Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kiza Hussein Mayeye (8 total)

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) Je, ni lini sasa Serikali mtatimiza ahadi yenu na kutekeleza mradi huu wa Maji katika Mji ya Manispaa ya Kigoma Mjini kufika katika Mji Mdogo wa Mwandiga?
(b) Serikali haioni sasa ni muda muafaka maji haya ya Ziwa Tanganyika kwenda katika Wilaya ya Kasulu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa maji kwa Mji wa Mwandiga unategemeana kabisa na utekelezaji wa mradi huu mkubwa ambao utakamilika mwezi huu Disemba. Mradi huu utazalisha lita milioni 42 na mahitaji ya Mji wa Kigoma ni lita milioni 20. Kwa hiyo, kutakuwa na maji ya kiasi kikubwa ambayo tutaweza kuyapeleka katika Mji wa Mwandiga. Kikubwa nataka niwahakikishie wananchi wa Mwandiga subira yavuta kheri na kheri itapatikana katika upatikanaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili kuhusu suala la upatikanaji wa maji katika Mji wa Kasulu nataka nimhakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Mbunge wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani. Serikali imefanya kazi kubwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa maji, sasa hivi Mji wa Kasulu upo miongoni mwa miji 17 ambayo kupitia fedha za India utapata maji. Kikubwa tumsubiri Mhandisi Mshauri atatushauri vipi ili tupate maji ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Kasulu wanapata maji kwa wakati. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maijibu mazuri, ametupa faraja watu wa Kigoma. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Hospitali hii ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni ni hospitali kubwa ukizingatia Kigoma tuko mpakani, inahudumia wananchi zaidi ya milioni mbili, lakini mpaka sasa hatuna vifaa muhimu kama CT-scan na vile vya kupimia saratani ya kizazi kwa wanawake. Naomba majibu ya Waziri, ni lini mtatuletea vifaa hivi katika hospitali hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Kigoma umekuwa ukikumbwa na changamoto nyingi za magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hasa katika Wilaya yangu ya Kigoma Vijijini. Nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wanamaliza tatizo la kipindupindu ndani ya Mkoa wa Kigoma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, S wali lake la kwanza ameuliza ni lini Serikali itapeleka mashine ya CT-scan na vipimo vya kupima saratani. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa mpango wa Serikali na aina ya huduma ambazo zinatolewa, sasa hivi katika ngazi za Hospitali za Rufaa za Mikoa, hatuna mpango wa kuweka CT-scan kwa sababu, moja, mashine hizi kwanza ni za gharama kubwa lakini pili zinahitaji utaalam ambao kwa sasa hivi katika ngazi za rufaa za mikoa hatuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi katika mikakati yetu ni kwamba mashine za aina ya CT-scan upatikanaji wake unaanzia katika Hospitali za Rufaa za Kanda. Hata hivyo, vipimo kwa ajili ya dalili za awali za saratani ya shingo ya uzazi vyote vinapatikana hadi katika ngazi ya vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi ambao wanatusikiliza kwamba huduma hizi zinapatikana. Kwa wale wanawake ambao hatujawagusa katika chanjo hizi, huduma hizi tumezisogeza, zaidi ya vituo 1,000 ndani ya nchi hii vifaa hivi vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili limehusiana na suala la kipindupindu. Ugonjwa wa kipindupindu ni mtambuka na sisi kama Wizara ya Afya ambao tunasimamia masuala yote ya afya, tunaendelea kushirikiana na mamlaka katika ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha kwamba mikakati yote ambayo sisi tumeiweka ya kutokomeza ugonjwa huu inatekelezwa kwa maana ya kutoa dawa, vipimo, kutibu maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa wa kipindupindu.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini napenda kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, upanuzi wa Bandari hii ya Kigoma unakwenda sambamba na Bandari Ndogo za Ujiji na Kibirizi ni lini sasa Serikali watakamilisha ujenzi wa Bandari ya Ujiji na Kibirizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mwezi wa Nne Mheshimiwa Zitto aliuliza kuhusu Azimio la Mawaziri wa Maziwa haya Makuu ambapo walikubaliana Kigoma kuwa Bandari ya mwisho katika usafirishaji wa mizigo kwenda Mashariki ya Congo na Burundi. Je, Serikali wamefikia wapi katika utekelezaji wa azimio hili na lini watakamilisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho Kigoma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bandari Ndogo za Ujiji na Kibirizi ni moja kati ya Bandari za kipaumbele ambazo zinatafutiwa pesa ya ujenzi na Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi ninavyoongea Mheshimiwa Mbunge nikutaarifu tu kwamba Bandari ndogo ya Ujiji na Kibirizi ziko kwenye lot moja na zilishatangazwa tenda ya kutafuta mkandarasi wa kujenga na tenda hiyo ilifunguliwa tangu tarehe 28 Agosti na sasa hivi taratibu za kumpata mnunuzi wa kuendelea kuzijenga na kusanifu zinaendelea, na tutakapopata tutamtaarifu lini hizo Bandari zitaanza makandarasi na kuanza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Mayeye, ni kweli kwamba kulikuwa na changamoto ya kulipa fidia kwa wananchi ambao wako eneo la pale Katosho na wananchi walishalipwa na walishaachia sehemu kwa ajili ya kujenga Bandari kavu ya Katosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizofanyika mpaka sasa hivi ni kusafisha eneo lote kuona mipaka, lakini vilevile tumetangaza tenda kwa ajili ya kumpata mtu wa ku-design na kujenga majengo mbalimbali ndani ya eneo hilo na tenda inategemewa kufunguliwa katikati ya mwezi huu.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, naomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) Wanawake wengi ndani ya Mkoa wa Kigoma hawana elimu ya kutosha kuhusu uzazi wa mpango na hata wale ambao ni wajawazito bado hawaelewi ni hatua zipi waweze kuziona na wakimbie katika vituo vya afya. Serikali mmejipangaje katika kuwapatia elimu wananchi wa Kigoma?
(b) Wilaya ya Kigoma Vijijini katika Vijiji vya Zashe, Mtanga, Kalalangabo, vijiji hivi vinakabiliwa na ukosefu wa wauguzi; hospitali ina muuguzi mmoja. Nini kauli ya Serikali katika kusaidia vijiji hivi viweze kupata wauguzi wa kutosha kwa haraka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wastani wa taifa wa matumizi ya njia za uzazi salama ni asilimia 38; asilimia 32 kwa njia za kisasa na asilimia sita kwa njia za asili, bado tuko nyuma sana, lengo letu lilikuwa tuifikie asilimia 45. Kwa hiyo, na sisi kama Serikali tumeliona hilo, tunaendelea kuweka afua mbalimbali za kutoa elimu kwa jamii, na mimi niendelee kusisitiza jamii kwamba njia za uzazi bora ni salama na tuachane na imani potofu na zitatusaidia sana kuhakikisha kwamba tunazaa, tunapata watoto kwa idadi na kwa wakati ambao na sisi tunawahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na hali ya watumishi. Tunatambua baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi. Katika mwaka huu wa fedha Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi wa afya 8,000; watumishi 6,200 kati ya hao katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na 1,800 katika Wizara ya Afya. Kwa hiyo zoezi hili litakapokamilika maeneo ambayo niliyoyataja yatakuwa ni sehemu ambayo yatapata watumishi.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Mji mdogo Mwandiga ni moja ya eneo ambalo linakabiliwa sana na changamoto ya kukosa majisafi na salama. Ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yenu ya kuleta maji ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na kufika katika mji mdogo wa Mwandiga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika Mkoa wa Kigoma una jitihada kubwa sana kwa Manispaa ile ya kutekeleza mradi wa zaidi ya Euro milioni 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukamilishaji wa mradi huu, sisi kama Wizara ya Maji, tutahakikisha kupeleka maji katika Mji wa Mwandiga. Nataka nimhakikishie ndugu yangu, safari moja huanzisha nyingine. Acha tukamilishe safari hii, lakini safari nyingine tutakamilisha katika kuhakikisha tunapeleka maji Mwandiga.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Chuo hiki cha Mwalimu Nyerere kilijengwa na Wazalendo wa nchi hii, tena kabla ya Uhuru na Mwalimu Nyerere alikipa jina ya Kivukoni lenye maana ya eneo lililopo Chuo kilipo. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hiki kuwa Chuo Kikuu, ili tumuenzi Baba wa Taifa, ukizingatia kwamba Barani Afrika kuna nchi nyingi ambazo wamezipa majina ya Waasisi kama Mandela South Africa, Kenyata Kenya lakini Nkurumah Ghana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Chuo hiki, Mheshimiwa Waziri kuna bweni ambalo limejengwa toka mwaka 2013 kwa ajili ya wanafunzi hawa wa Shahada ya Uzamivu, lakini mpaka sasa halijakamilika. Je, ni kwa nini halijakamilika na ni lini litakamilika na nini kauli ya Serikali katika kukamilisha bweni hilo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y. WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza linaenda kwenye majibu ya swali langu la msingi, tumesema mpango wa Serikali kwa sasa si kupandisha hadhi Vyuo. Vilevile tukubaliane kwamba ili kupandisha Chuo kuwa na level ya Chuo Kikuu, kuna vitu vingi inabidi kuzingatia, kwanza inabidi uunde Kikosi kazi cha Wataalam waende wapitie Mitaala, aina ya Walimu kama wanatosha, eneo lenyewe Hatimiliki ya eneo lao. Kwa hiyo kuna vitu vingi vya kuangalia, lakini kwa sababu tunazungumza kuna vitu vingi vya kufanya, tumesema tuboreshe hivi vilivyopo, itakapofika wakati, Serikali ikaona haja ya kufanya hivyo, tutafanya hivyo kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi ambazo zimewekwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anasema kuna bweni ambalo halijakamilika, naomba hili tulichukue tulifanyie kazi, lakini kwa kweli kama kuna bweni lipo pale na kuna upungufu wa mabweni, tutafanyia kazi ili liweze kukamilika.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali ya nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini naomba kuuliza maswali mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wapo walimu ambao mpaka wanastaafu walikuwa wako katika daraja jipya lakini mlipokuja ku-calculate mafao yao mka- calculate kwa kikokotoo cha mshahara wa zamani. Je, ni lini sasa Serikali mtaona umuhimu wa kuwalipa wastaafu hawa mapunjo yao ya mafao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pesa ya likizo na matibabu kwa walimu hawa ni takwa la kisheria kwa mujibu wa sheria za kazi lakini walimu hawa wamekuwa wakienda likizo au kwenye matibabu pasipo kupewa pesa zao kwa wakati. Je, ni lini sasa Serikali mtaona umuhimu wa kuwalipa walimu hawa pesa kwa wakati mara wanapokwenda likizo au kutibiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Kiza maswali yake ya nyongeza mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua wale waliolipwa mafao yao kwa kikokotoo cha zamani, naomba nitoe maelekezo kwa waajiri wao na Maafisa Utumishi kwenye Halmashauri zetu, twende case by case walifanyie kazi halafu sisi tutashauriana namna bora ya kulishughulikia ili kuondoa changamoto na malalamiko kwa watumishi hawa.

Swali la pili, ni nia ya Serikali kuendelea kulipa watumishi wake na kuwapandisha madaraja kwa wakati. Sasa hivi tumeshafanya calculation na tumejiridhisha kwamba tuna walimu zaidi 86,000 ambao wanaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 43, tuna walimu wa sekondari zaidi ya 18,000 ambao wanadai karibu zaidi ya shilingi bilioni 18. Jumla ya madai ya walimu wote ya madaraja, likizo na malimbikizo mbalimbali kwa maana ya areas zao ni jumla ya zaidi ya shilingi bilioni moja. Kwa hiyo, Serikali imefanya utafiti na uhakiki sasa tunafanya mchakato wa kutafuta fedha ili walimu wetu waweze kulipwa madai yao na kupunguza malalamiko ambayo kwa kweli ni mengi sana. Ahsante.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona naomba kuliza swali kama ifuatavyo:-

Halmashauri ya Kigoma Vijiji ina vijiji cha Mwandiga, Kiganza, Bitale, Mkongoro na Msimba ambavyo mpaka sasa wananchi wanateseka kwa kukosa maji, kipundupindu ni cha kwao, lakini kina mama hata ndoa zao zinakwenda kuhatarika.

Ni lini sasa mradi wa Ziwa Tanganyika na ule wa Kigoma Manispaa utafika katika vijiji hivi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kubwa tunapozungumzia maji, maji ni uhai na sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hatupo tayari kupoteza uhai wa wana Mwandiga. Mheshimiwa Mbunge nilivyokuja ziara katika yetu Peter Serukamba alipiga kelele sana kuhusu suala la kupelekewa fedha ili tutekeleze maji na Mheshimiwa Waziri ametuma fedha tayari na ile kazi itatekelezwa na watalaamu wetu wa ndani katika kuhakikisha wana Mwandiga wananufaika na mradi wa uwepo wa Ziwa Tanganyika kati eneo hilo. Ahsante sana.