Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita (19 total)

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara yake Wilayani Ngorongoro mwaka jana aliahidi nyongeza ya kilometa 50 kwenye ujenzi wa barabara unaoendelea. Je, ahadi hii itatekelezwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 imeainisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 65 kutoka Sanya Juu hadi Longido; ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi waliopo Mkoa wa Arusha, ninatambua juhudi nyingi wanazozifanya ili kuhakikisha miundombinu ya barabara katika mkoa inaimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Olenasha kwa sababu amefuatilia barabara hii ya Loliondo – Mto wa Mbu, na mimi niseme tu kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea Loliondo na aliahidi ujenzi wa barabara ya nyongeza kwa kilometa 50, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalishughulikia na tunaangalia kadri itakavyowezekana katika bajeti hii inayokuja nyongeza ya hii barabara tutaendelea kujenga. Kwa sababu barabara hii inayo urefu wa kilometa 218 kwa hiyo karibu asilimia 25 sasa barabara hii inajengwa, sasa tukiendelea kuongeza tutapata asilimia 50 na hatimaye barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara hii ya Sanya Juu hadi Longido imetamkwa katika Ilai ya Uchaguzi, na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kwamba tunaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tuna kipindi cha miaka mitano nah ii barabara tutaitazama katika bajeti zinzaokuja ili tuhakikishe ahadi za Chama cha Mapinduzi na tuna kipindi cha miaka mitano nah ii barabara tutaitazama katika bajeti zinazokuja ili tuhakikishe ahadi za Chama cha Mapinduzi zinatekelezwa kikamilifu. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kabla ya yote nipende kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutupatia mradi huu mkubwa wa kutuletea maji safi na salama kwa ajili ya binadamu na mifugo toka Mlima Kilimanjaro Mto Simba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa wananchi wa hizi Kata tatu zilizolengwa na mradi huu wana shauku kubwa ya kupata maji haya ikizingatiwa kwamba Wilaya hii ni kame, Je, mradi huu unategemewa kukamilika lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kufahamu uhaba wa maji katika Wilaya ya Longido Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji alipotembelea Longido mwaka jana aliwaahidi wananchi wa Kijiji cha Wosiwosi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Natron lenye maji yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu pamoja na wananchi wa Kata ya Tingatinga katika Kijiji cha Tingatinga kwamba atawapatia mabwawa ya maji; je, ahadi hii ataitimiza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee anavyowatetea wananchi wake wa Longido. Kubwa tu itambulike kutokana na changamoto kubwa sana kwa Mji ule wa Longido katika suala zima la maji, Wizara yetu ikaona haja ya kuwapatia wananchi wale maji safi na salama na ya kuwatosheleza, lakini anataka kujua ni lini mradi ule unakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ule unakamilika mwishoni mwa mwezi Mei. Mimi kama Naibu Waziri nilipata nafasi ya kufika pale katika kuhakikisha tunausukuma mradi ule ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nilipofika katika ule utekelezaji wa mradi nimemkuta Mkandarasi amelala, nilimtikisa kwa mujibu wa mkataba ili mwisho wa siku wananchi wake wapate maji. Nataka nimhakikishie tutashirikiana ili wananchi wake waweze kupata maji safi na salama kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ahadi ya Mheshimiwa Waziri ya mabwawa, nataka nimhakikishie ahadi ni deni. Sisi kama Wizara ya Maji kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameahidi tutatekeleza kwa wakati katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na naomba niulize swali dogo la nyongeza kuhusiana na mada hii iliyoko mezani.Kwa kuwa Wilaya ya Longido haina chuo hata kimoja, chuo chochote cha Serikali; na kwa kuwa Wilaya hii ya Longido ni ya wafugaji kwa karibu asilimia 100 na ni wilaya ya uhifadhi wa wanyamapori kwa sababu tuna maeneo ya WMA na ya uwindaji, je, Serikali haiwezi kuja kutujengea VETA hasa inayolenga tasnia ya ufugaji mifugo na uhifadhi wa wanyama na mazingira na ikiwezekana Chuo cha Walimu wa Sayansi kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa sayansi nchini na tuna ardhi ya kutosha na maji ya Kilimanjaro yanakuja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba mikoa na wilaya zote nchini zinakuwa na vyuo vya VETA. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeanza kwenye baadhi ya maeneo ambako tayari kuna ujenzi unaendelea na kuna mipango ya kuhakikisha kwamba wilaya zote zinakuwa na vyuo vya VETA. Kwa hiyo, hata Longido tutafika na wakati tunafanya hivyo, tutaangalia zile fani ambazo zitawasaidia wananchi wa pale kuweza kujiendeleza.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri aliyonipa Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa sababu ya kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kuinua hali ya elimu katika Wilaya ya Longido. Historia ya Wilaya ya Longido…
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Swali ni kwamba kwa upande wa ubora wa elimu ukizingatia kwamba ubora wa elimu unategemea uboreshaji wa shule kuanzia ngazi ya chekechea; na kwa kwa sababu vitongoji vya Wilaya ya Longido viko mbali na shule za msingi zenye elimu za chekechea (shule za awali).
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani katika kuhimiza wananchi wajenge shule na Serikali ipeleke walimu waliosomea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa tatizo la shule za msingi la miundombinu halina tofauti na Shule zetu za Sekondari katika Wilaya ya Longido; je, Serikali imejipangaje kutusaidia kuziba mapengo yaliyopo katika madarasa yapatayo 58, maabara 27, mabweni 73, nyumba za walimu
252, maktaba nane...
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna uhaba wa walimu wa sayansi wapatao 27? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS - TAWALAZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, katika muda mfupi tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge amefanya mengi, ofisini kwangu ameshakuja zaidi ya mara tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zake nazipokea kwa niaba ya Serikali, naomba sana nimhakikishie kwamba wananchi waendelee na juhudi wanazozifanya. Tunatambua juhudi zao. Pale ambapo atakamilisha darasa lolote la awali, tuwasiliane ili tuweze kupeleka walimu wa madarasa ya awali ambao wamesomeshwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu kumalizia maboma ambayo wananchi wameanzisha na yamefika kwenye lenta, naomba nimhakikishie kwamba katika fedha za ruzuku ya maendeleo ambazo tutazipeleka kuanzia mwezi wa Saba tumewapa kipaumbele Wakurugenzi wazingatie sana kumalizia maboma ambayo yameanzishwa na wananchi. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, wananchi wa Longido wamekuwa wakisubiri kwa hamu kukamilishwa kwa mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka Mlimani Kilimanjaro, Mto Simba kuja Longido. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mradi huu kwa kasi inayoendelea sasa hivi unatarajiwa kukamilika lini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa jinsi anavyofuatilia utekelezaji wa miradi ya maji katika Jimbo lake na Serikali hii ya Awamu ya Tano tayari ina mkataba wa zaidi ya bilioni 16 kwa ajili ya Halmashauri yake ya Longido.
Mheshimiwa Spika, uko mradi mkubwa unaotoa maji Mlima Kilimanjaro kilomita 64. Kulikuwa na matatizo ya kupata bomba la chuma lakini Serikali, Wizara imeingilia kati Mkandarasi ameingia mkataba na kiwanda cha kuzalisha mabomba na mabomba yameanza kuingia tayari kule site.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kwamba kuanzia sasa tunaenda haraka ili tuhakikishe wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido katika harakati za kujiongezea mapato ya ndani ya kuinua kipato cha wananchi wake walijenga mnada wa mifugo katika Kata ya Kimokouwa inayopakana na Kata ya Namanga iliyoko mpakani mwa Kenya na Tanzania ili pia kuwatengenezea wachuuzi wa mifugo mazingira rafiki ya kuweza kufanya biashara ya mipakani (cross border trade) na kwa kuwa baada ya Halmashauri kumaliza mnada ule wakaanza kuhamasisha wananchi waliokuwa wanapitisha ng’ombe maporini kupeleka kuuza katika minada ya Kenya ambayo ndiyo inayutumika katika maeneo ya Longido, jana Waziri akaenda akatoa maagizo ya kuwapangia bei ya kulitumia soko lile kitendo ambacho kimewakera wananchi…
Naomba Waziri mwenye dhamana aliyekwenda jana kutoa directives za bei ya mifugo atoe kauli itakayowafanya wananchi wa Longido na Halmashauri kuelewa kwamba soko hili ambalo wamejenga kwa nguvu zao wenyewe na wafadhili bila Wizara kuwekeza hata shilingi watatoa justification gani ya kwenda kulitwaa na kulipangia bei ambayo sio rafiki ni kandamizi, hii ni sawa na kuvuna usichopanda?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tasnia hii ya mifugo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zake. Tunafahamu kwamba Longido kumejengwa mnada kupitia miradi ya Serikali kupitia ule Mradi wa MIVAF unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada ule kimkakati uko mpakani na sisi katika tasnia hii ya mifugo kama Taifa kwa mwaka mmoja kwa tathmini tuliyoifanya ng’ombe 1,600,000 wanatoroshwa kwenda nje ya nchi. Pia tunapoteza jumla ya shilingi 263,000,000,000 kama Taifa ikiwa ni mapato yetu yanayotokana na tasnia hii ya mifugo hasa export royalty.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Kiruswa kwa sababu nafahamu kwamba ni Mbunge makini na ana timu makini iliyoko kule ya DC na Mtendaji kwa maana ya Mkurugenzi, watupe ushirikiano. Hatufanyi jambo hili kwa ajili ya kuwakomoa, tunafanya jambo hili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi yetu lakini tunafanya jambo hili kwa ajili ya kuhakikisha Taifa letu linanufaika na rasilimali zake. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Waziri hususan anaponieleza mkakati wa Serikali katika kuinua kiwango cha elimu ya awali. Namshukuru sana kwamba ametamka wazi kwamba kuna vitabu vya kiada vinachapishwa na kuna vitabu vya ziada viko katika mchakato wa kutolewa. Sasa swali langu la kwanza ni kwamba, je, vitabu hivi vitasambazwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa inaonekana Serikali imejikita kupeleka madarasa ya elimu ya awali katika shule za msingi kwa kuzingatia kwamba jamii nyingi za kifugaji wanaoishi katika Wilaya kwa mfano Wilaya yangu ya Longido, Simanjiro, Kiteto, Ngorongoro na Monduli hata Siha wanaishi mbali na shule kutokana na jiografia. Sasa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba elimu hii bora katika ngazi ya awali inawafikia watoto hawa wadogo ambao hawawezi kufikia hizo shule zenye madarasa ya awali?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusiana na vitabu katika jibu langu la msingi nimesema kwamba tayari vitabu sita vya kiada; na vitabu vya kiada ni vile ambavyo ni lazima kwa mujibu wa muhtasari mwanafunzi awenavyo tayari vimekwishachapwa ambavyo viko katika hatua ya uchapaji ni vitabu vya ziada yaani vya nyongeza zaidi ya vile ambavyo ni vya lazima katika muhtasari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na umbali wa shule, kama nilivyosema Serikali imetoa maelekezo kwamba kila shule ya msingi ni laizma iwe na darasa la awali. Kwa hiyo, nitoe wito kwake nafahamu kwenye jamii za wafugaji kunakuwa na changamoto kwamba Halmashauri ishirikiane na Serikali Kuu kuona kwamba kama kuna utaratibu wa tofauti na uliowekwa na Serikali wa kuchukuliwa kwa ajili ya jamii za wafugaji Serikali iko tayari. Lakini Halmashauri ndiyo ina jukumu la kutoa mapendekezo pale ambapo wanaona utaratibu wa kisera ni mgumu kulingana na mazingira yao.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza na kabla sijauliza maswali yangu kwanza nipende kumpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuinua sekta ya mifugo. Lakini hasa niishukuru Serikali kwa ajili ya soko hilo lililojengwa kule mpakani mwa Kenya na Tanzania katika Kijiji cha Eworendeke, na nitoe rai kwamba waachiwe halmashauri waendeshe kwa sababu ndio waliobuni Wizara itoe tu oversight.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza kwa kuwa jamii hii ya kifugaji ili mifugo iwaletee tija wanahitaji malisho, maji, tiba ya chanjo na kutibu magonjwa sambamba na masoko ya uhakika na ninashukuru kwamba soko la Eworendeke linaweza kuja kuwa soko la uhakika waondokane na adha ya kupeleka mifugo huko nje ya nchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia hasa wafugaji wa West Kilimanjaro waweze kupata hayo maeneo ya kulishia hasa ukizingatia kuna mgogoro mkubwa ambao umekuwa ukitokea kila wakati wa kiangazi kwenye yale mashamba pori yaliyotelekezwa na Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili linamhusu Waziri wa Maliasili kwa sababu maswali yangu yalichanganywa, kwa sababu niliuliza swali moja kwa ajili ya Wizara ya Utalii na majibu niliyopata sikuridhika nayo. Eneo lote la Wilaya ya Longido ni Pori Tengefu na dhana ya WMA ilipoanza mchakato ulifuatwa WMA ndiyo ikapatikana. Mchakato ukapitiwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, WMA ya Lake Natron imepitia mchakato wote. Ni kwa nini WMA hii haitangazwi na imebakia kutangazwa tu na kitu kinawezekana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge huyu mpya kwa kazi kubwa nzuri anayoifanya ya kuwasimamia wafugaji wa eneo hili la Longido.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kwanza, Mheshimiwa Mbunge namna ambayo tutakavyoweza kushirikiana nao kama Halmashauri, nataka nimhakikishie ya kwamba sisi kama Wizara tutawapa ushirikiano na hatutafanya kazi ile ya usimamizi wa moja kwa moja isipokuwa tutakuwa pale kwa pamoja kuhakikisha kwamba kodi zote za Serikali ambazo zinasimamiwa na Wizara zitakuwa zinapatikana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya suala la West Kilimanjaro, naomba nimhakikishie na niwahakikishie wafugaji wote wa eneo lile, ikiwa ni pamoja na Longido, Siha na kwingineko ya kwamba mkakati wetu mahususi wa Wizara ni kuhakikisha kwamba wafugaji ng’ombe hawafi tena. Wakati maeneo ya asili ambayo yanamilikiwa na Wizara yetu kwa maana ya ranchi ziko pale. Tumekubaliana ya kwamba wafugaji watapewa ruksa ya kupewa vitalu katika maeneo yale anaingiza ng’ombe wake, ng’ombe mmoja kwa kiasi cha shilingi 10,000; anamlisha, anamnywesha katika ranchi ile kwa muda wa miezi mitatu ananenepa na kumtoa kumpeleka sokoni.
Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kiruswa na wafugaji wote nchini ya kwamba tumejipanga vyema na tutawasaidia katika jambo hilo.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa majibu mazuri aliyoyatoa.
Kuhusu hili suala la WMA kutangazwa katika lile eneo naomba kwanza niweke vizuri tu kwamba WMA ni hatua ya kwanza ya uhifadhi ambayo inashughulikiwa na vijiji vinavyozunguka maeneo ya hifadhi, baada ya hapo inakuja pori tengefu baada ya hapo pori la Akiba, baada ya hapo hifadhi ya Taifa. Sasa tumeshafika tayari kwenye pori tengefu hatuwezi kurudi tena chini kwenye WMA, lile eneo litaendelea bado kuwa ni pori tengefu, lakini baadae tutaangalia kama sifa zinaliruhusu kuwa ni pori la akiba baada ya hapo tutaendelea kupanda zaidi badala ya kurudi nyuma. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa asilimia 95 ya wakazi wa Longido ni wafugaji na ndicho wanachokitegemea kwa uchumi wao; na kwa kuwa mvua kubwa za mwaka huu zimeharibu miundombinu ya mabwawa likiwemo bwawa la Kimokolwa lililopasuka, Emuriatata na Sinoniki; na kwa kuwa mabwawa mengine matatu yanayotegemewa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri ana mpango gani au ametutengea fedha kiasi gani kurekebisha miundombinu hiyo iliyoharibika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kiruswa anataka kujua ni kiasi gani tumewatengea? Tunayo hela ambayo tumeitenga kwa ajili ya kuweza kuwasaidia wananchi wa Longido kwenda kurekebisha miundombinu yao ya mifugo ikiwa ni pamoja na mnada wa mifugo wa pale Longido.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la miundombinu iliyopasuka kutokana na mvua nyingi zilizonyesha nchini, naomba mimi na yeye Mheshimiwa Mbunge tuweze kukutana na kuweza kulijadili na kuona ni namna gani tutaweza tukatoka kwenda kuwasaidia wananchi.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Longido ambao pia nina furaha kwamba Madiwani wao karibu wote leo wapo hapa kama wageni wa Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido sawa na Busokelo, kwamba tuna utajiri mkubwa wa madini ya rubi. Kwa kuwa madini ya rubi ukiyakata ili kuyaongezea thamani kulingana na utaratibu uliotolewa na Serikali yanasagika. Kwa kuwa Mawaziri walishatembelea na wakajua changamoto hiyo, wanatuambia ni lini utaratibu huo utakamilika ili wananchi waweze kuyauza mawe haya waendelee kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mimi pamoja na Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Nyongo tulikwenda Longido na hasa kwenye eneo la Mundarara anbako kuna machimbo ya rubi. Wananchi wa kule wanajihusisha na shughuli hiyo na changamoto aliyoizungumza Mheshimiwa Mbunge walitueleza kwenye mazungumzo yetu na wao. Jambo ambalo linapaswa lieleweke hapa ni kwamba Sheria yetu mpya ya Madini imezuia kabisa usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje ya nchi. Lengo ni kwamba tunataka teknolojia na ajira zibaki ndani ya nchi kuliko kuzisafirisha kwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madini ambayo yana upekee wa aina yake katika ukataji. Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini tunaandaa mwongozo wa namna bora zaidi ya kuwasaidia wananchi ili waweze kupata fursa ya kuuza madini haya.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Longido wanaoishi katika vijiji 32 vilivyopo Ukanda wa Magharibi unaokwenda mpaka Ziwa Natron waliungana wakatenga eneo la Hifadhi la Wanyamapori ambalo wameliita Lake Natron Wildlife Management Area, wakapita mchakato mzima na hatua zote za usajili ikabaki kipengele kimoja tu ambacho kipo katika dhamana ya Waziri ya kuwapatia user right yaani haki ya matumizi ya rasilimali ya wanyama pori katika eneo hili. Jumuiya hii imetumia rasilimali nyingi kupitia mchakato ambao wote mnaujua siyo wa bei nafuu na umetumia fedha za wafadhili na za Serikali, ni lini sasa Jumuiya hii itapewa user right wawe kuanza kulisimamia na kutumia rasilimali ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuna mchakato mrefu sana wa kusajili WMA na kama Mheshimiwa Mbunge ananihakikishia kwamba taratibu zote za awali zimekwishatimia, nitakwenda kufuatilia na kuona kama kipengele kilichobaki kinamhusu Waziri peke yake basi nitamshauri Mheshimiwa Waziri kutoa hiyo user right.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Waziri. Pamoja na majibu yake mazuri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza ni kuhusiana na uhalisia na Mto Ngarenanyuki. Mto huu ni moja ya mito michache ambayo imetokea katika maeneo yaliyohifadhiwa, unatokea katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha, chanzo chake ni salama na unapitisha maji mengi ya kutosha na kutiririsha katika nyanda za chini ambapo unapotoka ndani ya hifadhi, kijiji cha kwanza unafikia Kijiji cha Ngarenanyuki yanatiririka mpaka Kijiji cha Ngabobo na zamani za kale yalikuwa yanatiririka mpaka Kijiji cha Jimbo langu la Longido cha Ngereani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba; kwa kuwa maji haya yalipoingia Kijiji cha Ngarenanyuki wananchi wakagundua kwamba ni maji safi ya kuoteshea nyanya; wamekatakata mto mifereji mashine za kunyonya maji mtoni mpaka mto ukakaushwa na maji hayatiririki tena kwenda kwenye vile vijiji vya kusini zaidi. Serikali ina mpango gani wa kusanifu miundombinu ya umwangiliaji wa kisasa itakayowezesha matumizi bora ya maji haya ili yaendelee kutiririka kufikia jamii zilizo chini zaidi kwenye nyanda za chini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa tunakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na uwezekano wa maji haya kutosha wakulima wa nyanya waliopo Ngarenanyuki, Ngabobo Mpaka Ngereani kuwafikia wote kwa mtiririko wa asili. Serikali haioni kwamba ni bora sasa wajenge tanki kubwa la kuvuta maji Ngereani ili nao waendeleze kilimo cha umwangiliaji wa nyanya; hasa ukizingatia kwamba ni kilomita 10 mpaka 20 tu katikati Ngereani kutoka mtoni?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stephen Lemomo Kiruswa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yake yote mawili yamegusa utaalam ambao upo ndani ya Serikali ingawa haupo ndani ya Wizara yangu. Ni jambo la msingi alilolizungumza, kwamba kila Mtanzania anawiwa na dhima ya kulinda rasilimali za maji na hasa hasa kwa sababu haya maji mazuri yametoka katika eneo limeifadhiwa yalikuwa yanatiririka vizuri kwenda kwenye vijiji. Sasa wananchi wameya-tap na kuyachota na kupeleka kwenye miradi ya umwagiliaji bila kuzingatia ushauri mzuri wa kitaalam wa kutumia maji kidogo na kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi natoa ushauri kwa Tume ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bonde washirikiane, kwa sababu hizi ni mamlaka za Serikali, waende katika eneo husika wakawaelimishe wananchi kuhusu kilimo bora cha umwangiliaji bila kuchukua maji mengi kutoka kwenye mto ule ili maji yale yaifadhiwe yaendelee kutumika vile vile kwa shughuli zingine na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuhusu ujenzi wa tanki kubwa litatokana na ushauri ambao wataalam wataona kadri inayofaa katika kutumia maji ya Mto Ngarenanyuki. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamuuliza maswali ya nyongeza, nichukue fursa hii kumpongeza Naibu Waziri wa Utawala Bora na Utumishi japokuwa ni muda mfupi tu tangu apewe dhamana ya kusimamia nafasi hiyo utendaji wake unaonekana na kasi yake nafikiri ni sehemu ya kasi anayohitaji Rais wa nchi kuona katika utendaji wa Mawaziri wetu. Hongera sana mama, nakuomba uendelee kukaza buti umsaidie Rais kazi aliyokupa dhamana ya kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, swali langu la kwanza, kwa kuwa katika Wilaya ya Longido lenye jumla ya vijiji 49, kuna vijiji 22 ambavyo mpaka sasa hivi havina Watendaji wa Kijiji walioajiriwa, wako wanaokaimu tena wengine wamekaimu kwa miaka mingi. Ni lini sasa Serikali inakwenda kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Longido kibali cha kuajiri Watendaji hao ili kuziba pengo lililopo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba kupata majibu kwamba kwa kuwa katika baadhi ya zahanati tulizonazo katika Wilaya yangu ya Longido na vituo vya afya na kuna vingine viko mbioni kukamilishwa kama kile cha Kimokorwa, Engarenaibo na kadhalika ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi na naamini Serikali mwaka huu watatupatia bajeti ya kuvimalizia. Pia Hospitali ya Wilaya ambayo nayo imeanza kujengwa na inakwenda kasi na hata Siha nimeona Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa jumba la ghorofa linakalibia kukamilika.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi watapatikana ili facility hizi ziweze kutoa huduma shahiki kwa Watanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza yote kwa pamoja ya Mheshimiwa Mbunge Kiruswa wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana kwa pongezi, nazipokea, aendelee tu kuniombea kwa Mungu ili nisiwaangushe Watanzania wote na Mheshimiwa Rais mwenyewe. Pia na yeye binafsi nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwenye Jimbo lake la Longido hususani katika kufuatilia huduma zinazotolewa na watumishi wa umma kwa wapiga kura wake wa Jimbo la Longido.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu tu kwa ufupi na kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi zote za kukaimu; kwanza kukaimu ni nafasi ya muda, wala siyo ya kuthibitishwa. Naomba niwaeleze Watanzania wote kwa faida ya wengine, kwa sababu kuna wengine huwa wanafikiri kwamba ukipewa nafasi ya kukaimu, basi ndiyo leeway yako ya kuthibitishwa, hapana. Kukaimu unakaimu kwa muda na mara nyingi watu wengi wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu kwa sababu watu wamekuwa wakikaimishwa kienyeji bila kufuata utaratibu. Utaratibu ni kwamba unapotaka kumkaimisha kiongozi yeyote yule ambaye ameshafikia katika ile level ambayo tunaita superlative substansive post (nafasi ya uongozi) basi unatakiwa kupata kibali kutoka utumishi. Utumishi wakupatie kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwaka 2018 mwezi Septemba, Serikali yetu imetoa waraka kwamba nafasi zote zile za kukaimu zisizidi miezi sita. Unapotaka yule Afisa aendelee kukaimu, basi unatakiwa utoe sababu nyingine wewe kama Mwajiri kwa nini unataka aendelee kukaimu? Hiyo yote ni katika lengo la kuboresha ili viongozi wetu wasiwe wanakaimu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, kwenye jibu langu la msingi nimesema katika Jimbo lake la Longido tumetoa vibali na nafasi za ajira 177. Katika hizo 177, 65 zinakwenda katika Sekta ya Afya, 69 zinakwenda katika Sekta ya Elimu na zinazobaki nyingine zote zinakwenda katika kada nyingine mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika zile kada nyingine ambazo ni za kimuundo, zenyewe hazihitaji kukaimishwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mwaka huu wa Fedha 2018/2019, hizi nafasi 177 tutakuwa tumeshazijaza katika Wilaya ya Longido hususan Jimbo lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwanjelwa kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongeze jibu kwenye swali linalohusiana na Watendaji wa Serikali za Mitaa. Hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge wa Longido ni kweli, lakini naomba niseme tu kwamba kupata Watendaji kwenye ngazi za Halmashauri na huu ni mwaka wa bajeti kwenye Bunge hili Tukufu, tunatarajia Wakurugenzi ambao ndio waajiri wa watu hawa, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Mitaa watakuwa wameingiza kwenye bajeti zao ili tupitishe na waweze kupata ajira. Kwa hiyo, Wakurugenzi wanapaswa kujua upungufu wa maeneo yao ya kiutendaji, kama wakiwasiliana na Ofisi ya TAMISEMI kwamba hawa watu wanafanya kazi kubwa sana waweze kusaidiwa utendaji katika ngazi ya chini. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa moja ya changamoto za maendeleo vijijini ni ukosefu wa barabara zinazopitika na kwa kuwa TARURA imeundwa ili ku-address changamoto hiyo. Kwa kuwa katika Wilaya nyingi nchini, TARURA haina mitambo ya kutengeneza au hata kufungua hizo barabara vijijini ikiwemo Wilaya ya Longido. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wilaya zote ambazo TARURA haina mitambo ya kufanyia kazi wanapata mitambo hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niseme kweli tumekuwa na chombo hiki TARURA na imeanza kufanya kazi vizuri na Waheshimiwa Wabunge watakuwa mashahidi. Yako maeneo ambayo yalikuwa na changamoto kipindi cha nyuma sasa yanafayiwa kazi vizuri. TARURA watasimamia shughuli za ujenzi wa barabara za vijijini kama wanavyosimamia TANROADS, kwa maana hiyo wakipata fedha uko utaratibu wa kutangaza, tunapata wazabuni, wakandarasi mbalimbali wanakwenda kufanya matengenezo ya barabara kwa utaratibu ule ule kulingana na Sheria za Manunuzi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na TARURA wamefanya kazi nzuri na kwa muda mfupi wameshazitambua barabara zote na kuziingiza kwenye mfumo kwa sababu kulikuwa na changamoto ya barabara zingine ambazo zilikuwa hazitambuliki. Hivi karibuni wamepita karibu maeneo yote nchini kufanya sasa uhakiki kuona kama kuna sehemu barabara ilisahaulika iweze kuingia katika mtandao wa barabara.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo la Longido ni sehemu ambayo pia TARURA wamefanya kazi ya kutambua barabara. Kama nilivyosema ni kazi yetu sisi Bunge tukiwapa fedha za kutosha ninaamini barabara zote zitaboreshwa kulingana na changamoto zilizoko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza kuhusu watumishi waliochishwa kazi kwenye hili zoezi wenye vyeti vya Darasa la Saba wakaenda chuo; kwa mfano kuna waliokwenda Chuo cha Simanjiro cha Mifugo wakapata vyeti, waka- perform vizuri wakaenda kusoma Diploma ya Udaktari wa Mifugo katika chuo cha Serikali kule Tengeru, lakini baada ya zoezi kupita walipogundulika tu kwamba hawana cheti cha form four – lakini hawajadanganya – wakaachishwa kazi.

Je, Serikali inaweza kutoa tamko gani kuhusu hawa ambao wanaona kwamba wameonewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lazima tukumbuke kwamba tarehe 20 Mei, 2004, baada ya hapo wale wote ambao walikuwa wametoa taarifa zisizo sahihi tulitoa msamaha hadi tarehe 31 Desemba, 2017 kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi na wale wote waliojiendeleza, kwa mfano katika masuala ya recategorization.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, Serikali tunasisitiza, tunathamini, tunaheshimu recategorization kwa wale wote wanaojiendeleza kimasomo. Nimesema kwamba hadi hiyo tarehe 31 Desemba, 2017 kama walijiendeleza na vyeti vyao viko sahihi, watuletee Utumishi tutahakiki watarejeshwa kazini. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa moja ya chimbuko la migogoro ya mipaka katika vijiji vyetu ni kutokuwepo kwa alama imara na zinazoonekana kati ya mipaka iliyobainishwa kati ya Kijiji na Kijiji, Kata na Kata, Tarafa na Tarafa mpaka hata Wilaya na Wilaya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakiki kuweka alama madhubuti na kutengeneza ramani zitakazowezesha jamii zenye migogoro ya mipaka kujitambua na kuheshimu mipaka hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa katika Jimbo langu la Longido tuna migogoro michache sugu ambayo imekuwepo tangu Wilaya ya Longido ianzishwe zaidi ya miaka 20 iliyopita, ambayo ni mpaka wa Kijiji cha Wosiwosi Kata ya Gilailumbwa na Kata ya Matali Kijiji cha Matali ‘B’ na mpaka huo huo ulio Kaskazini mwa ziwa Natron una mgogoro na eneo la Ngorongoro ambapo Kitongoji cha Ilbilin kimevamiwa na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na kuanzisha vituo vyao vya kudumu pamoja na eneo la Engaruka na sehemu ya Kitumbeine vijiji vya Sokon na Nadare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili kuja katika Jimbo langu atusaidie kutatua migogoro hiyo sugu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishamkubalia hata kwenye Kamati, huyu ni Mjumbe wa Kamati yangu na ni Mjumbe makini sana na ni mchambuzi mzuri sana wa masuala ya ardhi. Tulishakubaliana kwamba tutatafuta nafasi ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwaka huu tufike huko kwenye site ili tuzungumze pamoja na viongozi wenzangu wa Wilaya namna bora ya kukabiliana na hiyo migogoro. Kwa hiyo, Dkt. Kiruswa nitakuja huko kushirikiana ili kuhakikisha hiyo mipaka inatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili juu ya alama zinavyoonekana, katika uwekaji wa mipaka ya vijiji na vijiji huwa kunakuwepo na alama. Labda nimjulishe kwamba Seriakli kupitia Wizara ya TAMISEMI ndiyo huwa inatangaza, Mheshimiwa Rais ndiyo huwa anatangaza uanzishwaji wa mamlaka wa WIlaya, Mikoa na Vijiji vinatangazwa kwenye Ofisi ya Rais, kwa hiyo kuna mipaka ambayo huwa inawekwa pamoja na coordinates zinawekwa kwenye GN, zinatangazwa kwenye GN kwamba Wilaya fulani na Wilaya fulani itapakana na alama za msingi huwa zinawekwa kwenye GN na kwenye vijiji tunapopima huwa kunakuwa na alama zinatangazwa na zinawekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kama kuna matatizo ya kutokukubaliana kati ya kijiji na kijiji huko kwenye Wilaya yake nitakwenda lakini alama hizi za vijiji huwa zinawekwa na wanakijiji wanakubaliana ni alama gani na kila tunapopima huwa tunaweka mawe ambayo yanakuwa na alama na namba ambazo zile coordinates ndiyo zinaingizwa kwenye GN inayotangazwa maeneo ya mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mawe yale huwa tunaweka, sema labda pengine mawe yale yanafukiwa chini labda yeye angependa yawekwe juu, kwa hiyo kama kuna maeneo ambayo yana mwingiliano mkubwa, tuko tayari kuweka alama zinazoonekana badala ya zile ambazo tunaweka chini. Lakini sehemu kubwa huwa tunaweka alama na zile alama zina namba ambazo huwa zinatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona, ili niulize swali la nyongeza kuhusu madini. Sisi katika Wilaya ya Longido tuna madini ya aina ya Ruby, na kuna mgodi wa miaka mingi, unaoitwa Mundarara Ruby Mine na sasa hivi wachimbaji wadogowadogo wameibuka wametokeza baada ya kujua madini haya yana thamani na ninaamini Serikali itakuja kuwajengea uwezo.

Lakini swali langu ni kwamba, huu mgodi ambao ulianzishwa tangu kabla ya uhuru, ni wa nani, na kama ni wa Serikali, Serikali inafaidikaje na huu mgodi na ni asilimia ngapi kama kuna ownership ya joint venture na mwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, pale Mundarara, kuna mgodi ambao ni mgodi wa uchimbaji wa Ruby. Mgodi ule kabla, miaka ya 60, ni kwamba mgodi ule ulikuwa ni mali ya Serikali, na sisi tumeweza kufuatilia na tuliunda Tume ili kuona ni namna gani mgodi ule uliweza kuporwa. Nipende tu kusema kwamba tumelifuatilia na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mgodi ule unamilikiwa sehemu na Serikali na kuna kampuni nyingine ambayo ilikuwa inamiliki, lakini mgodi ule mpaka sasa hivi, asilimia 50 tunaumiliki sisi yaani Wizara ya Madini kupitia Shirika la Madini yaani la STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mgodi huu ulikuwa na mikiki mingi, ambako Tume tumeituma, tumetuma Tume ya watu maalumu, wafuatilie, watushauri tuone namna gani ya mgodi ule kuurudisha Serikalini au kutafuta namna ya kuweza kuungana na mchimbaji mwingine au mwekezaji mwingine na Serikali iweze kupata mapato yake kupitia shirika la madini la STAMICO.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza kwa Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Spika, natanguliza shukrani zangu za dhati kwa sababu Mheshimiwa Prof. Mbarawa amepambana bega kwa bega nami mpaka yale maji ya Mlima Kilimanjaro yakawafikia wananchi wa Wilaya ya Longido. Sasa hivi ametutengea shilingi bilioni 2.9 kusambaza yale maji na wale wananchi wanaoishi pembezoni mwa bomba watapata maji wao pamoja na mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kilichobaki kuhusiana na mradi huo ni kwamba Mheshimiwa Rais alipokuja Namanga kuzindua mpaka wa pamoja mwezi Februari, 2019 aliwaahidi wananchi kwamba mradi huo kwa sababu unaleta maji mengi mpaka Longido utaongezewa extension ili uwafikie wananchi walioko njiani mpaka Namanga. Je, ahadi hii ya Rais itaanza kutekelezwa lini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais alitoa ahadi hiyo nasi wakati wote tunatekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wote wa juu. Kazi tunayofanya sasa hivi ni kufanya usanifu kutoa maji kutoka Longido mpaka huko kwenye mpaka wetu wa Namanga. Mara baada ya usanifu huo kumalizika kazi ya ujenzi itaanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kazi hii itaanza mara moja na tumejipanga kuhakikisha kazi hii tutaifanya kwa pesa zetu za ndani na kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani. Tunaamini tukifanya hivyo kazi itakamilika haraka iwezekanavyo.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Wilaya ya Longido na hata Monduli pia, tumepitiwa na umeme wa msongo mkubwa na napenda kuishukuru Serikali kwa sababu wameshalipa fidia kwa watu wale ambao walistahili kufidiwa, lakini pia naomba kuuliza kwa sababu vijiji vilivyopitiwa katika Wilaya yangu ya Longido ni vitano; Eorendeke, Kimokorwa, Oromomba, Ranchi na Engikaret kuna maeneo mahsusi ambayo jamii iliyatenga kama maeneo ya wazi wakitarajia kwamba fidia yake itakwenda kurudishwa ndani ya kijiji waweze kufanyia miradi ya maendeleo kama kujenga shule, zahanati na kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo ni pungufu sana ikiwa ni pamoja na barabara katika vijiji vile.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Wizara itarejesha hizo fedha za maeneo ambayo jamii iliyatenga kama maeneo ya wazi kwa vijiji husika au halmashauri ili tuweze kufanyia hayo maendeleo ambayo tayari wananchi wameshabainisha? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa na nimpongeze kwa kufuatilia masuala ya nishati hususan fidia ya wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli maeneo aliyoyataja ikiwemo Wilaya ya Longido yamepitiwa na njia ya msongo wa KV 400 kutoka Singida – Namanga na tumeshalipa fidia takribani kama shilingi bilioni 44 na maeneo aliyosema ambayo yalikuwa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za jamii, thamani yake ya fidia ni kama shilingi bilioni 10, utaratibu unaendelea wa kuweza kuyalipa katika maeneo mbalimbali ili pesa hizo ziweze kuchangia shughuli za maendeleo, nakushukuru.