Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rashid Mohamed Chuachua (16 total)

MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali yafuatayo ya nyongeza:-
Swali la kwanza, je, Serikali sasa haioni haja ya kuingilia kati na kutoa mwongozo kwa makampuni haya ambayo ni wawekezaji ili waweze kuwalipa wananchi hawa wanaotoa maeneo yao kwa kiwango kinachostahili, kwa sababu wengi wao hawajui thamani ya uwekezaji huo?
Swali la pili, katika eneo la Mji wa Masasi au Jimbo la Masasi, maeneo ya pembezoni karibu yote hayana mawasiliano, je, ni lini Serikali itajenga minara katika Kata za Marika, Mombaka, Temeke, Matawale, Surulu, Mwenge Mtapika pamoja na Chanika Nguo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote wanapofanya mikataba na wawekezaji mbalimbali wapate huduma ya ushauri kutoka kwa Wanasheria pamoja na wataalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mkataba umesainiwa kati ya kijiji na wananchi hata kama haukufata ushauri na pengine siyo mzuri kwa wale wanakijiji, ni ngumu kuwalazimisha upande mmoja katika mkataba kurekebisha, kwa sababu ni kinyume cha misingi ya mkataba.
Kwa hiyo, tutachunguza mkataba uliopo wa kijiji hiki kuona kama tunaweza wao wawili waliokubaliana wanaweza kukubali wakarekebisha ili waboreshe kile ambacho wananchi watakipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, amenipa orodha ndefu. Kama Serikali naomba tupewe nafasi, hiyo orodha tuiwasilishe kwenye makampuni mbalimbali ambayo yanatoa hiyo huduma tuone kampuni ipi itakuwa tayari kujenga minara katika maeneo hayo au kupitia mfuko wetu wa Mawasiliano kwa Wote halafu tutamjulisha kwa maandishi.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Swali la kwanza, namuomba Mheshimiwa Waziri anipe specific time, kwa sababu wanafunzi hawa hawafundishwi masomo ya sayansi, ni lini mpango wa Serikali wa kuwaajiri walimu hawa utatimizwa?
Swali la pili; naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anieleze ni lini Serikali itatenga pesa kwa ajili ya kukamilisha maabara kumi ambazo zipo katika mchakato wa kujengwa na vifaa katika maabara 14 za shule za sekondari? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri miongoni mwa matatizo makubwa sana tunayokabiliana nayo ni ukosefu wa walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari. Katika hili, ndiyo maana Serikali tumesema pale wazi kwamba tunachokifanya ni nini, tunajipanga kwa kadri iwezekanavyo, walimu wanavyopatikana baada ya udahili ule, watoto wanapohitimu masomo yao tunawaelekeza katika shule zile za sekondari. Inawezekana mwaka huu tukaja na approach nyingine tofauti, kwa sababu imeonekana maeneo mengine walimu wakipelekwa katika Halmashauri husika, walimu wale wengi wanaishia maeneo ya mijini. Sasa mwaka huu inawezekana tukawapeleka walimu moja kwa moja katika shule husika ili kuondoa tatizo la walimu katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, time frame, tulisema hapa kwamba katika michakato yetu ya ajira hapo itakapokamilika, ni kwamba walimu tunatarajia kuwaajiri ambao lengo ni kuweza kuwapeleka, kwa hiyo ni suala zima la utaratibu ambao unaendelea hivi sasa. Ndiyo maana mwaka huu tumejielekeza kwamba ikiwezekana kuna walimu wengine takribani 2,000 ambao tunaona kwamba walikuwa wana uwezo wa kufundisha sayansi, Serikali inaona kwamba itaweza kuwachukua walimu wale kwa mkataba maalum, ili kuwaingiza katika suala zima la ajira kupunguza tatizo kubwa la walimu wetu hawa ambao imekuwa kero sana kwa walimu wa sayansi. Sambamba na hiyo, tunafanya harakati nyingi sana, lengo letu ni kuboresha vijana wetu ili tupate walimu wengi wa sayansi katika maeneo yetu ili watoto waweze kufuzu masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ujenzi wa maabara kukamilika, ndugu zangu nimesema haya juzi tu, tena tumetoka katika mchakato wa bajeti. Nimesema haya mambo kila Halmashauri ina vipaumbele vyake na kila Halmashauri itenge vipaumbele kama tumejenga maabara kuna upungufu wa vifaa, lengo letu iwe ni kutenga vifaa. Naomba niwapongeze kwanza Wabunge wote na viongozi wote, tumesimamia vya kutosha katika ujenzi wa maabara katika Halmashauri zetu. Kwa mara ya kwanza tumefanya mapinduzi makubwa kama nchi ya Tanzania kuhakikisha tumejenga maabara katika kila shule ya Kata, hili ni jambo kubwa tena ni jambo la kujipongeza. Ujenzi huu ni lazima utakumbana na changamoto mbalimbali kama suala la upungufu wa vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuelekeze Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu najua uko makini na asubuhi tulikuwa tunaongea hapa katika suala la Halmashauri yako, kuhakikisha kwamba katika own source inayowezekana hivi sasa, kama kuna baadhi ya vifaa vinavyohitajika ili maabara zile ziweze kufanya kazi, muweze kuzitenga kusaida vijana wetu. Serikali pia vilevile tuko mbioni kuhakikisha kwamba tunaboresha shule zote ziweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi wetu hasa elimu ya sayansi.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo. Swali la kwanza, mwaka 2014 baadhi ya watumishi wa hospitali ya Mkomaindo walifanya ubadhirifu wa shilingi milioni 29 za dawa. Je, Serikali imechukua hatua gani mpaka sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Masasi linakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa watumishi wa huduma ya afya takribani watumishi 400. Je, Serikali haioni kwamba suala hili linapaswa kuchukuliwa kuwa ni la dharura ili watumishi hawa wapelekwe haraka iwezekanavyo katika Jimbo la Masasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi miongoni mwa maeneo ambayo nilitembelea ilikuwa ni Masasi nikiwa na Mbunge huyu na pale nilibaini changamoto kubwa na nilitoa maagizo mbalimbali. Hata hivyo, hivi sasa Ofisi yetu ya Rais, TAMISEMI, inafanya mchakato mpana siyo kuhusu suala la madaktari peke yake au idara ya afya peke yake kwa sababu kuna tatizo kubwa katika maeneo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeunda timu hapa si muda mrefu itakuwa kule site vizuri ili kubaini upungufu wote siyo Masasi Mjini hali kadhalika na Masasi Vijijji. Tuna ripoti inayoonesha kwamba hali ya afya ya pale siyo sawasawa hasa kutokana na baadhi ya Wakuu wa Idara kushindwa kutimiza wajibu wao. Kwa hiyo, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tumekuwa serious nalo na tunaenda kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siku tutakayokuja kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wazembe, tunaomba sana Waheshimiwa Wabunge waache kuleta vi-memo kwamba yule ni ndugu yangu, tutakwenda kuwashughulikia wale wanaoharibu fedha za Serikali na kwa hili tuko serious sana na wala hatuna masihara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la watumishi, Waziri wa Afya alishasema hapa mchakato unaendelea. Nimelisema jibu hili mara kadhaa, eneo hili la Masasi nimefika na nimeona mwenyewe Hospitali yetu ya Mkomaindo pale changamoto ni kubwa ikiwa ni pamoja na zahanati zetu, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo katika watu ambao wanaajiriwa hivi sasa, Masasi itapewa kipaumbele kupunguza tatizo hili kubwa la watumishi katika eneo hilo.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuwahudumia mahabusu na kwa kuwa fedha hizo huwa hazitoshi kuwahudumia mahabusu wao. Je, Serikali ina mpango gani kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuhakikisha kwamba Askari Polisi hawatoi tena fedha mifukoni kuwahudumia mahabusu wanaowekwa ndani kenye vituo vyao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali imesema ina mpango wa kujenga nyumba 4,136 kwa awamu. Je, kati ya nyumba hizo ni nyumba ngapi zitajengwa katika Wilaya ya Masasi?
swali la msingi nilionesha takwimu ambazo zinaonesha kuongezeka kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mahabusu ambapo nilisema kwamba mwaka 2015/2016 tulitenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 na mwaka unaofuata kwa maana ya mwaka huu tulionao tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.7. Hii inaonesha kwamba kadri tunavyokwenda mbele bajeti kwa ajili ya kuhudumia mahabusu inaongezeka. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaongeza bajeti kila mwaka ili kuweza kutoa huduma za mahabusu vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na nyumba ngapi zitajengwa Masasi, migao katika ngazi ya Wilaya bado haijafanyika, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapofanya mgao kwa ajili ya Mkoa wa Mtwara vilevile tutazingatia na Jimbo au Wilaya yake ya Masasi.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Niongezee tu sehemu ndogo ile ya upande wa vyakula kwa mahabusu na niunganishe pamoja na wafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na tatizo la kibajeti lakini pamoja na tatizo hilo pia kuna tatizo la matumizi ya fursa tulizonazo za uzalishaji katika taasisi zetu za Wizara ya Mambo ya Ndani. Mpango wa muda mrefu tunaopanga ikiwa ni ziada ya majibu aliyoyatoa ya kibajeti ni namna ya kutumia fursa tulizonazo hasa hasa katika magereza yetu. Magereza yetu yana mashamba makubwa, juzi nilienda Kigoma, mkoa ambao mazao yanakubali kuliko mikoa yote kwa msimu kama huu ambao una ukame lakini kwenye shamba lile lenye ekari karibuni 10,000 walilima kama ekari 50 hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika magereza yote tukilima vizuri, tutalisha magereza, tutalisha mahabusu na tunaweza tukalisha mpaka na shule za sekondari. Kwa hiyo, mpango tulionao ni kwenda kujitegemea katika uzalishaji ili tuweze kulisha wafungwa na mahabusu. Tunamwomba ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Tizeba na Mheshimiwa Mwijage watusaidie tu matrekta ili tuweze kwenda kulima kisasa hata NFRA tutawauzia mazao kwa ajili ya kuisaidia Serikali.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Ni kweli kuwa si kila msamaha wa kodi una madhara katika jamii na uchumi, hata hivyo ipo misamaha ya kodi isiyo na tija. Kwa kuwa hadi kufikia mwaka 2015/2016 misamaha ya kodi ilifikia asilimia 8.6 ya mapato yote ya kodi. Mpango wa Serikali ni upi kuhusu misamaha ya kodi kwa mwaka wa fedha 2017/2018? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ameuliza mpango wa Serikali kwa mwaka huu. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali sasa hivi iko katika mchakato wa kuangalia tax measures itakayohusishwa na misamaha ya kodi kwa mwaka huu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira, tarehe nane ni keshokutwa, Serikali yetu italeta mapendekezo yote na Bunge lako Tukufu litapitisha hayo mapendekezo ya Serikali. (Makofi)
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na swali langu. Lakini ukweli kwamba kuna shida ya kupatikana kwa malighafi ya korosho kwa viwanda vyetu vidogo vidogo vya ndani uko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ili kuweza kuingia kwenye mnada wa korosho unahitaji kuweka bond ya zaidi ya shilingi milioni 100 ili kuweza kupata kupata korosho, jambo ambalo wajasiriamali wetu wadogo wadogo ambao wana viwanda vidogo vidogo wanashindwa kulimudu.
Sasa ni lini Serikali itaona haja ya kuhakikisha kwamba utaratibu mzuri tulionao unaendelea, lakini pia inatangeneza utaratibu wa kuhakikisha kwamba wajasiriamali wenye viwanda vidogo vidogo nao wanapata fursa ya kununua korosho kwa ajili ya kuzichakata? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kuona kwamba na yeye anaunga mkono mfumo unaoendelea sasa, ni lengo la Serikali kuona kwamba wadau wote ambao wanashiriki katika mnyororo mzima wa thamani ya korosho wananufaika. Na kwa hali hiyo basi, niseme tu kwamba baada ya kuona manufaa makubwa ya mfumo huu, lakini pia baada ya kupata changamoto kwa wadau wengine kama ambavyo unavyoeleza. Serikali itakaa pamoja na wadau kuangalia namna bora zaidi ya kuhakikisha kwamba hivi viwanda vidogo navyo vinafanya shughuli zake bila kuathirika. (Makofi)
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali ya nyongeza mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Serikali ilitenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuwawezesha Mamlaka ya Usambazaji wa Maji (MANAWASA) waweze kusambaza maji ya kutosha katika Vijiji vya Jimbo la Masasi. Pia bajeti hiyo hiyo na kiwango hicho hicho cha fedha kilitengwa 2015/2016 na fedha hizo mpaka sasa hazijatoka. Ni lini Serikali sasa itapeleka fedha hizi ili kusudi wananchi waweze kupata huduma hii ya msingi na ni ya lazima?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba kufahamu, ni lini Serikali itapunguza gharama kubwa za maunganisho ya maji kwa wananchi ambao kimsingi hawamudu gharama hizo na tayari Naibu Waziri alipotembelea Jimbo la Masasi tulimdokeza? Asante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza amesema Serikali ilitenga shilingi bilioni moja mwaka wa fedha uliopita na mwaka wa fedha tulionao, ni kweli, fedha hii ilitengwa lakini kutokana na makusanyo ya Serikali kutokuwa mazuri, basi fedha hii haikupelekwa kwenye mradi. Hata hivyo, kwa sasa Serikali imeanza kukusanya mapato vizuri na ninyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, kwa hiyo, sasa tutaanza kupeleka fedha ili shughuli iliyotarajiwa kufanyika kutokana na hii fedha iweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, gharama za maunganisho, ni kweli nilipokwenda kule nilikuta kuna malalamiko ya gharama za maunganisho. Nilielekeza mamlaka ya MANAWASA waweze kupitia gharama hiyo pamoja Bodi na waweze kuja na gharama ambayo itakuwa ni rafiki kwa watumiaji wa maji. Nashukuru wameniletea taarifa kwamba maelekezo yote niliyowapa wameanza kuyafanyia kazi.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Kata nyingi katika Kata alizozitaja hakuna hata kijiji kimoja chenye maji ya bomba, na kwa sababu Serikali imetenga fedha katika mwaka uliopita wa bajeti, shilingi milioni 599 na fedha hizi bado hazijakwenda katika Halmashauri yangu wakati wananchi wameshachimba mifereji kwa ajili ya maandalizi.
Je, Serikali itapeleka lini fedha hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri yangu imeandika barua ya kuomba uchimbaji wa visima katika vijiji kumi vya Halmashauri yangu vilivyopo pembezoni, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima hivi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Chuachua kwa namna alivyoweza kuwahamasisha wananchi wa Masasi kujitolea kuchimba mitaro ili ile Mamlaka ya MWANAWASA iweze kuunganisha. Nilifika pale na nikaona hiyo kazi, tukacheza na ngoma. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Chuachua na nataka huu mfano uigwe na Waheshimiwa Wabunge wengine, kwamba ni vizuri tukahamasisha wananchi pale inapowezekana, kujitolea kuchimba mitaro ili kazi iweze kwenda haraka na wananchi waweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake kwamba ni lini fedha zitapelekwa? Tayari nimeshaidhinisha kupelekwa fedha, hasa kuanzia Masasi Mjini kwa ile kazi ambayo niliona inaendelea. Kwa hiyo, nimeshaidhinisha fedha, kwa hiyo, sasa hivi ziko njiani, muda siyo mrefu watazipata ili waweze kuunganisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili kuhusu ombi la visima, hili naomba nilipokee kwa sababu ameliuliza kama swali la nyongeza, nilipokee, nitakwenda kuangalia tuone namna gani tutasaidia kuweza kuchimba visima hivyo.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa hali iliyoelezwa Tunduma inafanana sana na hali iliyopo katika Wilaya ya Masasi. Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba kutakuwa na Chuo cha VETA ambacho kitahudumia karibu asilimia 54 ya watu wa Mkoa wa Mtwara pamoja na wale wanaotokea katika Wilaya ya Nanyumbu? Majibu ya Naibu Waziri hayaoneshi ni lini sasa mpango huo utaanza. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachohitajika ni wananchi kupata mafunzo na mafunzo sio majengo peke yake. Kwa hiyo, kwa upande wa Masasi au Nanyumbu tunacho Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi ambacho tayari kimo katika mpango wa kukiboresha kwa kukifanyia ukarabati wa zaidi na kukiongezea uwezo ili kiweze kutoa mafunzo ambayo yanafanana pia na yale yanayotolewa VETA. Vilevile kuna Chuo cha Ndanda, naomba pia wananchi waweze kutumia chuo hicho ili kuweza kupata mafunzo yanayostahili.
MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matibabu ya wazee yamekuwa siyo ya uhakika sana katika Zahanati zetu, katika Vituo vya Afya na Hospitali za Serikali.
Je, Serikali haioni sasa uwe wakati muafaka wa kufanya sensa na kuwapa Bima za Afya hawa wazee ili waweze kupata matibabu haya bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilishaliona hilo siku nyingi na jana nilipokuwa najibu maswali mengine nilieleza suala hili kwa mapana sana. Kwa sasa sera tu imetamka kwamba wazee wasiojiweza, maana yake siyo tu wazee wote, wazee wasiojiweza ndiyo wanaopaswa kupewa msamaha kwa mujibu wa Sera ya Afya ya 2007.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tamko la sera lipo, utekelezaji wake unahitaji sheria za ku-enforce lakini pia taratibu za namna ya kulitekeleza. Zamani huo utaratibu nilioueleza awali ndiyo ulikuwepo kwamba Maafisa wa Ustawi wa Jamii kwenye vituo wakishathibitisha kwamba mtu ni mzee, wanampa msamaha, wanagonga mhuri anapata huduma zote bure na katika hospitali zote hapa nchini. Mwezi Desemba mwaka jana Waziri wa Afya akatoa hilo agizo analolizungumzia hapa kwamba sasa wazee wapewe vitambulisho na Halmashauri zote. Baadaye tumeliboresha hilo agizo kwamba sasa kila mzee kwenye kila Halmashauri ambaye ana-qualify kupata msamaha alipiwe kadi ya CHF na Halmashauri yake ili anapoenda kutafuta huduma za afya azipate kiurahisi bila unyanyapaa wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, kwa hivyo, tunakoelekea ndiyo huko anakozungumzia Mheshimiwa Dkt. Rashid Chuachua kwamba tutakapotunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo ni ya lazima yaani Comprehensive Single National Health Insurance which is compulsory for every one ndipo sasa tutatengeneza utaratibu ndani ya sheria hiyo hapa Bungeni kwa mapendekezo yetu sisi ambapo wazee na makundi yote yanayopewa msamaha wa kupata huduma za afya basi wakatiwe kadi za Bima ya Afya na Serikali. Utaratibu wa kupata pesa kwa ajili ya kuwakatia hizo kadi za Bima ya Afya utatengenezwa kwenye sheria hiyo. Nadhani nimelijibu comprehensive. (Makofi)
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nikupongeze kwa sababu ulipopata tu Unaibu Waziri ulikuja Masasi na ukatembelea wakulima wa korosho. Kwa hiyo, changamoto za wakulima wa korosho unazifahamu. Nina maswali mawili yanyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa hadi sasa wakulima wa korosho waliouza korosho zao katika msimu uliopita wanadai fedha zao takribani zaidi ya shilingi milioni 90 katika Jimbo langu tu la Masasi kwa hiyo fedha hizo ni zaidi ya shilingi milioni 90. Je, ni lini Serikali itahakikisha wakulima hawa wamelipwa fedha zao?
Swali la pili, lini Serikali sasa itaingiza sulphur ambayo itauzwa kwa wakulima kwa sababu tunafahamu wakulima wananunua sulphur kwa mwaka huu. Sasa lini Serikali itaingiza sulphur hiyo na kuisambaza kwa bei nafuu kwa wakulima wetu, kwa sababu kwa sasa begi moja ya sulphur imefika shilingi 70,000 mpaka shilingi 80,000? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa umahiri wake wa jinsi anavyofuatilia wakulima wa zao la korosho katika Mkoa wa Lindi na Mtwara hususan katika Jimbo lake la Masasi na ninaomba kwa maana hiyo nijibu maswali yake yenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nikianza na lile la (a) ni kweli wakulima wa zao la korosho wanadai Serikali na naomba niseme tu kwamba Mkoa mzima wa Lindi na Mtwara ikiwemo Masasi wakulima wanadai zaidi ya shilingi bilioni 5.770 Serikali naomba niseme tu kwamba katika Mkoa wa Lindi wataanza kulipwa mwezi huu mwishoni na vilevile katika Mkoa wa Mtwara watalipwa mwezi ujao mwishoni.
Mheshimiwa Spika, nikija katika swali lake la (b) kuhusu suala zima la pembejeo, ni kweli kabisa tunaelewa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana ya pembejeo katika zao zima la korosho na ninaomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba kwa upande wa sulphur habari njema ni kwamba Serikali tumeagiza tani 35,000 na lita 520 za viwatilifu na tunategemea mwezi huu Aprili awamu ya kwanza itafika na awamu ya pili itafika mwezi ujao mwishoni.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba pembejeo hizi kuanzia sasa zitanunuliwa kwa bei ambayo kwa upande wa sulphur haijazidi shilingi 40,000; vilevile kwa upande wa vile viwatilifu haitazidi shilingi 30,000; kwa maana hiyo ni habari njema haitakuwa shilingi 70,000 au 80,000 kama Mheshimia Dkt. Chuachua alivyosema bali itakuwa shilingi 40,000. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Masasi imeandika andiko hilo TEA katika kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita na mpaka sasa hakuna majibu yoyote au matumaini yoyote ya kupatikana kwa fedha, je, ni lini sasa Serikali kupitaia TEA itatoa fedha hizo ili kuboresha miundombinu ya shule hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tangu tulipoambiwa Serikali ina mpango wa kuajiri Walimu 5,000 ni muda sasa umepita, lini sasa Serikali itatoa kauli ya kuajiri Walimu hao rasmi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anauliza juu ya Halmashauri kupeleka maombi TEA na kwamba mpaka sasa hivi bado majibu hayajaja kwa ajili ya upatikanaji wa fedha na miundombinu iweze kuboreshwa ili Form Five na Six zianze kufanya kazi katika Halmashauri ya Masasi. Ni ukweli usiopingika kwamba ili tuweze kuchukua vijana wa Form Five na Form Six ni lazima miundombinu ambayo inatakiwa iwe imakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri yake, hivi karibuni Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliwaita Wakurugenzi wote pamoja na Wenyeviti ili waweze kuweka vipaumbele katika maeneo ambayo wanaenda kuboresha katika suala zima la elimu na afya. Ni matumaini yangu makubwa kwamba pamoja na ombi ambalo limepelekwa TEA kwa vile priority yao ni suala la elimu watakuwa wameweka kama kipaumbele ili tuweze kukamilisha miundombinu ya shule hizo mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la kuajiri Walimu, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana wakati anahitimisha bajeti yake alisema hapa nasi sote tukiwa mashuhuda. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na imani kama ambavyo tulisema kwamba vibali vitapatikana kwa ajili ya watumishi wa afya na tayari kazi zilishatangazwa, hatua itakayofuata ni hao Walimu ambao Serikali imeahidi kuajiri.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa gari alizozitaja Toyota Land Cruiser na Grand Tiger ni gari mbovu sana ambazo hazifai kufanya kazi katika kipindi hiki ambacho Polisi wana majukumu makubwa. Pia gari la Leyland ambalo amelitaja siyo la kazi ngumu kwa sababu kwanza halina hata four-wheel drive. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kufanya jambo hili ni la dharura kwa askari wetu wa Jeshi la Polisi waishio Masasi ili waweze kupata gari haraka iwekekanavyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hali ya nyumba za Askari Polisi waishio Masasi ni mbaya sana maana zimejengwa tangu enzi ya mkoloni. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami hadi Masasi baada ya Bunge hili ili akashuhudie hizo anazoziita nyumba 15 zilizopo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya umuhimu wa kupeleka magari mengine katika Jimbo la Masasi ni muhimu na nilieleza hivyo kwenye jibu langu la msingi tunaamini kwamba kuna haja ya kupeleka magari Masasi. Kwa hiyo, tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba magari yaliyopo hayatoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli magari yale mawili ni ya zamani ingawa yakitengenezwa yatasaidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa tunatambua umuhimu wa Wilaya ya Masasi kuwa na magari ya ziada, kwa sasa hivi hatuna magari mapya lakini pale ambapo yatapatikana katika maeneo ambayo tutayaangalia kwa jicho la karibu moja ni Wilaya ya Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili nimthibitishie kwamba niko tayari kwenda pamoja naye katika Jimbo la Masasi kwa mara nyingine tena. Niliwahi kufika Masasi na nayafahamu mazingira ya Masasi lakini kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge anahisi kuna haja ya kuambatana naye kwa mara nyingine tena basi tutafanya hivyo ili kwa pamoja mimi na yeye tuweze kuona jinsi gani tunaweza tukakabiliana na changamoto mbalimbali zinazohusu vyombo vyetu vya usalama vilivyopo pale hususan Jeshi la Polisi.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa kuwa mpango ulikuwa ni kupeleka umeme katika vijiji saba na mkandarasi kwa sasa hayuko site isipokuwa kwenye kijiji kimoja ambacho amepeleka umeme kwenye kaya saba peke yake.

Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali haioni haja ya kumfukuza mkandarasi huyu ambaye hafanyi kazi kwa kasi inayohitajika kwa kuwa site hayupo na kwa sababu ni vijiji vichache sana ambavyo vimewekewa umeme na pia alipewa vijiji vichache?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tumeambiwa Mji wa Masasi umeungwa na Grid ya Taifa kutokea Mkoa wa Ruvuma lakini hali ya kukatikakatika kwa umeme ni mbaya zaidi kuliko hata kabla haijaungwa. Ni juhudi gani sasa zinatakiwa zifanywe na Serikali kuhakikisha kwamba inawaondoa wananchi wa Masasi katika adha hii kubwa nay a muda mrefu ya kukatikakatika kwa umeme? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Chuachua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mkandarasi ambaye yuko site, kwanza tunataka atimize wajibu wake kwa mujibu wa mkataba aliousaini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hilo litafuatiliwa ili kujua tatizo lake ni uwezo au ni jambo gani ili aweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Mheshimiwa Spika, kwa sehemu ya pili, niseme tu kwamba kwa ufahamu nilionao ni kwamba kwa sasa bado Masasi haijaungwa kutoka kwenye Gridi ya Taifa kutoka Mkoa wa Ruvuma kwa sababu hata hiyo line haijajengwa isipokuwa kuna mpango wa kufanya hivyo. Naamini endapo utekelezaji huo utafanyika, hali ya Mji wa Masasi itakuwa ni bora zaidi ikizingatiwa kwamba umeme ambao umekuja mpaka Songea Mjini Ruvuma ni wa KV 220 na capacity ya megawatt 60 ni mwingi na unatosheleza kupeleka mpaka maeneo hayo.
MHE.DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa sasa kuna upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi katika Halmashauri ya Masasi na walimu 46 wanahitajika ili kukidhi Ikama ya walimu wa masomo ya sayansi;

Je, ni lini Serikali italeta Walimu hao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba kwa kuwa suala la kukosekana kwa walimu wa sayansi ni suala la Kitaifa, na kwa kuwa wanafunzi wengi wanaomaliza kidato cha nne na kidato cha sita hawachagui kwenda kujiunga na masomo ya ualimu wa masomo ya sayansi, hivi Serikali haioni kunatakiwa kuwe na jitihada za maksudi za kuchochea watoto hawa ili waweze kujiunga na masomo ya ualimu wa sayansi hususan kwa kuondoa ama kupunguza ada kwa masomo ya Diplomaya Ualimu wa Sayansi na Degree ya Ualimu wa Sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia suala la elimu hasa katika masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua ni lini walimu wa sayansi watapelekwa katika maeneo haya. Ni kweli kwamba kuna upungufu wa walimu wa sayansi na hisabati katika shule zetu za sekondari lakini tumepata kibali mwaka wa fedha uliopita tukaajiri walimu 4,500 na sasa tunasubiria kibali kingine takribani walimu 15,000. Tukipatakibali hicho tutaajiri, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ambayo yana upungufu tutaanza nayo, pale palipo na upungufu mkubwa tunaanza na kuendelea katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuwa na walimu wa kutosha katika masomo ya sayansi ili kuweza kuboresha elimu hii ya sayansi hasa kwenye dhana nzimainayohusiana na Serikali ya Awamu ya Tano ya sera ya maendeleo ya viwanda na uchumi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anazungumzia kama kuna uwezekano wa kupunguza ada katika masomo na hasa katika Diplomaili wanafunzi wengi na vijana wengi wajiunge katika masomo ya sayansi na hasa Ualimu ili waweze kupunguza changamoto hii. Kwanza gharama inayotumika sasa siyo kubwa ni gharama ya kawaida kabisa na Serikali imejitahidi sana kupunguza michango mingi ambayo ilikuwa inafanyika. Sasa hivi tumeshapeleka vijana wengi katika Vyuo hivi, wataendelea kusoma na ada ni ya kawaida. Ahsante.(Makofi)
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni la muda mrefu na majibu pia ni ya zamani, lakini hali ya mauaji ya vijana wa bodaboda katika Wilaya Masasi bado inaendelea mpaka sasa. Hata wiki tatu zilizopita tumezika vijana wawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba swali la kwanza liwe Mheshimiwa Waziri atoe kauli sasa kwa kuwa Wasaidizi wake kule wameshindwa kudhibiti mauaji haya kauli yake ni ipi ili kuhakikisha kwamba vijana hawa hawapotezi maisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri naomba atueleze ni watuhumiwa wangapi mpaka sasa wamekwishafikishwa Mahakamani kwa makosa haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya Serikali kulingana na hoja ambayo ameizungumza ni kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba tunadhibiti mauaji nchi nzima, hata mimi na yeye Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anaonekana kutokuridhika na takwimu ambazo mimi naamini ni sahihi za mauaji ya watu wanne kwa mwaka 2018/2019, nitakuwa tayari tupange tuende katika Wilaya yake tuweze kuthibitisha hilo, nilifika katika Wilaya ya Masasi lakini tutakwenda tena kwa ajili ya suala hili kwa sababu suala linalogusa uhai wa Watanzania ni suala ambalo linahitajika kuchukuliwa kwa uzito unaostahiki. Kwa hiyo, ili kuweza kujua kama ana taarifa ambazo hazijafika katika Jeshi la Polisi tutazichukua na kuzifanyia kazi kwa pamoja na Jeshi la Polisi katika eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusiana na swali lake la kutaka kujua idadi ya watu ambao wamechukiliwa hatua, kwa wale watu wanne ambao nimewazungumza tayari watu wawili wameshakamatwa na wapo katika hatua mbalimbali za kisheria. (Makofi)