Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Khatib Said Haji (43 total)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. FIFA inaitambua TFF kuwa ndio chombo chenye mamlaka ya kusimamia mchezo wa soka Tanzania.
Je, TFF ni Tanzania Football Federation au TFF ni Tanganyika Football Federation? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama jibu ni Tanzania Football Federation; je, TFF ina mamlaka gani juu ya chombo cha ZFA kule Zanzibar? Kama jibu ni Tanganyika Football Association; ni kwa nini hamjaiandikia FIFA na kuiambia kwamba ZFA haihusiki na mambo ya Chama cha Soka cha Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tatizo la baadhi ya viongozi kule Zanzibar kutotii sheria za nchi siyo tu liko kwenye mambo ya siasa, sasa limehamia mpaka kwenye mambo ya michezo. Hivi tunavyozungumza Makamu Mwenyekiti wa ZFA amekipeleka Mahakamani Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), jambo ambalo FIFA wakiamua kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria zao, ni kwamba Tanzania itafungiwa uanachama muda wowote kuanzia sasa.
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya viongozi wa vyama vya soka wasiotii na kuheshimu sheria zilizowaweka kwenye madaraka yao?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, la kwanza, TFF ni Tanzania Football Association na siyo Tanganyika Football Association. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni Tanzania Football Federation na mamlaka yake yanakwenda mpaka Zanzibar… (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Jamani, mbona Mheshimiwa Nape akiongea mnachemka sana upande wa pili? (Kicheko/Kelele)
Mheshimiwa Nape, endelea kujibu maswali.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI. WASANII NA MICHEZO: Wanajua mimi kiboko yao! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ameuliza na ametoa mfano wa viongozi ambao wamepeleka masuala ya michezo Mahakamani. Taratibu za michezo duniani zinajulikana; na kama kuna watu wamepeleka michezo Mahakamani, kwa kweli hukumu yake kwa FIFA inajulikana. Kwa hiyo, tutachukua hatua tuangalie namna ambayo watarudi kwenye utaratibu wa kawaida ili kuepusha kuchukuliwa hatua za kufungiwa michezo.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mwaka 2012 katika Bunge hili niliuliza swali kama hili linalohusiana na Askari wa Jimbo la Konde kuendelea kukaa kwenye magofu yaliyoachwa na Mkoloni. Nataka Mheshimiwa Waziri, unijibu kati ya Mpango huo unaokuja, Jimbo la Konde kujengewa Askari nyumba hizo umo au haumo, kama haumo ni kwa nini?Mpango huo unaokuja, Jimbo la Konde kujengewa Askari nyumba hizo umo au haumo, kama haumo ni kwa nini?
NAIBU WAZIRI YA WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, programu hizi za ujenzi wa nyumba za Askari zinapofanyika zinaangalia maeneo yote ya pande za Muungano. Kwa mfano, mtakumbuka kwamba tulikuwa tuna mradi ambao haujakamilika hata hivyo wa ujenzi wa nyumba kupitia NSSF, kulikuwa kuna nyumba zilizojengwa pia Zanzibar ikiwemo Pemba. Katika mradi huo ambao utatarajiwa kujenga nyumba 4,136 kati ya nyumba hizo nyumba 150 zitajengwa Pemba.
Kwa hiyo, nataka nimtoe wasiwasi tu Mheshimiwa Khatib, kwamba labda baadaye tuonane tuone Konde ni ngapi lakini kati ya nyumba hizo nyumba 150 zitajengwa Pemba. Hata hivyo, huu mradi nimeuzungumza wa muda mrefu wa nyumba 3,500 kila mwaka kufikia 2025, pia utazingatia mahitaji ya sehemu zote. Huu mradi wa nyumba 4,136 utaanza mikoa 17 kwanza baadaye tutamalizia mikoa mingine.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tarehe 25 Septemba, 2015, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilitoa tathmini iliyoonesha kwamba vyombo vya dola vina asilimia 60 ya uvunjaji wa haki za binadamu katika nchi hii na asilimia 40 inafanywa na raia wa kawaida. Hivi Watanzania wamtegemee nani ikiwa vyombo vya dola vilivyopewa jukumu la kulinda usalama wa mali na raia ndiyo vinaongoza katika ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hii? Wamtegemee nani?
Swali la pili, dogo tu. Mheshimiwa Waziri, kule Zanzibar, takribani ni wiki ya pili sasa, kumekuwa na matukio ya maharamia wanaojifunika soksi kwenye nyuso wakisimamiwa na vikosi vya SMZ kufanya uharamia mbalimbali katika Mji wa Zanzibar. Mheshimiwa Waziri, jana alisema hapa hana taarifa, tunamwomba atoe tamko, wananchi wawashughulikie kwa mujibu itakavyofaa kwa sababu ni maharamia ambao huna taarifa kama wanafanya uharamia katika Visiwa vya Zanzibar. Atoe awaambie wananchi wawapige mawe na wachome gari zao moto ili tupate suluhu ya uharamia unaofanywa Zanzibar. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulishauri Bunge hili Tukufu kwamba, sisi Wabunge hapa tumeapa kuitii Katiba na sheria za nchi. Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kabisa kwamba kila mtu lazima aitii Katiba na kufuata sheria za nchi. Sasa hoja anayozungumza Mheshimiwa Mbunge kuhamasisha sheria za nchi zivunjwe siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hawezi akatamka kwamba watu wavunje sheria na sisi Wabunge ndiyo tunaozitunga hizi sheria tunapaswa tuwe wa kwanza kusimamia utekelezaji wake. Kwa hiyo, nashauri kwamba, Mheshimiwa Mbunge hilo tamko analotaka kutoka kwa Mheshimiwa Waziri haliwezekani kwa sababu Waziri hawezi kusimama mbele ya Bunge akahamasisha watu wavunje sheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kuhusiana na hoja yake kwamba, vyombo vya dola vinakiuka haki za binadamu, niseme tu kwamba, kwa kweli vyombo vya dola vimekuwa vikifanya kazi nzuri katika kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu na vinahakikisha kwamba vinafanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo anayo malalamiko au uthibitisho, akayawasilishe katika Tume ya Haki za Binadamu na upo mchakato wa namna ya kuwasilisha malalamiko hayo. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Imekuwa ni kawaida kwa Serikali kuleta majibu mara zote juu ya masuala yanayohusu vituo vya polisi, juu ya usafiri na uchakavu wa vituo hivi wakitoa majibu ya kufanana kwamba hali ya uchumi itakapotengemaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukishuhudia matumizi makubwa na ya nguvu yanayotumika kwa kununua mabomu, virungu, kila wapinzani wanapojaribu kufurukuta kwenye nchi hii. Mnatoa wapi bajeti ya kuwezesha mambo haya yakiwemo yale ya Operation Harass Wapemba kama mlivyofanya karibuni; mlitoa wapi fedha zile; mnaposhindwa kutekeleza mahitaji muhimu ya vituo vya polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba hali ya usalama ya nchi yetu na jinsi ambavyo imekuwa tulivu, ni jawabu tosha kwamba maamuzi ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inatawanya rasilimali zake kulinda ulinzi na usalama wa nchi yetu ni sahihi. Yote hayo yanafanyika kwa wakati mmoja. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa nchi hii wanakuwa salama wakati wa uchaguzi, baada ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunajaribu kuhudumia vituo vya oolisi, nyumba za askari na kadhalika, lakini wakati huo huo inapofika nyakati za uchaguzi tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba usalama wa nchi yetu unaendeleaa kuimarika.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu baadhi ya maeneo ambayo Mkaguzi Mkuu wa Muungano amekuwa akiyafanyia ukaguzi. Kwa nini mpaka sasa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo wa Jimbo, haujawahi kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema ukaguzi wa Mfuko wa Jimbo hufanywa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa pamoja huwa wanashirikiana kufanya ukaguzi huu na Mkaguzi wa Zanzibar, kwa upande wa Zanzibar. Kwa swali lako la kwa nini, nina imani kuwa Mfuko huu utafanyiwa ukaguzi pale muda utakapofika na ukaguzi huo utafanyika.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nikueleze tu kuridhika kwangu na majibu ya Kaimu Waziri Mkuu, majibu yamekwenda shule na yana viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu hayo, kwamba Rais hana mamlaka ya Kikatiba kusamehe watuhumiwa ambao mashauri yao yako katika hatu za kiuchunguzi; katika uongozi wa Awamu ya Nne tulimshuhudia Rais Jakaya Kikwete akitoa msamaha kwa watuhumiwa wa EPA na kutaka walipe na hakuruhusu wapelekwe mahakamani. Je, kutokana na kitendo hicho Rais Kikwete alivunja Katiba ya nchi kwa kutumia madaraka yake vibaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa mujibu wa majibu yako ni dhahiri kwamba watuhumiwa wa EPA bado wanastahiki kupelekwa mahakamani kwa sababu msamaha walioupata haukuwa wa Kikatiba, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuwafikisha watuhumiwa wale wa wizi wa EPA mahakamani ili kukabiliana na tuhuma zao? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali linaloulizwa hapa, lililoletwa mbele ya WIzara yangu ni je, Rais ana mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyetuhumiwa? Na jibu langu ni la Kikatiba, na ninalolisema ndivyo Katiba inavyosema, na mimi si mwanasheria tu lakini vilevile ni mwalimu wa sheria. Ninasema, chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45 Mheshimiwa Rais madaraka yake yako katika kumsamehe mtu ambaye tayari amehukumiwa na amepewa adhabu, inaitwa constitutional…(Makofi)
Kwa hiyo, naomba basi nikueleweshe...
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba makofi yapungue kidogo ili nieleweshe vizuri. Huu msamaha hana Rais wa Jamhuri ya Muungano tu, hata Rais wa Zanzibar chini ya Ibara ya 59 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambapo Rais pale ambapo kuna makosa anaweza akasamehe. Sasa umenitolea mifano miwili, mitatu ambayo Rais aliyepita unasema aliwasamehe watuhumiwa. Mimi kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Rais hakutumia kifungu cha 45 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika imani ya dini ya Kiislam, suala la ndoa na mirathi ni jambo ambalo halina mjadala wala mbadala. Je, mabadiliko yote ya sheria yanatuhakikishiaje kwamba hayataingilia uhuru na imani katika dini ya Kiislam? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu kwa kifupi sana Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ndiyo sababu. Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anakwenda Mahakama ya Rufani akidai si moja kwa moja, lakini kama nilivyowaeleza hapa kwamba mchakato tuliouanza Serikali wa majadiliano sisi Watanzania, maridhiano utumike badala ya sisi kuja na Muswada, wanaosema ndiyo, ndiyo tukapitisha sheria hapa, nadhani nimeeleweka na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nachukua nafasi hii kuishukuru kampuni ya Azam kwa kuleta usafiri huu kati ya Pemba na Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu ni hili kwamba meli hii ya Sealink ni meli kubwa na uwezo wa abiria wa Pemba na Tanga siyo mkubwa sana. Viko vyombo vilivyojaribu kufanya safari za pale lakini vikashindwa kulingana na runningcost zilivyo kubwa sana. Je, ikitokea meli hii imekatisha safari kama zilizotangulia, Serikali itakuwa tayari kukubaliana na mimi kuipeleka meli ya MV Dar es Salaam, ambayo kwa sasa imekaa haifanyi kazi na ni ya Serikali, ikatoe huduma kati ya Pemba na Tanga? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa ajali nyingi zinazotokana na vyombo vya baharini, moja ya sababu ni uzito unaopitiliza katika vyombo hivyo: Ni utaratibu gani unaotumika kujua uzito unaostahiki ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara katika vyombo vya baharini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Sealink 2 ya Azam Marine imefanya utafiti wa muda mrefu, ndio maana imeanza na safari moja kwa wiki na kama wateja wataongezeka wataongeza safari. Kama itatokea kwamba hiyo ikasimamisha, ina maana abiria hakuna wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, kuipeleka MV Dar es Salaam kufanya kazi hiyo, tatizo litakuwa lile lile, kwamba abiria hakuna wa kutosha. Sidhani kama nimemaanisha kwamba Serikali iendeshe meli hiyo ya MV Dar es Salaam kwa hasara, lakini kubwa ni kwamba MV Dar es Salaam haijakabidhiwa rasmi kwa TEMESA. Nadhani tumekuwa tukijibu maswali mengi kuhusu MV Dar es Salaam na hivi tunavyoongea sasa hivi kuna kampuni ya South Africa imekuwa contracted na ile kampuni ya Holland kufanya marekebisho ya ile speed. Ni mpaka pale watakapolikamilisha hilo, ndiyo tutakabidhiwa.
Mheshimiwa Spika, tutakapokabidhiwa tutajua nini cha kufanya, kwa sababu maombi yako mengi. Sasa tunaongelea Tanga, wenzetu wa Mafya wameomba, kwa hiyo, tutaangalia nini muafaka wa kufanya kwa MV Dar es Salaam itakapokabidhiwa rasmi Serikalini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu uzito, tuna taasisi yetu ya SUMATRA ndiyo inayosajili vyombo vyote vya majini na vitu vinavyotumia criteria ya kusajili ni pamoja na uzito wa mizigo, kiwango cha abiria, hivi vyote vinaangaliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, chombo chetu au taasisi yetu ya SUMATRA ndiyo yenye wajibu wa kuhakikisha kila chombo kinachoingia majini kinachukua kiwango cha abiria na uzito unaostahiki. Ndiyo maana kila mahali ambapo meli au boti imesajili, tuna wataalam wa SUMATRA katika maeneo hayo.
MHE. KHATIBU SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi ambayo haiko katika matishio ya kigaidi. Lakini cha kusikitisha sana katika mahabusu walioko magerezani miongoni mwao ni washitakiwa wa makosa ya kigaidi. Hivi nchi isiyo na tishio la kigaidi inawezaje kuwa na mrundikano wa mahabusu wanaotokana na makosa ya kigaidi? La kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri wa Vikosi vya SMZ-Zanzibar na Makamu wa Rais wa Zanzibar wamewahi kunukuliwa wakisema kwamba wamewaleta Masheikh wa Uamsho kutoka Zanzibar ili wanyee kwenye ndoo katika magereza Tanzania Bara. Hapa katika jibu imeambiwa siku 60 inatosha kutoa ushahidi na kama ushahidi haukupatikana watuhumiwa waachiwe huru. Masheikh wa Uamsho wana miaka minne sasa wako katika magereza na ushahidi umeshindwa kupatikana. (Makofi)
Nataka kujua, familia za watuhumiwa wale wanataka kujua, dunia inataka kujua, Wazanzibari wanataka kujua watuhumiwa wale wanawekwa kwa amri ya viongozi wa SMZ au wanawekwa kwa sababu wana kesi ya kujibu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi kwenye jibu (b). Muda wa kisheria wa kuondoa shauri mahakamani kama upelelezi haujakamilika ni siku 60. Maswali yake mawili yote hayapingani na majibu yangu ya msingi kama ambavyo walitaka kueleweshwa Wabunge pamoja na wananchi ambao wanatusikiliza hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kimsingi ni kwamba kesi za hawa watuhumiwa zote ziko mahakamani na kwa mujibu wa sheria zetu hatupaswi kuzungumza mashauri ambayo yapo mahakamani.


WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali alilouliza ni swali mtambuka ambalo liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vilevile Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kusisitiza yafuatayo na siyo lazima upende jibu lake lakini ndiyo ukweli wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nisahihishe kauli hatarishi sana kwa kwamba Tanzania haina tishio la ugaidi. Tumeshakabiliwa na matatizo ya kigaidi, umeshalipuliwa ubalozi wa nchi kubwa sana hapa nchini na baadhi ya Watanzania wamehusika, lakini leo hii tukiona kuna usalama nchi hii tuelewe kwamba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi ndiyo maana huoni hayo matukio mara kwa mara. Naomba nichukue fursa hii kuvipongeza vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ambayo vinafanya kuzima wimbi la ugaidi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ningemuomba Mheshimiwa Haji ajijibu mwenyewe lakini naomba mimi nijibu kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, suala la mtuhumiwa yeyote aliyeko mahakamni ni muda gani kesi yake ataruhusiwa kuendelea kukaa mahakamani kama upelelezi haujaisha? Naibu Waziri ameeleza ni siku 60. Lakini pale ambapo upelelezi haujakamilika Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa analeta maombi mahakamani na inaweza kuongezwa hizo siku lakini siyo hivyo tu, baada ya hapo suala linakuwa chini ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) ambaye kulingana na uzito wa suala lenyewe anaweza akaomba mahakama kuongeza muda na muda utaongezwa. Suala la ugaidi siyo suala dogo, ni suala ambalo upelelezi wake rahisi kwa sababu ni suala la kimtandao. Kutambua huo mtandao wa ugaidi siyo kitu rahisi tu. Usalama wa nchi hii…(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Mbunge leo aliyeuliza swali amekuja salama hapa kwa sababu kuna vyombo vya ulinzi vinamsimamia usalama wake.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimeridhika, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi iliyoridhia Mikataba ya Kimataifa ya Haki na Ustawi wa Mtoto. Kuna
Mkataba wa Convention of the Right of the Child (CRC) wa mwaka 1989 na pia kuna mkataba wa Itifaki ya Nyongeza wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto (African Charter of the Rights and Welfare of the Child) wa mwaka 1990.
Mikataba yote hii inatutaka nchi wanachama kuhakikisha kwamba watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wanapatiwa maisha bora na haki zao za msingi za kuishi kwa mujibu wa mikataba hii.
Je, ongezeko hili la watoto wa mitaani katika nchi yetu, ni jibu tosha kwamba Tanzania imeshindwa kuifanyia
kazi mikataba hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sheria za nchi yetu, Sheria Na. 15 ya mwaka 1984 Ibara ya (6) inasema; “Kila
mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi kutoka kwa jamii kwa maisha yake kwa mujibu wa sheria.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za nchi yetu zinakataza, Sheria za Kazi; Ajira kwa Watoto. Jamii inayopelekea wimbi kubwa la watoto wa mtaani ni kwamba imewasusa watoto, wazazi wameshindwa kuwahudumia
watoto na Serikali inakataza ajira kwa watoto. Sasa watoto hawa wanafanya kazi, siyo kwamba wanapenda, bali kwa kukidhi haki ya kupata maisha yao.
Je, Serikali inatoa jibu gani la miujiza, watoto hawa waweze kuishi huku ikitambua kwamba Sheria za Kazi
zinakataza kupata ajira na huku Serikali imeshindwa kuwahudumia watoto hawa? Je, waishi kwa miujiza gani?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru
sana kaka yangu, Mheshimiwa Khatib Haji kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali imeshindwa kufanyia kazi mikataba hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijashindwa kufanyia kazi Mikataba
ya Kimataifa inayohusu haki za watoto. Kwa taarifa tu, taarifa zetu zote ambazo tunaziwasilisha kwenye Kamati
inayoshughulikia masuala ya haki za watoto katika ngazi ya Umoja wa Mataifa na ngazi ya Afrika, tunapongezwa kwa kazi nzuri ambayo tunafanya katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto ikiwemo uamuzi wa Mheshimiwa Rais kutoa elimu bure, maana yake imewezesha watoto wa kike na wa kiume kupata elimu kuliko zamani. Haki kubwa ya msingi ya mtoto katika kuendelea ni pamoja na haki ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu ajira kwa watoto, kwamba tuna mikakati gani? Kwa mujibu wa Sheria
ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, jukumu la kwanza la kutoa chakula, malazi na mavazi kwa mtoto ni kwa wazazi. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuwataka Maafisa Ustawi wa Jamii wote kuwafikisha katika vyombo vya sheria wazazi na walezi wote ambao hawatimizi wajibu wao wa kuwatunza na kuwalea watoto wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mtoto imesema, pale ambapo mtoto huyo hana mlezi au mzazi, basi ni jukumu
ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kifungu cha 94. Sisi hapa wote ni Madiwani, tunao wajibu wa kuhakikisha Halmashauri zetu zinaweka mikakati madhubuti ya kutoa malazi, chakula, kwa watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu. Kwa hiyo, hilo suala tutaendelea kulihamasisha na kulisisitiza kwa Serikali za Mitaa.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kirithi viwanja vilivyokuwa mali ya Watanzania kutoka kwa wakoloni wakati sasa nchi imekuwa ya mfumo wa vyama vingi; na kwa vile Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuitunza mali hii ya mayatima, ni lini Chama cha Mapinduzi kitarudisha viwanja hivi kwa Halmashauri au Serikali ili irudi mikononi kwa Watanzania wote badala ya kuendelea kudhulumu haki hii ya watanzania?[Neno kudhulumu siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima napenda kuondoa neno kudhulumu na badala yake liwe kuirejesha haki hii kwa Watanzania wote.
NAIBU WAZIRI, HABARI UTAMADUNI SANAA NA
MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna hati yoyote inayoonekana kwamba Chama cha Mapinduzi kimechukua viwanja kutoka kwa mmiliki yoyote, hati zote zinaonyesha ni miliki ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo basi napenda kulithibitisha Bunge lako Tufu kwamba Chama cha Mapinduzi kinavifanyia ukarabati viwanja vyake kama zinavyofanya Halmashauri; kwa mfano uwanja wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Singida Mheshimiwa Martha Mlata anasimamia zoezi hili, upo uwanja wa Mbeya na wenyewe unafanyiwa ukarabati na Chama cha Mapinduzi kwa kushirikiana na wadau. Ahsante.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Swali la kwanza, malengo, dhamira ya kuanzishwa Mwenge wa Uhuru yameonekana kutotimizwa ikiwemo badala ya kueneza upendo Mwenge wa Uhuru umekuwa unaeneza chuki. Mfano, katika Mkoa wa Rukwa hivi karibuni Wenyeviti na Watendaji waliwekwa ndani kwa kosa la kutochangisha wananchi kuhudumia Mwenge wa Uhuru.
Je, kama ni mfano wa kuigwa na katika Afrika na Dunia hakuna nchi iliyotuigiza wakakimbiza Mwenge huu hamuoni kwamba kukimbiza Mwenge sio kuleta maendeleo katika nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili, nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mwenge wa Uhuru historia yake ni kuupamba Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ina historia yake ya kupata Uhuru kutokana na Mapinduzi. Kwa sababu Mwenge sio jambo la Muungano, hamuoni sasa iko haja ya kuacha kuuleta Mwenge huu kule Zanzibar ambapo hatuoni maana yake yoyote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango, uratibu na utekelezaji wa kimfumo na wa kifalsafa wa ukimbizaji wa mbio za Mwenge, huratibiwa kwa kufuata kanuni na utaratibu wa maandalizi uliowekwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Hivyo basi, kama ziko dosari ambazo zimekuwa zikijitokeza eneo moja hadi lingine hazitaki kumaanisha kwamba historia ya falsafa ya Mwenge ile ambayo imejengwa katika misingi ya uhuru wa nchi yetu, eti sasa ndiyo iondolewe kwa sababu ya dosari hizo ndogo zinazojitokeza. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali kwenye dosari ndogo tutaendelea kuzipitia na kuziondoa ili falsafa ya Mwenge wa Uhuru iendelee kubaki kama ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anasema Zanzibar si sehemu ya Mwenge huu wa Uhuru. Nataka kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya matunda mema ambayo yalizaliwa kwa sababu ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimo la Arusha na ukombozi wa Bara la Afrika. Hivyo, kwa sababu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matunda ya Mwenge wa Uhuru, Mwenge huu utaendelea kukimbizwa Bara na Visiwani na utaendelea kuenziwa na Watanzania wote Bara na Visiwani ukiwemo wewe Mheshimiwa Mbunge Haji kutoka Visiwani kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linaenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nichukue nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu waliopotea na chombo baharini, leo ni wiki hawajaonekana, niwaombee Mwenyezi Mungu awajalie kama bado wako hai awafanyie wepesi na kama wamefariki awaweke pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiona azma nzuri ya Serikali katika kupambana na dawa za kulevya; na ninaisifu sana, naipongeza Wizara hii kwa usimamizi mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kukinga ni bora kuliko kutibu, kwa muda mrefu imesemekana na ni ukweli usioshaka kwamba, Zanzibar imekuwa ni lango kuu la kupitisha dawa za kulevya. Tumeona juhudi ya Serikali pale inapowaonea huruma wananchi wake wa Zanzibar katika mambo tofauti mbalimbali yanapojitokeza. Je, ni lini Serikali itachukua kwa makusudi jitihada za kuiweka Zanzibar katika uangalizi maalum wa kukomesha kuwa corridor muhimu ya kupitisha dawa za kulevya ambazo uingiaji wake na matumizi yake makubwa inakuwa ni hapa Tanzania Bara?Ni lini Serikali itaonesha kujali na kuchukua hatua madhubuti kukomesha janga la Zanzibar kuendelea kuwa uchochoro wa dawa za kulevya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na yeye kumpa pole juu ya wananchi wake waliopotea na boti.
Lakini la pili, jibu lake kwenye swali lake ni kwamba nakubaliana na yeye Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ni corridor ya dawa za kulevya, lakini kwenye mikakati ya kupambana na dawa za kulevya kuna maeneo mawili; kuna supply reduction na kuna demand reduction, kwa hiyo, kwenye supply reduction wenzetu wa Tume ya Dawa za Kulevya ambayo inaongozwa na Kamishna Siang’a wanaongoza mapambano kweye eneo hilo na mikakati yao zaidi ni ya kiintelijensia na mambo mengi wanayoyafanya hayasemwi hovyo hovyo. (Makofi)
Kwa hivyo, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Khatib, Tume kwa sasa kwa kweli imepunguza sana supply ya dawa za kulevya kwenye nchi yetu, ikiwemo kule Zanzibar. Na hilo wala halina shaka na huo mfereji unaousema kwa hakika kwa sasa umezibwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye demand ni kutoa tiba na kuwasaidia kwenye impact reduction. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi au makundi katika jamii ambayo yanaajiriwa ajira za mkataba. Kwa mfano, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wabunge wanakuwa na ajira ya miaka mitano na mkataba wao baada ya hapo unakuwa umekwisha. Kama alivyo Mheshimiwa Rais, nembo ya Taifa hili ndivyo alivyo Mbunge nembo ya Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwaacha Wabunge baada ya kustaafu bila kuwapa pensheni na tunajua maisha yalivyo, hamuoni kwamba Wabunge wanadhalilika na makundi ya aina hiyo kiasi ambacho wanashindwa kumudu maisha. Je, ni lini Serikali itafikiria kuliona hili ili Wabunge wanapostaafu nao waweze kupatiwa pesheni? Ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, malipo yote ambayo yamekuwa yakifanywa kwa Waheshimiwa Wabunge yanalipwa kwa mujibu wa sheria, yanalipwa pia kwa kuzingatia masharti ya kazi ya Mbunge ambayo yanakuwa yameandaliwa pia kwa kufuata sheria za nchi tulizonazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wana ushauri, wana jambo linalohusu masuala ya kisheria ya haki na mafao yao Tume ya Huduma za Bunge inafanya kazi kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wote. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuone namna ya kuwasiliana na tume ya huduma ya Bunge ili kuangalia ni kwa kiasi gani yale yanayohusu Wabunge yaweze kushughulikiwa ipasavyo na Tume ya Huduma ya Bunge, ambayo tumeiweka kwa mujibu wa sheria.(Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natangaza interest kwenye suala hili, binafsi. Pili, si kila anayetetea matetemeko ya ardhi kama nyumba yake imeanguka, la hasha; hapa kwenye meza yangu nina memo chungu nzima za Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mheshimiwa Selasini, Waheshimiwa wote wakielezea shida ya jambo hili. Kwa hivyo nikuombe pamoja na uchache wa muda uwape nafasi wenzangu, ili nao wajichawanye kwenye jambo hili. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali, hivi sasa kuna utitiri wa matangazo ya biashara ya dawa za kuongeza nguvu za kiume. Kuna matangazo mengi yanayosambaa nchini kutangaza dawa zinazosaidia tatizo hili, jambo ambalo linaashiria ukubwa wa jambo hili. Sasa, je, Wizara inachukua hatua gani, kwa sababu, utumiaji wa dawa kiholela unazidisha matatizo ya maradhi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kabila moja kila unayekutana naye huko njiani anauza dawa hizi, sijui vipimo hivi wanavipata wapi? Kwa hivyo naomba Wizara itoe tahadhari na kuchukua hatua juu ya dawa za tatizo hili ambazo zinasambaa kila siku ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tendo la raha linahitaji furaha, na kuna taasisi ya World Happiness Report imeeleza kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani wananchi wake waliopoteza furaha. Je, Serikali miaka 50 ya Uhuru kwa nini bado nchi yetu bado iko kwenye nafasi ya 10 mwisho duniani kwa kupoteza furaha, mmekosea wapi? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kukubaliana na Mheshimiwa Khatib Said Haji, kwamba kwa hakika tendo la raha linahitaji furaha. Pia kwa msingi huo changamoto zinazowapata wanaume wa kisasa kwenye tendo hili zinatokana kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa furaha, msongo, lakini pia mwongezeko mkubwa wa magonjwa yasiyo ya kuambikiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni sababu kubwa kuliko sababu nyingine yoyote, kwamba, ukiwa na stress, ukiwa na anxiety, ukiwa na uchovu wa kupitiliza kwa hakika huwezi kuwa na ile furaha na ile hamasa ya kushiriki tendo la ndoa ipasavyo na hii ni sababu mojawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ashangaa sana watu ambao wanahangaika sana kutafuta dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa hayo makabila aliyoyasema ambayo yamekuwa yakizunguka na ku-take advantage ya changamoto hii ambayo inawakumba wanaume wengi hapa nchini kwa sasa kwa sababu pengine hawajui tu changamoto hii inasababishwa na nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii kwanza ni physical, ni changamoto ya kimwili. Kwa hivyo, lazima uwe na afya njema, uwe huna magonjwa, lakini pia hutumii madawa kwa muda mrefu, madawa ambayo yanaweza yakasababisha kupunguza nguvu za kiume, si dawa zote, lakini pia uwe umetulia, uwe una furaha, una amani kwenye moyo wako. Sasa huwezi kuipata hiyo raha unayoisema kama huna hiyo furaha kwa hiyo, nakubaliana na wewe Mheshimiwa Khatib Said Haji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, naomba nitumie jukwaa lako hili kutoa hamasa kwa mara nyingine tena kwa wanaume wote nchini na kwa wanawake vilevile kushiriki kwa kiasi kikubwa kwenye mambo yanayoendana na kulinda afya zetu. Kufanya mazoezi, kula vizuri, kupumzika, lakini pia kufurahi, kucheka, kushirikiana na wenzako, ili kuondoa msongo wa mawazo kwa sababu, msongo wa mawazo, sonono, wasiwasi, ni katika mambo makubwa sana yanayosababisha watu wapate erectile disfunction lakini pia hata wakose watoto wengine, kushika mimba inakuwa ngumu kwa hivyo, naomba nitumie fursa hii kutoa wito huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na utitiri wa matangazo ya dawa za kuongeza nguvu za kiume, Mheshimiwa Waziri wa Afya yuko hapa na amekusikia. Ataamua kutupa mwongozo kama tutoe tamko ama tusitoe tamko, lakini kwa sasa nimetoa hayo maelezo. Niwahamasishe watu tule vizuri, tulale vya kutosha, tufanye mazoezi na naamini kwa kiasi kikubwa tutaepukana na changamoto hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na furaha, kwamba, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi ambazo hazina furaha kwa kiasi kikubwa, sina uhakika na taarifa hiyo kwa sababu, sijaisoma, lakini ukweli ni kwamba, furaha inahusiana na vitu vingi sana katika nchi. Kuna nchi nyingine kwenye katiba zao wameweka kwamba, pursuit of happiness, kuitafuta furaha, ni katika malengo makubwa katika nchi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na sisi ningependa sana tuwe ni wananchi ambao tunapenda kuitafuta furaha kwa kushiriki kufanya kazi za kujiletea kipato, kupunguza stress, kupunguza umaskini, lakini pia kwa kufanya maboresho kwenye sekta ya afya, ili watu ambao watajikuta kwa bahati mbaya wamepata magonjwa, basi waweze kutibiwa vizuri, waweze kupona, warudi kuwa na furaha kama ambapo hawakuwa na magonjwa. Kwa hiyo, ni mambo mengi yanayohusika, mambo ya umaskini, mambo ya afya, mambo ya kijamii, mahusiano na watu, yote haya yanahusiana na furaha kwenye nchi. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nikijibu sehemu ya pili ya swali la kaka yangu, Mheshimiwa Khatibu Kai Haji, Mbunge wa Konde; tuna Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya Mwaka 2002 na kanuni zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria hizo dawa zote za tiba asili au tiba mbadala ni lazima zisajiliwe na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala baada ya kuwa zimethibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na TFDA kwamba hazina madhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tamko langu kwa nchi, yeyote anayeuza dawa za tiba asili ambazo hazijasajiliwa anavunja sheria; tutamkamata na tutamchukulia hatua, ikiwemo dawa za kuongeza nguvu za kiume. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo kauli ya Serikali, wanaofanya hivyo wanafanya kinyume na sheria. Naomba kutumia Bunge lako Tukufu niwatake Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwachukulia hatua wote wanaouza dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo hazijasajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika siku za karibuni kumekuwa na harakati nyingi zinazoonesha kutaka kuleta haki na kuondoa ukandamizaji wanawake na watoto, ni jambo jema. Kwa mujibu wa kitabu chetu cha Qurani waislamu, ni kitabu kisicho shaka ndani yake. Kwa sisi waislamu huu mjadala tu wa kukitilia shaka kitabu cha Qurani, pia tunaingia katika makosa. (Makofi)
Je, Serikali itakuwa tayari kiasi gani katika marekebisho ambayo yanatakiwa sana kuhakikisha hayaingilii imani yetu na kutuendesha, kutupeleka katika dhambi kubwa ya kukitilia shaka Kitabu cha Quran na Sheria zake? Ahsante Sana. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amejitahidi sana kujibu swali hili. Masuala haya ya imani Serikali imeyazingatia sana. Serikali haina dini lakini inaheshimu sana imani za dini. Ndiyo maana tulipotunga Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 zoezi la kuitunga ile sheria lilikuwa shirikishi, watu walishirikishwa wakitoa maoni yao ndiyo ikaja ile sheria. Ndiyo maana hata pamoja na changamoto za wanaharakati kutaka turekebishe ile sheria, tumesema hapana, lazima tuwashirikishe wananchi kwa upana wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuchukua nafasi hii kuwashauri Waheshimiwa Wabunge na wananchi wanaosikiliza kwamba Serikali haitakaa iingilie mambo ya dini. Hili suala linahitaji muafaka. Hata tulipoleta Sheria ya Kadhi hapa, mwaka juzi, hatukuendelea nayo kwa sababu ni masuala yanahitaji muafaka mpana. Kwa hiyo, wananchi muwe na amani. Hili zoezi litafanyika kwa kuwashirikisha. Hatuwezi tukawalazimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa mustakabali wa elimu, bahati nzuri Waislamu wanatambua umuhimu wa elimu, maana hata Mtume alisema kama inawezekana kuifuata huko chini, akaifuate. Ndiyo maana tulitunga ile Sheria ya Elimu mwaka 2016, tukaweka kulinda wanawake hawa wasiolewe waweze kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kwanza Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba mchakato wa Katiba Mpya haujakamilika anakwenda kinyume na dhana ya Mheshimwa Rais ambapo amesema Katiba Mpya siyo kipaumbele chake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali sasa. Swali la kwanza, kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa na tumeona nchi nyingi zimefaidika kwa kuwatumia raia wake walioko nje kwa kuwapatia hadhi ya kuwa na uraia wa nchi mbili.
Je, Serikali haioni kwamba tunapoteza fursa muhimu ambazo tunazipigania kwa raia wetu walioko nje ya nchi kuwa na uraia wa nchi yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amenijibu akisema kwamba Watanzania wenye nasaba watapewa hadhi maalum itakayowatambua lakini hivi karibuni zimetolewa kauli tata na Serikali za kuwavunja moyo na kuwatisha Watanzania walioko nje ya nchi kuhusu umiliki wa mali katika nchi yao ya Tanzania ikiwemo tishio la kuwanyang’anya ardhi na nyumba zao.
Je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kuwatoa hofu na wasiwasi huu uliotokana na kauli iliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba hatuzioni faida zinazoletwa na Diaspora wetu kama tutabadilisha na kuwapa uraia wa nchi mbili, sisi tunasema kwamba hawa watu kwanza hawapotezi haki yoyote. Kama tu watu ambao siyo raia wa Tanzania wanaruhusiwa kuwekeza Tanzania na kwa vile pia kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi sheria hairuhusu lakini bado watu hawa wanawekeza na ndiyo maana sisi kama Wizara tunawahamasisha na tutaendelea kuwahamasisha na kuwajulisha fursa mbalimbali tulizonazo katika nchi hii ili watumie fursa hizo kwa faida yao na familia zao hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba hivi karibuni Serikali au Tanzania imewavunja moyo wale Diaspora walioko nje kwa kuwanyang’anya ardhi, nafikiri nimeshasema na sheria zinasema wazi mwenye kuweza kumiliki ardhi Tanzania ni Mtanzania, ni raia wa Tanzania kwa sheria zilizoko hapa nchini lakini hawanyang’anywi ardhi kama wao ni raia wa Tanzania. Wako raia wa Tanzania ambao wanaishi nje ya nchi hii wanamiliki ardhi na wanaruhusiwa kuwekeza kama raia wengine wowote.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa hakuna shaka yoyote chanzo kikuu cha ongezeko la watoto hawa ni kutokana na wanaume wanaoshindwa kutimiza wajibu wao na kuwaachia ulezi wanawake peke yao. Katika Bunge lililopita nilishuhudia binafsi hapa Bungeni wanawake wakileta watoto waliotelekezwa na Waheshimiwa Wabunge. (Kicheko/ Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kupitia Waziri wa Afya, yuko tayari kutoa wito kwa wanawake wote waliotelekezewa watoto na Waheshimiwa Wabunge wawalete hapa na wakabidhiwe majukumu yao? (Kicheko/ Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, shida siyo kuzaa, shida ni matunzo na kulea na mimi nitoe rai kwa wanaume wote pamoja na sisi Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba tunashiriki kikamilifu katika matunzo na malezi ya watoto. Hata hivyo, nataka tujielekeze zaidi katika mfumo wa sheria na kutengeneza mfumo endelevu. Sheria yetu inatutaka twende katika Ofisi za Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zetu badala ya kuwaleta watoto hawa wote hapa Bungeni. (Kicheko)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sheria Namba 4 ya mwaka 1992 ya Jamhuri ya Muungano inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kimikoa, Kiwilaya na kadhalika kwa kadri anavyoona. Pia Sheria Namba 2 (E) ya mwaka 1997 ya Katiba ya Zanzibar, pia inampa mamlaka Rais wa Zanzibar, kuvigawa visiwa vya Zanzibar Kimikoa, Kiwilaya kwa kadri anavyoona. Je, ni nani aliye na mamlaka zaidi juu ya Zanzibar. Je huu siyo mgongano wa Kikatiba? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yeyote yenye Katiba zaidi ya moja, kama ilivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tofauti na India ambayo ni Muungano una Katiba moja. Tanzania ni sawa sawa na Ethiopia yenye Katiba 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ujue ni jinsi gani unatafsiri na kuisoma Katiba ziko njia kuu tatu; unaangalia Originalism, Textualism na Purposive. Kwa maana hiyo haya ni mambo ambayo pia yamerejewa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Kwa anayeangalia utaratibu wa kuziangalia Katiba mbili zinavyotekelezwa na zinapoonekana zina mgongano kazi ya kwanza ya Mahakama ni kufanya harmonization of interpretation. Hiyo nikusaidie nenda ukasome kesi ya Attorney General versus Butambala iliyoamuliwa na Mheshimiwa Jaji Samatta wa Mahakama ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ukitumia purposive approach hakuna mgongano kati ya Ibara hizo mbili. Maana yake Mamlaka ya Juu Residuary Power inabaki na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni muda gani kisheria jeshi la polisi linaposhindwa kupeleka ushahidi wa kesi unaopeleka mahakamani naweza kupeleka maombi ya kuondoa mashitaka hayo mahakamani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu ndugu yangu Khatib wa kutoka kwetu kule kwa mama, kwamba makosa ya jinai hayana ukomo kwa hiyo, inategemea kosa analolisemea ambalo anaweza akasubiria na akaenda kuomba liondolewe ni aina gani ya makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo kama makosa ni yale ambayo shitaka lake halina ukomo, basi ni vyema kuacha vyombo vingine ambavyo vinatoa hukumu vikatoa hukumu ndipo yeye akatambua kwamba jambo hilo limeshafika ukomo. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. TRA ni chombo cha Muungano na katika suala linalowakera Wazanzibari kwa ujumla wake ni pale wanapotozwa kodi Zanzibar na wakiingia na mizigo yao Tanzania Bara wakatozwa tena kodi mara ya pili. Suala hili limekuwa ni kero moja kubwa sana na Serikali imekuwa ikilipiga danadana kwa kuliingiza kwenye misamiati kero za Muungano, mchakato lakini halifikii mwisho. Naomba Waziri anijibu suala hili la Wazanzibari kutozwa kodi Zanzibar na wanapoingia Bara na mizigo yao wakatozwa tena kodi ni lini litamalizika na kupatiwa ufumbuzi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimwambie Serikali haina dhamira ya kuwapiga danadana wafanyabishara wa Zanzibar. Nimekuwa nikisema hapa Serikali yetu iko committed katika kuwalea wafanyabiashara wetu hasa sekta binafsi kwa sababu tunajua sekta binafsi ni injini ya uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utozaji wa kodi mara mbili na naomba niliweke vizuri sio kodi mara mbili ni kutozwa kodi ambayo iko tofauti kati ya mifumo miwili ambayo inatumika Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara. Katika hili, Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na ZRB wanashughulikia tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisimwambie ni lini kwa sababu ni suala la kimfumo, kipindi watakapokubaliana kutumia mfumo mmoja, tatizo hili litaondoka. Hili linafanyika ili kulinda tu ile fair competition katika soko letu na hili linafanyika kwa nia njema kabisa.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza na mimi nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu kukujalia wewe kurudi hapa katika hali ya afya na uzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nyoyo zetu zimefurahika na nafsi zetu zimeburudika kukuona tena katika kiti chako. Karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri; Tanzania kila mwaka tunakuwa na upungufu wa sukari kutokana na uzalishaji mdogo wa viwanda, lakini zipo taarifa za uhakika kwamba Kiwanda cha Kagera Sugar kimekuwa kikisafirisha sukari kupeleka Uganda kila mwaka.
Je, ni kwa nini sukari haitoshi katika soko la nchi yetu na Kiwanda cha Kagera Sugar kinaruhusiwa kuuza Uganda lakini Zanzibar haitoshi kwa Zanzibar, lakini hairuhusiwi kuleta Tanzania Bara? Kwa nini?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza na mimi niungane na wengine kukupongeza na kukutakia afya njema sana na karibu tena katika Bunge letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba ni kwamba suala la sukari na biashara yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki linayo protocol maalum. Protocol hiyo inaelekeza kwamba bidhaa hii haiwezi kuhama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine bila makubaliano kwanza kupitia katika Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Ndiyo maana hata sukari ikizalishwa namna gani Kenya au Uganda au Tanzania haiwezi kwa kirahisi tu kuvuka mipaka wa Tanzania kwenda au kutoka nje ya nchi hii.
Mheshimiwa Spika, kadri tulivyo na kumbukumbu, Serikali hii hajawahi kumpa kibali Kagera Sugar kupeleka sukari nje ya nchi. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ufanisi na utendaji wa Mahakama unategemea ushahidi katika utendaji wake, lakini imekuwa ni jambo la kawaida ukiwa katika Mahakama zetu mara baada ya kusomwa Shauri Namba, Waendesha Mashtaka kusimama na kuiambia Mahakama tunaomba Mheshimiwa Hakimu au Jaji uahirishe shitaka hili kwa sababu upelelezi haujakamilika, hivyo ni vitu vya kawaida sana.
Je, Serikali kwa kushindwa kupeleka ushahidi haraka katika Mahakama kwa kesi zinazoendelea ndiyo chimbuko la kusababisha mlundikano wa mahabusu katika Magereza yetu na jambo hilo ndilo linalosababisha wananchi wengi kukosa imani na Mahakama na kuona hazitendi haki, je, hamuoni kwamba kuchelewesha kupeleka ushahidi katika Mahakama mnasababisha lawama kwa Mahakama ambazo kimsingi siyo za kwao? (Makofi)
Swali la pili, katika nchi yetu lilitokea tukio kubwa na baya la ugaidi ambalo lilisababisha maisha ya watu wetu kupotea katika Ubalozi wa Marekani pale Dar es Salaam. Kuna watuhumiwa ambao walichukuliwa hapa kwenye nchi yetu na wakapelekwa Marekani kwa ajili ya mashtaka hayo na upelelezi wa makosa hayo, lakini haikuchukua zaidi ya miaka miwili watuhumiwa wale walionekana hawakuwa na makosa na wakaachiwa huru Marekani na Tanzania.
Je, ni kwa nini mpaka leo watuhumiwa wa ugaidi, Mashekhe wa Uamsho kutoka Zanzibar ambao hawakuua hata kuku katika mashtaka yao, mpaka leo mmeendelea kuwashikilia ilihali mmeshindwa kupeleka ushahidi. Mpaka lini Serikali mtaendelea kuwashikilia wazee wa watu wale na mmeshindwa kuthibitisha makosa yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upelelezi ni jambo la msingi ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Lazima Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na kujiridhisha juu ya makosa ambayo yamefanywa na mtuhumiwa ili hatimae mtuhumiwa yule aweze kutendewa haki. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba siyo dhamira ya Serikali wala Jeshi la Polisi kuchelewesha upelelezi, lakini kuna aina ya makosa ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ya ziada ambayo yanahusisha taasisi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kunahitaji kufanyika utafiti kutoka katika vyombo na mamlaka nyingine, masuala ya mawasiliano kwa mfano TCRA, kuna masuala yanayohusu uhamiaji, masuala ya taasisi nyingine mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, ili kuweza kuhakikisha kwamba mtuhumiwa yule anatendewa haki lazima Jeshi la Polisi lipate muda wa kutosha. Hakuna Serikali ama chombo chochote cha Serikali kinachohitaji kumkomoa mwananchi wake, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusiana na suala la watuhumiwa wa Uamsho. Tuhuma ambazo zinawakabili watu hawa ni nzito, kwa hiyo basi ni lazima uchunguzi wa kina vilevile ufanyike ambao utahitaji muda. Kwa hiyo, naomba jambo hili kwa kuwa liko Mahakamani siyo busara kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya nchi hii kulijadili katika Bunge hili Tukufu, tuacha mamlaka husika na mhimili wa dola ufanye kazi yake.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Tunatambua baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita baadhi ya nchi wafadhili zilizuia kutoa misaada yao kwa madai ya ukiukwaji wa uchaguzi wa Zanzibar na makosa ya mitandao hapa nchini. Serikali iliahidi kwamba mazungumzo yalikuwa yanaendelea ili kuhakikisha wafadhili wanaondoa vikwazo hivi. Nataka kujua je, mazungumzo yale yalifika wapi? Je, tumeanza kufaidika na misaada ile kutoka kwa nchi wafadhili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mazungumzo niliyosema yanaendelea sio kati ya Tanzania na nchi wahisani, hapana. Ni mazungumzo kati ya Serikali zetu mbili kuhusu hili. Sina uhakika sana kama kuna nchi zilizositisha misaada yao kwa sababu ya uchaguzi wa Zanzibar, hiyo siyo sahihi hata kidogo. Kitu ambacho kilikuwa kinasababisha mapato haya ya GBS yapungue ilikuwa ni kumalizika kwa muda wa mwongozo wa ushirikiano kati ya nchi yetu na nchi wahisani, ambapo napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba mwongozo mpya tayari umeshapatikana tangu Agosti, 2017 na tumeanza kuutumia kuanzia mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, mapato haya yanaendelea kupatikana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2015, wakati tukienda kwenye uchaguzi mkuu, kila chama kiliuza sera zake kwa Watanzania. Chama cha Mapinduzi kilitangaza sera kuwapatia wananchi wa Tanzania kila kijiji shilingi milioni 50 sera ambayo iliwavutia sana Watanzania. Je, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyoweka kwa Watanzania? Kama haijashindwa, ni lini pesa hizi zitapelekwa kwa vijiji vyote vya Tanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, ni kweli katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 tulieleza bayana ya kwamba moja kati ya mkakati mkubwa wa kuwawezesha wananchi kiuchumi ilikuwa pia ni pamoja na utengwaji wa shilingi milioni 50 kila kijiji.
Mheshimiwa Spika, narejea majibu yangu ya awali kwamba utaratibu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi huwa unakwenda sambamba na utayarishaji wa miundombinu rafiki ya kufanya mpango huu uweze kuwafikia wananchi kwa wakati. Tulijifunza katika mipango iliyopita ikiwa mabilioni ya JK na hivi sasa tunaendelea na mkakati wa kuona namna bora ya miundombinu ambayo itawekwa ili fedha hizi pindi tutakapoanza utoaji wake, ziwafikie walengwa kwa uhakika na pia iende kufanya kazi ambayo itakuwa imekusudiwa.
Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa kwamba ni mpango wa Serikali na bado upo katika mchakato wa kuona namna bora ya kuweza kuandaa miundombinu hiyo.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Jambo hili ni la muda mrefu na limekuwa likijitokeza kila mara. Si aibu wala si ajabu kwa lile linalotushinda tukawa wakweli na tukafanya lingine tunaloliweza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, haikuwa aibu kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hilo limefanyika; na hili la Akaunti ya Pamoja kama linatushinda ni kwa nini lisiondolewe na tukatafuta njia nyingine au utaratibu utakaotuwezesha kuliendesha jambo hili katika mustakabali huo, badala ya kuendelea kuvunja Katiba kwa kutotimiza takwa hili la kikatiba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khatib, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, masuala ya Muungano na zile changamoto zake tulishasema hapa Bungeni, changamoto zile 15 ambazo tulikuwanazo tayari 11 zimeshapatiwa ufumbuzi tumebaki na nne tu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii Akaunti ya Fedha ya Pamoja anayoizungumzia tusipokuwa makini na jambo hili, tusipokuwa na maridhiano, tunaweza tukaingia kwenye matatizo ambayo yatasababisha Watanzania kuanza kusema kwamba, afadhali hata hiyo Akaunti tusingekuwanayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko kwenye uendeshaji wa gari, tunapokuta kuna kibao kimeandikwa hapa uendeshe speed 50 au 80 na sisi hatuna budi kufanya hivyo. Katika jambo hili kuna umakini mkubwa ambao unatakiwa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Khatib Serikali ina dhamira ya dhati na wala hatuna kigugumizi na hatuna sababu yoyote ya kuuaibisha Muungano kwa sababu tulishaungana, haya mambo mengine yote haya tutayashughulikia vizuri. Atupe nafasi kwa sababu tumesema kile kikao kitafanyika, asiwe na haraka. Ahsante sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunitendea haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba Jimbo la Konde na Mji wa Konde ndiyo uliokuwa Makao Makuu ya Wilaya kabla ya mabadiliko yaliyofanyika na kupelekwa katika Jimbo la Micheweni lakini haikuondoa uhalisia kwamba Mji wa Konde ndiyo Mji Mkuu katika Wilaya ya Micheweni hilo analielewa. Pamoja na hilo, bado Mahakama ya Wilaya ya Micheweni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ipo katika Jimbo la Konde na miundombinu hii miaka yote, Mheshimiwa Waziri jibu lake ni hili kwamba Serikali mpaka ipate pesa ndiyo ifanyie marekebisho. Serikali hii hii...
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini hasa Waziri atachukua juhudi za kufanya marekebisho katika Kituo cha Polisi cha Konde ili askari wetu wapate uhakika wa maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khatib, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu linakuwa linafanafana lakini na mabadiliko yanaonekana, maana mwaka jana tulizungumza kwamba tukipata fedha na utaona kwamba mwaka huu tumepata fedha za kurekebisha baadhi ya changamoto hizi za Askari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na eneo hilo kama ambavyo nimemjibu Mheshimiwa Kadika kwamba dhamira ya Serikali ipo palepale na hatua ambazo tunapiga za kupunguza changamoto hizi nchi nzima, hatua kwa hatua na awamu kwa awamu tunazipokea jitihada za Wabunge ikiwemo hata Mheshimiwa Mbunge kama ataamua Mfuko wake Jimbo atoe kidogo fedha kwa ajili ya kukarabati hicho kituo tutamkaribisha sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muunganiko wa nchi mbili na unapotaja viwanda vya Tanzania huwezi kuvitenga viwanda vilivyoko Zanzibar. Nataka kujua ni sababu ipi ya msingi inayoifanya Kiwanda cha Sukari cha Mahonda – Zanzibar kisiruhusiwe kuingiza sukari yake katika soko la Tanzania Bara, sababu ya msingi hasa ni ipi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili swali limekuwa likijirudia mara kwa mara, lakini niseme tu kwamba pamoja na kwamba Tanzania ni moja, suala la ulinzi wa viwanda lipo kila mahali na kama ulivyoona hata Tanzania Bara imerundikana sukari ya kutosha. Kwa hiyo, pengine badala ya kutaka nyingine iingie tushughulikie kwanza hii hali mbaya ya kuingiza sukari ya magendo inayoendelea.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize kwa makini swali langu likukune mithili ya nazi na unipe jibu mfano wa tui. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nakubaliana na maelezo uliyoyatoa juu ya uanishaji wa kukua kwa uchumi wa nchi. Mheshimiwa Waziri lakini katika kipindi hiki ambacho tunashuhudia pato la Taifa likiwa limesimama la dola 976 mpaka mwaka 2016, tunashuhudia upungufu wa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, tunashuhudia bei za huduma zikitetereka mfano majengo ambapo sasa hivi yanakosa wapangaji, tunashuhudia fedha yetu ikiendelea kushuka… (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kuna uhusiano gani wowote ambao unaonesha kweli hali ya uchumi inakua wakati hali ya wananchi kukosa pesa inazidi kuongezeka miongoni mwetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nchi za kiafrika zimeingia katika mtego au mahusiano na China inayosababisha wote kukimbilia kukopa China. Jambo hili linasababisha wanaposhindwa kurejesha mikopo kukamatiwa mali zao na tayari baadhi ya nchi jirani zimeanza kukamatiwa mali zao na kudhibitiwa na China. Je, mnachukua tahadhari gani kwa nchi yetu kuja kutumbukia katika mfumo huo wa kuja kukamatiwa nchi yetu na ikawa koloni la China? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khatib Said Haji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimwambie pato la Taifa halijasimama wala halijashuka. Tumeendelea kuleta taarifa sahihi ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu ukuaji wa uchumi wa Taifa letu, tumeonyesha jinsi gani unakua na nimeonyesha vigezo hivi na kitakwimu Mheshimiwa Khatib tuwasiliane ili nikupatie takwimu ujue taifa letu linakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza amezungumzia wananchi kukosa pesa, naomba nimwambie Mheshimiwa Khatib na Bunge lako Tukufu kwamba money supply kwenye uchumi siyo kigezo cha kukua kwa uchumi wa Taifa. Money supply kwenye uchumi inaonesha kwamba Taifa hilo limeshindwa ku-control ukuaji wa uchumi wake. In short run inaweza ukajidanganya ukuaji wa uchumi upo lakini in long run matatizo na madhara yake ni makubwa sana. Nimpongeze sana Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na wataalam wake wanafanya kazi kubwa kuhakikisha hakuna pesa za ziada kwenye uchumi wetu ili tusiingie kwenye matatizo makubwa ya kiuchumi, hilo ni jibu la kwanza kwa swali la Mheshimiwa Khatib. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lako la pili, hizi ni speculative ambazo zipo kwenye vyombo vya habari. Napenda kumwambia kwamba kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tupo makini sana wapi tunakwenda kukopa, kwa riba ya kiasi gani na kwa nini tunakwenda kukopa. Ndiyo maana sasa hivi Bunge lako Tukufu linajadili Muswada wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma, ni umakini ule ule wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano kuhakikisha Taifa letu linakwenda kuwa salama. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, katika siku za karibuni kumejitokeza tabia chafu, mbaya na ovu kabisa ya mahabusu kufia kwenye Vituo vya Polisi. Mahabusu anapelekwa, wanashikiliwa, wanapata mateso ambayo yanapelekea vifo vyao. Hivi karibuni tu kuna baadhi ya jamii zimekataa kupokea maiti kwenda kuzika kutokana na kufia ndani ya Vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anatoa kauli gani kali ya kukemea tabia hii ambayo inatia aibu nchi yetu ambayo ni ya haki na demokrasia?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa mwananchi kufa, anakufa wakati wowote, mahali popote na ndiyo maana sijui kwenye Qurani, ila kwenye Biblia ukisoma Muhubiri 9:12 ni kwamba kifo ni mtego, kifo humnasa mtu wakati wowote, mahali popote. Kwa hiyo, mwananchi anaweza akafa akiwa polisi, anaweza akafa akiwa anafanya mapenzi, anaweza akafa akiwa kwenye gari anasafiri, anaweza akafia hata humu ndani ya Bunge. Kwa hiyo, isije ikachukuliwa kwamba anayefia kwenye Kituo cha Polisi ni kwamba ameteswa. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ninakiri kwamba kumekuwa na matukio ambapo wananchi wanafia mikononi mwa polisi na pale ambapo matukio hayo yanajitokeza tumekuwa tukifanya uchunguzi na pale inapobainika kwamba polisi wamehusika tumekuwa tukichukua hatua, ndiyo maana tunazuia wananchi wasichukue sheria mikononi za kuanza kuvamia vituo kwa sababu mtu amefia mikononi mwa polisi. Nimekuwa nikihoji huyu anayekufa akifanya mapenzi mbona hawaendi kuchoma kitanda na nyumba kwamba amefia mikononi mwa kitanda? Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Serikali wakati ikitoa ufafanuzi kuhusiana na kukosekana kwa taarifa za matumizi ya shilingi trilioni 1.5 ilielezwa kwamba kati ya fedha zile shilingi bilioni 200 ni makusanyo ya Zanzibar.
Sasa Mheshimiwa Waziri kabla nazo hazijatumbukia katika kero ya Muungano ni lini fedha hizi zitafika Zanzibar? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili liliulizwa wakati tukijadili bajeti ya Wizara yetu ya Fedha na Mipango na sisi kama Serikali tuliacha kulijibu makusudi kwa sababu tunafahamu mchakato wa kujadili hoja hizi za CAG ukoje, itakapokwenda kwenye Kamati ya PAC tukija hapa itajadiliwa kwa kina. Hata hivyo, naomba kusema yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni 203 ni fedha inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania Zanzibar na huwa hazivuki maji kuja Tanzania Bara. Zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kuingia moja kwa moja kwenye akaunti.
Naomba msikilize basi niwape elimu ili tuweze kuelewana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizo hukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania inayofanya kazi zake Zanzibar; na zinapokusanywa fedha hizo zinasomeka kwenye financial statement za Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa sababu zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Fedha hizo hazivuki maji kuja Tanzania Bara, huingia moja kwa moja kwenye akaunti kuu ya Pay Master General Zanzibar. Kwa hiyo, fedha hizo zimekwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya Mlipaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Toka asili bandari bubu ndiyo msaada mkubwa kwa wananchi hususani wa Visiwani baina ya Zanzibar na Mwambao wote huu wa Bahari ya Hindi. Linapokuja suala la bandari bubu na vyombo hivi mara nyingi vinaangaliwa vyombo vya baharini na vyombo vya maziwa vinakuwa vinaachiwa huru. Nataka kujua ni kwa nini bandari bubu ambazo wanazisema lakini zinakidhi viwango mfano Kipumbwi, Kigombe Tanga ambazo zinakidhi viwango hawazirasimishi haraka na kufanya kazi wananchi wakapata tija kwa safari zao?
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, bandari bubu ni bandari bubu tu, hakuna namna ambavyo unaweza ukaifanya ikawa rasmi kwa kuibadilisha kwa maneno. Ni lazima taratibu za Kiserikali na Sheria zifuatwe kuifanya bandari bubu iweze kuwa rasmi. Nimewahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba bandari bubu zote ambazo zinakidhi vigezo tumekuwa tukizitembelea na kutoa elimu na kuwapa mapendekezo mbalimbali Kiserikali ambayo yatasababisha ziweze kuwa bandari rasmi.
Mheshimiwa Spika, Serikali haiwezi kufurahia kuendelea kuwa na bandari bubu na wala hatuwezi kuruhusu bandari bubu ziwepo, kikawaida bandari bubu zote hatuziruhusu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, hizo bandari alizozitaja tutazitembelea, tutaongea na wadau, tukiona zinakidhi vigezo tutazisajili halafu zitakuwa bandari rasmi. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuchelewesha haki ni kunyima haki na si kesi za madawa ya kulevya pekee kuna mashtaka ambayo watuhumiwa wakipelekwa kule ni kama wanasahauliwa. Kuna kesi za ugaidi na kuna kesi …
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni kwa nini mashtaka ya kesi aina hii zinachukua muda mrefu kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa makosa yote ya kijinai na kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 umewekwa utaratibu wa namna gani kesi hizi zishughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hizi zinahitaji umakini mkubwa sana, si rahisi kwa namna yoyote ile kuziharakisha pasipokuwa uchunguzi wake umekamilika. Ndiyo maana nawaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kuvuta subira mamlaka zetu zinafanya kazi sasa hivi kuhakikisha kwamba kesi zinapungua na Mahakama imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kesi nyingi zinasikilizwa kwa wakati ili haki ionekane imetendeka.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza katika hili napenda kwa dhati kabisa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake katika kuhakikisha benki zinaendelea kupunguza riba za mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni kweli benki zimeanza kuitikia wito huu na kipekee niipongeze Benki ya CRDB kwa kuwa wa kwanza kuitikia wito huu. Hata hivyo, inaonekana mikopo ambayo inapewa unafuu wa riba na kwa haraka ni ya wafanyakazi na watumishi wa umma lakini mikopo ya kibiashara bado mabenki yanaonekana kusuasua katika kufikia lengo hilo. Je, Serikali inatoa kauli gani ya kuzitaka benki kushusha riba kwa mikopo ya kibiashara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mara nyingi tu katika Bunge hili nimekuwa nikisema kwamba kiwango kikubwa cha riba katika benki kinatokana na kiwango cha T-Bills ambacho kinapangwa na Serikali BOT. Je, Serikali inatoa kauli gani kuwa riba zinazotozwa na microfinances ambazo ndiyo kimbilio kubwa la wananchi wa kawaida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khatib Said Haji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali kwa nia thabiti kabisa imechukua hatua za kisera na benki zetu za kibiashara kwa kuanza wameanza na mikopo hii ya watumishi. Ni imani yetu kama Serikali benki zitashusha riba kwa wakopaji wote wakiwemo wakopaji wanaokopa kwa ajili ya biashara zao kwa kuzingatia watu hawa wanapatikana wapi na nini wanadhamiria kukifanya. Cha msingi nachotaka kuwaomba wafanyabiashara wetu ni kuwa na mipango thabiti wakati wanachukua mikopo hii ili kuhakikisha pesa wanazokopa zinaweza kurejeshwa na hivyo kuleta imani kwa benki zetu kwa wafanyabiashara wetu kwamba ni wakopaji wa uhakika na ni imani ya Serikali yetu kwamba riba zitaendelea kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba kwa kutambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo, kwa kutambua umuhimu wa Watanzania wanaokwenda kukopa katika microfinances, Serikali yetu ya Awamu ya Tano ilizindua Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo ya Fedha Desemba, 2017. Dhamira kubwa ya sera hii ni kuhakikisha kwanza tunawatambua wakopeshaji kwenye huduma ndogo za kifedha lakini pia kuhakikisha tunawalinda wakopaji kwenye sekta hii ya huduma ddogo za fedha ili wawe na uhakika wanakopa nini na sheria, taratibu na kanuni za utawala bora ziweze kufuatwa hata kwenye sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu inatambua mchango wa bei ya T-Bills. Sasa hivi tumeweza kupunguza bei ya T-Bills kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha pia bei ya fedha zinazokopeshwa inakuwa ndogo.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali langu nililomwuliza, ni kiasi gani cha mgawo wa fedha hizi za FIFA wamewahi kuipatia Zanzibar? Jibu lake, anakuja kusema kwamba kuanzia mwaka huu tutapata 1.25. Kwa hiyo, amekwepa kabisa kunijibu swali langu nililomwuliza. Nataka kujua: Je, mmewahi kuipatia mgawo wowote Zanzibar kutokana na misaada hii inayotoka FIFA?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Nataka nijue, kwa kuwa TFF siyo chombo cha Muungano, Mheshimiwa Waziri wa Michezo sio Waziri wa Muungano na Wizara ya Michezo siyo Wizara ya Muungano; kwa hiyo, anaposema sasa kwamba kuanzia msaada huu unaokuja, mgawo utaenda kwa ZFA na TFF, nataka nijue, mtatumia formula ipi wakati mkijua kwamba masuala ya michezo Zanzibar wana Wizara yao na Tanzania Bara wana Wizara yao: Je, hamwoni hapa kwamba kuna mkorogano ambao kwa miaka yote na ndio maana Zanzibar tunakosa msaada huu wa FIFA?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikianza na swali lake la kwanza, ametaka kujua kwamba, ni kiasi gani? TFF imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa Chama cha ZFA ambacho ni cha Zanzibar. Moja ya miradi ambayo tayari imeshapelekwa ZFA ni ujenzi na ukarabati wa Uwanja wa Gombani ambao uko Pemba. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba TFF imekuwa haipeleki msaada Zanzibar, hapana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambapo ameelezea kwamba suala la michezo siyo la Muungano, nadhani Mheshimiwa Mbunge alikuwa hajaelewa jibu langu la msingi ambalo nimelitoa. Ni kwamba, ZFA ni sehemu ya TFF. Kwa tafsiri hiyo basi, maana yake fedha ambazo zinaletwa TFF zinagawiwa kwa mashirikisho yote ikiwepo ZFA ya Zanzibar, lakini si kwamba, ZFA inaletewa fungu lake peke yake, hapana, kwa sababu, ZFA siyo mwanachama wa CAF, lakini ZFA vilevile siyo mwanachama wa FIFA. ZFA iko chini ya TFF.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwuliza swali alitaka kujua msaada unaopatikana kwa hawa mama zetu wanaokuwa wajawazito Magerezani na kujifungua. Zipo taarifa kwamba wako baadhi ya wanawake wanaoingia wakiwa sio wajawazito lakini wakapata ujauzito ndani ya Magereza. Inaeleweka kwamba walinzi wa wafungwa wa kike ni wanawake, mimba hizi wanazipataje Mheshimiwa Waziri?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna mimba ambazo zinatokea Magerezani. Hilo la kwanza. La pili, mimba tunazozizungumzia ni mimba ambazo mfungwa ama mahabusu anaingia gerezani akiwa tayari kule uraiani anakotoka ameshapata ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kulitokea jaribio hapa kwa Wabunge wakiwa wanataka tuweke sheria au utaratibu wa kuruhusu wenza wa mfungwa anayekuwa Gerezani ili waweze kupata fursa ya kwenda kufunguka wakiwa Gerezani, ya kwenda kujinafasi wakiwa Gerezani, lakini tulisema kwamba kwa sheria zetu na mila zetu, hatuwezi tukaruhusu hali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kuna baadhi ya halmashauri hufanya matumizi ya fedha hizi bila kumshirikisha Mheshimiwa Mbunge, na hayo yako hasa kwa upande wa Zanzibar. Je, Serikali inatoa kauli gani ili waache tabia hiyo mbaya na kujua kama Mbunge ndiyo mhusika mkuu na msimamizi wa Mfuko huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sijui huku Bara lakini kwa upande wa Zanzibar Mheshimiwa Mbunge baada ya kupitisha matumizi ya fedha hizi, halmashauri inakuwa haimshirikishi katika suala lolote tena. Je, mamlaka ya Mbunge katika kusimamia fedha zile kwa upande wa Zanzibar ni ya halmashauri au ni Mbunge anahusika mwanzo hadi mwisho? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, anataka kujua kama fedha hii inaweza ikatumika bila Mbunge kuhusika. Kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi ni kwamba Mwenyekiti wa fedha hii ya Mfuko wa Jimbo ni Mbunge mwenyewe na wametajwa vizuri wajumbe wa Mfuko wa Jimbo, Madiwani wawili kwa kuzingatia jinsia, Watendaji wawili wa Kata au Viti Maalum lakini na mtu mmoja ambaye anakuwa ni kutokana na NG’O katika Jimbo husika, halafu anaongeza na Katibu wa Mfuko huu anakuwa ni Mchumi katika halmashauri husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kuna fedha inataka kutumika, kwa vyovyote vile hata kama Mbunge hatakuwa Jimboni ni lazima Mkurugenzi wa halmashauri hiyo afanye consultation na Mbunge wa Jimbo kama Mwenyekiti na kama hatakuwepo maana yake Mbunge ataridhia labda Diwani miongoni mwa wale Madiwani kwa sababu shughuli haziwezi kusimama ili aweze kufanya kazi hiyo. Miradi inapopitishwa Mkurugenzi kazi yake ni kwenda kupitisha fedha ikatumike na siyo kupanga kwamba ongeza, punguza hiyo hairuhusiwi kabisa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linafanana na la kwanza, kama nilivyosema na naomba nirudie tumepata malalamiko kwa kweli karibu Wabunge wengi hapa wanalalamika. Wakurugenzi wa halmashauri hawana maamuzi katika fedha hizi, hizi fedha zinaenda kwenye vikao na Wabunge ambao ni Wenyeviti wenyewe wanajadili, na inawezekana Mbunge akaenda kwenye eneo A au Kijiji B akasikiliza kero za wananchi au Mwenyekiti wa Mtaa au Mheshimiwa Diwani au wananchi wa kawaida wakalalamika, Mbunge anaweza akasema napeleka shilingi laki tano hapa. Kwa hiyo Mkurugenzi hawezi kubadilisha haya maelekezo ya Mbunge kwa sababu ndiyo uwezo wake. Ndiyo maana inaitwa Fedha ya Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, kwa hiyo, wale Wakurugenzi ambao wana tabia ya kutumia fedha bila Mbunge tunaomba majina yao tutawashuhulikia kwa sababu Sheria imetaja vizuri namna ambavyo wanapaswa kufanya.

Mheshimiwa Spika, tumeelekeza, ukishapitisha fedha hizi kwenda kutumika ni lazima Kamati ya Mfuko wa Jimbo iende kufanya ziara ikakague hiyo miradi kama kweli ipo na kama imetekelezwa na anayetajwa pale ni Mbunge. Hii ni fedha ya Serikali, lazima isimamiwe vizuri na Sheria imeelekeza kwamba Mbunge inawezekana hana fedha mfukoni kutoa lakini kupitia Mfuko huu unaweza ukatamka neno kwa wananchi na roho za wananchi zikapona, ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, makofi kwa majibu ya Serikali kutoka kwa Wabunge yanaashiria kwamba yako matatizo katika uendeshaji na matumizi na usimamizi wa Mfuko wa Jimbo ambao lengo lake mahsusi ni kuhakikisha kwamba Wabunge wanachochea shughuli za maendeleo katika Majimbo yao.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali sisi mtuachie pia twende tukashauriane na Waziri mwenye dhamana ikiwezekana Serikali itoe waraka wa maelekezo tena kusudi kila halmashauri iweze kusimamia utekelezaji wa kisheria wa mfuko huo, lakini vilevile tuwaombe Waheshimiwa Wabunge kama Wenyeviti wa Mifuko hiyo, waone kwamba wana wajibu pia wa kuhakikisha kwamba matumizi ya fedha ya Mfuko wa Jimbo yanafanyika kwa kuzingatia Sheria.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 12 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka kwamba kila mtu anastahiki heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matukio ya vyombo vya habari kuwadhalilisha na kuwasingizia uongo baadhi ya watu na katika watu wanaosingiziwa wengine wana uwezo wa kwenda Mahakamani na wengine ni wanyonge ambao hawana uwezo wa kusimamia hizi kesi Mahakamani. Je, Serikali inatoa msaada gani wa kisheria kwa watu ambao wanadhalilika na kukosa haki za utu wao kutokana na kusingiziwa na makosa kama hayo na vyombo vya habari? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mara kadhaa nimeshuhudia baadhi ya magazeti kama Mwanahalisi na Tanzania Daima yakipewa adhabu mara kwa mara ya kufungiwa kutokana na kuzua au kuonekana wamesema uongo, lakini sijawahi kuona magazeti ya Tanzanite, Jamvi la Habari na Fahari Yetu yakichukuliwa hatua yoyote wakati ni kinara wa kuzua na kudhalilisha watu katika nchi yetu: Kwa nini Serikali haichukui hatua kwa vyombo hivi vya habari na mmiliki wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa ufafanuzi kwa maswali ambayo ameuliza Mheshimiwa Mbunge. Kwanza niseme kwamba kitu ambacho anazungumza siyo kweli kwa sababu sisi kama Serikali tunafanya kazi kwa kusimamia sheria pamoja na kanuni. Mara zote ndani ya hili Bunge tumekuwa tukitoa ufafanuzi kwamba sisi kama Wizara tumekuwa tukichukua hatua kwa magazeti yote ambayo yanakiuka sheria ambazo sisi wenyewe Wabunge tumezitunga ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwenye swali la Mheshimiwa Mbunge ambapo amesema kwamba hatuchukulii hatua magazeti ya Tanzanite, siyo kweli kwa sababu tumeshajibu mara kadhaa humu ndani kwamba tumeshaandikia onyo gazeti la Tanzanite, vilevile hata gazeti la Tanzania Daima pamoja na
kwamba mara nyingi limekuwa likikiuka hizo kanuni, lakini tumekuwa tukiliandikia onyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Sheria yetu ya Habari inazungumza kwamba kabla ya kuchukua hatua yoyote kwa chombo chochote cha habari, cha kwanza tunachokifanya, tunatoa onyo mara ya kwanza, tunatoa nafasi ya mara ya pili na pale ambapo tunaona sasa hali hiyo imezidi, ndipo ambapo tumekuwa tukichukua hatua ya kuweza kufungia hayo magazeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kweli kwamba tumekuwa tuna upendeleo. Sheria haina upendeleo, nasi kama Wizara tumekuwa tukichukua hatua pale ambapo tunaona tumeshaonya mara kadhaa lakini bado hawajajirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

NAIBU WAZIRI YA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida wananchi ambao wamekuwa hawana uwezo wa kifedha wa kupata huduma ya kisheria, wamekuwa wakisaidiwa kupewa huduma hiyo na Serikali kupitia Wanasheria wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, pale ambapo kuna changamoto yoyote ambayo inahusu malalamiko ya kutotendewa haki katika eneo lolote linalohusu sheria, basi mamlaka ya Serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba wamekuwa wakichukua hatua ya kuwasaidia, kuwasikiliza na kuwashauri wananchi ambao wamekuwa wakihitaji huduma hizo za kisheria kwa ajili ya kuweza kufanikisha mashauri yao ama kesi zao mbalimbali aidha iwe Mahakamani ama kesi za kawaida za upatanishi na usuluhishi. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wavuvi wengi walikuwa wanategemea uvuvi wa jongoo bahari kuendesha maisha yao na jongoo bahari ni dhahabu ya baharini. Jongoo bahari sasa hivi anafikia dola 30 kwa kilo moja, lakini Serikali imepiga marufuku uvuvi wa jongoo bahari, tunataka kujua kuna faida gani Serikali inapata kwa kupiga marufuku ya uvuvi wa jongoo bahari hali wananchi wanaathirika kwa kukosa mapato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khatibu, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ni kweli miaka ya hapa karibuni, ilipiga marufuku uvuvi wa majongoo bahari. Majongoo bahari ni miongoni mwa viumbe vilivyokuwa vinatishiwa kutoweka, kwa hivyo kwa kulinda rasilimali hii Serikali ikapiga marufuku katika eneo lote la pwani ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hapa karibuni kama anavyothibitisha Mheshimiwa Khatib na ni kweli, jongoo bahari ni mali na ni mali sana tumeliona jambo hilo na tumeiona fursa hiyo. Mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba wananchi walio wengi siyo tu kusubiri majongoo bahari yale ya asili kwa maana wild animals, sasa tunakwenda katika utaratibu wa kuwafuga pia kwa maana ya mariculture. Tunataka fursa hii ienee katika ukanda wote wa pwani tutafuga majongoo bahari, tutainua mwani, tutainua pia vile vile na mazao mengine ikiwemo kaa ambao wenzetu katika Mataifa mengine kama Uchina wanapenda na wanataka sana. Kwa hivyo Waheshimiwa Wabunge wale wa pwani wakae mkao wa utayari wa kupokea fursa hizi na tuwahamasishe Watanzania wavuvi wa pwani wakae katika vikundi ambavyo vitatusaidia kuwapelekea fursa hii kwa urahisi zaidi.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, mara nyingi tunaambiwa kwamba wale wanaotaka kupunguza mwili ama vitambi wanakatazwa kula aina ya nyama na badala yake wanaelekezwa kula samaki na nyama za kuku, lakini katika hizi nyama za kuku kuna hawa makuku kutoka nje ambao kama yanauzwa kama KFC ambayo yanamapaja kama watu, Mheshimiwa hebu tunataka ushahidi juu ya kuku hawa wa kizungu broilers hasa katika kuongeza vitambi. (Kicheko)

Je, hawana mahusiano ya moja kwa moja kuku hawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ulaji wa kuku broilers kwanza kuku ni katika protini na nimesema na nimesema katika jibu la msingi kuwa protini ni muhimu, protini ziko za aina inyotokana na wanyama na ile protini inayotokana na mimea. Lakini anataka uhakika ya kwamba broilers wanatatizo hilo la kuweza kumfanya mtu awe na kitambi au laa!

Mheshimiwa Spika, hakuna utafiti wa kisayansi unaokwenda kutupelekea kutuambia kuwa broilers wanashida katika afya ya wanadamu, jambo hili liko palepale, ulaji wa kupitiliza unaweza kukupelekea katika hayo matatizo. Lakini naomba niwahakikishie broilers hawana shida yoyote, kinachowafanya broilers wakue ni hormones, ambazo hormones kisayansi ni vitamins. Kwa hivyo sisi wanasayansi tunachokifanya vyakula vya broilers tunaweka vitamins za kutosheleza za kuhakikisha ukuaji wao unakuwa ni ukuaji wa haraka…

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kulinganisha na kuku wa kienyeji.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda nimuulize Mheshimiwa Waziri, umekuwepo utaratibu wa Waafrika wote, kutoka nchi mbalimbali wanapotaka kuja ndani ya Tanzania na usafiri wao binafsi wanaingia kwa kupata permit katika mipaka yetu. Je, ni kwa nini Wazanzibar ambao wanataka kuingia na magari yao Tanzania Bara kwa ajili ya matumizi na kurudi Zanzibar, hawapati ruhusa hiyo na badala yake wamekuwa wanawekewa vikwanzo kuingia na magari yao kwa matumizi binafsi na baadaye kurudi nayo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Khatib, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, amesema vizuri Mheshimiwa Khatib lakini angetusaidia pia kama hata yeye wakati ameingia Tanzania Bara na gari lake alipewa permit kwa ajili ya kuendesha gari lake hilo huku Tanzania Bara?

Mheshimiwa Spika, niliambie Bunge lako Tukufu kwa nini tuko katika mkanganyiko huo. Siku zote naposimama hapa nimekuwa nikisema kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania Bara na Mamlaka ya Mapato Tanzania Visiwani wanatumia mifumo tofauti ya uthaminishaji wa mizigo. Ndiyo maana magari yanapopita Zanzibar kuja huku Tanzania Bara lazima yafanyiwe uthamini upya ili kujiridhisha na kodi ambayo imelipwa ili kuleta fair competition kwenye biashara zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo linafahamika vizuri na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kutoka Zanzibar wengi wao katika hili hawakubaliani. Kwa hiyo, niombe tuweze kukubaliana kwenye jambo hili ili tuondoke kwenye mkanganyiko huu na tuweze kuwahudumia watu wetu vizuri.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, baadhi ya matukio yaliyojitokeza katika baadhi ya chaguzi za marudio ni lile tukio la Wakurugenzi kujificha pale inapotokea wagombea wa vyama vya upinzani wanarejesha fomu na hivyo kuwakosesha sifa ya kuwa wagombea.

Je, Mheshimiwa Waziri amesema Chama cha Mapinduzi kina mbinu nyingi, hii ni moja kati ya mbinu mnayoitumia ili kuhalalisha ushindi wa haramu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, mbinu za CCM ni za ushindi safi siyo ushindi mchafu, kwa hiyo siyo mbinu chafu hizo anazozungumza, ni ushindi safi, mipango, mikakati.

Sasa naomba nirudie kumjibu Mheshimiwa Khatib kwamba Wakurugenzi wala hawajakimbia, hakuna Mkurugenzi aliyekimbia na ndiyo maana maeneo yote ambayo maana yake wagombea wa Chama cha Mapinduzi walikuwa na sifa kuliko wagombea wengine wote na walijua mapema kwamba wasingeweza kuchaguliwa, lakini mpaka leo hatuna taarifa ya nani anayesema Mkurugenzi wa Halmashauri fulani amekimbia na amefungua kesi Mahakamani kudai hiyo haki yake, hakuna hiyo kesi mpaka leo. Kama wamekimbia wangeweza kulalamika, hatuna malalamiko officially. Ofisi ya Rais, TAMISEMI ndiyo inasimamia Halmashauri zote nchini na mamlaka za mitaa, hatuna taarifa ya hiyo kesi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie; Waheshimiwa wananchi wasitiwe hofu na watu ambao wanaogopa siasa za ushindani. Kinachofanyika hapa ni kushindanisha Chama cha Mapinduzi na kazi yake nzuri na vyama vingine ambavyo havijafanyakazi nyingine yoyote na huenda wakifanya ni mambo madogo madogo sana, mambo makubwa makubwa ya Tanzania haya yamesimamiwa na Serikali kwahiyo mnapopeleka wagombea kwanza lazima utegemee mambo mawili, aidha, unashinda au unashindwa. Ukishindwa kubali na ukishinda mshukuru Mungu. Ahsante. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nieleze kuridhishwa na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba wameanzisha kampeni ili kukabiliana na hali hiyo, lakini ukubwa wa tatizo uliopo katika lango lile la kuingilia bandari ya Tanga siyo jambo linalotaka kampeni bali ni jambo linalotaka hatua za dharura ili kuzuia isije ikatokea barabara ile ikabomoka kama ilivyotokea hapo nyuma. Je, Serikali iko tayari sasa kuliona hili na kulichukulia hatua hizo ninazoziomba?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, athari zilizopo katika eneo la Deep Sea Tanga linafanana kabisa na athari zilizopo katika eneo la Sijuu Kijiji cha Msuka Jimbo la Konde Kaskazini Pemba ambalo ndiyo Jimbo langu. Nina hakika Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika huko, kutembelea na kuiona hali ile: Je, Serikali iko tayari kuchukua hatua za dharura ili kuokoa vijiji vya maeneo yale visiendelee kumomonyoka kutokana na athari za kimazingira?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Konde, kaka yangu Mheshimiwa Khatib. Ni kweli kabisa kama anavyosema eneo hili la Deep Sea kuna hatua za dharura ambazo tumeanza kuzichukua mpaka sasa na sasa wataalam wetu wanafanya tathmini na baada ya tathmini hiyo wataleta andiko ofisini ili tuweze kuweka kwenye mifuko yetu ya kimazingira kuhakikisha tunapata fedha kuokoa eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama alivyosema kule kwenye Kijiji cha Msuka kwenye Jimbo lake Konde nilifika na nimhakikishie Mheshimiwa Khatib hatua zote hizi za kufanya tathmini kwenye maeneo haya ambayo yameathirika kwa nchi nzima tunayafanya kwa pamoja na nitafika tena kwa ajili kuhakikisha kwamba eneo hili tunalitatua kama tulivyokuwa tumepanga.