Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Catherine Nyakao Ruge (8 total)

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi ya upendeleo. Napenda kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa iliyobarikiwa kuwa na vivutio vya utalii vikubwa ikiwemo Mbuga ya Serengeti kwa upande wa mashariki (Easten Corridor) lakini pia upande wa magharibi (Western Corridor). Je, ni nini mkakati wa Serikali kwa upande wa Western Corridor ambao imeonekana umesahaulika lakini una vivutio vingi vya utalii especially kwenye Ziwa Victoria lakini pia kuna visiwa? (Makofi)
Ina mpango gani wa kuendeleza utalii katika corridor ya Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, historia huwa inaandikwa namna hii na mimi nakuwa ni Naibu Waziri wa kwanza kujibu swali la kwanza kutoka kwa Mbunge, Mheshimiwa Catherine Ruge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza kwanza Mheshimiwa Mbunge na napenda kumkaribisha katika jitihada hizi za kuweza kuwahudumia wananchi. Kuhusu swali lake la nyongeza kwa ufupi kabisa. Western Corridor anayoizungumzia ikiwemo eneo linalopakana na Serengeti upande ule wa magharibi, lakini pia Ziwa Victoria pamoja na visiwa vingine vyote ambavyo Mkoa wa Mara ni sehemu yake. Haya ni maeneo ambayo tayari Serikali imeshaweka mipango thabiti kabisa ya kuyaboresha.
Mheshimiwa Spika, hasa kuhusiana na Serengeti yako malango ya kuingia Serengeti yaliyozoeleka, mengi yanatokea upande wa Mkoa wa Arusha, lakini tumekwishaangalia hili na sasa kutokea Mkoa wa Mara, lakini pia kutokea Mkoa wa Shinyanga, tunakwenda kuboresha mageti ili tuweze kuwaruhusu watalii waingie kutoka kwenye kona zote zilizopakana na Serengeti ili kuweza kuruhusu idadi kubwa zaidi ya watalii kuingia katika maeneo haya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, tuko mbioni kuboresha maeneo hayo na wakati wowote ule tunamkaribisha Wizarani kuja kuleta maoni kwa ajili ya kuboresha utalii. (Makofi)
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ila napenda nikuambie Mheshimiwa Waziri ni asilimia chini ya 30 tu ya wakazi wa Mji wa Tarime wanaopata maji kutoka kwenye Bwawa la Nyanduruma na ambayo siyo safi na salama. Nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kuanzia Shirati kupitia Utegi, Ngiri Juu na kufikisha maji Sirali na Tarime, design ilimalizika mwaka 2011, lakini hapa kwenye jibu lako la msingi umesema design review itamalizika mwaka 2017. Lakini tunafahamu kwamba Benki ya Maendeleo ya Ufaransa, (France Development Bank) walikuwa tayari kufadhili mradi huu, ni nini sasa kinasababisha Serikali itafute mfadhili mwingine ili hali Benki ya Maendeleo ya Ufaransa iko tayari kufadhili mradi huu?
Swali la pili, kwa kuwa Mji wa Tarime ndiyo makao makuu ya Wilaya ya Tarime na ina taasisi mbalimbali kama hospitali, magereza, shule na kadhalika na ukosefu wa maji husababisha mlipuko wa magonjwa, ni lini sasa Serikali itachimba visima hasa kwenye taasisi hizi kama suluhisho la muda mfupi kwa kata zote za Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa review ya mradi bado haijakamilika, hili ni suala la kitaalam unaweza ukalipata juu juu, lakini sisi tunasema review inakamilika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili amedai kwamba anataarifa sijui umezipata wapi, mimi ninafikiri taarifa unazipata za uhakika kutoka kwa sisi wenye Wizara, usipate taarifa za kutoka mtaani. Taarifa za kwetu za ndani ni kwamba bado hatujapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa huo mradi na kwa sababu hatujui ni kiasi gani kinahitajika, kwa ajili ya huo mradi. Kwa hiyo, tukishajua kiasi gani kitahitajika ndio sasa tutachukua hatua za kutafuta fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli kwamba Tarime ni Makao Makuu ya Wilaya, lakini kwa kwa hatua za dharura Mheshimiwa Catherine ni kwamba tumechimba kisima kimoja tayari, tumekarabati visima viwili, tumeongeza mtandao wa kilometa 30 wa mabomba na ndiyo maana sasa tunaingia mkataba kwa ajili ya kuboresha chanzo cha Nyandurumo kama nilivyokuwa nimezungumza katika swali langu la msingi, lakini pia tutaendelea na kwa sababu tumetenga fedha niombe kwamba mwambie Mkurugenzi wako, aendelee kuweka mapendekezo kwa ajili ya kuongeza visima vingine ili maeneo ya mji, hospitali, taasisi za shule, ziweze kupata maji bila matatizo yoyote.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya ngongeza. Katika jibu lako la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri, ameonesha kwamba kuna mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vinne na tayari hekta 6,000 zimeshapangwa kwa ajili ya mradi huo. Ni dhahiri kulikuwa na wananchi wa vijiji hivyo wanaozunguka Bonde la Mto Mara ambao walikuwa wanafanya shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi wa samaki. Napenda kujua; Je, Serikali imetenga eneo gani mbadala na fidia ili wananchi waendelee kunufaika na shughuli zao sambamba na uwekezaji huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Mkoa wa Mara umekuwa uki-experience vipindi virefu vya ukame vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha uwekezaji huu hauendi kuathiri bioanuwai pamoja na mfumo mzima wa Serengeti Ecosystem ambayo Bonde la Mto Mara ni sehemu ya mradi huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna wananchi ambao wataathirika katika mradi huo ni dhahiri kwamba hatua zozote zitachukuliwa kuhakikisha kwamba madhara hayo yatapunguzwa ikiwa ni pamoja na kampuni ambayo itahusika katika kufanya uwekezaji kulipa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mradi huu ni mradi wa siku nyingi sana, umekuwa ukifikiriwa tokea miaka ya sabini, kimsingi eneo lile lina hekta 14,000 na kwa muda huo wote jitihada zimekuwa zikifanyika kuwaeleza wananchi kwamba sehemu hiyo itatumika kwa ajili ya shughuli ya kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari, lakini kama kuna wananchi ambao wataathirika watafidiwa kwa taratibu zilizopo za sheria zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali muhimu sana linalohusiana na athari za kimazingira ambazo zinaweza zikajitokeza kwa maji ya Mto Mara kutumika kwa ajili ya shughuli ya kilimo vilevile kwa ajili ya shughuli ya kiwanda kile. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla mradi haujaanza ni lazima tathmini ya kina ya mazingira ifanyike ikiwa ni pamoja na tathmini ya kijamii ili athari zozote zile ambazo zinaweza zikajitokeza ziweze kuangaliwa na ikiwezekana kama athari zile zitakuwa ni mbaya sana mradi usiendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikolojia ya Serengeti ni muhimu kwa ajili ya nchi yetu. Kwa hiyo kwa vyovyote mradi wowote ambao una hatari ya kuathiri katika njia mbaya hautaweza kuendelea. Nimhakikishie tu kwamba ni lazima tathmini itafanyika ili kuzuia uharibifu wowote.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Tatizo la uhaba wa maji katika Wilaya ya Serengeti hasa vijijini, limekuwa ni kubwa na la muda mrefu na kuanzia mwaka 2007 mpaka sasa hivi Serikali bado inatekeleza mradi wa maji katika vijiji kumi, ila mpaka ninavyozungumza kuna miradi miwili katika vijiji vya Kenyana, Nyamitita na Kibanjabanja haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua, ni lini sasa miradi hii itakamilika ili wananchi wa maeneo husika waweze kupata maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Catherine amezungumzia baadhi ya miradi ambayo ipo kwenye Halmashauri yake na kuniuliza ni lini miradi ile itakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba itabidi nifuatilie niweze kujua, kwa sababu hili ni swali la nyongeza, siwezi kuwa najua kila kijiji katika nchi nzima, mradi ule uko katika status gani? Kwa hiyo, naomba sana tuonane naye, anakaribishwa ofisini ili tuweze kuangalia. Nitampa status na taarifa kamili ni lini miradi ile itakamilika.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zenye matundu madogo na baruti limekuwa la muda mrefu kwenye Ziwa Victoria, lakini pia maziwa mengine hapa nchini. Ni nini mpango wa Serikali kuwekeza kwenye vizimba (fish cadge) njia ambayo ni salama na yenye ufanisi ili kuwawezesha vijana wa Kanda ya Ziwa kuendelea kujiajiri katika sekta ya uvuvi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Ziwa Victoria hakuna uvuvi wa mabomu, uvuvi uliopo ni uvuvi wa kutumia zana ambazo hazijaruhusiwa kutumia makokoro na zana zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wavuvi ili waachane kabisa na uvuvi ambao sio endelevu na katika hili tunahakikisha kwamba tunashirikiana na Halmashauri na vilevile Mheshimiwa Mbunge tunaomba na yeye atusaidie ili kuendelea kuhamasisha wavuvi wa kule anakotoka ile wafanye uvuvi ambao unaendana na taratibu za sheria.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ili na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya benki kutofanya vizuri au kuwekwa mufilisi husababishwana non- performing loans au mikopo chechefu. Hesabu za Benki ya Wanawake za mwaka 2015/2016 zinaonyesha asilimia 80 ya mikopo ni mikopo chechefu (non-performing loans). Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inainusuru benki hii ili isiende kuwekwa mufilisi ili iweze kuwasaidia wanawake wa Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, uendeshaji wa benki na taasisi zote za kifedha hufuata Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006. Nimesema Benki Kuu imekuwa ikisimamia taasisi zote hizi za kifedha kuhakikisha zinafanya vizuri. kutokana na tatizo la mikopo chechefu, Benki Kuu ya Tanzania imewaandikia na kutoa mwongozo kwa taasisi zote za kifedha kuhakikisha kwamba wanakuwa na mkakati na mkakati huo unawasilishwa Benki Kuu ya Tanzania ya jinsi gani wanashughulikia tatizo hili la mikopo chechefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho ndicho kinachoendelea kwa sasa kwa sasa mabenki yote yamekuwa makini katika kuhakikisha wanatoa mikopo kwa ajili ya nini na kwa nani kuzingatia na vigezo walivyojiwekea. Kama Serikali tuna uhakika kwamba tizo hili la mikopo chechefu litaondoka baada ya mabenki yetu na taasisi zetu za kifedha kuongeza umakini katika utoaji wa mikopo. (Makofi)
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Swali langu la kwanza, natambua halmashauri zetu zote Tanzania zinatakiwa kuwapatia asilimia mbili vikundi vya ujasiriamali vya watu wenye ulemavu. Swali langu, je, ni kiasi gani cha pesa kilitolewa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda Serikali imewaandalia mazingira gani watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki moja kwa moja kwenye uchumi huo kwa kupata fursa ya ajira, fursa ya kujiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na fursa ya kupata masoko kwa ajili ya bidhaa zao? Ahsante.
WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Catherine Ruge kama ifuatavyo, nikianza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi na nzuri na majibu mazuri aliyoyatoa leo Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiendelea na hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu jana suala hili la asilimia 10 katika mifuko ya Halmashauri za Wilaya ilijitokeza. Ninaomba nikubaliane na maelekezo ama kauli ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI jana kwamba maeneo yote yanayohusiana na asilimia 10 yatatolewa maelezo katika bajeti itakayoanza leo inayohusu Ofisi ya Rais, TAMISEMI na hivyo tutaweza kuwa na maelezo fasaha.
Lakini la pili, kuhusu namna nzuri ya kuwafanya watu wenye ulemavu kuingia nao katika uchumi wa viwanda, kama tulivyotoa maelezo jana wakati tunahitimisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, suala hili ni suala la kisheria liko ndani ya sheria ya watu wenye ulemavu namba tisa ya mwaka 2010. Kwa hiyo, sisi sasa tunachokifanya ni kusimamia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu kutoa rai kwa watu wote na wawekezaji wote ambao wanaanzisha viwanda katika nchi yetu ya Tanzania kuona kwamba wenye ulemavu nao wanaouwezo wa kutoa mchango katika ujenzi wa taifa kupitia auchumi wa viwanda hivyo basi wawape fursa kwa kuzingatia sheria ambayo tuko nayo na sisi kama Wizara tutaendelea kusimamia kuona jambo hili linatekelezwa.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nachelea kusema level ya seriousness kwenye hili jambo bado ipo chini sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2019 Serikali ilitenga shilingi milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari kwenye kata zenye mazingira magumu, lakini kwenye taarifa hii ya utekelezaji ukurasa wa 132 mpango huu umetekelezwa kwa asilimia sita tu. Ningependa kufahamu, ukiwa umebaki mwaka mmoja kukamilika kwa mpango huu ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa wabweni haya kwenye shule kumi ili kupunguza adha kwa wanafunzi wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Serengeti yenye Kata 30 ina shule za sekondari kwenye Kata 21 tu na Kata 9 hazina shule za Kata. Kata hizo ni Lung’avule, Getasamo, Kiambai, Morotonga, Sedeko na kadhalika. Ningependa kufahamu ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa shule za sekondari kwenye hizi kata tisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ruge amenukuu Mpango wa Taifa wa miaka mitano na mimi kwa niaba ya Serikali napenda nimuhakikishie kwamba mpango ule tunaendelea kuutekeleza mwaka hadi mwaka na itakavyofika mwisho mwaka wa utekelezaji wa mpango wa miaka mitano, malengo mengi yaliyomo yatakuwa yametekelezwa. Mheshimiwa Mbunge naomba asiwe na wasiwasi na awaarifu wananchi ambao anawawakilisha kwamba tutatekeleza mpango ule na utakapofika mwisho wa mwaka utekelezaji wake tutakuwa tumefikia malengo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kwenye Wilaya ya Serengeti kwamba ina kata 30; kata 21 zina shule za sekondari na kata tisa hazina shule za sekondari na akauliza lini tutajenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali lake la msingi ni wazi kwamba kata hizo ambazo hazina shule sekondari wanafunzi wake ni miongoni mwa wanafunzi ambao wanatembea umbali mrefu kufuata shule kwenye kata za jirani. Nimehimiza kwenye jibu la msingi kwamba Halmashauri iendelee kushirikiana na wadau wengine pamoja na wananchi kuhakikisha kwamba Kata hizo zinaanza ujenzi wa shule na Serikali itaingia kusaidia mara watakapoanza ujenzi huo. (Makofi)