Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro (3 total)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Sera ya Tanzania kuhusu Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika na nje ya Afrika iliipatia heshima kubwa nchi yetu ya Tanzania. Nataka kujua Sera hii ya Ukombozi mpaka sasa inaendelea hasa kwa zile nchi ambazo bado hazijapata uhuru kama vile Sahara na Palestina?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi karibu tulisikia kuzorota kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Tanzania mpaka ikapelekea mwakilishi wao kurudi nyumbani. Nini mustakabali wa kisera kwa pande hizi mbili ambazo zina mzozo huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando kwa maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Tanzania imejijengea heshima kubwa sana katika Sera yake ya Ukombozi wa nchi mbalimbali Barani Afrika. Heshima hiyo bado ipo kwa Tanzania kwa sababu bado Sera ya Tanzania ya kupinga unyanyasaji, ukoloni na kutweza utu wa nchi yoyote ile inaendelea. Hivyo, msimamo wa Tanzania katika suala la Sahara pamoja na Palestina bado upo kama ambavyo ulikuwepo mara tu baada ya uhuru.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza duniani kuwa na Ubalozi Palestina. Bado tuna heshima hiyo na bado tuna mahusiano hayo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusu mahusiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya. Mahusiano ya kidemokrasia na diplomasia kati ya Tanzania na nchi zote duniani yanaratibiwa na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na 1963.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mkataba huo kila nchi inawajibu wa kuheshimu vipengele vya mkataba huo na endapo pande mmoja haitaheshimu vipengele vya mkataba huo, nchi nyingine ambayo imekosewa inawezaikachukua hatua stahiki. Na pale nchi inapochukua hatua stahiki haimaanishi kuwa mahusiano ya kidiplomasia yamevunjika hapana ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa Vienna.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwakilisha.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika siku chache ambazo nimeridhika la jibu la Serikali, this is a very good answer from the Government. Kuna takwimu za kutosha, kuna maelezo ya kutosha. Hivi ndivyo ambavyo ningetarajia majibu ya Mawaziri wengine yawe kama haya. Nina maswali mawili ya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chuo chetu ni cha miaka mingi hivi sasa na kama uzoefu, basi upo wa kutosha: Je, Mheshimiwa Waziri katika muongo ujao, miaka kumi ijayo, anakionaje chuo chetu? Kitakuwa kimefikia hadhi na kiwango gani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kada ya wana- diplomasia ni muhimu sana, kuna ambao tunaamini kwamba chuo hiki kinapaswa kuwa ndiyo alama ya Tanzania maana Career Diplomacy na hata Political Diplomacy wote wanapita hapa ili kwenda ku-shape sera na mitizamo na namna ya kuilinda na kuitetea Tanzania.

Je, kwa kiasi gani chuo hiki kinaweza kutumika kuwa ni think tank ya kujenga sera na mikakati ya kidiplomasia ili kwenda kuitetea nje kwenye ushindani na ukinzani wa Kidiplomasia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Ally Saleh kwa pongezi alizozitoa kwa jibu ambalo tumelitoa. Pili, nichukue fursa hii kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza aliuliza: Je, tunakionaje chuo kwa miaka kumi ijayo? Naomba tumweleze Mheshimiwa Ally Saleh, Mbunge wa Malindi pamoja na Watanzania wote kwamba Chuo chetu cha Diplomasia ni chuo ambacho kinaheshimika sana Barani Afrika. Umeona idadi ya nchi ambazo zimeleta wanafunzi hapa na zinaendelea kuleta wanafunzi hapa, hiyo ni ishara tosha kwamba heshima ya chuo hiki ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Wizara ni kukifanya Chuo hiki sasa kivuke mipaka kwenda nje ya mipaka. Tuna makubaliano ya awali na ndugu zetu wa Argentina waweze kukitumia chuo hiki kupata elimu ya Diplomasia. Hiyo ni ishara kwamba tunavyokwenda miaka kumi ijayo, yajayo yanafurahisha zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili aliuliza; je, Chuo kinaweza kuwa kama think tank? Hivi sasa kada ya Diplomasia inakuwa vizuri, tumepata wataalam wengi na sisi kama Serikali tunaendelea kuimarisha hiki chuo kwa kuweza kusomesha waatalam wengi zaidi na kuleta wengine kutoja nje kwa kupitia nyanja za ushirikiano ili kukifanya chuo hiki kiendelee kuheshimika na kitoe waatalam wengi watakaosaidia Tanzania katika Diplomasia.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa majibu hayo mazuri ya
Mheshimiwa Waziri lakini je, Serikali ya Muungano au Wizara hii ya Mambo ya Nje inazishauri zile nchi wakati zina mpango wa kuja kutembelea Tanzania kuziarifu kuwa nchi yetu ya Tanzania ina sehemu mbili za Muungano na kila sehemu ina mahitaji yake ya kiuchumi. Hivyo basi, Wizara ingekuwa inazishauri kwa sababu ukiangalia nchi tisa tu ambazo zimekuja Zanzibar naamini zingekuja na hizi nchi nyingine 12 kuna fursa nyingi ambazo ziko Zanzibar ambazo bara hakuna na kuna fursa ambazo ziko bara ambazo Zanzibar hakuna.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara iweze kuzishawishi wakati nchi za nje zinapoweza ku-engage kuja Zanzibar kuja kutembelea Tanzania. Basi iziambie kuwa Tanzania ina nchi mbili na nchi hizo mbili kila upande una vipaumbele vyake vya kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo nataka niliseme, Wizara inafanya jitihada gani kuwashawishi wale viongozi ambao hawakuja Zanzibar kutembelea wakati wa ziara zao lakini kufanya ushawishi wakutane na viongozi wa Zanzibar huku Tanzania Barai ili wale viongozi wa Zanzibar waweze kutoa haja zao na kuweza kutoa ushahwishi wao wa kuiona Zanzibar nayo inanufaika na ugeni ule. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni nchi moja kwa mujibu wa Ibara ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Na masuala ya nje ni sual ala Muungano kwa m ujibu wa Ibara ya 4 nyongeza ya kwanza ya Katiba. Kwa hiyo, uhusiano wetu na mambo ya nchi za nje unachukulia maanani suala la kwamba ni nchi moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mahusiano yetu mara nyingi tukiwasiliana wanafahamu kwamba kuna nchi moja inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na hayo, Serikali na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba kwa sababu ya historia ya Muungano wetu na hali halisi kwamba ni Muungano ambao umetokana na nchi mbili tunahakikisha ya kwamba wakati viongozi hao wanapokuja nchini, tunajenga ushawishi mkubwa ili watembelee Zanzibar na ndiyo maana kuanzia 2015 mpaka sasa viongozi 21 waliotembelea nchini kwetu. Tisa kati yao wametembelea Zanzibar, vile vile ifahamike kwamba kuna wengine vile vile ambao wametembelea Zanzibar tu wala hawajatembelea upande mwingine wa Jamhuri.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya masuala ambayo yanapewa kipaumbele sana katika uhusiano wa Kimataifa ni Muungano wetu ndiyo maana hata kwenye Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kuna Idara maalum inahusika na mambo ya Zanzibar. Mualiko wowote au kiongozi yeyote akija ushawishi mkubwa unafanyika ili aweze kutembelea pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Spika, sasa mara nyingi kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi mara nyingine linakuwa ni suala la utashi wa kiongozi mwenyewe na hauwezi kumlazimisha. Kwa hiyo, nimueleze tu kwanmba kwa kweli Serikali inajitahidi sana kuhakikisha kwamba viongozi hawa wanapata fursa ya kutembelea maeneo yote na hasa kujaribu vile vile kuelezea kuhusu fursa za kiuchumi na za kitalii zilizopo Zanzibar.