Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ally Mohamed Keissy (35 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ila na mimi nichangie hotuba ya Mtukufu Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Hotuba ya Rais kwanza kutoa muda wa kuchangia ni kama vile tunapoteza muda, ile hotuba haina matatizo. Mwelekeo wake ni mia kwa mia hakuna mtu anaweza kuipinga. Ya kukazia ni yale mambo aliyoyaeleza mwenyewe tuyafuate na yatekelezwe haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuunda Mahakama ya Mafisadi ifanywe kwa haraka sana. Pili, wakati wa bajeti hapa Bungeni wanakuja Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS
wanakuja kufanya nini? Hilo nalo liondoke. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kufuta Sherehe za Uhuru na ikiwezekana afute na Sherehe za Mwenge iwe hata mara baada ya miaka mitano. Tunabana matumizi, Mwenge kila mwaka unapita na tunapoteza pesa. Nimezungumza mimi Mwenge ukipita Wilayani
kwangu siku tatu kazi hakuna. Siku ya kwanza wanalaki Mwenge, Ofisi za Halmashauri zinafungwa. Siku ya pili wanapokea Mwenge kwa hiyo wanakesha kwenye Mwenge. Siku ya tatu Mwenge ulipopita wanalala wamechoka. Sasa ndugu zangu ni uharibifu, ni lazima twende
kama anavyosema kazi tu, hiyo ndiyo kazi tu. Hatuwezi kufanya sherehe wakati watoto wanalia, hawana madawati, dawa, viatu na chakula, tupunguze sherehe za ajabu ajabu.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilishangaa sherehe za Mapinduzi Zanzibar wanapakia watu elfu moja kutoka Pemba. Sasa kulisha chakula watu elfu moja ni gharama wakati wananchi hawana hela? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tupunguze Majimbo yamekuwa mengi, Wabunge wamekuwa wengi gharama za kuendesha Bunge ni kubwa Rais alizungumza hapa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Bunge linatumia gharama kubwa. Mabunge mengine ni watu ishirini na tano au watu kumi na tano. Ndugu zangu hatuendi namna hiyo. Twende na Bunge la kisasa, tumekalia kusema ma-DC wapungue, Wakuu wa Mikoa wapungue na Wabunge
tupungue kutokana na idadi ya ukubwa wa Majimbo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Jimbo kama la Kwela kwa Mheshimiwa Malocha ukubwa wake ni sawa na Rwanda, anapewa pesa za kuendesha Jimbo sawa na Mbunge mwenye watu elfu mbili. Hapa uhalali uko wapi? Lazima twende na sera ya „Hapa Kazi Tu‟ na kazi ianzie kwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wanaunda mpaka vikosi vya michezo wanakwenda na ndege ya Rais na kurudi na ndege ya Rais, huu ni ubadhirifu wa hali ya juu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani wakati wa bajeti wanatoka wataalam wa Nkansi wanakuja Dar es Salaam wanakaa wiki mbili, wao na madereva wao, gari sita, zinakuja Dar es Salaam eti bajeti. Karne ya 21, Namanyere ije ifanyiwe bajeti Dar es Salaam! Mkurugenzi na kundi lake atoke Bukoba aje Dar es Salaam, atoke Tarime aje Dar es Salaam, ndugu zangu hii haiwezekani, kuanzia sasa bajeti zifanyike Wilayani itumike mitandao tu. Haiwezekani Madereva na Wakurugenzi wa kila Wilaya kuja Dar es Salaam
kuchezea hela za Serikali wakati wananchi hawana maji, dawa wala barabara. Tunafanya sherehe kubwa kama nchi za Kiarabu, haiwezekani lazima tubanane, tule kwa jasho letu, hatuwezi kwenda kienyejienyeji. (Makofi/Kicheko)
Kisa kingine kuhusu madereva wa Serikali, madereva hawa wanapunjwa, madereva wa Mashirika ya Umma wanakuwa kama wako peponi madereva wa Serikali hawapati chochote. Hata akistaafu anapewa shilingi milioni mbili, itamtosha nini shilingi milioni mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wa marine service wa Lake Tanganyika, Lake Victoria, Lake Nyasa, hawaajiriwi, ni vibarua miaka yote. Hawana likizo, hawana insurance yaani wamekaakaa tu, wanaona bora wagongeshe meli watu wafe kwa sababu hawathaminiwi
kabisa. Kwanza hii marine service ni shirika la nani, ni la umma kweli? Lazima anayehusika alichunguze hili shirika la marine service. Nimekutana na wafanyakazi wa Liemba wanasema Mzee hatuna hata likizo, insurance, mishahara duni, wakistaafu hawapewi chochote wakati TRA, Shirika la Nyumba wao ni kama wako peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu NASACO amezungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja, turudishe NASACO i-control mali bandari. Leo kuanzia Bagamoyo mpaka Dar es Salaam bandari bubu nyingi. Wazanzibar ndiyo wamefanya pa kupitishia mali na kufanya huku Bara ndiyo soko. Tunaibiwa mchana mchana! Mali yote inatoka Zanzibar inapitia vichochoroni hawalipi ushuru. Zinaletwa mali za ajabu ajabu, sukari, mafuta na kila kitu. Wanastarehe kuinyonya Bara hawalipi ushuru, hiyo haikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke mikakati anayekamatwa mara moja mali yake itaifishwe hamna kwenda Mahakamani. Pia chombo kinachopakia mali ambayo hailipii ushuru kitaifishwe, watashika adabu. Wote ambao wanahisiwa kwamba wanashirikiana na
wafanyabiashara kutuibia, cha kwanza kabisa mali zao zinyang‟anywe kabla ya kupelekwa mahakamani. Apewe form aulizwe hii mali umeipataje, akishindwa kujieleza anyang‟anywe kabla hajaenda Mahakamani. Akienda Mahakamani, Mzee mlango chini anapita anafungwa
miezi sita, anabakia anachezea ile mali. Kwanza mali yake inyanganywe mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mambo ya kuendelea kuleana yaishe sasa.
Nimezungumza sana habari ya Namanyere, miradi ya maji wanahamishwa Wakurugenzi, Maafisa Ugavi na Wahandisi wa Maji, naomba majibu yakatumbuliwe Wilayani Namanyere kuna watu wameiba pesa. Kule kwa vile tuko karibu na DRC-Congo wafanya kama hamna
Serikali, wanafanya mambo wanavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza hapa Bungeni, mtu anaandika gharama ya gari Namanyere Dar es Salaam gari tani kumi shilingi milioni kumi na mbili badala ya shilingi milioni tatu. Anaandika mabomba yameingia ndani gari tisini na nane milioni wakati bomba
hakuna yaani gari hewa, mabomba hakuna, Serikali imelala usingizi. Tunataka tutumbue majipu tupeni idhini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya mbolea haya, mbolea hazifiki kwa wakulima wanaandika hewa tupu mpaka majina ya marehemu wanaandika. Hatuwezi kukubali safari hii, namwambia Waziri wa Kilimo, Kamanda wangu Mwigulu, anipe kibali nitembee kijiji kwa kijiji,
nikague mimi mwenyewe simwamini DC, simwamini OCD, siiamini TAKUKURU maana ndiyo wamefanya njia za miradi yao. Nitatembea mwenyewe, Mheshimiwa Mwigulu nipe kibali nikakague kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba kama mbolea au mbegu imefika. Serikali ya CCM inatukanwa ni kwa sababu ya Watendaji hawa, wamefanya miradi yao binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo, kuanzia sasa bajeti ijayo hakuna kuja cha Mkuu wa Mkoa, hakuna kuja cha RAS, hakuna bajeti za Wilaya kupangiwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi. Kwanza mimi natoa pongezi sana kwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wote. Kusema kweli tunachotaka sasa ni Serikali kuipa fedha zote Wizara hii ili ikatekeleze mipango kama ilivyo kwenye bajeti yao. Mimi katika mkoa wangu wa Rukwa hasa Wilaya ya Nkasi nimeshukuru sana, miaka sita barabara yetu toka Sumbawanga - Mpanda ilikuwa haijakamilika kwa bajeti hii naona barabara Disemba itakuwa lami tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilikuwa napiga kelele sana kuhusu shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kwenda kukamilisha Bandari ya Kipili. Leo naona kwenye bajeti kuna pesa ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza barabara mpaka Bandari ya Kipili. Naipongeza sana Serikali na Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe masikitiko yangu makubwa, alipokuwa hapa ndani, leo ni Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi, aliniahidi barabara ya kutoka Kirando - Kazovu - Korongwe na shahidi ni Alhaji Iyombe alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na alikubali kunisaidia. Wakati wa kampeni zake tena alipokuwa Namanyere aliniahidi hii barabara atanisaidia. Vilevile aliahidi kwamba Namanyere Mjini atanipa pesa za kilometa tatu za barabara ya lami, lakini sikuona humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu usafiri Lake Tanganyika. Awamu ya Nne tuliahidiwa meli mbili, Awamu ya Tano hakuna cha meli, ni utengenezaji wa Liemba kwa shilingi bilioni 5.6. Ndugu zangu, tuliahidiwa meli moja leo hamna meli ni matengenezo, tuna meli kule MV Mwongozo haitajwi kabisa, ilikuwa pacha pamoja na ile iliyozama kule Bukoba, zilitengenezwa siku moja…
MBUNGE FULANI: MV Bukoba.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Ndiyo MV Bukoba, lakini sisi ile meli tunayo mpaka sasa, haina matengenezo haina chochote imekaa pale Kigoma kazi yake kukodishwa na wafanyabiashara kidogo kidogo haijulikani inafanya kazi gani. Tunaomba Serikali kama haina pesa za kutosha ya kununua meli mpya iifanyie ukarabati wa hali ya juu MV Mwongozo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kibaya zaidi ni kuhusu wafanyakazi wa Liemba, hii Marine Service inatesa watumishi. Mpaka leo mshahara wa mwezi wa nne wafanyakazi wa Liemba hawajapata, hawana bima ya afya, hawana hela ya likizo hata waliostaafu hawajalipwa mafao yao mpaka leo. Hata meli ya mtu binafsi ungesikia kelele, hii siyo meli siyo chochote na wakati wowote inaweza kutokea ajali maana hata engine zake zinazimika mara kwa mara ndani ya Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru sana Serikali, nilipiga kelele tokea bajeti ya kwanza kuhusu Bandari ndogo ya Kabwe lakini kwenye bajeti hii nimeona kwamba itaanza kutengenezwa mwezi Julai. Naomba Mheshimiwa Waziri hicho kipindi cha mwezi Julai itakuwa Bunge hapa hakuna na mimi nitakuwa Kabwe, nataka nihakikishe huo mwezi Julai bandari ya Kabwe imeanza kutengenezwa kama ulivyoahidi kwenye bajeti yako. Maana bajeti ya mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi bilioni moja kwenye bajeti kwa ajili ya Bandari ndogo ya Kabwe lakini sikuona chochote mnasema tu vifaa vimeshawasili Dar es Salaam. Mmesema bandari ya Kabwe na Lagosa zitaanza kujengwa mwezi Julai na kipindi hicho Mheshimiwa Waziri tutakuwa huko, nitakuwa kwenye jimbo langu nihakikishe bandari ya Kabwe imeanza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Serikali ni yetu wote, kuna mikoa hapa inapendelewa siyo uongo na ni mikoa ambayo iko mbele ukienda utafikiri uko Durban au uko Johannesburg na sisi wengine hata barabara za vumbi hatuna. Kuna watu wanadai viwanja vya ndege, kuna watu wanadai barabara za lami, sisi tunataka barabara za vumbi. Katika hayo maombi 3,000 watu walioomba kuhamisha barabara kutoka halmashauri kwenda TANROADS, lazima tufikirie mikoa mingapi ina lami, mingapi ina barabara za TANROADS ili tuinue mikoa ambayo iko nyuma kabisa. Kuna mikoa mingine iko kama peponi, leo unakuja kusema hapa maneno ya ajabu ajabu sijui kisungura na kadhalika, tuangalie mikoa hii.
Ndugu zangu, nchi hii tumetembea kila kona, labda ninyi hamjakwenda mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma mkaangalia jinsi tulivyokuwa nyuma katika suala la barabara…
MBUNGE FULANI: Na Simiyu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Nendeni Simiyu, ninyi mnataka mpaka lami ziwafikie kwenye majumba yenu binafsi, hilo Mheshimiwa Waziri hatutalikubali. Ni lazima tuangalie upya mkoa upi una kilometa nyingi za lami, una kilometa nyingi za TANROADS ili na sisi mikoa mingine bajeti iende kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wilaya nyingine zina lami mpaka kwenye mitaa, miji yao ina lami makao makuu ya Wilaya…
MBUNGE FULANI: Sema.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Lakini Wilaya nyingine hazina lami hata kilometa moja. Ni kweli, mwenzangu ametoka kuzungumzia hapa, utashangaa, unabandua lami unabandika lami wakati zina mashimo, sisi wengine za vumbi hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa, toka Kirando kwenda Kazovu kuna vijiji zaidi ya sita mpaka Korongwe, tangu uhuru hawajaona hata bajaji. Wananchi wanapata taabu, Ziwa Tanganyika likichafuka mitumbwi inazama, akina mama wanakufa hawana njia nyingine ya usafiri ni kwa mguu au kwa mitumbwi, Lake Tanganyika wimbi lake ni la ajabu utashangaa mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri aachane na wanaoomba viwanja vya ndege ndugu zangu hata abiria hakuna, wanapanda Wabunge, nilizungumze hapa, wanapanda Wabunge baada ya Ubunge kuisha hata tiketi hawakati, leo wanaomba viwanja vya ndege kila Wilaya atapanda nani. Akina mama na bibi zetu wanapanda magari, wanapanda treni, leo mnakwenda kuchukua mabilioni ya hela, tuchukue mfano kidogo wa uwanja wa ndege wa Mpanda nani anautumia? Tuseme ukweli nani anautumia uwanja wa ndege ya Mpanda, kuna ndege ya abiria inayokwenda Mpanda? Nimekwenda Tabora na ndege hakuna abiria anayepanda wala anayeshuka, Tabora hapo ndiyo mji mkubwa, leo unaomba kiwanja wakati abiria hakuna. Watu wa Tabora wanataka reli, watu wa Mpanda wanataka reli siyo viwanja vya ndege. Tusiwe tunadanganyana hapa, tugawane sawa hiyo keki. Mnabandua lami, mnabandika lami wengine hawajaona hata lami, ndugu zangu tunakwenda wapi, tuoneane huruma. Wengine nchi hii mpaka leo wanatembea kwa mguu hawana barabara, wewe unaomba kiwanja cha ndege, ndugu zangu, huoni hata aibu! Unakuja kuzungumza uwanja wa ndege mbele ya Bunge, mbele ya nchi hii wakati wenzako hawana barabara!
TAARIFA...
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi ninaosema reli ndiyo itakayotuletea uchumi, siyo ndege. Hayo makontena ya vifaa vya viwanda itapakia ndege? Wewe mwenyewe umelalamika ndege wanatoza shilingi 200,000 sanduku, ndege gani si unadanganya Bunge hapa, hakuna kitu kama hicho. FastJet bei yake ni rahisi kuliko ndege zote hapa leo unataka kuwapakazia FastJet begi shilingi 400,000 begi gani hilo jeneza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari, bandari yetu inatuletea msongamano mkubwa Dar es Salaam inatumiwa na nchi nyingi. Tuliomba bandari ya nchi kavu na kuokoa msongamano, reli ichukue mizigo mpaka Kibaha kule mbali au Chalinze ili magari yote ya kutoka nchi jirani yabebe mzigo kwenda nje. (Makofi)
Kwa kufanya hivyo, tutaondoa msongamano katika Jiji letu la Dar es Salaam. Hizi flyovers mnazoweka, sijui mnapanda mabasi yaendayo kasi haitasaidia kama bado mizigo inakwenda kuchukuliwa bandarini na magari makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mafuta lazima kuwe na mpango ili bomba la mafuta liende mbali kidogo na Dar es Salaam ili magari yote yakachukulie huko mafuta kwenda nchi za nje. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Sawa sawa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Bila kufanya hivyo msongamano utaendelea kuwa pale, magari kutoka bandari kupitia Mandela road ni foleni ya ajabu, saa tatu mpaka nne ni foleni, ndugu zangu tunapoteza muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri fanya kazi yako, wewe ni Waziri mzuri unafanya kazi, usitishwe na mtu yeyote, endelea kusaidia sehemu ambazo hazina barabara, hazina mawasiliano, lakini kusema mimi nataka uwanja wa ndege achana na viwanja vya ndege, achana kabisa havina maendeleo kwa nchi yetu bado changa vilivyopo vinatosha. Tuendelee na viwanja vya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Kigoma pembezoni kule vinatosha lakini vingine vya katikati ndugu zangu ni kupoteza wakati hakuna abiria, nimefanya utafiti hakuna abiria. Sisi wa kule Sumbawanga kiwanja cha Mbeya kinatosha sana, tusidanganye. Tunakwenda na ndege FastJet asubuhi abiria hawajahi, leo unataka kiwanja kijengwe Sumbawanga, Mpanda, Mbozi, Kibaha, ndugu zangu hela zitatoka wapi? Tuendelee kujenga barabara na reli ili nchi yetu itoke katika uchumi huu uende uchumi wa mbele, tusidanganyane! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani unakuwa Mbunge hapa unasema Morogoro wanataka kiwanja cha ndege, Tabora uwanja wa ndege, dai gauge Tabora reli itakusaidia.
Tarime uwanja wa ndege, utapanda wewe peke yako Mbunge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri ahadi ya Rais alipokuwa Waziri aliniahidi hapa akatuma na wataalam kwenda kukagua barabara kilometa 35 tu, aliniahidi atanisaidia alipokuwa Waziri na alipokuwa Rais, nakuomba itekelezwe. Shahidi ni Mheshimiwa Mzee Lukuvi alikuwa anaambatana naye na yuko humu aliahidi kujenga hiyo barabara. Kwa hiyo, naomba hiyo barabara tafuta hela popote ikatengenezwe kusaidia watu wa Kazovu na Korongwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ujumbe wangu umefika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, kwanza natoa shukrani za dhati kwa kunipa nafasi. Namshukuru sana Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani kuwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wote.
Ndugu zangu, hili Bunge tusifanye vichekesho au viigezo, tukumbuke Bunge la Tisa, sikuwa Mbunge, nilikuwa naangalia kwenye TV. Hapa Bungeni alikuwa rafiki yangu, kipenzi wangu, Waziri Mkuu anaitwa Edward Ngoyai Lowassa. Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa alijiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, hapa Bungeni. Cha ajabu jamaa wa pili hao hao wamemchukua kumpa tiketi agombee Urais awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, wanaona ajabu wakati si kweli kama Mheshimiwa Sospeter Muhongo alihusika na Escrow Account ila alisingiziwa kwa ufisadi wenu ninyi baadhi ya Wabunge, tunalijua hilo, lakini Mheshimiwa Edward Lowassa hapa alitolewa, alijiuzulu, lakini ninyi mkamkumbatia mkatembeza nchi nzima, je angekuwa Rais nchi hii ingekuaje? Ndugu zangu mnasahau matapishi yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sipendi kuwakashifu ninyi rafiki zangu, lakini mnashika pabaya lazima tuwaambie ukweli, mnakuwa na akili ya kusahau kama vile kuku wa kizungu au samaki anakwenda kunasa kwenye nyavu. Leo siku hata tano haijapita unasahau unataka ripoti ya kumkashifu Mheshimiwa Sospeter Muhongo na Magufuli kumchagua kuwa Waziri wa Nishati na Madini, akupe wewe kuwa Waziri, wakati ninyi hapa mmemtembeza Lowassa nchi nzima na Bunge hilihili, nchi nzima walifahamu kwamba amejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, sasa si ajabu hii? Mnasahau…
TAARIFA...
MHE. ALLY K. MOHAMED: Hiyo ya Rais Mwinyi usizungumze, Rais Mwinyi alikuwa amelala nyumbani kwake…
…kule Magereza Shinyanga ni tofauti kabisa, wala hakuwa fisadi kama unavyofikiria wewe. Unamsingizia, Mwinyi hakuwa fisadi, Mwinyi alijiuzulu kutokana na kashfa ya Magereza Shinyanga, tofauti kabisa na rafiki yangu. Achana na ninyi, mlimtembeza mtu mnamjua kabisa mtu kajiuzulu kwa sababu ya rushwa, mkamtembeza nchi nzima, mtacheka wenyewe. Nimeshawapasha! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Wizara ya Nishati na Madini, hasa REA, imesaidia kabisa katika vijiji vyetu kupata umeme. Ninachoiomba Serikali, iwapatie pesa ya miaka mitatu ya nyuma, REA walikuwa hawajapata pesa, wanadai karibu bilioni 272 maana yake Wakandarasi wako vijijini wanadai hizo pesa mpaka sasa. Haiwezekani hizi hela za mwaka huu, bajeti ya mwaka huu, bilioni zaidi ya 500 waanze kuzimegua ili kuwalipa Wakandarasi ambao wapo kazini, lazima tuhakikishe kabisa kwamba wanapewa hela zao za miaka mitatu ya nyuma, bilioni 272 Wakandarasi wakalipwe ili awamu ya pili ikamilike bila matatizo yoyote na hizi Milioni 540 zifanye kazi kwa vijiji vyote katika nchi hii kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nataka kuzungumzia alipoishia jirani yangu Mheshimiwa Silinde, kuhusu vinasaba. Vinasaba vimepitwa na wakati, vinasaba tumezungumza mara nyingi hapa, tuliruhusu vinasaba kwa sababu ya tofauti ya bei ya mafuta. Leo bei ya mafuta inalingana nchi nzima, nani atachakachua? Tuliamua hapa mafuta ya taa yapande bei ili wasiwe wanachakachua na mafuta ya taa kweli yameteremka hayaagizwi tena nchini kutokana na kwamba walikuwa wanachakachua kwa sababu bei ya mafuta ya taa, bei ya diesel vinalinganalingana.
Mheshimiwa Spika, tunaona uchungu, yule wa vinasaba kutokana na mafuta yanayoingia nchini kwa mwaka mzima zaidi ya lita bilioni mbili, anachukua zaidi ya bilioni tisa kwenye gharama ya vinasaba. Huyu wa vinasaba faida yake ni bilioni 14. Usimamizi wa EWURA unachukua zaidi ya bilioni 13.9, wakati ukaguzi wa mafuta TBS yenyewe inachukua bilioni 2.8 kwa ajili ya kudhibiti mafuta kama yana ubora. Sasa vinasaba vina faida gani?
Mheshimiwa Spika, halafu cha ajabu, EWURA hao hao wako chini ya Idara ya Maji wakati vipato vyao vyote vinachukuliwa katika Wizara ya Nishati na Madini. Wenyewe ukiwauliza hawahusiki kabisa moja kwa moja na Wizara ya Nishati na Madini, lakini mapato yao, kila kitu wanachukua kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, nilizungumza Bunge lililopita kabla halijaahirishwa. Mpaka hawa jamaa wakawa wanatumia pesa kwenda gym, wanalipa kila mfanyakazi wa EWURA Dola 400, akienda gym asiende gym. Wanajipangia mishahara wanavyotaka, wananyanyasa watu wanavyotaka. Hivi vinasaba vimepitwa na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu TRA kukagua magari ya mafuta, TRA wana vituo njiani (checkpoints) tatu au nne, lazima magari yapite, TRA ikague mafuta kama yameteremshwa njiani au hayajateremshwa njiani. Kama watumishi wa TRA ni wabovu wanagongesha mihuri, je hao EWURA ndiyo watakuwa waaminifu kama malaika? Ni kuongeza mzigo kwa walipakodi kupandisha bei ya mafuta bila sababu. Nashauri hizi pesa za EWURA ziende REA moja kwa moja kutatua matatizo ya umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka mzima pamoja na usimamizi, EWURA wanachukua shilingi 18 na senti 85 kutoka kwenye gharama za vinasaba, halafu wanachukua shilingi sita kwa ajili ya usimamizi, jumla bilioni 42 . Hizi pesa zikienda REA kule zitasaidia kutatua matatizo ya umeme vijijini, kuwalipa Wakandarasi. Kwa hiyo, naomba Serikali irudie upya hivi vinasaba, iangalie kama vina umuhimu ama havina umuhimu. TRA ndio wasimamizi wa mafuta kama yanavuka mipaka au hayavuki mipaka.
Ndugu zangu na uchakachuaji ulipitwa na wakati, tulikuwa tunachakachua kwa sababu mafuta ya taa yalikuwa chini kabisa, mia tano, mia sita, tumeongeza ile bei ili wananchi wapate umeme vijijini, sasa nashangaa bado wanaendelea na vinasaba ili kuumiza wananchi wetu na havina faida wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, hawa jamaa wa REA tuwape pesa kama inavyotakiwa. Hizi pesa ziende moja kwa moja REA zisipitie Hazina. Zikipitia Hazina zinakuwa na vigezo, miaka mitatu mfululizo, REA hawakupata hela kama inavyopangwa, miaka mitatu nimepiga hesabu hapa ni milioni 272, REA hawajapata hela. Wakandarasi wanadai kule vijijini, wanadai tozo kule vijijini, lakini sababu pesa ziko Hazina, hizi pesa zimeshatoka kabisa sasa kwa nini zisiende moja kwa moja REA ili REA wafanye kazi na tuwawajibishe kama hela hawajawapa wakandarasi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naishauri Serikali, kwanza naishukuru sana kupunguza tozo ya umeme ili wananchi wetu wapate, lakini vilevile ndugu zangu wa mijini wamekaa wanaiba umeme, tatizo kubwa. Ni tatizo kubwa, haiwezekani mtu ana AC tatu, ana kiwanda hawafuatilii, Serikali kama wanashindwa REA peke yake kufuatilia TANESCO watafute JKT wapite nyumba kwa nyumba hasa mijini. Watu wa mijini wamekuwa wezi wakubwa wa umeme, wanaiba umeme mchana kutwa, Manzese wanasaga usiku wanaiba umeme, viwanda vidogovidogo wanaiba umeme, wanaoumia ni watu wa kijijini ambao hawana utaalam wa kuiba umeme.
Mheshimiwa Spika, mpaka baadhi ya watu wakubwa Serikalini wanaiba umeme, mashule makubwa makubwa yanaiba umeme, mahoteli yanaiba umeme. Ndugu zangu hatuwezi kufika, tuibe umeme, tuibe na maji, halafu hapa tunakuja tunalalamika tunataka kila kitu wakati sisi wote tunasaidia wizi.
Mheshimiwa Spika, unakuta Mbunge anamwona mtu anaiba umeme, hatoi ripoti, bado anamsaidia, tuna kazi ya kuilaumu Serikali, hatuipigi vita kwa njia ya namna hiyo, tumsaidie Rais Magufuli kutumbua majipu hata katika wizi wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mkurugenzi wa TANESCO, Mkurugenzi wa REA, wanafanya kazi, inabidi tuwaunge mkono. Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo usisikie maneno ya majungu, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya Public Account Committee, ni uzushi yule James Rugemalila alikuwa anadaiwa kodi, ndipo tuliamua alipe kodi; hana kashfa yoyote, kashfa kama mnayo nyie kwa majungu yenu hatoki na anakaa pale kwa niaba ya Serikali ya CCM. Ataendelea kufanya kazi na katika Mawaziri wachapakazi hakuna kama Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, hana siasa. Mnataka kwenda kwa vigezo vya rushwa, huyu hali rushwa, wala kashfa ya ESCROW Account hamkumwona hata kapewa kiroba cha hela waliopewa hela walitajwa humu yeye hahusiki.
Mnamsakama bure hamfanyi lolote, aliyemchagua Rais Magufuli kwa niaba ya Serikali ya CCM, kwa hiyo hawezi kubanduka atachapa kazi. Ngojeni na ninyi wananchi watawachagua na kutokana na uongo wenu wameshawagundua hamuwezi. Mmeshapigika huko nje mnaleta fitina za uongo hapa, hamkubaliki kwa speed ya Magufuli inayokwenda kama umeme. Kwa hiyo, Rais Magufuli speed yake hamuipati, shemeji zangu nawaambia ukweli, mliboronga kuchagua mtu aliyekataliwa na Bunge, akajiuzulu, mkamtembeza nchi nzima, sasa safari hii ndugu zangu kaeni chonjo mtapungua siku hadi siku. Ahsanteni sana. (Makofi)
SPIKA: Mlichokoza wenyewe jamani, jamani taratibu tufike au siyo. Haya, ahsante sana Mheshimiwa Ally Keissy hayo ndiyo mawazo yake, msimlaumu wala msimshutumu. Mheshimiwa Ahmed Shabiby mchangiaji anayefuata na Mheshimiwa Stephen Masele ajiandae.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi katika kuongelea Wizara hii muhimu sana katika nchi yetu. Bila Wizara hii kuwepo vyanzo vya maji vyote vingekauka, kama Wizara hii haikuwepo hakuna miti katika nchi hii, ingekuwa jangwa. Kusema kweli lazima tufuate sheria. Leo kuna maziwa kwenye bahari, Lake Tanganiyika, Lake Nyasa, Lake Rukwa, Lake Victoria na mwambao wa bahari, lakini nyavu haramu zinakamatwa zinachomwa hatusikii kelele. Kwa sababu wanakwenda kinyume na sheria. Watu wanaojenga kwenye road reserve wanavunjiwa maghorofa yao, hatusikii kelele. Lakini kelele ng‟ombe anapoingia kwenye Game Reserve au National Park tunasikia kelele, kwa nini tusikie kelele? Tufuate sheria, kila kitu kina mpaka wake, haiwezekani mimi leo niingie kwenye nyumba ya mtu bila hodi. Ile ni sheria, ni nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu na ubaya wao, lakini tangu enzi za zamani walikuwa wanaita mashamba ya bibi, ilikuwa mwiko hata kuchuma jani. Leo tunakwenda kuchoma pori, tunafanya tunavyotaka na kila kitu, lazima tufuate sheria ndugu zangu. Morogoro tulikuwa tunaita Morogoro maji yanatiririka, leo Morogoro maji yako wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri, kabla ya Bunge kuisha nipe magari kwenda kwenye doria kule Lwafi Game Reserve na Rukwa, kupambana na waingiza mifugo mle ndani, wanatuharibia mbuga zetu. Nilizungumza na Mheshimiwa Nyalandu hapa akiwa Waziri, alikuwa tayari kunipa gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaingiza ng‟ombe kule, tuna mbuga kule, game reseve ya kilometa 6,800 lakini hakuna gari, majangili wanaua tembo hovyo, leo hata mavi ya tembo hatuyaoni. Wanachoma pori hovyo, ng‟ombe wamekuwa ndiyo nyati badala ya nyati mle ndani, hatuwezi kukubali, sheria zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kugeuza jangwa ndugu zangu, nchi itakwenda wapi? Tutapata wapi maji ya kunywa! Bora mimi Lake Tanganyika inaweza ikawa na maji mengi, ninyi mtakwenda wapi, Dodoma itakwenda wapi? Acheni kuwa na jazba, fugeni ng‟ombe kama Denmark, Denmark wana ng‟ombe chache lakini wanauza maziwa nchi nzima. Leo mnafuga ng‟ombe, ng‟ombe moja ana kilo 70 unasema una ng‟ombe! Hatuwezi kukubali kuharibu mazingira kwa ajili ya wafugaji, hatutakubali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu ni asilimia 75, wewe umezungumza wafugaji milioni mbili na wakulima wako wangapi nchi hii? Leo hawana sehemu ya kulima, watakosa maji wakulima wetu, tutapata wapi chakula tukikosa mvua, hatuna uwezo wa kumwagilia nchi nzima, kwa hiyo, ndugu zangu lazima tufuate sheria. Game reserves zipo kwa sheria national parks zipo kwa sheria na mfugaji yupo kwa sheria na mkulima yupo kwa sheria, hatukubali mkulima kwenda kulima kwenye game reserve wala mfugaji kwenda kwenye reserves.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoma nyavu hapa kila siku mnasikia, wavuvi haramu kule Ziwa Tanganyika. Mimi mwenyewe shahidi, nilishaenda kushuhudia wanachoma nyavu za milioni saba, milioni nane, Mwanza wanachoma nyavu, Bukoba wanachoma nyavu, Pangani wanachoma nyavu, huku kote wanachoma nyavu, hatusikii kelele, kwa sababu wanavunja sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zote zinavunjwa, juzi wamevunja nyumba Dar es Salaam kwenye njia za maji, nani anapiga kelele hapa, kwa sababu wamejenga kinyume na sheria.
Wewe unaingiza ng‟ombe wako kwa nguvu zako utegemee pesa zako na wakulima wetu wanapata shida, wanakwenda kuhonga Mahakimu, hakuna kesi ya mkulima ilishida, mimi nina ushahidi. Hakuna kesi ya mkulima na mfugaji imekwenda mahakamani mkulima akashinda, hakuna! Hatuwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwangu kule kuna ng‟ombe 200,000 wakati tulikuwa na ng‟ombe labda 200 au 300. Wafipa ng‟ombe wao ni wa kulimia. Mfipa kabisa mfugaji ng‟ombe 50, leo kuna ng‟ombe 200,000. Na mimi nimeshazungumza, walipe kodi. Hatuwezi kuwaachia namna hii walipe kodi, wana uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi inalalamika haina hela MCC imetufinya misaada, wakati kuna mahali wanasema wana ng‟ombe wengi, hawalipi kodi hawa. Vyanzo vingi vya hela hapa mnaviacha, ndiyo maana wanakuja kutambukatambuka hapa. Sisi hatukuona siku ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mkulima hapa nje, Wizara hii tumeona wafugaji wamejazana hapa. Ndugu zangu tukiachia watachunga ng‟ombe mpaka Ikulu. Hatuwezi, twende kwa sheria. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kule kwangu kuna matatizo, mamba ndiyo wametuzidia. Watu wangu waliumwa na mamba, tumepiga kelele walipwe hiyo fidia maana yake huwezi kulipa maiti aliyekufa, thamani yake ni kubwa sana. Lakini sheria inasema mtu akiliwa na mamba, akiliwa na tembo, alipwe. Kwa hiyo nafuata taratibu, nina watu wangu kule wameliwa na mamba Lake Tanganyika, walipwe fedha zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, lazima tuheshimu sheria nchi hii. Ni kama wewe una nyumba yako mimi nikuingilie mle ndani, ninywe chai bila idhini yako, ninywe maji bila idhini yako utanipeleka Polisi. Ni kama Katavi Game Reserve, Luafi Game Reserve, hizi zote zina sheria na sheria zimetungwa hapa Bungeni na nyingine tangu Mkoloni ametunga sheria hizi, tukiachia hivi wenyewe ndugu zangu ni mwaka mmoja hakuna mnyama nchi hii, kuna watu wanachukua national parks ndugu zangu, ajabu kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila national park, bila game reserve ndugu zangu mvua hakuna, vyanzo vya maji vitakwisha. Mnaweza ninyi, mna hela Wabunge mnanunua maji ya chupa, watu wetu hawana hela ya kununua maji. Hatuna hela ya kununua maji, ni haya maji ya mvua ndiyo yanakwenda ardhini tunachimba visima. Leo miaka mitatu ikiwa hakuna maji hapa, mvua hakuna, tutakufa na ng‟ombe wenu watakufa na mbuzi watakufa na kondoo watakufa na nguruwe vilevile, mtabaki na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaambia ndugu zangu, hakuna kwenda kinyume cha sheria, sheria ni msumeno, mtu yeyote anavamia ni kama vile wavuvi wanavua haramu, lazima wakamatwe wachomewe nyavu zao ili samaki waendelee kuishi. Samaki watakwisha, kwa hiyo tunaomba sheria itekelezwe. Hatuwezi kubembelezana, hatuwezi kutishana humu ndani, hakuna kumtishia mtu humu ndani. Mheshimiwa Maghembe amekuta sheria ipo. Nawapongeza TANAPA kwa kutupa madawati, kafanyeni kazi. Serikali yetu ina meno ya tembo yamejazana, msifanye kama Kenya. Uzeni, tupate pesa tununue magari na silaha kupambana na majangili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupambane na haya majangili kwa hali yoyote. Vijana wetu hawa ma-game rangers wakienda mule ndani wanapambana kwa bunduki na yale majangali, akimuwahi anamuua. Kwa hiyo na ninyi wafanyakazi wa Serikali ma-game rangers, mtu unamkuta game reserves, national parks, mpige risasi afe! Kwa sababu ukimuachia atakuua wewe. Kaenda kufanya nini mule ndani, kwa idhini ya nani! Kaenda mfano, Katavi National Park, kufanya nini mle ndani kama siyo jangili, nani kampa idhini? Ni kumtandika risasi tu maana yake ukichelewa kumpiga risasi anakupiga wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni watu wabaya, tumewakamata Namanyere na bunduki nakuambia Mheshimiwa Maghembe, lakini wanaachiwa polisi. Nimekuletea ushahidi, wamekamatwa majangili na nyama ya tembo kilo 200 imepakiwa ndani ya gari linaitwa Noah, lakini siku mbili tatu wanaachiwa. Wanakamatwa na bunduki, siku mbili tatu wanaachiwa mpaka vijana wa TANAPA wanachoka! Kesi zao zinaishia hovyo hovyo tu. Nimekuletea sijapata majibu mpaka leo, nina wiki ya tatu, kwa ushahidi kabisa kwamba majangili wamekamatwa kule Nkasi lakini wanaachiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Rais Magufuli anasema, unamkamata mtu red-handed na jino la tembo, unamkamata na bunduki, na nyama ya tembo, unampeleka mahakamani anashinda kesi, red-handed! Hapa kuna nini, rushwa kubwa, siyo ndogo. Hawa dawa yao ni kule wanapokamatwa maana yake ukimpeleka mahakamani anakushinda, ni kumtandika risasi mambo yaishe huko huko mbugani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuchezewa, kuharibu mapori yetu kwa ajili ya faida ya ninyi kizazi cha leo, kumbukeni kizazi kinachokuja. Je, miaka ya nyuma wangekuwa wanaharibu kama mnavyoharibu ninyi mikaa, kuni, ng‟ombe mle ndani, tungeishi hapa? Kumbukeni na ninyi bado mnaendelea kusihi nchi hii. Mwenyezi Mungu kawaambia dunia karibu miaka miwili iiishe? Mna ahadi ya Mwenyezi Mungu dunia karibu iishe? Kwa hiyo, kuna vizazi na vizazi vinavyokuja na hii ni mali yetu wote, lazima tuitunze na tufuate sheria, sheria ni msumeno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi jioni ya leo.
Waheshimiwa ndugu zangu Wabunge, ukiona mtu kapigika ujue amekwisha. Ndugu zangu wameshaona, wameshafanya utafiti huko nje, hali zao ni mbaya, speed ya Magufuli inawatisha, walipania mwaka huu ndiyo waingie Ikulu, Ikulu ndiyo hawataiona tena kwa speed ya Magufuli. Sasa hawa jamaa ni wa kuonea huruma tu wameshapigika vibaya, hawajiwezi…
Mheshimiwa Magufuli anasifiwa dunia nzima. Kwa ushahidi Nigeria nimesikia Nigeria wanamsifu, Kenya wanamsifu, Uarabuni wanamsifu, Ulaya wanamsifu, hapa wanakaa wanampiga vijembe!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo Katiba amevunja Katiba gani? Katiba kuwasaidia mafisadi kutuibia pesa? Mimi nilizungumza hapa Bungeni, mafisadi wauwawe mapema na makaburi yao yawekwe minyororo, nilimwambia Mheshimiwa Magufuli…
Kwanza hawa jamaa hakuna haja ya Kuwapeleka Mahakamani. Haiwezekani mtu ana nyumba 70 bado unampeleka mahakamani, alipata wapi? Wewe tuchukue watu wa vijiweni, nenda pale Nyerere Square wako watu wanahangaika pale. Wako tayari kufungwa miaka miwili miwili wapewe milioni 100 wako tayari, itakuwa fisadi unamfunga miezi sita au unampa kifagio anafagia Sinza akitoka anakula mabilioni ya shilingi ya hela? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wameshaona wamepigika, speed ya Magafuli inawatisha, hawana chao, iliyobaki jiungeni na CCM mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kugusia habari ya mapato ya Serikali, mapato ya Serikali yanavyopotea katika nchi hii.MHE. ALLY K. Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kugusia habari ya mapato ya Serikali, mapato ya Serikali yanavyopotea katika nchi hii.
Ninyi tulieni mmeshakwisha, speed ya Magufuli inawatisha, hamna leo, hamna lolote, mnajiona mmefanya utafiti huko nje hamuungwi mkono na wananchi wote. Mlituambia hapa hapa Bungeni kwamba tukapimwe akili zetu kama tunamuunga Mheshimiwa Lowassa!
Je, ninyi mlipimwa akili zenu wakati mnamuunga Lowassa? Mlifanya utafiti, mliandika na vitabu, mkapita nchi nzima kumwambia Lowassa ni fisadi, je, mmepokeaje huyo fisadi mwenzenu? Sasa mmegeuka ninyi ndiyo mmekuwa mafisadi, CCM imekuwa safi, tulieni.
Magufuli speed anayokwenda nayo ni hiyo hiyo hamna kupunguza, hamna kupunguza aendelee zaidi ya mara mbili au mara tatu, hamna chenu. Tumepewa wajibu wa kuiongoza Serikali kwa miaka mitano na mmeona speed inavyokwenda mkajua mwaka 2020 hamtapata kura, hamkutegemea speed hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia vinasaba. EWURA waliingia mkataba vinasaba na shirika moja bila kupitia tenda, huyo jamaa anajichukulia kila mwezi shilingi bilioni 9.8, tulieni ninyi vimeshawauma hivi hampati kitu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vinasaba anavyotumia EWURA kuweka kwenye Mafuta. Vinasaba vinagharimu shilingi 12.50. Vinasaba vyenyewe gharama yake ni shilingi 5.25 na mwenye vinasaba huyo mwenye hiyo kampuni anapata shilingi 7. Kwa hiyo anakusanya kila lita kwa mwezi jumla anapata shilingi bilioni 14 amekaa tu bila sababu yoyote!
Ndugu zangu wakati anaingia Mkataba Waziri Mkuu alikwa ni Mheshimiwa Lowassa ambaye mmemnadi nchi nzima, na hii kampuni ya vinasaba ni Lowassa ana ushirika ndani yake, vinasaba vya Lowassa. Ni kampuni ya Lowassa na ndiyo alituingiza mkenge, ni Lowassa alipokuwa Waziri Mkuu.
Hili fisadi, anachukua Lowassa kila mwezi shilingi bilioni 14 hii kampuni yake, sasa ndiyo nawaambia mkakae mkachunguze huko. Mafisadi wakubwa. Mnaniharibia hata kuchangia kwangu. Mmemnadi ninyi nchi nzima, juzi ndugu yangu Mheshimiwa Khatib hapa anasema mwaka 2020 mtamleta yule yule Mheshimiwa Lowassa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Serikali ilipiga marufuku kuagiza sukari nje. Ninachowaomba, wapige marufuku kuagiza mchele kutoka nje. Kuna mchele kutoka India, kutoka Thailand katika nchi yetu hii wakati mchele wetu uko mwingi, tuokoe hela za kigeni kama tunavyofanya mambo ya sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kuagiza mchele nchi za nje wakati tuna mchele umerundikana Kyela, Tunduma, Sumbawanga. Kwa hiyo upigwe marufuku mchele kuingizwa kama ilivyopigwa marufuku sukari ili kuokoa wakulima wetu.
Kuhusu usafiri mwambao wa Ziwa Tanganyika, Serikali ya Awamu ya Nne ilituahidi meli mbili, ninashangaa hata Awamu ya Tano hata meli hakuna ni kukarabati MV Liemba tu! Sasa inakuwa ni matatizo, hakuna cha kutengeneza meli mbili, hata hiyo moja nimeona kuna ukarabati MV Liemba. MV Liemba ina umri wa miaka 112, hatukatai kukarabati MV Liemba, ikarabatiwe, lakini tunahitaji na meli mpya.
Kuhusu suala la uvuvi, wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika wako duni sana. Tunaomba wafikiriwe ili na wao waweze. Zambia ina asilimia sita ya maji ya Ziwa Tanganyika lakini Zambia ndiyo inakuwa muuzaji mkubwa wa samaki na dagaa, ina asilimia sita ya maji lakini ndiyo muuzaji mkubwa wa dagaa na samaki za Ziwa Tanganyika, wakati sisi tuna asilimia 38 ya Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Idara ya maji, nimezungumza sana habari ya idara ya maji ni majipu na Namanyere. Siyo lazima kumngoja Rais au Waziri Mkuu nimezungumza mara kwa mara hapa. Wanaiba, wameandika gari hewa Dar es salaam na Namanyere na mabomba hewa hakuna kilichopelekwa, kila mara nazungumza hapa, ni hewa tupu hakuna kitu kinachofanyika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Namanyere wananchi wana taabu ya maji miaka na miaka, wananidanganya hapa eti watanipa bilioni tatu, hamna cha bilioni moja, wala 500 milioni. Kwa hiyo, naomba bajeti ya safari hii, mradi wa maji na Namanyere ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mafisadi hukumu yao haitoshi kuwapeleka tu mahakamani. Haiwezekani mtu anakamatwa na nyumba 70 au 40, Serikali inachukua muda kumpeleka mahakamani na anapata dhamana.
Kwanza naiomba Serikali zile nyumba zinyang’anywe, kama alikuwa polisi, nyumba ziende Polisi, kama alikuwa mtu wa TRA (Tanzania Revenue Authority) ili wafanyakazi wa TRA wakodishe zile nyumba. Haiwezekani wewe mtu umefanya kazi yako inajulikana mshahara wako ni mdogo leo unanunua nyumba 40 au 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato na matumizi ya Bunge, Wabunge wengi nilizungumza hata mara ya kwanza hapa, wanasafiri kama wakimbizi wa Burundi. Wanapishana airport kama Wakimbizi, Magufuli amedhibiti hii wanaanza kumpiga vita, ndugu zangu kwa vipi? Mpaka timu za mpira zinakwenda kwa ndege Rwanda, hamna lolote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba apige marufuku timu zote za Bunge kwenda nje ya nchi. Safari za hovyo hovyo marufuku, Wabunge tuishi hapa tufanye kazi majimboni kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, safari za nini kwenda nje? Hakuna cha kutoa safari kwa Wabunge, Wabunge tukae hapa hapa tufanye kazi kwenye Majimbo kwa wananchi waliotuchagua. Kwenda nje iwe marufuku na mimi ninamuunga mkono Mheshimiwa Magufuli azuie safari zote za Wabunge za michezo hovyo hovyo kwenda nje, Wabunge wakakae majimboni kwao baada ya Bunge kutekeleza majukumu yao Majimboni. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa, naipongeza Wizara ya Nishati na Madini hasa Mkurugenzi Mkuu wa REA na Mkurugenzi wa TANESCO kwa kusaidia mradi wa kupeleka umeme kwenye Bwawa la Mfii, tegemeo kubwa la
maji Namanyere kupunguza kutoka shilingi bilioni 59 mpaka shilingi bilioni 23.

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa ya deni ni kulipa. TANESCO inadaiwa shilingi bilioni 820 na TANESCO yenyewe inadai pesa. Kuna Mashirika maalum yanadaiwa pesa. DAWASA, Idara ya Maji, inadaiwa; yenyewe inauza maji, kwa nini isilipe hela za TANESCO? Wakala wa Umeme Zanzibar (ZECO) wanadaiwa pesa shilingi bilioni 123. Wakala tofauti na kitu chochote, ni sawa na mimi na duka langu, wewe unaleta mali yako nakuuzia kwa bei unayonipa mimi nakurudishia zile hela. Cha ajabu ZECO hairudishi hela TANESCO, ni aibu! Serikali nzima ya Bara inadaiwa shilingi bilioni 40, ZECO inadaiwa shilingi bilioni 123, tutafika wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba TANESCO wawe na mtindo wa kukatia umeme popote wanapodai.
Haiwezekani kuleana namna hii! Kuna Wizara zote za Serikali ya Bara zinadaiwa. Hakuna Wizara hata moja isiyodaiwa na TANESCO, ni ajabu. Mtu binafsi, mwanakijiji ambaye hana mbele wala nyuma, ananunua umeme kwa LUKU. Mwisho wa mwezi hana hela, hapati umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wizara za Serikali hapa pamoja na Mashirika ya Serikali makubwa, hayalipi deni la TANESCO. Haiji kwenye akili ya binadamu kabisa! Dawa ya deni ni kulipa. Mwanakijiji hana mbele, hana nyuma, hana chochote analipa deni la TANESCO, anawekewa LUKU. TANESCO lazima ifanye operation nchi nzima hasa miji mikubwa. Kuna wizi wa ajabu wa umeme katika nchi hii. Kuanzia Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Sumbawanga, popote pale kwenye mji mkubwa, kuna wizi mkubwa wa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Nishati na Madini, kama haina wafanyakazi wa kutosha wakaazime JKT. Wachukue kwenda nyumba kwa nyumba, kijiji kwa kijiji; haiwezekani Shirika kupata hasara namna hii! Kuna wizi mkubwa wa umeme! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naiomba Serikali, msongo wa umeme kutoka Mbeya kwenda Kigoma kupitia Sumbawanga na Mpanda, hii mikoa mitatu au minne hii, inaleta hasara kubwa sana kwa Shirika hili la Umeme. Tunatumia majenereta, mafuta yanalika kwa kiasi kikubwa, hakuna faida TANESCO inapata kwenye Mikoa hii ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Shirika hili linapata hasara, ndiyo maana Shirika hili linaingiza hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haiwezekani tusipate umeme wa gridi ya Taifa kutoka Mbeya kwenda Kigoma mpaka Nyakanazi ili kuondoa mzigo kwa TANESCO. Haiwezekani mchakato kila siku; tupate umeme wa uhakika. Kwingine wanapata umeme wa uhakika, lakini mikoa hii mitatu, ni majenereta tu yananguruma. Kwanza yanaharibu mazingira kwa kusababisha moshi mijini. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu REA. Tatizo la REA ndugu zangu ni kutokupata hela za Serikali. Tuliamua hapa mafuta shilingi 150 iende REA, lakini hela haziendi. Asilimia 40 ndiyo hela zinakwenda, zikiingia Hazina hela zile, hazitoki kwa wakati. Wakandarasi hawafanyi kazi kwa sababu hawapati pesa. Mradi wa shilingi milioni 200 utafika milioni 300 kwa riba kwa sababu pesa hazipelekwi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, hela tunazoamua hapa Bungeni za 150 kila lita ziende moja kwa moja REA. Haiwezekani zikifika Hazina zinakwama zinatoka kwa masharti au zinabadilishwa njiani, haiwezekani. Kwa hiyo, naiomba Hazina ipeleke hela za REA ili wananchi wafaidike na umeme. Hatuwezi kumaliza vijiji hivyo 7,000 kama pesa haziendi, tunadanganyana hapa. REA wanapata kiwango cha chini cha pesa, hawawezi kuendelea kuweka umeme vijijini kama hawapati pesa. Tumeamua hapa na mafuta ni hot cake, mafuta
yanauzika. Tunauza mafuta, hela zinaingia, lakini hazijulikani zinakokwenda. Haiwezekani, lazima
wapewe pesa zinazohitajika ili Wakandarasi waanze kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naishauri TANESCO, sehemu za mapori makubwa, REA wapeleke nguzo za zege kuondoa hujuma ya kuchoma mapori na nguzo kuungua. Kuna mapori mazito na watu wetu hata ukiwapigia mbiu, useme mpaka uchoke, lakini kila msimu
lazima wachome mapori. Hawa watu ni hatari sana! Kwa hiyo, nawaomba, sehemu ambazo ni misitu minene, waangalie kutafuta nguzo za zege ili kuepuka kuitia hasara TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimefurahi na REA III. Waziri ametuhakikishia kwamba transformer zote na waya zote watanunua katika viwanda vyetu. Hiyo itasaidia kabisa kwanza kuharibu hela zetu za Kigeni kwenda kununua transformer mbovu nje au China wakati Arusha
kuna transformer imara na zinatosha miradi yetu kuzalisha umeme. Tuna viwanda vingi pamoja na TANESCO ina-share katika East Africa Cable, wanunue waya pale. Haiwezekani kwenda kununua waya nje wakati tuna waya zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wajiepushe kupitia Wakandarasi ambao ukienda, inapitia kwa watu wanazidisha bei ajabu! Miradi ya ajabu; unakuta mtu unayechukua tenda kuagiza waya nje, haijulikani ananunua bei gani kule anakuja kutubamiza bei wakati tuna viwanda vyetu wenyewe hapa nchini. Huu ni ubadhirifu na ufisadi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bandari. Ndugu zangu hii nchi ina bandari Mungu kaibariki. Nilikwenda Bandari ya Mtwara hata Afrika Kusini hakuna bandari kama ya Mtwara. Bandari ya Tanga ambayo ingesaidia Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Mara na Tanga yenyewe, ni ajabu watu wa Tanga na Kilimanjaro wanatumia Bandari ya Mombasa. Ni aibu kubwa kwa Serikali, wakati tuna bandari yetu wenyewe. Mungu katupa bandari katika mwambao wa bahari, lakini ni ajabu tunatumia Bandari ya Mombasa kuliko kutumia Bandari ya Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mpaka watu wa Dar es Salaam, wafanyabiashara wa Dar es Salaam wanatumia Bandari ya Mombasa, ni aibu kubwa kwa Serikali. Ni aibu, tumekuwa kama Burundi au Rwanda ambao hatuna bandari! Tujiulize mara mbili mbili, kuna nini hapa?
Kuna mdudu gani? Lazima tuimarishe bandari zetu ili wananchi wafaidike na bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kwenda hovyo hovyo, tunafanya kazi hovyo hovyo. Serikali iwe kali kidogo kwa kiongozi yoyote anayeingia tenda, manunuzi ya ajabu ajabu yanayotuumiza sisi, mdudu wa manunuzi huyu; lazima achukuliwe hatua kali. Haiwezekani wewe kitu unajua, hata mimi ambaye sikusoma na wala sio Mkandarasi, unajua kabisa hiki kitu sh. 10/= unakwenda kuandika sh. 500/= na unatia saini cheque inatoka! Kusema ukweli hao ndio maadui wa nchi. Hawa nilikuwa nazungumza siku zote! Huyu mdudu manunuzi, tungewakamata hawa tukawapiga risasi siku ya Ijumaa au Jumapili watatu au wanne, wangeshika adabu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hii Serikali ni tajiri kuliko Ubelgiji, kuliko Ureno, leo unashangaa hapa wanasema Ureno inajenga reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro. Ni aibu, wakati sisi ni matajiri kuliko Ureno. Ureno maskini wa Mungu wale leo hata chakula
hawana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali ifuatilie. Naishukuru sana REA lakini wapewe hela kwa wakati ili wafanye miradi yetu na vilevile wafikirie vijiji ambavyo viko nyuma sana, kuna mikoa iko nyuma sana, ndiyo waelekeze REA III. Kuna mikoa mingine kuna umeme
mpaka chooni. Sasa watufikirie na sisi kule Rukwa ambao tumekuwa nyuma kabisa, tumepata umeme miaka miwili iliyopita. Ni ajabu kabisa katika nchi hii! Ndiyo tufikirie zaidi kutupelekea huu mradi wa tatu na wananchi wetu wapate mwanga. Wananchi wa kule siyo wezi kama hawa
wa Dar es Salaam au Dodoma. Huku kuna wizi; tukipita leo hapa hapa Dodoma, tutakamata wezi siyo chini ya 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Shirika lipate hasara, ni wizi mkubwa! Pamoja na mashule haya, viwanda hivi, wanasaga usiku, wote ni wezi. Kwa hiyo, nawaomba sana Wizara ya Nishati na Madini wanisikilize. Operation maalum ifanyike, pamoja na Waheshimiwa Wabunge humu tumo, haiwezekani. Ndiyo nimesikia juzi juzi wanalaumu sana Ma-DC. Leo kuna Wabunge walikuwa Ma-DC humu, walikuwa wanakemea mpaka bangi, Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi kule Kibondo, lakini leo ni Mbunge, akiona bangi,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Anaogopa kura zake zitapotea.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Keissy muda wako umekwisha, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa nichangie Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachangia kuhusu mapato. Naomba Serikali irudishe kodi ya mifugo ili Halmashauri zetu zipate pesa za kujiendesha. Miaka ya nyuma kulikuwa na kodi ya mifugo, nashangaa Serikali ikafuta kodi ya mifugo wakati Serikali yetu ni maskini na Halmashauri zetu zinaharibiwa na mifugo lakini hatuna chochote tunachopata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo mifugo peke yake, hata mashamba ya kuku. Watu wanaofuga ng‟ombe mijini wanauza maziwa lazima walipe kodi. Ulaya wanajiendesha kwa kodi, Uingereza hawana chochote siku hizi ni kodi. Nilizungumza hapa hata tv, watu wana tv mpaka 20, 30, Uingereza wanalipa kodi ya tv lakini hapa hakuna mtu analipa kodi ya tv. Kama Serikali Kuu imeshindwa kulipia kodi ya tv, halmashauri zetu zikusanye kodi za tv maana wanajulikana wenye tv 10, 20, alipe kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi karibu watumishi wote wa Idara ni makaimu muda mrefu. Ujenzi kuna Kaimu, maji kuna Kaimu, utumishi kuna Kaimu, kilimo ni Kaimu karibu idara zote ni makaimu, ndiyo maana utendaji wa kazi unakuwa sio mzuri. Wengine hawana uwezo na kama wana uwezo wapandisheni washike hizo idara tumalizane. Siyo miaka 10, 20 mtu anakaimu, hakuna anayepeleka watumishi kule kwetu. Cha ajabu juzi juzi tu hapa Mkoa wa Rukwa RAS alikuwa amestaafu, wamemfanyia sherehe ya kustaafu, juzi wamesema amerudi tena Rukwa, ndugu zangu si hatari hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara. Nimezungumza muda mrefu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi haina uwezo wa kujenga barabara katika mwambao wa Ziwa Tanganyika inataka nguvu ya Serikali. Akina mama wajawazito wanakufa wakifuata huduma ya afya kwenye vituo vya afya. Kuna kibarabara cha kilometa 35, wananchi wa kule tangu dunia kuumbwa hawajaona hata bajaji, kijiji cha Kazovu, Chongotete, Isaba, Bumanda, hawajaona lolote, wanapata taabu. Ziwa Tanganyika likichafuka hamna msalie Mtume wanazama. Tumekaa hapa viongozi tunajali mikoa mingine, unashangaa mkoa mmoja unapata shilingi bilioni 27, mingine shilingi bilioni sita wakati wana kila kitu. Watu wanaomba lami hata kwenye Wilaya zao sisi hatuna hata barabara za vumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni miaka 40 Wilaya Nkasi pale Namanyere lakini hakuna Hospitali ya Wilaya. Wilaya ya Nkasi pale Namanyere leo miaka 40 wanapata maji kwa 16%. Kila siku tunapiga kelele habari ya maji Serikali haisikii. Sasa itakuwa namna gani, tunakuja kutetea wananchi au tunakuja kula posho za wananchi hapa? Kama tumekuja kula posho hakuna haja ya kuwa Mbunge maana hapa tunawakilisha watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijali Mkoa wa Rukwa kwa sababu hii. Kuna mikoa wamegawa majimbo hata hayastahili kuwa majimbo. Tumelalamika kuhusu Jimbo la Kwela hapa, la Mheshimiwa Malocha lina kata 26, watu 400,000, jiografia yake ngumu ukubwa kama Burundi. Cha ajabu mwaka jana wamegawa majimbo hata hayastahili kuwa majimbo lakini Kwela wameiacha vilevile. Mimi nina kata kule kwangu, Kata ya Nkwamba na Kata ya Kolongwe ni kubwa kama majimbo mengine hata kugawa kata mnashindwa, kugawa tarafa mnashindwa? Mnapendeleana tu, kiongozi akitokea sehemu fulani anagawa anavyotaka, haiji. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa TASAF. Wengi wamelalamika kuhusu TASAF, kusema kweli TASAF ni donda, ni jipu. Wamepeleka pesa kuwapa watu ambao hawastahili…
MHE. ALLY K. MOHAMED: Wanagawa kwa kupendelea, akiwa Mwenyekiti mjomba wake anampa hata ana miaka 18 anachukua hela ya TASAF. Kwa macho yangu na kwa ushahidi katika Jimbo langu wapo. Hili jambo mfuatilie hatukubali, hela zinakwenda kwa watu ambao wana uwezo. Watu ambao ni yatima, wasimbe sijui wanaitwa hawapati, wanakwenda kupewa watu wenye uwezo miaka 18, 20, watoto wa viongozi, hii haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha afya cha Kirando nimelalamika miaka yote, kimezidiwa na wagonjwa mpaka wagonjwa wanatoka DRC Congo, kipandishwe hadhi kuwa hospitali lakini wapi masikio yamejaa pamba. Ndugu zangu nataka kituo cha afya cha Kirando kipandishwe hadhi kuwa hospitali. Mpaka wakimbizi kutoka DRC Congo wanakuja kutibiwa pale, vijiji vyote vya mwambao wa Ziwa Tanganyika wanakuja kutibiwa pale, hakitoshi, hali ni mbaya. Kimezidiwa sana kile kituo cha afya Kirando, hakifai. Wagonjwa wamekuwa wengi kuliko uwezo wa kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Jimbo, ndugu zangu naomba majimbo yapitiwe upya kuhusu Mfuko wa Jimbo. Haiwezekani tupewe pesa zile zile. Mimi mfano jimbo langu kata nzima imeongezwa kutoka jimbo lingine naendelea kupata hela ile ile, itawezekana wapi? Majimbo mengine ndugu zangu tukiyapima humu hayana uwezo. Unakuta Mbunge anasema mimi nataka madawati, wewe una jimbo la kuomba madawati hapa, huna uwezo. Lazima hata haya madawati tunayogawiwa twende kwa vigezo. Jimbo gani ambalo watoto wanakaa chini sana na majimbo gani watoto wana madawati. Tusigawe tu madawati kila mtu sawa, haiwezekani, kuna majimbo mengine ndugu zangu yako taabani hayajiwezi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nichangie kidogo kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa muda mfupi aliokuwa Waziri Mkuu alikuja Namanyere akafanya ziara katika Jimbo langu la Wilaya ya Nkasi akatembelea mpaka vyanzo vya maji ambavyo nilikuwa napiga kelele hapa kila mwaka habari ya shida ya maji Namanyere. Sasa mwaka huu tatizo la maji Namanyere litakuwa historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile namshukuru Waziri wa Maji, alifika Namanyere mpaka kwenye vyanzo vya maji na akaahidi kusaidia mitambo ya kusukumia maji. Namshukuru vile vile Waziri wa Mambo ya Ndani alifika Namanyere, pia Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Makamba alitembelea Namanyere. Mawaziri wote walitembelea Namanyere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa namshukuru Mheshimiwa Magufuli. Mimi nilikuwa Bunge la Nne hapa ndugu zangu, nilikuwa msumari nazungumza ukweli kuhusu mafisadi, wezi wa mali ya umma, nilizungumza mpaka makaburi yao yafukuliwe wafungwe minyonyoro kwenye makaburi. Nilizungumza vile vile safari za Wabunge kwenda nje hazina manufaa, tunapishana airport kama wakimbizi. Nilizungumza hapa kabla Mheshimiwa Magufuli hajawa Rais, nilisema hizi safari hazifai! Hebu niambieni Mbunge hata mmoja aliyekwenda nje alete tija hapa kama sio ubadhirifu wa hela humu. Wengine walikuwa wanarudia airport, nimezungumza hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi wakamate hata passport zao waangalie, kama walipewa hela wakaenda, passport zitaonesha. Wengine wanapewa siku kumi wanakaa siku mbili wanarudi. Ndugu zangu tumsifu Magufuli amedhibiti nchi! Nilimwambia Rais Magufuli Kinyerezi kwenye kuzindua mtambo wa umeme nikasema; spidi yako bado sijaiona, bado spidi ni ndogo. Nchi hii bado mafisadi wengi, wanatuibia! Juzi juzi tu tender ya EWURA wanataka kutuingiza kutuibia bilioni sita kwa mwaka, shilingi bilioni kumi na tatu za Kitanzania kwa miaka mitatu mkataba huo tutaibiwa bilioni 40 wakati hatuna zahanati, hatuna madawati, hatuna kila kitu. Ndugu zangu bado watu hawaogopi Serikali, wapo! Hao wanataka wabanwe ikiwezekana kunyongwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo. Nimezungumza, Mfuko wa Jimbo kwanza usimame. Wapitie upya majimbo sio sahihi. Uchaguzi uliopita safari hii tumezidishiwa Kata kutoka Kusini kwenda Kaskazini, majimbo yameongezeka. Jimbo langu kata nzima imehamia kwangu
lakini Napata mfuko wa jimbo ule ule, nitahudumiaje kata ile nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Simbachawene nikampelekea na taarifa kwamba kata nzima imekuja kwangu. Haiwezekani niendelee kupata mfuko wa jimbo ule ule. Simamisha kwanza nchi nzima, fanya mchakato upya. Wabunge wengi wamelalamika hapa. Halmashauri ya Mji wa Namanyere ina vigezo vyote cha ajabu wamekwenda kutoa halmashauri zingine hazina vigezo! Ushahidi tunao, upendeleo wa hali ya juu na ugawaji wa majimbo vile vile kwa upendeleo. Haiwezekani! Nchi ni moja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majimbo kama kwa ndugu yangu huyu hapa, Sikonge square kilometers 27,000, kwa Malocha, 15,000, kuna majimbo mengine square metre 1,000 humu, kuna mengine 200! Haiwezekani! Hatuwezi kwenda hivyo. Lazima twende sambamba, haiwezekani Mbunge yule yule anapata pesa ile ile, gari ile ile, mafuta yale yale, jimbo lake linakuwa kubwa kama Rwanda, kama Burundi, haiwezekani! Hii ni kuoneana. Lazima Namanyere sisi tupate halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa imeanza juzi juzi halmashauri tano, sita. Cheki Mkoa wa Rukwa, Mkoa mkubwa kabisa halmashauri zile zile nne, haiwezekani! Ni maonezi hatuwezi kwenda. Ahadi ya Rais alituahidi alipokuja, barabara ya lami kilometa tatu tunaitaka Namanyere,
alituahidi kilometa tatu za lami, tunazitaka! Mheshimwa Mwenyekiti, hospitali Namanyere. Tuna miaka 40 Wilaya ya Namanyere haina hospitali ya wilaya, miaka 40! Watu wanasema miaka 20, miaka mitano mpewe hospitali. Kuna wilaya zimeanzishwa juzi zina hospitali ya wilaya, sisi miaka 40 hamna hospitali ya wilaya. Haiwezekani, haya maonezi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu DC wetu wa Nkasi. Tangu ameanza hana gari, hana usafiri. Anahudumia wilaya square kilometers 13,500 hana gari! Leo kasimamia shule 105 kujenga madarasa matatu shule ya msingi katika kila shule kuhamasisha wananchi na anajenga, anasimamiaje? Hana gari DC, anaombaomba magari. Polisi Namanyere hawana hata matairi. Ndugu zangu tuoneane huruma, kuna wilaya
zingine zinapewa magari matatu, manne hata hadhi ya wilaya hazina, ziko humu humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge hata ukubwa wa Kata kama Kata yangu hakuna! Wanapewa kila kitu. Lazima tufanye mchakato upya. Ikiwezekana Rais Magufuli aangalie, kama majimbo mengine ayafute! Ayavunje majimbo na halmashauri zingine. Hatutaki mambo
ya kuoneana. Kupanua halmashauri ambazo hazina hata uwezo, hazikusanyi chochote! Mzigo kwa Serikali. Tuambizane ukweli hata kama unauma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri wa ziwa Tanganyika; Awamu ya Nne tumeahidiwa meli mbili katika ziwa Tanganyika lakini nakuja kusoma tena ni utengenezaji wa Liemba ina miaka 113. Ndugu zangu, tunataka usafiri wa ziwa Tanganyika, meli mpya! Liemba itengenezwe maana bado inafaa, bado ni nzuri ikarabatiwe, lakini meli mpya tunaitaka katika Ziwa Tanganyika, wananchi wanapata matatizo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pembejeo. Hao wanaogawa ruzuku ya pembejeo, ndugu zangu haiwezekani mtu anasema ana deni milioni 360 wakati tukipiga hesabu ni mbolea bilioni 1.8 alipeleka katika jimbo langu. Wanachakachua, lazima wafuatiliwe. Nimemwambia hata
Waziri wa Kilimo, Waziri Mkuu nimemwambia, katika Jimbo
langu la Nkasi kuna kata kadhaa, hakuna kuwapa pesa
wamechakachuka, ni wezi wa hali ya juu. Ndiyo hawa Rais Magufuli anawatafuta awafunge mara moja hao. Hawa hawafai katika nchi yetu, haiwezekani anakuja mtu na briefcase anapewa kuleta mbolea, analeta gari moja la mbolea anataka milioni 360, huu ni wizi wa hali ya juu. Hawa ni watu wabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya mbolea ndugu zangu bora iuzwe bei chini, mambo ya pembejeo hakuna tena ruzuku waache ruzuku, kila mtu anunue kama vile ananunua vocha ya simu, mambo yaishe! Wametajirika watu kwa hela za vocha hizi, nchi hii ni wezi wa hali ya juu. Waaminifu ni wachache! Kwa hiyo, agenda zangu ni hizi hizi; nataka Namanyere kuwa Halmashauri ya Mji. Mheshimiwa Waziri Mkuu uliona Namanyere ilivyokuwa, kuna halmashauri zingine ukitembelea hakuna lolote, mnawapa halmashauri, ni uonezi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika; namwomba Rais Mheshimiwa Magufuli aendeleze, azidishe mara mbili. Asionee huruma mtu yeyote anayeiba hela za walipa kodi. Wananchi wetu, ndugu zangu majimboni kwangu kuna matatizo. Nazungumza habari ya usafiri kutoka
Kilado kwenda Kazovu miaka 50, tangu uhuru hatujaona gari! Nashukuru Ofisi ya Rais imenipatia pesa, mwaka huu wananchi wa Kazovu wataona gari! Niseme nini sasa? Nikose kumshukuru? Nilikuwa napiga kelele hapa wananchi hawajona gari, hawajaona bajaji lakini mwaka huu wananchi wataona gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba na Waziri wa Ujenzi aniongezee tena hela nipasue ile barabara Kazovu kwenda Korongwe, wananchi wafurahie uhuru katika nchi yao. Rais asikate tamaa aendelee kupambana na watu kama hawa. Hakuna kuoneana aibu! Haiwezekani ndugu zangu katika nchi zingine, mtu anaimba wimbo wa matusi kumtukana Rais mwanzo mwisho anaachiwa! Nchi gani hii? Utawala gani huu? Wewe mtu unamtukana Rais unaachiwa? Aende Rwanda kule akaangalie au nchi za Kiarabu, watakunyonga! Wewe unamtukana Rais wa nchi, wewe umekuwa nani? Uhuru gani? Demokrasia gani hii? Unaimba nyimbo, wewe nyimbo na mtu wa studio anarekodi nyimbo, ama kweli sio utawala huu! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wangeniachia mimi dakika mbili niwaoneshe hawa! Haiwezekani! Kiongozi wa nchi anatukanwa na nyimbo, ukiisikia hiyo nyimbo ya Roma sijui Mkatoliki, ndugu zangu nyimbo ya aibu. Haiwezekani mtu unasikiliza nyimbo kama ile. Halafu unamshabikia mtu!
Haiwezekani! Kusema kweli ni makosa, ni kukosa adabu. Rais wa nchi hatukanwi popote pale. Haiwezekani! Nendeni nchi zingine, nenda Rwanda hapo, nenda Burundi, nenda DRC ukaangalie, watakushughulikia! Nyie mnacheka cheka hapa, haiwezekani kumchezea Rais namna hii. Huu ni utovu wa nidhamu. Huyu Rais anaheshimika, dunia nzima wanamsifu Magufuli. Leo nyie wenyewe ndiyo mnamwona hafai kwenu,
kote ukienda wanamsifu, Uarabuni wanamsifu, Ulaya wanamsifu, sijui ukienda… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji). MWENYEKITI: Ahsante
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kama Serikali haina makosa, Serikali inaleta pesa lakini tatizo ni kwa wafanyakazi wa Serikali. Mfano, natolea wazi kabisa miradi ya maji Wilaya ya Nkasi. Serikali inapeleka pesa, ukiuliza kule pesa zinakwenda, Namanyere zipo pesa za kutosha, cha ajabu ukimuuliza Mkurugenzi, Mhandisi wa Maji wa Mkoa, Mhandisi wa Maji wa Wilaya, TAKUKURU na kila kitu, pesa zinakuja lakini hizo pesa zinarudi Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafanya mikakati, wanawapa wazabuni ambao hawana uwezo. Mzabuni uwezo wake, license yake ni bilioni 750, anapewa mradi wa bilioni saba. Tumemwambia juzi mradi wa maji Namanyere, Mfiri, mradi uko chini ya kiwango, tumezuia pesa asilipwe mkandarasi kwa ushahidi kabisa, tumeleta taarifa, lakini cha ajabu amelipwa milioni 320 bila Mkurugenzi wa Namanyere kufahamu. Baada ya muda wa siku mbili tu yule msimamizi wa mradi, mfanyakazi wa Serikali, meneja wa mradi ametoa notice ya kustaafu kazi, inaonesha wizi wa hali ya juu, mkakati mnyororo unatoka Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tu Namanyere kaenda Mkandarasi ambaye aliiba milioni 200 Namanyere na kitu chochote hakionekani, anataka kupewa tenda mradi wa maji Kirando, wanasema mpeni huo mradi kwa sababu tutamkata zile milioni 200, wakati milioni 200 hata chembe ya kazi haikuonekana. Nilizungumza hapa Bungeni kwa uchungu wa hali ya juu. Hizi pesa Serikali inakusanya kwa hali ya juu lakini bado kuna wizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dokta Magufuli anajitahidi kukusanya pesa lakini bado wezi hawaogopi. Wakaone mfano Namanyere miradi ya maji inavyoibiwa, ni uchungu wa hali ya juu. Kodi ya wananchi inaibiwa, milioni 800, milioni 300, bilioni moja mradi wa maji Namanyere, lakini hakuna chochote kilichofanyika. Tukiulizia malipo, tunaambiwa malipo yanalipwa kutoka Wizarani moja kwa moja. Ndiyo kuna mafisadi Wizarani huko, hawana uchungu na nchi hii, wala hawaogopi kuiba katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchunguze na miradi ya gesi Pan African na Songas wanatuibia kwenye miradi ya gesi. Miradi ya gesi tunaibiwa kuliko makinikia ya dhahabu, hatuna faida na gesi, tunaibiwa. TPDC inakopa pesa lakini asilimia yake ndogo, sijui hawa ndugu zangu wasomi, wanasheria mikataba ikiandikwa wanakuwa wapi. Tunaibiwa mchana kweupe wala mikataba haisainiwi usiku, saa tatu asubuhi ofisi ziko wazi lakini tunaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi tukikusanya pesa hazionekani kwa sababu mafisadi bado wapo. Hawa mafisadi tulishazungumza kila mara, hawa mafisadi ndugu zangu tuwe kama Korea, tuwe kama China, wataogopa. Wizi uko palepale, nguvu zote tunakusanya lakini wizi uko palepale; chunguza mwenyewe. EFD machines kila sehemu inakusanya pesa, ziko wapi? Kama mafisadi bado, mapanya wapo katika Serikali kwa nini tunaoneana huruma, tusiseme ukweli. Tuwe na uchungu, maana yake haiwezekani miradi ya hela inakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ndugu zangu siwezi kuilaumu Serikali. Hela zinakuja, zinatiririka, lakini hakuna chochote kinachoonekana. Namanyere hela zimekuja lakini hakuna maji, hakuna mabomba yanayotoa maji, wizi uko palepale. Sasa tutafika? Hatuwezi kufika. Nataka Serikali ichunguze miradi yote ya maji. TAKUKURU nilishaandika ripoti yote mpaka imefika kwa Mkuu wa TAKUKURU lakini hakuna hatua inayochukuliwa. Tunalindana ndugu zangu, tunalindana! Kuna mnyororo wa kulindana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa REA; Sumbawanga, miji imeongezeka, leo tumesema nchi ya viwanda. Ndugu zangu viwanda vya namna gani wakati umeme hautoshi? Leo viwanda vya kusaga tu Sumbawanga Mjini vinafungwa, vinasimama kwa sababu umeme hauna nguvu, umeme hautoshi, kiwanda kikubwa cha kusaga unga kikubwa Sumbawanga kinashindwa. Leo ndugu zangu tunasema uchumi wa viwanda, tumuinue mkulima, asilimia 75 ni wakulima, mkulima gani atalima mahindi mwaka kesho au mwaka huu wakati mahindi yameshindwa kuuzika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza lakini Waziri anatujibu kama vile yeye hana habari, hana uchungu na wakulima. Mkulima hata hawezi kununua mbolea wala hawezi kulima mwaka huu, mahindi yameshindikana kuuza. Tunazungumza kila siku mtu auze mnasema asage, apeleke unga wapi, watu wenyewe wengine wanataka kula dona, wengine wanataka kula kande, utamlazimisha mtu kula sembe? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, kwa hiyo naomba waangalieni wakulima ndio wapiga kura, asilimia 75 unasema ni wakulima, nani atalima shamba sasa? Kazi ya ajira hapati, kwenda shambani mnamnyanyasa mkulima, mbona ninyi mishahara yenu mnatumia mnavyotaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mishahara yenu mnanywea pombe, mnaongeza wake hakuna mtu anawauliza! Mkulima akilima hukumsaidia kupanda, hukumsaidia kupalilia, hukumsaidia kuvuna, akivuna unampa masharti ya ajabu ajabu kwa nini? Kwa nini unampa masharti mkulima wakati hukumsaidia kulima? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kazi ngumu kama kilimo, mvua isipokuja hapati kitu, mbolea unamuuzia, sasa ndugu zangu, tutafika? Ninyi aah, mnapata posho hapa mnaingia kwenye mabaa hakuna mtu anawauliza!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwaonee huruma wakulima wetu wauze mahindi. Hawana cha kuuza katika Mkoa wa Rukwa. Mnaona wivu akiuza mahindi ajenge nyumba ya bati, kitu cha ajabu kabisa. Hatuwezi tukakutana na Waziri, sijui tukakutana na wanaolima mahindi, tuambizane ukweli hapa wananchi wajue kama mwaka kesho njaa itakuja kwa sababu ninyi mmeshindwa kununua mahindi na mkulima hana hela ya kununua pembejeo wala hana uwezo wa kulima. Tusianze kutafuta mchawi hapa, mchawi ni ninyi kwa sababu mmezuia kuuza mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Zambia wanauza mahindi mpaka 20,000 wanaingiza kule sehemu za Matai, Kalambo, wanauza mahindi wanavyotaka sisi tunazuia mahindi. Kulikuwa na njaa Kenya, kuna njaa tumesikia DRC Congo, kuna njaa Sudan, kwa nini mmeshindwa kupeleka mahindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sijakosea jana, kazungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa kuhusu Rais kutoa tenda. Ndugu zangu, wapi Rais anatoa tenda? Mimi nimeshangaa, toa ushahidi. Unasema kwamba Rais anampa rafiki yake au ni kampuni yake, toa ushahidi. Naomba aliyesema jana, Hansard ipo atoe ushahidi. Kama Rais anahusika na kutoa tenda ya uwanja wa ndege wa Geita na kama Rais ni rafiki yake, atoe ushahidi. Sio kwenye Bunge hapa kuropoka kuhusu Rais, ni makosa ya hali ya juu. Huna ya kuzungumza kaa, weka akiba ya maneno, siyo unakuja hapa Bungeni unaropoka wewe unavyotaka kwa sababu ni Bunge, hapana. Toa ushahidi, Kamati ya Maadili ikuite utoe ushahidi, kama hukutoa ushahidi uchukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unazungumza kuhusu Rais, Rais ana makosa gani? Vitanda vya Muhimbili Rais hakuchukua hela kupeleka kule Dar es Salaam? Muhimbili ni Kanda ya Ziwa kule? Amejenga flyover Dar es Salaam ni Kanda ya Ziwa? Ndugu zangu, tuwe tunaweka akiba ya maneno, siyo unazungumza, unabwata kama uko Manzese, hapa siyo Manzese. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia ukweli, utoe ushahidi. Mimi nashangaa, Waziri anasema anaropoka kuhusu Rais hakuna mtu alisema tukakaa kimya kama tumepumbazwa. Nashauri Mheshimiwa Waziri atoe ushahidi kamili kama Rais alihusika na tenda. Naishukuru Serikali, wananchi wangu wa Kazogo walikuwa hawaoni gari, mwaka huu wanaona gari. Tangu uhuru hawajaona gari, nimepewa hela wanaona gari, nikose kuishukuru Serikali? Barabara ya lami imekwisha toka Tunduma mpaka Kibaoni kupitia Namanyere, sitaishukuru Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ndugu zangu inafanya kazi, tatizo ni wasimamizi wanakula hela kama watu wa maji. Kuna wizi mkubwa kila Wilaya, kila Mkoa, tena wanaohusika ni Wizarani moja kwa moja. Nataka mfuatilie wala sina utani na hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba, Rais siku akija Namanyere, nitawasema waondoke na wafanyakazi ambao wanakula hela katika Wilaya ya Nkasi wakiongozwa na Idara ya Maji. Haiwezekani hela inafika Namanyere inarudi Dar es Salaam wanagawana Wakandarasi. Wanawapa Wakandarasi tenda wana briefcase, hawana uwezo, hata tipa hana, wala mashine hana, unampa tenda ya milioni 500 au 600 kwa sababu mjomba wako au shangazi yako, hilo haliwezekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami nichangie kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano imetusaidia vituo vya afya viwili vinajengwa, kila kituo kimepata shilingi milioni 500, tunaishukuru sana Serikali, kusema kweli inastahili pongezi za hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi ina miaka 42 haina Hospitali ya Wilaya. Unakuta Wilaya zinaanza miaka mitano iliyopita au miaka 10 iliyopita zina Hospitali za Wilaya, lakini Wilaya ya Nkasi ina miaka 42 tangu imeanzishwa haina Hospitali ya Wilaya, ni kutuletea vituo vya afya tu, ndugu zangu haiwezekani na sisi tunastahili kupewa Hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Nkasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji, kila mwaka napiga kelele hapa, kila Bunge napiga kelele kuhusu miradi ya maji. Miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ndio mmefanya kokoro yaani ni wizi wa hali ya juu. Nashukuru Naibu Waziri wa Maji alikuja na Waziri mwenyewe alikuja na amejionea jinsi wanavyoshirikiana namna ya kuziiba hela za Serikali kupitia kwenye miradi ya maji, hasa Wilaya ya Nkasi. Serikali naiomba iendelee kuchukua hatua wote waliohusika, hata kama wamestaafu, wako wapi, wachukuliwe hatua, hata kama wamehamishwa wachukuliwe hatua, ili hela za Serikali zirudi wananchi wafaidike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara, tumepata barabara kule lakini barabara ndugu yangu haiunganishi Mikoa miwili ya Rukwa na Katavi. Barabara inaishia Kizi na inaishia Stalike, pale katikati hatujui itakuwaje hamna barabara ya lami. Serikali inasema kwamba Mikoa iunganishwe kwa lami, lakini Mkoa wa Rukwa na Katavi haijaunganishwa kwa lami miaka yote. Ukishafika Stalike hapo ndiyo mwisho wako na ukitokea huku kwangu mwisho wako kwenye Jimbo langu, Kizi ndio mwisho wa lami. Sasa pale katikati ndugu yangu hakuna lami, naiomba Serikali ifikirie sana kuipa lami hiyo barabara ili kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha VETA; namuomba Waziri wa Elimu, namshukuru sana Waziri wa Elimu na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kunipatia majengo yaliyokuwa ya wakandarasi kwa ajili ya Chuo cha VETA pale Paramawe. Watu wa VETA Kanda ya Mbeya wameshakuja kukagua wamekubali kabisa, walitaka tuwape eka 25 kwa ajili ya chuo hicho, sisi tumewapa eka 50. Sasa naomba Wizara ya Elimu iwape nguvu, iwape pesa kumalizia yale majengo, yako majengo 14 tena grade one kabisa yale majengo, wamefurahi. Kwa hiyo, naomba Chuo cha VETA kianzishwe haraka pale kuna kila kitu, umeme upo, maji yapo na tumewapa eka 50 badala ya eka 25. Kwa hiyo, ninaomba Waziri wa Elimu yuko hapa ananisikiliza, haraka iwezekanavyo ili Chuo cha VETA kianzishwe katika Wilaya ya Nkasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika. Nafikiri hata asubuhi kuna swali moja liliulizwa kwamba namna ya kupeleka bidhaa Kongo; ndugu zangu bila cheleo cha kuvusha mali pale kati ya Ziwa Tanganyika haiwezekani. Hakuna usafiri wa kuaminika katika Ziwa Tanganyika. Meli tangu Mjerumani, ndugu zangu ninyi wote hamjazaliwa hapa, bado linadurumiza katika Ziwa Tanganyika, haiwezekani, haiwezi kusaidia kupeleka bidhaa Kongo au Burundi au Zambia, haiwezekani. Tunahitaji meli kubwa mpya kwa ajili ya kuhudumia Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbolea. Asubuhi ndiyo nazungumza hapa kuna Wabunge wengine ndugu zangu wanakuja humu Bungeni hawana Majimbo, anazungumza kabisa Mbunge sijui anatoka wapi, anasema Serikali naipongeza iligawa mbolea kwa uzuri sana nchi hii, ndugu zangu, huyu analima au halimi? Ana wakulima au hana wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuingilia Rais Magufuli, ndiyo tunamshukuru, ndiyo mbolea kufika vijijini kwetu. Yeye anazungumza kwamba waligawa mbolea vizuri na kusifu Serikali tangu mwanzo mpaka asubuhi wakati hajui lolote, hajui hata mbolea inatumika wapi au namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tunazungumza mambo mengine kuhusu sukari na bidhaa mbalimbali. Haiwezekani mimi mkulima, Serikali ni sawa na familia nyumbani kwako, wewe unalima gunia 10 nyumbani kwako, matumizi yako nyumbani gunia 20 za mahindi, wewe utakuwa huna akili kiasi gani ukauze mahindi yako wakati matumizi yako gunia 20 na umelima gunia 10, utakuwa una akili au mwendawazimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuja hapa unazungumza habari ya sukari ya Zanzibar wakati hata sukari yenyewe wanasema ni magendo, kila siku mnakamatwa na karafuu mnavusha. Mnakamatwa na madumu kule Zanzibar, Tanga, mmegeuza huku Bara ndiyo uchochoro wa kuingiza bidhaa zenu. Madumu ya mafuta yanakamatwa kila kukicha, inakamatwa sukari kila siku, Bagamoyo mnapakia sukari chini mnaweka mchanga juu, nani hajui, Serikali mnaifanyia mchezo. Dawa yao hawa kunyang’anya vyombo vyao na yule tajiri kumtia ndani, kutaifisha kila kitu, majahazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mzalishe kule, hawa ndugu zangu hawalipi ushuru. Container la spare parts za pikipiki hawa wanalipa shilingi 5,000,000wakati Dar es Salaam vijana wauza Kariakoo wanalipa shilingi 40,000,000 container la spare za pikipiki na hakuna pikipiki kule wanaingiza makontena na makontena wanayavusha kwa jahazi kuleta Bara huku, nani hajui? Leo mnageuza uchochoro huku kwetu? Mnataka kututania? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari mnalima tani 8,000 kwa mwaka, matumizi yenu tani 17,000 mtakuwa na akili sawasawa muuze sukari wakati ninyi wenyewe haiwatoshi au hamnywi chai? Kama hamna pesa ya kununua sukari mseme tuwasaidie, siyo kusema sukari inawatosha, inawezekana hawana pesa za kuweza kununua sukari, maana sukari tani 8,000 matumizi tani 17,000 sasa inakwenda wapi hiyo sukari? Mnaagiza sukari za magendo kutoka Seychelles, kutoka wapi Mauritius, mnaingiza sukari kutoka Brazil sukari hailipiwi ushuru, wala haina vigezo, haitakubalika, haikubaliki, sheria ni msumeno.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Taarifa ni ya kwake, maana hajui hata kulima huyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikiliza kwa makini, nakueleza hivi Mheshimiwa, mimi ni mkulima nalima gunia 10, mahitaji yangu ya kula nyumbani kwangu gunia 20, naweza kuuza gunia 10 zile? Nitakuwa na akili? Niue familia yangu? Wewe uuze sukari huku, baadae uje kununua sukari Bara upeleke Zanzibar una akili kweli? Ndio nilisema hujui biashara, mimi nimeanza biashara wewe hujazaliwa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuambia haiwezekani na Waziri wa Fedha yuko hapa, ni lazima kuanzia Tanga mpaka kule Mtwara idhibitiwe barabara mipaka yeyote anayeingiza mafuta ya kula, anayeingiza sukari, anayeingiza spare za pikipiki, spare za gari, ataifishwe vyombo vyake na yeye mwenyewe kukamatwa. Haiwezekani, tunalipa kodi ushindani wa biashara utakuwa hakuna. Ushindani wanaagiza tani 20,000 Zanzibar ongeza tani 8,000 tani 28,000 matumizi yao tani 17,000 tani 11,000 mkamuuzie nani? Mnageuza dampo huku, hakuna cha dampo huku, ujanja ujanja huo hakuna bwana. Unaogea sabuni halafu unaitupa chooni sabuni unaokota unaenda kuogea tena, haiwezekani.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuzungumzi habari ya Muungano. Tunazungumza habari ya ulipaji wa kodi na ukwepaji wa kodi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mneemeke kwa kuleta bidhaa zenu ambazo hazilipiwi ushuru, ushidani wa biadhara uko wapi? Haiwezekani, kwanza ninyi nawauliza swali moja, mfumo wa kodi wa Kimataifa jiungeni, jiungeni na mfumo wa kodi wa Kimataifa, lakini mmekaa hamjiungi na mfumo wa kodi wa Kimataifa kwa sababu mmezoea kukwepa ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Khatib alikuwa anazungumza hapa, mimi nilinyamaza nikawa kimya, sasa nakujibu mapigo...

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu mwenye busara unalima mikungu miwili ya ndizi, unakula mitatu, unauza ndizi zote watoto wako wale nini?

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa yake na yeye naona akapimwe akili, maana anaacha watoto wake wana njaa anasaidia watoto wa jirani, akapimwe akili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaeleza namna ya ukwepaji wa kodi. Hawa jamaa wamezoea kutuletea bidhaa, nafahamu container la spare za pikipiki linatozwa shilingi milioni tano hadi milioni sita. Nenda TRA pale Dar es Salaam milioni 40 vijana wa Kariakoo wanalipa, tutalinganishaje biashara? Mnateremsha kwenye majahazi usiku, nani hawajui wengi mnaweka bidhaa chini mnaweka mchanga juu, nani hajui? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima iwe macho kuangalia uhujumu wa namna hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wamekamata mafuta Tanga, nani hakuona kwenye television?

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana na naipokea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara ya Fedha kuanzia sasa iwadhibiti watu hawa, kila siku kutolewa kwenye television mafuta yanakamatwa, inakamatwa sukari, sasa ni kutaifisha vyombo vyao na wenyewe wafunguliwe mashtaka, wafilisiwe mali yao, wataacha kuleta mchezo wa kukwepa kodi. Kukwepa kodi ni kosa ndugu zangu, tunahitaji barabara, tunahitaji dawa katika hospitali, tunahitaji kila kitu kutokana na kodi, hii nchi inaendeshwa kwa kodi, acheni kukwepa kodi ndugu zangu tuwe macho.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa namshukuru Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Naibu Waziri, Mheshimiwa Aweso kusema kweli baada ya kulalamika hapa Bungeni walifunga safari ingawa Nkasi ni mbali walifika mpaka Nkasi kuangalia jinsi miradi ya maji inavyoibiwa.

Mheshimiwa Spika, katika kuibiwa hii Wizara ndiyo inaibiwa, yaani hakuna sehemu tunaibiwa kama Wizara ya Maji. Mheshimiwa Aweso alijionea mwenyewe alivyofika Kirando, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe alijionea mweyewe alivyofika Kabwe, wamejionea miradi ya kusadikika yaani ni miradi ya ajabu ajabu. Kabla ya wiki moja hajafika Mheshimiwa Kamwelwe pale tenki lilibomoka kidogo liue wanafunzi, yeye mwenyewe shahidi aliona. Alifika Mheshimiwa Aweso mwenyewe akasema hii miradi kusema ukweli wanapeana kijomba kijomba, kishangazi shangazi, hakuna kusema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kamwanda - Kirando nitakusomea, mradi huu umeingiwa mkataba wenye gharama ya shilingi bilioni 7.7 na mkandarasi Wimbe, mkandarasi ni class five ambao uwezo wake ni shilingi milioni 750 lakini akapewa kijomba kijomba mara kumi zaidi. Maelezo ya Bodi ya Usajili wa Wakandarasi tarehe 4 Julai, 2017 yalieleza kuwa mkandarasi huyu hana sifa za kutekeleza mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikutosha, hata guarantee ya benki hakuweka, hana uwezo. Baraza la Madiwani Nkasi lilimkatalia, lakini baada ya kusimamisha mradi alikwenda kukopa mabomba Kahama akaleta mabomba Kirando, yaani ni wizi wa hali ya juu. Tukazuia shilingi milioni 800 na huyu mkandarasi nilizungumza hapa Awamu ya Nne, mkandarasi huyu ndiye alipewa shilingi milioni 210 kwa mradi wa maji Kamwanda, alikula hela hakuna chochote kilichofanyika, huyu mkandarasi. Tender yake haikutangazwa, siri, ni ujambazi wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu mkandarasi ni jambazi na miradi mingi ya Mkoa wa Rukwa huyu bwana kaingia haitoi maji. Nenda Matala mradi wa shilingi milioni 450 hakuna maji yaani miradi ya Nkasi utadhani ni Zaire kule Congo hawawezi kujua watu, lakini miradi yote ya Nkasi ni wizi, ni wizi, ni wizi hakuna hata mradi mmoja ambao unasema unatoa maji. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, inasikitisha sana, Awamu ya Nne hapa imetoa shilingi bilioni 1 kwa ajili ya Bwawa la Mfili, alikwenda Naibu Waziri wa TAMISEMI, Ndugu yangu, shemeji yangu Kakunda kwenda kuangalia ule mradi thamani yake haifiki hata shilingi milioni 350 kwa ushahidi kabisa leo wanatoa shilingi milioni 300 kwenda kuweka mabomba, sijui kuweka mashine pale kwenye bwawa, bwawa lenyewe halina maji, amechimba kwa shilingi milioni 350, ni ujambazi wa hali ya juu. Hii Wizara kusema kweli inaibiwa hela zinatoka kule na zinarudi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viongozi wakubwa ndiyo wenye miradi hii wanajulikana, kwa ushahidi wananitafuta mimi tuzungumze nao na mimi nawakatalia. Eti Mbunge nyamaza ili waibe zaidi, haiwezekani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Isale - Kate, mikataba hii hapa wamefutafuta, wameongeza shilingi milioni 24 haijulikani za nini. Wanaweka shilingi milioni 300 eti kuzuia maji tu pale ili kuja huku, shilingi milioni 300. Ndugu zangu kodi za wananchi tuzioneeni uchungu, hii ni kodi ya wananchi. Serikali haifyatui noti ni kodi za wananchi, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walikwenda kujionea Mawaziri wenyewe, Engineer Kamwelwe alikwenda kuona kule Kabwe wameweka solar fake fake, betri fake fake tu alikwenda kuona mwenyewe, tenki kidogo liue wanafunzi alikwenda kuona mwenyewe. Mheshimiwa Aweso alifika mpaka Kirando, wakandarasi kawaambia. Sasa nataka kujua Mradi wa Kirando umesimama leo miezi sita na Mkurugenzi kasimamishwa kazi, natakakujua mradi wa Kamwanda utaanza lini kutoa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumezuia wizi huu, ukipiga mahesabu zaidi ya shilingi bilioni tatu ilikuwa ziende mimi ndiyo nimezuia hii, nastahili sifa. Hata wakichunguza Mradi wa Isale - Kate kuna wizi. Miradi yote ya Rukwa ukichunguza ni wizi wa mabilioni ya hela. Ni kweli lazima Tume itumwe kila mradi wa maji uchunguzwe. Haiwezekani Rais anajitahidi kukusanya pesa Idara ya Maji ni kama mfereji, ndiyo maana ikaitwa Idara ya Maji, unatoa watu, unamwaga tu. Ndugu zangu tuwe na uchungu na nchi hii, hatuwezi kukubali kuibiwa namna hii. Maji ni uhai, Namanyere tunapata maji asilimia 16 leo mnasema maji vijijini sijui asilimia ngapi Namanyere maji yako wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza hapa mimi Mbunge nakaa siku tatu siogi, Namanyere kuna maji yako wapi? Asilimia 16 Namanyere maji hayatoki zaidi. Hakuna mradi umekamilika, hata kama mradi unatoa maji ukilinganisha na fedha mzee ni balaa tupu. Hata mimi sikusomea huo uinjinia, sikuoma mahesabu lakini huwezi kunidanyanya bei ya bomba inajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza hapa miaka iliyopita kweli nina uchungu nimemwambia na alikuja mpaka Waziri pale aliyetoka tukamwambia usilipe hizi hela, usilipe shilingi milioni 300 hizi kwa hili bwawa maana thamani yake haifiki shilingi milioni 900 lakini cha ajabu alilipa hela. Ndiyo maana Rais akipita sehemu anasema wakamateni wakandarasi, msaidieni Rais Ndugu zangu yuko peke yake, hebu muoneeni huruma. Haiwezekani mtu anachimba bwawa la shilingi milioni 300 mnamlipa shilingi milioni 900 na tulizuia! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alikuwa Zumba na Zumba siku hizi ndiyo Naibu Katibu Mkuu hapa TAMISEMI, alikuwa kwenye bwawa na akasema huyu Mhandisi ondoka naye na hizi hela msilipe lakini walilipa. Zumba shahidi leo ni Naibu Katibu Mkuu, TAMISEMI, tusemeje sasa sisi? Mbunge anazuia, RAS anazuia, Mkurugenzi anazuia, DC anazuia lakini analipwa kijanja kijanja. Ndiyo maana tunasema huko Wizarani kuna mtiririko, kuna wizi, kuna ujambazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sifichi, sili kwao, mimi nakula hela yangu ya halali hapa nawaambia ukweli kabisa anayechukia achukie, hizi kazi wanapeana kijamaa, kijomba kijomba. Mtu hana guarantee ya benki, hana chochote, anapata ile 15 percent ndiyo anakwenda kununua magari na mabomba. Leo mradi wa Isale umesimama, kapewa shilingi bilioni 1.1 kaenda kununua magari mawili, kaenda kununua mabomba, kaishiwa hela anataka certificate, hakuna chochote. Ndugu zangu tuangalie hii miradi ni nani anaichunguza mpaka kupandishwa thamani, mradi wa shilingi bilioni tano, shilingi bilioni nne unakuwa wa shilingi bilioni saba? Nataka Mradi wa Kamwanda kuanzia sasa Mheshimiwa Waziri kaufanyie mahesabu uanze kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi hawana makosa au mimi kosa langu kusema panatokea wizi ndiyo mmesimamisha mradi? Maana yake mimi ndiyo nimesema kuna wizi, baada ya kusema kuna wizi shilingi milioni 800 hakupewa na mradi umesimama, wananchi wanateseka hawana maji, kosa lao ni nini? Ningeachia mradi tungeibiwa zaidi ya shilingi bilioni 3.5. Hata mtu fanya hesabu kidogo tu, mradi wa kutoka Kate mpaka Isale ni shilingi bilioni 5.4 na unakwenda zaidi ya kilometa 30, Mradi wa Kirando unachukua maji Ziwa Tanganyika nusu kilomita shilingi bilioni
7.7 Ndugu zangu hebu na nyie wenyewe semeni ukweli. Hata mtu mpumbavu hakusoma darasa la pili atajua hesabu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mradi wa kutoka Kate kwenda Isale una-supply vijiji saba njiani, kilometa 35, shilingi bilioni 5.4 na hapo bado kuna wizi ndani yake.

Mheshimiwa Spika, vijiji vya Nkasi karibuni vyote havina maji, Kata ya Mkwamba yote haina maji, vijiji vyote havina maji wala kisima hakuna. Visima wamechimba wakati wa Mzee Nyerere pia havitoi maji. Tuna matenki Kirando tangu enzi ya Nyerere bado Rukwa iko chini ya Mkoa wa Mbeya. Kuna vijiji vya Itindi, Isale, Gele, Masolo, Katongoro, Kakoma, Ipanda havina maji wala kisima hata kimoja.

Wananchi wanafukua maji kwenye madwimbwi wakati wa masika kama panya, hela inakwenda wapi?

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa hela, lakini watendaji ndiyo wanaiba hela hizi. Kwa Nkasi mimi siilaumu Serikali hata kidogo, Serikali inatoa hela lakini zinaliwa na wajanja wajanja wanapewa hela kijomba kijomba, kishangazi shangazi. Amesema Ester Bulaya hapa ni kweli yule mkandarasi hata kule Mtwara alikula hela, wala siyo uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kusema kweli ni hatari, maji Ziwa Tanganyika yapo wananchi hawapati maji. Ni kitu cha ajabu kabisa, mradi wa shilingi bilioni 7.7 ulikuwa tayari kwenye pipe na anapewa hela hawa mapema kabisa, walitaka kumpa shilingi bilioni moja wakati hakuna kitu, Mradi wa Isale amepewa shilingi bilioni 1.1. Nataka TAKUKURU wakachunguze miradi yote Wilaya ya Nkasi na TAKUKURU wamekwenda kule wameshakaa mwezi mmoja na nusu. Niliwaomba TAKUKURU wakakae kule Mkoa wa Rukwa, nilimwambia Mkurugenzi wa TAKUKURU mimi kaangalie miradi ya mkoa mzima wa Rukwa, mkoa mzima ni wizi mtupu na inawezekana nchi nzima lakini kule kwetu mzee walifanya maficho. Namshukuru Mheshimiwa Aweso aliwaambia wakandarasi mbele ya uso wake kwamba nyie hapa mlitaka kula.

Mheshimiwa Spika, mwenyewe Waziri wa Maji alifika mpaka Kabwe akashuhudia tenki linawekwa maji baada ya maji kujaa limepasuka lote pwaaa! Mpaka leo Mheshimiwa Waziri hawajenga lile tenki. Tulikwenda na wewe mpaka leo hawajenga lile tenki. Yule mkandarasi akaja kukuambia ooh mimi tunajuana tunajuana kitu gani?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie hizi Kamati zote mbili na naziunga mkono. Kwanza kabisa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli kwa uwezo na ujasiri wa kufanya bwawa la Rufiji kwa ajili ya umeme. Ni ajabu kabisa Wabunge wote wakikaa wanadai umeme kwenye vijiji vyao, wadai maji kwenye vijiji vyao, maji huwezi kupata bila umeme, hakuna chochote kinachofanyika kwenye kijiji chako bila umeme, wanadai REA awamu ya tatu kwamba wanataka vijijini umeme, vitongojini umeme, sasa bila ujasiri wa Rais Magufuli kupata umeme, nyie mtapata umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Ethiopia wanachanga pesa wanakata mishahara kwa ajili ya kujenga bwawa kubwa wapate umeme. Nyie Wabunge tukisema tuanze kuchanga pesa mtaanza kuruka ruka. Nchi nzima Ethiopia na umaskini wao wanachanga pesa kujenga bwawa kubwa la umeme, je, tukiamua watu hapa tuanze kuchangia bwawa la Rufiji kule mtakubali nyie?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anakubali kutoa fedha kujenga bwawa la umeme tupate umeme nchi nzima mpaka vijiji vyenu, leo mnakaa mnapiga kelele, mazingira, Marekani ndio baba wa Taifa kwa viwanda, anakataka kutia mkataba kwa ajili ya mazingira, mbona hamumchukulii hatua? Mnapiga kelele, Mheshimiwa Zitto, Kigoma hakuna grid ya Taifa kama kwangu Nkasi, tuache kelele tupate grid ya Taifa katika vijiji vyote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Rukwa unaitia hasara TANESCO umeme hautoshi mnatumia majenereta na mnachafua mazingia moshi kule kwenu. Ndugu zangu lazima tumtie nguvu Rais ajenge bwawa, kelele za hawa jamaa…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Mollel, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo mimi nawafahamu. Ukiona mti wako hauzai, ujue ni hatari kata panda mwingine, sasa ndugu zangu hawa wanapungua siku hadi siku, Madiwani wamepungua, Wabunge wanapungua mpaka ifike 2020 hali ni ngumu, tumuache Rais afanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia habari ya mkataba wa SONGAS na Serikali yetu. Hapo fungueni masikio vizuri sana, hapo tuelewane huu mkataba, ujasiri wa Rais auvunje, hatuweeze kwenda nao mpaka 2024, tutakufa. Huu mkataba ni adui mkubwa wa nchi hii, ni wizi wa hali ya juu na namwomba Rais walioshiriki wote Mkataba huu wakamatwe mara moja kuanzia sasa. Mkataba huu Serikali yetu ilichangia 73% dola bilioni 285 milioni, hawa jamaa wa SONGAS walichangia dola 106.3 milioni, sawa na 27%, bado haikutosha, hizi pesa sio zao, Serikali yetu ilikwenda World Bank kukopa na kuwapa. Badala ya wao watulipe sisi, lakini sisi ndio tunawalipa wao, jamani ndugu zangu ni hatari kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu kiningine kibaya katika Shareholder wakati sisi tuna 73% wenyewe 27% sisi tukapata 46% wenyewe 54%, ndugu zangu! Kingine cha ajabu, tukaingia mkataba nao kwa ajili ya kuweka capacity charge dola milioni tano kwa mwezi, sawa na shilingi kwa sasa 11, 475, 000,000 wakati sisi tuna 73% tunapunjwa kila mwezi capacity charge tunapunjwa 8,668,750,000.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally Keissy kuna taarifa, Mheshimiwa Ally Keissy.

(Hapa Mheshimiwa Ally K. Mohamed aliendelea kuzungumza bila kutumia kipaza sauti)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally Keissy microphone yako ilikuwa imezima kwa hiyo yatakuwa hayajaingia hayo uliyosoma baada ya kipaza sauti kuzimwa. Mheshimiwa Kubenea taarifa na Mheshimiwa Ally Keissy itabidili hayo uliyokuwa unasema urudie ili yaingie kwenye Hansard.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naona Mheshimiwa Kubenea hanielewi, mikataba mibovu tunazungumzia yote na wewe mwenyewe labda ulikuwa chama mtumishi wa Vyama vya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia haikuingia kwenye Hansard, nyamazeni.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma muache Mheshimiwa Keissy achangie kidogo ndiyo unaweza ukasimama kwenye taarifa, la sivyo utakuwa unampa Mheshimiwa Kubenea. Mheshimiwa Ally Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, labda niongee taratibu, nazungumzia mkataba wa SONGAS na Serikali. Huu mkataba ni ufisadi wa hali ya juu, namuomba Rais anisikilize na waliopo wakamwambie mkataba huu haufai kuanzia leo waufute. Huu mkataba Serikali ilichangia dola 285.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally Keissy kuna taarifa nyingine huko.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Musukuma moja kwa moja. (Makofi)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea. Hawa Songas capacity charge wakati sisi TPDC tumechangia asilimia 73 wanachukua 100% capacity charge wakati sisi tungepata asilimia 73 capacity charge na wenyewe wangepata asilimia 27. Wakati huo huo mitambo ikiharibika gharama ya kutengeneza mitambo yote ni juu ya TANESCO. Mpaka sasa TANESCO wameshagharamia matengenezo ya mitambo shilingi bilioni 3.22 pamoja na VAT shilingi bilioni 90 wakati wale Songas wamekaa starehe huko kwao wanakula tu zile capacity charge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi hao Songas na PanAfrica; PanAfrica wenyewe wamekaa katikati hata kodi hawalipi. Tangu Awamu ya Nne tumesema sisi hapa Bungeni kuhusu PanAfrica kulipa kodi, kodi walikuwa hawalipi, wanachukua net pesa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichunguza mikataba TANESCO haiwezi kupata chochote na itaendelea kufifia. Songas amechukua baadhi ya Watanzania ambao walikuwa madarakani TPDC na kuingia mikataba hii mibovu, ndiyo Wakurugenzi wake. Baadhi ya viongozi wa Serikali waliokuwa Wakuu wa Mikoa ndiyo washauri wake. Juzi walikuja kwenye Kamati niliwahoji ninyi kweli ni wazalendo? Mzungu alibadilika rangi. Nikawauliza ninyi ni wazalendo kuangamiza nchi namna hii? Mpaka tarehe ya leo wametudhulumu shilingi trilioni 1.3 73 ya asilimia zetu 73.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ndugu zangu tunakalia kudai watu nyanya sokoni kule ushuru na mambo madogo madogo wakati hela zinakwenda kuliwa na Wazungu. Nilimwambia yule Mzungu kama Tanzania kwa wajanja mnaifanyia hivi, je, DRC Congo kule? Belgium imekaa inanyonya DRC Congo inakuwa tajiri mpaka watupe masharti ya ajabu ajabu tuoane ndiyo watupatie pesa wakati hawana chochote si lolote, wananyonya nchi za Kiafrika mchana kweupe tena ni Mabeberu wana ndevu ndefu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu mambo ya nje, tuelekeze nguvu zetu DRC Congo, tuweke jicho letu DRC Congo. Congo ni nchi ambayo imekaa kitajiri kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Tuienzi DRC Congo tupeleke macho yetu DRC Congo. Tunakaa chini ya ua la waridi, Congo itatusaidia sana kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapitwa na nchi kama Rwanda inayoegamia Congo leo inasifika dunia nzima kwa kupora Congo. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, jicho letu tupeleke Congo. Nashangaa wanasema wameshindwa kupeleka mahindi kule kupitia Zambia wakati Lake Tanganyika kuna barabara ya kutosha kwenda DRC Congo kupitia Ziwa Tanganyika. Ndugu zangu tubadilike, tuwe na wachumi na wafanyabiashara katika Serikali yetu.

MBUNGE FULANI: Kabisa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Tuondokane na mambo ya ajabu ajabu haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashangaa kitu kimoja, Rais Magufuli aliwaita Wachungaji, Mashekhe na Maaskofu badala ya kuzungumza mambo ya maana akatokea jamaa mmoja akamwambia wewe mzee wakikushauri kuongeza muda usikubali, alitumwa na nani? Ukienda kila sehemu wanataka Rais Magufuli bila Rais Magufuli ndugu zangu nchi ilikuwa imeoza, tukubaliane kabisa nchi ilikuwa imeoza. Wabunge wanasafiri kama wakimbizi kwenda nchi za nje na impact hakuna leo, Rais kawabana wanabaki wanatapatapa wanahangaika. Hilo wazo alimtuma nani kwenda kumwambia Rais kwamba asiongeze muda, mlimtuma nyie. Wenyewe Wachungaji, Maaskofu na Mashekhe wana muda wa kuongoza, Shekhe ni mpaka achanganyikiwe akili au afe.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Keissy, kuna taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Haya, nipe taarifa nikujibu. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimesema lilikuwa limeoza siyo sasa limeoza, hiyo taarifa sipokei, napokea nusu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia habari ya TANESCO, mpaka leo TANESCO inadaiwa zaidi ya bilioni 600 na hao jamaa wa Songas. Songas wanawauzia umeme TANESCO senti sita, TANESCO wanauza senti 11, tukamuuliza anasema eti mimi nauza bei ya chini sana, wewe unauza huna gharama kama TANESCO. TANESCO wanagharamia kusambaza umeme nchi nzima wewe Songas una gharama gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa tunawaogopa vipi hawa Songas, tunawaogopa nini hawa PanAfrica? Lazima tuongoze kijasiri ili kujikomboa, tunaibiwaje shilingi trilioni 1.3 halafu tunaenda kuwaomba tena hela Wazungu? Hicho ni kitu cha ajabu mpaka Rais wa Marekani na mke wake wakaenda kutembea pale Ubungo, hamkusikia au mlisikia? [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WABUNGE FULANI: Tulisikia.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Ni kwa sababu ya maslahi yake. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujasiri Rais Magufuli namwomba anisikilize aingilie upya mikataba hii ya Songas, asilale usingizi, awatafute wote waliotia saini kwanza awalundike magereza mara moja. Kama walipata mali kwa njia ya rushwa kuingia mikataba ya namna hii, mali zao zitaifishwe mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita nilizungumza mara nyingi watu kama hawa ndugu zangu wanaoingia mikataba mibovu dawa yao ni kuwanyonga. Leo ukiwanyonga watu 200 Muhimbili wanazaliwa 500 kuna hasara gani? (Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nipatre kuchangia dakika zangu hizi 10. Kwanza kabisa, naunga mkono hoja kwanza kwa asilimia mia moja. Namshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada anazofanya pamoja na Mawaziri wote. Kusema kweli Mawaziri wanapishana kwenye anga za Wilaya na anga za Majimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais, Wilaya yangu ina miaka 40 lakini ilikuwa haina Hospitali ya Wilaya ila mwaka huu imepata fedha za Hospitali ya Wilaya pamoja na Vituo vya Afya viwili. Tumelalamika miaka na miaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nataka kuchangia kwenye Tume ya Uchaguzi. Wengi wanazungumzia habari Tume ya Uchaguzi, mimi nazungumzia Tume ya Uchaguzi, ipitie upya Majimbo na Kata. Hatulingani Majimbo. Unakuta Mbunge mmoja ana Kata nne, Kata sita, Kata saba mwingine Kata 28 au 29, anapata mafuta yale yale ya Jimbo, pesa ile ile ya Jimbo, mwingine amekaa tu anazunguka na bajaji na pikipiki anamaliza Jimbo lake. Naomba Tume ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mita aipitie Kata upya, kabla ya Uchaguzi Mkuu apitie Majimbo upya. Kama Majimbo hayafai, fyekelea mbali. Nadhani tunaelewana hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya wakulima wa Rukwa. Wakulima wa Rukwa ni wakulima wa mahindi na mahindi yetu hayo ni zao la biashara. Mwaka 2018 wameteseka sana, leo hi nimepata habari DRC Congo mahindi gunia ni shilingi 100,000/= lakini kwetu mahindi ni shilingi 30,000/= vikwazo vimekuwa too much. Vikwazo vimezidi. Mahindi yanatakwenda Kenya vikwazo, yanataka kwenda South Sudan, vikwazo; yanataka kwenda wapi, vikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima wetu mahindi ni kama zao la biashara. Kwanza hamwasaidii mbolea, hamwasaidi kupalilia, hamwasaidii kuvuna, wakivuna mnawawekea vikwazo, kwa vipi? Mwaka huu ndugu zangu sehemu nyingi mnasikia mvua hakuna. Kufa kufaana. Tuache tuuze mahindi tunapotaka, kila mtu ajue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanakalia kucheza bao, kucheza dhumna hawalimi shambani, wanaogopa kwenda kulima, walime wengine mwekewe vikwazo. Vikwazo mwaka huu hatuvitaki Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kila mtu ajue lake, tuuze mahindi tunavyotaka na ondoeni vikwazo kuuza mahindi popote tunapoweza. Nyie chukueni ushuru wenu, mambo yaishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika. Tufanye biashara. Ziwa Tanganyika tumezungukwa na nchi ambayo ni tajiri katika Afrika DRC Congo. DRC Congo hawana usafiri. Hivi tukitengeneza meli kubwa iwe inazunguka kutoka Kigoma iende Huvira, Kalemi, Moba, Zambia - Mpulungu, irudie huku kwetu, tutapata na pesa za kigeni. Tusijifungie kati. Congo kama Congo ni nchi tajiri. Tufunguke tufanye biashara DRC Congo. Huwezi kufanya biashara na masikini mwenzako, huwezi kuendelea, miaka yote utakuwa masikini. Tuelekeze nguvu zetu Congo. Congo kuna utajiri mkubwa! Tufanye biashara Congo. Tupeleke ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara kule Congo watu wafanye biashara zao, tusifanye vikwazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji. Kila mara nazungumza kuhusu maji. Hakuna Waziri anayefanya kazi kwa wakati huu kama Mheshimiwa Profesa Mbarawa, amejitahidi sana kutembea kila sehemu. Naomba aongeze ukali, tunaibiwa sana kwenye miradi ya maji. Bwawa la Fili- Namanyere, nimezungumza kila mara hapa, hata ukienda lile bwawa halizidi shilingi milioni 300, Mkandarasi akapewa shilingi milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukifanya hesabu za haraka haraka, uchukue grader na excavator zifanye kazi kwa mwezi mmoja thamani yake ni shilingi milioni 78. Hakuweka cement, hajaweka nondo, kachimba tuta; tuta lenyewe mita 100. Kokoto zenyewe hakuweka chochote. Mawe trip 100. Nimepiga hesabu lile bwawa kwa hesabu zangu za haraka haraka iko hapa karatasi, haifiki shilingi milioni 110, yeye kachukua shilingi milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri, kuna mabwawa hapa nikikusomea hapa, ni Nchi nzima. Mabwawa yaliyopo katika nchi hii, karibuni yote yana ufisadi ndani yake. Namwomba Mheshimiwa Profesa Mbarawa aunde Tume Maalum afuatilie bwawa moja hadi moja atagundua wizi wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anafoka. Siku anakwenda Mheshimiwa Rais ndio anakataa majengo, anakataa mabwawa, miradi ya maji anaikataa. Ndugu zangu, naomba Mawaziri mumsaidie kabla Mheshimiwa Waziri hajaja muanze kuwatumbua watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakusomea idadi ya mabwawa hapa ya nchi nzima ambayo ukiyapitia yote yana ufisadi wa pesa. Yaani ni mengi, ukiyapitia utapata kujua hata kule kwako labda yapo hayo mabwawa. Ni mengi ajabu, yana ukakasi wa wizi, yana matatizo na kila kitu. Naomba Wizara ya Maji iyapitie kabla Mheshimiwa Rais hajaenda akapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mabwawa ya idadi ambayo yameshajengwa Habia, Itimila, Kawa, Nkasi, Matwiga, Chunya, Mwanjoro kule Mkinga, Kilungadunga - Mkinga, Donda - Mkinga, Loliondo, Mafutela, Selewa -Kilindini na mabwawa kadhaa wa kadhaa. Ni hatari. Tunakusanya kodi kwa walala hoi lakini Wakandarasi wanakwenda kuchukua hela ambao siyo halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akija Rais katika Wilaya ya Nkansi, nitamwomba hata kwa dakika tatu akaangalie bwawa ambalo wanapiga kelele la Mfili akalione kama thamani yake kweli ni shilingi milioni 900. Tumesikia wanakwenda Mawaziri kwenye bwawa, tunamwambia asilipwe hela zake shilingi milioni 300 mpaka wataalam waje kilichunguza hili bwawa lakini walimlipa. Kaenda Mheshimiwa Waziri Kakunda kaenda kusema hili bwawa halifiki shilingi milioni 300. Tupo na RAS pale, tunazuia asilipwe Mkandarasi lakini analipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji Kirando walithamini shilingi bilioni 7.4 na cheque imeandikwa Mkandarasi apewe shilingi milioni 800 juu ya meza tukazuia. Wataalam wamekwenda ku-check ule mradi wa mamji utaona ajabu, wamegundua kwamba ni shilingi bilioni 4.6 na Mkandarasi wamempa kwa shilingi bilioni 4.6. Tumekoa shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Mweyekiti, sasa kama Namanyere ni mradi huu mmoja tu tumekuta tofauti ya shilingi bilioni tatu, miradi mingine ilikuaje katika nchi hii? Mheshimiwa Waziri, msaidieini Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kila akienda, hotuba zake za Mikoa ya kusini huko nimezifuatilia, zote zina mtatizo ya miradi miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ndege tu kupaka rangi. Wewe mwenyewe usingepaka rangi ndege. Walitaka kulipua shilingi milioni 300. Sasa kama mbele ya macho Jijini Dar es Salaam wanataka kulipua shilingi milioni 300, kule vijijini karibu na Zaire wanatulipua kiasi gani? Tunasema mpaka povu linatoka, lakini wanakaa maofisini wanaandika mikataba, Mawaziri wanasema hawawasikilizi. Mheshimiwa Prof. Mbarawa anasema mpaka povu linamtoka, Mdogo wangu Mheshimiwa Aweso amekuja kule amesema ufisadi umefanyika lakini hawachukuliwi hatua zozote, wamekaa wamestarehe, wanatuchezea akili tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu, tuonyeshe mfano. Tusisubiri mpaka Mheshimiwa Rais anakwenda kwenye miradi ndiyo anawatumbua majipu. Mawaziri fanyeni hiyo kazi. Haiwezekani sisi Wabunge kwa sababu ni wanasiasa tunaropoka, lakini ndugu zangu hesabu haidanganyi. Bei ya bomba inajulikana, bei ya kutengeneza barabara inajulikana, bei ya kila kitu inajulikana, lakini unakuta mikataba tunajiumiza wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni tajiri. Leo tungekuwa tuna uwezo wa kuzikopesha nchi za Ulaya kama Ureno, kama Spain, tuna uwezo wa kuzikopesha, lakini sisi leo ndiyo tunakopa. Ni aibu. Tuna kila kitu katika nchi hii. Tuna utajiri wa ajabu katika nchi hii. Ni sisi wenyewe tunajitafuna. Ni mikataba mibovu ndiyo inatumaliza katika nchi hii. Lazima tuiangalie mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa na mikataba halali leo nchi yetu ingekuwa na neema, ingeneemeka. Mheshimiwa Rais anafanya kazi mpaka anachoka, lakini wasaidizi ndugu zangu wamekaa maofisini, wanakula AC wanatuharibia nchi. Nimezungumza kila mara, mtu unamwona kabisa anaiba, muda wa mwezi mmoja ana jumba la ghorofa; miezi miwili ana magari matatu. Mshahara wake unafahamika; anatoa wapi hizo hela? Halafu TAKUKURU wanasema wanamchunguza, wanamchunguza kitu gani? Ushahidi upo. Hawa ni kuwatandika tu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza kabisa naunga mkono hoja Wizara ya Maji hii, kwa kuwa Mheshimiwa Prof. Mbarawa, Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu, Naibu Katibu wanafanya kazi ambayo sikutegemea. Mheshimiwa Prof. Mbarawa anafanya kazi kama vile Mhandisi anapita mpaka anachimba mifereji yeye mwenyewe kwa mkono wake, sijaona Waziri anafanya kazi kama Prosefa kwa vitendo. Lakini tatizo wanaomuangusha ni wafanyakazi wake, watendaji wake, namwambia ukweli awe mkali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua mfano Namanyere, nimezungumza sana kuhusu Namanyere mpaka sasa Namanyere wamepata maji asilimia 15, hata huo mradi uliokuja Mheshimiwa Profesa Mbarawa huo mradi wa sasa Namanyere wapata asilimia 46 katika Mji wa Namanyere ambayo siyo kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kawaida mijini lazima wapate maji asilimia 86 mpaka 85, lakini pamoja na huo mradi mpya Namanyere wamepewa Mkandarasi watapa maji asilimia 46. Kwenye kitabu chako hiki ukurasa 146, umeandika imetengwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kupeleka umeme kwa ajili ya mradi wa Bwawa la Mfili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa umeme umeshafika na transfoma ipo angalia wasikupige changa la macho pae tulipohitaji ni mtambo wa umeme mashine, pump ya umeme kwenye Bwawa la Mfili. Nakuomba vilevile Mheshimiwa Waziri Mkandarasi aliyepewa bwawa la Mfili na mtaalam anayeshiriki kumpa lile Bwawa la Mfili kawatapishe pesa mara moja. Haiwezekani ile bwawa thamani yake ifike milioni 900, wakati ukipiga hesabu za haraka haraka lile bwawa haifiki hata milioni 300, haiwezekani lazima ufanye jitihada kwa uwezo wako ninavyokuamini lazima mkandarasi apanue lile bwawa au atapike zile hela moja, hamna kuonea huruma! Wamezidi kuchakachua kwenye mabwawa haya mabwawa ya maji wamezidi nchi nzima nilikuambia unda tume ufuatilie mabwawa ya nchi nzima kuna uchafuaji wa hali ya juu, miradi ya maji wageuza kama ndiyo vichaka vya kuibia pesa katika nchi hii haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza Bunge la Awamu ya Nne hapa wanaandika kabisa Ofisini wamekaa Ofisini anaandika neno kodisha gari kutoka Namanyere kwenda Dar es Salam kwa shilingi milioni 14 wakati gari milioni tatu, nimepakia mabomba ya shilingi milioni 98, Mheshimiwa nilidai, hakuna mabomba waliyopakia wala hakuna gari iliyokuja Namanyere. Anakaa Ofisini anakula hela kijanja kijanja, wafuatilie wote, Wakandarasi wameshirikiana na Maofisa wako kuiba hela za miradi ya maji, unda tume, kagua mradi kwa mradi ninavyokuamini upitie nchi nzima watapike pesa mara moja. Hakuna huruma kuwachekea chekea, wengine wamejenga maghorofa, wengine wamenunua majumba kwa ajili ya miradi ya maji katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ninao, maana yake walitaka kunihonga na mimi nikawakatalia, shahidi na Mbunge wa Chemba Ndugu Nkamia walikuja mpaka Bungeni hapa, nikawaambia mimi sihongeki wananchi wangu wamejipanga foleni kunichagua niwatetee, leo Namanyere hawana maji, mnipe pesa wananchi waangamie, kupata maji kwa ajili ya utamaa tamaa, wako kwa majina, hakuna kufichika, Mradi wa Maji Kirando kabla hujakuwa Waziri walikula shilingi milioni 201 Kirando hakuna kitu kilichotengenezwa.Walijenga vizimba 18 na wakanunua pump moja kwa shilingi milioni 200 waliandika certificate za uongo hela wanachukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimwambia Waziri aliyeondoka mbele ya bwawa na RAS ambaye leo ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI, anafahamu alikuwa RAS Sumbawanga; tukamwambia usiwalipe hawa pesa iliyobaki shilingi milioni 300 kwa sababu hili Bwawa la Mfili lazima likaguliwe, lakini walilipwa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huyo Mkandarasi kama yupo hajafa atapike zile hela, akapanue Bwawa la Mfili…(Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipe taarifa..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakajoka taarifa.

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsikia nataka kumpa taarifa Mhehsimiwa Mjomba wangu Keissy pale, anasema kwamba fedha zote hizo anazozitaja zimeliwa na wakandarasi, zimeliwa na watu ambao ni watendaji wa Serikali kwenye Jimbo lake la Nkasi. Lakini namshangaa sana kwa sababu mimi najua kabisa Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kumaliza mafisadi nchini, sasa hizo hela wanakulaje wakati mafisadi tumeshawamaliza kabisa katika nchi hii?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona mjomba wangu amekwenda vibaya, hivi mafisadi wamekwisha, juzi walitaka kuiba hata za ndege hapa juzi, wewe huna habari, kupaka rangi ya ndege tukasema shilingi milioni 300 wamekwisha mafisadi! Hata humu Bungeni wako mafisadi watakwisha wapi mafisadi. Mafisadi watakwisha labda mwisho wa dunia ndiyo wataisha mafisadi, nani kakuambia, mjomba uwe macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji kadhaa katika Jimbo la Nkasi Kaskazini ukianzia Masoro, Kata nzima ya Mkwamba kule Riele, Itindi, Tambaruka, Swaila hawana hata visima vya maji, Kakoma, Lunyala hakuna hata visima wananchi wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuomba ndugu yangu hata angalau kisima kimoja kimoja katika vijiji vyangu hawana kabisa maji; maji ni uhai nakuelewa kwa sababu unatenda kazi, unafanya kazi, unakemea uovu, nimekuona kwa macho yangu sasa jitahidi kuwabana kabisa fukua makaburi, wameiba miaka ya nyuma mjomba wangu, labda kwako Tunduma kama hawajaiba, wameiba sana hawa watu wa maji bila kuwaonea huruma wameiba sana; walikuwa wanapeana kijomba kijomba tender kama ufahamu wewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapewa tender ana- raise certificate kazi haifanyaki hamna kazi, Namanyere kwa ushahidi kabisa wewe uliona wapi mjomba kazi itoke gari Dar es Salam mpaka Namanyere unapajua Namanyere, gari fuso shilingi milioni 12 uliona wapi wewe! Ni kwenda Lubumbashi na kurudi! Nilidai risiti ya hiyo gari haikuonekana kwa nini tusifukue makaburi mnaogopa kitu gani? Ushahidi upo, mabomba sikuona nimekwenda kwenye Full Council nadai mimi risiti kwa yule mtu wa maji haoneshi. Gari liko wapi, nioshe gari, nipe namba ya gari haoneshi, nikaenda TAKUKURU hamna kitu jamani, tufanyaje nchi hii, tumsaidie Rais.

Mheshimiwa Profesa Mbarawa ninakuamini unda tume pitia mabwawa yote nchi nzima, miradi ya maji nchi nzima utakuta ufisadi wa hali ya juu. Tunashida ya maji kweli Serikali inaleta pesa, lakini wapi hakuna chochote, hakuna chochote, mfano najua Namanyere, uende Namanyere wewe mwenyewe unafahamu Mheshimiwa Waziri, juzi uliunda tume, wakaja Namanyere mpaka Kirando ulikuwa mradi wa shilingi bilioni 7.4 baada ya kuleta wakandarasi wapya na watu wa tume, mradi umegundulika bilioni 4.6 wewe mwenyewe shahidi. Kabla hujakuwa Waziri ule mradi ulikuwa umeshaibiwa hela, ulikuwa umeshaibiwa shilingi bilioni 7.4, ulipokuja Waziri ukataa nikakushawishi wewe ukakataa ukasema huu mradi haiwezekani tutume watu wa kwenda kule. Tumegundua ule mradi ni shilingi bilioni 4.6 tumeokoa shilingi bilioni tatu, Mheshimiwa sasa tutasema namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawambia Waziri yuko Waziri mmoja nikimtaja itakuwa aibu, akanambia utajuaje haya mambo Mheshimiwa Keissy, nikamwambia nitakushtaki kwa Mheshimiwa Rais wewe nyamaza kimya, akanyamaza kimya, naweza kumtaja. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Mtajeee!.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Anajijua, alinitisha humu Bungeni, Waziri mmoja alinitisha Bungeni wewe usiingilie mambo ya utaalamu, unajuaje utaalamu nikamwambia mzee hata kipofu atajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Prof. Mbarawa nakuamini, unda tume pita kila kijiji, pita kila mkoa siyo kama Waziri wengine unamletea taarifa anakwambia unajuaje, kwani mimi ni sanamu nisikose kujua, nikose kujua mimi? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumtishia nitakupeleka kwa Mheshimiwa Rais akatetemeka, unakuwa Waziri tukikwambia wewe unasema Mbunge utajuaje unashirikiana na mafisadi haifai kuwa hata Waziri wewe, bora utumbuliwe tu. (Kicheko)

WABUNGE FULANI: Mtajeee!

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, huku nyuma. (Kicheko)

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Keissy angetutajua tu na sisi tumjui bwana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy naomba uendelee.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tutamtaja hata Mheshimiwa Rais akiniita faragha nitamtaja, si anasikia Mheshimiwa Rais nitamtaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu hii miradi ya maji tumsifu Mheshimiwa Prof. Mbarawa maana yake anafanya kazi kwa vitendo, Mheshimiwa Aweso anafanya kazi kwa vitendo na wasaidizi wake wanafanya kazi kwa vitendo, naomba muendelee na msikubali makadirio wanawaletea ya uongo uongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashauri angalia certificate wanazoleta lazima mzipitie, siyo wanaandika certificate mnazipitia haraka haraka mnalipa hela, wakati mwingine ni hewa, ni unafiki ulikwenda Mheshimiwa Waziri ulikuja kule Mradi wa Kata ya Isale tangu umeondoka mpaka leo kama siyo ....DC, DC ndiyo amekuwa kama mkandarasi wa Nkasi anahamasisha wananchi wachimbe mtaro ili walipe yule mkandarasi, yeye hafanyi kazi yoyote, angalieni certificate hizi na nimeshukuru kwa sasa nasikia sheria imebadilika mkimpa mtu mkandarasi kwanza afanye asilimia 30 ya kazi ndio alipwe pesa, hiyo ndiyo sheria nzuri, sio mnaanza kumlipa hela mkandarasi ajaanza chochote hayuko kwenye site anakula pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nikuombe Mheshimiwa Waziri nakuambia ukweli Mradi wa Maji Kirando alikula makandarasi shilingi milioni 201 lazima azitapike, amejenga tu vizimba 18 na kila kizimba kimetumia mifuko mitano ya cement na aliyekula hela za mradi wa Bwawa la Mfili lazima atapike huyo mkandarasi lazima maana yake yeye ndio aliyemshawishi yule mtu akaandika pesa kama waligawana sisi hatujui nataka kujua kazi yetu ya Namanyere, wana Namanyere wana shida ya maji hawapati maji chini ya asilimia 16 mzee, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkansi ina eneo kubwa sana la Ziwa Tanganyika na kuna aina nyingi za samaki na hata dagaa, lakini wavuvi wengi karibu wote hali zao ni mbaya sana hawana zana bora za uvuvi kabisa. Wavuvi wengi au karibu wote ni raia kutoka DRC-Congo ndiyo wanaofaidika na maliasili ya Ziwa Tanganyika, maana Vijiji karibu vyote vya mwambao mwa Ziwa Tanganyika upande wa Tanzania ni wavuvi kutoka DRC-Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kuna halali gani Wakongo kuwa upande wa Tanzania bila hata uhalali wa kukata leseni zinazostahili wageni toka DRC-Congo? Naomba Wizara yako ichukue hatua kwa wageni wote wanaokwenda kinyume, pia wale waliopewa majukumu huko. Nadhani wanafanya kutotekeleza sheria kwa ajili ya kupewa chochote na hao wavuvi wageni. Hata uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zilizopigwa marufuku mwambao mwa Ziwa Tanganyika wamezagaa Tanganyika karibu kila kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi kuna mapori shamba kama vile waliohodhi hawayatumii na walipata kwa kuwarubuni Wenyeviti wa Vijiji, wakati hakuna sheria wao kutoa ardhi zaidi ya hekari 50. Unakuta kuna mashamba pori ya hekari 100 na kuendelea. Mfano; shamba la Kowi, Kalumwalwedo,shamba la Msomali Tatumbila, shamba la Mastar Mashete, mashamba yote hayo yalipatikana kwa vijiji kukiuka sheria ya uwezo wao wa hekari 50 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna baadhi ya wafugaji walipewa block katika shamba, yaani Ranch ya Kalambo lakini hawajapeleka mifugo na wanakodisha hizo block tu, Wizara ikalitazame upya na kuwapatia wafugaji wenye ng‟ombe.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi haipati matangazo toka TBC redio hasa wananchi wanaokaa mwambao wa Ziwa Tanganyika, naomba Wizara yako iweke mnara wa kuongeza nguvu Redio Tanzania, Namanyele - Nkasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matangazo ya Bunge live; mimi nashauri liwe linaoneshwa siku ya Jumamosi saa tatu usiku kwa sababu mchana watu wote wako kazini wanatafuta riziki na sababu ya pili wanafunzi na walimu wao wako kazini na masomoni mchana hawana muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu hata ukichunguza mji kama Dar es Salaam kila mtu yuko na shughuli zake siku nzima hawana muda wa kuangalia tv mchana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya nne ni kwamba madereva wote wa magari ya abiria, malori, daladala na abiria zao wako safarini. Wapi nafasi wanayo? Tuache ushabiki, wanaotaka kuuza sura zao wakaombe kazi kwenye vituo vya tv.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla tuna pori la akiba la ukubwa wa kilometa za mraba za 6,462.26; pori la akiba la Rukwa ukumbwa wake kilometa 4,194 na pori la Rwamfi kilometa 2,228.26 hilo pori linahujumiwa sana na majangili yaani wawindaji haramu ni kwa kuwa hilo pori la akiba limepakana na nchi jirani inakuwa vigumu sana kwa wafanyakazi wa idara kwa sababu hawana magari ya doria. Niliahidiwa kupewa gari jipya na Waziri wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Nyalandu lakini mpaka leo sijapokea hilo gari kwa ajili ya kuokoa mali kwa ajili ya wanyama na miti. Tafadhali hilo gari ni muhimu kwa doria na pia kwa upande wa Ziwa Tanganyika, kwa hiyo, usafiri wa majini ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ahadi ya aliyekuwa Waziri Mheshimiwa Nyalandu itekelezwe maana pori hilo la akiba linashambuliwa sana na wafugaji na majangili na wakata mbao. Naomba jibu kabla ya mwisho wa Bunge la bajeti kuhusu hilo gari maana ahadi ni deni na dawa ya deni ni kulipa, pori linaangamia sana sana.
Mheshimiwa Waziri gari jipya ni muhimu sana kwa ajili ya doria ya hilo pori.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ALLY M. KESSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Waziri Mheshimiwa January Makamba, binafsi kwa ziara yake katika Jimbo langu la Nkasi Kaskazini na kusaidia sana kuelimisha wananchi na baadhi ya Madiwani ambao wanajali maslahi yao ili wananchi wazidi kuharibu mazingira katika vyanzo vya maji na Msitu wa Fili ili tuwe na shida ya maji Namanyere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, nataka kujua mpango wa kupunguza utoaji wa maji katika Ziwa Tanganyika umefikia wapi na lini utakamilika wa Nchi za Burundi, Zambia, DRC – Congo na Tanzania. Umefikia kurudisha kibanio katika Mto Lukuga uliopo DRC – Congo ili maji yasizidi kwisha ziwani na kuhatarisha viumbe hai. Kwa sasa ziwa linapungua sana tena sana kuanzia 1960 mpaka sasa ziwa limepungua zaidi ya mita tatu za maji alama ziko sehemu ya mawe yaliyokuwa karibu na ziwa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami nimepata muda wa kuchangia Mpango wa Maendeleo wa 2020/2021. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Ndugu Dotto na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha. Kusema kweli wanakusanya fedha jinsi inavyotakiwa, lakini nasi Wabunge ndio tunapanga matumizi hapa. Matumizi yanakwenda jinsi inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kidogo, mtaniwia radhi Waheshimiwa Wabunge. Sisi Wabunge lazima tuwe na uchungu na nchi hii kwa sababu, tumeletwa na kura za wananchi ambapo tulikotoka huko wana matatizo ya maji, tunadai barabara mbovu, tunadai sijui TARURA wapewe pesa, sijui nani apewe pesa. Nasi Wabunge vilevile ndugu zangu, tuwe na moyo wa kumsaidia Waziri wa Fedha kuhusu matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku mimi nakwenda kwenye mazoezi kasoro Jumapili, lakini Waheshimiwa Wabunge hawa; humu ndiyo kuna Kamati za Michezo, Mwenyekiti wao yuko Mheshimiwa Ngeleja na ataniunga mkono mwana-mazoezi mwenzangu ambaye kila siku tuko naye kwenye mazoezi Mheshimiwa Naibu Spika atasema ukweli lillah hapa leo Jumatatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wako wanakuangusha. Hawaendi kwenye mazoezi hata mara moja. Ni wachache sana. Wanakwenda kwenye mazoezi wakisikia kuna safari, kwa sababu wanafuata maslahi. Hawaoni huruma na wananchi waliowaacha kule Majimboni kwetu hawana maji wala chochote. Leo nimeshuhudia, wamesikia kuna safari ya kwenda Uganda, wamejazana kule Jamhuri Stadium kwa makundi, sio akina mama wala akina baba. Mimi nimewaambia, leo naenda kuwachafua Bungeni, naenda kusema ukweli Bungeni, mmezidi nyie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anakusanya fedha, huwezi ukamtuma mtoto wako akutekee maji kwa kutumia msege. Akutekee maji kwa kupitia msege au kajungio, maji hayawezi kufika. Sasa ni baadhi ya Wabunge hawa, ni sawa na msege, sawa na chujio la kuchujia chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama ndiyo mhimili wako, sisi ni mhimili, lazima tuchunguze safari za Wabunge kwa michezo wanapokwenda nje. Watatuletea aibu kubwa, kwa sababu huwezi kwenda kucheza mpira huna mazoezi; huwezi kuvuta kamba huna mazoezi; au kucheza netball bila mazoezi. Hii lazima tuchunguzane ndugu zangu. Siyo tunapiga kelele hatuna maji, hatuna barabara, hatuna umeme wakati nyie mnatanua, mnakwenda kustarehe huko. Hamna faida yoyote kwenda nje. (Makofi)

(Hapa, baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia sasa. Mheshimiwa Waziri nisikie vizuri, wewe umetoka katika Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma umepakana na DRC Congo. Katika nchi tajiri katika ukanda wetu ni DRC Congo. Lazima akili yako, macho yako, Wizara yko ielekeze kufanya biashara na DRC Congo kupitia Ziwa Tanganyika. Lazima tuunde meli pale kubwa ya kupakia ma-container kupeleka Miji ya Kalemii, Uvira, Moba na Bujumbura kupitia reli ya kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma enzi ya Mwalimu Nyerere tulikuwa na meli ya mafuta pale, inapeleka mpaka Zambia kupitia Bandari ya Kigoma, leo hakuna kitu. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, yeye anatoka Kigoma, anafahamu kabisa, DRC Congo mzee ndiyo nchi pekee tajiri katika ukanda huu wa kwetu na ina watu wengi na kila kitu. Tushirikiane na DRC Congo, ukikaa chini ya uaridi utanukia kidogo. Utafanya na masikini mwenzako, utapata kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima akili yetu ielekee DRC Congo kufanya biashara nao. Tusidanganyane hapa, Congo ndiyo pekee inayoweza kutuokoa. Leo nasikia kuna ujumbe mkubwa toka DRC Congo uko Uganda kule, wafanyabiashara wa DRC Congo. Nasi tuelekeze nguvu zetu kule, itatuokoa ile nchi…

MWENYEKITI: Wanataka kujenga barabara ya kilometa 1,000 kutoka Uganda kwenda DRC Congo. Uko sahihi Mheshimiwa, endelea.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, tujitahidi. Vilevile wafanyabiashara wetu wote, leo wanachukua ma-container China, biashara ni China. Cha ajabu kule China kabla hujatoa container kuna inspection, unaacha dola 1,000 kukagua eti bidhaa zao. Wakati wanatengeneza wenyewe! Ukifika Dar es Salaam tena, TBS wanakagua ile bidhaa, wanalipa dola 1,000 kule. Sasa sijui kama Wizara ya Fedha inafahamu hiyo dola 1,000, inarudi ngapi katika nchi yetu? Inachukuliwa China yote, kwa maslahi gani wakati tunanunua bidhaa kutoka China zao wenyewe, ulipie container? Ma-container mangapi kwa mwezi yanakuja Dar es Salaam? Tunapoteza shilingi ngapi? Dola ngapi tunapoteza kwa kila container kwa ma- container yanayoingia nchini kwetu kutoka China?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila container, uliza vijana wafanyabiashara wa Kariakoo, lazima waache dola 1,000 wanaita inspection kule China. Ukifika Dar es Salaam, lazima hilo container tena TBS wachukue pesa. Sasa tutafanyaje biashara, wanatuchukulia dola 1,000 Wachina kila container, wakati tunanunua bidhaa zao wenyewe? Je, kama hiyo dola inakuja kwetu Tanzania, tunajuaje kama inakuja yote dola 1,000 kwetu Tanzania? Lazima tuwe macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa ma-container nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri, lazima nipate majibu haraka sana kuhusu hiyo, kama wanakagua ma-container yetu au namna gani. Kuhusu Bandari ya Kigoma, imekufa, haina maslahi kabisa, imekufa Bandari ya Kigoma. Ukifika pale wanakula tu mishahara. Lazima tuifufue kwa ajili ya kusaidia kwenda Bujumbura na Kalemii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani ni kitu cha ajabu kusema kweli, tunaacha hela. Sisi bandari yetu tumezungukwa na nchi, tumezungukwa na Zambia, Malawi, Burundi na Rwanda. Akili yetu yote kwa sasa tuhakikishe bidhaa zote za kwenda Malawi, Zambia, Mashariki ya DRC Congo, Burundi na Rwanda zinapitia katika nchi yetu. Lazima akili yetu ilenge hapo. Akili yetu ilenge bidhaa zote za kwenda Rwanda, Burundi, Mashariki DRC Congo, Zambia na Malawi, lazima zipitie kwenye bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Tunduma pale lazima tufanye mikakati kupanua barabara. Msongamano wa magari ya pale Tunduma lazima tuupunguze ili biashara iende haraka haraka pale Tunduma, siyo gari inakaa siku tano, siku sita au saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fanya ziara, nenda pale Tunduma, utaona huruma. Magari yanalala mpaka 1,000 au 1,500. Sasa hii biashara mzee, nchi lazima tuwaze biashara. Haiwezekani kuweka magari mpaka 1,000 pale Tunduma kwa muda mrefu. Kuna malori ya mafuta, ukitokea moto pale Tunduma, mji mzima utaungua. Mji mzima wa Tunduma utakwisha. Malori yanayojaa Tunduma pale ni ya ajabu, msongamano ni wa ajabu, kwa nini msifanye taratibu za kuvusha magari haraka haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtafute mpaka mwingine kutoka nje ya Tunduma kule yapite magari, custom waongeze, tupate hela haraka haraka, tunakawaiza biashara. Ndiyo maana sisi Watanzania ukiambiwa saa 3.00 uje unakuja saa 5.00; ukiambiwa uje saa 6.00 unakuja saa 9.00. Hatuendi namna hiyo. Ukiambiwa saa 6.00 iwe saa 6.00. Kama hujafika saa 6.00 unaachwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuamke tufanye biashara. Sasa ni kipindi cha kufanya biashara. Tumwige Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli anataka mambo ya papo kwa papo. Aliyofanya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli hakuna mtu aliyetegemea, miradi hii ya kujenga reli ya mwendokasi, mambo ya umeme nani alitegemea? Kununua ndege haraka haraka, nani alitegemea? Inataka uamuzi wa ujasiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, unatamka kabisa wewe mkuu wa chama kabisa mwenyekiti wa chama au katibu wa chama unamuhusisha Rais Magufuli na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakati kila siku kwenye redio na television Rais anahamasisha wananchi chagueni kiongozi yeyote akiwa wa CCM akiwa CHADEMA, ACT Wazalendo chagueni; anatamka mwenye Mheshimiwa Rais;leo utamsingiziaje Rais anaingia kwenye mchakato wa uchaguzi, anahusika wapi?Pambaneni na Tume ya Uchaguzi, hamasisheni wenyewe huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wenyewe wameshachoka,kazi anayofanya Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli inaonekana, sasa mgombea gani atakwenda kugombea kwenye chama kingine aonekane? Wenyewe walikuwa wanadai ufisadi amepigana na ufisadi amemaliza, amewabana watu wote, amefungua mahakama ya ufisadi. Kila kitu walichokuwa wanadai kwenye mikutano ya hadhara Mheshimiwa Rais katanguliza mbele; sasa hawana hoja, hakuna hoja.

Mheshimiwa Spik, jana Mheshimiwa Waziri Jafo kawaambia, jamani hamna kuweka mpira kwapani, wote nendeni kwenye uchaguzi. Sasa mnataka kudai tume huru hiyo tume huru utaitoa wapi?Mbinguni kwa malaika? si binadamu wetu hawa hawa? Kwahiyo ndugu zangu hakuna haja ya kubabaika, tarehe 24 twendeni kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu zingine kama kule Nkasi chama kama cha CUF wala hukisikii kabisaa!Wala hatukijui kabisaa!Sasa nashangaa unasimama hapa unasema fomu zetu sijui umetunyima sijui zimefanya namna gani; nani anayekufahamu? nani anakujua?Ni mambo ya miujiza kabisa.

Ndugu zangu tusisingiziane mengi twendeni kwenye uchaguzi. Mambo yalijionesha mapema kabisa; madiwani wangapi wamehama, inajulinana, Wabunge wangapi wamehama, wenyeviti wangapi waliacha kazi. Sasa ninyi wenyewe mnavyojiona na mnavyojipima mmeona hamna hoja. Mmebaki wachache ndugu zangu, mti unaokauka hata ukiumwagia maji mizizi imeshakauka, hauwezi kustawi

MHE. MCH. PETER S. MSINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

SPIKA: Mchungaji unamnyanyukia Mheshimiwa Keissy?

MHE. MCH. PETER S. MSINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe taarifa tu.

T A A R I F A

SPIKA: Haya mpe taarifa.

MHE. MCH. PETER S. MSINGWA: Mzungumzaji anayezungumza kwamba kuna vyama vingine havipo kwenye maeneo yake; inawezekana kweli vyama vingine havipo kwenye maeneo yake lakini vyama vingine vipo. Isipokuwa nataka nimjulishe kwamba malalamiko ambayo wengine wanayatoa hapa; mfano mzuri ni mimi mwenye pale Jimboni kwangu Kata ya Gangilonga tangu siku ya kuchukua fomu ilifungwa mpaka mwisho mtendaji anaondoka; haijawahi kuchukuliwa fomu hata moja, hayo ndiyo malalamiko nilitaka apate taarifa; na maeneo mengine ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema, hatukimbii uchaguzi tunataka tuwe na uwanja fair.

SPIKA: Mheshimiwa Keissy unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa, siipokei taarifamaana clipya Mheshimiwa ninayo. Alipokwenda Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kule kwake Iringa alimsifu vibaya. Kwamba nakushukuru Mheshimiwa Rais miradi yote naiona Mheshimiwa Rais, kwahiyo sisi hatuna tatizo lolote. Clip yako tunayo Mheshimiwa na inatembea Mheshimiwa; wewe mwenyewe Mheshimiwa ulimpongeza Mheshimiwa Rais kwa hali na mali ulimpongeza Mheshimiwa sasa sijui kama wananchi wako watakuelewaje Mheshimiwa

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko nimekuona, taarifa.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kumpa taarifa ndugu yangu Keissy, na mimi nakubaliana naye, kwamba kwa mfano Jimbo la Kakonko yule aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Chiza kwenye by-election na timu yake yote wamerudi CCM leo. Kwahiyo ni kweli hawana wagombea. Nilitaka tu uwe na amani katika jambo hilo.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy muda umeisha.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa, anayosema unaona anayadhihirisha kabisa napokea taarifa Mheshimiwa Msigwa mwenyewe clip yake inatembea kabisa anaiona; sijui kama alikuwa si Msigwa huyu au namna gani, kavaa hivi hivi kila kitu na suti. Sasa nadhani clip yake labda nitamkumbusha, nitakutumia clip in box, labda utaisikiliza vizuri. Wewe mwenyewe ulikiri kwamba awamu ya nne imefanyakazi.

SPIKA: Awamu ya tano.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Awamu ya tano imefanyakazi nzito. Jana nililala Iringa kwa Mheshimiwa hapa, hata uchaguzi watu wamesharidhika, watu wamesharidhika Mheshimiwa Msigwa umebaki peke yako, usione aibu kurudi Mheshimiwa Msigwa rudi haraka tunakuhitaji. Ahsante sana nashukuru sana. (Makofi/ Vigelegele)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie. Mimi mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tupo humu na baadhi ya Wabunge wapo humu hawajamaliza hata jimboni kwake kutembelea vijiji. Lakini Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake wametembea kila jimbo katika nchi, kila kona na wakati huo huo nao ni Wabunge na wana majimbo yao. Wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaishia Dodoma - Dar es Salaam, hawaendi kwenye majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa moja ametoka kuzungumza hapa, wa Kamati ya Madini, kwenye kamati yetu; yeye hahudhuri vikao, ni kesi mahakamani kila siku Dar es Salaam, na yeye ananiambia Mheshimiwa Keissy mpaka hela nimeishwa, anajijua. Ametoka kuchangia hapa kwa hasira na kwa kupiga kelekele lakini ukienda kwenye record katika Kamati si mhudhuriaji.

Mheshimiwa Spika REA peke yake Tanzania tuna vijiji 12,268 vinawekewa umeme. Leo anazungumza kwamba wananchi hawajapata umeme nchini; labda kwake jimboni kwake; lakini sisi tunashukuru sana; majimbo yetu ya kule Mkoa wa Rukwa na Katavi ilikuwa ni mwisho kabisa wa nchi hatukuwa na umeme, hata mara moja kwenye vijiji vyetu. Kuna sehemu ambazo hazina hata barabara lakini REA wamepeleka nguzo na wanaendelea kufanyakazi na wananchi wanapata umeme.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Heche hawezi kusema Wizara haijafanya kazi, Wizara imefanya kazi; wewe ni jela na wewe, na kwasababu haudhurii vikao, kila siku Mahamani Dar es Salaam; na hiyo itaku-cost kwenye jimbo lako.

Mheshimiwa Spika, hii sekta ya nishati na madini ndiyo itakayotusaidia sana kwenye Serikali yetu, kwa sababu hatuwezi kwenda kwenye viwanda kama hatuna umeme, haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, umeme ndiyo nguzo kubwa ya viwanda, huwezi kujenga kiwanda bila umeme, na serikali ina umeme wa ziada na huu umeme wa Grid ya Taifa; ndiyo sababu Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma tunauomba kwa sababu serikali inapata hasara sana kwa mafuta. Ifanye jitihada ipeleke umeme wa Grid ya Taifa kwenye mikoa mitatu; kwa sababu Serikali na TANESCO inapata hasara kila mwezi mabilioni ya fedha kwa kutumia mafuta. Kwa sababu tutaokoa; kwa sababu kuna mpango kabambe wa Serikali wa kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa kwenye mikoa yetu hivi karibuni. Serikali mpaka ikifikia mwaka 2021 itamaliza vijiji vyote katika nchi hii kupelekewa umeme, lazima tushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Madini vilevile amesaidia sana; ametembea nchi nzima, kila kwenye mgodi anafika na wamesaidia sekta ya madini mpaka sasa kuongeza pato la Serikali. sasa nashangaa anasimama hapa Mheshimiwa anasema sekta ya madini inazidi kushuka chini. Chukua data kwa Mheshimiwa Waziri, chukua data Wizarani kiasi gani tangu wewe umeingia ubunge mpaka leo hii ni kiasi gani cha pesa kimeingizwa? Wizara ya Nishati na Madini imeigiza kiasi gani? Mheshimiwa lia na lwako.

Mheshimiwa Spika, kama jimbo langu hakuna hata kijiji kimoja kitakosa umeme mpaka mwezi Juni, 2020. Vijiji vyote katika jimbo Nkasi Kaskazini vitapata umeme sasa nashangaa.

Mheshimiwa Spika, Wizara imesaidia sana Mheshimiwa Waziri. Nguzo tulikuwa tunaagiza nje, transformer tunaagiza nje, waya tunaagiza nje kila kitu tunaagiza nje; leo vyote vinatoka ndani ya nchi yetu. Tumeokoa kias gani fedha z kigeni katika nchi yetu? Hatupotezi hata senti tano kwaajili ya mambo ya umeme, vyote vinazalishwa katika nchi yetu na watu wanapata ajira katika nchi yetu. Tulikuwa kila siku tunaagiza nje, leo ndugu yangu unakaa unaiponda Wizara ya Nishati na Madini badala ya kuwasifu! Acha!

Mheshimiwa Spika, tumeingia gharama bilioni sita kwa ajili mradi wa Nyerere kule ili tupate umeme wa kuendesha reli yetu inayotumia umeme; leo unashindwa na ku-suport Serikali? Lia na lwako Mheshimiwa. Ukiona namna hiyo ujue sasa; Mheshimiwa Heche nakuonea huruma rafiki yangu, wewe ni rafiki yangu sana; wewe wasema hali ni mbaya. Ninyi wenyewe mnasema kujenga smelter ni miaka miwili; Chama chao kina miaka 28 hata ofisi hawana. Miaka 28 unasema sawa nyumba ya kawaida wewe kujenga kiofisi unatumia block 3000 na bati hakuna ukuchojenga miaka 28,…(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Keissy!

MHE. ALLY K. MOHAMED: … hakuna, wanapanga kaofisi pale kwenye kanyumba ka kulala pale Kinondoni...

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa…

SPIKA: Mheshimiwa Keissy!

MHE. ALLY K. MOHAMED:… Makaburini pale, hata pa ku-park gari hakuna…

SPIKA: Mheshimiwa Keissy, Mheshimiwa Keissy kwa kweli kama kuna aibu kwa chama cha upinzani chenye ruzuku ya mamilioni, hata ofisi ya chumba na sebule kwa kweli? Mheshimiwa Kessy endelea bwana.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, tuna shida. Hata CUF pale Buguruni wana ghorofa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Chief Whip, changamoto nyingine zichukue tu kazifanyie kazi, maana kunijibu itabidi utuonyeshe ofisi ilipo. Mheshimiwa Keissy tumsubiri Chief Whip atutajie ofisi yao iko wapi? Taarifa atupatie.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Eeh!

Mheshimiwa Spika, iko pale Ufipa Street, tena…

SPIKA: Ngoja kidogo basi atulie halafu uongee

MHE. ALLY K. MOHAMED: …karibu na makaburi pale Kinondoni.

SPIKA: Ngoja kidogo Mheshimiwa Keissy, unataka kuonywesha ofisi ilipo. Mheshimiwa Ester endelea.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, CHADEMA ina ofisi zaidi ya moja. Tuna ofisi kwenye kanda zetu na hatujapanga; na kwa ruzuku hiyo hiyo na tunaitumia vizuri. Tofauti yetu sisi na ninyi…

MBUNGE FULANI: Mwongo!

MHE. ESTER A. BULAYA: …mlirithi majengo ya Umma enzi ya Chama kimoja. Sisi tumejenga wenyewe na tuna mkakati wa kujenga ofisi hapa Makao Makuu ya Dodoma nyingine ya kisasa bila kutumia…

MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba tusikilizane. Naomba tusikilizane Waheshimiwa. Taarifa hiyo anapewa Mheshimiwa Keissy. Mheshimiwa Keissy!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, taarifa siipokei maana yake Sabodo mwenyewe aliyewapa shilingi milioni 100 wajenge ofisi, lakini hawakujenga hata msingi. Sabodo aliwapatia shilingi milioni 100 na kwenye TV mlichangia pesa…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: nanyi akina mama mnakatwa kila mwezi shilingi 1,200,000/=, zinakwenda wapi? Nyie wenyewe mnakuja kuniambia Mheshimiwa tutetee, tunakatwa hela!

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, taarifa, taarifa!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Utanipaje taarifa wakati nyie wenyewe mmeliwa hela za Sabodo…

SPIKA: Naomba tusikilizane. Mheshimiwa Dkt. Mollel, tafadhali.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa mzee wangu mzuri sana, Mheshimiwa Keissy kwamba asipate shida, aendelee na msimamo huo huo kwa sababu mwenzetu pale amepata kile cheo. Alianzisha harakati ya kudai shilingi bilioni 13 ambazo hazionekani za CHADEMA. Kwa hiyo, mwisho wa siku akahongwa hicho cheo, ndiyo sasa hivi anapambana kukitetea ili asiendelee kudai shilingi bilioni 13. (Kicheko/Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu) (Hapa Mhe.Ester A. Bulaya – Chief Whip wa Upinzani alisimama)
SPIKA: Mheshimiwa Ester wewe ni Chief Whip unajua taratibu, kwamba taarifa hiyo anayepewa ni Mheshimiwa Keissy. Kwa hiyo, mwache mwenye taarifa yake kwanza aipokee au aikatae. Kwa hiyo, tunarudi kwanza kwa Mheshimiwa Keissy aliyepewa taarifa. Mheshimiwa Keissy
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa kwa sababu CUF wana ofisi Magomeni inajulikana, ni ya ghorofa pale Buguruni; TLP wana ofisi pale Magomeni; NCCR wana ofisi pale Pangani…

MHE. JOHN W. HECHE: Mnaruhusu hii nyumba ya Watanzania inafanyiwa hivi!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, sasa ile Ofisi pale jina la Ufipa lile makaburini, ndiyo ofisi yako. Hawana ofisi nyingine Makao Makuu, iko Ufipa. Vijana wa Ufipa!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, naendelea na mchango wangu kuhusu nishati na madini.

SPIKA: Endelea Mheshimiwa Keissy.

MBUNGE FULANI: Endelea, endelea, ongea na Spika. (Kicheko)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. ALLY K MOHAMED.: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini inafanya kazi na inajitahidi katika nchi hii, tulikuwa katika giza kwenye vijiji vyetu vyote katika nchi hii, lakini wanajitahidi na itafika mwaka 2022 hakuna hata kijiji kimoja katika nchi kitakosa umeme. Vijiji vyote vitawaka umeme. Hakuna hata kijiji kimoja kitakosa umeme!

Mheshimiwa Spika, hawaelewi. Waende mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambapo hata barabara hakuna, lakini leo nguzo zinakwenda na wananchi wanapewa umeme na wananchi wanaishukuru sana Serikali na mtaona wenyewe mwaka wa Uchaguzi ndugu zangu umeme utatupa kura kwa kishindo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, umeme utakuwa ndiyo miongoni mwa mambo ya kusema nasi tutakuwa kifua mbele kutetea kura zetu katika mwaka huu; mwezi Oktoba ni umeme katika nchi yetu. Hamwezi kuyumbisha wananchi, walikuwa ni shida. Mimi mwenyewe wakati naweka umeme katika Kijiji cha Kirando, hawa CHADEMA kwenye kampeni walisema haiwezekani labda umeme utoke DRC Congo, CHADEMA hawa! Leo ni ajabu, wanaona umeme unawaka Kirando na wameona ni waongo. Wenyewe kazi ni kuzusha vitu vya uongo; wanaweza kuwa na dhahabu wakakwambia shaba ukaamini. (Kicheko)

Sasa ndugu zangu tuwe wakweli. Leo ndugu zangu nyie umeme kwenye vijiji vyenu karibu vyote vinawaka umeme. Kaskazini huko mnakotoka nyie ndiyo mlianza kupata umeme, mkajiona nyie ndiyo safi. Sasa tunagawana kasungura kadogo kila kona. Kwa hiyo, ndugu zangu msituonee wivu, mwaka 2020 Oktoba, mtaona matokeo.

Mheshimiwa Spika, wakipita huko, wanaona kila kijiji kinang‟aa. Leo ukipaa kwenye ndege mzee hata ukienda porini unaona kijiji kinang‟aa kwa umeme. Sasa ndugu zangu tuangalie mabadiliko yanavyokuwa. Miaka hii minne hakuna vijiji visivyo na umeme. Tumeweka umeme zaidi ya 8,500. Anatoa tarakimu 2,800 ndiyo sijui ni kaya sijui nyumba wala haieleweki hesabu yake kama nilivyomwambia. Somo la hesabu mzee halidanganyiki! Hesabu haidanganyiki wala mtu hawezi kuamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa watu wanazidi hesabu ya wenye umeme kwenye hizo nyumba zako.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Ina maana nyumba laki 460,000 ndiyo zina umeme katika nchi hii kwa hesabu yake Mheshimiwa!

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Nyumba 4,600 ndiyo zina umeme.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: …wakati kila kona ya nchi hii kuna umeme, kila kona…

SPIKA: Mheshimiwa Keissy! Ahsante sana, inatosha, muda wako umeisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi kwa dakika tano nizungumze kuhusu Wizara muhimu sana, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ambayo inahusiana na ushirikiano wa nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyozungumza wenzangu kuhusu Ubalozi wetu mdogo pale Lubumbashi, madereva na wafanyabiashara wetu wanapata tabu sana pale. Ubalozi mdogo Lubumbashi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchumi wa nchi yetu Congo ni muhimu sana kuliko Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuikamata Congo kwa sababu ni nchi kubwa, ina watu wengi na ina kila kitu itasaidia sana uchumi wa nchi yetu na tukiimarisha reli ya kati. Niliomba siku nyingi na nilipokuwa Kamati ya PAC tuliomba Ubalozi mdogo Lubumbashi na kama haiwezekani tumtafute Mtanzania yeyote ambaye yupo pale apewe hadhi ya kibalozi kusaidia wananchi wetu wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Muungano. Yupo Mbunge anazungumzia mambo ya ajabu kabisa kwamba tumewapunja, sheria ya masuala haya ya mambo ya nje lazima Waziri mmoja atoke Zanzibar sijui Waziri wa Mambo ya Ndani atoke Zanzibar. Ndugu zangu tuna Mawaziri watatu muhimu, Waziri wa Ulinzi katoka Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, tuna Wizara kubwa ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano chini ya Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri yupo hapa Mheshimiwa Masauni bado mnataka nini zaidi? Ndugu zangu tukitaka hivyo hata sisi tutasema, kwa mujibu wa population ni four percent. Hata mimi Rukwa nitasema tunataka Waziri maana hatuna Waziri na tuna idadi ya watu kama Zanzibar mbona hatuna Waziri hata Naibu Waziri na hatulalamiki hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuja kulalamika hata Rais akitaka kwenda nje awachukue Wazanzibari. Rais Magufuli anasema safari za nje hakuna unakuja Bungeni unataka safari za nje, hakuna tegemea pesa zako uende nje. Tusianze kuleta mambo ambayo hayatakiwi kwenye Muungano, tumeshaungana ndiyo hivyo hivyo, sasa ninyi mnataka nusu kwa nusu ndugu zangu? Itawezekana wapi? Haiwezekani ndugu yangu! Nusu kwa nusu haiwezekani! Ninyi mpo four percent mtapata four percent ya kila kitu.
Mheshimiwa Khatib tulia, usipige kelele hapa kwamba mnataka Mabalozi wengi, hapana! Nchi yote tuna Mabalozi 21 mkipata hata Naibu Mabalozi shukuru Mungu. Mheshimiwa Khatib tukikuambia ulipie Balozi mmoja tu nchi yako italipa gharama ya Balozi kule nje?
Mheshimiwa Khatib tulia, usipige kelele hapa kwamba mnataka Mabalozi wengi, hapana! Nchi yote tuna Mabalozi 21 mkipata hata Naibu Mabalozi shukuru Mungu. Mheshimiwa Khatib tukikuambia ulipie Balozi mmoja tu nchi yako italipa gharama ya Balozi kule nje?
Tulieni! Hatuwezi kwenda hivyo unasimama hapa unasema sisi tumepunjwa, hamkupunjwa kitu bado tumewasaidia. Bungeni hapa mmekuja 54, mngejaa kule Zanzibar mngeenea kwenye Jimbo ninyi Ma-CUF, mngeweza kuenea kule kweli? Tukiwaambia tu sasa hivi nendeni kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine amezungumzia ndugu yangu, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya PAC kuhusu mgonjwa kutoka Zanzibar, mgonjwa yule alipelekwa na Serikali ya Zanzibar hakuna kukanusha hapa. Nilikuwa mjumbe wa Public Accounts Committee, mgonjwa yule alipelekwa na Serikali ya Zanzibar na atahudumiwa na Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika ilisema ahudumiwe kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafahamu kwa sababu nilikuwa mjumbe wa Public Accounts Committee hesabu hizi zilikuja kwetu. Huyu bwana alipelekwa na Serikali ya Zanzibar akatibiwe kule, Wizara ya Afya siyo ya Muungano. Kwa hiyo, hili deni ni la Serikali ya Zanzibar likadaiwe huko huko, hatuwezi kulipa sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndugu zangu tusiende papara kwa habari za kutaka zaidi vyeo au namna gani na sisi tutadai vyeo. Rais anapanga Mawaziri kutokana na jinsi anavyotaka yeye huwezi kumlazimisha awape Zanzibar Mawaziri 10 au 15, ninyi kwanza kule kwenu mna Mawaziri zaidi ya 20, mna Wabunge kule kwenu hawatoshi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine na nimezungumza mara nyingi hapa, Wizara ambazo siyo za Muungano muwe mnatungoja nje tunabaki peke yetu hapa tukimaliza za Muungano ndiyo tunawaita mnaingia ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani uje kuchangia Wizara ya Kilimo inakuhusu? Wizara ya Maji inakuhusu. Kwa hiyo, muwe mnachagua Wizara za kuchangia kuanzia sasa, changia Wizara inayokuhusu basi Wizara nyingine tuachiaeni wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naipongeza Wizara, Waziri na Naibu Waziri wake pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara, pia nampongeza Mkurugenzi Mkuu wa Bandari kwa jitihada yake binafsi kwa kutangaza tenda ya kujenga Bandari ya Kabwe mwaka huu, pia kwa kujenga barabara ya kwenda kwenye Bandari ya Kipili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu maalum ni kuhusu mtandao wa simu katika Kata nzima ya Korongwe. Kata hii ya Korongwe haina kabisa mtandao wa simu wa aina yoyote ile, imekuwa ombi langu kubwa sana na mara kwa mara ombi hilo nazungumza moja kwa moja na Mheshimiwa Waziri Mbarawa na kweli anafanya jitihada kubwa sana kuzungumza na jamaa wa Halotel lakini mpaka leo hawajatekeleza na hata dalili hakuna kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ombi la Mkoa wa Rukwa kuhusu barabara ya Namanyere-Kirando kuweka kwa kiwango cha lami kwa kuwa RCC Rukwa walikwisha pendekeza na kutuma maombi barabara hiyo ya kilometa 64 ijengwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Marine Service (MSCL) wafanyakazi wake karibu wote hawajapata mishahara yao, Wizara ifikirie sana kuhusu MSCL hailipi kabisa, mishahara ya wafanyakazi mfano, wafanyakazi wa MV Liemba muda wa miezi 13 hawajalipwa chochote, je wataishi vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari ya Kirando iliyopo Wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa, kuna mtumishi wa TPA hapo wa kuchukua ushuru wa mizigo inayopitia hapo katika kijiji hicho. TPA hawajaweka huduma yoyote ile katika kijiji hicho kilichopo kando ya Ziwa Tanganyika. Kwa kuwa, wafanyabiashara wengi wanapitia hapo nashauri sana TPA kujenga bandari ndogo ya maboti katika Kijiji hicho cha Kirando.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea Mkurugenzi wa bandari atalifanyia kazi suala hilo ili kutoa malalamiko ya wafanyabiashara kulipia wakati hakuna huduma kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa nawapongeza Wizara ya Elimu hasa Profesa Ndalichako, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa kazi wanayofanya. Namshukuru sana alinisaidia hata pesa kwa ajili ya high school yangu ya Kirando kwa ajili ya kujenga mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumzia mada moja tu kuruhusu watoto walioko shuleni kupewa mimba na kurudi kusoma. Ndugu zangu hapa Bungeni akinamama walio wengi wanaongoza mapambano mtoto asiolewe chini ya miaka 18. Leo kuna wasichana wanavunja ungo wana miaka 10 mpaka 12, wanaweza kupata mimba na mnaruhusu waende mashuleni. Mtoto yeyote anayefanya mapenzi na shule elimu yake inapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanithibitishie baadhi ya akinamama hapa walikuwa wanafunzi na tuko nao hapa, kama walianza mapenzi mapema huko shuleni elimu yake ilikuwaje? Wakituthibitishia walianza mapenzi bado wako shuleni na elimu yake ilikuwa pale pale mimi nitawaunga mkono, watueleze. Mimi kama Muislam, dini yangu inaniambia kabisa nisikurubie zinaa. Sasa kama Muislam anasimama hapa ana-support mtoto wa shule aanze zinaa huyo siyo Muislam, amekiuka maadili yake ya dini moja kwa moja.

TAARIFA...

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubali kabisa, naunga mkono. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwaambia ndugu zangu tusizalishe kundi la watoto wa mitaani. Watoto ambao watakuwa hawana walezi, watakuwa wazururaji hakuna atakayekubali mimba za watoto wa shule. Kwa hiyo, mnataka kuongeza watoto wa barabarani moja kwa moja, hatuwezi kukubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wengi mpaka sasa hivi tunajua siyo waaminifu, ndiyo watafungulia sasa, wataanza kuishi na watoto wetu mashuleni, hiyo hatutakubaliana.

TAARIFA...

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza taarifa yake naikataa na huyo Shekhe aliyekwambia siyo Shekhe ni shehena. Hakuna Shekhe atakuambia tukakurubie zinaa huyo siyo Shekhe ni mnafiki wa Mashekhe! Shekhe yeyote hawezi kwenda kinyume na Quran huyo ni mnafiki wala siyo Muislam, nakwambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusicheze na kuongeza watoto wa mitaani. Kwanza kuna UKIMWI, Sheria za Ndoa siku hizi kwa Mapadri na Mashekhe huolewi mpaka upimwe UKIMWI ndiyo ndoa inafungwa. Leo utashirikishaje watoto wafanye zinaa shuleni hawapimwi UKIMWI. Ndugu zangu tusikubaliane, mimi napinga hoja zenu, mmekaa wanawake mnataka kutuendesha, mwisho mtaruhusu ndoa za jinsia moja au ndoa za kusagana hapa, acheni.

Nithibitishie wewe kama kweli ulianza mapenzi bado uko mwanafunzi. Tuelezeni kati yetu nani alianza mapenzi bado mwanafunzi? Nashaanga Mwalimu mmoja anasimama hapa anasema turuhusu mimba, hao Walimu wa namna hiyo ndiyo siyo waaminifu. Inawezekana waliwapa watoto wetu mimba tuwachunguze, tuwachukulie hatua huko walikokuwa wanafundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana walikuwa wanaishi kimapenzi na wanafunzi. Ni makosa kabisa kuishi na mwanafunzi na makosa kabisa kutembea na mtoto chini ya miaka 18. Mtu aliyebaka kifungo chake ni miaka 30, tuache sheria ichukue mkondo wake lakini hatuwezi kuruhusu sisi kuwaozesha watoto wako shuleni.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ndiyo hiyo, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga hoja mkono mia kwa mia. Pia nashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Joyce Ndalichako kwa msaada mkubwa alionisaidia kwa shule ya sekondari ya Kirando kwa kunisaidia shilingi 138,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wanafunzi waliopewa mimba kurudi shule baada ya kujifungua haikubaliki kabisa, kwa kuwa kwanza tunapinga mimba za utotoni wakati tunasema mtoto anayestahili kuolewa ni miaka 18. Je, unahitaji sasa mtoto aolewe au azae chini ya miaka 18? Tunajikanganya na kuna sheria, mtoto anyonye kwa miaka miwili, pia tutaongeza watoto wa mitaani tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mtoto kama anaanza mapenzi angali mwanafunzi vipi achanganye masomo na mapenzi? Kwa hiyo, turuhusu hata watoto chini ya miaka 13 waolewe kwa kuwa hata akijifungua ataendelea na masomo. Tukiruhusu ni kuruhusu wanafunzi wazae na kupata UKIMWI. Naiomba Wizara ikatae kabisa suala la kuruhusu mwanafunzi aliyepewa mimba kurudi darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiruhusu wanafunzi wanaopata mimba warudi mashuleni tutafungulia kwa walimu wasio kuwa waaminifu kufanya mapenzi na wanafunzi na kuwasaidia kimasomo kwa mapatano ya kuishi nao kimapenzi. Mimi sikubaliani na kufanya zinaa kabla ya ndoa na kuongeza watoto wasio kuwa na baba zao na kuongeza mzigo kwa Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Wizara ya Afya namshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika jimbo langu na kujionea changamoto.

Nashukuru kwa kupewa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Kirando na kuokoa vifo vya hasa akina mama. Pia nashukuru sana kwa kupewa pesa mwaka huu kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Nkasi kwa kuwa tuna miaka 40 hatuna Hospitali ya Wilaya, shukrani sana kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tuna vituo vya afya viwili tu, naomba kujengewa kituo cha afya katika Kata ya Kabwe na Korongwe maana kata hizo ziko mbali na Makao Makuu ya Wilaya na wakazi ni wengi, pia usafiri ni mbaya sana na hata hivyo, nilipeleka gari la wagonjwa
nililopewa na Rais wetu ili lisaidie katika kata hizo mbili, hilo gari limekuwa ukombozi mkubwa sana tena sana, ni ukombozi sana kwa wagonjwa wa kata hizo mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana tena sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa msaada na ukombozi kwa hilo gari. Pia shukurani sana kwa Waziri Ummy Mwalimu na Naibu Waziri Dkt. Ndugulile kwa jitihada zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia nikiwa mchangiaji wa mwisho. Kwanza kabisa, nampongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa kushika nafasi ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu wake. Sina budi kabisa kumshukuru Mheshimiwa Profesa Mbarawa, kusema kweli wamenisaidia sana mimi katika Jimbo la Nkasi Kaskazini, kwa mara ya kwanza naisifu hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachoomba; mchakato wa ile Barabara ya Kirando – Kazovu mpaka sasa umechukua mwaka mzima na juzi wamekufa vijana watatu kwenye ule mto kwa kuvuka kuja ng’ambo ya pili, mpaka leo maiti moja imeonekana, mbili hazijaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna siku tatu wanafunzi kutoka Katete na Chongo kwenda Secondary School ya Kirando wanashindwa kuvuka ule mto na pesa zina mwaka mzima, mkandarasi yupo, lakini urasimu wa watendaji leo, kesho, mpaka leo daraja halijajengwa wala hakuna mpango wa kujenga daraja hivi karibuni. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akitoka hapa awahimize watu wake wajenge daraja haraka sana kuokoa maisha ya wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usafiri Ziwa Tanganyika, leo ni mara ya nne, walituahidi kwanza meli mbili, sasa imekuwa meli moja na hiyo meli moja haijulikani. Cha ajabu Burundi wameshajenga meli kubwa sana, DR Congo wameshajenga meli kubwa sana, wametupiga bao. Sisi tunabaki kwa sababu tuna Bandari yetu ya Kigoma na Ziwa Tanganyika, ni ajabu watu wa Kongo ambao hawana bandari upande wa pili na watu wa Burundi wasio na bandari watatumia ziwa letu kwa ajili ya kusafirisha mizigo. DR Congo wameunda mpaka meli ya kubeba mabehewa, sisi tumekaa tu tunaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa miaka nenda, miaka rudi, haiwezekani. Walitenga bilioni kumi kwa ajili ya ukarabati wa Lihemba lakini mpaka leo hakuna. Watumishi wa Marine Service miezi 23 hawajalipwa mshahara, kusema kweli hii inakuwa meli zetu zinakwenda kizobazoba tu, maana yake watumishi hawana mshahara, hawana chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza TANROADS Manager wa Mkoa wa Rukwa. Ukimpigia simu hata saa saba za usiku kwamba kuna shimo kwenye barabara au barabara imefanya hivi, mara ileile kesho yake tayari alishatuma watu kwenda kutengeneza. Kusema kweli TANROADS Manager wa Mkoa wa Rukwa anafanya kazi, halali usingizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza kabisa Engineer Eliud wa Mfuko wa Barabara, ndio alikuwa chachu kabisa kuisadia Barabara ya Kirando – Kazovu ambayo ndugu zangu wananchi wamenituma kule. Kuanzia sasa vijiji vyote vya mwambao wa Ziwa Tanganyika hawataki kusikia chama cha upinzani, pamoja na Madiwani wa CHADEMA wako kule kwetu, wameniambia kamwambie Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwamba kuanzia sasa sisi kura zote ni CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi kabisa, muulizeni hata Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Nditiye, alikwenda Kabwe akamkuta kule Diwani wa CHADEMA, amemhakikishia kabisa kura zote ni kwa CCM. Kwa hiyo, ndugu zangu CCM kusema kweli inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukimfufua mtu aliyekufa mwaka jana akaja leo akaangalia, atashangaa, itabidi arudi kaburini haraka kwa yale maendeleo aliyofanya Mheshimiwa Dkt. Magufuli katika nchi hii. Tuache mchezo, Serikali ya Dkt. Magufuli inafanya maendeleo. Wilaya ya Nkasi naishukuru Serikali, Kabwe leo wametujengea bandari, ilikuwa miaka yote katika vitabu vyote inaandikwa, bajeti ya Bandari ya Kabwe, lakini leo kuna Mkandarasi yuko kazini na asilimia 20 ya kazi ilishaanza kufanywa, unasema huwezi kuishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, upinzani wapeleke huko huko. Mwaka 2020 ndugu zangu watapata aibu kubwa maana yake vitendo vinaonekana, Mawaziri wanapishana. Mimi kwangu Nkasi ni mbali sana kuliko sehemu yoyote lakini Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa amefika, Naibu Waziri amefika kuja kuangalia maendeleo yanayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mkurugenzi wa TPA. Mkurugenzi wa TPA ndio chachu ya maendeleo ya Bandari ya Ziwa Tanganyika, amefanya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu linahusu kusaidia kufungua Chuo cha VETA katika Wilaya ya Nkasi, Paramawe kwenye majengo ambayo yako kumi na nne tuliyopewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Majengo hayo yamekwishakaguliwa na VETA Kanda ya Nyanda za Juu Mbeya na kuridhika kabisa kwani yana umeme na maji. Pia tumetoa eneo la ekari 50 kwa ajili ya Chuo cha VETA Paramawe – Nkasi, kwa hiyo, pa kuanzia tunapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana ziara ya Rukwa, Nkasi Waziri aliahirisha, ilikuwa ufike sehemu yaliyopo majengo hayo mazuri sana. Tunaomba sana msaada wa Waziri. VETA Kanda ilikwishayakubali na kuridhika kabisa. Tunaomba sana msaada wa hali na mali. Majengo yakikaa sana yanaharibika na utunzaji wake ni gharama sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi ina umri wa miaka 40 lakini Makao Makuu ya Wilaya Namanyere haina jengo la Mahakama ya Wilaya wala Mahakama ya Mwanzo. Cha ajabu sana kila mwaka hotuba ya Waziri utakuta Namanyere watajenga jengo la Mahakama lakini mwaka huu hakuna kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ajabu sana Makao Makuu ya Wilaya hakuna jengo la Mahakama ya Mwanzo wala ya Wilaya wakati wilaya mpya zimepewa fedha za majengo ya Mahakama ya Wilaya, hii si haki kwa Wilaya ya Nkasi. Wilaya ya Nkazi tunahitaji jengo la Mahakama kama Wizara iliyoadidi kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 na 2018/2019.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwanza nazungumzia habari ya Jimbo langu la Nkasi Kaskazini, Mheshimiwa Waziri namshukuru sana alifika ziara yake kule akaangalia Gereza la kule kwangu ni la kilimo. Kilimo Kwanza, lakini kilimo hawana dhana za kilimo, wapelekee trekta, Polisi wetu kule mataili ya gari ni shida Polisi Namanyere, petroli, mafuta ya dizeli ni shida ukienda vituo vya pembeni kama vile Kilando na Kabwe ndiyo halikadhalika havifai hata kuviona kwenye macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Idara ya Uhamiaji Kabwe ukienda kuangalia Idara ya Uhamiaji Mheshimiwa Waziri hali yao ni mbaya, wako mpakani Wakongomani wanaingia kila sehemu kwa gari pale Kabwe lakini hawana chochote cha kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri lazima uwafikirie vya pembeni pembeni, kwanza natoa pongezi sana kwa Polisi tuko hapa Bungeni. Nakaa kule Namanyere mke wangu yuko Namanyere analindwa na Polisi wala sina habari nikimpigia simu asubuhi vipi hali anasema hali salama, wote tuko hapa familia zetu ziko Vijijini kule, wanaotulinda kule ni Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nashangaa anakaa Mbunge anasema hapa habari ya Polisi ndugu zangu, hivi Polisi wakigoma masaa matatu tu kila mtu atatoka Bungeni hapa atakimbia mbio hakuna atakayebaki hapa, hakuna atakayebaki Polisi waseme leo tunamgomo kama Madaktari walivyogoma vile Muhimbili hakuna atakayebaki hapa. Lazina tuheshimu Jeshi la Polisi ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafanya kazi kulinda mali zetu na sisi wenyewe tumekaa hapa miezi mitatu tukipiga simu majumbani kwetu hali salama kabisa, hakuna hata mmoja ameingiliwa nyumbani kwake kuvunja nyumba, Namanyere sina hata mlinzi nyumbani kwangu yuko mke wangu na watoto lakini yuko salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa unasema habari ya Jeshi la Polisi, ndugu zangu tumefika pabaya ninamheshimu sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwamuzi aliouchukua kupiga marufuku mikutano. Tukiwa hapa Bungeni wanakwenda kule Majimboni nilizungumza Awamu ya Nne kuanzia asubuhi magazeti, radio, televisheni kutukana, anatoka na mwendawazimu mmoja anajiita Mwenyekiti anaanzisha mkutano kuanzia asubuhi ni kutukana, anamtukana Diwani, anamtukana Mbunge, anamtukana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli kulikuwa hamna nidhamu wote mnakumbuka hapa tulikuwa wakiita mikutano hawa jamaa ilikuwa ni hatari peoples wanaita peoples ni uharibifu wa hali ya juu. Nimeshuhudia kule kwangu hawa jamaa wamechoma nyumba, mpaka akinamama
wamepigwa na mimba zimetoka Kilando kwa ushahidi ninao. Leo mnakuja kusema Polisi, milijifanya Polisi nyie mlishika kwenu Sheria mkononi ilikuwa watu hawatembei ndugu zangu mnatishia namsifu Mheshimiwa Dkt. Magufuli amenyoosha nchi vibaya hii ilikuwa nchi imefikia pabaya. Mlijifanya nyie madume nyie lakini leo wamewashika kusema kweli tunaishi kwa amani na utulivu, tulikuwa sehemu mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kilando kule mpakani tena ndiyo kulikuwa kubaya zaidi mlikuwa mnakuja vifua mbele leo kusema kweli tunashukuru Serikali ya Awamu ya Tano tunatembea na sisi vifua mbele wakati wetu mlikuwa mnadhalilisha wakati wa uchaguzi mdogo tu mnaiba masanduku ya kura, mnachoma masanduku ya kura ushahidi kabisa Jimbo la Kwela kwa Malocha mlichoma masanduku nyie. Kilando wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa Chadema walichoma masanduku ya kura ilikuwa nchi imeharibika sasa imerudi nidhamu, hii ni nidhamu ya hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Jeshi la Polisi liendelee na mkazo huo huo, mlikuwa mmetupeleka kubaya mpaka wana CCM wanaogopa kuvaa mpaka nguo za kijani mnawatishia na nyie sasa ni wakati wenu kuacha kuvaa magwanda. Tunakwenda kinidhamu zamu kwa zamu. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Keissy sema!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu lazima tuliona sisi wote nchi ilipofikia tulifikia pabaya nimekaa kule mtu anakuja anaitisha mkutano mnakaa mnamuona kuanzia asubuhi ni matusi tu anamtukana Rais wa nchi. Nilimwambia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mimi Mheshimiwa Jakaya Mlisho Kikwete nilimwambia Mheshimiwa takuja kukata mtu kichwa halafu wewe ndiyo utakwenda Mahakamani sitakubali wewe Rais wa nchi unatukanwa nasikiliza na Mapolisi wanasikiliza hawachukue hatua yoyote tulifikia pabaya, hata Polisi walikuwa hawachukue hatua yoyote kwa ushahidi ninao nilizungumza. Wanakumbuka tulikuwa Wabunge Awamu ya Nne hapa nilizungumza, nikamwambia Mheshimiwa Kikwete hawa jamaa wakija kwangu Namanyere wakikutukana tu nitakata kichwa cha mtu, wamezidi hakuna nidhamu dunia nzima hakuna nidhani lazima tuheshimiane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Rais ameweka nidhamu ya hali juu tumuunge mkono na sisi tuendelee tufanye kazi naunga mkono Serikali kusema kweli ndiyo tulisema TV live namna wanazungumzia hovyohovyo live gani hii mazungumzo gani haya wana record kwenye you tube wanasambaza. Lakini hotuba zote mzee ni kichaka ni kuchochea angalieni ndugu zangu, nchi zingine angalieni Libya tangu leo amefariki Gaddafi miaka mingapi Libya imetulia?

MBUNGE FULANI: Haijatulia.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mpaka leo, Libya haijatulia mpaka leo mshukuru ninyi mmekaa hapa familia zenu kule nyumbani mkipiga simu ni salama, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kusema ukweli tukichunguza, labda kwenye bahari kuu, lakini kwenye maziwa samaki wamepungua sana. Nitatolea mfano Lake Rukwa. Lake Rukwa miaka kumi iliyopita kulikuwa na samaki wengi sana, wanalisha mpaka Zambia na sehemu mbalimbali za nchi hii. Leo Lake Rukwa hakuna samaki hata mmoja. Sisi kule kwetu Lake Tanganyika wanavulia mpaka vyandarua. Tunagawa vyandarua bure, wananchi wetu wanachukua vyandarua wanafanya ndiyo uvuvi.

Mheshimiwa Spika, hizi samaki tulizopewa na Mwenyezi Mungu; je, wazazi wa zamani miaka 50 iliyopita wangetumia uvuvi kama huu uliopo sasa, tungekuta samaki? Haiwezekani. Lazima tuwaelimishe wananchi wetu waache uvuvi haramu, uvuvi wa ovyo ovyo. Lake Victoria miaka kumi tu, leo ni asilimia 50 ya samaki. Miaka kumi ijayo Ziwa Victoria hakuna samaki hata mmoja, hakuna. Hata maziwa yote yatakuwa ni hivyo hivyo.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, huyu hajavua. Mimi nimevua tangu utoto wangu. Mpaka sasa piga simu kwa Afisa uvuvi, Kipili, atakwambia ni vyandarua vingapi vimekamatwa? Kwa ushaihidi vyandarua vinavua, wewe hujui chochote, wala hujaingia majini. Mwanamke gani akaingia majini kuvua? Acha kudanganya Bunge. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hizi samaki tumepewa sisi na vizazi vijavyo. Haiwezekani mtu ku-support uvuvi haramu, lazima tuwaelimishe wanachi wetu waache uvuvi haramu. Leo nenda Ziwa Tanganyika, wanakuja Wa-congoman, sisi watu wetu huku hawaendi Zaire kuvua, lakini nenda kwenye visiwa vya Mvuna, nenda Mwanakerenge, wamejaa Wa-congoman na nyavu haramu wanavua samaki na dagaa. Yeye anasema ana ziwa, alishaingia ziwani kuvua huyu? Haiwezekani! (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hizi samaki tumepewa za urithi kulinda vizaizi vijavyo. Leo sisi tunavua, wanavua vizazi miaka 15 iliyopita hakuna samaki. Mfano, Ziwa Rukwa muulize Mheshimiwa Malocha, Mbunge wa Ziwa Rukwa, waulize Wabunge wa Ziwa Rukwa, hakuna samaki Lake Rukwa, samaki zote zimekwisha na ilikuwa samaki malori na malori wanapeleka Zambia kuuza. Leo samaki Lake Rukwa hakuna.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo na Ziwa Tanganyika, ukianza tu mwezi wanaingia kuvua migebuka ndugu yangu haijafika hata nchi sita au nchi saba, wanaita nyamnyam. Migebuka kwa kawaida inangojewa iwe mikubwa, lakini wanaingia kuvua kuharibu samaki mpaka wanatupa kule Ziwa Tanganyika. Haiwezekani! Hizi tumepewa ni rasilimali yetu na vizazi vijavyo. Haiwezekani watu waingie kuvua jinsi wanavyovua.

Mheshimiwa Spika, nimeona viwanda vilivyokuwa Lake Victoria, leo vimebaki nusu, hakuna viwanda. Lazima tulinde vizazi vya samaki vinavyozaana samaki. Ile Sheria ya kuvua mita 500 kutoka mwambao wa Ziwa Tanganyika haitekelezeki. Jana tu nimepigiwa simu na mtu wa Kabwe, kuna kokoro zaidi ya kumi zinavutwa kule Kabwe, nimepigia Bwana Samaki simu, chunguza hizo kokoro. Kwa majina, ninao. Kokoro inavuta na mayai na kila kitu, imeharibu samaki. Ndugu zangu tusitake kupata kura kwa ajili ya kubembeleza ili tuharibu uchumi wa nchi. Tuelimishe watu wetu.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kubembeleza, Waheshimiwa Wabunge na Madiwani ndio wanaharibu nchi hii kwa kubembeleza kura wanadanganya wananchi. Tuwe wakweli. Hatuwezi kwenda kinyume tuharibu uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachangia habari ya mifugo. Tumenunua ndege Bombadier kwa ajili ya kukuza utalii. Tutakuza utalii kwa kutazama ng’ombe katika nchi? Tutakuza utalii kwa ajili ya kuja kutazama ng’ombe au kutazama twiga na tembo na simba na chui? Leo tunataka tupunguze mbuga za wanyama kwa ajili ya wachungaji. Ndugu zangu tufuge kisasa, siyo tuchunge.

Mheshimiwa Spika, hatutaki uchungaji! Ng’ombe ukimkuta kachoka, mchungaji kachoka, haiji. Hakuna ng’ombe zaidi ya kilo 150. Ukimchinja ukitoa utumbo na kila kitu unapata kilo 100 au kilo 70. Utasema nakuza mifugo? Haiwezekani. Lazima tuige nchi zinazoendelea kwa ajili ya ufugaji. Hatuwezi kuwa wachungaji kila siku, mchungaji anachoka na ng’ombe anachoka, haiji. Lazima tutafute sehemu ya kuchungia mifugo yao, wakae sehemu moja, siyo kuhama hama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nazungumza habari ya Nkasi, kuna ng’ombe zaidi ya 130,000. Nkasi ilikuwa ni sehemu ya kilimo, sasa imekuwa na mwisho italeta migogoro kwa ajili ya wachungaji. Wanakuja na mifugo, mifugo inakondeana kila sehemu wanataka majosho na Serikali ndugu zangu, tufuge ng’ombe wa kisasa. Tuna ng’ombe zaidi ya 25,000 lakini hata maziwa hatuna, nyama ya kisasa hatuna, tunaagiza nyama ya kisasa nje ili watu wale nyama. Ukitaka steki, hakuna nyama ya steki, maana yake ng’ombe kakonda ni mifupa mitupu. Haiji! Lazima tupunguze mifugo, tufuge mifugo yenye uwezo ili ng’ombe afike kilo 800 au kilo 900.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu hatuwezi kuwa wachungaji sehemu zote tunakwenda barabarani kuchunga, hakuna hicho kitu. Lazima tufuate sheria na sheria ni msumeno. Haiwezekani wewe kukutetea hapa kwa ajili ya kuja kuomba kura.

Mheshimiwa Spika, hata mimi niliingia Bungeni kwa kuomba kura, lakini nasema ukweli na watu wangu wananisikia. Siwezi kuwatetea wavuvi haramu wanakokoa kila kitu mpaka mayai ya samaki na mjukuu wangu aje kuvua wapi? Siwezi kumtetea mfugaji anaharibu ardhi, mito inakauka, vyanzo vya maji vinakauka, tutakunywa wapi maji? Wakati nchi yetu imebarikiwa na maji nchi nzima, lakini leo vyanzo vya maji vyote vimekwisha. Haiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatubembelezi kura kwa njia ya namna hiyo ya kudanganya danganya. Tuwaelimishe wananchi wetu, tuweze kwenda sawa na hili tutakwenda sawa. Hata akija kiongozi anaharibu nchi, ndiyo tumchague huyo, haiwezekani! Lazima twende na sheria, tufuate sheria. Sheria tumetunga Bungeni hapa, hakuna sheria Mheshimiwa Mpina alizotoa mfukoni kwake akaenda kwa wavuvi, hakuna. Sheria zimetoka Bungeni hapa, hazikutoka popote. Sheria ni msumeno, hata ningekuwa mimi Waziri nitakuwa hivyo hivyo, wewe ukiwa Waziri utakuwa ni hivyo hivyo au kwa sababu unaomba urudi Bungeni, hili Bunge ndugu zangu, umekuja, utatolewa, atakuja mwingine, ataendelea. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naunga mkono mia kwa mia utendaji wa Waziri na wasaidizi wake wote. Nachoomba kwenye jimbo langu ni kuimarisha chuo kipya cha VETA Paramawe kwa vifaa ili kiweze kusaidia vijana wa Nkasi na Mkoa wote wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni muhimu Wizara ione uwezekano wa kuongeza majengo kwa kuwa tuna kiwanja cha ekari zaidi ya hamsini. Pia ikiwezekana chuo kiwezeshwe kutoa kozi zote zinazotolewa na vyuo vingine vya VETA nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kukupongeza Prof. Ndalichako na wasaidizi wake wote, tuko pamoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ukieleza mambo aliyofanya Rais wetu wa Awamu ya Tano huwezi kuyamaliza. Kwanza nihesabie kuwa tangu nchi hii kuingia vyama vingi sijaona awamu yoyote wapinzani walikuwa ngunguri kuhama vyama vyao kuingia CCM ila Awamu ya Tano Madiwani wamekimbia kwao, Wabunge wamekimbia, hata Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Sifa kubwa anayo Mheshimiwa huyu utendaji wake wa kazi, akizungumza mpaka kule chini vijijini wanapata habari yao. Nidhamu ya hali ya juu imerudi katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi ilikuwa inachezewa, ukitoa ripoti kuhusu mafisadi hawatetemeki, hakuna kutetemeka, leo wanatetemeka vibaya. Hata wizi, wanaoiba wakijulikana hawana nafasi katika nchi hii. Mimi nakaa kwenye mipaka – hawa wanazungumza tu – wamsikie Profesa Lumumba wa Kenya alivyommwagia sifa Dkt. Magufuli; waende Burundi, hawatembei ndugu zangu, wamekaa hapa hawatembei, waende Burundi, waende Rwanda, waende Kenya, DRC Congo, Zambia anavyomwagiwa sifa Rais wetu haijatokea. Hawajapata kuona Rais anayetoa uamuzi mzito kama Rais wetu, miradi mikubwa mikubwa kwa muda mfupi, haijatokea katika Afrika, hakuna cha kumbeza watakaa wanazungumza sisi tunakwenda mbele, hawana jipya kwa sababu Rais kashatangulia mbele hatua 10,000 zaidi yao. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, walikuwa Bungeni hapa wenyewe wanalalamika safari za nje, kazibana; wamelalamika hapa mafisadi kawabana. Sasa ndugu yangu hawana jambo jipya, wanayumbayumba washika maji hawa ndugu zangu. Miti yao imeshakauka hata ukimwagia maji mti umekufa umekufa. Nawaomba ndugu zangu upinzani umebaki kama vile jani la mgomba lililokauka.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, Rais huyu, sikia vyombo vya habari, au labda televisheni na redio za nchi za nje, anavyosifiwa duniani hakuna mfano wake, na bado hasafiri, na bado hasafiri anasifiwa, je angekuwa anasafiri? Ingekuwa balaa. Kafanya mambo mazito katika nchi hii; hospitali mpaka kule Namanyere, mpaka Kirando, mpaka Wampembe kule mwisho wa nchi, hospitali zinang’aa kama mambo ya ajabuajabu.

Mheshimiwa Spika, hakuna sifa zaidi anayopata Mheshimiwa nendeni nchi za nje mkasikilize. Ukifika ametupa heshima ya ajabu, wakisikia unatoka Tanzania kwa Magufuli! umetoka Tanzania nenda popote. Ndugu zangu wamebana safari za nje hawa ndiyo hawajui chochote.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Utatoa taarifa namna gani wewe mimi nazungumza hapa, taarifa ya nini?

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Keissy umeshamaliza.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, Rais amefanya mambo makubwa kwa muda mfupi, haijatokea katika viongozi wa Afrika Mashariki na Kati na duniani. Kajizatiti kwa hela za ndani bila matatizo yoyote…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: …na wananchi tumuunge mkono. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Wizara ya Kilimo na kumpongeza Waziri na Manaibu wote wawili. Ombi langu ni kuhusu Skimu ya Umwagiliaji ya Lwafi iliyopo Jimboni Kwangu Katika Kata ya Kipili na Kirando. Skimu hii imegharimu pesa shilingi bilioni moja na mia nane milioni, kubwa sana haijasaidia wakulima wa mpunga wa kata hizo kabisa na wakandarasi wamepewa fedha zote hizo.

Mheshimiwa Spika, Skimu hiyo ilikuwa isaidie sana wakulima wetu, leo hii skimu hiyo ni bomu kubwa. Kusema kweli fedha iliyotumika hailingani na kazi, inaonesha wataalamu wetu hawakusimamia sawa au hawana utaalamu wa kutosha na kusababisha kupoteza pesa bilioni
1.8 bure. Naomba uchunguzi ufanywe na skimu ikamilike.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naunga hoja mkono asilimia mia moja au zaidi ya mia mbili. Namuunga mkono Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu, Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii inafanya kazi kubwa sana inasaidia wafugaji na wavuvi, kitu cha kushangaza kabisa utakuta Wabunge wengi hapa wanachangia kuisema Wizara ya Mifugo kwamba ndio inakamata mifugo ya wananchi. Kitu cha ajabu kabisa, mfugo unaingia National Park au Game Reserve anausikaje Mheshimiwa Waziri wa Mifugo kukamata ile mifugo, inakamatwa kwa sababu imefanya makosa imeingia kwenye National Park au Game Reserve. Mheshimiwa Waziri wa Mifugo hausiki, unakuta Mbunge anatoa na povu anasema Wizara ya Mifugo ndio inakamata mifugo, ni kitu cha ajabu kabisa sijaona. Unapochangia changia inapohusika kama huwezi kuchangia kaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kweli Mheshimiwa Waziri, Maafisa Mifugo wanakamata mifugo au mifugo inakamatwa na Wizara ya Maliasili wakati inaingia kwenye National Park au Game Reserve, unapochangia changia hoja sio kuchangia against Wizara, kama huna uwezo wa kuchangia kaa kimya. Huwezi kuingiza kitu ambacho cha uongo na kuisema mpaka povu zinakutoka kitu cha aibu, kama hujui kaa kimya.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naisifu Wizara, nazungumzia habari ya uvuvi. Wizara ya Uvuvi tuzungumze ukweli kila mara nazungumza hapa, tuelimishe wavuvi wetu, sisi Wabunge tuna kazi vilevile ya kuelimisha wavuvi wetu. Mimi mara mbili nimekwenda Kituo cha Kipili wakati wanachoma nyavu nimezuia wasichome wasichome nyavu tukaenda nikapima zile nyavu, unakuta kweli nyavu ziko milimita nane halali, amechanganya na kipande cha milimita sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyavu zinachanganywa, unakuta milimita sita, milimita nne wanachanganya nyavu, sasa utatetea wavuvi kwamba hawavui kiharamu, ndugu zangu tuseme ukweli, Serikali inafanya kazi ya ziada kulinda maliasili ya uvuvi. Haiwezekani sisi Wabunge tumekaa hapa, tunaisema Wizara ifanye kazi, iache wavuvi wafanye kazi wanavyotaka, wengine tuige mfano tuseme hata Congo kama Congo wanaharibu kule uvuvi wao haramu acha waharibu.

Mheshimiwa Spika, kuna nyavu zinatoka Congo zinakuja kwetu, tuziache? Nyavu zinatoka Burundi zinakuja kwetu, wanaita free mayai zinakuja wanavua kwetu, tunazikamata tunazichoma, hatuwezi kuita Serikali ya Congo au Serikali ya Burundi au Serikali ya Zambia haiwezekani! Kama anaharibu Congo na sisi aharibu huku kwetu, haiwezekani, hata kama samaki anatembea, acha atembee lakini haiwezekani na sisi tuingilie uharibu kama wanavyoharibu wenzetu haiwezekani! Kwanza ni dhambi kuvua visamaki vidogo vidogo hata Mwenyezi Mungu hapendi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali, juzi tumekutana na Katibu Mkuu, ameruhusu ring net wavue, lakini lazima tuwashauri na wavuvi wetu wale wasitumie ring net chini ya milimita nane na uvuvi lazima wavue mita 300 toka mwambao wa Ziwa Tanganyika na wavue usiku sio mchana, haiwezekani tuache tu kwa sababu ya kuomba kura kwa wavuvi au kwa wafugaji, tuingie hapa Bungeni tuharibu mali yetu, haiwezekani. Tuwe wa kweli, hawa samaki sio mali yetu peke yetu humu ndani, vizazi na vizazi, mimi nina miaka zaidi ya 70, ingekuwa wanavua tangu zamani kama wanavovua samaki tungewakuta sisi, tungekuta masanamu ya samaki tu, tuwe wakweli bwana, mtu lazima afuate sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tufuate sheria inavyotaka ya kulinda mali yetu, ni mali yetu wote tumepewa na Mwenyezi Mungu, haiwezekani kutetea mvuvi ambaye anavua kiharama unatoa povu zako, haiwezekani kumtetea mfugaji anaharibu mazingira mpaka povu zako zinakutoka, fuata sharia. Unasema wewe anaingia mnyama, kwanza atapata magonjwa kwenye wanyama wale wa asili, tembo mle ndani wamo, mna simba na chui, unapeleka ng’ombe zako wakaharibu mazingira unataka wapeleke magonjwa ya sotoka mle ndani.

Mheshimiwa Spika, Rukwa kule wamegawiwa vitalu Kalambo Ranch, vitalu zaidi ya 20 wameuza vile vitalu, lakini ukienda mpaka leo ni miaka 10 wamegawiwa vile vitalu mpaka leo hawana ng’ombe mle ndani, walionunua vile vitalu mpaka sasa hawana ng’ombe, wanakodishia watu na ng’ombe chache.

Mheshimiwa Spika, juzi wamegawa vitalu vingine kula Kalambo Ranch kule wapeleke ng’ombe mle ndani kule kwenye Kalambo Ranch, lakini kuchunga hovyo halafu wanaingia Game Reserve, National Park wasiwakamate kwa vipi, halafu hilo swali wanapeleka Wizara ya Mifugo inahusika wapi? Haiusiki Wizara ya Mifugo ya Uvuvi, sijaona siku moja Afisa Mifugo akaenda kukamata ng’ombe National Park hata siku moja, sijaona mimi, wanaokamata ni watu wa TANAPA au watu wa Game Reserve, leo unachachamaa na povu linakutoka, unamshambulia na kwa jina, mnamtaja kabisa Mheshimiwa Mpina. Tulitegemea Mheshimiwa Mpina utatusaidia kwa sababu wewe unafuga ng’ombe, aaha imekuwaje! Biashara gani, haiji hata kidogo! Unategemea Mpina kwa kwa sababu ametoka kwenye kufuga asaidie ufugaji haramu. Mimi natoka kwenye uvuvi na ndugu yangu Mheshimiwa Ulega asaidie uvuvi haramu kwa sababu ni mvuvi, haiji! Ni lazima tufuate sheria ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusije hapa unatoa povu zako bure, kuwakashifu Waheshimiwa Mawaziri, kuwakashifu Makatibu Wakuu kwa sababu wewe unataka kura kwa wafugaji haramu na wavuvi haramu, haiji. Waambieni ukweli, waelimisheni wavuvi, haiwezekani mvuvi, nimeona kwa macho yangu kule anavulia chandarua, unategemea sasa utakuta mazalia ya samaki, chandarua!

Mheshimiwa Spika, mimi nimekamata mwenyewe vyandarua, mimi mwenyewe nampigia Bwana Samaki Kipili, naye amekuta vyandarua vinavua samaki. Kwa sababu najua hata kura wasiponipa potelea pote, kwani nimezaliwa kuwa Mbunge mimi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani, sikuzaliwa kuwa Mbunge, lazima tufuate haki. Haiwezekani kokoro likavua Ziwa Tanganyika, makokoro bado yapo na uvuvi haramu bado upo, naomba operesheni ziendelee. Operesheni lazima ziendelee uvuvi haramu bado upo lazima operesheni ziendelee, lakini operesheni za hekima na busara, lakini tusiache operesheni. Tusitegemee tuache operesheni kabisa samaki watakwisha. Haiwezekani, lazima operesheni ziendelee kwenye maziwa yote na bahari hizi zote, tusikubali.

Mheshimiwa Spika, kuna mabomu yanapigwa, wote mnasikia kuna mabomu yanapigwa. Kule kwangu zamani ilikuwa mabomu mpaka kuna watu wameathirika vidole miaka ya nyuma ya zamani, siku hizi ndiyo hakuna mambo ya mabomu, lakini wako mpaka waliokuwa wanakatika vidole, bomu linachelewa mkononi kwake, samaki unakuta wamelegea wote. Sasa hii ndugu zangu tukianza kutetea, tufuate haki.

Mheshimiwa Spika, hatukuja hapa sisi kwa ajili ya kura za kuombaomba, hapana. Kura zetu tumekuja hapa kutetea Serikali yetu na kutetea wavuvi wetu na wafugaji wetu kuwatetea; lakini wewe una-base upande mmoja tu kwa sababu wameletana hapa wanataka kusema aa, yule Mbunge ndiye mzuri tukampe kura katutetea sisi wafugaji na wafugaji na wavuvi, hapana. Lazima tuwawajibishe wavuvi wetu, kama milimita nane itumike milimita nane, lakini kama unachanganya milimita nane na milimita sita, yote umechanganya ni haramu. Huwezi kuweka kwenye sanduku lako umechanganya bangi na sigara, tumbaku, unasema ni halali, utakamatwa tu, yote ni bangi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mchango wagu ndio huu. Lazima tuelimishe wavuvi wetu, tuelimishe wafugaji wetu, tufuge kihekima na busara ili nchi yetu ipate kuendelea. (Makofi)
The Finance Bill, 2016
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Wabunge wote tuliopo hapa tuna matatizo kwenye majimbo yetu, tuna shida ya maji, barabara na mawasiliano, hakuna Mbunge hata mmoja hapa asiye na shida kwenye jimbo lake, hatuna barabara kabisa. Kwa hiyo, Serikali lazima ijipange kukusanya kodi kwa kila mtu bila kuona huruma.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya makampuni ya simu yajiunge na Dar es Salaam Stock Exchange mara moja, tuwadhibiti. Vilevile tulipe kodi kwa wafuga kuku, wafuga ng‟ombe, baiskeli kama zamani Wakoloni walikuwa wanadai kodi kwenye baiskeli mpaka mbwa alikuwa analipiwa kodi, nashangaa siku hizi hakuna cha kodi, kila kitu kodi, bila kodi hatuwezi kwenda. Hizi hela za Wazungu zinazokuja hapa ni kodi yao, hata vyama za siasa vinavyopata ruzuku vikatwe kodi. Haiwezekani vinapata ruzuku ya Serikali vinachukua moja kwa moja, vinanufaika bila kukatwa kodi na vyenyewe vikatwe kodi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mkoloni tulikuwa na mikoa tisa na barabara zilikuwa mbovu ajabu katika nchi hii. Leo tunaongeza mikoa na watendaji, tunaongeza shida kwa Serikali, imekuwa nakama. Kila mtu anadai mkoa, kila mtu anadai jimbo, kila mtu anataka kila kitu wakati Serikali yenyewe tunataka matumizi yaende kwa wakati, tunataka barabara sisi, hatutaki mikoa kuwa mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo natoka hapa nakwenda Mbeya kwa saa nane zamani Mbeya huioni labda siku tatu, hapa na hapa mkoa, hapa na hapa jimbo. Serikali ipitie upya majimbo yaliyopo katika nchi hii, vigezo vitumike sio mimi nilikuwa mkubwa, mimi ndiyo Waziri Mkuu au mimi ndiyo Rais nagawa majimbo navyotaka, mkoa wangu unapata majimbo, Kilimanjaro leo majimbo tisa, Tanga majimbo 11, ndugu zangu, hatuendi hivyo, mikoa mingine kama Rukwa majimbo matano, lazima tupitie upya tubane hela za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na utitiri wa majimbo, tugawe majimbo kutokana na vigezo. Mimi nimetoka huko nagawa majimbo navyotaka, nagawa halmashauri navyotaka, tunaongeza gharama ya nini? Twende kwa vigezo tupate haki sawa kwa kila mtu. Haiwezekani mkoa mmoja idadi ya watu walewale majimbo 11, mikoa mingine kama nchi ya Burundi majimbo matano, haiji! Gharama za nini hizi? Lazima twende na wakati. Hatuwezi kudekeshana hapa, hatuwezi kubembelezana, majimbo yaende kwa vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siogopi kugombana na mtu, nasema ukweli, twende kwa vigezo, huwezi kunitisha, twende kwa vigezo. Tanga leo au Kilimajaro inaingia mara mbili kwa Mkoa wa Rukwa, nani atabisha hapa? Twende kwa vigezo, mimi nasema ukweli, hatuna barabara hatuna chochote, tubane hela za Serikali twende kwa vigezo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu alipe kodi, hawa wanaotembeza mali barabarani na wenyewe walipe kodi. Wengine wanatembea na mali kuliko mwenye duka. Leo mama muuza nyanya kila siku analipa sokoni Sh.500 kwa mwezi analipa Sh.15,000 wewe unatembea.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mtu ana ng‟ombe 300,000, ana ng‟ombe 30,000 halipi kodi, nazungumza kila siku hapa, mifugo ilipe kodi, kwa nini hamleti kodi ya mifugo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua property tax ya nyumba, ndugu zangu basi halmashauri wapeni wadai kodi za mifugo, hawana chanzo chochote cha rasilimali. Kwa hiyo, wapeni na wenyewe wadai kodi ya mifugo, wadai kodi ya mbwa na wadai kodi ya baiskeli.
Michango ya harusi, harambee za vyama, harambee za harusi na yenyewe idaiwe kodi.
Michango ya misiba tumeona mikubwa hata humu Bungeni. Waheshimiwa Wabunge wanachanga Sh.100,000 kwa misiba, idaiwe kodi. Hatuwezi kusamehe kodi, VAT ya Sh.18,000 itolewe kwa kila Sh.100,000, wanachanga Wabunge humu.
Sadaka zitolewe kodi. Wazungu wanalipia kodi kila kitu, hatuwezi kuendelea na Serikali yetu hii, Serikali yetu ina watu wengi ndugu zangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapitwa na Rwanda kwa makusanyo ya simu tu, ni kitu cha ajabu kabisa, wakati watu wana simu nne mpaka tano hapa Tanzania, hatuwezi kwenda namna hii bila kodi. Hatuwezi kumwambia Waziri wa Fedha leo tufute kodi ya pikipik na magari, akatoe wapi hela yeye wakati mnamdai maji, barabara na madawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nasema kila kitu kipangiliwe, ng‟ombe walipiwe kodi, baiskeli zilipiwe kodi, mifugo yote ilipiwe kodi, kuku alipiwe kodi na ruzuku ya vyama ilipiwe kodi na michango ya harambee yote ilipiwe kodi. Tuwe wakali kwa kodi, leo Uingereza hawana chochote lakini ndiyo wanaotusaidia sisi ni kwa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa wanyonyaji kwa Wazungu namna hii kwa sababu gani, haiwezekani! Tujibane tulipe kodi. Ni aibu wewe unazaa watoto wako unakwenda kulisha nyumba ya jirani, haiwezekani! Tubanane sisi wenyewe, hakuna kusema chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii migodi ibanwe, haiwezekani Mheshimiwa Mbunge kuja hapa anatetea migodi, ndiyo tunakuwa na mashaka na Wabunge wetu humu ndani. Unatetea mashirika ya simu wewe, unatetea migodi, tuna wasiwasi na Wabunge. Mbunge unasimama unatetea mgodi, unatetea shirika la simu, tuna wasiwasi na wewe. Ingawa ushahidi wa rushwa kuukamata ni taabu lakini tutakuuliza mara mbili wewe una nini hapa na hili shirika, umepewa nini wewe mwenzetu? Hapa hakuna kuteteana, tunakuja kujenga nchi yetu ili ijitegemee kama Rais wetu alivyosema. Haiwezekani wewe nchi yetu kubwa, ina kila kitu tunakwenda kuombaomba, haiji hiyo! Mbunge atakayesimama hapa kutetea habari ya kutolipa kodi tuna wasiwasi na wewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, yangu ndiyo hayo.