Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Augustine Philip Mahiga (20 total)

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, kumekuwa na utaratibu wa Watanzania wanaofariki nje ya nchi, ndugu zao wanaokuwepo hapa nchini hupata taabu, adha na kucheleweshwa kuletewa maiti. Inafikia familia za kimaskini zinauza hata vitu vyake ili kuweza kuleta ile maiti nchini. Je, ofisi za Ubalozi zimejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wenye hali duni maiti zao zinapopatikana kule ziletwe nchini haraka? (Makofi)
Swali la pili, kuna baadhi ya Balozi zina utaratibu wa kupanga siku maalum za kuwahudumia Watanzania, hususan tabia hiyo ilikuwepo katika Ubalozi wetu wa Afrika Kusini. Tabia ile ilileta matatizo na usumbufu kwa Watanzania ambao wanataka huduma katika ofisi za Ubalozi.
Je, sasa hivi wamejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wanaotaka huduma kwenye Balozi zao nje ya nchi yetu wanapata huduma haraka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa nyakati tofauti kumeripotiwa baadhi ya Watanzania ambao wamefiwa na ndugu zao kupata taabu katika kusafirisha miili, lakini katika hali ya jumla Balozi zimekuwa zikisaidia sana pale wanapopata taarifa sahihi kwa wakati. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba mara nyingine ucheleweshaji unatokea kutokana na Balozi zetu kuweza kupata taarifa kwa wakati, lakini katika hali ya jumla, kati ya masuala ambayo Balozi wetu zinatakiwa zishughulikie ni kuhusu maslahi ya Watanzania wanaoishi huko ikiwa ni pamoja na pale wanapopata taabu, wanapopatwa na matatizo ikiwa ni pamoja na kifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna changamoto ambazo zimetokea, kila wakati Wizara imekuwa ikichukua changamoto hizo na kuzifanyia. Kwa hiyo, tunaamini huko mbele tunakoelekea, changomoto hizi zitaendelea kupungua na hasa sasa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejikita katika kuleta ufanisi na nidhamu katika utumishi wa umma. Kwa hiyo, tunaamini upungufu na changamoto ambazo zimekuwa zikitokea nyuma, zitapungua kama siyo kuondoka moja kwa moja.
Ni rai ya Mheshimiwa Mbunge kuhusu Balozi zetu kupanga siku maalum kwa ajili ya kuwatumikia na kutoa huduma kwa Watanzania, pendekezo la Mheshimiwa Mbunge ni zuri, Wizara italiangalia, lakini ifahamike kwamba hakujaripotiwa kwa kiwango kikubwa kuhusu Watanzania kushindwa kupata huduma za kibalozi, lakini kama nilivyosema tutalipeleka na kuliangalia na iwe ni moja kati ya njia za kususluhisha changamoto ambazo zinatokea.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na kuwa Zanzibar ni mshirika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kuna mambo ambayo si ya Muungano kwa mfano kilimo, utalii, elimu ya msingi na sekondari, mifugo na mengineyo.
Je, kwa nini basi Zanzibar kama Zanzibar isiachiwe kujiwakilisha yenyewe katika masuala kama haya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika ulimwengu huu kuna nchi ambazo zimeungana lakini zinaridhia baadhi yao kutoa mamlaka kushiriki katika mambo mbalimbali katika Jumuiya za Kikanda na Kitaifa. Kwa mfano, Switzerland kupitia tamko la Khartoum inaridhia baadhi ya nchi kushiriki katika masuala mbalimbali. Pia New Zealand kuna kisiwa cha Niue Island kinashiriki katika baadhi ya mambo. Pamoja na hayo kuna Umoja wa Visiwa vya Bahari ya Hindi ambayo Tanzania si mwanachama, kwa nini basi Zanzibar isiachiwe kujiunga na Jumuiya kama hii ikashiriki katika kufanikisha masuala yake? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni kweli Serikali ya Zanzibar ina mamlaka katika sekta fulani za maendeleo kama vile kilimo, uchukuzi na kadhalika. Kutokana na makubaliano hayo chini ya Muungano mazao yatokanayo na uzalishaji ndani ya Zanzibar yanapata nafasi ya kuuzwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kuuza ndani ya Afrika Mashariki Zanzibar inahakikishiwa soko la nafuu. Kwa hiyo, kile kinachozalishwa kule Zanzibar kinapata nafasi kwenye Jumuiya ambayo Zanzibar ni sehemu ya Serikali ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kama ilivyo katika Muungano wetu kuna mambo ambayo yanaainishwa ambayo ni ya Muungano na kuna mambo ambayo yameainishwa na kukubalika ambayo yako chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika nchi ambazo umetoa mifano nao wanakuwa na taratibu za mgao wa madaraka katika sekta mbalimbali. Sisi katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania tumeainisha na kukubaliana kwamba masuala ambayo yatakuwa chini ya Muungano ni kama kwa mfano Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Mawasiliano ya Kimataifa. Haya inategemea na jinsi nchi ambazo zimeungana zinavyokubaliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna maeneo ambayo Tanzania inatakiwa kushiriki na labda bado hatujashiriki hilo ni suala ambalo linaweza kuzungumzwa na kuainishwa ndani ya Bunge hili. Kwa sasa hivi hapo tulipo Muungano wetu unakidhi kabisa katika nafasi yake ndani ya Jumuiya ya Kimataifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Njia zinazotumika kuzitangaza fursa zinazopatikana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa ni zile zile ambazo zinawafikia tu watu wanaoishi mijini na wachache waliopata shule ya kutosha, lakini elimu hiyo haiwafikii watu walio vijijini na hasa wanaoishi mipakani ambao wangependa sana kuzijua hizi fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kujua Serikali ina mpango gani tofauti wa kuhakikisha fursa zinazopatikana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaelezwa kwa wazi na kwa kina na kuwafikia Watanzania wote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nchi wanachama zinabadilisha sheria zao ili wananchi waweze ku-enjoy fursa zilizokuwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na wenyewe wana kaulimbiu yao wanasema Chungulia Fursa. Sasa Watanzania walichungulia fursa zilizopo ndani ya Afrika Mashariki wakalima mahindi kwa kiasi kikubwa ili waweze kufaidi Soko la Afrika Mashariki kwamba wauze mahindi ndani, lakini wauze mahindi nje ya nchi hii kwa maana kwenye nchi za Afrika ya Mashariki. Serikali ya Tanzania ikapiga marufuku mahindi kuuzwa nje ya nchi.
Je, Serikali haioni kwamba inawanyima Watanzania fursa za ku-enjoy Soko la Afrika ya Mashariki? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tunawafikiaje wananchi walio katika vijiji? Hakuna tofauti ya kuwafikia wananchi walio katika vijiji kama tunavyowafikia katika kampeni zetu, katika kutangaza sera za Serikali kwa kutumia vyombo vilivyopo na njia zilizopo. La kwanza, ni kutumia redio na television. Wananchi wengi siku hizi wanazo redio na wengine wanatazama television.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya pili ambayo tunaitumia kuwafikia wananchi wetu ni kufanya makongamano katika maeneo ya vijijini, hasa yale ambayo wananchi wamekuwa karibu na miji. Hili limekuwa na mafanikio mazuri sana kwa sababu, wananchi wengi wamekuwa wakifuatilia kwa makini siyo tu redio, na warsha ambazo zinapelekwa kwao. Na hii tumeanza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba Serikali yetu ina mkakati wa kuhakikisha kwamba tunacho chakula cha kutosha katika nchi yetu. Baada ya hapo hakuna kizuizi cha kuweza kuuza mahindi nje ya nchi. Sasa hivi kuna utaratibu wa kutengeneza maghala na kufanya tathmini inayoeleweka kwamba chakula cha kila mkoa au kutoka mkoa hadi mkoa kinaweza kukidhi mahitaji ya wananchi. Baada ya hapo, hakuna kizuizi cha kuweza kuuza mahindi nje ya mipaka yetu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu ya historia ya Mheshimiwa Waziri. Halmashauri ya Wilaya ya Chemba tayari tumeshatoa jengo kwa ajili ya Hakimu wa Wilaya na Hakimu wa Wilaya ya Chemba ameshateuliwa kama Waziri hana habari. Sasa swali langu ni kwamba, kama majengo haya Waziri anasema inategemea na upatikanaji wa fedha ndio mahakama itajengwa, Hakimu ameteuliwa kuja kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri kwa taarifa tu ni kwamba, Wizara ya Mheshimiwa Waziri tayari imeshanunua kiwanja Chemba na wamekwenda kukikagua. Sasa anaponiambia hapa kwamba inategemea na upatikanaji wa fedha, naomba anihakikishie hizo fedha kwenye bajeti ya mwaka huu zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba pesa hizo zimetengwa na ninaposema upatikanaji wa pesa ni kama fedha hizo tukiziomba zilizotengwa tutaweza kuzipata kutoka Hazina ili tuzielekeze katika kufanya shughuli za kazi na huduma katika Wilaya ya Chemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumhakikishia hilo. Ahsante.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majibu niliyoletewa na Serikali ni dhahiri kuwa suala hili bado halijawekewa mkazo na bado wananchi wanapata shida wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola. Sasa Serikali haioni ni wakati sasa wa kujifanyia tathmini mahususi na kuja na mikakati thabiti ili wananchi wa Taifa hili wapate kuwa na kusimamia haki zao? Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tathmini ni muhimu na ni endelevu. Wizara yangu inaendelea kufanya hivyo na kusisitiza kwamba Tume ya Haki za Binadamu inafanya hiyo. Pia ninapenda kusisitiza kwamba suala la haki za binadamu lazima iwe ni sehemu ya utamaduni wa Taifa; na kuifanya ni sehemu ya utamaduni wa Taifa itabidi tutengeneze mkakati wa somo la Haki za Binadamu liingie katika mitaala ya shule zetu zote na katika ngazi zote. Somo la Haki za Binadamu na Utawala Bora liwe ni sehemu ya lazima kwa mafunzo yote ya vyombo vyetu vya usalama. Kama ni ulinzi, kama ni Polisi, Usalama wa Taifa au Uhamiaji, iwe ni sehemu muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Askari wetu wanaoshiriki katika vikosi vya kulinda amani duniani huwa wanapewa kozi ya haki za binadamu kwa wiki sita na Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa na Taasisi mbalimbali za Kimataifa ziko tayari kuisaidia Tanzania kuweka Chuo cha Haki za Binadamu ambacho kitatengeneza mitaala katika shule mbalimbali. Hiyo nimehakikishiwa na ninadhani inaweza kutokea tukishachukua maamuzi. Watu wako tayari kutusaidia ili haki za binadamu na utawala bora iwe ni sehemu ya utamaduni wa Taifa hili.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla ya swali la nyongeza kwanza nilitaka kusema kitu juu ya mfumo wetu huu wa Bunge Mtandao, pengine hili linafaa kurekebishwa.

Mheshimiwa Spika, muuliza swali yupo nje ya Bunge na swali limekuja hakuna access aliyopewa muuliza swali kuweza kulipata swali in advance. Kwa hiyo, nimesikiliza swali moja kwa moja bila ya kuwa na taarifa kwa sababu mwenye swali hakuwa na njia ya ku-access.

SPIKA: Mheshimiwa Ally Saleh, hilo lilikuwa tulifanye kwa utaratibu mwingine ni kwamba tu mfumo mtandao unakupiga chenga, lakini hayo mambo yako covered kabisa. Kwamba mwenye swali Mbunge yeyote kama hayuko Bungeni analitaarifu Bunge na anataarifu ni nani amuulizie swali lake na huyo anayemuulizia swali lake anatumiwa majibu yote na kila kitu anatumiwa; kwa hiyo, hayo yote yako covered, mfumo mtandao yaani uko kisawasawa, uliza swali lako Mheshimiwa Ally Saleh. (Makofi)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, lakini mwenye swali ndio kaniambia kwamba hakuna taarifa yoyote aliyoitoa. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Ally Saleh, Spika akishakujulisha unamuamini Spika au unamuamini mwenye swali ambaye wala Bungeni hayupo? (Kicheko)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, nashukuru; dhana ya swali hili ni kwenye haki jamii na kwamba, issue kubwa ni kupunguza idadi ya msongamano. Mheshimiwa Waziri hapa amesema kwamba kuna tatizo la idadi ya Majaji au Mahakimu, sasa je, anafikiri katika muda gani Wizara inajipa muda gani kuhakikisha kwamba hali itakuwa inatosha kiwango cha Mahakimu, Majaji na kulingana na kasi ya matendo ya jinai?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, amezungumza habari ya moja katika tatizo ni suala la ushahidi. Je, Mheshimiwa Waziri hafikiri kwamba kuna haja sasa ya kukazia kwenye suala la kukusanya ushahidi kujaribu kutumia mbinu mpya na za kisasa zaidi ili ushahidi ukamilike na ufikishwe Mahakamani kwa wakati, ili raia waweze kupata haki?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, katika Awamu hii ya Tano tumejitahidi sana, Serikali sio tu katika kuteuwa Majaji na Mahakimu, lakini pia katika kufungua Mahakama mpya kwenye Wilaya mbalimbali. Kwa kufuata utaratibu huu inaonekena kwamba katika kipindi cha maendeleo cha miaka mitano hii mafanikio ukilinganisha kipindi cha nyuma imekuwa ni asilimia 33.5.

Mheshimiwa Spika, kwa kutazama mwelekeo huu ninadhani tutaweza kufikia hatua nzuri tukimaliza mpango huu wa maendeleo ambao tunaona unamalizika mwaka huu na tukifuata utaratibu tuliokuwa katika mpango uliopita tunaweza kufikia zaidi ya asilimia 50 kwa kuweza kukamilisha mwelekeo wa ujenzi na uteuzi katika miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika, katika suala la upelelezi na mashahidi, mfumo mzima wa Mahakama sasa hivi ni kufanya kazi kwa karibu na mtambuka na vyombo vyote vinavyofanya kazi pamoja na haki, hasa Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini pia tumeanzisha utaratibu wa electronic ambapo tunaweza kusajili, tunaweza kupata ushahidi kwa kutumia electronic katika mikoa mitatu sasa hivi na nia yetu ni kuhakikisha kwamba mfumo huu wa electronic unaenezwa kwenye mikoa mingine. Na kwa kweli, umesaidia sana katika kuharakisha mfumo mzima wa kutoa haki ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. WAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekubali na kukiri kwamba toka mwaka 1972 wazee wa CCM wamekuwa kwenye Baraza za Mahakama: Je, ni lini Serikali italeta sheria tuweze kubadilisha wazee hawa watoke kwa wananchi na siyo kwenye vyama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wazee hawa wanatoka kwenye Chama cha Mapinduzi, haoni wanakwamisha juhudi za Mahakimu kwa kutoa haki kwa mahabusu wanaotoka Upinzani? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza lazima tutoe heshima kwa wazee wetu kwa busara zao. Kama wanatoka Chama hiki au chama kile, lakini wazee wetu ni wazalendo, wazee wetu ni walezi, wazee wetu ni kioo cha jamii, tuwape heshima wanayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, tuko katika mchakato wa kubadilisha mfumo mzima wa Mahakama na hasa katika makosa ya jinai. Sheria hii ilipitishwa mwaka 1972 na ndiyo maana tumeona umuhimu huo na mchakato huo unaendelea na pale utakapokamilika tutawajulisheni. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, samahani, nakurudisha hapa. Katika swali la msingi anasema kwamba umekiri wazee wa CCM ndio wazee wa Baraza. Ni kweli umefanya hivyo? Maana kwenye jibu lako mimi sijaona hilo. Ndiyo swali lake hasa! Unaweza kuchukua dakika moja kulijibu.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kufafanua hilo. Sijakiri hivyo, lakini nilichosema katika maelezo yangu ni kwamba wazee wazee wetu tulionao katika jamii zetu, tuwape heshima na tutambue busara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimesema kwamba kama sheria hii ilipitishwa mwaka 1972, Mahakama iko katika mchakato wa kutazama umuhimu wa kurekebisha taratibu hizo za Kimahakama na hasa kwa matumizi na uchaguzi wa wazee ambao watakuwa wanasaidia Mahakama zetu za mwanzo na za juu. Nadhani hiyo ndio ufafanuzi nilioutoa. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, binafsi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yenye ufasaha wa hali ya juu sana. Ni majibu ambayo yanatoa matumaini makubwa siyo kwa Wilaya ya Kilindi tu, lakini maeneo mengine ya Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, pamoja na shukurani hizo, nina swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Mahakama hizi ni chakavu na Mahakana zinazofanya kazi ni tatu tu.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuanzisha hata Mahakama za Mwanzo I Mean kuanzisha hata ofisi ndogo ili huduma hii ipatikane kwa muda mfupi wakati tukisubiria ujenzi wa Mahakama hizi za Mwanzo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nitoa shukurani za pekee kwako. Jana ulikwenda kufungua Mahakama ya Wilaya ya Kondoa na ulifuatana na Jaji Mkuu. Katika hotuba yako ulidhihirisha kwamba ni jitihada za Serikali kujenga Mahakama, kuboresha Mahakama na kujenga Mahakama za karne ya 21 ambazo zina TEHAMA na vifaa vya kisasa vya kielektroniki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba kwanza kuna huu mpango mahususi wa Mahakama ya Tanzania ya kujenga Mahakama katika ngazi zote mwaka huu na mwaka ujao. Nataka kuwahakikishia kwamba kitendo cha sisi kuamua kupeleka mashauri kutoka Mahakama hizo chakavu na kwenye maeneo ya awali na ya muda, utaendelea kuboreshwa.

Mheshimiwa Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo haitasimamisha hata kidogo usikilizaji wa mashauri katika Mahakama hizo na jitihada za uboreshaji na ujenzi tutazikamilisha katika mwaka huu wa fedha na kuendelea katika mwaka ujao wa 2021. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mbulu Vijijini, Mji wa Haydom hauna Mahakama na kutoka Haydom mpaka Mahakama ya Wilaya ni kilomita 86 na tunayo ahadi ya kujengewa Mahakama ya Mwanzo pale. Kutokana na Mbulu tumeshawapa eneo:-

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kutenga bajeti ya kujengewa Mahakama ya Mwanzo katika Mji mdogo wa Haydom? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nasema Wilaya ya Mbulu ina mahitaji mengi ya huduma, mojawapo ni Mahakama. Kwa mpango nilionyesha hapa, nitafanya ushauriano na Mahakama Kuu na Msajili wa Mahakama tuone kwamba pale Haydom tutachukua hatua gani. Ila kama iko kwenye mpango; na nadhani iko kwenye mpango, nitathibitisha, tutajitahidi kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Spika, nataka pia nichukue nafasi kusema, kuna Mbunge alisema juzi kwamba kuna mahabusu ambao wanachukuliwa na bodaboda kutoka Magereza kwenda Mahakamani katika Gereza la Ulanga. Nimezungumza na DPP ambaye alikuwa kule Ulanga hivi karibuni, anasema hakuna haja ya kutumia pikipiki wala gari kupeleja mahabusu katika Mahakama ya Ulanga kwa sababu watu wanaweza kutembea siyo zaidi ya mita 500 kutoka kwenye Gereza lile mpaka kwenye Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alivyosema, taarifa ile ilikuwa imetiwa chumvi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nishukuru sana majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza katika majibu ya Serikali nimeeleza kwamba kuna juhudi zinafanyika za kupata eneo ili jengo la Mahakama ya Wampembe lipatikane. Lakini niseme tu kwamba tatizo la kupata eneo si tatizo kupata eneo mimi na wananchi tunaahidi kutoa eneo kwa haraka. Tunaiomba Serikali kupitia na kwa vile sasa hivi tunaenda kwenye bajeti.

Je, Serikali itakuwa tayari kuweka au kutenga pesa ya ujenzi wa jengo hilo la Mahakama ya Wampembe kwa mwaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kupitia bajeti ya Serikali tumekuwa tukiahidiwa wananchi wa Nkasi kupata Mahakama ya Wilaya miaka mitatu mfululizo na leo kwenye kupitia majibu ya swali hili Serikali inatoa ahadi kwamba mwezi wa tani ujenzi huo utaanza. Je, zile sababu ambazo zipelekea tukashindwa kujenga na wananchi wakaanza kutuona Wabunge tunapoenda kuwaaambia tutapata jengo kwamba ni waongo? Je, zimeondoshwa? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ingawa hatutajenga Mahakama katika eneo hilo mwaka huu katika bajeti yetu lakini tutatoa kipaumbele katika bajeti itakayofuata mwaka kesho kama inaavyosema tufanye kazi kwa pamoja na tutajitahidi kutumia Mahakama ambayo sasa hivi iko katika hilo jengo ambalo tumeliazima lakini tunajitahidi tuingize katika bajeti ya mwaka kesho suala hili la ujenzi wa Mahakama haki. Tunatoa kipaumbele kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili tumejitahidi na mmjeitahidi na tunashukuru tumeondoa vikwazo vyote tumeingiza kwenye bajeti ya mwaka huu na mwezi Mei, nakuhakikishia ujenzi wa Mahakama hiyo utaanza bila wasiwasi ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale ni wilaya ambayo ilianzishwa mwaka 75 leo ina umri wa miaka 45. Wilaya ile ina kata 20 lakini Mahakama mbili tu Mwanzo, na Mahakama ya Mwanzo ya Liwale Mijini ndio inayochangiwa na Mahakama ya Wilaya kwa maana kwamba Mahakama ya Wilaya hawana jengo. Lakini nilipouliza swali hili mwaka 2017 Mheshimiwa Kabudi akiwa hapo kwenye hicho kiti alisema mwaka 2018 inajengwa hospitali ya Wilaya. Je, Serikali kwenye majibu yale mlikuwa mnanidanganya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelewa ni kwamba huwa kunakuwa na jitihada za pekee, kama Waziri anatoa majibu, anafanya kila njia kuweza kuhakikisha kwamba inatekelezwa. Ningependa kurudi na kutazama rekodi za mazungumzo hayo na jitihada ambazo zilifanywa, lakini Liwale ni mahali ambapo kama ulivyoona mchakato wa kufungua Mahakama katika Wilaya za Lindi na Mtwara, umekuwa ukiendelea kwa kasi sana. Kama kulikuwa na ahadi kama hiyo, Wizara tungependa kufuatilia na Mahakama iendelee kujitahidi kutekeleza ahadi hizo.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kwa ridhaa yako naomba niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji wake wa Ilani wa ujenzi wa Mahakama za Wilaya nchini Tanzania. Tunashuhudia Mahakama mbalimbali za Wilaya zikizinduliwa zikiwemo za Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha Mahakama za Mwanzo za Kariakoo, Magomeni, Ilala, Temeke na Mbagala?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ni mahali pa watu wengi, mashauri ni mengi na kioo cha Taifa na cha Wizara yangu. Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba Mahakama hizi zinakuwa na sura nzuri na zinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha ina maana tatu. Kwanza ni kufanya ukarabati wa kuhakikisha kwamba Mahakama hizi ziko katika hali nzuri. Kuboresha pia kunamaanisha kwamba, Mahakama hizi zipewe teknolojia ya kisasa hasa katika uwezo wa kuandikisha Mahakama na kuweza kusikiliza kesi hizi. Tunaingiza utaratibu wa teknolojia ya kuweza kusikilizwa kesi hizi na kuandikisha na Mahakama za Dar es Salaam zinapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mkakati wetu wa kutumia magari ya kusikiliza kesi, tumeanza utaratibu huo na kufanya majaribio katika Mkoa wa Dar es Salaam. Katika uboreshaji wa aina hii mwanzo itakuwa ni Dar es Salaam kabla hatujapeleka sehemu nyingine zaidi.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba kuna changamoto kubwa sana ya ukatili kwa wanawake, ikiwemo na watoto kwenye masuala ya ubakaji. Nasi tunafahamu kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kuwahakikishia usalama Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye makosa ya ubakaji, kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu cha 5 cha Sheria ya Sexual Offences Special Provisions Act ya Mwaka 1998 ambayo imeenda kufanya marekebisho ya Kifungu cha 130 cha Sheria ya Adhabu (Penal Code), tunaona kwamba, kigezo au masharti ya kuthibitisha kosa la ubakaji ni mpaka yule aliyebakwa athibitishe kwamba kulikuwa kuna kuingiliwa (penetration). Mazingira hayo ni magumu sana katika utaratibu wa kawaida kuthibitisha kwamba mtu amekuingilia, yani ku- prove penetration siyo kitu kirahisi na hasa kwa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni swali la kwanza. Nataka kufahamu: Je, Serikali haioni katika mazingira haya kwamba kufanyike marekebisho ya sheria, ili standard of proof au ili kuthibitisha kosa la ubakaji ipunguzwe kiwango chake ili kusiwe kuna haja ya ku-prove penetration kwa sababu, watoto siyo rahisi kwao kuweza kuthibitisha jambo kama hilo, lakini mazingira yote kiujumla ya kosa hilo yaangaliwe ili kuweza kutoa haki. Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuongeza adhabu kwa wale watakaothibitika kwamba wamefanya kosa la ubakaji ili adhabu yao iwe kali ili kuhakikisha kwamba makosa haya ya ubakaji yanakwisha na watu
waogope?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali haioni kwenye kosa la ubakaji, mbakaji apewe adhabu ya kuhasiwa ili asije akarudia tena kufanya kosa kama hilo ambalo linaleta ukatili mkubwa sana kwa wanawake na watoto na linawaathiri kiasi kwamba, hata kama mtu amechukuliwa hatua, bado wale ambao wameathirika wanapata athari kwa muda mrefu zaidi? Nashukuru.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kusimamia haki za watoto na hasa wanawake katika kutoa ushahidi kwenye makosa ya aina hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika majibu yangu nimesema, la kwanza tumeondoa baadhi ya vigezo ambavyo vilikuwepo vya hasa watoto kuweza kutoa ushahidi wenyewe na kuachia Mahakama uamuzi wa busara na wa kitaalam kuweza kutoa ushuhuda huo kama kitendo hicho kimetokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimesema katika jibu langu kwamba sasa hivi kuna mfumo wa kutazama na kuboresha mfumo mzima wa kesi za jinai. Na katika hilo litakuwa hilo lingine linalohusiana na ubakaji; na kama itatoa mapendekezo, nina hakika pia mapendekezo hayo yatafuatana na adhabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kweli kwamba, kwa makosa haya adhabu ambazo zipo mpaka sasa, ni kali na inafika mpaka miaka 30 na mmejadili katika Bunge hili. Kama itabidi kuongeza adhabu hizo baada ya marekebisho na mapitio ya sheria hizi, ninashauri kwamba Bunge hili likae na tushauriane na tuweze kuzungumzia suala hili. Linahitaji uamuzi wa kisheria kama tunataka kufanya adhabu kali zaidi kuliko zilizopo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia mwenyewe Magerezani kuwaona watu wenye makosa kama haya wamepewa adhabu ya miaka 30 na wengi wao pengine watafia Magerezani. Ahsante sana. (Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba tu niongezee katika majibu mazuri sana aliyotoa Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria. Kuhusu swali la nyongeza la kwanza la Mheshimiwa Zainab kwamba bado vigezo inaonekana ni vikubwa sana katika kuthibitisha makosa; napenda tu kumwambia kwamba katika ile Sheria ya Sexual Offences Special Provisions Act ilipopitishwa, mojawapo ya masuala iliyoyaondoa kwenye Sheria ya Ushahidi ilikuwa ni ile requirement ya colaboration. Colaboration ilikuwa ni lazima uoneshe kwamba kuna ishara fulani zilizosalia baada ya lile tendo la ubakaji na hiyo ilikuwa inadhalilisha. Kwa hiyo, sheria hiyo iliondoa kitu hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku ni lazima haya yote yafuate misingi ya sheria za jinai, kwamba, lazima kuthibitisha pasipo kuacha shaka ili pia anayetuhumiwa asije akatuhumiwa isivyo sahihi au akapewa adhabu isivyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili suala la kuongeza adhabu, tayari sheria ile kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri, imeongeza adhabu imekuwa kali sana ni miaka 30. Sasa hili pendekezo la kuhasiwa lina tatizo moja, litatusababisha kuvunja Katiba, kwa sababu, Ibara ya 13(6) inaeleza kwamba ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha. Kwa hiyo, tukichukua pendekezo la kuhasiwa linatupeleka tena katika upande mwingine ambapo tutaweza kuvunja Katiba. Nafikiri adhabu zilizopo zinajitosheleza kwa sasa. Ahsante.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama sambamba na majibu mazuri ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Katiba na Sheria na swali zuri ambalo ameliuliza Mheshimiwa Zainab Katimba. Nilitaka tu kuweka mkazo. Sheria peke yake, hata tuwe na sheria kali kiasi gani hatutamaliza tatizo la ubakaji na ulawiti wa watoto na wanawake nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimesimama hapa kuendelea kutoa msisitizo kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutimiza wajibu wetu wa malezi na ulinzi wa watoto. Inasababisha mtoto anabakwa miezi mitatu bila mzazi kujua. Unajiuliza hivi huyu mtoto ana wazazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, narudisha mzigo kwa wazazi na walezi tutimize wajibu wetu, tuwafuatilie watoto wetu, tuwakague watoto wetu, tuwaulize watoto wetu, tujenge urafiki wa watoto wetu kutueleza changamoto na matatizo ambayo wanayapata. Tutaweka sheria kali, wazazi wata-negotiate na wabakaji mwisho wa siku hakuna hatua ambazo zitachukuliwa. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Sambamba na hilo nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na mpango mzuri wa RITA kuwa ifikapo 2025 kwamba idadi ya watanzania wasiokuwa na vyeti itakuwa imepungua kwa kufikia 46.5% ambayo bado ni idadi kubwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya kampeni maalum ya muda maalum ili kuhakikisha kwamba idadi ya watanzania wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa inapungua hadi kufikia 10%?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha usajili kwa kupitia njia ya mtandao, na baadhi ya wananchi wengi bado hawajui kutumia mtandao. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka kompyuta katika kila Tarafa hapa nchini ili wale wananchi ambao hawana uwezo wa kutumia mitandao hiyo wakaenda kujisajili katika maeneo ya Tarafa? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mbunge kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Moja ikiwa inahusiana na kampeni ya kuwafikia watu waone umuhimu wa kuandikisha watoto kabla ya miaka mitano na kampeni ambayo sasa hivi tunaendelea nayo ya kusajili watoto waliozaidi ya miaka 15. Mbali na mfumo wa kuandikisha katika shule, kampeni zetu zinaendelea, RITA wanampango kwenye redio, wana mpango kwenye television na pia katika matukio mbalimbali ya kitaifa. Kuna vipeperushi ambavyo vinaeleza kila pale ambapo tuna nafasi, lakini pia tunashirikiana na mitandao mingine kama vile Uhamiaji na NIDA ili kupeleka taarifa hii hasa NIDA ambao ili kuandisha na kumpa mtu kitambulisho cha Taifa wanahitaji vyeti vya kuzaliwa.

Mheshimiwa Spika, mtandao huu tutautumia kwa makini, na tusaidiane na ninyi Wabunge katika hotuba zenu, katika mikutano yenu umuhimu wa kuwahamasisha wananchi wajiandikishe kwa kutumia ofisi zetu zilizoko kwenye Kata na kwenye Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, masuala ya kompyuta na mtandao, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kutuelimisha na sisi Wabunge tuanze kutumia tablets na tunajifunza. Hii ni elimu endelevu kwa kuanzia hapa Bungeni ambayo lazima iwafikie wananchi, hatujauliza gharama za sisi hapa Wabunge kupewa tablets lakini kuna gharama. Itakuwa ni busara sana na wazo hili tunalichukua kuweza kufikisha vyombo hivi vya kompyuta siyo tu kwenye Serikali za Mitaa, lakini kufikisha mpaka kwenye Tarafa. Nashukuru Wizara ya Elimu ambayo sasa hivi imeingiza mfumo wa kufundisha kompyuta na matumizi ya IT.

Mheshimiwa Spika, suala hili ni changamoto kwa Taifa, nawaomba Wabunge kama kutakuwa katika bajeti za Wizara mbalimbali tukiomba fedha za kuleta mfumo wa Information Technology mtupitishie fedha hizo. Katika hili suala la uandikishaji naomba mtusaidie sana ili watu wa kawaida waweze kunufaika na kuwa na kompyuta. Siyo tu kwa ajili ya kuandikisha ili wapate vyeti, lakini kompyuta ni sawa na kujifunza kusoma na kuandika katika karne ya 21. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya Serikali kuahidi kwamba inaenda kujenga jengo hilo la Mahakama ya Wilaya katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, bado Mahakama ya Bariadi inapitia changamoto ya upungufu wa Mahakimu, hivyo kusababisha kesi nyingi kuchelewa: Je, Serikali ina mpango gani kwa wakati huu mfupi kuisaidia Mahakama ya Bariadi ili iweze kukidhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wakati wananchi wa Itilima wanatembea kilometa 37, wenzao wa Wilaya ya Kyerwa wanatembea zaidi ya kilometa 100. Wananchi wa Murongo, Kaisho, Bugomora, Bugara, wanatembea umbali mrefu kufuata hiyo huduma katika Mahakama iliyoko Wilaya ya jirani…

MWENYEKITI: Swali! Uliza swali!

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali. Ni mkakati gani wa muda mfupi kuwasaidia wananchi wa Kyerwa waweze kupata huduma katika wilaya yao kabla ya kufikia mwaka 2019/2020. Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Bariadi inafanya kazi nzuri sana. Hivi karibuni nilipitia kule na nikaona msongamano wa kesi mbalimbali. Ni moja ya majukumu makubwa ya Wizara hii, siyo tu kujenga Mahakama katika ngazi mbalimbali, lakini kutoa mafunzo kwa Mahakimu kadri ujenzi unavyoendelea. Hii inaenda sambamba na kuwasaidia wananchi kwa kuwapa haki ya kusimamia mashauri yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Mahakama ya Wilaya ya Kyerwa inahitaji kupata Mahakama yake mara moja. Katika mpango wa Mahakama ya Tanzania kama nilivyoeleza siyo tu tunataka kuleta Mahakama karibu na wananchi, lakini kuhakikisha kwamba tunapunguza kero ambazo wananchi wanapata ili kupata haki yao na kwa wakati. Kutokana na mkakati huo, tutaendelea kusomesha Mahakimu katika ngazi mbalimbali na tutaendelea kupanua ujenzi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali hasa katika wilaya hiyo ambayo Mheshimiwa umeizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya nyongeza, la kwanza ni kwamba kwa miaka miwili sasa, kumekuwa na matokeo ya kutisha ambayo kwa kweli, si asili ya Kitanzania, yakitokea kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu ni pamoja na kutekwa, kupigwa, kuteswa, kubamiza upinzani na mambo kama hayo, Je, Serikali kwa nini haijitokezi ikasimama ikahesabiwa ili tuone kama kweli haki zinalindwa Kikatiba na Kisheria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kwa muda sasa takribani, pengine miaka miwili, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, haina Uongozi, na kwa hivyo pengine kuna ombwe la kutazama matukio mbalimbali ya haki za binadamu. Najua hivi sasa kuna mchakato wa kutafuta hao watu wa kujaza nafasi za Tume ya Haki za Binadamu, lakini Je, kwa nini Serikali inaachia hali kudorora mpaka Tume muhimu kama hii ikakosa uongozi kwa zaidi ya miaka miwili? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio ambayo umeyataja, na ambayo yametokea, yanajulikana Serikalini na Vyombo husika na hasa Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Usalama vimekuwa vikifuatilia matukio hayo. Mara nyingi tunapata taarifa na majibu yanaridhisha, lakini kazi upelelezi na kazi ya kufatilia vituko kama hivyo na vitendo kama kama hivyo, inaweza ikachukua muda na Serikali imekubali kuchukua majukumu hayo na maswali haya yanaulizwa na wananchi kama unavyouliza, yanaulizwa pia Kimataifa na tuko tayari kutoa taarifa sahihi hapo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vitakapokamilisha uchunguzi wa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kuhusu uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu, Tume ile ina Bodi tayari, ina watendaji tayari mchakato wa kumtafuta Mwenyekiti, au Mtendaji Mkuu, imekamilika na kilichobakia sasa ni kufikisha jina hilo baada ya upekuzi kukamilishwa na Vyombo vya Usalama na kuipeleka kwa Mamlaka ya uteuzi na hiyo inaweza kutokea wakati wowote, lakini kazi imekwisha kamilika na inaweza kutokea wakati wowote. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaliyojibiwa kwa ufanisi, na weledi wa hali ya juu, pamoja na hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza na kabla sijauliza maswali hayo nataka nipongeze sana Serikali kwa hatua iliyochukua kwa kusitisha mikataba yote ambayo ilikuwa inaonekana wazi haizingatii maslahi mapana ya wananchi wa Tanzania. Vilevile niipongeze Serikali kwa kuchukua hatua mbalimbali alizoziainisha Mheshimiwa Waziri za kuhakikisha kuwa sasa mikataba itakuwa inafatiliwa kwa ukaribu zaidi. Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kutokana na mwenendo mzima na utaratibu wa malalamiko mengi yanayojitokeza katika sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji na katika sekta nyingine muhimu za kiuchumi ni dhahiri mikataba mingi iliyoingiwa imekuwa haiwanufaishi wadau wa sekta hizi hasa wakulima, wafugaji na wavuvi. Ningependa sasa Serikali ituambie wana mkakati gani maalum wa kuhakikisha kuwa mikataba inayoingiwa na wawekezaji wa kilimo, ufugaji, uvuvi, uletwaji wa pembejeo mbalimbali, masoko n.k sasa hivi yanapitiwa upya na kuhakikisha kuwa yanazingatia maslahi mapana ya sekta hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mkoa wangu wa Songwe na hususani Wilaya ya Ileje ina migodi ya makaa ya mawe, wa Kiwira pamoja na ule Mlima Kabulo na kwa muda mrefu sasa mgodi ule haufanyi kazi kwa sababu mkataba wake ulisitishwa na mgodi ule ulikuwa unaajiri takribani watu 7000 na zaidi. Je, ni lini sasa mkataba ule utapitiwa upya ili ule mgodi uanze kufanya kazi? Naomba sana Serikali izingatie hilo kwa sababu tayari tunaathirika kiuchumi.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kila wizara na kila sekta inapeleka rasimu za mikataba ambayo wangependa waingie na wadau wao hapa nchini au nje ya nchi kwa Mwanasheria Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza hapo mwanzoni mikataba mingine ni mizuri, mingine ina mapungufu, mingine ni mibaya ile ambayo ni mizuri kila wizara ambayo tayari imeshatoa taarifa yake hapa wametueleza mafanikio yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tu Wizara ya Madini imetueleza jinsi faida inavyopatikana kutoka sekta ya madini, kutokana na mikataba ya uuzaji madini yetu ulimwenguni. Na mashirika yote yaliyo chini ya Wizara ya Madini ikiwa ni pamoja na STAMICO wamekuwa wakirejesha Serikalini pato kubwa ambayo hiyo ni sehemu ya faida hiyo. Ni lazima tuangalie kwa makini mikataba mingi ina udanganyifu na tunaposaini mikataba hii tunaweza kudanganywa na ndio maana wizara yangu imeona kuna umuhimu wa kufanya marekebisho na kusahihisha mapungufu yote ya wizara zote na taasisi zote zoezi hilo linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na madhumuni ya kumuweka wakili wa Serikali kumsaidia Mwanasheria Mkuu ni hilo kuangalia ubora wa mikataba yote ambayo Serikali na Wizara zake na taasisi zote inaingia na zoezi hilo linaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mgodi wa Kiwira ninaamini kwamba Mheshimiwa Mbunge jana ulisikiliza hotuba ya Waziri wa Madini alivyosifia ule mgodi mpya wa Kibulo ambao ulianzishwa mwezi Novemba, 2018 na ilipofika Machi, 2019 umeshatoa faida ya milioni 12.9 na kuilipa Serikali milioni 4.7 ni malipo mengine yanayofikia milioni 2.7. pia mgodi ule tayari umeshaleta kinu ambacho kinachakata mkaa unaouzwa katika nchi zifuatazo, Kenya Uganda, Rwanda, Burundi na China.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna sehemu ambazo lazima tuangalie mkataba huu ili tuweke maboresho hasa katika ajira lakini kipimo cha mikataba isiwe tu udhaifu wake lazima tutazame pia faida zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali kama haya tuanze kuyauliza je faida ni zipi na hasara ni zipi. Na nadhani katika mgodi wa Kiwira na migodi mingine ya makaa ya mawe tutaendelea kupata nishati mpya kabisa na imetathminiwa kimataifa kwamba mkaa unaotoka Tanzania na hasa unaotoka kule Liganga ni kati ya mikaa bora duniani ambayo haitosi gasi chafu kama mikaa mingine duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa kwamba tutatazama masuala ya ajira lakini nina hakika kutokana na faida kubwa tunayopata na mgodi wa Kiwira kama Waziri Biteko alivyotueleza jana tupo katika mwelekeo mzuri, ahsante. (Makofi)
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa majibu mazuri katika swali langu namba 396, lakini kutokana na mfumo dume tulionao katika nchi yetu ya Tanzania, hizo sheria kihalisia hazitekelezeki ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba elimu haijawafikia wananchi wetu na hususan akina mama wenzangu ndiyo wanaonyanyasika sana na sheria hizi, inapofika wakati wa mirathi mama anakosa kupata haki iliyokuwa sahihi. Ifahamike wazi ya kwamba Wizara inasema inapitia RITA, hiyo RITA huenda ikawa iko Dar es Salaam, lakini katika Mkoa wa Rukwa na Mikoa mingine RITA hiyo haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda kuuliza swali langu; je, Wizara au Serikali ipo tayari kuweka mkakati maalum wa kutoa mafunzo endelevu na hasa kwa kina mama kuelewa haki zao katika kuhakikisha kwamba wanatimiziwa haki zao? Kwa sababu wanahitaji uwakilishi wa sisi Wabunge ni dhahiri kusema ya kwamba…(Makofi)

SPIKA: Sasa swali.

MHE. SILAFU J. MAUFI: ...hata Wabunge elimu hiyo hawana; je, wako tayari Serikali kutoa mafunzo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wanawake hawa wajane wamekuwa ni wengi, wanaume wagane ni wachache kwa sababu mwanaume mgane ni wa dakika mbili baada ya muda anaweka mke mwingine ndani, kwa hiyo, anakuwa siyo mgane tena, lakini mjane anaendelea kuwa mjane. (Makofi)

Kwa kuwa wako wengi na wako katika makundi mbalimbali; je, Serikali inaona mkakati gani wa kuwawekea mpango wa kuwawezesha kimkopo ili kina mama hawa waweze kujendeleza na kuhudumia familia zao? Naomba majibu hayo. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, mimi naungana mkono na mama, kwa kweli katika utekelezaji wa sheria hizi hasa za mirathi akina mama wamekuwa siyo tu wanasumbuliwa, lakini wanabaguliwa. Tatizo hili linajionesha kadri tunavyokuwa mbali na miji hasa kwa akina mama walioko vijijini. Ni kweli kwamba katika mfumo dume, zile mali mara nyingi ziko chini ya mwanaume na wanawake inapokuja kwenye mirathi wanawekwa pembeni au ndugu wa yule aliyefariki mwanaume wanamnyanyasa yule mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaona umuhimu na ninakubaliana na wewe kwamba RITA ipewe jukumu kubwa la kuelimisha wananchi wote kwa ujumla, naomba mashirika mbalimbali ya akina mama tushirikiane katika kueneza elimu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nakubaliana kwamba mbali na elimu hizi za vipeperushi au machapisho kuna haja ya kuwa na mkakati maalum, mkakati ambao hata Wizara yangu, Majaji, Hakimu watakuwa wanaelezwa na kushirikiana na utawala kwa ujumla katika Mikoa na katika Wilaya. Pendekezo hili na jinsi lilivyoungawa mkono hapa nitalipa kipaumbele katika Wizara yangu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Spika, moja ya kesi ambayo inavuta hisia ya watu wengi ni kesi ya Mashehe wa Uamsho kutoka Zanzibar ambayo ilianza awamu iliyopita na kurithiwa na awamu hii. Sasa ni zaidi ya miaka saba na hata kuanza bado:-

(a) Je, ni sababu gani iliyosababisha ucheleweshaji huu mkubwa wa uoaji haki?

(b) Je, ni muda gani kesi iliyokosa ushahidi inatakiwa kufutwa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kesi anayoiuliza Mheshimiwa Mbunge bado ipo Mahakamani na hivyo kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Bunge, suala lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kujadiliwa Bungeni. Ni vyema tukasubiri vyombo husika vikafanya kazi yake na kutoa maamuzi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, zipo sababu zinazoweza kusababisha ucheleweshaji wa kukamilika upelelezi wa kesi ya jinai, nazo zinaweza kutokana na sababu zifuatazo:-

(i) Asili na namna kosa lilivyotendeka na wahusika wanaotuhumiwa kutenda kosa hilo iwapo wametenda kosa hilo wakiwa maeneo mbalimbali kwa maana ya kuwa hawakai eneo moja na wana mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.

(ii) Aina ya kosa husika, mathalani kesi yenye viashiria vya ugaidi, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, rushwa na kadhalika. Watu wanaofanya makosa ya aina hii wana mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.

(iii) Upelelezi kuhitaji upatikanaji wa taarifa, nyaraka na mashahidi nje na ndani ya nchi. Katika mazingira hayo upelelezi wake huchukua muda mrefu kukusanya ushahidi huo.

(iv) Mheshimiwa Spika, kesi ambayo haina ushahidi haiwezi kufikishwa Mahakamani. Hata hivyo, kutokana na uzito wa kosa la kesi iliyo katika hatua za upelelezi, kesi hiyo inaweza kukaa muda mrefu katika hatua hiyo kabla ya kuamua vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo changamoto za ukusanyaji wa ushahidi ndani na nje ya nchi wa kesi hii, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa sasa hivi taratibu za upelelezi wa kesi hii zinahitimishwa na hivi karibuni hatua za kusikilizwa kwa kesi hii zitaanza.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa uendeshaji wa mashauri yaliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bukombe kutokea Wilaya ya Mbogwe yanakuwa yakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mashahidi kutofika kutoa ushahidi kutokana na umbali, je, Serikali inaonaje ikianzisha Chamber Court Wilayani Mbogwe ili kukabiliana na changamoto hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Masumbwe na Ilolangulu na kuifanyia ukarabati Mahakama ya Mwanzo Mbogwe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama yalivyo majibu yangu kwenye swali la msingi, ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya 33 nchini umepangwa kukamilika ndani ya miezi sita, kuanzia mwezi Juni na kukamilika mwezi Disemba, 2020. Hivyo, naendelea kumwomba Mheshimiwa Mbunge kuwa na uvumilivu ili jengo hili likamilike ambalo litatatua changamoto alizozitaja kwenye swali lake la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania imejiwekea Mpango wa kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama kwa awamu. Aidha, Ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Masumbwe na Ilolangulu utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Ujenzi wa Majengo ya Mahakama 33 za Wilaya nchini utajumuisha Mahakama za Mwanzo katika jengo moja. Kwa mpango huo, Mahakama ya Mwanzo Mbogwe itakuwa ni sehemu ya Jengo la Mahakama ya Wilaya Mbogwe.