda kuona hali ambayo ipo sasa hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo inajenga hospitali kubwa na nzuri, je, ni kiasi gani cha wahudumu au Madaktari wanaweza kuwatengea kwa msimu huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mwamoto na Mheshimiwa Dkt. Mathayo huko aliko kwamba nitafika Same baada tu ya Bunge la bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwamoto kwa kufanya ufuatiliaji wa kina na wa karibu, katika kipindi cha miezi minne au mitano ameweza kufanikiwa na Serikali imepeleka pale zaidi ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya kujenga hiyo hospitali ya wilaya na Mheshimiwa Rais juzi ameweka jiwe la msingi. Nimhakikishie tu kwamba tutashirikiana na wenzetu wa utumishi kuhakikisha hospitali ile inapata watumishi wa afya kwa mujibu wa kitange na uwezo wa Serikali.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali moja tu dogo la nyongeza. Kwa kuwa tunazungumza habari za stahiki za Maaskari Wilaya ya Kilolo toka imeanzishwa sasa hivi takribani miaka 17 Askari wamekuwa wakiahidiwa kuwa na Ofisi ya Wilaya ya Kilolo na nyumba za Maaskari, mpaka leo ni kila mwaka tumekuwa tukiahidiwa. Sasa nataka nijue kutokuwa na nyumba na Ofisi si wanakosa stahiki zao la halali?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Venance Mwamoto kwa jina la utani mzee wa vinungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba siyo Jeshi la Polisi pekeyake tuna tatizo la ofisi pamoja na makazi kwa Askari. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba tunaendelea kutenga fedha ili kupunguza kama siyo kumaliza kabisa suala la makazi na ofisi kwa ajili ya Jeshi la Polisi. Nitumie fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akitupatia fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za Askari na mpaka sasa kuna nyumba za Askari ambazo zinaendelea kujengwa kwenye mikoa mbalimbali. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Venance Mwamoto na baada ya Bunge hili nilimwahidi nitakwenda Kilolo kwa ajili ya kujionea hali ilivyo. Ahsante
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa Mkakati wa East African Community ni kuhakikisha wanaondoa umaskini si kwa Kagera tu bali na mikoa mingine. Tatizo kubwa la Mkoa wa Kagera pamoja na kuwa na viwanda vingi ni barabara zao kutopitika kwa muda mrefu na kusababisha viwanda vyao visifikiwe kwa wakati na kusafirisha mali nje. Je, Serikali ina mkakati gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna baadhi ya mikoa ambayo pia imekuwa ina tatizo ambalo linafanana ikiwepo Mkoa wa Iringa tuna uwanja wa ndege, pamoja na kuwa kuna mazao mengi ambayo yanatoka na yanafika nchi za Afrika Mashariki lakini Serikali imekuwa ikisuasua katika ujenzi wa uwanja ule.

Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba ule uwanja wa ndege unamalizika ili tupate na watalii wa kutosha waweze kwenda Ruaha National Park kwenye Jimbo la Ismani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambako maswali ya Mheshimiwa Mwamoto yamelenga, naomba kuyajibu maswali yake mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba hapo katikati kulikuwa na changamoto ya barabara, baadhi ya barabara kwa kweli zimekuwa na hali mbaya lakini Serikali imekwishapeleka fedha na kuna tangazo la kutafuta wakandarasi kwa ajili ya kurekebisha barabara za Bukoba na maeneo mengine mbalimbali ya nchi yetu ili ziweze kupitika kupeleka mazao sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, tumekwisha tangaza tenda na kuna mkandarasi ambaye yuko tayari kwenye Uwanja wa Ndege wa Iringa, tunasubiri taratibu za mwisho za kuwalipa ili waweze kufanya ukarabati unaostahili. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na TASAF, naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Mpango mzima wa TASAF, moja ya kazi kubwa ni kuzisaidia kaya maskini angalau zipate mlo. Hata hivyo, kuna watu ambao walisahaulika hasa wenye ulemavu, sehemu nyingi walikuwa wameachwa. Je, katika huo Mpango ujao, Serikali itakuwa tayari kuzingatia watu wenye ulemavu wote wakiwepo wa Kilolo na sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la kaka yangu Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika kutambua kaya maskini, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba tunazingatia vitu vingi wakiwemo na walemavu wenye watoto na wasio na watoto; wazee wenye watoto na wasio na watoto wakiwemo hata na watoto wenyewe ambao pia wote hao tunawapa category ya kwamba ni kaya maskini sana. Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kaka yangu wa Jimbo la Kilolo kwamba walemavu wako katika kundi ambalo tunasema ni kundi la kaya maskini na wenyewe wataangaliwa na kuhudumiwa. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kuhusu viwanja, pamoja na kwamba hata viwanja vitakavyofanyika michezo ya AFCON naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa jana tumehakikishiwa kwamba timu yetu itakayoshiriki michezo ya AFCON itashinda nataka kujua tu wamefanya maandalizi gani, watuambie maandalizi yaliyofanyika ili tuwe na uhakika kwamba timu yetu sasa tunaenda kubakiza kombe hapa Tanzania?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyonyeza la Mheshimiwa Mwamoto kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana, lakini vilevile naomba nirejee kauli ya Waziri Mkuu ya jana, kwamba tumejipanga vizuri. Timu yetu ya Taifa ya Vijana Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) iko kambini kwa wiki tatu sasa na kazi yetu kubwa sasa hivi ni kuipambanisha na timu mbalimbali za wakubwa wao hasa wa chini ya umri wa miaka 20, kuweza kuwaimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kulikuwa na mechi kubwa sana na timu nzuri katika Afrika Mashariki Azam FC under 20 na matokeo yake ni kwamba Serengeti Boys imewachapa kaka zao magoli matano kwa bila. Tukumbuke vilevile kwamba Azam FC ina baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho timu ya Serengeti inakwenda Arusha angalau kuji-acclimatize (kujizoesha) na hali ya Arusha na kuweza kupambana na timu mbalimbali kabla ya kwenda Uturuki kwa mwaliko wa UEFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tujivunie ubora wa timu yetu, kwamba imeweza kutambuliwa kama moja ya timu bora katika Afrika kuitwa kwenye mashindano ambayo yanaunganisha timu nne za Afrika na timu nne za Ulaya. Tunakwenda kule na mechi yetu ya kwanza itakuwa tarehe 4 mwezi wa tatu dhidi ya Guinea; na baadaye tutacheza na Australia na kumalizia na timu yka Uturuki. Sasa hivi naongea na wenzetu wa TBC tuweze kupata live coverage kutoka huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashindano hayo yataisha tarehe 11 Machi na timu hiyo haitarudi Tanzania, tunaitafutia pesa lazima iende Spain ikafanye mazoezi na mashindano kidogo na wenzao na baadaye iende Cameroon ikashindane na baadhi ya timu kule ndipo itarejea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, wiki ya kwanza mwezi wa Aprili tumekaribishwa na Rwanda kujipima nguvu na timu nne bora za Afrika ambazo ni Cameroon, Rwanda na Uganda. Baada ya hapo inarejea nchini kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya Nigeria ambayo nina uhakika tutaishangaza Afrika katika matokeo yake. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambazo zinafanywa na Serikali, kundi la watu wenye ulemavu limeongezeka na ni walemavu wa tofauti. Je, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakubali kukutana na makundi hayo ili iwe rahisi kuwasaidia kwa sababu wana changamoto zinazotofautiana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, Balozi wa Watu Wenye Ulemavu, lakini pia babu yangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mwamoto, hajaanza leo kuhakikisha kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanakaa sawa, toka akiwa DC anafanya hivyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nimefanya ziara nyingi hapa Tanzania kwenye mikoa mingi na katika zile ziara zangu, ni lazima nikutane na makundi ya watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, niko tayari kwa hilo ambalo amelizungumza.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri na kazi nzuri ambayo Wizara ya Nishati na Madini inafanya, sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulianza toka mwaka 1998, mpaka leo ni takribani miaka 20. Namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri, kama atakuwa tayari sasa kuambatana na Mheshimiwa Profesa Norman King Sigalla ili kwenda kujionea mwenyewe hali inayoendelea ili wananchi wa Makete ambako kumekuwa na matatizo mengi kule yanatokea na barabara hawana, waweze kuwa na imani na Serikali yao.

Swali la pili linalohusu umeme; kwa kuwa kilio na hamu ya Watanzania ni kuona umeme unapita kila sehemu: Je,
sasa, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kutoa ushauri kwamba sehemu ambako kuna miradi mikubwa na hakuna umeme, umeme uweze kupelekwa; kikiwepo Kijiji cha Iyai, ambako Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika, Kijiji cha Kising’a, Winome, Nyanzwa, Ilindi, Msosa, Kitimbo na Ikula? Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha hizo ambazo ilitoa ahadi yenyewe umeme unafika ili wananchi wale waweze kupata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ya Mheshimiwa Mwamoto ameuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Profesa Norman, kwamba ni lini nitakuwa tayari kutembelea Jimbo la Makete? Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba tulifanya ziara Jimbo la Makete mwaka 2018 mwezi Desemba. Katika mambo mbalimbali ambayo nilishuhudia ni uwepo wa uhitaji wa umeme, lakini uwepo wa vyanzo vingi vya kuzalisha umeme hususan vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Serikali kupitia agizo la Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwamba sasa mchakato wa ujenzi wa bwawa la Lumakali uanze na kwa hatua za awali tumepata mfadhili ambaye ni World Bank ambaye ana-support hatua hizi za kurudia tena upembuzi yakinifu kwa sababu ulichukua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kama jibu langu la msingi lilivyosema, kwamba mradi huu utaanza kama ilivyokusudiwa, mapema mwezi Januari, 2021, kwa sababu Serikali ina dhamira ya dhati ya kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia chanzo hiki cha maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ameyataja maeneo. Ni kweli tumefanya ziara katika Jimbo la Kilolo zaidi ya mara tatu. Mwezi Machi, 2018, mwezi Novemba, 2018 na hivi karibuni tulikuwa na Kamati ya Bunge katika Jimbo lake katika maeneo ya Dinganayo, Ikuvala, lakini maeneo hayo pia tumewasha umeme na wiki hii tutawasha umeme katika maeneo ya Ngelango, Itungi na Mlavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameeleza jambo la msingi, kwamba kwa kuwa Serikali tulitoa maelekezo, maeneo yote ambako miradi hii ya umeme vijijini yanaunganishiwa, taasisi za Umma na hasa maeneo ya viwanda yapewe kipaumbele. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, mara baada tu ya kujibu swali hili, naomba tukutane naye, tuelekee ofisini tuone namna ya kufuatilia na kwa kuwa amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa miradi ya nishati vijijini na hasa hili eneo la viwanda ambalo amelitaja, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha, eneo hilo litakuwa limepatiwa umeme ili wananchi wale wapate ajira na pia Serikali ipate mapato kupitia vile viwanda. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba anijibu swali langu la nyongeza. Mheshimiwa Waziri alifika katika Kata ya Ruaha Mbuyuni na akaona jinsi matatizo ya maji yanavyosumbua. Wananchi wamekuwa wakipata kipindupindu kila mwaka na yeye aliahidi mambo makubwa. Sasa je, ni lini wananchi wa Ruaha Mbuyuni ambao wanategemea kupata kituo cha afya watapata maji pale?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Mbunge wa Kilolo, Mzee wangu, kwa kazi kubwa sana anayoifanya, lakini tulipata nafasi ya kufika Ruaha Mbuyuni. Changamoto kubwa tuliyoiona kwa Wahandisi wetu walitengeneza tenki la maji lakini hawakuwa na chanzo cha maji. Kwa hiyo tuliwaagiza watu wa rasilimali za maji wa bonde lile waende na wameshafanya tafiti kikubwa tunawaagiza watu wa DDCA waende kuchimba kisima haraka katika kuhakikisha mradi ule unafanya kazi kwa wakati.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mhehimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa tatizo hili sasa ni kubwa na linafahamika kwa muda mrefu hususani Mkoa wa Iringa.

Je, Waziri atakuwa tayari kuja Iringa kuona hali ambayo inaendelea kwa sababu hali ni mbaya hiyo elimu ambayo ilitakiwa itolewe haitolewi kwa muda na watu wanazidi kuathirika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa shule nyingi wanakunywa uji, je, sasa haoni ni wakati muafaka sasa wa kuchanganya chakula lishe kwenye uji wao ili iwe rahisi zaidi watoto wote wakapata kwa sababu ndio wanaoathirika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza kwa kuwa ni mdau wa masuala ya lishe, lakini nipongeze vilevile Bunge lako Tukufu kwa sababu wana Chama cha Waheshimiwa Wabunge ambao wanasimamia masuala ya lishe ambacho kinaongozwa na Mheshimiwa Dunstan Kitandula, yote hii inaonesha kwamba na nyinyi kama Bunge mnalisimamia suala hili kikamilifu.

Pia kwa njia ya kipekee vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuzindua mpango mkakati wa masuala ya lishe nchini na kutoa maagizo kwa Wakuu wote wa Mikoa na kuwapa malengo ambayo ya kusimamia katika masuala haya ya lishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niko tayari muda wowote kwenda Iringa kwenda kuwahamasisha masuala ya lishe katika mkoa huu. Vilevile ninachotaka kukisema ni kwamba hali ya udumavu tunaiona katika mikoa inazalisha chakula kwa wingi Rukwa, Katavi pamoja na Iringa ni mikoa ambayo kwa kiasi kikubwa sana inazalisha chakula kwa wingi, lakini kuna udumavu mkubwa sana kuliko mikoa mingine ambayo haizalishi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, yote hii inaonesha kwamba elimu ya lishe bado ni changamoto kubwa sana na hili sisi kama Wizara tuko tayari kwenda kule kushirikiana na timu zetu za mikoa kuhakikisha kwamba tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii sasa hivi kama Taifa tunaona hali ya udumavu inazidi kupungua, lakini tumeanza kuona vilevile lishe iliyopitiliza imeanza kuongezeka, asilimia 10 ya Watanzania wana lishe ambayo imepitiliza, maana yake ni nini? Ni kwamba wote hapa wengi hatuzingatii misingi ya lishe, tunakula bora chakula kuliko chakula kilicho bora.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yake mazuri, yeye mwenyewe anajua kwamba minara ya Waheshimiwa Wabunge wengi haifanyi kazi ikiwemo mnara wa kwangu Kilolo na ameahidi mara nyingi kufika kuhakikisha kwamba minara inafanya kazi. Sasa je, atakuwa tayari kwenda kabla ya Bunge hili, kufika Kilolo na kuhakikisha kwamba mnara ule unafanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niwe mkweli, Mheshimiwa Mwamoto amekuwa akifika mara nyingi sana ofisini kufuatilia masuala ya minara kwenye jimbo lake. Ni kweli pia kuna minara kama mitatu, minne hivi ambayo haipeleki mawasiliano vizuri sehemu kubwa, nadhani ni kwa sababu ya watumiaji wengi sana, kwa hiyo, inakuwa na uhafifu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapeleka timu ya wataalam waende wakaiongezee nguvu minara kwenye maeneo yake ili iweze kuwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimuulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, katika historia ya Wahehe, moja ya sifa ni kumpiga Mjerumani na Mjerumani alipigwa katika Kijiji cha Lugalo Iringa na ikasababisha kiongozi wao Zelewisky kupigwa na kaburi lake liko pale. Je, Serikali sasa haioni kwamba kile kilikuwa ni kivutio kizuri tosha mpaka sasa hivi kimetelekezwa kwa miaka yote na Waziri yuko tayari kufika pale?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Venance Mwamoto, kamwene bwana!

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kufika katika eneo hili na wakati wowote muda ukipatikana tunaweza tukachomoka na Mheshimiwa Mwamoto tukaenda kuona eneo hili, lakini kwa ujumla wake tu maeneo yote ya malikale na maeneo ya makumbusho kwa kweli tumeyafanyia mkakati mzuri sana wa kuyaboresha kwa sababu Idara ya Malikale ambayo iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa ina uwezo mdogo sana wa kuyasimamia maeneo haya kifedha, kwa hivyo ilikuwa inayaendeleza kidogo kidogo. Kwa kuzingatia umuhimu wa maeneo haya, kihistoria lakini pia kama urithi kwa nchi yetu ambao unapaswa kudumu kwa vizazi na vizazi, tumeamua kuyakabidhi baadhi ya maeneo nyeti ikiwemo eneo la Kalenga na eneo la Isimila kwa taasisi za uhifadhi ambazo zina msuli mkubwa kidogo kifedha kwa mfano TANAPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano eneo la Kalenga na eneo la Isimila na vivutio vyote vilivyoko Mkoa wa Iringa vya Malikale tumewakabidhi Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili waweze kuviendeleza na kuvisimamia.

Kwa hivyo tumegawa maeneo haya kutokana na shirika lipi ambalo lina msuli mkubwa kifedha, liko jirani na maeneo haya. Kwa hivyo, maeneo mengi kwa kweli kwa sasa yataendelezwa yatakuwa na hadhi ya kisasa na yatatoa huduma nzuri zaidi kwa watalii wa ndani na wa nje.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Wilaya ya Kilolo inapitiwa na barabara kuu (High Way) kutoka Tanzania kwenda Zambia, lakini pia ni barabara ambayo ukitoka Mikumi ni mpakani na Ruaha Mbuyuni mpaka ukifika Ilula ni kilometa zaidi ya 200, lakini hapo hakuna kituo cha afya. Mara nyingi accidents zimekuwa zikitokea, wananchi wa Mbeya, Malawi, Zambia, wamekuwa wakipata matatizo na wamepoteza maisha kwa sababu, inabidi waende wakatibiwe Iringa Mjini ambako ni mbali; na kwa kuwa, wananchi sasa wa Ruaha Mbuyuni wameonesha nia ya kujenga Kituo cha Afya, je, Serikali itakuwa tayari kuwasaidia kwa haraka ili kuokoa maisha ya watu ambao wamekuwa wakiyapoteza pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwa swali mojawapo la nyongeza hapa, hivi leo asubuhi kwamba, ni nia ya Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja yatazingatiwa katika kuboresha. Kama wananchi wamechukua juhudi za kuanza ujenzi tunawapongeza sana, sisi kama Serikali tuko pamoja nao na mimi hivi karibuni nitaenda kutembelea Jimbo la Mheshimiwa Mwamoto. Hivyo nitaomba tutembelee eneo hili tuone juhudi za wananchi ili tuweze kutia nguvu katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Mji wa Ruaha Mbuyuni baada ya kuonekana kuna shida kubwa sana ya maji na kipindupindu kinatokea kila mara na akaahidi pale kwamba kichimbwe kisima kwa tahadhari ili wananchi waanze kupata maji. Lakini kwa masikitiko makubwa wale wataalam wamepuuzwa hakuna aliyefika pale. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakubali tena kwenda kuona hali ilivyo na wananchi wanazidi kuteseka?

Swali la pili, kwa kuwa Serikali kuna wahisani ambao huwa wanansaidia Serikali, kuna tatizo kubwa katika Kijiji cha Udekwa na Mlafu, tayari Serikali ya Italy, kupitia Shirika linaitwa WAMAKI liko tayari kusaidia, lakini linataka commitment ya Serikali, yenyewe litasaidia kiasi gani, ili na wao waweze kusaidia fedha. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kusaidia ili WAMAKI waweze kutoa maji safi na salama kwa kata mbili.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kabisa nilifika Kilolo na nimeona kazi nzuri ambayo inafanywa na Mheshimiwa Mbunge Venance Mwamoto katika Jimbo lake. Lakini kikubwa tulifika kweli Ruaha Mbuyuni na tukaona changamoto ile na tukatoa agizo, watu wa Bonde walikwenda walishafanya tafiti ya upatikanaji wa maji. Labda nimuagize sasa Mhandisi wa Mkoa, ahakikishe kabisa kile kisima kinachimbwa ili wananchi wale waweze kupata maji na anipatie taarifa.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu suala lake la pili, pamoja Serikali imekuwa ikitatua tatizo la maji, imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tupo tayari kukaa nao, tuangalie ni namna gani tunaweza tukashirikiana katika kuhakikisha tunatatua changamoto hii. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) umefanikiwa kwa kiwango kikubwa na umenufaisha nchi na sisi Wabunge tukiwa wamojawapo. Je, Serikali itakuwa sasa tayari kutoa takwimu ni Wilaya, Mkoa na Kijiji gani mpango huu umefanyika vizuri ili iwe mfano kwa Wilaya au Mikoa mingine ambayo imeshindwa kufanya vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Mwamoto, kama ifauatvyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango mzima huu wa TASAF, takwimu zipo na muda wowote anapozihitaji tutampatia kwa sababu ni zoezi endelevu. Sisi kama TASAF tumejipanga kuonyesha kwamba sasa hivi tutakuwa tunaonyesha zaidi multiply effect ya walengwa wote na mpango mzima mpaka leo hii tumetumia shilingi ngapi ili kuonyesha kwamba impact yake inaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nimweze kuuliza swali la nyongeza, tulipata Kilolo Kata ya Dabaga, Nangage, na Boma la Ng’ombe tulipata mradi kupitia mradi kupitia EU ya kilometa 18 wa lami na moja ya sharti ilikuwa ni lazima wananchi wakubali kutengenezewa barabara bila fidia, wananchi waliitikia na kubomoa wenyewe nyumba zao na baadhi ya miundombinu. Sasa tulikuwa tunaomba kwakuwa mradi huo ulikuwa haujaanza Serikali itakuwa tayari sasa kuwaondoa wasiwasi wale wananchi wale ambao wamekosa kabisa amani itakuwa tayari kusema lini au mradi huo ukoje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza niseme tu barabara hii inasimamiwa na wenzetu upande wa TARURA lakini nafahamu pia hatua nzuri ambayo imefikiwa. Labda kubwa tu nimpongeze tu Mheshimiwa Mwamoto kwa kuwaamasisha wananchi kwa ridhaa yao wenyewe najua na wewe umewaamasisha sana na niwapongeze kwa kweli kwa kukubali kwamba wanaona faida ya hii barabara ya ambayo itapita maeneo pamoja na kwamba barabara ni ya kwao na maendeleo ya wananchi wenyewe. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Mwamoto kwa kazi nzuri uliyoifanya nafikiri ni jambo la kuingwa na maeneo mengine tukipata wananchi kwa ridhaa yao kupisha mradi inatuarakishia kwenda kufanya maendele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie wananchi hawa ambao wamepisha barabara hii muhimu tu kwamba ipo tu kwenye hatua ya ujenzi na mkandarasi ameshapatikana kwa taarifa nilizokuwa nazo na inafadhiliwa na hii barabara na wenzetu wa EU kwa hiyo wavute subira kwamba barabara hii kwa vile mkandarasi amepatikana itaenda kujengwa kwa haraka na huduma itakuwepo katika maeneo haya ya kilolo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa barabara ambayo inatoa Makao ya Wilaya kwenda Utegi inasumbua kwa muda mrefu na kwa muda mrefu imekuwa ni ahadi ambayo bado haijafanyiwa kazi. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kuiangalia wakati inasubiri hiyo ahadi ya Rais ya muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi za Rais ziko nchi nzima na Wilaya ya Kilolo pia tulikuwa na ahadi kama hiyo ambapo Rais alikuwa amesema barabara ya kutoka Kilolo - Iringa ingeanza kujengwa mara moja. Sasa tayari tunaelekea kwenye uchaguzi na ilikuwa ahadi ya kabla ya uchaguzi. Je, Serikali inasemaje ili wananchi wa Kilolo wajue umuhimu wa Serikali ya Awamu ya Tano? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme Serikali inatekeleza maagizo na ahadi zote za Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia itaendelea kutekeleza maagizo yote ya Viongozi wetu Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Utegi itajengwa kutokana na upatikanaji wa fedha ndiyo maana usanifu umeendelea. Kwa hiyo, tukishamaliza usanifu, tukapata fedha itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini barabara yako Mheshimiwa kama ambavyo tumeshaongea hata nje ya hapa kwamba barabara ile tayari imeingizwa kwenye Mpango wa Benki ya Dunia. Ni taratibu zinaendelea baadaye itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Jimbo la Kilolo na Wilaya ya Kilolo ni kubwa sana na Mheshimiwa Waziri anajua; na kwa kuwa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Kilolo ambayo ni Ilula ilianzishwa muda mrefu, zaidi ya miaka mitano, kwa kigezo kwamba ili kupunguza ukubwa wa wilaya na jimbo ili kuwafikia wananchi. Je, sasa haoni ni wakati muafaka sasa wa kuipa hadhi ya kuwa halmashauri kamili kwa sababu vigezo vyote vilivyotajwa hapa vimekamilika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ina ukubwa na sifa zote zinazokubalika; na kwa kuwa vikao vingi vimeshakaliwa, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kufika Wilaya ya Kilolo na kujionea mwenyewe jinsi mambo yalivyo tayari kwa kugawa kutupa halmashauri kamili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya kaka yangu, Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la Mji wa Ilula nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, ziara yetu ya kwanza ambayo nilifanya mimi na yeye ambayo impact yake ndiyo maana Kilolo leo hii imepatikana hospitali ya wilaya ya kisasa. Licha ya ziara ile, jambo lingine kubwa tulitembelea eneo la Ilula na maeneo mbalimbali na ni kweli; Halmashauri ya Kilolo ni kubwa sana maana inapatikana mpaka huku na Kibakwe, ukiangalia jiografia yake ni kubwa sana. Kwa hadhi ya eneo lile, hasa Ilula, inapaswa kuwa halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, maelekezo ya Serikali ya hivi sasa kwamba status quo inabakia kwamba mpaka pale Serikali ijipange kwa sababu maeneo yote sasa hivi yamesimamishwa kupandishwa hadhi, lakini japo kuwa hadhi inastahili lakini kwanza kipindi cha sasa itasubiri kwanza mpaka hizi halmashauri ambazo zimeshapandishwa tuweze kuziwekea infrastructure za kutosha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo jambo hilo naomba nimwambie kwamba lipo katika pending issue pale ambapo sasa tukipewa go ahead na utaratibu utakapokwenda vizuri tutalifanyia kazi wala Mheshimiwa Venance Mwamoto asihofu.

Mheshimiwa Spika, ajenda ya ukubwa wa halmashauri yake kama nilivyosema awali mimi na yeye tumeshatembea sana mpaka katika yale madaraja yaliyokuwa hayapitiki. Nimhakikishie kwamba tumefanya kazi kubwa, Mheshimiwa Venance Mwamoto asihofu, pale muda utakaporuhusu jambo hilo Serikali italiangalia kwa jicho la karibu sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi. Swali hili nauliza kwa mara ya tatu leo, kwa kuwa Milima ya Kitonga, Ruaha Mbuyuni mpaka Mikumi Iyovi, Malolo, kituo wanachotegemea cha Polisi ni kimoja cha Ruaha Mbuyuni, lakini hawana gari la Polisi na hivi juzi nimetoa pikipiki mbili kwenye kile kituo. Sasa je, Serikali haini ni wakati muafaka wa kuniunga mkono kwa sababu, accident inapotokea wanapata shida kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kuchangia pikipiki kwa askari wetu, lakini na mimi namjibu tena kwa mara nyingine kwamba, pale ambapo magari yatafika tutaangalia uwezekano wa kuweza kupeleka pale kwa sababu, sasahivi tunavyozungumza hatuna magari ambayo yamepatikana kwa hiyo, avute subira Mheshimiwa Mbunge.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya watu wenye ulemavu naomba niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na uhakiki wa simu, uhakiki wa passports zetu na shughuli za kibenki. Na kuna walemavu wengi ambao hawana vidole, na wanatumia vidole ili kuhakiki; je, Serikali imeweka mpango gani madhubuti wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimeipokea changamoto hii na ninaomba tufanye kazi kwa pamoja Wizara yetu ya Fedha, hasa kwenye taasisi zetu za kifedha na mabenki yetu na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ili tuone jambo hili tunalishughulikia kwa haraka na ndugu zetu hawa waweze kupata huduma hii.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba Magereza mengi nchini zina mlundikano mkubwa wa wafungwa lakini wapo wafungwa ambao wamefungwa kwa ajili ya kesi ndogo ndogo kwa mfano wizi wa kuku, kugombana na waume zao na kadhalika na wamefungwa kwa sababu ya kukosa hela ya faini. Je, kwa kuwa faini hizo ni ndogo, Serikali haioni sasa kuna haja ya wafungwa hao kuwatoa na kufanya shughuli za kijamii nje ya jamii ili waweze kufidia fedha hizo ambazo Serikali inapoteza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie pia kwamba utaratibu huo upo tuna idara maalum chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo inashughulika na wanasema huduma za jamii moja kati ya jukumu lake ni kuhakikisha kwamba inazingatia aina ya wafungwa wenye sifa kama ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja ili kuweza kuwapatia kazi zingine za kufanya nje, pamoja na utaratibu mwingine ambao nimeuzungumza wakati najibu swali la msingi la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utaratibu huo tunao.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa kuwa swali limekuwa likijirudia kila mara na majibu ambayo yanatofautiana, sasa niombe, tu kwa kuwa umbali huo ni mrefu na gari hakuna, Serikali itakuwa tayari sasa kutoa gari na kuongeza mafuta kwa ajili ya kwenda Kilolo na kurudi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tutakuwa tayari kupeleka gari Kilolo pale ambapo fedha zitakapopatikana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa kazi nzuri ambayo anafanya kusambaza baadhi ya mashine kwenye Hospitali mbalimbali za Rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa kuwa wagonjwa wa ugonjwa wa Kisukari umeongezeka kwa kasi na kwa kuwa mashine za kusafirishia figo ziko sehemu chache ikiwepo Dar es Salaam, KCMC na Dodoma na wagonjwa wanapata shida sana kwenda kusubiria kusafisha figo, je Serikali sasa haioni imefikia wakati muafaka wa kuhakikisha kila Hospitali ya Rufaa kunakuwa na mashine hizo za kusafishia figo? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Kaka yangu Venance Mwamoto kwa swali zuri, Mbunge wa Kilolo, ni kweli kuna ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hasa wagonjwa wa Kisukari, wagonjwa wa Moyo, Saratani na kuhusu sasa tuweke huduma za dialysis za kusafisha damu katika Hospitali za Rufaa za Mkoa nakubaliana naye na habari njema tunategemea kupata mashine zaidi ya sitini kutoka Saudi Arabia, ambazo tutaziweka katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo nakabaliana nayo sasa kama Waziri ni upatikanaji wa wataalamu ambao wanatakiwa kutoa huduma hiyo, lakini tunaongea na Serikali ya Saudi Arabia ikiwezekana tuwe na mpango wa haraka wa kupeleka wataalamu katika Hospitali zao na Hospitali nyingine kwa mfano KCMC, Muhimbili, JKCI na Bugando ili tuweze kuongeza ujuzi. Mashine tutaweka, naomba niseme siyo kuanza na Hospitali zote, tutaangalia kwa mfano Katavi, hatutegemei mtu atoke Katavi mpaka Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaangalia maeneo ambayo hayafikiki Katavi, Ruvuma, Rukwa, Lindi kwa hiyo, tumebainisha kama Hospitali tano za kuanza nazo. Labda nitoe angalizo tusisubiri mpaka muda wa kwenda kupata huduma za dialysis, yapo mambo ambayo tunaweza kufanya kama wananchi kama Watanzania, ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kufanya mazoezi mara kwa mara kuangalia ulaji wa vyakula vyetu, lakini pia kupunguza matumizi ya tumbaku na sigara itatuepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba unisikilize vizuri.

Kwa kuwa ni-declare interest kwamba niliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya kwa hiyo najua matatizo ya Mabaraza ya Kata. Mara nyingi wanaolalamika ni wale ambao hawana uwezo, ndiyo wanadhulumiwa ardhi na mashamba yao, wanaowadhulumu ni watu wenye uwezo na kwa sababu Halmashauri hazina uwezo wa kifedha wanaotoa gharama ya kuendeshea kesi hizo mahakama hiyo ni wale waliolalamikiwa wenye fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri haki itapatikana? Mimi nafikiri naomba unijibu. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, haki inapaswa kupatikana hata kama hauna pesa, maelekezo ni kwamba zile bei ni kweli wanakubaliana, kwanza bahati nzuri viwango vya kutoza ni viwango ambavyo kwenye ngazi ya Kata ya Diwani na Ward DC yake wanaweza ku-moderate, Halmashauri zinaweza kusimamia, Mkuu wa Wilaya anaweza kuingilia, Mkuu wa Mkoa anaweza kuingilia, kwa hiyo, kuna flexibility kubwa sana ambayo unaweza ukaangalia hapo, lakini mahali pengine ilipotokea tumetoa maelekezo isitokee mtu ambaye hana uwezo asitendewe haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanapanga viwango vya kawaida na maeneo mengine tumetoa maelekezo unakuta kwamba kwa mfano hata hukumu imetoka, lakini ile gharama ya kwenda kuchapisha ni kubwa anatozwa mwenye kesi, ikikosa anapeleka mtu mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nitoe maelekezo ni kwamba hili jambo ni jambo muhimu, jambo la kisheria na lililenga kimsingi kusaidia watu wa ngazi ya chini au maskini ndiyo Mabaraza ya Kata lililenga naomba viongozi wetu wakiwemo na Waheshimiwa Wabunge tuwasiliane, kama kuna mahali Mheshimiwa Mwamoto kuna mwananchi amedhulumiwa au hakusikilizwa kwa sababu hana fedha nipo tayari twende sasa hivi tukamsikilize na apate haki yake, ahsante.