Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Salma Rashid Kikwete (8 total)

MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:-
Sayansi na teknolojia imeleta mapinduzi makubwa sana kwa maendeleo ya mwanadamu, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi ambazo zimerahisisha sana mawasiliano na huduma za kifedha; pamoja na mazuri hayo baadhi ya vijana na makundi rika mengine husikiliza simu kwa kutumia headphones na hatimaye hupoteza uwezo wa kusikia (uziwi):-
(a) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kutoa tamko kwa vijana hao kuacha matumizi yasiyokuwa na tija?
(b) Je, Serikali haioni ni vema simu zinazoingizwa nchini ziingizwe bila headphones kwa ajili ya kuwanusuru na uziwi vijana hao ambao ni tegemeo la Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, Mama yangu, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kitaalam hakuna taarifa za kitabibu kuhusu madhara ya utumiaji wa mara kwa mara wa headphones kwa muda mrefu. Aidha, vifaa vyote vya mawasiliano zikiwemo headphones huwekewa viwango na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano Duniani (International Telecommunication Union – ITU) kwa ajili ya matumizi salama, hivyo, hakuna madhara ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa kuwa vimethibitishwa Kimataifa. Kwa hapa nchini Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wana jukumu la kuhakiki viwango vya vifaa vya mawasiliano kabla havijaanza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kutoa tamko kuwaasa vijana wanaotumia muda mwingi kwenye matumizi ya headphones waache na watumie muda mwingi katika ujenzi wa Taifa kwa kufanya kazi kwa ufanisi ili kuwa na maisha bora. Wizara yangu kwa kushirikiana na taasisi husika itaendelea kutoa elimu katika masuala mbalimbali ya matumizi ya TEHAMA ili kuleta tija na uelewa sahihi wa matumizi ya TEHAMA pamoja vifaa vyake.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, headphones ni sehemu ya kifaa ambatanishi (accessory) cha simu ambacho humpa mtumiaji husika uhuru wa kusikiliza sauti inayotoka kwenye simu yake kutegemea na kitu anachosikiliza bila kusababisha uchafuzi wa mazingira wa sauti (sound pollution) au usumbufu usio wa lazima kwa watu wengine. Aidha, vifaa vya mawasiliano vina nyenzo nyingine zikiwemo vipaza sauti (speakers) ambazo humwezesha mtu kusikia pasipo kuweka kifaa masikioni.
Mheshimia Naibu Spika, kwa misingi hiyo na kwa kuwa Serikali haijapokea malalamiko ya kuwepo kwa changamoto iliyotajwa, sio wakati muafaka kuzuia kuingia kwa headphones nchini.
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:-
Kwa kuwa watoto wengi hasa waliozaliwa kuanzia miaka ya 1990 na kuendelea hawazijui sarafu za senti tano, kumi, 20, 50 na shilingi moja.
(a) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kurudisha sarafu hizo kwenye mzunguko wa matumizi kwa mfano kilogramu moja ya mchele kuuzwa shilingi1,892.50 au shilingi 1,895.75 badala ya shilingi 1,900?
(b) Kwa kuwa mada ya shilingi na senti inafundishwa katika shule zetu hasa za msingi, je, ni lini jambo hili litatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki Kuu ya Tanzania imepewa kisheria jukumu la kuzalisha fedha za noti na sarafu kulingana na mahitaji na mazingira ya kiuchumi yaliyopo. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, Benki Kuu imezalisha matoleo ya noti na sarafu yenye thamani mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya soko. Mambo muhimu yanayozingatiwa wakati wa kuondoa na kuingiza katika soko noti na sarafu ya thamani ndogo na kubwa ni mfumuko wa bei wa bidhaa za huduma, kulinda thamani ya shilingi na wepesi wa sarafu kubebeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuondoa na kuingiza katika soko sarafu zenye thamani ya juu ni moja ya mikakati na juhudi ya Benki Kuu katika kulinda na kuipa shilingi hadhi ya wepesi wa ubebaji. Sarafu za shilingi zenye thamani ndogo zikiwemo senti tano, kumi, 20, na 50 pamoja na shilingi moja, tano, kumi na 20 kwa uhalisia ubebaji wake ni mgumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa kuwa hatuna sera ya kupanga bei ya bidhaa na huduma kwa sasa, ni vigumu kurejesha sarafu hizi katika mzunguko wa fedha kwa njia anayopendekeza Mheshimiwa Mbunge.
Tatu, sarafu ndogo ya fedha itarejea kwa urahisi katika mzunguko ikiwa teknolojia ya kufanya miamala ya fedha kwa njia ya mitandao itasambaa kote nchini na jamii itakuwa tayari kufanya miamala hiyo kwa njia ya mitandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mada ya shilingi na senti inafundishwa mashuleni ili kuwapa wanafunzi maarifa ya kihesabu kama vile kuhesabu, kujumlisha, kutoa, kugawanya, kuzidisha, kulinganisha na kutafuta uwiano wa thamani mbalimbali ya fedha. Sambamba na maarifa ya mada ya senti na shilingi yanatolewa mashuleni, kigezo kikubwa cha kurejesha sarafu ndogo katika mzunguko wa fedha ni kuimarika kwa thamani ya shilingi au utayari wa wananchi kubeba mzigo mkubwa wa sarafu kwa ajili ya kununua bidhaa na huduma ndogo ndogo. Hata hivyo, sarafu zote zilizowahi kutolewa na Benki Kuu tangu mwaka 1966 bado ni halali kwa matumizi halali ya fedha hapa nchini za zinatumika kwenye miamala isiyo ya fedha taslimu.
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:-
(a) Kwa kuwa elimu ni haki ya kila mtoto, je, Serikali inawasaidiaje watoto wenye usonji ili nao wapate elimu?
(b) Je, Walimu wanaofundisha watoto hao wanatosheleza kwa mujibu wa ikama?
(c) Kwa kuwa watoto hao wana mazingira tete, je, Walimu wao wana utaalam wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usonji ni ulemavu ambao huathiri mfumo wa mawasiliano katika ubongo, mahusiano na utambuzi. Wanafunzi wenye usonji wamekuwa wakifundishwa na Walimu watalaam wa ulemavu wa akili waliopatiwa mafunzo kazini. Hadi sasa tuna wanafunzi 1,416 wenye usonji na Walimu 157 walio katika shule 18 za msingi nchini. Walimu hao ni wachache na hawatoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wapo Walimu waliopata taaluma hiyo kwenye Chuo cha Patandi, lakini hawako kwenye shule maalum, nasisitiza tena agizo langu nililolitoa kwenye Mkutano wa Kumi kwamba Halmashauri zote ziwahamishie Walimu hao kwenye shule zenye wanafunzi wenye ulemavu ikiwemo wenye usonji ifikapo mwezi wa Desemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa elimu maalum nchini kwa wanafunzi wenye ulemavu wasioona, viziwi, albino, usonji, viziwi–wasioona, walemavu wa akili, walemavu wa viungo, uoni hafifu, wenye vipawa na vipaji pekee pamoja na wenye matatizo ya ujifunzaji utaendelea kupewa kipaumbele. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo miundombinu, vifaa maalum kwa mahitaji maalum, kutoa mafunzo zaidi kwa Walimu pamoja na kugharamia kwa ujumla elimu msingi bila malipo kwa wanafunzi wote ikiwemo wenye mahitaji maalum.
MHE. SALMA R. KIKWETE Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Wazazi na Walezi wanatoa ushirikiano katika kuwatetea na kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ubakaji, ulawiti na unyanyasaji unaoendelea kwa sasa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete Mbunge wa Mchinga kama kwamba je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wazazi na na walezi wanatoa ushirikiano katika kuwatetea na kuwalinda watoto dhidi ya ubakaji, ulawiti na unyanyasaji unaoendelea kwa sasa?

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali hili kama ifuatavyo; katika kukabiliana na tatizo la Ubakaji, Ulawiti na Unyanyasaji wa watoto, Serikali imechukua hatua zifuatazo: Kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA wa mwaka 2017/2018-2021/2022) ambapo kupitia Mpango huu Serikali imekuwa ikitekeleza afua zinazolenga Kutoa Elimu ya Malezi ya watoto kwa wazazi/walezi; Kutoa msaada wa Kifamilia na Mahusiano; na Kusambaza Agenda ya Taifa ya Wajibu wa Wazazi/Walezi katika malezi chanya ya familia.

Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni pamoja na; Kuandaa programu ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto, kupitia program hii vituo vya majaribio 30 vya kijamii vya malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto vimejengwa katika mikoa miwili ya Dar es Salaam ambapo ni vituo 10 na Mkoa wa Dodoma vituo 20 na Serikali inaendelea kuhamasisha ujenzi wa vituo vingine katika mikoa iliyobaki.
MHE. ERIC J. SHIGONGO K.n.y. MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kivuko kutoka Mchinga Moja kwenda Mchinga Mbili ili kurahisisha huduma kwa wananchi ikiwemo wanafunzi wanaovuka bahari kwa miguu kwenda Shule ya Sekondari Mchinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya kivuko katika barabara ya Mchinga –Kijiweni, eneo la kutoka Mchinga Moja kwenda Mchinga Mbili lililo katika Jimbo la Mchinga, Wilaya ya Lindi. Serikali kupitia TARURA Mkoa wa Lindi, imeshafanya tathimini ya awali ya kutatua changamoto hiyo ambapo kiasi cha shilingi milioni 147 kitaweza kujenga kivuko cha waenda kwa miguu (pedestrian suspended bridge).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA Wilaya ya Lindi itatenga bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 147 kwa ajili ya kujenga kivuko cha waenda kwa miguu. Aidha, ujenzi wa kivuko hicho utaondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika Jimbo la Mchinga kulinga na upatikanaji wa fedha.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Moka-Mtumbikile - Matimba kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete Mbunge wa Jimbo la Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ilitenga Shilingi milioni 622.52 kwa ajili ya ujenzi wa vented drift yenye urefu wa Mita 45 na upana wa mita 7; ujenzi wa boksi kalavati kubwa katika mto Nangaru lenye urefu wa mita 26.8 na upana wa mita tisa; Kuchonga barabara yenye urefu wa kilomita 10.3, Kuweka changarawe kilomita mbili na kuchimba mifereji ya kuondoa maji barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA itajenga barabara ya Moka-Mtumbikile-Matimba kwa kiwango cha changarawe kadri ya upatikanaji wa fedha baada ya kukamilisha ujenzi wa vikwazo (Bottlenecks) vya barabara hiyo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA K.n.y. MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa katika Shule ya Msingi Kingurungundwa iliyopo Mchinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsate sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuna shule za msingi kongwe 2,147 nchini ambazo zilianzishwa kabla ya kupata Uhuru mwaka 1961. Hali ya miundombinu ya shule hizo ni mseto zikiwemo zenye hali nzuri na nyingine zenye miundombinu chakavu.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeanza kufanya tathimini ya hali ya miundombinu ya shule zote za msingi kupitia mradi wa BOOST ili kubaini mahitaji ya ujenzi wa miundombinu mipya ya shule na hali ya uchakavu wa miundombinu iliyopo. Tathimini hiyo imeanza mwezi Aprili, 2022 na itakamilika mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathimini hiyo yatatumika kuandaa mpango wa uendelezaji na ukarabati wa miundomibinu ya shule za msingi kwa miaka mitano, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 ikiwemo Shule ya Msingi Kingurungundwa.
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Jimbo la Mchinga kutoka kwenye chanzo cha maji cha Ng’apa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imeendelea kuboresha huduma ya maji katika Manispaa ya Lindi kwa kujenga miradi ya maji inayotumia chanzo cha visima vya Ng’apa. Maji yamefika eneo la Mitwero na kazi inayoendelea ni kuyafikisha maji Mchinga ambapo Kata za Mchinga, Mvuleni, Kilolambwani na Kilangala zenye jumla ya vijiji 18 zitanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, wananchi katika vijiji nane katika Kata ya Mbanja inayopitiwa na bomba kuu kwenda Mchinga watanufaika. Kwa sasa, Mkandarasi anaendelea na kazi. Kazi zinazoendelea ni ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilometa 42, ulazaji wa mabomba ya usambazaji kilometa 12.9 na ujenzi wa matanki manne yenye ujazo wa lita 100,000, mawili yenye ujanzo wa lita 200,000 na moja la lita 680,000. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.