Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sonia Jumaa Magogo (7 total)

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa tatizo la wananchi wa Mufindi Kusini linafanana kabisa na tatizo linalowakumba wananchi wa Handeni Mkoani Tanga. Je, Serikali ina mpango gani kuondoa au kupunguza adha hii ya maji inayowakuta wananchi wa Handeni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwanza katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kumetengwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa maji. Pia wananchi wa Handeni wapo katika mradi ule wa HTM. Sisi kama Wizara tutasimamia mradi huu wa maji ili uweze kutekelezwa wananchi waweze kupata maji. Ahsante sana.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, Serikali ina mkakati gani juu ya vijana ambao wamekuwa wakipata ajira za muda mfupi na kushindwa kuendelea na ajira zile, lakini kwa kigezo cha umri wamekuwa wakishindwa kupata mafao yao ambayo yangeweza kuwasaidia katika kuendeleza maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kumekuwa na tofauti ya pensheni za kila mwezi kutoka mfuko mmoja na mwingine. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha wazee hawa wanaostaafu wanapata pensheni iliyo sawa ya kila mwezi na ambayo inaweza kuwasaidia kuendesha maisha yao? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza alikuwa anazungumzia kiujumla kuhusu fao la kujitoa na amewazungumzia vijana ambao bado hawajafikia umri wa kupokea pensheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumesema awali katika Bunge lako kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hili la fao la kujitoa. Hivi sasa tupo katika utaratibu wa kushirikiana na wadau ili kutengeneza kwa pamoja mfumo mzuri ambao utawa-cover watu wote katika makundi tofauti tofauti. Hivyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu jambo hili bado linafanyiwa kazi na Serikali tutakuja na mpango mzuri wa kuweza kusaidia kutatua changamoto hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu pensheni, tayari SSRA wameshatoa miongozo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kulipa kima cha chini cha pensheni sawa kwa mifuko yote na ambayo hivi sasa imeanza kutekelezwa. (Makofi)
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha na kujenga nyumba za walimu ili kuondoa adha ya tatizo hili ambalo limekuwa kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu ya majengo ya shule nyingi ambazo kipindi cha mvua watoto wamekuwa wakipata wakati mgumu? (Makofi) Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama tulivyojibu kwenye jibu la swali la msingi ni kwamba tunayo changamoto kubwa sana katika nchi ambayo ilitokana na kutekeleza mpango wetu wa maendeleo wa elimu ambao sasa hivi kuanzia mwaka 2015 mwezi Desemba, tunatoa Elimu Msingi Bila Malipo. Hiyo imevutia wanafunzi wengi zaidi kudahiliwa katika shule kuanzia elimu ya awali, elimu ya msingi na sekondari. Kwa hiyo, tuna uhaba mkubwa sana wa madarasa, nyumba za walimu na vyoo.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imejenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo katika shule za msingi 6,200 nchi nzima na kazi bado inaendelea, tunaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na wananchi. Katika shule za sekondari tumezifikia shule za sekondari 3,159, hii ni kazi kubwa na ndiyo maana nikatoa wito kwamba jambo hili haliwezi kufanywa na Serikali peke yake, tuna jumla ya shule 22,000 za msingi na sekondari. Sasa kama tumefikia shule 9,000 bado tuna kazi kubwa ya kufanya, tunataka mpaka ifikapo mwaka 2020 angalau tuwe tumezifikia shule 17,000, hatuwezi kuzifikia shule 17,000 peke yetu bila ushirikiano wa wananchi.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyogeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa wakulima wengi wa mihogo ni wadogowadogo na hawana mitaji na wamehamasishwa na wawekezaji kulima zao hili kwa wingi, je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, vilevile napenda kujua Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia elimu wakulima hawa ili waweze kuzalisha zao hili kwa wingi na kwa kiwango kinachohitajika?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sonia Magogo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kwamba wakulima wengi ni wadogo, hawana mitaji, kwa kweli hilo sio kwenye sekta ya kilimo cha muhogo peke yake bali wakulima wetu wengi hapa Tanzania hasa hawa wadogowadogo wanalima kilimo cha kawaida, kilimo cha kutegemea mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu zaidi ni pale alipouliza katika sehemu ya pili ya swali lake kuhusu elimu, hilo ndilo jambo la muhimu zaidi kwa sababu elimu itahusu kilimo bora cha muhogo, utafiti na kutumia mbegu bora. Kwa hiyo, tunashirikiana kwa karibu sana sisi mapacha, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda kuhakikisha kwamba mkulima anaongeza uzalishaji kutokana na ile elimu atakayopata kutoka kwa Maafisa Ugani walioko kwenye kata na vijiji. Hilo ndiyo jambo la msingi sana. Waziri wa Kilimo ameshaagiza Maafisa Kilimo wote nchini wale ambao hawajayajua vizuri mazao fulani kwenye maeneo yao wanatakiwa wapatiwe mafunzo wao wenyewe kwanza kabla hawajaenda kuwapatia wakulima. Ahsante sana.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Wilaya ya Handeni ni Wilaya kubwa sana lakini kwa bahati mbaya hawana Baraza la Ardhi kiasi kwamba yanapotokea matatizo yanayohusu ardhi inawabidi wananchi kusafiri mpaka Wilaya ya Korogwe:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi hawa Baraza la Ardhi?

Swali la pili; kumekuwa na migogoro ya muda mrefu katika Vijiji vya Sezakofi Kata ya Ndolo, Wilaya ya Handeni na Kata ya Kwagunda Wilaya ya Korogwe:-

Je, Mheshimiwa Waziri ni lini atakwenda kuwaona wananchi hawa ili kusikiliza kero zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Sonia ameuliza ni lini tutaweka Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Handeni, kwa sababu sasa hivi wanakwenda Korogwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu nimfahamishe kwamba ni dhamira njema ya Serikali kuhakikisha kwamba inakuwa na Mabaraza ya Ardhi katika kila Wilaya. Mpaka sasa tuliyonayo kisheria ni mabaraza 97 ambapo 53 yanafanya kazi na 44 hajaweza kuanza kufanya kazi. Tatizo kubwa lililopo katika uanzishwaji wa mabaraza, jambo la kwanza ni ile rasilimali watu wa kuweza kuhudumia mabaraza hayo lakini pia na maeneo au majengo kwa ajili ya kufanyia shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, pia tunapeleka baraza pale ambapo pengine pana mashauri mengi kiasi kwamba panahitaji nguvu ya ziada. Ni hivi karibuni tu tumeongeza mabaraza mengine likiwemo la Mbulu na maeneo mengine kwa sababu tu tayari tulishapata nafasi ya ofisi katika eneo lile na sisi jukumu letu kama Wizara ni kupeleka watumishi pamoja na samani za ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaangalia tawimu zilizopo kwa Handeni kama kweli ni nyingi kiasi cha kutaka kuwa na baraza, basi nitawaomba uongozi wa pale watuandalie eneo ambalo litakuwa ni ofisi linalokidhi vigezo vya kuwa Baraza la Wilaya. Vinginevyo nitawaomba waendelee kutumia Baraza la Korogwe kwa sababu lipo karibu na bado hawana mashauri mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ameuliza ni lini nitakwenda katika eneo la Handeni kwenye Kata ya Sasako na Kwagunda kwa ajili ya kutatua migogoro. Naomba nimthibitishie tu kwamba ni dhamira njema ya Wizara kuhakikisha kwamba tunafika maeneo yote yenye migogoro lakini kabla hatujafika, uongozi uliopo katika maeneo yale unafanya kazi nzuri sana ya kuweza kutatua migogoro. Pale ambapo inashindikana na uongozi uliopo pale, basi Wizara ipo tayari kufika. Kwa kesi yake huyu, basi tutaangalia uwezekano wa kuweza kwenda kutatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mbunge wa eneo lile, Mheshimiwa Mboni, amekuwa akiulizia pamoja na jirani yake Mheshimiwa Kigoda, nikawaambia tutafika pale. Nilikuwepo mwaka 2016 lakini nitatafuta muda tena kama bado kuna kero, tutaenda kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nataka kutoa nyongeza nimfahamishe Mheshimiwa Sonia kwamba takwimu zinaonyesha kwamba mashauri mengi ya ardhi yalikuwa yanatoka Wilaya ya Lushoto ndani ya Mkoa wa Tanga. Kwa hiyo, Serikali hivi sasa imefanya jitihada ya kuongeza Baraza jipya la Lushoto ili kupunguza load ya mashauri ndani ya Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa tumeanzisha baraza, ukiacha Korogwe ambao walikuwa wanahudumia mpaka Lushoto, sasa Lushoto wanajitegemea. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo maana yake hata Handeni sasa mtapata huduma nafuu zaidi kwa sababu nusu ya matatizo ya kero ya ardhi ya Tanga sasa yamepatiwa ufumbuzi kwa kumpeleka Mwenyekiti mpya Wilaya ya Lushoto.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, asilimia kubwa ya wananchi wetu kipato chao ni cha chini na wamekuwa wakitegemea hpspitali zetu za Serikali kama msaada mkubwa pindi wanapopata changamoto za afya. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba, hawa madktari bingwa wachache ambao tunao hawapati vishawishi vya kwenda kufanya kazi nje ya nchi ama kwenye private hospitals?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ukiangalia idadi ya madaktari bingwa ambao tunao bado ni chache sana, lakini hospitali nyingi za mikoa hazina madaktari bingwa. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha madaktari hawa wanagawiwa kwa uwiano mzuri, ili kuepusha usumbufu wa Wananchi wengi kutoka mikoani na kufuata huduma Hospitali ya Muhimbili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako kwamba, katika nchi ambazo tumejaliwa kidogo kwamba, madaktari wetu hawatoki sana kwenda nje ya nchi kulinganisha na nchi nyingine katika Bara la Afrika, Tanzania ni mojawapo.

Mheshimiwa Spika, na moja ya mkakati ambao tumeuweka wa kuhamasisha madaktari wetu na wataalam wetu wa afya kuendelea kukaa nchini ni maboresho ambayo tunaendelea kuyafanya katika sekta ya afya; vituo zaidi ya 352 tumeviboresha, hospitali za wilaya 67 tumejenga, sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa hospitali za rufaa tano za mikoa na maboresho mengine makubwa ya kimiundombinu, ya vifaa, ambayo sasa hivi yamesababisha kwamba, hata huduma zile kubwa za kibingwa ambazo zilikuwa zinafanyika nje ya nchi sasa hivi zimeweza kufanyika nchini. Kwa hiyo, hili nalo limesaidia sana kuwafanya wataalam wetu wazalendo kubaki, pamoja na motisha nyingine za ndani ambazo tumeendelea kuwapatia watalaam wetu katika sekta yetu ya afya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Sonia Magogo ameulizia suala la uwiano; ni kweli tunakiri tumekuwa na changamoto kubwa sana ya uwiano wa upatikanaji wa Madaktari Bingwa katika baadhi ya mikoa. Na hili sisi kama Wizara tumeshaliona na moja ya mkakati ambao tumeufanya sisi kama Wizara ni kuhakikisha kwamba, wataalam ambao tunaenda kuwasomesha kwa fedha ya Serikali tunachukua katika maeneo ambayo yamekuwa na uhaba mkubwa wa wataalam kwa lengo kwamba akimaliza na tumewasainisha kitu kinaitwa bonding kwamba, ukimaliza na iwapo kama umesoma na fedha za Serikali basi tutakurudisha kulekule katika maeneo ambayo ulikuwa umetoka, ili uweze kupata utaalam huo.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha mpito ambapo huduma hizi hazijaweza kupatikana katika baadhi ya mikoa ndio tumekuwa tunaendesha kambi; Madaktari Bingwa hawa wachache tulio nao tumekuwa tunawazungusha ndani ya nchi kwa kambi maalum katika baadhi ya mikoa, ili waweze kutoa hizo huduma kwa wale Wananchi, ili angalau katika ile mikoa basi huduma zile ziweze kupatikana.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Afya nina maswali mawili ya nyongeza. Mahakama kuu ilitamka kuwa vifungu vya Sheria ya Ndoa ambavyo vinaruhusu ndoa za utotoni havistahili kutumika hivyo vifanyiwe marekebisho ndani ya mwaka mmoja na kuweka umri wa miaka 18 kuwa ndio umri wa chini wa mtoto kuweza kuolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu ilikata rufaa juu ya shauri hilo. Je, Serikali haioni kwa kukata rufaa inaendelea kukubali athari zinazompata mtoto kiafya na pia kuondoa haki ya fursa za kimaendeleo kwa mtoto?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wanawake wengi wamekuwa wakipata shida sana pindi wanapotengana na wenza wao ama kupoteza wenza wao hasa wa vijijini na hii ni kutokana na kutokujua sheria mbalimbali na kupelekea watoto wengi kukosa haki zao za msingi kama afya, malazi, chakula na elimu.

Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wanawake hawa kuanzia ngazi ya vijiji ili kuweza kuwasaidia watoto hawa kupata elimu kuanzia ngazi ya chini?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Sonia Magogo kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Suala la marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 maelezo yalishatolewa ndani ya Bunge lako tukufu na Waziri wa Katiba na Sheria, kwa hiyo nisingependa kurudia maelezo ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa sababu suala hili sasa hivi liko chini ya Waziri wa Katiba na Sheria na yeye ameahidi ndani ya Bunge lako tukufu kwamba linafanyiwa kazi. Suala la kutoa elimu kwa kina mama na watoto ambao wanapata matatizo au changamoto au haki zao mara wanapotengana na waume zao, kwa kweli niyashukuru sana Mashirika yasiyo ya Kiserikali yamekuwa yakifanya kazi kwa karibu sana na Serikali katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya haki za wanawake na watoto katika ndoa na mara ambapo kunakuwa ndoa imevunjika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi tumepitisha Sheria ya Legal Aid Act, No. 1 ya Mwaka 2017, na lengo letu kwa kweli ni kuhakikisha sasa wanawake hasa wa vijijini wanapata huduma za msaada wa kisheria pale ambapo kunakuwa na changamoto ndani ya ndoa. Mheshimiwa Sonia nikiri kwamba tutaongeza jitihada za kuelimisha jamii katika ngazi zote hasa katika ngazi ya vijijini ili kuhakikisha kwamba wanawake wanatambua haki zao. Pia tutawaelimisha na wanaume kwa sababu mwisho wa siku ili tuweze kupata mafanikio mazuri lazima tuwaelimishe na kuwahamasisha wanaume kuheshimu na kutambua haki za wanawake na watoto ndani ya ndoa na nje ya ndoa.