Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Goodluck Asaph Mlinga (46 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kuwapa pole wananchi wangu Ulanga kwa janga la ajali ya kivuko. Ajali hii ya Ulanga siyo ya kwanza, nashangaa Ulanga sijui tumeikosea nini Serikali hii. Daraja mwaka wa tatu haliishi, miradi yote mikubwa inakuja inakwisha, ile ya Kigamboni imekwisha, mradi wa mabasi yaendayo kasi umekwisha, daraja la Ulanga haliishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wakandarasi waliopewa mradi ule kila mwaka wanaomba kuongezewa muda. Nashangaa wakati wanaomba kujenga lile daraja walikuwa hawajui kama kuna kipindi cha masika? Kwa mfano, sasa hivi hawapo, ujenzi hauendelei. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Fedha alisimamie suala hili kwa sababu sasa hivi mafuta hayaendi Ulanga, bidhaa haziendi Ulanga, vile viboti vidogo walivyoweka kwa ajili ya kuwavusha watu mvua zikinyesha haviwezi kufanya kazi. Mimi mwenyewe shahidi juzi nilivyoenda nimenusurika kifo. Tumefika katikati ya mto boti limezimika. Kwa hiyo, ili kuwanusuru wananchi wa Ulanga naomba tuwasaidie kile kivuko kisitumike tena, daraja liishe wananchi wanufaike na daraja lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili, naomba nimpongeze Rais Magufuli na uongozi wote uliochaguliwa. Nampongeza Mheshimiwa Magufuli kwa utendaji wake, nawashangaa ndugu zangu Wapinzani wanasema kuwa Mheshimiwa Magufuli anatekeleza Ilani yao, sasa kama anatekeleza Ilani yenu mbona mnalalamika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuongea Bungeni, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya familia, kwa ofisi za Bunge kwa namna walivyoshughulikia ugonjwa wa mama yetu mpendwa Celina Kombani, walivyoshughulikia shughuli yote ya msiba. Napenda kutoa shukrani za pekee kwa mama yangu Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Angellah Kairuki na Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa jinsi walivyolichukulia suala lile na kuchukua nafasi ya mzazi. Naomba waendelee kutuchukulia hivyohivyo kama watoto wao, hatuna cha kuwalipa bali tunawaombea maisha marefu yenye afya na mafanikio makubwa. Pia siwezi kusahau uongozi wa Chama cha Mapinduzi kwa namna walivyotusaidia katika msiba ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Rais mstaafu Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa uongozi wake mahiri wa miaka kumi kwa kutunza amani na utulivu. Pia napenda kuipongeza Serikali ya CCM kwa kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa demokrasia ya hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa kusoma kwake hotuba kwa umahiri. Ila nilikuwa napenda kumwambia kuwa katika level ya Ubunge kuna vitu vya ku-present mbele za watu siyo kila anachoandikiwa asome. Akili za kuambiwa uchanganye na za kwako. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ku-declare interest nimeoa mchaga, Mheshimiwa Mbowe ni mkwe wangu, sasa mkwe kuonyesha udhaifu mbele ya mkwe wake ni aibu. Tunapozungumzia Upinzani Bungeni tunamzungumzia Mheshimiwa Mbowe. Sasa naomba nimpe taarifa kuwa mkwe wake nipo humu Bungeni, hatakiwi kuonyesha udhaifu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mpango wa kuimarisha umeme vijijini, naomba niwape taarifa, kipindi cha masika Ulanga umeme haupatikani. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Muhongo umeme umefika Ulanga lakini zile fito walizoweka za kupeleka umeme kipindi cha masika zote huwa zinavunjika kwa hiyo hatupati umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mto Kilombero pale unatuletea mafuriko kila mara. Naomba ufanyike mradi kama ulioko Mto Ruvu. Badala ya mto ule kutuletea mafuriko tutumie yale maji kwa kuyanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau upande wa viwanda, Ulanga kuna Kiwanda cha Pamba lakini hakijaingizwa katika mpango huo wa kufufuliwa. Nimeona sehemu zingine tu lakini Ulanga imesahaulika. Bila kuisahau Morogoro, Morogoro ndiyo ulikuwa mkoa ambao unaongoza kwa kuwa na viwanda vingi lakini sasa hivi yamebaki magofu, sijaona mpango wa kufufua viwanda vya Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi na kwa sababu ndiyo naanza haya yanawatosha. (Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ulanga imekuwa na ongezeko kubwa la mifugo kutokana na kuwa na eneo zuri kwa ajili ya malisho pamoja na migogoro inayoendelea katika wilaya za jirani kati ya wakulima na wafugaji. Hivyo, naiomba Serikali, kwanza kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuweka mazingira bora kwa ajili ya wafugaji ili kuweza kujenga majosho na marambo kuepusha wafugaji hawa kutohamahama kwani katika wilaya yangu japo huwa kuna ng‟ombe zaidi ya 20,000 lakini hakuna huduma hata moja ya mifugo. Pia kuipatia usafiri Idara ya Mifugo ili iweze kutoa huduma kama chanjo kwa mifugo hiyo na kutoa huduma kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yana mifugo mingi mpaka sasa ni yafuatayo:-
(i) Kata ya Iragua – ng‟ombe zaidi ya 6,000 hakuna majosho;
(ii) Kata ya Lukande – ng‟ombe zaidi ya 4,000 hakuna huduma yoyote;
(iii) Kata ya Mawimba – ng‟ombe zaidi ya 3,000 hakuna huduma yoyote;
(iv) Kata ya Milola – ng‟ombe zaidi ya 4,000 hakuna huduma yoyote; na
(v) Kata ya Uponera – ng‟ombe zaidi ya 2,000 hakuna huduma yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ulanga kuna miradi mingi ya kilimo cha umwagiliaji lakini hakuna hata mradi mmoja uliokamilika. Hivyo, naiomba Serikali kunipa majibu ni lini miradi hiyo ya umwagiliaji itakamilika ili iweze kusaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Ulanga?
Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi; Wilaya ya Ulanga tuna Mto wa Kilombero lakini watu wanaoishi kuzunguka mto huo hawajawezeshwa namna bora ya kufanya uvuvi na kupelekea uvuvi haramu ambapo kumeleta uhaba wa samaki. Hivyo, naiomba Serikali kuweka mpango mzuri ili watu wanaoishi maeneo ya mto wafaidike na uvuvi.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami siko mbali na Waheshimiwa Wabunge wengine. Cha kwanza naomba nikupe pongezi wewe kwa umahiri wako wa hali ya juu. Mheshimiwa Tulia ninachokuomba wewe tulia, hawa tuachie sisi; sisi tutawatuliza. (Kicheko)
Waheshimiwa Wabunge, naomba niwaambie kitu kimoja; hawa Wabunge wa Upinzani siyo kwamba wanamchukia Mheshimiwa Tulia na siyo kwamba hawamtaki, wanampenda na wanamwamini. Mkitaka mliamini hilo, mwaangalie asubuhi, wanakuja hapa, anawaombea dua, wanaenda kufanya uhalifu mtaani. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Watanzania kupitia Bunge hili, wanachofanya Wabunge wa Upinzani wakitoka hapa, wengi wanashinda kwenye jackpot, kwenye betting station, kwenye bars, usiku kucha, wakija hapa wanaombewa dua, wanaenda tena kufanya uhalifu. Naomba niwaambie, Wabunge wa Upinzani wakati Serikali ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete (Mstaafu), walisema Rais yule ni dhaifu. Alipoanza Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli, wakasema Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete (Mstaafu), hachomoki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaulize, kati ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete na wao nani hachomoki? Wakienda mtaani wanakutana na IGP Mangu, mzee wa Tii Sheria Bila Shuruti, hawachomoki; wakienda Serikalini wanakutana na JPM akisaidiwa na Mheshimiwa Samia Suluhu, hawachomoki; wakija Bungeni wanakutana na Mheshimiwa Tulia, umetulia kwenye kiti chako, hawachomoki; wakija kwa Wabunge, wanakutana na Mlinga, hawachomoki! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mpango kwa kazi yake nzuri anayofanya. Kuna methali isemayo kuwa mgema akisifiwa, tembo hulitia maji. Mheshimiwa Mpango amepanga kote amemaliza, sasa akaamua kutupanga na sisi Wabunge. Mheshimiwa Mpango, mimi sikatai kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge, ila masikitiko yangu ni kuwa Mheshimiwa Waziri Mpango umefikiria, umefika mwisho ukaamua utugeuze na Waheshimiwa Wabunge kama source of income. Hilo halikubaliki! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango hii ya Mheshimiwa Mpango, tukiliruhusu hili mwakani atasema tuuze magari yote ya Serikali, tutumie baiskeli na pikipiki; mwaka unaofuata atasema Ikulu tupangishe, Rais akaishi Mbagala. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango hii, hatuwezi tukakubali, inatakiwa kitendo cha kuwapa misamaha ya kodi viongozi wa Tanzania ilikuwa kama chachu; ilikuwa tuanze viongozi tuwasamehe kodi, tuje wafanyakazi tuwasamehe kodi. Tafuta vyanzo vingine, lakini siyo hili. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mpango amesema katika bajeti yake tukate makato kwenye miamala ya transaction za simu; jamani Mheshimiwa Mpango, kwa sababu huijui adha ya wapiga kura, hizi Tigo-Pesa na M-Pesa, wanatumia wananchi wa kawaida kabisa ambao wameshindwa kumudu gharama za Benki. Kwa sababu ungewahi kuwa hata Mwenyekiti wa TUGHE, ungejua mpiga kura maana yake nini. Makampuni ya simu haya hatujayatoza kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami, nenda kaangalie transaction za Tigo, Vodacom kwa kiwango kile kile cha pesa, gharama zinatofautiana. Ndiyo ujue hawa watu hawalipi kodi. Miamala ya internet hailipiwi kodi; mpaka leo hii Tanzania hatuna mfumo rasmi wa ukusanyaji kodi katika makampuni ya simu. Wafanyakazi ndiyo wanakandamizwa. Mfanyakazi kabla hajaingiziwa hela yake kwenye akaunti ameshakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Wizara ya Fedha mnakaa mnakubaliana na mmiliki wa kampuni ya simu, ulipe kodi kiasi gani; hatuendi hivyo. Inatakiwa muweke mfumo maalum wa makampuni ya simu yawe yanalipa kodi, kulingana na sisi tunavyotumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba Waziri anafahamu, TRA ndiyo wanaokula pesa za makampuni ya simu, TCRA ndiyo wanaokula fedha za makampuni ya simu; hawa hawalipi kodi. Mnakula nao, mna kazi ya kuwakandamiza Watanzania wadogo, wananchi wa Tanzania leo hii tutawaambia nini tutakaporudi huko? Wafanyakazi wetu kwa mfano Walimu, wanafanya kazi ngumu sana katika nchi hii. Napendekeza kwa upande wa Walimu, kile Chama cha Walimu, tuwaondolee kwa sababu kile inawanyonya na hiyo iwe option, Walimu wanapoanza kazi kujiunga ili kuwapunguzia mzigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu hawa tuwaondolee malipo ya NHIF. Serikali iwalipie asilimia 100 ili tuwapunguzie mzigo Walimu. Walimu wa Ulanga kule, Mwalimu anaenda kituo cha kazi hajawahi kufika kijijini, hakuna nyumba, hakuna umeme, makato ni makubwa katika mshahara wake, kwa nini asijiburudishe na wanafunzi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye tozo za watalii, ndiyo maana nasema Mheshimiwa Mpango, umekuja na mipango ambayo haitekelezeki. Umeongeza VAT kwa watalii, unategemea hawa watalii watakuja? Si wataenda sehemu nyingine? Kwani tembo tunao sisi tu? Hata nchi nyingine wanao tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, amekuja kwenye tozo za magari; naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, hivi anapoandika jina pale Profesa Maji Marefu, inaigharimu nini Serikali mpaka aongeze kwenda milioni 10? Kwa nini asishushe iwe shilingi milioni mbili? Sisi haitugharimu chochote, tunachotaka ni mapato, pale huongezi mapato; wale watu wataacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja suala la tatu, unapoongelea kuinua maisha ya wananchi wa Tanzania ni pamoja na wananchi wa ulanga.

TAARIFA ....

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naifuta hiyo kauli, lakini sikudhamiria kama walivyofikiria. Nawaomba radhi Walimu wote, sikudhamiria kama walivyofikiria, nimetoa mfano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapoongelea kuinua kipato cha wananchi wa Tanzania ni pamoja na wananchi wa Ulanga. Barabara kutoka kivukoni mpaka Mahenge haipitiki. Ulanga tunalima ndizi; karibu kila familia inalima ndizi, barabara ile mngetuwekea lami, tungekuwa tunauza ndizi Mjini. Kila familia ingeweza kuongeza kipato chao. Ulanga tunalima mpunga lakini barabara haipitiki, hatuwezi kutoka kuuza mpunga mjini. Robo ya mpunga wa Tanzania unatoka Ulanga, lakini leo hii hatuwezi kuleta mpunga mjini kwa sababu ya gharama kubwa za usafirishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea viwanda, tunaongelea umeme. Ilagua leo hii hakuna umeme tunashindwa kutengeneza viwanda vidogo vidogo, mtuwekee umeme ili tutengeneze viwanda vidogo vidogo ili tuongeze mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea kuinua kipato cha Mtanzania ni pamoja na mawasiliano ya wananchi wa Ulanga. Wananchi wa Ulanga leo hii hawana mawasiliano ya simu, ukizingatia hata watu wa Ilagua, mtu anatembea kilomita 20 kwenda kumpa taarifa, badala angetumia muda ule kuzalisha mali ili Serikali ipate kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea kuinua kipato cha Mtanzania ni pamoja na huduma za afya. Wananchi wanatumia muda mwingi kwa ajili ya kusotea kupata huduma za afya. Wananchi wangu wa Lupilo hawapati huduma za afya nzuri, kwa hiyo, wanatumia muda mwingi kutembea kwenda mbali kupata huduma za afya, badala muda huo wangeutumia kuzalisha ili Serikali ipate kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho, nataka kumwambia Mheshimiwa Waziri ameongelea suala la Wabunge kuwa sawa na wafanyakazi wengine. Waheshimiwa Wabunge tumeingia NHIF, nilishasema katika Bunge lako hili, kwa nini sisi Wabunge tumeingia, Mashirika ya Umma hayaingii NHIF, nataka nimwambie leo hii Mheshimiwa Waziri, baadhi ya makampuni ya private insurance walinifuata, wakaniambia dogo, unapiga mayowe mno Bungeni, badala uongee herufi kubwa tukupooze unaenda kupiga makelele. Naomba niwaambie kupitia Bunge lako hili, kwanza mimi bado mdogo, siwezi kuongea herufi kubwa. Suala la pili hawawezi kunipooza mpaka wawapooze Watanzania na umaskini walionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hawa waingie NHIF ili kuongeza kipato cha Serikali. Mashirika mengi kama PSPF, PPF, NSSF,TANESCO, LPF, NMB, TCRA, NHC hawataki kwenda NHIF kwa sababu kuna yale makampuni ya private insurance wana hisa mle; na kama hawajaingiza majina yao, wameingiza majina ya wake zao; na kama hawajaingiza majina ya wake zao wameingiza majina ya watoto wao ili tusiwagundue. Mheshimiwa Mpango, naomba ulisimamie hili ili haya Mashirika yote ya Umma yaingie NHIF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo yangu ni hayo machache, sina mengine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hali mbaya ya Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, majengo ni chakavu na machache. Wataalam (wahudumu wa afya) wapo wachache na wasio na sifa, gari la wagonjwa lipo moja ambalo nililikarabati mimi Mbunge na mahitaji ni makubwa sana; upatikanaji wa dawa bado hauridhishi kutokana na kuchelewa usambazaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, NHIF bado kumekuwa na ugumu kwa baadhi ya mashirika ya umma kujiunga kama takwa la kisheria. Mfano BOT mpaka sasa hawajajiunga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kwa niaba yake naomba radhi kwa hotuba ambayo ameitoa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani hapa Bungeni. Kwa sababu nilishajitambulisha kuwa nilioa huko; kwa hiyo, aibu yake, aibu yangu. (Makofi/Kicheko)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Waheshimiwa Wabunge, ni kweli naomba niwaambie, kama kweli ningekuwepo humu Bungeni asingeweza kutoa ile hotuba na hata mkichunguza mtagundua ile hotuba kama haijaandikiwa mlangoni, basi iliandikiwa humu humu, haraka haraka. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nitoe semina kidogo kwa Waheshimiwa Wabunge.
MWENYEKITI: Mheshimwa Goodluck naomba ukae, kuna taarifa. Wacha tusikilize taarifa...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Goodluck, naomba uendelee.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na umbo langu dogo, lakini leo naomba nitoe semina kwa Wabunge wa Kambi ya wenzetu wa Upinzani.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Waheshimiwa Wabunge, wakati tunakuja kuapa aliitwa Mbunge mmoja mmoja pale mbele, hawakuitwa kundi, sawa! Kwa hiyo, naomba tunapofanya vitu, tufanye kwa maslahi ya Taifa, kwa mtu mmoja mmoja.
Nawapa mfano; sisi Wabunge wa CCM hatuna msalie Mtume. Ukituzingua, tunakupiga chini! Yule mnayemsujudu sasa hivi yuko upande wenu wa Upinzani, Mheshimiwa Lowassa; alituzingua, tukampiga chini.
Mheshimiwa Pinda mwaka 2015 alitetereka, tukataka tumtose, akachomokea dirishani. Kwa hiyo, CCM hatuna habari ya kuambiwa. Kwa hiyo, naomba tusifanye vitu kwa kuambiwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Goodluck naomba ukae. Naomba ukae! Toa taarifa.
T A A R I F A....
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo anayesikika Mwenyekiti, amesema, Mwenyekiti amesema; kila mkisimama hapa, Mwenyekiti amesema. Mimi namfahamu huyo Mwenyekiti kwa sababu nilioa huko tangu wakati niko kwenye mpango mkakati wa kumpata binti yao, yeye Mwenyekiti; nimeoa, yeye Mwenyekiti, nimezaa; mtoto wa kwanza, yeye Mwenyekiti; nimezaa mtoto wa pili, yeye Mwenyekiti. (Makofi/Vigelegele)
Waheshimiwa Wabunge, naomba niwape taarifa tu, sasa hivi niko kwenye mpango yakinifu kwa ajili kumpata mtoto wa tatu lakini yeye haonyeshi hata utaratibu wa kuachia hicho kiti. Huyo atawaambia Mwenyekiti amesema mpaka lini? Sio kila anayevaa kilemba ni fashion, wengine wanaficha mapembe, wengine wananyoa vipara.
Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, naomba tulielewe hilo. Hivyo vitu mtuachie sisi vijana tuvifanye; mambo ya Mwenyekiti kasema, Mwenyekiti kasema!
Waheshimiwa Wabunge, juzi nilisikitika sana kusikia Mbunge amesema anahoji mshahara wa Rais. Cha kusikitisha zaidi huyo aliyehoji mshahara wa Rais yeye anachangia kwenye Chama kila mwezi shilingi milioni tatu lakini hahoji hizo shilingi milioni tatu zinaenda wapi. Mshahara wa Rais uko kwenye Katiba. Angehoji kwanza, shilingi milioni tatu anazochanga kila mwezi kule zinakwenda wapi? Ni kwa sababu Mwenyekiti amesema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha zaidi, kwanza naomba niwapongeze Wazanzibari…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa nane wa hotuba ya Waziri Mkuu umezungumzia masuala ya siasa. Kwa hiyo, nimechagua kuchangia upande wa siasa. (Kicheko/Makofi/Vigelegele)
Waheshimiwa Wabunge, imenisikitisha zaidi hii Mwenyekiti amesema. Ndugu zangu Wazanzibari mmeingia kwenye mkenge wa Mwenyekiti amesema. Mmeambiwa msusie uchaguzi, mbona wao Uchaguzi wa Meya hawajasusia?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Waheshimiwa Wabunge wa Zanzibar, mmeambiwa msusie uchaguzi; sawa jamani! Mmeambiwa msusie uchaguzi. Zanzibar kuna misemo isemayo hivi...
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa Goodluck, naomba ukae chini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nianze kwanza na hoja zilizochangiwa na upande wa Upinzani, kila Wizara inayokuja hapa Wazanzibari wanataja Maalim Seif, Maalim Seif, Maalim Seif.
wananchi ili tuje tuwatetee siyo kumlilia mtu na familia yake. Ninachosikitika zaidi kuna wababa wenye jinsia kama mimi wanamlilia baba mwenzao siwaelewi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie suala la pili, sasa hivi kumekuwa na ugumu Watanzania kupata viza za kwenda China. Ukitaka viza ya China inachukua hadi wiki tatu kuipata, ukiuliza sababu wanasema Watanzania wanafanya uhalifu China. Naomba niulize Watanzania wanaoishi China na Wachina wanaoishi Tanzania wapi wanaofanya uhalifu? Sasa hivi kuna maji feki, matunda feki, mayai feki na maziwa feki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Wachina walioko Tanzania hawafiki hata robo ya Watanzania walioko China kwa nini Wizara wa Mambo ya Nje inakubali na inasimamia unyanyasaji wa namna hii kwa Watanzania? Kila leo tunasikia wanafungwa, sisi tukiwakamata Wachina siku ya pili tunawarudisha kwao, mbona hao wanaokamatwa China hawarudishwi huku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hilo hilo, kupata viza ya kwenda Uingereza ni zaidi ya kwenda peponi.
Ukitaka viza ya Uingereza kuna manyanyaso sijui mpaka upate mwaliko, mbona wazungu wakija huku mnawagongea visa airport pale hamuwahoji wanakuja kufanya nini? Hiyo ni kero kubwa, naomba Waziri wa Mambo ya Nje alitolee ufafanuzi, kwa nini Watanzania tunapotaka kwenda nje tunanyanyaswa kwani sisi hatuwezi kwenda kutembea Uingereza, kwani hakuna watu wenye uwezo wa kwenda kutembea huko, mbona mnatuwekea matuta mengi tunapotaka kwenda Uingereza? Waziri naomba alisimamie suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanatoka nchi za nje ili mradi wawe wazungu hata nauli za kujia Tanzania wamekopa, lakini nashangaa Wizara ya Mambo ya Nje inakuja baadaye inawabadilisha wale watu wanakuwa wawekezaji. Tena wawakezaji hao wanadhaminiwa na nchi yetu wanakwenda kukopa kwenye benki zao kwa kutumia ardhi yetu huku Wizara ya Mambo ya Nje ikiwa inaangalia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba aliangalie na suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la lingine ni la uraia pacha, limezungumzwa tangu nikiwa mdogo, uraia pacha, uraia pacha. Hivi kuna ugumu gani katika suala hili la uraia pacha? Naomba Mheshimwa Waziri atuambie ni madhara gani tutapata kutokana na Watanzania kuwa na uraia pacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la mjusi, naona Wabunge wengi wanapiga kona. Mimi nitajitolea kama kuna ugumu wa kumsafirisha huyo mjusi kumleta Tanzania, nitakubali posho zangu zikatwe mjusi arudishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, hayo tu yananitosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nianze nyuma niende mbele. Naomba nianze na hilo la Tume ya Uchaguzi kwa sababu limeongelewa sana.

Mheshimiwa Mewnyekiti, wewe ni Mwanasheria na Katiba ya mwaka 1977 na marekebisho yake yaliyofanywa mara kwa mara, wewe ulihusika. Tume ya Uchaguzi imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 74 1(a). Katiba imeelezea Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi anapatikanaje; japokuwa anachaguliwa na Rais, lakini (a) inasema, “Mwenyekiti ambaye atakuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani, au mtu mwenye sifa ya kuwa Wakili na amekuwa na sifa na hizo kwa muda usiopungua miaka 15.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipengele (b) kimetaja “Makamu Mwenyekiti,” naye, hivyo hivyo atakuwa Jaji wa Mahakamu Kuu na sifa ambazo zinafanana. Wajumbe wengine watachaguliwa kwa mujibu wa sheria ambazo zimetungwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 74(3) imetaja watu wafuatao ambao hawataweza kuwa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi; imetaja Waziri au Naibu Waziri, Mbunge, Diwani, kiongozi yeyote wa chama cha siasa. Sasa hawa wamewekwa kwa mujibu wa Katiba na wamewekwa na sifa. Hapa tumeona wapinzani wakiwasifia Majaji. Mfano, Jaji Rumanyika wamekuwa wakimsifia, sasa wangewekwa sifa sawa na walizochaguliwa Wakurugenzi hawa sio wangesema makada wa CCM au wanataka watumie mfumo gani kuwapata? Wangesema waje humu tuwapigie kura si bado tungewachagua hao hao wa CCM maana yake Wabunge wa CCM ni wengi.

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanataka wajumbe wa namna gani wachaguliwe kuwa…

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa

T A A R I F A

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayeendelea kuzungumza. Tunavyosema Tume Huru ya Uchaguzi, tuna maana tume ambayo baada ya kuchaguliwa hata angekuwa ni Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Zitto ndio Makamishna au ndio Mwenyekiti na sijui nani wa tume kwa muundo uliopo hiyo tume haiwezi kuwa huru kwa sababu hiyo ina watumishi wengine wa kuazima kwenye TAMISEMI ambao msingi wao wa uteuzi ni makada na ushahidi upo na hawawajibiki kwa tume, wanawajibika kwa wale waliowaajiri ambao ni makada vilevile. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga unasemaje kuhusiana na taarifa hiyo?

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa kwa sababu namuheshimu nitaendelea. Tume hiyo hiyo ambayo wanailaumu wanasema si huru, katika majimbo 262, mwaka 2015 CCM imechukua majimbo 188, CUF wamechukua majimbo 35, CHADEMA wamechukua majimbo 34, NCCR moja, ACT moja, Mheshimiwa Lowassa ambaye alikuwa mgombea wa UKAWA amepata kura milioni sita, Mheshimiwa Magufuli amepata kura milioni nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tume hiyo hiyo ambayo siyo huru kuna Wabunge kama Mheshimiwa Halima Mdee ni mara ya pili anaingia Bungeni, Mheshimiwa John Mnyika anaingia mara ya pili, Mheshimiwa Sugu anaingia mara ya pili, Mheshimiwa Zitto mara ya tatu tena kabadilisha na majimbo bado kashinda, Mheshimiwa Mbowe mara ya pili, Mheshimiwa Selasini mara…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo tume ya namna gani ambayo wao wanaitaka, hao watu wangeingiaje

MWENYEKITI: Taarifa

T A A R I F A

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa poyoyo kwamba mimi kuingia mara mbili mara ya kwanza walikufa watu wawili…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sugu, hebu futa hilo neno uliloanza kutumia

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuta poyoyo. Mimi kushinda mara ya pili, mara ya kwanza kuna watu walizikwa, vita brother, matairi yamechomwa, watu wamelazwa, watu wamepigwa risasi, watu wamekaa hospitali mwaka mzima, unaona wewe. Mara ya pili…

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Mlinga taarifa hiyo unasemaje?

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sishangai kuniita poyoyo kwa sababu umesikia mwenyekiti wake ametetea bangi kwa hiyo sio suala la kushangaa…

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye mada. Naomba nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa…

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilindie muda wangu.

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa WABUNGE FULANI: Kaa chini wewe, kaa chini wewe. MWENYEKITI: Ukiona nimenyamaza nimeikataa, endelea Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimeitwa poyoyo japokuwa imefutwa, lakini sishangai kwa sababu umesikia Mwenyekiti wake ametetea bangi kwa hiyo sishangai wafuasi wake kutetea mambo ya kijinga.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga naomba ukae. Sasa naku-address wewe Mheshimiwa Mlinga. Nakuomba sana ile kauli ya kumuhusisha kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwamba ameruhusu bangi, naomba uifute tu hiyo, uendelee kuchangia, futa kauli hiyo.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nafuta hiyo kauli na naendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Manaibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa TAMISEMI…

MWENYEKITI: Nimekataa taarifa please.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Jafo ameitendea haki Wizara hii. Wizara hii ni kubwa sana na ina bajeti kubwa mno lakini ameitendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Ulanga naomba nitoe shukrani kwa mwaka wa fedha uliopita tumepata shilingi milioni 117 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekondari ya Celina Kombani tumepata milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wa kituo cha afya cha Lupilo, tumepata milioni 214 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma, tumepata ujenzi wa shule na madarasa zaidi ya milioni 400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata pikipiki 19 na gari moja ya ukaguzi wa elimu, kwa kweli kazi inafanyika. Hata hivyo, nina jambo moja la uboreshaji wa kitengo cha ukaguzi. Wizara hii ni kubwa na bajeti yake ni kubwa ambayo inatolewa lakini bado kuna upungufu kwenye ufuatiliaji wa matumizi ya hizi pesa. Kuna kitengo cha financial tracking cha TAMISEMI, lakini hiko kitengo kinapata bajeti ndogo mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anakagua kwa mfano Ulanga, tunakaguliwa kila mwaka lakini CAG wanavyokagua wanafanya random sampling yaani kama miradi 10 wanakagua miradi mitatu na wanatoa maksi kwa miradi yote kumi. Binafsi kitengo cha financial tracking kilivyokuja Ulanga kilikuta madudu sio ya kurudi nyuma. Kwa mfano tulipanga matumizi ya milioni 75 kwa ajili ya posho ya mkurugenzi ya safari lakini mkurugenzi alitumia posho shilingi milioni 192 lakini financial tracking ndio waliogundua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa Ulanga walichukua zaidi ya milioni 760 hawakuzipeleka benki na walizitumia binafsi. Ilifika kipindi watumishi wanaokusanya pesa wanaziweka kwenye akaunti zao binafsi, lakini Kitengo cha Financial Tracking ndio kilichogundua haya. Sasa mambo ambayo yalifanyika Ulanga yana-reflect halmashauri nyingine yanavyofanyika. Kwa hiyo nashauri Kitengo cha Financial Tracking cha TAMISEMI kiwezwe ili kiweze kufanya kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwa Walimu. Nimekuwa msemaji sana wa Walimu. Walimu bado wananyanyaswa mno, upandishaji wa madaraja umekuwa wa shida, wanapata manyanyaso makubwa kutoka kwa Maafisa Utumishi kwani wamekuwa wazembe katika kufuatilia taarifa za Walimu kwa ajili ya kupandishwa madaraja. Matibabu yamekuwa shida, nilishuhudia kesi moja Mwalimu amesimamishwa kazi kwa kuambiwa mtoro kwa sababu aliandikiwa ED na kituo cha afya cha private, lakini wanasema eti vituo vya afya vya private haviko kwenye standing order mbona sisi Wabunge tunatibiwa Apollo, Apollo iko kwenye standing order. Kwa mfano Dar es Salaam kuna Hospitali ya Hindu Mandal na Mwananyamala, sitojitendea haki kama nitaenda Mwananyamala nitaacha kwenda Hindu Mandal. Mbona NHIF wame-credit hivi vituo vya private, kwa hiyo Walimu wote hawa wananyanyaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye posho za Madiwani. Ukimuuliza Waziri swali hapa Bungeni atakwambia Madiwani walipwe posho kulingana na uwezo wa halmashauri lakini kila kukicha TAMISEMI wanatoa waraka...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlinga kwa mchango wako.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, naomba niwape pole wananchi wangu wa Ulanga kwa hii hali ya mvua inayoendelea, barabara hazipitiki, mafuriko kila kona. Pia naomba niwapongeze wafanyakazi wa Halmashauri kwa kukubali kufanya kazi katika mazingira magumu kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwakyembe kaka yangu, Wilayani kwangu hakuna jengo la Mahakama ya Wilaya, wanatumia jengo la Mkuu wa Wilaya, naomba unijengee. Hakuna nyumba za watumishi wa mahakama, wananchi wangu wanatembea umbali mrefu kufuata hizi huduma za mahakama. Kwa hiyo, naomba nisaidie hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara ya mwisho wakati nachangia tarehe 25 ilitokea tafrani ya kutoeleweka kwa lugha ambayo niliitumia, nilisema Mheshimiwa Pinda ametokea dirishani. Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana na mimi kuwa kiswahili kilianzia maeneo ya Pwani kwa hiyo sisi kwetu Upogoroni maneno ya kiswahili yalichelewa kufika, matokeo yake tuna umaskini kidogo wa maneno.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia yangu ilikuwa kusema hivi, sisi Chama cha Mapinduzi hatuna msalie Mtume katika maslahi ya wananchi. Inapotokea sintofahamu mahali tunakuita tunakuhoji, ukituridhisha tunakuruhusu uendelee. Kwa hiyo, wapinzani naomba mtuige na ndiyo maana tunaendelea kutawala nchi hii kwa sababu ya mfumo huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo usemao mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Naomba nimpe hongera baba mkwe wangu Mheshimiwa Mbowe kwa kuwaruhusu wapinzani kuendelea kuchangia Bungeni kutokana na ushauri niliompa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mbunge atakayepinga ni mimi niliyeleta semina humu Bungeni ya Mwenyekiti kasema ndiyo iliyopelekea Wabunge wa Upinzani kuruhusiwa kuchangia. Nilisema kuwa nina umbo dogo lakini nina mambo makubwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lissu pamoja na kujinadi amebobea sheria alishindwa kumshauri Mbowe ili waendelee kuchangia. Mheshimiwa Mchungaji Msigwa pamoja na uchungaji wake alishindwa kumshawishi Mheshimiwa Mbowe waendelee kuchangia humu Bungeni. Mheshimiwa Sugu pamoja na kuzaliwa mjini kashindwa kumshawishi Mheshimiwa Mbowe kuendelea kuchangia humu Bungeni, ni Mlinga pekee ndiye aliyemshawishi Mheshimiwa Mbowe mpaka Kambi Rasmi ya Upinzani wakaendelea kuchangia humu Bungeni. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inakuwa funzo kwa Wabunge wa Upinzani, bila ya mimi mngekuwa mabubu mpaka Bunge hili linaisha. Naomba mpelekeeni salamu baba mkwe wangu, najua haingii Bungeni ananiogopa, aingie mimi ni mtoto wa mjini, nimeshasahau. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote ni mashahidi, hakuna Mbunge aliyekuwa anaikashifu Zanzibar kama Mheshimiwa Tundu Lissu. Wanasema hivi, ukitaka umuumize adui zaidi jifanye kuwa rafiki yako. Mheshimiwa Tundu Lissu alitumia njia ile akaona hailipi, akawageuza Wazanzibar kuwa rafiki yao matokeo yake akawashawishi wasiingie kwenye uchaguzi, CUF kwisha Zanzibar. (Makofi)
Kwa mara ya kwanza wakati ninamsikia Mheshimiwa Tundu Lissu kuwa ni mwanasheria nilishtuka lakini nilipoingia Bungeni nilisikitika baada ya kuhakikisha kweli ni Mwanasheria na Wakili. Hofu yangu, kama ni Mwanasheria na Wakili ambao tunawategemea kutetea na kututunzia sheria mcharuko kiasi hiki hao waalifu wakoje?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, wote ni mashahidi wa ukanyagaji wa demokrasia unaofanywa na chama ambacho Tundu Lissu ndiyo anakitetea kwenye upande wa sheria. Tumeshuhudia Mheshimiwa Lowassa alivyoingia CHADEMA, ameingia siku hiyo hiyo, amepewa fomu ya Urais siku hiyo hiyo, ametangazwa siku hiyo hiyo. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, wanachama wa CHADEMA Jimboni kwangu walikuwa wanasema mimi nimerithishwa, nikawauliza kati ya mimi na Lowassa ni nani aliyepata fursa ya kugombea kwa kufuata taratibu za demokrasia? Nimepita kura za maoni, sawa, tulikuwa wagombea nane nikawapiga, nikaenda Uchaguzi Mkuu nikakutana na mgombea wa CHADEMA ana umri wa miaka 40 hana jino hata moja nikampiga.
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jamani nilishasema Upogoroni maneno yamechelewa kufika, sijajua kuwa hilo neno lilikuwa zito kiasi hicho, nimelifuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashangazwa na Kambi ya Upinzani kuhoji habari ya Escrow mpaka leo hii wakati baba mkwe wangu alichukua gari ya Serikali, mafuta ya Serikali, alienda kuchukua dola milioni moja Kenya, Nairobi, mbona Kambi ya Upinzani hamlizungumzii hilo?
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Ulanga ina hali mbaya sana. Watumishi ni wachache sana kiasi cha kukwamisha matibabu, mfano Madaktari ni wachache, wahudumu pia hakuna, wala mtaalam wa X-Ray machine; wodi ni chache, ndogo na zilizochakaa. Hii inapelekea wagonjwa kuchanganywa ambapo ni hatari; chumba cha upasuaji hakipo katika standard, hakina monitor; Madaktari wanatumia uzoefu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashuka na nguo za wagonjwa zinafuliwa kwa mkono (hakuna mashine ya kufulia). Hii ni hatari kwa afya za wafanyakazi. Pia gari la wagonjwa lipo moja ambalo nilinunua mimi Mbunge. Kutokana na jiografia ya Jimbo ilitakiwa kuwa na magari angalau matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Wahudumu wa Afya wanajinunulia uniform mwaka wa saba huu (hakuna uniform allowance); kuna upungufu mkubwa wa dawa hasa za ugonjwa wa kifafa, ukizingatia Wilaya ya Ulanga ina wagonjwa wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni marupurupu ya wahudumu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa namna ya pekee, naomba nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya na ma-RPC wakiwakilishwa na Bwana Mroto – RPC wa Dodona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wanawalaumu Polisi wakati sisi usiku tumelala na wake zetu tunapata joto wenyewe wamekumbatia bunduki wanapata ubaridi kwa ajili ya kuhakikisha sisi tunalala salama mpaka asubuhi. Inasikitisha kuona sisi Wabunge kama wawakilishi tukitumia Bunge kama jukwaa kwa ajili ya kuwapiga na kupambana na Jeshi la Polisi, hiyo haipendezi kabisa.

Mheshimiwa Spika, watu wanashindwa kutofautisha kati ya Polisi na Afisa Maendeleo ya Jamii. Polisi siyo Afisa Maendeleo ya Jamii ndiyo maana imeitwa Police Force, sawa? IGP Siro kama upo humu ndani wewe siyo Kamishna wa Maendeleo ya Jamii, kwa hiyo, asikuchezee mtu, umepewa nguvu kwa mujibu wa Katiba, kwa hiyo komaa! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wanalalamika kuhusu shughuli za kisiasa, hao wanaolalamika ni wale waliovamia treni kwa mbele. Kwa wanasiasa sisi wenyewe wakongwe wa siasa ambao tunaijua alichofanya Nyalandu kutoka CCM kwenda CHADEMA ile ni siasa siyo mpaka ufanye mkutano wa hadhara, alichofanya Maalim Seif kutoka CUF kwenda ACT ile ni siasa kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata anachofanya Lipumba kuondoa wasaliti ndani ya CUF ile ni siasa tosha siyo mpaka mikutano ya hadhara. Wanachofanya akina Zitto Kabwe, wale wanaoongea na waandishi wa habari, ile ni siasa kubwa sana katika nchi siyo mpaka mfanye mikutano ya hadhara, hizo ni siasa za zamani na zinaharibu maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, naomba Jeshi la Polisi likomae.

Mheshimiwa Spika, pia mnaozuiliwa siyo ninyi tu, kwa mfano mimi Ulanga niligundua ufisadi wa shilingi bilioni 2.9, wananchi wangu waliandaa mkutano mkubwa na mapokezi ya kunipokea mimi. Polisi waliniambia Mheshimiwa Mlinga utakapofanya hilo, kuna wahalifu wako ndani ambao wanaumia na ule ufisadi uliougundua kwa hiyo usifanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, siyo wao tu, siyo kila kitu lazima tuseme na siyo kila barua unayopewa na Polisi lazima uweke katika vyombo vya habari, hiyo haiwezekani. Kwa hiyo, Polisi wanawazuia siyo ninyi tu hata sisi sehemu yoyote, sasa mkiachiwa mkadhurika mtasema Polisi hawafanyi kazi. Kwa mfano, Mheshimiwa Tundu Lissu alipopigwa risasi angepewa tahadhari tangu mwanzo mngesema kaonewa. Kwa hiyo, muwe mnawasikiliza, hawa wanafanya kazi kwa taaluma, wameenda wamesomea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote, kuna matatizo katika Jeshi la Polisi la nyumba za askari. Sisi Morogoro pale tumeanza mkoani tunajenga nyumba kwa ajili ya maaskari wetu.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la uniform kwa Polisi. Juzi wakati tunaangalia Ripoti ya CAG shilingi bilioni 16 za uniform za polisi ni hewa, wanasema nyaraka hazionekani lakini hata nilipopita karibu na IGP nikagundua hata ile uniform yake bado ni ya zamani. Kwa hiyo, najua kabisa hii bilioni 16 hakuna uniform hata moja iliyonunuliwa na Polisi hawawezi kusema wao wenyewe kwa sababu mfumo wao wa chini hawezi kumhoji wa juu. Kwa hiyo, uniform Polisi mpaka wanaokwenda kucheza gwaride tena katika sherehe kama za Uhuru yaani mtu baada ya miaka mitano ndiyo anapata uniform, kwa hiyo, bado hatuwatendei haki.

Mheshimiwa Spika, suala la vitendea kazi, siku moja nilishuhudia askari anaenda kuchukua maiti hawana hata ile mifuko ya kuwekea maiti kwa hiyo hawana vitendea kazi. Kwa mfano, camera, posho, mtu anapewa kazi akachunguze kesi ya mauaji hapewi hata shilingi 10, unategemea nini kitakachotokea? Yule anayetuhumiwa si anamhonga hela kiasi tu anaachana nayo?

Mheshimiwa Spika, mafunzo kwa Jeshi la Polisi bado yanatolewa kwa upendeleo yaani mtu mpaka awe anamjua mtu wa juu ndiyo anapewa nafasi kwa upendeleo. Hilo hamuwatendei haki polisi wetu.

Mheshimiwa Spika, bado kuna mapungufu mengine kwa mfano, Dar es Salaam, eti unakuta katikati ya Mji Dar es Salaam kuna tochi yaani askari anakaa anapiga tochi katikati ya Da es Salaam. Kwa mfano, maeneo ya Tegeta, Mbezi, Oysterbay kuna tochi, hivi tochi Dar es Salaam inafanya kazi gani? Tunajua Sheria za Usalama Barabarani hazihitaji gari moja kukaa mbele ya lingine mita tatu, sasa Dar es Salaam hiyo mita tatu unaitolea wapi, Askari anakukamata. Eti Dar es Salaam umekanyaga Zebra askari anakukamata. Kwa hiyo, hapa naomba muwe mnaangalia hizi sheria zenu ziwe zinaendana na mazingira.

Mheshimiwa Spika, lingine ni ulevi, sizungumzii askari wote. Ulevi unaruhusiwa lakini mahali pa kazi hauruhusiwi. Siku moja nilikuwa naongea na Mheshimiwa Waziri nampa taarifa na yeye akanipa kesi yake siku moja na yeye alilindwa na askari ambaye amelewa, nikamwambia wasiwe wanapewa silaha, wawe wanachunguzwa kwanza kama wamelewa au la.

Mheshimiwa Spika, lingine ni counseling, askari kabla hawajapewa silaha wawe wanafanyiwa counseling kwa sababu hujui mtu ametoka katika mazingira gani huko alipotoka. Ndiyo maana ukichunguza wako maaskari wanaua wenzao maeneo ya kazi, wako maaskari akipewa silaha baada ya saa mbili anajipiga risasi. Kwa hiyo, muwe mnawafanyia counseling mgundue wana shida gani kwa sababu hata mishahara yenyewe ni midogo.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine tena nilipewa na askari. Kuna maaskari mwaka 2013 walilipa fedha kwa ajili ya kupatiwa viwanja Chalinze Mzee na kampuni moja inaitwa Ardhi Plan International, askari zaidi ya 1,000 na wamelipa hiyo hela ikiwa ni pamoja na hati lakini hakuna hata askari mmoja aliyepewa hati. Naambiwa hizo pesa zimepigwa na viongozi wa Polisi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri unapo-wind up tafadhali nahitaji majibu, hawa askari wanapata lini hati zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Uhamiaji, ameongea Mheshimiwa mwenzangu Bashe. Uhamiaji ndiyo jeshi ambalo linafanya vibaya kwa sasa hivi. Uhamiaji mmegeuza watu kuwa mitaji yenu. Mtu akigundua kijana anatembea na mke wake anaenda kuongea na watu wa Uhamiaji wanampa nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, leo hii wanakukamata wanakwambia wewe siyo raia wa Tanzania na ni wengi. Kuna kesi moja nilipeleka mimi kwa Mheshimiwa Waziri na hata Kamishna wa Uhamiaji nimemwaambia, kwa hiyo, Uhamiaji imegeuzwa silaha kwa ajili ya kuwapigia watu. Kama alivyoongea Mheshimiwa Bashe, tukianza kuchokonoana kutafutana uraia tutakaobaki raia halali wa nchi hii ni Wapogoro na Wazaramo peke yetu, wengine wote ni wahamiaji. (Kicheko)

WABUNGE FULANI: Aaaa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Ndiyo! Kwa sababu Wangoni tunajua mmetoa Afrika Kusini, Wachaga ninyi ni Wasomali, kwa hiyo, tutakaobaki ni sisi peke yetu. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Mlinga, taarifa. Watakaobaki ni Wagogo peke yake maana ndiyo wa katikati. (Makofi/ Kicheko)

Endelea Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Uhamiaji imegeuka fimbo kwa wananchi wetu wa Tanzania. Pia Uhamiaji wamewageuza hawa watu wanaoishi sasa hivi, kwa mfano, watu wa Congo wa Dar es Salaam ndiyo mitaji yao. Leo Afisa Uhamiaji akiona mambo yake magumu anamtafuta mtu mmoja wa Congo anampiga blahblah pale anachukua hela, watu wa Uhamiaji.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la zimamoto. Tunashukuru kwa kutupa Maaskari wa Zimamoto hata Ulanga tumepata. Hata hivyo, unatuletea Askari wa Zimamoto Ulanga hata koleo la kubebea mchanga hana, gari hana, anafanyaje kazi? Ina maana moto unapowaka naye anasaidia kuja kutuangalia? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la NIDA kuhusu vitambulisho. Leo miaka minne NIDA wametengeneza vitambulisho milioni nne. Sasa hata tukiwapa huo mwezi Novemba bado hawatakuwa na uwezo wa kutengeneza hivyo vitambulisho kwa Watanzania. Watanzania tuko zaidi ya milioni 50, kwa hiyo, muda tuliowapa ni mdogo na kazi yao wanayoifanya ina changamoto nyingi.

Mheshimiwa Spika, la mwisho nimalizie na suala la kupata uraia. Kuna shida kubwa, watu wana muda mrefu hawajapata uraia. Mtu ameomba uraia miaka 10/15 iliyopita hajapewa mpaka leo, hili linatengeneza mazingira ya rushwa. Wako hata hapa Wabunge wana wake ambao siyo raia lakini wameshughulika sana na imeshindikana. Kwa hiyo, hili linachangia kuleta rushwa katika kitengo hicho cha kuwapa watu uraia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Umwagiliaji wa Suga uliopo katika Kata ya Suga Wilayani Ulanga umejengwa miaka mingi lakini umeshashindwa kufanya kazi hivyo kuitia Serikali hasara.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Mradi wa Minepa. Mradi huu upo Kata ya Minepa na umeshaanza kazi, lakini gharama za mradi na ubora wake haviendani kabisa na kuna malalamiko mengi kutoka kwa mkandarasi.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Mradi Mkubwa wa Lupiro. Huu ndio mradi utakaolikomboa eneo la Wilaya ya Malinyi, Ulanga na Kilombero. Tayari tafiti zilishafanyika na thamani ya mradi ni bilioni 52, hivyo tunaomba fedha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mkononi nina kitabu kimeandikwa hivi: Ilani ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ni wakati wa mabadiliko wa kuondoa umaskini chagua CHADEMA tarehe 25 Oktoba, 2015. Kitabu hiki ukurasa wake wa 13 kimeandikwa hivi: “CHADEMA inaamini maendeleo ya kweli yataletwa na Serikali itakayokuwa na nia na mkakati wa kweli wa kupambana, kuondoa rushwa na ufisadi na siyo kwa maneno kama ilivyozoeleka”.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba waende wakatembelee Keko na Segerea watapata majibu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu hicho hicho ukurasa wa 23 kinasema hivi: “Ujenzi wa miundombinu ya afya lazima uendane na huduma husika. Baada ya miaka 50 ya Uhuru ujenzi wa miundombinu ya afya umeelekea maeneo fulani na machache”. Naomba kuwapa taarifa kuwa sasa hivi vituo vya afya 400 vimeshajengwa vimeisha na hospitali 67 za wilaya zinaendelea kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu hicho hicho, ukurasa wa 53 unasema hivi: “Vipaumbele havijawekwa kwenye uendelezaji wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme wa bei nafuu vilivyopo nchini, mfano Stigler’s kwenye banio la Mto Rufiji”. Ilani ya CHADEMA hiyo Rais anafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 40 CHADEMA itafanya nini? Kujenga reli mpya na kukarabati zilizopo kwa viwango vya kisasa na kuzingatia maslahi ya nchi ni pamoja na kujenga uwezo wa kuzalisha mataruma na reli nchini vinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, CHADEMA itafanya nini? Kuboresha bandari zilizopo na kujenga mpya kuwa vitega uchumi vya Taifa ili kuboresha biashara zilizopotea katika bandari za nchi jirani. Serikali ya CCM inafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, unasema hivi: “Kujenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora na hasa zile za vijijini.” Tumeanzisha hadi TARURA tunajenga barabara hadi vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, unasema: “Kujenga Shirika la Ndege la Taifa litakalojiendesha kwa misingi ya faida”. Mpaka sasa hivi tumeshanunua ndege saba (7), shirika linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, unasema: “Kujenga miundombinu ya kisasa ili kuondoa msongamano wa magari hasa katika Jiji la Dar es Salaam na Mwanza”. Fly over za kufa mtu zinajengwa Dar es Salaam. (Makofi/Vigelegele)

TAARIFA

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mlinga, kuna taarifa, Mheshimiwa Eng. Ngonyani.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kumpa taarifa msemaji wa sasa kwamba kwa kawaida hizi Ilani za vyama mbalimbali tunavyoandaa huwa tunadesa. Kwa hiyo, asishangae kuona Ilani ya CHADEMA anayoisoma ndiyo Ilani hiyo hiyo ya Chama cha Mapinduzi.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck Mlinga, endelea na mchango wako.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Taarifa aliyonipa naipokea nilikuwa naelekea huko. Hii Ilani iliandikwa na mtu mmoja anaitwa Mheshimiwa Edward Lowassa na iliandikwa kwa muda wa wiki mbili kabla ya uchaguzi.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yale ambayo alitoka nayo CCM ndiyo alienda nayo CHADEMA kwa kuamini atatumia kuwashawishi watu. Kwa hiyo, usije ukaona leo hii watu sasa hivi wanakomaa na pedi za kike na mawigi kwa sababu hawana cha kuongea.

TAARIFA

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck Mlinga kuna taarifa, Mheshimiwa Selasini.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpa taarifa kwamba Ilani ya CHADEMA huwa inatengenezwa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, nataka nikubaliane na yote aliyosema na ndiyo maana kila mara tunasema kwamba brain ya kuongoza nchi hii itatoka CHADEMA. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck Mlinga, endelea na mchango wako.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ukitaka uthibitishe kuwa anachoongea siyo cha kweli, waulize kama Ilani inatengenezwa mwaka mmoja kabla Mgombea wa Urais anapatikana kwa muda gani kwa sababu uchaguzi 2015 mgombea alipatikana kwa wiki mbili. Kwa hiyo, sitopokea taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote ambayo wao walikuwa wanayapigia kelele Serikali ya CCM inayafanya. Ndiyo maana leo hii hawana hoja na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja tunaenda kuwapiga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la kuongeza mapato kwa Serikali. Mimi niliwahi kupeleka kampuni moja kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango ambayo ilikuwa inalalamika imeshindwa kusajiliwa nchini, kampuni ya betting, kwa sababu ilianza biashara kabla ya muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna makampuni mengi sana ya betting ambayo watu wengi wa Tanzania wanacheza na hayalipi kodi, hiyo inaitwa online betting. Kampuni ile ilipoenda kufanyiwa upembuzi TRA ililipishwa kodi za shilingi milioni 400. Sasa hiyo ni kampuni moja, je, ni kampuni ngapi ambazo zinafanya betting Tanzania online zikiwa nje ya nchi hazilipiwi kodi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uchunguzi tukagundua kwa nini watu wanacheza online betting kwa kampuni za nje na siyo Tanzania matokeo yake inaikosesha Tanzania kodi. Sababu kubwa ni game winning tax kwa sababu watu wanaamini wanapocheza kamari kwenye makampuni ya nje wanapata zawadi kubwa ambayo haikatwi kodi lakini makampuni yetu ya Tanzania kuna kodi ya GGR asilimia 25 na winning tax asilimia 20. Kwa hiyo, tunaikosesha Serikali yetu mapato makubwa sana kutokana na game winning tax matokeo yake watu wengi wanacheza kamari za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ameliongea mwenzangu, niliongea mwaka jana, nalo ni suala la plate number. Plate number za magari haiongezi gharama katika uzalishaji wake utakapoandika jina la mtu, yaani utakapoweka namba ya kawaida na ukaandika jina la mmliki wa gari gharama ya uzalishaji ni ile ile haiongezeki. Nashangaa Serikali kwa tamaa mmeenda kuweka shilingi milioni 10, haya nikiwauliza leo hii watu wangapi wamesajili kwa majina yao baada ya kuongeza hiyo kodi, hakuna hata mtu mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini mngeweka kwenye magari kuandika plate number Sh.2,000,000 na pikipiki Sh.500,000, kuna makabila kama Wahaya wangeandika pikipiki zao zote kwa sababu wanapenda kuonekana. Aidha, Wachaga wangesajili magari yao yote kwa majina. Kwa hiyo, hii ni hela ya bure, Serikali mngefanya hivyo mngepata fedha za bure. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu nalotaka kuliongelea ni utalii. Tujiulize kwa nini Morocco wana National Parks kumi lakini wanaingiza watalii zaidi ya milioni kumi kwa mwaka? Tanzania tuna National Parks 16 lakini tunaingiza watalii milioni 1 kwa mwaka. Hii yote ni kwa sababu hatufanyi promotion za kutosha kwenye utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya National Parks Tanzania tuna wanyama wengi. Ngedere wako hadi Ikulu wanamsumbua Rais lakini kwa nini watalii hawaji Tanzania? Ni kwa sababu ya mipango yetu mibovu ya ku- promote utalii inasababisha tusipate watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Balozi wetu wa China, shemeji yetu Mheshimiwa Kairuki anafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuleta watalii katika nchi yetu. Watumieni Mabalozi wetu kutangaza utalii siyo Mabalozi wanakaa wanakunywa wine tu huko nje, watangaze utalii wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nilijaribu kuliongelea jana ni balaa la UKIMWI katika nchi yetu. Serikali yetu wameshindwa kubuni mikakati inayoendana na wakati kwa ajili ya kupambana na vita dhidi ya UKIMWI. Matokeo yake kila siku iendayo kwa Mungu vijana 80 wanapata maambukizi ya UKIMWI wenye umri kuanzia 14 - 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, athari yake nini? Kwanza vijana hawa wako katika foolish age, wanaamini hawana cha kupoteza na hawana majukumu mazito. Kwa hiyo, sisi tunaposema Hapa Kazi Tu wao wanasema Hapa Zinaa Tu. Matokeo yake baada miaka 10 hatutakuwa na kina Tulia Ackson, Jenista Mhagama na Angellah Kairuki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali isipofanya mikakati ya dhati kwa ajili ya kutokomeza janga la UKIMWI tutakwisha. Jamii imesahau kabisa kama janga hili bado lipo na ugonjwa huu hauna dawa. Zamani Serikali ilikuwa na mikakati, katika vituo vyetu vya radio ilikuwa kila baada ya matangazo fulani kunakuwa na tangazo la UKIMWI lakini sasa hivi hamna hata TBC yenyewe ukisikiliza unaweza ukakaa siku nzima usione tangazo la UKIMWI. Matokeo yake redio na televisheni zimekuwa ndiyo kwanza vyanzo vya ku-promote ngono na mapenzi. Sasa hivi kila redio kubwa na ndogo ukisikiliza usiku wana-promote mambo ya ngono.

Mheshimiwa Naibu Spika, mitandao ya kijamii, sasa hivi kuna ma-group ya WhatsApp ya ngono, Instagram wana- promote ngono, watu tunajiuza hadharani lakini Serikali imekaa kimya wanasema wanapambana na vita dhidi ya UKIMWI, mnapambanaje?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba Waheshimiwa Wabunge wanipongeze kwani katika Bunge hili la 2015-2020, mimi ni Mbunge wa kwanza kupeleka ambulance ya kisasa Jimboni kwa kutumia gharama zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kufika hapa mpaka leo hii maana huko nje magazeti yote Mlinga, Mlinga, kamtu kenyewe hata kwenye mkono hakaenei. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yangu ya Wilaya Mheshimiwa Waziri ina shida sana. Japokuwa mimi Mbunge nimejitahidi nimepeleka ambulance lakini kuna upungufu mkubwa wa vifaa tiba, hata mashine ya kufulia hakuna, watumishi hakuna, wapo wachache mno. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba katika bajeti yako unikumbuke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Idara ya Maendeleo ya Jamii hakuna watumishi wa kutosha, hakuna vitendea kazi, wako maofisa hata pikipiki hawana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba unikumbuke katika bajeti yako hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala la NHIF. Waheshimiwa Wabunge ni-declare interest mimi nilikuwa Compliance Officer - NHIF. Nafahamu shida zilizopo katika shirika hili lakini hata hivyo nashukuru viongozi waliopo wamejitahidi. Kuna suala la mashirika ya umma kukataa kwenda kujiunga na NHIF na kusababisha huu mfuko ufe. Kama sisi Wabunge tumejiunga na NHIF, haya mashirika yana nini mpaka washindwe kwenda kujiunga na NHIF? Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge niwape siri moja, hii mifuko binafsi ya insurance ina mikono ya wakubwa.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: TCRA hawataki kujiunga na NHIF kwa nini? EWURA hawataki kujiunga na NHIF kwa nini? Kama sisi Wabunge tumeweza kujiunga kwa nini wao wasijiunge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikiwa Compliance Officer nilishawahi kwenda TRA kuonana na Mkurugenzi Mkuu ili wafanyakazi wa TRA wajiunge na NHIF. Jibu alilonipa, haki ya Mungu ni kwa sababu ilikuwa ofisini kwake lakini angekuwa ofisini kwangu asingetoka. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na bahati nzuri ameshatumbuliwa jipu, aliniambia sisi pesa sio tatizo maana nilimwambia NHIF mnachangia kidogo mnapata matibabu mengu, wigo wa matibabu ni mpana. Halafu pia sheria inataka mashirika ya umma yajiunge na NHIF. Akaniambia sisi hela kwetu sio shida, nikamuangalia kimoyomoyo nikasema hizi fedha za kwako?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri afuatilie hilo, mashirika mengi ya umma hawataki kujiunga na NHIF kwa sababu wanapewa ten percent wanapokwenda kujiunga na mashirika binafsi ya insurance. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinanisikitisha sana nacho ni ubakaji wa wazee, sijui Wizara hii mnaliangaliaje suala hili. Kuna mikoa ubakaji wa wazee umeshamiri. Huwa najiuliza shida ni nini au wanawake wa maeneo ya huko wagumu kuelewa somo mpaka hawa watu wanaenda kubaka wazee? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba mfanye utafiti mgundue ni nini kinachosababisha tatizo hili. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utulivu Waheshimiwa Wabunge, nimepata tuhuma nyingi sana jamani. Nimeitwa teja, jamani Waheshimiwa Wabunge hebu mnitazame, teja anaweza akawa anashinda amevaa suti zimenyooka namna hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba ukiniita mbilikimo nitachukia kwa sababu ukweli mimi ni mbilikimo na kila nitakapokuona nitakuchukia lakini ukiniita teja siwezi kuchukia kwa sababu sio ukweli na ukweli huwa unauma, kwa hiyo siwezi kuchukia. Nimepata vitisho vingi, lakini naamini Serikali yangu ipo. Kama wanajeshi walienda kuwakomboa wananchi wa Kongo wakaisambaratisha M23 watashindwa kunilinda mimi tena Mbunge? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waheshimiwa Wabunge wamefurahi lakini naomba mnisaidie kumwambia Waziri wa Ujenzi, naomba Daraja la Kilombero liishe mwaka huu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, naomba kumalizia kwa kusema naomba uje ukitembelee Kituo changu cha Afya cha Lupilo. Sitaki kuongelea hapa lakini naomba uje ukitembelee kituo changu cha afya uone jinsi kilivyo, hakifananii kufanya matibabu ya binadamu, sisemi lakini naomba tuondoke wote uende ukajionee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, ndio hayo tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na wimbi kubwa la wanyama waharibifu katika kata za Ketaketa, Ilangu, Mwayasuga na Chilombora, hasa viboko wanaharibu mazao kwa kiasi kikubwa sana na kupelekea njaa. Afisa Wanyamapori yupo mmoja hawezi kutokana na ukubwa wa eneo.

Naomba mtuongezee maafisa ili kunusuru mazao na kupunguza hali ya wasiwasi kwa wananchi (usalama).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Selous Game Reserve; kumekuwepo na mgogoro katika maeneo ya kata nyingi hasa Ketaketa, Ilonja, Mbuge na Lukande kwa sababu watu wanazaliana hivyo kuwa na ufinyu wa ardhi kwa ajili ya kilimo na makazi. Nashauri tuweke utaratibu wa watu kulima maeneo ya Selous ili watu hawa waweze kujipatia chakula ili kuweza kupambana na maisha kwa sababu tukiwaacha watakosa shughuli ya kufanya matokeo yake wanawinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kubwa la Ulanga limetengwa kama eneo oevu (buffer zone) hivyo hakuna sehemu nyingine ambayo watu wanaweza kulima hivyo kupelekea watu kukosa chakula. Serikali iharakishe mchakato wa kumilikisha kipande cha eneo oevu ili watu wapate maeneo ya kulima ukizingatia watu wengi wameshavamia kiholela bila ya utaratibu kwa kuwa hakuna mwongozo.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, jamani Wabunge wakati tunachangia hapa kuna vitu vya kuongea. Jana kuna Mbunge mmoja aliongea hapa alikuwa anafananisha mwenendo wa utendaji wa Serikali yetu, sawa sawa na mauaji ya Kimbari. Jamani wanaofahamu yale mauaji jinsi yalivyotokea siyo ya kuyataja, jambo la kusikitisha zaidi yule Mbunge ni Mchungaji. Ninatamani niwaone hao waumini wake anaowasalisha, na kama kweli ni waumini basi yatakuwa yale makanisa ambayo wanasali bila nguo.(Makofi)
Mheshimiwa Nape, wewe ni rafiki yangu, ni kaka yangu, ni mwanachama mwenzangu wa CCM, lakini kwenye hili, ndugu yangu utanikosa na utanisamehe. (Kicheko/Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, hamna kabila ambalo wako strategically kwenye maisha kama Wachaga, lakini Mchaga mtoto, sauti ikishaanza kukomaa, baba anamwambia mtoto hapa nyumbani siyo mahali sahihi pa kukaa. Hata hivyo, Mheshimiwa Nape, hawa watu wanatoa mtaji, mtu anaoa mtaji kwa mtoto wake nenda kaanze maisha.
Leo hii Mheshimiwa Nape unakubali kubeba hiki kimeo, unaiachia TBC bila shilingi! Kwenye hili ndugu yangu, siko na wewe. UKAWA moto, Mlinga moto, CCM moto, kazi unayo kaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu zaidi, TBC imeachwa bila shilingi. Katika Wilaya 81 TBC haipatikani, hasa Wilaya za mipakani; wanasikiliza redio za Uganda, Rwanda, Malawi na Congo. Cha kusikitisha zaidi kabisa TBC ndiyo inaongea taarifa za ukweli kuhusu Serikali. Sasa nchi zetu za majirani wakiamua kutuhujumu tunatokea wapi? Kwa hiyo, katika huu muda mfupi, hii nusu saa iliyobaki, tafuta mifuko ya mbele ya nyuma, ongezea hela kwenye TBC. Najua shilingi unazo nyingi, lakini mimi nitatoa hata noti nitaondoka nazo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni timu ya Taifa. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi, ule mchakato wa kuwapata wachezaji wa timu ya Taifa huwa ni wa ukurupukaji. Utasikia ikitokea mechi ndiyo wanaanza kukusanya wachezaji, tena wachezaji wenyewe mnawatoa mjini. Nimewaambia Waheshimiwa Wabunge mwambieni Waziri wa Barabara aweke lami Ulanga upite uje uchukue wachezaji kule wapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hiyo timu ya Taifa wana maslahi duni, hawana mtu wa kuwafanyia counseling. Mtu anatoka na stress zake za maisha, hajalipa kodi ya nyumba, kesho unamwambia akacheze na Misri, atawafungia wapi? Hii tutakuwa tunacheza makida makida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna timu imeenda India under seventeen sijui, sina uhakika sana, lakini ile timu nenda kaulize wale watoto wamewatoa wapi? Hawajawapa chochote, wamewabeba tu juu juu, wamewapeleka huko India, mnategemea mtapata nini? Wanaenda kuwakilisha au wanaenda kuchukua ushindi? Mimi nadhani hawa wote wanaenda kuwakilisha, lakini hatuna strategy kwa ajili ya kuendeleza michezo yetu.
Mheshimiwa Nape, wakati unahitimisha naomba uniambie ni manufaa gani Taifa limepata kwa ile sports academy iliyoanzishwa? Kama ipo bado. Maana yake inaweza isiwepo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uwanja wa Taifa umejengwa kwa shilingi bilioni 60. Ukihitimisha ningependa kujua mpaka sasa hivi ule uwanja umeingiza kiasi gani? Isije ikawa pango la watu wapigaji wa pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kocha wa Taifa, Serikali iliyopita nilikuwa nasikia Mheshimiwa Rais anasema anatoa hela, nataka nijue, utaendelea ule utaratibu au ndiyo vile? Ndugu zangu UKAWA leo pumzikeni. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye vyombo vya habari. Waheshimiwa Wabunge, naomba nimpongeze ndugu Reginald Mengi kwa mfumo aliouweka katika vyombo vyake vya habari (IPP Media). Angalia gazeti la Nipashe, linaandika habari ina-balance ndiyo maana linaendelea ku-exist wafanyakazi wanalipwa vizuri, ndiyo maana hawachukui habari za mtaani. Wamiliki wa vyombo vya habari, naomba mumuige Reginald Mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaanzisha vyombo vya habari, mnategemea waandishi waende wakajikodolee hela huko. Kuna gazeti juzi liliandika habari za Mlinga, lile gazeti tangu lianze halijawahi kufika Ulanga. Zilipelekwa copy 1,000! Waheshimiwa Wabunge, niliwaambia mimi ni mdogo kwa umbo, mkifika Ulanga kule mimi ni mkubwa kuliko hili jengo. (Kicheko)
Waheshimiwa Wabunge, kweli zile copy zilipofika Mto Kilombero zikatumbukia, zikapotelea huko. Ni kweli Waheshimiwa Wabunge, naomba TBC wamuige Reginald Mengi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze ndugu Ruge wa Clouds Media; watangazaji wanatangaza unaona kabisa wanavyo-relax, yaani wanapata vitu vizuri kutoka kwa mwajiri wao. Siyo watangazaji wanatanga wamenuna, wanafanya kazi kama wamelazimishwa. Kwa hiyo, naomba muwaige hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye issue ya live. Live, live mnataka nini? Si mna majimbo ninyi. Mlipoomba kura si mliombea majimboni, mnataka muonekane ili iweje? Wabunge wanatukana, wengine ndiyo wanatoa mifano sijui ya Kimbari, mnataka muonekane live ili iweje?
Waheshimiwa Wabunge, Wabunge wengi wanaotaka live walikuwa hawaendi majimboni, wanapiga simu kwenye ma-bar, niangalieni nitaongea; sasa hivi mtakufa kibudu humu humu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa kuonekana live, kupiga makele, leo hii tungekuwepo na Mheshimiwa Kafulila, tungekuwepo na Mheshimiwa Mkosamali, walikuwa waongeaji wazuri, wanavimba kwenye ma-desk haya mpaka basi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije issue ya wanamuziki. Naomba nimpongeze Diamond popote ulipo. Ingekuwa amri yangu, tungechonga sanamu la Diamond tukaliweka pale kwenye ule mnara wa askari. Ule mnara tumeuchoka, tungetoa tungeweka sanamu ya Diamond. Ametufikisha mbali! Ni alama, ameitangaza nchi yetu huko mbele; na Serikali hatuna mpango wowote wa kusaidia wanamuziki, wanapenya wenyewe, tunaenda kukutana nao mbele na sisi tunajifanya tunawasaidia, yuko wapi Mr. Nice? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungewawekea mfumo mzuri hawa watu wasingekuwa wanapata shida leo. Yuko wapi Saida Karoli, Kanichambua Kama Karanga? Eeh, hatujawawekea mfumo mzuri.
tumeweka vyombo vya kuwatapeli; sijui kuna BASATA, sijui kuna COSOTA hawa ni wapigaji wa hela za wasanii tu, hamna lolote wanalolifanya. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayaongea haya, ninamaanisha kwa sababu tunawaacha wanamuziki wanafanya wanayoyataka, matokeo yake ndiyo haya ya akina chura, sijui akina nani, mnakuja mnawafungia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, ni haya tu yananitosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. UKAWA naona mnashusha pumzi, kuweni na amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja. Waheshimiwa Wabunge, Jimbo langu la Ulanga na Wilaya nzima imebarikiwa kuwa na madini ya kila aina kasoro tanzanite. Isipokuwa shida kubwa tunayoipata, wanasema mbega aliponzwa na uzuri wake, ndiyo shida kubwa tunayoipata Jimbo la Ulanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Nishati na Madini, imejitenga kabisa na wananchi wa Tanzania. Wao wamekuwa madalali. Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini wanatembea na ramani za madini ya nchi hii makwapani, kazi yao kubwa ni kutafuta wawekezaji, wanawapa leseni, hawajali pale wanaishi watu; hawajali wale watu wanatakiwa wafidiwe na kama hata ni kufidiwa ni shilingi ngapi? (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, mtakubaliana na mimi, nendeni sehemu zote ambazo kuna uchimbaji mkubwa wa madini, watu wa pale wanaishi maisha duni sana, malalamiko makubwa sana yamejaa pale. Mheshimiwa Waziri nakuamini, Profesa maana yake ni mtu wa research, fanya research, haya yanatokana na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeongea hivyo Mheshimiwa Muhongo, anajua namaanisha nini? Katika hotuba yake ame-specify kuna miradi mikubwa ya madini ambayo inatakiwa ianze; madini ya graphite ambayo katika Tanzania yako sehemu mbili; Ulanga na Ruangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo wale wawekezaji waliowapa leseni wameshakuja kule wanataka kuwahamisha watu. Mheshimiwa Waziri ametuma watu wake waje kule waangalie: Je, kuna umuhimu wa wananchi kuhamishwa au lah? Wananchi wamelalamika, watu aliowatuma wamesema wamempa ripoti, wamesema watu hawatakiwi wahamishwe, Mheshimiwa Profesa Muhongo suala hilo limekwenda kwake, lakini bado ana kigugumizi. Kwa nini anashindwa kutoa kauli? Kuna nini katikati hapa? Wananchi wangu hawana amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie, hii Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2010 ilitoa hadi leseni ya Waziri mwenzao ilimpa mbia afanye uchimbaji wa madini kwenye nyumba ya Waziri mwenzao, Marehemu Mama Kombani. Hii Wizara ya Nishati na Madini iltoa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ikampa mwekezaji achimbe madini; ilitoa Mahakama ya Wilaya; ilitoa eneo la wakazi zaidi ya 15,000, imempa mwekezaji achimbe; yaani hawajali, wanapotoa hawaangalii kama kuna watu wanaishi. Mheshimiwa Muhongo naomba alifanyie kazi. Wale wawekezaji aliowapa leseni, hawawezi kuchimba graphite, labda wakachimbe Jimboni kwake, lakini siyo Ulanga. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, napenda kuongelea suala la umeme. Umeme unazalishwa Kidatu tangu mwaka 1970. Kutoka Kidatu kwenda Ulanga ni kilomita 150. Imechukua miaka 20 Ulanga kupata umeme. Hata sasa hivi, umeme upo, kwa wiki unawaka mara moja. Mheshimiwa Profesa Muhongo, nilimwambia akatoe zile fito, aweke nguzo za kupitishia umeme. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, Waheshimiwa Wabunge kuna jipu. Mheshimiwa Profesa Muhongo nimeshamwambia zaidi ya mara mbili, kuna hii sheria iliyopitishwa mwaka 2015 ya uagizaji mafuta kwa pamoja. Hiyo sheria inampa mamlaka Waziri ku-declare mafuta ya on transit yatumike nchini.
Hebu Waheshimiwa Wabunge fikirieni, imepaki meli pale ina mafuta lita laki tano; Waziri anaidhinisha yatumike nchini. Yale mafuta huwa hayalipiwi kodi, halafu sheria inampa nguvu Waziri kusema yeye ndio ataamua, yaani emergency condition ambazo yeye ata-declare. Sasa hiyo emergency condition hawajasema kuna sheria, yaani Waziri kichwani mwake siku hiyo kaamka kasema emergency condition leo ni hii, ana-declare. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Muhongo asisubiri aje aongee Mheshimiwa Zito hapa, asisubiri aje aongee Mheshimiwa Godless Lema, ni mimi Mlinga nafagia nyumbani, sawa! Naomba wakati anahitimisha aseme, la kwanza, kiasi gani cha mafuta ambacho amesha-declare cha on transit kitumike Tanzania? Kiasi gani cha kodi ambacho kimeshalipwa na ni lini analeta sheria hii tuifanyie marekebisho; hatuwezi tukamwamini. Dhamana yetu hatuwezi tukampa yeye. Mheshimiwa Profesa Muhongo, mimi leo sina mengi, ni hayo tu yanamtosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa muda huu mchache ulionipa ngoja nifafanue masuala machache. Kwanza nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini kuna upungufu mchache ambao unasababisha Jeshi la Polisi kupata madoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni rushwa. Kwa research ambayo nimeifanya 85% ya wanaopata huduma ya Jeshi la Polisi wanaipata kwa rushwa. Hawawezi kupata huduma hiyo mpaka watoe rushwa. Mfano mlalamikaji akifika kituo cha polisi hawezi kupata huduma yoyote atatengenezewa mazingira mpaka atoe hela ndiyo ahudumiwe, wataambiwa karatasi hakuna, gari halina mafuta au askari wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili mlalamikiwa, huyu ndiyo balaa kabisa. Ukiwa mlalamikiwa yule askari mpelelezi inatakiwa umuheshimu kama baba mkwe wako, atakuita muda wowote, mahali popote anapotaka. Anaweza akakuita baa akakwambia lipia vinywaji, anaweza akakuita wapi akakwambia toa hela hii hapa. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu dhamana. Dhamana haipatikani bila ya kutoa rushwa. Hilo ni suala la kwanza nililotaka kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni ubambikiaji wa kesi. Ubambikiwaji wa kesi ni pale Polisi anapo-exaggerate, yaani anapoikuza ile kesi tofauti na ilivyokuwa. Kwa mfano, kesi ya madai inageuka kuwa ya jinai, Polisi anafanya hivyo ili kutengeneza mazingira ya kupata pesa. Pili, kesi ya uzururaji inakuwa ya ukabaji. Tatu kesi ya kuku inakuwa ya ng’ombe. Nne kesi ya matusi inageuka kesi ya kuua kwa maneno. Niwapongeze askari wanawake kwenye hili hawapo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine traffic. Traffic ni janga lingine la Taifa. Kwa Dar-es-Salaam wanawaita wazee wa Max Malipo na mikoani wanawaita TRA ndogo. Traffic wameacha kazi yao ya kuangalia usalama barabarani sasa hivi wanakusanya mapato na nimethibitisha mmewawekea malengo. Makosa ambayo wanatoza fine ni ya uonevu. Unaenda kumtoza bodaboda Sh.200,000/= fine na ndiyo maana sasa hivi bodaboda zimejaa kwenye vituo vyote vya Polisi. Kwa hiyo, tunaomba waliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni makosa ya mitandaoni. Makosa ya mitandaoni saa hizi imekuwa too much. Kwenye mtandao hajulikani kiongozi au mtu wa kawaida, wanatukanwa wananchi, wanatukanwa Wabunge wetu, Mawaziri hadi Rais anatukanwa. Mheshimiwa IGP yupo hapa tumemwekea nyota mabegani hizo ni nguvu, atumie nguvu zake wasimchezee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, natoa account ambazo kwenye mitandao ya kijamii zinamtukana Rais. Kuna Kwinyala, Malisa GJ, CHADEMA in Blood, Yeriko Nyerere na dada yao Mange Kimambi, wamekuwa wakimtukana Rais. Jamani hakuna nchi ambayo Rais anachezewa, nitolee mfano Kagame, umeshawahi kusikia mtu anamtukana Kagame? Polisi tumieni nguvu zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni hayo tu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo langu la kwanza, naomba nikumbushie siku nachangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha nilisema tukikubali mipango hii ya Mheshimiwa Mpango, tutauza hadi Ikulu, tumeyaona leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tumechangia, Mheshimiwa Waziri ametuelewa na hii ndiyo mara yake ya kwanza sasa hivi ana miezi minane tu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge naomba tumpe nafasi, Waziri atajirekebisha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba nichangie masuala yanayoendelea sasa hivi kwa upande wa wafanyabiashara. Wafanyabiashara wetu sasa hivi hatuwapi nafasi, wanapotoa ushauri Serikalini, Serikali inawapa nafasi finyu ya kuwasikiliza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba ukitoka hapa kakae na wafanyabiashara wetu. Mimi nina uhakika tukisikiliza maoni yao tutafika mbali. Haya yaliyotokea sasa hivi hayatatokea tena, ni masuala madogo tu ya kukaa na kuyarekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la tatu, katika Jimbo langu la Ulanga kuna migodi mikubwa ambayo inatarajiwa ianze, kwa kiasi kikubwa italisaidia Taifa letu katika kuchangia uchumi. Hata hivyo, wananchi wa kule hawasikilizwi na kusababisha miradi hii kuchelewa kuanza ambapo ingechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, naomba Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu upo naomba uje Ulanga utusikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, katika Wilaya yangu ya Ulanga tunalima mazao mengi ikiwemo mpunga zao ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia uchumi wa Taifa letu. Leo hii Wizara ya Maliasili inapanga kwenda kuwanyang‟anya wananchi wa kule ardhi ambayo ingechangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Wilaya ya Ulanga. Rais alipokuja aliahidi lile eneo watawaachia wananchi ili waweze kulima na kuchangia mapato ya Taifa hili.
Endapo tutawanyang‟anya wananchi eneo lile nakuhakikishia robo tatu ya mapato ya Ulanga na Malinyi yatashuka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba suala hilo ulitazame katika jicho la pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, jana kuna kiongozi mmoja alinishangaza sana, aliuliza Serikali ya CCM itatumia miujiza gani kutekeleza ahadi zake. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Tanzania kuwa Serikali ya CCM haitumii miujiza inatekeleza ilani yake kwa mipango na mikakati na itafanikisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namshangaa, kwanza ajiulize yeye huyo kiongozi form six amepata division zero, lakini huyo huyo ana miujiza ya kuwaongoza wanasheria maarufu kama akina Tundu Lissu wakatulia, ana uwezo wa kuongoza madaktari wenye Ph.D na wakatulia. Kwa hiyo, sisi hatutumii miujiza tunatumia taratibu, kanuni na uadilifu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la sita, kumekuwepo na sintofahamu Wakuu wetu wa Wilaya, Wakuu wetu wa Mikoa kutumia sheria ya kuwaweka ndani wafanyakazi wenzao kama Madiwani na watendaji wengine kama Wakurugenzi wa Halmashauri, kile kitendo cha kuwaweka saa 24. Wakuu wa Wilaya wametumia ile kama silaha yao ya kuwakandamiza viongozi kwa ajili ya kuwalipizia visasi. Kwa mfano, kila siku tunasikia Mkuu wa Wilaya amemweka ndani Mkurugenzi, kila siku Mkuu wa Wilaya amemweka ndani Diwani, vile vitu vinadhoofisha maendeleo ya nchi yetu. Watu wamekuwa hawafanyi kazi kwa juhudi zote, wanafanya kazi kwa uoga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie hapo.
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hili ni Bunge, katika nchi yoyote Bunge ni kitu kikubwa ambacho kinaheshimika. Ndani ya Bunge ili kuleta balance na kuwa na nidhamu kuna kiongozi wa upande wa Serikali (Chief Whip) na kuna Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote tunayoazimia inatakiwa twende extra miles. Kwa nini nasema hivyo? Tukiacha Mheshimiwa Halima Mdee, juzi Mheshimiwa Nassari ameenguliwa Ubunge kwa mujibu wa Katiba, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani yupo na hajui nini kinachoendelea. Mheshimiwa Esther Bulaya, Mheshimiwa Sugu na Mheshimiwa Mnyika wamewahi kusimamishwa Ubunge Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani yupo. Imefika wakati wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kujitafakari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwa Mheshimiwa Halima Mdee. Mheshimiwa Halima Mdee nipo naye kwenye Kamati moja, ndani ya Kamati ana mchango mkubwa na mzuri kweli kweli. Mimi sijui nini kinamkuta akiwa hapa na mimi ni rafiki yangu na amenishauri vitu vingi sana lakini hapa mambo anayoyafanya; amewahi kufanya kosa mara ya kwanza na ya pili ameadhibiwa, hayo mambo tulitakiwa tufanye sisi kwa umri wetu na uchanga katika Bunge lakini anayafanya yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Halima Mdee alishawahi kupewa nafasi mama yake mzazi kumuombea msamaha katika Bunge hili, hakuna Mbunge aliwahi kupewa nafasi hiyo. Sisi tusio na mama tukifanya makosa tunafanyaje? Mwenzetu amefanya makosa mpaka inafika kipindi wazazi wake wanakuja kumwombea msamaha, sasa hii imekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa matukio hayo naunga mkono Maazimio ya Kamati. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia muda huu na mimi nichangie machache niliyonayo. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, jamani Waheshimiwa Wabunge sisi tumechaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuwasaidia. Sasa basi tunaposhangilia hapa na tunapopitisha hivi vitu viwe kwa ajili ya maslahi ya wananchi. Kila Kamati iliyosimama hapa ilikuwa inalalamika kuhusu ufinyu wa bajeti. Bahati nzuri sasa hivi imeturudia sisi wenyewe na hii iwe fundisho kila kitu kinachokuja mnapitisha. Mimi ingekuwa amri yangu hizi meza zingekuwa za chuma ili kabla mtu hajapiga awe anafikiria maumivu. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Kamati imepewa bajeti ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya safari za nje. Jamani hebu tujiulize Kamati ya chini kabisa ilikuwa na watu sio chini ya 18, hivi shilingi milioni 10 unaenda nchi gani, unatumia usafiri gani, bajaji? (Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kitu ambacho nime-experience katika hizi Kamati kuwa Serikali inapokuja kujibu, inakuja timu ya watu 30 anayeongea ni mtu mmoja. Jamani huu ni ufujaji wa fedha hizi za wananchi kwani hamna kazi nyingine? Utakuta wanakuja wengi anajibu mtu mmoja, nusu saa halafu mistari yenyewe miwili wanaondoka, VX 8 zimekuja. Jamani huu ni ubadhirifu wa fedha za Watanzania. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu ni kuhusu Wizara ya Mambo ya Nje, sasa hivi kila mkoa unaoenda unakutana na Wachina. Jamani hawa Wachina nawahakikishia tukianza kukutana nao labour ward haki ya Mungu nchi hii mwaka 2030 tunafanya sensa wao watakuwa wengi kuliko sisi. Kwa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje, naomba mliangalie suala hili. Wako Wachina wanaishi hawana passport hawajui viza ndio nini, wanaingia tu lakini sisi kwenda kwao wanatudhibiti. Kwa hiyo, naomba mliangalie suala hili. (Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo tulifanya ziara kwa Mpiga Chapa wa Serikali. Jamani Mawaziri, namwomba Rais aende katika Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali, sijawahi kuona ofisi mbovu kama ile yaani ukienda huwezi ukategemea kama wanafanya kazi ya printing, haina tofauti na station ya TAZARA au ile station kubwa. Kwa hiyo, naomba Rais aende akatembelee pale, ina hali mbaya. Hawafanyi kazi yaani wakiletewa ku-print kazi ya Serikali wanaenda ku-print kwa Wahindi sasa siri za Serikali zinakuwa wapi tena? Siri si zinavuja huko mitaani halafu tunalalamika Serikali yetu haina siri. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne, jamani mimi Mlinga sipingi vita dhidi ya madawa ya kulevya. Ninacholalamika na kulaani ni mtu kutumia madaraka yake kupigana vita binafsi kuigeuza kuwa vita ya Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho ndicho ninachopinga. Mimi Mlinga niko tayari kusimama mbele ya Rais kumwambia chanzo cha vita hii. Kumwambia ukweli, vita haijaanza kwa ajili ya madawa ya kulevya, vita imeanza na ugomvi binafsi, baada ya kuona ita-backfire wakaigeuza kuwa vita ya madawa ya kulevya. Niko tayari kusimama mbele ya Rais achunguze chanzo ni nini? Wale wasanii waliowekwa ndani chanzo kilikuwa nini, haikuwa vita dhidi ya madawa ya kulevya. Niko tayari kusimama mbele yake kumwelezea aangalie ukurupukaji huu utatusababishia uvunjifu wa amani Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmemtaja Gwajima ana watu, mmemtaja Mbowe wa CHADEMA watakaa pembeni, mtawataja akina Manji watu wa Yanga watakaa pembeni. Jamani uchungu wa mambo haya, kama una familia ukija kutajwa utayaona machungu yake, siyo rahisi hivyo mnavyofikiria. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii umeniharibia heshima yangu mimi Mlinga na nina wananchi wangu kule Ulanga, nina mke wangu ana ndugu zake, nina watoto wangu wanasoma shule, hivi watoto wangu wanatembeaje huko walipo jamani. Leo hii nimekutaja wewe unahusika na madawa ya kulevya, hivi watu wanaonifahamu wanatembeaje huko waliko? Jamani haya mambo myasikie yasije yakawakuta. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amemteua IGP, Waziri wa Mambo ya Ndani, jamani mbona mko kimya, hamna shughuli za kufanya, kwa nini mnaachia watu wanadhalilishwa? Nchi yetu ina wakuu wa mikoa 25, nime-experience kinachoanzia Dar es Salaam Wakuu wa Mikoa wote wanafuata. Hivi kila Mkuu wa Mkoa akisimama akianza kufanya yale yanayofanyika Dar es Salaam jamani tutakuwa wapi? Kwa hiyo, tufikirie vitu kabla ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema sisi Wabunge siyo kwamba tunawaonea watu wivu.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo langu la kwanza naomba nitoe shukrani kwa Serikali kwa kunifanyia ukarabati Kituo cha Lupilo na kunijengea theatre. Hii inadhihirisha uchaguzi wao wa kumchagua Rais jembe na Mbunge jembe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije kwenye suala la elimu. Wizara ya Elimu kila siku inatoa miongozo, juzi hapa wamesema private school wapunguze ada, wawawekee kiasi cha ada yaani wao Serikali ndiyo wawe waamuzi, lakini hao hao Serikali wanaziwekea kodi nyingi hizi shule za private, sasa tunafanya nini? Ninyi Serikali si mna shule zenu na si mna shule nyingi, kwa nini msiwe mnatoa miongozo kwa shule zenu ili zifaulishe? Ada tunalipa sisi wazazi ninyi nini kinawakereketa? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mzazi mwenyewe ataamua, atachagua mwenyewe shule ya kumpeleka motto wake. Hawa wanapandisha ada kwa sababu demand imekuwa kubwa wasingekuwa wanapandisha ada. Wazazi wenyewe wawe waamuzi, waamue wapeleke au wasipeleke watoto wao katika shule hizo. Kwa hiyo, fanyeni maamuzi kwa shule zenu. Mlikuwa na shule Mzumbe, Pugu, ziko wapi sasa hivi, sifuri tupu! Kwa hiyo, fanyeni maamuzi kwa shule zenu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kwenye hizo hizo shule za private, kwa mfano Jimboni kwangu mimi kuna shule inaitwa Kasita Seminary, Regina Mundi zinafaulisha kweli! Shule hizi zinafaulisha kwa sababu wanaweka madaraja kutoka kidato kimoja kwenda kidato kingine. Mwanafunzi asipofikia wastani wanamrudisha darasa. Sasa ona wanafaulisha, ninyi mnawaamuru watu waende tu, mbona wanapata sifuri? Halafu mnakuja mnalalamika oh, wanapata sifuri; wenzenu wana mikakati na nyie pangeni shule zenu, wekeni mikakati vizuri, faulisheni! Wazazi wenyewe ndiyo wataamua, watakubali watoto wao waende mbele au warudi nyuma. Kwa hiyo, fanyeni ya kwenu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatujaja kugombana na wazazi. Mama yangu Ndalichako, mwaka juzi wakati wa kampeni hukuwepo. Sisi tuliokuwepo tulitoa ahadi hizi nzuri kwa wananchi wetu. Hatujaja kugombana na wamiliki wa shule za private, tumekuja ku-entertain, tunataka elimu ya Tanzania iwe juu, lakini sio kwa hiyo miongozo mnayotoa kila siku. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kwenye mikopo. Serikali ya Chama cha Mapinduzi jamani nyote ni mashahidi, Mheshimiwa Rais alisema kitu chenyewe ni mkopo halafu kinacheleweshwa lakini sasa hivi hakipo kabisa, siyo kinacheleweshwa hakipo kabisa, ndiyo. Hatujaja kugombana na wanafunzi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanasema ukisoma shule ya private hupati mkopo. Wengine wamesoma shule za private kwa sponsor na ni wengi. Kwa mfano, shule ya mama yangu Tibaijuka karibu nusu wanakuwa na ma-sponsor sasa leo hii anafauli kwenda chuo kikuu amepata divison one, eti mnamwambia kwa sababu umesoma shule ya private haupati mkopo. Hatuko kwa ajili ya hiyo, hatujaja kugombana na wanafunzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne ni hili ambalo sasa hivi limekuwa kama linashika headlines la dawa za kulevya. Jamani mimi naomba niwaambie, sisi viongozi na naomba ni-quote Ahadi Namba 8 ya mwana TANU, nitasema ukweli uongo kwangu mwiko. Kwa hiyo, nitakachosema mtu yeyote akitaka anihukumu akihukumu chama changu kwanza na kama wewe mwana CCM utanichukia, rudisha kadi ndiyo unichukie. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wa dawa za kulevya hamna asiyewajua, tunawajua! Humu ndani wapo, nje ya Bunge wapo, kwa nini hatuwataji tunakaa kimya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kwa ridhaa yako unaniruhusu mimi nitawataja hata humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa za kulevya ni pamoja na bangi. Kuna Mbunge alisimama humu alisema bangi hazina madhara, alijuaje kama hazina madhara kama hatumii? Tungeanza na huyu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wenzangu, naomba niwahakikishie kama tutakuwa wanafiki mbinguni sisi ndiyo tutakaokuwa kuni. Tunawafumbia macho wafanyabiashara wa dawa za kulevya na tunakula nao. Nimpongeze sana ndugu ya Makonda wa Dar es Salaam kwa kuthubutu kutaja neno dawa za kulevya lakini nimhakikishie katika kila marafiki watano wanaomzunguka, watatu ni wafanyabiashara ya dawa za kulevya, aanze na hao! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais watu wasikuchezee akili…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Goodluck.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana. Kwanza, wiki iliyopita kwa siku mbili mfululizo nimetuhumiwa kuwa nabebwa na kiti chako kuwa natumia nafasi yangu vibaya, kwa hiyo naomba; unapopata tuhuma kama hizi, ninapopata nafasi kama hii inabidi na mimi nijitetee kwa nafasi yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulifanyika uchaguzi wa Wabunge la Afrika Mashariki. Wajumbe walioletwa kutoka upande wa CHADEMA walipata kura nyingi za hapana; lakini naomba nifafanue kupitia mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The Treaty For The Establishment of East African Community 1999) ambao umekuwa Revised mwaka 2006, Article 50; Election of Member of the Assembly namba moja, inasema hivi "The National Assembly of each Partner State….
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba muda wangu ulindwe, Mheshimiwa dada yangu Halima Mdee amesahau kumalizia Utawala Bora. Naomba niendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, Article 50, election member of Assembly inasema hivi:- “The National Assembly of each partner state shall
elect…”
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi kuwa CCM tulikuwa tuna nafasi sita, tulileta watu kumi na mbili. Najenga hoja, najenga hoja nimetuhumiwa.
T A A R I F A....
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Alipokuwa anaelekea Mheshimiwa Nassari ndiyo huko huko ndio nilikuwa naenda. Kifungu namba moja kinasema hivi; a partner state shall elect assembly, yaani kwa Kiswahili Bunge la nchi mwanachama
litachagua. CHADEMA mlichagua huko hapa mlileta tu-approve, hapa tofauti ni lugha. Ndiyo maana nasema CHADEMA mna Wanasheria wengi, lakini hao Wanasheria wanashinda mahakamani kuwatetea watu ambao wanamtukana Rais badala ya kuwasaidia nyinyi humu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo lilipigiwa kelele ni suala la gender. Katika hicho hicho kifungu namba moja ukiendelea kukisoma mbele kimezungumzia gender, interest groups. Nikauliza ninyi mtuambie, mnatulaumu sisi hatujachagua hii kanuni mlisoma? Imezungumzia gender, nikawaambia mniambie kati ya Masha na Wenje nani alikuwa anawakilisha hizo gender? Mmekataa kusema, matusi yangu yako wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema hivi tuwe tunaangalia viongozi tunaowachagua, wakati sisi tunachagua Mwenyekiti wetu wa Chama wa PhD, ninyi mlichagua Mwenyekiti wenu wa Chama form six zero.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili, naomba niishukuru Serikali kwa uje…
KUHUSU UTARATIBU....
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba muda wangu ulindwe, nimesema sisi wakati tunachagua Mwenyekiti PhD holder wao
walichagua form six zero, sijasema wao nani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa sababu nilisha-declare humu ndani kuwa yule ni baba mkwe wangu naomba niyafute hayo maneno.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende upande wa Jimbo langu la Ulanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee niishukuru Serikali kwa ujenzi wa Daraja la Kilombero. Kwa Waheshimiwa Wabunge ambao
mmeshatembelea lile Jimbo la Ulanga mliuona ule Mto Kilombero, limetusaidia kwa kiasi kikubwa sana. Watu walikuwa wanakufa upande wa pili huku wakiiona hospitali ipo upande wa pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa namna ya pekee kabisa, shukrani za pekee kutoka kwa wana Ulanga. Naiomba Serikali ijaribu kutusogezea kipande cha lami kutoka Kilombero mpaka Mahenge Mjini, hiyo itakuwa imetusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mvua zinanyesha, kwenye Jimbo langu la Ulanga tumekumbwa na adha kubwa ya mafuriko, madaraja yamebomoka, hamna mawasiliano kutoka Kata moja kwenda nyingine. Naiomba Serikali kwa jicho la pekee walitazame Jimbo la Ulanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Walimu. Serikali ilisimamisha kupandisha madaraja Walimu kwa muda mrefu kwa ajili ya kupisha uhakiki, maajabu yangu yanayokuja, kuna Walimu wamekaa miaka kumi na mbili hawajapandishwa madaraja. Leo hii Serikali imekuja na uamuzi kuwa Mwalimu hawezi kupandishwa daraja mpaka aende mafunzo. Hao waliokaa miaka kumi na mbili wakisubiria kupandishwa madaraja haijatoa mwongozo watawafanyaje? Wengine wanakaribia kustaafu na wamefanya kazi muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, katika Jimbo langu la Ulanga wananchi wamejitolea hasa Kata ya Ilagua wamejenga shule wameweka watoto wanasoma, wenyewe wazazi wameajiri Walimu, lakini Serikali mpaka leo hii wameshindwa kuzisajili hizo shule. Naomba Serikali kwa fursa ya pekee kabisa muwasapoti wananchi wa Ulanga kwa kuzisajili shule hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la nne, katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Wakuu wa Idara wengi wanakaimu, hii inachelewesha maamuzi. Kwa hiyo, naomba Utumishi kwa kushirikiana na TAMISEMI, mfanye mchakato wa haraka hawa Wakuu wa Idara wathibitishwe ili kutochelewesha maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la tano; katika historia yangu ya maisha nilimsikia mtu mmoja marehemu aliyekuwa anaitwa Kombe. Kombe kwa nilivyosoma kwenye vitabu ni kwamba alipigwa risasi na watu, Maofisa wa Serikali; lakini kwa macho yangu nimeshuhudia hivi karibuni Waziri mstaafu na Katibu Mwenezi Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi alitolewa bastola hadharani, bila kificho na watumishi wanaosadikiwa kuwa ni wa Serikali. Nilitegemea Mheshimiwa Waziri Mkuu atatoa kauli, Mawaziri mtatoa kauli, Wabunge mtatoa kauli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi, kama yule Waziri mstaafu ametolewa bastola hadharani Serikali ikakaa kimya, leo hii tutakuwa na uhakika gani hawa wanaoua maaskari si Watumishi wa Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema hivi; Waheshimiwa Wabunge tuwe tunaangalia vitu vya kutumia kabla
hatujaingia humu Bungeni. Kuna Wabunge wameingia wamelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushahidi Mheshimiwa Nasari ameingia na Konyagi amezuiliwa hapo getini na mpaka saa hizi amelewa.
Naomba tuangalie vitu vya kutumia kabla hatujaingia humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba moja kwa moja niende katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Ulanga. Hospitali ya Ulanga hali yake ni mbaya sana kiasi kwamba haiendani na hali ya Mbunge kama ilivyo, Mbunge mahiri na machachari. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, katika Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, watumishi ni wachache, yaani wachache kupindukia. Madaktari ni wachache, wataalam kama wa X- ray yuko mzee mmoja ambaye alishastaafu miaka mingi iliyopita ndiye tunamtumia huyo huyo kwa kumwajiri kwa mkataba. Pia ultrasound na yenyewe haina mtaalam, Serikali imejitahidi imenunua ultrasound mpya lakini hamna mtu wa kusoma. Hali hii imesababisha kumtafuta mtu kutoka Hospitali ya Saint Francis – Ifakara ambaye anapaswa kusafiri mpaka Ulanga kwa ajili ya kuja kusoma hivyo vipimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wodi zilizopo ni za tangu enzi za Mkoloni, na ni chache. Mheshimiwa Waziri naomba ujaribu kutembelea uone kwa kiasi gani Wilaya ya Ulanga tunavyopata tabu. Wagonjwa wanachanganywa, kwa mfano akinamama ambao wamefanyiwa operation wanaenda kulazwa wanachanganywa na wagonjwa wengine. Hali hii inapelekea hatari kwa magonjwa nyemelezi ambayo yanaweza yakasababishwa kutokana na vidonda vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chumba cha upasuaji cha Hospitali ya Ulanga kina hali mbaya sana, kiasi cha kwamba kama ingekuwa Hospitali ya Private ingefungiwa. Chumba cha upasuaji hakina monitor matokeo yake Madaktari wanatumia uzoefu wao binafsi kama waganga wa kienyeji kwa ajili ya kuwafanyia operation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Ulanga mashuka ya wagonjwa yanafuliwa kwa mkono, kiasi cha kwamba inapelekea hatari kwa hawa wafanyakazi. Hebu fikirieni mashuka ya wagonjwa yanafuliwa kwa mkono, Mheshimiwa Waziri akienda kweli machozi yatamtoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Ulanga haina gari ya wagonjwa, gari iliyokuwepo niliyonunua mimi ambayo haiendani sawa na ukubwa wa Jimbo. Gari yenyewe ni haice, nimejitahidi nimenunua basi Serikali iseme jamani kijana wetu umejitahidi hata mniunge mkono muongeze lingine. Liko lingine ambalo nimelichukua najikongoja kulitengeneza sasa hivi mwaka mzima lakini nimeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wa Hospitali ya Ulanga, uniform mwaka wa saba huu wanajinunulia wenyewe, hakuna uniform allowance, hebu fikirieni Maaskari wananunuliwa uniform, sehemu zingine wananunuliwa uniform, Ulanga pamoja na hali ngumu ya uchumi lakini wanajinunulia wenyewe, kwa hiyo naomba muwaunge mkono kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa; Wilaya ya Ulanga, ndio inaongoza kwa wagonjwa wa kifafa duniani, dawa za ugonjwa wa kifafa zinatolewa bure Tanzania lakini cha ajabu dawa hizi Ulanga zinauzwa. Ukienda Hospitalini hazipo, lakini kwenye maduka ya private zipo. Kwa hiyo naomba mliangalie hili hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nipingane kwa nguvu zote kutokana na maoni ya Kamati wanasema huduma za NHIF ziboreshwe ili mashirika ya umma yajiunge. Wewe ni shahidi ili nyumba uimalizie vizuri inatakiwa uhamie ndani ndiyo utamalizia, ukisema nisubiri niimalize hutoweza kuhamia. Kwa hiyo tunataka, kwa sababu NHIF inaendeshwa kwa michango, haya Mashirika ya Umma yaingie, yakishaingia michango yao ndiyo itakayoboresha hizo huduma. Kwa sababu gani tunasema huduma bora, NHIF ndiyo yenye vituo vingi Tanzania, hakuna shirika lingine la bima ya afya ambalo linatoa huduma katika vituo vingi, NHIF inatoa huduma bila kikomo. Shirika gani la bima ya afya ambalo linatoa huduma bila kikomo tuseme tusubiri huduma ziboreshwe? NHIF ina wanufaika wengi kuliko bima za afya zingine, tunataka huduma zipi ndizo ziboreshwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo yangu ni hayo machache kwa ajili ya kutunza muda. Ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe pole kwa Wana-Ulanga wakatoliki kwa msiba wa Father Mdai ambaye amefariki Ijumaa. Suala langu la pili, naomba nitoe pole kwa wananchi hawa wa Ulanga kwa barabara mbovu zilizotukuka lakini naomba niwahakikishie kuwa Mbunge wao nipo na nitapambana mpaka kieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi nitakuwa upande wa binadamu maana maliasili wao wamejisahau kama siyo Watanzania na kama si binadamu, wanawachukia binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Ulanga kuna tatizo kubwa la wanyama waharibifu hasa aina ya boko katika kata za Ketaketa, Ilonga, Mwaya, Iyuga na Chilombola. Boko hawa wamekuwa wakiharibu kwa kiasi kikubwa mazao ya wananchi mazao ya wananchi na kupelekea njaa, lakini wananchi wanapowagusa wale boko Maafisa Wanyamapori wanawakamata wanawafungulia mashtaka wanawapa kesi za kuhujumu uchumi. Wanyama wanapovamia tukiwaambia Maafisa Maliasili hawa–responds katika muda ambao unatakiwa. Tumeomba watuongezee ma–game kwa ajili ya kupiga hawa wanyama hawataki, tukitaka tuwavune hawa boko ili wananchi nao wapate kitoweo hawataki.

Sasa mimi naomba niiombe Wizara ya Maliasili mimi kama Mbunge nita–recruit ma–game wa kienyeji katika kila kata kama wao hawatafanya; katika kila kata ambao kazi yao kubwa itakuwa kufukuza hao boko ambao wanaharibu mazao ya wananchi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika Jimbo la Ulanga mazingira yake eneo kubwa ni milima na maeneo machache yaliyoko tambarare yote ni maeneo ya maliasili. Upande mmoja lipo eneo tepe tepe wanaliita eneo oevu ambalo kwa kiingereza analiita buffer zone, upande mwingine liko Ilumo na upande mwingine iko Selous Game Reserve.

Kwa hiyo, sasa mshangao wangu mkubwa wakati Wizara inafanya utafiti mwanzo inaweka hiyo mipaka walisahau kama wananchi wanazaliana. Kwa hiyo sasa hivi wananchi ni wengi na eneo ni dogo na hivyo wananchi wanakosa eneo la kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaposogea katika maeneo ya hifadhi kidogo watu wa maliasili wanakuwa wakali. Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alipendekeza na aliunda Tume ifanye mchakato ili kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima, lakini mpaka leo hakuna majibu. Mwaka jana baada ya mimi kuwakomalia Wizara wakaja wakatuchukua Wabunge wakatuzungusha na ndege kipindi cha kiangazi, wakasema mnaona wananchi wanavyoharibu maeneo? Mimi nikawakatalia niawaambia kwa nini mnatuzungusha kipindi cha kiangazi? Kwa nini msituzungushe kipindi cha masika. Kwa hiyo, sasa naomba Wizara kupitia hiyo tume yake itoe majibu haraka ili wananchi wapate maeneo ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nilikuta suala la Operation Tokomeza. Nimeenda nimekuta wananchi wana majonzi makubwa, wananchi wengi wa Ulanga wamekamatwa na mpaka sasa hivi wako ndani na hawajafunguliwa mashitaka yoyote. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara kupitia ofisi ya DPP waharakishe ili watu wenye hatia wahukumiwe na watu ambao hawana hatia waachiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo mambo yangu yalikuwa ni machache, hayo yanatosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante sana. Kwanza kwa namna ya pekee naomba kutoa pole kwa Mbunge mwenzangu, jirani yangu Mheshimiwa Hadji Mponda kwa kufiwa na mpiga kura wake, Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Mwambungu. Pili, naomba kutoa shukurani za pekee kwa Baba Askofu Agapitus Ndorobo wa Dayosisi ya Mahenge kwa shule zake za Regina Mundi, Kasita Seminary, St. Agness na St. Joseph zimekuwa Kinara kwa kuitangaza Ulanga kwa ufaulu. Kwa hiyo, mnaposikia Kasita Seminary kuna watu wanaisikia inafaulisha lakini hawajui kama ipo Ulanga kwa Mlinga.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kuipandisha elimu ni pamoja na barabara kwa Majimbo yetu ambayo yana mazingira magumu kama Jimbo la Ulanga. Sasa hivi kuna maeneo hayafikiki kabisa. Kwa mfano, kuna eneo linaitwa Isaka hata baiskeli haiendi na ni zaidi ya kilometa 25, kuna eneo linaitwa Lyandu hakufikiki, kuna eneo linaitwa Majengo kilometa zaidi ya 27 hata baiskeli haifiki, kama Waziri wa barabara upo na unanisikia, naomba uli- note hilo kuwa kinachochangia elimu katika Wilaya ya Ulanga kushuka ni pamoja na miundombinu mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa shukrani na kuwapongeza Maafisa Utumishi wa Wilaya ya Ulanga. Mheshimiwa Spika hapa alilipongeza Bunge kwenye suala la vyeti fake kuwa hakuna hata mtu mmoja nami naomba niwapongeze Maafisa Utumishi wa Wilaya ya Ulanga kwani Mtumishi mmoja tu ndiye aliyepatikana kwenye suala la vyeti fake na bahati nzuri alilala mbele kabla Rais hajatoa agizo kuwa hawa watu wafukuzwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika Jimbo langu la Ulanga wananchi wamejitolea kuna maeneo wamejenga shule, iko shule ya Mikochi, iko shule ya Kipingo na shule ya Mbenja katika kata ya Ilagua lakini suala zito limekuwa kwenye usajili. Wazazi wamejitolea, wajenga majengo, wametafuta walimu, wanawalipa wenyewe Serikali suala la kuisajili wanasema eneo hilo mpaka wapate kibali cha maliasili yaani Serikali hiyo hiyo, Mawaziri hao hao, wameteuliwa na mtu huyo huyo mmoja, lakini kutoka ofisi moja kwenda nyingine inachukua miaka mitatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba unisaidie unisajilie shule zangu ili tuweze kupata walimu wa Serikali na tuweze kupata vituo vya kufanyia mitihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni madai ya walimu, hivi naomba niulize, nilishawahi kumuuliza ofisa mmoja mkubwa Wizara ya Elimu akasema tatizo zinalochelewesha madai ya walimu kwa sababu walimu wapo wengi. Nikamuuliza walimu wengi kwa sababu sisi tunazaa sana? Tungekuwa na watoto wachache walimu

wangekuwepo wengi? Kwa nini tunawanyanyapaa? Wabunge leo hii maslahi yetu yakicheleweshwa macho yanatutoka na tunaibana Serikali na wanawahi kututekelezea, kwa nini kwa walimu iwe tatizo hili na wakati Walimu ndiyo waliotufundisha? Huwezi kuoa bila kuandika barua ya uchumba, lakini walimu ndiyo waliotuwezesha sasa hivi tunawasahau. Humu Wabunge wengine ni maprofesa, wengine madaktari kwa sababu ya hawa walimu, lakini inapofika suala la maslahi yao tunaongea, kwenye kuibana Serikali hatuibani, inaishia kupiga makofi tu yamekwisha. Naomba kwa uchungu kabisa nitajitolea kuwa Balozi wa Walimu katika Bunge hili, yaani sitoki mpaka masuala ya walimu yaeleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano suala la nauli, walimu wanaenda likizo nadhani kwa miaka miwili mara moja na hapewi nauli, lakini Maofisa wengine kila mwaka wanaenda likizo na wanapewa nauli, tena nauli zenyewe ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyeo katika Jimbo la Ulanga kuna walimu miaka 15 kafanya kazi hajapandishwa daraja ukiuliza kwa nini? Wanasema hatujapata bajeti, hivi wakati mnamuajiri mlikuwa hamjui kama atatakiwa apandishwe cheo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ukaguzi; kinachochangia Wilaya ya Ulanga elimu kushuka Wakaguzi hawana gari, kwanza ofisi yenyewe ukiiona huwezi kutamani, hawana usafiri, Jimbo lina mazingira magumu mnategemea wataendaje! Mheshimiwa Waziri naomba unisaidie gari Wakaguzi wa Elimu wa Ulanga ili waweze kwenda kuzikagua shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna chama kimoja kinaitwa CWT (Chama cha Walimu), naomba nitumie kauli ambayo siyo nzuri, hiki chama kimekuwa kinawakandamiza walimu; kwa sababu mwalimu anapoajiriwa anatakiwa achangie humu kwa lazima, kuna Walimu Ulanga hawajui hata CWT ndiyo nini, anaiona kwenye salary slip kuwa amekatwa hela lakini hajawahi kupata chochote na hajawahi kusaidiwa chochote na hiki chama. Nilitoa pendekezo hapa mwaka jana kuwa walimu wajiunge kwa hiari kwenye huu mfuko ilia one kama una msaada ndiyo ajiunge, kama hauna masaada asijiunge. Wizara mnaliona, mnalifhamu na mnaliachia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nadhani upo, kuna shule inaitwa Kwiro sekondari nilisoma hapa ndipo nilipoanzia form one, hii shule ina wanafunzi 520 wa sayansi lakini haina mwalimu wa hesabu, hawa ni wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita hivi mtu anasomaje sayansi bila kusoma hesabu? Alipangiwa mwalimu mmoja kwenda hapo na mpaka leo hii haja-report, kwa hiyo, hawa wanafunzi wanasoma lakini somo la hesabu hawasomi, sasa watafanyaje mtihani wa kidato cha sita hawana mwalimu wa hesabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ya sekondari hii imechukua jina la Mama yangu Waziri mwenzenu wa zamani, Celina Kombani. Hii shule inatarajia kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita lakini haina bwalo la chakula na haina jiko na nimeshaandika barua kwako, naomba unisaidie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la VETA; Mheshimiwa mmoja hapa alichangia kuwa wanafunzi wanaofeli waende VETA, naomba nimpe taarifa kuwa VETA siyo pango la vilaza, wako watu wana akili zao kule. Mheshimiwa Waziri, VETA walikuja Ulanga, tuliwapa eneo, walilikagua na walikubali lakini sasa hivi wameingia mitini, naomba tulifuatilie suala hili ili waje kujenga hiki chuo na eneo tulishawapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho ni suala la mikopo ya elimu ya juu. Tumeongeza asilimia kufikia 15, Mheshimiwa Waziri naomba ufanye assessment, nenda kaangalie hiki kilio cha wafanyakazi hii asilimia 15 inavyowaumiza, tuwaonee huruma. Mimi naomba tuleteile sheria hapa Bungeni ili tufanye marekebisho, kwa sababu

wote ni mashahidi mfanyakazi yoyote anapopata ajira cha kwanza kwenda kuchukua mkopo na anachukua mkopo mpaka kwenye cealing ya mshahara wake. Mkopo wa Bodi ya Mikopo walikuwa wanachukua asilimia nane sasa hivi asilimia 15, hebu fikirieni maisha yakoje huko uswahilini na sasa hivi hakuna posho zozote sasa hivi ninyi wenyewe mnajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kabisa, Serikali imesema kuwa haitoajiri tena walimu wa masomo ya arts; Mheshimiwa Waziri Serikali hii ndiyo ilikuwa inasimamia hawa wanafunzi waende wakasomee ualimu masomo ya arts leo hii inasema hawawaajiri, sasa hawa watu watakwenda wapi? Watakwenda kuajiriwa sehemu gani?

Kwa hiyo, naomba mlifikirie upya, ninyi ndiyo muwatafutie alternative “B” kuwa watafanyaje. Wataendelea kukaa uswahili hivi na wameshasoma halafu sasa hivi mnawaambia lazima walipe mikopo baada ya muda fulani, hizi hela wanatoa wapi? Wakiwa wakabaji sheria zinakuwa kali mtaani. Huo ndiyo mchango wangu mdogo kwa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwenyekiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze moja kwa moja kwenye mjadala, japokuwa wameni-pre-empt kwa kiasi kikubwa, nitaomba niyarudie yale lakini ni kwa msisitizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la kwanza ni ushukaji wa elimu kwa shule za Serikali za Tanzania. Kwa muda wa miaka miwili sasa Waziri wa Elimu amedumu katika Wizara hii lakini tumeshuhudia kwa uangukaji mkubwa wa shule za sekondari za Serikali. Mpaka sasa hivi anaweza akajipima yeye mwenyewe ni kwa kiasi gani ni mzuri na kwa kiasi gani ni mbaya. Kwa hili naingiwa hofu, sielewi, sijui Maprofesa wa Tanzania wana tatizo gani? Ingekuwa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais, angechaguliwa mtu kama Musukuma au Mheshimiwa Lusinde ambao wameishia darasa la saba kuwa Mawaziri wa Elimu kwa sababu wanajua matatizo gani yaliwafanya wasiweze kusoma. Maprofesa wa Tanzania wamekuwa wakiongoza kutoa miongozo, matokea yake elimu zinafeli. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu matokeo ya kidato cha nne shule za Sekondari katika kumi bora hamna na ndiyo tulizoeaga Mzumbe, sijui Kilakala sijui wapi, hazipo. Katika shule 100 bora za sekondari, shule za Serikali ziko nne. Jamani, hii si aibu!

Mheshimiwa Waziri wa Elimu una kitu gani cha kutuambia hapa? Hii ume-prove failure, haiwezekani. Halafu sasa ukija unawapiga vita watu wenye shule za sekondari za private. Sasa kwa mfano hizi shule za sekondari za private tungeziondoa katika orodha ya zile shule 100, wewe si ungekuwa Waziri wa masifuri! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, angekuwa Waziri wa masifuri maana yake shule za Serikali zote zimefeli, shule za private ndiyo zinaongoza. Sasa ana nini cha kujivunia? Ukimwuliza tangu aingie madarakani yeye vita yake na shule za sekondari za private. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri wa Elimu amekuja na nyingine, bado anawakomalia, hakuna kukaririshwa madarasa. Sasa unasema watu wasikaririshwe madarasa lakini unaruhusu watu form four wa-re-sit, ungeondoa sasa, hamna watu kurudia mitihani ya kidato cha nne. Hapo tungekuelewa! Unasema wanafunzi wasikaririshwe madarasa, unataka wawahi wapi? Wanakuhusu nini? Tunasema elimu haina mwisho. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikupe kwa nini wanafunzi wa shule za sekondari za Serikali wanafeli? Mazingira mabovu ya walimu. Leo hii walimu wanadai malipo yao ya muda mrefu, mnasema mnahakiki, mnataka watoe risiti. Mbona sisi Wabunge tukileta madai yetu hamtuambii tulete risiti? Mnawaambia walimu walete risiti, mnawacheleweshea malipo. Walimu mnawapangia maeneo ya vijijini, hajui akaishi vipi, nyumba hakuna, ukienda walimu wanaishi kama makondoo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu hawana break. Wote mtakuwa mashahidi, ukienda kwenye shule mwalimu anaingia saa moja asubuhi mpaka saa kumi na moja jioni kama mfungwa. Wanafunzi wanaenda break saa nne, walimu hawana. Ule muda wa break ndio anatumia kusahihisha madaftari ya wanafunzi. Hamwangalii hili!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhalilishaji, leo hii mwalimu hana bosi. Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Utumishi, Waziri, wote mabosi zake. Huyo mfanyakazi wa namna gani? Hata sisi tungeweza? Sisi tungeweza kila mtu awe bosi wetu? Spika awe bosi wetu, Rais awe bosi wetu, sijui nani awe bosi wetu? Kwa hiyo, mnawachosha walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mwalimu akitaka kuhama ni msala (kazi), anaambiwa atafute mtu wa kubadilishana naye. Hebu niambie mimi nataka kwenda Dar es Salaam, naambiwa nitafute mtu wa kubadilishana Dar es Salaam. Hiyo kazi mimi nitaweza? Hiyo ni kazi ya mwajiri au mwalimu mwenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuchangishwa michango isiyo ya muhimu. Eti leo hii walimu wanaandikiwa barua na Mkuu wa Wilaya watoe michango ya Mwenge. Jamani! Mshahara wenyewe anaoupata mdogo, halafu mnamwambia atoe mchango wa Mwenge, huu ni uonevu wa hali ya juu. Mbona Wabunge hatuambiwi tuchangie Mwenge? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, hakuna malipo ya overtime. Mimi nimetoka kwenye semina; kila semina tunayoingia tunaulizia kwanza malipo, lakini walimu wanafanya kazi mpaka weekend, lakini hawapati malipo yoyote, jamani huu ni uonevu. Halafu elimu inashuka, Mheshimiwa Waziri anakazana na shule za private badala akazane na shule zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie upande wa NHIF. Kamati imezungumzia suala la huduma za Bima za Afya kwa watu wote. Mheshimiwa Waziri wa Afya ukija naomba uniambie, NHIF haiwezi ikatoa huduma kwa watu wote, kama mashirika ya umma yenyewe ambayo yanatakiwa kisheria yajiunge kule hayajajiunga, tunawang’ang’aniaje watu wa mtaani ambao kwenye sheria haiwahusu? Tuanze kwanza na hilo. Kwa hiyo, akija Mheshimiwa Waziri wa Afya naomba aniambie, mpaka leo hii mashirika mangapi ya Serikali ambayo yameingia?

Mhshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa za kiintelijensia kuwa BoT baada ya mimi kuongea Bungeni kuwa mashirika yote yanatakiwa yahamie NIHF wamesaini mkataba wa siri na Jubilee Insurance wa miezi mitatu, ili tukiliamsha huku Bungeni waseme mkataba unaisha keshokutwa. Kwa hiyo, sasa hivi wanasaini mikataba ya miezi mitatu mitatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akija naomba aniambie. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala ambalo alizungumzia Mbunge mwenzangu kuhusu vitendo vya ushoga. Jamani vitendo vya ushoga vimeshamiri katika nchi yetu. Sasa basi ubaya unaokuja, watoto wadogo wa kiume wanavyokua wanajua ushoga ni fashion na hii inayoharibu yote ni mitandao ya kijamii. Wanajitangaza sasa hivi kwenye mitandao ya kijamii, Mawaziri mnawaangalia. Sasa sijui mnataka wafanyaje? Mbona wengine wanaotukana wanawakamata, lakini wanaojinadi katika mitandao ya kijamii mnawaachia? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Afya ukija naomba mtujibu, mmechukua hatua gani kuhakikisha ushoga hauendelei katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine nilikuwa sijalimalizia, Mheshimiwa Waziri hajatuambia, vile vitabu vibovu tulivyovizungumza vilivyokuwa vimeandikwa mbele nyuma na nyuma mbele, vimeishia wapi? Hatujapewa majibu na Serikali hii kuwa wale watu wamechukuliwa hatua gani? Vile vitabu vimetengenezwa vingine au vinaendelea kutumika vilevile? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba niishie hapo kwa leo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niweke rekodi sawa, jana katika Uwanja wetu wa Ndege wa Dar es Salaam ilitua ndege ambayo imeaminishwa kuwa ndiyo ndege kubwa kuliko zote kuwahi kutua. Nasema hapana, kwa sisi ambao tulikuwa wa kwanza kwenda Dar es Salaam, tarehe 06 Novemba, 2009 ilitua ndege aina ya Antonov An 225 ambayo ilileta mitambo ya Richmond, ndege hiyo ilikuwa na uzito wa tani 285 wakati iliyotua jana ina tani 276, hiyo ndege ilikuwa na urefu wa mita 84, ile iliyotua jana ilikuwa na mita 73; hiyo ndege ilikuwa na bawa lenye ukubwa wa mita 88, ile ina mita 80; hiyo ndege ilikuwa na injini sita, ile ya jana ina ijini nne; kwa hiyo tupo vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili, kusifia sio unafiki, hata dini zetu zinatuambia unapotaka kuomba lazima usifie. Kwa sisi Wakristo unapotaka kumuomba Mungu unaanza Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike, sasa hapo swala ikishakolea unachomeka matatizo yako. Ndugu zangu Waislam tunasema Bismillah Rahman Raheem, Ewe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mwenye kurehemu, mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo; ukimaliza hapo unachomeka matatizo yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu, ninyi mkisimama mnaanza kukejeli Serikali, mnaitukana Serikali, mambo ya wapi hayo? Mimi sijawahi kumuona mtu anasema Mwenyezi Mungu ile mvua ya jana iliyonyesha ni mbaya imetuletea mafuriko, leo naomba hiki, mbona sijawahi kuona mkimwambia Mungu, kwa nini mnaikejeli Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Lakini nimhakikishie sio kila neema anayoileta kwa Watanzania kuna watu wote wataifurahia, hata Mwenyezi Mungu neema anayotuletea sio wote wanaifurahia. Kwa mfano mvua inaponyesha ni neema kwa wakulima, lakini wauza mitumba, wamachinga wanachukia. Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Rais hao wanaochukia neema anayoileta awachukulie sawasawa na wale wamachinga ambao wanaichukia mvua, aichukulie sawasawa na wauza mitumba ambao wanaichukia mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu hawana jema. Katika miradi yote ambayo imefanywa sijawahi kuona hata mradi mmoja ambao wanausifia, imeletwa reli wanalalamika, leo tunaanzisha mradi wa Stiegler’s Gorge wanalalamika, elimu bure mnalalamika, ununuzi wa ndege mnalalamika. Hebu waambieni Watanzania ni kitu gani chema kwenu ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa maana yangu. Hiki kitabu mnachokiona cha hotuba ya Waziri, hii picha ya mbele sio Daraja la Ulaya wala sio Daraja la Kigamboni, ni daraja ambalo limejengwa katika Jimbo langu la Ulanga, daraja la kimataifa. Kwa hiyo, mnapoona ninyi mmepata ndege, mimi napata vitu kaa hivi, nimshukuru Mheshimiwa Rais, na tunalifungua wiki ijayo kwa hiyo vitu vinafanyika, tafuteni utaratibu mzuri wa kushauri na kuomba, mtavipata. Lakini tangu bajeti imeanza mnatukana matusi, sijaona mpinzani ameomba hata bomba la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niishukuru Serikali kwa kutupa pesa kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 68 za lami kutoka Kidatu mpaka Ifakara. Lakini ninachoomba watumalizie na kile kipande kingine toka Ifakara mpaka Mahenge.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja, a luta continua.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na nimpongeze kwa hotuba yake nzuri ambayo imeitoa leo, nilikuwa na karatasi karibia nane za kuchangia, lakini nimejikuta kila akitoa hotuba nachana moja baada ya nyingine na sasa nimebakiwa na kipande nusu ambayo nitaitoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa programu yake ya elimu bure, katika hili Mheshimiwa Rais ametusaidia hasa ambao tunatoka majimbo ya vijijini ambayo asilimia kubwa wazazi ni wakulima. Kuna changamoto chache fedha hii imekuwa ni kidogo sasa hivi utakuta katika shule zetu za kule vijijini walimu yale mazoezi ya kila Jumamosi wanaandika ubaoni. Kwa hiyo, naomba waongeze pesa ili walimu waweze kwenda kisasa na kuwapunguzia mzigo wa kuandika ubaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine sasa hivi Serikali ambacho inatakiwa tu kuifanya ni kuwafanya walimu waifurahie ile kazi kama kazi zingine wasiichukulie kama tunavyowachukulia, wawajengee nyumba, wawapandishe madaraja kwa muda, maana yake kumekuwa na changamoto kuna walimu wanafundisha hadi miaka 12 hawajapanda daraja hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hili linahusu upande wa TAMISEMI kidogo, lakini naomba mshirikiane na Wizara. Hawa Walimu ambao wametolewa sekondari kupelekwa shule za msingi kuna sintofahamu, kuna walimu ambao wana diploma wameachwa sekondari, wamechukua walimu wenye degree wamewapeleka shule za msingi hili ni tatizo kwa sababu mliwaachia Walimu Wakuu na Maafisa Elimu walisimamie wenyewe matokeo yake wamefanya ndivyo sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ukaguzi ameliongelea Mheshimiwa Maghembe; Wakaguzi wengi hawa hata vyombo vya usafiri. Sasa kwa ambao tunatoka majimbo ya vijijini inawawia vigumu kwenda kukagua hizo shule matokeo yake wamekuwa wakikagua makaratasi na ndiyo maana ufaulu unashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea suala la vitabu wiki iliyopita kwa kweli hili ni tatizo, tuna shule zaidi ya 170,000 vitabu vya darasa la nne ambao wanatakiwa wafanye mtihani mwezi wa Novemba mpaka leo hii havijatoka. Hebu niambie, kuvisambaza hivi vitabu Serikali yetu ninavyoifahamu na ukosefu wa magari katika Wilaya zetu huko kwenye sekta ya elimu vinaweza vikachukua zaidi ya mwaka mmoja. Kwa hiyo, wananfunzi wa darasa la nne mwaka huu ninauhakika watafanya mitihani wakiwa hawajapata vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kukariri madarasa, hii iko kwenye secondary schools. Wizara tulitoa maoni, Kamati wametoa maoni na Wabunge tunaomba kusisitizia, endapo tutaruhusu wanafunzi waende ili mradi waende baada ya miaka mitano tutazalisha kizazi cha wanafunzi ambao hamna kitu. Kwa sababu huwezi ukampeleka mwanafunzi kidato cha pili kama hakuelewa kidato cha kwanza na hawezi akafanya chochote kidato cha pili kama hajafanya kidato cha kwanza.

Kwa hiyo, mngeliachia kwa shule za private wao wana utaratibu mzuri wafanye kwa ajili kuzalisha matokeo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nichangie kwenye upande wa Loans Board. Niipongeze Serikali kwa kuongeza fedha za loans board, lakini limetokea tatizo sasa hivi hakuna kigezo maalum cha kusababisha wanafunzi wapate mikopo. Kwa mfano, mwenyewe nina ushahidi, kuna Taasisi moja ya Solida Made ambayo ilikuwa inasomesha wanafunzi, inawasaidia kutoka shule za sekondari mpaka Chuko Kikuu. Mwaka huu walikuwa na wanafunzi zaidi ya 400, walikubali kuwalipia ada za Chuo Kikuu wale wanafunzi ambao hawana uwezo, ambao waliwasaidia tangu shule za msingi, lakini walivyofika Chuo Kikuu Serikali ikagoma kuwapa mkopo ikasema hawana utaratibu huo. Zile taasisi walichotaka ni Serikali iwagharamikie fedha za chakula, lakini ada watawalipia wenyewe, Serikali ikakataa. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu anaweza akanitolea ushahidi nilifika ofisini kwake, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo nilifika ofisini kwake, lakini wamekataa kuwapa wanafunzi hawa mikopo. Taasisi imetusaidia kuwalipia ada, lakini ninyi mmekataa kutoa fedha za chakula, kwa hiyo hili ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niliongea wiki iliyopita Waziri alisema hakunielewa vizuri na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi. Kumekuwa na tatizo ya Vyuo Vikuu, wanafunzi wetu wa kike wanapata shida mno. Katika vyuo vyetu vikuu kuna walimu ambao wanajulikana kabisa kuwa hawa Walimu ni madume ya mbegu, wanafelisha wanafunzi wa kike, wanataka wawape rushwa za mapenzi ndiyo wawafaulishe. Mheshimiwa Waziri nitashirikiana na wewe kama utanipa ushirikiano, nitakuletea majina ya walimu wa Vyuo Vikuu vyote Tanzania ambao ni madume ya mbegu kazi yao ni kufelisha wanafunzi na kutaka rushwa za ngono. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara chini kitengo chake cha P4R kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule za sekondari. Kwanza niwapongeze katika kujenga shule mpya na nyumba za Walimu. Mimi mwenyewe binafsi nimepata shilingi milioni zaidi ya 500 kwa ajili ya kukarabati shule yangu moja ila ninachoomba hii fedha ya P4R iende moja kwa moja kwenye Halmashauri lakini wasitumie Wakandarasi, kwa sababu tumeshuhudia wakitumia Wakandarasi fedha inakwenda nyingi lakini inafanya kazi kidogo lakini mkitumia Force Account ile fedha kidogo inafanyakazi kubwa. Naomba mtoe maelekezo hii fedha mtumie force account

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kushuka kwa ufaulu. Muda wangu bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia zaidi ya asilimia 60 wanapata division four na division zero, naomba mtumie nguvu kubwa katika kuwekeza katika vyuo vya ufundi hii miaka minne ambayo mwanafunzi anasoma kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne tungewekeza kwenye ufundi angeweza ku-achieve kitu kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka niiase Serikali yangu. Serikali yangu tumeichukulia shule za private kama adui, yaani tunavyoichukulia CHADEMA na CCM na ndiyo Serikali na shule za private. Imekuwa kumiliki shule ya private ni sawa na kupita na mihadarati katika kituo cha Polisi.

Naomba niwatoe hofu Serikali, mitaala mnatunga ninyi, mitihani mnatunga ninyi, tarehe ya kufanya mitihani mnaweka ninyi, kusimamia mnasimamia ninyi, mitihani mnasahihisha ninyi, matokeo mnatangaza ninyi, hofu yenu ni nini na shule za private? Fanyeni vizuri hizi shule za private zitakufa zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulinda muda, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie maoni ya Kamati, hotuba yake ni nzuri sana, tangu nimfahamu Waziri hotuba hii ni ya kwanza, good! Endelea hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa namna ya pekee naomba niishukuru taasisi moja ya kidini ambayo inachimba visima bure katika Jimbo langu la Ulanga, taasisi inaitwa AlFayed Charitable Foundation chini ya usimamizi wake wa Ndugu Khadija Ahmad, nadhani unaifahamu hii taasisi, hapa ndiyo najua uwezo wa wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii taasisi kiongozi wake ni mwanamke na inafanya kazi vizuri, kwa hiyo hongera sana wanawake, imeshachimba visima 57 na wana utaratibu wa kuchimba visima 300. Kwa hiyo, Jimboni kwangu suala la maji mambo ni poa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niweke katika record, katika Bunge lililopita wakati yupo Naibu Spika, Mbunge machachari kabisa kwa upande wa CCM alikuwa Mheshimiwa Luhaga Mpina, sasa hivi kwa bahati mbaya machachari tumeongezeka na bahati mbaya wewe upo huko, kwa hiyo, tuache tukushughulikie sehemu zile ambazo unakosea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapongeza zoezi la kupinga uvuvi haramu, kwa mfano Mto Kilombero samaki wamekwisha kabisa, lakini zoezi hili linaloendelea lina ukatili mkubwa, lina dhuluma kubwa, lina filisi watu, lina rushwa kubwa na linaleta usumbufu kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sidhani kama watendaji wa Serikali wana nia nzuri kama ya wavuvi ambao wanaishi katika yale maeneo na sijawahi kuona mkakati wa Serikali, labda tuseme mnawawekea pumba hawa samaki au mnawalisha au mnafanya nini, kwa nini mnakuwa wakatili kiasi hiki? Sielewi! Tunawafanya Watanzania kama siyo wapiga kura wetu, humu ndani tumeingia kwa kupigiwa kura, kwa hiyo tuwathamini watu waliotupigia kura.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili ni suala la nyavu na hii naomba niliseme wazi. Mheshimiwa Waziri Wizara yako imekithiri kwa rushwa, nasema hivyo kwa sababu viwanda vinavyotengeneza nyavu za samaki ni vichache na havina uwezo wa kukudhi soko, leo hii meli iko bandarini hawaruhusiwi kuingiza nyavu pale wanawekewa mlolongo mrefu na kwa taarifa nilizonazo wale wenye viwanda wamei–corrupt Wizara matokeo yake hamna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingiza nyavu ili wao wauze, lazima tuseme ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa spika, suala langu la tatu ni biashara ya samaki. Samaki wengi tunaokula wanatoka nje ya nchi, hata watu wanaoruhusiwa kuingiza wote ni watu weupe, wote ni Wahindi, watu weusi wote wamezuiliwa na hii ni kwa sababu ya rushwa. Mheshimiwa Rais wetu mweusi tangu wa kwanza, kwa nini hatuwaamini watu weusi? Viongozi, Mawaziri wote watu weusi kwa nini hatuwaamini? Akija muhindi, mwarabu tunamtetemekea, kwa nini tusiwaruhusu watu weusi ambao wana uwezo na wana uchungu wa nchi hii wasiweze kuingiza samaki?

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la malisho ya mifugo, katika jimbo langu la Ulanga tuna mapori mengi kweli …

T A A R I F A . . .

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Murrad utaniwia radhi nimewagusa, lakini hili suala linaumiza sana, kwa sababu watu wote wanaoingiza samaki hamna mtu mweusi hata mmoja, akienda wanasema hana uwezo! Kweli watu weusi hatuna uwezo? Hakuna watu wenye hela? Mabasi mbona wapo watu weusi wanamiliki akina Kimbinyiko wote siyo watu weusi? Hata Shabiby yule ni mweusi umeona lakini hawaruhusiwi wanaambiwa hawana uwezo pamoja na Mheshimiwa Murrad. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la malisho ya mifugo, kwa mfano Ulanga tuna maeneo mengi sana ya mapori, lakini wafugaji wanapotaka maeneo ya kulisha wanaambiwa maeneo hamna, kwa hiyo hawa watu wamekuwa wanahangaika. Naishauri Serikali tuwatengee maeneo ya malisho, tukishawatengea maeneo ya malisho sasa hivi ziko mbegu ambazo zinapandwa kwa muda mfupi zinaota nyasi nzuri kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Spika, kuhusu majosho ninaishukuru Serikali imeniahidi kunijengea majosho na malambo kwa ajili ya mifugo, napendekeza hizi mbegu za mifugo za madume bora ziweze kuuzwa kwa bei nafuu ili wananchi wetu waweze kumudu.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la watu wa maliasili kukamata mifugo na kuishikilia kwa muda mrefu na kuhitaji pesa kubwa, hii imekuwa unyanyasaji mkubwa sana kwa wafanyabiashara wetu wa mifugo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la masoko kwenye minada yetu wafugaji wanapopeleka mifugo sokoni wauze ama wasiuze wanatozwa ushuru, hili limekuwa linaleta usumbufu mkubwa, Serikali imeniahidi katika Jimbo langu la Ulanga litaweka utaratibu wa masoko mazuri ya mifugo, minada iwe ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la upigaji chapa, suala hili siliungi mkono kabisa, kwanza ni unyanyasaji wa wanyama, pili ni gharama wafugaji ambao hatuwasaidii kitu tunaenda kupiga chapa tu kwao tunataka pesa, tatu ni usumbufu kwa wafugaji wenyewe na hata kwa wanyama. Sababu wanayosema wanapiga chapa kwa wanyama ni eti wasichanganyike na wanyama wengine ambao wanatoka nje ya nchi. Jamani mbona watu wa mipakani hatuwapigi chapa, kwa nini tupige chapa mifugo? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naona hili zoezi lifutwe kwa sababu kwanza lina haribu hata thamani ya ngozi, kwa sababu ngozi ukishaipiga chapa thamani yake inashuka. Leo hii tunasema Tanzania ya viwanda, viwanda vya ngozi vitakosa mazao ya ngozi kwa sababu ya ubora mdogo wa ngozi.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo, machache mimi siungi mkono hoja, nataka huu mkazo wa kusitisha hii operation ya kuzuia uvuvi haramu, iundwe Tume ya Kibunge, litakapotolewa hilo ndipo nitaunga mkono hoja, la sivyo nitafanya kampeni ya Mbunge mmoja baada ya mwingine kuhakikisha bajeti hii haipiti na Mheshimiwa Waziri unajua uwezo wangu, nitafanya kampeni ya Mbunge kwa Mbunge kuhakikisha bajeti yako haipiti mpaka iundwe Kamati kwa ajili ya kuondoa hii operation haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niende moja kwa moja Ulanga. Jimbo la Ulanga au Wilaya ya Ulanga kwa ujumla ina kilometa za mraba 11,000 na inakadiriwa kuwa na watu 200,000; lakini asilimia 47 ya eneo hilo ni hifadhi na eneo lililobaki ni milima mikali na mabonde makali na eneo lingine ni madini, kama unavyoijua Ulanga ilivyo, lakini hiyo sio shida. Maeneo ya hifadhi ambayo tumezungukwa, tumezungukwa na Selous Game Reserve, Bonde la Mto Kilombero na Hifadhi ya Ilumo na hifadhi ndogo ndogo 14.

Mheshimiwa Spika, shida inakuja kwenye mipaka, upande ambao tumepakana na Selous Game Reserve kuna Kata tatu, Ilonga, Ketaketa na Mbuga, lakini kama kawaida ilivyo ya watu wa maliasili wameongeza mipaka kinyemela katika hizi kata tatu. Kuongeza mipaka sio shida, watu hao maeneo ya kijiji watu ambao walikuwa wanalima wakikanyaga hayo maeneo wanakamatwa na kuachiwa wanatozwa faini ya shilingi 500,000 hadi shilingi 1,000,000.

Mheshimiwa Spika, nilikuja kwa Waziri, Waziri akafanya mawasiliano watu wa Selous wakamthibitishia hilo eneo sio la Selous na wakasema pia, sio eneo la kijiji. Waziri akawauliza mamlaka ya kuwakamata watu na kuwatesa mnayatoa wapi? Wakashindwa kumjibu na Waziri ameniahidi ataenda, ili kutatua mgogoro huu kuangalia nini kilichopo, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, upande mwingine tumepakana na Bonde la Mto Kilombero ambayo ni Kata ya Ilagua, Lupilo, Minepa pamoja na Milola. Mwaka 2012 Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Halmashauri waliweka mipaka, lakini leo hii Wizara wamekuja wanaondoa watu katika yale maeneo ya ile mipaka ambayo iliwekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali leo tunafanya hivi kwesho tunaamka na hili, hii mpaka lini? Kwa hiyo, naomba Waziri Kigwangalla, najua wewe ni mahiri sana, naomba ulifuatilie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni operation ya tokomeza. Operation ya tokomeza iliumiza watu wengi sana katika Jimbo langu la Ulanga, lakini mpaka leo hii kuna watu ambao walihakikiwa kwa ajili ya kulipwa hawakulipwa, hasa katika Kata ya Iputi nina wananchi wangu sita ambao mpaka leo hii hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jimbo langu la Ulanga kama nilivyosema limebarikiwa kuwa na hifadhi nyingi. Kuna vijiji ambavyo vimefuata taratibu zote kwa ajili ya uvunaji wa mbao, lakini tatizo kubwa Wizara mpaka leo hii hawataki kutupa nyundo. Mkurugenzi wangu leo hii yuko hapa na anasema ikifika Jumatatu kama hamjatupa nyundo nitaita Madiwani wote pamoja na wananchi wangu wa Ulanga tutakaa tutaweka kambi katika Wizara mpaka mtupe hiyo nyundo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la mkaa, nchi yetu, kama tunavyojua maisha yetu ya vijijini sio watu wote wenye uwezo wa kutumia gesi, lakini Wizara wakimkamata mtu ana debe moja la mkaa wanamtoza faini shilingi 500,000. Sasa kama mnaona hawa wauza mikaa wanafaidi si Wizara ya Maliasili nawashauri mchome ninyi mikaa muweke ma-agent watu wawe wanaenda kununua huko kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la utalii, ulitutuma China, tulienda tukaangalia pamoja na fursa za utalii, China wana mnyama mmoja tu anaitwa panda, lakini wanapata mamilioni ya pesa kwa ajili ya huyo mnyama.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tuna wanyama wa kila aina, lakini hatutangazi na nikabaini hata sisi wenyewe ni fursa kwa utalii, tulienda na Mheshimiwa Kanyasu, Mbunge wa Geita, kwa urefu wake Wachina walikuwa wanamshangaa na mimi nikapiga chapuo hapo hapo nikawaambia kuwa huyu ni mfupi Tanzania wako warefu kuliko huyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba ni-declare interest kuwa na mimi ni mchimbaji ambaye mpaka leo bado sijafanikiwa. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Rais kwa mpango wake wa kuzuia makinikia kupekwa nje ya nchi. Kwa nini nasema hivyo? Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa dhahabu nyingi katika Bara la Afrika na nchi ya 16 duniani tukitanguliwa na China, Australia na Russia. Katika orodha ya nchi matajiri wa uzalishaji wa mali tupo lakini mafanikio ya Serikali na wananchi yako chini. Kwa hiyo, hapa nimeona dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kujenga ukuta katika mgodi wa Mererani kwa sababu haya ni madini adimu katika dunia hii yanatoka Tanzania tu. Licha ya hivyo, Tanzania pia ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa gesi katika Bara la Afrika na ni ya 22 katika dunia katika uzalishaji wa gesi. Hapo ndipo unapoona dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kulinda rasilimali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Spika naye kwa kuona kuwa suala la gesi ni muhimu kwa sababu nchi matajiri duniani ndiyo zinaongoza katika utoaji wa gesi na madini ya aina mbalimbali. Katika orodha za nchi maskini duniani Tanzania ni ya 25 toka mwisho tukitanguliwa na Central Africa, Congo na Malawi. Kwa suala la madini nchi yetu ipo juu, vinara katika kutoa madini lakini katika nchi maskini na kwenyewe tuko juu, ndiyo tunaona kuwa Mheshimiwa Rais ana dhamira nzuri na nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri pia Mheshimiwa Rais afanye pia reshuffle katika Wizara ya Madini kwa sababu watendaji wa Wizara ndiyo waliopelekea nchi hii kufika hapa leo hii. Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri tunajua mnafanya kazi vizuri lakini nawapa angalizo watendaji wa Wizara zenu ni wapigaji, nimeshaongea hapa tangu mwanzo kuweni nao makini hasa wanasheria. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili naomba nije kwenye Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro na Wilaya zake za Ulanga, Malinyi, Kilosa, Mvomero, Morogoro Vijijini, Matombo ni wilaya tajiri, tunatoa dhahabu tena dhahabu zake siyo kama za Wasukuma kule, dhahabu zetu sisi ni asilimia 98. Tunatoa rubi, graphite, copper, uranium kwa hiyo mkoa wetu ni tajiri kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatoa angalizo kwa Serikali hasa Wizara, kuna watumishi wa Wizara ya Madini wamehodhi maeneo makubwa kwa kutumia majina mengine. Anapotokea mtu anapotaka kuchimba unasikia eneo hili lina mtu, kumbe mtu mwenyewe ni mfanyakazi wa Wizara ya Madini. Kwa hiyo, tunaomba leseni zote ambazo ziko Mkoa wa Morogoro zifuatiliwe kwa undani zinachimbwa au lah, wamiliki halisi ni watu gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa Ulanga. Jimbo langu la Ulanga miaka ya 90 kuna kijiji kimoja kinaitwa Lukande kilikuwa kinajulikana Thailand. Thailand walikuwa wanaijua Lukande kuliko Dar es Salaam, lakini kijiji hicho mpaka leo hii kimechimbwa madini yameachwa mashimo tu hawajanufaika lolote. Sasa hivi chini ya uongozi wa Mbunge wao kijana machachari nahakikisha hamna wizi wowote wa madini utakaofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu lina makampuni makubwa mawili ya uchimbaji wa graphite ambayo ni TanzGraphite na Mahenge Resource. Mahenge Resource ndiyo tumeitambulisha juzi, inaanza mchakato wa kutaka kuongea na wananchi ili kuwaahamisha na kufanya malipo, TanzGraphite ina miaka sita lakini bado ina ubabaishaji, wamefanya uthamini wa mali za wananchi mwaka mmoja na mwezi mmoja, leo hii wanataka kuja kuanza kulipa. Sheria inamtaka ukishafanya uthamini miezi sita ina-expire lakini wao imepita mwaka mmoja na mwezi mmoja wanataka kulipa, wanataka kulipa kwa mkataba upi wakati tayari ile tathmini imesha-expire.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu, nimewaambia wao wenyewe kuwa uthamini unatakiwa ufanywe upya, maana tukiongea sisi Wabunge wanasema wameongea wanasiasa, tafadhali naomba tusidharauliane kwenye kazi, wafanyekazi yao na mimi kama Mbunge niwatetee wananchi wangu. Nahikikisha hakuna mwekezaji atakayewekeza kwa kukiuka sheria. Nawahakikishia wananchi wangu wa Ulanga na wananchi wa Ipanko walale usingizi mzuri, hakuna uwezekazaji mpaka wananchi wote wamelipwa haki yao inayostahili kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine kwa wananchi wa Ulanga, tunaomba ofisi ya Madini ifunguliwe katika Wilaya ya Ulanga. Ulanga tuna madini mengi, lakini hakuna Afisa Madini ambaye anayeishi huko huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee pia kuhusu wachimbaji wadogowadogo, Mheshimiwa Waziri tumeshaongea sana kuhusu wachimbaji wadogowadogo, hasa wa gemstone nikiwemo na mimi ambaye mpaka leo hii sijanufaika. Uchimbaji wa madini ni kama kamari lakini Serikali unapochimba haiangalii umewekeza shilingi ngapi na umepata kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nimechimba miaka miwili, nimetumia shilingi milioni mia moja, siku napata jiwe la shilingi milioni ishirini, Serikali inataka kodi hapo hapo, haijui mimi nimewekezaje. Ndiyo maana tunawaambia, mtoe semina na muwekeze kwa wachimbaji wadogowadogo, muwe nao karibu mtajua matatizo gani wanayapata. Sasa wewe hujui mtu amewekeza kiasi gani, haujui amepata kiasi gani, unaenda kumdai kodi, kwa mfumo huo hamtopata kodi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana leo hii Mererani mmjenga ukuta sawa, lakini wale wachimbaji wadogo wadogo wanawapiga chenga. Cha msingi ni kuwafanya wawe marafiki inakuwa rahisi hata wao kujitolea kutoa kodi kwenu, kwa sababu inakuwa tayari mmeshawajengea mazingira ya ukaribu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuliongelea ni kuhusu kujenga ule mtambo wa kuchenjua dhahabu. Serikali ituambie sasa ni lini mtambo huo utakuwa tayari, kwa sababu tunajua dhahabu bado kabisa haijachimbwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kidogo mpaka Waziri aje na majibu ya hoja zangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nataka nimpe taarifa kaka yangu Mheshimiwa Silinde amesema kwamba Serikali inatumia kichaka cha uhakiki kama kujificha. Kwa faida ya Bunge, mimi professional yangu ni Mtawala. Elimu ya juu nilisoma Utawala na ya juu zaidi nikasoma Sheria za Upatanishi na Usuluhishi. Kwa hiyo, migogoro hapa ni kaburi lake.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia uhakiki wa Watumishi Serikalini, hata wale wanaoenda kuhakikiwa wanajiandaa jinsi ya kukwepa ule uhakiki. Kwa hiyo, mnaweza ukazungumza uhakiki kwamba Serikali haimalizi uhakiki, mkumbuke hata wale wanaoenda kuhakikiwa na wale waliowaingiza wale watumishi hewa, kwa sababu wanajua wakigundulika na wenyewe watakuwa matatani, kwa hiyo wanajiandaa jinsi gani ya kukwepa huo uhakiki. Kwa hiyo, wasiituhukumu Serikali tu wakasema uhakiki hauishi. Sisi watawala tunaelewa uhakiki maana yake ni nini na changamoto zake ni zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili ambalo nilikuwa natamani sana kulizungumza leo kwa kupata nafasi hii, nchi yetu mwanzo ilikuwa nchi ya wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara. Kuna kundi lingine limeongezeka kubwa sana. Sasa hivi nchi yetu ni ya wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na wacheza kamari. Bahati nzuri imezungumzwa, sasa hivi wanafunzi wote wa Vyuo Vikuu wakipata mikopo wanajazana kwenye vituo vya kucheza kamari.

Mheshimiwa Spika, pia wazee wetu wakipata pension wanaenda kucheza kamari; wake zetu, zamani sisi enzi zetu wakati tunaoa, unaambiwa ili uwe na maisha mazuri, ukipata kahela kako mpelekee mkeo akatunze. Ukimpelekea mke, ukija kuchunguza simu zake, unakuta meseji za Biko na Tatu Mzuka. Madereva wa Bodaboda wote, yaani vijana wote tunavyozungumza sasa hivi, wote wanacheza kamari. Hili ni janga la Taifa. Gaming Board watafute namna gani ya kuliratibu.

Mheshimiwa Spika, madhara ya kamari ni makubwa kuliko biashara nyingine. Rafiki yangu Mheshimwia Musukuma hapa alikuja na zao lake mbadala kwa ajili ya kutuletea uchumi tukalikataa, tukasema lina madhara, lakini ninavyokwambia kamari madhara yake ni makubwa kuliko bangi au kuliko hata viroba. Kwa hiyo, tutafute utaratibu wa kuendesha kamari, lakini siyo kama sasa hivi inavyoenda.

Mheshimiwa Spika, labda tu kwa watu ambao hawajui madhara ya kamari; kwanza, imevunja nguvu kazi za nchi yetu. Zamani ilikuwa ukienda vijijini unawakuta vijana wanacheza pool table. Sasa hivi pool table haipo, vijana wote kwenye betting maana kamari zenyewe ziko nyingi, zimeongezeka, mara kuna Tatu Mzuka, Biko, sijui Mkeka Bet, sijui nini bet, yaani ziko nyingi kweli kweli na zinaongezeka kwa kasi, umeona.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nguvu kazi ya vijana imepotea. Vijana wote wanaamini watakuwa matajiri, kwa sababu matangazo yale ambayo tumeyaruhusu kiholela sasa hivi inawafanya vijana wengi wawe na tama. Mtu anasema nitapata kesho, nitapata kesho. Kwa hiyo, akipata kihela kidogo, kwenye kamari.

Mheshimiwa Spika, madhara mengine ni addictive. Mtu yeyote anayecheza kamari hawezi kuacha. Nao walivyokuwa wataalam, anakupa Sh.5,000/= leo umeshinda. Ukishinda Sh.5,000/= hiyo huwezi kuacha, hata ucheze shilingi milioni 20 hutaacha. Kwa hiyo, inasababisha hiyo addictive, wenyewe wanaita uteja.

Mheshimiwa Spika, lingine madeni. Watu sasa hivi wanaenda kukopa kwenye Vicoba ili wacheze kamari. Kwa hiyo, inasababisha Taifa la watu kuwa na madeni. Ndiyo maana hata ukienda kwenye Vicoba mikopo hailipiki, watu wanakopa kwa ajili ya kwenda kuchezea kamari. Hivyo, malengo ya Taifa letu yanapotea kwa sababu wengi wanaweka malengo kwa kutegemea kamari.

Kwa hiyo, ndiyo hivyo. Ninachoomba Gaming Board watafute utaratibu wa kuendesha haya mazoezi ya kamari, lakini siyo kwa mfumo huu. Watafute mfumo mwingine. Wametoa matangazo; kuna tangazo wamelitoa zuri, lakini hilo tangazo linapita kwa watu kiasi gani? Maana yake wanasema, usitumie fedha yenye malengo mengine kuchezea kamari. Hebu niwaulize, leo hii Tanzania nani ambaye ana pesa ambayo haina malengo imekaa tu? Kila pesa tunayoipata ina shughuli , ada za shule, nini na vitu vingine, lakini watu wanaishia kwenye kamari.

Mheshimiwa Spika, kuna mwanafunzi mmoja alijinyonga juzi juzi hapa kwa sababu alitumia pesa ya ada kwenye kamari na akaliwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wakati ana wind-up atuambie ni namna gani Gaming Board watatafuta utaratibu wa kuendesha kamari bila kusababisha matatizo ambayo yanatokea sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, wakati Serikali yetu ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, tulikubaliana Serikali nzima tubane matumizi yasiyo na tija ili hiyo pesa tuipeleke sehemu nyingine ya maendeleo. Kweli tulifuta safari za nje kama Bunge, sasa hivi hatuendi nje. Taasisi za Serikali zilitoa fedha zao kutoka kwenye mabenki ya biashara wakapeleka Benki Kuu. Pia pakatolewa maelekezo kuwa tutumie huduma zinazozalishwa na taasisi za Serikali. Hata matibabu ya nje yalizuiliwa. Mpaka mtu aende kutibiwa nje inatakiwa utaratibu mrefu na ionekane kuna haja ya muhimu kabisa huyu mtu kwenda kutibiwa nje.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea, Benki Kuu ya Tanzania ndiyo taasisi inayotumia fedha nyingi katika matibabu bila msingi wowote. BoT Mfanyakazi akiwa na mafua anaenda kutibiwa Uingereza au India. Wanatumia fedha nyingi na wamesahau kuwa hizi fedha ni za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, Taasisi zetu za Serikali zimewekewa utaratibu maalum kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Tunaitumia NHIF, hata Bunge tulikuwa tunatumia Private Company sasa hivi tumeingia NHIF, BoT wanatumia Private Insurance gharama ya matibabu ambayo wangeitumia NHIF shilingi bilioni moja wanatumia shilingi bilioni 12 kwa mwaka. Angalia ufisadi wa hali ya juu uliopo. Shilingi bilioni moja kwa shilingi bilioni 12 kwa sababu watu wana maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, wanasema wao hawawezi kwenda NHIF kwa sababu haina matibabu nje ya nchi. Sasa naomba niulize, wao wanasema taasisi yao ni nyeti, Usalama wa Taifa wako NHIF, Bunge tuko NHIF, PCCB wako NHIF. Mke wa Rais aliugua, alilazwa Muhimbili, lakini BoT hawakubali. Wanasema wao taasisi yao ni nyeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge tulikubali hadi matezi dume tulipimwa kwenye Dispensary ya Bunge hapa hatukuona tatizo, lakini wao mtu akiugua kidogo wanataka kwenda nje.

Mheshimiwa Spika, naomba ulisimamie hili. Kuna ufisadi mkubwa katika mchakato huu wa BoT kwenda kupata matibabu kwa kutumia Private Insurance.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, siungi mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri mpaka atakapokuja na majibu ya haya niliyoyatoa. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi kidogo nataka nianze kwa historia. Katika ukuaji wa lugha matendo huzaa nomino. Enzi hizo wakati mimi niko mdogo kulikuwa kuna Mwanamuziki mmoja anaitwa Mbaraka Mwishehe na mwingine alikuwa anaitwa Juma Kilaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Juma Kilaza alikuwa ni mtu mwenye majigambo sana, yaani yeye kila kitu anajua, anajifanya anajua kuimba muziki. Sasa wakasema tukate mzizi wa fitna, wakaweka pambano. Baada ya kuweka pambano la muziki, Mbaraka Mwishehe akaonesha shamra shamra zake, Juma Kilaza akaonyesha udhaifu wake. Kuanzia siku hiyo, mtu yeyote ambaye alikuwa hajui akawa anaitwa Kilaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo miaka ya nyuma wakati niko mdogo Ubunge Jimbo la Temeke kuna mtu mmoja Lamwai na mwingine alikuwa anaitwa Kihiyo. Wakagombea, baada ya kugombea Mheshimiwa Kihiyo aliweka vyeti feki, Lamwai akaenda Mahakamani kuweka pingamizi. Baada ya kuthibitisha yule mtu kuwa vile vyeti alifoji akang’olewa Ubunge, kwa hiyo tangu siku hiyo mtu ambaye hajasoma alikuwa anaitwa Kihiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudi sasa hivi. Rais wa TFF juzi alisema kwa sababu katika nchi ameshaonekana mtu mbishi sana ambaye anajifanya anajua sana lakini hajui, hakubali chochote, akatoa mfano wa Mheshimiwa Tundu Lissu akasema kuwa msilete Utundulisu kwa sababu ya matendo yake huo ndio ukuaji wa lugha haizuiliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa, jana ilizuka mijadala miwili humu ndani, mwisho alimalizia Mheshimiwa Joseph Selasini kwa kuomba Mheshimiwa Rais aingilie kati suala la Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Ester Matiko. Nataka nimwambie Rais wangu mimi bado kijana mdogo sana, asije akaingia kwenye huu mtego hata wakimfuata kwa kuburuza magoti. CHADEMA ndio wamekuwa wakizunguka dunia nzima kusema Rais hafuati Katiba..

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Hansard yako ya jana isomwe, nataka nimpe taarifa sijawahi mimi kusimama katika Bunge hili kumwomba Mheshimiwa Rais aingilie kati suala la Mheshimiwa Mbowe na Matiko. Kwa hiyo, naomba mzungumzaji aweke kumbukumbu zake sahihi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga futa jina la Selasini, endelea.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka kujua kama wanawajali au hawawajali. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitamkwa humu Bungeni, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Rais hawa ndio wanaozunguka dunia nzima…(Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga wewe sema tu nafuta jina la Mheshimiwa Selasini ili tuendelee.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Basi ili aridhike nalifuta hilo jina la Mheshimiwa Selasini, lakini message imefika. Kwa hiyo namuomba Mheshimiwa Rais aje akaingia kwenye huo mtego, kwa sababu hawa ndio wanazunguka dunia nzima kusema Rais wetu hafuati Katiba, hafuati sheria, hafuati kanuni za nchi hii, hafuati taratibu, yeye ni dikteta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nataka nizungumze kuna kitu sasa hivi watu wanazunguka duniani wanasema Tanzania hakuna freedom of expression. Wote ni shahidi, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vyombo vingi vya habari katika Bara la Afrika. Tanzania ina magazeti 216 yakiwemo ya CHADEMA. Nchi yetu ina Redio 158, nchi yetu ina TV 34 na hazijawekewa mazuio ya kuandika. Tuna Online TV 224, tuna blogs zaidi ya 60. Hivi vyote vinafanya kazi bila ya kufuatiliwa. Kwa kuthibitisha hilo tuambiwe ni Mwandishi wa Habari gani sasa hivi yuko jela, kama hakuna freedom of expression.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchora katuni mmoja anaitwa Masoud, kwa katuni anazomchora Mheshimwa Rais, ningekuwa mimi nisingemwacha, lakini yote haya yameruhusiwa watu wanafanya lakini watu wengine wanazunguka dunia nzima wanasema Tanzania hakuna freedom expression.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi anayoitolea mfano, kwa mfano mwenzetu mmoja yuko Marekani, hiyo nchi ya Marekani kuna uhuru lakini wanaweka mipaka, hata hiyo freedom of expression. Marekani freedom of expression ipo lakini usije ukaongopa, usije ukadhalilisha mtu, usije ukamsingizia mtu kitu, usije ukavuruga usalama wa nchi na kwa kuthibisha hilo kuna mtu mmoja anaitwa Edward Snowden, waulize kwa nini Marekani wanamtafuta yule pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa upande wa Mahakama. Najiuliza Mahakimu wanafanya kazi kubwa kwelikweli, wanafanya maamuzi magumu, hivi kwa nini Hakimu hapewi ulinzi, OCD anapewa ulinzi. OCD ambaye kazi yake kukamata tu mtu, lakini Hakimu kazi yake kumuhumu mtu aozee jela au anyongwe, kwa nini hapewi ulinzi. Naomba Mahakimuwapewe ulinzi kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, leo kumezuka mjadala wa mwisho humu. Watu wanataka wafungwa waruhusiwe kufanya matendo ya ndoa na wake zao. Wafungwa wana haki nyingi sana na ndio maana wameitwa wafungwa. Lakini sasa tukianza kuwawekea huru, maana yake tendo la ndoa ndio tendo zito kuliko yote duniani.

Mheshimwa Mwenyekiti, wanaume sisi tunakuwa majambazi, tunaenda kuiba hela tunapokea rushwa ili tufanikiwe kupata hilo tendo kirahisi. Leo hii mfungwa ambaye amefungiwa gerezani anaambiwa aruhusiwe kufanya tendo la ndoa na mke wake au na mume wake. Hilo suala halikubaliki sisi ndio tutakuwa wa kwanza katika nchi zenye demokrasia duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami naomba niweke maneno yangu machache. Katika Bunge hili baada ya kuapishwa huwa tunapewa vitabu vya kanuni, sasa kwa bahati mbaya Wabunge wengi huwa hawavisomi hivi vitabu vya kanuni, wanasoma mistari michache ambayo wao wanaona wameilewa, lakini hawafanyi jitihada za kuelewa kanuni zote zilizoandikwa katika kitabu hiki cha kanuni.

Mheshimiwa Spika, naomba nisome kanuni ya 72, Sehemu ya Sita inasema hivi:

“Spika atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa, utaratibu bora unafuatwa Bungeni, na uamuzi wa Spika kuhusu jambo lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho.”

Mheshimiwa Spika, hili Bunge ni la kwako, hizi kanuni ndio zinazokulinda tafadhali asikuchezee mtu yeyote kazi unayoifanya ni nzuri sana na Wabunge tunailewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeomba kuchangia kwa kuwa juzi nilichangia kuhusu Kamati hii ya Madili lakini jana wakati naingia katika viwanja vya Bunge katika lile geti la usalama kwenye kamera pale kwenye sehemu ambayo tunapekuliwa nilikutana na Wabunge wawili Mbunge mmoja anaitwa Haonga na mwingine wa Mbeya simkumbiki jina lake, nitalikumbuka baadaye, walinizodoa sana, walinitukana sana.

Mheshimiwa Spika, nakupa tu taarifa hii, kwa kuwa mimi kijana nikawaambia kuwa wafanye haya mambo wakiwa katika viwanya Bunge, wakithubutu kufanya nje ya viwanja vya Bunge watakuja kuwasimulia ndani nitakachowafanya. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, juzi nilisema kuwa katika hili Bunge tuna viongozi wetu. Sisi wa Chama cha Mapinduzi tuna viongozi wetu usipohudhuria vikao vitatu unaandikiwa barua, uki-misbehave unaitwa kwenye Kamati za Chama, hawa wenzetu viongozi wao wanapokutana, wakimaliza suala la kuchangishana hamna jambo lingine, kuwa mbunge ahudhurie kwenye vikao asihudhurie lwake, inafika kipindi mpaka Mbunge anafukuzwa Ubunge, kiongozi wao hajui. Kiongozi wao mwenyewe ukihesabu katika vikao vinavyozidi 150 kwa mwaka anavyohudhuria hata vikao hata 20 havifiki. Kwa hiyo hawa wenzetu hawana viongozi. Kwa hiyo ifike mahali tubadilishe hizi kanuni Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni asipohudhuria vikao kadhaa na yeye mwenyewe aenguliwe, wapewe hata CUF. Leo hii tujiulize CUF kwa nini hawasimamishwi, CUF kwa nini hawa-misbehave Bunge? CUF kwa nini hawatoi kauli chafu? Kwa nini ni wao tu? Kuna chama cha ACT humu kwa nini hayawakuti, ni wao tu CHADEMA?

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mfano Mheshimiwa Lema wakati anafanya utumbo wake juzi na kiongozi wake wa Kambi ya Upinzani yupo, hafanyi kitu ananyamaza tu na mimi nilisema, kwa hiyo tubadilishe hizi kanuni hawa viongozi wao wawajibike kwa mambo wanayowafanya Wabunge wao. Tabia mbaya za viongozi wa upinzani, kwanza la utoro, hata ukifanya tathmini ya mahudhurio ya Wabunge wa Upinzani ni nusu ya vikao na ni nusu ya Wabunge, Wabunge wengi. Mheshimiwa Lema siku ambayo unamsikia anazungumza ndio kaingia Bungeni, lakini siku zote hayupo. Anakuja humu kwa ajili ya interest zake na ukiona kaingia ujue ana jambo lake binafsi, sio jambo la watu wa Arusha.

Mheshimiwa Spika, ndio maana ulisema kuwa ukiweka masuala yako binafsi katika Bunge hili, lazima utaharibikiwa, sehemu, acha ya huyo, kuna Mbunge mwingine wa ACT anazunguka huko mitandaoni, anasema anawasainisha wananchi ili wakatae maazimio ya Bunge. Siku moja nitakuja kuwaambia, anayofanya ana interest yake binafsi, sio kama ya jamii kama wanavyojua. Siku moja nitawaambia wananchi na wataelewa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tunasema, Bunge letu linaenda vizuri na ndio maana maendeleo yanapatikana, barabara zinajengwa na miradi mikubwa inafanyika na wageni wanakuja.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja ya Kamati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa namna ya pekee naomba nipongeze mhimili wa Mahakama kwa kufanya kazi vizuri. Hata huo mrundikano wa kesi tunaouona ni kwa sababu watu wana imani kubwa na mahakama na ndiyo maana wanakwenda kupeleka mashauri yao. Hapa nimeona complain kubwa katika Kitabu cha Hotuba ya Kambi ya Upinzani wanasema mahakama haina uhuru, yaani kama mahakama inaingiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru wa mahakama umeanzia kwenye Katiba ibara ya 107B, ambayo inasema: “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji wa haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria ya nchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuipa mahakama uhuru wake umeanzia kwenye Katiba, lakini wenzetu wanashindwa kutofautisha kati ya Mahakama za Hakimu Mkazi, wanawapongeza Majaji kama sio sehemu ya mahakama. Utaratibu wa maamuzi ya mahakama ya chini kupelekwa katika Mahakama ya Rufaa ni utaratibu wa kimahakama; uwe umeshinda au umeshindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wao hawaziamini mahakama za chini lakini wanawapongeza Majaji, hawajui Majaji na wenyewe ni sehemu ya mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala la Katiba. Kupanga ni kuchagua. Hata baba anapopata hela nyumbani matatizo yapo mengi anaamua na ndiyo maana hata wao hela ya ruzuku inapopatikana wanaamua kukopeshana Wabunge kununua magari; japokuwa hawana ofisi wanashindwa kujenga ofisi, wanakopeshana Wabunge kununua magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuendelea kudumisha utawala wa sheria na Katiba pamoja na kuboresha sheria mbalimbali. Tumeshuhudia Sheria ya Madini imefanyiwa marekebisho, sheria ambayo ilikuwa kandamizi. Pia Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo ilikuwa kandamizi ambapo ilikuwa inatoa mianya ya baadhi ya Wenyeviti ruzuku inapopatikana wanaolea mke wa pili na watatu badala ya kufanyia vitu vingine vya vyama. Sheria za Mitandao, sisi viongozi ni waathirika wakubwa sana wa sheria mbovu za mitandao ya kijami. Tulikuwa tunashuhudia Wabunge, wanamziki na watu maarufu wanazalilishwa. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kuweka sheria kali za mitando ili kukomesha tabia hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Statistics, jana hapa tulishuhudia Mheshimiwa Mbunge akisema Mkoa wa Tabora peke yake wanafunzi waliopewa mimba kwa mwaka mmoja ni 70,000. Takwimu hizi zinaenda kwa watu huko, watu wengi hawasomi wengi wanapata data kutokana na kusikiliza. Sasa sheria zikiwa mbovu watu watakuwa wanapata taarifa ambazo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Vyombo vya Habari, vyombo vya habari zimekuwa nguzo kubwa ya kuzalilisha watu na kutoa taarifa za uongo. Kwa hiyo, hata sheria kali zilizowekwa sitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa upotoshaji mkubwa ambao unafanywa na vyombo vya habari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Mbunge mmoja ameomba uwekwe utaratibu katika Katiba Maalum juu ya upatikanaji wa Viti Maalumu vya Wanawake. Navyofahamu mimi kila chama kimepewa mamlaka ya kuteua Wabunge wa Viti Maalum. Kwa mfano, CCM kuna makundi ya wanawake mikoani wanachaguana wenyewe mikoani, vyuo vikuu, vijana na walemavu. Kwa hiyo, kila kundi limeweka utaratibu wake wa kuwapata kwa kupigiwa kura. Sasa wenzetu wana utaratibu wao ambapo wameachia watu wachache wanafanya huo uchaguzi na ndiyo maana umeona analalamika kuwa Mheshimiwa Polepole amewasema vibaya lakini hao hao wanalalamika kwa Katiba haijasema wanapatikanaje.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa namna ya pekee, naomba nipongeze uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga ukiongozwa na DC mahiri, mchapakazi, Ngolo Malenya kwa utaratibu wake wa kuweka mikakati na kutekeleza kwa ajili ya kuinua elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kule vyombo vya habari hakuna Lakini vyombo vya habari vingekuwepo tungeenda sambamba na watu wengine, lakini mimi nitazifikisha habari za Ulanga katika Bunge hili ili mjifunze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Ulanga tumeweka lunch program kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari. Wanafunzi wanaenda wanakula chakula huko huko wanapata muda wa kutosha wa kujisomea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna kambi kwa ajili ya wanafunzi wale wanaojiandaa kufanya mtihani. Sasa hivi tuna kusanya vyakula kwa ajili ya kupeleka katika shule ambazo watafanya mtihani kidato cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumebuni miradi kwa ajili ya kuinua vipato vya walimu. Tumewapa mashamba, yaani mwalimu akienda kule inaitwa “gusa unite.” Akikaa huko, hawezi kuondoka tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeunganisha wadau wa elimu, tumepata zaidi ya shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Tumebuni utaratibu wa kufanya mabonanza kwa ajili ya kuwapa motisha wale walimu ambao wanafundisha katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Ulanga kuna maeneo hayafikiki kwa baiskeli, hakuna mawasiliano wala umeme. Kwa hiyo, tumeweka motisha kwa ajili ya kuwasaidia walimu kama hao wapate moyo kwa ajili ya kufundisha. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri katika maombi yetu tumeomba tuwekewe VETA ili kuwaunga mkono Ulanga kwa jitihada zote za kuinua elimu hizi wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako. Unajua Profesa Ndalichako yuko tofauti na Maprofesa wengine, Profesa wa CCM, Profesa ambaye yuko updated kama iPhone. Naomba nimpongeze yeye pamoja na Naibu Waziri, pamoja na Katibu Mkuu wake Akwilapa pamoja na AveMaria. Wamekuwa wasikivu, wamekuwa wakiweka mikakati mizuri na kuitekeleza kwa ajili ya kuboresha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukilalam ika mwanzo lakini amekuwa akitusikiliza na kuyafanyia kazi. Ila kuna kazi kidogo naomba akae vizuri na watu wa private schools ili aweze kwenda sawa kwa sababu TAMISEMI wamekuwa kama kivuruge; wanataka kusimamia shule za private na hao hao wamekuwa wanamiliki shule za Serikali. Sasa huyu referee mchezaji amekuwa anaharibu mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko kodi nyingi sana na ziko ambazo zimetolewa lakini bado wanachokonoa private kwa chini kwa ajili ya kuwadai hizo kodi. Kwa mfano, kila mwanafunzi mmoja anatakiwa alipe fire shilingi 20,000/=. Huu ni wizi mkubwa ambao Serikali inafanya kwa shule za private. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa elimu bure. Walioongea hapa wanasema elimu bure imefanywa kwa mustakabali wa siasa. Ndiyo nakubali, si iko kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Sasa nataka wakawaambie waliowaambia elimu bure imefanywa kwa ajili ya siasa. Ulanga kwa mwaka huu wa fedha ambao unaisha, tumepata gari moja kwa ajili ya ukaguzi wa elimu. Ulanga tumepata pikipiki 19, wale waratibu wa elimu zamani walikuwa wanatembea kwa mguu, sasa hivi kila mratibu wa elimu ana pikipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata shilingi milioni 214 kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo wananchi walianza kujenga. Tumepata zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na madarasa katika shule mbalimbali. Naipongeza Serikali kwa kutoa ajira kwa walimu 4,000 Ulanga; na yenyewe tumepata japokuwa kidogo. Naiomba Serikali iongeze jitihada ya kuajiri walimu kwa sababu mtaani wako wengi, kuna walimu zaidi ya 100,000. Kwa hiyo, Serikali iongeze ajira kwa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ulanga tunazalisha wanafunzi wa form four 1,000 - 1,200 kwa mwaka. Wanaokwenda kidato cha tano na cha sita hawazidi 200. Wanabaki 1,000; hao 1,000 tunawapeleka wapi? Ndiyo maana nimekuomba Mheshimiwa Waziri, tusogezee VETA, eneo tayari tunalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kukarabati shule kongwe lakini kwangu mmeisahau shule moja inaitwa Kwiro. Kwiro ni shule ya zamani wamesoma vigogo wakubwa, nikiwemo mimi. Kwa hiyo, naomba muikarabati hiyo shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuongeza fungu la Bodi ya Mikopo kufika shilingi bilioni 423, lakini changamoto imekuwa kubwa kwa sababu wanafunzi ni wengi. Serikali imeshindwa kuchanganua kupata wanafunzi masikini halisi na wanafunzi wenye kipato cha juu. Kwa hiyo, tatizo limekuwa kubwa. Pia makato ya Bodi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nianze na barabara ya Kidatu – Ifakara; barabara hii ilizinduliwa tarehe 5/5/2018, tulizindua nikiwemo na mimi na Mheshimiwa Waziri na Wabunge wote wa Morogoro. Rais alizindua ujenzi na barabara ikaanza kujengwa, lakini baada ya muda mfupi mkandarasi akaondoa vitu site; mpaka sasa hivi ninavyoongea ni mwaka mmoja sasa barabara hii haijawekwa hata kilometa moja ya lami.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa mwongozo kwa Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi watatue tatizo la mgogoro wa kikodi wa VAT lakini mpaka leo hii Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Ujenzi wanaogopana kama mtu na baba mkwe wake. Mheshimiwa Rais ameshawaambia wakae watatue huu mgogoro lakini wanaogopana; kama wameoleana si wamwambie Mheshimiwa Rais awahamishe Wizara waje Mawaziri wengine watatue huo mgogoro kama wao wanashindwa? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni barabara ya Ifakara – Mahenge. Barabara hii ina urefu wa kilometa 74. Sasa hivi Ulanga tuna deposit kubwa ya graphite na kuna kampuni kubwa tatu tayari zimeshaanza uwekezaji na kwa mwaka tutatoa tani zaidi ya laki tano.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya barabara ile hii biashara haiwezi ikafanyika. Endapo barabara hii itakuwa tayari Serikali ina uwezo wa kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa mwaka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati ana- wind up atuambie mkakati uliofikiwa kwa ajili ya barabara hii.

Mheshimiwa Spika, barabara nyingine ni ya Liwale – Ulanga. Ukiacha ahadi ya Mheshimiwa Rais, ni mkakati wa Serikali kuunganisha barabara za mikoa na ni muhimu sana katika uchumi wa Wanaulanga. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atuambie amefikia wapi kuhusiana na ujenzi wa barabara hii umefikia.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la viwanja vya ndege. Naipongeza Serikali kwa umaliziaji wa Terminal III lakini wasisahau na viwanja vingine kwa vifaa, maana tumeshuhudia ndege zikisukumwa na watu. Bahati mbaya ikatokea wafanyakazi wa airport wakawa na miili kama mimi watasukumaje hizo ndege? (Kicheko)

Suala lingine ni uhalifu wa mitandaoni, hii naongelea kuhusu TCRA. Uhalifu wa mitandaoni umegawanyika katika sehemu tatu: Udhalilishaji, wizi na upotoshaji.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia udhalilishaji mkubwa na TCRA wamekuwa wakikaa kimya. Wameanzia kwa viongozi wa siasa sasa hivi wamekuwa wakitengeneza picha za ngoni za viongozi wa dini. Hali imekuwa mbaya na TCRA wamekaa kimya.

Mheshimiwa Sika, suala lingine ni la wizi wa mitandao. Wizi huu makampuni ya simu yanahusika. Tumeona meseji za tafadhali tuma pesa kwenye namba hii, waganga feki, unaweza ukatumiwa meseji ukaambiwa mtoto wako ameanguka shuleni, hizo meseji ni za uongo. Meseji nyingi zinatoka Kampuni ya Vodacom na baada ya uchunguzi wangu nikakuta wafanyakazi wanahusika. Kwa hiyo, makampuni ya simu walipeni vizuri wafanyakazi wenu na wekeni mfumo ambao mtaangalia hawa wafanyakazi wasiwe wanashiriki katika wizi wa mitandaoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na taarifa nyingi za upotoshaji. Taarifa hizi nyingine zinatolewa na Wabunge wakiwa wanapotosha taarifa za Serikali katika mitandao na wanafahamika lakini TCRA wanashindwa kuwachukulia hatua. Naomba suala hili lishughulikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la ATCL na nitaongelea kwenye nauli. Nauli za ATCL zimekuwa kubwa tofauti na matarajio ya Watanzania. Kwa mfano, kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam nauli hadi Sh.600,000. Sasa mimi nakuwa nimepanda nalipa nauli au nimekodisha ndege? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, napenda kuongelea usafiri wa Noah. Enzi zenu kipindi hicho kulikuwa na mabasi tu, sasa hivi kuna usafiri wa Noah ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi kuna Noah zaidi ya 16,000 zinasafirisha Watanzania zaidi ya milioni 115 kwa mwaka. Hizo Noah 16,000 zimeajiri makondakta na madereva 32,000. Ukichukulia kila kondakta mmoja na dereva mmoja akiwa anahudumia watu wanne, kuna wananchi zaidi ya 128,000 wanahudumiwa na watu hawa. Bado wanalipa kodi, TRA, SUMATRA, bima na wanatumia mafuta lakini kumekuwa na sintofahamu ya hawa madereva wa Noah na huu usafiri wa Noah Serikali imekuwa ikiwasumbua hasa SUMATRA…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, siungi mkono mpaka niambiwe suala la VAT linaishaje.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi niungane na Wabunge wenzangu wengi kuwapongeza Jeshi letu la Ulinzi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Lakini nilikuwa natoa ombi kwa Wabunge na hata Kanuni zetu inabidi tuzibadilishe, inapofika kipindi tunapojadili bajeti ya Jeshi, Wabunge wote tuwe kitu kimoja. Ukitaka ujue ubora na kazi kubwa wanayoifanya Jeshi angalia yaani ukiona majirani zetu wametulia ujue Jeshi wako kazini. Maana kuna kipindi fulani makelele makelele yalikuwa yanasikika huko lakini sasa hivi yametulia. Kwa hiyo, nikupongeze sana Ndugu Venance Mabeyo kwa kazi kubwa ambayo unaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilikuwa napenda kupata majibu, hivi wanajeshi wanapokwenda kwenye makambi kule kuna vitu gani wanapewa, mbona wakija mtaani wanakuwaga na vurugu sana, kwa sababu mwanajeshi akimkuta mtu wa kawaida kavaa nguo inayofanana na Jeshi anamvua, mwanajeshi akiwa baa akifanyiwa kitu cha hovyo inakuja kambi nzima baa kuleta vurugu, hivi kuna kitu gani mnawapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ulinzi wa mipaka. Jukumu la Jeshi letu ni kulinda mipaka ya nchi yetu, sina hofu sana naamini kazi nzuri wanayoifanya, lakini sasa hofu yangu inapokuja ninapoona kwenye makambi ya majeshi na maeneo ya majeshi yanapoingiliwa na wananchi wa kawaida. Wananchi wanalima, wanajenga, wanauziana yale maeneo, sasa najiuliza, hivi kwenye mipaka yetu kukoje? Sina hofu sana, lakini kuna umuhimu wa kufanya ukaguzi kwenye mipaka kwa sababu siku tunaweza tukakagua mipaka ya nchi tukakuta nchi iko nusu tayari watu wameshajigawia huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni jambo la matibabu, hili ndiyo jambo kubwa sana ambalo linalalamikiwa na wanajeshi wengi. Tunajua wanajeshi wengi wanaishi kwenye makambi na sina imani kama wake zao na wenyewe ni wanajeshi. Naamini wake zao wengi wanafanya kazi nyingine na wako maeneo ya nje ya makambi na watoto wao pia wanaishi nje ya makambi kwa sababu wengine ni wanafunzi. Sasa suala la matibabu limekuwa kizungumkuti, wengi wanatibiwa katika zahanati na hospitali za jeshi ambazo ziko kwenye kambi za Jeshi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapata taabu sana wanapopata rufaa, matibabu ambayo hawawezi kutibiwa kwenye kambi zao, mpaka waende Lugalo. Lugalo kuna urasimu wa matibabu, wanajeshi wenye vyeo vya chini wanapokwenda pale wakiwa wanaugua wanawekwa pending mpaka watibiwe watu wakubwa. Hilo suala mimi nimeshakutana nalo na Waziri analifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanashindwa kujiunga na mifuko mingine ambayo wafanyakazi wangine wanatibiwa, wanasema na hoja ya usiri. Hoja ya usiri ipi, kwenye matibabu hakuna usiri, wanasema wataanzisha mfuko wao wa wanajeshi kwa ajili ya matibabu. Kazi yao waliyonayo tu ya kulinda nchi ni ngumu, sasa wanataka kuanzisha kazi nyingine tena. Changamoto watakayopata, kwanza wana vituo vichache vya matibabu, pili mfumo wa malipo kuuandaa ni kazi, tatu kuandaa mfumo kwa ajili ya ukaguzi na kuhakiki madeni hiyo Jeshi hawataliweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nawashauri, Jeshi wangejiunga katika mfumo wa matibabu ambao wanaupata majeshi yote ya ulinzi, kama Polisi, kama Jeshi la Magereza, kama Usalama wa Taifa, kama PCCB, kwa sababu hata wakistaafu wanajeshi hawathaminiwi tena. Kwa hiyo, mimi naunga mkono hoja lakini suala la matibabu ya wanajeshi ni muhimu sana wakajiunga na mfumo mwingine ambao wanatumia majeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kutuchagulia Mkaguzi na Mdhibiti kuu wa Hesabu za Serikali mpya na mchapa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwape udhibitisho; Ofisi ya CAG haikuwa safi kama walivyokuwa wanaifikiria. Nataka niwape mfano; mfumo wetu wa ukaguzi katika halmashauri zetu ukaguzi wa miradi unafanyika kwa sampling, yaani katika miradi kumi unakaguliwa miradi mitatu, ile miradi mitatu ndiyo inatoa remarks ya ile miradi kumi; sasa pale ndipo mianya ya rushwa inapopitia. Inatolewa pesa inakaguliwa miradi mizuri mibovu inaachwa, hatimaye remarks inatoka hati safi lakini vitu vinakuwa hovyo. Kwahiyo naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuchagulia CAG mpya; na napenda nimuambie kuwa aendelee kufanya reform katika ofisi ya CAG ili wananchi wapate haki zao na huduma wanazostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili nataka niongelee elimu. Tanzania ina idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 55 na watu wazima wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 25, lakini production iliyoko katika nchi yetu haiendani na idadi ya watu waliopo; kwanini idadi ya watu haiendani na production iliyopo? ni kwasababu kubwa ya elimu ambayo wanaipata; yaani mitaala yetu ya elimu hai-fit nchi yetu ya Tanzania na nje. Kwa mfano shule ya msingi wanafunzi wanafundishwa darasa la kwanza mpaka form four lakini akienda mtaani hawezi hakafanya kitu kwa sababu mitaala ya elimu haimuruhusu yeye kwenda kuwa productive katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napendekeza mwanafunzi wa darasa la kwanza mpaka form four ukiacha masomo ya msingi anayosoma awe anapewa elimu ya msingi ambayo itamwezesha kutumia rasilimali inayozunguka maeneo yake. Kwa mfano, maeneo ya Kanda ya Ziwa wanafunzi wa elimu ya msingi wafundishwe uvuvi na uchimbaji wa madini ya dhahabu; maeneo ya Lindi wafundishwe kilimo bora kama cha korosho; maeneo ya Mara na Singida wafundishwe uvuvi wa kisasa; Dodoma wafundishwe uvuvi wa kisasa katika elimu ya msingi ili asipoendelea chuo aweze kupambana na maisha; maeneo kama Rukwa wafundishwe tiba asili. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa chuo kikuu, leo hii tumeshuhudia wanafunzi wanaomaliza chuo kikuu ni zaidi ya laki tano kwa mwaka lakini hawa wanafunzi wanapokwenda mtaani…

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, mnacheka lakini tiba asili inalipa kwelikweli.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo.

MWENYEKITI: Worldwide inalipa sana.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Sawasawa.

MWENYEKITI: Kabisa, angalieni dawa za Mchina ziko dunia yote. Endelea Mheshimiwa Mlinga, walikuwa wanacheka dawa za asili kwa Rukwa lakini mimi nawaambia ile ni mtaji mkubwa. Ukienda Nairobi unakuta mabango yameandikwa mganga maarufu kutoka Tanzania (Rukwa). Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hata wale wenye shida ya nguvu za nanihii tiba asili ndiyo imekuwa mtatuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa chuo kikuu, leo hii tumeshuhudia utitiri wa vyuo vikuu lakini kozi ambazo wanaziweka katika vyuo hivyo haziko productive katika nchi yetu. Leo hii tunasikia Wizara ya Elimu wanatangaza walimu wa arts hatuwahitaji tena lakini vyuo bado vinazalisha wanafunzi wa arts na bado vinakwenda kudahili wanafunzi tena wanapewa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza mitaala yetu ya elimu ya chuo kikuu iwe inatolewa kulingana na mahitaji ya nchi yetu. Kwa mfano, mtu anamaliza Business Administration hawezi kuanzisha hata genge la nyanya; mtu anamaliza Public Administration hata uongozi wa familia yake hawezi, watoto wanavuta bangi. Wanasheria, tumeshuhudia wako Wabunge wanasheria lakini wanaongoza kwa kufanya makosa, kila siku wako mahakamani.

Kwa hiyo, napendekeza hata vyuo vikuu mitaala iendane na mahitaji ya nchi yetu yaani watu wanapotoka hapo wawe productive na siyo kuvunja sheria na mambo mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la mapato napendekeza kwenye kipengele kimoja tu, tunapoteza mapato mengi sana katika nchi yetu. Nitolee mfano, tuna madereva wengi sana katika nchi yetu zaidi ya laki tano, lakini wengi wameajiriwa katika ajira ambazo siyo rasmi. Kwa mfano, madereva teksi wako zaidi ya 4,000 hawalipii kodi, NSSF wala matibabu. Madereva wa daladala zaidi ya 20,000 hawalipi kodi. Madereva wa mabasi makubwa zaidi ya 5,000; madereva wa mabasi ya kati zaidi ya 5,000 na madereva wa Noah zaidi ya 16,000 lakini hawalipi kodi. Napendekeza kwa mfano vile vitambulisho tulivyowapa Wamachinga tungewapa na madereva ili wawe wanalipia hata laki moja kwa mwaka ili iwe kwa ajili Pay As You Earn, NHIF na NSSF ambayo itawasaidia hata wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka nipendekeze kwenye utafiti. Benki yetu Kuu ya Tanzania tuna Kitengo cha Utafiti lakini wanafanya tafiti matokeo yake ripoti wanazifungia kwenye makabati. Tumeshuhudia tuna mazao kama tumbaku ni crisis katika soko; tuna korosho ni crisis katika soko; tuna pamba crisis ni katika soko, lakini BoT tangu imeanzishwa kuna Kitengo cha Utafiti, sasa tuwaulize wanafanya nini zaidi ya kupokea mishahara tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tafiti wanazozifanya BoT katika mambo mbalimbali ya mining, kilimo, biashara, hizo ripoti wawe wanaziweka wazi. Tuna matajiri katika nchi yetu; ikusanye matajiri na benki, iweke ripoti katikati itoe ushauri watu wakopeshwe hela matokeo yake wafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda EPZA nikakuta wanaagiza nyuzi kutoka India wakasema wao pamba inayozalishwa Tanzania yote zingekuwa zinatengenezwa nyuzi wana uwezo wa kuzinunua zote. Sasa waulize BoT wanashindwa kumshauri hata Mohamed Dewji akapewa mkopo akatengeneza kiwanda cha nyuzi akanunua pamba zote za Wasukuma zikatengenezwa nyuzi akapeleka EPZA wakaenda kuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunategemea nyuzi kutoka India wakati Wasukuma kule na watu wengine hawana sehemu ya kuuza pamba zao. Kwa hiyo, napendekeza hiki Kitengo cha Utafiti cha BoT wafanye kazi yao, waache kupokea mishahara waweke ripoti wazi matajiri tunao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, uchangiaji wangu utakuwa reference Ulanga. Mimi naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika nchi yetu ya Tanzania; na sasa mimi nitawapa ushahidi wa Ulanga.

Mheshimiwa Spika, tutaanza kabla mtoto hajazaliwa, yaani kwa maana ya wajawazito jinsi gani Mheshimiwa Rais alivyowajali. Kabla ya uhuru mama zetu wengi walikuwa wanajifungulia kwa wakunga wa jadi, walikuwa wanajifungulia njiani na katika zahanati ambazo zilikuwa hazina vifaa na hata kama zina vifaa, vifaaa vyake ni duni. Vikajengwa vituo zaidi ya 340 vya afya; kwangu nikapata kimoja, kituo hicho cha afya kinaitwa Lupilo. Kabla kituo cha afya hiko hakijaboreshwa kilikuwa kwa mwezi wanajifungua watoto wanaojifungulia katika kituo cha mama wajawazito hapo ilikuwa 25 hadi 30. Baada ya kuboreshwa kujengwa chumba cha upasuaji pamoja na wodi, sasa hivi wanajifungua akina mama 145 hadi 160 kwa mwezi. Hayo ni mafanikio makubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa dawa, mtoto anapokuwa, mwanzo bajeti ya dawa ilikuwa kidogo sana na ilikuwa inapatikana kwa mashaka; lakini sasa hivi sio Ulanga nchi nzima bajeti ya dawa imeongezea zaidi ya mara dufu.

Mheshimiwa Spika, mtoto anapokuwa nahitaji kwenda shule, Ulanga sisi tunafuga sana kuku na mifugo midogomidogo pamoja na nguruwe. Ilipokuwa muda wa kufika wa kuwapeleka watoto shule walikuwa wanapita wagambo kuwalazimisha wazazi wawapeleke watoto shule, wazazi wakawa wanalazimika kuuza mifugo yao ikiwemo kuku ili waweze kuwapeleke watoto shule, sasa hivi elimu bure. Idadi ya wanafunzi wanaoenda darasa la kwanza imeongezeka kwa asilimia 56; haya ni mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia zamani ilikuwa suala la madawati ni la halmashauri na wazazi, tumeanza katika Bunge hili, Bunge peke yake kwa ushawishi wa Rais tumeweza ku-contribute zaidi ya madawati 500 kila Jimbo, haya ni mafanikio makubwa mno.

Mheshimiwa Spika, mtoto anapokuwa anamaliza kidato cha tano na sita anatakiwa kwenda chuo kikuu, tumeshuhudia katika Serikali hii Serikali imetenga mkopo zaidi ya mara mbili kwa ajili ya wanafunzi. Mkopo wa elimu ya juu imefika zaidi ya bilioni 450; haya ni mafanikio makubwa sana. Mwanzo waliokuwa wanasoma shule za private walikuwa hawapati mikopo lakini sasa hivi tumeshuhudia wanaosoma shule za Serikali pamoja na shule za private wote wanapata mikopo haya ni mafanikio makubwa ambayo hayana ubaguzi.

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye mawasiliano ndiyo kabisa. Jimbo langu la Ulanga lilikuwa na mawasiliano; kwa sababu wewe ulishafika Ulanga; unaweza ukaongea na simu ukiwa Ulanga pale, Mahenge Mjini ukiwa Minepa pamoja na Lupilo basi yaani jimbo zima lilikuwa na mawasiliano asilimia tano tu. Hivi navyokwambia asilimia 95 ya jimbo lina mawasiliano. Tena kipindi kile kwa bahati mbaya wale wazee ambao walikuwa na wake wawili na watatu ilikuwa ikiingia giza anapotaka kwenda kwa mchepuko anaaga anasema nakwenda kuongea na Mbunge yaani mawasiliano yalikuwa yanapatikana kwenye vichuguu tu ambayo yalikuwa mbali na mji. Kwa hiyo sasa hivi kusambaa kwa mawasiliano kumesababisha hadi kuimarika kwa ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, daraja la mto Kilombero, wewe ni shahidi ilikuwa Ulanga kipindi cha masika huwezi kufika, ilikuwa ni kisiwa. Serikali ya Awamu ya Tano imekamilisha ujenzi wa Daraja la Kilombero. Mimi hata sasa hivi naamua naenda jimboni lakini kipindi hicho muda huu mimi siwezi kwenda jimboni yaani masika Mbunge alikuwa haonekani mpaka masika iishe, hayo ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, barabara nchi nzima, kutoka Kidatu mpaka Ifakara ilikuwa ni kipindi cha masika unatumia zaidi ya siku mbili hiyo barabara lakini sasa hivi tunajenga barabara ya lami inapita kwenye Jimbo la Mheshimiwa Lijualikali na Mheshimiwa Profesa Jay hayo ni mafanikio makubwa tu, sio kwa Ulanga kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache na mimi nampongeza Mheshimiwa Rais namkaribisha sana Ulanga, Ulanga wanahitaji wamuone tu, hata asipoongea kitu akifika Ulanga ni ushindi wa kishindo mwaka 2020. ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami naomba nitoe maoni yangu machache kuhusiana na upandishaji wa hadhi wa pori hili kuwa National Park.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kupandisha hadhi pori hili kwa sababu tukiangalia wenzetu wa Kaskazini kule Mji kama wa Arusha umeendelea sana kutokana na utalii, namii kwa mfano Jimbo langu la Ulanga sehemu kubwa sana ni Selous Game Reserve sasa kwa kupandisha hadhi kuwa National Park kuna vitu vingi sana tutapata fursa vikaweza kuonekana. Kwa mfano tu nilienda maeneo ya Monduli nikakuta watalii wanaangalia ngoma za Maasai ambao wanaruka ruka, lakini kwetu Ulanga tuna ngoma inaitwa Sangula ni ngoma nzuri sana, nadhani itajulikana hata Kimataifa pia kuna milima mizuri na mambo mengine.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba niongelee suala la Stigler’s. Mheshimiwa Rais wakati anatoa kauli wakati wa anazindua ujenzi wa bwawa hili alisema kuwa watu watakuwa wanaruhusiwa kwenda kufanya uvuvi lakini tunafahamu sheria za TANAPA na Sheria za Uhifadhi haziruhusu watu kwenda kwenye maeneo haya, kwa hiyo naomba hili liwekwe clear.

Mheshimiwa Spika, pia tunapokuja kutoa matamko hayo pia tuangalie na Sheria hizi za Uhifadhi na Sheria za TANAPA kwa sababu Sheria ya Uhifadhi wa Misitu ya Wanyamapori inasema kuwa, ng’ombe wakikamatwa au mifugo ikikamatwa inataifishwa lakini ile Sheria ya TANAPA ni ya kupiga faini, hivyo tunataka sheria moja uniform ambayo itakuwa haiathiri mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu zito nililokuwa nataka niongelee ni kuhusu wafanyakazi, naona Wizara wanalikwepa na Kamati wanalikwepa. Wote tunafahamu Game Reserve zinakuwa chini ya TAWA, mfanyakazi wa TAWA kima cha chini cha mshahara hakizidi shilingi laki nne. Leo hii inapandishwa hadhi inaenda kuwa chini ya TANAPA na TANAPA mshahara kima cha chini siyo chini ya shilingi milioni moja, leo hii inapoenda kupandishwa hadhi TANAPA hawataki kuwarithi hawa wafanyakazi ambao wamefanyakazi kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba Waziri wakati ana-wind up atuambie hawa wafanyakazi wa TAWA na wenyewe waende wawe chini ya TANAPA irithi pori pamoja na wafanyakazi kwa sababu wamefanyakazi muda mrefu, vyuo wanavyosoma ni vilevile, fani ni ile ile, mapori ni yale yale wanyama ni wale wale, kwa nini TANAPA ing’ang’anie kwenda kuajiri wafanyakazi wengine wakati wafanyakazi wapo ambao wana uzoefu na taaluma zile zile. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba atoe kauli kuhusiana na hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la vitendeakazi. TAWA wana miliki wanyama wote ambao wako ndani ya mbuga na nje ya mbuga lakini vifaa hawapewi, TANAPA wanamiliki wanyama wachache ambao wako kwenye National Park tu lakini wanapewa kila kitu resources zote wanazo, tunaona kwa mfano tembo walioonekana Dodoma TAWA ndiyo wanahusika, tembo wanaoingia maeneo ya makazi yote ni TAWA lakini hawana vifaa kama alivyosema Mheshimiwa Suzan unakuta Kanda nzima wanapewa gari moja ama mawili. Kwa mfano wa Ulanga kule sasa hivi tembo wanasumbua mitaani lakini hawana vifaa. Kwa hiyo naomba TAWA waongezewe vitendeakazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja lakini naomba suala la wafanyakazi litolewe kauli. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nataka niunganishe kwa kaka yangu, Mheshimiwa Kubenea aliyepita kuchangia sasa hivi kuwa sheria siyo msahafu kwa hiyo muda wowote tukiona haifai tunapiga chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa namna ya pekee naomba nitoe nitoe pongezi zangu kwa Mheshimiwa Spika kwa kuunda Kamati hii ya Sheria Ndogo…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naendelea; pongezi zangu kwa Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwa kipindi kifupi cha miaka minne nilichokaa kwenye Kamati hii nimeona umuhimu wake jinsi gani ulivyokuwa mkubwa. Sheria ni nyingi mno na zinaumiza wananchi, na ndiyo maana mmeona hata wengine afya zetu zimekuwa ni ngumu kukua kutokana na kazi kubwa ambayo ipo kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na Ofisi ya Mpigachapa wa Serikali. Sheria nyingi zimekuwa zikitungwa lakini inatumia muda mrefu sana kufika mpaka zitoke kwa sababu katika Ofisi ya Mpigachapa wa Serikali wanatumia vifaa vya zamani na ni chakavu na watumishi ni wachache. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iweze kuiwezesha Ofisi ya Mpigachapa ili sheria zinazotungwa ziwe zinaweza kutoka kwa wakati kwa sababu kuna sheria zinaweza zikatoka tayari zimeshapitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka nizungumzie, kwa uzoefu niliopata sheria nyingi hazishirikishi wadau vya kutosha. Utakuta taasisi ama halmashauri wanaita wadau wanasikiliza lakini hawazingatii vya kutosha yale maoni. Yaani kana kwamba wanakuwa tayari sheria walishatunga wameshaweka kwenye vichwa vyao kwa hiyo wadau wanakwenda kuwasikiliza kama kukamilisha ratiba. Kwa hiyo, unakuta sheria zinatungwa lakini haziendani na mazingira yaliyopo. Wote mtakuwa mashahidi kanuni za kikokotozi zilivyopita na zikaleta taharuki katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebaini watendaji wengi wanafanya kazi kwa mazoea, hasa hawa watunzi wa sheria.

Kwa hiyo, wamekuwa wakifanya ilimradi wanafanya, matokeo yake makosa yamekuwa mengi mno katika hizi sheria. Kwa hiyo, Kamati sasa ya Sheria Ndogo imekuwa inafanya kazi ya kutunga sheria, siyo kuzirekebisha, maana yake mnapita neno kwa neno. Kwa hiyo, makosa yamekuwa mengi, makosa mengine ya kiuandishi, mpaka unajiuliza huyu mtunzi wa sheria anajua anakwenda kutumia hii sheria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine zimekuwa hazizingatii uhalisia. Kuna sheria moja ya BASATA niliiona inasema katika kila kumbi ya sherehe iliyopo manispaa, tozo ya BASATA ni shilingi 500,000. Sasa unamuuliza aliyepitisha hii sheria anazijua manispaa zetu za Tanzania? Nitolee mfano Singida, Singida hauwezi kwenda ukakuta ukumbi ambao unazidi 500,000, sasa tozo ya BASATA peke yake ni shilingi 500,000, je, unauliza, ukumbi huu sherehe itatozwa kiasi gani. Au sheria nyingine za BASATA zinasema eti kuwa ukitaka kujenga ukumbi wa sherehe popote pale lazima michoro iende ikapitishwe na BASATA wakati wengi wanaotengeneza hizi kumbi za starehe za kufanyia sherehe tunajua wanajenga kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ambayo niliiona ya hovyo ni sheria ambayo inasema kila msanii ambaye atakwenda kufanya tangazo anatakiwa tozo ya BASATA alipe shilingi milioni mbili. Sasa unauliza; anajua mazingira ya wasanii wetu wa Tanzania? Wengine wanakwenda kufanya matangazo kwa ajili ya kuuza sura, wengine wanakwenda kufanya matangazo kwa ajili ya kupata uzoefu, wengine wanafanya bure ili waonekane; kwa hiyo, sheria nyingi hazizingatii uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije kwenye halmashauri…

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naipokea taarifa yake, lakini bado uhalisia uko palepale. Kwa mfano mimi Mlinga nina kibanda changu pale cha chipsi nataka msanii aje aonekane anakula ili wateja waje, mtaji hauzidi laki tano halafu wanataka nimlipe huyo msanii milioni mbili kwa hilo tangazo, kwa hiyo bado hazizingatii uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye halmashauri. Sheria nyingi ambazo zinaletwa kwenye Kamati yetu na zinazotungwa katika nchi yetu zinazotoka halmashauri – na hii ni kwa wingi wake – lakini hata hivyo, siyo sababu tosha ya kufanya sheria hizi ziwe na makosa. Tumegundua sheria nyingi za halmashauri ni copy and paste. Yaani mtu anachukua sheria ya Igunga anaenda kui-apply Ulanga, anachukua sheria ya Mpwapwa ambalo ni Jangwa anakwenda kui-apply Gairo au Kilosa. Kwa hiyo, sheria nyingi haziendani na yale mazingira, yaani ni copy and paste. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii napenda kupeleka lawama nyingi katika Kitengo ha Sheria cha TAMISEMI. Wamekuwa hawako makini katika kazi zao, na hata uandishi wa hizi sheria unaweza ukakuta kwenye ganda la sheria wanasema sheria inayohusu Igunga lakini ukienda ndani utakuta ni wilaya nyingine. Kwa hiyo, hata kusoma hawazisomi, siyo kupitia tu kuangalia je, sheria hizi zitaumiza wananchi au hazitaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kutoa angalizo; TAMISEMI wangetoa mwongozo kwa hizi halmashauri zote kwa sababu Madiwani wengi kutokana na asili yao ya maeneo wanayotoka wengi hawana uelewa na elimu ya kutosha. Kwa hiyo, wametunga sheria ambazo nyingi zinaumiza wananchi, hiyo inawawezesha hawa Madiwani wajue nini wanakifanya na madhara ya hivi vitu ambavyo wanavipitisha kwa sababu wakishavipitisha kuvirekebisha inachukua muda sana.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na nitoe angalizo kwa Mawaziri; msiwe mnasaini sheria hizi bila kuzipitia. Wengi mmekuwa…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: …mkifanya makosa ambayo yanafanywa na watendaji wetu. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia nitoe mchango wangu mdogo.

Mheshimiwa Spika, nataka nianze walipomalizia wenzangu kwenye jambo hili la Tume huru ya uchaguzi; katika uhalisia kijana anayedai, anayeomba kuoa katika familia ni kijana ambaYe ana base yaani ameshaonyesha ana mwanga, anajua maisha yake ataishi vipi aidha anafanya kazi au analima ana shamba. Sasa wapinzani kitendo cha kudai Tume huru ya uchaguzi wakati hakuna mlilowafanyia wananchi ni sawa sawa na kijana ambaye kula na kulala bure anayedai kuoa.

Mheshimiwa Spika, wapinzani walipewa Wabunge zaidi ya 100, Madiwani zaidi ya 1500, hamna walichokifanya. Sasa hivi umefika wakati wa uchaguzi wanadai waongezewe tena ili wafanye mabadiliko. Kama mlishindwa hivyo hata tukiwapa Nchi hamna kitu mtakachokifanya.

Mheshimiwa Spika, Chama Cha Mapinduzi tuko tayari kwa uchaguzi. Tumefanya mambo mengi sana. Nimpongeze Mheshimiwa Rais katika kila Nyanja. Niwape mfano, upande wa Vijijini; wananchi wetu wa Vijijini asilimia 90 ni wakulima na wengi wanalima kwa ajili ya chakula. Mwanzo Mwananchi akilima kidebe chake kimoja hawezi kukatisha mageti yalikuwa kibao lakini Rais wetu kwa kuliona hili akaondoa ushuru wote kwa hiyo wakulima sasa hvi ukilima ukiwa chini ya tani moja hulipii ushuru wa namna yoyote. Hizo ndiyo base zetu zinazotufanya twende kwenye uchaguzi kifua mbele.

Mheshimiwa Spika, kwenye mazao ya biashara kama Pamba, Tumbaku, Kahawa, Mkonge, Miwa kodi zilikuwa zaidi ya 140 lakini zimepunguzwa sasa hivi ziko chini ya 125. Hizi zote zinatufanya sisi twende kifua mbele kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, mtaani, bodaboda niwatolee mfano; wenzetu walikuwa wanawapa viroba bodaboda sisi tumewaondolea kero. Kwa mfano; trafiki walikuwa wanawasumbua sana. Bodaboda akikatiza anapigwa fine 60,000 au 100,000 au 120,000 lakini sasa hivi kipindi kile Waziri ni Kangi alipiga marufuku bodaboda fine ni moja tu na bodaboda zote ambazo zilikuwa kwenye vituo vya Polisi zimefagiliwa zote wamerudishiwa wenyewe sasa hawana watu wa kuwasaidia na hao ndiyo walikuwa watu wanaowasaidia katika kampeni.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Machinga; Machinga zamani walikuwa wanalipia ushuru kila kona wanayokatiza sasa hivi Machinga anapewa kitambulisho cha shilingi 20,000 marufuku kusumbuliwa anakwenda kufanya biashara popote, wao walikuwa wanawatumia katika maandamano.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa wasomi; elimu ya juu tunakumbuka tulikuwa tuna maandamano kila siku, kila Chuo utasikia leo mgomo, kesho mgomo. Zamani mikopo ilikuwa inatolewa kwa matabaka sasa hivi mikopo hakuna kutoa kwa matabaka. Kwa hiyo, Wanafunzi wanapata mikopo kwa hiyo wamekosa watu wa kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, madarasa yanajengwa; juzi World Bank wametuidhnia mkopo wa Dola milioni 500. Wapo wapinzani ambao walikuwa wanakwenda wengine walikwenda hadi nje ya Nchi. kwenye hili nataka kujua, Tume ya Maadili ya viongozi wajibu wapo ni upi? Kiongozi anapotoka kwa ajili ya kwenda kuichafua Nchi huko nje, Tume ya Maadili isiishie tu kuangalia mikopo, madeni na mali zetu, iangalie na viongozi kama hawa. Niwaambie tu viongozi, wazee wetu ambao mnatulea tuko humu, watu kama hawa sijui mmewaleaje mimi hata sielewi.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa ardhi; tumeshuhudia zamani hati ya nyumba, ya kiwanja walikuwa wanapata matajiri tu sasa hivi hadi masikini wa kawaida. Mimi kule Ulanga wamefanya pilot study yaani wamechukua eneo kama ndiyo case study, kila Mtu anayemiliki ardhi anapewa hati bure. Sasa hati ilitoka kutoka miaka 10 hadi wiki mbili. Wizara ya Ardhi pale Mtu anapimiwa kiwanja ndani ya wiki mbili ameshapata haki yake. Zote hizo tunakwenda kifua mbele kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara na nishati kwenye REA; Vijiji vyote sasa hivi vinapata umeme hizo zote ni nyenzo zetu kwenye uchaguzi ndiyo tunakwenda navyo.

Mheshimiwa Spika, unyenyekevu wa viongozi wetu wa juu; Chama Cha Mapinduzi viongozi wa juu wananyenyekea viongozi wa chini lakini wenzetu viongozi wa juu wanawalangua viongozi wa chini, wanawachangisha michango. Hizo zote ni nyenzo zetu za kwenda kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Rais wetu, kiongozi ,mwenye maono. Kwanini nasema hivyo? Rais wetu alipoingia madarakani alipiga marufuku safari za nje. Hebu imagine na corona hii maana yake kipindi kile Wabunge badaa ya vikao vya Bunge wote walikuwa wanakwenda nje. Vikao vinapotaka kuanza ndiyo wanarudi sasa Wabunge wangerudi na corona hii tungekuwa wageni wa nani? Kwa hiyo, Rais wetu alikuwa na maono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za Wilaya; vituo vya afya zaidi ya 400, hospitali za Wilaya zaidi ya 67, hospitali za rufaa. Hivi na corona hii tungekuwa wageni wa nani tusingekuwa na vituo vya afya hivyo na hospitali za Wilaya?

Mheshimiwa Spika, nataka nijikite kidogo kwenye janga la corona; kwanza naomba Wabunge tuambiane ukweli, tofauti ya corona na HIV maana yake wengi wanailazimisha Serikali ianze kupima watu, hiyo siyo suluhu. Tungekuwa na mahali tukishawapima hawa watu tunawapeleka hiyo ingekuwa sawa lakini eti unampima mtu halafu unamuachia aende akarudi nyumbani. Janga la corona uamuzi uko mikonini mwa kila Mwananchi, kila Mwananchi usafi wako ndiyo utakaokupelekea wewe kutokuwa na corona au la!

Mheshimiwa Spika, cha msingi hapa naomba katika Majiji, Wilaya, Halmashauri zetu tutunge Sheria ndogo ndogo za dharura. Kwa mfano; kwenye vyombo vya usafiri kama bajaji na daladala na usafi katika mitaa yetu hiyo itatusaidia. Niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutokurupuka katika janga hili maana yake kuna Nchi kwa mfano; Nchi za wenzetu jirani wamekimbilia kuna Nchi moja hapo walifunga mipaka wiki tatu zilizopita walizuia Ndege lakini wagonjwa kila siku wanazidi. Sisi hatujafunga mipaka mpaka leo tuna wagonjwa 20. Kwa hiyo, naomba niendelee kuwaasa wananchi wote, kuwapongeza madereva bajaji, madareva bodaboda na wananchi wengine kwa kuendelea kuzingatia haya.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba niongelee suala pensheni; Mheshimiwa Jenista Wazee wa Ulanga watakulaani. Nimetoka Ulanga Wazee zaidi ya 57 wastaafu, walimu waliostaafu tangu mwaka juzi hawajapata kiinua mgongo, hawapati pensheni yao ya mwezi. Hebu imagine mtu amefanya kazi miaka 30 alizoea kila mwisho wa mwezi anapata mshahara leo hii ana mwaka wa pili hajapata pensheni yake, hapati pensheni ya mwezi. Nimeenda Ofisi ya Kanda Morogoro hawana majibu wanasema iko Dodoma. Jamani huo uhakiki gani mtakuja kuwaua wazee wa watu. Wametaka kuja Dodoma kwenye Bunge hili nimewaambia hapana wageni hawaruhusiwi wamesema bora wafe na corona kuliko kufa na njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba nikupongeze wewe na huu mfumo wa E-parliament kwa kuwa na maono. Hivi leo hii na mavitabu yale tungepona na hii corona? Leo nimeona kuna kigazeti kimoja kimeandika “mnyukano mpya wa Lissu na Ndugai”. Wewe uko imara ndani umewagonga na kanuni wametoka nje na nje wakikuchokoza najua watakutana na bakora.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi leo naomba nianze nyumbani kidogo kwa sababu Muswada wenyewe unahusiana na taarifa. Rais wangu ni msema ukweli, na msema ukweli ili awe mpenzi wa Mungu inabidi akubali kuambiwa ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya uchumi sasa hivi ni ngumu sana huko mtaani. Mimi kama Mbunge kijana ninayewawakilisha vijana na vijana ndiyo wanaoongoza kwa kutokuwa na ajira, kweli kuna hali tete, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Rais hapo alipopashika sipo, abadilishe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ni kwa ajili ya wafanyakazi. Wafanyakazi ndiyo wanaosaidia kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, leo hii wanaishi katika maisha ya tension, wengi wanakwenda ofisini hawajui kama watarudi salama, kuanzia Makatibu Wakuu hadi Watendaji wa Mtaa, kweli wanaishi maisha magumu. Wote mtakuwa mashahidi juzi kuna Mkuu wa Wilaya mmoja alitaka ku-demote walimu wakuu zaidi ya 500, kweli hatuwatendei wafanyakazi wetu haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi Bungeni sasa. Kwanza naomba niendelee kumtakia afya njema Spika wetu wa Bunge, mimi ni mmojawapo kati ya watu ambao walikuwa wanamuombea kwa dua zote ili arudi salama tuendelee kulisukuma gurudumu hili. Kwa upande mwingine siyo kama wenzangu wa upande wa pili ambao walisema wamem-miss Spika, maadili ya Katiba ya nchi yangu na jinsi nilivyolelewa hairuhusiwi mwanaume kumwambia mwanaume mwenzako nimeku-miss.
Naomba niwashukuru wapinzani kwa kurudi Bungeni kwa sababu kitendo cha kuingia na kutoka kilikuwa kinaambatana na matukio mengi, pamoja na wizi, uporaji na unyang‟anyi pamoja na ujambazi, kwa hiyo, kitendo hicho naamini sasa hivi hakitakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Muswada. Imeshajengeka tabia kila kitu kizuri sasa hivi kinachofanyika ni kwa ajili ya kuwabana wapinzani, Muswada mzuri umeletwa, Wabunge inatakiwa tuchangie, tuishauri Serikali lakini tumekuwa wakosoaji. Sasa leo muswada mzuri umeletwa mnasema uko kwa ajili yenu ninyi. Jamani, hivi CHADEMA kweli mko wengi kuliko CCM mna maslahi mapana kwa wananchi wa Tanzania kuliko CCM! Ninawaomba Watanzania, niwataarifu kuwa hakuna wasaliti kama Wabunge wa UKAWA, hawa watu ni wasaliti kuliko yule aliyemsaliti Yesu Kristo wa Nazareth.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu kimekuwa cha kupinga. NHC sasa hivi wanafanyakazi, wanasema wanafuatwa wao. Polisi wakifanya mazoezi wanasema wanafanya mazoezi kwa ajili yao, jamani kitu gani ambacho tutakifanya kiwe kizuri kwenu ninyi?
Mheshimiwa Rais amesema siasa mpaka mwaka 2020, ninyi mnasema amewazuia ninyi. Jamani Chama cha Mapinduzi kina uongozi kuanzia Mwenyekiti hadi Mtaani tuko, wengi kama hiyo siasa CCM ndiyo tunaihitaji zaidi kuliko ninyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefika kipindi mpaka wanamkufuru Mungu, wanasema kupatwa kwa jua kumetokea kwa ajili yao ili kuwe na giza wasiweze kufanya maandamano.
Mimi naomba niwaambie, haya mambo ya kuambiwa kila kitu anachosema Mwenyekiti mkikubali mtakuja kuamuliwa hadi mambo yenu ya nyumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu ni mzuri na ninachoomba Serikali isibadilishe hata nukta, hivi ulivyo ndiyo usainiwe kwa ajili ya kuwa sheria. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Usuluhishi wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. GODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nataka niliambie tu Bunge lako tukufu kuwa Marekani imepata uhuru mwaka 1776 ina miaka zaidi ya 300 tangu ipate uhuru na Bunge. Kama wangekuwa kutunga sheria kuna mwisho, basi Bunge la Marekani leo hii lisingetunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa dhati kabisa niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu bila ridhaa yake Serikali isingeweza kuleta Miswada namna hii. Na huu ni muendelezo wa mapinduzi makubwa ya kimaendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiambie Serikali, msione haya kuleta Muswada hata kama tutaupitisha asubuhi, jioni mkagundua una upungufu, uleteni tutaubadilisha! Hiyo ndiyo kazi ya Bunge. Kwani mishahara na posho tunapata kwa sababu gani? Ni kwa sababu hiyo! Msione haya. Wenzetu wapinzani hata Katiba zao walipoona hazikidhi haja zao, walizibadilisha. Mfano mkubwa, kikomo cha Mwenyekiti kilikuwa miaka kumi, leo hii wamebadilisha Mwenyekiti amekuwa Mswati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais katika Mkutano uliopita, walitukejeli, walisema sisi wanafiki na hata uchaguzi wa Rais ulipokwisha wakasema hawamtambui. Nikashangaa juzi wanamuandikia barua, mnamuandikia barua mtu ambaye hamumtambui? (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuliowahi kufika Dar es Salaam mapema pale Kariakoo kuna msemo unasema tajiri hanuniwi! Ukivuka maji ukienda Zanzibar wanasema wewe susa sie twala! Ndiyo kilichowakuta hao. Leo hii Wapinzani badala ya kushauri vitu vya msingi katika Taifa letu, kama hivi vilivyoletwa, wanasema wanahitaji muafaka. Nataka nimuambie Rais wangu mpendwa, muafaka wa Watanzania ni Watanzania kupata umeme kila kijiji. Muafaka wa Tanzania ni Watanzania kupata elimu bure na bora, muafaka wa Tanzania ni Watanzania kupata huduma bora za afya kwa kujenga vituo vya afya kila kata, muafaka wa Tanzania ni Watanzania kupata maji safi na salama na sio kupatana na Wahuni wa kisiasa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu utaratibu!

KUHUSU UTARATIBU

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, tafadhali muda wangu ulindwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mjadala, Kifungu kwa kifungu tulijadili kwenye Kamati, siwezi ku-stick. Kuna Wabunge kama akina Mheshimiwa Msigwa hawajasoma sheria. Leo hii nikigonga kipengele kwa kipengele maana mimi ni Mwanasheria, nitawatoa nje. Naomba niendelee. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati kwenye maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye mjadala huu walikuwa wanazungumzia suala la Tume Huru ya Uchaguzi. Wote mashahidi, hivi Tume Huru ipi ya uchaguzi ambayo tunahitaji? Ni ile ambayo mgombea wa CHADEMA alipata kura 6,000,000? Ni ile ambayo CHADEMA walipata Wabunge 75? Ni ile ambayo CUF walipata Wabunge 42? Ni ile ambayo hata chama cha ACT, chama cha mfukoni walipata Mbunge mmoja? NCCRwalipata Mbunge mmoja? Tume Huru ipi ambayo mnaihitaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliongea na Mbunge mmoja wa CHADEMA, nilimuuliza Tume gani Huru ambayi mnaihitaji zaidi ya hii ambayo imewaingiza humu Bungeni? Akanijibu jibu rahisi? Akanijibu chizi karogwa tena, sikumuelewa maana yake nini? Ndani ya Bunge hili, tuko Wabunge 390 Watanzania tuko zaidi ya milioni 55…[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mlinga, muda wako umekwisha. Lakini pia…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba nichukue fursa hii kwanza kuipongeza Serikali kwa kuleta mabadiliko haya ya sheria tisa kwa mpigo. Lakini kama walivyotangulia wenzangu, kuna sheria nyingi ambazo zimepitwa na wakati, zingine zipo zinaumiza watu, nyingine zipo lakini hazina manufaa. Kwa hiyo zipo ambazo ni za kuboresha, zipo ambazo ni za kuzifuta kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Sheria ya Ubakaji, kutokana na ongezeko kubwa la ubakaji ilitakiwa sheria iletwe tubadilishe sasa, siyo kufungwa miaka 30 tu, ilitakiwa wahasiwe wabakaji. Pia sheria ya traffic; pikipiki inabeba abiria mmoja inalipa traffic case shilingi 30,000, basi linabeba abiria 60 eti la lenyewe shilingi 30,000 hiyohiyo. Kwa hiyo, hizi sheria zinatakiwa zinabilishwe siyo tunabeba kila kitu walichoacha wazungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije sasa kwenye sheria ambazo tumezibadilisha. Sheria ya kwanza napenda kuipongeza Serikali, hii Sheria ya SSRA. Tulianzisha SSRA kwa sababu kulikuwa na mifuko mingi ya hifadhi ya jamii kwa hiyo ushindani ukawa mkubwa, mifuko mingine ikawa ina- misuse jinsi ya kupata wanachama na wakawa wanatumia pesa vibaya sasa mingine ikawa inaelekea kufa kwa hiyo tukaona ili kunusuru tukai-merge ile mifuko tukaiunganisha tukapata mifuko miwili; PSSSF na NSSF. Kwa hiyo, sasa jukumu la SSRA likapungua kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukaona bora tuiondoe kisheria kwa sababu ushindani ulikuwa umeisha, majukumu yamepungua sana na matumizi bora ya rasilimali ya taifa ambayo tunahitaji sana kwa sasa hivi kwa ajili ya kuijenga nchi yetu tuipeleke sehemu nyingine na majukumu kidogo yaliyobaki tuyaweke chini ya Wizara. Kwa hiyo, sasa SSRA ilibaki ni mzigo kwa Taifa letu na ikawa haina msaada tena. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa ajili ya kuleta sheria ya kuifuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la michezo ya kubahatisha. Napenda niipongeze Serikali kwa sababu mwenyewe nilikuwa mpinzani sana wa hii michezo ya kubahatisha lakini naipongeza Serikali kwa kusikia kilio changu na kuleta haya mabadiliko ya sheria kwa sababu kumekuwa na wimbi kubwa sana la vijana wanaocheza michezo ya kubahatisha kwa mfano bodaboda na wanafunzi, akina mama wafanyabiashara wote, VICOBA wote wanakopa hela wankawenda kucheza kamali, mama wa nyumbani unampa pesa akanunue nyama anaenda kupikia watoto nyanya chungu hela anachezea kamali. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa sababu athari zake zilikuwa kubwa sana katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii michezo ya kubahatisa ni ajira. Tumeshuhudia katika nchi yetu sasa hivi kuna shida kubwa ya ajira kwa sababu vyuo vya kawaida na vyuo vikuu kwa mwaka vinatoa wanafunzi zaidi ya laki sita na kumekuwa na tatizo kubwa la ajira. Kwa takwimu ambazo nimezipata ajira ya moja kwa moja ambayo inaletwa na michezo ya kubahatisha ni 20,000, wananchi 20,000 wameajiriwa ambao ni wengi kuliko watendaji wa kata ambao hawazidi 4,000 na ni wengi kuliko watendaji wa vijiji ambao hawazidi 15,000. Na ajira za indirect, zisizo rasmi, ni zaidi ya laki moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ambayo inatoa ajira nyingi katika nchi yetu ni elimu ambayo imeajiri watu takribani watu laki tatu na nusu, kwa hiyo, inayofuatia kwa sasa hivi ni hii ajira ya michezo ya kubahatisha ambayo ni zaidi ya laki moja, na inafuatiwa na afya ambayo ni wastani wa lai moja. Kwa hiyo, lazima tuiwekee utaratibu rasmi kwa ajili ya kuiboresha na kui-monitor.

Mheshimiwa Naibu Spika, michezo ya kubahatisha ni chanzo cha mapato cha Serikali. Niipongeze hii Sekta ya Michezo ya Kubahatisha, hasa hii taasisi ya Gaming Board. Nimeangalia mapato yao, mwaka 2016/2017 ilikuwa bilioni 30, lakini 2017/2018 imepanda kwa shilingi bilioni 78, yaani ime-double, na 2018/2019 bilioni 95.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kipato hiki ni kikubwa sana ambacho katika matumizi ya kawaida ni bajeti ya Wizara mbili; Wizara ya Michezo na Wizara ya Mazingira ambayo ni bilioni 30 na bilioni 36, yote inakuwa accommodated kutokana na michezo ya kubahatisha, na pia Wizara ya Viwanda na Biashara bilioni 100 ambayo kwa wastani ni hela ambayo inaingizwa kutokana na michezo ya Kamali tu. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kuleta sheria nzuri ya kuratibu hii michezo ya kamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Tumeshuhudia ongezeko kubwa la watumiaji wa mitandao ya internet. Kwa takwimu za TCRA watu takribani milioni 23 wanatumia internet katika nchi hii, kwa hiyo kumetokea na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hususani instagram, facebook, twitter na snapchat. Watu wamekuwa wakipiga picha mbaya za ajali, tukio mtu amepata ajali familia ina utaratibu wa kuhabarishwa lakini sasa hivi unaweza ukashtukia ukamuona ndugu yako amekufa kwenye mitandao ya kijamii. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kuleta sheria kali kwa ajili ya kuratibu hivi vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda niwapongeze vyombo vya habari, watumiaji binafsi wa vyombo vya habari, mitandao ya kijamii ambao wanatumia mitandao vizuri kwa ajili ya kuelimisha na kuacha kuposha kutuma picha mbaya na napenda niwataje; kwa mfano Millard Ayo amekuwa akitumia mitandao ya kijamii vizuri, huwezi ukakuta picha za marehemu katika mtandao kwa mfano wa Millard Ayo; Lemutuz, Michuzi Blog, wamekuwa wakitumia vizuri mitandao ya kijamii, huwezi ukakuta picha za hovyo, kwa hiyo, naomba niwapongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache napenda kuunga mkono hoja na tuipongeze Serikali na tuiunge mkono kwa mabadiliko ya sheria hizi. Ahsante sana. (Makofi)