Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Majurah Bulembo (32 total)

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Najielekeza hapo kwenye wavuvi. Kwa kuwa wavuvi katika Ziwa Victoria nyavu wanazotumia wanazinunua madukani na Serikali ipo na bandari ipo; Serikali ituambie ni lini itayafunga yale maduka yanayouza nyavu zisizotakiwa kuvuliwa na lini itaweza kuleta sheria hapa Bungeni kuzuia viwanda vinavyozalisha nyavu zinazosababishia wavuvi hasara? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Jumuiya anapomuuliza mdhamini wake inakuwa shida kidogo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na uvuvi haramu kwa ujumla, Serikali sasa hivi inachokifanya, inashambulia maeneo yote, yaani hatuendi kwa wavuvi peke yao, tunamchukulia hatua yeyote aliyeko katika ule mnyororo wa thamani wa uvuvi kwa maana kwamba mzalishaji wa zana haramu, msambazaji, mtunzaji, mhifadhi na yeyote. Kwa hiyo, anayeuza akipatikana anachukuliwa hatua kama mhalifu mwingine yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tumekwenda hatua zaidi hata ya kudhibiti uingizwaji wa nyavu nchini, acha wenye viwanda ambao tunawakagua mara kwa mara na kwa kweli mwenye kiwanda hapa nchini akipatikana anazalisha nyavu zisizoruhusiwa tunachukua leseni yake na kufunga kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunakagua hata uingizaji, kwa sababu wako watu wanaagiza nyavu kutoka nchi za nje kwa kisingizio kwamba zinapita Tanzania zinakwenda nchi nyingine, lakini baada ya kuwa wamesha-clear pale bandarini, wanafanya maarifa hizi nyavu zikifika mpakani Tunduma au pengine, zinarudi nchini. Kwa hiyo, hata hawa sasa hivi tunashughulika nao, tunahakikisha wanatoka nje ya mipaka yetu na hizo nyavu zao. Tukimkamata tunamchukulia hatua kama sheria inavyotaka.(Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa kituo cha Mbezi Luis kimeshapata mwekezaji LAPF, Serikali inatuambiaje kuhusu kituo cha Boko na cha Temeke, wamewatafuta akina nani watakaosaidia kujenga vituo hivi kwa haraka ili kuondoa msongamano Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bulembo, Mbunge Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana
swali la Mheshimiwa Mbunge na ndiyo maana nimesema Mbunge Maalum kwa sababu ana hadhi maalum katika nchi hii kutokana na nafasi zake alizokuwa nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi Serikali tumepata wadau wetu wa LAPF tumeanza na kituo kile lakini hata hivyo tunaenda kutafuta wadau wengine kwa ajili ya kujenga kituo kile katika eneo la Boko na kituo cha Kanda ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niwaelekeze wenzetu wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na wadau wengine hasa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, ikiwezekana wakae na Halmashauri ya Mkuranga, kwa sababu eneo la kimkakati tayari lipo ambalo halina haja ya kulipa fidia kuona ni jinsi gani tuta-fast track hiki kituo ambacho tunaweza tukakijenga eneo la Mkuranga kwa watu wa Kusini ili wakapata unafuu zaidi.
Kwa hiyo, tunachukua mambo yote haya kwa kushirikisha wadau mbalimbali lengo ikiwa ni kujenga vituo ambavyo vitasaidia suala la usafiri katika nchi yetu.
MHE. ABDALLA M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijauliza swali, naomba unipe nafasi kidogo niseme maneno mawili kidogo.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Silinde kama ameona mali za Chama cha Mapinduzi zinaweza kuja kuombwa Bungeni, nafikiri ni dalili nzuri kwamba naye anaelekea kuja CCM, karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu linasema hivi, maombi haya yanayoletwa kwa ajili ya Shule ya Jumuiya ya Wazazi, Wizara naomba iniambie; je, kwa nini msishirikiane na Mbunge mkaimarisha shule nzuri ya Julius Nyerere ambayo inaonekana imeharibika, haifai, haina huduma nzuri, mpaka mwende kutafuta mali za CCM? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Alhaji Bulembo alikuwa anatoa ushauri na mimi napenda kumpongeza sana kwa juhudi kubwa anayofanya katika shughuli zake.
Mheshimiwa Spika, nadhani ushauri huu kama Serikali tumeupokea, kwa sababu Mheshimiwa Alhaji Bulembo wewe ni mlezi wa watoto na ndiyo maana umeamua kujenga shule hizi na kuzisimamia. Kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuboresha maeneo mbalimbali ili watoto wetu waweze kusoma kwa kadiri iwezekanavyo.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Waziri kwa sababu nchi hii ina tatizo kubwa sana la sukari na katika Mkoa wa Kagera umesema tuanzishe viwanda vya maziwa, ukitoka pale Bulembo kwenda Busheregenyi, kwenda Msira kwenda Rugongo, kwenda sehemu za huko kama unaenda Kasharu; maeneo yale ni maeneo ya tingatinga kuweza kulima mashamba ya miwa na watu wajasiliamali wadogo wakaanzisha viwanda vidogo vidogo.
Ni lini unaenda Misenyi kukaa na wananchi? Ofisi yako ikawaambie kwa sababu uwezekano wa kupatikana miwa upo ili waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo?(Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, namsukuru Mheshimiwa Bulembo. Hilo la kwenda Busheregenyi kwa bibi zangu halina mjadala, lakini napenda nikueleze kwamba ninaye mwekezaji sasa katika maeneo hayo ambaye anataka kuingia ubia na Jeshi la Magereza sehemu Kitengule, kushirikiana na Jeshi la Magereza kutumia uoto ule kuweza kulima miwa ya kuzalisha sukari. Kwa hiyo, tutalijadili mimi na pacha wangu, yule mwekezaji yupo serious anataka kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatafuta wawekezaji lakini Waheshimiwa Wabunge muelewe, mwekezaji humleti leo akaanza leo. Mkijua huo mchakato wa kuweza kuchukua ardhi mpaka kuzalisha, ndiyo maana nikaanzisha ule utafiti wa wepesi wa kufanya biashara. Ndiyo mambo ambayo tunayarekebisha na tutayarekebisha kusudi angalau wawekezaji wachukue muda kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala na Mheshimiwa Bulembo ni kwamba Busheregenyi mnaweza kupata huduma Kagera Sugar na mkapata huduma Magereza watakapokuwa wameanzisha kiwanda wale wawekezaji.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kama alivyosema muuliza swali wa kwanza TBC wameweza kupata shilingi bilioni tatu, naomba kumuuliza Mheshimiwa mjibu swali.
Ni lini Serikali itaweza kununua vifaa vidogo TVU au AVIWEST vifaa vile tukio linapotokea wanaweka pale pale tunakwenda kwenye breaking news, lakini TBC leo kwenye breaking news wanakodi vifaa, kifaa kimoja kinanunuliwa kama shilingi milioni 50 au shilingi milioni 60, hii ni aibu katika Serikali yetu.
Serikali waniambie ni lini wataweza kununua vifaa hivyo na kuvisambaza Tanzania kwa sababu masafa marefu hayasikiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, kama nimempata vizuri Mheshimiwa Mbunge hii TVU ni kwa upande wa televisheni na ambapo tayari TBC imeshanunua vifaa hivi, ahsante.(Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa watu wanaokwenda kwenye Magereza ni wahalifu na huwa wamehukumiwa, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani iniambie na itoe kauli hapa, ni lini Gereza la Muleba litaenda kuzungushiwa fensi, maana yake leo Gereza la Muleba lina uzio kwa maana wafungwa wakiamua kuondoka leo, kesho wanaondoka, mtawakamata wale viongozi bure, sasa nataka commitment ya Serikali ni lini itafanya emergence ya kwenda Muleba kuweka uzio wa Magereza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli Gereza la Muleba linahitaji kuwekewa uzio, tunatambua na tumejipanga kwamba wakati wowote ambapo tutakamilisha kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio huo tutafanya hiyo kazi. Jambo hilo tunalitambua na lipo katika vipaumbele vyetu.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na swali la msingi kwa kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema watoto wote wasome bure, katika jimbo la Kaliua shule ya msingi Ushokola walimu wanafundishia nje na walimu hawatoshi. Ni lini Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itaona hili tatizo la Kaliua kuongezea walimu wa shule za msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Bulembo, Senior MP, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la bwana Bulembo bahati nzuri siku nne zilizopita nilikuwa na viongozi kutoka katika Wilaya ya Kaliua, walifika ofisini kwangu pale lakini ili kujadili ajenda za kimaendeleo. Ninasema Senior MP kwa sababu mwanzo alikuwepo na hivi sasa mnajua kazi zake kubwa anazozifanya katika nchi hii na juzi alikuwepo kule Mkoa wa Tabora nadhani ndio maana ameweza kufanya verfication ya tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kikubwa zaidi nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge; nilikubaliana na viongozi waliotoka Kaliua kwamba nitafika Kaliua. Naomba nikuhakikishie kwamba nitatembelea shule ile ili kubaini mahitaji halisi. Hata hivyo Serikali tutaweka mpango, namna ya kufanya ili tuweze kujenga miundombinu na kuwapatia walimu ili vile vile wananchi wa eneo lile wapate fursa ya kusema tulitembelewa na mjumbe wa Kamati Kuu ambaye anasimamia suala zima la utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Vicheko/Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kama alivyosema muuliza swali wa kwanza TBC wameweza kupata shilingi bilioni tatu, naomba kumuuliza Mheshimiwa mjibu swali.
Ni lini Serikali itaweza kununua vifaa vidogo TVU au AVIWEST vifaa vile tukio linapotokea wanaweka pale pale tunakwenda kwenye breaking news, lakini TBC leo kwenye breaking news wanakodi vifaa, kifaa kimoja kinanunuliwa kama shilingi milioni 50 au shilingi milioni 60, hii ni aibu katika Serikali yetu.
Serikali waniambie ni lini wataweza kununua vifaa hivyo na kuvisambaza Tanzania kwa sababu masafa marefu hayasikiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, kama nimempata vizuri Mheshimiwa Mbunge hii TVU ni kwa upande wa televisheni na ambapo tayari TBC imeshanunua vifaa hivi, ahsante.(Makofi)
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama alivyojibu mjibu swali, kwa kuwa hawa Wazee wa Mahakama wanalipwa nafikiri Sh.5,000/= au Sh.7000/=. Je, huo mchakato wanaoufanya wanajiandaa kuongeza kiwango cha hawa Wazee kwa sababu ni kazi ya hiyari? Isije kuwa wanashindwa kwenda Mahakamani ndiyo maana haki inachelewa kupatikana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hapa Mheshimiwa Bulembo kwamba tunachokifanya ni kufanya tathmini ya kina jinsi gani tutafanya kuhakikisha wananchi wanapata haki. Siwezi kusema kwamba kiwango hiki kitaongezeka kwa sababu kuna mambo mengi ndani yake yanaendelea hapa, isipokuwa kwamba tuamini Serikali inafanya kazi na mwisho wa siku ni kwamba miongoni mwa kuondoa kero nyingi za wananchi ni kushughulikia Mabaraza ya Kata, ili kulinda haki za watu kwa kuyashughulikia na kuyaunda vizuri Mabaraza ya Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inafanya kazi hii hatima yake itakapofika, basi tutapata mwelekeo maalum wa Serikali wa jinsi gani jambo hili tunaenda kuli- handle vizuri kwa maslahi mapana ya wananchi.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Dar es Salaam pale kwenye kulaza bomba la kutoka Bagamoyo kuja Chuo Kikuu kuna watu walivunjiwa na watu wengine wakakataa wakapelekwa mahakamani, walipopelekwa mahakani wameshindwa mpaka leo wanasema wanalindwa na wakubwa hawataki kuvunja nataka Wizara iniambie wanavunjiwa lini ili Dar es Salaam tupatae maji Chuo Kikuu? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanayo taarifa kwa sababu wameshapewa notice kwamba wanavunjiwa, kwa hiyo ni wakati wowote hatua za kuvunja zile nyumba zitafanyika.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi, naomba kuuliza Wizara ya Kilimo hapo. Kwa kuwa wakulima wa kahawa ni sawasawa na wakulima wa pamba. Wakulima wa pamba wamewaruhusu waliofanya biashara ya mkataba waweze kuendelea na shughuli hiyo, lakini wakulima wa kahawa katika nchi wa mkataba hawazidi watano mpaka sita. Kwa nini Wizara inakuwa double standard, msimu umeanza sasa hivi wiki ya pili watu hawa hawataki kuwapa kibali cha kuweza kukusanya kahawa kwa sababu ni biashara yao. Naomba tujue hawa haki yao wanaipata wapi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, utaratibu tuliouweka sasa hivi lengo lake la kwanza ni kuhakikisha kwamba wakulima wanapata malipo stahiki kwa jasho lao. Mfumo tuliokuwa nao sasa hivi kwa kiwango kikubwa ulikuwa hautoi malipo stahiki kwa jasho la wakulima na moja ya njia zilizotumika kuwanyima haki wakulima ilikuwa ni mfumo wa kununua kahawa kwa kulipa advance kutoka kwa wafanyabiashara na hasa katika Mkoa ambako Mheshimiwa Bulembo anatoka maarufu kwa jina la Butura. Ili kukabiliana na Butura, lazima kuweka mfumo unaofafana maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, jana nilisema hapa ndani wakati nachangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali kwamba pale ambapo mikataba hiyo iliingiwa officially kwamba kuna mkataba na mamlaka za Serikali zinatambua mikataba hiyo kama ilivyo kwenye pamba, pamba mtu haingii mkataba mtu na mtu mmoja, mikataba hiyo inaingiwa kupitia mamlaka za Serikali, kama wako wakulima wa kahawa ambao wameingia mikataba kwa njia hiyo, nilielekeza kwamba wapeleke habari hiyo haraka Bodi ya Kahawa ili waweze kupata utaratibu wa kuuza kahawa kwa mtu waliyeingia naye mkataba.
Mheshimiwa Spika, ile mikataba ya kuingia kienyeji ndiyo utaratibu uliokuwa unasababisha watu kupoteza haki yao na jasho lao kwa kuuza kwa watu ambao wanawapa malipo kidogo kwa kahawa ya bei kubwa.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama alivyosema Ranchi ya Missenyi ni ya mfano na huo mfano ni kutokuwa na mifugo.
Swali langu la msingi sababu inayosababisha Ranchi ya Missenyi isiwe na mifugo ni kwa sababu zile blocks mmewapa watu ambao siyo wafugaji wa mbali, wao kazi yao ni kukodisha. Je, kwa utaratibu mpya mlionao mtawajali wakazi wa eneo la Misenyi, kwamba ndio wapewe maeneo hayo ya ranchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba palikuwa na kasoro kadha wa kadha ambazo zilisababishwa na kuwapatia watu ambao si wafugaji na matokeo yake wakawa wanakwenda kuwakodisha watu wengine. Hivi sasa baada ya kuingia sisi tumekubaliana kufanya mabadiliko na ndiyo maana tumezirudisha ranchi zile Wizarani kwa ajili ya kuanza kugawa upya na tumeanza kazi hiyo ya kupokea maombi, kuyapitia na kujiridhisha kwamba huyu kweli ni mfugaji na tuweze kumpatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida tu ni kwamba pamoja na kufanya hivyo, tumekubaliana kwamba hatupo tayari kuona ng’ombe yoyote aliyepo katika maeneo yanayozunguka ranchi zetu anakufa kwa sababu ya kukosa malisho na maji, hivyo tumekubaliana ya kwamba wafugaji wanaozunguka pamoja na wafugaji wa Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Diodorus Kamala waweze kulipia kwa muda wa miezi mitatu. Ng’ombe mmoja analipia shilingi 10,000 anaingia katika ranchi, anapewa eneo, ananenepeshwa na akimaliza anatoka badala ya ile kuendelea kuwapga faini kwa sababu ya kuingia katika eneo la ranchi. Hivyo, tumekubaliana kurasimisha hatua hizi.
MHE. ALHAJ ABDALAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Swali la kwanza, kwa kuwa suala la madawati limekuwa ni tatizo la muda mrefu na historia iko wazi, kila mtoto akianza shule anaenda na madawati, madawati hayo huwa yanaenda wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuyatunza yale madawati yanapokuwepo shuleni ili angalau na wengine wanaokuja waweze kuyakuta ili ugonjwa wa madawati uweze kuisha katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Alhaj Abdalah Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, inashangaza kama yeye mwenyewe ambavyo ameonesha kushangaa kwamba shule inatengenezewa madawati ya kutosha halafu baada ya muda mfupi au baada ya muda baadhi ya madawati yanaonekana hayapo. Mimi nisisitize kwamba ni jukumu la msingi la Mkuu wa Shule au Mwalimu Mkuu kuhakikisha kwamba mali za shule zinatunzwa ipasavyo na tutalifuatilia hili. Kuanzia sasa hivi tunaiweka katika vigezo vya tathmini ya mwalimu kuhakikisha kwamba vifaa vya shule ikiwemo madawati vinatunzwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, nadhani na swali lake la pili nakuwa nimeijibu kwa namna hiyo. Ahsante sana.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ukitoka Dodoma hapa kama unaelekea Dar es Salaam, ukianza Wilaya ya Gairo kabla ya kufika Jimbo Mvomero, hapa katika maeneo ya Magole wapi kila sehemu unakuta vijana wamebeba nyanya, karoti, na kadhalika huko Morogoro na ukifika pale kituo cha mizani. Ni mkakati gani Serikali wanafanya maalum kwa ajili ya Morogoro kuwasaidia hawa vijana wadogo wadogo ili kukuza uchumi wao, kwa sababu wanashinda barabarani, mwisho watagongwa na magari. Naomba Serikali iseme ni mkakati gani kuhusu Morogoro mnawasaidia hawa vijana wanaoshinda barabarani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama ambavyo nimesema hapo awali, jukumu letu ni kuhamasisha kwanza kuwatambua hawa wafanyabiashara wadogowadogo sana yaani (Micro Entrepreneurs). Ninalosisitaza ni kwamba mara nyingi hata tunapozungumzia maeneo ya uwekezaji au katika shughuli za kuwezesha tumekuwa tunawaangalia zaidi hawa wakubwa kuliko hawa wadogowadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa sasa imeshajipanga kuona kwamba hawa wajasiriamali wadogo wadogo wawe wa matunda, wawe wa biashara nyingine, wanasaidiwa ili kuweza kupata maeneo ambayo yatawawezesha kufanya shughuli zao vizuri na tunasema kwamba uchumi uanzie shambani hadi sokoni na maeneo mengine kama viwandani.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi lililoulizwa kuhusu Dar es Salaam naomba Wizara ya Maji ituambie kwa sababu baada ya Ruvu Chini na Ruvu Juu kukamilika sasa katika Jiji la Dar es Salaam maji yanamwagika sana karibu asilimia 40. Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuondoa umwagikaji wa maji ili kuisaidia pesa ile ikarudi Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kuhusu suala zima la upotevu wa maji. Serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi sana katika kuhakikisha inatatua tatizo la maji. Hata hivyo, ipo hali ya kuona upotevu mkubwa wa maji barabarani ama mitaani na kuwa si hali nzuri sana kuona wananchi hawana maji lakini maji yanapotea.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wangu aliagiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Maji na kufanya nao kikao na akawagiza kujenga na kutengeneza miundombinu ambayo rafiki ambayo itakayoweza kudhibiti upotevu wa maji mpaka kufikia kiwango kile cha kimataifa cha asilimia 20 ambacho kinakubalika. Kwa hiyo, Serikali inaendelea na jitihada katika kujenga na kukarabati katika suala zima la kudhibiti upotevu wa maji.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mji wa Bukoba una maji mengi kutokana na Serikali kufanya vizuri, lini Wilaya ya Misenyi itapata maji kutoka kwenye chanzo cha Bukoba Mjini kwa sababu hawana uwezo wa kutumia yale maji yote?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nampongeza mzee wangu Mheshimiwa Bulembo. Moja, nimhakikishie maeneo ambayo sijawahi kufika ni Bukoba, baada ya Bunge hili nitafika Bukoba tunaangalie hali halisi na namna gani tunaweza tukashauriana kuweza kutatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji, kama nilivyoeleza, Bunge lako Tukufu limetuidhinishia bajeti yetu Sh.727,345,000,00, yote hii ni katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Sisi Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kikubwa Waheshimiwa Wabunge, tunaomba ushirikiano wa dhati katika kusimamia na kufuatilia miradi hii ya maji ambayo tunatekeleza katika maeneo yao.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa swali la msingi la Ulyankulu liko katika Majimbo mengi ya nchi hii, kutokuwa na shule za form five na form six. Serikali inatoa commitment gani na lini itaanza kufanya operation katika kila jimbo kupata shule za form five na form six? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, maombi yaliyopo katika Wizara yetu ambayo sisi tukiyapokea tunayapeleka Wizara ya Elimu kwa ajili ya usajili kwa sababu anayesajili ni Wizara ya Elimu ni mengi, lakini mengi yamekuja hivi karibuni, mwezi wa Nne mwishoni, mwezi wa Tano wakati tayari masuala ya bajeti yalikuwa yameshakamilika. Kwa hiyo, naomba sana nimwahidi Mheshimiwa Bulembo pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote na Bunge zima kwamba mwakani tutaweka utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba inavyofika Desemba, 2018, basi shule zote ambazo zina maombi maalum katika ofisi zetu za Serikali tutazisimamia ili ziweze kupata usajili.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimesimama kulihakikishia Bunge lako Tukufu Wizara yangu ambayo ndiyo ina jukumu la kusajili shule haina tatizo lolote la kusajili wakati wowote shule ambayo imekidhi vigezo. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Wakurugenzi na Maafisa Elimu kwa ujumla kama kuna shule ambayo inahitaji usajili, tunasajili wakati wowote ilmradi shule imekidhi vigezo. (Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kutokana na swali la msingi la ubovu wa barabara ya Serengeti, Wizara ya Maliasili inaniambiaje; kwa sababu barabara zimekuwa mbovu, Hoteli ya Seronera, Lobo, Ngorongoro na Lake Manyara zilikuwa ni hoteli katika nchi hii katika Hifadhi ya Serengeti? Leo hii watalii wakienda, wanabebewa maji kwenye ndoo. Wizara inayajua hayo? Inazirudisha lini hoteli hizi Serikalini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba tulikuwa na hoteli ambazo zilikuwa zinamilikiwa na Serikali katika miaka ya nyuma na hoteli hizi nyingi zilibinafsishwa. Kati ya hoteli 17 ambazo zilikuwa zimebinafsishwa ilionekana karibu hoteli 11 zilikuwa hazifanyi vizuri ikiwemo hizi hoteli chache ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumeliona hilo, tumeanza kufuatilia kupitia mikataba ile ambayo walipewa ili kuhakikisha kwamba kama tumeona kwamba hawakufanya yale waliyostahili kuyafanya na uwekezaji waliotakiwa kuufanya, Serikali iweze kuzichukua hizo hoteli na kuwapa wawekezaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baadhi ya hoteli sasa hivi zimechukua hatua, zinaboresha huduma zao. Hili analolisema la maji, kwa kweli sasa litaendelea kupungua hasa baada ya kuanza kutekeleza miradi mbalimbali ya kuhakikisha maji yanakuwepo katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi lililoulizwa na Mheshimiwa Azza, kule Mkoani Mara kuna Wilaya moja inaitwa Serengeti, katika ile Wilaya ya Serengeti kuna Bwawa moja linaitwa Manchira, limeanza tangu mwaka 1988, mpaka leo maji hayatoki unaambiwa kuna chujio. Naomba tamko la Serikali, lini maji yale yataanza kutoka kuwasaidia wananchi wa Serengeti, maana ni miaka 10 leo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, hakuna jambo lisilokuwa na mwisho na sisi kama viongozi wa Wizara hii ya Maji, jukumu letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge Baba yangu Mzee Bulembo, hebu tuonane tuweze kupata mawazo ya pamoja ili tuweze kusukuma katika kuhakikisha wananchi wale wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi naomba kuuliza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, wananchi wa Makoko katika mji wa Musoma waliachia eneo wananchi 95 mwaka 1982 mpaka leo ni miaka 36 hawajalipwa haki yao ya bilioni 1.4 Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi hao? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bulembo kwa sababu amelisemea jambo mahususi ambalo linahusu fidia, niseme tu nimelipokea na nitalishughulikia kujua status yake kwa maana ya jambo ambalo linahusisha fidia ili kuweza kujua kama tathmini na masuala yote ya uhakiki yalishafanyika na kama inastahili kutakiwa kulipwa.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri kuhusu swali lililopita, naomba kuiuliza Serikali, barabara ya Kyaka 2 kutoka Katoro - Ishembulilo - Kashamba - Kyaka; eneo lile ni bovu sana kila mwezi Aprili barabara haipitiki. Pamoja na kwamba amesema inahudumiwa na TANROADS, naomba commitment ya Serikali ya kuweka madaraja kwenye maeneo yale ili mwezi wa Aprili kuwe kunapitika kama sehemu nyingine. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Bulembo kwamba nimemsikia, nami nimwelekeze tu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera aende kuangalia eneo hili na kushauri tufanye nini juu ya kutengeneza daraja eneo hili korofi. Kama ilivyo kawaida, maeneo yote korofi nchi nzima tunaendelea kuyashughulikia wakati tukiendelea na harakati za kuboresha barabara kuhakikisha wananchi wetu wanapita muda wote katika maeneo yao.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwenye jimbo la Chalinze hakuna Hospitali ya Wilaya, mwenzi mmoja uliopita tulimsumbua Mheshimiwa Kangi Lugola tulikutana tumepata ajali, magari yetu yakaanza kusoma majeruhi, tukauliza shida ni nini? TAMISEMI kwa nini? Mnaweka hela Kibaha Mjini Kibaha Vijijini na kuna Tumbi? Kwa nini hamuwezi kupeleka hela katika Jimbo la Chalinze kupata Hospitali ya Wilaya kwa sababu kuna umbali mrefu watu wakipata ajali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, najua iko kiu kubwa sana Waheshimiwa Wabunge maeneo mengi ambayo wangependa Hospitali za Wilaya na tunaita Hospitali za Halmashauri ziweze kujengwa. Sasa katika hii ambayo umesemea kuhusiana na Chalinze kuwa na Hospitali ya Wilaya, sina uhakika katika orodha ya Hospitali za Halmashauri ambazo zimetengewa bilioni 1.9 kama Chalinze ipo au haipo. Kama inakidhi vigezo katika bajeti tunayoenda nayo kuna Hospitali tisa nazo tutaziingiza nje ya zile 67 sasa, kama na Chalinze ni mojawapo hilo sioni kama…
MHE. ALHAJI ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Misenyi katika Mkoa wa Kagera ni wilaya iliyoanza mwaka 2007 mpaka leo ina miaka 11, lakini haina Mahakama ya Wilaya. Wilaya ile ni ya mpakani, kuna wahamiaji haramu, kuna nyarubanja kahawa, kuna matatizo mengi sana. Sasa nataka kuiuliza Serikali yangu, ni lini wilaya hii itapata haki ya kuwa na Mahakama ya Wilaya ili kuwapunguzia adha wananchi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Alhaji Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba, Wilaya ya Misenyi inayo mashauri mengi hasa yanayohusu masuala ya ardhi na mimi mwenyewe binafsi mwaka jana nilitembelea Wilaya ya Misenyi na nilifika na kuoneshwa eneo ambalo limetengwa ili kujenga Mahakama ya Wilaya ya Misenyi. Kwa hiyo, niahidi kwamba, tulikuwa tumepanga kuanza kujenga Mahakama ya Wilaya ya Misenyi mwaka 2017/2018, tunabadilisha mipango ili tuweze kuiwezesha Mahakama hiyo kuanza kujengwa mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati wa bajeti tunaweza kuwa na maelezo mazuri zaidi ni lini ujenzi wa Mahakama ya Misenyi utaanza na kama nilivyosema mimi mwenyewe nimefika na kweli Misenyi kuna mashauri mengi sana ya ardhi.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na Naibu Waziri anayejibu maswali kule Kagera walifika na wakafanya mambo lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa bei elekezi kama alivyouliza Mheshimiwa Bilakwate kahawa ikauzwa kwa Sh.1,000, huku Karagwe hamna shida lakini ukija Muleba, Bukoba Vijijini, Misenyi bei ya Sh.1,000 watu hawajalipwa mpaka leo, mnasubiri nini? Si muende kama milivyoenda kwenye korosho watu wapate haki zao? Kahawa ipo kwenye maghala lakini mpaka leo watu hawajalipwa na ninyi Wizara ya Kilimo mmenyamaza. Nataka nipate majibu, ukienda Muleba, Chama cha Msingi Magata, Misenyi, Katoro, Kaibanja, Kazinga watu wana shida na kahawa mmeshachukua na hela hawajalipwa, ni lini watalipwa hela zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Alhaj Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, sisi Serikali hatujanunua kahawa ya wakulima wa Tanzania popote pale. Wakulima hawa kwa kupitia vyama vyao vya msingi na vyama vikuu waliamua kwa hiari yao kwenda kuuza kahawa wenyewe kule mnadani Moshi. Kilichotokea kwenye Wilaya hizi alizozitaja Muleba, Bukoba na Bukoba Vijijini na sehemu nyingine ni kwamba kahawa yao wameshakoboa, wamefika pale Kilimanjaro Moshi kama nilivyosema kutokana na kuyumba kwa bei kwenye soko la dunia na uzalishaji mkubwa uliotokea kwa nchi ya Brazil kuingiza sokoni zaidi ya magunia milioni saba mwaka jana ikaathiri bei nzima ya kahawa na kusababisha bei kushuka chini mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu walienda kuuza wenyewe maana yake ile bei imewakuta wao moja kwa moja. Kilicholewesha mpaka sasa kutolipwa fedha zao ni hiki Chama cha KCU hakijauza kahawa yote. Kwa hiyo, sehemu nyingine hawajalipwa kwa sababu wenyewe hawajauza kahawa hiyo. (Makofi)
MHE. ALHAJI ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na jibu zuri la Mheshimiwa Waziri mhusika, kuna viongozi wa Serikali na hata humu Bungeni waliokopa SUMA katika matrekta hayo. Mheshimiwa Waziri licha ya kuwatangaza wamefikishwa kwa Spika ili tutangaziwe humu Bungeni tujue ni wapi wanaodaiwa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wako viongozi wa Serikali na baadhi ya Wabunge waliokopa matrekta haya. Juhudi tulizozifanya ni kwamba, tuliziandikia mamlaka za ajira za kila mmoja, kwa hivyo, Mheshimiwa Spika anayo orodha ya Wabunge na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waliohusika tumeandika barua TAMISEMI na Wizara zote kwa ujumla, kila mamlaka ya ajira imeandikiwa barua. Ni mategemeo yangu kwamba, kila mamlaka ya ajira itachukua hatua stahili ili kuweza kuzipata fedha hizi.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi sitaki kukuuliza maswali kila siku lakini naomba swali hili utoe tamko. Wananchi wa Makoko katika Manispaa ya Musoma wanadai fidia mwaka wa 13, swali hili nimeshaliuliza humu, Katibu Mkuu amewapelekea barua ya kuwapa subira. Watu wamekufa, wamerithi, wameacha maeneo yao; miaka 13 Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naomba utoe tamko hapa Bungeni watu hawa watalipwa lini.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alhaj Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi lipo katika maeneo mengi. Kila mwaka wakati tunawasilisha bajeti yetu nimekuwa nikisema kwamba fedha zikitengwa tutalipa fidia. Kwa bahati mbaya fedha zinazotengwa au zinazotolewa hazikidhi kulipa watu wote kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha tunaoumalizia tumelipa fidia eneo la Kilwa kwa ajili ya Navy Base kuwepo pale lakini bado tunatarajia Wizara ya Fedha itatupatia fedha kabla ya mwisho wa mwaka huu wa bajeti ili tuendelee kulipa fidia hizo. Tunatambua kwamba eneo la Makoko linastahili kulipwa fidia pamoja na maeneo mengine kadhaa na tutafanya hivyo kadri fedha zinapopatikana.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na aliyejibu swali sasa hivi, Jiji ambalo lina watoto wengi kuliko hili, moja ya nane ya Dodoma ni Jiji la Dar es Salaam. Hao wa Dar es Salaam ambao sasa limeitwa Jiji la Utalii, lina wageni wengi na ni wengi, yaani ni wengi kuliko; hatua zipi za makusudi zinachukuliwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuondoa ombaomba ili hawa watalii wanaonyang’anywa, wanaoibiwa waweze kuwa na raha katika Jiji la Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, sina takwimu za papo kwa papo, lakini kwa ujumla najua katika sensa yetu tuliyofanya, tulibaini kama watoto zaidi 6,000, lakini nahitaji nifanye uhakiki kujua katika Majiji haya ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma na maeneo mengine ni wapi ambapo takwimu zipo nyingi.

Mheshimiwa Spika, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo taarifa tutampatia. Sisi kama Wizara, tumeendelea kulifanyia kazi suala hili, lakini kama alivyosema katika jibu la msingi la Mheshimiwa Kandege ni kwamba jukumu la malezi ya mtoto ni la familia. Pale inaposhindikana ni jamii ambayo inaizunguka na mwisho pale inapoonekana kabisa hakuna wa kuwasaidia wale watoto, sisi kama Serikali tunachukua majukumu hayo.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba tunatimiza majukumu yetu ya msingi ya kuwalea watoto kama ilivyoainishwa katika sheria.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza, Tarafa za Luoimbo, Suba na Nyancha ni tarafa zinazounganika, watu wanapita sehemu hiyo na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi na muda wa ahadi za Rais kweli zitatekelezwa zote, je, imo ndani ya bajeti inayokuja kwamba inaanza kutengenezwa hata kama haitaisha kwa mwaka huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini wananchi wa Rorya wataweza kuwa na matumaini kwamba Serikali yao inawakumbuka katika kilio chao hiki cha mafuriko ya kila mwaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba ipo kwenye bajeti ya mwaka huu, naomba anipe muda tupitie bajeti ya mwaka huu tutaangalia kama ipo. Cha muhimu ni kwamba mimi nilienda Rorya, nimefanya ziara ya kikazi, ni miongoni mwa wilaya za mwanzo kabisa nimezitembelea. Nimeenda Luoimbo, Suba na hii ni wilaya moja ilikuwa Tarime na Rorya imegawanywa hivi karibuni na imekuja na changamoto. Naomba wananchi wa Rorya, Mara na Watanzania wote waendelee kuiamini Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ahadi hizi zote zitatekelezwa kabla ya uchaguzi wa mwaka wa fedha ujao. Tathmini imeshafanyika, tunahitaji shilingi bilioni 1.15 ya kukamilisha kazi hii. Ahsante.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Maswali yangu mawili ya nyongeza.

(a) Pamoja na wataalam kuangalia athari ya fidia lakini wataalam hawa kwa nini hawakuangalia upande wa pili wa Mkoa wa Kagera? Uwanja wa Mkoa wa Kagera unaweza ukapakia Airbus kutoka Bukoba, ikajaa bila kwenda popote, kwa sababu watu wa Uganda, Burundi, Congo, wote wanapandia pale.

Je, upanuzi huu kwenda Daraja C mnategemea ufanyike lini? Naomba wataalam waangalie faida wasiangalie hasara peke yake.

(b) Kwa sababu kuna uwanja wa ambao ulikuwepo miaka yote, awamu zote kuanzia Mwalimu Nyerere zaidi ya miaka 41, Omukajunguti, leo hii Bukoba haiwezi kupanuliwa, kwa nini uwanja huu usiendelee kubaki ndani ya mamlaka ya viwanja vya ndege ili miaka ijayo mkitaka kupanua labda pesa zipo tusihangaike kutafuta mahali pa kwenda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo siyo ya Bukoba peke yake, lakini ya nchi nzima. Nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumeliona hilo kwamba Uwanja wa Ndege wa Bukoba ni muhimu sana. Ndiyo maana katika mipango yetu na wakati mwingine Mheshimiwa Mbunge avute subira, ataona namna tulivyojipanga, kama nilivyosema kuuboresha uwanja huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga ili uwanja huu tuweze kuuwekea pia VIP Lounge, tumejipanga pia kwa ajili ya kufanya maboresho kama nilivyosema ili tuweze kutoa huduma ya ndege nyingi. Kwa maana hiyo, ili kuweza kukidhi mahitaji ya matumizi ya uwanja huu, tutakapofanya maboresho, ikiwa ni pamoja na kuweka taa za kuongoza marubani, ina maana tutaongeza idadi ya miruko. Kwa sababu siyo suala la kuongeza ndege kubwa peke yake linaweza kukidhi mahitaji ya Bukoba, lakini ni pamoja na kuongeza idadi ya miruko katika uwanja huu. Kwa hiyo, tukifanya maboresho, idadi ya miruko tutaiongeza wakati tunatazama siku za usoni tufanye nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, matumizi ya uwanja wa Omukajunguti, niseme tu uwanja huu bado unamilikiwa na Serikali na bado utaendelea kumilikiwa na Serikali kwa sababu maendeleo ya nchi hii yanakwenda kwa kasi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, nasi wakati tunasonga mbele tunaendelea kutazama matumizi mazuri na maboresho ya uwanja huo wa Omukajunguti.

Nimhakikishie tu Mheshimiwa kwamba tunautazama vizuri na nitoe tu maelekezo kwa wenzetu upande wa TAA tuutazame uwanja huu kama kutahitaji kuweka uzio, tuweke kwa maana ya kuulinda. Pia niwasihi tu wananchi wa Bukoba na watu wanaozunguka eneo hili tusivamie eneo hili, eneo hili litakuja kutupa manufaa sisi na Watanzania wote kwa ujumla. Ahsante.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi, niipongeze Wizara ya Kilimo na Waziri Mkuu kwa kazi waliyoifanya Kagera. Wakulima wa kahawa Mkoa wa Kagera wa Muleba, Misenyi na Bukoba Vijijini kupitia KDCU na KCU mpaka leo kuna ambao hawajalipwa malipo yao ya kupeleka kahawa KDCU na KCU. La pili, bado kuna wakulima ndani wana kahawa…

MWENYEKITI: Swali ni moja tu Mheshimiwa.

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe tamko kwa wale wakulima ambao hawajalipwa haki yao, ni lini watalipwa haki yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alhaj Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna baadhi ya wakulima waliouza kupitia Vyama vya Ushirika vya KCU na KDCU hawajalipwa malipo yao mpaka sasa hata wale wa Tarime Vijijini katika Mkoa wa Musoma. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, walioenda kuuza kahawa ile ni wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika kwenye mnada wa Moshi, kwa hiyo watalipwa baada ya kahawa yao kuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea katika msimu wa mwaka jana kahawa ilianguka sana sokoni kwa hiyo wakulima wale waliona siyo busara kuuza kwa bei ya chini kuliko gharama za uzalishaji walizoingia. Pia, kahawa hii ambayo ikikobolewa inatoka madaraja zaidi ya matano, wakati mwingine inachelewa kwa sababu imeuzwa daraja moja, madaraja mengine hayajauzwa. Kwa hiyo, wanasubiri ili kuuza kahawa yote na kwenda kuwalipa wakulima na wanachama wao. Kwa hiyo, naomba waendelee kuwa na subira kwa sababu kahawa hiyo wameuza wenyewe kila wanapouza watalipwa.
MHE. ALHAJI ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana,kutokana na swali la msingi, barabara ya Korogwe – Magoma- Mashewa – Mtoni Mombo – Kibaoni – Kalahani – Maramba kwenda Tanga Mjini ina tatizo kama la Mlalo lakini barabara ile tatizo kubwa kuna makalavati madogo madogo ambayo mngeyafanyia haraka ili wananchi waweze kupita. Je, Wizara inatuamnia nini wale wananchi watoke kwenye kisiwa kilichopo sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo haya Mheshimiwa Mbunge aliyoyataja yana changamoto, Mheshimiwa Bulembo nikuhakikishie kwamba nilivyofanya ziara maalum kuangalia maeneo ambayo yameathirika na mvua katika maeneo ya Mkoa wa Tanga nikianza kule Kilindi, nimekwenda Handeni lakini kwenye maeneo hayo umeyataja tumefanya ziara na Waheshimiwa Wabunge kwa hiyo nimeona. Na yale maeneo ambayo kimsingi yameharibiwa na yana nafasi ya kufanyiwa matengenezo kwa sababu yapo maeneo mengine ambayo bado maji yanapita kwa wingi sio rahisi kwa muda huu kufanya matengenezo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa maeneo hayo tulitoa maelekezo kwa maana kwamba TANROADS na TARURA washirikiane maeneo ambayo tuliyaona kwamba kwa haraka waweze kuweka makalavati na maeneo hayo mengi mengine ujenzi umekwishafanyika. Lakini kwa maeneo ambayo changamoto zake zinahitaji utatuzi wake kufanyika baada ya mvua kukoma, haya nayo tunayaweka kwenye utaratibu kama nilivyozungumza tumeshayatambua, tunayatengea fedha. Tunawahakikishia wananchi kwamba wanapita kwenye maeneo yale.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uvute subira tumetambua maeneo yote, tutaendelea kuyashughulikia kulingana na changamoto na hali ilivyo kutokana na sehemu mahsusi.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni kanuni namba ngapi zinazoelekeza kampuni ikiuzwa asilimia mia iendelee kutumia kibali cha kampuni nyingine na jina tofauti la kampuni nyingine?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini brand ya Garda World itumike kama nembo badala ya kutumika kama kampuni nyingine na kwa hali hii hamuoni haki za watumishi wa kampuni ya zamani zinapotea kwa kuhalalishwa na Serikali yenyewe?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu Maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Alhaj Abdallah Majura Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa usahihi kilichouzwa ni hisa. Hivyo wamiliki wa hisa wamebadilika lakini kampuni inabaki kama ilivyo. Hivyo Ultimate Security Company iko palepale, kwa usajili uleule na watumishi walewale na mikataba yake ileile na mali zake zote na vibali vyake vilevile na biashara yake yote. Hivyo uhalali wa kutumia vibali unapatikana na sheria iliyotumika ni Companies Act, No.12 kama ilivyorejewa 2002, Cap. 212, section 74 - 83. Hicho kinachoitwa jina lingine ni “brand name” ambalo inaruhusiwa chini ya Sheria ya Trade Marks, No.12 ya 1986, Cap.326 na Trade Mark hiyo imesajiliwa na BRELA chini ya sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, haki za watumishi zinabaki kama zilivyo na kilichonunuliwa ni hisa. Hivyo, kampuni na vyote vilivyomo ikiwa ni pamoja na watumishi na haki zao zinabaki kama zilivyo kwa mujibu wa mikataba yao.