Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Timotheo Paul Mnzava (7 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naishukuru Serikali kwa kazi waliyoifanya. Pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa barabara hii kwa mara ya kwanza kabisa iliwekwa kwenye Ilani mwaka 2010 na mwaka 2015 na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii Serikali haioni iko haja sasa ya kutenga fedha zaidi na kuongeza kasi ya utekelezaji ili tujenge barabara hii isivukwe na muda wa Ilani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Korogwe Vijijini wamekuwa wakisubiri utengenezaji wa barabara hii kwa hamu na kwa muda mrefu, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuongozana nami kwenda Korogwe akaone hali ya barabara hii na kutoa neno la matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Timotheo, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Timotheo kwa sababu amekuwa anafuatilia sana mambo mbalimbali kuhusu eneo lake, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwa ufupi nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kama ilivyo kawaida kwamba Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho ya barabara katika eneo lake. Kwa hiyo, nimuahidi tu tutaendelea kutenga fedha kadri tunavyopata bajeti ili tuendelee kuboresha barabara katika eneo hili. Niliwahi kutembelea katika eneo hili lakini nakubalia nitakuja kwa sababu zipo changamoto nyingi ili nije kuona pia na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kazi kubwa inayofanywa na TARURA inapunguzwa faida au kufifishwa faida yake kutokana na ukosefu wa fedha za kujenga madaraja muhimu. Wananchi wa Korogwe wamekuwa wakipata shida ya muda mrefu ya Madaraja yao ya Mbagai, Makondeko na Mswaha. Serikali haioni kwamba iko haja ya kuweka jicho maalum kwenye bajeti inayokuja kwa ajili ya madaraja kwenye barabara ambazo zinatengenezwa na TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, ni Mbunge mpya lakini anafanya kazi kubwa sana ya kutetea wananchi wake wa Korogwe. Jambo la pili ni kwamba huu mpango mkakati ni wa kudumu na ndiyo maana imeanzishwa TARURA ili wataalam wetu hawa wakilala, wakiamka wafikirie barabara zetu za vijijini na mijini. Kwa hiyo, naomba tu aamini kwamba kazi hii inaendelea kufanyika vizuri na huu ni mwaka wa bajeti na bajeti ya barabara hizi inabidi ianzie katika vikao vyao vya ndani kuanzia kwenye mtaa, kijiji, halmashauri yao na hatimaye hapa Bungeni. Sisi kama Serikali tupo tayari kushirikiana na wananchi wa Korogwe na Mheshimiwa Mbunge wao ili kuhakikisha kazi hii inafanyika vizuri na kuondoa kero zilizopo pale.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ilivyo Igalula kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini hususan kwenye Kata za Kizara, Makumba, Kalalani, Mkalamo, Elewa na Lutindi na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu changamoto hizi. Ni lini Serikali itatoa utatuzi wa changamoto hizi zinazowakabili watu wa Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba nilishatembelea Korogwe Vijijini na hilo eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge nililiona, ni kweli kwamba kuna mnara wa mawasiliano lakini hauna nguvu ya kutosha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatuma wataalam kwanza wakaongeze nguvu kwenye hicho kijiji cha kwanza alichokitaja halafu na nitatoa orodha nyingine kesho aangalie vijiji vingine ambavyo tumeviorodhesha kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano maeneo hayo.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kwenye hili na anazungumza eneo ambalo analifahamu. Pamoja na majibu yake mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza mradi huu ulibuniwa muda mrefu sana na ni mradi ambao una uwezo wa kuhudumia eneo kwa maana hekta karibu zaidi ya hekta 5000 na tathmini ambayo unasema ilifanyika ya usanifu uliofanyika ulifanyika muda mrefu.

Je, Serikali iko tayari sasa kuharakisha mapitio ya usanifu upya ili kujua gharama halisi kwa mazingira tuliyokuwanayo sasa na kwa namna ya kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili tunayo Skimu ya Songea na Makalala kule Magoma, lakini pia skimu ya Kwamkumbo pale Mombo ambapo wananchi wamekuwa wakiathirika wakati mvua maji yakiwa mengi yanaenda kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na kusababisha hasara kubwa.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari, kuwatuma wataalam wa umwagiliaji waende kwenye maeneo haya na kuona namna ya kutatua changamoto hizi za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kufahamu Serikali kuharakisha mchakato wa kuweza kupitia upya tathmini ya mradii huu. Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tangu siku zile nilivyofika mimi katika bonde hili na kufika bwawa lile tayari tushawaelekeza viongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro wanalifanyia tathmini upya bwawa lile ili kujua gharama halisi na kuanza utekelezaji kwa mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu athari ya mafuriko katika skimu hizi tatu alizozitaja za Skimu ya Songea na Makalala, kwamba nitumie nafasi hii kwanza kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro kwenda haraka katika mabwawa haya kufanya tathmini na kuona namna gani tunaweza kujenga miundombinu ile yamatuta kwa ajili ya kukinga mafuriko ya athari ya mabwawa haya.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni miongoni mwa halmashauri ambazo zilielekezwa kuhamisha Makao yake Makuu ya halmashauri kutoka Mjini kwenda kwenye maeneo yake ya utawala, lakini kuna changamoto kubwa sana ya barabara haswa kwa wananchi wa Tarafa ya Bungu barabara ya kutoka Makuyuni Kwemshai na barabara ya Makuyuni, Zege Mpakayi.

Je, Serikali iko tayari sasa kuwa na mkakati maalum wa kusaidia uboreshaji wa miundimbinu ili wananchi hawa waweze kufika kiurahisi kwenye maeneo ya Makao ya halmashauri mpya zilizoanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa kwanza nimpongeze kwa namna anavyohangaika na barabara za eneo lake na nimshukuru alinipa ushirikiano wa hali ya juu nilivyotembelea maeneo haya na maeneo mengine ambayo hakuyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu labda ni kwa kutoa kumbukumbu sahihi kwa mvua ambazo ambazo ziliathiri Mkoa wa Tanga zilikuwa ni kubwa sana kiasi kwamba urejeshaji wa maeneo ambao tumeyafanya hadi sasa tumetumia bilioni 7.8 kurejesha eneo la Tanga peke yake kwa mvua za mwezi Octoba peke yake na nikubaliane na yeye kwamba sasa tumefanya tena kwenye uratibu huu wa mvua zilizonyesha kuanzia Octoba kuja Januari kwa upande wa Tanga pia kumbukumbu kwamba kuna mahitaji makubwa ikiwepo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetambua maeneo yote yenye shida hizi ikiwepo maeneo uliyoyataja na tunafanya utaratibu wa kuwa na fedha tena kama tulivyofanya Awamu ya I ya mvua za mwezi Octoba tutakwenda kufanya kazi kubwa kufanya marejesho ya maeneo haya ambayo nayataja kwa sababu nafahamu eneo la kwako pia ndiyo limekumbwa na maporomoko ya udongo wananchi wamepata athari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunatambua hivyo na tutakuja kufanya uharaka wa kurejesha maeneo hayo uliyoyataja,ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza, niruhusu niendelee kuwapa pole wananchi wa Jimbo langu la Korogwe Vijijini na Mkoa mzima wa Tanga kwa mafuriko makubwa yaliyotupata siku chache zilizopita. Tunaendelea kutumaini juhudi ya Serikali kurejesha miundombinu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; moja ya sababu ya nchi tunazoshindana nazo kwenye soko la mazao ya viungo na mazao ya bustani kufanya vizuri ni wao kuwa na mamlaka za kusimamia mazao haya. Je, ni lini Serikali yetu itaona umuhimu wa kuanzisha Mamlaka ya Kusimamia Mazao ya Viungo na Mazao ya Biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe, ni wakulima wakubwa na wazuri sana wa mazao ya viungo na zao la chai, lakini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya bei kwenye zao la chai. Je, ni upi mkakati mahususi wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanaboresha bei ya zao la chai ili kuweza kuwaletea tija wananchi na wakulima wa zao la chai nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Wizara ya Kilimo inafahamu umuhimu wa kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia mazao ya horticulture na mazao ya viungo. Hivi sasa tunapitia mfumo na muundo wa Wizara kupunguza idadi ya bodi na kuanzisha mamlaka chache ambazo hazitazidi tatu, mojawapo ikiwa ni Mamlaka ya Maendeleo ya Mazao ya Horticulture.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu akijaalia hivi karibuni Bunge hili litapokea sheria ambayo itaonesha mabadiliko ya muundo wa taasisi mbalimbali ndani ya Wizara ya Kilimo ili kuipa sekta hii nafasi inayostahili kwa sababu ni subsector ndogo katika Sekta ya Kilimo inayokua kwa kiwango kikubwa sana na inahitaji attention inayostahili. Kwa hiyo nimtoe hofu kwamba tuko katika hatua za awali na kabla ya kufika Bunge lijalo la Bajeti tutakuwa tumeshaanzisha Mamlaka ya Mazao ya Horticulture.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la chai; ni kweli kama Serikali hatua tunazochukua mojawapo sasa hivi tuko katika hatua za mwisho za kuanzisha a primary market katika eneo la Dar es Salaam ili tuwe na mnada wa kwetu hapa Tanzania. Tumesha-earmark eneo na sasa hivi tuko katika hatua za awali kutengeneza utaratibu ili chai yetu badala ya kwenda kuuziwa katika soko la Mombasa sasa ianze kuuziwa katika soko la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutatumia mfumo wa TMX ili kuwaruhusu wanunuzi duniani waweze ku-bid. Mchakato huu unawahusisha Sekta Binafsi ambao wamewekeza katika chai ili kuhakikisha kwamba zao la chai linapata soko na bei ya uhakika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tunaamini kwamba ndani ya muda mfupi tutaanzisha soko la kwetu ndani ya Tanzania na chai yetu itauziwa hapa na itapunguza gharama na kumpatia mkulima bei nzuri.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni Wilaya ya Korogwe zimeathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya maji na kusababisha shida ya upatikanaji wa maji.

Je, Mheshimiwa Waziri anasema ni upi mkakati maalum na wa dharura wa Serikali kurekebisha miundombinu hii na kurudisha miundombinu hii na kurudisha huduma ya maji kwa wananchi wa Korogwe Vijijini kama wanavyofanya wenzenu kwenye upande wa barabara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tukutane leo saa 7.00 ili tujue namna ya kuweza kuwasaidia wananchi wa Korogwe.