Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Ali Juma (2 total)

MHE. JUMA ALI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro huu ni wa muda mrefu toka mwaka 1979, viongozi mbalimbali wametembelea katika eneo lile lakini hadi leo halijapatiwa ufumbuzi. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari mimi na yeye pamoja na viongozi wanaolizunguka lile eneo tukae pamoja ili tuupatie ufumbuzi mgogoro huu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mgogoro huu ni wa muda mrefu na nataka nimfahamishe Mheshimiwa Juma kwamba mimi binafsi nimefika eneo hilo, nilifanya mazungumzo na uongozi wa kikosi pamoja na uongozi wa eneo na wananchi wa pale tulizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kinachokwamisha kutatua sasa hivi ni suala la fedha za kupima kwa sababu Jeshi lilisharidhia kufanya mabadiliko ya mipaka yake ili wananchi ambao sasa hivi wanaonekana wapo ndani ya eneo la kambi waweze kutolewa. Hata hivyo, nitakuwa tayari kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge ili kumueleza zaidi ni hatua gani ambazo zinastahili kuchukuliwa kwa mujibu wa ziara niliyoifanya pale na fedha zikipatikana. (Makofi)
MHE. JUMA ALI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Mapato ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu yanategemeana na leseni pamoja na vibali kwa meli zinazotoka nje kuvua Tanzania na kwa kuwa 1.4 ndiyo imegoma kuleta meli kutoka nje kuja kuvua hapa: Je, Serikali haioni kwamba huu ni mgogoro wa 0.4?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kama hivyo ndivyo ilivyo, ni lini Serikali itaiondoa hii 0.4 ili tuweze kupata mapato na nchi yetu iweze kusonga mbele? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu ya msingi, Serikali ilirekebisha Kanuni na kuweka nyongeza ya vipengele kikiwemo kipengele hiki cha USD 0.4 kwa kilo ya samaki aina ya jodari kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali na kuweza kuinufaisha nchi yetu kutokana na rasilimali hii. Sasa kutokana na changamoto hii aliyoisema ya wateja kutokutokea kwa kugomea hii 0.4, nimeeleza katika jibu la msingi kwamba Serikali iko katika majadiliano ya kutazama juu ya Kanuni hii na baada ya kukubaliana, tutaamua hatua itakayofuata kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu.