Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Augustino Manyanda Masele (46 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii mchana huu ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa hapa Bungeni tarehe 20 Novemba, 2015. Waswahili husema, ada ya muungwana ni vitendo, Mheshimiwa Rais kauli hii ameenda nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais alipokuja hapa Bungeni alizungumzia mambo mbalimbali na kutoa mwelekeo wa Serikali yake itakavyofanya kazi. Baada ya hapo tumeona hakika kwamba anafanya kulingana na jinsi anavyosema. Tunampa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Mbogwe kwa kuniamini kwa mara ya pili niwawakilishe katika Bunge hili. Nasema ahsate sana na naahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imempata kiongozi na imempata muungwana ambaye hakika anajua matatizo ya nchi hii. Sisi Wabunge na wananchi kwa pamoja tunachotakiwa kufanya ni kumuunga mkono moja kwa moja ili aweze kufanya kazi zake na tufanye lile ombi lake la kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili amtie moyo na nguvu aweze kuzitekeleza ahadi zote alizoziahidi na kuitendea haki Ilani ya Uchaguzi ya chama chetu, Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kwenye kampeni zake na katika kauli zake amekuwa akisisitiza sana juu ya suala la kuwa na nchi yenye viwanda. Nchi yetu ili iwe na viwanda ni muhimu kuwa na umeme wa uhakika. Jambo hili linawezekana kwa sababu ameweka jembe katika Wizara hii, Waziri Mheshimiwa Profesa Muhongo ambaye kila mmoja ni shahidi wa kweli juu ya utendaji kazi wa mtu huyu. Mtu huyu tumuombee kwa Mungu aweze kutimiza ndoto zake juu ya taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda haviwezekani bila ya kuwa na umeme wa uhakika. Ukiwa na umeme wa uhakika utakuwa na uwezo wa kuweza kuvutia wawekezaji wa viwanda kutoka ndani na nje ya nchi. Kwa ajili hiyo ndugu yangu Mheshimiwa Muhongo Mungu akutie nguvu uweze kuitendea haki nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ya Tanzania kijiografia ni nchi ambayo imebarikiwa na Mwenyezi Mungu. Tunazo rasilimali mbalimbali, tunayo bahari, ardhi ya kutosha, anga la kutosha, maliasili za kila aina na wanyama wa kila aina. Kwa ajili hiyo, utajiri huu tukiutumia vizuri na tukienenda sambamba na Rais wetu, hakika tutafika haraka kwenye Tanzania ya watu wenye maisha ya kipato cha kati. Tunachotakiwa kufanya ni kupiga kazi na kushirikiana kwa pamoja kupiga vita rushwa na aina mbalimbali za uzembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la viwanda bila mawasiliano haliwezekani. Kwa maana hiyo, niiombe Serikali itilie mkazo ujenzi wa bandari katika bahari zetu, katika maziwa yetu na kuimarisha reli. Reli ndiyo usafiri wa uhakika wa kuweza kusafirisha mizigo mingi inayotoka nje ya nchi na inayotoka ndani ya nchi kwenda nje ya nchi. Ili reli yetu iweze kufanikiwa kufanya kazi zake vizuri basi ni vizuri tukawa na treni, ikiwezekana kama umeme utakuwepo ziwepo reli za umeme. Maana umeme ukishakuwa wa uhakika maana yake tutakuwa na treni zinazoendeshwa kwa umeme, zitapunguza muda wa kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kwenda katika nchi za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niishauri Serikali itekeleze kwa wakati ujenzi wa reli ya kutoka Isaka - Msongati - Kigali nchini Rwanda. Kwa sababu nchi yetu iko vizuri kijiografia na wenzetu hawa wa Rwanda, Burundi, Mashariki ya Congo tumepakana nao. Kwa maana hiyo uchumi wa nchi hizi unaweza ukainufaisha nchi yetu kwa uzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la elimu. Nchi yetu ili iweze kuendelea kwa uhakika ni vizuri tukawa na vijana wasomi ambao watahusika katika uendeshaji wa viwanda. Kwa maana hiyo suala la teknolojia ni jambo la muhimu na la msingi sana. Kwa maana hiyo, watu wa COSTECH, kwa maana na Commission for Science and Technology tunatakiwa tuwape nguvu na kuwapa kipaumbele ili waweze kutoa vijana ambao watakuwa wameelimika vizuri na katika vyuo vikuu mbalimbali masomo ya sayansi tuyape kipaumbele. Tutakapokuwa na wasomi wazuri hata viwanda vitakuwa vinaweza kuajiri watu ambao wana weledi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu mfano, katika nchi hii migodi imekuwa inafanya kazi vizuri kutokana na wataalamu wa Kitanzania lakini management tu ndiyo unaweza ukakuta wamepata kutoka nje. Kwa mfano, katika mgodi wa Mkoa wa Geita pale GGM, Watanzania wengi wanafanya kazi pale na wanafanya kazi nzuri. Hata Mgodi wa Tulawaka ambao ulichukuliwa na Serikali, Watanzania wanafanya kazi pale ya uzalishaji wa dhahabu, kwa kweli inaonekana Watanzania tunaweza, kwa maana hiyo tujipe moyo na tujitahidi tu kujiamini kwamba tunaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwa mara nyingine nchi hii imejaliwa kuwa na neema ya maji basi maji ya Ziwa Victoria ambayo yamefika katika Wilaya ya Kahama kutoka Mwanza, tunaiomba Serikali itoe fedha kwa ajili ya kuyafikisha katika Wilaya yetu ya Mbogwe ambayo iko umbali wa kilomita 60 tu kutoka maji ya Ziwa Victoria yalipofikishwa. Itakuwa ni jambo la kheri na inaweza ikatusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo mara zote yamekuwa yakisababisha ukame katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Kwa hiyo, kupatikana kwa maji ya Ziwa Viktoria katika Wilaya yetu ya Mbogwe inaweza ikawa ni ufumbuzi wa muda mrefu wa tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niiombe Serikali kwa wakati wake izisaidie halmashauri, wilaya na mikoa mipya ili ziweze kujenga ofisi zake kwa wakati na tuweze kupiga hatua kama ilivyo katika mikoa mingine.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masele ahsante.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hii hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango inayohusu Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Spika, mipango ndiyo msingi wa maendeleo. Kusipokuwa na mipango kutakuwa na ubabaishaji. Kwa maana hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuja na Mpango mzuri wa Maendeleo wa miaka mitano ambao ndiyo utatuongoza katika uhai wa Bunge letu la Kumi na Moja. Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, katika hotuba yake ameonesha vipaumbele mbalimbali ambavyo vinatuongoza katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa nchi ya watu wa kipato cha kati. Mikakati yenyewe utaiona katika ukurasa wa 25, ambapo amesema Serikali imeweka mikakati ya kujenga na kuboresha miundombinu wezeshi na mambo mbalimbali ambayo ameyasema hapo.
Mheshimiwa Spika, napenda zaidi nijikite katika suala la mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga. Ulimwenguni pote maendeleo tumeyasoma katika historia na katika vitabu mbalimbali yanasema dhahiri kwamba mageuzi yalitokana na ugunduzi wa moto na ugunduzi wa chuma. Sasa makaa ya mawe yanahusika na uzalishaji wa chuma. Uzalishaji wa chuma hapo hapo tunapata chuma na umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sasa Serikali ikiwezekana ilitazame vizuri suala la mradi huu, kwa sababu inaonekana uko katika sehemu mbili; unaweza ukainufaisha Wizara ya Nishati na Madini na vilevile Wizara ya Viwanda. Kwa bahati mbaya sana, inaonekana mkazo hauwekwi katika kuhakikisha kwamba huu mradi wa chuma wa Liganga unafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kwa vipi Serikali imeweza kufanikiwa kujenga lile bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam ikaacha kitu muhimu cha kufanikisha uchimbaji wa chuma? Hiki chuma kinaweza kikatusaidia katika mapinduzi ya viwanda. Maana viwanda vinajengwa kwa kutuma chuma, reli tunaweza tukaijenga kwa kutumia chuma hicho hicho, bandari, madaraja na kila kitu, nondo mbalimbali zinaweza zikapatikana kutokana na chuma. Hata sasa hivi nchi hii ina maradhi na cancer mbaya sana ya vyuma chakavu. Watu wanachukua vyuma kutoka kwenye madaraja, kwenye kila sehemu na matokeo yake sasa kunakuwa na uharibifu mbaya sana kwenye miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kurahisisha na kuweza kuzuia watu kutoka kwenye eneo la kwenda kuchukua vyuma chakavu katika maeneo ya barabara; unakuta alama za barabarani zinaondolewa, madaraja yanabomolewa; ili watu waweze kuchukua vyuma kwenda kuuza kama vyuma chakavu, kwa nini Serikali isije na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba chuma cha Liganga kinachimbwa na upatikanaji wa vyuma hivi ukawa ni mwepesi ili kuweza kurahisisha viwanda vya aina mbalimbali; vidogo, kwa vya kati na vikubwa viweze kujengwa katika nchi yetu?
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la reli ya kati. Reli ya kati ni reli ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yetu na sehemu ya kupumulia kwa Bandari ya Dar es Salaam. Bandari yetu ya Dar es Salaam ina changamoto kubwa, kwa sababu ndiyo lango kuu la uchumi wa nchi hii pamoja na nchi jirani ambazo ni landlocked, kama nchi ya Congo, Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi mpaka Uganda; watu hawa wanategemea Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, badala ya Dar es Salaam kutegemea tu barabara itakuwa kwa kweli inazidiwa kimashindano na bandari nyingine za nchi jirani. Kwa maana hiyo, naunga mkono kwa dhati kabisa ujenzi wa reli ya kati na reli nyingine zote zinazokwenda kaskazini huko, Arusha na Kilimanjaro pamoja na reli mpya ya kutoka Mtwara kwenda Mbambabay. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ifanye kila linalowezekana hata kama ni kwa kukopa, pamoja na kwamba deni linaonekana linaongezeka kuwa kubwa, naamini kwamba hawa watakaokuja kuwepo, watakuja kulipa wakati utakapotimia, lakini fedha tunazozikopa tuziweke katika vitu ambavyo tuna imani kwamba vitakuja kuwa ni vya kudumu na wao watakaokuja kulipa walipe wakijua kabisa kwamba sisi tuliokuwepo tulisimama vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua Serikali inayo mpango mzuri wa kujipanga kukusanya mapato na tunaamini kwamba nia njema hiyo itaungwa mkono pamoja na Bunge letu Tukufu na naamini kabisa kwamba tutaweza kufanikiwa kwa kutekeleza hii mipango ambayo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije katika suala la utalii. Habari ya utalii inaeleweka wazi kwamba ndiyo imekuwa ni chanzo cha fedha za kigeni. Kwa ujumla nashukuru kwamba, Serikali imefanikiwa kuwa inaboresha huduma hizi za utalii na matokeo yake watalii wanazidi kuongezeka. Vile vile nina changamoto katika mapori ya akiba ambayo yapo katika nchi hii. Mojawapo ya pori, lipo katika Wilaya yangu ya Mbogwe, pori la Kigosi Myowosi, tumechangia na Mkoa wa Kigoma pamoja na Wilaya nyingine za jirani za Kahama na Bukombe.
Pori hili Serikali ni sawa na kama imelitekeleza na matokeo yake sasa kunakuwa na shida, vurugu za kila aina kwa sababu wananchi wanapeleka huko mifugo kupata malisho, lakini ukiangalia Serikali yenyewe haijaweka miundombinu wezeshi ya kuweza kuwafanya wananchi waweze kuona kwamba kuwepo kwa hili pori kuna faida kwao, kwa maana ya utalii lakini badala yake wanaona ni bora waingize mifugo yao mle na wakati mwingine hata kulima kwa sababu Serikali yenyewe ambayo imelitenga hailiendelezi.
Kwa hiyo, nashauri tu kwamba, Serikali kama kweli ina nia njema, basi ile mamlaka ya mapori ya akiba ambayo tuliambiwa kwamba sheria yake italetwa hapa Bungeni, basi ije haraka ili iweze kutusaidia kujua kwamba kweli haya mapori sasa Serikali ina chombo kinachoyaangalia na kuyaendeleza.
Mheshimiwa Spika, niseme kuhusu suala la maji ya Ziwa Victoria, Wilaya yetu ya Mbogwe na Mkoa wa Geita tuko karibu na ziwa victoria na kwa maana hiyo nashauri kwamba uwepo mpango kabambe wa kuweza kuzipatia Wilaya zilizo jirani na hili ziwa huduma ya maji kutoka katika Ziwa Victoria. La mwisho, nizungumzie habari ya Wilaya na Mikoa mipya ambayo Serikali imeanzisha kama maeneo mapya ya utawala ili kuweza kuhudumia wananchi kwa karibu zaidi.
Mikoa hii na Wilaya hizi zinazo changamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa ziingizwe katika mpango wa miaka mitano ili kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao wamesogezewa hizi huduma, wajisikie kwamba kweli Serikali inawatendea haki. Kwa ajili hiyo, basi kuwe na mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba zinatengwa fedha madhubuti kwa ajili ya ujenzi wa huduma mbalimbali zikiwemo majengo ya utawala, hospitali na miundombinu mbalimbali inayohusiana na utoaji huduma kwa wananchi. (Makofi)
Suala la madini pia liko katika Wilaya yangu. Wachimbaji wadogo wadogo katika Wilaya yetu ya Mbogwe tunayo madini ya dhahabu na kuna Resolute wanafanya utafiti lakini wamekuwa wakifanya utafiti muda mrefu sana matokeo yake sasa kunaanza kuwa na ugomvi kati ya wananchi na huyo mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara ya Nishati na Madini ihakikishe kwamba kwa kweli huyu mwekezaji anaanzisha mgodi, la sivyo arudishe leseni yake wananchi wengine wagawiwe ili waweze kuchimba na kuweza kujinufaisha katika maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, naomba nikupongeze kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja. Ahsante kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. Tanzania ya viwanda inawezekana sana, kikubwa ni Bunge hili na Serikali yake kuunga mkono azma ya Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli yenye kauli mbiu ya Tanzania ya Magufuli ni Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili ya mvua ni mawingu, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza vyema kwa kuongeza makusanyo ya kodi kwa kila mwezi. Makusanyo kupitia kodi mbalimbali yanaiwezesha Serikali kufikia hatua ya kuwa na akiba ambayo itapelekea fursa ya kuwekeza katika sekta hii muhimu ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali yetu itilie mkazo katika mabadiliko ya fikra katika vichwa vya Watanzania hasa wale wanaohusika katika kutengeneza mazingira wezeshi na kuvutia wawekezaji katika sekta ya viwanda na katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinyume na matarajio ya walio wengi kuna Watanzania wenzetu wanaweka urasimu mwingi na usio wa lazima, ama kwa makusudi au kwa kutengeneza mazingira ya kuomba rushwa. Lazima Serikali yetu hasa kupitia Kituo cha Uwekezaji (Tanzania Investment Centre) wawekwe Watanzania wenye nia njema na nchi hii, watakaokuwa na uchungu na wenye uzalendo na mapenzi mema wawasaidie wawekezaji wazawa na wawekezaji kutoka nje waweze kuwekewa mazingira wezeshi yatakayolitoa Taifa hili kwenye aibu ya kuifanya nchi kwenye orodha ya nchi zenye mazingira mabovu sana ya uwekezaji. Ni vyema tukajipanga upya kwa kuondoa urasimu usiokuwa wa lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) katika uwekezaji katika eneo la makaa ya mawe na chuma Mchuchuma na Liganga, Serikali ichukue hatua za makusudi kuharakisha uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma, vilevile ili chuma kizalishwe hapa nchini na chuma hiki kitachochea mapinduzi ya viwanda nchini mwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ni la wakulima, asilimia zaidi ya 70 wanategemea kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara na ili waweze kunufaika ni vyema viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa vikatiliwa mkazo ili kuongeza thamani kwa mazao yanayozalishwa hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Geita ni mkoa mpya, hata hivyo unazo fursa mbalimbali kuanzia mazao, dhahabu, mifugo, uvuvi na kadhalika. Ninaishauri Wizara ya Viwanda na Biashara kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji (Special Economic Zones).
Ninaamini maeneo yatakuwepo katika Wilaya mbalimbali ikiwemo Mbogwe. Tunawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje waje Mkoani Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Serikali ikawekeza zaidi katika maeneo ya upatikanaji wa umeme wa uhakika, maji yapatikane kwa urahisi, miundombinu ya uhakika kwa maana ya reli, barabara, bandari, mapinduzi ya viwanda na mazingira wezeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii nikiamini kabisa kuwa kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara hii kutaleta changamoto chanya katika kutangaza na kuinua sekta ya utalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa sekta ya utalii katika nchi yetu ni mkubwa sana kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha uingizaji wa fedha za kigeni kupitia watalii mbalimbali wanaoitembelea nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu limejaaliwa kuwa na vivutio vya utalii kuanzia mbuga za wanyama (national parks) na mapori ya akiba (game reserves), utalii wa mali kale, fukwe mbalimbali zenye mandhari nzuri na zenye kiwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto lukuki hasa katika mapori ya akiba yakiwemo mapori ya akiba ya Kigosi Moyowosi ambavyo kimsingi yanazo changamoto nyingi hasa miundombinu ya barabara za viwanja vya ndege na huduma za hoteli za kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kujenga barabara za kudumu kuyaunganisha mapori yetu haya ya Kigosi na Moyowosi kuanzia Kata ya Iponya, Wilayani Mbogwe kuunganisha na makao makuu ya mapori huko Kifura katika Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikifunguliwa na ikaimarishwa itasaidia sana shughuli za ulinzi wa wanyama pori kwani doria zitaweza kufanyika kwa urahisi hivyo kudhibiti uwindaji haramu hasa ujangili unaofanywa na waharibifu kutoka ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, uwepo wa barabara za uhakika katika mapori haya kutasaidia doria zitakazosaidia kuyabaini makundi makubwa ya mifugo yaliyovamia mapori haya na kuharibu ikolojia ya mapori haya mazuri na tegemeo la Taifa katika ukuaji wa sekta ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uwepo wa Shirika la Ndege lenye ndege zake za uhakika zenye kufanya safari zake katika Mataifa mbalimbali duniani kutasaidia kuvitangaza vivutio mbalimbali tulivyonavyo hapa nchini. Hii itaongeza idadi ya watalii wanaotembelea hapa nchini na kuvitembelea vivutio hivi na hivyo kuchangia pakubwa katika Pato la Taifa na pengine kusaidia kuwavutia wageni wawekezaji katika sekta hii kutoka katika mataifa ya nje tajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni jukumu la Serikali na Bodi ya Utalii nchini kuhakikisha kuwa vivutio hivi vingi tulivyonavyo vinatangazwa duniani kote ili viweze kuwezesha watalii wengi zaidi kuja hapa nchini na kuchangia katika upanuzi wa ukuaji wa uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kabisa kuunga mkono hutuba ya Waziri wa Nishati na Madini asilimia mia moja. Nishati na Madini ni sekta muhimu sana katika kuchangia Pato la Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ni kichocheo kikubwa katika kuleta mapinduzi na mageuzi ya uchumi kutoka uchumi duni na tegemezi na kuwa uchumi wa kisasa na wa kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yetu vyanzo vingi kama siyo vyote vya nishati kama vile maji, jua, upepo, makaa ya mawe, gesi, joto ardhi na hata nishati kutokana na madini ya Urani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na neema hii kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia katika nchi yetu, kinachotakiwa hapa hivi sasa ni kuwekeza zaidi katika nyanja za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu kupitia Shirika la Usambazaji Umeme nchini TANESCO na kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetekeleza miradi mingi mikubwa na midogo mbalimbali nchini naipongeza sana Serikali na hasa baada ya kugunduliwa kwa kiasi kikubwa cha gesi hapa nchini kumepelekea kuzalishwa kwa umeme wa gesi katika miradi ya Kinyerezi I na II na kuondokana na utegemezi wa uzalishaji wa umeme na maji na mafuta mazito.Uzalishaji huu wa gesi nchini ni chachu ya kuzalisha umeme kwa wateja na hasa wale wa vijijini na wa kipato cha chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa jitihada zake kupitia Shirika la Umeme nchini na Wakala wa Nishati Vijijini REA kwa utekelezaji wa miradi ya Electricity V na ile ya Wakala wa umeme Vijijini katika maeneo kadhaa ndani ya Wilaya ya Mbogwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali maeneo yaliyopelekewa huduma; Mbogwe, Ngemo, Nanda, Ilolangula, Isebya, Ikobe, Ikuguigazi, Lulembela, Nyakapera, Bukandwe, Masumbwe, Iponya, Nhomolwa na Lugunga. Hata hivyo zipo Kata mbili za Nyasalo na Bungonzi bado hazijapatiwa huduma hii muhimu ya umeme na inayo matumani makubwa kwa Serikali kupitia mpango wake kabambe wa REA Phase III. Vijiji vyote na Kata zote zitapata huduma hii muhimu ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Madini nchini imekuwa na mchango mkubwa katika ukuzaji wa Pato la Taifa. Wilaya yetu ya Mbogwe wamejali kuwa na madini ya dhahabu na zipo leseni za utafiti muda mrefu. Hata hivyo, zipo changamoto nyingi katika eneo hili la leseni za utafiti hasa utafiti wenyewe kuchukua muda mrefu.
Kampuni ya Mabangu inayo leseni ya muda mrefu wa utafiti katika maeneo ya Kata za Nyakafura, Lugunganya na Bukandwe. Utafiti katika eneo la leseni ya Mabangu Resolute umechukua muda mrefu sana na kupelekea malalamiko yasiyokuwa ya lazima kutoka kwa wananchi hasa wenye nia ya kushiriki katika shughuli za uchimbaji mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yametolewa mara kwa mara kwa Wizara kuitaka Kampuni ya Mabangu na mshirika wake Resolute wafungue mgodi na wakishindwa kufungua mgodi ni vyema wakaliachia eneo hilo wakapewa wachimbaji wadogo wadogo. Tunaikumbusha Wizara kuitaka Mabangu na Resolute wafungue mgodi kwa maslahi ya Wilaya yetu ya Mbogwe. Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Wizara hii ndiyo uti wa mgongo wa Tanzania ya Viwanda. Sekta zote za uzalishaji wa kilimo na sekta nyingine zote, za biashara, utalii, miundombinu ya umeme usafirishaji wa bidhaa na watu, vifaa ya ujenzi ili viweze kufikiwa na kusafirishwa Wizara hii ina mchango mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri. Kipekee nimpongeze kwa dhati Mhandisi Patrick Mfugale kwa utumishi wake uliotukuka na mchango wake wa kipekee katika ujenzi wa barabara za lami na sasa amekuwa kiongozi wa timu ya wahandisi ambao wamefanya upembuzi yakinifu na upembuzi wa kina hadi kuanza kwa ujenzi wa reli ya standard gauge unaofanywa na Kampuni za Yapi Merkez Insaat Ve Sanayi na Mota-Engil inayojenga reli aina hii kutoka Dar es Salaam – Morogoro, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara hii kwa kazi nzuri ya ujenzi wa barabara za lami chini ya usimamizi wa Mhandisi Patrick Mfugale. Niiombe Serikali ione uwezekano wa kumpatia nishani kwa ajili ya kuutambua mchango wake kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa ujenzi wa madaraja makubwa pamoja na flyovers, mradi wa DART, pamoja na Daraja la Mwalimu Nyerere – Kigamboni. Niombe pia Mradi wa Daraja la Kigongo – Busisi lisanifiwe na kujengwa ili kurahisisha mawasiliano katika Kanda ya Afrika Mashariki na kuondoa vikwazo vya vivuko kwenye Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali na Wizara izipandishe hadhi barabara za Bwelwa – Ushirombo – Ivumwa, Nyaruyeye, Nyarugusu, Nyabulolo – Buyegu, Geita. Ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Butengolumasa, Iparamasa, Mbogwe, Masumbwe. Barabara hii ni kiungo cha barabara ya Isaka – Masumbwe, Mbogwe, Iparamasa, Butengo Lumasa, Chato, Muleba, Bukoba, Mtukula hadi nchini Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ununuzi wa ndege ni hatua maridhawa katika kuitangaza nchi yetu Kimataifa na hivyo kusaidia kukuza sekta ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iendelee kutenga pesa kwa ajili ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili ujenzi wa minara katika maeneo yenye usikivu hafifu yapatiwe huduma hii hasa katika Kata za Ilolangulu, Ikobe, Isebya, Nyasato, Ikunguigazi (Kagera). Shirika la Simu Tanzania (TTCL) lipatiwe uungaji mkono kifedha ili liwekeze zaidi na limudu ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya uhai ili na mimi niweze kushiriki katika kuchangia hotuba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyowasilishwa hapa Bungeni leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni kila kitu na ardhi ni ishara mojawapo ya uwepo wa dola. Hakuna nchi inayoweza kuwepo duniani isipokuwa na ardhi; na ardhi ndiyo inayotunza maisha ya kila kiumbe kilichopo katika dunia hii. Kwa maana hiyo, ardhi isipoendelezwa vizuri na isipopangwa inavyostahili, hakuna maendeleo. Ardhi inavyopimwa ni kipimo cha ustaarabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulimwenguni pote ambapo tumetembea na wengine tumeona, wenzetu wamestaarabika baada ya kuwa na matumizi mazuri ya ardhi. Kwa maana hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na hotuba nzuri na mikakati mizuri ambayo kwa kweli inatia matumaini kwamba huenda sasa Taifa letu likazaliwa upya na sisi tukawa miongoni mwa watu watakaoweka historia ya kufanya kazi na wewe Mheshimiwa Waziri pamoja na Wataalamu wako ambao kwa kweli mtatuweka katika historia ya kukumbukwa. Kazi yetu sisi ni kuunga mkono hatua mbalimbali ambazo mnazichukua na pale ambapo mtahitaji msaada wa Bunge hili, msisite kuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sheria na machapisho mbalimbali ambayo ametupa leo. Namuahidi kwamba kwa kweli tutachukua nyaraka hizi kwenda kuzifanyia kazi ili ziwe sasa ni kiongozi kwetu, tusiwe na kisingizo cha kwamba pengine labda ni kutokufahamu kwetu ndiko kumesababisha maeneo yetu mengine yasipangwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ndiyo kielelezo cha mipango yote ya maendeleo iwe katika kilimo, ufugaji, uwekezaji katika reli, barabara na makazi ya wanadamu. Kwa maana hiyo, uwepo wa harakati mbalimbali katika maisha ya mwanadamu na hasa tunapojikuta kwamba katika Taifa la Tanzania tunaendelea kuongezeka lakini ardhi inabaki pale pale. Kwa maana hiyo ni lazima tuwe sasa waangalifu kwa namna gani tunavyoweza kupanga matumizi endelevu ya hii rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia kuwa nayo. Hii peke yake ndiyo rasilimali ambayo kila mmoja anakuwa nayo; masikini kwa tajiri, hata yule aliyekufa naye anahitaji ardhi kwa sababu atatakiwa ahifadhiwe katika nyumba yake ya milele ambayo ni ardhi. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba kabisa kwamba mipango yote ambayo imo ndani ya hiki kitabu cha bajeti, ikitekelezwa ipasavyo na nina imani kabisa kwamba tutapiga hatua. Hatutakuwa na migogoro baina ya wafugaji na wakulima, baina ya wananchi na wawekezaji. Kwa maana hiyo niseme kwamba miji yetu itapangwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama ambavyo mara nyingi nimeendelea kusema, kitu ambacho ni cha muhimu kama ardhi, kinatakiwa kuwa na wataalam kuanzia ngazi za kijiji, Maafisa Mipango Miji wawekwe huko. Hata kama ikionekana kwamba labda pengine ajira zao zinaweza zikawa ni nyingi sana, basi angalau wasogee mpaka hata kwenye ngazi ya kata; wawepo wawe wanaratibu na kuweza kutoa taarifa za wepesi na mapema kabisa juu ya maendeleo ya makazi kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, hata Mabaraza haya ya Ardhi ya Vijiji na Kata wawepo wataalam. Sasa kwa sasa hivi unakuta tu kwamba watu wanawekwa pale kwa sababu mtu amekaa muda mrefu pale au ni mzee maarufu; sasa mzee maarufu na upangaji wa kitu muhimu kama ardhi, naona havihusiani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa ombi na ni rai yangu kwa Wizara hii ambayo kwa kweli tunaitegemea sana, iwe ni chanzo cha ustaarabu katika Taifa letu. Miji mingi inakuwa kwa kasi, lakini ni kwa namna gani ambavyo Serikali na yenyewe imejipanga kwenda na hii kasi ya mabadiliko ya wananchi kuhamia kutoka vijijini na kwenda kwenye centres, Serikali inakuwa nyuma. Kwa hiyo, naomba sasa kwamba Wizara hii ya Ardhi pamoja na Serikali yenyewe itoe kipaumbele cha rasilimali kwa maana ya fedha, utaalamu na vifaa; kwa maana bila kuwapa vitendea kazi watumishi wetu hawa, tatizo hili litaendelea kuwa sugu.
Kwa maana hiyo, niseme tu kwamba ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi na Naibu wake, Mheshimiwa Angeline Mabula, wameonyesha dhahiri kwamba katika awamu hii ya Serikali ya Awamu ya Tano wameanza vizuri na ninaomba tu kwamba mipango yote ambayo mmeileta hapa Bungeni, tunaipa baraka zote mwende mkaitekeleze….
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri. Hongera Mheshimiwa Waziri kwa hotuba madhubuti. Wizara hii ni miongoni mwa sekta kiongozi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ya pekee na kwa namna anavyofanya kazi na kuonesha ushirikiano mkubwa kwetu sisi watu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, hasa kuhusiana na hatua mbalimbali za uendelezaji wa Mapori ya Akiba ya Kigosi Moyowosi. Pori la Akiba la Kigosi Moyowosi ni pori zuri sana, hata hivyo liliachwa bila uangalizi madhubuti, matokeo yake pori hili likavamiwa na makundi makubwa ya ng’ombe wa ndani na wengine kutoka nchi jirani, hasa nchi ya Rwanda na Burundi.

Mheshimiwa Spika, kutelekezwa kwa Pori hili la Akiba la Kigosi Moyowosi kulisababisha miundombinu yake kukosekana, barabara katika pori hili ndio uti wa mgongo wa ulinzi na usalama kwa pori lenyewe na wanyama wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa barabara za kudumu ndani ya pori hili kumedumaza maendeleo ndani ya pori hili, matokeo yake mwanya unapatikana kwa majangili kuua wanyama, uvamizi wa wakulima na wafugaji na wahamiaji haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege ndani ya Pori la Akiba la Kigosi Moyowosi ni chachu ya ukuzaji wa utalii ndani ya pori hili. Kiwanja cha ndege kifufuliwe, ili kiwe kiungo muhimu na Hifadhi za Taifa za Mahale na Gombe, pia Rubondo National Park. Hongera Mheshimiwa Waziri kwa uamuzi wako wa busara wa kuonesha nia ya kulipatia Pori la Akiba la Kigosi Moyowosi magari mawili kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za utawala na ulinzi wa pori lenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameonesha nia ya kulikarabati grader lililopo Kifura ili lifufuliwe na kuanza kutumika kufungua barabara ndani ya pori hili. Nakuunga mkono Mheshimiwa Waziri, songa mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzishwa kwa Mamlaka ya Wanyamapori (Tanzania Wildlife Authority – TAWA), ni hatua muhimu sana katika kuyaunganisha na kuyasimamia mapori yote ya akiba nchini. Ninaamini hatua hii itaongeza ufanisi kiutendaji kama ilivyo kwa TANAPA na Ngorongoro Conservation Area Authority na kwa mantiki hiyo, mchango wa mapori ya akiba nchini, chini ya TAWA kuongezeka katika Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho ni kuhusu uanzishwaji wa Game Rangers ndani ya Pori la Akiba la Kigosi Moyowosi na kufungua barabara ndani ya pori hili. Mungu ibariki sana Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii kwa mara nyingine niweze kutoa mawazo yangu katika kuunga mkono hotuba nzuri ya Waziri wetu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Waziri Lukuvi aingie katika Wizara hii tumeona mabadiliko makubwa na tuna matarajio makubwa ya kuona mambo mengi yakiwekwa sawa hasa suala zima la maandalizi ya kuipanga upya nchi yetu. Nchi yetu imeingiwa na tatizo moja ambalo kimsingi tulikuwa tumeepukana nalo la mapigano ya sisi kwa sisi. Suala la ardhi limeonekana kuwa ni chanzo cha migongano baina ya wananchi, wafugaji na wakulima. Jambo hili lisiposhughulikiwa vizuri linaweza likawa chanzo cha vurugu nchini, chanzo cha kutoweka kwa amani iliyojengeka kwa muda mrefu katika nchi yetu. Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi na wataalam wako nashauri kwa kweli speed uliyoanza nayo endelea nayo. Kwa wale watu ambao wanakuwa na ardhi ambayo wanaimiliki bila kuiendeleza basi hatua unazochukua za kuwanyang‟anya ardhi na kuwapatia wananchi ambao hawana ardhi uendelee nazo na kasi yako isirudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba yapo maeneo mapya ya utawala, tuna Mikoa mipya ya Geita, Katavi, Simiyu na sasa Njombe pamoja na Mkoa mpya wa Songwe. Naomba maeneo haya ambayo yameanza upya pamoja na Wilaya zake mpya basi Wizara iyatazame kwa upya ili kusudi yawezeshwe kuwa na master plan pamoja na upimaji wa kisasa, tusije tukajikuta tena kwamba maeneo haya yameanza upya lakini yakapata athari ile ile ambayo imeikuta mikoa mingi kabla ya utaratibu huu mzuri ambao umekuja nao wa kuwa na hii unayosema ni Integrated Land Management Information System. Jambo hili ni la kisasa ina maana kwamba kutakuwa na takwimu nzuri kabisa za matumizi mazuri ya ardhi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kusema tu wazi kwamba Wizara hii ni mama ambapo kila Wizara na Idara ya Serikali haiwezi ikafanya kazi zake bila kushirikiana na Wizara hii ya Ardhi. Iwe Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Mazingira, zote zinategemea uwepo wa mipango mizuri ya matumizi ya ardhi inayofanywa na Wizara yetu hii ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba nchi yetu sasa imekuwa ni kitovu cha wawekezaji, watu wengi wanavutiwa kuja katika nchi yetu. Ni jambo jema na ni la kheri lakini kheri inaweza ikapata tena kikwazo pale inapotokea mwekezaji amekuja kama mgeni wetu lakini anafika mahali anaanza kuwa ni chanzo cha ugomvi baina yake na wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili naomba sasa Serikali yetu kupitia Wizara yetu ya Ardhi ilitilie maanani kwa kuanzisha utaratibu wa kuwa na benki ardhi kwamba kuwepo na maeneo ambayo yametunzwa kama Special Economic Zones ambapo mwekezaji yeyote anayekuja aelekezwe mahali ambapo atafanya kazi zake kwa amani. Hali hiyo itatujengea heshima kwa wageni wetu na kwa mataifa mengine ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo niishie hapo, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Niwapongeze tu ndugu zangu Mawaziri na sisi kama Wabunge tuko pamoja na tuko nyuma yao. Mungu akubariki sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Baada ya kuunga mkono hotuba hiyo, napenda kulipongeza Jeshi letu kwa kazi kubwa linazofanya katika kulinda usalama wa mipaka yetu na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa letu na kushiriki katika kukabiliana na majanga mbalimbali yanayolikumba Taifa letu kwa nyakati mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kuwa Serikali iongeze bajeti kwa Wizara hii ili kuziwezesha taasisi ndani ya Wizara hii za Nyumbu na Mzinga ili zijikite kikamilifu katika shughuli za utafiti wa kisayansi na ugunduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia inaonesha dhahiri kuwa taasisi za ulinzi na usalama hasa Majeshi ya Ulinzi katika nchi mbalimbali duniani zimeshiriki kikamifu katika kuleta mapinduzi ya viwanda na zana za kivita. Mfano, mifumo ya computer ilibuniwa na Jeshi la Marekani kabla ya kuingizwa katika shughuli za kiraia. Ugunduzi na ubunifu wa vifaa vya kivita kama vile vifaru, ndege za kivita, meli za kivita, makombora ya masafa mafupi, ya kati na marefu yote ni matokeo ya shughuli za kijeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda kuishauri kulitumia vema Jeshi la Wananchi katika harakati za uvuvi wa bahari kuu (deep sea fishing) ili meli za kivita ambazo zinakaa muda mrefu bila kufanya kazi, zitumike katika kukuza uchumi wa Taifa letu wakati huu amani ikitamalaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishauri Serikali kulitumia vizuri Jeshi la Kujenga Taifa kwa kulipatia zana za kisasa za uzalishaji mali, yakiwemo matrekta ili kuzalisha mazao ya chakula na biashara kama vile kahawa, mahindi na mpunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri JKT iwezeshwe kuwa chimbuko la ufugaji bora wa ng‘ombe wa nyama na maziwa. Ni imani yangu kuwa Serikali ikiliwezesha Jeshi letu wakati huu, upo uwezekano mkubwa wa kuwa mchangiaji mkubwa katika shughuli za ukuzaji uchumi kama majeshi ya nchi nyingine yanavyofanya, mfano, Ethiopia hapa Barani Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kwa kweli kukupongeza wewe kwa ujasiri mwingi ambao umeuonesha ndani ya Bunge hili na kwa vyovyote vile sisi Wabunge wenzako tupo pamoja na wewe na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uwe na afya njema, uitende kazi hii ya Watanzania kwa moyo mkunjufu na hongera sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii ya kuweza kushiriki katika kuichangia bajeti ya Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, bajeti ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano ya uhai wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imejikita katika mambo mengi ya msingi yakiwemo masuala ya maji, barabara, umeme na mazingira pamoja na uboreshaji wa Reli ya Kati; na kwa hakika suala zima la madini nalo limewekwa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba kwa kweli Taifa letu linanufaika kutokana na maliasili tulizonazo ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Geita ni Mkoa mpya, mkoa huu unatarajia kwa kweli uungaji mkono wa Serikali ili uweze kwenda kwa sababu ni miongoni mwa mikoa mipya minne au mitano sasa ambayo imeanzishwa na Serikali yetu kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wananchi. Kwa maana hiyo, mikoa hii inahitaji kwa vyovyote vile uangalizi mzuri katika utekelezaji wa bajeti hizi ambazo zinakuwa zinaandaliwa kila mwaka ili kusudi ikiwezekana mikoa hii iweze kupiga hatua, iende sambamba na maeneo mengine ambayo yametangulia katika kupiga hatua za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Geita ipo karibu na Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa katika Afrika na ni la pili katika ulimwengu huu, kwa maana hiyo linayo maji ya kutosha; na sisi wana Geita tunamshukuru Mungu kwa kutujalia kuzaliwa katika eneo hili ambalo lina maji mengi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoweza kuwa na ujasiri mwingi wa kuweza kupeleka maji haya Ziwa Victoria kutoka Mwanza mpaka Kahama na Shinyanga na hatimaye kuyapeleka katika Mkoa wa Tabora. Naomba sasa kwa vyovyote vile Serikali yetu ijitahidi sasa kutuletea maji katika Wilaya yetu ya Mbogwe pamoja na Mkoa wetu wa Geita ili tuweze kufikia hatua ambayo kwa kweli itakuwa ni njema hasa kuwa na maji safi na salama ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua maji ni uhai. Ukiwa na maji safi na salama una uhakika wa kuwa na maisha mazuri kwa sababu magonjwa mbalimbali ambayo yanaangamiza maisha ya mwanadamu yanatokana na maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa mfano typhoid, kipindupindu ambacho kimekuwa kikiwasibu Watanzania katika maeneo mbalimbali kinatokana na miundombinu mibovu ya maji. Wakati mwingine maji yanapokuwa hayawezi kupatikana wananchi wanapata shida namna ya kuweza kuyafanya mazingira ya makazi yao yawe salama, kwa maana ya kwamba maji ndiyo yanayoweza kuwasaidia wakati wa kusafisha mazingira yao. Wakati mwingine iwe ni katika kusafisha nyumba, viwandani au kusafisha mahali popote pale; na wakati mwingine hata katika kilimo cha umwagiliaji maji yanasaidia. Katika kuhakikisha kwamba mazingira yanakwenda sawasawa maji ni muhimu na ni uhai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo,niombe tu kwamba Serikali yetu inapopata nafasi, kwenye maeneo yote ambayo kwa kweli tumejaliwa kuwa na maziwa; kwa mfano Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa na Ziwa Nyasa, Serikali yetu ifanye kila linalowezekana pale ambapo rasilimali zinapatikana kuhakikisha kwamba, wananchi hawa wanapewa maji ya kutosha. Ili Tanzania ya viwanda iweze kupatikana ni lazima kwa kweli suala zima la maji lipewe kipaumbele cha kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi katika kuuliza swali niliuliza suala la kuwepo kwa mapori ya akiba katika nchi yetu hii. Mapori haya kimsingi bado sijaelewa vizuri, kwamba hivi Serikali ilipoyatenga mapori haya kuwa ya akiba ni kwa ajili ya baadaye kuyafanya yawe national parks au baadae yaje yawe maskani ya wananchi au makazi? Kama yametarajiwa kuja kuwa ni maeneo ya kuwa national parks na maeneo ya kuweza kuwafanya wanyama waendelee kudumu ni kwa vipi mapori haya yenyewe hayawezi kutengwa angalau sehemu fulani ikawa na eneo ambalo limehifadhiwa kwa ajili ya wanyama hawa wa kuzaliana ili waweze kupitisha kizazi hata kizazi na hatimaye waongezeke? Isije ikatokea kwamba baadaye hawa wanyama wakaisha tukaanza na sisi kuwa tunakwenda kufanya utalii katika nchi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza sana kuona kwamba wakati mwingine katika maeneo yetu kwa sasa kama pori la Kigosi Moyowosi kimsingi hayatunufaishi kwa vyovyote vile. Pori la Kigosi Moyowosi linafanyiwa ujangili, tembo wanauawa na hakuna habari ya asilimia 25 ambayo tulitakiwa tuwe tunapewa kama mchango kutokana na uwindaji. Shughuli hii kwa kweli haina maslahi kwetu na kwa maana hiyo ndiyo maana unaweze ukakuta watu wanaamua kuhamishia mifugo humo ndani angalau waweze kulisha mifugo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, kama kweli ina nia njema ya kuweza kutusaidia, basi mapori haya iyaboreshe, iyawekee miundombinu na iyatangaze ulimwenguni huko ili kusudi watu waje kufanya utalii na hatimaye maeneo yetu ya Wilaya ya Mbogwe pamoja na Mkoa wa Geita basi yaweze kunufaika katika suala zima la utalii. Tunayo mapori mengine ya Kimisi, Burigi katika Kanda ya Ziwa, hayana mchango wowote hayaonyeshwi katika Serikali hii kwamba kuna mpango wa kuweza kuyaendeleza mapori haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kwa kweli ijiangalie, katika mpango wake wa maendeleo unapokuja mbele huko tuone kwamba utalii uliokuwa umewekwa katika kanda ya Kaskazini basi uhamishiwe katika kanda ya ziwa kwa sababu tunalo pori lenye kilomita za mraba elfu 21, ni eneo kubwa hili, kama Serikali haiwezi kulijenga vizuri na kulifanyia miundombinu ya uendelezaji hatimaye watu watahamia katika mapori haya na mwisho lengo la kuyatenga haya mapori lisije kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, niseme tu kwamba kwa kweli suala la kiinua mgongo cha Wabunge waliangalie kwa jicho la pili kwa sababu sheria yenyewe iliyopo hapa ya viongozi wa kisiasa inatoa nafuu (msamaha) katika suala hili. Kwa hiyo, niombe tu kwamba, kwa sababu sheria ipo na iheshimiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tena juu suala zima la kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa hili, naomba Serikali kwa kweli iangalie namna ambavyo mazao kama pamba…
Ohh! Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na wewe kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hoja. Serikali yetu ya Awamu ya Tano imekuja na mipango kabambe kwa ajili ya kufufua uchumi wa nchi hii na kwa maana hiyo, sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ndiyo tunahusika kwa namna zote kuisimamia Serikali kuhakikisha kwamba inafanikiwa katika mipango yake ya kila siku, basi tuwe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba tunaiunga mkono Serikali yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utaanza na suala zima la uhamishaji Makao Makuu kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma. Ni wazo zuri na ni la kimaendeleo lakini limechelewa. Pamoja na kuchelewa huko, tunatakiwa tujipange sawasawa kuhakikisha kwamba hatushindwi njiani. Kwa maana hiyo, mipangilio iwe thabiti tusije tukajikuta kwamba sasa tunakwamisha Serikali katika utendaji kazi wake kwa sababu sasa watumishi watakuwa mguu mmoja nje, mguu mmoja ndani. Kwa hiyo, nishauri Serikali kwa kweli ijipange vizuri na Maafisa Masuuli kama Waziri wa Fedha alivyoainisha kwenye mpango wake kwamba jambo hili waliweke katika bajeti ili liweze kutekelezeka kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia niishauri Serikali kuhakikisha kwamba inaweka katika mipango yake ya bajeti gharama za ujenzi wa Halmashauri katika Wilaya mpya kama Mbogwe na nyingine. Pia itenge bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mikoa mipya ambayo imeanzishwa kama Mikoa ya Geita, Songwe, Simiyu, Njombe na Katavi ili wananchi wa mikoa hii na wao waweze kupata huduma karibu zaidi kama Serikali ilivyojipanga kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala zima la utaratibu wa Serikali kufuta retention na kuziagiza taasisi mbalimbali kupeleka pesa zao katika akaunti ya Benki Kuu. Jambo hili ni zuri kwa sababu linaongeza udhibiti wa mapato na matumizi ya Serikali ili kuweza kufahamu thamani halisi ya yale mapato ambayo yanapatikana. Hata hivyo, niishauri Serikali iwe makini kuhakikisha kwamba pesa ambazo zimepangwa kwa ajili ya taasisi hizi zinaenda kwa wakati ili miradi ya maendeleo ambayo imepangwa kwenye sekta hizo isikwame. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala zima la miradi ya kielelezo. Miradi hii mingi imeainishwa lakini mradi mkubwa ambao unatakiwa tuufanye haraka ni mradi wa reli ya kati na ujenzi wa Bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na pia bandari zile za maziwa makuu kama Mwanza, Bukoba, Karema, Kigoma na nyingine nyingi. Nasema hivi kwa sababu tumepakana na nchi mbalimbali ambazo nyingi zinategemea sana Bandari ya Dar es Salaam ambayo inaunganishwa na maziwa makuu kwa kupitia njia ya reli. Sasa reli ya kati kutoka Dar es Salaam – Tabora – Kigoma - Mwanza na nyingine ambayo itaanzia Isaka - Kigali, zote hizi zina muunganiko mzuri wa kuweza kutumiwa na nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, naiomba Serikali ihakikishe inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mradi huu kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo ambao ni nchi ya China ambayo imekubali kufadhili mradi huu, ufanyike kwa umakini na kwa haraka ili kuweza kuhakikisha kwamba Tanzania ya viwanda inafikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala zima la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Nikiwa mwanakamati wa Kamati ya Bajeti, tumeona kwamba ili Serikali iweze kufanikiwa katika lengo hili ni vema basi ikaongeza chagizo lake katika bajeti kutoka shilingi milioni 59 kwa mwaka mpaka kufikia shilingi bilioni 200 ili kwa miaka yake minne iliyosalia lengo la kukipatia kila kijiji shilingi milioni 50 liweze kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala zima la kubadilika kwetu kwa mindset kwa maana ya Watanzania. Imeonekana kwamba wakati mwingine Watanzania tunakuwa na matatizo ya kutengenezwa kwa kuwa na urasimu mkubwa ambapo wawekezaji wanapokuja hapa nchini hucheleweshwa, matokeo yake wanaamua kukimbilia katika nchi nyingine ambazo na zenyewe zina uhitaji wa wawekezaji kama sisi. Kama tusipobadilika tunaweza tukajikuta tunaachwa na wenzetu nchi zenye ushindani na sisi, wakapokea wawekezaji wa kutosha na matokeo yake nchi zao zitaneemeka kiuchumi kuliko sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema haya, ahsante kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa viwanda na biashara katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Zipo changamoto nyingi katika kutekeleza sekta zilizopo chini ya Wizara husika hasa changamoto ya urasimu usiokuwa wa lazima kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda nchini. Wawekezaji ni lulu inayosakwa na mataifa mbalimbali duniani ni lazima kuwa makini. Nashauri Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kwamba Tanzania Investment Centre (TIC) inatoa huduma zote zinazotakiwa kwa mwekezaji katika sehemu moja hasa suala la vibali na uhakiki ufanyike under one roof.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara ni Wizara mtambuka inayopashwa kufanya kazi zake kwa kushirikiana na wadau na Wizara zingine kama vile Wizara ya Fedha kupitia sekta za mabenki, bima na TRA. Benki zinapofanya kazi zake vizuri na kuwa na riba rafiki katika uwekezaji mitaji katika sekta ya viwanda na kodi mbalimbali zinazotozwa zikiwa rafiki zitasaidia katika sekta zilizoko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa viwanda nchini kunategemea kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa malighafi kama vile chuma na umeme wa uhakika. Kwa kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa kwa uwepo wa kiwango kikubwa madini ya chuma na makaa ya mawe na kwa kuwa makaa ya mawe yanapatikana Mchuchuma na Chuma cha Liganga, katika zoezi zima la uzalishaji chuma, makaa ya mawe hutumika na kinachozalishwa huwa ni chuma pamoja na umeme.

Nashauri Wizara kupitia Shirika la Maendeleo Nchini (NDC) lifanye kila linalowezakana kuhakikisha kwamba uzalishaji wa chuma Mchuchuma na Liganga unakamilika kwa sababu upatikanaji wa chuma na umeme nafuu utarahisisha uwekezaji katika viwanda nchini. Pia uwepo wa usafiri madhubuti wa reli na barabara na huduma bora katika bandari zetu hasa bandari ya Dar es Salaam kwani hili ni lango kuu la shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini kutasaidia ukuaji wa sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara inao mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya viwanda vya nguo katika Ukanda wa Ziwa ambako zao la pamba linazalishwa kwa wingi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya nguo na ukamuaji wa mafuta, kwani uongezaji thamani wa mazao yetu utaleta tija kwa wakulima wetu na kuboresha maisha yao na kuchangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia
nafasi hii adhimu ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hotuba za Kamati zetu mbili za
kudumu za Bunge; Kamati ya Nishati na Madini na Kamati ya Bunge ya Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii ili kwa namna moja au nyingine,
niweze kwanza kuipongeza Serikali yetu kupitia Wizara hizi mbili pia. Wizara ya Nishati na Madini
imefanya kazi kubwa, nzuri na ya kutukuka kwa Taifa letu hili la Tanzania; tumeona juhudi zilivyo
nzuri katika kuhakikisha kwamba umeme unapatikana katika Taifa letu na umeme wa uhakika.
Kwa hiyo, naomba tu kwa kweli Serikali kupitia Hazina, itoe pesa kwa wakati katika miradi
mbalimbali ambayo imeletwa na Wizara hii ndani ya Bunge lako na kuidhinishwa ili ikapate
kutekelezwa katika mwaka unaohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Wizara hii pia ambayo imeonesha kwa mfano kabisa,
kuwachukua Watanzania wenzetu na kuwapa full scholarship katika Mataifa mbalimbali
kuweza kujielimisha na kupata taaluma muhimu katika Sekta mbalimbali za Nishati na Madini
katika Taifa letu. Nina imani baada ya muda siyo mrefu, Tanzania itakuwa na wataalam
waliobobea wa hali ya juu na Taifa letu litapata manufaa makubwa katika sekta hizi zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Nishati na Madini ijitahidi sana kuisimamia
Sekta ya Umeme nchini, maana hii ndiyo injini ya mapinduzi ya viwanda kule ambako
tunatarajia kwenda. Kwa sababu umeme unapokuwa unapatikana katika bei ambayo ni
ndogo, tunaamini kwamba tunaweza tukavutia wawekezaji wa ndani na nje kwa urahisi zaidi.
Hata katika Wakala wa Umeme Vijijini, napendekeza Serikali iendelee kutoa pesa kwa wakati ili
hata hii REA Phase III iweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwa macho yetu wote kwamba Tanzania imepiga
hatua katika usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali vijijini na naomba tu kwamba
ule mtandao wa umeme vijijini uendelezwe zaidi. Pale ambapo tumefika, kasi iongezwe zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu, napo tuongeze jitihada katika
kuhakikisha kwamba Reli ya Kati inaendelezwa. Naipongeza kwanza Serikali kwa kuingia
mkataba na Waturuki kutaka kujenga hii Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Serikali yetu kwa dhamira ya dhati ya Rais wetu,
Mheshimiwa Dkt. Joseph Pombe Magufuli tutafika kule ambako tunatarajia ili tuweze kuwa na
treni ambazo zinaweza kwenda mwendo kasi; bullet train, tuweze kuzipata katika Tanzania hii,
watu na vitu viweze kufika mahali panapostahili kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kabisa kwamba Taifa la Tanzania tumejaliwa kuwa
katika eneo ambalo kijiografia linatupa nafasi nzuri ya kuweza kuwa tegemeo katika ukanda
wetu wa Afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Kwa maana hiyo, upanuzi wa bandari zote; ya
Tanga, Dar es Salaam, Bagamoyo pamoja na kule Mtwara ni bandari ambazo ni za muhimu
sana. Ni muhimu kabisa Tanzania ikawa na kipaumbele cha peke yake katika hizi bandari, kwa
sababu zote zinategemewa. Bandari ya Mtwara, Mataifa ya Msumbiji, Malawi hata Zimbabwe
wanaweza wakaitumia bandari hii. Kwa maana hiyo, ile reli ya kutoka Mtwara mpaka
Mbambabay ni ya muhimu sana kwa sababu itakuwa na matokeo mazuri sana katika ukuzaji
wa uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Reli ya Kati inaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi hizi
za Zaire kwa maana ya DRC, Rwanda na Burundi pamoja na Nchi ya Uganda. Bandari ya
Tanga imeteuliwa kabisa na nchi ya Uganda na kwa maana hiyo, ujenzi wa reli ya kutoka
Tanga - Arusha mpaka Musoma na yenyewe ni muhimu ikapewa kiaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, niseme kabisa kwamba Taifa letu la Tanzania
katika mchango wake wa kuleta uhuru katika Mataifa mbalimbali ya Afrika, bado inayo nafasi
nzuri tena katika kuchangia ukuzaji wa uchumi katika Mataifa yote haya ya Afrika ambayo
Tanzania yenyewe ilishiriki katika kuyaletea uhuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme dhahiri tu kwamba kwetu huko Geita ni sehemu
ambayo tunayo madini ya dhahabu. Naishauri Serikali ifanye kila linalowezekana kuharakisha
kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo ya Wilaya yetu ya Mbogwe
na wachimbaji waliotapakaa katika Mkoa wa Geita, wapate kutengewa maeneo ya kufanya
shughuli zao za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya, nakushukuru kwa mara
nyingine kwa kunipatia nafasi hii. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe Mkoani Geita naomba kuelezea kuvunjwa moyo kwa hatua ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuliweka kando ombi letu la maji ya Ziwa Victoria kufikishwa Wilayani Mbogwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetumia muda wangu mwingi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe kuiomba Wizara na kuielezea kwa undani kuhusu tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji hasa nyakati za kiangazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kihistoria Wilaya ya Mbogwe ilikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Kahama na kwamba Wilaya zote za uliokuwa Mkoa wa Shinyanga zimepatiwa maji ya Ziwa Victoria, mfano, Kahama, Shinyanga, Kishapu, Maswa, Bariadi na Meatu, ziko vizuri na sasa maji hayo yanapelekwa Mkoani Tabora. Sisi tunatengwa hasa baada ya Wilaya yetu ya Mbogwe kuhamishiwa Mkoani Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mahitaji ya maji na suluhisho lake la kudumu hasa katika nyakati hizi mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Licha ya kwamba kwa sasa maeneo yetu bado yana misitu na miti kiasi, lakini suala la uharibifu wa mazingira litasababisha ukame utakaosababisha uhaba wa maji na suluhisho la kudumu ni kupata maji kutoka Ziwa Victoria ambayo yako jirani kabisa katika Mji wa Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwamini Mheshimiwa Waziri Lwenge na Naibu wake Mheshimiwa Kamwelwe kutokana na ahadi ambazo wamekuwa wakiwapatia wananchi wa Wilaya ya Mbogwe kuwa ipo siku maji ya Ziwa Victoria yatafika Wilayani kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, nimevunjika moyo baada ya kuipitia na kuisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuona ndoto ya maji ya Ziwa Victoria imeyeyuka na kupotelea mbali. Hata hivyo, bado nikiwa Mbunge, nitaiishi ndoto hiyo na kumwomba Mungu siku moja maji ya Ziwa Victoria yafikishwe Mbogwe tokea Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbogwe tunaomba maji ya Ziwa Vivtoria. Mungu ibariki Serikali ya Tanzania na Mungu ibariki Mbogwe na ombi letu la maji ya Ziwa Victoria lifike kwa Mwenyezi Mungu na limfikie Mheshimiwa Rais na Mawaziri wetu wa Maji, waiishi ndoto yetu ya kupata maji ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi nyingine tena mchana huu ili tuweze kuitendea haki hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee nakushukuru wewe mwenyewe kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naanza kwa kuunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Wizara hii ndiyo ambayo kwetu sisi Wakristo, kuna maneno fulani yamo kwenye vitabu vitukufu, yanasema: “Tazama nakwenda kufanya nchi mpya na mbingu mpya, ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya.” Nchi hii tunaiona inavyobadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona Tanzania mpya inakwenda kuzaliwa. Unaweza ukaona kuanzia Mwalimu Nyerere mpaka Rais Kikwete, makao makuu ya nchi hii yalikuwa Dar es Salaam; kuanzia kwa Rais Magufuli, makao makuu ni Dodoma sasa. Kuanzia mkoloni, Nyerere mpaka Rais Kikwete tulikuwa na meter gauge, kuanzia Mheshimiwa Magufuli na kuendelea tunakwenda kuwa na standard gauge. Hiyo ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Rais wetu alipokuwa Mgombea, aliimbia Tanzania na Dunia nzima, watu wakataka kwenda mahakamani akasema, M for change, wakasema ameibia sera fulani, lakini alikuwa anasema Magufuli for Change na M4C hiyo kweli tunaiona. Hongera Rais wetu. Tunaweza tukasema hakika ya kwamba huyu anaweza akawa ni miongoni mwa Manabii wa kizazi kipya.
Anaitabiria Tanzania mambo mazuri na kila mmoja anaona. Kwa maana hiyo niseme, Wizara ya Miundombinu kwa maana ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ndiyo inakwenda kuifanya Tanzania hii iwe mpya ili hata Mataifa mengine watakapokuja hapa, watauona uso wa Tanzania ukiwa umepambwa na flyovers, ukiwa na madaraja ambayo yako kwenye viwango, ukiwa na treni ambazo zinakwenda kwa haraka. Kwa maana hiyo, hata uwekezaji katika Taifa hili utakuwa ni wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta nyingine muhimu za viwanda, uzalishaji, kilimo, zinategemea sana ni namna gani tunavyokuwa na mawasiliano ya haraka. Hata Mwekezaji akija hapa, atapenda sana kuona ni namna gani itakavyoweza kuwa anasafirisha bidhaa zake kama ata- import au ata-export, muda gani anautumia hapo? Ndipo tutaona kwamba watu hawa wanaweza wakaja kutusaidia na tukaenda kwenye Tanzania ya viwanda tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, naomba niseme neno moja ambalo napenda Watanzania walisikie, kwamba kuna baadhi ya Watanzania wanafanya michango yao katika Taifa hili, wakati mwigine wasitambuliwe. Nichukue hata dakika chache kumsifu bwana mmoja anaitwa Engineer Patrick Mfugale. Amekuwa ni chachu katika TANROADS na hata sasa kwa wale wasiojua, ndiye anayeongoza timu inayojenga standard gauge ya Tanzania. Kwa maana hiyo, mtu huyu ni hazina ya nchi hii na hongera sana kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la miundombinu ya barabara hasa Jimboni kwangu. Namuomba Mheshimiwa Waziri, barabara yetu ya Mtengorumasa – Iparamasa - Mbogwe mpaka Masumbwe inayotuunganisha Watanzania na watu wa Uganda na Mikoa jirani ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora mpaka Dar es Salaam, ijengwe kwa kiwango cha lami. Watanzania wa maeneo haya na wenyewe wangependa kufaidi keki ya nchi hii kwa kupata sehemu ya keki hiyo kupitia barabara ya lami kwenye barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara ya kutoka Kahama mpaka Geita, nashukuru ipo kwenye bajeti ya
mwaka huu, naomba utekelezaji wake ufanyike haraka iwezekanavyo. Pia, niende haraka sasa, niseme tu kwamba Bandari ya Dar es Salaam ndiyo lango kuu ambalo nchi nyingi zinategemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati wa uongozi wake, ahakikishe yale magati namba moja mpaka saba, uchimbaji wake ufanyike kwa haraka; na gati namba 13 na 14 ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele kila wakati katika Bunge hili, ujenzi wake ukamilike. Bandari za Tanga, Bagamoyo na Mtwara, nazo zipewe umuhimu wa pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa standard gauge hatua ya kwanza umeanza, naomba na mchakato wa hatua zile nyingine zilizosalia ukamilike ili kwamba ile ndoto ambayo tumekuwa tukiiwaza kwa muda mrefu, Tanzania inayokwenda kuwa na barabara nzuri na treni inayokwenda kwa kasi inayotumia umeme, iweze kufikiwa kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii inayo majaliwa ya kuwa na madini mengi; tuna Mchuchuma, Liganga, tuna nickel kule Kabanga na graphite kule Lindi. Maeneo haya yote uchimbaji wake utategemea sana miundombinu ya barabara na Reli zitakazojengwa na Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwatie moyo tu viongozi wa Wizara hii, wapige kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ununuzi wa ndege mpya, nalo ni maono mapya ya Mheshimiwa Rais wetu, nayo yanafanyiwa kazi. Tumuombee Mungu ndoto yake hii iweze kutimia katika kipindi cha uongozi wake. Ndiyo Tanzania mpya hiyo itakayokuwa na Shirika la Ndege la Kimataifa na ndiyo tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na niunge mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ardhi katika maisha ya mwanadamu ndiyo rasilimali msingi katika maendeleo ya mwanadamu kwa vile miundomisingi yote hufanyika juu ya uso wa nchi. Uso wa asili, maji, barabara, Maziwa, reli, makazi na shughuli za kilimo, wanyama wa kufugwa pamoja na pori la akiba na hifadhi zote ziko juu ya uso wa nchi na kwa ajili hiyo basi ni vema Serikali kupitia Wizara hii ikajipanga kikamilifu kupata mipango miji iliyosanifiwa kikamilifu na kuendelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Ardhi nchini ikiwemo kubwa kabisa uhaba wa wataalam pamoja na vitendea kazi hali inayopelekea kutokuwepo kwa matumizi bora na endelevu ya ardhi mjini na vijijini. Ongezeko la watu pamoja na mifugo ni changamoto nyingine kubwa inayopelekea mwingiliano wa shughuli za kibinadamu kwa maana ya wakulima na wafugaji pamoja na changamoto ya ucheleweshwaji wa malipo ya fidia kwa wananchi ambao ardhi yao inatwaliwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji. Katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda maeneo ya kimkakati kama vile, special economic zone na kadhalika. Uharibifu wa mazingira vile vile hufanyika juu ya uso wa nchi. Hivyo basi, ipo haja kwa Wizara hii kuwezeshwa kiutendaji kwa kuongezewa bajeti yake ili iweze kuajiri wataalam wengi zaidi pamoja na vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yetu ya Mbogwe tunayo nafasi nzuri sana ya kuweza kujipanga vizuri katika Sekta hii ya Ardhi kwa vile wilaya yetu ni mpya kabisa hata ujenzi holela haujawa wa kiwango cha juu. Tunachohitaji Wilaya na Halmashauri ya Mbogwe ni kuunga mkono katika jitihada za kuipima ardhi yetu. Hivyo basi, tunaiomba Wizara ituangalie wananchi wa Mbogwe kutupatia Afisa Mipango Miji ili asaidie katika kupanga kitaalam wilaya yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jitihada za kupata maendeleo katika shughuli za upimaji Wilayani Mbogwe Mfuko wa Jimbo umechangia ununuzi wa kifaa cha upimaji kiitwacho Total Station, kinachotakiwa kingine kiitwacho differential ili tuweze kukamilisha uchapishaji wa upimaji wa ardhi hasa viwanja na mashamba ya wananchi na hatimaye waweze kumilikishwa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipongeza kwa dhati Shirika la Nyumba NHC kwa kazi nzuri sana linazozifanya. Naishauri Serikali kuliwezesha Shirika hili ili liweze kujenga nyumba nyingi zaidi nchini ikiwepo Wilayani Mbogwe. Naunga mkono juhudi na jitihada zinazoendelea kufanywa na Wizara hii. Ombi, letu Mbogwe ni kupewa Afisa Mipango Miji katika Halmashauri ya Wilaya Mbogwe pale Wizara itakapoanza kuajiri watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019. Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kujenga uchumi wa kisasa unaoongozwa na falsafa ya uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na sera msingi ya kuimarisha miundo msingi ya uchumi ikiwemo kujenga reli ya kisasa ya standard gauge, ununuzi wa ndege moja kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kuanzisha mchakato wa kujenga bwawa la kuzalisha umeme megawatt 2,100 ili kuunganisha nguvu za uzalishaji umeme kwa kutumia maji na ule wa kutumia nguvu za gesi asilia ili kuwezesha ujenzi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kwa kiwango kikubwa pia kuboresha na kuboresha bandari zetu katika mwambao wa bahari ya hindi na zile za maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa. Lengo kuisaidia nchi yetu kuwa kiongozi katika kukuza biashara katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa jitihada zinazozifanya za kuboresha huduma za afya kwa Watanzania ambapo vituo vya afya na hospitali nchini zimeboreshwa kwa kuongeza vifaa tiba, madawa na wataalam na matokeo yake vifo vya akinamama na watoto vimepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naiomba Serikali iongeze nguvu katika kukiimarisha kitengo cha kukabiliana na maafa hasa baada ya nchi yetu kuanza kutishiwa na matukio na matishio makubwa ya majanga ya kiasili ambapo siku za karibuni tumeshuhudia matukio ya matetemeko ya ardhi yametikisa maeneo ya nchi yetu hasa katika kanda ya ziwa Mkoani Kagera na hata tarehe 25 Machi, 2018, Kata za Ngemo na Ushirika zilipatwa na janga la kupigwa na tetemeko la ardhi ambapo madhara katika majengo ya Taasisi za Umma na watu binafsi yaliathiriwa vibaya na watu kujeruhiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo cha kuratibu na kukabiliana na maafa kiimarishwe maana kutokana na mabadiliko ya tabianchi tumeanza kuona vimbunga kutokea baharini vikianza kulikaribia bara la Afrika ikiwemo nchi yetu kuhusiana na vita dhidi ya madawa ya kulenya. Naipongeza Serikali kwa namna inavyokabiliana na janga hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naishauri Serikali kuongeza jitihada za kusambaza dawa za kutibu waathirika wa dawa za kulevya yaani methadone dawa hizi ziweze kupatikana katika Wilaya nchini. Naipongeza sana Serikali kwa jitihada zake za kutupatia fedha shilingi milioni 800 kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya viwili vya Iboya na Masumbwa ambapo ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naishukuru sana Serikali kwa jitihada zake za kuanza ujenzi wa hospitali ya Wilaya na ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe pamoja na Ofisi na Makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kujadili na kutoa mchango wangu katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kuhusiana na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Wasaidizi wake kwa kuja kwa wakati na mpango mzuri wa mapendekezo haya. Mimi katika kuchangia niseme tu kwamba vipaumbele ambavyo vimewekwa na Serikali katika miradi ambayo itapewa kipaumbele, nami nipendekeze kwamba suala zima la ujenzi wa Mji Mkuu wa nchi yetu wa Dodoma liwekwe katika mipango ya Serikali, jambo hili liwe la kudumu, ili kwamba kwa sababu huko mbele hatuna mpango mwingine tena wa kuja kuhamisha Makao Makuu ya nchi yetu kutoka hapa tulipo Dodoma kwenda sehemu nyingine, basi maandalizi yawepo ya Serikali ya muda mrefu ya kuhakikisha kwamba Mji huu unapangwa vizuri. Mji huu uje uakisi Tanzania mpya ambayo tunaitarajia kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ninaiomba sana Serikali ije na mpango mkakati kabambe kabisa wa kuhakikisha kwamba Mji huu unapimwa, unawekewa miundombinu yake halisi ambayo ita-reflect uwepo wa Dodoma mpya, Dodoma ambayo itakuwa na miundombinu mizuri ya zile gari ambazo zinaendeshwa kwa umeme hapa Dodoma, flyovers ambazo tunaziona kwenye nchi za wenzetu zijengwe Dodoma, Dodoma hii iwe na uwanja wa ndege ambao ni wa kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo niombe Serikali iliangalie eneo la uwanja wa ndege la Msalato kama eneo lenyewe linaweza lisiwe kubwa sana basi Serikali ione uwezekano wa kupanua eneo hilo ili kusudi tuepukane na uwezekano wa baadae kuja kuanza kubomolea watu, kufidia watu na kuwahamisha katika miaka mingine ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya nikijua kabisa kwamba nchi hii ni yetu wote na kwa maana hiyo tufikiri sana, niombe sana kwamba yale maeneo ambayo yanatengwa kwa ajili ya ujengaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali ya nchi hii, hata maeneo Maalum kama strategic cities au satellite cities kama kule Kigamboni inavyofanyika kule Dar es Salaam, na hapa Dodoma mipango hiyo iwepo, tusije tukachelewa tukaja tukafika mahali sasa tukajikuta kwamba sasa tunapotaka kujaribu kufanya master plan nyingine mpya tunaanza kujikuta tupo kwenye crisis. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali yangu iwe makini kabisa katika kuhakikisha kwamba tunapokwenda na mipango hii mizuri, ujenzi wa miundombinu ya umeme, kwa mfano hiyo Stiegler’s Gorge kwa maana hiyo tuna uhakika wa kuja kupata umeme wa kutosha na Tanzania ya viwanda inaelekea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kusema ni kuhusiana na kuiomba Serikali ijiandae kuweka taratibu nzuri kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya mpya, kuna maeneo mengi watu wanakaa kwenye majumba ambayo kwa kweli hayastahili. Kwa mfano, katika Halmashauri yangu ya Mbogwe, Ofisi ya Halmashauri ni jengo ambalo lilikuwa guest house zamani, sasa ukiangalia kwa kweli haikubaliki. Niombe kwa kweli Serikali ifanye utaratibu iweke katika mipango yake kuhakikisha kwamba maeneo kama haya mapya yanapata ofisi na nyumba za wafanyakazi ambazo zinalingana na hadhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa pia kuishauri Serikali ni kuhusiana na viwanda vya mbolea. Nchi hii ni nchi inayotegemea kilimo kwa kiasi kikubwa na bahati nzuri Serikali yetu na nchi yetu imejaliwa kupata gesi ambayo ni malighafi nzuri ya kuweza kutumika katika ujenzi wa viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali jambo hili iliangalie na ilione kwamba ni jambo la msingi, iwa- encourage watu wanaoweza kuja kuwekeza katika sekta hii ya viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea inatumika katika mazao yote; mazao ya chakula na mazao ya biashara yanategemea sana mbolea, Sasa mbolea ikipatikana kwa bei rahisi maana yake uzalishaji utakuwa ni wa hali ya juu na uzalishaji ukishakuwa mzuri maana yake sasa hata hiyo Tanzania ya viwanda ambayo itakuwa inahitaji malighafi kutoka kwa wakulima itashamiri kwa wepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo ninaunga mkono hoja zote ambazo zimeletwa na Serikali za kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa viwanda hivyo vya makaa ya mawe, kufua chuma kule Liganga na ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge, ni ukombozi na zaidi niiombe Serikali iendelee na upanuzi wa bandari zote zilizopo kule Tanga, Bagamoyo, Dar es Salaam pamoja na kule Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara kuna bandari moja nzuri sana, Kamati yetu ilitembelea kule, ile bandari nadhani Mungu aliiumba pamoja na ile Dar es Salaam kwa sababu namna ambavyo Bandari ya Mtwara ilivyokaa imekaa sawa sawa na Bandari ya Dar es Salaam, hiyo ni ishara kwamba Mungu anaendelea kutupenda na hivi ni vitu ambavyo anatujaalia tuvitumie katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inaanza kuwa ni center ya maendeleo kwa nchi nyingine za jirani zinazotutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mungu aibariki Serikali yetu na Mungu awabariki wote mlionisikiliza. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kukushukuru wewe Mwenyekiti wetu kwa kunipatia nafasi siku ya leo nami niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/2018 kama ilivyowasilishwa na Waziri wetu Dkt. Philip Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu la Tanzania limekuwa ni Taifa la mfano katika dunia hii. Taifa letu limejitoa muhanga katika kuwakomboa Waafrika wenzetu katika nyanja za kiuchumi na kisiasa. Sisi kama Taifa tumetumia utajiri wetu kuhakikisha kwamba wenzetu wanajikomboa. Sasa wakati umefika na wakati wenyewe unamweka mbele Rais wetu Dkt. John Magufuli kuvipigana upya vita vya uchumi, ndiyo maana ameamua sasa kuhakikisha kwamba madini na rasilimali zetu zote zinanufaisha Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema neno moja kwamba Mwenyezi Mungu ametujalia sana na ametupenda akatupatia rasilimali nyingi na hasa nijikite katika suala zima la vyanzo vya nishati ya umeme. Nishati ya umeme ndiyo msingi wa mambo mengi iwe kilimo, iwe ujenzi, iwe kila kitu ukiwa na umeme wa uhakika utajenga viwanda na ukiwa na umeme wa uhakika utafanikiwa katika mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo Mungu katupa gesi, Mungu katupa maji, tunao upepo, tunalo jua la kutosha. Hivyo, niombe Serikali ihakikishe tu kwamba kwa kweli suala zima la uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vyote hivyo ikiwemo makaa ya mawe yatumike katika kuhakikisha kwamba umeme unapatikana kwa wakati na kwa wingi unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali yangu kwa kuhakikisha kwamba tunaanza mara moja ujenzi wa Reli ya Kati kwa standard gauge. Kuwepo kwa usafiri wa reli ya kati ambao uko katika standard gauge ni ukombozi wa aina yake katika Taifa letu la nchi jirani za Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu hiki cha bajeti cha Mheshimiwa Mpango nizungumzie habari ya Bandari ya Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam imekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ile changamoto ya kodi ya ongezeko la thamani kwa usafiri wa bidhaa zinazokwenda nchi za nje.

Mheshimiwa Waziri amesema inakuwa sasa inachajiwa asilimia sifuri ya VAT, yapo malalamiko pia kwa upande wa mawakala wa meli zinazoleta mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam nao wanalo lalamiko linalofanana na hili kwamba VAT inatozwa kwa mawakala hawa na hawa mawakala wanapochajiwa wanaweka hiyo chaji kwenye wamiliki wa zile meli, kwa maana hiyo gharama za uendeshaji katika Bandari ya Dar es Salaam zinaonekana kwamba ziko juu zaidi na wenye meli wanakuwa wana-opt kwenda kwenye bandari zingine za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba na hao mawakala wa meli katika Bandari ya Dar es Salaam na wenyewe wachajiwe kiwango cha asilimia sifuri ili kuhakikisha kwamba hizo meli zisije zikawa zinaelekezwa upande mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozunguzia habari ya ujenzi wa viwanda ni pamoja na viwanda vya mbolea ambavyo tumehaidiwa kwamba kwa sababu tumepata gesi hapa Tanzania na kwa maana hiyo Mtwara na Lindi tungeweza kupatiwa viwanda vya mbolea. Kwa bahati mbaya sana sioni hapa kwamba hizi jitihada za kuweza kujenga hivi viwanda vya mbolea ambavyo vingeweza kukuza kilimo chetu katika Taifa hili vimewekwa katika sehemu gani. Nimwombe Mheshimiwa Waziri aliangalie jambo hili kwa jicho la pekee kwa sababu kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa hili na Watanzania walio wengi wameajiriwa katika sekta hii muhimu ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuiomba Serikali katika Wizara ya Nishati na Madini, katika Jimbo la Mbogwe tunao wawekezaji ambao wamekuwa wanafanya utafiti kwa muda mrefu katika eneo la Nyakafuru, naomba mara moja kwa kweli na hawa watu wamulikwe ili kuhakikisha kwamba madini yaliyopo katika Wilaya yetu yanawanufaisha wananchi wa Wilaya ya Mbogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia na kwa mara nyingine naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya nchi nzima. Wilaya yetu ya Mbogwe tumebahatika kupatiwa jumla ya shilingi milioni 800. Kituo cha Afya Masumbwe kimepatiwa shilingi milioni nne na Kituo cha Afya Iboya shilingi milioni 400; fedha hizi zimetengwa mahususi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya upasuaji, nyumba za waganga, nyumba kwa ajili ya maabara na famasia na majengo kwa ajili ya kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali kwa mikakati yake pia ya usambazaji wa dawa muhimu za binadamu kupitia MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu ya Awamu ya Tano inafanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha kuwa tunapata magari kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa (ambulances).

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kutupatia magari ya kubebea wagonjwa katika vituo vyetu viwili vya afya vya Iboya na Masumbwe. Hongera sana Serikali kwa kazi nzuri. Aidha, nashauri Serikali iendelee na mkakati wake wa kuunga mkono jitihada za wananchi kujenga na kumalizia majengo ya vituo vya afya na zahanati katika vijiji na kata mbalimbali Wilayani Mbogwe. Wilaya ya Mbogwe inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na Hospitali ya Wilaya. Naomba sana Serikali itoe fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hii ya Wilaya ili kusaidia utoaji wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya afya na zahanati Wilayani Mbogwe ili kupunguza utegemezi wa wagonjwa wa Wilaya yetu kutibiwa katika Hospitali za Wilaya za Bukombe, Kahama na Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua Serikali yetu inafanya kazi kubwa sana kuhakikisha afya za Watanzania walio wengi zinaboreshwa. Ninaamini wazi kuwa siku za usoni Taifa letu la Tanzania litakuwa likitoa huduma bora zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali zetu za Jakaya Kikwete, Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili zimepata sifa kutokana na utoaji wa huduma bora kabisa za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya viwanda itajengwa na Watanzania wenye afya bora na kwa hakika Wizara ya Afya imejipanga vyema kuhakikisha nchi yetu inakuwa na Watanzania walio na afya bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali iendelee kutoa kipaumbele katika kutoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha miradi ya maendeleo katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za uhaba wa watumishi, vifaatiba na madawa zinapaswa kushughulikiwa ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana karibu kabisa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi ili kusudi na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipende tu kuwapa pole wananchi wangu wa Kata za Ngemo na Ushirika waliopata tatizo la kuharibikiwa nyumba zao kutokana na tetemeko lililotokea tarehe 25 Machi, 2018. Kwa maana hiyo, nipende tu kuishauri na kuiomba Serikali iendelee na utaratibu ule uliotajwa katika ukurasa wa 69 katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inayohusiana na uratibu wa maafa, kwa maana ya kwamba mabadiliko ya tabianchi katika nchi yetu yamekuwa yakileta madhara kwa maana ya kwamba mpaka sasa tumejikuta mambo ambayo yalikuwa hayapatikani katika nchi yetu sasa yameanza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona tetemeko la ardhi lilitokea Kagera na sasa katika Wilaya ya Mbogwe tumepata tatizo hilo tarehe 25 usiku na kwa maana hiyo inaonesha kwamba huenda majanga kama haya yakaendelea kutokea. Kwa hiyo, naishauri Serikali iendelee kujiimarisha zaidi ili kwamba mambo haya yatakavyojitokeza katika kiwango ambacho siyo cha kawaida tuweze kukabiliana nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu sasa kwa kuanza kuipongeza kwanza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Pombe Joseph Magufuli akisaidiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Suluhu Hassan pamoja na Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. Serikali hii inafanya kazi nzuri, tuwe wakweli na tuache habari ya ushabiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za Serikali hii ni zile ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele ndani ya Bunge hili, tumeiomba sana Serikali ijenge reli kwa kiwango cha Standard Gauge, kazi hii imefanywa, upanuzi wa Bandari ya Dar es salaam Serikali inaendelea kufanya. Tumezungumzia habari ya Shirika la Ndege, watu wote humu tumekuwa tukipiga kelele, Serikali imesikia na ndege hizo imeanza kuzileta, lakini sasa naona tena watu wanaanza kugeuka kuwa vinyonga. Tunayoyazungumza humu yanapoanza kutekelezwa tunageuka tena tunaona kwamba Serikali haifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali iendelee na mpango wake wa kuwaletea maendeleo Watanzania. Watanzania hawa wanapenda sana kuona kwamba nchi yao ambayo imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi, ni nchi nzuri na ina kila kitu. Kilichokuwa kinakosekana ni namna gani ambavyo tumejipanga kuweza kuzitumia rasilimali tulizonazo hapa nchini kuweza kujikomboa kiuchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imekuwa ni Serikali sikivu, tunaona namna ambavyo Serikali inaendelea kusambaza umeme kila mahali. REA Awamu ya Tatu inaendelea vizuri, hata katika Wilaya ya Mbogwe kazi zinaendelea na wananchi wanaona kwa macho yao na siyo tu Mbogwe ni Tanzania nzima miradi hii inaendelea kufanyiwa kazi na watu wanaona. Wakati mwingine niseme tu kwamba watu wanaamua kufanya ushereheshaji, mtu anaiona kazi lakini anaamua kugeuza na kuanza kubeza. Niiombe Serikali iendelee mbele wala isigeuke nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha niiombe Serikali kwa sababu ni Serikali yetu wote iendelee kuona utaratibu wa namna ya kuzisaidia Wilaya na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa kazi zinazofanywa na Wizara hii katika sekta zote za ujenzi, uchukuzi na mawasiliano. Kazi nzuri zimefanyika katika sekta ya ujenzi, barabara nyingi zimejengwa kwa kiwango cha lami na kiwango cha changarawe pamoja na madaraja makubwa ya nchi hii. Sasa kuna maandalizi kati ya Kigongo - Busisi kwa kuwa daraja hili linachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki na kati za Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, DRC na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa daraja la Kigongo - Busisi kutaleta mapinduzi katika sekta ya uchukuzi kwani kwa sasa usafiri wa vivuko vya MV Sengerema na MV Misungwi vinazidiwa na wingi wa magari ya mizigo na magari ya abiria na kwa hakika ujenzi wa daraja hili litaleta tija. Pamoja na mgawanyo wa mamlaka za Wakala wa Ujenzi wa Barabara wa TANROADS na TARURA, bado naiomba TANROADS waendelee na utaratibu wa kuunganisha Mkoa wa Tabora kupitia Wilaya ya Urambo, Kaliua, Mkoani Tabora na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkoani Shinyanga Wilaya ya Mbogwe hadi Mjini Geita, Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza TANROADS Mkoa wa Geita chini ya uongozi wa Meneja, Haroun Senkunku na msaidizi wake Ndugu Maribe pamoja na watumishi wote wa TANROADS Mkoa wa Geita wanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano. Ujenzi wa barabara zote zinazojengwa na kusimamiwa na TANROADS Mkoa wa Geita zina kiwango cha kuridhisha. Ninachoomba na kushauri ni TANROADS kukichukua kipande cha Iboya – Bwendamwizo – Nyikundu - Ivumwa hadi Migo Wilayani Geita inaendana na barabara ya lami inayotokea Mjini Kahama kwenda Geita Mjini ambako ni Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ione umuhimu wa kuimalizia barabara hii kwa kuwa kupitia Kikao cha Bodi ya Ushauri cha Mkoa wa Geita tuliomba barabara kutoka mji wa Ushirombo hadi Mbogwe kwenda Geita Mkoani, kilichotokea kipande ni sehemu hii ya maombi yetu ilichukuliwa na kipande cha Iboya - Bwendamwizo - Nyitundu - Ivumwa hadi Wigo kuelekea Mkoani Geita kiliachwa. Hivyo, naiomba Wizara isikie kilio chetu ikipandisha hadhi kwenda TANROADS ili Wilaya ya Mbogwe ipate barabara ya kuunganishwa na Mji Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa za ujenzi wa bandari, reli, viwanja vya ndege, madaraja makubwa na meli za vivuko katika maeneo mbalimbali nchini. Hongereni sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri ambazo imeendelea kuzifanya. Serikali yetu kupitia Wizara hii imekuwa ikitenda haki. Niseme kabisa kwamba hata katika Wilaya yetu ya Mbogwe TANROAD kwa maana ya Mkoa wa Geita chini ya uongozi wa Meneja wa Mkoa, Bwana Haruna Senkuku na Wasaidizi wake wamefanya kazi nzuri sana katika kuhakikisha kwamba Wilaya yetu mpya ya Mbogwe inapata barabara za Mkoa na kuifungua katika upya wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo hiyo barabara kutoka Butengoromasa kupita Iparamasa - Mbogwe mpaka Masumbwe. Barabara hii tumeomba ikapandishwa hadhi na zaidi sana tunaomba Wizara iendelee na mchakato wa kuweza kuifanyia usanifu wa kina na upembuzi yakinifu ili kusudi ikiwezekana iweze kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuweza kufungua mawasiliano ya muda wote wakati wa masika na wakati wa kiangazi, barabara hii iweze kupitika kwa urahisi na kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisemee pia kuhusu barabara iliyopandishwa hadhi ya kutokea Ushirombo kwenda Makao Makuu ya Wilaya ya Mbogwe kuelekea Mkoani Geita. Hapa namwomba Mheshimiwa Waziri atusikilize vizuri kwa maana ya kwamba barabara hii tulikuwa tumeomba ichukuliwe na TANROAD kutoka Ushirombo kupita Bwera kwenda mpaka Wigo ambapo barabara hii inakutana na barabara ya kutoka Kahama kwenda Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, TANROAD wamechukua sehemu ya barabara hii. Sasa nikaiomba Wizara, kwa nini isitusaidie kuchukua tena hiki kipande cha kutokea Iboya kwenda Wigo ili kusudi barabara hii iwawezeshe Wanambogwe kwenda Mkoani Geita Makao Makuu ya Mkoa wetu wa Geita?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Waziri atumie wataalam wake waende kukagua hii barabara, ikiwezekana basi ikamilishwe kwa sababu imechukuliwa kipande kwa kupitia Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Geita. Tulikuwa tumeomba hii barabara ipandishwe lakini Wizara kwa busara zao wamechukua nusu. Tunaomba tu Wizara ichukue hatua za ziada ili kuweza kuikamilisha hii barabara, itakuwa imefanya jambo la msingi sana.

Mheshimwi Mwenyekiti, naomba pia Wizara itutazame tena kwa upya ili Mkoa wetu wa Geita uweze kuunganishwa na Mkoa wa Tabora kupitia Wilaya ya jirani kwetu kwa ndugu yangu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa. Huyu ni jirani yangu na naomba sasa kwa kweli waangalie uwezekano wa kutupandishia hii barabara kutoka Masumbwe kupitia Ushetu kwenda Kaliua mpaka Urambo. Hii barabara itatusaidia sana Wana-Geita kuweza kuunganishwa na Mkoa wa Tabora na Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa kwamba kwa uangalizi mzuri wa Mheshimiwa Profesa Mbarawa, barabara hii itapandishwa na itatusaidia sana katika kuhakikisha kwamba Mkoa wetu Mpya wa Geita na wenyewe unaenda kwa kasi katika nchi yetu hii ambayo tunaitarajia kuwa nchi ya viwanda katika muda mchache ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tena kuhusiana wa ukurasa wa 33 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Kuna utaratibu wa kujenga daraja la Busisi Kigongo. Daraja hili liko katika barabara ya Geita Usagara. Daraja hili kwa kweli endapo Serikali itafanikiwa kulikamilisha, naamini kwamba barabara hii ya kutoka Geita - Kagera mpaka Musoma Mkoani Mara, itakuwa ni ufumbuzi mkubwa sana katika suala zima katika ukuzaji wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba daraja hili endapo Mungu akitujalia likakamilika litakuwa ni sehemu ya Utalii, maana ni sehemu ambayo kwa kweli kimsingi ujenzi ukikamilika litakuwa ni la aina yake, kama ambavyo sasa hivi kuna daraja hilo la Kigamboni, hata hili la Kilombero pamoja na daraja la Mkapa, yamekuwa ni madaraja ambayo ni ya mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu wazi kwamba habari ya Wizara hii siyo ya kubahatisha. Kikwetu huwa tunasema hii ni Wizara ya mashikolomageni. Hii Wizara ni ya vitu vipya. Wizara hii imekuwa ikituletea flyovers, madaraja ambayo hayajawahi kuonekana katika Afrika Mashariki na Kati. Kwa hiyo, nawaombea Mungu aendelee kuwapa ujasiri, waendelee mbele, watutendee haki kwa kututoa kimasomaso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma tulikuwa tunaonekana kama watoto yatima, nchi kubwa kama Tanzania inakosa ndege. Kwa maana hiyo, kwa kweli tulikuwa tunadhalilika, wakati mwingine tunapita nchi jirani ya Kenya kwenda Dar es Salaam. Unatoka Mwanza unakwenda Nairobi, halafu ndiyo unakwenda kuzunguka kwenda Dar es Salaam. Ilikuwa ni aibu kubwa. Kutokana na ujasiri wa Wizara hii pamoja na wakala mbalimbali akiwemo Bwana Mfugale, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema jambo hili kwa nia njema kabisa na ninaamini kila Mtanzania mwenye nia njema atawaombeeni kwa Mungu ili kusudi kwa kweli wapate thawabu hata siku ya mwisho, maana wanatuletea mambo mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala zima la ujenzi wa reli ya standard gauge. Hatua iliyofikiwa na Serikali ni nzuri na niseme tu kwamba hata ile reli ya kutokea Isaka kwenda Kigali Rwanda mpaka Msongati, naomba Mheshimiwa Waziri wetu aiangalie reli hiyo na yenyewe iweze kuchukuliwa hatua tuone mwelekeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunayo reli ya kutokea Dar es Salaam mpaka Arusha pamoja na Mkoani Mara, Serikali ilione hilo ili nchi yetu iweze kupiga hatua kwa hatua, kwa maana kwamba kuwe na balance ya maendeleo sehemu katika mbalimbali za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Pamoja na juhudi kubwa sana za Serikali ya Awamu ya Tano za kuifanya Tanzania kuwa Taifa la uchumi wa kati kupitia sera ya Tanzania ya viwanda, sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano inao mchango mkubwa katika mwelekeo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kujenga barabara za lami, madaraja makubwa, reli ya kisasa standard gauge, upanuzi wa bandari, ununuzi wa meli mpya katika maziwa yetu makuu pamoja na vivuko, ujenzi wa flyovers Jijini Dar es Salaam na mipango ya kuendeleza ujenzi kama huo Jijini Mwanza na Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Serikali kwa mpango wake wa kuendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi, hatua hii ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa kanda ya ziwa na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki
na nchi za Afrika ya Kati kwani daraja hili litarahisisha usafirishaji wa watu na mizigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe tunaipongeza Serikali kupigia TANROADS Mkoa wa Geita chini ya uongozi madhubuti wa Meneja wa TANROADS Mkoa Ndugu Haroun Senkunku na msaidizi wake na watumishi wote wa TANROADS Mkoa wa Geita kwa kazi nzuri ya kupigiwa mfano.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha napenda kuuliza, je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimaye kuanza kujenga kwa kiwango cha lami kwa barabara za Butengolimasa – Iparamasa – Mbogwe hadi Masambwe, barabara ya Katoro – Lulembela hadi Ushirombo na barabara ya Ushirombo hadi Bwehwa – Mbogwe ili kusaidia kukuza uchumi wa wananchi wa Wilaya yetu ya Mbogwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika Tanzania mpya ni hakika na siyo nadharia. Naipongeza kwa hakika Serikali kwa wazo la kushirikiana na Serikali ya Rwanda kujenga reli ya standard gauge kutoka Isaka – Kigali – Msongali. Reli hii itakuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi baina ya nchi zetu mbili za Tanzania na Rwanda, naiombea mafanikio mipango yote ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ununuzi wa ndege na kulifufua shirika letu la ndege la ATCL kutaweza kuchangia katika kuitangaza nchi yetu kimataifa na kuleta tija katika sekta ya utalii kutokana na Taifa letu kuwa na vivutio vngi vya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe pia Serikali itupie jicho ujenzi wa uwanja wa ndege wa mjini Geita uliopo eneo la Buhalahala, Geita ili kuiwezesha sekta ya usafiri wa anga kuchangia iwezekanavyo kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na wale wa maeneo jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza ni hatua chanya katika kurahisisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda kwa sekta ya utalii na ukuzaji wa uchumi kwa ujumla wake. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kuendelea na hatua kama hizi kwa viwanja vyote vikubwa vya ndege vya KIA, JNIA Dar es Salaam, Songwe na viwanja vingine vya ndege nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe pia Serikali kuendelea na upanuzi wa bandari katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa na kwa Mkoa wa Geita Bandari za Pores, Nungwe, Nkome, Chato, Nyamirembe na Bukondo. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Pamoja na pongezi hizo ninapenda kuiomba Wizara, Wilaya yetu ya Mbogwe ipo katika mchakato wa kuanzisha kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Mbogwe, je, Serikali haioni kwamba muda umefika sasa kuhakikisha kwamba shule ya sekondari Mbogwe inafunguliwa rasmi hasa baada ya ujenzi wa mabweni na bwalo tayari vimekamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo ni kutokuwepo kwa chanzo cha uhakika wa maji, niiombe Serikali itoe kipaumbele cha kuifungua shule hii ya Mbogwe haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu ni muhimu kuanzishwa kwa vyuo vya ufundi katika kila Wilaya, niiombe Serikali yetu ihakikishe chuo cha ufundi kinaanzishwa katika Wilaya yetu ya Mbogwe, pia tunaiomba Serikali itoe kipaumbele katika kuhakikisha kuna kata tunazojitahidi kukamilisha shule zao za kata za Wanda, Isebya na Ngemo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitahidi sana katika kuchangia nguvu zao katika kujenga madarasa na maabara pamoja na nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ni changamoto kubwa. Kuna upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi, niiombe Serikali itupatie ili hatimaye vyuo vya ufundi viweze kupata wanafunzi wazuri wa kuweza kujiunga na vyuo hivi vya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha naiomba Serikali kuhakikisha inatusaidia kupatiwa fedha zaidi ili kuhakikisha nyumba za walimu pamoja na vifaa vya kujifunzia ikiwa ni pamoja na vitabu na vifaa vya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa mkakati wake wa kutoa elimu bure kwa elimu ya msingi hadi sekondari. Naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Engineer Isack Kamwelwe ambaye kwa upendo mkubwa aliweza kufanya ziara ya kikazi Mkoani Geita na hatimaye alifika Wilayani Mbogwe ambako alitembelea Mradi wa Maji wa Mji wa Masumbwe na kutembelea Makao Makuu ya Wilaya ya Mbogwe eneo la Kasosobe ambako alielezwa juu ya uhaba wa maji ulivyo mkubwa kiasi kwamba kila mahali panapochimbwa visima virefu vya maji, maji yamekuwa hayapatikani na matokeo yake ni upotevu wa nguvu, pesa na muda mrefu bila kupata maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu la muda mrefu limekuwa ni kuiomba Wizara kutusaidia kupatikana kwa maji toka Ziwa Victoria, maji ambayo tayari yamefikishwa katika Wilaya jirani ya Kahama na Mheshimiwa Waziri kwa uungwana wake aliahidi kulifanyia kazi ombi hili muhimu. Sisi wananchi wa Wilaya ya Mbogwe tunayo matumaini makubwa na Waziri katika kuhakikisha kwamba tunapata maji ya uhakika toka katika chanzo cha KASHWASA. Wananchi wa Wilaya ya Mbogwe hatuna msaada mwingine isipokuwa kwa Waziri na Serikali yetu, tunaomba msaada.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Mbogwe amewasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya kuomba pesa kwa ajili ya kuunganisha umeme katika vyanzo vya maji vya visima virefu katika vijiji vya Bulugala, Lulembela, Shenda na Masumbwe. Imani yetu ni kwamba fedha zitatolewa kwa wakati ili Shirika la Umeme nchini liweze kufunga umeme katika vyanzo hivi vya maji ambavyo vinatumia mashine zinazotumia dizeli, matokeo yake ni gharama kubwa za uendeshaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingine ya uchimbaji wa visima katika maeneo ya Luhala, Kabanga, Ilolangula na Iponya iko mbioni kukamilishwa. Tunaiomba Serikali itoe fedha kwa wakati ili vyanzo hivi vya maji katika visima hivi vikamilike na kupunguza kadhia ya uhaba wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba Wizara itusaidie wananchi wa Wilaya ya Mbogwe kupatiwa wataalam na vitendea kazi hasa gari.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Hoja yangu katika mchango wangu ni kuishauri Serikali kwamba ijikite katika kujenga jeshi lenye nguvu kwa kujenga viwanda vya zana za kivita. Tanzania ya viwanda na ujenzi wa uchumi wa kisasa hauwezekani bila kuwa na nguvu za kijeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa mengi ulimwenguni yameundwa baada ya vita kupiganwa na zikawepo nchi mbalimbali na ambazo zimejikuta zikianza kujenga viwanda vyenye kulenga katika kulinda mipaka ya Mataifa husika. Kwa misingi hiyo, ni vyema Taifa letu likawekeza zaidi katika Viwanda vya Ndege za kivita, Viwanda vya Makombora, Viwanda vya Magari ya Kivita na Mitambo vikiwemo vifaru, magari na meli za kivita zikiwemo manowari (submarine).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujifunze kutoka Mataifa machanga ambayo yalitutangulia kupata uhuru kwa kipindi kifupi cha miaka kumi, mfano, Mataifa ya Uchina (1949), India (1948), Israel (1948) na Pakstani (1948). Mataifa haya yamefanikiwa pakubwa kwa kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha silaha kwa kushirikiana na Mataifa yaliyowatangulia katika utafiti, sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa yaliyotangulia ni pamoja na Marekani, Urusi, Ufaransa, Italia na hata Uingereza na Mataifa mengine ya Ulaya. Nafahamu jeshi letu linazo taasisi za Nyumbu na Mzinga. Naishauri Serikali kuhakikisha inazitengea taasisi hizi fedha za kutosha ili ziweze kuwekeza zaidi katika utafiti, sayansi na teknolojia, ikibidi kununua watalaam katika Mataifa yaliyoendelea katika nyanja za viwanda vya zana za kijeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifano kuhusu Mataifa mengine namna yalivyofanya. Marekani walimchukua Albert Cinstein Mvumbuzi wa bomu la nyuklia tokea Ujerumani na kulisaidia Taifa la Marekani kujiundia silaha za Kimarekani. Marekani pia wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuchukua teknolojia kutoka Taifa la Urusi na kinyume chake pia yaani Urusi kuchukua teknolojia tokea Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania haiko peke yake, inayo Mataifa rafiki ambayo yanaweza kuisaidia, kwani ni dhahiri haliwezi kusubiri mpaka kugundua silaha zetu wenyewe. Iran imekuwa ikisaidiwa na Urusi kuwa na viwanda vya silaha za kivita. Israel ikisaidiwa na Marekani kujenga viwanda vya silaha za kivita wakati wa Dola la Kisovieti. Wachina walimchukua mtaalam wa vita kutoka Ukraine akasaidia uundaji wa meli za kivita Uchina na ku-copy teknolojia kutoka Urusi. Vile vile Iran imepata teknolojia ya matumizi ya nuclear toka Urusi kwa kuwa tu Iran inao utajiri mkubwa wa mafuta ya Petrol.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo Tanzania ni tajiri mkubwa wa rasilimali kuanzia madini, gesi, maliasili na kadhalika. Kwa hiyo, kulingana na ukubwa wa nchi yetu na utajiri tulionao, ipo haja kubwa kwa nchi yetu kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika viwanda vya zana za kijeshi vya Mzinga na Nyumbu. Hatuna kisingizio hata kidogo. Ni muhimu sana kuwa na Sera ya Taifa ya Ulinzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ikiwekeza katika Sekta ya Ulinzi tukawa na viwanda kwa ajili ya ndege za kivita, meli za kivita, vifaru na ikiwezekana tuwe na matumizi ya amani ya madini ya Urani ambayo yanazalishwa nchini mwetu, maeneo ya Namtumbo na Bahi hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hizi hotuba mbili za Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Hotuba zote hizi zilizoletwa mbele yetu ni hotuba nzuri ambazo sisi kama wawakilishi wa wananchi tunao wajibu wa kuziunga mkono na kuhakikisha kwamba zinafanyiwa kazi ili Watanzania waweze kupata manufaa ambayo yamekusudiwa.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Mipango katika hotuba yake ya Uchumi wa Taifa katika mwaka wa fedha 2018/2019 ukurasa wa 28 mpaka 33 ameeleza miradi ya kielelezo. Miradi hii mingine tayari imeshaanza kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Jambo hili ni jambo la muhimu kwa ajili ya ujenzi wa Tanzania ya Viwanda. Viwanda vitakavyokuwa vinazalisha mali au vitendea kazi mbalimbali vitakavyokuwa vinazalishwa kwenye viwanda ambavyo tunavitarajia vitahitaji kusafirishwa na sehemu ya muhimu ya kuweza kusafirisha vitu hivi ni reli.

Mheshimiwa Spika, Tanzania yetu ni Tanzania ambayo ina Watanzania wengi ambao ni wakulima na tunahitaji malighafi za viwandani ambazo zilizo nyingi zinatokana na kilimo. Kwa maana hiyo, ushauri wangu ni kuishauri Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba sekta hii ya kilimo nayo inapewa kipaumbele, hasa kuhakikisha kwamba mbolea inapatikana kwa wingi na kwa bei ambayo ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ihakikishe kwamba viwanda vya mbolea vinajengwa hapa nchini kwa kasi kubwa. Kama ambavyo tumeona kiwanda kikubwa cha DANGOTE kimesaidia sana upatikanaji wa cement na kwa maana hiyo ujenzi wa nyumba na shughuli mbalimbali za ujenzi zimekuwa zikienda vizuri kwa sababu saruji inapatikana kwa bei ambayo ni rahisi kidogo.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, niombe tu Serikali iendelee kuhakikisha kwamba viwanda vya mbolea ambavyo tulikushudia vijengwe kutokana na kupatikana kwa gesi hapa Tanzania basi navyo vijengwe na vianze uzalishaji ili kusudi wananchi wetu waweze kuzalisha mazao ya biashara na chakula ili Tanzania ambayo tunaitarajia iwe Tanzania ya viwanda basi iwe na Watanzania ambao wanapata chakula na wanapata malighafi ambazo zinaweza zikafanyiwa kazi katika viwanda ambavyo vinazalishwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningeshauri Serikali yangu ni kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vya zana za kivita; katika Mkoa wa Morogoro tunavyo vya Mzinga na Nyumbu. Niseme kabisa wazi kwamba Tanzania ya viwanda haiwezekani bila kuwa na Tanzania ambayo imeimarika kiulinzi. Kwa maana hiyo, niombe Serikali ihakikishe kwamba Mashirika yetu ya Nyumbu na Mzinga yanapewa pesa ya kutosha na kwa wakati ili kusudi basi majeshi yetu yaweze kuwa na zana za uhakika pindi hali ya hewa itakapokuwa imebadilika basi tuweze kukabiliana nayo. Ijulikane wazi kwamba katika mataifa yote ambayo yamefanikiwa kiuchumi pia yapo imara kiulinzi. Naishauri tu Serikali ihakikishe kwamba upande huu na wenyewe unafanyiwa kazi na unaeleweka.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa kuja na mpango mwingine kabambe wa uzalishaji wa umeme. Najua kabisa kwamba sekta ya umeme ndiyo sekta mama ambayo inaweza kutusaidia kuhakikisha kwamba Tanzania yetu inakwenda haraka katika suala zima la ujengaji wa viwanda. Kwa hiyo, naunga mkono asilimia 100 ujenzi wa bwawa la uzalishaji wa umeme la Stiegler’s Gorge Serikali iendelee nalo na tuhakikishe kwamba tunakwenda kwa haraka sana ili tuhakikishe kwamba hizo megawatt 2,100 zinaingizwa katika Grid ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nalo linatakiwa kwa kweli Serikali ilipe kipaumbele ni suala zima la viwanda vya chuma Liganga na Mchuchuma kule. Tumekuwa tukizungumza jambo hili kwa muda mrefu sana na kwamba kwa wale ambao wamekuwa wakiangalia vyombo vya habari wamekuwa wakiona ni jinsi gani ambavyo Watanzania wanapata shida sana ya upatikanaji wa vyuma. Matokeo yake sasa wanaingia hata kwenda kuharibu miundombinu ya barabara, wanaenda wanaokota vyuma vya kwenye barabara hata kwenye reli kwa ajili ya kuuza kama vyuma chakavu. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba upatikanaji wa vyuma hapa nchini inaonekana ni mdogo na kwa hiyo kama supply inakuwa ni ndogo, matokeo yake sasa watu wanaamua kuchukua sasa scraper na vitu vingine ambavyo wakati mwingine ni vya maana kama alama za barabarani na zenyewe zinachukuliwa na kwenda kuuzwa kama vyuma chakavu ili kusudi viwanda vya vyuma viweze kufanya kazi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Tanzania ya viwanda bila kuwa na upatikanaji wa chuma kule Liganga na Mchuchuma kwa kweli tutakuwa bado ndoto yetu haitafikiwa kwa wepesi. Nije sasa katika suala zima la… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru niseme kwamba kwanza naipongeza Serikali tena kwa kuja na mpango wake wa kujenga Makao Makuu ya nchi yetu na kuifanya Dodoma kuwa Mji Mkuu na Mji ambao kwa kweli sasa hivi umepewa hadhi ya kuwa Jiji, niseme tu Serikali iendelee kutoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa mji huu ili uendelee kuwa mji wa kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2018/2019. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo mengi muhimu ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili na nusu cha uhai wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo wananchi wa Wilaya ya Mbogwe ni uhaba wa miundombinu ya majengo ya halmashauri pamoja na makazi na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Tunaiomba Serikali itusaidie kuhakikisha hospitali yetu ya Wilaya ya Mbogwe inaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanambogwe tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia huduma ya maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria maji ambayo tayari yako katika Wilaya jirani ya Kahama ambayo ni wilaya mama ya Wilaya za Bukombe na Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya mpya ya Mbogwe tunaipongeza Serikali kwa kutupatia jumla ya Sh.800,000,000 kwa ajili ya Vituo vya Afya vya Iboya na Masumbwe. Kila kituo kimepewa Sh.400,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu, wilaya yetu ya Mbogwe tayari inaendelea na ujenzi wa shule ya sekondari ya kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Mbogwe, hata hivyo shule hii imeshindwa kufunguliwa kutokana na uhaba wa upatikanaji wa maji. Tunayo matumaini makubwa kuwa Serikali itasaidia juhudi za uongozi wa wilaya katika kuhakikisha kuwa shule hii ya pekee ya kidato cha tano Wilayani Mbogwe inafunguliwa mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali kuongeza juhudi za kutupatia watumishi katika sekta za afya na elimu kwani tunao upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta hizi muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ambao ni Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini unafanya kazi zake vizuri, kinachotakiwa ni kuongeza ushirikiano baina ya idara hii na uongozi mzima wa wilaya ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Baraza la Madiwani ili kujenga umoja na mshikamano katika kutatua kero na matatizo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Wakala wa Maji Vijijini na Mijini ni wazo jema hasa ikizingatiwa kuwa wakala mbalimbali za Serikali zimeonesha mafanikio makubwa na kuwa na ufanisi wa kuwahudumia wananchi katika sekta hii muhimu ya maji hasa ikizingatiwa msemo usemao maji ni uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya mazingira ni jambo mtambuka kwani mabadiliko ya tabia ya nchi yamekuwa na athari mbaya kwa maisha ya mwanadamu na kusababisha ukame, uharibifu wa vyanzo vya maji, ukosefu wa mvua. Ni wajibu kwetu kama Taifa kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa kuanza jitihada za kupanda miti na kuihifadhi na kujiepusha na tabia ya ukataji miti ovyo. Aidha, naishauri Serikali kufanya jitihada za makusudi kuongeza matumizi ya nishati mbadala ya kuni na mkaa kwa kuwekeza zaidi katika matumizi ya umeme, umeme jua na gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uti wa mgongo wa Taifa letu limekuwa likitilia mkazo yaani kilimo, naishauri Serikali kuweka mkazo zaidi katika uwekezaji wa viwanda vya mbolea nchini hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na hazina kubwa ya gesi asilia ambacho ni chanzo muhimu cha malighafi ya utengenezaji wa mbolea. Mbolea ikipatikana kwa bei nzuri itasaidia kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo ambacho ni chanzo muhimu cha malighafi katika sekta ya viwanda ambayo imekuwa ni kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa napenda kuchangia zaidi katika suala la mazingira hasa juu ya uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti hovyo kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uchomaji wa mkaa, kuni, utayarishaji wa mashamba na kadhalika. Uharibifu huu unafanyika bila ya kuwepo hatua madhubuti za kuhakikisha nchi yetu haiwi jangwa. Watanzania walio wengi hawana destruli ya kupanda miti ni mabingwa wa kukata miti na hawaelewi kuhusu uharibifu wa mazingira. Ifike mahali Serikali ichukue hatua kali kabisa dhidi ya Watanzania wenzetu wanaoharibu mazingira kwa kukata miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri zitungwe sheria za kumtaka kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kupangiwa utaratibu wa kupanda miti angalau 10 kwa mwaka kwa kuwa miti ndiyo chanzo cha mvua na hifadhi ya mazingira. Bila kuchukua hatua za makusudi, Tanzania inakwenda kugeuka jangwa ndani ya kipindi kifupi. Hivyo basi ni wajibu wa Serikali kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko kubwa la watu na wanyama wafugwao kunachangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa mazingira. Kuna umuhimu mkubwa kuingiza masomo yanayohusiana na uhifadhi wa mazingira katika mitaala ya elimu nchini kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Madhara ya uharibifu wa mazingira ni pamoja na ukame, mafuriko na mmomonyoko wa ardhi. Ipo sababu ya msingi kabisa kwa Serikali kusisitiza umuhimu wa kuwataka Watanzania kujenga tabia ya kupenda mazingira kwa kuzuia ukataji miti badala yake wawe wanapanda miti katika mashamba yao na kwenye makazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri ufuatao:-

(i) Uzazi wa mpango upewe kipaumbele;

(ii) Idadi ya mifugo inayohamahama ipunguzwe;

(iii) Watanzania wanaofanya biashara ya mkaa wapewe masharti ya kuwa na mashamba ya kupandwa kwa ajili ya ukataji miti ya kuchoma mkaa; na

(iv) Kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 apewe malengo ya kupanda angalau miti 10 au zaidi katika mashamba na kwenye viwanja vya makazi, maeneo ya biashara na makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili kusudi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu ya Maji na Umwagiliaji chini ya Mheshimiwa Waziri Kamwelwe.

Mheshimiwa Spika, maji ni uhai. Kwa hakika ndiyo maana Serikali yetu imekuja na mpango mzuri na miradi mingi mikubwa imeorodheshwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Mbogwe ni miongoni mwa Wilaya ambazo tulifanikiwa kunufaika na miradi ya World Bank tukapata maji katika eneo la Nyerere, Mji wa Masumbwe, Shenda, Bulugala Kata ya Nyasato na Lulembela, Kata ya Lulembela. Miradi hii inafanya kazi vizuri, naipongeza Serikali. Pia tumeleta makadirio ya maombi ya fedha kwa ajili ufungaji wa umeme katika hivi vyanzo vya maji vya visima virefu katika hii miradi minne World Bank.

Mheshimiwa Spika, nataka niiambie tu Serikali kwamba Wilaya yetu ya Mbogwe ilikuwa ni sehemu ya Wilaya ya Kahama ambayo kimsingi ilionekana dhahiri kwenye Serikali kwamba tuna upungufu wa maji ardhini na kwa maana hiyo Serikali ikaamua kuleta maji kutoka Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, nimpongeza Mheshimiwa Waziri Kamwelwe aliwahi kufika Mbogwe. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ombi letu ulilikubali na ukafika na uliojionea hali halisi. Wilaya yetu ya Mbogwe tuna Makao Makuu yetu ambayo yako katika Mji wa Kasosobe na wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri ulifika na ukajionea hali halisi kwamba pale kumefanyika jitihada za kuchimba maji lakini kutokana na upungufu wa maji ardhini visima hivi vimekuwa vikitoa maji machache ambayo yanastahili kwa ajili ya kuweka pump za maji peke yake. Kwa hiyo, niiombe tu Serikali ifikirie uwezekano wa kutupatia maji kutoka Ziwa Victoria kwa sababu Wilaya ya Kahama ipo jirani na kwetu pale, ikiwezekana basi pesa zipatikane za kuweza kutuletea maji hayo ili hatimaye tuwe na uhakika wa maji muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji ni kitu muhimu sana kwa mambo yote, iwe uwekezaji wa viwanda ambao sasa tunafikiria kwamba Tanzania itakwenda kuwa ni Tanzania ya viwanda, viwanda bila maji haiwezekani. Maji yanahitajika pia kwa mifugo na shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Kwa maana hiyo, niiombe Serikali iendelee kuweka pesa katika Wizara hii na zitolewe kwa wakati. Pale tunapopitisha bajeti ni vizuri sasa Wizara ya Fedha ikazitoa pesa hizo kwa wakati na miradi ile ambayo imependekezwa itekelezwe kwa mujibu wa bajeti ya mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, tunayo pia miradi ambayo imetengewa pesa kwa ajili ya kuchimba visima katika Kata ya Ng’homolwa, Kijiji cha Chakabanga, pia katika Kijiji cha Lugunga Luhala. Vijiji hivi vimefanikiwa kupata maji wamechimba wakapata maji na kwa maana hiyo certificates zimepelekwa kwa Waziri ili kusudi tupatiwe pesa na utandazaji wa mabomba uweze kufanyika. Kwa maana hiyo, naomba Serikali utupatie hizo pesa kwa ajili ya uendelezaji wa visima hivi kwa maeneo ambayo tumefanikiwa kupata lita za ujazo ambazo zinaweza zikafaa kwa ajili ya uanzishaji wa visima vikubwa au visima virefu ili wananchi wetu waweze kupata hii huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi ya vyanzo vya maji pia yanatakiwa yapewe utaratibu mzuri wa hifadhi ya mazingira. Kwa sababu bila kuwa na mazingira yaliyo safi hakika tunaweza kujikuta tunapata shida zaidi. Ni dhahiri kwamba vyanzo hivi vya maji tunavyokuwa tunavianza na kuvisambaza kwa wananchi, vilevile tutarajie kwamba kutakuwa na maji machafu. Kwa maana hiyo, niombe tu kwamba wakati Serikali inakuja na mipango hii ya maji safi na salama basi tuwe na mipango mahsusi kwa ajili ya treatment ya maji machafu ambayo yanazalishwa kutokana na matumizi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua wazi kwamba maji ndiyo chanzo kikubwa cha maradhi. Kwa maana hiyo, tukiwa na maji ambayo ni salama nina uhakika magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu na magonjwa mengine ya matumbo yanaweza yakadhibitiwa tukajikuta kwamba hata ile huduma ya dawa hospitalini bajeti yake inaweza ikapungua endapo watu hawaugui magonjwa maambukizi ya kuwadhuru wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, niombe tu Serikali iendelee pia na utaratibu huu wa kuhakikisha kwamba tunapanda miti kwenye vyanzo vya maji. Vyanzo vya maji vikiwa vimepandwa miti naamini kwamba kwa namna ya moja au nyingine tutakuwa tumesaidia kuhakikisha kwamba ukame unadhibitiwa na tutakuwa na uhakika wa kupata mvua za kuaminika. Wakati wote tutajikuta kwamba tumeondokana na ukame ambao unasababisha upungufu wa maji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa ambazo tayari tumeshapeleka Wizarani, ninayo imani kwamba miradi yetu ambayo tumeiomba kwa Serikali itafanyiwa kazi. Kwa maana hiyo, niseme tu kwamba Wanambogwe tunaiunga mkono Serikali na niseme kwamba naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nitoe mchango wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri na hotuba ya Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti kuhusiana na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kwanza kuipongeza Serikali, Mheshimiwa Waziri pamoja na Mawaziri wote na Watanzania wote kwa ujumla, kwa namna ambavyo wanaunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kwamba Tanzania yetu inakwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha Serikali chenye mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2019/2020, ukurasa wa 34 - 49, vimeelezwa vipaumbele mbalimbali ambavyo Serikali yetu tayari imeshaanza kuvitekeleza na vingine viko katika hatua nzuri na naamini kabisa kwamba vipaumbele hivi vitakapokuwa vimekamilika, vitaifanya Serikali na Taifa letu la Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa ambayo kwa kweli yatakuwa yamepiga hatua kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa maji wa Rufiji wenye megawatt 2,100; ujenzi wa reli ya kati, maendeleo ya ujenzi tumeyaona na juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa amekwenda kukagua utekelezaji na tukapata taarifa pia kwa Mkurugenzi wa Shirika la Reli, Bwana Kadogosa, alieleza mambo mengi. Tunaamini kabisa kama wale wa Shirika la Voda wanavyosema kwamba yajayo yanafurahisha, nami nina imani kabisa kwamba kwa kweli ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano hakika yajayo yanafurahisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ambayo imejaaliwa kwa mambo mengi na naomba Watanzania wote tushikamane kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunaiunga mkono Serikali yetu. Katika mambo yote ambayo Serikali yetu imejipanga kuyatekeleza, tushikamane pamoja na tuone kwamba miundombinu ambayo inajengwa na Serikali ni kwa ajili ya Watanzania wote. Ndege zinazonunuliwa, reli na treni zitakazokuwa zinahudumia Watanzania, zitakuwa ni kwa ajili yetu wote na kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba tunayo mambo machache ambayo kimsingi tunatakiwa tuyazingatie na kupambana nayo hasa juu ya suala zima la hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Bila kumung’unya maneno, nataka niseme tu kwamba uharibifu wa mazingira ni adui mkubwa ambaye anaweza akasababisha harakati zetu za kujikomboa na kutaka kulifanya Taifa letu liende mbele kukwama. Kwa ajili hiyo, napendekeza kwa kweli habari nzima ya utunzaji wa mzingira ipewe kipaumbele katika maeneo yetu ya utawala katika mikoa, vijiji, wilaya na kila sekta ijipambanue katika kuhakikisha kwamba tunahifadhi mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji wa miti ovyo, tumeziona athari zake katika Kanda ya Ziwa na hasa mikoa ya Shinyanga, Tabora hata kwetu Geita, athari zake tunaziona. Kwa maana hiyo, naomba kwa kweli Watanzania wenzangu ambao bado hawajapata athari ya ukataji wa miti, waje wajifunze Kanda ya Ziwa ili waweze kuona ni namna gani mvua haziwezi kupatikana kwa uhakika na kwa maana hiyo tunapata shida kweli kweli. Kwa hiyo, naomba Serikali yetu ijipange kuhakikisha kwamba tunakuwa na mkakati wa upandaji miti katika maeneo ambayo yameathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni eneo la mazingira wezeshi kwa wawekezaji, yaani yale mazingira ambayo yanaweza kusababisha uvutiaji wa wawekezaji kutoka nchi za nje kuja kuwekeza katika nchi yetu. Katika tafiti mbalimbali zimeonesha wazi kwamba Tanzania haina mazingira rafiki ya wawekezaji katika sekta mbalimbali. Wakati tunapojiandaa kutengeneza Tanzania ya viwanda, basi mazingira ambayo yanatuonesha kwamba sisi tunakuwa ranked wa namba za mwisho, tuyarekebishe ili kusudi kusababisha nchi yetu iweze kuwa ni eneo la kupendelewa na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kweli katika hatua mbalimbali ambazo imezifanya. Katika sekta ya afya ambayo kimsingi Taifa lolote ambalo linataka kuendelea lazima watu wake wawe na afya njema na Serikali yetu imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya. Tumeona jinsi ambavyo vituo vya afya vimeboreshwa na hata upatikanaji wa dawa na wenyewe umekuwa wa kuridhisha. Kwa hiyo, naipongeza Serikali na naomba iendelee na moyo huo na ikiwezekana kwa kweli maeneo ambayo bado hayajapata huduma za Hospitali za Wilaya kama huko kwetu Mbogwe, basi Serikali ione uwezekano wa kutuingiza katika utaratibu ikiwezekana miaka ijayo tupatiwe Hospitali ya Wilaya ili kusudi wananchi wa kwetu huko nao waweze kupata huduma za afya katika ukamilifu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la viwanda. Napendelea kabisa Serikali yetu pia ilitupie macho suala zima la utengenezaji wa viwanda vya mbolea. Kama ambavyo tumeweza kufanikiwa katika sekta ya viwanda vya kutengeneza saruji, basi na utengenezaji wa mbolea Serikali ione uwezekano huo ili kusudi suala zima la sekta ya kilimo iweze kupata msukumo wa peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda pia vya utengenezaji wa madawa ya binadamu na wanyama pamoja na viuadudu ni muhimu. Naomba viwanda hivi na vyenyewe vipewe kipaumbele ili kusudi Tanzania yenye watu asilimia zaidi ya 75 wanaotegemea kilimo, basi kilimo hiki kiwe na tija. Watu wetu watakapokuwa wamepata miundombinu ya madawa na viuadudu na vile visumbufu vya mimea, naamini kwamba uzalishaji wa mazao ya biashara na ya chakula utakuwa uko katika hali nzuri na matokeo yake Tanzania ya viwanda itakuwa imefikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa mara nyingine kwamba naisifu Serikali kwa kazi zake nzuri ambazo imeendelea nazo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili kusudi niweze kuchangia katika hotuba za Kamati zetu mbili Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Taifa lolote ulimwenguni linapimwa uwezo wake na nguvu zake kutokana na nguvu za kiuchumi na nguvu za kiulinzi na usalama. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika Taifa letu vimefanya kazi kubwa kwa uhakika na tunaendelea kupata heshima ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu kutokana na uzalendo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiambie Serikali tu kwamba kuna jambo moja ambalo linajitokeza ambalo si jema sana la ugomvi baina ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na wananchi hasa katika suala zima la ardhi. Migogoro ya ardhi imekuwa inatia doa amani yetu na kwa maana hiyo naishauri Serikali ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba maeneo yote ya Jeshi la Wananchi na Jeshi la Magereza na vyombo vingine vyote vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi ardhi zake zipimwe na zijulikane kabisa kwamba hairuhusiwi raia yoyote kusogea na kujenga karibu na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imeonekana wazi kwamba vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimekuwa vikichukua maeneo makubwa muda mrefu lakini raia kutokana na kwamba tunazidi kuongezeka, tumeendelea kuwa tunasogea kwenye maeneo haya na kuchukua maeneo na hatimaye kuanzisha mizozo isiyokuwa na umuhimu. Kwa maana hiyo naiomba Serikali itenge pesa makusudi kabisa ili kusudi maeneo yetu vyombo vya Ulinzi na Usalama yapimwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusiana na beacon, ni alama ambazo zinaonyesha ramani yetu au mipaka yetu ikoje katika mustakabali wa usalama wa Taifa letu na kwa maana hiyo kwa sababu kuna beacon ni mbalimbali zimeng’olewa katika mipaka yetu na nchi jirani ambazo zinatuzunguka, basi ni jambo la muhimu kuhakikisha kwamba Serikali kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Nchi za Nje pamoja na Wizara ya Ardhi wafanye jitihada kuhakikisha kwamba beacon zetu zinarejeshwa mahali ambapo zilikuwepo hapo mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la diplomasia ya uchumi, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa jitihada ambazo ameendelea nazo za kufufua Shirika letu la ndege. Diplomasia ya uchumi isingewezekana kama kusingekuwa na jitahada mahususi za Mheshimiwa Rais wetu za kuhakikisha kwamba tunakuwa na Shirika la Ndege ambalo litakuwa linatuunganisha na Mataifa mengine ya nje. Kwa maana ya kwamba wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini kwetu hata kama wangekuwa wanapatikana huko nje ingekuwa ni tatizo zaidi kuwafikisha katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata watalii vilevile wanaweza wakaja pamoja na kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi yetu unaendelea kuimarika kutokana na kwamba mchango wa shirika hili utaendelea kuonekana. Niiombe sasa Wizara ya Fedha ihakikishe kwamba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama muda wote vipatiwe pesa zake kwa wakati hasa katika masuala mazima ya miradi yake ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la nishati na madini, niipongeze Wizara yetu ya Nishati kwa jitihada nzuri na za makusudi ambazo zimeendeelea kuonekana na hasa kwa jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Rais wetu ameendelea kuzionyesha na kwa kuthubutu kuhakikisha kwamba mradi mkubwa wa Stiegler’s gorge unaanza kutekelezwa mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata jana tumeshuhudia uendelezaji wa mradi wa Rusumo katika Mto Kagera mradi ambao utaendelea kutuletea huduma ya umeme wa megawati karibu 27 ambazo zitakuwa zinagawanywa katika Taifa na sisi tutanufaika kwa utaratibu huo. Kwa maana hiyo nchi yetu itakapokuwa inaendelea katika sera yake ya kukuza viwanda na kuwa Tanzania mpya ya viwanda ninaamini kwamba matarajio hayo tunaweza kuyafikia muda si mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimeendelea kuwa na mashirika yake ya uzalishaji mali ikiwemo Shirika la SUMA JKT na hata Magereza, Jeshi la Ulinzi na Usalama linayo Mashirika yake ya Mzinga na Nyumbu. Vyombo hivi vimekuwa vikifanya kazi zake nzuri na kwa maana hiyo naiomba Serikali kwa makusudi mazima ihakikishe kwamba inaviongezea nguvu kuhakikisha kwamba vinashiriki katika uzalishaji mali na kuweza kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima linalohusiana na suala la vitambulisho vya Taifa. NIDA wamekuwa ni wakala wa kuzalisha hivi vitambulisha vya Taifa, lakini kimsingi wameshindwa kufikia malengo kutokana na kwamba wanapungukiwa pesa pamoja na vitendea kazi vingine zikiwemo mashine za kuzalisha hizo kadi za vitambulisho vya Taifa. Kwa maana hiyo naomba Serikali kwa makusudi mazima ijipange vizuri kuhakikisha kwamba NIDA wanawezeshwa ili kusudi waweze kuvitoa vitambulisho hivyo ambavyo ndio vitakuwa vinaonesha uraia halali wa Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukiendelea kuiona kwamba nchi yetu inasonga mbele, tuwe katika utaratibu unaokubalika kwa kuhakikisha kwamba vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinakaa katika utaratibu unaokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika Wizara ya Madini, kwanza niishauri tu kwamba katika kile kikao cha wadau cha tarehe 22 na tarehe 23 naomba Wizara iyatekeleze maazimio yote ambayo yaliazimiwa na kikao hicho cha wadau. Pendekezo lingine ninalotaka kulitoa kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba Mataifa mengine yaliyoendelea yamekuwa yakishindana katika uzalishaji na kulimbikiza silaha za maangamizi. Naishauri Serikali yangu ya Tanzania yenyewe ijitahidi katika kuhakikisha kwamba tunalimbikiza vitu vya thamani ikiwemo dhahabu na Benki yetu Kuu ihakikishe kwamba inanunua dhahabu na kuiweka katika Hazina ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja ya Kamati zote mbili. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kukupongeza kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hotuba nzuri ya Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Hotuba yake inaweka msingi wa bajeti ya Serikali itakayojadiliwa hapa Bungeni kwa kipindi cha miezi mitatu kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea mbele, naomba niunge mkono hoja hotuba ya Waziri wetu Mkuu kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu wetu alifanya ziara katika Mkoa wetu wa Geita na alifika pia katika Wilaya yetu ya Mbogwe akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Niseme tu kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano imejipambanua kuwa ni Serikali ya viwanda; na pia inaendena na kauli mbiu ya Chama chetu cha Mapinduzi inayosema ya kwamba, “Tanzania mpya na CCM mpya na CCM mpya ni Tanzania mpya.” Kwa sababu mambo mengi ambayo yanatendwa na Serikali hii yanatia moyo na yanaonyesha kwamba kweli tunakokwenda ni Tanzania mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano, zipo sekta mbalimbali muhimu ambazo Serikali yetu imezitilia mkazo ikiwemo sekta ya elimu. Sekta ya Elimu ni sekta nyeti na Serikali yetu imeweka msimamo mzuri wa kuweka elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Hongera sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika Sekta ya Afya, sisi sote ni mashahidi ya kwamba Serikali yetu imejenga Vituo vya Afya vingi katika sehemu mbalimbali za nchi hii ikiwemo katika Wilaya yangu ya Mbogwe. Tumepewa vituo vya Afya viwili; Kituo cha Afya cha Iboya na Kituo cha Afya cha Masumbwe. Vituo hivi vyote kwa pamoja vimepewa jumla ya shilingi milioni 800 na kwa kweli utekelezaji wake kwa kutumia ile force account, tumeweza kuyaona manufaa ambayo yamepatikana baada ya kuwa tumepata majengo mazuri. Ukifika kwenye Kituo cha Afya utajua kabisa kwamba kwa kweli mgonjwa akifika hapo hata kama alikuwa na hali mbaya anarejeshewa matumaini ya kuishi tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kututengea awamu hi shilingi milioni 500 za kuanza ujenzi wa hospitali yetu ya Wilaya ya Mbogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yanaendelea kufanyika katika Wilaya yetu ya Mbogwe ikiwemo ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri yetu. Tuipongeze kabisa Serikali kwa sababu hatua za ujenzi zinaendela vizuri, miradi mbalimbali ya maji pia inaendelea kufanyika. Upo upanuzi wa mradi wa maji wa Nyakafuru, upo mradi wa Mbogwe, upo mradi wa Uhala katika Kata ya Lugunga. Yote haya wana Mbogwe tunasema ahsante sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala zima la ujenzi wa reli ya standard gauge. Ujenzi huu ni hatua ya maendeleo ya hali ya juu sana. Nchi yeu tumeshuhudia Serikali ikitekeleza mradi huu kuanzia Dodoma mpaka kule Dar es Salaam, ujenzi unaendelea vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba ujenzi huu utaendelea mpaka kufika Kigoma na Mwanza na hata ile reli ya kutoka Isaka kwenda Kigali tunaamini Serikali yetu kwa kushirikiana na wenzetu wa Rwanda tutaishuhudia ikitekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi mapana ya kulinda muda, niipongeze sana Serikali kwa ujasiri wake mkubwa wa kuanza na kuendelea kujenga mradi wa uzalishaji umeme wa maji katika mto Rufiji maarufu kama Stiegler’s gauge. Sisi sote ni mashahidi ya kwamba hapa zitapatikana Megawatts 2100 ambazo aitaingizwa katika gridi ya Taifa. Ninaamini ya kwamba, Tanzania ya viwanda bila ya umeme isingewezekana lakini kwa kufuatana na juhudi mahususi za Serikali jambo hili limetiliwa mkazo na ninaamini ya kwamba itakapofika mwaka 2020 tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kui-supply Tanzania umeme vijiji vyote na vitongoji vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wote Waheshimiwa Wabunge mtakuwa ni mashahidi wa namna ambavyo Wakandarasi mbalimbali wameendelea kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Jambo hili linafanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Wilaya yangu ya Mbogwe. Naiomba tu Wizara ya Nishati iendelee kumsukuma Mkandarasi ili aweze kumaliza mradi huu wa awamu ya tatu ya REA ili kwamba Watanzania wengi wa Mbogwe waweze kupata huduma hii muhimu ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika sekta ya barabara. Serikali yetu ya Awamu ya Tano pamoja na Awamu ya Nne wagombea wake waliwahi kuahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wangu wa Masumbwe, tuliahidiwa kupatiwa lami kilometa tatu. Kwa maana hiyo, naishaurri tu Serikali katika bajeti yake ya mwaka huu ikumbuke kuzitimiza hizi ahadi za viongozi wetu wakuu wa Serikali katika maeneo mbalimbali ambako tunaamini ahadi hizi ziliwekwa na nitilie tu mkazo ujenzi wa barabara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Masele kwa mchango wako.

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono kwa asilimia mia kwa mia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu akiwa Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali Bungeni, hotuba yake imetoa mwelekeo mzuri kabisa wa vikao vyetu vyote vya bajeti za Wizara mbalimbali zitakazofuata. Serikali ya Awamu ya Tano imejenga msingi madhubuti wa kujenga Tanzania ya viwanda ikisadifu na kauli mbiu ya Chama cha Mapinduzi ya CCM mpya na Tanzania mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Magufuli akisaidiwa na Makamu wake wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa imedhamiria kwa dhati kujenga uchumi wa kisasa kwa kuja na mpango wa kuwa na miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (Standard Gauge – SGR), mradi mkubwa wa maji wa kufua umeme kutoka Mto Rufiji (Stigler’s Gorge) utakaosaidia kufua umeme wa MW 2,100, hii ikiwa ni katika kuhakikisha Tanzania ya viwanda inafikiwa kwani viwanda bila umeme haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya nishati kutokana na vyanzo mbalimbali kunasaidia sana utekelezaji wa miradi mbalimbali ya usambazaji wa huduma ya umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijijini maarufu kama REA. Kwa hakika huduma hii imeleta mabadiliko makubwa katika shughuli za maendeleo vijijini na hivyo kupunguza uhamaji wa watu kutoka vijijini kuhamia vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naipongeza Serikali kwa kuja na mpango kabambe wa kuimarisha huduma katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vingi vya afya katika sehemu mbalimbali ikiwwemo Wilayani Mbogwe ambapo vituo vya afya vya Iboya na Masumbwe ambavyo kwa pamoja vimepatiwa jumla ya shilingi milioni 800 na kwa hakika vituo hivi vimeboreshwa kwa kiwango kikubwa. Kwa hili, tunaipongeza sana Serikali, pia Serikali imetupangia shilingi milioni 500 tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya elimu, suala la elimu bila malipo limeleta changamoto kubwa sana na wananchi wengi wamejitokeza kupeleka watoto wao kuandikishwa darasa la kwanza. Katika hali hii Watanzania wengi wamepata fursa ya kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge kunategemewa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano na uchukuzi, jambo ambalo litaokoa kwa kiwango kikubwa uharibifu wa barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imepiga hatua kubwa sana katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege mpya utachangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii kwa kuleta wageni toka ng’ambo na kuleta chachu ya upatikanaji wa pesa za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni sekta nyeti sana nchini kwani kinaajiri watu wengi sana karibu asilimia 75. Hivyo napenda kuishauri Serikali kuwekeza zaidi katika suala la utafiti wa ardhi, mbegu, magonjwa pamoja na visumbufu vya aina mbalimbali. Upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbolea na mbegu bora kutasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na ya biashara ili yaweze kuwa ni chachu ya kuifanya Tanzania ya viwanda iweze kutimia maana viwanda vyetu vitatumia malighafi kutokana na mazao ya kilimo. Naiomba Serikali izidi kuwekeza ama kukaribisha wawekezaji katika viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nitumie muda huu kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili, Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na watumishi wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kuja na mpango mzuri huu wa kuyapandisha hadhi mapori haya ya Ugalla na Kigosi ili kuweza kuunganisha pamoja na Azimio la jana la Mwalimu Nyerere National Park ambayo ilikuwa ni Pori la Akiba la Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda yetu ya Ziwa imekuwa ni sehemu ambayo kwa kweli ni chanzo cha uharibifu mkubwa wa mazingira hasa kwa wananchi wetu kuweza kuwa wakataji wa misitu na uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, hatua ya Serikali ya kuyapandisha mapori haya hadhi na kuyaita Hifadhi za Taifa ni hatua muhimu kwa maendeleo ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa maana hiyo mimi nitakuwa na mapendekezo tu machache juu ya jambo hili ya kwamba sasa kwa sababu tumeanza kuwa na national parks nyingi katika Kanda hii ya Ziwa, tukianza na zile za Burigi, Chato, Ibanda na Rumanyika na sasa tutakuwa na hii Hifadhi ya Kigosi pamoja na Ugalla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Wizara pamoja na Serikali zianzishe Vyuo vya Utalii pamoja na Vyuo vya Misitu pamoja na Mamlaka za Manyamapori na vyuo mbalimbali vya kuweza kufundisha watu juu ya elimu ya utalii kwa sababu vitu hivi ni vitu vigeni katika maeneo haya na kwa maana hiyo wananchi wetu watahitaji kupata elimu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika upande wa Azimio la Kuridhia Mkataba wa Minamata na matumizi ya zebaki. Mimi niseme tu kwamba kwa kweli jambo hili naliunga mkono kwa sababu sisi pia ni waathirika wa masuala haya ya matumizi ya zebaki kwa sababu ni wazalishaji wa dhahabu na tuna wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatumia mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa maslahi ya muda, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa muda. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Aloyce Kamwelwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imethibitisha kwamba ni Serikali ya watu iliyowekwa na watu kwa ajili ya watu na ndiyo maana utaiona tu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Kamwelwe imesheheni miradi mbalimbali ya maendeleo yenye kulenga kuitengeneza Tanzania mpya katika sekta mbalimbali za Uchukizi, Ujenzi na Mawasiliano. Nimpongeze Mheshimiwa Rais, Makamu wake, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji mbalimbali ambao wamehusika katika maandalizi ya hotuba nzuri hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ipo barabara ya kutoka Butengorumasa- Iparamasa-Mbogwe-Masumbwe inatakiwa sasa iendelezwe ili iweze kuiunganisha sasa Mkoa wa Geita, Mkoa wa Shinyanga, Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii itarahisisha sana mawasiliano baina ya Wananchi wa Mikoa hii niliyoitaja kwa sababu Wananchi wa Geita hawatakuwa na sababu sasa ya kupita Nzega ndiyo aende Tabora. Atatakiwa tu anatoka Geita anapita Mbogwe, anakwenda Ushetu, anakwenda Kaliua, Kaliua sasa hapa anachangua; kama anakwenda Kigoma atapita Urambo atakwenda Kigoma huko, akifika Kaliua anaweza akakata kuelekea Mpanda- Sumbawanga au anarudi kwenda Tabora, Tabora anakuja Singida mpaka hapa Dodoma na Dar es salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba barabara hii kwasababu sehemu ya Butengorumasa-Iparamasa-Mbogwe mpaka Masumbwe imeshapandishwa kuwa barabara ya TANROADS, nilikuwa naomba na hiki kipande kilishosalia sasa cha kutoka Masumbwe-Mwabomba-Nyankende-Bomba A-Uroa-Uyoa- Sungwa-Mwamnange-Buhindi mpaka Kaliua na yenyewe ichukuliwe na Serikali ili iweze kupandishwa kwa kiwango cha TANROADS na ikibidi ufanyike usanifu wa kina ili hatimaye ije ijengwe kwa kiwango cha lami ili iweze kuwasaidia wananchi wa maeneo haya waweze kuwa na mawasiliano ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa kukubali ombi la kuipandisha hadhi barabara ya kutoka Bwelo, Makao Makuu ya Wilaya ya Mbogwe kwenda Karumwa katika Wilaya mpya ya Nyang’hwale, jambo hili na lenyewe litatufungua kwahiyo tutakuwa na urahisi wa kuwez kutoka Wilaya moja hadi nyingine bila ya kupata kikwazo cha aina yoyote katika usafiri wa watu na vitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuipongeza Serikali kwa hatua yake ya kutenga fedha kwa ajili ya usanifu wa reli na kuanza kuijenga kwa kiwango cha Kimataifa (standard gauge) na mpaka sasa ujenzi unaendelea kutoka Dar es salaam mpaka Morogoro na hatua ni nzuri na hatimae tutaona kutoka Morogoro kuja Dodoma na baadaye Dodoma-Tabora-Isaka-Mwanza na kutoka Tabora hadi Kigoma baadaye Kaliua mpaka Mpanda na Kadema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa lolote na tunaamini kabisa kwamba uwepo wa miundombinu namna hii ambayo ni rafiki itachochea ukuaji wa uchumi katika Taifa letu hasa ikizingatiwa kwamba Nchi yetu imejaaliwa kuwa ni lango la Nchi mbalimbali ambazo ziko land locked ambazo hazina Bahari na bahati nzuri sisi tumekuwepo katika ukanda ambao tuna Bahari, tuna Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo uwepo wa Maziwa na Bahari unarahisisha uwepo pia wa Bandari na Serikali yetu imejipambanua katika kuhakikisha kwamba zinakuwepo Bandari ambazo zina uhakika na zinazoweza kutoa huduma kwa nchi zetu ambazo ziko jirani na sisi. Kwa mfano, Bandari ya Dar es salaam, Bandari ya Tanga, Bandari ya Mtwara na ile Bandari ya Bagamoyo ambayo inatarajiwa kujengwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali iendelee kuziangalia pia zile Bandari za kwenye Maziwa kwa mfano, tunazo Bandari katika Ziwa Victoria, kwa Geita pekee tunayo Bandari ya Nyamirembe, Bandari ya Nkome, Bandari ya Nungwe, zote hizi zinahitaji kuwekewa miundombinu ili kusudi ziweze kutoa huduma kwa Wananchi wa Mkoa wa Geita na ili waweze kuwasiliana na wenzano wa Mikoa ya jirani, kwa mfano, Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Mara na Nchi jirani kwa maana ya Uganda na Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mawasiliano ya anga, niipongeze Serikali kwa kununua ndege mpya na ambazo zinaendelea kufanya kazi. Vilevile niipongeze Serikali kwa kuendelea na upanuzi wa viwanja vya ndege ikiwemo kiwanja cha ndege cha Mwanza. Niungane na Wabunge wenzangu ambao wanatoa mapendekezo kwa Serikali kwa sababu nedge zimepatikana basi zianze kuwepo route za kutoka Mwanza kuja Dodoma ambapo ndiyo Makoa Makuu ya Serikali ili kusudi Wananchi wa Mwanza na Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa waweze kufika kwa urahisi katika Makoa Makuu ya Nchi pamoja na kwenda sehemu za Dar es salaam na Mikoa mingine kama kule Mbeya kwa uwanja wa Songwe na uwanja wa Nduli kule Iringa na sehemu zingine ambazo kama Kilimanjaro na sehemu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba Serikali yetu imejipanga na ndiyo maana inatekeleza kwa kiwango kikubwa mambo mengi ambayo yanahitajika kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema maneno haya kwa sababu kazi kubwa iliyofanywa na Wizara hii inatosha na niseme tu kwamba naiunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri asilimia 100 kwa 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai, na pili nikushukuru wewe kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kushiriki katika kuchangia hotuba ya Waziri wetu mpendwa, Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kusema naunga mkono hoja asilimia 100 kwa 100, na nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake yote kwa ujumla kwa utendaji wake mzuri wa kazi. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu na wataalam mbalimbali wa Wizara hii kwa umahiri wao wa utekelezaji wa mipango yote ambayo tumeanza nayo ya miaka mitano. Hongereni sana kwa consistency ambayo mmekuwa nayo. Tumeanza na mpango wa mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu, sasa wa nne; utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali za vipaumbele hauna mashaka unatekelezwa kwa kiwango ambacho kinaridhisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa reli ya kisasa uko vizuri, ujenzi wa Bwawa la Umeme la Stiegler’s Gorge au Bwawa la Mwalimu Nyerere unakwenda vizuri; upanuzi wa bandari zetu unakwenda vizuri, ujenzi wa meli katika maziwa makuu; Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa mambo yanakwenda vizuri; ujenzi wa Daraja refu kabisa ambalo litakuja kuwa la kihistoria la Kigongo – Busisi mpango unakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ununuzi wa ndege za kisasa umeendelea kutekelezwa vizuri; yote haya yamo katika mipango yetu ambayo tumeanza nayo tangu uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ulipoingia madarakani. Miradi mbalimbali inatekelezwa, mpango wa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne unatekelezwa bila wasiwasi na Watanzania wanafurahia; uboreshaji wa huduma za afya na wenyewe unatekelezwa na tunashukuru na ninaipongeza Serikali sana kwa sababu Watanzania sasa afya zao zinaimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya napenda sasa niendelee kuchangia katika baadhi ya maeneo. Eneo mojawapo ambalo ninapenda kuchangia ni kuhusiana na suala zima la ujenzi wa wilaya hizi mpya na mikoa mipya. Wilaya yangu ya Mbogwe ni miongoni mwa wilaya mpya; niipongeze sana Serikali kwa sababu imeendelea kufanya kazi zake vizuri inatupatia pesa tunajenga makao makuu ya wilaya kwa maana ya halmashauri na ofisi za mkuu wa wilaya na tumepewa pia pesa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, naomba tu Serikali iendelee kutupatia pesa ili tuweze kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa uhakika kabisa na wa thabiti wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma na ninaamini kabisa kila mmoja ni shuhuda kwamba ofisi mbalimbali za Wizara mbalimbali zimejengwa kupitia mipango hiihii ya Serikali ambayo tunaendelea kuitekeleza. Niombe Serikali iendelee na mkakati wake sasa wa kumalizia ujenzi wa Uwanja wa Msalato ili kwamba Makao Makuu yetu ya nchi yaweze kufikika kwa kufikia hata ndege na usafiri wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuyapandisha mapori ya akiba kuwa hifadhi za Taifa; Mapori ya Kigosi, Mto Ugala, Selous, Ibanda, Burigi Chato, mapori haya yanahitaji sasa uwekezaji mkubwa. Tuiombe Serikali itenge pesa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika mapori haya ili sasa huduma za utalii ziweze kufanyika kwa wepesi zaidi na uchangiaji wa Pato la Taifa kupitia hii Sekta ya Utali iweze kuonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo ninapenda kuishauri Serikali iendelee kuwekeza katika viwanda vya utengenezaji wa mbolea kwa sababu Watanzania walio wengi wanashiriki katika shughuli za kilimo, na kwa maana hiyo tuiombe Serikali iwekeze zaidi katika kuvutia wawekezaji wa viwanda vya mbolea ili uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara uweze kuimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ikijitosheleza kwa chakula ninaamini kabisa hata ukuaji wake wa uchumi utakuwa ni wa uhakika zaidi kwa sababu wazalishaji mali wenyewe watakuwa wana nguvu za kutosha na kwa hakika wataweza kufanya uzalishaji katika sehemu mbalimbali za Serikali na hata katika viwanda na maeneo mbalimbali ya uzalishaji mali watafanya kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tena kuishauri Serikali sasa kuwekeza zaidi katika eneo la upimaji wa ardhi. Nchi yetu ina tatizo kubwa la ujengaji holela katika miji yetu, niombe kabisa Serikali ilipe kipaumbele suala zima la upimaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali ya miji inayochipukia na miji mikubwa ambayo tayari tunayo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia habari ya maendeleo hatuwezi kuzungumza maendeleo bila kutaja suala zima la mawasiliano kwa njia ya barabara. Niombe Serikali iendelee kutoa pesa katika wakala mbalimbali ikiwemo TANROADS na TARURA ili ujenzi wa barabara za lami kuunganisha maeneo mbalimbali kwa maana ya mikoa na makao makuu ya wilaya uendelee kwenda kwa kasi inayokubalika. Pia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini na wenyewe ujengewe uwezo, vitafutwe vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuweza kuisaidia wakala hii ambayo ni changa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kwamba REA inafanya vizuri kwa sababu imekuwa na chanzo cha uhakika cha tozo ya mafuta. Tumejikuta kwamba sasa hiki chanzo kinausaidia sana Wakala wa Umeme Vijijini kuweza kufanya mageuzi makubwa sana ya upatikanaji wa umeme katika vijiji vyetu na kwa maana hiyo ninaamini kabisa kwamba hata TARURA ikiwezekana kitafutwe chanzo kingine ambacho kitauwezesha kuwa na pesa za uhakika za kuweza kutekeleza miradi yake kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakala mwingine ni Wakala wa RUWASA ambao na wenyewe ni Wakala wa Maji Mijini na Vijijini. Wakala huu na wenyewe ni wakala ambao ndiyo umeanza, niiombe Serikali na yenyewe iendelee kuujengea uwezo wakala huu ili uweze kusambaza maji kwa uhakika kwa Watanzania ili waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kwamba watu wakipata maji safi na salama afya zao zitaimarika na magonjwa mbalimbali ambayo yanatokana na maji yanaweza yakazuilika tunaweza tukajikuta hata bajeti ya matumizi ya afya inaweza ikashuka kwa sababu kama tusipokuwa na wagonjwa wengi maana yake sasa hata mahitaji ya madawa yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hao napenda kushukuru, ahsante sana kwa kunipata nafasi na Mungu awabariki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kuniwezesha kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika hizi hotuba za Wenyeviti wetu wawili wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Spika, nianze na hotuba ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Hotuba hii imeeleza vizuri kazi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika kwa Wizara mbili ambazo tunazisimamia, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, nchi yoyote duniani ambayo imeendelea kiuchumi ina tabia ya kuwa na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni imara. Kwa maana hiyo tunapotaka kujenga Tanzania ya Viwanda, ni muhimu pia kuwa na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo pia vimewekeza katika masuala mtambuka ya silaha za kivita zikiwemo ndege, meli, mizinga na vitu vingine vyote ambavyo vinahusiana na habari ya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, naishauri Serikali iendelee kuvipatia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama bajeti inayostahili ili kusudi mashirika yetu ya Nyumbu na Mzinga yaweze kuwekeza zaidi katika miundombinu ya uboreshaji silaha na nyenzo za kivita ili kuweza kulihami Taifa letu ambalo lina rasilimali nyingi ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia kuwanazo.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, kutokana na utajiri wa nchi yetu ulivyo mkubwa nina uhakika kwamba tunao maadui wa kutosha kutoka nje na ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, tusipokuwa na vyombo madhubuti tunaweza tukajikuta ujenzi wa uchumi wetu ukawa sasa unapata pingamizi mbalimbali. Kwa maana hiyo, naishauri tu Serikali iwekeze vyakutosha katika vyombo hivi.

Mheshimiwa Spika, pia nalipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuendelea na kuwa na mpango madhubuti wa kuweza kuwachukua vijana wetu na kuwajengea uzalendo katika makambi mbalimbali na pia Shirika letu la SUMA kwa kazi nzuri ambazo imekuwa ikizifanya.

Mheshimiwa Spika, naipongeza JKT kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uzio wa Mererani na kazi nyingine ambazo Jeshi letu hili limekuwa likizifanya. Naiomba tu kwamba Serikali iendelee kuiunga mkono inavyostahili.

Mheshimiwa Spika, aidha, nalipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya ulinzi wa raia na mali zao na kwa vyovyote vile tunashukuru kwa sababu matukio ya uhalifu yamepungua katika nchi yetu. Kwa hiyo, naomba tu kwamba vyombo vyetu hivi vya ulinzi na usalama viendelee kuungwa mkono kwa kupewa pesa kwa ajili ya kujenga nyumba za maaskari wetu na kwa maana hiyo tuweze kuwarahisisha maisha Askari wetu.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limekuwa ni chombo madhubuti ambacho kimekuwa kikisaidia kuwarekebisha Watanzania wanaokuwa na matatizo ya kiuhalifu. Kwa maana hiyo, naomba tu Serikali iendelee kulisaidia jeshi hili katika kuhakikisha kwamba msongamano katika Magereza unapungua na ikiwezekana Serikali itoe pesa zaidi kuweza kujenga Magereza mengi zaidi ili kuweza kuwapa nafasi watu hawa, pamoja na kwamba ni wavunjifu wa sheria na wakosaji, lakini ni muhimu wakapatiwa matunzo mazuri wanapokuwa katika kipindi chao cha kutumikia adhabu zao.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekuwa na zoezi la kuwapatia raia wa nchi hii vitambulisho vya Taifa. Zoezi hili linafanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), lakini tumeshuhudia katika siku za karibuni kwamba mamlaka hii imekuwa na changamoto kubwa ya kushindwa ku-cope na mahitaji ya Watanzania. Watanzania walio wengi hawajapata vitambulisho hivyo. Tatizo kubwa linaonekana ni fedha. Kwa hiyo, naiomba tu Serikali isaidie mamlaka hii ili iweze kusaidia kutoa vitambulisho vya kutosha na wananchi wetu waweze kutambulika kama raia wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nije kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Naipongeza Wizara hii kwa sababu imekuwa ni kiunganishi kati ya Taifa letu na Mataifa mengine ya nje na tumeona ukuaji wa diplomasia ya uchumi, watu kutoka Mataifa mbalimbali wamekuwa wakija katika Taifa letu na kuwekeza na kwa maana hiyo kuchangia ukuaji mkubwa kabisa wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iendelee kutoa pesa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Balozi zetu mbalimbali duniani ambapo tumeshuhudia wakati mwingine Serikali ikiingia gharama kubwa kupanga majengo kwenye Balozi zetu huko nje. Naomba Serikali iwekeze zaidi katika ujenzi wa nyumba na Ofisi ya Kibalozi huko Mataifa ya nje.

Mheshimiwa Spika, nichangie katika Wizara ya Nishati. Naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo imeendelea kuongeza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme ikiwemo Kinyerezi I, II, III pamoja na mradi mkubwa wa Julius Nyerere Hydroelectrical Project ambao unajengwa ambao utakuwa ni mkombozi wa matatizo ya umeme hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini wazi kabisa kwamba ongezeko la Megawatt 2,115 itakuwa ni ingizo kubwa ambalo litasaidia sana katika kulifanya Shirika la Umeme (TANESCO) pamoja na Miradi ya REA kwenda katika maeneo mbalimbali nchini na Watanzania wengi watanufaika kwa kuwa na umeme ambao utakuwa na bei nafuu; na kwa maana hiyo Tanzania ya Viwanda itawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Serikali yetu kwa kuja na Mpango Mkakati na kubadilisha Sheria za Madini ili kuhakikisha kwamba Taifa letu linanufaika. Naipongeza Serikali kwa kuingia mkataba mpya na Kampuni ya Barrick ambako sasa imeanzishwa Kampuni ya Twiga ambayo Serikali yetu sasa itakuwa na hisa za asilimia 16 na manufaa yake tutayaona muda siyo mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba hata Makampuni mengine ambayo yamewekeza katika madini Serikali...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Augustine Manyanda Masele.

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi katika suala la ardhi na changamoto zake kwa wakulima wetu. Suala la kupima na kujua hali ya udongo kabla ya kutumia mbolea ni jambo la msingi sana, lakini kwa bahati mbaya sana wananchi wamekuwa hawapati huduma za kitaalam kupima acidity na alkalinity of soil kutokana na kutokuwa na vituo vya kupimia udongo na ubora wake. Nashauri Serikali ianzishe vituo vyenye kujitosheleza kwa wataalam na vifaa vya upimaji ili kujua ubora wa udongo na aina ya mbolea inayofaa kwa wakulima kulingana na mazingira husika na ikiwezekana kila wilaya au tarafa au kata viwepo vituo vya kupimia ubora na aina ya udongo na mbolea inayofaa kwa ajili ya kurutubisha na kushauri aina ya mbegu inayotakiwa.

Mheshimiwa Spika, viwanda vya mbolea pamoja na viuadudu pia viuatilifu ni vema vikawekezwa zaidi nchini ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma hizi kwa bei nafuu ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na yale ya biashara.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo ni jambo la msingi sana, hivyo basi naishauri Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika Sekta hii ya Viwanda. Viwanda kwa ajili ya kuongeza ubora na thamani vinatakiwa kuwekeza katika Viwanda vya Nguo, Viwanda vya Kubangua Korosho, Viwanda vya Kukamua Mafuta ya Alizeti, Michikichi, Karanga, Pamba. Aidha, viwanda kwa ajili ya kuchakata matunda pia ni vema vikaongezwa ili kuwakomboa wakulima wa matunda.

Mheshimiwa Spika, suala la vipimo kwa ajili ya mizani ya kupimia uzito kwa ajili ya wakulima wetu bado kuna shida kubwa hasa kutokana na wanunuzi mara zote ndio huwa ni wamiliki wa mizani ambayo siku zote huichezea kwa lengo la kuwapunja wakulima, hivyo basi ni vyema Serikali ikaweka mkazo kuhakikisha kwamba wakulima wanamiliki mizani yao wenyewe na Mamlaka au Wakala wa Vipimo nchini kuihakiki mizani hiyo mara kwa mara ili kuepusha wakulima kupunjwa.

Mheshimiwa Spika, suala la mabadiliko ya tabianchi; iko haja kwa Serikali kuwekeza zaidi katika Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa kwani kwa sasa utabiri wa hali ya hewa nchini unafanyika kwa kubahatisha na matokeo yake wananchi wanapata hasara kwa kutokupata taarifa sahihi na matokeo yake wananchi wanapambana na ukame au mafuriko na hivyo kuathiri wakulima kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaathiri moja kwa moja Sekta ya Kilimo kwa vile uharibifu wa mazingira kwa kukata miti husababisha ukame na mmomonyoko wa udongo, naishauri Serikali kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti na kuwashauri wakulima kutokata hovyo miti basi wahakikishe wanaacha baadhi ya miti mashambani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri Mkuu ni hotuba kiongozi kwa Wizara zote Serikalini, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefafanua kwa upana juu ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano ikiwemo masuala ya elimu, afya, miundombinu ya mawasiliano na uchukuzi, kilimo, ujenzi, bandari, reli ya kisasa, ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa viwanja vya ndege, kilimo na mifugo, maji, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda kwenda Tanga, ununuzi wa meli mpya na vivuko,ujenzi wa madaraja makubwa nchini, umeme na ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme wa maji wa Mwalimu Nyerere Hydropower Station pamoja na uzalishaji wa umeme kutoka katika vyanzo vingine kama vile gesi, makaa ya mawe, umeme jua na joto ardhi. Miradi hii itasaidia kuliwezesha Shirika la Umeme nchini TANESCO na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kusambaza umeme nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imeleta mapinduzi makubwa katika kupeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, huu ni mwanzo mzuri katika kulijenga Taifa letu.

Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) huu ni ukombozi katika kuhakikisha kwamba barabara zetu za lami na changarawe ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuokoa fedha za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ya awamu ya tano imefanya kazi kubwa sana katika kuleta mageuzi makubwa ya uchumi nchini ambapo tumeshuhudia mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, masuala la mapambano dhidi ya rushwa yameimarishwa ambapo fedha nyingi zimeokolewa. Pia Serikali yetu imeimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi, tunaipongeza sana Serikali yetu ya awamu tano kwa kuimarisha makusanyo ya mapato, niombe Serikali iendelee kuimarisha na kupanua wigo wa ukusanyaji wa kodi.

Mheshimiwa Spika, kufunguliwa kwa shirika letu la ndege la ATCL ni jambo kubwa na la kujivunia, ndege mpya zimenunuliwa na hivyo kuinua sekta ya utalii nchini na kuleta fedha za kigeni nchini na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama vinachangia pakubwa katika kuhakikisha utulivu na usalama wa nchi, hivyo nashauri Serikali ivipatie vitendea kazi vya kisasa ili kufanya vyombo vyetu viende na wakati.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili pia na niweze kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Kama wenzangu walivyokwishakutangulia kusema Wizara hii inao watendaji wazuri sana. Na kwa maana hiyo, nipende tu kwa kweli, kuwapongeza; nimpongeze Ndugu yangu Mheshimiwa Medard Kalemani na dada yangu Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kazi nzuri sana ambayo wanaendelea kuitendea nchi yetu. Ninaamini kabisa kwamba, Tanzania ya viwanda inakuja na niseme tu kwamba, kwa kweli, ninaunga mkono shughuli mbalimbali ambazo zinafanywa na Wizara hii ukiwemo mradi mkubwa wa Stiegler’s Gorge ambao unatekelezwa na Taifa letu ambao tunatarajia kupata megawati 2100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninajua kwamba, lengo letu kama Serikali ni kupata megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025. Nina imani kubwa kwamba, ndani ya kipindi hicho kama kweli watendaji hawa wataendelea na morali waliyonayo ninaamini kabisa kwamba, Tanzania itafikia uzalishaji wa megawati 10,000 kipindi hicho kitakapokuwa kimefikia na Tanzania ya viwanda itawezekana kwa sababu, hakuna viwanda bila kuwa na nguvu za umeme zinazoweza kuwa za uhakika tukaweza kufanikiwa kwenye sekta hiyo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, kwa kweli Wizara hii imekuwa ni Wizara ya mfano.

Mheshimiwa Spika, na kwa wale ambao wanapinga kuendelea kuzalisha umeme katika Stiegler’s Gorge na wanaosema kwamba, wao wanataka return kwenye REA ambayo imewekezwa katika Tanzania hii, basi mimi niwaombe kwamba, kwa kweli, wabadilike mawazo kwa sababu, Watanzania ambao wamepata huduma hii ya umeme kupitia Mradi wa REA na TANESCO leo hii ukisema kwamba, uuzime au uondoe hiyo huduma, kelele ambazo utazisikia hapo hutakaa usahau. Kwa hiyo, nimeona kwa mfano kabisa katika Wilaya yangu ya Mbogwe baada ya huduma hii ya umeme kuwekwa kwa Wananchi, Wananchi kwa kweli wamefurahia huduma hizi na kwamba, maisha yamekuwa marahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe tu kwamba, utekelezaji wa Mradi huu wa REA Awamu ya III uendelezwe kwa kasi zaidi na kwamba, wakandarasi kama wewe Mheshimiwa Kalemani umekuwa ukifika mara kwa mara katika Wilaya yangu ya Mbogwe na umehamasisha utekelezaji wa Mradi huu wa REA Awamu ya III, lakini naona kasi bado kidogo, lakini naomba tu kwa kweli, Mungu akujalie na msaidizi wako Mheshimiwa Mgalu muendelee kufanya kazi hii kwa ustahimilivu ambao mnauonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine nikushukuru Mheshimiwa Waziri baada ya kuwa umekuja umeweka umeme katika eneo la Nyakafuru, wachimbaji wangu wadogowadogo katika eneo hilo la dhahabu ninaamini kwamba, kwa kweli shughuli za uzalishaji wa dhahabu katika eneo la Nyakafuru litakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ninachotaka kuomba tu ni kwamba, REA imekuwa inatoa huduma katika maeneo machache. Naomba ule mradi wa densification na wenyewe ufanyiwe wepesi, ili kusudi uanze utekelezaji mara moja. Na vile vijiji ambavyo bado havijafikiwa katika utekelezaji wa REA naomba Serikali ifanye haraka ili ikiwezekana mwaka 2020/ 2021 vijiji vyote viweze kuwa vimepata hii huduma ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu, tumeshuhudia kwamba maeneo mbalimbali yanachangamka sana yanapopata huduma hii ya umeme. Kwa hiyo, niombe tu kwamba, kwa kweli, kwa wale ambao watakuwa hawahitaji umeme kwao basi, huko Mbogwe sisi tunauhitaji kwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo mimi naomba tu niendelee kuwaombea kwa Mungu Wizara hii waendelee kufanya kazi zao kwa ukamilifu, ili kusudi Tanzania ya viwanda iweze kufikiwa. Baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri asilimia 100 kwa 100, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze na mimi kuchangia hotuba ya Waziri wetu wa Fedha na Mipango siku hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja asilimia mia moja kwa mia moja. Nayasema haya kwa sababu hotuba ya bajeti iliyosomwa kwetu hapa ikitanguliwa ikitanguliwa na hotuba ya hali ya uchumi wa nchi yetu imeonyesha dhahiri kwamba ni hotuba ya Serikali ya watu, iliyowekwa kwa watu, ili itimize malengo kwa ajili ya watu. Ninayo imani kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi itatenda yote ambayo imeahidi kupitia bajeti hii, ninao uhakika kwa sababu bajeti zote ambazo zimepita zimetekelezwa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Serikali yetu imekuwa ni Serikali sikivu inajali watu inatekeleza mipango inayoipanga kwa wakati. Niseme tu kwamba katika kuanza kuchangia kwangu nitajikita zaidi katika suala zima la kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima wameajiriwa katika sekta hii na kwa ajili hiyo Serikali inatakiwa iweke msukumo zaidi katika sekta hii ambayo kimsingi inatakiwa iende sambamba na kaulimbiu ya Serikali yenyewe ya Tanzania ya viwanda. Maana mataifa yote ambayo yameendelea yalianda na mageuzi ya kijani, baadaye ya kaja mageuzi ya viwanda na mambo yote haya yakafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili hiyo niseme kwamba Serikali iwekeze zaidi katika tafiti mbalimbali, ziwekewe pesa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba utafiti unafanyika katika udongo. Udongo ukishajulikana tuna imani kwamba yale mapungufu ambayo yanakuwa yanajulikana kwamba haya ndio mapungufu basi hata mbolea ambayo itakuwa inatakiwa kwenye aina fulani ya udongo itajulikana. Tofauti na sasa hivi ambapo mbolea za aina moja zinakuwa zinapelekwa katika aina mbalimbali za udongo. Udongo mwingine upo ambao ni alkaline na mwingine ni acidic, kwa hiyo, matokeo yake unakuta kwamba saa nyingine wakulima wanaweza wakajikuta kwamba saa nyingine uzalishaji katika mashamba yao unakuwa ni hafifu kutokana na kwamba utumiaji wa mbolea unakuwa hauendani sambamba na mahitaji kwa wakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imejikitika kuhakikisha kwamba maeneo ya vipaumbele hasa katika miundombinu iwe ya barabara, ya reli, miundombinu ya umeme, maji na mambo yote haya ndio hasa kiini cha maendeleo ya Watanzania wenyewe. Ninashangaa pale watu wanaposema Serikali yetu inajali zaidi maendeleo ya vitu badala ya watu nashangaa kidogo, kwa sababu haiwezekani ukawa na maendeleo ya watu ukayatenga na maendeleo ya vitu. Kwa mfano, ujenzi wa hospitali, ujenzi wa barabara kwa sababu hospitali inaenda na afya ya mwananchi. Kwa hiyo, mwananchi ambaye atakuwa na afya goigoi hawezi kujenga uchumi, hawezi kushiriki katika uzalishaji mali na kwa maana hiyo mimi nina imani kabisa kwamba Serikali yetu iko kwenye njia sahihi na nikuombe Mheshimiwa Mpango na Naibu wako pamoja na wasaidizi wako muendelee kupiga kwenye bull kama ambavyo mmeendelea kufanya, watu wote hawa ambao tuko hapa tunajaribu kuzungumza, wakati mwingine tunajaribu kupiga makelele ya kujaribu kuwatoa kwenye target, ila naomba tu kwa kweli muendelee kushikilia kama hivi ambavyo mmepanga na mtekeleze kwa umakini mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imekuja na utaratibu wa ujenzi wa bwawa kubwa la uzalishaji umeme la Stiegler’s Gorge na ni juzi tu nimemuona Mheshimiwa Waziri mwenyewe amekwenda kuhakikisha kwamba ujenzi unaanza na mkandarasi amekabidhiwa site. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba utekelezaji wake ufanyike na kama ambavyo wameahidi wanasema kwamba baada ya miaka hiyo mitatu hizo megawatts 2,115 zitazalishwa, basi na yote yakafanyike ili sasa wale matomaso, wale wanaotaka mpaka waone, basi waje waone haya maajabu ya Serikali ya awamu ya tano yanafanyika wakati wao wenyewe wakiwa hai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ni Serikali sikivu na siku zote imekuwa ikisema na kutenda. Imesema inaanza ujenzi wa Standard Gauge Railway, ujenzi huo umeanzaDar es Salaam - Morogoro, wale ambao hawajawahi kutembelea wakaone, wataona ujenzi unaendelea. Morogoro – Dodoma ujenzi unaendelea na niombe tu kwamba hata ule mpango wa kujenga ile reli ya kutoka Isaka kuelekea Rusumo, ni- declare interest kwamba hiyo reli itapita pia katika Jimbo langu la Mbogwe.

Kwa hiyo, mimi ninaomba kwamba kwa kweli Serikali ya Tanzania na Serikali ya Rwanda mfanye hima kuhakikisha kwamba mnaijenga hiyo reli kwa sababu uwepo wa barabara ambayo sasa hivi inatoka Isaka kwenda Kigali, Rwanda, tumeona matokeo yake. Wakati ambapo barabara ya lami ilikuwa bado haijajengwa, maendeleo katika kanda yetu kwa kweli hayakuwa mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mpaka sasa baada ya kuwa ukamilifu wa barabara ya lami kutoka Isaka kwenda Kigali, Rwanda ilipokamilika na Kampuni ya Codify ikiwa imeshiriki katika ujenzi huo, tumeyaona maendeleo ya kasi ambayo yamejitokeza katika Miji ya Isaka, Kahama, Masumbwe, Ushirombo, Ruzewe, kote ambako barabara hii imepita, tumeyaona nageuzi na wengine hata wale ambao wanajua kwamba ambapo barabara ya lami kutoka Dar es Salaam kuja kukomea Dodoma hapa, kutoka hapa Dodoma kuelekea Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga mpaka Mwanza, tulikuwa tunasafiri kwa siku zaidi ya tatu. Sasa lakini kwa wakati huu, hali kama inakuwa ni nzuri tu, unafika siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na unapotumia muda mfupi katika masuala mbalimbali, unahakikisha kwamba unashiriki katika ujenzi wa uchumi. Maana wanasema wazungu time is money. Kwa hiyo, unapokuwa unaweza ku-manage muda, ni hakika kabisa kwamba utakuwa mzuri sana katika ujenzi wa uchumi na kwa maana hiyo sisi tunapotengeneza miundombinu ya barabara...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ooh basi nakushukuru niombe kuunga mkono tena kwa mara nyingine, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hutuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Hotuba hii imejaa majibu ya kero mbalimbali za wananchi katika sekta zote muhimu za kijamii kama vile elimu, miundombinu, umeme, reli, barabara, maji, afya, viwanja vya ndege, bandari, madini na kadhalika. Aidha, kero mbalimbali zilizokuwa zinakwaza mazingira wezeshi katika kuvutia uwekezaji nchini Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha vikwazo vilivyokuwa vinasababisha mazingira magumu kuvutia wawekezaji kuja hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi mbalimbali na tozo zilizokuwa zinakwamisha uwekezaji katika sekta mbalimbali, Serikali imechukua hatua kwa kukutana na wadau ana kwa ana. Kwa mano, Mheshimiwa Rais amekuwa akikutana na wadau muhimu katika sekta za madini na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali ambapo katika mikutano yote ambayo Mheshimiwa Rais amepata fursa ya kukutana ana kwa ana na wadau kero za nyingi zimetatuliwa na kurejesha imani ya wafanyabiashara kwa Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu wezeshi, kwa mfano Serikali imeweza kuanza ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa standard gauge (SGR) ujenzi wa Reli hii ukikamilika utachangia kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ambayo ni bandari muhimu kwa nchi ambazo hazipakanina bahari za Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemocrasia ya Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, uwepo wa SGR katika Tanzania itakuwa ni ukombozi wa moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi kwa ujumla katia kusafirisha watu na mizigo ambapo huduma za usafirishaji utasaidia kupatikana kwa vitu na vifaa kwa bei nafuu na hivyo kudhibiti mfumko wa bei nchini kwani maeneo mengi reli hii inapitia katika mikoa mingi hapa nchini. Pia Serikali imeanza kuchukua hatua kuifufua reli ya Kaskazini lengo ni lilelile la kujenga uchumi kwa usawa katika nchi yetu katika maendeleo ya watu na vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za afya zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa ambapo vituo vya afya vingi vimejengwa na kukarabatiwa zikiwemo hospitali za wilaya na mikoa na zile za rufaa, ambapo watanzania wanapata huduma hizi muhimu na kuweza kupunguza kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanja vya ndege vingi vimeendelea kujengwa pamoja na Serikali kununua ndege mpya ambazo zitarahisisha usafirishaji wa watu na vitu hasa watalii. Utalii ni sekta muhimu katika kuchangia katika kukuza uchumi kwa kuwa chanzo kikubwa cha fedha za kigeni nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanza kwa ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme wa maji katika bwawa la Stieglers Gorge utakaozalisha megawatts 2115 ni mwelekeo sahihi katika kuelekea Tanzania ya Viwanda. Kukamilika kwa mradi huu mkubwa tunayo imani kubwa kuwa tatizo ka mgao wa umeme litakuwa limepata ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza sana Serikali kwa kutekeleza kwa vitendo kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kuja Dodoma na kuweza kufanikiwa kukamilisha ujenzi wa Ofisi za Wizara mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba hapa Dodoma. Nasi tunaipongeza Serikali kwa kuipatia fedha Wilaya ya Mbogwe ili iendelee na ujenzi wa majnengo ya Ofisi za Mkuu wa Wilaya na jengo la Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo maombi kwa Serikali kutoa fedha kwa ajili ya unejzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Butengolumasa, Iparamasa, Mbogwe, Masumbwe, Mwabomba, Nyankende, Bugomba na Ulowa, Ulowa hadi Kalina ili kuwa chachu ya maendeleo katika maeneo ambako barabara hii inamoitia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ba Mipango.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. AGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika na mimi nashukuru kwa wewe kuweza kunipatia nafasi hii ili niweze na mimi kutoa mchango wangu katika huu muswada muhimu wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi la kwanza naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na zaidi sana langu itakuwa tu ni ushauri, kuona kwamba ni namna gani hii mamlaka itakavyokuwa inaweza kuwasiliana na Idara ya Mifugo pamoja na idara nyingine za Serikali; kwa maana ya kwamba mara nyingi magonjwa mengi yanatokana na mifugo kwa sababu ya maisha tunayoishinayo.
Sasa nilikuwa nataka kujua ni jinsi gani ambavyo Ofisi hii ya Mkemia Mkuu wa Serikali itakavyoweza kushiriki katika kujua magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza yakawa yanatokana na mifugo na mimea vilevile ili kwamba tusije tukawa na double standard au kuwa na duplication ya kazi, kwamba labda pengine tukimaliza kuwa na Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali basi kunakuwepo na kitengo kingine kinachohusiana na mambo ya mifugo na mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni juu ya vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa sababu tunaona katika ulimwengu huu kweli kuna wakati mwingine kuna silaha mbalimbali ambazo zinatengenezwa za kemikali, nyingine za kibaiolojia, sasa hapa sijui ni namna gani vyombo vya ulinzi na usalama vitakavyohusishwa, lakini naamini Serikali inayo nafasi nzuri ya kuweza kuwahusisha wataalam wetu wa vyombo hivi, ili kuweza kunusuru Taifa letu lisiweze kuingiliwa na watu kama magaidi na wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua kumekuwa na tahadhari imetolewa na Kamati yetu, katika taarifa yao wakawa wanaonesha wasiwasi juu ya kuwepo kwa double functions za mamlaka mbalimbali, kwa mfano TBS na hii TFDA, lakini naamini kwamba si tu hizo, vilevile kuna EWURA maana hawa watu wa EWURA na wenyewe wanahusika na mafuta, maji na mengine hayo yaliyopo hapo. Sasa nikasema tu kwamba ni vizuri tu Serikali ikawa na coordination nzuri ili kusudi tusije tukajikuta kwamba wakati mwingine hii Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali isije ikazidiwa kazi. Maana kuna wakati mwingine tunaweza tukasema kwamba sasa hizi idara nyingine ziache kufanya kazi zake badala yake majukumu yote yapelekwe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri tu kwamba hizi taasisi nyingine na zenyewe zipewe uzito kama unavyostahili. Na kikubwa zaidi mimi nilichokuwa nataka nishauri ni kwamba, Serikali iiwezeshe sasa hii Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ili tusije tukajikuta kwamba tumeanzisha kitu kama hiki, lakini yanapotokea majanga tunajikuta kwamba sasa wakati mwingine matokeo yanakuwa yanachelewa na wakati mwingine unaambiwa kwamba, labda sampuli zimepelekwa Nairobi au nyingine zimepelekwa Afrika ya Kusini, ili kuweza kupata matokeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri tu kwamba Serikali yetu ijiandae sasa, tunapoanzisha kitu kama hiki kisije kikawa ni kiini macho. Zaidi sana tuishauri tu Serikali iangalie maoni mbalimbali na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge, ili hatimaye tuweze kufanikiwa katika hii azma tuliyoikusudia katika kupitisha muswada huu kuwa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Ahsante.