Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jerome Dismas Bwanausi (31 total)

MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa matatizo haya ya KNCU yanafanana na matatizo yaliyopo katika Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU cha Mkoa wa Mtwara na Vyama vyake vya Msingi, nataka niulize swali; kwa kuwa wakulima wa korosho wa Wilaya ya Masasi wanadai bilioni nne ambazo ni malipo ya tatu ya malipo ya korosho na hadi sasa kumekuwa na ubabaishaji mkubwa juu ya kupatikana kwa malipo hayo. Je, Mheshimiwa Waziri atatoa maelekezo gani kwa Mrajis wa Vyama kuhakikisha kwamba anafanya uchunguzi wa haraka ili wananchi wale waweze kulipwa malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba changamoto ya CORECU ni changamoto ambayo ipo katika Vyama vya Ushirika vingi, vingi vina madeni. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge, tukitoka hapa leo tukutane ofisini kwangu niweze kupata hili analosema kwa mapana na marefu ili tuanze kufanyia kazi mara moja na nimfahamishe tu kwamba, tayari kuna kikao kinaendelea huku cha Vyama Vikuu vya Ushirika na itakuwa ni fursa vilevile ya kulizungumzia katika wakati huu. Kwa hiyo nimwahidi tu kwamba, tutalifanyia kazi.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linaelekea kwa Naibu Waziri. Katika mikoa ya Mtwara na Lindi tuna tatizo kubwa sana la usambazaji wa umeme kwa kuwa haikuwahi kupata Phase I ya REA wala fedha za MCC. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akalithibitishia Bunge hili kwamba, katika awamu hii ya tatu ya REA vijiji vyote vitapewa umuhimu wa kupewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kabisa Mtwara na Lindi yamekuwa ni maeneo ambayo kwa miaka mingi hayapati umeme, lakini baada ya ugunduzi wa gesi miaka miwili iliyopita, kati ya maeneo ambayo tuliyapa vipaumbele kuyapatia umeme wa gharama nafuu ni pamoja na Mtwara na Lindi. Hii ni kwa sababu tulianza sasa kutumia umeme wa gesi kwa mikoa yote hiyo miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie tu kwa mikoa hii miwili tuliwatengea kisima ambacho kwa ujumla wake kinapata megawatt 18 za umeme wa gesi. Kwa hiyo, watu wa Mtwara na Lindi wanaweza kupata umeme na tena wa gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kwenye REA Awamu ya Tatu inayokuja kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, tutahakikisha kwamba vijiji vyote vya Mtwara na Lindi ambavyo vimebaki kutopata umeme kwenye REA Awamu ya Kwanza kwa sababu haikuwepo na Awamu ya Pili ambayo imekwenda kwa kiwango kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahakikisha vijiji vyote vya Mtwara na Lindi ambavyo vimeingia kwenye mpango huu wa REA Awamu ya Tatu vitapata umeme wa uhakika.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali na naomba niulize maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini swali langu la kwanza; kwa kuwa Serikali imeamua kuifanyia kazi barabara hiyo ya ulinzi; na kwakuwa kuna vijiji kumi vya ulinzi ambavyo vipo katika Jimbo la Lulindi na hakuna daraja pale, daraja lake la Mto Myesi Mbagala lilichukuliwa na maji wakati wa mafuriko 2012.
Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuwaagiza watu wa TANROADS Mkoa wa Mtwara walifanyie tathmini daraja hilo ili liweze kujengwa wakati huu barabara hii ikitengenezwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba, kwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliahidi kusaidia ujenzi wa madaraja matatu ambayo yalizolewa na maji katika mafuriko ya mwaka 2013 na 2014; madaraja ya Mto Mwiche katika kijiji cha Shaurimoyo, Nakalola na Nanjota na tayari lile la Nanjota limeanza kufanyiwa kazi; je, Mheshimiwa Waziri atalithibitisha vipi Bunge hili kwamba yale madaraja ya Shaurimoyo pamoja na Nakalola sasa litaingia kwenye mpango wa kujengwa?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikujulishe kwamba nilikuwepo katika hilo eneo. Nilikwenda na Mheshimiwa Mbunge, niliwaona wale watu jinsi wanavyopata shida kwa sababu zile kata zote zilikuwa zimekatwa kabisa, hakukuwa na mawasiliano; na kwa kweli tuliagiza angalau daraja moja liunganishwe kwa haraka ili watu waanze kupata sehemu ya mawasiliano waweze kwenda Masasi kujipatia huduma zao za kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, madaraja hayo mengine mawili yametengewa bajeti na nawaagiza TANROADS watoe kipaumbele ili Kata zile zote ambazo zilikuwa zimetengwa ziweze kupata huduma kwa urahisi zaidi kama ilivyokuwa awali. Kwa kutegemea hilo daraja moja tu haitoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu daraja la ulinzi, naomba nalo likafanyiwe tathmini kama ambavyo mwakilishi wa wananchi wa kule ameomba na ninafahamu kuna vijiji vingi ambavyo vipo katika ule mpaka, barabara ilikuwa ni ya Jeshi, lakini kwa sasa kuna makazi mengi na watu wanalima sana kule. Kwa hiyo, naomba vilevile pamoja na daraja hili katika barabara ile ya ulinzi walifanyie tathmini halafu waje na taarifa ambayo itatusaidia kufanya maamuzi ya nini kifanyike.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru majibu ya Naibu Waziri. Swali langu la kwanza, kwa kuwa malipo ya bonus ni haki ya wakulima kwa maana ni malipo ya tatu ya korosho na wananchi wale tangu mwezi Disemba wanazungushwa kupata fedha yao. Je, Serikali haioni kuna haja ya kutoa kauli sana kwamba wananchi wale waweze kulipwa fedha zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa mchanganuo wa fedha zinazopaswa kulipwa kwa wakulima ulishatolewa Bodi ya Korosho tangu Aprili na Serikali imepata kigugumizi hadi sasa kutotoa kauli ya wananchi wale kulipwa na Waziri naye aliahidi kuja pale. Je, leo Waziri anaweza kutoa kauli ya Serikali kuhusu ujio wake katika eneo hilo? Pia ni kwa nini asitoe tamko kuwaambia vyama kuanzia sasa wawalipe wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu bonus ni kweli kabisa kwamba wananchi wamepunjwa bonus mpaka Sh.200 katika kilo. Kama nilivyosema awali, Serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu ubadhirifu ambao umefanywa na Vyama vya Ushirika ili wale wote ambao wamehusika na mapunjo hayo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. Nitumie fursa hii kuvitaka Vyama vya Msingi kuhakikisha kwamba wakulima wanapata salio la bonus yao ambayo hawajalipwa mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la sisi kwenda, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara baada ya Bunge la Bajeti tutafanya utaratibu kwenda kuongea na wananchi na kufuatilia kwa ukaribu zaidi ili waweze kulipwa bonasi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kuwaeleza na kuwashauri Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wa maeneo yanayolimwa korosho kwamba kinacholeta changamoto kubwa katika malipo stahili kwa ajili ya korosho ni kwa sababu Vyama vya Msingi pamoja na wakulima wanachukua madeni kutoka kwenye mabenki ili kuwalipa wakulima kabla korosho ile haijapata mteja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuwashauri kwamba wawe na subira, wasiwe na haraka ya kwenda kuchukua mikopo, badala yake wakusanye korosho kwa utaratibu wetu ule wa stakabadhi ghalani ili korosho ile iweze kununuliwa na hivyo kuondokana na utaratibu ambao inabidi ulipe interest za benki. Mara nyingine viongozi ambao siyo waadilifu wa Vyama vya Ushirika pamoja na Maafisa Ushirika wanatumia mtindo huo kama ni mwanya wa kuwaibia na kufanya makato ambayo yanawafanya wakulima wasiweze kupata fedha wanayostahili. Wawe na subira, waweke korosho yao, wauze kwa pamoja, waache kuchukua kwanza mkopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba migogoro hii ya wakulima na wafugaji inasambaa karibu maeneo mengi hapa nchini ikiwa ni pamoja na katika Jimbo la Lulindi katika Vijiji vya Sindano, Maparawe, Mapili pamoja na Manyuli.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuja kule kusaidiana na kusuluhisha matatizo yaliyopo kati ya mpaka wa Tanzania na Msumbiji hususani katika eneo la kando kando mwa Mto Ruvuma ambako wananchi wengi ndio hulima lakini tayari kuna uvamizi mkubwa wa wafugaji ambao sasa upotevu wa amani umeanza kuwepo katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, changamoto za migogoro ya wafugaji na wakulima na migogoro ya ardhi ya aina mbalimbali ni kweli kwamba ipo karibia kila kona ya nchi yetu. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tupo tayari kwenda kila Jimbo katika kila kona ya kuangalia namna gani ya kutatua, Wizara na Serikali kwa ujumla inafikiria kutafuta suluhu ya jumla; suluhu ambayo itasaidia katika maeneo yote badala ya kila wakati labda Waziri na Naibu Waziri kukimbia kila mgogoro unapotokea. Kwa sababu mnafahamu Waheshimiwa Wabunge kwamba nchi yetu ni kubwa inawezekana tukashindwa kufika kote kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo nimeshafika Lulindi kwa Mheshimiwa Bwanausi lakini nilienda kushughulikia kero nyingine kabisa ya korosho. Kwa hiyo, bado ni Tanzania yetu hiyo hiyo kama inaelekea kwamba utatuzi wa jumla hautaweza kushughulikia kero aliyoileta Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari kwenda kule na labda itakuwa vilevile ni fursa ya kwenda kumalizia viporo vya korosho nilivyoviacha.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili kama ifuatavyo:-
Swali langu la kwanza; Mheshimiwa Waziri atakiri kwamba wananchi wa Kata ya Mkundi, Kata ya Mpindimbi na Kata ya Singano wanapata tatizo kubwa sana kutokana na kutokuwepo kwa madaraja haya. Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Awamu ya Nne na Rais wa Jamhuri ya Muungano, aliahidi kwamba atasaidia jambo hili ili madaraja yale yajengwe. Je, nini kauli yake leo; kwa sababu hata usanifu katika madaraja hayo haujafanyika? Nini maelekezo yake kwa Watendaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa barabara ya Ulinzi ambayo inaunganisha kati ya Tanzania na Msumbiji ni barabara muhimu sana ya kiuchumi kwa wananchi katika maeneo yetu: Je, ni hatua gani zimeshafikia sasa katika maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo katika awamu hii ambayo ameisema kwamba shilingi milioni 140 zimeshapatikana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ahadi hii ya kuifungua hii barabara na pamoja na kuwawezesha wananchi wa Kata hizi za Mkundi, Mpindimbi na Singano zimetolewa na viongozi wetu. Naomba kumhakikishia kwamba haya niliyoyasema katika jibu langu la msingi ndiyo hatua madhubuti za kufikia utekelezaji wa ahadi hizi za viongozi walizozitoa katika nyakati mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo hayo ambao wanaathirika, kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha madaraja yale yanarudishwa, lakini vilevile barabara ile ya Ulinzi inafunguliwa. Nini tunakifanya katika hiyo Shilingi milioni 140?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utangazaji wa tenda kwa ajili ya kazi hii utafanyika hivi karibuni na vilevile kazi hii ya upembuzi yakinifu nayo itafanywa na Mtendaji wa TANROADS Mkoa wa Mtwara. Labda kwa taarifa hii naye nimkumbushe kama alikuwa amejisahau kwamba kazi ya kuhakikisha hayo madaraja yanafanyiwa usanifu ili yaweze kukamilika kama viongozi wetu walivyoahidi, ifanywe haraka ili kazi ile itekelezwe kama viongozi walivyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Kwa kuwa Naibu Waziri anayeshughulika na barabara yupo, je, anaweza akalithibitishia Bunge hili kwamba fedha hizi TANROADS
wameshazitenga kweli kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii? Swali langu la pili, je, ni lini madaraja haya yatajengwa, kwa sababu wananchi hawa wa maeneo ya Miesi, Kata za Mkundi na Mpindimbi kwa miaka minne sasa wanapata tatizo kubwa sana baada ya madaraja haya yaliyokuwepo kuzolewa na mafuriko, je, ni lini baada ya bajeti
kazi itaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge sana kwa harakati zake kubwa na kazi kubwa anayofanya katika Jimbo lake kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za maendeleo. Kama tulivyosema, kutokana na kazi hiyo nzuri
ambayo ameifanya ndiyo maana sasa, kwa sababu barabara ile ilikuwa chini ya barabara ya Halmashauri lakini kutokana na msukumo mkubwa ndiyo maana TANROADS imeamua kufanya assessment ya barabara ile na kukubali
kwamba madaraja haya yataweza kujengwa.
Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge hilo ondoa hofu kwa sababu kwanza imeshafanyika hiyo tathmini na kuona kwamba shilingi bilioni tatu na ofisi ya ujenzi naamini katika harakati za hii bajeti ambayo itakuja hapa tutaona katika jedwali hilo ambalo linaeleza kwa sababu tathmini wameshaifanya tayari.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, suala la ni lini barabara hii itajengwa. Barabara hii itajengwa mara baada ya kutengwa kwa bajeti, kwa hiyo, naomba nikuondoe hofu Mheshimiwa Dismas kwa sababu wananchi wa eneo lile wana umuhimu mkubwa wa barabara hii ambayo ni barabara ya kimkakati kwa suala zima la uchumi wa korosho katika maeneo haya, naomba ondoa hofu. Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wananchi wa Lulindi wanapata huduma ya ujenzi wa barabara.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninaomba sasa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba, TTCL walishalipwa fedha za sola za Kimarekani 94,000 na ilikuwa ni mwaka 2015. Je, Serikali kwa nini haijawasisitiza TTCL kukamilisha kazi hii ambayo imechukua muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, miongoni mwa kata ambazo Kampuni ya Viettel ilikuwa imeshinda zabuni mwaka 2015 ni pamoja na kata ya Sindano, lakini hadi sasa kazi hiyo haijafanyika. Je, Mheshimiwa Waziri atalithibitishia Bunge hili kwamba Viettel watakwenda kufanya hiyo kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeisisitiza sana TTCL ikamilishe kazi iliyoianza. Na kama utarudia tena sehemu ambayo nilijibu swali la msingi ni kwamba, kazi hii waliikamilisha, lakini waliikamilisha kwa kutumia teknolojia ya CDMA na sasa wanaondoka katika teknolojia hii ya CDMA kwa sababu teknolojia hii haiwawezeshi wao kuongeza hizi huduma za nyongeza za mobile money na banking kwa hiyo, wanabadilisha mtandao na mtakumbuka kuna wakati hapa Dodoma walizindua ile ya 4G LTE kwa hiyo, sasa wapo katika mpango huo wa kuzindua huo mtandao mpya na hivyo kazi hiyo tutahakikisha inakamilika mapema kama ambavyo wao wameahidi by June, 2017 watakuwa wamefika kule Lupaso na Lipumbiru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu Viettel, ninafahamu Viettel wamekuwa na matatizo kidogo kwa sababu ya mikataba na tunarekebisha kwa sababu, kuna baadhi ya kodi walikuwa wanatarajia wasilipe. Kwa hiyo, wameingiza vifaa vyao vya kuweza kutuletea mawasiliano, lakini vimekwama kidogo kwa sababu ya malipo ya kodi na tutahakikisha hilo linasuluhishwa haraka, wanalipa kodi inayotakiwa, ili hatimaye vifaa hivyo viende vikafanye kazi, vikasimikwe kule kulikokusudiwa.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, Mkoa wa Mtwara na Lindi ndiyo mikoa ambayo ina vijiji vingi sana ambavyo havijapatiwa umeme. Je, ni lini mikoa hii itapewa kipaumbele maalum ili vijiji vingi viweze kupata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa Mikoa ya Mtwara na Lindi maeneo mengi hayajafikiwa na miundombinu ya umeme. Nimhakikishie Mheshimiwa Bwanausi na namshukuru sana, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini hapo nyuma, tumeshirikiana sana na amefanya kazi kubwa kwenye jimbo lake, naomba nimpongeze kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumeipa kipaumbele kikubwa sana mikoa hii miwili. Tarehe 15 hadi tarehe 18 tutakuwa tunafanya kazi ya kuzindua na kuelekeza Wataalam wetu wa TANESCO kupeleka umeme katika mikoa hii miwili, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; tunarekebisha miundombinu ya Mtwara. Hivi sasa tunajenga transmission line ya kutoka Mtwara umbali wa kilometa 80 na umeme wa KVA 132, ili umeme huo upelekwe Mtwara Mkoa mzima na maeneo mengine ya Lindi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bwanausi Serikali imetumia hatua kubwa sana na imegharimu shilingi bilioni mia nane sabini na nane kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Bwanausi, lakini nampa uhakika kwamba, Serikali inaipa vipaumbele sana Mikoa ya Lindi na Mtwara na mwaka 2020 na 2021 vijiji vyote vya Mtwara na Lindi vitakuwa vimepata umeme.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi imeshaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Mtwara. Je, Mheshimiwa Waziri anawathibitishia nini wananchi ambao walipaswa kulipwa fidia zao wanalipwa fidia haraka ili kupisha ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, tulishajadiliana kuhusu suala hili na tulikubaliana kwamba tuangalie namna zile fedha zilizotengwa ni kiasi gani kitumike kwa ajili ya fidia na kiasi gani kiendelee kukamilisha ujenzi wa barabara ile. Nimuombe tu tuwasiliane ili hatimaye tukubaliane yeye na sisi. Ninachomhakikishia wote wanaostahili kulipwa fidia katika barabara ile watalipwa fidia, hakuna ambaye hatalipwa fidia. Hilo ndilo ninalokuhakikishia na nilikwambia hivyo kabla, nakushukuru sana.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo la Mheshimiwa Mama Kilango linafanana na tatizo lilipo kwangu kuhusiana na mbaazi ambapo wananchi wengi wamelima mbaazi kwa wingi na walihamasishwa kwamba kuna soko kubwa kule India.
Naomba Serikali itoe tamko ni lini mbaazi zile ambazo wananchi wanazo kwa wingi zitaanza kununuliwa?
WAZIRI WA VIWANDA, BISHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, ningekuwa na uwezo hili ndiyo swali ambalo ningependa nisiulizwe leo. Tunalo tatizo la mbaazi, Mheshimiwa Modi, Waziri Mkuu wa India alikuja hapa na akatuhakikishia soko la mbaazi nchini kwake, wananchi walisikia na mimi siwezi kukana nilikuwa mojawapo ya watu waliowahamasisha wananchi walime mbaazi na wamelima. Kilichotokea kwa maandishi, Serikali ya India imetuandikia barua kwamba haitanunua mbaazi zetu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais akanituma India, nimekwenda India na vielelezo kwamba kulingana na mkataba wa tarehe 14 Januari 2000, Tanzania na India tulikubaliana kwenye suala hili mnapaswa mnunue mbaazi zetu. Tukazungumza vizuri na Serikali ya India wakapitia makabrasha yao wakaona kweli kuna haja ya kununua mbaazi zetu. Wakatuuliza takwimu tunazopaswa kupeleka kule, nikaangalia takwimu mara ya mwisho tulikuwa tumepeleka tani 280, tukakisia kwamba tutawaletea tani 300, nikatoka na bashasha na nderemo narudi nyumbani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufika hapa yule Waziri wa Biashara akapandishwa cheo na kuwa Waziri wa Ulinzi ikabidi nifanye kazi sasa ya kuanza kujenga urafiki na Waziri mpya kumueleza katika makabidhiano waweke suala langu. Hapa nilipo kila siku nimeweka Afisa Mkurugenzi anayewasiliana na India kuangalia kitu gani kinachoendelea.
Mheshimiwa Sapika, katika nchi nyingine, watu wako sensitive na watu wao, kilichotokea India walikuwa wana deficit ya tani milioni tano za mbaazi sasa wananchi wao wamelima wame-bridge ile gap na wananchi wa India Serikali haifanyi lolote mpaka iwafikirie wao. Mimi sifanyi protectionism, lakini na mimi nataka kuangalia watu wangu, masoko yangu yanakuwaje ndiyo maana naweza nikafanya mambo mengine mtu anasema Mwijage unakurupuka, hapana, naagalia maslahi ya wakulima wangu na ndiyo maana mimi naonekana kama mtu wa korosho na mimi naangalia korosho zangu ziende namna gani.
Mheshimiwa Spika, hili ndiyo tatizo lililotupata kwenye mbaazi na nalifuatilia na napozungumza Bwana Gugu, Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa kabla ya saa 6.00 unieleze huyo mhindi ameshasema kitu gani. (Makofi/Kicheko)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu kwa kujibu maswali kwa ufasaha sana na natambua kazi nzuri inayofanywa na Waziri wa Kilimo akimsaidia katika kuhakikisha kwamba tunaboresha soko la korosho, nataka niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, msimu wa ununuzi wa korosho umeshaanza, na katika Wilaya ya Msasi kuna uhaba mkubwa sana wa magunia kiasi cha kupelekea wananchi wote kuchanganyikiwa kutokana na kutopata magunia ambayo yanawawezesha wao kwenda kuuza korosho zao katika maghala.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawambia nini wananchi wa Wilaya ya Msasi ambao hivi sasa hawajui la kufanya baada ya Serikali kushindwa kuwapelekea magunia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakulima wa Wilaya ya Masasi katika msimu wa mwaka 2015/2016 hawajalipwa kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia sita. Katika msimu wa 2016/2017 hawajalipwa kiasi cha shilingi bilioni moja, na katika msimu huu wa sasa tayari minada mitatu imefanyika lakini kumekuwa na kusua sua kwa kuwalipa wakulima. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya madeni makubwa haya yaliyopo kwa wakulima wa Wilaya ya Masasi?
Je, pia Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuandamana na mimi kwenda Masasi pamoja na Mbunge wa Msasi kwenda kushuhudia tatizo la magunia lakini pia kuangalia mnada?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kukiri kabisa kwamba nimkweli kumekuwa na uhaba wa magunia kwa wakulima wa korosho katika Mikoa ya Lindi na Mtwara hususani katika Wilaya ya Masasi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuchelewa huko naomba niliambie Bunge lako Tukufu, ni kwamba kumetokana na mkandarasi aliyekuwepo kuchelewa kufikisha magunia haya kwa wakati. Nimemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika ambaye ndiye muhusika kwamba mkandarasi huyu awe amepewa seven days awe ameshakabidhi magunia haya pamoja na kamba kwa wakulima hawa wa korosho, failure to do that basi zabuni yake ivunjwe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nitoe habari njema kwa wakulima wote wa korosho hususani katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwamba meli itawasili katika Bandari ya Mtwara kesho kutwa Jumapili tarehe 12/11/2017, magunia milioni moja pamoja na kamba yatafika mahali pale. Vilevile na mimi katika swali la Mheshimiwa Mbunge niko radhi kwenda huko Mtwara na nategemea kwenda wiki ijayo kuhakikisha na kujiridhisha kabisa kama magunia haya na yameshafika kule site.
Mheshimiwa Spika, vilevile ni kwamba vyama vile vya msingi vya ushirika ambavyo viko kule, vilikuwa vimefanya uzembe katika kugawa magunia haya kiholela; na mimi namuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika ambaye ndiye anayehusika na vyama hivi kwamba avunje bodi zote za msingi za vyama hivyo vya ushirika. Mimi nitafuatilia kwa ukaribu ili kuhakiksha kabisa kwamba hili jambo limefanikiwa na linatendeka kwa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la (b) kuhusu wale wote ambao wamefanya ubadhirifu katika kuhakikisha kwamba zao la korosho haliendi jinsi vile ambavyo inapaswa. Ninatoa rai kwa vyombo vya dola vyote, wale wote waliosababisha ubadhirifu huu katika zao hili la korosho wahakikishe vyombo vya dola kwamba wanawakamata, wanawapeleka mahakamni na hatua kali sana za kisheria zinachukuliwa na sisi kama Wizara kwa sababu huyu ni mtoto wetu tutafuatilia kwa karibu. Ahsante.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lulindi nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kuwa Kituo cha Afya cha Nagaga kilichopo katika Jimbo la Lulindi, Wilayani Masasi liliungua moto miaka mitano iliyopita. Je, Serikali haioni umuhimu sasa katika mgao huu wa magari yaliyopatikana kupeleka katika Kituo cha Afya cha Nagaga ili huduma za afya ziendelee kuboreka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli uko uhitaji mkubwa sana wa magari ya wagonjwa. Kama ambavyo Serikali ingependa yote tukaweza kuyatatua kwa mara moja, lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba bajeti hiyo kwa sasa haiwezekani kwa wakati mmoja tukatekeleza yote hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge ajue nia njema ya Serikali ndiyo maana katiak orodha ya Wilaya zile 27 ambazo zinaenda kujengewa Hospitali za Wilaya ni pamoja na Wilaya yake. Kwa hiyo, aelewe dhamira njema ya Serikali na kadri uwezo utakavyokuwa unajitokeza hakika hatutawasahau.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini pia niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali Walimu na kuhakikisha kwamba inalipa malimbikizo yao, lakini nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza sababu zilizotolewa na Serikali ya kukiondoa chuo hiki kuwa sekondari kwa sasa si sababu muhimu sana, kwa hiyo bado tunasisitiza Mheshimiwa Waziri kwamba. Je, hawaoni kwa kukiondoa Chuo kile cha Ualimu cha Ndwika kumefanya Kanda ya Kusini kuwa na vyuo vichache vya ualimu hivyo bado umuhimu wa chuo kile kurudi Serikali iutazame upya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, pamoja na kulipa malimbikizo ya Walimu lakini je, nini mikakati ya Serikali kuhakikisha sasa malimbikizo haya ya Walimu hayarudii kama ilivyokuwa mwanzo?
NAIBU WAZIRI ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukanda wa Kusini, au niseme mkoa anaotoka Mheshimiwa Mbunge tayari una vyuo vingine vitatu vya ualimu. Mkoa wa Mtwara una Chuo cha Ualimu cha Kitangali kilichopo Newala, lakini vile vile kuna Chuo cha Ualimu cha Mtwara Ufundi pamoja na Mtwara Kawaida. Hata hivyo, ifahamike kwamba vyuo hivi vyote ni vyuo vya kitaifa na udahili wake unawachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli huu kama Mheshimiwa Mbunge bado anafikiri kuna haja ya kurudisha shule hiyo ya sekondari kuwa chuo, nimshauri tu wajipange wakae katika halmashauri yao, walete mapendekezo wizarani na kwa vyovyote vile si msahafu, kama kuna haja za msingi bado Serikali inaweza kufikiria kurudi huko tulipotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, ni kweli kwamba kwa sasa Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba hakuna tena madeni ya Walimu ambayo yatajilimbikiza. Hatua mbalimbali tayari zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku sasa, kwa mfano kuhamisha Walimu kwa utaratibu wa kawaida bila kuwalipa stahiki zao. Vile vile kuhakikisha kwamba kila mwajiri anatenga fedha kwa ajili ya likizo za Walimu, lakini pia pale wanapostaafu kuhakikisha kwamba fedha za kusafiri zinakuwa zinatolewa. Kwa hiyo tunachofanya sasa ni kuhakikisha kwamba hakuna kulimbikiza tena madeni ya Walimu na inawezekana tu kufanya hivyo kama stahiki zao zote zitalipwa kwa wakati muafaka.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, tatizo lililoko Mikindani ni kubwa na halmashauri haina uwezo wa kumudu tatizo hilo. Wale waliotembelea Mikindani na wanaopita pale watakubaliana na mimi kabisa. Je, Serikali haioni sasa jukumu hili likabebwa na Serikali Kuu kuisaidia Halmashauri ya Mikindani kwa sababu matuta haya yalijengwa miaka 50 iliyopita na sasa ukarabati wake unahitaji fedha nyingi? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, tatizo lililopo Mikindani linafafana na tatizo lililopo Masasi. Mji wa Masasi umezungukwa na milima na hivyo kuleta athari kubwa sana ya maji kutoka milimani kuingia pale mji. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutembelea Masasi na Mikindani kwenda kujionea hali halisi ili Serikali iingilie kati? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, kwanza nitatembelea Mikindani na Masasi baada ya Bunge hili ili kwenda kujionea hali halisi ya anayozungumza Mheshimiwa Mbunge. Kabla sijatembelea, nitatuma wataalam wa Ofisi ya Makamu wa Rais waende Miji wa Mikindani mapema wakatazame haya aliyouliza Mheshimiwa Ghasia na aliyozungumza Mheshimiwa Bwanausi na baada ya hapo tutafanya tathmini tuone nini kinahitajika kufanyika. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kata ya Mchauru, Kata ya Sindano na maeneo ya Njawara na Ntona yako mpakani mwa Tanzania na Msumbiji na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulithibitisha kwamba pembezoni au kwenye mipaka ya nchi yetu watahakikisha minara inajengwa. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atahakikisha kwamba wananchi wale wanapatiwa mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bwanausi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Bwanausi kwamba kati ya Waheshimiwa Wabunge walioleta barua zao mwanzoni kabisa kuhusu masuala ya mawasiliano alikuwa ni yeye. Namshukuru Mungu vilevile kwamba tumeendelea kupokea barua kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wengine wanaoeleza changamoto ya mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Bwanausi na wananchi wa Jimbo lake kwamba tutafanya ziara pale, tutaainisha maeneo ambayo tunaweza tukaweka minara kwa sababu siyo lazima ukiomba minara mitano uwekewe mitano. Unaweza ukaomba minara mitano, ukawekewa miwili na ikaweza ku-cover eneo kubwa sana; lakini unaweza ukaomba minara mitatu ukawekewa hata mitano kutokana na jiografia. Ndiyo maana naeleza kwamba ni lazima twende tukajiridhishe tukiwa na timu ya wataalam kuhakikisha kwamba tunaweka mawasiliano ambayo yatahakikisha yanawafaidisha wananchi kwa ujumla wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya mipakani vilevile kuna programu maalum ambapo tunashirikiana Mfuko wa Mawasiliano na TCRA kuhakikisha mawasiliano yanayohusu Watanzania yanabaki kuwa ya Watanzania na yanayohusu nchi nyingine yanaendelea kuwahusu wao.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali. Kwa kuwa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi imeshaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa 50, je, ni lini wananchi wa maeneo ya Nagaga, Mbuyuni, Chiungutwa pamoja na Mpeta watalipwa fidia zao ili barabara hii iweze kuendelea kufanyiwa kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inafanya juhudi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba tunaboresha barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameizungumza. Sasa yupo mkandarasi anatengeneza barabara kutoka Mtwara kuja Mnivata, lakini tutatoka Mnivata – Tandahimba – Newala mpaka Masasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge anauliza, ni muhimu ili utaratibu wetu uweze kuendelea wa kutengeneza hii barabara kuiunganisha na Mtwara, tuhakikishe tunalipa fidia. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu suala hili la fidia tumelizungumza na nilimwambia kwamba muda sio mrefu nitampa majibu kwa sababu nilikuwa naweka msukumo ili wananchi waweze kulipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli fidia hii ikilipwa pia inatupa sasa fursa ya kuendelea kuboresha barabara hii ili tuweze kuiunganisha kutoka Mtwara kuja Masasi iweze kukamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bwanausi naomba avute subira na kweli najua kwamba kasi iko kubwa ya Serikali kulipa fidia na katika maeneo mbalimbali tunaendelea kulipa fidia lakini na wananchi wa eneo hili la kwako tutaweza kuwalipa mara moja. Ahsante. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mradi wa uzambazaji wa umeme REA III katika Jimbo la Lulindi ni wa kusuasua sana na mkandarasi hadi jana alikuwa hajafunguliwa LC. Je, Mheshimiwa Waziri anataka kuwaambia nini wananchi wa Jimbo la Lulindi ambao wanasubiri kwa hamu umeme huo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Bwanausi anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumeshafanya uzinduzi kwa Mheshimiwa Bwanausi na kijiji cha Kalipinde tayari kilishawashwa umeme na baada ya kutoka Kalipinde inakwenda kata inayofuata. Ni kweli kabisa mkandarasi hatua ya kwanza alianza kwa kusuasua kwa sababu kulikuwa na masuala ya kiutawala na kiusimamizi yaliyokuwa yanaendelea. Hivi sasa naipongeza Wizara ya Fedha imeshafungua LC, advance payments zimelipwa, ni matumaini yetu sasa mkandarasi atakwenda kwa speed. Nimhakikishie Mheshimiwa Bwanausi kwamba mara baada ya Bunge tutamfuatilia mkandarasi huyu ili awashe umeme vijiji vingi kwenye jimbo lako.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Suala la kupitika barabara ni suala muhimu sana kwa ajili ya uchumi na maendeleo ya wananchi; na kwa kuwa, Madaraja ya Mipande, Mtengula, Chawara hadi kule Buyuni, lakini pia Daraja la Mwitika Maparawe ni madaraja ambayo yamezolewa na mafuriko kutokana na mvua kubwa. Je, nini kauli ya Wizara ya TAMISEMI katika kuhakikisha madaraja haya yanarudishwa ili kuwe na mawasiliano ya usafiri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Bwanausi, kwanza kwa kufuatilia madaraja hayo, kwa sababu nikiri wazi kwamba alifika ofisini kwangu na nilimwelekeza aende akakutane na Mkurugenzi wetu wa Barabara Vijijini, Ndugu Digaga na amefanya hivyo. Ofisi yangu sasa hivi wanakwenda kufanya tathmini ya kina ya nini kifanyike kwa sababu wananchi wa eneo hilo wamekwama sana katika suala la usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama alivyofika kwangu na kama nilivyomwelekeza kufika TARURA, ofisi yetu italifanyia kazi kwa nguvu zote eno hilo.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa, bado wananchi wa jimbo langu hasa wanaoishi kandokando mwa Mto Ruvuma wameendelea kupoteza maisha na kupoteza viungo vyao kwa kasi kubwa sana. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari sasa kuendelea kutimiza makubaliano yetu ya kuchimba visima katika vijiji sita vilivyobaki ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata unafuu wa kuathirika na suala la mamba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba, lipo tatizo kubwa, lakini tatizo lililopo ni kwamba, wenzetu wa TAWIRI ambao wanatoa vibali vya kuvuna mamba wanatoa idadi ndogo sana ya vibali, kama alivyoeleza ni mamba tisa, lakini takwimu zinaonesha katika eneo hilo pekee lina mamba zaidi ya 300. Je, yupo tayari kutoa vibali zaidi ili wananchi hao waweze kuondokana na tatizo hili kwa kuvuna mamba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Bwanausi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nitumie nafasi hii kumpongeza kwa namna anavyofuatilia haki za wananchi wake walioshambuliwa na mamba. Kuhusu swali lake la kwanza amesema tatizo la wananchi kushambuliwa na mamba bado linaendelea na palikuwa na makubaliano na Wizara yangu kupitia TAWA ya kuchimba visima. Kama makubaliano hayo yalifanyika na Serikali haina kipingamizi, nitawaelekeza TAWA kuhakikisha kwamba, makubaliano hayo yanatimizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, ni kweli kwamba, kabla ya kuvuna mamba Shirika letu ya Utafiti la TAWIRI huwa linafanya utafiti kujiridhisha na idadi sahihi na kama idadi hiyo ni tishio katika eneo husika. Nitawaelekeza pia, TAWIRI wafanye upya utafiti na iwapo itathibitika kwamba, idadi ya mamba waliopo sasa ni tishio tutatoa tena kibali cha kuvuna mamba hao kupunguza athari kwa wananchi.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa asilimia ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Tunduru pamoja na vijiji vyake 92 ni wa chini sana; na kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha kidogo kidogo katika mradi mkubwa wa Tunduru:-

Je, Serikali haioni sababu sasa ya kutafuta fedha za kutosha ili mradi huu ukamilike kwa haraka na wananchi waweze kupata maji kwa urahisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, vijiji vya Lakalola, Nakachindu, Namwanga, Nangwale, Tupendane, vimekuwa vikikabiliwa na tatizo kubwa sana la maji katika Jimbo la Lulindi pamoja na kule Rivangu na Wakandarasi wako site; kuna OBD and Company na Sing Lyimo Enterprises, lakini tangu wapeleke certificate mwezi Novemba, 2018 hadi sasa Wakandarasi hao hawajapata fedha zao ili kuendelea na kazi:-

Je, nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Niwe mkweli, tuna changamoto kubwa sana Tunduru na hata Mkoa wa Ruvuma, tulifanya ziara tukaona changamoto hiyo. Kubwa tunaloliona, tuna ubabaishaji mkubwa sana wa Mhandisi wetu wa Maji wa Mkoa. Sisi kama Wizara tumeshamwondoa na tutaendelea kuwaondoa Wahandisi wote wababaishaji katika Wizara yetu ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa tunatambua kabisa utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha. Tulikuwa tuna madai zaidi ya shilingi bilioni 88 ya Wakandarasi. Tunashukuru sana Wizara ya Fedha imetupa shlingi bilioni 44, tumeshaanza kuwalipa Wakandarasi na mwezi huu wa Nne mwishoni watatupa shilingi bilioni 44 nyingine katika kuhakikisha tunawakamilishia Wakandarasi madai wanayotudai. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu na kuweza kuwahudumia wananchi. Ahsante sana.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lulindi. Swali langu la kwanza; Serikali iliahidi miaka miwili iliyopita kwamba itahakikisha inajenga minara katika mipaka yetu yote ya nchi, ikiwemo mpaka wa Tanzania na Msumbiji, lakini vijiji ambavyo viko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ujenzi wake umekuwa ukisuasua sana, hivyo kuwafanya wananchi wa Jimbo la Lulindi kutumia minara iliyoko Msumbiji.

Je, Mheshimiwa Waziri atawaambia ni lini maeneo ya Namtona na Chikolopola yatawekewa minara?

Swali la pili; vibali vya ujenzi kutoka NEMC kuchukua muda mrefu sana kuvipata: Je, Wizara inashirikiana vipi na Wizara inayohusika na NEMC ili kuhakikisha NEMC hawakamishi ujenzi wa minara hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba tuna changamoto kubwa sana kwenye mipaka ya nchi yetu kutokana na mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi za jirani. Hivi karibuni kilifanyika kikao kikubwa sana cha East African Communication (EACO) pale Arusha, ambako wataalam wa Mamlaka za Mawasiliano za nchi za Afrika Mashariki walijadili kwa kina namna ya kuondoa changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mbunge kwamba changamoto hizo zinakwenda kutatuliwa na mpaka sasa hivi baadhi ya Makampuni ya simu tumeshaanza kuyaelekeza yaende yakafanye tathmini ya kiufundi namna ya kuondoa mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi nyingine. Kwamba ni lini tutapeleka mawasiliano; wakati wowote. Kama nilivyojibu katika swali langu la msingi tayari mkandarasi yupo, ameshajulikana ni Tigo na atapeleka mawasiliano kabla ya mwezi Januari mwaka 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, ameuliza kwa nini vibali vya ujenzi kutoka NEMC vinachelewa? Ukweli ni kwamba katika taratibu za ujenzi wowote lazima taratibu zifuatwe. Moja kati ya taratibu ni kupata kibali kutoka NEMC. Wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ndugu zetu wa NEMC wa kuhakikisha kwamba minara inakopelekwa lazima kusiwe na madhara kwa binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kushirikiana nao katika hali ambayo tunaamini kuwa hakuna ucheleweshaji mkubwa sana. Panapokuwa na ucheleweshaji mkubwa, huwa tunawashauri Wakandarasi wale au watoa huduma watafute eneo lingine ambalo haliwezi kuwa na changamoto kwa wananchi.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi. Tatizo lililopo Kibiti pia lipo katika Jimbo la Lulindi na sisi hatujapitiwa na utaratibu huo wa kupewa umeme mbadala na kutumia gesi kwa ajili ya majumbani. Sasa nataka kumwomba Mheshimiwa Naibu Waziri atueleze maana sisi tunategemea umeme hali ya usambazaji umeme katika jimbo la Lulindi inasikitisha na iko katika kiwango cha chini sana. Je, nini kauli ya Serikali?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Bwanausi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika baadhi ya maeneo utekelezaji wa kandarasi umesuasua hasa mwanzoni lakini kwa upande wa Mheshimiwa Bwanausi yapo maeneo ambayo yalikuwa mbali sana na mtandao wa umeme, kwa hiyo, imechukua muda mrefu kwa wakandarasi kuyafikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Bwanausi kwa ushirikiano na Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara pamoja na mkandarasi, sasa hivi mkandarasi mkandarasi anakamilisha shughuli za kusimika nguzo katika maeneo 22 ya Mheshimiwa Bwanausi. Ni matarajio yetu katika Jimbo la Bwanausi, maeoneo ya vijiji 22 yatawashwa kabla ya mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya kila namna kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaongeza kasi. Tarehe 22, mimi mwenyewe nitakuwa Mtwara ili kuweka msukumo mkali kwa wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi hizo kwa wakati.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa wananchi wa Vijiji vya Myesi, Utimbe, Naliongolo na maeneo ya Mchoti wamekuwa wakipoteza maisha, pia kujeruhiwa kutokana na wingi wa mamba waliopo katika Mto Ruvuma. Serikali kupitia Bunge Tukufu ilishawagiza TAWA ili waende kuchimba visima kuwaokoa wananchi hawa kutokana na kutegemea Mto Ruvuma kwa matumizi ya maji yao. Je, Serikali inatoa tamko gani kuwaelekeza TAWA waende wachimbe visima hivyo haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI WA WALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanausi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri kwamba itakuwa swali la tatu la aina hiyo nalijibu lenye uhusiano na wingi wa mamba kwenye maeneo mbalimbali ya Mto Ruvuma. Ni kweli kwamba kuna ongezeko la wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo mamba na wamekuwa wakiathiri matumizi ya asili ya wananchi ya maji ya Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliekeleza hapa kwamba katika ushauri tuliopata kutoka kwa wanasayansi wa Wizara yetu ni kwamba maeneo ambayo wananchi wanatumia yanaweza kuwekewa kingo maalum ili kuzuia mamba kufika na ushauri wa pili ilikuwa ni kuchimba visima kandokando ya eneo hilo. Kwa kushirikiana na Wizara husika, Wizara yangu ilizungumza na watu wa Wizara ya Maji na waliahidi kupeleka visima maeneo hayo. Naomba nichukue ushauri wa Spika kuwaekeleza tena TAWA kufanya tathmini na kupitia na kuona kama TAWA tunaweza tukafanya kazi ingawa kazi ya msingi kabisa ya kupeleka maji maeneo hayo itafanywa na Wizara ya Maji.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini kwa kuwa wananchi hawa wa maeneo ya Mipande na Mtegula, lakini pamoja na Mwitika - Maparawe, wamekuwa wanapata adha kubwa sana kutokana na kukosekana kwa madaraja haya makubwa; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishahaidi kuyashughulikia madaraja haya, naomba Serikali itoe kauli ni lini madaraja haya ya Mtengula - Mipande na Mwitika - Maparawe yatajengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa madaraja haya ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi jumla ni manne na tayari daraja la Shaurimoyo na Nanjocha yalishajengwa kwa kutumia TANROADS. Je, Serikali haioni umuhimu TANROADS kumaliza madaraja haya mawili yaliyobaki? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli madaraja haya yamekuwa na kadhia kubwa sana na nikiri wazi Mheshimiwa Bwanaus alikuja pale mpaka nikamkabidhi kwa Mkurugenzi wetu wa TARURA Bwana Seif wakaweza kuongea vya kutosha na ndiyo imewezesha sasa hivi usanifu unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kutokana na shida iliyo pale na hili ni agizo la Mheshimiwa Rais na Serikali imeshakamilisha kile kipande kingine cha madaraja, jukumu kubwa sasa ni kwamba usanifu huu utakapokamilika tutaangalia ni wapi fedha zitapatikana. Mimi na kaka yangu Kamwelwe tunashirikiana kwa karibu zaidi na baada ya usanifu tutashirikiana kuona jinsi gani tutafanya ikiwezekana wenzetu wa TANROADS waweze kusaidia katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Lulindi kwamba kama Mheshimiwa Rais alivyoelekeza madaraja haya yatajengwa ili wananchi hawa wanaopata shida kwa kipindi kirefu waweze kuondokana na adha hii inayowakabili.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri.

Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Mapili na Namyomyo, Chikolopola, Lupaso pamoja na maeneo ya Lipumburu wamekuwa wakipata shida ya mawasiliano kwa muda mrefu sana. Ahadi ya Serikali ni kwamba kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha minara inajengwa hasa maeneo ya kandokando mwa vijiji vilivyomo mipakani mwa nchi yetu na nchi jirani. Kwa kuwa kuna tatizo kubwa sana la ucheleweshaji wa kupatikana vibali vya ujenzi iliyopelekea hata kwenye jibu la msingi, kwamba mradi mmoja unasainiwa mwezi Desemba, 2018 lakini unakuja kumalizika kutekelezwa Desemba, 2019.

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha inaondoa tatizo la urasimu wa upatikanaji wa vibali ili minara ijengwe kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuahidi kwamba katika Bunge lililopita kwamba atatembelea vijiji hivi vilivyopo mpakani mwa Tanzania, Msumbiji ili kuzungumza na wananchi. Je, yupo tayari sasa baada ya Bunge hili kutembelea vijiji hivyo pamoja na Kijiji cha Lupaso ambacho Kiongozi Mkuu wa nchi mstaafu ndiyo nyumbani kwake? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukuru Bunge lako tukufu ambalo lilitunga Sheria ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Mfuko huu utahakikisha kwamba sasa nchi nzima inakuwa na mawasiliano. Ijumaa nilikuwa na mkutano na watoa huduma wote wa mawasiliano tukizungumzia miradi ya kata 521. Tumekubaliana baada ya wiki mbili tunakutana, kwa hiyo, hayo majibu ya msingi yaliyotolewa Mheshimiwa Bwanausi, vijiji vyote hivyo vyote vitapata mawasiliano na hiyo ndiyo ahadi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili la vibali, suala la vibali sasa hivi halina mgogoro tena, NEMC wamejiandaa vizuri tukiomba vibali tunavipata haraka. Ufumbuzi wa kutoka vibali haraka ulitokana na mradi wa makaa ya mawe pale Mtwara, Mheshimiwa Rais alielekeza kwamba sasa vibali vinatakiwa vitoke haraka na sasa vibali vinatoka haraka hakuna kikwazo tena cha kutoka vibali. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuuliza swali.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaelekea kwenye msimu ujao wa zao letu la korosho na nilitaka nipate maelezo kutoka Serikalini, mpaka hivi sasa wakulima hawajapata taarifa zozote juu ya uwepo na lini na bei elekezi ya pembejeo. Kwa hiyo, ningeomba Serikali itoe maelezo ili kuhakikisha wakulima wanapata ufahamu juu ya uwepo wa pembejeo lakini bei elekezi itatolewa lini, lakini pia ni lini itasambazwa?(Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli sasa hivi ni msimu wa kilimo cha zao la korosho hasa katika kupulizia madawa ikiwemo sulfur na maeneo mengine. Sasa hivi Serikali tumejipanga tumehakikisha kwamba sulfur ipo ya kutosha katika maeneo yote tumeshapaleka na bado tunajaribu kufanya tathmini kuangalia kama kuna sehemu tuna upungufu ili tuhakikishe kwamba hayo madawa yanakuwepo. Sambamba na hilo tumeanza kujiandaa kabisa katika msimu unaokuja ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Bodi ya Korosho ambayo tayari tumeshaiteua kwa ajili ya kuanza kazi na kuweza kupanga mikakati mbalimbali ya kuendeleza hili zao la korosho.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute tu muda ni kwamba kila tumejipanga na kitakwenda vizuri na nina uhakika wakulima wa korosho watafurahi sana, ahsante.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na ninatambua kazi nzuri inayofanywa na Waziri na Naibu Waziri katika Wizara hii. Ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Swali langu la kwanza, je, kwa kuwa vijiji vya Nairombo, Nanjota, Msanga ni vijiji ambavyo vinapitiwa karibu na bomba kuu la Mradi wa Chiwambo pamoja na Mradi wa Shaurimoyo ikiwa ni pamoja na Kijiji cha Nakachindu. Je, Serikali ipo tayari sasa wananchi hawa ambao wako karibu na bomba kuu waweze kupatiwa maji?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ni kwamba tunao mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma ambao unakaribia kukamilika wenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 na mradi huu wakati ukiandaliwa kijiji cha Chipingu ambacho kipo karibu na mradi kilikuwa hakina umeme wa REA na sasa pale pana umeme wa REA.

Je, Wizara ipo tayari sasa kupeleka umeme kwenye mradi huu ambao ni kilometa mbili ili wananchi waweze kupata maji kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo lake lakini kwa kuwa mfatiliaji wa mara kwa mara Wizarani katika kuhakikisha suala la maji linatatuka katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo hususan kwa vijiji ambavyo vipo karibu na bomba kuu kupatiwa maji na tumefanya mageuzi makubwa sana katika Wizara yetu ya Maji. Moja ya mageuzi hayo ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote ambavyo vinapitiwa na bomba kuu kilometa 12 katika upande wote wa bomba kuu vinapatiwa maji.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama viongozi wa Wizara hatutokuwa kikwazo katika kuhakikisha vijiji vile ambavyo vipo karibu na bomba kuu vipatiwe maji. Lakini kuhusu suala zima la mradi ule wa maji kupatiwa umeme wa REA nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutafanya mawasiliano na Mhandisi wa Maji atuletee document na sisi kama viongozi wa Wizara ili tuweze kuwezesha mradi ule uweze kutekelezeka wa REA, ahsante sana.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya kutoka Masasi hadi Newala Serikali imekwishadhamiria kuijenga kwa kiwango cha lami na kwamba inatarajia kutangazwa zabuni mwezi wa saba.

Je, wananchi wa Kijiji cha Mpeta, Chiungutwa, Nagaga, Mkangaula pamoja na Msanga ambao walipaswa kulipwa fidia ni lini Serikali itawalipa fidia ili kupisha ujnzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu wa Serikali kulipa fidia kabla ya kuanza ujenzi na kwa kuwa utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu, barabara ya uchumi hii kutoka Mtwara – Masasi – Newala utaanza hivi karibuni, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi hawa wa maeneo ya Mpeta, Chiungutwa, Kangaula na Lulindi kwa ujumla kwamba watalipwa fedha zao mapema, ili kupisha ujenzi kuanza kwa maana hiyo kwa sababu, tutaanza hivi karibuni ina maana kwamba ni hivi karibuni watalipwa kabla ujenzi haujaanza.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.

Kwa kuwa barabara ya kutoka Mwitika kwenda Maparawe na kutoka Chiungutwa - Mipande hadi Mtengula haipitiki kutokana na madaraja hayo kung’olewa na mafuriko miaka mitano iliyopita na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba madaraja hayo yatajengwa.

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli zipo ahadi za Mheshimiwa Rais zipo ahadi nyingi na niseme tu kwamba ni ukweli baadhi ya ahadi zimetekelezwa 100%. Zipo baadhi ya maeneo ambazo tumetekeleza kwa kiasi fulani na tunaendelea kutekeleza na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge ahadi zote za Mheshimwa Rais na viongozi wakuu tunaendelea kuzitekeleza.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Bwanausi umezungumza juu ya haya madaraja na utakuwa shaidi kati haya madaraja ambao yalikuwa ni sehemu ya ahadi madaraja manne kama zikosei matatu tayari yamekwisha tekelezwa, tumebakiza lile daraja moja naomba uvute subira kwa sababu tunawenda hatua kwa hatua kwa dhamira ile ile kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho makubwa katika kutekeleza ahadi ya kiongozi wetu mkuu Mheshimiwa Rais wetu, ahsante sana.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uwepo wa mamba pia ni sehemu ya kivutio kwa watalii lakini kutokana na ongezeko kubwa sana mazalio ya mamba katika Mto Ruvuma na kuleta athari kubwa sana kwa wananchi.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuja kwenye Jimbo langu kuona athari kubwa zinazojitokeza na kutafuta changamoto za kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba limekuwepo ongezeko kubwa sana la mamba katika maeneo yetu mengi mamba, boko na wanyama wengine ambao hawatumiki moja kwa moja sana na kuhamasisha utalii na katika eneo hili la Mto Ruvuma ambalo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akisema wamesababisha shughuli za uvuvi na shughuli za matumizi ya maji ya kawaida ya Mto Ruvuma kushindikana.

Mheshimiwa Spika, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyomjibu hivi karibuni kwenye swali lake la msingi kwanza tulielekezwa watu wetu wa TAWA kuhakikisha kwamba wanapeleka visima vya maji karibu katika vijiji ambavyo viko karibu na maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, pili, tuliwaagiza watu wetu wa TAWIRI kufanya utafiti na kutueleza mamba waliopo wamezidi kwa kiasi gani ili tuweze kuweka mkakati wa kuwavuna, lakini nimhakikishie pia Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kwenda katika eneo hilo kwenda kuangalia hali halisi na kuzungumza na wananchi.