Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zainab Mndolwa Amir (45 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Philip Isdor Mpango (Mbunge) kwa kuwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu na maoni yangu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019utakuwa katika sehemu tatu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweke kipaumbele katika viwanda hususani kujenga, kufufua viwanda vyetu mfano, katika Mkoa wa Morogoro kuna viwanda kama vile Canvas, Polyster, Ceramic, Magunia, Tannaries (Kiwanda cha Ngozi), Moro Shoe, Moproco. Vyote hivi vipo katika Manispaa ya Morogoro, viwanda hivi vingine vinafanyakazi na vingine wawekezaji hawaviendelezi. Hivyo Serikali isimamie na kuwapa muda wawekezaji hao kuviendeleza na wakishindwa virudishwe kwa Serikali ili wapewe wawekezaji wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vikifanyakazi kama miaka ya 1980 na 1990 vitaleta ajira kwa Watanzania pia kuongeza Pato la Taifa la Tanzania, kulipa kodi ya bidhaa zinazozalishwa kutokana na ujenzi wa reli itakayojengwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (treni ya mwendokasi itaongeza chachu ya ajira ya wananchi wa Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani na Morogoro ambao watapata ajira katika viwanda hivyo vilivyopo Mkoa wa Morogoro).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kodi, niipongeze Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kukusanya kodi kwa wafanyakazi hususani katika Miji Mikuu mfano Dar es Salaam. Nashauri katika kipaumbele kimojawapo Serikali iandae utaratibu maalum ambao utamwezesha mfanyabiashara alipe kodi kwa wakati na afurahie kuchangia Pato la Taifa na siyo Serikali iwe adui kwa mlipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iboreshe mazingira ya mwananchi wakati wa kuanza biashara. Kuna tatizo katika utaratibu uliopo, nashauri katika Mpango wa Maendeleo 2018/2019 Serikali impe muda angalau miezi mitatu (grace period) mwananchi anayeanzisha biashara na baada ya hapo ifanye makadirio kwa malipo ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa mfanyabiashara anakadiriwa malipo ya kulipa kwa mwaka kabla ya kuanza biashara na sehemu kama vile Kariakoo makadiro ni makubwa mno ambayo si chini ya milioni mbili kwa mwaka, na hii hupelekea wafanyabiashara kushindwa kulipa kodi na
hatimaye kufunga biashara. Hivyo maoni yangu Serikali ipitie tena utaratibu huu kupunguza makadirio ili mwananchi aweze kumudu kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri faini wanazotozwa wafanyabiashara ambao wanakutwa na makosa, mfano ya kutotoa risiti za EFD ni kubwa mno shilingi milioni tatu kulinganisha na bidhaa aliyouza na hii hupelekea mwananchi kushindwa kulipa faini na hatimaye kufunga biashara zao. Pia nashauri wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama wamachinga hususani waliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Kariakoo) Serikali iwasajili ili waweze kuwa na mchango kwa Pato la Taifa kwa kulipa kodi na kwenda sambamba na kauli mbiu ya Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli ya ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya Serikali imefanya jitihada kubwa katika kutatua matatizo mbalimbali yakiwemo kutoa madawa, vifaa tiba, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Maoni yangu Hospitali ya Taifa Muhimbili ni Hospitali ya Rufaa Tanzania, wakati tunaelekea katika Mpango wa Maendeleo wa Bajeti wa mwaka 2018/2019 Serikali ijenge eneo ambalo litasaidia wananchi wanaowasindikiza wagonjwa wao kutoka katika mikoa mbalimbali Tanzania ambao hawana ndugu au jamaa Jijini Dar es Salaam, waweze kupata sehemu za kufikia baada ya kumkabidhi mgojwa wodini. Maana kuna baadhi ya wagonjwa wanahitaji huduma za karibu kutoka kwa ndugu zao ambazo wahudumu wakati mwingine ni vigumu kuzifanya. Wakati mwingine wagonjwa wanaopewa rufaa kuja Muhimbili ni watoto zaidi ya miaka 5 – 15 ambao wanahitaji huduma ya karibu ya mzazi au mlezi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/ 2019.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa taarifa ya 2017 – 2018 Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuwezesha sekta ya utalii, maliasili na ardhi iweze kuwekeza kwa muda muafaka, hatimaye kuweza kuingizia Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi wetu ili kuweza kutunza mazingira yetu ili yasiharibike na hususan ndani ya hifadhi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwekeze vya kutosha kutangaza vivutio tulivyonavyo nchini kwetu, si kwa mbuga za wanyama na Mlima Kilimanjaro tu bali hata vivutio vingine kama Mapango ya Amboni na kadhalika ili kuweza kuliletea pato Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge utaratibu wa kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati ili kuweza kulimaliza tatizo hili na wananchi waendelee na shughuli za uchumi na uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhakiki mashamba (makubwa) yaliyotelekezwa ili kuyabaini na Serikali kutoa ardhi hiyo kwa wananchi waliokosa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi la Wanyamapori wawe na utaratibu wa kutoa fidia kwa wananchi ambao watajeruhiwa au kuuawa na wanyamapori.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kuchangia katika ofisi ya TAMISEMI na ofisi ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi nzuri inayoifanya. Naipongeza kwa juhudi kubwa anazozifanya Mheshimiwa Jafo katika Wizara yake, hususani katika kazi zake zinazoonekana dhahiri katika kujenga vituo vya afya pia katika kujenga zahanati, na pia namshukuru sana kwa kupandisha Hospitali yetu ya Temeke kuwa Hospitali ya Rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba na kushauri Serikali; Hospitali ya Wilaya ya Temeke imepandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa lakini hospitali ile inachukua wagonjwa kutoka Wilaya za karibu hususani Mkuranga na Wilaya ya Kigamboni.

Nakuomba Mheshimiwa Waziri, najua kuna utaratibu unafanya kuboresha zahanati zilizokuwa Mkuranga pamoja na Kigamboni; naomba wakati unafanya utaratibu huo uitupie macho Hospitali ya Temeke. Hospitali hii wodi zake zile kweli ni chakavu na ni za siku nyingi. Nakuomba sana uipe kipaumbele, uiboreshe, kwa sababu wananchi wa Mkuranga wakipata transfer ni lazima waende Tumbi na Tumbi ni mbali sana kutokana na jiografia yake kwa hiyo wanachotakiwa ni kuwaleta Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Jafo unaandaa mazingira nakuomba sana Hospitali yetu ya Wilaya ya Temeke ambayo sasa hivi ndio itakuwa ni hospitali ya rufaa iboreshwe, majengo yake yawe ya hadhi ya rufaa. Kwa sababu eneo ni dogo nashauri Wizara angalau zile wodi namba moja, namba mbili , namba tatu majengo yake yawe ya ghorofa ili iweze kukidhi idadi ya wagonjwa. Pia si majengo tu kuna vifaa muhimu pia vinatakiwa hospitali vifaa kama x- ray mmejitahidi, lakini vifaa vingine ni vile vidogo vidogo lakini tunaona si vya muhimu. Katika wodi za wagonjwa lazima kuwe na vikabati vya kuhifadhia chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa ukifika Hospitali ya Temeke sasa hivi kuna matatizo, unapompelekea mgonjwa wako chakula unaweka chini chakula hakuna vikabati vya kutosha kwa hiyo naomba sana katika kuboresha hizo hospitali na vifaa vingine ambavyo mnaviona ni vidogo vinahudumia wananchi, vinahudumia wagonjwa wote ni muhimu sana katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Ni ukweli usiopongika kwamba Hospitali ya Muhimbili inachukua wagonjwa wengi kutoka mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani. Serikali imejitahidi katika kujenga vyumba vya upasuaji na kuongeza wodi, lakini kuna changamoto moja inayoikabili hospitali ya muhimbili naona watu wengi hawaioni, lakini sisi wakazi wa mjini Dar es Salaam tunaiona. Si wagonjwa wote wanaoletwa katika Hospitali ya Muhimbili wana wenyeji katika Mkoa wa Dar es Salaam. Wanapopewa rufaa wakifika pale emergence na kukabidhi wagonjwa wao huwa wanaambiwa kwamba mgonjwa wako ameshapatiwa kitanda, kwa hiyo yeye aondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine hawana ndugu wala jamaa Dar es Salaam. Tunaiomba Wizara angalau itenge jengo maalum ambalo litasaidia wale wasindikizaji ambao wanakuja kuleta wagonjwa wao waweze kupata eneo la kijisitiri na kusubiri matokeo ya wagonjwa wao kama ni vipimo na kuwahudumia. Kuna huduma nyingine haziwezi kufanywa na daktari, haziwezi kufanywa na nesi. Nurse hawezi akamlisha mgonjwa, kufua nguo za mgonjwa na labda mgonjwa akiwa amejisaidia, ni mtu wa karibu mno anatakiwa azifanye zile huduma.

Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Jafo, Hospitali ya Muhimbli ipatiwe eneo maalum ambalo litakalokuwa na wahudumu watakaoweza kukaa na kuwaona wagonjwa wao jinsi wananvyoendelea na vipimo na kuweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali. Kama ikiwezekana wawe na hata identy card ya kuonesha kwamba huyu mgonjwa wake yuko Sewa Haji au yuko Kibasila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili iweze kusaidia hata wale walinzi wetu wawapo katika maeneo ya ulinzi naomba sana hospitali zetu; nitolee mfano Hospitali ya Mwananyamala; naitolea mfano; ukipeleka mgonjwa hospitali ya Mwananyamala na Mwenyezi Mungu akamtanguliza mbele ya haki akitoka wodini, anapopelekwa chumba cha maiti ili kumtoa kila siku ni 20,000. Akikaa siku 10 ni shilingi 200,000, akifia nyumbani na kuletwa ndani kwenye mortuary ya hospitali unakuta anakuwa-charged shilingi 30,000. Sisemi utofauti wa malipo ninachosema yule ni Mtanzania halisi ambaye wakati wa uhai wake alikuwa analipa kodi na kodi hiyo ilikuwa inalipwa na Serikali inakusanya, iweje Mtanzania huyu amekufa na ametibiwa na ndugu zake kwa gharama nyingi sana maiti mnaitoza malipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaombeni kama inawekana, kwa ushauri wangu nawaomba mtoe yale malipo ya maiti. Nadhani pale mimi ninatolea mfano tu, kuna hospitali nyingi naona Waheshimiwa Wabunge sidhani kama mmefanya uchunguzi, ukiweka maiti yako hospitali si kama unaweka kwa sababu hutaki kumzika, huenda unasubiri ndugu na jamaa; kwa kweli gharama ni kubwa sana. Huyu maiti wa Tanzania ni Mtanzania alikuwa analipa kodi.

Naomba sana Mheshimiwa Jafo uliangalie kwa makini katika bajeti yako, muondoe haya malipo ya kumtoa maiti wetu katika hospitali hizi za Serikali, iwe huduma kama huduma nyingine. Kwa sababu inaonekana kama tumekosa sehemu nyingine ya kukusanya mapato, tutafute eneo lingine Serikali si kwenye maiti, tuwaonee huruma wafiwa na tumuonee huruma pia marehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia pia Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Hospitali ya Mkoa wa Morogoro chumba chake cha kuhifadhia maiti kipo nje ya uzio wa hospitali na kiko karibuni sana na shule ya sekondari ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilisoma pale miaka ya 1980, ni kero sana ile mortuary, iko karibu na madarasa kiasi kwamba ndugu waliofiwa na ndugu yao wakati wanakuja kuchukua marehemu wao wanahisia mbalimbali wengine hulia, wengine huja pale labda kuaga kwa mapambio na mwalimu anapofundisha darasani hakuna usikivu. (Makofi)

Naombeni Mheshimiwa Jafo wakati unapanga bajeti yako uliangalie kwa jicho la huruma wanafunzi wa Morogoro Sekondari wanapata tabu kwa kuwepo chumba cha maiti karibu na madarasa. Naomba ulifanyie kazi kwa sababu hili ni tatizo kubwa ingawa Mheshimiwa Abdul-Azizi ataniunga mokono ni Mbunge wa Morogoro na anaona tatizo hili, yeye alisoma Forest, mimi nimesoma Morogoro miaka ya 1980 lakini tatizo ni kubwa sana. Hata wakati mnafanya mtihani mwalimu unakuta anaweka stop watch kwa sababu wangoje zile kelele zipungue, nawaombeni muhamishe ile mortuary ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda kuchangia kwenye utawala bora, muda hautoshi mambo ni mengi. Kuna baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanawaweka ndani kwa masaa 24 wananchi wetu bila sababu na wakati mwingine sababu zenyewe hazijulikani, anakuambia wewe kaa ndani. Sasa nataka Serikali inijulishe, je, kama kuna sheria hii ni makosa gani ambayo Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anatakiwa amuweke mtu ndani kwa masaa 24?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibainikwa kwamba amemuweka kimakosa, je, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya atachukuliwa hatua gani? Maana sasa hivi hatuelewi, hata sheria kila mtu anachukua mamlaka mikononi. (Makofi)

Nakuomba Mheshimiwa George Mkuchika unijibu swali hili, ni sheria gani inawaruhusu wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwaweka ndani wananchi na baadae anawatoa? Je, ikibainika kwamba hana kosa lolote je, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya atachukuliwa hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndugu tuliwarudisha juzi wa darasa la saba, wengine wamefariki, je, Serikali ina mpango gani kwa wale ndugu ambao jamaa zao wamefariki; na hapa juzi tumetangaza kwamba waterejeshwa, je, stahiki zao zitakuwaje? (Makofi)

Kwa hiyo, naomba wakati wa kutoa maelezo tufahamishwe, kwamba stahiki za wela ambao wamepoteza maisha wengine kwa presha tu baada ya kusimamishwa, je, stahiki zao zitapatika vipi? Kwa sababu wameondoka mbele haki wameacha familia na juzi tumesema kwamba warudi makazini na hawapo duniani? Tunaomba Serikali itupe majibu kwa wale ambao wametangulia mbele ya haki na sheria imesema warudi kazini, walipwe mishahara yao tangu pale waliposimamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mengi ya kuyazungumza lakini naomba sana walimu wengi wana matatizo, wengi wamezungumza, na sisi wote tumepita kwa walimu lakini sekta hii hatuipi uzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kuongeza mishahara nashauri walimu wawe wa kwanza, utaona, kwamba utakapowaongezea mishahara walimu wengi, hata kama mtu kapata division one atakuwa interest ya kusoma ualimu. Kama walimu wangekuwa wanalipwa mishahara kama tunayolipwa sisi, wengi na mimi pia ni mwalimu nisingekuwa hapa, lakini kutokana na ualimu kuonekana kama ni kazi dhalili watu wengine wanaacha ile kazi wanaondoka. Kwa hiyo, naomba sana tuwaboreshee walimu mishahara yao stahiki zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi. Watakapofanya ya kazi kwa weledi wanafunzi wetu watafaulu vizuri kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana, naomba haya yasiishie kwenye vitabu hivi tu, mmeandika mambo mazuri lakini yasiiishie kwenye maandishi. Hii bajeti iliyopagwa itolewe kwa wakati ili muweze kufanya kazi zenu barabara, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya njema ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi yake nzuri anayoifanya pamoja na Naibu Mawaziri wake na wafanyakazi wa Wizara wote kwa ujumla. Nampongeza kwa sababu tunaona msongamano Mkoani Dar-es-Salaam umepungua kwa kupata mwendokasi na sasa hivi katika bajeti hii nimeona barabara mbalimbali zimetengewa bajeti ya matengenezo ili kuepuka msongamano huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna changamoto nyingi zinajitokeza. Bajeti hii imepangwa na kwenye vitabu inaridhisha na inaonekana ni nzuri sana, Dar- es-Salaam ni uso wa nchi yetu kwa sababu watu mbalimbali wanavyotoka nchi za nje hufikia Dar-es-Salaam na baadaye ndio wanakuja mikoani, kwa hiyo, naomba bajeti iliyotengwa ifike kwa wakati. Vilevile tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri atutafutie wakandarasi ambao wana kiwango cha hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona barabara yetu ya Kilwa ilitengenezwa chini ya kiwango baada ya muda mfupi imeharibika na hapa tumeona pia itatengenezwa kwa mwendokasi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri mkandarasi atakayempata aiboreshe ile Barabara ya Kilwa iwe yenye ubora kwa sababu ilitengenezwa mara ya mwanzo lakini haikuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia kuhusu Kivuko cha Magogoni. Ni muda mrefu sana wananchi wa Dar es Salaam, hususan waishio Kigamboni walikuwa na tatizo la kivuko na msongamano wa magari lakini tunashukuru Serikali ikatujengea Daraja la Nyerere. Napenda kueleza Bunge lako Tukufu, wananchi wa Kigamboni bado wana changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uvuke katika daraja lile kwa gari ndogo tu ni shilingi 2,000 ukizingatia wananchi wake wengi shughuli zao zote ziko ng’ambo ya bahari, lazima wavuke asubuhi wawapeleke watoto shule, ofisi nyingi ziko ng’ambo ya bahari, hospitali pia, changamoto ni nyingi na kwamba ni ghali mno kuvuka katika daraja lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa gari ndogo ni Sh.2,000, mtu akivuka tu kwenda na kurudi Sh.4,000. Wakati mwingine watu pia wanakuwa na wagonjwa hospitalini wanaenda mara tatu kwa siku, gharama ya kivuko ni kubwa mno Mheshimiwa Waziri. Namwomba pamoja na Wizara ya TAMISEMI, ingawa nilishauliza swali hili kwamba NSSF nao walijenga lakini ninachokiona kwa Daraja la Kigamboni, wananchi wa Kigamboni wamepewa mzigo mkubwa sana. Hawana faraja na lile daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijua kwamba wananchi wa Kigamboni wamepata faraja kwa uwepo wa daraja lile angalau watavuka labda kwa bei nafuu, lakini kwa bei ya Sh.2,000 kwa gari ndogo na gari kubwa mpaka Sh.7,000 mpaka Sh.15,000 ni ghali mno. Naiomba Wizara hii kwa kushirikiana na TAMISEMI waliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi imefikia wakati wananchi wa Kigamboni ambao wanatumia vyombo vya moto, magari yao hawavuki nayo. Ukienda katika Kata ya Kigamboni utakuta watu wengi wameweka parking za magari, anaweka gari lake anavuka kwa panton kwa shilingi 200, anaenda kufanya shughuli zake mjini kisha anarudi analipa shilingi 1,000. Kwa hiyo, anakwepa kuvuka kwenye daraja kwa sababu ni ghali mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wafanye utaratibu kabisa, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile analifahamu hili, wananchi wa Kigamboni wanafurahia daraja, lakini daraja lile halina neema kwao. Wanasema maisha bora kwa watu wa Kigamboni kwenye daraja lile hayapo ni ghali mno. Kwa sababu, hata kama ni mshahara Sh. 4,000 mtu anavuka kila siku kwenda na kurudi, mwisho wa mwezi aki-calculate ina maana unaishia kwenye usafiri. Nadhani katika madaraja yote Tanzania ni Daraja la Kigamboni tu ambalo watu hutozwa nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea kwamba watu wa Kigamboni watapata neema kwa sababu madaraja ni huduma kama huduma nyingine. Kama ni masuala ya kukusanya kodi basi lile daraja lingejengwa Ruvu au Wami kwa sababu ni magari mengi sana yanapita maeneo hayo na Serikali ingekusanya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri, naona ananitazama lakini naomba aandike haya ninayozungumza na ayazingatie akishirikiana na TAMISEMI, wawaonee huruma wananchi wanaoishi Kigamboni kwa sababu daraja lile halina manufaa kwao, ni ghali mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wapunguze na ikiwezekana wavuke hata kwa kutumia smart card, hata kama wakiambiwa shilingi 10,000 kwa mwezi au shilingi 20,000 hata mtu akivuka mara tano mara kumi lakini ana kadi maalum ili kupunguza gharama ile. Wakati mwingine wanashindwa kabisa magari yao huacha ng’ambo na kwenda kwa kutumia panton. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia kuhusu barabara zetu. Tumeona Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa na imeona jambo la muhimu barabara ya Dar es Salaam – Morogoro na sisi ni mashahidi tunapita kila siku katika barabara zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja niliuliza hapa kwamba ni lini Serikali itafanya mkakati wa kukarabati barabara zetu na mojawapo ni eneo korofi sana la Chalinze hadi Mlandizi. Nikajibiwa kwamba eneo lile ni korofi kwa sababu inapita mizigo mizito lakini mimi ninachosema siyo mizigo mizito tu pia kiwango cha barabara ni cha hali ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mkandarasi aliyejenga maeneo yale hakuzingatia eneo lenyewe husika labda lina maji ya aina gani ili atumie material husika. Kwa sababu kama ni mzigo mzito umetokea Kurasini bandarini, ukapita barabarani ukafika mpaka Mlandizi pale barabara angalau ni nzuri, lakini kutoka Mlandizi mpaka Chalinze ile barabara ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo suala la mzigo mzito kwa sababu mzigo ni uleule uliotoka bandarini na ndiyo uleule uliopita katika eneo lile na ndio uliofika Chalinze na kwenda Chalinze ukaenda Morogoro au Tanga na barabara kule ni nzuri. Kwa hiyo, hapa tatizo ni wakandarasi wetu, wanajenga barabara chini ya viwango. Namwomba Mheshimiwa Waziri pindi atakapoanza kutengeneza hizi barabara atafute wakandarasi wenye viwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwawekee masharti hawa wakandarasi, ikiwa watajenga barabara chini ya kiwango na ikifikia muda fulani na tumewalipa pesa, kwa pesa zao wenyewe waweze kugharamia barabara zile kwa maana kwamba wazitengeneze kwa fedha zao kwa sababu wanapewa fedha lakini barabara ziko chini ya kiwango na kuipa Serikali hasara kila mara kwenda kukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika taarifa hii kwamba barabara ya Chalinze mpaka Mlandizi kuna kilometa kama 12 zimeshaanza kukarabatiwa toka Machi lakini mimi napita mara kwa mara, ukarabati unaofanyika pale ni kuziba viraka. Kuziba viraka siyo kwamba ndiyo unatengeneza barabara, barabara ile ina mabonde kama matuta ya viazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ile barabara ijengwe kwa kiwango hata kama ni cha zege ili kuhimili mizigo mizito inayopita. Kwa sababu wanakarabati kwa kuweka viraka kusema ukweli bado tutapiga mark time, bado hatujatengeneza barabara zetu. Naiomba Serikali, kama mnavyosema Serikali hii ni sikivu, iwe sikivu kweli, haya yaliyoandikwa yatekelezwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zina matatizo pia. Kuna barabara ya kutoka Magole - Gairo ni mbovu. Mnaona maeneo ya Magubike tukipita barabara ni mbovu, naomba Serikali yetu pia itengeneze barabara hizo. Barabara nyingine ziko kwenye kingo za milima angalau Serikali wakati wanajenga zile barabara kuu zile waweke pavements ili wakati wa mvua kubwa mmomonyoko usiathiri barabara zetu na kuleta matatizo.

Kwa hiyo, haya aliyoyaandika Mheshimiwa Waziri katika kitabu hiki ni mazuri lakini changamoto zinakuja utekelezaji upo? Serikali itoe fedha kwa wakati na wakandarasi wanaoomba nawaomba wazingatie ubora na viwango vyao ili waweze kutengeneza barabara zetu ziwe za viwango na siyo kutengeneza barabara ili mradi barabara tu na kuipa Serikali hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri haya yote yaliyoandikwa yawe yanatekelezeka maana nimeona Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengi hapa wamechangia wakisema kwamba mambo mengi yalikuwepo bajeti zilizopita lakini mpaka leo ni ahadi tu kwenye vitabu lakini utekelezaji wake ni wa chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, kama ni Serikali sikivu aishauri iweze kukarabati na kujenga barabara zetu kwenye kiwango kinachohitajika ili kuepuka ukarabati wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mbarawa, kama ni Serikali sikivu naomba aishauri iweze kukarabati na kujenga barabara zetu kwenye kiwango kinachohitajika ili kuepuka ukarabati wa mara kwa mara. Ukarabati huu wa mara kwa mara huipa Serikali hasara pia na badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma. Badala ya kujenga barabara nyingine, tunarudi kujenga barabara ambazo zilishajengwa na zimejengwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nashukuru sana kwa mchango huu namwomba Mheshimiwa Waziri yatekelezwe kwa wakati na Serikali itoe fedha kwa wakati kama ilivyoahidi na kama ilivyoandika ili barabara zetu ziwe za kiwango.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, nami napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa afya njema kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Fedha. Pili, napenda kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii nami niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara katika nchi yetu na wafanyabiashara wa Dar es Salaam wanachangia pato kubwa la Taifa, lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi sana. Moja ya changamoto ni utitiri wa kodi. Ili mfanyabiashara aanzishe biashara, kuna process nyingi anapitia. Lazima apate leseni na hupewi leseni mpaka ukakadiriwe mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiutaratibu ingefaa zaidi mtu kabla ya kufanya biashara kwanza apewe muda maalum halafu baadaye ndiyo wanamkadiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano Dar es Salaam, ukienda pale Mnazi Mmoja Anatoglo, unataka leseni unaambiwa kwanza nenda TRA pale Summit Tower Lumumba. Ukifika Lumumba wanakuuliza eneo la biashara liko wapi? Unaambiwa liko Kariakoo. Wanakadiria biashara kulingana na eneo na wala siyo biashara unayoifanya. Hii ndiyo inayopelekea wafanyabiashara wengi kufunga maduka yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaambiwa huko Kariakoo ni mkoa wa kodi shilingi milioni tatu. Mtu anakadiria akiwa ofisini; hajui biashara unauza shilingi ngapi na hujaanza kuweka hata display. Ni tatizo kubwa sana kwa wafanyabiashara na hii ndiyo inawafanya wafanyabiasha wengi kufunga biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia TRA sasa hivi imepata mwanya; usipotoa risiti kutokana na matatizo ya EFD sasa hivi, kitu cha Sh.5,000/= unaambiwa faini yake shilingi milioni tatu. Mwingine anashindwa sasa kulipa shilingi milioni tatu, mtu wa TRA anapata mwanya anakwambia sasa tuzungumze. Mnakosa mapato, mtu anapewa shilingi milioni moja yanaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri katika kuliendea hili, najua binadamu siyo malaika, anafanya makosa na makosa mengine yanatokana na hizi mashine; na mashine zenyewe inaelekea labda zina hitilafu. Wakati mwingine umetoa bidhaa unataka uandike risiti
unakuta mteja kaondoka, kumbe ameshawasiliana na TRA anakuja kukukamata anakwambia toa shilingi milioni tatu. Tuweke faini ambazo ni reasonable zinazolipika ili Serikali iweze kupata mapato yake kulikoni kuishia katika rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kikosi cha Zimamoto sasa hivi kimetokea kule Dar es Salaam, kinataka kila frame ya duka iweke Fire Extinguisher. Najiuliza sana Mheshimiwa, mfanyabiashara anafungua duka 12.00 asubuhi, anafunga saa 11.00 jioni. Short ya meme ikitokea usiku wa manane fire extinguisher iko ndani ya duka lake, itamsaidia nini kuzima moto kama siyo biashara? Mfano tu, tutoe sisi Wabunge wote, watu wa Zimamoto waje waseme kila Mbunge achukue fire extinguisher aweke chumbani kwake, kweli itawezekana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba utitiri huu wa kodi unapelekea wafanyabiashara kuonekana mwisho wa mwaka akipiga hesabu hapati faida, anafunga duka lake. Tuelekeze nguvu zetu katika kuwasaidia wafanyabiashara ambao huwa wanaleta ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ambayo siyo rasmi hususan ya Machinga pia wanakwamisha wafanyabiashara kufunga maduka yao Kariakoo. Mfanyabiashara analipa kodi ya takakata na asipokutwa na dust been analipa faini shilingi 50,000/=. Nje, Machinga hana dust been na hajui takataka zake anatupa wapi, anauza bila risiti. Ile kauli mbiu ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti, ni kwa baadhi ya wafanyabiashara, lakini sio wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, sekta isiyo rasmi isajiliwe, watu waweze kulipa mapato na kila mtu kama ni haki wote wafanye biashara kwa haki na walipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tendency ya watu watu wetu wa Tanzania wanaona biashara zinazouzwa barabarani ni rahisi kuliko za madukani. Kwa hiyo, wafanyabiasha wanakwazika, hawapati faida katika maduka yao, mwisho wa mwaka umemkadiria mapato makubwa, hajui atalipaje, ndiyo maana maduka yanafungwa. Kwa hiyo, naomba irekebishwe, mtu apewe grace period at least miezi mitatu kisha ndiyo wanamkadiria. Mapato, maana yake amepata. Mtu hajaanza kuweka bidhaa unamkadiria mapato, ameuza nini? (Makofi)

Waheshimiwa kuna kodi nyingine ambazo kwa kweli zinasikitisha sana. Nitazungumzia tozo ambazo zinatozwa marehemu kwenye hospitali zetu. Mtu amefiwa na ndugu yake, amemuuguza kwa gharama kubwa, anaenda kulipa matibabu pale na yuko mortuary. Akifika mortuary tena anambiwa marehemu kalala siku tatu, Sh.60,000/=. Pale siyo guest. Yule ni Mtanzania, alikuwa analipa kodi wakati wa uhai wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, katika tozo alizozifuta naomba afute na tozo za maiti katika hospitali zetu. Tutafute sehemu nyingine ya kukusanya kodi lakini siyo kwa maiti, tuwaonee huruma wafiwa na marehemu wenyewe ambao wameshatangulia mbele ya haki na wakati wa uhai wao walikuwa wanalipa kodi kama Watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia pia suala la viwanda. Tuna viwanda vingi takriban 53,050 katika nchi yetu na kuna viwanda 3,306 ambavyo vinafanya kazi. Naishauri Serikali, kwanza tuanze na vile viwanda vikubwa vilivyobinafsishwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi hapa kaona kuna watu walimilikishwa mashamba wakashindwa kuyaendeleza, wakafutiwa hati zao. Sasa twende kwenye viwanda pia; viwanda vingi vilikuwepo na wawekezaji wameshindwa kuviendeleza. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati wanatafuta mapori ya kufyeka na kutengeneza viwanda vipya, tuanze kwanza na viwanda vya zamani, tuvifufue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitolea mfano hapa Mkoa wa Morogoro, kuna takriban viwanda vingi. Mwaka 1985 Morogoro ukifika ilikuwa unapata ajira, lakini nyumba hupati. Kulikuwa kuna kiwanda cha Canvas, Ceramics, Moproco, Magunia, Tanneries, Morogoro Shoes, Polyster; viwanda ni vingi zaidi ya kumi. Kuna Sukari Kilombero na Sukari Mtibwa. Viwanda vile tuvifuatilie. Viko zaidi za kumi na ajira zake siyo watu wawili watatu, vinaajiri watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunatafuta mapori ya kujenga viwanda, naishauri Serikali ipitie viwanda vyote vile vya zamani ambavyo hawaviendelezwi; kuna viwanda vya mafuta Moprocco, tulikuwa tunapata mafuta mazuri sana, lakini sasa hivi uzalishaji wake ni wa kusuasua. Tuvifuatilie tuone kama wale wawekezaji wameshindwa kuviendeleza tuvichukue ili tuwape wawekezaji wengine kuliko kuhangaika sasa hivi wananchi hawana ajira, viwanda vikubwa unaambiwa kiwanda kinahitaji watu wanne watano. Haiwezekani hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni sana wakati tunatafuta mchakato wa kukata mapori, tuangalie viwanda. Tanga kulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, kimekufa. Sasa hivi wanaweka depot ya mafuta. Kiwanda cha Mbolea kilikuwa kinasaidia wakulima wetu, naomba sana Waheshimiwa kila mkoa unajua kabisa Tanga kuna wakulima wa matunda. Tuanzishe viwanda vya matunda ili wakulima nao wapate sehemu ya kuuzia bidhaa zao. Tuanzishe viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana hapa hapa Tanzania kuwezesha wakulima wetu kulima na kwenda kuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano General Tyre. Kiwanda hiki malighafi zake zinapatikana mikoa miwili tu; mpira unapatikana Tanga na Morogoro, lakini mashamba yake pia yana mgogoro mpaka sasa hivi. Ndiyo maana mwekezaji anashindwa kufanya uzalishaji. Kwa hiyo, nashauri kwa kuwa ardhi ya Tanga na Morogoro iko katika mikoa mingine, tuhamasishe wakulima wetu, tuwape mikopo Serikali isimamie hili ili mikoa mingine ilime kilimo cha mpira ili kuweza kupata malighafi katika kiwanda chetu cha General Tyre. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia pia mambo ya miundombinu. Madaraja yote Tanzania watu wanapita bure, lakini daraja la Kigamboni kuna tozo, watu wanatozwa pale. Wanatozwa kwa sababu NSSF pia imeshiriki ujenzi wa daraja lile. Sasa naishauri Serikali, ni muda mrefu sana sasa lile daraja watu hata ukiwaelezea wanaona limekaa kibiashara zaidi. Walielewa na matarajio ya wananchi wengi ni kwamba Daraja la kigamboni litakuwa kama lilivyokuwa Ruvu, daraja la Mkapa na Daraja la Kilombero watavuka bure. Sasa liko kibiashara zaidi, linawakwaza wananchi wa Mkoa Dar es Salaam hususan Wilaya mpya ya Kigamboni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa huruma yake, najua kuna deni kubwa NSSF wanadai, lakini tuwasaidie watu wa Kigamboni. Kama ni kulipa hilo deni, basi madaraja ya Mkapa na Kilombero nayo yatozwe ili kusaidia daraja la Kigamboni nao watu wapite bure kama madaraja mengine. Kwa sababu inaonekana sasa lile halifanyiwi service, ni daraja kama madaraja mengine. Pale linaonekana liko kibiashara zaidi, hata ukipita, utakuta Polisi wana SMG wanalinda yale maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuangalie, hii huduma tunayoitoa kwa wananchi wetu iwe sawa na huduma katika mikoa mingine. Najua NSSF wanadai, lakini watafute mbinu ambayo itasaidia sasa wananchi wa Kigamboni nao wapate faraja katika daraja lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Tanga. Nikinunua bidhaa kutoka Kariakoo nikipeleka kwetu Bumbuli nalipia tu usafiri, silipii chochote. Sasa Tanzania ni Muungano, ni nchi moja, angalau hata nikitoka Zanzibar, nikiingia Dar es Salaam, basi ushuru mdogo mdogo hata kama ni zawadi tuachiwe. Maana ukifika pale inaonekana ni nchi mbili tofauti, unadaiwa ushuru. Tufanye kama ninavyotoka hapa Tanga kwenda zangu Dar es Salaam nikiwa na bidhaa hata kama ni zawadi nilipie tu katika chombo cha usafiri, lakini siyo kulipia ushuru kama ilivyokuwa sasa na kuwapa nafuu ndugu zetu Wazanzibari na wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nami fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyokuwa mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda hautafikiwa ikiwa Serikali yenyewe ni kikwazo katika kufikia Tanzania ya viwanda. Nayasema haya kwa sababu mimi nipo katika Kamati ya Viwanda na Biashara, lakini kumekuwa na kusuasua kwa Hazina kupeleka fedha katika Wizara hii kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoishauri ni Serikali itenge fedha ya kutosha katika Wizara hii ili kuweza kufikia hiyo Tanzania ya viwanda. Tunaona takribani miaka mitatu mfululizo mpaka sasa hivi fedha inayotolewa ni kiwango cha chini sana na haikidhi. Licha ya kuwa ni kiwango cha chini, lakini pia haifiki kwa wakati. Kwa hiyo, naishauri Serikali, fedha ambayo inatengwa katika Bunge hili la bajeti ifike kwa wakati ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wale wamiliki wa viwanda ambavyo vinatumia sukari ya viwandani. Wamiliki wale wanadai fedha nyingi sana, kwa sababu waingizapo sukari hiyo huwa wanatozwa asilimia 15, lakini mpaka sasa hivi wafanya biashara hao wakubwa wanaidai Serikali shilingi bilioni 43. Hadi sasa hivi ni shilingi bilioni sita tu ambazo wamelipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshangaa, wakati wanailipa ile asilimia 15 wale wafanyabiashara walikuwa wanalipa hela cash na ile fedha yao ni ya kuweka ili watakapomaliza kuitumia ile sukari watatoa taarifa yao na kurudishwa, lakini wanaporudishiwa wanarudishiwa kidogo kidogo. Sasa naiuliza Serikali, ni kwa nini, wakati wale wafanyabiashara wanalipa cash na hawalipi kidogo kidogo? Mpaka sasa hivi ni mwaka wa nne huu kumekuwa na kusuasua kwa ulipaji wa hiyo fedha. Naishauri Serikali, ili ifikie Tanzania ya viwanda iwasaidie wananchi, iwasaidie hawa wafanyabiashara kulipa fedha hiyo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimdanganye Mheshimiwa Rais, Rais anataka Tanzania ifikie katika uchumi wa viwanda na ili kumsaidia, Wizara kama Wizara pamoja na Mheshimiwa Waziri ni kumpa ushirikiano. Wale wenye viwanda wanalalamika mpaka sasa hivi fedha zao wanadai ni mwaka wa nne, wamendika barua nyingi na mpaka sasa hivi fedha zao hawajarudishiwa. Shilingi bilioni 43 mpaka sasa ni mwaka wa nne wamelipwa shilingi bilioni sita na hizo shilingi bilioni sita siyo kwa mfanyabiashara mmoja, kila mtu amelipwa kidogo kidogo. Mwingine shilingi bilioni moja, mwingine bilioni mbili. Kwa hiyo, Serikali yenyewe inakwamisha hii Tanzania kufikia uchumi wa viwanda. Naishauri Serikali iwalipe fedha zao kwa wakati kwa sababu ule ni mtaji wao na ni haki yao kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiyti, kingine ni kwamba viwanda vilibinafsishwa miaka ya 1990 na viwanda vile wakati vinabinafsishwa nia na madhumuni ni kuviendeleza na kuweza kuwapatia ajira wananchi wetu na pia kupata pato la Taifa, lakini kuna wenye viwanda waliomilikishwa, wamechukua viwanda vile na kwenda kukopa fedha na kufanyia miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati, tuliomba kuundwe Tume Maalum, kwa sababu, sisi kama Kamati tuliomba tutembelee vile viwanda kuangalia makaratasi, kuwaambia kwamba viwanda vilivyobinafishwa vingine vinafanya kazi vizuri, vingine vimefungwa, vingine vimeuza mitambo yao; lakini haitasaidia endapo sisi wenyewe kama Kamati hatutakwenda kwenye eneo husika na kujua hali halisi. Tumeomba kuvitembelea mpaka sasa hivi, hatujapata nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ili kufuatilia viwanda vilivyobinafsishwa na viweze kufanya kazi sawa sawa iundwe Tume Maalum ambayo itasaidia kufuatilia vile viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kuviangalia kama kweli vinafanya kazi kwa kusuasua na kama vingine havifanyi kazi kabisa ili wapewe wawekezaji wengine ambao wataweza kuviendeleza na kusababisha uzalishaji uwe mwingi na ajira ipatikane kwa wananchi wetu na pia kulipa kodi. Kwa sababu tunajua kuna maeneo mengi kuna viwanda ambavyo vilikuwa ninafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 1985 nilikuwa nasoma Shule ya Sekondari Morogoro, Form One; mwaka ule ukifika Morogoro viwanda vilikuwa vingi, unapata ajira mara moja, lakini ni vigumu sana kupata eneo la kuishi. Kulikuwa na viwanda vya Canvas, Ceramic, Polyster, Moro Shoe, vilikuwa vingi sana lakini viwanda vile vimekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, wakati Serikali inatafuta wawekezaji kwenda kukata mapori na kuanzisha viwanda vingine kwanza vifuatiwe vile viwanda kwa sababu maeneo yapo, majengo yapo kinachotakiwa ni kubadilisha tu miundombinu iliyokuwepo pale na kiuweka ya kisasa ili kuweza kuleta uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ulipishwaji wa kodi kwa wafanyabiashara kabla ya kuanza kufanya biashara. Tumewaona wafanyabiashara wengi ambao wanataka kuanzisha biashara zao hususan mijini kwenye maduka, kwanza ili wapate leseni ni lazima wakalipe mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, itoe muda maalum ambao utamsababisha yule mfanyabiashara anapotaka leseni, natolea mfano kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ukitaka kufungua duka lako unakwenda pale Anatoglo (Mnazi mmoja) unataka leseni, hawakupatii leseni wanakwambia kwanza nenda summit tower pale makutano ya Lumumba na Uhuru ili kuweza kupatiwa tax clearance na hiyo tax clearance huwezi kupewa mpaka utoe mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, mimi biashara ndiyo nakwenda kufanya au mfanyabiashara anataka aanze biashara, unamkadiria mapato; hayo mapato ameuza kitu gani? Hii ndiyo inakwamisha wananchi. Inakwamisha wafanyabiashara kushindwa kuendelea baada ya mwaka mmoja hufunga maduka yao na kuacha kwa sababu Serikali inatakiwa impe muda na kama imempa mashine ya EFD itatumia ile mashine kuweza kukadiria mapato na kuweza kumkadiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, mwananchi atakapofungua biashara kwanza apewe muda maalum angalau miezi mitatu ndipo aanze kulipa mapato, lakini kitendo kinachofanywa na Serikali sasa hivi kupitia TRA kuanza kumpa mtu makato kabla ya kufanya biashara, kusema kweli ni kitendo cha dhuluma na hiki hupelekea wafanyabiashara wengi kufunga maduka yao hususan maeneo ya mijini ninayozungumzia ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia biashara zinazofanywa, wanaolipa kodi ni wachache. Kuna kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais inasema “ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti”, lakini sasa hivi ukifika Mkoa wa Dar es Salaam kuna wafanyabiashara. Hatuwakatai kwamba ni wafanyabiashara ndogo ndogo nao wana wajibu wa kufanya baishara, lakini wanauza mbele ya maduka ambayo wanalipa kodi. Wafanyabiashara wale hawalipi kodi yoyote kwa Serikali na ukiuliza unaambiwa ni wapigakura wetu. Tunaisaidia Serikali au tunaangamiza Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni na madhumuni ni kupata kodi; na kama umempa kitambulisho cha shilingi 20,000/= basi tuwatafutie maeneo maalum. Kwa sababu tendency ya Mwafrika, tendency ya Mtanzania anaona biashara inayouzwa barabarani ni rahisi mno kulikoni ya madukani; na hii ndiyo maana inapelekea wafanyabiashara wengi wanafunga maduka yao kwa sababu hata kama ukiuza wanaona barabarani ndiyo rahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawe mwenyewe ukipita maeneo ya Kariakoo utaona msongamano mkubwa kwenye barabara. Hata barabara ya Msimbazi ni vigumu kupita watu, wafanyabiashara wamepanga biashara zao mpaka milangoni mwa maduka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali itenge maeneo maalum kwa wale wafanyabiashara wanaolipa kodi ili waweze kuwa na uwezo sasa wa kuuza na kuweza kulipa kodi na ikifikia mwisho wa mwaka wasiweze kufungiwa maduka yao. Wale wanaoambiwa kwamba wao ni wapiga kura hawatakiwi kulipa kodi ni kitambulisho tu ambacho kinamwidhinisha afanye biashara, basi watengewe maeneo yao. Naishauri Serikali ifuatilie jambo hili ili kuweza kuwa na mapato zaidi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishauri Serikali itumie malighafi inayopatikana katika viwanda vyetu. Malighafi hiyo itasaidia kukuza kilimo chetu ambacho kitapelekea wananchi kupata kipato na kulima zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara ya Viwanda na Biashara, watendaji wengi wamekaimishwa. Naishauri Serikali sasa ijaze zile nafazi zilizokaimishwa ili wale Watendaji wawe na nafasi ya kuweza kutoa maamuzi yao katika kuendeleza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kipindi cha Januari, 2017 mpaka Januari, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu. Ili kutekeleza kwa vitendo Maoni na Mapendekezo ya Kamati, Serikali itoe bajeti ya kutosha ili itumike kwa muda sahihi kuweza kutekeleza mambo yote yanayojadiliwa na kupendekezwa katika Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge na iboreshe maghala ili kuweza kuhifadhi mazao ya nafaka sehemu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iongeze viwanda vya pembejeo za kilimo, madawa na mbolea nchini ili wakulima waweze kupata zana hizo kwa wakati na kuvitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kutoharibu vifaa vya uvuvi mfano ngalawa ambazo si zana haramu katika uvuvi; hivyo visiharibiwe.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa taarifa yake nzuri ya kipindi cha Februari, 2017 hadi Januari, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto hususan katika Kikosi cha Zimamoto kilichopo Mkoa wa Dar es Salaam kinawalazimisha wafanyabiashara waliopo karibuni Wilaya ya Ilala kununua mitungi ya gesi (Fire extinguish) kwa lazima na kuiweka ndani ya duka la kila mfanyabiashara. Mfanyabiashara asipotekeleza hutozwa faini, badala ya mmiliki wa nyumba kununua mitungi hiyo na kuiweka pembezoni mwa jengo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza je, ikiwa moto utatokea usiku na wakati huo mfanyabiashara ameshafunga duka, amelala nyumbani kwake, je mtungi huo uliopo ndani ya duka utamsaidiaje mfanyabiashara kuokoa mali zake? Je, hatuoni kuwa huu ni mradi maalum wa Kikosi cha Zimamoto na siyo kulinda mali za wafanyabiashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu wafanyabiashara hao wanaelemewa na milolongo ya kodi nyingi na wakati mwingine kushindwa kuendesha biashara zake na kupelekea kufunga duka. Naomba Wizara husika isaidie kuondoa kero hii na kiuhalisia haina tija yoyote kwa mfanyabiashara ambaye anachangia pato la Taifa kwa kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufinyu wa fedha hupelekea msongamano wa wafungwa magerezani na pia kuna uchakavu wa majengo ya Balozi za Tanzania. Naomba Serikali itenge fedha za kutosha na kwa wakati ili kupeleka katika Wizara husika kuondoa tatizo hilo. Mwisho nakupongeza Mheshimiwa wa Kamati Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu kwa taarifa yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Mbunge) pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mbunge) kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iondoe malipo katika hospitali za Serikali kwa maiti ambazo zimehifadhi wa katika vyumba vya kuhifadhia maiti kwa kuwa wakati wa uhai wao walikuwa wanachangia Pato la Taifa kwa kulipa kodi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wote walio chini ya miaka mitano wapate huduma za afya bure kama ilivyo kwa wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa za ugonjwa wa saratani ni ghali mno, hivyo nashauri Serikali ipunguze bei ya dawa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa wale wagonjwa wasio na uwezo wa matibabu ya moyo hususani watoto, Serikali iweze kugharamia matibabu hayo. Kuna baadhi ya chanjo za watoto ambazo wakati wanachanjwa huwaletea homa kali sana. Nashauri Serikali ifanye maboresho kwa chanjo hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano waendapo kliniki kuchunguzwa afya zao nashauri Serikali itoe vyakula vya lishe kama ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya usafishaji figo ni gharama sana. Hivyo naishauri Serikali ipunguze gharama za tiba hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iweke stand by generators katika hospitali zote za Wilaya ili kuweza kusaidia wagonjwa na wauguzi umeme unapokatika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali nyingi majengo yake ni chakavu, ukarabati ufanyike katika hospitali hizo, naishauri Serikali iweke nyavu za kuzuia mbu katika wodi za Hospitali ya Muhimbili na ukarabati wa vyoo na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iboreshe miundombinu ya hospitali zetu hususani upatikanaji wa huduma ya maji katika hospitali zetu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, madaktari na wauguzi waongezwe mishahara na posho ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kuondoa tatizo la rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iboreshe kambi za wazee, kujenga/kukarabati nyumba zao, chakula cha kutosha na kuwapatia vifaa muhimu katika kambi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, namuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu Waheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Waziri) na Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Naibu Waziri) ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika Wizara hii ambayo kimsingi
ni tegemeo la Watanzania wote hususani katika masuala ya afya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naipongeza hotuba nzuri iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, naipongeza Serikali, ila nashauri kutokana na Hospitali ya Rufaa Muhimbili iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam kupokea wagonjwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na wengi wa wagonjwa hawana ndugu Mkoa wa Dar es Salaam hivyo, naishauri Serikali ijenge eneo maalum ambalo litawasaidia ndugu waletao wagonjwa wao kuweza kukaa na kutoa huduma za dharura ambazo wauguzi hawawezi kuzifanya na itasaidia ndugu wa mgonjwa kufuatilia maendeleo ya mgonjwa wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itafute eneo lingine la kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro maana chumba cha kuhifadhia maiti kipo karibu na Shule ya Sekondari Morogoro, hivyo kusababisha ndugu wa wafiwa wanapokuja kuchukua maiti wao hulia na kelele hizo za vilio zinasababisha wanafunzi waliopo madarasani kukosa usikivu wa kufuatilia masomo wawapo darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za kiuchumi, barabara zote za lami nchini zilizojengwa chini ya kiwango, mfano barabara ya Chalinze hadi Mlandizi, zifanyiwe ukarabati ili kuepusha ajali za barabarani. Barabara zilizojengwa pembezoni mwa milima, mfano Milima ya Usambara katika Mkoa wa Tanga zijengewe pavements au uoto ambao utazuia mmomonyoko wa ardhi, hususan kipindi cha mvua ambayo uharibu barabara hizo na kutopitika kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba njia ya reli ya Dar es Salaam – Tanga ikarabatiwe ili iweze kupitika na kuweza kusaidia usafirishaji wa mizigo na abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kutafuta njia mbadala ya msongamano wa magari eneo la mizani, hususan Vigwaza Mkoa wa Pwani, ukizingatia magari ya abiria yanatembea kwa ratiba maalum hivyo, husababisha usumbufu na abiria pia, hupata usumbufu kwa kusafiri kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iboreshe viwanja vya ndege. Mfano uwanja wa ndege uliopo Mkoa wa Morogoro wakati wa usiku haufanyi kazi kutokana na ukosefu wa taa uwanjani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta za uzalishaji; kilimo, wakulima wahamasishwe kulima mazao ambayo yatatumika kama malighafi katika viwanda vilivyopo nchini, mfano, kilimo cha alizeti, tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda, viwanda vipya vinavyojengwa vijengwe nje, mbali na makazi ya watu. Viwanda vinavyojengwa viwe ambavyo malighafi zake zinapatikana hapa nchini ili wakulima wetu wapate soko la kuuza bidhaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara, wafanyabiashara wakadiriwe na Mamlaka ya Mapato (TRA), kulingana na biashara wanayoifanya na si eneo wanalofanyia biashara. Mfano, maeneo ya Kariakoo katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyabiashara wanakadiriwa kutokana na eneo. Pia, wafanyabiashara wakati wanaanzisha biashara zao wapewe muda maalum (Grace Period) angalau wa miezi mitatu kisha ndio wafanyiwe makadirio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu; maslahi ya Walimu yaboreshwe ili wawe na utulivu wanapofundisha. Madarasa yaongezwe kuepuka msongamano wa wanafunzi katika shule zetu. Wanafunzi wapatiwe angalau mlo mmoja kwa siku wawapo shuleni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, pamoja na Naibu Mawaziri wake kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iondoe tozo, malipo kwa wananchi wa Kigamboni wanaotumia vyombo vya moto kupita katika Daraja la Kigamboni (Daraja la Nyerere), ni ghali mno na kipato cha Watanzania na hali ya uchumi ni ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakandarasi wanaojenga barabara za lami chini ya kiwango wawajibike kuzikarabati zitakapoharibika kabla ya muda maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iondoe msongamano katika mizani iliyopo Vigwaza, Mikese na Morogoro. Kwa magari ya abiria (mabasi) yawe na eneo maalum la kupima uzito maana mabasi mara nyingi huenda kwa ratiba maalum, abiria wengine ni wagonjwa, watoto na mabasi hutumia muda mwingi katika mizani hiyo. Pia nashauri barabara zote zilizopo pembezoni mwa milima zijengewe pavements ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi na ili zisiharibu miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya Dar es Salaam hadi Tanga ifufuliwe ili kuweza kusaidia mizigo mizito hususani malori kutumia reli ili kuepuka uharibifu wa barabara. Katika barabara kuu zijengwe kalvati ambazo zitakuwa na uwezo wa kuhimili wingi wa maji kipindi cha mvua za masika ili kuepuka maji kupita juu ya barabara na kuharibu miundumbinu. Mfano, barabara ya Dodoma - Morogoro eneo la Mbande hadi Kibaigwa ni eneo korofi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wa ndege wa Morogoro ambao upo maeneo ya Kihonda Bima, uwanja ule uboreshwe ili ndege ziweze kutua usiku na mchana na ukizingatia Morogoro kuna Mbuga za Wanyama za Mikumi na Selous ambazo ni vivutio vikubwa vya watalii, kwa kutumia uwanja huo tutaweza kuwavutia watalii wengi kuja Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itoe fedha kwa wakati ili kuwezesha Wizara kufanya kazi kwa muda uliopangwa kujenga miundombinu ya nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZAINABU M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu nashauri Serikali iwekeze katika mchezo wa mpira wa miguu pia isisahau kuwekeza katika michezo mingine ambayo tayari imeshiriki katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu na imesajiliwa, kufuata taratibu zote za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Roll Ball – Timu hii ya mchezo wa Roll Ball imeshindwa kushiriki kwenda kuwakilisha nchi katika nchi ya Kenya kwa sababu ya kukosa wadhamini. Hivyo Serikali ione haja ya kusaidia mchezo huu ambao utasaidia kuleta ajira pia kusaidia nchi kujitangaza Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu itolewe kwa wasanii wetu hususan wanaoimba muziki wa kizazi kipya, kuweza kutunga na kuimba nyimbo zenye maadili yanayoendana na utamaduni wa nchi yetu. Serikali itunge sheria ya kudhibiti vijana ambao wanavaa nguo fupi (nusu uchi) ambazo haziendani na maadili yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali, iweke mkakati maalum wa kuhamasisha michezo mashuleni, kuanzia shule za awali, shule za msingi, sekondari hadi katika vyuo ili kuweza kuibua vipaji kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Taifa upo katika Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo pindi mechi zinapochezwa katika uwanja huo wananchi wa Wilaya ya Temeke hawafaidiki na fedha zinazopatikana katika viingilio. Hivyo naishauri Serikali kwa kushirikiana na TFF iweze kutoa kiasi cha fedha kwa Wilaya ya Temeke ambayo itasaidia katika kuboresha miundombinu na shughuli nyingine za kijamii katika Wilaya hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mungu awape afya njema Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake ili kuweza kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wanafunzi wawe na ufaulu wa kiwango cha juu ni lazima Serikali ifanye yafuatayo:-

(i) Iboreshe na iwaongezee walimu mishahara na posho;

(ii) Iwapandishe madaraja wale waliofundisha zaidi ya miaka mitatu;

(iii) Ijenge madarasa ya kutosha na maktaba pamoja na maabara katika shule za sekondari na shule za msingi;

(iv) Ijenge nyumba bora za walimu na ni muhimu ziwe na umeme ili walimu waweze kuandaa maazimio na maandalio ya kazi kwa masomo ambayo watayafundisha siku inayofuata darasani;

(v) Isajili shule za awali (chekechea) ili kuweza kutambulika kisheria. Pia itengeneze mitaala kwa shule hizi na ziwe na miundombinu inayolingana na uhitaji wa watoto hao wa chekechea;

(vi) Ipeleke mashuleni vitabu vya kiada na ziada kwa wakati;

(vii) Itengeneze mitaala ya sekondari inayomuandaa kijana/mwanafunzi kujiajiri. Mfano kuwe na masomo ya needle work, cookery, wood work, metal work, fine arts na kadhalika kama ilivyokuwa zamani katika shule mfano Morogoro sekondari.

(viii) Iwe na mtaala wa michezo ili kuweza kukuza vipaji kwa wanafunzi wetu;

(ix) Ijenge ofisi za walimu na kuweka samani katika ofisi hizo ili walimu waweze kuzitumia katika shughuli za kiofisi;

(x) Ijenge vyoo vya walimu na wanafunzi katika shule zetu. Mfano, katika Shule ya Msingi Yombo Dovya iliyopo Kata ya Makangarawe, Wilaya ya Temeke hakuna matundu ya vyoo vya kutosha; na

(xi) Iandae angalau mlo mmoja kwa siku katika shule zetu ili kusaidia wanafunzi waweze kuhamasika kuhudhuria masomo. Pia kupata mlo ambao utawasaidia kuwa na afya njema na kuelewa vyema masomo yao maana mwanafunzi akiwa na njaa hafundishiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namtakia Waziri wa Elimu na Naibu wake afya njema na Mwenyezi Mungu awape umri mrefu ili waweze kuyatekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa afya njema Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Engineer Isack Aloyce Kamwelwe (Mbunge), pamoja na Naibu Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mbunge). Pia nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii.

Kutokana na upatikanaji wa visima virefu maeneo ya Kimbiji, Dar es Salaam hivyo naishauri Serikali katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 itenge fedha kwa ajili ya kusambaza maji hayo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam. Wakulima wengi wa mboga mboga Mkoani Dar es Salaam wanatumia maji ambayo si safi na si salama kwa umwagiliaji. Hivyo naishauri Serikali iwawezeshe wakulima hao wachimbe visima virefu kwa ajili ya kupata maji safi na salama ya kumwagilia mboga zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali isimamie vya kutosha malalamiko ya wananchi wanaobambikiziwa bili hewa za maji ili haki iweze kutendeka. Naishauri Serikali iboreshe miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam katika maji taka. Kwa kuwa wakati wa mvua septic tanks zinafumuka na kumwaga maji machafu yenye vinyesi ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, mfano katika Milima ya Uluguru, Morogoro. Naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu jinsi ya kuvuna maji ya mvua na jinsi ya kuyahifadhi kwa sababu wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iweke chujio la maji madhubuti katika Bwawa la Mindu lililopo Mkoani Morogoro kwa kuwa wakati mwingine maji huwa na uchafu wa rangi ya kijani. Pia yawekewe dawa ya kusafisha maji kwa sababu wakati mwingine yanakuwa na harufu ya samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji zipelekwe kwa wakati katika eneo husika ili kuweza kuondoa matatizo ya upatikanaji wa maji katika nchi yetu. Naishauri Serikali wakandarasi ambao wameonesha kiwango cha chini cha utekelezaji wa miradi ya maji wachukuliwe hatua za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nawatakia afya njema na umri mrefu ili kuyatekeleza majukumu yenu ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa afya njema ili na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Pili napenda kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia na tatu, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake pamoja na Naibu wake na pongezi nyingi ziende kwa Kamati ambayo imetoa maoni, naomba Serikali izingatie maoni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuja na mpango wa elimu bure, lakini haikuwa na maandalizi ya kutosha. Wazazi na Taifa likahamasika kupeleka wanafunzi mashuleni, lakini katika shule zile madarasa na madawati ni machache. Serikali ikajitahidi kufanya harambee kwa taasisi mbalimbali pamoja na wadau kuleta madawati, lakini ilikuwa haifikirii kwamba yale madawati yanaenda kuwekwa wapi. Matokeo yake wanafunzi wakawa wengi kuliko madarasa yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta darasa moja kuna wanafunzi 100 mpaka 120 na natolea mfano hivi karibuni nilienda katika shule ya msingi Ungindoni iliyopo Kata ya Mjimwema, Wilaya ya Kigamboni, wanafunzi wanakaa zaidi ya 120 kiasi kwamba mwalimu anashindwa kumsaidia yule ambaye ni slow learner ili aweze kufaulu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatakiwa ijipange, isilaumu walimu kwamba hawafundishi ndiyo maana watoto wanafeli. Kuwaadhibu walimu kwa kufeli kwa watoto wetu kwa kweli wanawaonea. Kama Serikali ingekuwa ina-provide incentives zote kwa walimu, mishahara mizuri, mazingira mazuri ya kufundishia, nyumba bora na mishahara ya walimu inatakiwa iongezwe kwa kiwango cha juu ili walimu waweze kuvutiwa na fani hii. Tunaona tuna ukosefu mkubwa wa walimu kutokana na wengi hawapendi kujifunza fani hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke sote sisi tumepita kwa walimu, madaktari wamepita kwa walimu, wanasheria wamepita kwa walimu lakini walimu wamefanywa kuwa madaraja kwa taaluma nyingine, hatuwajali. Mheshimiwa Ndalichako mama yangu nakuomba sana, wewe umepitia kwa walimu mpaka umekuwa Profesa, wasaidie walimu hawa katika kuboresha maslahi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai yao sasa hivi imekuwa kama ni wimbo wa Taifa maana yanaandikwa kwenye vitabu hayatekelezwi. Mimi naona sasa imekuwa mgomo baridi kwa wao kutojituma ili kuleta ufaulu wa hali ya juu. Shule za private zinafaulisha kwa sababu utakuta mwalimu anatoka Serikalini anakwenda kufundisha private kwa sababu ya incentive anazopata, mshahara na mazingira mazuri, kwa nini Serikali haioni haja basi na sisi kuboresha mazingira ya walimu wetu katika shule hizi za Serikali? Kwa nini sisi ambao tumepitia kwa walimu tunadharau walimu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, nakuomba mama yangu umepitia kwa mwalimu mpaka umefikia hatua hii na angalia yule mwalimu uliyemuacha kule kijijini ulikosoma hali yake ilivyo. Nakuomba tuwaboreshee maslahi yao ili walimu hawa waweze kufanya kazi zao sawasawa ili kusaidia wanafunzi wetu kuweza kufaulu kwa kiwango cha juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea shule ya msingi Yombo Dovya iliyopo Kata ya Makangarawe, Wilaya ya Temeke, shule ile kwa kweli ni mtihani. Ina wanafunzi walemavu na wa kawaida, madarasa hayatoshi. Nimejitolea pale tani moja ya mifuko ya saruji na mabati 20 lakini pia hayakidhi mahitaji. Vyoo ni vichache, walimu wanangojea wanafunzi wakajiasaidie na wao waingie katika vyoo vilevile, ofisi za walimu hawana meza za kutosha, wanatumia madawati kama meza zao, huwezi kujua kama hili ni darasa au ni ofisi ya walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwajali walimu wetu, hii ndio source ya kushuka kwa elimu yetu. Tusiwaadhibu walimu wala shule zile kuzifungia, sisi Serikali ndio wenye matatizo. Serikali inatakiwa ku-provide kila kitu ili walimu waweze kufanya kazi kwa bidii na kujituma.
Nadhani tukifanya kila kitu wanafunzi wetu watafaulu kwa kiwango cha juu na hatuwezi kumtafuta mchawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwafukuza walimu kwamba hawajafaulisha tunawaonea. Kuwasimamisha au kufungia shule kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe mimi siafiki, kwa sababu mwalimu hawezi kujenga darasa wala maabara, kwa nini unamuadhibu kwamba kasababisha wanafunzi wafeli. Inayotakiwa iadhibiwe ni Serikali ambayo haijaweka mazingira rafiki ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana pindi tutakapopitisha bajeti yako Mheshimiwa Waziri uwajali sana walimu ndio kila kitu, bila walimu sisi tusingefika hapa, bila walimu wewe Mheshimiwa Waziri usingekuwa Profesa.

Kwa hiyo, haya ya kujenga maabara, ukanunue vitabu bila kumwezesha mwalimu huwezi kumlazimisha ng’ombe kunywa maji kama hataki kunywa maji. Utamwekea mazingira, lakini kama mshahara yake hujamboreshea, hujamwekea nyumba bora zenye umeme, anafanya andalio la somo na azimio la kazi kwenye giza hawezi kufanya kazi vizuri. Ndiyo maana wengi hawataki kukaa vijijini wanakimbilia mjini angalau kufanya biashara huku wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa tueleze una msimamo gani kwa walimu wetu wa Tanzania kuwaboreshea maslahi yao ambayo yataleta ufaulu wa juu kwa shule zetu. Kwa sababu ukisema uwafukuze walimu unawaonea, ufungie shule zile pia unazionea kwa sababu hawana uwezo. Hata wewe mshahara wako huwezi ukasema ukajenge maabara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ishauri Serikali na Rais walimu ndiyo kila kitu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ZAINABU M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuumba sisi kuwa wanadamu kisha akatupa akili na ufahamu ili kuweza kujadili mambo mbalimbali kuhusu Taifa letu. Pili, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ni kitovu cha biashara katika nchi yetu na wafanyabiashara wa Dar es Salaam huchangia pato kubwa katika Taifa hili lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi sana. Ili uanzishe biashara kuna taratibu za kufuata hadi biashara yako ifunguliwe, kwanza lazima upate leseni, lakini kinachotokea kwa wafanyabiashara hao wanaanza kulipa mapato kabla ya kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawaumiza sana wafanyabiashara. TRA wanakadiria watu mapato kulingana na eneo analilopo na siyo biashara wanayoifanya. Wanapoenda kudai leseni wanaambiwa kwanza waende TRA wakakadiriwe mapato, nauliza inawezekanaje mtu hajaanza kufanya biashara anakadiriwa mapato, kauza nini huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali Taasisi ya Mamlaka ya TRA itoe grace period kwa wafanyabiashara. Wakati wanataka kuanzisha biashara zao kwanza wapewe leseni, pia wapewe muda wa kufanya biashara hiyo angalau miezi mitatu wakati wanatumia mashine za EFD kisha ndiyo wakadiriwe. Kitendo kinachofanywa na TRA kuwakadiria watu mapato kabla ya biashara kwa kweli, kinawaumiza sana wafanyabiashara, hususan wa Jiji hili la Dar-es-Salaam. Naomba sana Serikali ilichukue hili na ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishauri Serikali wale ndugu zetu wafanyabiashara ndogondogo Wamachinga ni wafanyabiashara pia lakini watengewe maeneo maalum. Sasa hivi ukifika katikati ya Kariakoo maeneo ya Narung’ombe, Kongo, Mchikichi, wafanyabiashara ndogondogo wameweka bidhaa zao mbele ya maduka ya wafanyabiashara ambao wanalipa kodi kihalali. Kutokana na buyer behavior ya watu wetu wa Tanzania wenye kipato cha chini kuona kwamba biashara zilizokuwa barabarani ni rahisi kuliko za ndani hupelekea watu wenye maduka kushindwa kufanya biashara zao vizuri na Taifa kukosa mapato kutokana na kwamba wafanyabiashara wale wanaosambaza barabarani kutolipa mapato ya aina yoyote.

Kwa hiyo, naishauri Serikali itenge maeneo maalum kwa ajili ya Wamachinga ili nao waweze kufanya biashara pia walipe kodi kwa Taifa letu. Najua kwamba Machinga ni wapiga kura pia wafanyabiashara wa madukani ni wapiga kura wa Taifa hili, kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine sasa hivi kumetokea mtindo kwa Kikosi cha Zimamoto kupita katika maduka ya wafanyabiashara Kariakoo kuwalazimisha waweke fire extinguisher ndani ya maduka. Fire extinguisher ina kilo 5 na kila mtungi mmoja ni Sh.200,000 na kila mwisho wa mwaka ulipe Sh.40,000 unaweka ndani ya duka, je, moto ukitokea saa 8.00 za usiku wakati mfanyabiashara huyo yuko nyumbani kwake ile fire extinguisher itamsaidia nini kuokoa mali zake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni dhahiri kwamba Kikosi cha Zimamoto kimeanzisha mradi mwingine kwa wafanyabiashara ili kuwakandamiza. Naishauri Serikali ikutane na Kikosi cha Zimamoto, iwashauri wale wamiliki wa majengo waweke fire extinguisher kwenye corridors za nyumba na siyo ndani ya maduka ya wafanyabiashara, kwa sababu huwezi kujua moto utatokea wakati gani. Ni bora fire extinguisher ziwekwe kwenye corridor kuliko ndani ya maduka ya wafanyabiashara, hii itasaidia moto ukitokea wakati wowote aidha, asubuhi, mchana hata usiku kuweza kutumia fire extinguisher kuzima moto ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuelekea Tanzania ya Viwanda kuna viwanda vingi ambavyo vimepewa wawekezaji. Nitatolea mfano Kiwanda cha Nguo cha Karibu Textiles Mills ambacho kiko Wilaya ya Temeke. Kwa sasa hivi kiwanda kile kimefungwa na kimegeuzwa kuwa ghala la kuhifadhia soda. Nimetembelea mwezi uliopita pale wameweka soda na kiwanda kile kilikuwa kinazalisha nguo, vitenge, khanga pia mashuka na kilikuwa kinaleta ajira kwa zaidi ya watu 1,000. Kwa sasa hivi Mheshimiwa Waziri kimegeuka kuwa ghala la kuhifadhia soda na hakuna kiwanda tena pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, wakati tunaelekea Tanzania ya Viwanda badala ya kutafuta maeneo ya kuanzisha viwanda vingine ni bora kwanza tuvifufue vile viwanda ambavyo vimepewa wawekezaji. Maeneo mengi yalikuwa na viwanda, nitakutolea mfano Mkoa wa Morogoro, mwaka wa 1980 ulikuwa ukifika Morogoro unaweza kupata ajira mapema kuliko kupata chumba cha kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna Kiwanda cha Canvas Mill, Ceramics, Polyester, Moro Shoe, Tanneries, Magunia, Kiwanda cha Tumbaku, Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Kiwanda cha Sukari Kilombero, vyote hivi vilikuwa Mkoa wa Morogoro, lakini kwa sasa hivi viwanda vile wamepewa wawekezaji na haviendelezwi. Morogoro ni katikati ya Dar es Salaam na Dodoma, viwanda vile vifufuliwe na kupewa wawekezaji na kusimamiwa vizuri, iwe ni sampling area. Sasa hivi tunajenga treni ya mwendokasi ambayo itarahisisha watu kufika kwa urahisi Morogoro, italeta ajira kwa watu wa Morogoro, Mkoa wa Pwani pia wa Dodoma wanaweza kupata ajira katika Mkoa wa Morogoro. Badala ya kutafuta maeneo ya kwenda kuanzisha viwanda vingine ni bora tuvifufue viwanda vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona viwanda vingi pia Mkoa wa Tanga. Kilikuwepo Kiwanda cha Mbolea, Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Amboni, Kiwanda cha Gardenia na Mbuni, viwanda vile vyote vifufuliwe kuliko kwenda kuanzisha maeneo mengine mapya, ili viweze kutoa ajira kwa watu wetu. Mkoa wa Tanga unazalisha matunda mbalimbali lakini katika hotuba ya Mheshimiwa tunashauri, kuanzishwe Kiwanda cha Juice ambapo itasaidia wakulima kwenda kuuza matunda yao katika kiwanda kile, kuliko sasa hivi matunda ikifika msimu yanaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushauri Mheshimiwa sana wakati unaelekea kuanzisha viwanda vipya vile vya zamani visimamiwe kwa uhakika ili kuleta ajira na pato la Taifa letu. Naomba haya yazingatiwe kwani yatasaidia sana kuliendeleza Taifa letu kuliko kuanza kukata misitu huko na
kutafuta mashine za kufunga, tuboreshe mashine katika viwanda vya zamani ambavyo vitasaidia kuleta ajira kwa kwa wananchi wetu na pia kuchangia katika pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naomba maoni ya Kamati yazingatiwe ili kuelekea Tanzania ya Viwanda. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji chini ya Waziri Mheshimiwa Charles J. P. Mwijage, pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayofanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naishauri Serikali ifufue viwanda vilivyopewa wawekezaji mfano, Kiwanda cha Nguo cha Karibu Textile Mills (KTM) ili kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naishauri Serikali kupitia upya viwanda vilivyo katika Mkoa wa Morogoro, mfano Morogoro Shoes Company, Polyester, Magunia, Tannaies, Ceramic, Canvas, Moprocco ambapo katika miaka ya 1980 vilikuwa vinazalisha bidhaa mbalimbali, pia vilikuwa vinatoa ajira kwa Watanzania na pia kuongeza pato la Taifa letu. Hivyo wawezeshaji ambao wameshindwa kuviendeleza viwanda hivyo wapokonywe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali ijenge Kiwanda cha Matunda (juice) ili wakulima wa Mkoa wa Tanga waweze kuuza matunda katika kiwanda hicho. Hivyo ni muhimu Serikali ijenge kiwanda katika Mkoa wa Tanga kwa sababu Mkoa wa Tanga wananchi wake hulima kwa wingi matunda ya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, naishauri Serikali iishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iwakadirie wafanyabiashara mapato mara baada ya miezi mitatu (grace period) ndipo TRA wafanye makadirio ya mapato na siyo kuwakadiria kabla ya kuanza biashara. Hii hupelekea wafanyabiashara hao kushindwa kuendelea na biashara na kufunga na kulikosesha Taifa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, naishauri Serikali ikutane na watendaji wa taasisi ya Fair Competition Commission (FCC) ili iwashauri FCC watoe elimu kwanza kwa wafanyabiashara kabla hawajaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Siyo FCC kusubiri wafanyabiashara walete bidhaa kisha kuanza kuwatoza faini kubwa na mara nyingine kuziteketeza na kuwasababishia hasara kubwa wafanyabiashara hao na pia kulikosesha Taifa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, naishauri Serikali ionane na kikosi cha Zimamoto cha Mkoa wa Dar es Salaam ili kuondoa bugudha iliyopo, maana wafanyabisahara wanalazimishwa kununua fire extinguisher kilogramu tano kwa shilingi 200,000 kisha kila mwaka kulipia shilingi 40,000.

Mheshimiwa Mwenyekitik, ushauri wangu ni kwamba Zimamoto wawaelekeze wamiliki wa majengo ya biashara Dar es Salaam (Kariakoo), waweke fire extinguisher katika corridor za nyumba hizo na siyo ndani ya maduka, sababu moto ukiotokea usiku fire extinguisher limefungiwa ndani ya duka halitasaidia kuokoa mali za mfanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, naishauri Serikali itenge maeneo maalum kwa wafanyabishara ndogo ndogo (Wamachinga) wa Mkoa wa Dar es Salaam na siyo kuweka biashara zao mbele ya maduka ya wafanyabishara. Hii itasaidia Wamachinga kuweza kulipa pato la biashara zao, huduma za jiji, huduma za usafi kwa urahisi na kuweza kuliingizia pato Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawatakia kazi njema na Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu katika kuyaendea majukumu yenu ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein A. Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iongeze muda wa compulsory program kwa vijana wetu (mwaka mmoja), ili kuweza kuwajengea uwezo wa kujifunza mambo mbalimbali mfano; ujenzi, uashi, kilimo, ufugaji na kadhalika ili wamalizapo kuwa na uwezo wa kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwasaidie familia ya Wanajeshi wetu ambao mara nyingi hupoteza maisha wakiwa katika harakati za kulinda amani katika nchi za jirani mfano kuwasomesha watoto wa Marehemu, maana mara nyingi warithi wa familia hawawatendei haki watoto hao walioachwa na marehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuleta mahusiano mazuri baina ya wananchi na wanajeshi wetu, naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa Wanajeshi wetu wa Tanzania kutokuchukua sheria mikononi kwa wananchi wetu. Mara nyingi kuna matukio mengi yanatokea Wanajeshi kuwapiga wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iboreshe maslahi ya Wanajeshi wetu, mishahara iongezwe ili waweze kufanya kazi kwa weledi, pia wajengewe nyumba bora na kupatiwa usafiri wa kuwapeleka makazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iboreshe makambi yetu ya kujenga Taifa hususani Mahanga (bweni) na maofisi maana majengo mengi ni ya muda mrefu na chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwombea Mheshimiwa Waziri Dkt. Hussein Ally Mwinyi kila la kheri, afya njema na umri mrefu ili aweze kuwatumikia Watanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mhandishi Dkt. Charles John Tizeba (Mbunge), pamoja na Naibu wako Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa (Mbunge) kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Wizara hii ya Kilimo. Naishauri Serikali iongeze idadi ya wataalam mabwana shamba na mabibi shamba ili wawasaidie kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima wetu ili waweze kulima kilimo cha kisasa na chenye tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itoe mbolea na madawa kwa wakati ili iwasaidie wakulima kuweza kuitumia kwa wakati na kuweza kupata mazao bora na mengi kwa chakula na biashara. Serikali iwaruhusu wakulima waweze kuuza mazao nje ya nchi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na nchi. Naishauri Serikali iwasaidie na kuwawezesha wakulima walime mazao ambayo yatatumika kama malighafi katika viwanda vyetu na kuepuka kuagiza malighafi za viwanda vyetu kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iendeleze kilimo cha umwagiliaji katika Mikoa yote ya Tanzania ili kuweza kupata mazao mengi bila kutegemea mvua ambayo kwa wakati mwingine haina uhakika kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Naishauri Serikali skimu iliyopo Wami Dakawa iboreshwe ili kuweza kupata mpunga mwingi kwa kuboresha miundombinu yake ambayo ni ya muda mrefu. Pia kuongeza eneo kutoka hekari zilizopo 2,000 hadi 5,000 ili kuweza kuwapa fursa baadhi ya wakulima wapate eneo linalotumia kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwashirikishe wakulima katika upangaji wa bei ya mazao na siyo Serikali kutoa bei elekezi kwa wakulima ambayo wakati mwingine haina tija kwa wakulima kulingana na gharama walizotumia katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namuomba Mwenyezi Mungu Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako awape afya njema na umri mrefu ili muweze kuwatumikia Watanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nawapongeza Mheshimiwa Luhaga J. Mpina (Mb) Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Mheshimiwa Abdallah H. Ulega (Mb) kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali itilie mkazo katika sekta ya ufugaji wa nyuki, maana katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 Serikali haijaonesha mkakati wowote katika kuwasaidia wafugaji wa nyuki nchini mwetu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iwasaidie wavuvi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupata vyombo vya uvuvi vya kisasa ili waweze kuvua samaki wengi ambao watakidhi matumizi ya wananchi na viwanda vyetu maana kuna wakati mwingine katika Soko la Kimataifa lililopo Ferry (Kivukoni) Mkoa wa Dar es Salaam kunakuwa na uhaba mkubwa wa samaki.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali inunue meli kubwa ya uvuvi ambayo itakuwa na uwezo wa kwenda katika maeneo ya maji yenye kina kirefu na kuvua samaki wengi ambao watatumika na wananchi wa Dar es Salaam pamoja na viwanda vyetu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, asilimia kubwa ya wananchi waishio Mkoa wa Dar es Salaam hutumia kuku waliofugwa kisasa na hukua kwa wiki tatu hadi nne, pia hutumia na mayai ya kisasa. Kuna sintofahamu inayosemwa na baadhi ya watu kuwa nyama ya kuku hao pamoja na mayai yanayofugwa kisasa yana madhara kwa afya ya binadamu. Naishauri Serikali itoe kauli ili kuondoa sintofahamu ya kuwa kuku wa kisasa na mayai yana madhara kwa mlaji ili mfugaji aweze kutumia mbinu mbadala, ikibainika kuwa kuku hao na mayai yana madhara kwa afya ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iongeze ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea kozi (fani) za mifugo na uvuvi ili kuweza kupata wataalam wengi ambao watasaidia kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwamilikishe wafugaji ardhi ya kutosha kwa ajili ya malisho na kuweza kuchimba mabwawa kwa ajili ya wanyama (mifugo yao) ili kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima ambao inaendelea kuwepo hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali pindi mfugaji akilisha mifugo yake katika shamba la mkulima, Serikali isimamie (mfugaji)) aweze kulipa fidia kwa mkulima maana mazao hulimwa kufuata hali ya mvua. Hivyo fidia hiyo ilingane na mazao yaliyoliwa ili mkulima awe na uwezo wa kutumia fidia hiyo kuweza kununua mazao (nafaka) hiyo ili kumsaidia kwa matumizi ya familia yake.

Mheshimiwa Spika, mwisho namuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri Luhaga J. Mpina (Mb) na Naibu Waziri Abdallah H. Ulega (Mb) ili muweze kuyaendea majukumu yenu ya kila siku.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb) pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ijenge uzio wa senyenge katika hifadhi za mbuga zetu ambazo zinapakana na makazi ya wananchi ili kuepusha wanyamapori kutoingia katika makazi ya raia na kusababisha maafa hadi kupelekea kifo kwa wananchi. Pili, Serikali itafute matumizi ya mkaa mbadala ili kuepuka ukamataji wa mkaa unaotokana na misitu. Pia mkaa huo mbadala utaepusha wananchi kutokata miti hovyo na kuharibu misitu yetu na kupelekea ukame.

Tatu, naishauri Serikali iongeze vyuo ambavyo vitasaidia nchi kuweza kupata wataalam wa kutosha ili kusimamia maliasili yetu pamoja na kukuza utalii wetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali iboreshe kiwanja cha ndege kilichopo katika Mkoa wa Morogoro Mjini ili kuweza kutumika nyakati zote za usiku na mchana ili kuwasaidia watalii ambao watakuja kutembelea mbuga ya wanyama ya Mikumi National Park kufika kwa urahisi. Pia Serikali iboreshe miundombinu iliyopo ndani ya mbuga zetu za wanyama na ili kuweza kurahisisha watalii kufika maeneo mbalimbali ndani ya mbuga kwa urahisi katika vipindi vyote vya msimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali iongeze magari ya kisasa ambayo yatatumika ndani ya mbuga zetu mara tu watalii wanapotaka kwenda kuwaona wanyama na vivutio mbalimbali. Pia nashauri kuutangaza mlima wetu wa Kilimanjaro kama kivutio cha watalii hususan kwa watalii wa nje ya nchi. Ili kuepuka nchi ya Kenya kutangaza mlima Kilimanjaro kuwa upo nchini mwao.

Mheshimiwa Spika, mwisho namuomba Mwenyenzi Mungu awape afya njema na umri mrefu ili kuweza kuwatumikia Watanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchimba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa hotuba yake nzuri, lakini naomba kutoa ushauri kama ifuatavyo:-

(i) Serikali ifunge vifaa vya kudhibiti mwendo katika magari ya mizigo (malori) maana mara nyingi husababisha ajali.

(ii) Ili kuondoa sitofahamu kwa Watanzania, Kitengo cha Madawa ya Kulevya pindi wanapoteketeza madawa hayo mfano cocaine na heroine ioneshe hadharani kama wanavyoonesha bangi.

(iii) Serikali iharakishe upelelezi katika kesi zinazowakabili wananchi. Upelelezi uwe unafanywa kwa haraka ili kuepusha mlundikano wa kesi na mlundikano wa mahabusu katika magereza yetu.

(iv) Kikosi cha Zimamoto hususan Mkoa wa Dar es Salaam kimebuni mradi wa kuwauzia wafanyabiashara vifaa vya kuzimia moto (fire extinguishers). Hii hupelekea kuongezeka kwa utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wawaendee wenye nyumba (wamiliki wa majengo) wanununue fire extinguisher waweke katika corridors za majengo na siyo ndani ya maduka. Maana wakati mwingine moto hutokea nyakati za usiku wakati mmiliki wa duka yupo nyumbani amelala. Kwa hiyo, fire extinguisher haina msaada wowote maana ipo ndani ya maduka siyo nje katika corridor.

(v) Askari wa usalama barabarani (traffic) ni kero sana kwa watumiaji wa vyombo vya moto. Mara nyingi kuna makosa mengine askari wa usalama barabarani anapaswa kumwelimisha anayeendesha chombo cha moto na siyo kosa la kutoza faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi inaonesha kabisa wapo barabarani kuisaidia Serikali kukusanya mapato ya nchi na siyo kuelimisha jamii au madereva katika kulinda usalama wao na mali zao. Serikali itoe semina kwa askari wa usalama barabarani ili wawe na weledi na kujua majukumu yao na siyo kuleta kero kwa watumiaji wa vyombo vya moto.

(vi) Kuna baadhi ya askari wetu wamepandishwa vyeo lakini mishahara yao haijapandishwa. Suala la kupandishwa cheo kwa askari liende sambamba na kuongezwa mishahara.

(vii) Serikali ipunguze gharama za kupata passport ya Sh.150,000 maana ni ghali mno ukizingatia kipato au kima cha chini cha Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwombea Mheshimiwa Waziri kila la kheri na Mungu ampe umri mrefu na afya njema katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya tote ninampongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William V. Lukuvi pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Angelina S. Mabula, kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya wananchi hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam hununua nyumba maeneo ya makazi ya watu kisha kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo kwa kujenga karakana au viwanda vidogo. Naishauri Serikali iwachukulie hatua za kisheria wale wote wanaofanya ubadilishaji wa matumizi ya ardhi bila kuzingatia sheria zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ili kupata wataalam wa ardhi wa kutosha Serikali ifanye mpango mkakati wa kudahili wanafunzi wengi katika vyuo vyetu hapa nchini katika fani mbalimbali zihusuzo mambo ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itenge maeneo ya ardhi na kuwamilikisha kisheria wafugaji wote nchini na wakulima ili kuondoa migogoro ambayo hutokea mara kwa mara katika sehemu mbalimbali hapa nchini mwetu. Kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kuweza kujua sheria za ardhi na kupunguza migogoro katika sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kulipa fidia kwa wakati kwa wale wananchi ambao ardhi zao zimetwaliwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Walipe fidi hizo ili wananchii waweze kutumia fidia hiyo kuweza kutafuta maeneo mengine ya makazi au mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuharakisha upatikanaji wa hati miliki za ardhi na pia vibali vya ujenzi kwa haraka maana katika maeneo mengi kuna urasimu wa upatikanaji wa hati miliki na building permit huchukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kurasimisha pia maeneo yaliyojengwa kiholela (squatters) hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam; kwa mfano Manzese, Tandale na kadhalika ili wananchi waweze wapate hati ambazo zitawasaidia kuweza kupata mikopo benki na kuboresha nyumba zao, pamoja na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itoe fedha zilizotengwa katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 kwa wakati ili kuisaidia Wizara kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwomba Mungu awape afya njema na umri mrefu Mheshimiwa William
V. Lukuvi, pamoja na Naibu wako Mheshimiwa Angelina S. Mabula ili muweze kuwatumikia Watanzania katika Wizara hii muhimu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa weledi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ipandishe madaraja Walimu waliofundisha kwa zaidi ya miaka mitatu ili kuweza kuwa- motivate na kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamisho wa Walimu; kumekuwa na changamoto kwa Walimu pindi ambapo anataka kuhama kutoka eneo (Mkoa, Wilaya) kwenda sehemu nyingine. Aidha, kumfuata mwenza wake au kwa matatizo ya kiafya. Suala la Mwalimu husika kutafuta Mwalimu mwingine wa kubadilishana nae ni gumu. Hivyo, nashauri Serikali isimamie zoezi hilo na sio kuachiwa Mwalimu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho ya mazingira magumu; kuna baadhi ya Walimu hususan wa vijijini, vituo vyao vya kazi vipo mbali sana na huduma za kijamii mfano mabenki na ofisi za Serikali hivyo hulazimika kutumia fedha nyingi kwa usafiri. Hivyo, naishauri Serikali itenge fungu maalum la posho kwa Walimu hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu kuongeza ujuzi (elimu); naishauri Serikali itenge fedha katika bajeti hii 2018/ 2019 ili iwasaidie Walimu ambao watahitaji kwenda kusimama katika vyuo vyetu. Maana elimu hiyo itasaidia kuwajengea uwezo zaidi wa kuwafundisha watoto wetu wa kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu wa madarasa na uhaba wa shule katika Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam. Hususan shule za sekondari kutokana na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza mwaka 2018. Hivyo, naishauri Serikali itusaidie kutatua upungufu huo uliojitokeza ili kuondokana na wanafunzi hao kusoma kwa session yaani asubuhi na jioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa nyumba za Walimu katika sehemu mbalimbali katika nchi yetu. Naishauri Serikali iwajengee nyumba bora ambazo zitawekwa na umeme ili kumsaidia Mwalimu kuweza kuandaa andalio la somo, azimio la kazi na kusoma mada mbalimbali ambazo atawafundisha wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa samani (meza, viti na kabati (shelves), katika Ofisi za Walimu. Katika Shule ya Msingi Yombo Dovya Kata ya Makangarawe, Jimbo la Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, katika ofisi za Walimu hakuna meza, makabati na viti. Hivyo, Walimu hulazimika kutumwa madawati kwa kukaa na kufanyia shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iweze kutenga fedha katika bajeti 2018/2019 kwa ajili ya kutengeneza samani hizo ili ziweze kutumika katika shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Yombo Dovya. Pia shule hiyo ina uhaba wa vyoo vya Walimu, Walimu hulazimika kutumia vyoo vya wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika Shule ya Yombo Dovya kuna wanafunzi walemavu nao pia hawana choo ambacho kitawasaidia kulingana na walemavu. Hivyo basi kutokana na changamoto hizo, naishauri Serikali itenge fedha ambazo zitasaidia kutatua tatizo hilo la kujenga matundu ya vyoo vya Walimu na wanafunzi walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ushauri wangu atauzingatia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Januari Yusuph Makamba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Mussa Sima bila kuwasahau wafanyakazi wa Wizara hiii kwa kusimamia na kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa mazingira naishauri Serikali itenge fedha za ndani katika bajeti ili kuweza kutekeleza majukumu yake na sio kutenga fedha za wahisani kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri katika kampeni ya upandaji miti Serikali ione haja sasa ya kupanda miti yenye faida zaidi ya moja, nashauri ipandwe miti mingi ya matunda kwanza tutahifadhi mazingira pia yatapatikana matunda ambayo ni muhimu kwa binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko ya plastiki si vizuri kwa mazingira na naunga mkono usitishwaji wake. Ushauri maelekezo ya awali ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kutumia Kiwanda cha Mgololo kutengeneza mifuko mbadala na kiwanda hicho hutumia malighafi ya misitu (miti).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihamasishe wananchi kila mkoa kuanza kulima kilimo cha miti ambayo itatumika katika viwanda vitakavyotengeneza mifuko hiyo kikiwemo Kiwanda cha Mgololo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya mita 60 ipitiwe upya maana kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi maeneo ikiwemo mito maziwa (Victoria) na kadhalika na kusababisha migongano isiyo ya lazima katika ya Serikali na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utupwaji hovyo wa chupa za maji, juice pembezoni mwa barabara kuu ziendazo mikoani. Serikali ifanye utaratibu wa kutoa elimu hususan kwa wafanyakazi wa magari ya abiria licha ya kuwa na vyombo ndani ya mabasi vya kuhifadhia taka, lakini bado utupwaji upo na unaharibu mazingira. Hivyo, wafanyakazi hao wa magari ya abiria wapewe elimu ya kutosha ya uhifadhi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Wizara ya Nishati ili kupunguza ukatwaji wa miti ambayo hutumika kusambaza umeme mijini na vijijini na Wizara ya Nishati ianze mara moja utumiaji wa nguzo za zege ambazo kila mara imeahidi kutumia ili sasa kuepuka kukata miti mingi ambayo itapelekea nchi kugeuka jangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Mungu ampe Mheshimiwa Waziri umri mrefu na afya njema katika kuyatekeleza majukumu yako ya kila siku.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa taarifa yetu nzuri, pia naomba mapendekezo yaliyopo Serikali, iyafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ubinafsishwaji uliofanywa wa viwanda zaidi ya 156, lakini ni vichache tu ambavyo vinafanya kazi. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, tunaomba vile viwanda ambavyo havifanyi kazi, kwa sababu wamiliki wake wamevigeuza matumizi na wengine wamekwenda kukopa fedha kwenye mabenki na kufanya biashara ambazo hazihusiani na mikataba walioingia, tunaomba Serikali iunde Kamati Maalum ya kuvichunguza viwanda vile na kuvirudisha Serikalini ili kuweza kupatiwa wawekezaji wengine kuweza kuviendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo katika viwanda ambavyo vinazalisha vinywaji baridi, tumetembelea viwanda vingi lakini changamoto kubwa ni uingizwaji wa sukari ya viwandani, sukari ya viwandani haipatikani hapa nchini, huagizwa nchi za nje na Serikali ilipanga tozo kwa viwanda hivyo ambavyo vinatumia sukari ya viwandani asilimia 15. Wakati vinaingiza vinakatwa tozo ya asilimia 15 na Mamlaka ya Mapato (TRA), lakini sasa hivi ni takribani miaka mitatu Serikali hiyohiyo imechukua fedha za wenye viwanda haijarudisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mabilioni ya shilingi wenye viwanda wanadai, na tulikwenda katika viwanda hivyo wakatuonesha barua mbalimbali walizoziandika ambazo wameomba Serikali iwarudishie kwa sababu fedha hizo walizikopa katika taasisi mbalimbali hapa nchini na zinatozwa riba, kwa hiyo Serikali imeshikilia fedha yao takribani miaka mitatu sasa hivi. Kwa hiyo Serikali kama Serikali tunahamasisha, wanahamasisha uchumi wa viwanda hapa Tanzania lakini yenyewe pia inakwamisha kwa upande mwingine kwenye viwanda vyetu kuweza kuendeleza viwanda kwa kushikilia fedha ambazo zinatumika kwenye viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tunaomba wale wenye viwanda ambao fedha zao walizoziingiza katika sukari ya viwandani zirejeshwe kwa wakati ili ziweze kutumika katika mitaji yao kwa sababu walilalamika sana wakasema na mitambo mingine imesitishwa kwa sababu hawana mtaji wa kutosha. Pia kama inawezekana, waweze kusitisha utozaji ule, Serikali ianzishe viwanda vya ndani ambavyo vitazalisha sukari ya viwandani kuliko kuagiza halafu wanatozwa tozo hawazirejeshi kwa wafanyabiashara hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nazungumzia kuhusu utitiri wa kodi; utitiri wa kodi umesababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao. Tunajua kabisa mtu akianza kufanya biashara anatakiwa alipe mapato kwa Serikali kwa kiasi anachopata, lakini sasa hivi Serikali inaanza kumtoza mtu mapato kabla hajaanza kufanya biashara. Naishauri Serikali iwapatie wafanyabiashara hao muda maalum (grace period) angalau ya miezi mitatu, wafanye biashara kisha ndiyo waweze kuwakadiria mapato yao, hiyo itasababisha watu kuweza kujua mapato wanayopata kwa wakati na kuwa na willingness ya kulipia mapato hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia pia katika Wizara ya Mazingira; tunaomba Wizara ya Mazingira kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwe na uvunaji endelelevu wa miti. Wizara iandae maeneo maalum ya kupanda miti ambayo itatumika katika viwanda ambavyo vinatumia malighafi ya miti kwa sababu kuna viwanda vingine vinatumia miti, lakini sasa unakuta ukataji wa miti unakuwa hovyo na kusababisha ukame katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara itenge maeneo maalum ya kupanda miti ambayo itasaidia pia katika viwanda vyetu kama malighafi. Pia itasaidia katika matumizi ya nyumbani kama mkaa na kuni kwa sababu gesi tunaona ni ghali mno na watu hawawezi kutumia gesi ambayo ni ghali kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kulikuwa na gesi asilia ambayo tunaomba Serikali iharakishe usindikaji wa gesi asilia ambayo itakuwa na unafuu zaidi kwa wananchi kuliko kuendelea kutumaini kwamba tutumie gesi tusitishe mikaa, mkaa kusitisha itakuwa ni ngumu, lakini Serikali ina mpango mkakati kupanga maeneo ambayo miti itapandwa, watu watakata miti na Serikali itapata mapato na watumiaji wa mkaa watatumia na pia mazingira yataboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuzungumzia kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki; mifuko hii Serikali inataka isitishe kutokana na uchafuzi wa mazingira. Hata hivyo, tunaishauri Serikali kabla ya kusitisha itupe njia mbadala au mifuko mbadala ya kuweza kutumia, ambayo badala ya kutumia plastic sisi tutatumia mifuko ambayo inaendana na mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia Serikali katika ofisi ya mazingira wakati wa kampeni ya upandaji mti, naona sana miti inayopandwa ni ya vivuli, lakini naishauri Serikali tuwe na mkakati wa kupanda miti ambayo itakuwa ya matunda pia kwenye sehemu ambazo zina rutuba sio kupanda miti ya vivuli tu. Kwa hiyo, nashauri Serikali wakati wa zile kampeni za upandaji miti tuangalie sehemu zenye rutuba tuweze kupanda miti ambayo pia tunaweza kupata matunda, vivuli na kutunza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri pia Serikali iweze kufuatilia haya yote katika Kamati yetu, kwa sababu mengi tulishayaeleza, ambayo tumependekeza Kamati yetu, tunaishauri Serikali iyatilie mkazo ili kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipongeze hotuba nzuri ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Pia, nina mambo ambayo nataka kuishauri Serikali ambayo mengine ni kero kwa wananchi na yanahitaji kufanyiwa kazi ipasavyo na maoni mengine ni kuishauri Serikali ili kuweza kupiga hatua mbele katika kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Serikali imejitahidi kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati, maoni yangu nashauri Serikali iweke vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitali ili kuweza kuondoa msongamano katika hospitali za rufaa. Katika Hospitali ya Rufaa Temeke, Dar es Salaam ina uchache wa wodi za wagonjwa na majengo mengi ni chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge wodi za zamani maghorofa, ili kuweza kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya wagonjwa kwa sababu hospitali hii ya Temeke, hupokea wagonjwa kutoka wilaya za jirani za Mkoa wa Pwani kama vile Wilaya ya Mkuranga, pia Wilaya ya Kigamboni. Serikali iwapatie hospitali ya rufaa Temeke mashine ya kufulia mashuka ya wagonjwa, maana kwa sasa yanapelekwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kufuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika hospitali za rufaa mfano Muhimbili, Mloganzila, Serikali ijenge maeneo maalum ambayo yatatumiwa na ndugu wa wagonjwa wakati wagonjwa wao wanasubiri, siyo wagonjwa wote wanandugu au jamaa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Huduma ya kuhifadhi maiti iwe bure, maana mara nyingi tunaona inawakwaza wafiwa kwa kushindwa kulipia maiti zao na hatimaye Serikali inapewa lawama kuwa haina huruma na wananchi, ukizingatia wakati wa uhai wake marehemu alikuwa anachangia pato la Taifa kwa kulipa kodi kupitia huduma mbalimbali alizokuwa anazifanya, kama vile kununua mahitaji yake ya kila siku, kuna kodi za Serikali inachukua. Huduma hii ya kuhifadhi maiti iwe bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na sheria ya kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa akinamama wanaojifungua watoto chini ya miezi tisa (njiti) na kwa akinamama waliojaliwa kujifungua watoto zaidi ya mmoja ili kuweza kuwapa muda wa kuwalea watoto wao, maana miezi mitatu wakati mwingine ni michache mno, ukilinganisha na mwanamke aliyejifungua mtoto mmoja na ambaye ametimiza miezi tisa tumboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa biashara na viwanda, nashauri Serikali itoe muda maalum grace period angalau wa miezi mitatu, kisha ndipo waanze kumkadiria mtu ambaye anataka kuanza kufanya biashara na siyo mfumo unaotumika sasa wa kulipa mapato kabla ya mwananchi kuanza biashara yake. Hili si jambo zuri kabisa. Kuna asilimia 15 ambayo wenye viwanda vinavyotumia sukari ya viwandani huilipa waingizapo sukari hiyo nchini, lakini wafanyabiashara hao wanaidai Serikali fedha nyingi sana na wamefanya taratibu zote zinazohitajika ili waweze kujereshewa fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwalipe wenye viwanda hivyo ambavyo wanadai ili fedha hizo ziweze kuwasaidia kuendesha viwanda vyao, maana suala la kutolipwa kwa wakati kunaathiri uzalishaji katika viwanda vyao. Ni muhimu kwa kuelekea uchumi wa viwanda, kuwalipa kwa wakati na siyo kidogo kidogo kama ifuatavyo Serikali sasa hivi, walipe kwa mkupuo kama wao walivyokuwa wanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuijenga nchi yetu ni muhimu Serikali itatue changamoto zote ambazo zipo ndani ya uwezo wake ili kuweza kufikia lengo la kuondoa umaskini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipongeze kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii chini ya Waziri Mheshimiwa Dkt. Augustine Philip Mahiga, naishauri Serikali iwajengee nyumba maalum Majaji na Mahakimu kutokana na kazi zao za kusimamia sheria na maslahi mbalimbali na waweze kuwa na ulinzi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara hii ikamilishe upelelezi wa kesi kwa wakati ili kupunguza msongamano wa watuhumiwa magerezani na mahabusu. Fedha zinazotolewa za bajeti zipelekwe kwa wakati ili kutekeleza na kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati. Pia naishauri Serikali ikarabati Mahakama za Mwanzo hadi Wilaya, mfano, Mahakama ya Mwanzo ya Temeke Dar es Salaam ni chakavu na ndogo haikidhi mahitaji; Serikali iongeze vyuo vya mafunzo ya Mahakama ili kuweza kupata wataalamu wa sheria wa kutosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali itenge fungu la fedha katika bajeti hii na ifike kwa wakati ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri zetu nchini waweze kuweka utaratibu maalum wa kutoa vibali vya ujenzi za kumbi za starehe kwamba zisiwe karibu na makazi ya watu ili kuepusha usumbufu kutokana na kelele zinazotokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kumbi hizo.

Mheshimiwa Spika, ili kulinda sanaa zetu, nashauri Serikali iweke utaratibu wa kisheria utakaowezesha vituo vyote vya Radio na Television nchini kupiga muziki wa wasanii wa nyumbani kwa asilimia 70 ili pia kukuza soko la bidhaa za wasanii wa ndani.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali irejeshe viwanja vya wazi ambavyo vilikuwa vikitumika kwa michezo mbalimbali na vimebadilishwa matumizi bila kufuata utaratibu maalum.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kutunga Sheria kali ambayo itakataza wasanii wa muziki na maigizo hususan wa kike kuvaa nguo au mavazi ambayo yanakiuka maadili na utamaduni wa Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iwe na vazi rasmi la Taifa ambalo litamtambulisha Mtanzania yeyote yule awapo nje ya nchi yetu na popote pale atakapokuwa hivyo jitihada za makusudi zifanyile ili kufanikisha suala hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika wizara hizi mbili, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Utawala Bora. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi pia kwa kunipa afya njema nami niweze kuchangia kwa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwenye elimu, elimu bila malipo ni suala zuri katika Serikali yetu, lakini wakati inaanzisha elimu bure bila malipo Serikali haikufanya utafiti wa kina. Watu walihamasika sana kuwapeleka watoto wao kujiandikisha, lakini ukatokea upungufu wa madarasa, ofisi za Walimu, vyoo na maabara. Naishauri Serikali hususani mijini maeneo ni madogo ya shule zetu ijenge madarasa kwa style ya ghorofa ili iweze kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi kuliko sasa wanafunzi wanaingia kwa session, wengine wanakuja asubuhi wengine jioni na inapelekea wale wanaokuja jioni hususan katika Jiji la Dar es Salaam kuchelewa kurudi majumbani na wakati mwingine mpaka nyakati za usiku unakuta watoto wako barabarani wanasubiri usafiri wa kurudi nyumbani. Naishauri Serikali sasa itenge fungu maalum ambalo litafika kwa wakati ili liweze kujenga madarasa ya kutosha, vyumba vya Walimu, vyoo pamoja na maabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika barabara zetu hizi za mijini na vijijini Serikali imejitahidi sana hususani katika wilaya yangu ninayotoka ya Temeke imejenga barabara za kiwango cha lami, lakini bado kuna changamoto kubwa sana katika barabara za lami hizo hakuna alama za barabarani hususani katika maeneo yetu, hupeleka magari makubwa ambayo kwa mfano Dar es Salaam kuna barabara ya Mandela, kipindi cha jioni kunakuwa na foleni kubwa sana katika daraja la Mfugale kupelekea magari makubwa kupita katika barabara za mitaani ambazo hazina alama za kuonyesha ni tani gani ya kiasi gani cha gari inatakiwa kupita kwenye eneo hilo. Kwa hiyo nashauri Serikali iweze kuweka alama za barabarani kwenye barabara zetu ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Pia iongeze fungu kwa TARURA kama walivyosema wenzangu kwa sababu kila mtu anahitaji barabara ya lami, lakini kutokana na uchache wa fungu hilo ndio maana kuna maeneo mengi wanajenga barabara za changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu hospitali zetu za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Naishauri Serikali ipeleke vifaa tiba vya kutosha katika hospitali hizo kwa sababu tunaona kuna msongamano mkubwa katika hospitali za rufaa, endapo Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha Madaktari Bingwa wakawepo pia na wauguzi wa kutosha katika vituo vyetu vya afya na hospitali za wilaya hakutakuwa na msongamano mkubwa katika hospitali ya rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano, sasa hivi Hospitali ya Temeke imekuwa hospitali ya rufaa, lakini kunakuwa na msongamano kutokana na hospitali hiyo inahudumua Wilaya ya Kigamboni, pia inahudumia wagonjwa kutoka Wilaya ya Mkuranga na vituo vingine vya jirani. Kwa hiyo naishauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kupeleka miundombinu ikiwepo vifaa tiba vya kutosha katika vituo vya afya kuondoa msongamano katika hospitali zetu za rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hospitali hizo siyo wote wanaoenda kutibiwa wana uwezo wa kulipa gharama ya bili, wengi wanalipia kwa cash na pia hupelekea kutibiwa ugonjwa wao kwa gharama kubwa sana na wakati mwingine wagonjwa hao hupoteza maisha. Naishauri Serikali kupitia TAMISEMI iondoe ile tozo ya maiti kwa sababu ni kero kwa Watanzania, ni kero kwa walipa kodi. Ikumbukwe kwamba marehemu huyo pia alikuwa analipa kodi kwenye Serikali wakati akiwa ananunua bidhaa mbalimbali, hivyo basi katika tozo zote tunashauri Serikali iondoe tozo katika huduma ya kuhifadhi maiti, imekuwa ni kero kwa sababu tunaona maeneo mengi ndugu zetu walioondokewa na ndugu zao huchelewa kuchukua miiili yao kwenye mortuary kutokana na kiwango kikubwa cha kulipia. Naishauri Serikali katika bajeti yao iangalie suala hili ni muhimu sana na ni kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia katika eneo la watumishi. Mheshimiwa Waziri hapa amesema kwamba watumishi lazima wapewe elimu na watumishi hawa wamesema baada ya kuajiriwa wanatakiwa walipe. Naongezea kwa kusema kwamba, sio tu wale ambao wameajiriwa pia wateuliwa wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, wapate elimu ya kutosha ya kujua mamlaka yao ni mwisho wapi kuongoza, kwa sababu tunaona kabisa kuna maeneo mengi ambapo wanatumia mihemko ya kisiasa. Wewe kama kiongozi wa
nchi, kama kingozi wa eneo, kama kiongozi wa mkoa, wilaya unapaswa kufuata maadili au ethic za uongozi, hata kama una itikadi ya chama, lakini hupaswi kuionesha hadharani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia hivi karibuni kuna Mkuu wa Mkoa anatoa tamko kwamba nitahakikisha kwamba Serikali za Mitaa zote, majimbo yote yatakuwa chini ya CCM. Kwa kweli jambo hilo kama ni kiongozi na umesomea uongozi kabisa huwezi kutamka hivyo. Kwa hiyo tunaomba wapatiwe elimu jinsi ya kuongoza kwa sababu hata Rais wetu anaongoza watu tofauti na huduma anatoa na kama ni maendeleo ni maeneo yote bila kujali itikadi. Kwa hiyo elimu si kwa wale ambao wameajiriwa tu pia kwa wateule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia eneo moja la watumishi. Kuna watumishi ambao ni kina mama ambao hupata ujauzito na kujifungua, siyo wote ambao wanajifungua kwa njia ya kawaida, wengine hujifungua watoto wa chini ya umri, watoto njiti (pre-mature) lakini wanapewa likizo sawasawa na yule aliyejifungua kwa kawaida na likizo hiyo ni ya miezi mitatu tu. Ikiwa mwanamke amejifungua mtoto wa miezi mitano, anahitajika kukaa hospitali kwa miezi minne, unakuta likizo ya uzazi inaishia pale pale hospitalini. Mwingine mashallah Mwenyezi Mungu amemjalia akapata watoto wawili, watatu mpaka wanne lakini likizo ni ile ile ya miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali watumishi wa Serikali wanaotakiwa kukaa likizo ya uzazi, kwa wale wenye mahitaji maalum kama hao, waipitie sheria ile na kuweza kuongeza angalau wapewe muda maalum wa kuweza kukaa na kuwahudumia wale watoto, kwa sababu muda mwingi unakuta wako pamoja hospitalini na wengine wamezaa watoto zaidi ya mmoja tofauti na mwanamke mwingine. Kwa hiyo, naishauri Serikali ione haja sasa ya kupitia sheria na kuongeza muda kwa akina mama ambao wamejifungua watoto njiti au mtoto zaidi ya mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la kukaimishwa, sehemu nyingi wafanyakazi wamekaimu. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kwa sababu kuna shortage ya wafanyakazi na watu wako competent mmeshawakaimisha mnajua kabisa wana uwezo wa kufanya hizo kazi, iwaajiri moja kwa moja kwenye nafasi zao na siyo kuwakaimisha kwa muda mrefu. Huwezi kuwa kwenye nafasi ya kukaimu zaidi ya miaka miwili, mitatu. Kwa hiyo, naishauri Serikali, sioni haja ya kuendelea kuwa na makaimu wakati uwezo wa kazi wanao, naomba wawaajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni hali ngumu ya maisha kwa wananchi wetu, kila kukicha afadhali ya jana. Naishauri Serikali ione haja sasa ya kuongeza kipato cha mwananchi wa kawaida hasa mfanyakazi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, awali naipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Kangi A. Lugola. Pia nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Eng. Masauni kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kwamba bajeti inayopitishwa ifike kwa wakati ili kuweza kutekeleza shughuli ambazo zimepangwa kufanyika katika kipindi cha mwaka 2019/2020 ili kufikia malengo yaliyopangwa kufikiwa. Upelelezi wa kesi mbalimbali nashauri ukamilike kwa wakati ili kuweza kuondoa msongamano wa watuhumiwa katika Magereza na mahabusu nchini.

Mheshimiwa Spika, Vitambulisho vya Taifa vinachukua muda mrefu hadi mwananchi kupata. Nashauri huduma hii ya utoaji vitambulisho iboreshwe ili kuharakisha; kila Mtanzania anayestahili kupata kitambulisho hiki, apewe kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, vile vile nashauri Jeshi la Zimamoto lipatiwe vifaa vya uokoaji vya kutosha na vya kisasa ili kuweza kuharakisha uokoaji pindi majanga mbalimbali yatokeapo yaweze kushughulikiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iboreshe nyumba za Askari ili kuweza kuwa na makazi bora na ya kisasa zaidi maana nyumba zilizojengwa kwa mabati (full suit) zimepitwa na wakati.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali kwamba kwa wanawake wafungwa wanaojifungua katika Magereza wapewe muda maalum wa kuwatunza watoto wao, pia wapunguziwe kazi ili kuweza kupata nguvu baada ya kujifungua.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ipunguze gharama za hati za kusafiria (passport) maana sio Watanzania wote wana uwezo wa kugharamia kupata passport na ukizingatia passport ni haki ya kila Mtanzania bila kujali uwezo wake wa kipato.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa Polisi Jamii. Sungusungu wengi hawana mafunzo na elimu ya kutosha katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Hivyo hupelekea migogoro na wakati mwingine husababisha mauaji kwa watu wasio na hatia.

Mheshimiwa Spika, nashauri elimu itolewe kwa wanachi ili kuondoa mila potofu za kuua watoto, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi kwa njia ya kujipatia utajiri.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ijenge na iboreshe vituo vya Polisi ili kukidhi mahitaji. Pia kuwe na vitendea kazi hususan magari ili waweze kufika katika matukio kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na msongamano mkubwa katika vituo vya Polisi. Kutokana na shughuli za upotevu wa simu ili mwananchi kupatiwa Loss Report lazima aende Polisi. Hivyo, naishauri Serikali ianzishe kitengo maalum cha kushughulikia wananchi wanaokuja kuchukua Loss Report hususan za simu. Maana watu hujazana CRO na kusababisha wananchi wenye mahitaji ya dharura kushindwa kuhudumiwa kwa wakati, mfano, Dar es Salaam. Pia kiusalama katika vituo hivyo inakuwa siyo nzuri watu wa aina mbalimbali hujazana eneo moja kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, namwomba Mungu azidi kuwapa afya njema Mheshimiwa Kangi na Naibu wake Mheshimiwa Masauni, pia umri mrefu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, niwapongeze Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali fedha zinazopitishwa katika bajeti zifikishwe kwa wakati ili majukumu yaliyopangwa yaweze kutekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipimo cha Dengue ni ghali sana kwa wananchi wenye kipato cha chini. Mfano katika Hospitali ya Temeke ni Sh.40,000 na Regency Hospitali ni Sh.77,000 na hata kama una Bima ya NHIF ya Bunge unalipia cash hususan Regency Hospitali. Nashauri kutokana na ugonjwa huu kuwa katika Mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam na kadhalika na kipindi hiki cha mvua watu wengi huugua na kushindwa kupata fedha za kulipia kipimo cha Dengue, Serikali ipunguze gharama za upimaji wa ugonjwa huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa Temeke Dar es Salaam, eneo lake ni dogo na wodi nyingi ni chakavu na hazikidhi mahitaji ya wagonjwa. Nashauri zile wodi za zamani zibomolewe yajengwe maghorofa. Mfano mzuri Regency Hospitali Dar es Salaam eneo lilikuwa dogo likabomolewa wakajenga maghorofa ili kukidhi mahitaji wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa Muhimbili na Mloganzila Dar es Salaam. Naishauri Serikali ijenge jengo la kusubiria wagonjwa kwa wale ndugu na jamaa wanaowasindikiza wagonjwa wao watokao Mikoani ili waweze kutoa msaada wa kijamii kwa wagonjwa wao maana siyo wagonjwa wote wana ndugu katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wale wananchi wanaonunua miwani hovyo bila kupimwa iwe kwa ajili ya urembo au la, wasivae bila kupewa ushauri kutoka kwa madaktari wa macho. Maana kuna baadhi ya wananchi wamepata matatizo ya macho kwa kununua miwani bila kufuata ushauri wa daktari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilitoa ushauri Serikali iondoe tozo katika maiti hususani katika hospitali zetu zote. Maana ni kero kwa wafiwa na wakati mwingine walimuuguza ndugu yao kwa kipindi kirefu na walitumia gharama nyingi sana na marehemu wakati wa uhai wake alikuwa na mlipa kodi mzuri kwa kununua bidhaa mbalimbali kwa mahitaji ya kila siku. Hivyo, naishauri Serikali iondoe tozo/ malipo kwa maiti katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matangazo mengi haswa Dar es Salaam ya Waganga wa Jadi na vipeperushi vingi hugaiwa katika makutano ya barabara. Naishauri Serikali hawa Waganga wa Jadi watoe matangazo yao katika vyombo husika kama redio, televisheni na magazeti na siyo kubandika katika nguzo za umeme, miti na kutoa vipeperushi barabarani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINABU M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako Mbunge, pia Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa pamoja na wasaidizi wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuyatekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, wanafunzi wanaoenda kusomea fani ya ualimu wawe na vigezo vinavyohitajika kitaaluma, kwa sababu baada ya mafunzo ya ualimu wataenda kutoa elimu kwa watoto na jamii. Hivyo isiwe mazoea kwa mwanafunzi aliyepata division III au IV ndio aende kusomea kozi ya ualimu. Hivyo nashauri Serikali izingatie hili wachukue wanafunzi waliofaulu kuanzia division one na two. Ili kuleta tija katika elimu.

Naishauri Serikali ili kuweka msingi mzuri katika elimu mitaala iwe na masomo ya ziada kama ilivyokuwa katika miaka ya 1980, mfano Morogoro sekondari mitaala yetu ilikuwa unasoma masomo ya ziada (woodwork, cookery, needle work, metal work, fineart) pamoja na masomo yote ya kawaida. Hivyo mwanafunzi ndani ya miaka minne anakuwa na msingi wa kupata mafunzo ya masomo ambayo baada ya hapo kama hakupata nafasi ya kuendelea na kidato cha V – VI, atakuwa na uwezo wa kujiajiri kutokana na masomo ya ziada aliyosomea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali irudishe mitaala ile katika shule zetu za sekondari kuanzia kidato cha I – IV. Naishauri Serikali fedha zifikishwe kwa wakati ili kuweza kutekeleza majukumu kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhaba wa zana za kufundishia teaching aids, katika shule zetu. Nashauri Serikali itenge fungu la kutosha ili shule zetu ziwe na zana za kufundishia ili mwanafunzi aweze kuwa na uelewa zaidi katika somo analofundishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhaba wa nyumba za walimu hususani maeneo ya vijijini. Hivyo nashauri Serikali ijenge nyumba za walimu maana hutembea umbali mrefu sana kutoka walikopanga nyumba zao hadi kufika katika shule afundishayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwa na wakaguzi mara kwa mara katika shule zetu, nashauri Serikali iwe na vitendea kazi vya kutosha mfano magari ili kuwawezesha wakaguzi kufika kwa urahisi katika maeneo husika ya shule na sio kutoa taarifa ambazo si za uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa walimu hususani katika shule zilizopo vijijini. Naishauri Serikali iweke miundombinu mizuri na motisha nzuri kwa walimu wanaofundisha shule za vijijini ili kuweza kuwavutia walimu wengi kufundisha vijijini na sio kukimbilia mijini kufundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweze kutoa semina mbalimbali kwa walimu ili kuweza kuwajengea uwezo katika sekta hii na kujua wajibu na majukumu yao ya kila siku. Pia waweze kuwalea wanafunzi kwa maadili mema ya kiutamaduni wa mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa vyumba vya madarasa, hii hupelekea mlundikano wa wanafunzi katika chumba kimoja cha darasa, na humuwia vigumu mwalimu kuwafikia kuwafundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja. Nashauri Serikali ijenge vyumba vingi vya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iongeze mishahara kwa walimu na wakufunzi ili waweze kutoa elimu kwa usahihi. Maana wengi wanakuwa na msongo wa mawazo na kushindwa kufundisha vizuri wanafunzi wetu na matokeo yake wanafunzi hufeli katika masomo yao. Wakiongezewa mishahara na posho mbalimbali watahamasika kufundisha kwa weledi mkubwa zaidi na kupelekea wanafuzni kufaulu na kuwa na Taifa lenye watu waliopata elimu bora.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Atashasta Nditiye kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kusimamia miradi mbalimbali katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iweke vifaa vya uokoaji maeneo ya barabara kuu, mfano, gari la zimamoto, winchi, magari ya breakdown ili kuweza kusaidia uokoaji pindi ajali itokeapo na pia kuondoa msongamano barabarani wa magari endapo gari litapinduka na kuzuia magari, itachukua muda mfupi kushughulikia zoezi la kutoa gari hilo na magari kuendelea na safari.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali ifanye ukaguzi wa mara kwa mara hususan SUMATRA katika magari ya mizigo (maroli) ili kuona ubora wake maana mengi ni machakavu pia ubebaji mzigo mara nyingi ni hatarishi kwa vyombo vingine vya usafiri. Mara nyingi magari haya hutazamwa uzito wa mzigo uliobeba katika mizani tu, ukilinganisha na magari ya abiria ambapo kila kituo kikubwa cha mabasi, hufanyiwa ukaguzi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha hasa katika magari makubwa ya mizigo kwa madereva wake, kuacha tabia ya kupaki maroli pembezoni mwa barabara mahala pasipostahiki, mfano Kibaigwa, Chalinze na kadhalika (double parking) na kupelekea usumbufu kwa magari yanayopita maana barabara inakuwa finyu na mara nyingine hupelekea ajali kutokea.

Mheshimiwa Spika, vile vile naishauri Serikali iweke vidhibiti mwendo katika magari ya mizigo maana yanaenda kwa mwendo wa kasi wa kupelekea kusababisha ajari kwa magari mengine, mfano mabasi ya abiria ambayo wamewekwa vidhibiti mwendo na hatimaye kupelekea vifo kwa wananchi wasio na hatia.

Mheshimiwa Spika, naishauri pia Serikali iboreshe viwanja vyote vya ndege nchini ili viweze kufanya kazi kwa masaa 24, yaani usiku na mchana. Viwanja vingi vya ndege mfano, Kiwanja cha Ndege Dodoma wakati wa usiku ndege haiwezi kutua kutokana na ukosefu wa taa za kuongozea ndege.

Mheshimiwa Spika, naishauri vile vile Serikali iboreshe mizani iliyopo maeneo ya Mikese, Morogoro, maana kumekuwa na msongamano mkubwa wa magari na ukizingatia eneo la mizani lipo karibu kabisa na barabara kuu na hii ndiyo sababu, kumekuwa na msongamano hivyo nashauri Serikali iboreshe.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawaombea Mheshimiwa Waziri na Naibu wake afya njema na maisha marefu ili wazidi kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa fursa hii ili kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili nami kwa siku ya leo kuweza kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitaanza kwa fedha zitolewazo katika Wizara hii ya Uchukuzi, kinachotakikana hapa fedha zifikishwe kwa wakati ili miradi iliyopangwa na Serikali iweze kutekelezeka kwa wakati. Endapo Bunge litapanga bajeti na fedha hazitafika kwa wakati ndiyo chanzo cha miradi mingi kutotekelezeka. Naishauri Serikali ipeleke fedha kwa wakati katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuzungumzia kuhusu minara ambayo imejengwa katikati ya makazi ya watu hususan katika Mkoa wa Dar es Salaam. Watu wengi wanasema kuwa minara ile ina madhara, wengine wanasema ina mionzi, lakini ningependa kuona sasa Serikali itoe tamko na kutoa hofu kwa wananchi wetu, kwamba ile minara kama ina madhara yoyote au haina madhara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake watu wengi hutoa maeneo yao katikati ya mji ili kuweza kuweka ile minara ya simu, lakini wengine wanasema ina mionzi lakini bado utafiti haujafanyika. Naomba kama Serikali itakapokuja hapa kujibu itueleze kwamba, je, minara ile ina madhara yote kwa binadamu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona majengo marefu yanajengwa katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam, lakini majengo hayo hayana ile fire escape, tumena majengo ya kizamani, wakati mimi nasoma Chuo Kikuu cha Mzumbe, mwaka 1993/95 kuna majengo mabweni ambayo ngazi ambazo ziko nje ya jengo, ambayo hiyo hata ikitokea hatari ya moto watu huweza kukimbia, lakini majengo mengi yanayojengwa katika Mji wetu wa Dar es Salaam, hayaonyeshi kama hatari yoyote ikitokea watu wakimbilie eneo gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri katika ujenzi unaojengwa sasa hivi, ionyeshe fire escape kwamba watu ikitokea tahadhari yoyote ya moto au chochote watu wanaweza ku, isitokee eneo hilohilo wanaloingilia ndiyo eneo hilohilo wanalotokea ili kuwaondosha madhara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea kuhusu barabara zetu zinazojengwa hivi sasa, barabara nyingi kuu zinazojengwa zina matatizo sidhani kama wakandarasi hao wako competent au vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia barabara hii ya Chalinze mpaka Mlandizi, barabara hii ni ya muda mrefu na hata katika bajeti ya mwaka jana niliizungumzia, kwamba barabara ile imejengwa chini ya kiwango na pia hupelekea ajali nyingi hususan magari ya mizigo, na bado hapo katika hotuba ya Wizara Waziri anasema kwamba upembuzi yakinifu unaendelea kwa kilomita 12. 6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado ipo haja, kwa umuhimu wa barabara hii nadhani ipi haja sasa, barabara hii ijengwe kwa kiwango ambacho ni madhubuti, itapelekea kutosababisha ajali katika barabara hii. Kwa sababu barabara hii ni kubwa, ya kupitisha magari ya kwenda Mikoa ya Kaskazini pia kwenda Mikoa ya Iringa, Mbeya na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pia wakandarasi wetu, katika barabara kuu. Nitatolea mfano barabara ya Dodoma mpaka Morogoro, utakuta mkandarsi amepewa labda eneo la kukarabati, anachimba shimo, utakuta wiki tatu wiki mbili shimo lile halikarabatiwi na huweza kusababisha ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri wakandarasi wetu pindi wanapopewa hii mikataba, watahadharishwe kwa sababu unakuta eneo wamechimba mashimo, wanataka wajenge na unakuta wiki mbili wiki tatu bado lile shimo halijazibwa na hii hupelekea kusababisha ajali kwa magari yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na pia ipo haja sasa ya kujua kwamba kwenye kitabu cha Waziri amesema kuanzia Morogoro mpaka hapa Dodoma ni kilomita 260 na upembuzi yakinifu unafanywa ili barabara hii ijengwe kwa kiwango, lakini sasa hivi naona kuna uakarabati unaendelea, hususan maeneo ya Dumila, barabara inatanuliwa, lakini sasa sijajua kama ndiyo imeingizwa kwenye hii bajeti au lile ni zoezi lingine linaendelea labda bajeti itakuja na barabara ile pia itabomolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua, pindi unapokuja hapa, lile zoezi linaloendelea maeneo ya Dumila pale, la kupanua barabara, lile linahusiana na huu upembuzi yakinifu unaoendelea? Maana yake naona ni vilaka vinazibwa, na eneo lile lina usumbufu wameweka mapipa barabarani na barabara yenyewe ni mbovu. Nataka nijue hawa wakandarasi wetu wanapopewa hii miradi, je, wanaelezewa kiwango cha upana wa barabara? Sidhani kama magari yetu sasa hivi yameongezeka ukubwa au upana, kwa sababu sasa hivi kinachoonekana ni barabara zinaongezwa upana. Kwa hiyo, nashauri Serikali, pindi mnapotoa tenda kwa wakandarasi wetu, muwaeleze upana halisi unaofaa katika barabara zetu za Tanzania, ili kuepusha upotevu wa fedha za Serikali katika kukarabati kila siku katika barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuelezea kuhusu reli, reli sasa hivi inajengwa reli hii ya mwendokasi, lakini bado kuna tatizo katika makutano ya pale Kamata. Ule ujenzi wa reli umepelekea sasa hivi kutokana na mvua za Dar es Salaam kuwa na mafuriko. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri, yule mkandarasi aliyepo maeneo yale aweze kufanya jitihada za makusudi sasa kuweka miundombinu ambayo itawezesha sasa barabara ipitike kwa urahisi ambayo sasa hivi inaleta mafuriko kutokana na ujenzi unaoendelea, amezungusha mabati yake ambayo yanapelekea sasa hivi mafuriko katika eneo lile la Kamata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuelezea kuhusu reli yetu hii, reli inayojengwa ya mwendokasi watu wengi katika vijiji vyetu huwa wanaona kama ni jambo geni kwao, na ninashauri sasa hii reli inayojengwa sasa hivi ya kisasa ianze kuwekwa alama, mwisho ambao mwananchi anapaswa afanye shughuli zake. Kwa sababu isijeikatokea mwananchi sasa ameona reli imepita karibu na eneo analoishi, akaanza kuanza ujenzi ambao baadaye utapelekea sasa migogoro ya ardhi wakati sasa reli ilishakamilika na kukabidhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sasa wakati ujenzi unaendelea, alama ziwekwe katika hii reli ambayo inaanza ya mwendokasi, mpaka huku Makutupora, mpaka Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuelezea kuhusu hii double parking, kuna maeneo mengi ambayo yako katika vituo, hizi barabara kubwa. Kwa mfano natolea mfano maeneo ya pale Kibaigwa, maroli makubwa yameweka double parking pande zote, kiasi kwamba yanasababisha magari ambayo yako katika mwendo anashindwa kupishana. Nashauri elimu itolewe kwa hawa wenye magari makubwa kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitoe shukrani kwa Wizara ya Viwanda na Biashara, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote kwa kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itoe tax period kwa wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha biashara zao, ndipo walipe/wakadiriwe mapato. Tatizo watu wanalipa kabla ya kuanzisha biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iunde Tume Maalum ya kufuatilia viwanda vilivyobinafsishwa na kuona utendaji wake na kuisaidia Serikali kufikia Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zinazotolewa na Hazina ni chache na hazifiki kwa wakati, naishauri Serikali itoe fedha kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti wa masoko kwa mazao yetu nje ya nchi ufanywe kwa umakini na kuwe na mikataba maalumu ndipo uhamasishaji wa kulima zao husika uanze, kuepuka usumbufu kama ulivyotokea katika zao la mbaazi kukosa soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wenye viwanda vinavyotumia sukari ya viwandani wanaidai Serikali bilioni 43.2. Hadi sasa ni shilingi bilioni 13 tu ndizo zilizolipwa, hivyo Serikali iwalipe wafanyabiashara hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ijaze nafasi ambazo watendaji wake wanakaimu ili kuweza kuwa na maamuzi katika masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vitumie malighafi zinazopatikana nchini mwetu ili kukuza kilimo chetu, pia kusaidia bidhaa kuwa na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipunguze utitiri wa kodi kwa watu wanaotaka kuanzisha viwanda ili kuweza kuwapa fursa na wawekezaji wengine kuvutiwa na uwekezaji hapa nchini mwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nawaombea afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri Joseph G. Kakunda ili kuweza kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mbunge na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali bajeti itakayopitishwa na Bunge itolewe kwa wakati ili kuweza kusaidia Wizara kutekeleza miradi ya maendeleo iliyokusudiwa kutekelezwa. Serikali imshauri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano pindi anapofanya uteuzi wa Maafisa wa Jeshi katika ngazi mbalimbali, angalau azingatie jinsia, maana takribani maafisa wa juu wote wa Jeshi ni wa jinsia ya kiume, takribani 90%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione umuhimu wa kuwapatia bima ya afya wanajeshi wetu wote hapa nchini pamoja na familia zao kuliko kutegemea kupata matibabu katika hospitali za kijeshi maana wakati mwingine wanajeshi hawa hulazimika kutumia gharama (fedha zao) kugharamia matibabu katika hospitali ambazo siyo za Jeshi. Hivyo bima ya afya ni muhimu kwa wanajeshi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwa wale wanajeshi ambao wamepata mafunzo au kozi ambayo itawawezesha kupandishwa vyeo kutokana na mafunzo hayo, wapewe haki yao ya kupandishwa vyeo hivyo. Serikali iwajengee nyumba za kutosha Maafisa wa Jeshi, pia wanajeshi wetu ili wawe na makazi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke mipaka upya katika maeneo yote ya Jeshi nchini ili kuondoa migogoro ambayo inaendelea baina ya Jeshi na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namuomba Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mbunge na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu yake yote katika Wizara hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Pia pongezi hizi pia ziwafikie watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, maoni au ushauri wangu ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, fedha zinazopangwa na kupitishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kilimo zitolewe kwa wakati ili kuweza kutekeleza miradi hiyo na kuleta tija katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali itafute masoko ya uhakika ya mazao yetu nje ya nchi ili kuweza kupata fedha za kigeni, pia wakulima kuweza kulima zaidi na kupata kipato cha kujikimu.

Mheshimiwa Spika, tatu, pindi wakulima wanapolima na kuvuna mazao yao na kuamua kuyauza Serikali wakati wa kuuza isiingilie kati kwa kuwapangia bei ya kuuza kwa sababu wakati wa kulima walitumia jitihada za wenyewe bila kupata msaada wowote wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, nne, Serikali kwa kutumia wataalam wetu wa kilimo itoe elimu ya kutosha kwa wakulima wetu jinsi ya kutumia mbegu bora, mbolea na madawa ya kuua wadudu ambao wanaathiri katika ukuaji wa mazao ili kuweza kulima kisasa zaidi na kupata mazao bora na yenye tija.

Mheshimiwa Spika, tano, Serikali ihamasishe wakulima kulima zao la mpira katika mikoa mingine kama ilivyofanya katika zao la korosho ili kuweza kupata malighafi ya kutosha katika Kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha maana kinategemea malighafi kutoka mikoa miwili tu Tanzania nzima; Tanga na Morogoro na hii wakati mwingine husababisha kiwanda kusimamisha uzalishaji kutokana na ukosefu wa malighafi.

Mheshimiwa Spika, sita, Serikali ihamasishe wananchi (wakulima) walime mazao ambayo yatatumika kama malighafi katika viwanda vyetu vya hapa nchini, hivyo kuweza kujihakikishia soko la uhakika.

Mheshimiwa Spika, saba, Serikali iwalipe kwa wakati wakulima ambao mazao yao yanauzwa katika vyama vya ushirika, pia mazao ambayo Serikali imeamua kuyanunua hususan zao la korosho kuwalipa fedha zao ili wakulima hao waweze kupata fedha za kuandaa mashamba yao pindi msimu wa kilimo ukifika, pia waweze kupata fedha zao na kuweza kuzitumia katika kuhudumia familia zao.

Mheshimiwa Spika, nane, Serikali iboreshe mnyororo wa thamani wa mazao yetu ili kuweza kuuza katika soko la dunia kwa kuwa ubora wake utakuwa umeongezeka.

Mheshimiwa Spika, tisa, Serikali katika maeneo ambayo wakulima wanatumia zaidi kilimo cha umwagiliaji, iwawezeshe wakulima hao kuwapatia vifaa mbalimbali ambavyo vitasaidia katika umwagiliaji wa mazao yao maana wakulima wengi hutumia njia za kienyeji, mfano, kuchimba mifereji katika kumwagilia mazao yao.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawaombea afya njema na umri mrefu katika kutekeleza majukumu yao Waziri na Naibu Mawaziri wake pamoja na watendaji wote wa Wizara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara hii katika kusimamia majukumu yao ya kila siku ili kuhakikisha masuala yahusuyo mifugo na uvuvi yanatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, Maoni; fedha zinazotengwa katika Wizara hii hazitoshi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Naishauri Serikali itenge fedha za kutosha na pia fedha hizo zitolewe kwa wakati ili miradi iliyopangwa iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kuondoa gharama za leseni katika vyombo vya uvuvi kama ilivyo katika trekta. Naishauri Serikali kutokana na wingi wa ngozi zinazotokana mara baada ya kuchinja mifugo yetu kwa ajili ya nyama. Vijengwe viwanda vya kutosha hapa nchini mwetu vya uchakataji wa ngozi ili kuweza kupata ajira pia kuongeza Pata la Taifa.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iboreshe majosho yote nchini kwa ajili ya mifugo; na majosho hayo yatumike kwa mifugo tu na si shughuli zingine za kibinadamu. Naishauri Serikali itenge maeneo maalum ya malisho ya mifugo mifugo ili kuondoa kabisa migogoro iliyopo sasa baina ya wakulima na wafugaji ya kugombania maeneo kwa ajili ya kilimo kwa wakulima na kwa ajili ya malisho kwa wafugaji.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kuzingatia sheria na kanuni zilizopo pindi mifugo ikikamatwa. Kuna baadhi ya watendaji wa Wizara hawafuati sheria na taratibu zilizopo; hutaifisha mifugo hiyo ambapo ni kinyume cha sheria na kuanza kuipiga mnada na hivyo kuendelea kuleta mahusiano mabaya baina ya watendaji na wafugaji.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ipunguze tozo katika maziwa. Kwa mfano katika usindikaji wa maziwa, ladha ya maziwa, vifungashio na leseni za usafiri. Naishauri Serikali Ranchi zote walizopewa wawekezaji na kushindwa kuziendeleza zirudishwe Serikalini ili Serikali iweze kuziendeleza kwa kuziboresha na hatimaye zitumike kama maeneo ya malisho kwa wafugaji waishio pembezoni mwa ranchi hizo. Pia ranchi hizo zitumike kama shamba darasa kwa wafugaji wetu ili kuepuka kutohamahama kwenda kutafuta malisho.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iboreshe vyombo vya uvuvi katika bahari kuu. Pia kuwepo na meli kubwa za uvuvi. Ili viwanda viweze kupata malighafi za kutosha pia itapunguza uingizwaji wa samaki kutoka nje ambapo wakati mwingine samaki hao si bora kwa mlaji au kwa matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali ijenge viwanda vya kuchakata samaki katika mikoa iliyopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Spika, mwisho nawatakia Waziri na Naibu Waziri afya njema na umri mrefu katika kuyatekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ndani ya Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ushauri; Serikali itenge fedha za kutosha, pia ambazo zinapitishwa na Bunge zitolewe kwa wakati ili kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iainishe vivutio katika kila Wilaya ili kuweza kujua vivutio mbalimbali vilivyopo kisha kuweza kuzitangaza kama vivutio na sehemu ya utalii. Kwa mfano kuna chemchemi iliyopo maeneo ya Kisaki Mkoani Morogoro, maeneo ya Morogoro Vijijini ambapo Chemchemi hiyo ni ya maajabu maana maji yake ni ya moto kwa centigrade 100, lakini eneo hilo bado Serikali haijalibainisha na kufanya moja ya kivutio. Naishauri Serikali ilitangaze eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuwekeza katika miundombinu kwenye vivutio vya utalii kwa kujenga barabara, viwanja vya ndege, mahoteli n.k ili kuvutia watalii kufika kwenye vivutio hivyo kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali ipitie upya tozo mbalimbali zinazotozwa katika huduma za utalii na kuziondoa zile ambazo zinaifanya nchi yetu Tanzania kuwa ghali zaidi ukilinganisha na washindani wetu wa nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuajiri askari wa kutosha kwa ajili ya kulinda hifadhi zetu maana kumekuwa na uhaba wa watumishi hususani askari wa kulinda hifadhi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, ili kuondoa migogoro baina ya wananchi waliovamia hifadhi zetu na Serikali, elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi hao. Pia Serikali iweke mipaka inayoonekana kiurahisi ili wananchi wasivamie hifadhi za taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali malipo yanayolipwa (kifuta jasho) kwa wananchi walioharibiwa mazao yao, waliojeruhiwa na hata kuuawa na wanyamapori. Kifuta jasho hicho hakiridhishi hivyo Serikali angalau ione haja ya kuongeza ili angalau mwananchi aweze kuona haki imetendeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri na Naibu wako ili kuweza kutekeleza majukumu yenu ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ifuatavyo:-

Kwanza, fedha zinazotengwa katika bajeti zitolewe kwa wakati ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Pili, itoe elimu ya kutosha hususani kwa wachimbaji wadogo wadogo jinsi ya utunzaji wa mazingira ukizingatia wakati wachimbaji madini huacha mashimo makubwa ambayo huharibu mazingira yetu. Elimu itolewe ili baada ya kuchimba wayafukie mashimo hayo.

Tatu, iwapatie wachimbaji wadogo wadogo zana/ vifaa vya kufanyia shughuli zao za uchimbaji ili waweze kupata madini kwa urahisi pia kuweza kupata mapato kwa Taifa.

Nne, iandae vifaa vya uokoaji vya kutosha katika migodi yetu ili pindi zikitokea ajali za kufukiwa wachimbaji ndani ya migodi iwe rahisi kuwaokoa.

Tano, ili kukuza soko la ndani la madini kwa kuvutia wawekezaji, Serikali iendelee kuwatafutia wachimbaji wadogo masoko ya uhakika ili kuuza madini yao ndani ya nchi na kuepusha utoroshwaji wa madini nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mwisho, namwomba Mungu ampe afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri wa Madini pamoja na Naibu Waziri ili kuweza kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuwapongeza Waziri wa Nishati pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii ya Nishati katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Naishauri Serikali kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitolewe kwa wakati ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, pia naishauri Serikali ianze kutumia nguzo za zege katika usambazaji wa umeme mijini na vijijini maana ni madhubuti na pia tutaepuka na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo kwa ajili ya kupata nguzo za miti.

Mheshimiwa Spika, tatu naishauri Serikali ipunguze gharama ya uunganishaji wa umeme hususan maeneo ya mijini maana ni ghali sana. Ikipunguzwa wananachi watakuwa na uwezo wa kugharamia na kupata umeme maeneo mengi ya nchi yetu. Kuna vijiji vimepitiwa na nguzo za umeme jirani kabisa lakini hadi sasa vijiji hivyo havina umeme. Serikali ione sasa haja ya kuvipatia vijiji hivyo umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Spika, nne bei ya umeme hususan mijini kwa matumizi ya majumbani kwa unit ni ghali mno. Naishauri serikali hii ya wanyonge angalau ipunguze bei ya umeme kwa unit maana ni kubwa sana. Pia naishauri Serikali kuhusu PINOT Project ya usambazaji gesi majumbani kwa bei nafuu, iliyofanywa maeneo ya Mikocheni Jijini Dar es Salaam. Huduma hii isambazwe katika maeneo mengi ili iweze kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ianzishe kozi katika vyuo vyetu vikuu hapa nchini kwetu vya kudahili wanafunzi kusomea masuala ya gesi ili tuweze kuwa na wataalam wa kutosha kutoka hapa hapa nchini. Pia gharama za kusoma kozi ya gesi nje ya nchi, kwa mfano Uturuki, China na kadhalika ni gharama kubwa sana. Hivyo kozi hii ikianzishwa katika vyuo vyetu wanafunzi watapata fursa ya kusoma kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iajiri watendaji wa watumishi wa kutosha katika Wizara wengi wamekaririshwa na hawawezi kutoa maamuzi katika maumbo mbalimbali wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, mwisho nawaombea afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri wa Nishati pamoja na Naibu wake ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia Watanzania katika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini mwetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema ili niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, ili kufikia Tanzania ya viwanda nashauri fedha zinazotengwa katika bajeti zipelekwe kwa wakati ili kuharakisha miradi iliyopangwa itekelezwe ipasavyo.

Nashauri kwa wamiliki wa viwanda vinavyotumia sukari ya viwandani walipwe kwa wakati fedha zao ambazo wanadai sasa takriban miaka minne hawajalipwa asilimia 15 withholding tax ambayo inapelekea wamiliki wa viwanda kupunguza uzalishaji pamoja na kupunguza wafanyakazi sababu mitaji yao imeshikiliwa na Serikali. nashauri walipwe ili uzalishaji uongezeke na kupata pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, nashauri askari wa usalama barabarani wasiwabambikizie makosa madereva, watumie weledi wao kubaini makosa mbalimbali, maana utakuta trafiki anatumia kifaa cha kumulikia speed maarufu tochi, badala ya kupiga picha namba ya gari wanapiga picha bodi ya gari na kutumia picha hiyo kukamata magari yote ya kampuni husika maana jina na rangi za magari zinafanana. Hivyo nashauri askari wapatiwe mafunzo ya kutosha kuondoa kero.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ningependa kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu ya kila siku katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni; fedha zinazopitishwa na Bunge katika kila Wizara kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hazifiki kwa wakati na pia fedha zitolewazo hazipelekwi zote na hazitoshelezi kuweza kuendeleza miradi hiyo. Naishauri Serikali katika kila Wizara fedha zinazopitishwa na Bunge ziwe zinaakisi hali halisi ya kuweza kuitekeleza miradi ya maendeleo katika Wizara husika na pia fedha hizo zitolewe kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa malimbikizo ya madai; katika hotuba ya Waziri, ulipaji wa madai umeelezewa katika ukurasa wa 15-16 kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri. Kuna madai ambayo ndani ya hotuba hii hayajatolewa maelezo kabisa. Wamiliki wa Viwanda ambao wanatumia sukari ya viwandani, takriban miaka minne wanaidai Serikali bilioni 45 na ni kiasi kidogo sana ambacho Serikali imewalipa shilingi bilioni sita tu ndizo zilizotolewa. Hii hudhoofisha mustakabali mzima wa kuelekea Tanzania ya viwanda, maana wafanyabiashara hawa wanaidai Serikali na kukwamishiwa mitaji yao na kupunguza uzalishaji katika viwanda vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuchelewa kurejesha kwa ushuru wa forodha 15% (Refundable Import Duty 15%) katika sukari ya viwandani. Serikali imeleta changamoto kwa wahusika jambo lililopelekea kiasi cha mitaji ya wazalishaji wetu kushikiliwa na Serikali na kuwapunguzia mitaji yao. Nashauri fedha hizo zilipwe ili wamiliki wa viwanda hivyo waweze kufanya kazi ya kuzalisha bidhaa zao bila kusuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2019/2020, ambapo katika kitabu cha hotuba ya Waziri, kuhusu kipaumbele cha viwanda na kilimo, kwa upande wangu sijaona sehemu yoyote katika hotuba hii inayozungumzia kuhusu jitihada za Serikali katika kuchukua hatua za kisheria kwa vile viwanda vilivyobinafsishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iunde Tume Maalum ya kufuatilia viwanda vyote vilivyobinafsishwa ili kujionea hali halisi ya utendaji wake maana kuna baadhi vimekiuka kabisa ili dhana na masharti waliyopewa wakati wa zoezi hilo la ubinafsishaji matumizi ya eneo lililobinafsishwa. Hivyo kipitia Tume, hiyo Serikali ivibainishe na kuvichukua viwanda vyote ambavyo havijaendelezwa na kuwapa wawekezaji wengine ili kufikia lengo la Serikali kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, kuondoa tozo za kuhifadhi Maiti katika Hospitali zetu za Serikali maana imekuwa kero kwa wafiwa na wakati mwingine hushindwa kulipa na kupelekea Serikali kuchukua jukumu la kuzika. Hivyo naishauri Serikali huduma ya kuhifadhi maiti katika hospitali zetu za Serikali iwe bila gharama (bure).

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, igawe taulo za kike bure katika shule za msingi na sekondari na pia kurudisha Corporate Income Tax kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato na kubakia 30%, ile ile na kusimamia muuzaji wa mwisho kupunguza bei ya taulo hizo ili kila mwanamke kuanzia mijini na vijijini wawe na uwezo wa kununua na kutumia, kuepusha kutumia bidhaa zisizofaa katika kujisitiri wakati wa hedhi na hii njia huleta maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, namwomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake ili waweze kuyatekeleza majukumu yao ya kila siku.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumpongeza Mheshimiwa Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa William Olenasha Mbunge, Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanafanya katika Wizara hii ili kuboresha taaluma hii ya ualimu hapa Tanzania kwa kuleta Muswada wa Sheria ya Bodi ya Taaluma ya Walimu Tanzania wa mwaka 2018 (The Tanzania Teacher’s Professional Board Bill, 2018). Muswada huu ni mzuri kwa maslahi ya walimu wa Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maoni na ushauri kwa Serikali kama ifuatavyo:-

(i) Malipo ya kupata leseni yaendane na kipato cha walimu maana walimu mishahara yao ipo chini sana na wengi wanadai stahiki zao kwa muda mrefu. Hivyo, malipo ya kupatiwa leseni yakiwa madogo yatasaidia kila mwalimu kuweza kupata leseni kwa wakati mara tu Muswada huu utakapopitishwa.

(ii) Taaluma nyingi zina utambuzi wa bodi, isipokuwa taaluma ya walimu. Hivyo basi nashauri Mwenyekiti wa Bodi badala ya kuteuliwa na Waziri wa Elimu, ateuliwe na Mheshimiwa Rais kama zilivyo bodi nyingine.

(iii) Walimu ambao si raia wa Tanzania (expertise) nao pia licha ya kuwa na leseni zao kutoka nchi husika, Bodi hii ya Walimu itakayoanzishwa iweze kumpa mwalimu ambaye si raia leseni na mkataba maalum ili aweze kufanya kazi yake kwa weledi. Hii itasaidia mwalimu huyo kufuata matakwa yote ya nchi na kutoa elimu yenye tija kwa watoto wetu.

(iv) Bodi ihakikishe walimu kuanzia shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya ualimu na walimu wa vyuo vikuu wote wanapatiwa leseni hizi mara baada ya Muswada huu kupitishwa na kuwa sheria.

(v) Walimu hao wakishapewa leseni kusiwe na masharti magumu ya kutomruhusu kwenda nchi ya jirani pindi atakapohitaji kwenda kufundisha huko.

(vi) Baada ya Bodi ya Taaluma ya Walimu Tanzania kupitishwa na kuwa sheria, Serikali ione haja sasa ya kukaa pamoja na Tanzania Service Commission, ambacho ndicho chombo kinachoshughulikia maslahi ya walimu Tanzania ili kuweza kuboresha stahiki za walimu wetu. Maslahi pamoja na kuwepo kwa Bodi ya Taaluma ya Walimu itaweza kuleta tija kubwa sana kwa elimu ya Tanzania maana itaweza kuinua kiwango cha elimu na kuleta ufaulu wa hali ya juu katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nawatakia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Prof. Joyce L. Ndalichako pamoja na Naibu, Mheshimiwa William Tate Olenasha afya njema na umri mrefu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuwatumikia Watanzania.