Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Augustino Manyanda Masele (18 total)

MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Mbogwe mwaka 2012 watumishi iliyokuwa Wilaya ya Bukombe walihamishiwa Wilayani Mbogwe lakini hawajalipwa stahiki zao za posho ya kujikimu pamoja na zile za usumbufu.
Je, ni lini watumishi hao watalipwa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, idadi ya watumishi waliohamishwa kutoka Wilaya ya Bukombe kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ni 73 ambao wanadai posho ya kujikimu na usumbufu ya shilingi milioni 164.14. Kati ya madai hayo fedha ambazo zimeshalipwa kwa watumishi ni shilingi milioni 15.15 kwa watumishi 18. Hivyo, kiasi ambacho watumishi bado wanadia shilingi 148. 99.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeomba fedha hizo katika Wizara ya Fedha na Mipango ili kulipa deni hilo kwa watumisi 55 waliobaki. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kufuatilia Hazina fedha hizo ili ziweze kupatikana na kulipwa kwa watumishi wanaodai.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Barabara ya Butengo Lumasa – Iparamasa – Mbogwe – Masumbwe ni barabara muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Mbogwe na Mkoa wa Geita kwa ujumla:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia usanifu wa kina na upembuzi yakinifu barabara hii na hatimaye kuijenga kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Butengo Lumasa – Iparamasa – Mbogwe hadi Masumbwe yenye urefu wa kilometa 95 ni barabara ya mkoa inayounganisha barabara kuu za Isaka – Lusahunga na Usagara – Biharamulo na pia inaunganisha Wilaya za Mbogwe na Chato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haijafikiria kuiingiza barabara hii katika mpango wa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimaye kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kadri ya upatikanaji wa fedha ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 jumla ya shilingi milioni 100 zilitumika katika matengenezo ya kawaida na katika mwaka 2015/2016 kiasi cha shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya kawaida na shilingi milioni 345 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo na kazi zinaendelea.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya barabara, hoteli na airstrips katika Pori la Akiba la Kigosi ili kuweza kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea vivutio vilivyopo katika Pori hili zuri la Kigosi na Muyowosi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mchango wa sekta ndogo ya utalii katika uchumi wa Taifa na maendeleo ya jamii ni mkubwa sana hususan kwa kuongoza katika kuipatia Serikali fedha nyingi za kigeni na pia kuchangia Pato la Taifa kwa ujumla kwa kiwango cha asilimia 17. Aidha, Wizara yangu inaamini kwamba kwa kuboresha miundombinu, vivutio na utoaji huduma, sekta hii inaweza kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na upatikanaji wa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mapori ya Akiba ya Moyowosi na Kigosi yenye jumla ya kilometa za mraba 21,060 yanapakana na Mikoa ya Kigoma, Shinyanga na Geita. Eneo kubwa la mapori hayo ni ardhi oevu ambayo inawezesha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha mwaka kwa ajili ya ustawi wa wanyamapori. Mapori haya ni moja kati ya maeneo ya mkakati ya Wizara katika kuinua utalii wa Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa Magharibi ambapo kwa sasa yanatumika kwa shughuli za utalii wa uwindaji. Aidha, baadhi ya maeneo ndani ya mapori haya yana rasilimali za wanyamapori na uoto wa asili mzuri unaofaa kwa shughuli za utalii wa picha na hivyo kuhitaji uboreshaji wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 3(c) ya Ilani ya CCM 2015 – 2020 inasisitiza juu ya umuhimu wa suala hili na inaelekeza Serikali kuboresha miundombinu ndani ya mapori ya akiba ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya kuhakikisha kwamba mazao yatokanayo na maliasili yanaendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi na fursa za ajira katika kuwaongezea wananchi kipato.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Kwa kuwa Jimbo la Mbogwe limejaaliwa kuwa na madini ya dhahabu na utafiti umekuwa ukiendelea bila uchimbaji kufanyika katika maeneo ya Nyakafuru, Kenegere na kadhalika.
Je, ni lini Wizara ya Nishati na Madini itayaachia maeneo haya na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, eneo la Nyakafuru lenye leseni ya ukubwa wa kilometa za Mraba 17.53 linamilikiwa na kampuni ya Mabangu Mining Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited kupitia leseni PL 5374 ya 2008, leseni hii imeisha muda wake tarehe 23 mwezi wa 10 mwaka huu na kuombewa extension. Hadi sasa mashapo yamefikia tani milioni 3.36 zenye wakia 203,000 za dhahabu yamegunduliwa, na jumla ya dola za Marekani milioni 1.83 zimetumika kufanya utafiti katika eneo la mradi.
Mheshimiwa Spika, eneo la Kenegere lina leseni ya utafiti PL 4582 ya 2007 ambayo imeombewa pia extension kupitia PL 6748 ya 2010. Lakini kuna PL 8329 ya 2012 zinazomilikiwa na kampuni ya Resolute Tanzania Limited ambapo mradi huo kwenye ukubwa wa kilometa za mraba 13.18 upo katika hatua ya upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Spika, kampuni hiyo imetumia zaidi ya dola za Marekani milioni 23 kufanya utafiti na imeainisha mashapu ya dhahabu tani milioni 13 zenye wakia 545,000.
Mheshimiwa Spika, pia eneo la Kanegele lina lesni ya utafiti wa madini PL 10159 ya 2014 yenye ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 6.39 pamoja na leseni ya kuhodhi eneo RL 0014 ya 2014 yenye ukubwa wa kilometa za 2.94, kampuni pia inamiliki na leseni ya kampuni ya Resolute Tanzania Limited kupitia kampuni yake tanzu ya Mabangu. Mipango ya uendelezaji wa mgodi katika eneo hilo inaendelea kwa kuzingatia mwenendo wa bei ya dhahabu katika soko la dunia.
Mheshimiwa Spika, ili kutohodhi shughuli za utafutaji zinazoendelea katika eneo hilo Wizara ilishauriana na uongozi wa Wilaya ya Mbogwe tarehe 20 Aprili, 2015 na kuamua kutenga maeneo ya Shenda kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Aidha, Kampuni ya Resolute Tanzania Limited imeridhia kutoa leseni ndogo tatu katika eneo la Bukandwa.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) walipewa kandarasi ya kujenga Ofisi na Makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe lakini ujenzi huo umesimama.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza tena ujenzi huo na kuukamilisha kupitia TBA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilitenga fedha kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa nyumba 149 za viongozi katika maeneo mapya ya utawala katika mikoa 20 ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba za Wakuu wa Mikoa nne, Wakuu wa Wilaya 21, Makatibu Tawala wa Mikoa nyumba nne, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa nyumba 40, Makatibu Tawala wa Wilaya nyumba 38 na Maafisa Waandamizi nyumba 42.
Mheshimiwa Spika, mkataba wa ujenzi wa nyumba 149 za TAMISEMI ulitiwa saini tarehe 3 Mei, 2014 kati ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama ya shilingi 17,988,016,924.56. Hadi mradi unasimama kiasi cha shilingi 4,169,477,121.62 sawa na asilimia 23.2 kilikuwa kimetolewa kwa ajili ya ujenzi kwa gharama hizo. Kiasi hicho cha fedha kiliwezesha kuanza ujenzi wa nyumba 84 kati ya nyumba 149 za miradi. Katika Wilaya ya Mbogwe mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba nne, zikiwemo nyumba moja ya Mkuu wa Wilaya, nyumba moja ya Katibu Tawala na nyumba mbili za Maafisa Waandamizi kwa gharama ya jumla ya shilingi 500,585,277.70.
Ujenzi wa nyumba hizi kama zilivyo nyumba nyingine chini ya mradi huu umesimama kutokana na ukosefu wa fedha. Mradi huu umepangwa kuendelea kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Serikali imefanikiwa kupeleka umeme katika Wilaya ya Mbogwe kupitia Electricity V na REA lakini huduma hii haijawafikia wananchi walio wengi; Je, ni lini Serikali itaongeza usambazaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi wengi walio tayari kulipia gharama za kufungiwa umeme katika nyumba zao hususan katika Miji ya Masumbwe na Lulembela?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza nchi nzima tangu Mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele-mradi vitatu vya Densification, kwa maana ya vitongoji, Grid Extention kwa maana ya vijiji vyote pamoja na Off- Grid Renewable katika maeneo ya visiwa. Mradi huu unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na umeme ikiwa ni pamoja na vitongoji vyote nchi nzima, taasisi zote za umma, mashine za maji pamoja na visiwa vyote nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Miji ya Lulembela na Masumbwe imewekwa katika utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu utakaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika Miji ya Masumbwe unaojumuisha vijiji vya Budoda, Ilangale, Masumbwe, Nyakasaluma na Shenda; na katika Lulembela unaojumuisha Vijiji vya Bugomba, Kabanga, Kashelo, Mtakuja, Nyikonga pamoja na maeneo mengine. Ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti utapelekwa kwenye maeneo yote yenye urefu wa kilometa 38.7; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 110; ufungaji wa transfoma 20; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wapya 678. Kazi hii itakamilika mwaka 2020/2021 na itagharimu shilingi bilioni 5.18.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Leseni ya utafiti wa uchimbaji wa dhahabu ya Mabangu imechukua muda mrefu sana katika Kata za Nyakafuru na Bukandwe.
Je, ni lini mgodi wa uchimbaji dhahabu baina ya Mabangu na Resolute utaanza uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Nyakafuru (Nyakafuru Gold Mining Project) unahusisha leseni 22 za utafutaji wa Madini zinazomilikiwa na Kampuni ya Mabangu Mining Limited ambayo ni Kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited. Mashapo (deposit) katika mradi huu yamesambaa katika leseni hizi ambazo maeneo yake yana ukubwa ya kilometa 1.4 hadi 25.17. Mashapo yaliyogunduliwa katika leseni hizi kwa pamoja ndiyo yanaweza kuchimbwa kibiashara. Hata hivyo kati ya leseni 22, leseni tisa kampuni imeamua kuziachia.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kampuni ya Mabangu Limited ni Kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited, na kwa kuwa Kampuni ya Resolute Tanzania Limited iliyokuwa inamilikiwa na Golden Pride ya Nzega inadaiwa kodi na TRA, Kampuni ya Mabangu sasa inahusishwa na deni hilo la shilingi bilioni 147.007. Kutokana na Kampuni hiyo kuhusishwa na deni hilo, anayetarajiwa sasa kuwa mbia wa Kampuni ya Manas Resources mwenye jukumu la kufadhili mgodi ameamua sasa kupeleka mbele ufadhali wake.
Mheshimiwa Spika, mpango wa mradi wa Nyakafuru sasa utaanza kuzalishaji dhahabu mwezi Juni, 2019 baada ya masuala ya kodi kukamilika na kupata leseni ya uchimbaji pamoja na mazingira.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Katika Wilaya ya Mbogwe kuna Kitalu cha Kigosi North kilichopo katika Pori la Akiba la Kigosi.
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kulipa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe asilimia 25 ya ada ya uwindaji?
(b) Je, ni lini Serikali italitengeneza greda lililoko Kifura Kibondo Makao Makuu ya Mapori ya Kigosi Moyowosi ili lisaidie matengenezo ya barabara ndani ya mapori haya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kiasi cha asilimia 25 kwenye Halmashauri za Wilaya zinatokana na malipo ya ada ya wanyamapori (game fees) wanazowinda kwenye maeneo yanayopakana na Wilaya husika kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo na uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitalu cha Kigosi North kimekuwa kikitumika kwa ajili ya utafiti wa madini uliokuwa unafanywa na Kampuni ya TANZAM na siyo kwa shughuli za uwindaji wa kitalii. Hali hiyo inafanya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe isipate fedha za asilimia 25 kwa ajili ya uwindaji wa kitalii katika kitalu hicho. Kitalu cha Kigosi East ndiyo kitalu kilichotengwa kwa shughuli za uwindaji wa kitalii kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2018. Hata hivyo, mwekezaji katika kitalu hicho amejaribu kuleta wageni mara mbili mwaka 2013 na 2014 kwa ajili ya kuwinda lakini hakuweza kuwinda kutokana na kuwepo kwa ng’ombe wengi badala ya wanyamapori katika kitalu hicho. Kwa sababu hiyo, hakuna wanyamapori waliowindwa kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2016 kutokana na kuwepo kwa ng’ombe na hivyo kitalu husika kurudishwa Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jitahada za Serikali za kuondoa mifugo katika maeneo yote ya hifadhi, ni wazi kuwa mazingira ya asili pamoja na wanyamapori watarejea na hivyo kuwezesha kitalu hicho kutumika kwa uwindaji wa kitalii kuanza kufanyika. Kufanyika kwa uwindaji wa kitalii katika kitalu hicho kutawezesha upatikanaji wa fedha ambazo zitaweza kuanza kuwasilishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. Wizara yangu inatoa wito kwa Wilaya zote zenye uvamizi wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kuhakikisha mifugo inaondolewa ili kurejesha hadhi ya vitalu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutengeneza greda, Wizara yangu tayari imeshatengeneza greda lililopo Kifura katika Pori la Akiba Moyowosi Kigosi na sasa linafanya kazi.
MHE. AUGUSTINO M. MASELLE aliuliza:-
Ni Sera ya Taifa kuwa na Vituo vya Afya kwa kila Kata, na wananchi katika baadhi ya Kata wamejitahidi kujenga majengo kwa ajili ya vituo hadi kufikia usawa wa renta kwa nguvu zao:-
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo ya vituo vya afya vya Ikobe, Ilolangulu, Kagera na Bukandwe?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Watumishi wa Afya Wilayani Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Maselle lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutelekeza Sera ya Afya ya kuwa na kituo cha afya katika kila kata. Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ina vituo viwili vya afya ambavyo ni Kituo cha Afya Iboya na Masumbwe, vituo vingine viwili vya Nhomolwa na Kagera viko katika hatua ya ukamilishaji wa ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia uhisani wa Canada, Benki ya Dunia na Sweden imetoa kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuboresha na kujenga miundombinu ya vituo vya afya vya Masumbwe na Iboya sawa na shilingi milioni 400 kwa kila kituo ili kuboresha huduma za mama na mtoto. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imetenga kiasi cha shilingi milioni 35 kupitia ruzuku ya Maendeleo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo katika vituo vya afya Nhomolwa na Kagera pamoja na shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la wazazi katika zahanati ya Ilolangulu. Zahanati ya Bukandwe itatengewa fedha katika bajeti ya mwaka wa 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeajiri wataalam wa afya 2509 ambapo kati ya hao 16 walipangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe na watumishi 13 wameripoti na kupangiwa vituo vya kazi. Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa afya kadri wanavyohitimu na kupangwa moja kwa moja kwenye vituo.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Visima virefu vimechimbwa katika Vijiji vya Lugunga na Kabanga (Mkweni) na maji yakapatikana lakini shughuli za ulazaji mabomba na ukamilishaji imekwama. Je, Serikali iko tayari kutoa utaalam na fedha kukamilisha miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mbogwe hadi sasa ina jumla ya watu 137,636 na asilimia 65 wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia miradi ya maji minne ya skimu ya usambazaji maji, visima virefu 20, visima vifupi 460 na matanki 55 ya kuvuna maji ya mvua.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe inategemea kujenga miradi ya maji miwili katika Vijiji vitano ambavyo ni Lugunga, Luhala, Kabanga, Nhomolwa na Nyanhwiga. Mradi mmoja wa Kabanga – Nhomolwa na Nyanhwiga ni kutoka chanzo cha kisima kirefu cha Kabanga nan mradi wa pili ni Lugunga – Luhala ni kutoka chanzo cha kisima kirefu cha Lugunga na utahudumia Vijiji vya Luganga na Luhala.
Mheshimiwa Spika, usanifu wa Mradi wa Kabanga – Nhomolwa umekamilika na uko katika hatua ya manunuzi ili kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi huu. Aidha, miradi wa Lugunga – Luhala bado upo kwenye Halmashauri ya Mbogwe na imetengewa shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuanzia ujenzi wa miundombinu ya miradi hii.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iko tayari kutoa wataalam ili kutatua changamoto za utekelezaji wa miradi hii kulingana na mahitaji.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini mgodi utafunguliwa katika eneo la Nyakafuru Wilayani Mbogwe baada ya utafiti kuchukua muda mrefu kwenye eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Nyakafuru lenye leseni ya ukubwa wa kilomita za mraba 17.53 linamilikiwa na Kampuni ya Mabangu Limited Resources, kampuni ambayo Kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited kupitia leseni ya kutafuta madini PL Na.5374 ya mwaka 2008. Leseni hiyo ambayo ilihuishwa mara mbili na baadaye kuongezewa muda wa kipindi cha miaka miwili yaani extension kuanzia tarehe 24 Oktoba, 2016 ili kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na itamaliza muda wake tarehe 23 Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 yaani The Written Laws Miscellaneous Amendment Act 2017 yaliondoa uhitaji wa leseni ya utafutaji wa madini kuongezewa muda wa kufanya utafiti baada ya muda wa leseni kuhuishwa kwa mara ya pili kumalizika. Kwa sasa sehemu ya eneo hilo la leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa mashapo yanayofikia takribani tani 3.36 yenye dhahabu ya wakia 203,000 yamegunduliwa na jumla ya Dola za Kimarekani milioni 1.83 zimetumika kufanya utafiti katika eneo la mradi. Aidha, Tathmini ya Athari ya Mazingira ilishafanyika na kupewa cheti cha tarehe 16/10/2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, Kampuni ya Mabangu Mining Limited kupitia Kampuni mama ya Resolute (Tanzania) Limited inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kiasi cha jumla Sh.143,077,421,804 ikiwa ni deni la kodi ambalo wanatakiwa kulilipa. Mgodi wa Nyakafuru unaweza kuendelezwa baada ya deni hilo kuwa limelipwa.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliweka kiasi cha shilingi bilioni 1.5 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kuanza kujenga hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, kutokana na ukomo wa bajeti uliowekwa, fedha hiyo iliondolewa katika bajeti:-
Je, Serikali itakuwa tayari kutenga fungu maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliweka kipaumbele na kutenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe lakini kutokana na ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 bajeti hiyo haikupatikana. Hata hivyo, Serikali imetoa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo viwili vya Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ambavyo ni Iboya kilichopokea shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Masumbwe kilichopokea shilingi milioni 400 pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, katika Mkoa wa Geita, Serikali imeweka kipaumbele na kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya Wilaya Nyang’hwale ambapo zimetengwa jumla ya shilingi bilioni tatu.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Pori la Akiba la Kigosi Moyowosi linakabiliwa na tatizo sugu la kutokuwa na barabara za uhakika kwa ajili ya shughuli za utalii na doria.
• Je, ni lini Serikali italifufua greda aina ya katapila lenye namba za usajili ST 892 lililosimama kufanya kazi tangu mwaka 2015 ili lisaidie kukarabati barabara?
• Kwa kuwa gari aina ya Grand Tiger linalotumika kwa shughuli za utawala limekufa, je, ni lini gari hilo litatengenezwa au kuleta gari lingine ili lisaidie shughuli za utawala katika Pori la Kigosi Moyowosi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua umuhimu wa barabara na miundombinu mingine katika hifadhi zetu ili kuimarisha utalii na kufanya kazi za doria ipasavyo. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali iliamua kufufua mtambo, hususani greda lililokuwa limeharibika kwa muda mrefu katika Pori la Akiba la Moyowosi Kigosi ili liendelee kutumika kuimarisha barabara zilizopo ndani ya pori hilo. Greda hilo aina ya katapila lenye namba za usajili ST 892 limetengenezwa na linafanya kazi.
Aidha, Wizara ipo katika harakati za kufufua gari aina ya Grand Tiger ambalo hutumika kwa shughuli za utawala katika Pori la Akiba Moyowosi Kigosi ambapo mafundi wameshafanya tathmini ya ubovu wa gari hilo na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya matengenezo hayo.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Serikali iliahidi kuanza utekelezaji wa mradi wa umeme wa ujazo (Densification) Mkoani Geita kuanzia mwezi Oktoba, 2018 lakini hadi sasa mradi huo haujaanza:-

Je, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa katika Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya tatu ya mradi kabambe ya kusambaza umeme vijijini unahusisha mradi wa ujazilizi (Densification) kwa kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji ambavyo vimeshafikishiwa umeme lakini baadhi ya Vitongoji havijafikiwa na umeme. Mradi wa Grid Extension unahusu kupeleka umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme na mradi wa Off- Grid electrification wa kuendeleza na kusambaza nishati jadidifu katika maeneo yaliyo mbali na Grid ikiwa ni pamoja na visiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikamilisha kupeleka umeme katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa ujazilizi mwezi Septemba, 2018 katika awamu hiyo Vijiji na Vitongoji 305 vya Mikoa ya Arusha, Iringa, Mara, Mbeya, Njomba, Pwani, Tanga na Songwe ambapo jumla ya wateja 29,950 wameunganishiwa umeme na gharama ya mradi ilikuwa ni shilingi bilioni 68.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya mradi ya ujazilizi utapeleka umeme katika mikoa 26 Tanzania Bara katika Vitongoji 1,103 vikiwemo Vitongoji vya Wilaya ya Mbogwe kwa kuunganishia umeme wateja wa awali 69,079. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 197.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi utaanza mwezi Machi, 2019 kwa muda wa miezi 12.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga shilingi bilioni 23.9 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 52 na Hospitali 27 za Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ni miongoni mwa Hospitali hizo 27 na imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Mikoa ya Kanda ya Ziwa imeathirika na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu mkubwa wa mazingira:-

Je, ni lini Serikali itajenga vyuo vya uhifadhi wa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira na elimu ya utalii hasa baada ya kuanzishwa kwa hifadhi za Taifa Burigi- Chato, Kigosi, Ibanda – Rumanyika, Rubondo na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina vyuo vinavyotoa mafunzo katika fani za uhifadhi wa wanyamapori, utalii na misitu ambapo uhifadhi wa mazingira ni sehemu ya mafunzo hayo. Mafunzo hutolewa katika ngazi za astashahada, stashahada, shahada na elimu nyingine za juu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Chuo cha Pasiansi kilichopo Kanda ya Ziwa katika Mkoa wa Mwanza kinatoa Astashahada ya awali ya uhifadhi wa wanyamapori na himasheria, na Stashahada ya uhifadhi wa wanyamapori na himasheria, Chuo cha Wanyamapori - MWEKA kilichopo Kilimanjaro, kinatoa Astashahada na Shahada ya uhifadhi wa wanyamapori na utalii. Chuo cha mafunzo ya Uhifadhi wa maliasili kwa jamii - Likuyu Sekamaganga kilichopo Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Namtumbo kinatoa mafunzo kuhusu mbinu za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa askari wanyamapori wa vijiji (VGS), viongozi na wajumbe wa Kamati za Maliasili za vijiji.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Chuo cha Misitu Olmotonyi kinatoa mafunzo yanayohusu misitu katika ngazi za astashahada na stashahada pamoja na mafunzo ya ufugaji nyuki katika chuo cha Ufugaji Nyuki – Tabora. Vilevile, Wizara kupitia Chuo cha Viwanda vya Misitu kilichopo Moshi hutoa mafunzo ya teknolojia ya viwanda vya misitu katika ngazi ya astashahada ya awali, astashahada na stashahada.

Mheshimiwa Spika, pia Wizara kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii inatoa mafunzo ya utalii, ukarimu na uongozaji watalii katika ngazi za Astashahada na Stashahada.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha vyuo vilivyopo na haina mpango wa kujenga chuo kipya ili kukidhi mahitaji ya nchi nzima.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Kampuni ya Mabangu ina leseni ya utafiti wa madini katika maeneo ya Nyakafuru, Bukandwe na Kanegere Wilayani Mbogwe; kampuni hiyo inafanya utafiti kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya Resolute lakini utafiti huo umechukua muda mrefu.

(a) Je, ni lini kampuni hizo zitafungua mgodi katika eneo lao la utafiti?

(b) Kama kampuni hizo zimeshindwa kuanzisha mgodi; je, Serikali iko tayari kuona uwezekano wa kuligawa eneo hilo kwa wachimbaji wadogo wa Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Nyakafuru, Bukandwe na Kanegere katika Wilaya ya Mbogwe yana leseni ya utafiti mkubwa yenye ukubwa wa kilometa za mraba 17.53 inayomilikiwa na Kampuni ya Mabangu Mining Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited kupitia leseni ya utafutaji wa madini namba PL 5374/2008. Leseni hiyo ilitolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 1998 tarehe 24/10/2008 kwa kipindi cha miaka tatu ya awali.

Aidha, kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010, leseni hiyo ilihuishwa kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka mitatu na mara ya pili kwa miaka miwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwaka 2016 kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, leseni hiyo iliongezewa muda (extension) kwa kipindi cha miaka miwili ili kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu kabla ya kuwasilisha maombi ya leseni ya uchimbaji na hivyo leseni hiyo kumaliza muda wake tarehe 23/10/2018. Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 eneo la leseni hiyo limerudishwa Serikalini baada ya kumaliza muda wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi katika eneo la Nyakafuru Wilayani Mbogwe utafunguliwa baada ya kampuni yaMabangu Mining Limited kuomba leseni ya uchimbaji wa madini kwa mujibu wa sheria na endapo Serikali itaridhia maombi hao, leseni itatolewa na shughuli inaweza kuanza, ahsante.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Mbogwe wanapata changamoto kubwa katika kupata huduma za kimahakama kwa kuzifuata Wilaya za jirani:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Wilaya Mbogwe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uhaba wa majengo ni moja ya changamoto inayoikabili Mahakama ya Tanzania. Mahitaji ya Majengo ya kuendeshea shughuli za Mahakama hapa nchini ni makubwa. Kwa msingi huo, Mahakama imejiwekea utaratibu wa kujenga majengo haya kwa awamu kulingana na mpango wa ujenzi na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Mbogwe ni miongoni mwa Majengo ya Mahakama za Wilaya 33 yaliyopangwa kuanza kujengwa mwezi Juni na kukamilika mwezi Disemba, 2020 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Kwa sasa Mahakama ipo katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za awali ili ujenzi wa majengo hayo uanze kwa muda kama ilivyo katika mpango wa Mahakama. Tayari Mshauri Elekezi amefanya mapitio ya michoro na ujenzi unatarajiwa kuanza kama ilivyopangwa.