Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Deogratias Francis Ngalawa (31 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukupongeza kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Naitwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa namna kilivyoiandaa Ilani yake. Ilani yake ni Ilani nzuri ambayo imetengeneza mpango mzuri wa mwelekeo wa Taifa ambako linatakiwa kwenda. Katika chaguzi zetu tuliinadi Ilani na wananchi wakatuchagua. Kwa hiyo, napenda kukipongeza chama. Hawa wanaotoka sasa ni kwa sababu hoja zao nyingi zinapwaya, hawana kitu cha kukizungumzia zaidi ya kutengeneza vijembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kujikita katika hotuba ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake katika ukurasa wa 12 ameizungumzia reli toka Mtwara – Songea – Mbamba Bay mpaka Liganga. Mimi napenda kumshukuru kwa hilo na tulipokuwa tunaizungumzia hiyo reli ya kutoka Mtwara mpaka Liganga ni kwa maana tunazungumzia suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga limekuwa ni suala la muda mrefu. Nadhani sasa ni kipindi cha miaka 50 limekuwa likizungumziwa na halina utekelezaji wowote. Nimshukuru Waziri Profesa Muhongo, tarehe 4 na 5 alifika kwenye makaa ya mawe Mchuchuma na vilevile alifika pale chuma – Liganga; alijionea type ya wawekezaji ambao tunao na namna gani wanaweza wakaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisikitike, wana wa Ludewa wana masikitiko makubwa. Wameachia ardhi yao miaka ipatayo 10, ardhi ile haitumiki, hawaitumii kwa maana yao na hakuna utaratibu wowote wa matumaini wa kulipwa fidia katika maeneo ambayo wao wameyaachia.
Sasa nipende kuliambia Bunge lako, wananchi wanataka fidia ya maeneo waliyoyaacha na kibaya zaidi hata ule mpango wa kimkakati wa huyu mwekezaji bado hauonekani!
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Waziri Muhongo tarehe 5 Mchuchuma, pale Nkoma Ng‟ombe na vilevile tulikuwa Liganga pale Mndindi; Serikali imekuwa ikiwakilishwa na NDC na wawekezaji ni Wachina, lakini katika majadiliano na maongezi yao wana contradiction kubwa. Ile miradi ni mikubwa, kuna mamilioni ya tani za makaa ya mawe, leo nchi inazungumza kwamba haina umeme! Lakini tunaamini mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma ukianza umeme katika Taifa hili inaweza ikawa ni historia.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme utakaozalishwa Liganga una uwezo wa ku-supply ndani ya nchi hii katika miaka isiyopungua 150, lakini leo Taifa bado halijachukua hatua madhubuti. Ni miaka mingi, sisi wengine toka tunasoma, kabla hatujazaliwa tunaambiwa kuna makaa ya mawe – Mchuchuma, tunaambiwa kuna chuma – Liganga! Mwekezaji aliyepo ameonesha incompetence kubwa mbele ya Waziri Profesa Muhongo! Hakuna maandalizi ya kutosha ya hiyo miradi kuanza!
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nipende tu kushukuru na kumshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, aliwaeleza wananchi wetu ukweli kwamba Taifa tunapoamua kuingia mikataba hii iwe ni ya wazi na kusiwepo na uficho wowote.
Mimi ninaamini Waziri usingekuja Ludewa, usingekuja pale Nkoma Ng‟ombe – Mchuchuma, usingekuja Liganga bado wananchi wetu wangekuwa wanaendelea tu kudanganywa danganywa na tusingejua fate yoyote ambayo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nipende kuchukua fursa hii kwamba, tupate wawekezaji ambao ni serious. Tupate wawekezaji ambao wana uhakika, ili mwisho wa siku watu wetu tuwajengee matumaini, ili nchi iweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukizungumza sana Bungeni kwa nini nchi haiendi, wakati tuna madini ya kutosha, tuna mazao ya kutosha, lakini hatuchukui hatua. Huyu mwekezaji amekuwa akikumbatiwa! Haoneshi dalili yoyote ya namna gani tunaweza kwenda! Fidia hataki kulipa, anaulizwa kama hizo hela anazo anasema hela hana anasubiri kukopa nje ya nchi! What type of mwekezaji is? Sasa investor wa namna hii kweli tunakaa na kumkumbatia namna hii? Mimi nadhani siyo sawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Ludewa wanaisubiria Liganga ianze mara moja kwa sababu, imeshakuwa ni hadithi za muda mrefu. Liganga aanze, Mchuchuma aanze, tuachane na hii biashara kwamba hatuna umeme, hatuna umeme, hatuna umeme! Hii inatakiwa kubaki kuwa ni historia. Lakini mimi ninamuamini Waziri Muhongo atalishughulikia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ya Itoni – Njombe kuelekea Manda; barabara hii Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba iwekwe lami, lakini nashukuru TANROADS juzi imetangaza kipande cha kilometa 50 kutoka Lusitu kuelekea Mawengi kwamba kitawekwa lami. Kwa hiyo, tunaomba hili lizingatiwe na lifanyiwe kazi haraka vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna barabara kutoka Mkiu kwenda Madaba na yenyewe Mheshimiwa Rais ameizungumzia kwa kiwango cha lami. Tunaomba lami hiyo iwekwe na wananchi wana matumaini, wana mazao yao mashambani, ila usafiri umekuwa ni shida, pindi hizi lami zikiwa tayari naamini kabisa mazao yatafika kwenye maeneo ya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna suala la miundombinu ya mawasiliano ya simu. Leo hii Tarafa nzima ya Mwambao, Ukisi kule Ziwa Nyasa tunapakana na Malawi, vijiji 15 havina mawasiliano ya simu kabisa! Sasa sijajua Serikali inajipangaje na inawaonaje hawa watu? Hawa watu wako mpakani! Huku tunapakana na Kyela na Dkt. Mwakyembe! Huku tunapakana na Nyasa na Engineer Manyanya! Hapa katikati pamekuwa hamna mawasiliano ya aina yoyote! Wananchi wale wameniambia wataanza wao kutafuta hayo mawasiliano. Hatuna mawasiliano ya barabara, hatuna mawasiliano ya simu! Kwenye upande wa barabara wanasema wao wataanza na jembe la mkono. Na ninaiomba Serikali sasa ituunge mkono, ili tuweze kuviunganisha hivi vijiji na waonekane na wao wapo ni sehemu ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiahidiwa muda mrefu juu ya daraja la Mto Ruhuhu unaounganisha Wilaya ya Ludewa na Wilaya ya Nyasa. Wananchi wanapata shida na kivuko kile na kivuko kimekuwa hakifanyi kazi. Dada yangu Injinia Manyanya unalifahamu hilo. Tunaomba Serikali ilichukue hilo na ilifanyie kazi, ili mwisho wa siku tuweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi sisi wana wa Ludewa. Mheshimiwa Rais alipokuja Ludewa alitoa ahadi ya kipande kidogo cha lami cha kilometa 25 kutoka Ludewa mpaka Lupingu. Kwa hiyo, tungeomba ahadi hizo zitekelezwe.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umeisha!
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabla ya yote nipende tu kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nipende kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, pia na watendaji wote na viongozi wakuu wa taasisi ambazo zipo chini ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza ambacho pengine ningependa kuchangia leo ni juu ya mtandao wa mawasiliano ya simu. Ikumbukwe kando kando ya Ziwa Nyasa yaani Ziwa Nyasa lilivyo eneo kubwa ni eneo la Ludewa. Upande wa Nyasa kama Wilaya lina urefu wa kilometa 112 na upande wa Kyela lina urefu kama kilometa 10; lakini sisi Wana-Ludewa tuna kilometa zipatazo kama 220, cha kushangaza na cha kusikitisha, mpaka hivi ninavyoongea kando kando mwa Ziwa Nyasa tuna tarafa moja na tuna kata sita, hakuna kijiji wala Kata ambako kuna mawasiliano ya simu. Ikumbukwe kwamba eneo lile la ziwa lipo mpakani mwa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, enzi zile sisi tukiwa watoto, yule bwana mkubwa akija unakuta kuna Sub Marine imesimama juu, wazee wetu walikuwa wanakimbia wanajifungia kwenye mahandaki, lakini mahandaki hayo sasa hivi hayapo. Kwa hiyo, eneo hili hata kama ni kutoa taarifa za kiulinzi na kiusalama tunashindwa. Kwa hiyo, nipende tu kumuomba Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele cha juu lile eneo kwa sababu ni eneo kubwa, kwa sababu ukiangalia ni kama vile tumetengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nyasa yenye kilometa 112 vijiji vyake vyote vinamtandao wa mawasiliano, Kyela yenye kilometa kama 10 vijiji vyake vyote vina mtandao wa mawasiliano. Lakini unapoanza mipaka, beacons za Ludewa hakuna kijiji hata kimoja; vijiji 15, tukiweka kata sita vinakuwa vijiji 18 kata sita hakuna kijiji wala kata ambayo ina mawasiliano ya simu. Kwenye hili tunajiona kama ni wakiwa na kama vile tumetengwa. Ukija pia kwenye eneo hilo hilo la barabara yaani barabara zimeishia Nyasa na Kyela. Eneo la Ludewa halina kabisa. Tuna vijiji 15 ambavyo havijawahi kufika hata baiskeli, wananchi wameamua kuchimba wenyewe kwa mkono. Kwa hiyo, tunaiomba sasa Serikali ije iwaunge mkono wananchi wale ili waweze kupata barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hata nikizungumzia suala la road upgrading Ludewa imeachwa kabisa. Kuna upgrading Makete kama mkoa, kuna upgrading Makambako, Wanging’ombe na Njombe lakini Ludewa imeachwa. Sasa huwa tunashindwa kujua Ludewa ina matatizo gani mpaka tusi-upgrade barabara hata moja? Mimi nipende kutoa masikitiko ya Wana-Ludewa kwa sababu inakuwa sio jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ndani ya mkoa yanafanyia road opening, paving way, lakini eneo la Ziwa Nyasa ambalo lipo mpakani mwa nchi; hata kipindi kile wakati wale jamaa wanakuja kuja na ule mtafaruku tukawa tunashindwa wapi pa kwenda, barabara sehemu ya kukimbilia hatuna, mawasiliano kusema kwamba tutatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama hakuna. Sasa nipende tu kujua labla pengine Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha utatuambia inawezekana Ludewa ina makosa ambayo imeifanya ndani ya Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja upande wa bandari. Tunaishukuru Serikali kwa zile meli tatu, meli mbili za mizigo na meli moja ya abiria. Vilevile kuna ujenzi wa gati ndani ya Ziwa Nyasa bado tunakuja kuona hapo hapo, upande wa Wilaya ya Nyasa kuna gati zinajengwa na kwenye bajeti mmeweka, upande wa Kyela kuna gati zinajengwa lakini ni upande wa Ludewa tu pekee yake ndiko hakuna gati.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunakuja tunajiuliza maswali mengi sana, Ludewa ina tatizo gani na nchi hii? Kyela wanawekewa gati, Nyasa inawekewa gati. Halafu mahali huku ndiko ambako tunasema leo tuna uchumi wa viwanda. Tunapozungumzia uchumi wa viwanda huwezi ukaisahau Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma inakuja lakini miundombinu hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu angalia upande wa barabara; tunashukuru barabara ya Itoni - Njombe - Manda - Ludewa, mkandarasi yupo, ipo kwenye mobilization finalization, lakini kuna zile barabara ambazo ndio zinakwenda kwenye ile miradi, kuna barabara ya Mkiu kuelekea Madaba.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunaambiwa inafanyia rehabilitation, lakini mimi nilikuwa najua tungeiweka sasa kwenye upembuzi yakinifu baadae iende kwenye usanifu wa kina ili twende kwenye lami, kwa sababu barabara hii ndiyo inayoelekea kwenye mradi mkubwa wa Liganga. Kwa sababu utakuta sasa miundombinu Ludewa ni miundombinu ya kizamani na hakuna consideration ambayo inafanyika kwa ujio wa miradi mikubwa kama ya Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unaponiambia kwamba kuna flagship project za Liganga na Mchuchuma; na ndiyo maana huwa tunauliza, hii Liganga na Mchuchuma itaanza lini? Maana tungeweza kupewa schedule kwamba mwaka huu mpaka mwaka huu kuna hiki kuna fidia inafanyika, mwaka huu mpaka mwaka huu kuna hiki kinafanyika then baada ya hapo tunajua sasa mradi una- takeoff. Kwa inawezekana tunaona kwamba hata hii miundombinu inakuwa haiwekwi kwa sababu hata huo mradi wenyewe haufahamiki utaanza lini? Kama ungekuwa unafahamika utaanza lini mimi ni naamini kwamba hizi barabara zingeanzwa kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababau Nchi inavyoelekea kwenye viwanda mnakitegema chuma cha Liganga, Nchi inavyoelekea kwenye viwanda mnakitegemea umeme utakaozalishwa Mchuchuma, megawati 600; lakini kwa nini leo hatuweki hiyo miundombinu?. Wenzetu wote ambao wako ndani ya Mkoa kuna activities zinafanyika lakini ni Ludewa tu. Ukija gati inafanyika Nyasa na Kyela; Ludewa inaacha, ukija mawasiliano ya simu kuna Nyasa na Kyela; Ludewa inaachwa. Ukija barabara zinaishia kwenye beacon ya Kyela na huku inaishia kwenye beacon ya Nyasa lakini Ludewa inaachwa. Sasa lazima tujiulize panashida gani na Ludewa?

T A A R I F A...

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Hiyo taarifa siipokei, kwa sababu haiwezekani watu wengine wanapewa fursa wengine hawapewi halafu uniambie kwamba… tena unanifundisha hata namna ya kusema, haiwezekani, tunazungumza vitu vilivyo-live. Mimi bajeti ninayo kila kitu kipo humu wakati mwingine mnaaweza mkaenda mbali labda kwingine labda pengine huku kwa sababu kuna Mawaziri na Ludewa hayupo Waziri, ndiyo mnataka kuniambia hicho, kwa nini Ludewa isipewe? Hiyo ndio hoja yangu mimi ya msingi

T A A R I F A...

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa siipokei. Mimi naongea kwa niaba ya wananchi wa Ludewa na wananchi wa hii. (Makofi)

Kwa hiyo, kama sehemu kipo na wakati huo mahitaji yetu yanalingana naona ni kama tunabaguliwa. Kwa sababu katika eneo la Ziwa Nyasa sisi ndio wenye eneo kubwa kuliko Nyasa, kuliko Kyela, sasa kule kuna kitu gani kikubwa ambacho hiyo miundombinu inapewa kipaumbele kuliko huku kwingine, kwa nini? Maana ukiniambia unajenga chuo lakini barabara hamna chuo hicho kitakuwa hakina maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima ifike mahali kwamba hizi fursa lazima tupewe wote sawa. Kama ni chuo hata Nyasa kinajengwa, kipo kwenye programu, kwa hiyo, maana yake utakuwa una barabara, una gati na hicho chuo kitakuja. Ndiyo maana tunazungumza hapa Ludewa ina tatizo gani? Kama ni uvuvi, uvuvi mkubwa unafanyika Ludewa kuliko Nyasa na Kyela, wao wanajua, sisi ndio mabingwa wa kuvua, mabingwa wakuvua ni Wakisi kuliko Wamatengo, kuliko Wanyakuysa, sisi ndio tunaowafundisha, tumeenea kwenye mabwawa yote ya Tanzania. Ndiyo maana tunazungumza, kwa nini hatupewi kipaumbele? (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Marehemu Deo Filikunjombe, Mungu amuweke mahali pema, amekuja hapa, amezungumza sana juu ya haya mambo; kapita kaenda. Ndiyo kwa maana sisi tunasema kwamba tunakosa gani? Licha ya kwamba tumekuwa tukiwasiliana na Waheshimiwa Mawaziri juu ya masuala haya. Si kwamba ni mara yangu ya kwanza mimi kuzungumza hapa Bungeni, nimezungumza sana na Mheshimiwa Mbarawa, ni mezungumza sana tu na Mheshimiwa Ngonyani, na inafikia kipindi hata Katibu Mkuu nimejaribu kuwa nampigia simu amekuwa hapokei, na mpaka nikajitambulisha naitwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa still yet hapokei! Inawezekana Ludewa kuna matatizo. Ndiyo maana tunazungumza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama ni suala la fursa basi tupewe fursa sawa. Leo hii Ludewa barabara hazipitiki, hii barabara tunayozungumza ya Mkiu – Madaba imekata, watu wanakaa siku mbili njiani why, wakati wenzetu wanapeta? Vijiji havijawahi kufika baiskeli hata siku moja, pikipiki haijawahi kufika vijiji 15. Wananchi wameamua wenyewe kuchimba, kwa nini Serikali isije? (Makofi)

Tumeamua wenyewe clips za wananchi kuchimba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri niliwaonesha kwamba tumeamua kuchimba wenyewe kwa majembe kwa nyundo kwa mitalimbo. Leo hii tunapokuja kuzungumza unasema tusilinganishe, tusilinganishe kwa base ipi? Ifike mahali fursa lazima tupewe sawa, mimi langu ilikuwa ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

HE. DEOGRATIAS F. NGALAWA …kufikisha ujumbe huo na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. DEOGRATIUS M. NGALAWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa ruhusa ya kuja kuongelea mambo mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wajumbe wameyajadili kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji katika Kamati hii, wamechangia Waheshimiwa Wabunge 23. Kwa kuongea wamechangia Waheshimiwa Wabunge 16 na kwa maandishi wamechangia Waheshimiwa Wabunge saba. Napenda niwataje Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hasa kwa maandishi kwa sababu hawa walioongea wameonekana hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maandishi ni Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mheshimiwa Oran Njeza, Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir, Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela na mwisho ni Mheshimiwa Silafi J. Maufi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi katika taarifa hii ya Kamati walijikita sana kwenye maeneo ya madeni. Walijikita pia kwenye maeneo ya mradi wa umeme wa maji wa Mto Rufiji ambao tunaita Stieglers Gorge, miradi ya REA I, REA II na REA III bila kusahau Densification Project.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile walizungumzia matumizi ya gesi kwa maana ya kuwepo kwa master plan ili kuweza ku-utilize gesi ambayo ipo kwa sasa ambayo inatumika kwa kiasi kidogo. Pia walizungumzia Taasisi ya GST, elimu kwa wachimbaji, ruzuku kwa wachimbaji wadogo, makusanyo ya maduhuli na suala zima la biashara ya Tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kifupi wazungumzaji wengi wameipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji mahiri wa miradi yetu mingi ambayo inatekelezwa sasa na Serikali hii ya Awamu ya Tano. Wachangiaji wengi waliojikita katika madeni hasa ya TANESCO na TPDC ukiangalia lengo lao kubwa lilikuwa ni kuzifanya hizi taasisi mbili ziweze kujiendesha bila kutegemea ruzuku au mkono wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja zilijikita zaidi katika kuhakikisha kwamba wanayasaidia mashirika haya mawili ya TANESCO na TPDC kuondokana na ule mzigo wa madeni na hasa TANESCO. Kwa sababu deni la TANESCO wadaiwa na wadai unakuta kwamba TANESCO bado anabaki kuwa na deni kubwa. Kwa hiyo, nguvu zilielekezwa nyingi kwa wachangiaji wengi kuona kwamba hili shirika la TANESCO, Serikali iweze kuhakikisha kwamba inalisaidia ili iweze kujiendesha yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa eneo la TPDC; pia TPDC ana madeni, lakini madeni ambayo TPDC anayo ni madeni machache kuliko madeni ambayo yenyewe inadai. Hata ukijaribu kuiangalia TPDC kwa undani na kwenye maelezo ya taarifa yetu, unakuta kwamba TPDC bado inabaki na hela nyingi kiasi ambacho yenyewe inaweza ikajiendesha. Kwa hiyo, michango mingi ilikuwa inaonesha kwamba TPDC ina mzigo mkubwa na Serikali inatakiwa kuingiza mtaji mkubwa ili kuhakikissha gesi ile ambayo inatumika itengenezewe miundombinu ya kutosha kwa sababu gesi inayozalishwa ni nyingi kuliko ambayo inatumika sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wengine walijikita sana kwenye mradi wa umeme wa maji wa Mto Rufiji naamini kwamba hii Mheshimiwa Waziri na baadhi ya Wajumbe waliizungumzia kwa kina kwamba huu mradi siyo kwamba umeanza, ila upo katika maandalizi ya kuanza. Sasa na ni vizuri mara nyingi mradi kabla hujaingia kwenye ile process yenyewe kuufahamu, kabla haujaileta bajeti hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bajeti itakuja wakati tayari kila kitu kipo kwenye table na vitu hivyo vinakuwa vinaonekana. Kwa hiyo, sisi kama Kamati tunaipongeza Serikali kwa hatua ambazo inazichukua kwa sababu umeme huu wa stieglers Gorge utatuletea Megawati 2100 na vilevile itaendana sambamba na linkage ambayo inawekwa na philosophy ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na miradi ya umeme wa REA. Wachangiaji wengi wamezungumzia upungufu ambao umefanyika katika mradi wa REA awamu ya kwanza na REA awamu ya pili; na mara nyingi ni kule kurukwa kwa baadhi ya vijiji. Umeme unatoka kijiji hiki hapa, kinaruka unaenda kwenye kijiji kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia, wengi wameshauri kwamba ule upungufu ambao tayari umeshaonekana katika hii miradi ya REA I na REA II maana yake ni kwamba sasa kwenye REA III yafanyike maboresho. Bahati nzuri Serikali imekuja na utaratibu wa Densification Project ili kuweza ku-clear upungufu wote ambao umefanyika katika REA I na REA II na bahati nzuri baadhi ya Wakandarasi tayari wameshapewa tender na wapo site wanafanya kazi hii ya marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matumizi ya gesi; wachangiaji wengi wameona kwamba gesi iliyopo ambayo inazalishwa na TPDC ni nyingi. Kwa hiyo, kuna haja sasa ya Serikali kutengeneza miundombinu wezeshi ya kuifanya TPDC iweze kupeleka gesi maeneo mbalimbali na hususan kwenye majumba yetu. Kwa hiyo, hiyo master plan itaonesha maeneo ambako gesi inapita na hata kama wawekezaji watakuja, maana yake watatumia ile master plan ambayo ipo. Vilevile wachangiaji wengine walizungumza kwamba kuna baadhi ya nchi jirani ambazo na zenyewe zinaenda na mifumo hii. Kwa hiyo, maana yake TPDC iwezeshwe ili kuweza kuingia kwenye soko la kiushindani la Kimataifa, kwa sababu gesi iliyopo ni nyingi na watumiaji ni wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia limeongelewa kuhusu Geological Survey of Tanzania (GST) kwamba ndio iwe mtafiti pekee wa madini Tanzania na in case kama kuna wawekezaji wa uchimbaji, basi wapate consent au washirikiane na taasisi hii katika kufanya utafiti huo. Kwa sababu inaonekana baadhi ya taasisi za nje zinafanya hujuma ya kufanya tafiti kwa muda mrefu kiasi ambacho hata zile taarifa nchi inakuwa hazina.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa kuiunganisha na GST kwa kupata consent ya GST maana yake ni kwamba, nchi kwanza itapunguza ule urasimu ambao unafanywa na pia nchi itakuwa na clear picture ya maeneo ambayo yana madini na vilevile itawafanya baadhi ya wachimbaji wetu wadogo na wa kati kutokutumia gharama zao nyingi katika kuwekeza mahali ambako hawana uhakika wa madini ambako yapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwamba GST ikishakuwa mbele ya wachimbaji wetu wa kati na wa chini, maana yake ni kwamba mtu ataenda kuwekeza na atakopa mikopo benki kwa ajili ya uwekezaji huu akijua picha halisi na hali halisi ya madini iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia limezungumziwa suala la elimu kwa wachimbaji. Elimu kwa wachimbaji ni muhimu na hata sisi Kamati tumesisitiza hilo kwa sababu kuna athari nyingi ambazo zinatokea kule kwa sababu ya kukosa uelewa na kukosa elimu ya kutosha juu ya maeneo hayo, kunakuwepo na athari nyingi na ajali nyingi, kwa mfano kuangukiwa kwa vifusi na vitu vya namna hiyo. Hayo yameelezwa, nasi kama Kamati tuliona jambo hili ni la muhimu kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, lilizungumzwa pia suala la ruzuku kwa wachimbaji wadogo. Hapa pia lilizungumzwa na suala la elimu na ndiyo maana unaona hata kwenye ripoti ya Kamati na Wajumbe walipokuwa wanachangia, kuna baadhi ya pesa za ruzuku ambazo Serikali imepeleka, lakini ilienda kufanya kazi ambayo haikukusudiwa. Watu walienda kuelekeza kwenye maeneo ambayo hawakuyaombea. Kwa hiyo, hapa upatikane usimamizi wa kutosha ili kuhakikisha kwamba hela inayotolewa na Serikali inasimamiwa na inafanya klengo lililokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika upande wa madini kuna makusanyo ya maduhuli. Napenda kuipongeza Wizara ya Madini kwa ukusanyaji wa maduhuli asilimia 84 ya lengo ambalo ni la mwaka mzima kwa kukusanywa ndani ya nusu mwaka. Kwa hiyo, kama Kamati tunaipongeza, iendelee na utaratibu huo. Vilevile wapo walioipongeza Serikali kwa kuchuka hatua kuhusu utoroshwaji na ubadhirifu ambao unapatikana kwenye madini yetu ya Tanzanite. Serikali imeshachukua hatua kubwa ya kujenga ule ukuta na pia kupitia mikataba ambayo inaonekana inaitia hasara nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia kwenye Kamati yangu wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi inayozifanya, ni kazi njema, ina nia njema na imeonesha uzalendo mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili na maendeleo ya watu wake wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua hatua hii kukupongeza wewe, Mawaziri wote, kuwapongeza Wabunge wote waliochangia kwenye Kamati yangu na naomba sasa taarifa hii ya utekelezaji ya Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ipokelewe na Bunge lako na kuwa ni taarifa rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niongee katika Bunge lako Tukufu. Kwanza nianze na pongezi kwa Serikali yetu na kufuatia ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale Ludewa tarehe 26 Januari, 2017, imeleta matokeo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofika Ludewa aliambiwa juu ya taabu kubwa ya barabara, hasa ile barabara inayotoka Mkiyu kuja Madaba ambayo inapita kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma na pia kuna ile barabara ambayo inatoka Mchuchuma kwenda Liganga. Mpaka hivi ninavyozungumza, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeanza toka ile Julai, 2017 na unaisha mwezi Oktoba mwaka huu. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napongeza miradi ya REA inayoendelea katika Jimbo langu. Wakandarasi wapo na wanaendelea na kazi hivi ninavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali katika miradi hii ya Vituo vya Afya. Zile shilingi milioni 500 tumepata katika Vituo vya Afya viwili; Vituo vya Afya vya Manda na kule Mlangali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, alipita Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mheshimiwa Engineer Nditiye, tumeona impact ya ile ziara. Sasa hivi ninavyozungumza, minara nane ya mitandao ya mawasiliano ya Halotel imeanza kujengwa. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hatua ambazo inachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie na mambo mengine yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma ni mradi wa kimkakati. Napenda sasa kuiomba Serikali kwamba hii miradi lazima tuiwekee programu. Kwa sababu ni miaka mitano, lazima tuwe tunajua mwaka wa kwanza tunafanya kitu gani? Mwaka wa pili tunafanya kitu gani? Mpaka ile miaka mitano itakapofika na iweze ku-take off. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa naamini kwamba, hizi barabara zinazotengenezwa sasa kuelekea kwenye hii miradi miwili ni miundombinu wezeshi kuelekea huo mradi kuanza. Pia, tuna ule mradi wa Makambako – Songea, Madaba – Ludewa, kwa maana ya Gridi ya Taifa na yenyewe sasa hivi tayari imeshafika Ludewa, bado tu muda kidogo uende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itupe ule mpango kwamba sasa tutakapokuwa tumemaliza stage hii tunakuja stage hii, ili tuweze kuzifanyia assessment, hata tunapokuja katika Bunge hili, tuna uwezo wa kusema kwamba, okay, kwa namna tunavyokwenda basi, mradi huu utakuwa umekamilika kwa kiasi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi jinsi tulivyo, tunashindwa kufanya assessment kwamba sasa huu mradi umefikia wapi? Labda ningependa tu Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hili, tujue kwamba sasa huu mradi hasa hasa unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, kuna changamoto ambazo huwa zinaelezwa kwenye hotuba mbalimbali za Waheshimiwa Mawaziri, mwaka 2016/2017 na 2017/2018, lakini naamini kwamba zile changamoto ziko ndani ya uwezo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali ifanye jitihada na safari hii ije na majibu kwamba sasa mradi huu unaenda kwa stage hizi, mpaka itakapofikia muda fulani huo mradi utaanza, kwa sababu maswali yamekuwa mengi sana. Ikumbukwe tunaambiwa kwamba huu mradi ni wa kimkakati. Kwa hiyo, naamini mradi wa kimkakati ni lazima upewe kipaumbele kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tulivyo hatuna uwezo hata wa kutoa majibu sahihi kwa wananchi wetu wanapokuwa wanatuuliza kwamba huu mradi utaanza lini? Kwa hiyo, naamini kwamba Serikali itakapokuja basi, itakuja na majibu ili kuona namna gani ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mradi wa barabara ya Itoni – Njombe, Ludewa – Manda. Mradi huu vilevile una impact katika ile miradi mikubwa ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga, lakini unaenda kwa utaratibu mno. Hii barabara imepangiwa lots nne; mpaka sasa hivi tupo kwenye ile lot ya kwanza tu. Kwa hiyo, unakuta sasa inatuchukua mwaka wa pili ule mradi toka uanze, lakini barabara hii bado haijakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu hii barabara ni muhimu kwa ajili ya kufungua uchumi wa nchi, Serikali sasa itupatie na lot nyingine, hasa ile lot ya kuanzia pale Njombe kuja Lusitu ili tuweze kuona kwamba sasa ile miradi tunayoizungumzia ya Mchuchuma na Liganga inaweza ika-take off kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuimarika kwa miundombinu hiyo ya barabara itawezesha wananchi kujiandaa na ujio wa hiyo miradi. Kwa sababu impact ya miradi ile inatarajia kuleta watu wasiopungua 300,000 ndani ya Ludewa na Mkoa wa Njombe kwa ujumla wake. Kwa hiyo, maana yake ita-stimulate uchumi, mazao ya wakulima wetu yatapata tija, kwa maana ya bei na kwa maana ya mzunguko wa biashara. Kutakuwepo na usafirishaji wa aina nyingi na barabara zitakazotumika ndiyo hizi ambazo tunazizungumzia sasa hivi na pia tutaanzisha hivyo viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa ambazo tutakuwa tunazizalisha kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuisihi Serikali na kuiomba kwa moyo mkunjufu kabisa, ituongezee lot ya pili kwenye barabara ya Itoni – Njombe, Ludewa – Manda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye eneo la afya. Kwenye eneo la afya tuna upungufu mkubwa sana wa wahudumu au wafanyakazi wa afya. Kwa kweli, tatizo hili limeshakuwa kubwa na bahati mbaya zaidi ni kwamba hata ujenzi unaoendelea kwenye maeneo mbalimbali bado unahitaji sana nguvu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, sasa hivi kule kwetu Ludewa tunajenga Vituo vya Afya 17 na sasa hivi vipo kwenye viwango mbalimbali; na hizo zote ni nguvu za wananchi. Wananchi wale wana uwezo wa kujenga mpaka kufikia kuezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali sasa hebu itupie jicho kule, ikiwezekana iwasaidie hawa wananchi na wadau mbalimbali ambao wanashughulika na ujenzi wa hivyo Vituo vya Afya. Wananchi wameingiwa na hamasa kubwa kwa ajili ya utekelezaji ambao Serikali inaufanya. Kwa hiyo, naamini kwamba wakiungwa mkono ile sera au Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayozungumzia Kituo cha Afya Kila Kata, ina uwezo wa kutekelezwa kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye upande wa elimu, bado tuna upungufu mkubwa wa Walimu katika nchi nzima. Tuna upungufu wa Walimu 90,000 nchi nzima kwa data ambazo tunazo sasa hivi. Kwa hiyo, Serikali ijaribu kuona uwezekano wa kupata Walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la juu ya ubora wa elimu ambayo inatolewa sasa hivi. Ukijaribu kuangalia kwa kiasi kikubwa, matokeo mabaya yanayoipata nchi sasa hivi kutokana na hii mitihani ya NECTA, vilevile inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa Walimu. Kwa hiyo, wakati mwingine tunaweza tukawalaumu wanafunzi, lakini vilevile kuna tatizo la msingi kwa Walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali, umeshafika muda sasa kwa sababu, elimu ni profession kama zilivyo professions nyingine za Uhasibu au Sheria, tuunde sasa chombo madhubuti, Teachers’ Profession Board, ambacho kila Mwalimu atakapokuwa ame-graduate, lazima apite huko kwa ajili ya kupata utaalam zaidi na kupimwa, kufanyiwa assessment kabla hajaenda kuwafundisha watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini tukishafanya hivyo, tutapata quality ya Walimu ambao ni wazuri na product itakayotoka kwa wanafunzi wetu, itakuwa ni product nzuri. Ilishafika wakati kwamba Ualimu ilikuwa ni kimbilio la kila mmoja. Kwa hiyo, lile kimbilio la kila mmoja nadhani sasa hivi wakati wake umeshapita. Kwa hiyo, nashauri tupate chombo madhubuti kitakachosimamia quality ya elimu. Kwangu nashauri tuwe na Teachers’ Profession Board.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado miundombinu ya shule zetu ni chakavu. Wananchi wanajitahidi na wanaendelea vizuri na ile dhana ya kusema elimu bure imeleta sokomoko kubwa kwa wananchi wetu. Hivyo, bado naiomba Serikali na sisi Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu, tujaribu kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili baadhi ya yale mambo ambayo hayapo kwenye elimu bure, basi wananchi wetu wayachukue na ile itawatengenezea ile sense ya ownership.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwambia mtu elimu bure kila kitu, anaondoka na anaacha kila kitu. Tukitengeneza ile sense ya ownership, maana yake mtu anajua kile kitu ni chake na atakuwa na uwezo wa kukisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwanza kwa kupata nafasi ya kuweza angalau kujadili hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kwanza kabisa napenda kutoa kilio changu cha wana wa Ludewa, kwa sababu Ludewa sasa inaonekana ni eneo ambalo limesahaulika kwenye mambo mengi. Hivi ninavyoongea sasa, Jimbo la Ludewa lina uhaba wa Walimu 496, tuna shule 108; katika shule hizo 108 ni shule saba tu ndizo ambazo zina Walimu wanaoweza kukidhi. Shule nyingine zote 101 zina Walimu wanne kushuka chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ambayo ina Walimu wawili na shule zilizo nyingi zina Walimu watatu. Kwa hiyo, cha kwanza napenda tu kutoa masikito yangu kwamba tuna uhaba wa Walimu 496 na bahati mbaya kabisa katika kipindi hiki mmetupatia Walimu 30. Hata hivyo kuna Walimu 25 ambao wanastaafu Septemba na kupelekea uhaba wa Walimu 521.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuwasiliana na TAMISEMI, sasa napenda kutoa kilio hiki kwako Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe ndiye msimamizi wa elimu Tanzania. Kwa hiyo, naomba tu mwisho wa siku nikuletee majina kwa watu ambao wanataka kwenda kufundisha Ludewa na ikiwezekana basi mfanye utaratibu mtuletee Walimu. Kwa kweli hali ni ngumu na ndiyo maana nimeamua nije nizungumze katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hata vyuo vyetu vikuu havipeleki wanafunzi kwenda kufanya field kule, kwa sababu ya miundombinu mibovu ya barabara na miundombini mibovu ya mashule yetu, kiasi ambacho kimepelekea hata wanafunzi wenyewe wanaotoka kule kuomba msaada huo. Kwa hiyo, naomba nikuwasilishie hilo na hasa Chuo Kikuu cha Dodoma, kwamba hawawezi kupeleka Ludewa, lakini maeneo mengine yote ya Tanzania wanafunzi wanaweza kwenda kufanya field. Hii inapelekea shule zetu za Ludewa kuwa na pass ya chini kabisa na vijana wetu wengi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda ku-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule. Nianze na ada elekezi. Nadhani shule hizi za binafsi ndiyo zinazoleta fundisho kwa Serikali yetu kwamba ni namna gani shule zinapaswa ziwe na ninadhani zimeshaweka standard ya kuweza ku-move. Kwa hiyo, sababu ya kuweka ada elekezi, siyo za msingi na wala hazifai. Ninajiuliza swali, tusingekuwa na shule za private, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya na Uganda. Je, kule Uganda tungeweza kupeleka hizo ada elekezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suppose huku tungekuwa hatuna na kipindi kile kabla ya St. Marys kuanza, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya. Kwa hiyo, kosa letu ni kuboresha elimu, kutengeza miundombinu mizuri, mpaka inapelekea kuwa tunaongoza kwa hamsini bora. Hilo ndiyo kosa ambalo Serikali imeliona. Nadhani Serikali ingeshukuru, kwa sababu ninaamini kabisa wanafunzi wengi ambao wanang‟ara ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, ni wale ambao wanatoka private school, wanatuwakilisha. Kwa hiyo, tungewatengenezea miundombinu mizuri, ikiwezekana hata kuchukua mishahara mlipe nyie Serikali, kwa sababu watoto wanaofundishwa ni watoto wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sababu zile za msingi kupelekea kuweka hizo ada elekezi hamna. Kwa sababu usi-justify makosa unayoyafanya, usi-justify kutokuweka jitihada zozote ili uweze ku-capitalize kwenye shule za binafsi. Play your part, fanya shughuli zako, ninaamini ukitengeneza miundombinu mizuri, ukiwa na Walimu wa kutosha, hakuna mtu atakayeenda kwenye shule zenye gharama kubwa. Kwa hiyo, isifike kipindi Serikali inashindwa kufanya wajibu wake, kwa madai tu iende ika-suppress kwenye hizi shule za binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi ziachwe ziendelee, kwa sababu yale mazingira yaliyowekwa vizuri, wamiliki wa shule wengi wamekopa mikopo, wana madeni yenye riba kubwa. Kwa hiyo, maana yake utakaposema unatoa ada elekezi, tutashindwa kulipa yale madeni na mwisho wa siku sasa wakati huku tayari shule za private zimeshakaa vizuri, tunabomoa wakati huku kwetu kwenye government schools hatujaparekebisha bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya ujenzi wa Shule ya VETA Shaurimoyo, katika Jimbo la Ludewa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hajaiweka kabisa. Shule hii ya VETA kimsingi ilikuwa inaanzishwa pale kwa ajili ya kupokea miradi mikubwa miwili ya makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga, kuwaandaa vijana kwenye shughuli za kiufundi ili kuweza kushiriki katika hiyo miradi inayokuja. Nakumbuka mwaka 2012; kama siyo 2012, ni mwaka 2013, Serikali iliji-commit kwamba itajenga chuo hiki. Naamini sababu zile zile za kukitaka kukijenga hazijatoweka, sababu hizo zipo. Mlipeleka wataalam, ardhi imepimwa, hati mmepata, michoro mnayo, BOQs zote mnazo na mlisema mlishatenga hela kwa ajili ya kujenga hicho Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza tena swali hili, Chuo hicho kwanini kimeachwa? Matokeo yake, vile ambavyo wala havikuwepo katika kipindi hicho cha miaka miwili, mitatu iliyopita, leo ndiyo vimewekwa. Sasa watu wa Ludewa wanajiuliza maswali ya msingi, pana tatizo gani? Kwanini kisijengwe na kwanini hakuweka kwenye program yake? Kwenye hili Mheshimiwa Waziri hatutakubali kwa sababu kinachoonekana ni kuibagua Ludewa na Ludewa haitaweza kubaguliwa kwa sababu na yenyewe ipo katika nchi ya Tanzania.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja lakini tunaomba Chuo Ludewa.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuzungumza na kuchangia hoja ya Wizara ya Viwanda. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwa kishindo na Mawaziri wote kwa namna nzuri wanavyofanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu inajikita zaidi kwenye maeneo ya biashara. Hoja ya nchi kutaka kwenda kwenye viwanda ni nzuri, lakini kitu ambacho nakuwa na wasiwasi nacho ni namna ya utekelezaji wa hoja zetu. Ninavyojua, suala la viwanda ni mtambuka, sasa sijajua kwamba Serikali imejiandaaje katika kuhakikisha kwamba inawaandaa Watanzania katika mapokeo hayo. Ki-mind set Watanzania bado hawajawa tayari kwenye hilo, hivyo wanahitaji training ya namna gani ya kuweza kuipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunapozungumza, tuna wafanyabiashara wengi sana ambao wako informal na kundi hili la wafanyabiashara ni kubwa. Asilimia 70 ya wafanyabiashara wote wa Tanzania wako kwenye kundi ambalo ni la informal. Kwa hiyo, bado Serikali haijafanya mchakato mzuri wa kuhakikisha kwamba tunawaandaa wafanyabiashara wetu ili mwisho wa siku waweze ku-formalise biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini hizi biashara ziko informal? Ziko informal kwa sababu sheria haziko friendly. Tuna kundi kubwa la wafanyabiashara ambao wanashindwa ku-formalize biashara zao kwa sababu ya usajili; namna ya kuzisajili zile biashara inakuwa ni ngumu; na namna ya kupata leseni inakuwa ni ngumu. Leo hii tunaambiwa TIN number ni bure lakini ukijaribu kuangalia na kwenda, kupata hizo TIN number kwa ajili ya kufanyia hizo biashara, zile TIN number zina usumbufu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaambiwa, unapotaka kuanza kufanya biashara zako ni lazima kwanza utoe kiwango fulani cha hela hata kabla hiyo biashara hujaifanya. Sasa lile linawasumbua sana wafanyabiashara wetu mpaka inafikia kipindi kwamba anaamua acha afanye biashara kiholela, Serikali inakosa kodi na watu wanaweza wakafanya biashara nje ya mfumo sahihi. Nadhani umefika wakati sasa tuendeshe training na ikiwezekana hawa watu wetu tuwatengenezee namna ya kujua fursa za biashara zilizopo na ikiwezekana tupate elimu nzuri ya namna hawa watu wetu watafanya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la elimu ya ujasiriamali na fursa za biashara bado tuko nyuma. Kuna fursa nyingi ambazo vijana wetu na watu wetu wanazo na wanatakiwa kuzifanya, lakini hawajawa exposed. Nadhani ifike wakati sasa Serikali ifanye hatua za makusudi kuendesha training kwenye vijiji, kwenye mitaa, ili mwisho wa siku watu wajue ni vitu gani wanaweza kufanya. Kwa sababu fursa zipo zinawazunguka, lakini watu hawajui wafanye nini na mbinu gani watumie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna Maafisa Biashara kwenye Manispaa zetu, kuna Maafisa Biashara kwenye Halmashauri zetu, lakini tukijaribu kuwauliza Mpango Kazi wao ni upi? Walio wengi wala hawajui. Waulize Maafisa Biashara kwenye Halmashauri zetu, kuna wafanyabiashara wangapi ndani ya Halmashauri? Hawezi kukupa takwimu. Kwa hiyo, hili nalo ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ifike mahali Serikali lazima itambue ina wafanyabiashara wangapi? Hata tunapozungumza kwamba kuna mfumo ule PPP maana yake nini? Kwa sababu kuna watu wengine hawajui. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, maana yake kwanza tutawatambua wafanyabiashara na mwisho wa siku ni kwamba hata unapoamua kupanga kodi, unapanga kodi kwa watu ambao unawafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la viwanda. Kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 52, umezungumzia mradi wa kasi mpya wa kuzalisha chuma ghafi. Mara nyingi huwa napata shida, pale unapozunguza kwamba utatekelezwa halafu usiseme utatekelezwa lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ndiyo tupo kwenye bajeti ya kwanza ya utekelezaji wa miaka mitano kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Naamini unapozungumza mradi, lazima uwe na mahali pa kuanzia na mahali ambapo panatakiwa kuishia. Kwa sababu ukiileta statement too general unakuwa hujatupa tool ya sisi kuku-assess wewe, kwa sababu hata mwakani tukija, utasema hivi hivi, kwamba mradi huu utatekelezwa na Kampuni ya Maganga Matitu Resources Development. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifike mahali sasa unapozungumza mradi, hata kama utataka kuutekeleza mwaka 2018, mentioned, kwamba mradi huu utatekelezwa muda fulani na unatarajia labda kwisha muda fulani, hivyo tutakwenda vizuri. Kitu chochote unachokiita ni project lazima kiwe na mwanzo na lazima kiwe na mwisho. That is a project. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini statement zisiwe too general. Leo hii unasema unatekeleza mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma kuendeleza utekelezaji wa mradi unganishi wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga, kwenye ukurasa wako wa 161. Chuma cha Liganga tumeshaanza kukisikia toka 1906, kwa hiyo, ni kabla hatujazaliwa na inawezekana hata kabla babu zetu wengine hawajazaliwa. Kwa hiyo, ifike kipindi sasa Serikali iseme, wakati tunauliza swali hili kwenye Wizara ya Madini walituambia kwamba fidia itaanza kulipwa mwezi Juni, mwaka 2016 na mradi utaanza mwezi Machi, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa natarajia kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ange-mention hii kitu, kwamba mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga utaanza Machi, 2017 kama swali lilivyokuwa limejibiwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini ili tuwe tunakwenda kwa takwimu. Kwa sababu usipotoa takwimu na muda (time frame) maana yake hatutaweza kuku-assess na kuku- pin.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii Serikali tumeshazungumza kwamba ni Serikali ya viwanda na tunatarajia kwamba tutaenda kwa kasi kubwa. Natamani kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, aseme kinaga ubaga, kwamba tutaanza muda fulani ili tutakapokuja hapa mwakani tuwe na maswali ya kumuuliza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, hivi viwanda vya kimkakati kwa sababu ameshasema ni National Flagship Project, haitakiwi kuwa na majibu general. Leo hii watu hawajaandaliwa kwa maana hii miradi itahitaji support. Licha ya ukubwa wa hivi viwanda vinavyokuja kule, nilikuwa natarajia kwamba Mheshimiwa Waziri angesema, kwa sababu makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga inaanza, kutakuwa na vitu vya ku-support patakuwa na SIDO; hawa watu tuwaandalie uwezo wa kiufundi ili mwisho wa siku waweze kuji-engage kwenye zile bidhaa au kazi zitakazofanyika na hiyo miradi mikubwa inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunavyozungumza hakuna barabara ya lami inayoelekea huko. Wimbo huu umekuwa ukiimbwa muda mrefu na hata marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe alikuwa akiizungumzia kwa kasi sana hii kitu. Mungu amlaze mahali pema peponi. Haijafanyiwa kitu chochote! Kwa hiyo, tuombe kwamba hivi vitu vingine lazima viwe na support ya sekta nyingine ili kuhakikisha kwamba hili gurudumu linakwenda. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuongea tena katika Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja zangu zinajikita katika maeneo machache sana kama mawili hivi au matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kabisa ni juu ya flagship project, makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma Liganga. Kwa hiyo, tunapozungumza ni flagship project maana yake ni project ambazo zinatiliwa mkazo kwa kiasi kikubwa ili kuweza kuifanya nchi isonge mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, najikita kwanza kwenye fidia. Mradi hauwezi ukaanza kabla fidia haijalipwa na katika valuation ya ulipaji wa fidia, tunaona ripoti inasema wananchi wale wa Ludewa kwa maana ya Chuma na Liganga wanatakiwa walipwe shilingi bilioni 14. Hapo hapo nikijaribu kuangalia bajeti iliyokuwa imepangwa na Wizara hasa Wizara ya Viwanda inaonyesha ni shilingi bilioni 10.
Sasa nakuja kujiuliza swali la msingi, hii shilingi bilioni nne iko wapi? Kwa sababu katika majibu ya awali ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, pindi nilipokuwa nimeuliza swali tarehe 19 Aprili, tuliambiwa kwamba fidia inalipwa mwezi Juni, mwaka 2016. Kwa sasa tumebakiwa na muda mchache sana kuifikia Juni. Tumebakiwa na kama siku kumi au kumi na moja Juni hiyo ifike.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu tulishawaaminisha Wanaludewa kwamba tunalipa hiyo fidia na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri akasema miradi hiyo itaanza mwezi Machi, 2017, nikiwa namaanisha kwamba fidia hizo zitakuwa tayari zimeshalipwa, lakini bado napata utata mmoja, kwenye strategic plan. Kwa sababu naamini nilivyokuwa nimejibiwa kwamba hizi fidia zitalipwa mwezi Juni na mradi ule unaanza 2017 mwezi Machi, naamini kwamba ningeona kwenye ripoti. Ripoti ingesema kwamba mradi huu unaanza Machi, 2017 ili kutengeneza assurance. Tusipozungumza hivyo, bado mwakani tutakuja na hadithi hizi. Hatutaweza kum-pin Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu ni moja tu, tunapozungumzia project, project ina time frame. Kwa hiyo, mwisho wa siku ni lazima utueleze mkakati wako na namna utakavyoanza na maadam umeshatu-assure kwamba mwezi Juni, 2016 unalipa fidia, watu wa Liganga na Mchuchuma na Mradi unaanza mwezi Machi, 2017, kwa hiyo, ipo kwenye plan yako. Hiyo plan inapaswa na sisi tuifahamu. Bila hivyo, nasi inatupa matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Mchuchuma, kwa mujibu wa wataalam na Wizara unatarajia kutupa umeme wa megawatt 600, kwa maana ya hii Mchuchuma coal. Kwa hiyo, naamini kuna haja sasa ya kutengeneza nguvu ya kutosha, huu umeme tuufanyie kazi ili uweze kuongeza kwenye pato la nchi, ili twende kwenye uchumi wa viwanda ambao tunautaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachojua, kwenye flagship project kama hii, kuna maeneo mtambuka; kuna suala la VETA. Suala hili la VETA lilizungumzwa sana na hata kipindi hicho Hayati mtangulizi wangu, Marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe, Mungu amweke mahali pema peponi, alilizungumza kwa kasi, aliliuliza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na majibu nakumbuka yalitolewa na Mheshimiwa Mhagama kwamba feasibility study ilishafanyika, michoro ilishakuwa tayari, hati ipo na inatakiwa kuanza kujengwa. Kwa maana ya kuwaandaa vijana kushiriki kwenye mazoezi maalum kwa maana ya kazi na mambo mengineyo ambayo yatakuwepo katika hiyo miradi ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijaribu kuangalia documents zetu ambazo sisi Wabunge tumepewa, hiki Chuo sasa hakipo kabisa. Kwa hiyo, inamaanisha kwamba hatuna maandalizi ya kutosha kwa sababu ile VETA ilivyokuwa imewekwa pale, ilikuwa ni kuwaandaa watu katika kazi za ufundi ili ku-support operations ambazo zinakwenda kufanyika ndani ya miradi hii mikubwa inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii shughuli ni mtambuka na inashirikisha vitu vingi, naiomba Wizara ya Madini, Viwanda na hata na Wizara ya Elimu ambayo inashughulika na mambo ya ufundi, tukae pamoja kuhakikisha kwamba miradi hii wakati inaanza, basi tuanze vile vile maandalizi ya ujenzi wa VETA. Kwa sababu ni kitu cha muhimu na bahati nzuri Bunge lako Tukufu lilishaelezwa kwamba kile chuo kitajengwa. Kama hakitajengwa, lazima tupewe sababu za msingi, zimeyeyukia wapi? Kwa nini hakijengwi? Kwa sababu tulishawaaminisha watu VETA ilishaenda mpaka Shaurimoyo kwa ajili ya kutayarisha eneo; eneo walipata limepimwa hati ipo, michoro ipo na BOQ zote zipo, kwa nini hiki chuo kisijengwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo, kwa kweli tunapaswa tulifuatilie na madamu kwa sababu Serikali ilishasema na sababu za kujengwa zilikuwepo, naamini zile sababu hazijakwisha, bado zipo, kwa hiyo, kijengwe ili tuweze kutoa mafunzo kwa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la Maganga Matitu Resources. Suala hili la Maganga Matitu Resources, hawa wako kwenye partnership na NCD.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa katika mipango ya uanzaji wa miradi ya Mchuchuma wa makaa ya mawe na Liganga chuma. Wizara ya Nishati na Madini tarehe 19/4/2016 ilijibu kuwa fidia ya kulipa wananchi itafanywa mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe fidia hii ilipaswa kulipwa mwezi Februari 2016. Wizara ya Viwanda na Biashara imetenga sh. 5,000,000,000 Liganga na kwa Mchuchuma sh. 5,000,000,000 kiasi kilichopangwa ni sh. 10,000,000,000 ambacho ni kidogo ukilinganisha na fidia ya sh. 14,000,000,000. Naomba maelezo pesa nyingine ambazo ni pungufu zitapatikanaje ili ziweze kulipwa katika kipindi kifupi kilichobaki cha Juni, 2016.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi naomba moja
kwa moja nijikite kwenye Wizara ya Miundombinu. Ikumbukwe kuwa Wilaya yetu ya Ludewa,
eneo kubwa liko mpakani mwa Malawi. Tanzania imepakana na Malawi, lakini eneo kubwa la
mpaka ni eneo la Wilaya ya Ludewa, ukilinganisha na Wilaya za Kyela na Nyasa. Lakini mpaka
sasa ninavyozungumza, eneo lile halina mawasiliano ya barabara, katika eneo la tarafa ile ya
mwambao ambayo ina kata tano na vijiji 15 vilivyoongozana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuna kipindi palitokea mgogoro, sasa mimi nikawa
najiuliza maswali, hivi mgogoro ule ungeendelea wakati hatuna barabara ya uhakika hali
ingekuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kukwambia na niiambie na Wizara wananchi wale
kwa sababu ya kuchoshwa kwa kutokuwa na barabara wameamua kuanza kulima wenyewe
kwa kutumia jembe la mkono. Wanalima kwa sururu, wanalima kwa jembe, wanalima kwa
chepe na mitarimbo. Ile ni dhamira ya dhati kabisa kuionesha Serikali kwamba wale watu wana
uhitaji wa hicho kitu. Vile vijiji vyote tumepangana, tunalima kwa jembe la mkono. Sasa niiombe
Serikali iwa-support wale watu na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri niliwaonesha
hata clips za watu wakiwa wanalima kwa jembe la mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, usafiri mkubwa tunaoutegemea ni usafiri wa maboti, kwa
sababu meli inaweza ikapita mara moja kwa mwezi na isitoshe lile Ziwa huwa linachafuka sana,
kwa hiyo, inafikia kipindi usafiri unakosekana kabisa. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba sasa
ichukue hatua kwa sababu wenzetu wa Nyasa wanayo barabara inayopita kando kando ya
Ziwa; wenzetu wa Kyela, wanayo barabara inayopita kando kando ya Ziwa. Kwa hiyo,
tuwaombe sasa na sisi upande wa Ludewa tuwe na barabara ambayo inaunganisha, kwanza
itakuza utalii, halafu pili italeta maendeleo kwa sababu kuna mazao kule ya uvuvi ambayo
yanapatikana kwa wingi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia eneo lile halina mawasiliano ya simu kabisa. Mimi
ninaamini katika nchi nane tulizopakana nazo, eneo ambalo halina mtandao wa mawasiliano
ya simu inawezekana ikawa ni mwambao wa Ziwa Nyasa. Tuna kata tano, tuna vijiji 15 halafu
viko mpakani. Sasa cha kushangaza tumekuwa tukifatilia hii kitu sijajua tatizo liko wapi lakini
ningependa tu niseme watu wa Ludewa nao wangependa kuwa na maendeleo, wangependa
kuwa na mawasiliano ya simu maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu bandari. Pamoja na kuwa wakati mwingine
meli ile inatembea mara moja kwa mwezi, lakini bado bandari zake ziko kwenye umbali mrefu
sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa zoezi zima la uwezeshaji vituo vya afya kuweza kutoa huduma za upasuaji, jengo la mama na mtoto na maabara. Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa wazee, akina mama na watoto kutembea umbali mrefu kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ludewa tunashukuru kwa kupewa shilingi milioni 500 kwa Kituo cha Afya Mlangali na shilingi milioni 400 kwa Kituo cha Afya Manda na madawa shilingi milioni 300. Kwa sasa Wilaya ya Ludewa kupitia nguvu za wananchi na wadau mbalimbali tunajenga vituo vya afya 17 ambavyo tunaweza kujenga mpaka ngazi ya uezekaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tunaiomba Serikali kuunga mkono jitihada za wananchi katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2015-2020) katika ngazi ya umaliziaji majengo hayo pamoja na zahanati 22 zinazojengwa katika vijiji mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tatizo la dawa limekuwa ni sugu katika baadhi ya zahanati bila kusahau watumishi katika zahanati na vituo vya afya. Ikumbukwe jiografia ya Halmashauri ya Ludewa kimiundombinu si mizuri kwani tuna vijiji 15 havifikiki kwa mawasiliano ya barabara yaani huko vilipo vijiji hivyo havijawahi ona gari toka kuumbwa kwa ulimwengu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa inaomba kupatiwa magari (ambulance) walau mawili ili kutoa huduma ya usafiri pindi itokeapo dharura ya mgonjwa anapozidiwa na anapopewa rufaa kwani miundombinu ni mbali toka sehemu moja kwenda nyingine ukizingatia hakuna huduma ya mawasiliano kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nijaribu kujadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Moja kwa moja nijikite juu ya suala la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Liganga na Mchuchuma ni suala ambalo hata tafiti zake zimefanyika toka mwaka 1929. Serikali imekuwa ikilizungumzia suala hili kwa miaka chungu nzima, lakini tulijaribu kupata faraja hasa sisi watu wa Ludewa pale tulipoambiwa kwamba miradi hii inaanza. Ikumbukwe katika Bunge lako Tukufu niliuliza swali tarehe 19/4 juu ya fidia kwa wale ambao wamepisha hii miradi kufanyika. Tulijibiwa kwamba Juni ndugu zetu wale wa Ludewa wangeweza kulipwa fidia yao na vilevile Bunge liliambiwa mradi ule ungeweza kuanza Machi, 2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ludewa waliaminishwa na sasa wanapiga kelele sana juu ya hili. Nipende tu kutoa taarifa katika Bunge lako kwamba hawa watu wanajiandaa kuja Dodoma kujua hatma yao. Vinginevyo waruhusiwe yale maeneo waliyopisha kwa sababu ni maeneo ya kilimo na ndiyo wanayoyategemea waendelee na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango Mheshimiwa Waziri anazungumzia sana hili suala la Liganga na Mchuchuma, lakini jinsi ninavyoiona ni kwamba, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Mpango unazungumza hapa kwamba mradi wa umeme wa megawatt 600 unaendelea, sasa najiuliza unaendelea wapi? Mimi sijaona kitu chochote kinachoendelea pale Mchuchuma. Hakuna kitu kama hicho! Labda Mheshimiwa Waziri aje atueleze na alithibitishie Taifa kwamba nini kinachoendelea kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa juu ya Power Purchase Agreement ndiyo inayosumbua, lakini mpaka sasa hatujui fate yake na mradi utaanza lini? Je, coordination ipoje kati ya Wizara na Wizara na kati ya Waziri na Waziri? Huyu anasema fidia italipwa Juni, sasa hivi tokea Juni ni miezi minne imeshapita hakuna fidia na wala hakuna tamko la Serikali linalosema kitu chochote juu ya fidia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapotuaminisha kwenye Bunge sisi tunaenda kuwaambia wananchi Serikali imesema moja, mbili, tatu, nne; sasa leo hii nikienda kule mimi ndiyo ninayeonekana mwongo! Sasa suala la mimi kuonekana mwongo haiwezekani, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na tamko ili tulichukue na kulipeleka kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nijikite kwenye miundombinu. Leo hii tunasubiri suala la standard gauge kwa reli ya kati, tunaowategemea kuja kufanya hii kazi ni Wachina. Leo hii kitu kidogo kabisa cha Liganga na Mchuchuma tunakaa tukiyumbishana kwa suala la Power Purchase Agreement. Ninachofahamu mkataba huu siyo wa jana wala sio wa juzi, lazima kuwepo na continuity, walipoishia wenzetu sisi tuendelee. Kama pana tatizo basi tujue kwamba hili ni tatizo la msingi na tupeane maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tukiwafuatilia Mawaziri wetu hawana majibu na tunarushiana mpira. Ukienda kwa Waziri wa Madini anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Viwanda anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Fedha anazungumza hivi, inafika wakati tunakata tamaa juu ya suala hili. Waziri alikuja Mchuchuma Januari na alikuwa anazungumzia hili, sasa haya mazungumzo yanachukua muda gani, lazima tuwe na time frame! Ifike mahali tuseme itakapofika tarehe hii basi hii kazi iwe imekwisha, hapo tutakuwa tunaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya miundombinu. Kule kwetu Ludewa tumepakana na nchi ya Malawi, kuna eneo la kilometa zinazokadiriwa kuwa 200, eneo hilo halina miundombinu ya barabara hata moja na hilo ni eneo la mpakani. Nakumbuka juzi juzi hapa wenzetu walikuwa wana-demand lile ziwa na pakawa na kitu kama mgogoro. Sasa najiuliza, eneo la mpakani lenye urefu wa kilometa 200 halina miundombinu ya barabara, halina mawasiliano ya simu, hakuna umeme, je, likitokea la kutokea defense yetu ipoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kulieleza Bunge lako, wananchi kule wameamua kuchukua hatua kulima barabara kwa mikono. Tumeshalima kilometa 40 kwa jembe la mikono na sururu. Sasa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kiulinzi na kiusalama na kiutalii Mheshimiwa Waziri aliweke kwenye mpango. Ziwa letu lina matatizo makubwa. Hivi ninavyozungumza wiki iliyopita watu watatu wamefariki kwa sababu ya usafiri na huwa linachafuka halitoi taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuchukua fursa hii kuomba Serikali iwasaidie wale watu ambao wameamua bila kulipwa kulima barabara kwa kutumia mikono yao. Eneo la Ziwa Nyasa, eneo kubwa ni eneo la Ludewa kuliko Kyela, Mbinga na Nyasa. Kwa hiyo ni lazima hawa watu tuwape kipaumbele. Tuna vijiji vinavyokadiriwa 20 hakuna mawasiliano ya simu kabisa yaani ukishazama huko umeshazama, taarifa zako huwezi kuzipata. Kwa hiyo, ifike kipindi watu hawa tuwaonee huruma na Serikali itu-support kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu, mpaka sasa Ludewa ina deficit ya Walimu 521 lakini tunapangiwa Walimu 40. Tumejaribu kulipeleka kwenye Idara na Wizara husika watusaidie. Sasa Mheshimiwa Mpango aliweke kwenye mpango wake kwamba Ludewa tuna uhaba wa Walimu na hata ukiangalia performance imeshuka sana kwa sababu hiyo. Kuna shule kama nane (8) hivi zina Walimu wawili au watatu, maximum ni Walimu wanne na tuna shule za misingi 108. Kwa hiyo, hivi vitu ni lazima tuviweke kwenye mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la afya, kweli Ilani ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia vituo vya afya kila kata na pia inazungumzia zahanati kila kijiji. Labda tuzungumze sasa hapa wajibu wetu sisi kama Wabunge ni nini? Wabunge ni wahamasishaji wa maendeleo na vilevile tuna wajibu wa kukusanya nguvu na ku-mobilize watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, najikita moja kwa moja kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Ikumbukwe katika Bunge lako tarehe 19 mwezi wa Nne niliuliza swali Liganga na Mchuchuma, fidia kwa waliopisha maeneo itakuwa ni lini? Nikajibiwa kwamba italipwa mwezi Juni, 2016. Pia Bunge lako lilitaarifiwa kwamba Mradi wa Liganga na Mchuchuma ungeweza kuanza mwezi Machi, 2017. Sasa kitu ambacho nakiona ni kwamba, Serikali haina dhamira ya dhati juu ya Mradi wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kufuatilia maelezo ya Mheshimiwa Waziri, naomba ninukuu kwa kusoma, Mheshimiwa Waziri anasema:-

“Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2016/ 2017 Wizara kupitia NDC iliendelea na majadiliano juu ya mauziano ya umeme kati ya Shirika la Umeme TANESCO na kampuni ubia. Mfumo uliokubalika na pande zote mbili ni mwekezaji kujenga mtambo wa kufua umeme, kumiliki na kuendesha, (build, own and operate). Mauzo ya umeme kwa TANESCO hayajumuishi gharama za uwekezaji kuhusu ujenzi wa mradi. Kamati ya Taifa ya uwekezaji imepitia kwa mara nyingine vivutio vilivyoombwa na mwekezaji kwa lengo la kutafuta manufaa zaidi kwa Taifa katika mradi huo”.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mradi wa Liganga na Mchuchuma umewekwa kama ni mradi kielelezo (flagship project). Hata hivyo, kitu ambacho nakuja kukiona hapa inaonekana kwamba hakuna master plan ya mradi huu kuanza. Leo hii tunauzungumzia hata fidia haijalipwa, wakati mwekezaji anasema tayari ana hela za kulipa, lakini sisi kama Serikali yenyewe inazungumza kwamba bado wanaendelea na mazungumzo juu ya power purchase agreement kati ya mbia na TANESCO. Sasa najiuliza pana tatizo gani? Kwa sababu tungepewa schedule of activities mpaka mradi ku- take over, lakini leo hii bado tunazungumzia kwamba tunaendelea na majadiliano sasa tujiulize haya majadiliano yataendelea mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia Wizara hii mwaka wa jana tulizungumza kwamba tungepewa road map. Ifike mahali kwamba tujue kwamba mwezi huu mpaka mwezi huu, mwaka huu mpaka mwaka huu activity fulani inafanyika ili tuweze kujua kwamba itakapofika muda fulani mradi huu uwe ume-take over. Hiyo tulikuwa tunaizungumza hivyo kwa maana ya tuweze kum-pin mtu ambaye anatuletea shida hapa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kama tunaamua kuzungumzia tu kwamba tutaendelea tu na majadiliano itafika 2020 huu mradi haujaanza, fidia haijalipwa, hayo makubaliano ya TANESCO hayapo, hizo incentives ili Serikali ije itoe GN haziatakuwepo. Kwa hiyo, napenda kusikitika kwamba huu mradi hatujauwekea kipaumbele. Inawezekana zipo incentives ambazo zinatakiwa na mwekezaji lakini vile vile lazima tuangalie multiplier effect ya mradi wenyewe upoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaleta ajira 33,000, hiyo hatujaiangalia, lakini tunaangalia zile taxation tu za mwanzo. Ifike mahali; kwa sababu Baraza la Uwekezaji Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, kwa hiyo, maana yake huu mradi unafahamika vizuri. Kama kuna shida basi tujue kwamba huu mradi haufanyiki ili watu waendelee na mambo mengine. Leo hii ndugu zetu wa Ludewa kule wamepisha mradi lakini fidia hawana, maeneo yale yanashindwa kuendelezwa, yanashindwa kulimwa, lakini hakuna tamko lolote la Serikali ambalo linawapelekea sasa wananchi wale wafanye nini. Mwekezaji anasema hela anayo, kama hela ya mwekezaji inaleta shida, basi Serikali ingebeba jukumu la kulipa fidia huku ikiendelea na hayo mazungumzo ili iwafanye wale watu waendelee na shughuli nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia licha ya ajira 33, 000 zitakazokuwa zimeletwa na mradi huu, tunatarajia kwamba huu mradi ungeweza kuleta population ya watu wasiopungua laki tatu ndani ya eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuja kwa mradi huu maana yake ungeweza kuanzisha viwanda vingine kwa ajili ya kuweka value addition ya mazao yanayolimwa na mikoa na wilaya jirani. Hata hivyo, inaonesha ni kwamba Serikali yenyewe ime-base tu kwenye maeneo machache, kitu ambacho na chenyewe si sawa kiuchumi. Ifike mahali kwamba hiyo tax kwa mfano tukii-wave, kuna impact nyingine kwa jamii kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza kwamba huu mradi haupewi kipaumbele kwa sababu pia unakuta hata ile miundombinu yenyewe haijawekwa. Leo hii tuna barabara inayoenda kwenye chuma cha Liganga, barabara ya kutoka Mkiu kuelekea Madaba, mpaka leo hii tunaambiwa tunafanya rehabilitation hakuna utaratibu wowote kusema inaingia kwenye upembuzi yakinifu, iende kwenye usanifu wa kina, barabara zijengwe ili kwenda kwenye huo mradi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nchi inazungumza haina chuma, lakini chuma kimelala pale Liganga, leo chuma tunaagiza. Kwa hiyo ikifika mahali unakuta sasa hivi vitu vinasuasua. Tumezungumzia juu ya Reli ya Mtwara kuja Mbamba Bay kutoka Mbamba Bay inakuja Mchuchuma inakwenda Liganga; sijajua utaratibu ukoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unaweza kuona kwamba Serikali na yenyewe inakwepa. Kama tatizo ni mwekezaji, basi ifute huo utaratibu ili tujue kwamba huu mradi haupo tunatafuta mwekezaji mwingine ili tuweze ku- move, kwa sababu haiwezekani miaka mitano, sita tunazungumzia Liganga tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Liganga kwa mara ya kwanza imezungumziwa mwaka 1929. Sasa mwaka1929 mpaka leo tunazungumza tu Liganga, wazee wetu wanakufa, watoto wetu wanakufa sisi wote tutaenda tutakufa Liganga itaendelea kubaki palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozunguzia uchumi wa viwanda Tanzania huwezi ukaiondoa chuma cha Liganga na huwezi kuondoa makaa ya mawe Mchuchuma. Makaa ya mawe Mchuchuma yanatoa megawati 600, leo nchi inatumia megawati 1050... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kusimama kwenye Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuchangia mjadala wa Wizara ya Ulinzi na Usalama. Kwanza nilipongeze Jeshi letu kwa kazi ambazo linazifanya, kwa kweli ni kazi zilizotukuka na zinastahili kupewa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite moja kwa moja katika suala la ulinzi na usalama. Mimi natoka Ludewa ambako Ziwa Nyasa lipo na kama kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani kwenye ukurasa wao wa 14 na 15 walizungumzia juu ya mgogoro wa Ziwa Nyasa. Labda tu nipende kuweka vizuri taarifa yao kwamba Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu; limezungukwa na Tanzania, Malawi na Msumbiji. Kwa hiyo, katika hali ya kawaida Malawi hawezi ku-demand eneo la Msumbiji, analo-demand ni eneo la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulinzi na usalama eneo lile ni pana hasa eneo la upande wa Ludewa. Eneo la upande wa Ludewa bado ninaendelea kusisitiza kwamba lina urefu wa kilometa zisizopungua 250 around the shore of the lake, lakini kiusalama na kiulinzi bado limewekwa nyuma. (Makofi) (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukijaribu kuangalia eneo lote hilo lenye urefu huo mkubwa bado hakuna vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vipo huko. Napenda kuchukua tu fursa hii kuliomba jeshi, kuiomba wizara na kumuomba Mheshimiwa Waziri kwamba kuna haja ya kuweka mkakati wa makusudi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumza hivyo? Nazungumza hivyo kwa sababu eneo lile halina mawasiliano ya simu; eneo hilo halina miundombinu ya barabara kwa urefu wote huo niliokua nimeuzungumza. Kwa hiyo basi, ifike mahali sasa kwa sababu ya haya mambo yanayoendelea hapa sasa hivi inakuwa ni ngumu sana incase ikitokea kitu chochote wananchi kuripoti, incase kuchukua kitu chochote, wananchi hata kukimbia basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ikizungumzwa kwamba hapa pana mgogoro na ilifika mahali kipindi kile yanachimbwa mafuta, unakuta ndege ya Malawi inakuja Tanzania na wananchi hawana facilitation yoyote ya kusema kwamba wanaweza wakaripoti. Kwa hiyo, ina maana kuwa kama litatokea janga lolote uwezekano ni mkubwa sana kwenda hayo maeneo na ukakuta kwamba mambo yameshaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napende tu kuisihi Wizara ikiwezekana sasa na kama itakuwa imeruhusu basi kuwepo na vyombo vya kiulinzi ambavyo vina-patrol, angalau kuwepo hata na marine boats ambazo zitakuwa zinazungukia kule kwa ajili ya kuimarisha usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naweza kulizungumzia ni juu ya Uwanja wa Ndege Sagalu, uwanja ule ni wa Jeshi lakini kwa mara ya mwisho inaweza kuwa ni miaka 30 iliyopita, ule uwanja umeshakuwa ni pori. Sasa kwa sababu kuna ujio wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga naamini kabisa facility ya uwanja ni muhimu. Labda twende kuliuliza Jeshi kwamba incase kama utakuwa hauna matumizi kwa sasa, turudishieni Halmashauri ili tuweze kuandaa mazingira ya kufanya kazi nyingine yoyote ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kusema hivyo basi naamini; tuna kambi moja ya Jeshi pale Manda ambayo ipo mpakani kabisa mwa Mto Ruhuhu. Sasa ukiangalia lile eneo lote mpaka unakuja unaigusa Kyela hakuna chombo chochote cha ulinzi, hakuna mawasiliano ya simu na hakuna mawasiliano ya miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, nichukue tu nafasi hii kuishauri Serikali kwamba ipeleke vyombo vya usalama kule angalau basi hata wananchi wafarijike incase kama kitatokea kitu chochote waweze ku- accommodate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ningependa kukizungumzia hapa ni juu ya dhana ya viwanda kwa Jeshi. Ifike mahali sasa Jeshi letu lijiendeshe kisayansi, kwa sababu ninaamini kwamba Jeshi letu lina multi professionals, lina madaktari na ma-engineer. Kwa hiyo nalo lipange mpango mkakati na ifike mahali jeshi lenyewe kama Jeshi lijitegemee na lisiwe inategemea ruzuku tu peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ninaamini kabisa jeshi lina uwezo wa kujiendesha kisasa kama ilivyoanza ule Mradi wa Nyumbu bado unaweza likaanzisha miradi mingine yoyote ambayo inaweza ikaliingizia kipato japo kwamba litaendelea kupata ruzuku kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache mimi niishie hapo, ila napenda tu kwa dhati ya moyo wangu, eneo lile la Ziwa Nyasa sasa hivi lipewe kipaumbele kwani wananchi wameamua kulima barabara wenyewe. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara ya Ulinzi maeneo ambayo ni magumu basi tutakapoomba baruti watuletee, na maeneo ambayo yana madaraja ikiwezekana basi tupate hayo madaraja. Kuna baadhi ya maeneo Jeshi huko nyuma lilishaweka madaraja; sasa bahati nzuri maeneo yale imeshapita barabara yale madaraja yanakuwa sasa hivi ni kama hayana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tungeomba sisi tutakapokuwa tunaomba yale madaraja basi tuletewe kwa ajili ya kufanya facilitation ya wananachi wetu kule ili paweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kutoa shukrani zangu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa mambo yafuatayo ambayo yanafanyika sasa hivi kule Ludewa. Kuna barabara ya lami kutoka Njombe kwenda Ludewa - Manda, umeme wa Gridi ya Taifa ambao unatoka Makambako kwenda Songea unakatisha pale Madaba unakuja Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna miundombinu wezeshi ambayo inaweza ikaifanya chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma kuanza kwa maana ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara za Madaba kwenda Mkiu na barabara kutoka Nkomang’ombe kuelekea Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo kuna baadhi ya mambo ambayo napenda kuyaelezea kidogo hasa kuhusu makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga. Chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma ni miradi kielelezo katika Serikali hii ya Awamu ya Tano lakini bado hatujaona mpango ambao unaweza ukaonesha kwamba chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma yanaanza lini. Kwa sababu hii project, project inatakiwa iwe na mwanzo pia iwe na mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijaweka ule utaratibu mzuri wa kusema kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, mwaka huu tunafanya kitu hiki, mwaka wa pili hiki, mwaka wa tatu mpaka ule wa tano. Kwa hiyo, statement ambayo inakuja ni statement ya jumla sana kiasi ambacho sasa hata ku-access huu mpango ambao ni mradi kielelezo cha Taifa inakuwa ni mgumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa Serikali sasa ianishe kwamba kwamba kwa sababu huu leo ni mwaka wa pili unakwisha tunaelekea kwenye mwaka wa tatu, bado hatujaona zile activities ambazo zinatakiwa zifanyike katika huu mradi husika. Tukiweka na kuainisha maana yake tutakuwa tumeweka vizuri kiasi ambacho unaweza sasa kufanya tathmini kwamba mwaka huu tunafanya hiki, mwaka wa pili tunafanya hiki na hata kama tunakwama sehemu tunakuwa tunajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hilo ningependa tu Serikali ije na ile mipango kwa sababu kuna eneo pale ambalo wananchi wetu wamepisha mpaka leo bado hawajalipwa fidia na wala hatujui fidia ile italipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mpango ambao tumesema kuna Power Purchase Agreement, ni kweli tunapata maelezo lakini hatujui kwamba sasa hiyo Power Purchase Agreement itakamilika lini kiasi ambacho sasa itapelekea ile Government Notice kutoka. Naamini kwamba hii yote ipo ndani ya uwezo wa Serikali, Serikali ikijipanga haya mambo yanaweza yakaisha na mwisho wa siku hata hawa watu ambao wamepisha ile miradi kwa sababu yale maeneo waliyoyapisha ni makubwa kiasi ambacho sasa wanashindwa kufanya kitu chochote na hawajui kwamba fidia yao watalipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulichangia ni juu ya suala la zao la mahindi. Nyanda za Juu Kusini ambako Ludewa ipo, zao la mahindi ni zao la biashara. Kwa wengine wanaweza wakasema kwamba ni zao la chakula, lakini hakuna zao kubwa na muhimu ambalo linatiliwa nguvu kubwa na wananchi wetu kama zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba tunapolima mahindi yanapotosheleza kwa chakula, mengine yanayosalia ndiyo ambayo yanaenda kwenye biashara ambazo zinawafanya watu wetu walipe ada, wajenge nyumba na wafanye maendeleo yao mengine. Kipindi cha sasa wananchi wetu wame-stuck na walikuwa wanaitegemea Serikali kwa kiasi kikubwa kununua yale mahindi, sasa hivi mahindi hayanunuliwi na mwisho wa siku sasa inabaki kwamba uchumi wa wananchi mmoja mmoja na uchumi wa maeneo husika unabaki ku-stuck.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba mahindi yale ambayo wakulima tuliwahamasisha walime kwa kiasi kikubwa basi yanunuliwe sasa. Hali ni ngumu kwa wananchi wetu kule na tunaulizwa maswali mengi sana na bahati mbaya zaidi sasa hivi Serikali imezuia kuuza haya mahindi kwenye maeneo mengine. Tunaweza tukasema hivyo kwa sababu kuzuia kwake hatujapewa sasa altelnative kama lipo soko la ndani basi soko hilo lipo wapi ili mwisho wa siku hawa watu wetu waweze kuuza mahindi yao ili tupate faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya suala la maji. Maeneo ya kusini kuna ufadhili mkubwa sana ambao wananchi au Serikali inapata kutoka kwa donor funded. Kwa hiyo, katika ufadhili huo kuna sehemu ambayo Serikali inatakiwa ichangie, tunajikuta sasa kuna miradi mingi, kuna proposal nyingi tunaziandika lakini inapofika sasa kuchangia Serikali tunakwama sana na wale wafadhili wanatupa support ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sasa Serikali pindi tunapokuwa tunaleta kwenye meza zenu kwa wataalam na kwenye mamlaka husika, basi tupewe ushirikiano wa kutosha ili tuweze kutatua hili tatizo la maji kwa sababu hawa wadau wana-support kwa kiasi kikubwa ili mwisho wa siku matatizo na kero za maji ziweze kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi wa viwanda maana yake ni lazima twende kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo. Sasa kitendo cha kutokununua mazao ya wakulima au kutokutafuta masoko, uwezekano ni mkubwa sana wa kuona kwamba hatutaweza kufanikiwa kwa kiasi kile ambacho tumekilenga. Hii ni kwa sababu wananchi wanakosa matumaini, wanakata tamaa na mwisho wa siku sasa drop inakuwa kubwa katika kuhakikisha kwamba hawa watu wanaendelea ku-concentrate na ile motivation inakuwa hamna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa Serikali ije na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunatengeneza utaratibu mzuri (platform) ya kuhakikisha kila ambacho kinazalishwa kinakuwa kipo motivated ili mwisho wa siku tuweze kuendelea na kuhamasisha hawa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara kandokando ya Ziwa Nyasa; kule wananchi wamejitolea kwa kiasi kikubwa kulima kwa majembe ya mkono. Kwa hiyo, pindi mara nyingi tunapoomba msaada kwamba hawa watu wasaidiwe kutokana na kero ambayo inawakuta mpaka imefikia kipindi wao wenyewe wanaamua kuchukua uamuzi tuwasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru TASAF; tumelima barabara ya kilometa 28 lakini tunashukuru TASAF kwa kuweza kutu-support na matokeo yake sasa tunatumia zana ambazo ni mashine kwa maana ya grader na excavators ili kuhakikisha kwamba tunazipanua hizi. Vilevile katika maeneo mengine ambako wananchi wanajitolea zaidi, tunaomba mkono wa Serikali ufike kwa sababu kero hiyo ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ludewa kuna Vijiji 15 ambavyo havijawahi kuona gari toka kuumbwa kwa ulimwengu. Sasa imefikia wananchi wameamua sasa kushika majembe na sululu ili waweze kupata hizo barabara. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwenye maeneo kama hayo tunapokuja kuomba msaada kwa sababu ile ni kazi ya Serikali na wananchi basi tushirikiane na wananchi hawa kuwatia moyo kuhakikisha kwamba haya malengo yanakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo nalizungumza ni lile eneo ambalo ni kando kando ya Ziwa Nyasa ambalo ni mpakani mwa Malawi na Tanzania, ni eneo muhimu kiulinzi na kiusalama. Kwa hiyo, wananchi wanapochukua hatua hizo tunaamini kwamba Serikali ije nayo ituunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuishukuru Serikali lile eneo la mwambao wa Ziwa Nyasa ambalo ni eneo kubwa kuliko eneo lingine lolote, tulikuwa hatuna mtandao wa mawasiliano ya simu; tunaishukuru Serikali sasa hivi angalau asilimia 75 ya eneo hilo sasa kuna mtandao wa simu. Nipongeze na niweze kuishukuru kwa hayo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono mapendekezo. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kujadili hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Kwanza, nipende kumpongeza Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Profesa

Mbarawa, niwapongeze Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Injinia Nditiye na ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema Wizara inafanya kazi yake ipasavyo japo kuna upungufu kwenye maeneo mbalimbali. Nianze na barabara ya Itoni – Ludewa – Manda. Tukumbuke kwamba barabara hii inaenda kwenye ile miradi yetu ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma na ina kilometa 211 lakini mpaka sasa inajengwa kilometa 50 na ujenzi wake unaenda kwa kusuasua sana. Kwa hiyo, niwaombe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla wake waongeze nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna barabara ya Mkiu – Madaba na Mchuchuma – Liganga. Barabara hizi sasa hivi zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri na timu yake waanze kuiweka kwenye ule mpango sasa wa kujengwa kwa lami kwa sababu inaenda kwenye ile miradi kielelezo, miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara kupitia chombo chao kinachoitwa Tanzania Road Fund. Kwa kweli, kinafanya kazi nzuri na tumejaribu kuwa tunawasiliana nao kwa kina na hivi ninavyozungumza kule kwetu Ludewa tuna vijiji 15 ambavyo havijawahi kuona gari wala baiskeli lakini Wizara imekuwa sikivu kupitia mfuko huu. Leo hii tumeshapata fedha kidogo ambapo tunaanza kufungua angalau vijiji viwili, vitatu katika kipindi kijacho kifupi. Kwa hiyo, napenda kuwapongeza lakini tuendelee kuitia moyo Wizara iwakumbuke sana watu wa kule Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara inayotoka Lupingu - Matema. Barabara hi inapita mpakani mwa nchi na ina kilometa zipatazo 139 lakini haipitiki. Ndiyo maana sasa tunasema ifike mahali eneo la mpaka ni lazima tuwe na barabara na tuiombe sasa Wizara iingize kwenye mpango ili angalau mwisho wa siku tuweze kuwahakikishia usalama, ulinzi na kuongeza utalii kwenye lile eneo. Tuna ziwa letu zuri linalopita kwenye Bonde la Ufa, kwa hiyo, kuna haja sasa ifike wakati tutengeneze barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Nditiye, kwa mara ya kwanza amefika Ludewa na amezungukia vijiji 15. Moja kati ya vijiji ni hivyo ambavyo havijawahi kupata barabara. Ziara yake imekuwa na tija, leo hii tunajengewa minara nane ya mawasiliano kupitia effectiveness ya ile ziara yake. Leo hii tunapata angalau vituo vya kupakia na kushusha abiria vipatavyo vitano kupitia ile ziara yake. Kwa hiyo, nimshukuru na ikiwezekana aendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nipende kukwambia wewe na Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Nditiye amepewa Uchifu kule kwa sababu ya ile ziara tu iliyopita. Watu wameona jitihada za Serikali hii na wameona kwamba Naibu Waziri anafanya kazi zake nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Serikali kwa ajili ya barabara ambayo tumeipata ya Makonde – Mawenji. Barabara hii ilikuwa haipitiki kabisa lakini leo hii angalau tunaona zinakuja hela kwa ajili ya kuitengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ujenzi wa meli mbili za mizigo ambapo tayari umeshakamilika katika Ziwa Nyasa na kuna ujenzi ambao sasa hivi unakaribia kwisha wa meli za abiria. Kwa hiyo, tuiombe Serikali ifanye jitihada za haraka kwa sababu wale watu wanasumbuka sana usafiri umekuwa haupo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Matangazo ya shirika hili la utangazaji la Taifa hayafiki katika Wilaya ya Ludewa na maeneo mbalimbali ya Ludewa. Hivyo tunaiomba Wizara kuangalia suala hili ili Ludewa ipate matangazo ya TBC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umefika wakati sasa wa kuwa na utaratibu wa mpango wa kujua matangazo ya TBC juu ya uwekaji wake awamu kwa awamu katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hii itaondoa usumbufu wa kuulizauliza lini itakuwa ni zamu ya maeneo fulani na pia kujua TBC itachukua muda gani kufika nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vazi la Taifa. Kuna mchakato ulianza wa Vazi la Taifa, lakini mpaka sasa hakuna mwendelezo wowote wa kupatikana kwa vazi hilo. Vazi hilo ni muhimu kwani linaweka utambulisho wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maandalizi ya Timu Zetu katika Mashindano ya Kimataifa. Serikali itenge pesa za kutosha katika maandalizi ya michezo mbalimbali katika fani za mpira wa miguu, pete, wavu na kadhalika kabla ya kwenda katika mashindano mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ajira za Maafisa Michezo na Utamaduni. Serikali haitengi bajeti kwa ajili ya ajira za Maafisa Utamaduni na Michezo katika kuibua aina mbalimbali za michezo. Ukitoa soka na riadha bado tuna michezo mingi sana, ipewe kipaumbele. Kwa mfano volleyball, tennis, basketball, tufe na kadhalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Itoni Njombe – Ludewa -Manda imeanza kujengwa tayari kilometa 50 lakini ujenzi wake unaenda taratibu mno. Ikumbukwe barabara hii inaenda kwenye miradi kielelezi ya Mchuchuma na Liganga. Barabara hii ina vipande vinne vya ujenzi (lots), tunaiomba Serikali kwa umuhimu wa miradi hii tuongezewe kipande kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kandokando ya Ziwa Nyasa - Lupingu- Matema (kilometa 139). Eneo hili ambalo linapakana na nchi ya Malawi halina barabara kabisa na hivyo kufanya vijiji 15 kutokuwa na mawasiliano ya barabara. Hata hivyo, wananchi wameanza jitihada za kulima kwa kutumia zana duni za majembe, nyundo, mitalimbo, mapanga na kadhalika. Hivyo, tunaiomba Serikali kuchangia jitihada za wananchi kwa kutoa fedha kwa mfumo wa Force Account. Eneo hili lina tija kwa nchi, kwani lipo mpakani mwa nchi kwa hiyo lina umuhimu kiutalii, kiulinzi na kiusalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ndiyo pekee katika mpaka wa nchi ambalo halina barabara. Mbamba Bay - Lituli (kilometa 112) barabara ipo, Matema - Ikombe (kilometa 10) barabara ipo lakini eneo hili ambalo ndiyo katikati halina huduma ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ione sasa umuhimu wa kuunda Bodi ya TEHAMA nchini kutokana na kukua kwa teknolojia ya TEHAMA ili kudhibiti mfumuko wa watu wasiozingatia taratibu na kanuni za uendeshaji wa TEHAMA. Imefikia wakati sasa wa kuwa na Bodi ya Wanataaluma ili kutengeneza udhibiti na uendeshaji mzuri. Pia viwango vya elimu katika kada hiyo vizingatiwe ili kuepuka muingiliano na pia vifaa vilivyoisha muda wake viharibiwe ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeanza ujenzi wa minara katika Kata za Lupingu, Makonde, Kilondo na Lumbila. Tunaipongeza Serikali kwa zoezi hilo lakini imenza kazi hiyo katika Kata ya Lupingu, Vijiji vya Nindi na Ntumbati. Zoezi hilo ambalo limeanza katika vijiji hivyo linaenda taratibu mno. Tunaiomba Serikali iongeze msukumo katika ujenzi wa minara hiyo ya mawasiliano ya simu. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Engineer Nditiye kufuatia ziara yake aliyoifanya Jimboni Ludewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuiombe Serikali sasa kutupatia vituo vya kupakia na kushusha mizigo katika vijiji vya Nkwimbili (Yigha), Makonde, Nsele, Chanjale na Nkanda vilivyopo kando kando ya Ziwa Nyasa. Hii ni kutokana na umbali kati ya kijiji na kijiji na pia ndiyo njia pekee ya usafirishaji kwa maeneo hayo na usafirishaji wa mizigo hasa ya kibiashara umekuwa mgumu sana, imefikia wakati sasa wananchi kupitia Serikali kuondoa kero hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la wananchi walioachia maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa bandari kwa vijiji vya Manda na Lupingu katika Wilaya ya Ludewa. Ni lini fidia italipwa na ujenzi wa bandari hizo utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Shirika la Posta Tanzania, Serikali imekuwa ikilipa shirika hili mzigo wa kuwalipa pensheni wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta la Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupelekea shirika kuyumba katika uendeshaji. Mpaka sasa Serikali inadaiwa shilingi bilioni 4.7. Hali hii inaliyumbisha shirika kwa kiasi kikubwa. Je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa kuondoa kero hii kwani inafifisha uendeshaji wa shirika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TTCL, natoa wito kwa Serikali kulipa uwezeshaji shirika ili liweze kutengeneza mtandao mpana wa kimawasiliano nchini. Aidha, shirika hili lipewe nguvu za ushindani katika soko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Bonde la Mto Ruhuhu; mwaka 2016/2017 kuliwekwa lengo la ujenzi wa bwawa la umwagiliaji katika Bonde la Mto Ruhuhu ambalo linalounganisha Wilaya za Ludewa na Nyasa. Cha kushangaza bajeti ya mwaka 2017/2018 na mwaka 2018/2019 haijawekwa kabisa. Sasa ningeomba Serikali inipe ufafanuzi kuna tatizo gani lililotokea mpaka likaondolewa kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019 na hata kwa mwaka uliowekwa tengo hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Bonde la Umwagiliaji Lifua, tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kwa ajili ya Skimu ya Umwagiliaji ya Lifua ambayo kilimo cha mpunga kinastawi sana. Skimu hiyo imekamilika kwa asilimia 75. Tungeomba sasa Serikali itupe asilimia 25 zilizobaki ili tukamilishe kwa kiasi cha asilimia 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uchimbaji wa visima katika vijiji vya Tarafa ya Masasi, kufuatia uwekwaji wa umeme wa REA katika vijiji vya Tarafa ya Masasi yaani Iwela, Kimetembe, Nkomang’ombe, Luilo, Lifua, Kipangala, Kingole, Lihagule, Kiyogo, Manda, Igalu, Mbongo, Ilela, Ngelenge, Kipingu na Kipangala, tukichimba visima hivyo walau vitatu kila kijiji nina imani kwa kushirikiana na wananchi, tutatatua tatizo la maji kwa asilimia kubwa katika tarafa hii. Nina imani tukiweka mpango kazi tatizo hili litaisha katika maeneo haya ambayo water table ipo jirani sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya maji katika Wilaya ya Ludewa; kumekuwa na tatizo kubwa kwa wakandarasi wengi wa maji kutolipwa mapema pindi wanapowasilisha certificates zao Wizarani kwa malipo ili kazi iendelee. Inachukua muda mrefu sana toka wawasilishe certificates na malipo jambo linalopelekea miradi mingi kuchelewa na kukwama. Hii inapelekea hata lengo la pesa iliyo katika bajeti kubaki huku miradi ikiwa bado haijamilika. Kuna haja ya kuangalia namna nzuri ya malipo na ikiwezekana tutumie mfumo wa force account ambao umeleta ufanisi mkubwa katika miradi ya ujenzi hasa wa vituo vya afya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakupongeza kwa kunipa fursa ya kuweza kujadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa napenda tu kuzungumzia suala la Mchuchuma na Liganga. Suala hili limekuwa likizungumzwa muda mrefu sana. Huu mfupa umekuwa mkubwa na mgumu. Liganga na Mchuchuma imeanza kuzungumzwa toka mwaka 1929 kipindi cha Mkoloni. Mkoloni alishindwa na hizi Serikali nyingine zote zimekuwa zinaweka mipango lakini ni mipango ambayo kwa kweli haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kitu kinachoitwa mradi ni lazima uwe na mwanzo na mwisho. Lazima kuwepo na activities au programs za kuhakikisha kwamba tunaanza hivi, tunapita hapa mpaka mwisho wa safari inakuwaje. Kitu kinachoshangaza katika Mradi wa Liganga na Mchuchuma ni kwamba hatuoni ile mipango ambayo inawekwa, kwamba sasa Liganga na Mchuchuma imewekwa kwenye Programu ya Miaka Mitano ya Serikali; Liganga na Mchuchuma imezungumzwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi; Liganga na Mchuchuma inawekwa kwenye kila bajeti ya mwaka ambazo tunazipitisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ule Mpango wa Miaka Mitano sasa tunaingia mwaka wa tatu lakini bado hatujaona Liganga na Mchuchuma hasa ina tatizo gani. Tuliambiwa kwamba tatizo ni incentives, tunajaribu kujiuliza hizi incentives Serikali inashindwa kuchukua hatua ili tuweze kuona namna gani tunazi-accommodate na baada ya hapo hii miradi iweze kuanza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia kitabu cha bajeti, nimeona Liganga imewekewa shilingi bilioni 5 na Mchuchuma imewekewa shilingi bilioni 5, lakini sasa haifafanui activity ya hizi shilingi bilioni 5 zilizowekwa kwenye Liganga na Mchuchuma ni kwa ajili ya nini hasa? Kwa hiyo, naamini kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake basi atatueleza hizi shilingi bilioni 5 ni kwa ajili ya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya fidia pale, mpaka leo imekuwa ni kizungumkuti. Alipita Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 26 Januari, 2017, tulilizungumzia kwa kiasi kikubwa suala la fidia na ikaonekana kama fidia imekuwa exaggerated na ikasemekana kwamba itaweza kuundwa Tume au tukafanya review ya ile fidia ili wale watu waliopisha ile miradi iweze kufanyika pale walipwe kwa sababu sasa hivi wala hawajui nini cha kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye incentives kule tunaona kuna suala la Power Purchase Agreement. Mara ya kwanza ilikuwa ungetumia ule mfumo wa Build, Own and Transfer lakini baadaye kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ya mwaka 2017, wakaja tena na mfumo ule mwingine kwa maana ya kubadilisha kwamba itakuwa ni Build, Own and Transfer. Sasa hatujajua ni incentives zipi ambazo zinasababisha ule mradi usianze? Kwa hiyo, naamini Mheshimiwa Waziri atakapokuja basi atatuambia wamefikia wapi. Hizo incentives ambazo zinasemwa kwamba zinashindikana kufanya ule mradi uanze ni zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwamba kuna miundombinu wezeshi ambayo inafanya sasa ule mradi unaweza ukaanza, lakini pia inahitaji maamuzi magumu. Naona upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ambazo zinakwenda kwenye ile miradi, kwa maana kuna barabara inayotoka Mchuchuma kwenda Liganga na pia kuna barabara ambayo inatoka Mkiu kupitia Liganga kwenda Madaba. Naona zoezi lile linakwenda vizuri na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina safari hii utaisha mwezi Oktoba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona umeme wa Gridi ya Taifa ambao vilevile utashushwa pale eneo la Liganga na pia moja kwa moja utaelekea kule Mchuchuma. Jitihada hizi za Serikali tunaziona, miundombinu wezeshi hii ya Serikali tunaiona. Napenda kuiomba Serikali, suala la fidia basi mwaka huu iwe mwisho. Wale watu wamesubiri kwa muda mrefu, tuondokane nalo hilo. Kama itashindikana mwekezaji kulipa basi Serikali ichukue jukumu hilo na kuhakikisha kwamba hii adha ya fidia kwa wananchi wetu wa Mkomang’ombe na kule Mundindi inaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchuchuma na Liganga tumekuwa tukiiongelea muda mrefu sana. Mimi na watangulizi wangu wote nane wamekuwa wakiongelea Mchuchuma na Liganga katika Bunge lako hili. Mwaka 2017 zaidi ya asilimia 80 ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiiongelea Mchuchuma na Liganga. Tukijaribu kuangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Mchuchuma na Liganga haijapewa ile weight yake yaani ni maneno ya mistari 11 tu, basi Liganga na Mchuchuma imeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe tunasema kwamba Liganga na Mchuchuma ni miradi kielelezo. Miradi kielelezo ya nchi sikutegemea kwamba ingeweza kupewa weight ndogo kiasi hiki. Tungeweka weight kubwa na tujue tatizo ni nini? Angedadavua kiasi cha kutosha ili Waheshimiwa Wabunge tujengewe uelewa ili mwisho wa siku tuweze kuishauri Serikali vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nanukuu maelezo ya Mheshimiwa Waziri ya masuala ya viwanda mama na miradi kielelezo ya nchi, Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Anasema, katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi Unganishi wa Mchuchuma na Liganga, Serikali iliunda Timu ya Wataalam wa Serikali ikiwa na jukumu la kuchambua vivutio vilivyoombwa na wawekezaji. Vilevile uchambuzi ulifanyika kwa kuzingatia marekebisho ya Sheria ya Madini, 2010; Sheria ya The Natural Wealth and Resources Permanent Sovereignity Act, 2017; na The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Renegotiation of Unconscionable Terms), 2017 na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na Serikali. Timu hiyo imekamilisha taarifa ya awali ambayo inasubiri kutolewa maamuzi na mamlaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo haya ni ya kila siku na kwenye kila bajeti huwa yanakuja haya haya, kwamba tunaendelea na mchakato. Sasa ifike wakati Serikali ije na maamuzi magumu kuhusu mradi huu. Kwa hiyo, bado Taifa linasimama na naamini kwamba unapozungumzia viwanda ndani ya nchi hii, unazungumzia Liganga na Mchuchuma kwa sababu multiplier effect yake inaenda mbali. Kwa hiyo, ifike mahali sasa tuchukue maamuzi magumu. Nami naamini kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ina uwezo wa kuchukua maamuzi magumu na kuhakikisha kwamba miradi hii ina-take-off. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye upande wa biashara, mimi huwa najiuliza, tunawajua wafanyabiashara wetu? Tunayo database ya wafanyabiashara wetu? Kwa sababu tunaweza tukawa tunazungumza biashara na inaweza ikaleta impact gani wakati hatuwafahamu wafanyabiashara wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mlivyo-categorize, kuna wafanyabiashara wa kati, wadogo na wakubwa. Je, tunayo hiyo database ya hao watu kiasi ambacho tunaweza tukawa na uhakika kabisa kwamba tunapozungumzia suala la biashara impact yake ni hii na revenue tutakayoipata kwa wafanyabiashara ni hii hapa ili mwisho wa siku sasa tutengeneze platform kwenye kila maeneo, tunaweza tukaweka semina kwa wafanyabiashara wa kati, wadogo na wakubwa. Otherwise tutatakuwa tunatwanga maji kwenye kinu kama hatuwajui wafanyabiashara wetu ni nani na tunatarajia nini kutoka kwao na impact kwa wananchi wetu kiuchumi kuanzia mtu mmojammoja, vikundi na mpaka Taifa inakuaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ifike mahali sasa hawa Maafisa Biashara wetu kwenye Halmashauri, kwenye mikoa, ni lazima watengeneze database za wafanyabiashara wetu. Kwa sababu database hiyo inaweza ikatumika kama role model kwa watu ambao wanataka kuingia kwenye biashara ili waweze kujua kwenye biashara playground yao ikoje? Sometimes tukiwa na role models wana uwezo wa kushawishi watu wengine kuja kuingia kwenye mfumo wa kibiashara. Tusipotengeneza semina hizi wezeshi hatutaweza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la mbolea kwa Wilaya ya Ludewa. Mbolea ya kupandia inachelewa kufika kwa wakulima na matokeo yake uzalishaji wake unakuwa hafifu na pia mbolea hiyo inauzwa kwa bei kubwa mno tofauti na bei elekezi iliyotolewa na Serikali. Serikali ije na mfumo madhubuti wa upelekaji kwa wakulima mbolea inayohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko ya mazao, wakulima wa Tanzania wanazalisha mazao kwa wingi mno na hasa pale Serikali inapotoa hamasa kwa wakulima kufanya hivyo. Serikali ichukue hatua ya utafutaji masoko kwa wakulima wetu hasa masoko ya nje mazao kama mahindi, maharage, viazi na kadhalika. Wakulima wetu wasaidie kutafuta masoko kwani kutofanya hivyo kuna shusha morari kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukulima kwa kanda (zone) Tanzania ina maeneo mengi ya ukulima wa mazao mbalimbali katika maeneo mbalimbali nchini, sasa tuanze mkakati wa kulima mazao kutokana na hali ya hewa husika katika maeneo husika. Mfano kuwepo na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kama center ya uzalishaji wa mazao ya chakula na kuwepo na mpango mahsusi ambao utaleta kilimo cha tija. Pia yawepo maeneo mahsusi ya kilimo cha miwa kwa ajili ya kuondoa tatizo la sukari, pia maeneo mengine (kanda) kwa ajili ya alizeti, karanga, mawese ili kuondoa tatizo la mafuta ya kula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila eneo likipewa zao maalum na jitihada ziwekwe ili kila kanda ifanye jitihada za ukuzaji wa mazao mbalimbali. Kilimo cha namna hii kikipewa kipaumbele tutajinasua na upungufu wa chakula na pia kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu ili kuongeza thamani mazao ya wakulima. Kilimo kiki-link na viwanda vyetu, lengo la Serikali ya viwanda litafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa mbegu, Serikali iweke nguvu za kutosha katika utengenezaji wa mbegu za mazao. Mbegu imekuwa changamoto kubwa, ifike mahali ziwepo center’s za utengenezaji mbolea hasa za kitafiti kutokana na ardhi mbegu hizo zinaenda kufanyiwa kazi.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kuboresha maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa inayozunguka na milima mizuri ya Livingistone. Maeneo haya yanafaa sana kwa utalii kwa sababu ya beach nzuri zilizopo mwambao wa Ziwa Nyasa. Katika eneo la Kata ya Lumbila, Tarafa ya Mwambao palijengwa boma la Mjerumani ambalo limezama ndani ya Ziwa Nyasa na Wajerumani kuhamisha boma hilo kule Tukuyu. Boma la Mjerumani la Tukuyu asili yake ni Lumbila. Kwa hiyo, Serikali ione uwezekano wa kuweka kumbukumbu kihistoria kwani historia hiyo haifahamiki. Maeneo haya yakipewa usimamizi na kushirikiana na wananchi tutapata maeneo mazuri na mengi ya kihistoria. Maeneo haya bado yana picha nyingi za kihistoria ambazo zimehifadhiwa hasa katika makanisa ya Katoliki, kuna historia nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, eneo kubwa la Wilaya ya Ludewa ina vijito vya maji vinavyotiririka toka Milima ya Livingstone kuelekea Ziwa Nyasa. Vijito hivi baadhi vinatoka umbali wa kilometa 200. Hivyo kufanya maeneo mengi kuwa kijani (greenish) muda wote wa mwaka na kufanya mandhari nzuri ya maliasili ya nchi hii. Ifike wakati Serikali iwe na mkakati wa makusudi wa kutenga fedha za uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, kuna haja ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara nyingine kama miundombinu na ulinzi ili kufanikisha utalii kuweza kufanyika katika maeneo ya kando kando ya Ziwa Nyasa. Kuna wageni wengi toka nchi mbalimbali hasa za Ulaya kutembelea maeneo haya hasa yaliyokaliwa na wageni Wamisionari. Wageni hawa wanapokuja wanakumbana na mazingira magumu hasa miundombinu ya barabara na mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, tamaduni zetu hasa ngoma za asili zimeendelea kufifia mwaka hadi mwaka kutokana na kutopewa kipaumbele kikubwa. Kufifia kwa tamaduni hizi kumepelekea kumomonyoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya vijana na watoto wetu. Lazima kuwe na mkakati wa moja kwa moja wa kuhamasisha watu kupenda tamaduni za makabila yetu. Viwepo vipindi maalum vingi vya ngoma zetu na pia kuwe na muda maalum hasa kuanzia baada ya shughuli za kilimo katika maeneo ya vijijini. Ni vizuri walau kwa mwaka mara moja katika vijiji vyetu. Ngoma hizi zinazohusha akina baba, akina mama na watoto kujenga mahusiano baina yao toka katika maeneo mbalimbali, hamasa iende maeneo mbalimbali hasa mashuleni sherehe na mengineyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefikia wapi juu ya suala la mpaka eneo la Ziwa Nyasa baina ya nchi yetu na Jamhuri ya Malawi. Suala hili limekuwa ni la muda mrefu sana na hakuna ufumbuzi uliofikiwa juu ya suala hili la mpaka. Naomba kufahamu suala hili limefikia wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha mjadala tupate ufafanuzi wa kina juu ya mahali walipofikia katika maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Ludewa ambayo imepakana kwa eneo kubwa na nchi ya Malawi kuliko Wilaya za Kyela na Nyasa lakini hatuna customs ambazo zingerahisisha kwa watu wanaosafiri kwenda Malawi badala ya kupitia Kyela ambako ni mbali na kunaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotaka kusafiri kibiashara na kushindwa kulitumia soko la nchi jirani. Wilaya ya Ludewa ni eneo zuri kwa uzalishaji wa mazao ya biashara kama mahindi, maharage, chai, pareto, alizeti na kadhalika. Kuna umuhimu wa kuwa na bandari na TRA kurahisisha mienendo ya watu na bidhaa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Askari Polisi; Serikali ichukue hatua stahiki za kukarabati na kuendeleza nyumba za Askari Polisi hususani Wilaya ya Ludewa. Kuna nyumba za Polisi zilianza kujengwa toka mwaka 2012, lakini mpaka sasa hazijakwisha wakati askari wanaishi uraiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ludewa; Serikali ione sasa kuna haja ya kujenga kituo cha Polisi cha Wilaya kwani Wilaya hii ni ya siku nyingi toka tarehe Mosi Julai,1975. Tuiombe sasa Serikali kufikiria kujenga kituo cha Polisi kwani ongezeko la watu na uhalifu unaongezeka kadri muda unavyokwenda. Ni tumaini la wana Ludewa kuwa suala hili litapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu majengo ya Magereza; Majengo mengi ya Gereza la Ibihi lililopo Ludewa yamechakaa mno kiasi ambacho yanahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa sana, naomba Serikali kuliona hilo. Pia gereza hili la Ibihi ni gereza la kilimo ambalo lina ekari nyingi sana lakini lina changamoto kubwa ya kutopata trekta kwa ajili ya kulimia na kuleta ufanisi. Tayari gereza hili lilishaomba kupewa mkopo wa trekta jambo ambalo mpaka sasa hawajafanikiwa. Niiombe Serikali kuliona hilo na wapewe trekta ili ifanye kazi kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uchakavu wa sare za Askari Magereza na wafungwa. Sare zao zimechaka mno, tunaomba Jeshi la Magereza kuliona hili kwani linaaibisha taasisi hii nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Uhamiaji; Serikali ijaribu kuiangalia Idara hii hasa katika upande wa ofisi na watumishi. Wilaya ya Ludewa haina ofisi ya Uhamiaji na pia watumishi ni wachache mno. Ludewa ipo mpakani mwa nchi hivyo kuwa na watumishi wa kutosha ni jambo muhimu kwani zipo dalili za kuwa na wahamiaji haramu. Pia idara hii ipewe vitendea kazi kwani Ludewa ina eneo kubwa la mpaka kuliko Wilaya ya Nyasa na Kyela. Wapewe magari, maboti, pikipiki na kadhalika kwani miundombinu ya eneo hili ni migumu mno.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kujadili Hotuba za Kamati ya Nishati na Madini, pamoja na Ulinzi na Mambo ya Nje. Kwangu nijikite tu kidogo kwa sababu ya muda niongelee tu kidogo kuhusu suala la Stiegler’s gorge. Tunapokuwa tunaongelea long term investment haiwezi kuwa ni kitu ambacho kinaweza kuzuka tu katika kipindi kifupi, tunayo short term plan, tunayo medium na zile long term. Wakati tunajadili suala la long term plan wakati huo short term plan zile zinaendelea. Kwa hiyo, unaponiambia kwamba huu mradi utakamilika baada ya miaka saba ni kipindi kifupi sana hasa kwa sisi ambao tunaona kuna faida kwa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri pia watu ambao wanatoa hoja hizi wakawa wanasubiri na kusikiliza wenzao wanaweza kuzipangua vipi zile hoja zenyewe. Kwa sababu unazungumzia suala la MW 300, hata hivyo, sasa hivi Taifa halipo kwenye crisis, Taifa tayari linao umeme wa kutosha na pengine ni wa ziada. Kwa hiyo tunapoongelea mipango mikubwa, ni lazima tuongelee mipango mikubwa ya miaka mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea gesi lazima useme hii gesi ya MW 300 life span yake ni ya muda gani? Inaweza ikawa kumbe ina life span ya miaka 20, lakini unapoongelea Stiegler’s gorge vile vile na yenyewe uende uone kwamba ina life span ya miaka mingapi? Kwa hiyo huwezi ukavilinganisha vitu ambavyo unaweza ukavifanya kwa short term plan, medium plan na long term plan. Kwa hiyo, wakati mwingine tunapokuwa tunaizungumzia hii miradi na hasa miradi mikubwa, kwa sababu tayari Taifa limeshajipambanua, tunaenda kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ni lazima tupate nishati ya kutosha, kwa hiyo hata ingekuwa huu mradi unaanza baada ya miaka 15 tunachokiangalia ni viability ya business yenyewe na tunachoangalia ni sustainability ya business yenyewe. Kwa hiyo, mwisho wa hapo ndio unaweza ukazijenga hoja zako vizuri. Sisi hatuna crisis kusema kwamba kesho ni lazima tufanye ili niweze kuja ku-support kwenye viwanda ambavyo tunataka kuviendeleza. Kwa hiyo, kuna tabia ya kuwa sisi Wabunge tunajenga hoja unapotaka kujibiwa wewe unakuwa haupo, matokeo yake sasa next time unakuja unalijadili tena suala lile lile kitu ambacho si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niende kwenye madini. Tunalo suala la Liganga na Mchuchuma. Kwa kweli nimeona Wabunge wengi walikuwa wameizungumzia, lakini kuna haja Serikali ikaweka concentration kubwa na kama kwenye mpango wa maendeleo ilivyokuwa imezungumzwa kwamba kuna haja ya kujenga kiwanda cha kufua chuma pale Liganga. Ningeomba Serikali ijikite kwa sababu hadithi hii imekuwa ni hadithi ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nina imani Serikali ya Awamu ya Tano itaweka concentration kubwa na nina imani kwamba ni Serikali sikivu hiki Kiwanda cha kufua Chuma pale, kitakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kwenye suala la REA, REA wanafanya kazi nzuri, japo upo upungufu wa hapa na pale lakini kazi inayofanywa ni nzuri na ni kubwa. Sisi wote tunatoka kwenye majimbo, tunaona jitihada zinazofanyika za kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vingi vinapata umeme na vita-stimulate uchumi wa maeneo ambayo sisi tunafika. Kwa hiyo tuipongeze Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya na tujaribu kuitia moyo na kuwatia nguvu ili waweze kuzidisha mapambano na hatimaye tukaondoa ule umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la ulinzi. Kule maeneo ya Ziwa Nyasa hakuna doria yoyote ambayo inafanyika, hatuna boti la kiulinzi. Niiombe Serikali itupatie ulinzi kwenye maeneo yale na maeneo ya maziwa mengine ili kuweza kuondoa sintofahamu ambazo zinatokea hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Madini. Kwanza kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Dada yangu Angellah na marafiki zangu, Waheshimiwa Stanslaus Nyongo na Doto Biteko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye dira ya Wizara hii ya Madini. Ukiangalia dira ya Wizara inasema ni kuwa Wizara inayoheshimika Afrika katika kuendeleza rasilimali za madini ili ziweze kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Taifa, niishie hapo. Mimi natoka Ludewa, kule kuna chuma ambayo naamini ni madini na kuna makaa ya mawe ambayo naamini kuwa ni madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijaribu kuangalia kile chuma cha Liganga naona hakuna link kati ya Wizara ya Viwanda na Wizara ya Madini. Ndiyo maana unaweza ukaona hata kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri hajagusia kabisa chuma cha Liganga. Pamoja na kuwa kwamba huu ni mradi kielelezo ambapo tuna imani kwamba katika programu yetu ya miaka mitano ipo na katika programu ya mwaka moja moja ipo, naamini hapa kuna shida ya kutokuwa na link nzuri ya kuona kwamba hiki chuma kinaweza kuisaidia nchi kwenda. Kwa sababu ya ile dira ambayo sasa tumeshaizungumza naamini kabisa tunge-link haya madini na tukapata ule mwelekeo ambao ni sahihi chuma hiki cha Liganga kingeweza kupewa kipaumbele na kuleta tija kubwa sana kwa maslahi ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia miundombinu ya reli na majengo mbalimbali, ukijaribu kuangalia soko la ndani tu peke yake hiki chuma cha Liganga kinaweza kuleta tija kubwa. Kwa hiyo, napenda tu kuwepo na link kati ya Wizara hizi mbili badala tu ya kusema kwamba hii imeenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Biashara. Ni kweli chuma ni biashara, ni kweli chuma ni uwekezaji lakini chuma ni madini. Kwa hiyo, at least Mheshimiwa Waziri angeweza kukiongelea tuone ni namna gani kinaweza kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda kukizungumzia ni juu ya suala la makaa ya mawe. Tumeona hapa makaa ya mawe yamezungumzwa Kiwira na Ngaka. Tunayo makaa ya mawe Mchuchuma, licha ya ule Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma kwa maana ya kuzalisha umeme, bado kuna eneo kubwa la Ludewa linayo makaa ya mawe. Je, Serikali imefanya utaratibu gani kwa sababu Ketewaka tunayo makaa ya mawe mengi sana. Maeneo yale yote ya Mwambalasi kuna makaa ya mawe mengi sana, lakini sioni kama Wizara imeshajielekeza kuona licha ya ule mkaa wa mawe ambao unaweza ukazalisha umeme pale Mchuchuma kuna sehemu nyingine ambazo vilevile zingeweza kutumika na kama ambavyo Ngaka wanauza bado na maeneo mengi ya Ludewa yangeweza kuchimbwa huo mkaa na ukauzwa na ukaleta tija. Tija kwa maana ya wananchi ajira na kwa maana ya Serikali kupata kodi. Kwa hiyo, nadhani GST iendelee kufanya kazi yake nzuri na tuweze kuainisha kwa kiasi kikubwa tuna mkaa kiasi gani maeneo yale kwa ajili ya faida ya wananchi wetu na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao hawa wachimbaji wadogo. Serikali imechukua hatua, niipongeze kwa ajili ya kuwapa mikopo lakini wachimbaji wadogo wanaopata mikopo ni wachache. Kwa hiyo, naamini kwamba tungeweka utaratibu mzuri wa kuwapa elimu hawa wachimbaji wadogo ili waweze kukopa hata kwenye mabenki badala ya kusubiria ruzuku kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tunao wachimbaji wadogo sana, Ludewa yapo machimbo sehemu za Amani kule, Kata ya Mundindi wapo wachimbaji wadogo wengi lakini hawajui nini wafanye. Wale watu hawana elimu ya kutosha, nadhani sasa Serikali ifike wakati ipeleke elimu ya kutosha kwa wale wachimbaji ili ikiwezekana sasa wajue namna gani ya kuendesha biashara, namna gani ya kutunza kumbukumbu, namna gani wanaweza wakakopeshwa na mwisho wa siku waweze kuendeleza biashara in sustainable way.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo suala la tanzanite. Tanzanite inapatikana Tanzania tu lakini ukienda kwenye soko la nje madini yaliyopo kule ni mengi zaidi na yanapelekwa na nchi ambayo siyo Tanzania. Nakumbuka mwaka jana tuliongelea hapa juu ya certificate of origin, kwamba mtu yeyote ambaye anaweza akasafirisha yale madini awe na certificate ambayo inatoka kwenye nchi husika. Sijajua Wizara mpaka sasa imeshafikia wapi katika kuhakikisha kwamba haya madini yanapokuwa yanauzwa kule ili isionekane kwamba hawa watu wametorosha au wamefanya biashara haramu, kuwepo na certificate maalum ya kuonesha kwamba madini haya yametoka Tanzania. Kwa kufanya hivyo, maana yake tutapunguza sasa ile watu kutorosha madini kupitia kwenye mipaka na maeneo mbalimbali tuweze kupata ile faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kujenga ule ukuta. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na pia DC wa Simanjiro Bwana Chaula kwa kufanya usimamizi mzuri na kuhakikisha kwamba ule ukuta umekamilika na pia niishukuru Wizara kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna suala hili la GST. GST imepewa majukumu makubwa sana ya kufanya tafiti za madini kwa nchi lakini ukijaribu kuangalia bajeti ambayo wanawekewa ni ndogo sana. Kwa hiyo, kila mmoja hapa na katika Wilaya na Jimbo lake wanahitaji kuona kwamba ni madini kiasi gani yapo na namna gani tunaweza tukayatumia wananchi waweze kunufaika na madini hayo, lakini bajeti wanayopewa GST hailingani na haitoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naamini kabisa tunao wataalam pale GST lakini ni wachache. Serikali ichukue sasa hatua kuelimisha wataalam wetu wawe wengi ili mwisho wa siku tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni juu ya gharama za tafiti. Watu wengi sana wameshika haya maeneo na wana leseni lakini gharama zile zinakuwa ni kubwa kwa maana GST iko centred sehemu moja. Kwa hiyo, kila mmoja anayetaka kuja kuitumia GST kwa ajili ya kumfanyia tafiti maana yake ni asafiri kutoka aliko aje Dodoma. Sasa wananchi wetu hawana uwezo mkubwa kiasi hicho. Naamini kwamba wangeweka utaratibu ambapo accessibility yake iwe ni jirani ili hiki chombo kiweze kutumika kwa unafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu-create awareness kwa wananchi wajue hizi shughuli, kwa sababu GST iko Dodoma na naamini wengi wenye machimbo haya hawaijui GST, wala hawajui GST maana yake nini. Kwa hiyo, yawepo matangazo ya kutosha, tu-create awareness ya kutosha ili wananchi wetu waweze kujua kazi ambazo zinafanywa na GST na wakati mwingine kuepukana na matapeli ambao wanawazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uwekezaji, tumekuwa na wawekezaji wengi sana wageni na inafikia mahali sasa kile kitu ambacho kinafanyiwa tafiti kule Serikali iko unaware. Kwa hiyo, ifike mahali sasa hawa wageni wanapokuja kufanya tafiti kuwepo na element ya Serikali ili kuweza kujua ni madini kiasi gani, kwa sababu unaweza ukapelekewa ripoti ambayo si sahihi, ripoti ambayo hailingani pengine na hali halisi iliyopo na hii naamini kwamba imeligharimu sana Taifa huko tulikotoka. Kwa hiyo, tukifanya utaratibu huo tutaona tija ya madini yetu na hawa wanaofanya tafiti hasa mashirika ya kigeni lazima yaweze kusimamiwa na tujue ni nini ambacho kinafanyiwa tafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni juu ya utoaji wa leseni. Mara nyingi unakuta kwamba mtu ambaye madini yapo kwenye eneo lake hajui kama pana madini lakini unaambiwa kwamba eneo hili tayari lina mtu na tayari ana leseni, Serikali ya Kijiji na Wilaya hazijui, nadhani tuweke utaratibu sasa ili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuongea na kuchangia hotuba. Kwanza naipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambazo inazifanya hususan maeneo yetu ambako tunatoka. Kwa hiyo, nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuishukuru Serikali hasa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, Waziri wetu na Manaibu wake pia Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara nzima, nianze kuiongelea barabara ya Itoni – Njombe – Ludewa – Manda. Barabara hii imewekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na barabara hii kwa kweli ina urefu wa kilometa 211.6 mpaka kufika kule Manda. Itajengwa katika lots nne na kwa sasa imeanza ujenzi wa lot Na. 2, Lusitu - Mawengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii, hivi tunavyoongea toka ilipoanza kujengwa ilipaswa iwe imeisha lakini mpaka sasa barabara hii haijaisha. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa ijaribu kufanya jitihada za haraka ili kipande hiki korofi kiishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna eneo la Lusitu kwenda pale Itoni, lot Na. 1, kwa kweli kipande hiki kinasumbua sana. Hivi ninavyozungumza, malori mengi sana yamekwama kwenye maeneo ya Njomlole kule, maeneo ya Luponde na kusababisha adha kubwa ya usafiri mpaka ikapelekea wiki iliyopita baadhi ya wenye magari kutokupeleka magari Ludewa kwa sababu ya adha hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sasa Serikali angalau itufikirie kwa kipande cha kutoka Itoni kwenda Lusitu na wakati huo huo ile barabara ya Mawengi - Lusitu ikifanyiwa jitihada kubwa. Kwa sababu nakumbuka Mheshimiwa Waziri alikuja mwezi wa Nane akaona na akatoa maagizo, lakini inaonekana kama yale maagizo hayakufanyiwa kazi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeza Serikali kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya kutoka Mkiu – Liganga – Madaba na ule wa kutoka Mchuchuma kwenda Liganga. Kwa kweli barabara hizi ni muhimu, upembuzi umefanyika. Sasa naiomba Serikali iweke jitihada kubwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa lami ya barabara hizi kwa sababu barabara hizi ndiyo zinakwenda kwenye ile miradi ambayo tunaita ni flagship projects ya Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye jitihada za haraka kwa sababu ya umuhimu wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru Serikali kwa kuiweka kwenye mpango wake wa Bajeti wa kuifungua barabara inayopita kando kando ya Ziwa Nyasa; barabara kutoka Lupingu – Makonde - Lumbila mpaka Matema. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa iweke misisitizo mkubwa kwa sababu eneo hili la Ziwa Nyasa ni eneo la Kitalii na pia ni eneo la kiulinzi na usalama. Kwa hiyo, ninaamini kwamba kazi hii mtaifanya na mtaifanya kwa kutumia nguvu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie daraja la Mto Ruhuhu. Daraja la Mto Ruhuhu lilipaswa liishe toka mwaka 2017, lakini mpaka leo hii daraja hili halijaisha na daraja hili lipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, tunaomba basi mwaka huu hili daraja likamilike ili lipitishe wananchi ambao wanatoka Ludewa kuelekea kule Nyasa, kwa sababu kwa mwaka 2018 tu, tayari wananchi zaidi ya watano wameliwa na mamba kwenye mto huu huu kwa sababu ya kutokuwepo kwa daraja pale. watu wanapita kwa mitumbwi na wakati mwingine hata ile Panton iliyopo pale inakuwa haifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali na kusisitizia kwamba ikiwezekana hili daraja liishe mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameniahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kazi inayofanya kule Ziwa Nyasa. Tumeona Mheshimiwa Nditiye akiwepo pale na bahati nzuri na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara. Kwa hiyo, nashukuru kwa kunipa tu vile vituo vya kupakia na kupakua abiria na mizigo ili kuweza kuwarahisishia wale wananchi wanaoishi Kanda ile, usafiri wa kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kushukuru Wizara kwa ajili ya minara ya mawasiliano ya simu. Minara hii tayari imeshajengwa na iliweza kuwaka kwa siku tatu tu lakini mpaka sasa hivi imezima. (Makofi)

Kwa hiyo naomba sasa Wizara kupitia mawasiliano kwa wote, kazi waliyoifanya ni kubwa na kazi waliyoifanya ni nzuri, niwapongeze na nimpongeze Mheshimiwa Engineer Ulanga na timu yake yote na nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kazi hii ni njema lakini wale watu wanasubiri kwa kiasi kikubwa mawasiliano kwa sababu mawasiliano yamekuwa ni tatizo kubwa kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niiongelee kidogo TTCL ni Shirika letu, Shirika la nchi na la umma, kuna haja ya kuweka utaratibu mzuri ili iweze kushindana na taasisi nyingine hasa kwenye eneo la manunuzi. Manunuzi inavyoonesha kwamba inachukua muda mrefu kiasi ambacho hawawezi ku- compete na wenzao. Wenzao wao private sectors wao wanafanya mambo yao kiurahisi, kwa hiyo kuna haja ya Serikali sasa kuipa uwezo wa kujiendesha yenyewe na hizi sheria za manunuzi tuweze kuzirekebisha ili hili shirika liweze kujiendesha vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Wizara hi ya Kilimo. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Hasunga na Manaibu Mawaziri wake, Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Mheshimiwa Mgumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi sasa ime-target kwenda kwenye uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda hautaweza kuja kama kilimo chetu hakijawa ni kilimo cha ufanisi kwa sababu naamini kwamba viwanda hivi malighafi zake zitatoka kwenye kilimo. Sasa nipende tu kujua mpango mkakati wa Wizara wa ku-boost up hivi viwanda ili viweze kuimarika ukoje, kwa sababu naamini asilimia zaidi ya 75 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima, sasa mpango upoje wa kuwainua hawa wakulima ili waweze kuhakikisha wkamba wanatengeneza malighafi za kutosha kwa ajili ya ku-boost up hivi viwanda, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vinasimama na kujitegemea bila kutegemea kwa kiasi kikubwa malighafi kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wana uwezo wa kuhakikisha kwamba kilimo kinakuwa endelevu, lakini kitu kikubwa ambacho kinazuia hiyo, ni miundombinu ya maeneo ya uzalishaji. Maeneo ya uzalishaji miundombinu yake kufikika ni migumu sana na hii ndiyo inayopelekea wakulima wetu kupata faida kidogo. Sasa ifike mahali maeneo ya uzalishaji miundombinu yake iwe ya uhakika. Mfano, kule kwetu Ludewa; Ludewa ina uwezo wa kuilisha hii nchi kupitia mahindi lakini miundombinu yake siyo mizuri sana, barabara zetu siyo nzuri sana. Kwa hiyo niiombe sasa Serikali iboreshe miundombinu ya barabara ili iweze kuwafikia wale wakulima na tuweze kuilisha hii nchi na tuweze kutoa malighafi ya kutosha ku-support hivi viwanda ambavyo sasa tunategemea viwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kilimo kupewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa, hivi viwanda ambavyo tunavitegemea kwamba ndiyo iwe engine ya uchumi wa hii nchi tutakuwa tunapoteza muda. Kwa hiyo, napende kusema kwamba hii miundombinu ambayo ipo lazima iboreshwe hususan barabara wakulima wetu wanapata shida sana. Mfano, katika kipindi hiki cha masika, kuna mazao ambayo yanavunwa kipindi cha masika lakini yanashindwa kutoka kwenye eneo la uzalishaji kuja sokoni. Kwa hiyo tukiweza kuhakikisha kwamba tunatengeneza miundombinu vizuri hasa ya barabara, naamini kwamba kilimo kina uwezo mkubwa wa ku-support viwanda ambavyo sisi tumejielekeza kama nchi kwenye uchumi wa hivyo viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza kilimo, tunazungumza mbegu. Mbegu zetu nyingi siyo bora, lakini nauona mpango wa Serikali sasa wa kuhakikisha kwamba tunawaletea wakulima wetu mbegu bora ili tuweze kufanya uzalishaji mkubwa na ambao ni wenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitu kingine ambacho wakulima wetu wanapata nacho shida ni suala la mbolea. Mbolea kwa kweli haziendi kwa target, hazi-meet target za wakulima. Kipindi cha ukulima mbolea hazipo, lakini wakati unaelekea kwenye maeneo ya mavuno ndiyo zinakuja mbolea za kupandia. Kwa hiyo kuna haja sasa Serikali ikajipanga mbolea ziende katika kipindi husika. Kama ni mbolea ya kupandia basi iende katika kipindi cha kupandia, kama ni mbolea ya kukuzia iende kwenye kipindi cha kukuzia. Hilo litaleta tija kwa wakulima na pia Serikali itapata faida kwa kupitia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wana tatizo kubwa la soko. Tumeona mwaka jana wakulima wetu walikuwa na mazao mengi, walizalisha kwa kilimo kikubwa hususani mahindi. Mahindi kwetu kule Ludewa ni zao la biashara si zao la kilimo, kwa hiyo tunapozungumza mahindi kama zao la biashara kulikuwa na kuna haja sasa ya Serikali kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapata soko la kutosha ili kuwahamasisha wakulima wetu kulima kwa bidii na kwa tija, la sivyo tukitegemea tu soko moja la NFRA halitoshi. Kwa hiyo nchi ijipange sasa kutafuta masoko ya mazao ya mahindi na mazao mengine yote ya chakula ili wakulima wetu walime kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia kama nchi tunalo gap kubwa, tunalo gap la mafuta ya kula, sasa sijajua kama nchi tumejipangaje. Ifike mahali sasa tuweke kilimo kwa zone kwa sababu tunategemea mafuta kutoka nje wakati wakulima wetu wana uwezo wa kufanya hivyo vitu. Sasa ni nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunaliziba hilo pengo kuhakikisha kwamba mafuta tutayotegemea yatoke hapa nchini na ikiwezekana mafuta hayo tuweze kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna tatizo la mbolea. Kama nchi tumejipangaje kuwa na viwanda vyetu wenyewe vya mbolea badala kutegemea mbolea kutoka nje. Kwa hiyo mimi niseme tu, uchumi wetu wa viwanda utategemea kwa kiasi kikubwa kilimo na kilimo ni lazima tukipe kipaumbele kikubwa. Tukizungumzia viwanda usisahau kiwanda cha chuma kule Liganga na usisisahau makaa ya mawe Mchuchuma. Viwanda hivi ndivyo viwanda flagship ambavyo vina uwezo wa kuzaa viwanda vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna kila haja ya kuhakikisha kwamba kilimo chetu kiwe ni kilimo cha uhakika, tuondoke kwenye kilimo cha kutegemea mvua twende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Hii nchi ina mabwawa mengi, hii nchi ina mito mingi, kwa hiyo twende kwenye kilimo cha uhakika ili hatimaye wakulima wetu walime kwa tija na waone faida ya wao kuwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Benki ya Kilimo, iko Dar es Salaam. Mimi ningependekeza kuwa hii Benki ya Kilimo ije Ludewa ambako wakulima ndipo wapo. Benki ya Kilimo kukaa Dar es Salaam mtu wa Ludewa aende Dar es Salaam kwenda kukopa mkopo; kwanza hata hiyo elimu ya mkopo hana. Kwa hiyo Benki hizi ambazo zinawa-target wazalishaji ziende kwa wazalishaji wenyewe ili hatimaye tuione hiyo tija. Kwa sababu leo hii unaponzungumza hapa kwenye taarifa unaiona kabisa Benki ni ya kilimo sawa lakini wakopaji wakubwa si wakulima. Kwa hiyo ifike mahali sasa kila kitu ambacho tunakilenga basi tukipe kipaumbele ili hatimaye tuone kwamba wakulima wetu wanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo bado niendelee kusisitiza kwa Serikali kuhusu masoko ya mazao, bado ni machache. Na pia tuzungumzie suala la wale walio supply mbolea. Lipo hili ombi ambalo linaonekana kwamba walio supply mbolea walio wengi walighushi; lakini mimi ninaamini kwamba wapo walio supply mbolea hawakuwa na shida yoyote. Kwa hiyo wale ambao hawakuwa na shida yoyote walipwe sasa, kwa sababu tunasumbuliwa sana, kwa sababu hatusemi sasa ni nani ambaye ameghushi, ni nani ambaye amekuwa ni fisadi kwenye huo mfumo. Wale ambao wanaonekana wapo clean walipwe fedha zao, kwa sababu tunao watu wengi wako stranded sasa hivi huu ni mwaka wa tatu wanasubiri malipo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hebu jaribu kuliona hilo ili mwisho wa siku hawa watu waweze kukopa.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ngalawa.

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala unaoendelea wa Kamati ya Kudumu ya Miundobinu na ya Viwanda. Kwanza nipende kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri na njema inayowafanyia Watanzania kwa sasa. Tumeona barabara zikiwa zinajengwa katika maeneo mbalimbali, tumeona minara ya simu, madaraja, bandari na vitu vingi. Hata hivyo, napenda kujikita kidogo kwenye taasisi ya TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS inafanya kazi nzuri na iliyotukuka lakini kuna baadhi ya maeneo kuna upungufu kidogo. Kuna maeneo ambayo ujenzi tayari unaendelea, lakini watu wa maeneo husika hawajalipwa fidia mpaka sasa. Mfano wa barabara ya kutoka Itoni – Njombe – Ludewa – Manda kile kipande cha Lusitu – Mawengi kimeanza kufanyiwa kazi na sasa hivi kilometa kama 12 tayari zimeshakamilika barabara ya zege, lakini watu wa maeneo ambako barabara inajengwa walio wengi bado hawajalipwa fidia kwenye maeneo yao hayo.

Kwa hiyo naiomba sasa Serikali iweze kulipa fidia kwenye barabara ambazo inazifanyia kazi, sio Ludewa tu, pia na maeneo mengine ya nchi ambako barabara zinajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilizungumzie kidogo Shirika la Posta; Shirika hili kweli limebeba madeni makubwa, kama ilivyozungumza Kamati, ya kulipa wale wafanyakazi waliokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mzigo ule ni mkubwa sana kwa Shirika la Posta. Tunaomba sasa Serikali iweze kuchukua huo mzigo na ikiwezekana iongezee mtaji shirika hili ili liweze kujiendesha kibiashara, ili liweze kujiendesha kwa kutumia resources ambazo inazitoa kuwalipa wale watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukifuatilia kwa kiasi kikubwa juu ya madeni haya ambayo Shirika la Posta linaidai Serikali kwa sababu waliopaswa kulipa zile pensheni wale watu wa Jumuiya, ni Serikali. Kwa hiyo posta inalipa kwa niaba ya Serikali, kwa hiyo matokeo yake sasa inaondoa mtaji wa uendeshaji inalipa yale madeni na Serikali imekuwa kidogo hailipi kwa wakati. Ndiyo maana unaona sasa hivi kuna madeni mengi sana Shirika la Posta inaidai Serikali. Kwa hiyo naomba na kushauri Serikali ichukue ule mzigo wa kuwalipa wale ile pensheni na pia iwaongezee mtaji ili iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa maeneo ya mawasiliano. Mawasiliano ya simu kwenye maeneo mengi yamekuwa ni mazuri na tumeona, lakini upo upungufu. Imejengwa minara mingi sana, lakini kuna baadhi ya maeneo minara ile inachukua muda mrefu sana kuanza kuwashwa baada ya kuwa imejengwa. Mfano, maeneo ya kwetu kule ipo minara kadhaa ambayo tayari imeshajengwa, lakini mpaka sasa bado haijawashwa. Kwa hiyo niiombe Serikali iiwashe minara ile na tuone namna gani ya kuweza kuisadia hii UCSAF kuipa hela za ku-operate ili Watanzania walio wengi waweze kupata mawasiliano ya uhakika na yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Kamati ya Viwanda; kuna hili suala la Mchuchuma na Liganga, suala hili limeshakuwa ni la muda mrefu na tumesema kwamba miradi hii ni miradi kielelezo, lakini ukijaribu kufuatilia na kuiangalia hata kwenye taarifa yenyewe ya Kamati imepewa weight ndogo sana. Miradi kielelezo ninavyofahamu mimi ndiyo ingekuwa chachu ya kuchochea uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaagiza chuma kutoka nje ya nchi wakati chuma Liganga kipo. Naamini tungetengeneza concentration kubwa kwenye eneo hilo, tungeweza kupata impact kubwa ya kiuchumi kwenye eneo letu. Ukijaribu kuangalia mradi wa Mchuchuma na Liganga, tafiti zinaonesha kwamba zinaajiri Watanzania wasiopungua 32,000, lakini multiplier effect yake inaenda mpaka kwa Watanzania 300,000. Sasa ajira za watu 300,000 ni ajira kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna haja sasa pamoja na kwamba wanapitia ule mkataba lakini muda umekuwa ni mrefu sana. Yaani kuanzia tunaingia Bungeni hapa toka 2016 ule mkataba unaendelea kupitiwa, umepitiwa 2016, ukapitiwa 2017, 2018, 2019 mpaka leo 2020 bado tunazungumzia tu kupitia mkataba. Nadhani sasa ufike wakati hili suala liishe ili tujue sasa hatma ya miradi hii ya Mchuchuma na Liganga imefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa watu wa maeneo ya kusini na Tanzania kwa ujumla tunaona kabisa miradi ile ni miradi yenye tija, kwa sababu leo hii tunaagiza chuma kutoka nje wakati chuma tunacho. Miradi hii ikianza bado leo hii tunazungumzia suala la viwanda, viwanda ni umeme, viwanda ni nishati. Tunao pale umeme wa megawati 16 pale Mchuchuma, makaa yale yamekaa tu. Kwa hiyo, naomba Serikali iipe uzito unaostahili hii Miradi ya Mchuchuma na Liganga, la sivyo kila siku tutakuwa tunazungumzia Mchuchuma na Liganga na inawekwa kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu pia kuna fidia ya watu ambao wamepisha ile miradi kwenye maeneo yale ya Mchuchuma na Liganga na inawekwa kwenye bajeti kila mwaka. Mwaka huu 2019/2020 zimewekwa bilioni tano kwa watu wa Liganga pale Mundindi na imewekwa bilioni tano kwa watu wa Mchuchuma pale Nkomang‟ombe, lakini hatuoni jitihada ambazo zinafanyika kuwalipa fidia watu hawa kwa sababu hizi zimeshaanza kutengwa leo ni mwaka wa tatu lakini hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sasa Serikali iichukue yenyewe, kwa sababu mwanzo hii fidia ilisemekana kwamba italipwa na mbia, lakini sasa maadam wameingia kwenye eneo la majadiliano ya kimkataba, fidia hii ichukuliwe na Serikali yenyewe ili iweze kulipwa tuondokane na malalamiko ya wananchi ambao wamepisha hiyo miradi kwenye maeneo yale husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna hii pia la reli ya kutoka Mtwara kuja Songea - Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga, sijajua mpaka sasa wamefikia wapi na sijaiona kwenye ripoti. Kwenye ripoti humu sijaiona kama imezungumziwa chochote lakini nakumbuka kwenye bajeti ya mwaka jana wamesema kuna mbia amepatikana na wanaendelea na mazungumzo. Kwa hiyo naiomba Serikali ije sasa na maelezo tuone kwamba reli ya Mchuchuma imefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu unaoendelea wa Kamati za Huduma ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Ukimwi. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaendelea kuifanya. Tumeona Vituo vya Afya vingi vikijengwa, tumeona Hospitali zikijengwa na tumeona Zahanati zikijengwa. Kwa kweli mambo yanaenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kwenye eneo la kinga. Tuna tiba na kinga. Ukiangalia Wizara ya Afya imejikita sana kwenye eneo la kitabibu, lakini ni Wizara hii ambayo inashughulika pia na kinga. Kwa hiyo, napenda sasa kuishauri Serikali, ifike mahala tuweke concentration kubwa kwenye maeneo ya kinga ambayo yatazuia gharama kubwa kutumika katika maeneo ambayo ni ya tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mifano ya nchi kama Rwanda ambako tumeenda. Wapo Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao kazi yao kubwa ni kuelimisha watu wale vyakula vya namna gani kwa maana ya lishe na kutoa elimu mbalimbali za kinga dhidi ya mimba, dhidi ya ujauzito na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, naamini kwamba tukijikita kwa kiasi kikubwa kwenye kinga, tutaokoa gharama kubwa zinazotumika maeneo ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru na kumpongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile; wametengeneza concentration kubwa kwenye hivyo vitu. Sasa naomba nguvu ile ile ambayo imetumika sana kwenye afya, tumeona Serikali ikiwa imeokoa hela nyingi sana za kupeleka wagonjwa nje ya nchi, kutoka 600 mpaka watu 50 kwenda nje, siyo jambo dogo. Hilo ni jambo kubwa sana nami nasema kwamba endeleeni kukomaa kwenye hilo ili mwisho wa siku ikiwezekana tupeleke watu sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza, kazi mnayoifanya ni kubwa na Watanzania wanaiona. Pia tuwaimarishe watumishi wa ya Maendeleo ya Jamii ili waweze kutoa huduma kule vijijini ya namna ya Lishe na namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ili tuweze kuokoa gharama kubwa inayotumika kwenye afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masuala ya maboma ya Vituo vya Afya, Zahanati na Shule. Maeneo mengi ya Majimbo ambako tunatoka, wananchi wametumia nguvu zao nyingi na kubwa katika kuhakikisha kwamba wanaisaidia Serikali yao kujenga Zahanati na Vituo vya Afya. Sasa umeshafika wakati wa Serikali angalau kuwasaidia hawa wananchi kwa ajili ya kuezeka na baadaye kukamilisha. Wananchi wetu wakielimishwa wala hawana shida yoyote. Ludewa ninakotoka kuna zaidi ya maboma ya Vituo vya Afya 14 na mengine yameshaezekwa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, kinachoitajika tu pale ni kuwa-support ili kuweza kumalizia na baada ya hapo, utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi kwamba Kila Kijiji kiwe na Zahanati na Kila Kata iwe na Kituo cha Afya, tutakuwa tumetekeleza kwa kiasi kikubwa sana, zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunajenga shule nyingi, kwa sababu tumeshasema kwenye kila kijiji tunatakiwa shule. Kwa hiyo, nadhani kuwekwe mpango madhubuti wa timu maalum ya kwenda kupitia maeneo hayo, yaje na taarifa ili tuweze kupata takwimu sahihi za kuweza kusaidia hiyo kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwamba Mheshimiwa Waziri na Watendaji huko Serikalini wana uwezo wa kuifanya hiyo kazi na mwisho wa siku tukaitekeleza ilani kwa asilimia 100, hiyo inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uhaba na watumishi kwenye maeneo ya afya. Uhaba huu umekuwa ni mkubwa sana. Kama wenzangu walivyokuwa wamezungumza huko mwanzo, ile hali ya uzalendo ni kama imepungua. Sasa tujiulieze, imepungua kwa kiasi gani, hasa wale watu kwenda kujitolea? Wasomi wetu wanaomaliza sasa hivi wengi wapo mitaani, lakini bado tunalalamika tuna uhaba wa walimu na watumishi wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifanyike program maalum ya kuhakikisha kwamba watu wanajitolea na wale wanaojitolea ndiyo wawe wa kwanza kuajiriwa. Kwa sababu wapo watu ambao wanajitolea, nafasi za kazi zinatangazwa, lakini wale wanaojitolea wanaachwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tungetengeneza utaratibu mzuri kwamba wale wanaojitolea, basi ndiyo wawe wa kwanza kuajiriwa kwa sababu wameonyesha uzalendo wa moja kwa moja kuanza kazi mwaka wa kwanza, miaka miwili, lakini kazi inapotangazwa, wanaachwa. Nadhani siyo jambo sahihi, maadam tu wana zile sifa ambazo zinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao watu wanaoitwa uthibiti ubora. Kuna malalamiko makubwa sana kwenye uthibiti ubora hasa wa elimu. Zamani hawa watu tulikuwa tunawaita Wakaguzi. Hawa watu wanaoenda kukagua shule, maana yake wanakagua shule; na ile kazi ni kubwa. Ukijaribu kuangalia kwenye level ya wilaya, yuko Mthibiti Ubora Mkuu wa Wilaya na wapo Maafisa Elimu. Hawa watu bado wanalalamikia masuala ya nyongeza, zile fedha za nafasi; wanaita fedha za nafasi, kitu cha namna hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Serikali ingejaribu kuangalia uwezekano wa hawa watu, yale malalamiko ambayo wanasema kwamba wanaonekana kama ni second class, yaondoke ili waweze kuwa sawa na wenzao na waweze kufanya kazi zile kiufanisi. Kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa, kuna uhaba mkubwa wa magari, kuna uhaba mkubwa wa vifaa na umbali wa maeneo wanayokwenda. Kwa hiyo, wanajikuta kwamba wanafanya kazi kubwa na ambayo kwa kweli wanahitaji kupewa msaada.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ahsante kwa nafasi na ninaunga mkono hoja zote zilizotolewa hapa na Wenyeviti wote wa Kamati, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyoko mezani. Kwanza niishukuru Serikali, nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu, Katibu Mkuu na Idara zote zilizopo chini ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kutoa pongezi kwa Taasisi ya REA, kwa kweli kazi inayofanywa ni kazi nzuri na tunaiona. Nakini nipende kusema kwamba kwa Ludewa bado mkandarasi hafanyi vizuri sana kwa sababu mpaka sasa ni kijiji kimoja tu ndicho kimewashwa. Kwa hiyo ninaamini kwamba kwa jitihada za Mheshimiwa Waziri na Mtendaji na Mkuu wa REA kadiri tunavyokuwa tunazidi kuwasiliana ninaamini kwamba sasa hivi mkandarasi atajiweka sawa na kuweza kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kuongelewa vyanzo vya nishati, hasa umeme. Tumeona kuna umeme wa maji, kuna umeme wa gesi, kuna umeme wa makaa ya mawe, upepo na jotoardhi; nianze na maji. Tunavyo vyanzo vingi sana vya maji na hasa hata kwetu kule Ludewa tuna mito mingi sana ambayo inamwaga maji ziwa nyasa na inaweza ikawa ni miongoni mwa vyanzo vizuri vya umeme.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo ningeomba sasa Wizara ijipange na iweke master plan ya maeneo yote ambayo yanaweza kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha umeme wa maji ambao ndio unaonekana ni rahisi. Kwa hiyo kuna haja sasa Serikali ikaweka mpango mkubwa na tuweze kuona ni namna gani tunaweza tuka-meet zile megawatt 10,000 ambazo Serikali imezipania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, tunao umeme wa makaa ya mawe na hata nchi nyingi sasa hivi, including Marekani inaanza kutumia umeme wa makaa ya mawe. Tunayo makaa ya mawe pale Mchuchuma ambayo yanaweza yakatoa megawatts 600. Kwa hiyo, naamini kwamba Serikali ikijipanga vizuri, ikachukua na kuanzisha utaratibu mzuri wa kuweza ku- tap yale makaa ya mawe pale bado Serikali na nchi itaweza kufaidika kwa kiasi kikubwa na tukawa na umeme wa kutosheleza kwa sababu tayari tumejipanga kwamba Serikali na nchi imejipanga katika mfumo wa viwanda na viwanda vinahitaji umeme. Kwa hiyo kuna haja sasa makaa ya mawe kule Mchuchuma yakawa ni moja kati ya resourceful ya kuweza kufikia hizi megawati 10,000.

Mheshimiwa Spika, lengo letu kufika 2025 ni kuwa na megawati 10,000 sasa labda pengine nijaribu kuangalia mpango ukoje wa Serikali ili kuweza kufikia hizo megawati 10,000 tunazoziendea, kwa sababu naamini kwamba tuna ile mipango ya kufikia ule muda wenyewe na kuna ile mipango ya mwaka mmoja mmoja na kuna ile mipango ya kati. Sasa Serikali ije na majibu tuone kwamba mpaka sasa kwa mwaka huu ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. DEOGRATIUS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia Muswada huu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na timu zao kwa namna nzuri ambavyo wameuwasilisha Muswada huu. Muswada huu ni muhimu sana kwa namna ambavyo umeelezwa, kwanza kwa ajili ya usalama na ulinzi, pili kukuza uchumi na tatu kwa ajili ya masuala ya kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TTCL ilikuwa tayari imeshazama, kwa hiyo mpango ambao Serikali imeuleta ni mzuri. Pamoja na Waheshimiwa wenzangu wote kuchangia lakini mimi kubwa najikita katika masuala matatu. Suala la kwanza liwe ni suala la mtaji, la pili miundombinu na pia wakati mwingine lazima tuziangalie hizi sheria zetu hasa tunapoyapeleka mashirika ya umma kwenda ku-compete na mashirika mengine. TTCL inatakiwa kupewa mtaji, ikishapewa mtaji naamini kabisa ni shirika ambalo linaweza likafanya kazi yake vizuri na likapeleka gawio Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mtaji siyo lazima utoke direct kwenye Serikali lakini bado Serikali ina uwezo wa kutoa guarantees na kulifanya hili shirika liweze kusimama na kujiendesha kibiashara. Kipindi kile TTCL ilikuwa haiwezi sana ku-move, inawezekana ni kwa sababu tu ya mwingiliano wa maslahi ya kibiashara, kwa sababu kuna component ambapo Airtel naye alikuwa tayari ni shareholder pale wakati wanafanya the same business.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali kama hiyo shirika lisingeweza kwenda kwa sababu kuna mdau mwingine
ambaye alikuwa ndani ya TTCL yenyewe na yeye anafanya biashara ambazo zinafanana lakini sasa hivi huyo mdau hayupo. Kwa hiyo naamini kwa sababu ya shirika kuwa ni asilimia 100% government ownership lina uwezo wa kwenda na ku-compete kama ambavyo yanafanya mashirika mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumziwa suala la Mkongo wa Taifa. Mkongo wa Taifa ni mali ya Serikali kwa hiyo katika hali ya kawaida huu Mkongo wa Taifa kwa sasa kwa namna tunavyokwenda apewe TTCL moja kwa moja ili aweze kuimarisha hiyo miundombinu na aingie kwenye soko akiwa tayari ana nguvu za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo ilo eneo la Data Center kwa sababu ni mali ya Serikali hatuna sababu TTCL isipewe umiliki wa moja kwa moja Data Center hizo. Vilevile tuangalie hizi Data Center ambazo zinaanzishwa nje ya ule mfumo wa Data Center ya Kitaifa, naamini kwamba Serikali ina nguvu na uwezo wa kutosha kuhakikisha ina-control hiyo na wote ambao wanatumia data wakatumia data hizi za TTCL ili mwisho wa siku ziweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii Sheria ya Procurement, TTCL sasa hivi anaenda kwenye ushindani, hawa wenzake hawana vizuizi katika kufanya business na katika kuagiza baadhi vifaa ambavyo vinaweza vikafanya waweze ku-dominate soko la biashara. Kwa hiyo, kuna haja ya kuangalia kwa maana ya kutoa exemption fulani fulani katika hii Sheria ya Procurement ili kuifanya hii TTCL iweze kufanya biashara yake smoothly.

Mheshimiwa Naibu Spika, la sivyo wakati wengine wana uwezo wa kuagiza vifaa na components zozote bila kizuizi chochote sisi wakati tunaiwekea kizuizi kampuni yetu ya TTCL, naamini kabisa uwezekano wa kuingia kwenye competition na kudumu kwenye soko utakuwa ni mdogo. Hatukatai kwamba hii sheria ipo, ni kweli ipo lakini kwenye baadhi ya maeneo ambayo tunaona kwamba inaweza ikawa ni kipingamizi au kizuizi cha kufanya biashara yake vizuri basi TTCL apewe hizo exemptions ili aweze kufanya hiyo biashara ili mwisho wa siku ijiendeshe kwa faida na Serikali ipate gawio lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo upungufu ambao TTCL ya sasa inayo na naamini upungufu huo ndiyo uliopelekea kubadilishwa kwa sheria. Upungufu wa kwanza ni kwamba mdau aliyekuwepo ndani alikuwa na yeye ni mshindani kwenye biashara. Kwa hiyo, kutoweka kwake ndiyo maana sasa tunaileta ile sheria ya kwamba kwa nini tunatoka sasa kwenye kampuni kuja kwenye shirika? Tunatoka kwenye kampuni kuja kwenye shirika kwa sababu ni 100% government ownership, ni jibu rahisi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunapokuwa tunazungumzia biashara, biashara inafika kipindi inakuwa na kikomo, biashara inategemea mazingira, jibu linakuja kwamba mazingira ya sasa hairuhusu TTCL kujiendesha kama inavyojiendesha na ndiyo maana Serikali inaleta Muswada huo. Kwenye business life cycle, business inapitia challenges nyingi, sasa hatuwezi kubaki stagnant eti kwa sababu tu kwa nini ulianzisha vile, kwa nini ulianzisha vile, teknolojia imebadilika, mazingira ya ufanyaji biashara yamebadilika na ndiyo maana na sisi sasa tunapaswa kubadilika ili tuweze ku-move. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuwa haiwezi kutoa mchango wake kwa sababu kulikuwa na percentage kwenye share, hilo nalo limepelekea Serikali kuleta Muswada huu kwa sababu huwezi kupeleka tu kama unavyotaka wakati huo kuna mwingine mnaye pale mnapaswa mjadiliane. Kwa hiyo, inategemea wakati mwingine mnaweza mkawa na convincement power ya namna gani ili kuweza kumshawishi mbia muweze kwenda sawa. Sasa hivi ni 100% government ownership, kwa hiyo inaweza ikatengeneza bila kuhujumiwa na mtu mwingine yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mamlaka au madaraka au uhuru usiokuwa mipaka. Nakubali CEO na Bodi yake ifanye kazi kwa uhuru, lakini lazima kuwepo na scenario ambayo Serikali kama mwenye kampuni aweze kuona nini kinachoendelea. Mimi siamini kwamba Waziri atakuwa kazi yake kuleta directions tu kwa Bodi au CEO na atakuwa anafanya hivyo kwa sababu ya kupewa ushauri fulani fulani. Kwa hiyo, naamini ile component pale ya Waziri iendelee kuwepo kwa maana Waziri ndiyo aliyepewa mamlaka na Serikali katika kuhakikisha kwamba anahakikisha ile taasisi inakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna uhuru usiokuwa na mipaka ila ijaribu tu kuangaliwa kwamba ule uhuru au ile dhamana ambayo Waziri anayo ifanyiwe marekebisho kiasi ambacho haitaifanya kampuni iweze kutetereka au kurudi nyuma katika kufanya biashara zake za kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niishie hapo, lakini niendelee kusisitiza tu taasisi hii inayokuja ni lazima ipewe mtaji, taasisi inayokuja ule Mkongo wa Taifa uumiliki kwa 100%, Data Center imilikiwe na TTCL na taasisi zote za kiserikali zitumie data za TTCL kwa sababu TTCL ni baba na mama wa hivyo vitu. Kwa hiyo, inapokuwa kwamba wewe mwenyewe unayo taasisi ambayo inafanya kazi hiyohiyo halafu wewe ni mmoja unatoka unaenda kufanya kazi kwenye taasisi nyingine nadhani haiwi nzuri sana. Nipende kushauri kwamba taasisi zote za kiserikali, taasisi za umma zitumie TTCL katika matumizi yake ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi hii.