Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rev. Dr. Getrude Pangalile Rwakatare (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. GERTRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa
Mwenyekiti, niungane na wenzangu wengi kwa kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa uongozi wake mzuri. Naomba nimpongeze kwa kipekee Waziri wa Ujenzi na wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri na kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa juhudi za Mheshimiwa Rais wetu kutuletea Ndege mbili jumlisha nne, jumla yake sita. Hii imeturahisishia usafiri mikoani na imetuondolea aibu Kitaifa, nasi tuna ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa ujenzi wa daraja la Kilombero, limekamilika na limekuwa kiunganishi kati ya Wilaya ya Kilombero na Ulanga. Ni ukombozi mkubwa, Tunampongeza Mheshimiwa Rais wetu na Mheshimiwa Waziri na timu yake. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuona barabara ya Kidatu – Ifakara – Malinyi –Songea; Ifakara – Kihansi Road zote ziko ndani ya Bajeti ya 2017/2018 na Dumila – Kilosa – Mikumi, kweli mnachapa kazi Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaombea Mungu awape uwezo na afya mfanikiwe, Mungu aibariki Wizara ya Ujenzi, Waziri wake na timu nzima. Amina.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
HE. DKT. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. Namshukuru Jehova Mungu wa Mbinguni, Elishadai, mwenye uwezo wa kunirudisha tena Bungeni. Namshukuru kwa afya na uzima, wote tumeweza kufika salama na kulinda familia zetu, Mungu wetu ni mwema. Bwana asifiwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda nimshukuru Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniona, kunikumbuka na kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mungu ambariki sana, sana, sana na Mungu amlinde. Namwahidi nitamwombea, Mungu ampe afya njema, Mungu aweze kumpa uongozi bora na kuwe na amani na utulivu kabisa siku zote za uongozi wake. Mungu ampe maisha marefu, aishi akiona vijukuu hadi vitukuu kwa utukufu wa Bwana. Kwa kweli ni mwema, ni mwaminifu; kwa kweli ni mchapakazi, ni jembe; ni komandoo na anaweza. Ahadi yangu kwake sitamwangusha, nitaendelea kumwombea siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niwashukuru wanawake wote wa UWT Tanzania nzima kwa maombi, kwa simu zao za kunitia moyo na kunipongeza. Naahidi pia kwamba nitafanya kazi na UWT kwa uwezo wangu wote. Wanawake, kaeni mkao wa kula, nakuja tufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kushukuru Kanisa langu la Mlima wa Moto, Mikocheni ‘B’, Assemblies of God kwa maombi yao; nikianza na Wachungaji, Wazee wa Kanisa na Washirika wote. Ahsanteni kwa maombi yenu. Nashukuru. (Makofi)

Mungu wetu ni mwema.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuishukuru familia yangu. Mama yangu mzazi, familia yangu, kaka zangu, dada zangu na watoto wangu wote. Ahsante kwa kunivumilia na kunitia moyo. Mungu awabariki. (Makofi)

Pia naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na pia Watanzania wote, kwa msiba mkubwa tulioupata kwa kupotelewa na watoto wetu kwa ajili ya basi huko Karatu. Mungu aziweke roho zao mahali pema, peponi.

Nawaombea wazazi wao faraja, nawaombea Mungu awape amani, wakubali yote kwa sababu kazi ya Mungu haina makosa. Bwana alitupa na Bwana ameatwaa, jina la Bwana libarikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii niweze kuchangia katika hotuba hii nzuri ya Wizara ya Viwanda Biashara…

WABUNGE FULANI: Waliongea bila kutumia vipaza sauti.

MHE. DKT. GETRUDE P. LWAKATARE: Eeh, jamani, mimi Mchungaji, msinitanie! (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii niweze kuchangia katika hotuba hii nzuri ya Wizara ya Viwanda Biashara nikianza kumpongeza kwanza kabisa Waziri, Mheshimiwa Mwijage, shemeji yangu. Anafanya kazi nzuri kwa kweli. Kazi imepata mtu! Siyo mtu amepata cheo, lakini ukweli cheo kimepata mtu sahihi. Anafanya kazi nzuri, tunafurahi na timu yake yote. Yaani kama uhamasishaji, ameufanya, tumeona wawekezaji wakiingia na kutoka Tanzania; tumeona kwamba viwanda vingi vimefunguliwa na hata hivyo tunaona pia juhudi yake, bado anajitahidi. Hata kama watu wakitupa madongo, nasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Jamani, mtoto wa Kihaya anafanya kazi nzuri, tumshukuru. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumtia moyo Mtumishi wa Mungu Mheshimiwa Mwijage pamoja na timu yake ya kwamba aendelee mbele, azibe pamba masikio; mema ayachukue, lakini yale ambayo ni ya kukatisha tamaa ayaache. Abantu baabi! Wahaya wanasema: “watu wote siyo wema, wengine wabaya.” Kwa hiyo, jipe moyo, songa mbele.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa asilia inajulikana kwamba watu wengi humshukuru na kumsifu mtu akifa. Siku ya tanzia ndiyo wanasema ooh, alikuwa hivi, alikuwa hivi. Kwa hiyo, usijali, songa mbele. Rome was not built in a day, you have tried. Umejaribu ulivyoweza. Lazima tuanze kidogo, polepole tutapanda, huwezi kuamini, pengine baada ya miaka mitano Tanzania ndiyo itaongoza kwa viwanda vingi kuliko kote East Africa nzima. Kwa dira hii tunayoiona tumeridhika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe ushauri kwa sababu kwa kweli kazi ni nzuri sana na mwanga tunauona. Ushauri wangu wa kwanza, ni punguzo la kodi. Jamani kodi Mheshimiwa Waziri ungekaa na Waziri wa Fedha mkaangalia ni jinsi gani mnaweza kutoa incentive ya kutosha kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na hata wa nje. Yaani kodi ni kikwazo, kwa sababu kwa kweli ukihesabu, kodi ni nyingi mno. Zinakatisha tamaa, hata mwisho ukijaribu kujumlisha unakuta kwamba faida ni ndogo sana. Inakatisha tamaa wawekezaji na wengine wanafunga kabisa viwanda au wanafunga kabisa biashara zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya Viwanda inawezekana, lakini pia tuangalie hao wanaowekeza; wanakopa, wana madeni na wana mambo mbalimbali. Kwa hiyo, lazima tuangalie na sisi kama Serikali tuone tunawasaidiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ushauri wangu mwingine, nasema pia ili kuwa na Tanzania ya viwanda, ni lazima kuwe na umeme wa uhakika. Umeme wetu kwa kweli siyo wa uhakika. Kama mnavyoona, mara nyingi unakatika na pia tozo inakuwa kubwa mno. Hasa ukiwa na kiwanda, ndiyo kabisa, yaani jiandae kulipa mamilioni. Hata kama unatumia diesel, vile vile hata diesel ni bei. (Makofi)

Kwa hiyo, unakuta kwamba mwenye kiwanda anakata tamaa, maana yake faida ni ndogo mno. Kama kweli tungekuwa nao bega kwa bega kwa kuwasaidia pamoja na kuhamasisha kuja kuwekeza Tanzania, pia tuwasaidie na wao waweze kupata faida ili walipe madeni yale ambayo wamekopa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MCH. DKT. GETRUDE J. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Pia nashukuru kwa kazi yako nzuri sana ya kiwango unayoifanya, Mungu akubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi adimu ya Rais wetu wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa kweli Rais Magufuli anastahili pongezi za dhati. Kama mtu haoni alichokifanya basi hana macho, huyu ni kipofu. Kama kweli yeye ni Mtanzania anasimama hapa siku zote anapinga ufisadi, anapinga mambo mabaya, halafu tena haoni alichokifanya, basi huyu mtu siyo Mtanzania halisi anajifanya tu. Inabidi tumwombee Rais wetu kwa hali na mali. Katika Isaya 54:17, unasema; kila silaha itakayoinuka juu yake isifanikiwe kwa Jina la Yesu. Kila ulimi utakaosimama kumpinga, tunaupinga wenyewe kwa Jina la Yesu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa fupi Jumapili ni Ibada Maalum ya kumwombea Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, kuombea Taifa letu na Bunge letu. Tutakuwa Mikocheni B, Kanisa la Mlima wa Moto, njooni jamani tukutane na Mungu aliye hai.

Hata kama unabisha lakini Mzungu si mmemwona, Mzungu si amekuja, amekuja mwenyewe bila kuitwa kwa tiketi yake. Amesema amekuja na ndege yake mwenyewe. Sasa kama amekuja kukubali yaishe kuna ubaya gani?

Si lazima tujipongeze. Hata kwa yale mazuri jamani pia tunapingana kwa vipi? Amekutana Ikulu, kumbe ulitaka akutane naye wapi Feri, Kariakoo au Buguruni au wapi? Nyumbani kwake si Ikulu amekutana naye, ni vizuri na wote tunashukuru, Mungu amejibu maombi.

Waseme wasiseme lakini hata nchi jirani wote wanasema, wanatupigia simu hongereni Tanzania, hongereni kwa kazi nzuri, hongereni kwa Rais mzuri. Kwa hiyo, lazima tumpongeze sana, amejitahidi kwa muda mfupi kaondoa wafanyakazi hewa, amegundua makontena ya mafisadi, amenunua ndege, amejenga barabara na kadhalika, si lazima tumshukuru. Mnataka nini jamani gunia la chawa au awabebe mgongoni? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametoa vifaa tiba Wilaya zote na ambulance amejitahidi kama mwanadamu. Elimu bure, jamani kazi alizofanya ni kama miaka 60, mimi naongeza na 30 kama miaka 90, Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye bajeti yetu, napenda kuipongeza bajeti kuu ya Wizara ya Fedha chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri wake, kwa kweli ni bajeti ya kihistoria iliyoacha simulizi mitaani. Ni bajeti iliyomjali hata mtu wa chini, mnyonge hadi mama lishe hadi mfanyakabiashara ndogo ndogo, wote wameguswa. Nje wenzetu wanafurahia lakini hapa ndani watu wanabisha. Sasa walengwa wamefurahia lakini wewe kwa sababu siyo mlengwa ndiyo maana hata wala huoni umuhimu wake, pole. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama jinsi alivyoweza kufuta road licence, tazama jinsi ilivyoweza kupunguza kodi mbalimbali yaani ili mradi wamefanya walichoweza. Jamani kuna mabadiliko mabwa mwaka huu. Watu wanasema ni mwaka wa neema, ni bajeti ya neema wamefanya kile ambacho walichoweza kufanya, lazima tuwapongeze. Mheshimiwa Dkt. Mpango hongera sana, pongezi nyingi na mama pale, pongezi nyingi na Wizara nzima kwa kazi nzuri na mabadiliko makubwa waliyoyaleta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie jambo moja ambalo ni kodi kwa ajili ya shule binafsi nikisema kwamba mimi pia ni mdau mmojawapo, na- declare interest. Mheshimiwa Waziri Dokta Mpango kodi katika shule binafsi zimezidi. Kuna kodi zaidi ya 25, mpaka unashangaa sisi nasi tunachima madini au nini, wakati sisi tunafundisha watoto wenu. Waangalieni sana kodi ni nyingi hata akikaa na timu yake ingetakiwa wafute kodi zote katika shule kwa sababu shule ni huduma siyo biashara na huduma tunazofanya ni kwa faida ya Taifa zima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa walikuwa wanakwenda Kenya, Uganda na nchi nyingine za jirani lakini sisi tumefanya hawa watoto wasome Tanzania, waweze kujifunza historia yao, wajifunze jiografia yao, wajue viongozi wao, lakini zamani walivyokuwa wanakwenda nchi jirani utakuta akiulizwa wewe Rais wako nani, inabidi aseme Uhuru Kenyatta. Kwa sababu akisema mimi Rais wangu Dokta John Pombe Magufuli atakoseshwa, japo yeye ni Mtanzania yuko nchi ya kigeni, lakini sisi tumeleta fikra za watoto kubadilika kwa kusoma wakiwa wadogo ndani ya nchi baadaye wakiwa wakubwa ndiyo waende siyo mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi mtusaidie yaani jamani tunachajiwa hata majengo, tunaambiwa property tax, hasa yale majengo si ya shule, si watoto wenu ndiyo wanasoma? Mbona shule za Serikali hawatozi kwa nini sisi tu ndiyo mtutoze? Unaambiwa hata vile viwanja tumejenga shule wanakuambia bwana lazima ulipe kodi kama vile kiwanja cha biashara yaani kama kiwanja umefanyia biashara kubwa fulani. Hakika wakitusaidia katika hilo itakuwa ni unafuu kwa ajili yetu na hata kwa ajili ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiangalia wenyewe ile karo tunayotoa ni ndogo mno. Watoto hawa wanakunywa chai asubuhi, saa nne wanakunywa tena na wenzao wa day scholars, mchana wanakula chakula, jioni wale boarders wanakula mlo kamili, sasa hivi vyakula vyote ni gharama. Vilevile wanapewa magodoro na vitanda, wana matron na patron wanaowalinda, kuna daktari na manesi wanaowatunza watoto wetu ili wakae vizuri. Waangalie watuhurumie, watusaidie tufanye kazi pamoja kwa sababu hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MCH. DKT. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi. Naomba awali ya yote nimshukuru Mungu, Baba yetu wa Mbinguni ambaye ametuazima uhai, anatupa afya njema na tuko Bungeni kwa furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa niwadhibitishie kwamba ndani ya Bunge mna Bishop, ndani ya Bunge mna Mchungaji ambaye haachi kuomba kwa ajili ya Spika, Naibu Spika, Wenyeviti wote na Bunge zima; wa CCM na hata Wapinzani, wote ninawaombea Mungu awape kibali kwenye Majimbo yenu kwa jina la Yesu. Namwomba Mungu awape afya njema katika Jina la Yesu. Naomba
Mungu awape maneno matamu, kila mnalolisema liwe sukari masikioni mwa wasilizaji. Yaani mwende kifua mbele kwa kibali kwa wanaume na wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa napenda nitoe shukrani za dhati kwa Rais wangu kipenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameniteua na leo niko Bungeni pamoja nanyi. Mungu ambariki, ampe maisha marefu. Tunapongeza kazi anazozifanya mpaka nchi jirani wanatetemeka. Kwa kweli ni mtu mwema, ni jembe, yeye hakika ni bulldozer, anafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwa mwenye dhamana ya Wizara hii. Namshukuru kipekee kabisa na nimpe pongezi nyingi Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi nzuri unayoifanya. Wanawake wenzako tunajivunia. Kwa kweli hujatuaibisha. Kila kitu unafanya kwa umakini.

T A A R I F A . .

MHE. MCH. DKT. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naikataa ila namwombea, Mungu amsaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na wasaidizi wake wote. Tunasema mabadiliko makubwa tunayaona, asiyekuwa na macho shauri yake. Ukweli tumeona kwamba huduma zilizokuwa zinapatikana nchi za nje, sasa hivi zinapatikana hapa hapa Tanzania, umejitahidi. Siyo hivyo tu, upatikanaji wa dawa sasa hivi ni 85% na bado unasema utaongeza zaidi. Jamani, uimarishaji wa huduma katika vituo vyetu vya afya na hospitali, tumeona huduma za afya zimeimarika kwa kiwango kikubwa sana, tunashukuru na kwa sababu muda wangu ni mfupi, ningependa tu niende moja kwa moja kwa kile ambacho ningependa kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kuhusu kinga, tiba bila malipo. Magonjwa mengi yanayotupata Watanzania kwa sababu wengi wanakosa elimu ya kutosha. Nilikuwa naomba tuongeze, kwa mfano, UKIMWI; UKIMWI ni ugonjwa ambao unaweza kuepukika. Tuombe viongozi hata wa dini kwenye mahubiri yao waongeze juhudi ya kuweza kuwaambia watu, wanandoa waweze ku-stick na rafiki au na mke mmoja ambaye ataweza kumsaidia, yaani kama Waebrania 13:4 inasema: “Ndoa iheshimiwe na watu wote, malazi yawe safi.”

T A A R I F A . . .

MHE. MCH. DKT. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea. Ni nzuri na ninaombea. Awalete wengi niwaombee wapone, Mungu yupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasema kwa habari ya kitabu cha Waebrania 13:4, “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, malazi na yawe safi, washerati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu ya magonjwa yasiyotibika.” Magonjwa yasiyotibika ni UKIMWI na mwengine. Kwa hiyo, kama mtu akiweza kukaa na mke wake bila kwenda mchepuko au nyumba ndogo, uhakika watampendeza Mungu, lakini zaidi sana watajikinga na magonjwa. Watalea watoto wao, kifo ndiyo kitawatenganisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema yeye ambaye ametupa zawadi ya uhai, ametupa zawadi ya afya, ametupa zawadi ya maji, ametupa zawadi ya ulinzi, na hakika tunasafiri na kurudi kwa sababu ya ulinzi wake. Mungu wetu ni mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tena kuchukua nafasi hii niweze kumuweka kila mmoja wetu hapa mikononi mwa Mungu aweze kuwatetea nakuwalinda kwenye Majimbo yenu kazi zenu ziweze kwenda salama.

WABUNGE FULANI: Ameeen!

MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Lakini zaidi ya yote tuombe maombi rasmi kwa ajili ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, hakika kabisa tumepata chuma, tumepata jembe, lakini tumepata baba yeye hakika ana upendo, ana huruma, anafanya kila kitu ili mradi kuhakikisha Watanzania tukoa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba apate kibali kwa watu wote wanaume, wanawake jina lake liwe sukari midomoni mwa watu, jina lake liwe chumvi na ulinzi wa Mungu uwe juu yake kwa jina la Yesu. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Ameen.

MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua pia nafasi hii niweze kumkumbuka Mheshimiwa Dkt. Reginald Mengi mfanyabiashara mashughuli pia tukikumbuka katika bajeti yetu ya maji yeye ndio aliyeanzisha maji ya chupa Kilimanjaro, yeye ameanzisha ITV mambo mengi tu amefanya, ana huruma anakula na watu wenye shida, watu walemavu, kwa hivyo amefanya kazi nzuri Mungu aiweke roho yake mahali peponi.

WABUNGE FULANI: Ameen!

MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Tunaomba pia kwa ajili ya faraja katika familia yake, tunaomba kuwe siku zote na amani Mungu atende na hakika msiba huu uishe salama kwa Utukufu wa Bwana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwisha kusema hayo ningependa niweze kutoa pongezi maalum kwa Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa kwa ajili ya kazi nzuri na timu yako mnayoifanya katika Wizara hii ya Maji. Kwa kweli tunaona mabadiliko makubwa na pia tunaona kwamba mko wasikivu katika mambo ambayo tunawashauri mnafanya na tunaona kwa kweli hata kule kwetu Kilombero kuna mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nijikite kwenye maji safi na salama hakika kabisa mnajua maji ni kila kitu na lengo letu ni kumtua mwanamke ndoo ili aweze kupumzika maji yafike nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano natoka Mkoa wa Morogoro kuna Mito 177 hiyo mito ni ya kudumu sio ile mito ya kukauka, pia katika Wilaya ya Kilombero ambako natoka pia kuna mito 38 ya kudumu na sio mito ile ya kukauka, tukijumlisha tuna mito mingi. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi hawajafikiwa maji safi na salama inabidi wakachote mtoni, inabidi wakatafute ni shida. Lakini nilikuwa naomba katika bajeti hii Mheshimiwa Waziri tunaomba utuhurumia watu wa Kilombero ya kwamba uweze kuangalia kwa maana maji yapo Mungu ametupa neema tatizo kubwa ni miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ni mibovu ni mizee ya siku nyingi na vilevile watu wengi wameongezeka zamani Kilombero tulikuwa watu 300,000 siku hizi tunakaribia milioni moja kwa sababu watu wengi wanahamia kwa ajili ya kilimo na kwa ajili ya kufuata maji. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri iangalie Kilombero kwa hali ya huruma kabisa tumevumilia miaka mingi. Nakumbuka ya kwamba miundombinu ile ilikuwa kama Ifakara Mjini ilikuwa ni ya watu 7000 enzi hizo sasa hivi wako watu wengi zaidi ya 300,000 yaani Mji wa Ifakara peke yake. Kwa hivi tunaomba kwa kweli mtusaidie ili na sisi tuweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumependa pia kumpongeza Waziri ya kwamba hakika kwa utendaji wake bora na timu yake tumeona ya kwamba sasa hivi kipindupindu ni kama kinatokomea vile kwa maana kwa kweli hatusikii tena magonjwa ya kipindupindu na hiyo ni kwa sababu maji yapo watu wanapata maji ya kutosha, watu wanapata maji na ndio maana unakuta magonjwa yale nyemelezi ya siku nyingi sasa hivi yamepungua. Kwa hivi tunasema ahsante kwa kazi nzuri mnayoifanya muendelee mbele ila zingatia Kilombero iipe kipaumbele cha peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tena nichukue nafasi hii nikiangalia kwamba sisi tunasema Kilombero ni ghala la chakula au Morogoro ni ghala la chakula lakini pamoja na kwamba Mungu ametubariki na mito 177 kimkoa, mito 38 Kilombero lakini ulimaji wa kilimo cha umwagiliaji ni percent 2.7 tu, maji yapo tatizo lile lile ni miundombinu mtusaidie kwa sababu sisi hatuna shida kama mmeweza kuchota maji kutoka kwenye maziwa mkawapelekea watu ni rahisi zaidi kama watu wana mito kila kitu kipo ni miundombinu tu kuwapelekea watu. Tena hii inakuwa ni kama ulinzi wa vyanzo vya maji kwa sababu kama watu watapata maji ya kutosha wana haja gani kuharibu vyanzo vya maji wale ndio wanakuwa walinzi wetu. Kwa hivyo tujitahidi kutoa maji ya kutosha ili watu wale wasiwe waharibifu wa vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu nilikuwa napongeza Serikali kwa ajili ya mradi mkubwa wa Stigler’s Gorge kwa kweli ni mradi mzuri hakika kabisa utatupa umeme wa kutosha na hata ziada lakini ninavyoona kwa uharibifu wa bonde la Kilombero itakuwa ni ngumu ule mradi kuweza kwenda smoothly kwa sababu watu wengi wamevamia vyanzo vya maji. Kwa hivi dawa ni ile ile tufanye juu chini kwa uwezo wote kama ikiwezekana tukisambaza maji kila mahari watu waweze kupata maji ya kutosha kwa matumizi yao, kwa matumizi labda ya wanyama wao hakika tutaweza kuufanya ule mradi wa Stigler’s Gorge uweze kumalizika vizuri na hakika utakuwa Baraka kwa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ningependa pia kuwapongeza kwa ajili ya sehemu ambazo hazina maji naona mnasaidia kuweka visima lakini tatizo kubwa ni uangalizi management ndio inapungua kwa hivi tunaomba muimarishe kwenye upande wa management kwa sababu watu wengi wanakuwa wanaharibu ile miundombinu kwa hivi mwisho unakuta maji hayawafikii watu sawasawa kwa sababu wengine wanachukua njiani, wengine wanafanya hivi tuangalie pia management yetu katika wizara yetu ili hakika maji tunayowapelekea watu yawafikie na yaliwafikia ni ulinzi na kama ulinzi pia na hapo tunaweza kuwa tuna save pesa badala ya kupoteza pesa. Kwa maneno haya machache ningependa kuunga mkono hoja mia kwa mia na Mungu awabariki. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DKT. GERTRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri mnayoifanya, tunashukuru kwa jitihada zenu zote japo bajeti hii ni finyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Wabunge wenzangu kuomba nyongeza ya bajeti hiyo. Maji ni uhai, maji ni afya na maji ni viwanda. Kila taasisi inahitaji maji mashule,vyuo, hospitali na kadhalika, tunaomba Wizara hii muhimu ipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri Wizara kuungana na Wabunge kupiga vita, wafugaji wanaonywesha mifugo yao kwenye vyanzo vya maji. Kwa mfano,Wilaya ya Kilombero ni bonde zuri kwa kilimo, lakini mifugo imesababisha mito kukauka, wakulima kunyanyasika na wageni wafugaji kwa sababu ya mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Mfuko wa Maji Vijijini uanzishwe kama ilivyo kwenye umeme itasaidia sana.

Mwisho ninawapongeza sana kwa miradi mingi ya maji inayofanya vizuri sana, tunawaombea bajeti iongezwe ili mfanye vizuri zaidi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GETRUDE P. RWAKATALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa hotuba nzuri. Barabara ya Kidatu – Ifakara ujenzi wake unasuasua kwa nini? Tunaomba Waziri Mkuu aingilie kati. Tunaomba Wizara ya Ujenzi iingilie kati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MCH. DKT. GERTRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nimpongeze sana Waziri Mheshimiwa Kangi Lugola kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ujambazi umepungua kwa kiasi kikubwa sana, tunatembea kwa uhuru, ajali za barabarani zimepungua mno na uvamizi wa mabenki pia umepungua sana. Hongereni.

Mheshimiwa Spika, naomba nyumba za askari Ifakara - Kilombero zijengwe, wana shida kubwa ya makazi. Pia tunaomba Mahakama ya Ifakara ijengwe, wakati wa masika, mafuriko yanaathiri wafungwa, mafaili, ofisi na ni kero kubwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kwa kazi nzuri sana wanayofanya na timu yake. Kukarabati shule kongwe ni kazi nzuri sana, ajira kwa Walimu wapya, ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike na kutoa elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri kuhusu adhabu ya watoto watoro zaidi ya siku 90 itolewe, pia kwa candidate classes. Hivyo ilivyo inaharibu jina la shule, nafasi ya shule, maana watoto kama hawa hujitokeza siku za mitihani tu. Kukariri darasa kungezingatiwa ili elimu iimarishwe na ukaguzi wa shule uwe wa mara kwa mara.