Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Justin Joseph Monko (17 total)

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, na niwashukuru sana wana-CCM na Chama changu cha Mapinduzi na hasa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa kuniwezesha kuwa mwakilishi wao hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yaliyozungumwa katika Jimbo la Morogoro Kusini yanafanana sana na Jimbo la Singida Kaskazini. Jimbo la Singida Kaskazini wakati unaongelea usambazaji wa umeme REA Awamu ya Tatu tulipata Mradi wa REA Awamu ya Pili katika vijiji vya Mrama, Makhandi, Mitula, Merya, Mipilo, Magojoha, Msange, Madasenga, Njia Panda, Mohamo, Mwamba na Mgori. Hata hivyo, mwaka 2016 mwishoni mkandarasi huyo alifilisika wa SPENCON na kazi hiyo ilisimama tangu mwaka 2016 na hadi sasa mradi huo haujaendelea mpaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri atuambie Serikali inatueleza ni lini mkandarasi mwingine atapatikana kwa sababu mkandarasi huyu aliyekuwepo tunaambiwa hawezi kuomba tena kazi hiyo ya kuendeleza shughuli hiyo ya REA Awamu ya Pili, atapatikana mkandarasi mwingine na kumalizia shughuli hiyo ili wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini waendelee nao kunufaika na nishati ya umeme? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali hili la nyongeza la Mheshimiwa Monko. Na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Monko kwa kuaminiwa na wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge, na tumeweza kuwapa pole wananchi wa Mikoa ya Singida na Kilimanjaro baada ya kutokea matatizo ambayo hayakutarajiwa ya mkandarasi SPENCON ambaye kwa kweli alifanya kazi kama asilima 65 na akashindwa kumalizia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyopata kusema pia, Serikali kwa kuliona hilo ikachukua hatua stahiki kupitia Wakala wa Umeme Vijijini na kuanza harakati za kutafuta mkandarasi mpya kwa ajili ya kumalizia kazi zilizosalia katika Jimbo la Singida Kaskazini pamoja na majimbo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mchakato huu ambao umefanyika na Wakala wa Umeme Vijijini tumefanikiwa kumpata mkandarasi katika Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ameshaanza kazi na mimi nimejiridhisha, nilienda nikamuona, lakini katika Mkoa wa Singida mchakato unaendelea kwa sasa kwa wakandarasi wale watarajiwa kuwasilisha performance bond na baada ya hapo mkataba wa awali ambao wameuwasilisha kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapitio na tunatarajia mwezi Machi mwaka huu kazi zianze.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, na baada ya kikao hiki cha Bunge lako tukufu naomba tuonane naye kwa ajili ya kumweleza kazi zitakazofanyika na vijiji ambavyo vitafikiwa ili aweze kuwaambia wananchi wake. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi pamoja na majibu ya kukatisha tamaa ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. (Kicheko)
Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba barabara hii ni muhimu sana katika eneo hili na ametueleza kwamba katika bajeti ya mwaka 2018/2019 wametenga kujenga kilometa tano tu katika barabara ambayo anasema ina urefu wa zaidi ya kilometa tisini na kitu.
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba kuendelea kutenga kilometa tano zitawafanya wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini na Mkoa wa Singida na Manyara kusubiri ujenzi huu kwa zaidi ya miaka 19 ijayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imekuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na imetusumbua sana wakati wa uchaguzi kila mara.
Je, Serikali sasa ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 15 zilizosalia katika kufika katika mji wa Ilongero ili kusudi kuwaondolea walau kuwapunguzia wananchi adha hii wanayoipata kwa sasa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara au ujenzi wowote ule unahitaji kupata pesa ya kutosha. Ninamwomba tu Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba nchi yetu ni kubwa na kila sehemu inahitaji ipate huduma kutokana na mfuko na kipato cha Serikali kilichopo na sio kwamba tuna-concentrate na barabara moja tu. Tunakiri kwamba kweli barabara ile ni muhimu lakini Tanzania ni kubwa na yote inahitaji pesa kutoka Wizara hiyo hiyo moja.
Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupata kilometa tano ni mwanzo, lakini pesa itakapopatikana tunaweza tukajenga hata kilometa nyingi lakini angalau hizo tano zilizopatikana ni muhimu azipokee na ashukuru kwamba tunafanya jitihada kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kweli barabara hii ipo kwenye ahadi na hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi barabara hii inasomeka, lakini siyo hiyo tu peke yake ni barabara ambayo inatoka kuanzia Karatu ambayo ipo Arusha, inapitia Mbulu inakuja mpaka hapo tunapopazungumza Haydom inakwenda mpaka Simiyu. Pesa zitakapopatikana na tukumbuke kwamba tuna ahadi mpaka mwaka 2020, pesa itakapopatikana hizi barabara zote zitajengwa kwa kiwango cha lami. Tuna nia nzuri kama Serikali kuhakikisha kwamba Wananchi wanapata huduma nzuri za barabara.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida pia tumehamasika sana kulima pamba na katika Jimbo langu la Singida Kaskazini pamba imelimwa kwa ekari 1,300 na tulipata pembejeo kutoka Serikalini ikiwemo dawa. Dawa hii ambayo tuliitumia kulingana na maelekezo ya wataalam; pamoja na Bodi ya Pamba kuja kupiga kwenye pamba lakini pamba hiyo imepukutisha majani na hivi sasa ninavyozungumza wananchi wa Kata za Ilongero, Ughandi, Mtonge, Kinyeto, Muhunga na Msange wanashindwa kabisa kupata mazao katika pamba ambayo wamelima katika msimu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuuliza Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na hasara hii ambayo wananchi wameipata?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuwapa pole sana wananchi wa jimbo lake kutokana na tatizo lililojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama alivyosema ni kwamba sisi kama Serikali tutatuma wataalam wetu kwenda kwenye jimbo lake kwanza kuthibitisha kama tatizo hilo limetokea, na kama ni kweli limetokea basi ninaagiza Bodi ya Pamba, na sisi tuna mfuko wetu kwenye Bodi ya Pamba kwamba maeneo yote ambayo yamelimwa pamba tutatoa vile viuatilifu kwa bure isipokuwa mbegu wataendelea kununua. Ahsante.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Singida Kaskazini lina Kata 21 na Vijiji 84. Kata za Muhunga, Ngimu, Itaja, Makulo na Ughandi hazina kijiji hata kimoja ambacho kimepitiwa na miradi ya umeme wa REA II na REA III. Je, ni lini wananchi hawa watapata fursa hiyo ya kupata umeme ambao ni muhimu sana katika shughuli za maendeleo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wa REA Awamu ya Tatu ambao umeshaanza sasa yapo maeneo ya wananchi ambayo tayari wameshajiandaa pamoja na taasisi ambayo yanarukwa na umeme, katika mpango wa upatikanaji wa umeme huu ambao unaendelea sasa. Serikali ina kauli gani kwa wananchi katika maeneo hayo ambayo tayari wameusubiri umeme huu kwa muda mrefu na wako karibu na njia za umeme? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Monko, ni Mbunge mgeni lakini kwa kipindi kifupi cha kuchaguliwa kwake amefanya kazi kubwa ya kufuatilia miradi ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kiti chako pia kimekuwa kikiagiza mara kwa mara kupitia Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wenyeviti na Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako tukufu kwa miradi yote ya REA kwa ujumla yake, kulikuwa na agizo la kufuatilia ufunguaji wa Letter of Credit.
Naomba niliarifu Bunge lako tukufu na niishukuru Kamati ya Bajeti, Wizara ya Fedha na Benki Kuu na nikutaarifu kwamba mpaka sasa Wizara ya Nishati kupitia REA tumefanikiwa kufungua Letter of Credit kwa makampuni 14 yenye jumla ya shilingi bilioni 220. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba kuanzia sasa utekelezaji wa miradi ya REA Awamu ya Tatu itapata kasi kubwa. Niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba wategemee sasa miradi kushika kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, swali lake la kwanza ametaja Kata kadhaa ambazo amesema amesema hakuna hata Kijiji kimoja ambacho kina umeme katika REA zote zilizopita mpaka sasa. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli kwa mradi huu unaoendelea wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili yatafikiwa maeneo yote. Kwa hiyo, maeneo na kata ambazo amezitaja zitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili utakaoanza Julai, 2019 na kukamilisha Juni, 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, katika maeneo ambayo Mradi wa REA umeanza, Mheshimiwa Mbunge amesema zipo taasisi za umma zimerukwa na yapo maeneo ambayo wananchi wamepitiwa na umeme mkubwa lakini hawana dalili za kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Nishati imetoa maelekezo kwa wakandarasi wote nchi nzima. Hapa namwomba mkandarasi wa Mkoa wa Singida na wakandarasi wote; na kama nilivyosema sasa mambo ni mazuri, wahakikishe kazi inakwenda kwa mujibu wa scope na yale maeneo ambayo yameainishwa yapate huduma hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Suke lililopo katika Kijiji cha Msange lilifanyiwa upembuzi tangu mwaka 2010 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwenye Kata ya Msange, Makhojoa, Mwasawila na nyingine. Bwawa hili lilihitaji shilingi 1,300,000,000 na tangu mwaka 2010 hatujatengewa fedha mpaka sasa.
Je, ni lini tutapata fedha hizo kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa bwawa hilo ili wananchi waache kutegemea kilimo cha mvua? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwona mtu mzima analia, ujue kuna jambo. Naona Mheshimiwa Mbunge amelia sana kuhusu wananchi wake. Nataka niwahakikishie tutaona haja basi katika bajeti ya mwaka 2019/2020 ili tuangalie namna gani tunaweza tukasaidia hili jambo ili wananchi wake waweze kunufaika na mradi huu.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Katika Jimbo langu la Singida Kaskazini tunazo sekondari tatu ambazo zilipandishwa hadhi ikiwepo katika Tarafa ya Mgori Mwanamema, Ilongero pamoja na Mtinku. Shule hizi bado zina changamoto zikiwepo za vitanda, magodoro na kadhalika na zingine zimeshindwa hata kupangiwa wanafunzi katika mwaka huu kwa sababu hazijakidhi vigezo. Je, Serikali itatusaidiaje ili kukamilisha vigezo hivyo na shule hizo zianze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Monko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, amezitaja shule tatu katika jimbo lake ambazo zimepandishwa hadhi, lakini kati ya shule tatu Shule ya Mwanamema Shein kama ilivyo jina lake ni shule ambayo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa na sasa hivi wamepangwa vijana kupelekwa pale. Wengine walikuwa wanakuja ofisini kwangu kusema bwana hii Shule ya Mwanamema Shein sisi hatuitambui tunaomba tuhamishe watoto, nimewaambia hatuwezi kuhamisha watoto pale. Watoto waende wakasome pale Shule ya Mwanamema Shein na watapata elimu nzuri, tumepeleka walimu wazuri pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Monko pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba zile shule ambazo zina usajili wa Wizara ya Elimu lakini zinatakiwa kuongezewa miundombinu kidogo tu ili kusudi ziweze kuchukua vijana wengi zaidi kuliko capacity yao ya sasa hivi, wiki ijayo Wizara ya Fedha itapeleka fedha kwenye hizo shule, kama walikuwa wanakosa bwalo watajengewa bwalo, kama walikuwa wanakosa darasa moja watajengewa darasa moja ili kusudi mpaka mwezi wa nane vijana wa second selection waweze kuripoti shuleni.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kweli Serikali imeweza kufanikiwa kujenga kituo kama alivyosema kilichogharimu shilingi milioni 400 katika Wilaya ya Mkalama, lakini Wilaya ile inahitaji vituo vingi vya afya na yapo majengo ambayo wananchi tayari wameshaanza kuyajenga na yamefikia katika kiwango cha kupaua. Je, Serikali iko tayari sasa kuja kukamilisha kituo kingine cha afya ili wananchi waweze kupata huduma bora? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo la Singida Kaskazini tunavyo vituo viwili vya afya. Kituo cha Mgori na Kituo cha Ilongero na vituo hivi havijapata fedha za ukarabati na havifanyi upasuaji ukizingatia kwamba Halmashauri yangu haina hospitali. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha vile vituo vianze kutoa huduma ya upasuaji na wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini waweze kupata huduma? (Makofi). Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli ambao uko dhahiri na sisi Waheshimiwa Wabunge wote ni mashuhuda jinsi ambavyo Serikali imetilia maanani suala zima la afya kwa maana ya kujenga vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya pamoja na kuziboresha Hospitali za Rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu hii kasi ambayo tumeianza siyo ya nguvu za soda, tutaendelea nayo kuhakikisha kwamba tunaboresha masuala mazima ya afya ikiwemo katika Jimbo la Mkalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Monko ni shuhuda kwamba hivi karibuni Kituo chake cha Afya cha Mgori kimepelekewa pesa. Hii yote ni kuonesha jinsi ambavyo Serikali inajali afya za wananchi na jinsi ambavyo inaboresha huduma za afya. Naomba awe na subira kwa kushirikiana na Serikali hakika tutapiga hatua mbele zaidi.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kijiji cha Ndwamughanga kilichopo katika Jimbo la Singida Kaskazini kina vitongoji ambavyo vipo Mukulu ambavyo viko kilomita 23 kutoka Makao Makuu ya Kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiomba Vitongoji hivi visajiliwe kama Kijiji kwa muda mrefu. Je, ni lini Vijiji hivi vya Mukulu vinaweza kupata usajili wa kuwa kijiji kinachojitegemea ukizingatia umbali ili wananchi waweze kupata huduma za Kiserikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema kuna Kitongoji ambacho kipo kilomita 20 kutoka katika Kijiji ambacho ndiyo kimezaa hicho Kitongoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sifa za Kitongoji kutoka katika Kitongoji kuwa Kijiji sasa sina uhakika na sifa ya hicho Kitongoji ambacho kinalazimika kufuata huduma ya kilomita 20. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuzingatia vigezo na sifa za kitongoji kubadilika kuwa kijiji pindi zitakapokuwa zimekamilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI haitasita kuhakikisha kwamba Kitongoji hicho kinakuwa Kijiji kama sifa stahiki zinakidhi.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika,nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya kutoka Singida – Kinyeto - Mahojoa - Sagara yenye urefu wa kilomita 42 ambao tuliiombea kwa Mheshimiwa Rais kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kweli kwa sasa imeharibika kwa kiwango kikubwa sana. Je, Serikali ipo tayari sasa kutenga fedha za ziada za dharura katika kuhakikisha kwamba madaraja yaliyovunjika katika msimu huuna barabara yanarekebishwa?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Monko anakiri kwamba barabara hiyo ilikuwa imejengwa kwa kiwango cha lami na mvua imenyesha madaraja yameanza kubomoka. Tukubaliane kwamba kila neema wakati mwingine inakuja na adha yake, kama ambavyo ilikuwa nia ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika, ni vizuri tukaenda tukajua uharibifu uliotokea na gharama zinazohitajika ili kuirudisha barabara katika hali yake ya kuweza kupitika kama tunavyotarajia kwa wananchi wetu.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo walilonalo wananchi wa Tanga linafanana sana na tatizo walilonalo wananchi wa Mkoa wa Singida. Jimbo la Singida Kaskazini na Mkoa wa Singida kwa ujumla ni wakulima wakubwa sana wa vitunguu pamoja na alizeti. Hivi tunavyozungumza, soko la kitunguu gunia moja linauzwa kati ya shilingi 10,000/= mpaka shilingi 40,000/=, badala ya shilingi 80,000/= mpaka shilingi 120,000/= ilipokuwa katika msimu wa mwaka uliopita.

Je, Serikali iko tayari kuingilia kati suala hili na kuwanusuru wananchi ambao wanaendelea kupata hasara kutokana na kazi kubwa waliyofanya?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alichokisema. Kwanza tunatoa tahadhari kwa Watanzania, wakulima pamoja na wafanyabiashara, lipo tatizo hapa nchini ambalo ni kubwa, watu wanakuja katika vijiji kununua, wengine wananunua kwenye mashamba bila kufuata utaratibu. Hilo tunashirikiana na Wizara ya Kilimo na tunashirikiana na Shirika la Vipimo kuhakikisha kwamba utaratibu wa kisheria unafuatwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hao watu ambao wamekuwa wananunua halafu wanasafirisha nje ya nchi bila kuwa na vifungashio vinavyokubalika kisheria, hao wanakiuka sheria na kwa kweli itabidi tuchukue hatua kali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuingilia kati suala la bei, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaingilia kati na tutatoa maagizo kwa maandishi kuanzia leo.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa maswali ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Awali ya yote kwanza napenda niishukuru sana Serikali kwa fedha ambazo imetupatia sisi kwa ujenzi kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo, hospitali teule ya Wilaya ya Mtinko ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema tangu ilipopandishwa hadhi mwaka jana haijapangiwa Madaktari wala Wauguzi wa kufanya kazi na kuongeza huduma katika hospitali hiyo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuwasiliana pia na Wizara ya Afya ili kuhakikisha kwamba hospitali hiyo inapata Wauguzi na Madaktari wa kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anajua tofauti ya kituo cha afya na hospitali ya Wilaya na wananchi wale ambao ni zaidi ya wananchi 80,000 hawana kituo chochote cha afya na wamejenga jengo hilo kwa zaidi ya miaka nane na halmashauri yetu imeshindwa kutenga fedha za kukamilisha jengo hilo. Je, Wizara iko tayari kutenga fedha ya kukamilisha jengo hilo la kituo cha afya cha Makuro na kutenga fedha kwa ajili ya majengo mengine ili kituo cha afya cha Makuro kiweze kuanza kufanya kazi kwa Tarafa ya Mtinko. Ahsante?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Monko kwa kuendelea kuwasimamia wananchi wa Jimbo lake la Singida Kaskazini. Sasa naomba nimjibu swali lake la kwanza na la pili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anazungumzia habari ya kupata Wauguzi na Madaktari. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumelipokea jambo hili, katika wale Wauguzi na Madaktari ambao tumewaomba kibali maalum Ofisi ya Utumishi wakipatikana, basi tutaangalia pia eneo hili ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anazungumza habari ya kutenga fedha ya kukamilisha boma hili ambalo limejengwa kwa nguvu za wananchi. Namkaribisha Mheshimiwa Mbunge ofisini kwetu tuzungumze, tuone kitakachowezekana, lengo na makusudi ni kwamba jambo hili likamilike na nguvu za wananchi ziweze kuungwa mkono, zisipotee bure ahsante.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Singida- Ilongero –Ngamu ambayo pia inaunganisha Mkoa wa Manyara ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Singida. Barabara hii ilitangazwa kipande cha kilometa 12.6 kutoka Njuki kwenda Ilongero kujengwa kwa kiwango cha lami tangu mwezi Novemba mwaka jana.

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni lini ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo kutoka Njuki kwenda Ilongero utaanza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumejipanga kujenga barabara hii muhimu kutoka Singida- Ilongero- Ngamu tunakwenda mpaka Hydom na tumetenga fedha katika mwaka huu wa fedha unaoendelea, zoezi la usanifu ili
kujenga barabara hii yote inaendelea. Hata hivyo, kipande hiki cha barabara anachokizungumza kutoka eneo la Njuki kwenda Ilongero ni sehemu muhimu sana kwa kuwahudumia wanachi wa Singida Vijijini. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na utaratibu wa harakati za manunuzi, zikikamilika tu tutaanza ujenzi wa barabara hii muhimu, kwa hiyo Mheshimiwa Monko avute subira tunakwenda Ilongero kujenga barabara hii.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Singida Kaskazini lina miradi ya REA II, REA III, phase I pamoja na umeme wa backborne kwenye vijiji 54. Hadi sasa ni vijiji 13 tu ndiyo ambavyo vimekwishakufikiwa na umeme na vingine mpaka sasa bado. Je, Mheshimiwa Waziri wa Nishati yuko tayari kuambatana nami kutembelea Jimbo la Singida Kaskazini kujionea changamoto zilizopo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Monko amerejea Mradi wa REA awamu ya pili ambapo kwa kweli kama Serikali tuliwaomba radhi wakazi wa Mkoa wa Singida na Kilimanjaro baada ya makosa ambayo yalitendeka katika Mradi wa REA awamu ya pili na tukafanya kazi na kumweka Mkandarasi mpya ambaye anaendelea na kazi kwa kushirikiana na REA.

Mheshimiwa Spika, swali lake ameulizia utayari wetu wa kuambatana naye; nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge nipo tayari mimi pamoja na Waziri kwa wakati tofuati kutembelea Jimbo lake kama ambavyo tulishafanya mwezi wa Nane tulitemebelea Jimbo lake ikiwemo Kijiji cha Iddi Simba na tuliwasha umeme pia aliwakilishwa na Mheshimiwa Mbunge Aisharose Matembe. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge niko tayari muda wowote kutembelea eneo lake na kuendelea kuwasha umeme na kukagua kazi inavyoendelea. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa ambayo inafanya kwenye ujenzi wa reli mbalimbali ikiwepo ya standard gauge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kipande cha reli kutoka Manyoni kwenda Singida ambacho ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Singida. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua kipande hiki ambacho hakijafanya kazi kwa muda mrefu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilijenga kipande cha reli hii ya kati kuelekea Singida lakini baada ya ukarabati mkubwa wa barabara ya kutoka Dodoma kwenda Singida hapo katikati mizigo mingi imekuwa inatumia barabara. Suala hili tumeshaanza kulifanyia kazi ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza tukakarabati hiyo reli na kushawishi sasa wabeba mizigo ikiwepo ni pamoja na kuweka taratibu na sheria ndogo ndogo ili wengi watumie reli badala ya barabara. Kwa sasa suala hili Serikali inalifanyia kazi.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kwa kuwa Serikali imetueleza kwamba ina mikakati mbalimbali ya kuongeza nyumba za walimu na tatizo hili lililopo katika Jimbo la Kalenga linafafana sana na Jimbo la Singida Kaskazini.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa katika bajeti hii ya mwaka 2020/2021 kuanza kutenga fedha kwa ajili kutoa posho maalum kwa walimu ili waweze kukodisha nyumba na waishi katika maeneo ambayo yanastahili, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni mapenzi ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kwamba tuwe na uwezo wa kuwawezesha walimu wetu wafanye kazi katika mazingira raisi sana na lipokee ushauri wake na kwa sababu yeye ni Mheshimiwa Mbunge na mchakato huo bahati nzuri unaanzia kwenye ngazi ya halmashauri.

Kwa hiyo, ningeomba Waheshimiwa katika halmashauri zetu pale mchakato unaondelea sasa tunatengeneza bajeti tuangalie uwezekano wa kupunguza adha hii kwa walimu wetu; na sisi kama Serikali ngazi ya TAMISEMI tutalipokea na kuanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini nitoe wito kwa watanzania tunaoishi katika maeneo ambayo tunatoka hata Waheshimiwa Wabunge na wadau mbalimbali wa elimu hata tukijenga zile nyumba za kawaida na kuweza kuwapangisha walimu kwa bei nafuu walimu wataishi karibu maeno ya shule wataweza kutoa huduma mbalimbali. Tushirikiane pamoja kuweza kupunguza changamoto ya walimu, walimu wafundishe katika maeneo salama, rafiki pia na kodi ambayo ni affordable ili waweze kufanya kazi katika urahisi wake, ahsante sana.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuulizwa maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ukamilishaji wa maabara katika sekondari ni sehemu muhimu sana ya utoaji wa mafunzo kwa vitendo; na kwa kuwa Halmashauri nyingi nchini zimeshindwa kukamilisha maabara kwenye sekondari zetu: Je, Serikali ina mpango gani wa kukamlisha maabara hizo ili vijana wetu waweze kufanya mafunzo kwa vitendo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa katika swali la msingi, Mheshimiwa Waziri amesema, Mkoa wa Singida utapata vifaa kwenye shule 59: Je, ni shule zipi katika Jimbo la Singida Kaskazini zitakazopatiwa vifaa vivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge sawa na Waheshimiwa Wabunge wengine kwa kuendelea kufuatilia na kusimamia elimu ili vijana wetu wapate maisha mazuri huko baadaye kwa kujiendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza, kama Serikali ina mpango wa kupeleka fedha kukamilisha maabara katika mashule yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ina mpango mkakati, fedha hizi ambazo tunapata za kutoka Halmashauri zetu, fedha za kutoka Serikali kuu, fedha za kutoka katika wafadhili mbalimbali, pamoja na kazi nyingine za kujenga madarasa, lakini pia tunatumia kukamilisha maabara hizi. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba, mwaka huu wa fedha tumetenga fedha nyingi pia. Wakati ukifika tutaanza kutekeleza mradi huu na kila Halmashauri na kwenye mashule tutapeleka fedha ili kukamlisha maabara, likiwemo la Jimbo la Mheshimiwa Monko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anauliza, shule ambazo zina mpango wa kupelekewa vifaa vya maabara. Katika Jimbo la Mheshimiwa Monko, Singida Vijijini, shule kwa mfano ya Sekondari Madenga, Shule ya Sekondari Nyeri, Shule ya Sekondari Ugandi, Shule ya Sekondari Dokta Salmini, Shule ya Sekondari Mandewa, Shule ya Sekondari Mtururuni, Shule ya Sekondari Mganga na Shule ya Sekondari Utemini. Shule hizi pamoja na nyingine zitapata vifaa vya maabara mwaka huu ambao tunaendelea nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali inakiri kwamba, sheria na taratibu zinaruhusu uchaguzi huo; na kwa kuwa, wanatambua kwamba, maeneo mengi yalikuwa pia yana makaimu na chaguzi hizo hazikufanyika. Je, Serikali sasa inatoa maelekezo gani kwa watendaji wanaohusika ili wawe wanachukua hatua zinazostahili kwa wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sasa hivi tuko kwenye mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utaondoa kabisa makaimu hawa ambao wamekuwa ni kero kwa maeneo mengine na tumesikia chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, wametangaza kujitoa katika uchaguzi huu na kuwakosesha wananchi haki yao ya kimsingi ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa Katiba yetu na Serikali ya Vyama Vingi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na kadhia hii ambayo inaendelea nchini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua kwa nini nafasi hizo zilikuwa hazijazwi kama ambavyo inatakiwa na kanuni. Ni kweli kwamba, kumekuwa na nafasi wazi mpaka tunaingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu na hii ilitokana na aidha, watendaji wetu katika ngazi zile kutokuwa na uelewa mkubwa wa kanuni zetu, lakini vilevile tumeshaelekeza sasa kwamba, tunacho chuo hapa cha Serikali za Mitaa cha Hombolo. Baada ya uchaguzi huu Wakurugenzi na sisi Wabunge tunaomba tushiriki kuhakikisha kwamba, viongozi wetu watakaopatikana wa vijiji, vitongoji na mitaa wapate mafunzo pamoja na watendaji wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko sababu mbalimbali zimeainishwa ambazo Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji au Kitongoji anaweza kupoteza nafasi yake, mojawapo ni kwamba, kama Mwenyekiti kwenye Kijiji hajasoma mapato na matumizi kwa muda wa miaka mitatu mfululizo inaweza ikamfanya akapoteza nafasi yake. Vilevile Mwenyekiti huyo kama atakuwa hajaitisha mikutano mara tatu mfululizo bila sababu za msingi, au inaweza ikaitishwa mikutano ya kisheria yeye Mwenyekiti asihudhurie katika hii mikutano, sababu nyingi ambazo zimetolewa ikiwepo kufukuzwa na chama au kufariki au kujiuzulu mwenyewe. Kwa hiyo, tunaomba tutoe wito kwamba, baada ya uchaguzi huu basi viongozi wetu ngazi husika hasa Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zetu na Miji watoe elimu, watoe maelekezo na Waheshimiwa Wabunge wakati wowote ikitokea nafasi wazi au ukahisi, tuwasiliane tutachukua hatua kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anazungumzia habari ya CHADEMA kujiondoa katika nafasi za kugombea. Ni kweli na sisi kama ofisi tumepata taarifa kwenye mitandao labda huenda wakatoa tamko rasmi, lakini Kauli ya Serikali ni kwamba, uchaguzi huu unaendelea kama kawaida kama ulivyopangwa kwenye ratiba. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika tarehe 24 Novemba, mwaka huu 2019, wananchi wote ambao wamejiandikisha na vyama vile ambavyo vipo kwenye mchakato waendelee na mchakato wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wametoa tamko jana kwenye mitandao, lakini itakumbukwa kwamba, kwenye taratibu zetu ni kwamba, wale ambao walikuwa na malalamiko wameandika mapingamizi yao na kesho ndio siku ya mwisho, wao jana ndio wametoa tamko. Kwa hiyo, kama wamejiondoa hawana sababu yoyote ya kulalamika kwamba, hawakutendewa haki, tulieleza tukarudia mara kadhaa kwamba, watu wenye sifa ya kutoa mapingamizi ni wale ambao ni wagombea. Wenzetu walitaka watoe kauli Bungeni, kwenye mitandao, mtaani na Serikali iamue, Serikali inafanya kazi kwa karatasi kwa mawasiliano, hatuna document mezani hatuwezi kujadili jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito, yale maagizo ya kuhamasisha wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo bahati nzuri Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya kazi kubwa Watanzania wanamuunga mkono. Mwenye mamlaka ya kutoa maelekezo nchini Tanzania ni Rais wa Jamhuri ya Muungano pekee na sio kiongozi wa chama cha siasa. Kiongozi wa chama cha siasa atatoa maelekezo kwenye chama chake kwa wanachama wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama, tumepata taarifa kwenye mitandao wanahamasisha watu, wanaharibu mazao ya watu na wanatishia watumishi wa umma. Wakuu wa Wilaya popote mlipo kama kuna mtu anahisi hakutendewa haki kwenye uchaguzi huu na anafanya fujo mtaani, sheria stahiki zichukue mkondo wake. Hatujawahi kutunga sheria katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema ukigombea ukinyimwa haki au ukahisi kunyimwa haki ukafanye fujo. Ukigombea ukinyimwa haki au ukahisi kunyimwa haki ziko taratibu za kisheria wazifuate, wasipofuata vyombo vya usalama vitashughulika nao na Watanzania wawe na amani, uchaguzi uko palepale, amani na tulivu, tunachapa kazi na hakuna ambaye atawaambia wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo, sisi TAMISEMI tupo pale kila mahali, ukishiriki kuhamasisha fujo na viongozi wetu wachukue taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, atakayebainika tusilaumiane mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.