Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anne Kilango Malecela (12 total)

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa mfano tu Wilaya ya Same mwaka 2016, wasichana wadogo waliopata mimba na kufukuzwa shule ni 64 ambao hawa ni wa O-Level ikiwa ina maana mimba hizi ni za utotoni. Mwaka huu 2017 mwezi wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu, miezi mitatu tu wamefukuzwa wanafunzi wa shule kwa mimba za utotoni 42 na kati ya hao akiwepo mtoto wa darasa la sita ikiwa ina maana ni kati ya miaka 12 mpaka 14.
Mheshimiwa Spika, hivi Serikali haioni kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na mitaala ambayo itawafundisha watoto hawa kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, ambayo itawafanya waelewe athari za kupata mimba utotoni ambazo ni muhimu sana? Mitaala hii itaweza kuwasaidia watoto hawa kujitambua na kufahamu umuhimu wa kutokukubali kupata mimba utotoni.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali
inafanya jitihada kubwa sana kupambana na madawa ya kulevya sasa hivi na naiunga mkono, nai-support na tunashukuru sana. Jitihada hii ni kwa sababu Serikali imeona athari hasa inayowapata vijana wa kiume na wa kike kwa
kutumia madawa ya kulevya, lakini watoto wa kike
wanapata athari mara mbili, kwanza athari ya madawa ya kulevya na mimba za utotoni.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mkakati
mkubwa kama ule wa madawa ya kulevya ili tupunguze athari za mimba za utotoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali linalohusiana na masuala ya mitaala kama ifuatavyo:-
Kimsingi katika elimu ya Msingi na elimu ya Sekondari wanafunzi wanapewa maarifa kuhusiana na masuala ya Kibaiolojia na sayansi yanayohusisha hata masuala ya maumbile ya miili yao, kwa hiyo kimsingi suala hilo linafanyika labda tunaloweza kuahidi hapa ni kutoa msisitizo wa kuona kwamba wanafunzi hao wanapewa dozi zaidi hasa kwa kuwachukua hawa watoto wa kike na kuwapa elimu ya ziada kwa ajili ya kuwanusuru katika mazingira hayo.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza tunao mpango wa kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao ni jumuishi kwa sekta takribani tisa za Serikali yetu na mpango huu umezinduliwa mwaka jana mwezi Desemba na Mawaziri tisa wa Serikali hii ya Awamu ya Tano na Mawaziri wameonesha comittment kubwa sana ya kuweka utaratibu
wa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni lakini pia mimba za utotoni na vitendo vyote vinavyohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, tunachokihitaji kwa sasa ni
kupewa fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango huo na kwenye mpango huu tunalenga kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kiwango cha asilimia isiyopungua 50 kufikia mwaka 2022. Kwa hivyo, mpango huu kama tutapangiwa fedha, tunapanga kuanza kuutekeleza mwezi Julai mwaka 2017. Kwa hivyo, mpango tunao pia tuna mikakati mbalimbali inayoendelea kama ya elimu ya malezi chanya (Positive Parenting Education) kwa watoto ambao umefanyika kwenye Wilaya 72 za Nchi yetu
na tunawalenga zaidi viongozi wa kimila, wazazi pamoja na watu mashuhuri wenye kufanya maamuzi kwenye jamii.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata taabu kidogo maana yake na mimi ni mwalimu, iwapo Serikali tutaacha kwenda kwenye specialization na tukafanya watoto wote wakasoma sayansi. Mimi nina wasiwasi kwamba tutapata wanasayansi wabovu zaidi.
Je, Serikali haioni kwamba specialization ni important kuliko ambavyo sasa tunakwenda kumfanya kila mtoto asome sayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, specialization inaanza na msingi na niseme tu kwamba tunawahitaji wataalam wa aina tofauti tofauti. Kuna hao specialization ambao wanakuwa wamekuwa vertical yaani anajikita katika eneo moja pia tunawahitaji wale ambao wanakua kimapana (wide knowledgeable people) ambao wanaweza wakaoanisha upande huu na upande huu. Kwa hiyo, katika ku-specialize kupo lakini lazima kuwe na msingi ni wa eneo gani ambalo huyu mtu atafanya specialization. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Hivi Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwaangalia na wanawake wa vijijini, kwa sababu mipango mingine yote imefeli kwa wanawake wa vijijini kupata mikopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa yeye pia ni Kada wa Chama cha Mapinduzi, naomba nimkumbushe kwamba kwenye Ilani ya Uchaguzi pamewekwa maelekezo kwamba kila Halmashauri nchini itenge asilimia tano ya bajeti yake kutoka kwenye Own Source kwa ajili ya kuwakopesha akinamama, huu Mfuko unajulikana kama Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wanawake wote, wakiwemo wanawake wa vijijini, hata wale anaowapenda sana wa kule Same, nao wanaweza wakatumia fursa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu ssi Waheshimiwa Wabunge ni kuingia kwenye vikao vya Halmashauri wakati tunapanga bajeti na kushiriki kuhakikisha asilimia tano ya akinamama inatengwa, asilimia tano ya vijana inatengwa. Pia tusiishie hapo, pesa zinapopatikana tuziweke pembeni pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wabunge ni Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ambayo huwa inahusika kugawa hizi pesa kwenye vikundi mbalimbali. Kwa hiyo baada ya kuwahamasisha wananchi wetu waombe mikopo hii ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, pia tushiriki kwenye vikao vile vya Halmashauri ambavyo vinagawa pesa hizi kwenye vikundi mbalimbali vya akina mama ili ziwafikie kwa uhakika wananchi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kupitia Benki ya Wanawake tunatengeneza mifumo sasa ambayo itawafikia Watanzania popote pale walipo, hata wa kijijini, sasa hivi matumizi ya simu ni kwa zaidi ya watu milioni 36 hapa nchini, kwa hiyo njia hii itawafikia watu wengi zaidi hapa nchini kwetu. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wananchi wa Madaba wameonesha kuhamasika sana kulima tangawizi, hata mimi ninalima tangawizi Madaba. Je, Serikali haioni kwamba kiwanda cha Mamba Miamba ambacho kitakuwa tayari by March next year, kitahitaji tangawizi nyingi sana siyo kutoka Same tu pamoja na Madaba.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wananchi wa Madaba ardhi ya uhakika ili walime tangawizi kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuchukue kilio cha mama vilevile kama kilio cha Mheshimiwa Joseph Mhagama. Serikali inaona umuhimu huo na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha mambo pale yanakaa sawasawa wananchi walime tangawizi waje, kulisha katika kiwanda cha Mama Anne Kilango Malecela. (Makofi
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshmiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa masoko ya nje yanatawaliwa sana na ubora wa mazao na kwa kuwa wanunuzi wa tangawizi kule nje wanapenda sana organic ginger. Sasa Serikali ina mpango gani wa kupeleka elimu kwenye zile sehemu ambazo zinalima sana tangawizi kama vile Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Ruvuma?
Mheshimiwa Spika swali la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba Miamba kilichopo Wilayani Same kinategemea kuanza kusindika tangawizi ya kupeleka nje ya nchi katikati ya mwaka 2018.
Je, Serikali itatumia njia gani kuwafanya wananchi ambao wamekata tamaa kulima tangawizi kutokana na bei kushuka sana ili waendelee kulima tangawizi kwa sababu kiwanda hiki cha Mamba Miamba kitahitaji malighafi kwa wingi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa idhini yako napenda nichukue fursa hii kumtambua Mama Malecela kama Malkia wa Tangawizi. Suala la tangawizi amelifanyia kazi sana. Nichukue fursa hii kushukuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo ameshughulikia pacha wangu, zimetengwa pesa nzuri zaidi ya shilingi bilioni
• kusudi hicho kiwanda kiwe na hadhi ya Kimataifa, kizingatie ubora kama nilivyoeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu maswali mawili uliyoniuliza, moja la ubora, Wizara yangu inayosimamia SIDO kwa kutambua suala la viwango, maeneo yote ninaojenga sasa katika mikoa yote mipya tunajenga ofisi za SIDO, sheli, maabara, mahali pa kuchakatia chakula kwa viwango vitakuwa ni kipaumbele; Katavi, Rukwa, Geita, Simiyu ndiyo nakwenda kuanza nalo na pesa tayari ninazo kama nilivyoeleza juzi. Kwa hiyo, nitawafundisha wananchi hasa akina mama kuzalisha vyakula kwa viwango vya kuuza Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa suala la pili kwamba tutafanyaje, ndiyo tangawizi ilikuwa inauzwa Sh.3,500 najua leo bei imeshuka, sawa sababu mojawapo ni muanguko wa bei za bidhaa, commodity price duniani zote zime-dive. Tutafanya nini?
Kazi ninayofanya sasa ni kutafuta masoko makubwa, masoko mengi ya Kimataifa ile demand pool iwawezeshe wananchi wetu waweze kuuza zaidi lakini zaidi kupitia ESDP II tutaongeza tija (productivity) katika uzalishaji kusudi watu walime sehemu kubwa kwa gharama ndogo ile productivity iweze kupeleka hiyo tangawizi. Kwa sababu kiwanda chako hakina mfano, tangawizi yote itakwenda Mamba, ichakatwe, tupeleke Bandari ya Tanga iende duniani kuuzwa.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Tanzania, wanajenga sana zahanati, madarasana mifereji.
Je, Serikali haiwezi kuwa na mpango Maalum kwamba wananchi wakijenga kiasi fulani Serikali nayo inakuwa na kiasi fulani inachukua kumalizia kwa sababu watanzania wanajenga mno? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ni kama amerudia yale ambayo nilikuwa nawaasa Waheshimiwa Wabunge, kwamba hakika kwa kushirikishana wananchi pamoja na Serikali kwa pamoja tunafika na ndiyo maana nikatoa mfano nilivyokuwa nimeenda Moshi Vijijini, Kituo cha Afya ya Kiaseni nimekuta wananchi wamejitoa na Serikali nayo ikapeleka nguvu, hakika tukishirikishana tutaweza kutoka. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Kwa kuwa mwaka 2015 nilipokuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki nilitoa ufadhili wa gari la golisi kwenye Kituo cha Kata ya Maore kwa ajili ya Jimbo la Same Mashariki; nina uhakika Serikali inalifahamu hilo. Kwa kuwa, lile gari sasa halina matairi, linahitaji kufanyiwa maintainance kubwa. Je, Serikali mnatoa ahadi gani leo hapa ili wananchi wa Same Mashariki wasikie?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mhesimiwa Mbunge Anne Kilango Malecela kwa kusaidia kazi za Ofisi ya Polisi katika Jimbo la Same Mashariki kuweza kufanya kazi na wanakukumbuka sana. Nimefika mwenyewe Same nimeona wakikukumbuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inatambua jitihada alizofanya Mheshimiwa Mbunge na tutaongea na Kamanda wa Polisi wa Mkoa ili tuweze kuona namna ambavyo tunaweza tukaunga mkono jitihada hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge ulizifanya. Hata hivyo niendelee kukuomba uendelee kuwakumbuka wananchi wa Same kwani wanakukumbuka sana ili vitu kama vile matairi wasiendelee kuvikosa, waendelee kupata kama ulivyokuwa unafanya.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Kwa kuwa Kata ya Mkomazi ni jirani sana na Kata Ndungu na kwa kuwa pale kwenye Kata Ndungu kuna skimu kubwa sana ya umwagiliaji ambayo inasaidia kilimo kikubwa cha mpunga. Skimu ile sasa imeonekana kwamba imechoka sana na maisha ya wananchi wa Kata ya Ndungu, Kihurio mpaka Kalemawe yapo hatarini; je, Mheshimiwa Waziri atakapotoka Korogwe pale Mkomazi kwa sababu Ndungu ni jirani anatuambia nini, atakuja kuona skimu ile?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nirudie tena ukisoma Tenzi za Rohoni inasema unapotembea na kuzuru wengine naomba usinipite Mwokozi, sitompita Mheshimiwa mama Anne Kilango katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. (Makofi/Kicheko)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii. Kwa kweli wananchi wa Wilaya ya Same kwa ujumla wao wanajitahidi sana kujenga zahanati. Ningemwomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa Serikali kwenda kuona jitihada zile, naomba atuambie hapa ndani atakwenda lini na atatoa msaada gani kwa sababu hali ya wananchi hasa wa milimani upande wa afya ni mbaya sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Anne Kilango Malecela na wananchi wote wa Wilaya ya Same kwamba nitakapokwenda katika Wilaya ya Same sitaishia katika Jimbo la Same Magharibi peke yake bali nitapita mpaka kwenye Jimbo la Same Msahariki. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, swali langu kubwa hapa lilikuwa ni barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani, basi naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja kubwa kidogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani zipo za aina mbili, ya kwanza ni barabara inayounganisha Kiwanda cha Tangawizi na masoko ya ndani na nje ya nchi na barabara hii inatokea Mkomazi Kisiwani kwenda Same na barabara ya pili ni barabara zinazounganisha walima tangawizi (wakulima) na kiwanda chao.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2009 alikuja Mamba Miamba yeye mwenyewe akaona jitihada za wananchi, akatoa bilioni 2 za kujenga barabara za kuwaunganisha wakulima na kiwanda chao. Je, Mheshimiwa Waziri huoni kwamba ili uelewe tatizo kubwa la miundombinu ya kiwanda kile ni vyema wewe mwenyewe ukawaahidi wananchi wa Mamba Miamba utakwenda lini kule ili uweze kujibu haya maswali vizuri, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nipo tayari kwenda, lakini uniruhusu nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua kupatikana kwa kiwanda hiki ni pamoja na juhudi zake, lakini niwashukuru na kuwapongeza Mkuu wa Wilaya kwa sababu Mkuu wa Wilaya pia amekuja akiwa na ombi la kutembelea maeneo haya. Natambua kwamba lazima tuboreshe barabara ambazo zinawahudumia wananchi kupeleka malighafi kwenye kiwanda hiki, lakini pia kutoa mazao yanayotokana na kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia barabara hii ambayo nimeizungumza ni muhimu sana kwa sababu inapokwenda kuunganisha Mkomazi pia inatoa huduma kwa ajili ya utalii. kwa hiyo, nipo tayari Mheshimiwa Mbunge nitakuja Same tutembelee maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza; je, Serikali ina mpango gani wa kuwavutia zaidi wawekezaji ambao wakija watawekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani mazao yetu kuliko viwanda vingine vyovyote.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi wake hasa kwenye suala la viwanda ambalo linahusisha masuala la vitunguu na tangawizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili niseme kwa ufupi ya kwamba, kama Serikali tumeona ni vema kuendelea kutumia Balozi zetu, vilevile tumeona ni vema kufanya makongamano mbalimbali ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ninavyozungumza mwaka jana Desemba, tulifanya mazungumzo na kongamano kubwa na Wafanyabishara kutoka China. Mwezi Desemba pia tulifanya kongamano kubwa na wafanyabiashara kutoka Jordani, tarehe 18 mwezi wa Nne tulifanya Kongamano kubwa sana na wawekezaji kutoka Ufaransa kwa lengo hilo hilo. Vile vile tarehe 23 - 24 Aprili tulikutana na watu kutoka Israel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu kuwavutia wawekezaji wengi zaidi na kuwaomba kuja kuwekeza hasa katika maeneo haya ya kuongeza thamani. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hiyo Serikali inaendelea kuifanya. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, Wilaya ya Same, ni Wilaya ambayo takribani, eneo lake katika Mkoa wa Kilimanjaro ni 40% ya eneo zima la Mkoa wa Kilimanjaro. Lakini Wilaya ya Same mara kwa mara inatengewa pesa kidogo sana inapewa pesa zilizoko chini ya wilaya ambazo ni ndogo zaidi ya wilaya ile. Naomba Serikali ione kwamba haioni umuhimu wa kutenga pesa zinazolingana na ukubwa wa Wilaya ile ya Same ambayo ni takribani 40% ya eneo lote la Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili nakuja kwenye barabara hii ya Hedaru – Vunta – Myamba barabara hii ni korofi mno, sijawahi kuona barabara kama hii, Awamu ya Nne niliwanyenyekea hapa Bungeni kwamba barabara ya Mkomazi, Kisiwani Same, waiweke kwa vipande vipande, walifanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa barabara hii yenye kilomita 42.2 hii TARURA Same wamefanya tathmini ya kutengeneza barabara yote kwa ujumla, wakapata ni bilioni 1.8.Je, Serikali hamuoni kwamba kwa sababu wananchi hawa wanahangaika mno mkatengeneza vipande vipande ili mmalize tatizo lote, kuliko mnavyochukua vimilioni viwili vitatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kwanza kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza nimpongeze kipekee Mheshimiwa Kilango Malecela jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wake wa Same na sisi sote ni mashahidi Kiwanda kile cha Tangawizi kimejengwa ni kwa ajili ya kazi kubwa aliyofanya yeye.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mgawanyo wa fedha umekuwa hauendani na uhalisia na hili ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI baada ya kuliona hilo sasa hivi tuna-commission consultant kwa ajili ya kuja na formula nzuri itakayosaidia ili tunapogawa fedha twende na uhalisia. Kwa sababu formula inayotumika ndiyo iliyokuwa inatumika mwanzo kabla TARURA haijaanza kufanya kazi. kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Kilango Malecela na Wabunge wengine tuvute subira kwa sababu tayari consultant anafanya kazi atatuletea majibu na formula ambayo itakuwa nzuri kwa kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili anaona iko haja kwa ajili ya ukorofi wa ile barabara tuanze kujenga kwa kiwango cha lami walau kilometa chache chache at the end tuje tukamilishe kilometa zote 42. Ni wazo jema kwa sababu vinginevyo tunakuwa tunarudia fedha inatumika lakini kwa mazingira na jiografia ya barabara ambayo Mheshimiwa ametaja iko haja kubwa sana.