Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Goodluck Asaph Mlinga (11 total)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Mradi wa umwagiliaji Lupilo umesimama na haujulikani ni lini utaendelea kujengwa:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Jimbo la Ulanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechagua skimu za kimkakati katika maeneo ya uwekezaji wa kilimo ikiwemo Bonde la Mto Rufiji na Kilombero. Skimu hizo ni pamoja na eneo la Lupilo Ulanga, eneo la Sonjo Kilombero na eneo la Itete Malinyi. Ili kuendeleza skimu hizi Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa skimu za Lupilo na Sonjo pamoja na ujenzi wa skimu ya Itete.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza skimu ya umwagiliaji ya Lupilo, Serikali imefanya upembuzi yakinifu wa skimu ya Lupilo yenye eneo la hekta 4000. Kazi zilizofanyika ni pamoja na uchunguzi wa udongo, uchunguzi wa athari za mazingira, upimaji, uchunguzi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii, uchunguzi wa rasilimali maji, usanifu wa awali na makisio ya gharama za ujenzi wa skimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa na gharama za ujenzi wa skimu ya Lupilo Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuendeleza skimu hii.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia matibabu kwa watumishi wa Serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini:-
(a) Je, hadi sasa ni Taasisi na Mashirika ya umma mangapi yamejiunga na mfuko huo?
(b) Je, ni Taasisi na mashirika ya umma mangapi hayajajiunga na mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Ulanga lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia matibabu kwa watumishi wa Serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 idadi ya wanachama katika mfuko ni 792,987 kutoka
wanachama 474,760 mwaka 2012. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, mfuko umefanya maboresho mbalimbali ya vitita vya mafao na namna ya kuchangia kwa makundi mbalimbali ya jamii. Maboresho haya yamewezesha kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanachama walio katika mfumo huu wa bima ya afya nchini na kufanya wanufaika kufikia asilimia nane. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2016
idara za Serikali, taasisi na mashirika ya umma zilizotumia huduma za bima ya afya za NHIF zimefika 307. Idadi hii imetokana na jitihada za makusudi za kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na Bima kwa watumishi wa umma.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mashirika, taasisi na idara za Serikali ambayo hayajajiunga na mfuko yapo 23 yakiwemo TRA, BOT, TANESCO, NHC, TPA, PSPF, LAPF, PPF, EWURA, NCA na GEPF. Mfuko unaendelea na jitihada za kukutana na uongozi wa mashirika haya ya umma kwa lengo la kutoa elimu na kuwahimiza juu ya umuhimu wa kujiunga kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Mfuko.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y. MHE. GOODLUCK A. MLINGA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kuwapatia wananchi wa Kata za Lupiro, Iragua, Milola na Minepa eneo la ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero kwa ajili ya makazi na kilimo pindi tu atakapoingia madarakani. Je, utekelezaji wa ahadi hiyo imefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi kumaliza matatizo ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo maeneo ya kata nne zilizotajwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 22(e). Hata hivyo, utaratibu wa kushughulikia ahadi hiyo katika kata hizo haukutajwa kuwa ni kwa kumega sehemu ya ardhi oevu katika Bonde la Mto Kilombero. Napenda kutumia fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kazi ya kushughulikia tatizo hili la ukosefu wa ardhi kwa wananchi wa kata hizo limeanza kupitia Mradi wa KILORWEMP, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Wilaya za Malinyi, Kilombero na Ulanga.
Mheshimiwa Spika, kazi hii inafanyika kwa umakini mkubwa ili kuepuka kukiuka misingi na dhana nzima ya uhifadhi, kwanza kwa kuzingatia vigezo na umuhimu wa ardhi oevu na pili kwa kuhakiki mipaka halali ya vijiji yaani village approved survey plans. Aidha, kupitia Land Tenure Support Program unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji inaandaliwa hadi hatua ya kutoa hati miliki za kimila kwa vijiji vyote vinavyozunguka Bonde la Mto Kilombero.
Mheshimiwa Spika, suala hili pia linafanyiwa kazi sambamba na maombi ya wananchi kupitia wawakilishi wao wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Madiwani ambayo yamekuwa yakipelekwa katika ngazi mbalimbali likiwemo Bunge lako Tukufu. Kazi hii ni shirikishi, wananchi wa kata na vijiji katika Wilaya husika wanashirikishwa kikamilifu hadi kufikia maridhiano ya pamoja. Kwa mfano, katika Kijiji cha Igawa, Kata ya Igawa, Wilaya ya Malinyi, baada ya kufikia maridhiano na kwa kuzingatia vigezo vya pande zote, eneo la kijiji liliongezeka kutoka kilometa za mraba 39.8 hadi 86.97 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 118.5. Eneo la Kijiji cha Sofi Majiji liliongezeka kutoka kilometa za mraba 93.9 hadi ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 16.1. Kuongezeka au kupungua kwa eneo kunatokana na vigezo vilivyowekwa ingawa hadi sasa hakuna kijiji kilichopoteza eneo.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ (K.n.y. MHE. GOODLUCK MLINGA) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanyama waharibifu kama vile viboko na tembo kwenye maeneo ya mashamba katika Kata za Ruaha, Chilombola, Ilonga, Ketaketa, Mbuga ya Lukande na Lupilo.
Je, Serikali ina mpango gani kuzuia uharibifu huo wa mazao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo na ongezeko la wanyama wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Kata ya Ruaha, Chilombola, Ilonga, Ketaketa, Mbuga ya Lukunde pamoja na Lupilo. Kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyama waharibifu hususan tembo na viboko, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kunusuru maisha na mali za wananchi. Hatua hizo ni pamoja na:-
(a) Kufanya doria za wanyamapori wakali na waharibifu ili kudhibiti madhara ya wanyamapori hao kwa kutumia Askari Wanyamapori waliopo katika Pori la Akiba Selous eneo la Ilonga, Kikosi Dhidi ya Ujangili pamoja na Askari Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya Mahenge;
(b) Kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii kuhusu kujiukinga na wanyamapori wakali na waharibu wakiwemo tembo na viboko;
(c) Kuendelea na mbinu mbalimbali za kupunguza madhara yatokanayo na uvamizi wa tembo na kukuza kipato kwa mfano matumizi ya mizinga wa nyuki, oil chafu na kilimo cha pilipili kuzunguka mashamba na kadhalika; na
(d) Aidha, Wizara imekuwa inafanya majararibio ya kutumia ndege zisizokuwa na rubani yaani drones kwa ajili ya kufukuza tembo pindi wanapovamia makazi na mashamba ya wananchi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Ulanga imezungukwa na Hifadhi ya Selous Game Reserve hivyo kufanya wananchi wa Kata za Mbuga, Ilonga, Kataketa na Lukunde kukosa maeneo ya kilimo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa maeneo hayo maeneo ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Selous lilianzishwa kati ya mwaka 1896 na 1912 na Serikali ya Kikoloni ya Wajerumani. Wajerumani waliligawa pori hilo katika maeneo manne ambayo ni Ulanga, Kusini, Muhoro na Matandu. Mnamo mwaka 1951 pori hili lilisajiliwa rasmi kwa GN Na. 17 chini ya Fauna Consveration Ordinance CAP. 302.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba la Selous ni muhimu sana kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni siyo tu kwa Taifa letu bali pia Kimataifa. Pori linaliingizia Taifa fedha za Kitanzania na za kigeni kupitia utalii, lina misitu ya Ilindima inayosaidia upatikanaji wa maji, linachangia kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi na makazi na mazalia ya viumbe hai wakiwemo wanyamapori, samaki na viumbe wengine. Kutokana na umuhimu huo Umoja wa Mataifa umelitambua eneo hili kuwa urithi wa dunia. Sambamba na hilo Serikali ya Kikoloni ilianzisha pori tengefu la Kilombero mwaka 1952 ili kuunganisha mfumo wa kiikolojia katika maeneo hayo awili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto za matumizi ya ardhi katika maeneo yaliyotajwa, Serikali inatekeleza mpango wa Kilombero na Lower Rufiji Wetlands Ecosystem Management Project, mradi huu unahusisha kutatua matatizo ya mipaka ya vijiji na mapori ya hifadhi yaliyo katika Wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero pamoja na kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kupitia hati miliki za kimila.
Aidha, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mradi wake wa Land Tenure Support Programme (LTSP) inaendelea kuhakiki mpaka wa pori tengefu la Kilombero ambalo ni sehemu ya Wilaya ya Ulanga na kupima ardhi ya vijiji kwa ajili ya urasimishaji wa ardhi kwa wananchi na hatimaye kupata hati za kumiliki. Serikali inaamini kuwa kupitia miradi hii miwili changamoto ya matumizi ya ardhi kwa shughuli za kilimo, ufugaji na makazi zitatatuliwa kikamilifu.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Wilaya ya Ulanga ina ongezeko la mifugo; ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe lakini hakuna huduma za mifugo kama vile majosho:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majosho?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu ongezeko la mifugo katika wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Ulanga inayokadiriwa kuwa na idadi ya mifugo kama ifuatavyo: Ng’ombe 70,000; mbuzi 16,000 na kondoo 6,373.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imepokea ombi la Mheshimiwa Goodluck Mlinga na kwa kushirikiana na wadau wengine litazingatiwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Ifakara mpaka Mahenge Mjini ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao kama mpunga, mahindi, ufuta, ndizi na maharage. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck A. Mlinga Mbunge wa Ulanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ifakara, Mahenge yenye urefu wa kilometa 70 ni sehemu ya barabara ya Mikumi - Ifakara - Mahenge - Lupiro - Malinyi - Londo, Lumecha ambayo ina kilometa 587.8 inayounganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma. Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unatekelezwa kwa awamu kulingana upatikanaji wa fedha ambapo kwa sasa tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mikumi mpaka Kidatu ambayo ina kilometa 35 pamoja na ujenzi wa daraja la Magufuli katika mto Kilombelo na barabara unganishi yenye urefu wa kilometa 9.142.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasasa ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Kidatu - Ifakara yenye kilometa 66.9 unayojumuisha Daraja la Mto Ruaha Mkuu (Great Ruaha) umeanza. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni kwa barabara ya Ifakara mpaka Mahenge, Lupiro - Malinyi - Londo hadi Lumecha umekamilika toka mwezi huu mwanzoni. Hivyo ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki ikiwemo na sehemu ya Ifakara mpaka Mahenge yaani kilometa 70 utatekelezwa kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-

Wilaya ya Ulanga ina Shule za Msingi zaidi ya 50 na Sekondari zaidi ya 17 lakini haina Chuo chochote ambacho Wanafunzi wanaomaliza masomo kwenye shule hizo wanaweza kujiunga:-

Je, Serikali inasema nini juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Ulanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya elimu na mafunzo katika kuandaa rasilimaliwatu itakayochangia katika kufikia azma ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha vyuo vilivyopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza nafasi za udahili na kuimarisha ubora wa elimu na mafunzo yatolewayo. Aidha, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa vyuo vya VETA za Mkoa na Wilaya kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ulanga ni moja kati ya Wilaya zenye uhitaji mkubwa wa vyuo vya elimu na mafunzo. Wilaya ina chuo kimoja tu cha ufundi stadi cha Mtakatifu Francis kinachomilikiwa na sekta binafsi. Wakati Serikali inaendelea na jitihada zake za upanuzi na ujenzi wa vyuo, natoa wito kwa Wilaya zote zenye uhaba wa vyuo vya elimu na mafunzo kutumia vyuo vilivyopo nchini.
Kumekuwa na tatizo kubwa katika jamii yetu la ubakaji wa watoto wadogo chini ya miaka mitano na vikongwe:-

Je, Serikali imeshawahi kufanya utafiti ili kujua chanzo cha tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili hasa ubakaji kwa watoto na vikongwe. Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi za mwaka 2018 za makosa ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, hali ya vitendo vya ukatili kwa watoto nchini imeongezeka kutoka matukio 13,457 mwaka 2017 hadi matukio 14,419 mwaka 2018 ambalo ni ongezeko la makosa 1,034 sawa na asilimia 7.7. Mikoa inayoongoza kwa matukio haya ni pamoja na Tanga ikiwa na matukio 1,039, Mbeya 1,001, Mwanza 809, Arusha 792 na Tabora 618. Makosa yanayoongoza ni ubakaji (5,557), mimba za utotoni (2,692), ulawiti (1,159), shambulio (965) na kujeruhi (705).

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009 Serikali kwa kushirikiana na UNICEF ilifanya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto. Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 60 ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hufanyika majumbani ambapo vitendo hivi hufanywa na watu wa karibu na watoto wakiwemo baadhi ya wazazi, walezi, watoa huduma wa vyombo vya usafiri, majirani na wanafamilia na asilimia 40 ya vitendo hivyo vya ukatili hufanyika shuleni. Aidha, sababu kubwa ya vyanzo vikubwa vya ukatili ni pamoja na imani potofu, elimu au hali duni ya umasikini, kutetereka kwa misingi ya malezi ndani ya familia, mila na desturi potofu na utandawazi. Aidha, hakuna utafiti uliofanyika kuhusu ubakaji wa vikongwe ingawaje vyanzo vya ukatili vinashabihiana na ule wa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua jukumu lao la malezi na matunzo kwa watoto na wazee ambao ni hazina na tunu muhimu katika Taifa letu. Mwisho, napenda kutoa rai kwa jamii kutoa taarifa na ushirikiano kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika hao.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-

Nchi yetu imebarikiwa kuwa na Hifadhi nyingi zenye wanyama wengi wa kuvutia lakini mapato yatokanayo na utalii ni kidogo: Je, Serikali ina mikakati gani ya kuongeza mapato ya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MAIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Mathalan idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia watalii 1,505,702 mwaka 2018. Katika kipindi cha mwaka 2018 pekee Sekta hii imechangia katika uchumi wa nchi Dola za Marekani bilioni 2.4, sawa na takriban trilioni 5.4. Sekta hii imechangia kwa wastani wa asilimia 17 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha, inatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja milioni 1.6. Hata hivyo, kiwango cha mchango wa sekta hii bado ni kidogo ukilinganisha na rasilimali tulizonazo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Wizara yangu imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini na mchango utokanao na sekta hii. Mikakati hiyo ni pamoja na kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kupitia Mradi wa REGROW ambapo Serikali inaendelea kufungua utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini kwa kuimarisha miundombinu ili kuboresha shughuli za utalii hususani katika hifadhi za Taifa za Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Nyerere. Aidha, Serikali imeanzisha Hifadhi mpya za Taifa sita ambazo ni pamoja na Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa, Rumanyika-Karagwe, Mto Ugalla, Nyerere na Kigosi. Lengo la Serikali ni kufungua na kutumia fursa za utalii nchini katika mikoa yote.

Mheshimiwa Spika, kadhalika Serikali imekusudia kuongeza mazao ya utalii. Hivi sasa, hapa nchini tumejikita zaidi katika kuziendeleza hifadhi za Taifa. Tunataka kuhakikisha kw amba mazao mengine ya utalii kama utalii wa kuvinjari kwa meli, utalii wa kupunga upepo fukwe na utalii wa mikutano ukiongezeka.

Mheshimiwa Spika, sanjari na juhudi hizo, Mwezi Septemba, 2019 Wizara yangu kwa kushirikiana na Nyanda za Juu Kusini iliandaa kwa kushirikiana na Sekta Binafsi maonesho makubwa ya utalii Jukwaa la Uwekezaji yajulikanayo kama Karibu Utalii Kusini ambapo zaidi ya washiriki mia tano kutoka ndani na nje ya nchi walishiriki. Vilevile, Mwezi Oktoba, 2019 Wizara iliandaa Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo lililohusisha wafanyabiashara wakubwa wa utalii takribani 400 na Mawakala wa Kimataifa 200 kutoka ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kigoma na Tabora imeanza maandalizi ya maonesho makubwa ya Kimataifa ya jukwaa la utalii na uwekezaji yanayojulikanayo kama Great Lakes International Tourism Expo ambayo yatafanyika Mwezi Juni, 2020. Imani yangu kuwa mikakati hii itasaidia kutangaza vivutio vya utalii, vya uwekezaji na kuongeza watalii nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati hiyo, Wizara imeendelea kuimarisha shughuli za utangazaji wa vivutio vya utalii wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kufungua masoko mapya nchini China, India, Urusi na Israeli. Aidha, katika kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali, Wizara imekamilisha ujenzi wa mfumo funganishi wa kieletroniki kwa ajili ya kusajili na kutoa leseni, na kukusanya takwimu sahihi.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Awamu ya Tano, katika kuboresha miundombinu nchini ikiwemo viwanja vya ndege, ujenzi wa reli, upanuzi wa bandari, kuimarika kwa Shirika la Ndege ambalo limeanza kuhudumia watalii wa ndani na nje ya nchi. Juhudi hizi zitasaidia sana kukuza Sekta ya Utalii nchini. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-

Majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Ulanga ni machache, madogo na machakavu hasa yale ya kulaza wagonjwa:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo na ujenzi wa majengo mapya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuikarabati na kuipanua Hospitali ya Wilaya ya Ulanga ambapo mwezi Mei, 2019, Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 400 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri imetenga shilingi milioni 60 kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kukarabati Hospitali ya Wilaya hiyo. Ahsante.