Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mohamed Omary Mchengerwa (49 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapa pole Waheshimiwa Majaji na Mahakimu wote ambao wametajwa ndani ya Bunge hili ambao hawawezi kufika ndani ya Bunge hili kujitetea. Kanuni zetu za kilatini Mheshimiwa Tundu Lissu atakuwa mwenyeji kwenye hili right to be heard, rule of law ambazo zinatuongoza anazifahamu vizuri, lakini nitambue mchango Jaji Mkuu Mheshimiwa Mohamed Othmani Chande, amefanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba mahakama zetu zinakwenda vizuri kupunguza kesi za mahakama ambazo zilikuwa msongamano kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Rufiji kwa kunielewa, wananifahamu kule Rufiji naitwa jembe, wengine wananiita sururu. Ninashindwa kutambua uwezo wa kisheria au uwezo wa kufahamu wa ndugu yangu Tundu Lissu, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifuatilia mchakato na namna ambavyo akiendesha Bunge kwa muda mrefu sana kwa zaidi ya miaka sita nimekuwa nikimfuatilia. Mheshimiwa Tundu Lissu namfananisha na mwandishi wa vitabu vya movie, aki-act mwaka 1940 ile movie ya Ndugu Charlie Champlin. Kuna movie moja, political satire, hii ukiifuatilia vizuri inaendelea kiundani, Mheshimiwa Tundu Lissu ni mtaalam mzuri wa kuiga kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee uteuzi wa Mawaziri. Tunaongozwa hapa na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, kama ambavyo imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara. Lakini katika Katiba hii, Ibara ya 54 na 55 inazungumzia kwa uwazi uteuzi wa Mawaziri. Ibara ya 56 inazungumzia mchakato mzima wa nani anaweza ku-qualify kuwa Waziri yaani kwamba mchakato huu, mtu atakuwa Waziri baada tu ya kuapishwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaongozwa na Sheria Na. 15 ya mwaka 1984 kama ambavyo Mheshimiwa Tundu Lissu ameizungumzia. Katika instrument of appointment ya Mawaziri ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu amekuwa akiikazania kwa muda mrefu, siyo yeye tu hata Mwenyekiti wa Chama chao amekuwa akizungumza sana kuhusiana na sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge hili lipate fursa ya kutufundisha kizungu inaonekana kuna shida ya kufahamu kizungu. Kwa mujibu wa Sura ya 299 ya sheria inayompa mamlaka Mheshimiwa Rais ya kuwaapisha pamoja na kuunda instrument yaani sheria hii inaitwa The Minister‟s (Discharge of Ministerial Functions) Act, Sura ya 299. Ukisoma kifungu cha tano cha sheria hii kinasema hivi ninaomba wataalam wa linguistic watusaidie ili waweze kumuelewesha huyu bwana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha tano cha sheria hii kinasema hivi; “The President may, may na shall ina maana kubwa sana kwa kizungu. Wataalam wa linguistic watusaidie kumfahamisha may ina maana gani na shall ina maana gani. Siyo hivyo tu kifungu hiki kimekwenda moja kwa moja kuzungumzia kwamba from time to time by notice published in the Gazette specify the departments, business and other matters responsibility for which he has retained himself or he has assigned under his direction to any Minister, and may in that notice specify the effective date of the assumption of that responsibility. (Makofi)
Sheria hii inasema wazi ni wakati gani. Mheshimiwa Rais wakati wowote anaweza kutengeneza instrument kwa sababu sheria hii haija-specify ni wakati Mheshimiwa Rais anapaswa kutoa gazette la Rais. Sheria hii haitoi muda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais hajavunja Katiba yoyote kwa mujibu wa sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende mbele zaidi, amezungumzia suala zima la ESCROW kuna Majaji walishutumiwa not kushtakiwa. Naomba nimkumbushe vifungu vya sharia vinasema allegation however strong it may it cannot convict the accused person, hata kama shutuma zitakuwa na uzito wa kiasi gani haziwezi kumtia hatiani mshitakiwa.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 112 inazungumzia Tume ya Utumishi wa Mahakama. Tume hizi zimepewa uwezo mkubwa wa kujadili nidhamu za Majaji na Mahakimu. Ibara ya 113 inakazania kwenye suala hili zima. Bunge halina mamlaka juu ya Mahakama, hali kadhalika Serikali haina mamlaka dhidi ya Bunge na Mahakama. Kilichofanyika baada ya mapendekezo ya Bunge, Mheshimiwa Rais alikabidhiwa mapendekezo ya Bunge, kwa mujibu wa Ibara hii ya 113 Mheshimiwa Jaji Mkuu aliunda Tume, Tume ya Utumishi wa Mahakama ipo kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Tume Rais hana mamlaka ya kumfukuza Jaji isipokuwa tu Ibara ya 113 inampa mamlaka Mheshimiwa Rais iwapo itaonekana Jaji amefanya utovu wa nidhamu na maadali baada ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kutoa mapendekezo yake. Jambo hili lilifanyika na Waheshimiwa Majaji hawa baada ya kupitia na jambo kubwa ambalo lilifanyika, Mheshimiwa Jaji Mkuu pamoja na Tume hii walitumia the Code of Ethics for Judicial Officers, pia kwa kuzingatia the independence of the judiciary walizingatia haya yote kimsingi na ilionekana kabisa wazi kwamba hakuna jambo lolote lililofanyika na taarifa hii ipo mbele ya Mheshimiwa Rais kwa tafiti zangu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaenda kwa haraka. Kuhusu Mahakama ya Mafisadi imekuwa ikipigiwa kelele sana, sasa sijui kwa nini ndugu zetu hawa wanakuwa waoga, wanaogopa nini? Kwa mujibu wa taratibu na sheria kinachoweza kufanyika ni kufanya mabadiliko ya Sheria hii ya Uhujumu Uchumi ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu ameizungumza hapa, Sura ya 200 imezungumzia kiundani kabisa. Division hizi za Mahakama Kuu zipo nyingi Tundu Lissu anafahamu, tunayo Division ya Ardhi, tunayo Division ya Biashara, tunayo Division ya Kazi, kwa mujibu wa taratibu na sheria hii kwa kufanya mabadiliko Mheshimiwa Jaji Mkuu anaweza akaunda special court kwa kupitia muundo huu ambao nimeuzungumzia hapa ambao inakua division ya Mahakama Kuu hakuna tatizo lolote wala Katiba haijavunjwa kutokana na hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka nizungumzie Muungano. Mheshimiwa Tundu Lissu anasahau kwamba Muungano wetu uliasisiwa na Waasisi hawa wawili, Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao. Kupitia Sheria Na. 4 ya mwaka 1964 iliondoa haya matatizo yote ambayo anazungumzia Mheshimiwa Tundu Lissu. Hata Mwenyekiti wa Marais Afrika anatambua mchango wa Tanzania katika kukomboa Bara la Afrika, siyo kwenda kusababisha Mapinduzi ya Zanzibar, Tanzania ilifanya kazi kubwa Afrika nzima siyo huko. Mimi nilichotegemea ni kwamba kwa Wapinzani wanapaswa kuleta hoja ya kusaidia Wizara hii ya Katiba na Sheria. Siyo kuanza kuzungumza maneno ambayo ni ya uchochezi maneno ambayo hayafai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea Mheshimiwa Tundu Lissu hapa angekuja na akatuambia ni namna gani tutaweza kulizungumzia Fungu Na. 40 ambalo Mheshimiwa Waziri hajalizungumzia, ni namna gani Mahakama itaweza kupatiwa fedha zake kwa mujibu wa taratibu na suala hili halijazungumzwa na Mheshimiwa Waziri. Lakini pia nilitegemea watu wa Upinzani wangezungumzia kuhusu Fungu Na. 55 la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili tume hii iweze kuongezewa fedha.
Ninaishauri Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuweza kuona mchakato wa kuongezea fedha Tume hii ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia niongelee suala la Mahakimu. Mahakimu wetu wanafanya kazi ngumu, nawapongeza sana kwa kuchapa kazi Mahakimu na Majaji wote Tanzania. Ninaomba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kuona uwezekano wa kuwaongezea mishahara Mahakimu wetu, pia kuangalia kuwapatia non- practicing allowance pamoja na rent assistance kwa ajili ya kuwapunguza ukali wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya mishahara kati ya Mahakimu na Majaji ni kubwa sana, ninaomba Mheshimiwa Waziri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuweza kufikiria uwezekano wa kupunguza ukubwa wa tofauti ya mshahara kati ya Hakimu na Jaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka Tundu Lissu pia amezungumzia kuhusiana na Mkuu wa Wilaya kutoa maelekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kusimama ndani ya Bunge lako hili Tukufu, lakini nichukue fursa hii kuwaombea Wabunge wote afya njema ndani ya Bunge lako hili, Mwenyezi Mungu awajaliwe afya njema pamoja na akili timamu katika kuisimamia Serikali yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu, lakini pia nichukue fursa hii kuwakumbuka wazee wetu waliotangulia, nikianza na Bibi yetu Bibi Titi Mohamed ambaye alikuwa Mbunge wa kwanza katika Jimbo la Rufiji, ambalo leo hii historia yake inapotea, hata pale tunapoona sherehe za kumkumbuka mama Bibi Titi Mohamed amekuwa akisahaulika, nichukue fursa hii kumkumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwakumbuke wazee kina mzee Ngauka, mzee Mkali pamoja na Marehemu mzee Mbonde, Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi! (Makofi)
Mheshimiwa Naib Spika, nimkumbuke pia Profesa Idrissa Mtulia ambaye ni Babu yangu huyu, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rufiji na Dkt. Seif Seleiman Rashid ambaye pia alikuwa Mbunge wa Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nizungumze hili kwa kuwa Rufiji imetoa mchango mkubwa sana katika Taifa hili letu. Asilimia zaidi ya 60 ya wapigania uhuru wa nchi hii wote walitoka Rufiji na kama hakutoka Rufiji basi atakuwa na asili ya Rufiji, hata wale Wamakonde watakuwa ni asili tu ya Rufiji. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hili kwa kuwa Rufiji imekuwa ikisahaulika sana kwa muda mrefu sana! Nimesikiliza kwa umakini sana hotuba za Mawaziri wetu wote hata waliopita. Hotuba hata ya Waziri wetu wa Kilimo ameshindwa kuizungumzia Rufiji. Mimi sielewi unapozungumzia kilimo ukashindwa kuisema Rufiji, Bonde la Mto Rufiji, lakini pia hata Mawaziri wengine hata nikija pale kwa Maliasili na Utalii tunafahamu atasoma hotuba yake siku ya Jumanne, lakini nafahamu matatizo makubwa ya kero za wananchi wa Jimbo la Rufiji na inawezekana siku ya Jumanne nisiwepo, niseme tu, Wizara ya Maliasili na Utalii iliweza ku-introduce kodi ya kitanda ambayo ni gharama kubwa kila mwananchi wa Rufiji analazimika kulipa shilingi 130, 000/= kwa kitanda anachokilalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hilo japokuwa nitachangia kwa maandishi. Nirudi katika hotuba yetu hii ya siku ya leo ya Wizara hii. Nimesikiliza kwa makini hotuba ya wenzetu Wapinzani baadhi ya waliokuwa wakichangia, lakini pia mchango alioutoa Mheshimiwa Keissy, siku ya jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Kessy amezungumza mambo mengi sana ya msingi ambayo, niseme Mheshimiwa Waziri ayachukuwe kwa kina sana, ule mgawanyo wa pato hili la Taifa, mgawanyo huu uende vyema na sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji tuweze kunufaika na pato hili la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wengine katika Bunge lako hili Tukufu wameomba wanunuliwe ndege, wengine wameomba meli, wengine wajengewe reli; tunafahamu siku Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hoja zake hapa atajikita sana kwenye reli na ununuzi wa ndege, lakini atasahau yale maeneo ambayo yanahakikisha Chama cha Mapinduzi kinaingia madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Rufiji limemchagua Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa sana wakiamini kwamba kero hizi za kwao walizonazo toka Rufiji inazaliwa mwaka 1890, kabla ya 1900 Rufiji ilikuwepo. Pia kwa kutambua kwamba Rufiji ni kubwa kuliko Mkoa wa Kilimanjaro, Rufiji peke yake, Rufiji hii ambayo ina shule moja tu ya Sekondari kidato cha tano na sita, basi Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu atusaidie sisi Rufiji na nazungumza kwa uchungu kabisa, tuweze kupata angalau barabara ambazo zitawasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo huu wa Pato la Taifa nawaomba Waheshimiwa Mawaziri wawe wanazingatia mchango wa Taifa katika Pato la Taifa. Sisi Rufiji tunayo Selous ambayo ni Hifadhi ya Taifa kubwa kabisa Afrika, lakini pia tunayo misitu, katika pato la Taifa Rufiji tunachangia zaidi ya asilimia 19. Mchango huu mkubwa wa Pato la Taifa tunaochangia Rufiji, mchango huu wote unakwenda kujenga barabara na kutengeneza reli maeneo mengine ya nchi na sisi Rufiji ambao tulikuwepo hata kabla ya uhuru, tunapoizungumzia Rufiji tunazungumzia wakati wa mkoloni ambao tulikuwa na wilaya sita nchini, Wilaya ya Rufiji ilikuwepo. Hakuna asiyefahamu boma lile la Utete, hakuna asiyefahamu katika historia ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani kubwa sana na Waziri wangu huyu, Profesa, sina ubavu wala uwezo wa kumpinga, kwa sababu kwanza yeye ni Profesa na uwezo wake umejidhihirisha baada ya Mheshimiwa Rais kumteua kwa nafasi aliyopata leo hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, yeye atakuwa shahidi mara ngapi nimemfuata kwa ajili ya kuzungumzia barabara zetu za Rufiji, atakuwa shahidi mkubwa. Nimemfuata mara kadhaa, lakini si kwake tu, nimekwenda mpaka kwa Makamu wa Rais kwa ahadi yake ya tarehe 9 Septemba, 2015 aliyoahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ya Nyamwage kuelekea Utete. Rufiji ndiyo wilaya pekee ambayo haiunganishwi na lami japokuwa Rufiji ina zaidi ya miaka 55 katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali itufikirie, kipindi hiki kwa kweli tunawaomba sana. Ahadi za Marais, tukianzia ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati anakwenda kule Selous alipita barabara ya Mwaseni- Mloka, Ikwiriri kwenda Mwaseni, Mloka kule, akielea Selous, barabara hii ni mbovu sana. Leo hii kutoka Mwaseni - Mloka kufika Ikwiriri unatumia zaidi ya saa kumi kwa kilometa 90 peke yake, lakini kutoka Nyamwage kuelekea Utete, kilometa 33 tunatumia zaidi ya saa tano. Hii ni aibu, aibu kubwa sana kwa Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana basi Serikali yetu iweze kutufikiria. Ombi maalum kabisa kwake Mheshimiwa Waziri, nina imani na yeye kama nilivyosema, atufikirie barabara zetu hizi ambazo Marais wetu walituahidi. Barabara ya Nyamwage kuelekea Utete kwenye Makao Makuu ya Halmashauri yetu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri akisimama atueleze anafanya nini kuhusiana na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 257 wa kitabu chake umezungumzia barabara hii itakarabatiwa tu ukarabati wa kawaida. Sasa tunashindwa kuelewa, kwa sababu katika kikao chetu cha mkoa cha barabara Mhandisi wa Mkoa alituahidi kwamba barabara hii itarekebishwa kwa kiwango cha lami, lakini nashangaa katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri amezungumzia ukarabati mdogo. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri suala hili atujibu wakati anajibu hoja zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara ya kutoka Ikwiriri kuelekea Mwaseni, Mloka ni kilio kikubwa. Huku ndiko Serikali inakusanya zaidi ya asilimia 19 ya Pato la Taifa, watalii leo hii wanatumia zaidi ya saa kumi, tunawa-discourage. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa barabara hii ni barabara ya TANROADS sasa wafikirie ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda wangu ni mdogo, nikumbushie barabara ya Bungu kuelekea Nyamisati kwa ndugu yangu, Mwenyekiti wa Wandengereko, Mheshimiwa Ally Seif Ungando na barabara ya Kibiti kuelekea Ruaruke pamoja na suala zima la minara ya simu, nimwombe sana…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha!
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia afya njema sote kuwa hapa. Pia, shukrani za kipekee niwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Rufiji kwa namna ambavyo wameniamini na wakanichagua kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa mara ya kwanza Jimbo la Rufiji tumeweza kuandika historia kwa sababu katika nchi hii toka tumepata uhuru na toka mfumo wa vyama vingi ulipoanza haijawahi kutokea Rufiji kwa Mheshimiwa Rais kupitia Chama cha Mapinduzi kupata kura nyingi. Kwa hiyo, nawapongeza sana wananchi wote wa Jimbo la Rufuji. Pongezi pia nikupe wewe Mwenyekiti, naamini kwa uzoefu na uwezo ulionao wa kisheria utatusaidia na utaliongoza Bunge hili vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwa Mpango huu wa Maendeleo kama ulivyowasilishwa, binafsi nina masikitiko makubwa sana kwa sababu sielewi sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji tuna matatizo gani katika nchi hii kwa sababu katika Mipango yote ya Maendeleo Rufiji tumeachwa mbali kabisa. Labda nilikumbushe Bunge lako kwamba Rufiji tumechangia asilimia kubwa ya upatikanaji wa uhuru wa nchi hii, tukizungumzia Pwani lakini na Rufiji kwa ujumla.
Pia Rufiji inabaki kuwa ni miongoni mwa Wilaya pekee ambazo tumeshawahi kuendesha Vikao vya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi lakini sasa ukiangalia Mipango mingi ya Maendeleo imetuweka mbali kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianzia suala zima la kilimo kama lilivyozungumzwa katika ukurasa wa 17, napata tabu kabisa kwa sababu Mpango huu wa Maendeleo hauzungumzii kabisa ni namna gani Rufiji itarudi katika ramani ya kilimo. Sote tunafahamu kwamba Rufiji miaka ya themanini ndiyo Wilaya pekee ambayo ilikuwa na uwezo wa kulisha nchi hii. Tunalo Bonde la Mto Rufiji, bonde hili ni zuri sana na tunaiomba Wizara pamoja na Kamati zinazohusika basi kufikiria ni namna gani wataweza kuliendeleza bonde hili. Pia tunafahamu kuna baadhi ya miradi kwa mfano ule mradi wa RUBADA ambao ulikuja pale Rufiji, naamini kabisa mradi huu ni mradi ambao watu wameutengeneza kwa ajili ya kujipatia pesa na hauna faida yoyote kwa Wanarufiji. Kwa hiyo, naomba kwanza Serikali ikae chini na kufikiria ni namna gani wataweza kupitia kumbukumbu zote walizonazo ili kuangalia ufisadi mkubwa ambao umeshawahi kufanywa katika mradi huu wa RUBADA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Rufiji tunayo ardhi nzuri na ardhi kubwa isiyokuwa na tatizo lolote la migogoro ya ardhi, tunaiomba Serikali sasa kufikiria mpango wa kuanzishwa Chuo cha Kilimo Rufiji ili sasa kiweze kusaidia suala zima la kilimo kwa sababu tunayo ardhi nzuri sana. Pia mchakato wa uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao, naishauri Serikali uanzie Rufiji kwa sababu tunayo ardhi nzuri yenye rutuba na tunalo bonde zuri. Niseme tu katika nchi hii hakuna ardhi iliyo nzuri kama ya Jimbo letu la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala zima la viwanda, kumbukumbu zangu zinanionesha kwamba Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wake tarehe 9 Septemba, Makamu wa Rais alituahidi mchakato wa ujenzi wa viwanda Rufiji. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa hivi viwanda ambavyo vitajengwa kuanzia Rufiji kwa sababu kila aina ya kilimo sisi tunacho na tunaishauri Serikali sasa mchakato huu uanze haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye tatizo la maji. Ukurasa wa 46 wa Mapendekezo ya Mpango huu wa Maendeleo umezungumzia suala la maji. Sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji pamoja na Majimbo ambayo tunakaribiana, nazungumzia Kisarawe, Mkuranga, Kibiti pamoja na Rufiji yenyewe, tuna shida kubwa sana ya maji. Labda niseme katika Jimbo langu ya Rufiji ni 5% au 6% tu ya wananchi ndiyo wanaopata maji safi na salama. Katika eneo dogo la Tarafa ya Ikwiriri ambayo ndiyo walikuwa wakipata maji safi mota imeharibika huu ni mwezi wa tatu. Mchakato wa tathmini ya utengenezwaji wa mota upo katika Wizara hii ya Maji, huu ni mwezi wa tatu hatujui Katibu Mkuu wa Wizara hii anafanya mchakato gani ili kuweza kuharakisha mota hii kuweza kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoweza kuona maeneo mengine, Ziwa Viktoria wana uwezo wa kutoa maji sehemu moja na kupeleka sehemu nyingine katika Mikoa mbalimbali na sisi tunaishauri Serikali sasa Mpango huu wa Maendeleo kufikiria mchakato wa kuboresha huduma ya maji kwa kutoa maji katika Mto wetu wa Rufiji na kusambaza katika Wilaya zetu zote ambazo zinazunguka katika Jimbo la Rufiji, hii itasaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo, kwa mfano kule Ngarambe kuna tatizo kubwa sana la maji. Akinamama pamoja na watoto wanawajibika kuamka alfajiri kwenda kuchota maji na wengine hawarudi majumbani, wanachukuliwa na tembo, wanauwawa na maeneo mengine wanachukuliwa na mamba! Kwa hiyo, shida ya maji katika Jimbo la Rufiji ni kubwa sana. Tunaomba Mpango huu wa Maendeleo kulifikiria suala hili la maji kwa kuliboresha vizuri kwa kutumia Mto wetu wa Rufiji katika kuliweka sawa.
Mhershimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala zima la afya, mimi nina masikitiko tena makubwa. Niseme tu kwamba tunayo Hospitali yetu ya Wilaya pale iliyojengwa mwaka 60 lakini toka mwaka 60 hakuna ukarabati wowote ambao umeshawahi kufanywa. Mimi mwenyewe nilishaanza mapambano kuweza kuhakikisha kwamba tunapata wawekezaji kutusaidia. Sasa tunaiomba Serikali kuharakisha huu Mpango wa PPP ili wawekezaji wa kutoka Uturuki waweze kutusaidia kujenga hospitali ya kisasa kabisa ambayo itakuwa na European Standard yenye mashine zote za kisasa. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kuharakisha Mpango huu wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tukija suala zima la elimu, niharakishe kidogo kwa sababu ya muda, niseme tu kwamba sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji tuko nyuma sana kwenye suala zima la elimu, hata Serikali imetuacha yaani tumekuwa kama watoto wa kambo, hatujui sisi tuna matatizo gani? Suala la elimu ni shida kubwa hasa ukizingatia Rufiji ni kubwa kuliko hata Mkoa wa Kilimanjaro lakini tuna shule moja tu ya sekondari ya kidato cha tano na cha sita kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa. Tunaiomba Serikali kufikiria mchakato wa kuboresha elimu katika Jimbo letu la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo, kwa mfano kule Mtanange na maeneo mengine watoto hawasomi kabisa kutokana na umbali wa shule za msingi ambapo mtoto inabidi asafiri umbali wa zaidi ya saa tano, saa sita kwenda kufuata shule. Hali hii imewafanya wazazi wengi kushindwa kuwapeleka watoto wao shule. Kwa hiyo, naona kabisa kwamba mchakato huu wa elimu bure sisi wa Rufiji tutaachwa kando kabisa kwa sababu wazazi watashindwa kuwapeleka watoto wao shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija suala zima la mchakato wa benki, mimi niseme Rufiji ni Wilaya ya sita wakati wa mkoloni na ni Wilaya ya 21 wakati tunapata uhuru lakini utashangaa Wilaya hii ya Rufiji kwa namna ambavyo Serikali imeamua kuiacha hatuna hata benki kabisa. Tunawajibika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 120, kwa wale wananchi wanaotoka kule maeneo ya Mwaseni na Mloka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishauri Serikali huu mchakato wa uanzishwaji wa Benki za Ardhi, kama ulivyoainishwa katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 35, tunaiomba Serikali sasa kufikiria benki hizi waanze kujenga katika Jimbo letu la Rufiji kwa sababu tunayo ardhi ya kutosha, hatuna migogoro ya ardhi, ardhi ni bure kabisa tunawakaribisha lakini tunaiomba Serikali pia kuona namna gani ya kuwekeza kwenye suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala zima la miundombinu, nina masikitiko haya mengine kwamba Rufiji japokuwa ni Wilaya ya zamani lakini tunabaki kuwa ni Wilaya pekee ambayo hatuna hata nusu kilometa ya lami. Kama tulivyoona Mapendekezo haya, hakuna hata sehemu moja ambayo inazungumzia Rufiji tutasaidiwa vipi kuboresha miundombinu yetu. Mama yetu Makamu wa Rais pamoja na Rais mwenyewe alituahidi kwamba tutajengewa lami barabara ya kutoka Nyamwage - Utete, ili iweze kusaidia kupunguza vifo vya akina mama ambao inabidi wakimbie Utete kwa ajili ya kwenda kujifungua. Pia barabara ya kutoka Ikwiriri – Mwaseni - Mloka yenye kilometa 90, tunaiomba Serikali kuharakisha mchakato wa ujenzi wa barabara hii na barabara nyingine kutoka Mwaseni - Mloka - Kisaki pamoja na kutoka Mwaseni - Mloka - Kisarawe. Barabara hizi iwapo zitajengwa zitasaidia kufungua biashara na wananchi wa Jimbo langu la Rufiji wataweza kufanikiwa katika mambo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaishauri Serikali na tunaiomba iharakishe mchakato wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi pale Ikwiriri. Tulishatoa ardhi kubwa lakini mpaka leo hii Wizara husika haijachukua hatua zozote za mchakato wa ujenzi wa Chuo hiki cha Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaishauri Serikali kuachana kabisa na mchakato huu wa mambo ya retention. Suala hili litatuletea shida kubwa na tunaiomba Serikali kuepukana nalo, kuacha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuishauri Serikali kuanzisha community centre. Community centre hizi zitaweza kusaidia wananchi wetu kwa maeneo mbalimbali ya vijiji ili waweze kujifunza mambo mbalimbali kwa ajili ya kunyanyua uchumi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naomba maombi yangu haya yote kama nilivyozungumza yaweze kuchukuliwa na kufanyiwa kazi. Vinginevyo kama Serikali haitachukua basi sitaunga mkono kabisa mapendekezo mwezi Machi yatakapoletwa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipewe taarifa kuhusu ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma ambacho kiliidhinishwa na Serikali ya Awamu ya Nne kujengwa katika Wilaya ya Rufiji ambayo tayari ilitenga eneo zaidi ya hekari 200 ambazo hazijatumika mpaka sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu ujenzi wa Chuo hiki utaanza lini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukuwe nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo kwa weledi wake na uchapa kazi katika Wizara hii ambayo anaimudu sana. Sina shaka na uchapa kazi wa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo machache, naomba uweze kutusaidia sisi Wananchi wa Jimbo la Rufiji wenye wimbi kubwa la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rufiji ina ardhi yenye rutuba na bonde zuri katika kilimo. Serikali haijawahi kufikiria uwekezaji wa namna yoyote katika bonde hili toka Adam na Hawa mpaka sasa. Hali hii imepelekea uchumi wetu kuwa na hali mbaya. Ukosefu wa maji, hakuna shule za sekondari (Kidato cha Tano) japo kuwa Rufiji ni kubwa kuliko Mkoa mmoja wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamepata chuki sana dhidi ya Serikali na hili ni dhahiri na matokeo ya uchaguzi uliopita uliokuwa na ushindani
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya njema kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Pili, niwaombe Watanzania nchini kuendelea kupuuza kauli za wanasiasa waliochoka (wazee) ambao mimi nawaita wanasiasa wenye vioja wasiokuwa na hoja. Hivi karibuni kwenye Kigoda cha Mwalimu yupo mwanasiasa mmoja amediriki kumtukana Rais wa Awamu ya Nne, tunamshauri afuate Kanuni 21 ya Kanuni za Uongozi zinazowataka viongozi kufanya tafiti kabla ya kutoa kauli zao, nimeona niliseme hilo kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, nikupongeze kwa kuchaguliwa na Bunge hili kuwa Naibu Spika wa Bunge letu hili. Tunaongozwa na Ibara ya 86 ambapo sisi Wabunge ndiyo tumekuchagua. Pia Ibara ya 89 inatoa Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo ni jukumu letu sisi Wabunge kuzifuata ili sasa tunapokuwa na malalamiko tuyaelekeze huko kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wapongezwa sana humu ndani ya Bunge lako hili Tukufu na mimi niseme tu kwamba, nawapongeza akinamama wote ndani ya Bunge hili na bila kumsahau mke wangu mpenzi Tumaini Mfikwa (Mrs. Mchengerwa na binti yangu Ghalia).
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme hayo nikinukuu yale maneno ya Bibi Titi Mohamed aliyotoa miaka ile ya 55 ambapo bibi huyu kwa mujibu wa wazalendo, wapigania uhuru wa nchi hii wanasema alikuwa ni baada ya Mwalimu Nyerere maana alikuwa tayari kuvunja ndoa yake kwa ajili ya kupigania uhuru wa nchi hii. Nami nawapongeza akinamama wote nchini kwa juhudi kubwa za kupambana na mfumo dume katika nchi yetu hii unaotumiwa na Viongozi wa Chama cha Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona nianze na hilo na nirudi sasa kujikita kwa mujibu wa Kanuni ya 106 ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili ambayo inanipasa nizungumze bila kuomba mabadiliko katika bajeti yetu hii iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Nami niseme kwamba naunga mkono hotuba hii ya bajeti kwa asilimia mia moja, lakini nitakuwa na reservation zangu ambazo nitaomba Mheshimwa Waziri wa Fedha atakapofika hapa aweze kujibu baadhi ya hoja za msingi ambazo naamini kwamba zitasaidia katika kuinua uchumi wa nchi yetu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianzia kwanza kwa Kanuni za Sera ya Fedha zilizotolewa mwaka 2016 lakini pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika ukurasa wa 16 unaozungumzia takwimu za umaskini. Nimefanya tafiti sana na kugundua kwamba takwimu zilizotolewa na Mheshimiwa Waziri amezipata kutoka kwa Halmashauri ya kuonesha kwamba Mkoa wa Pwani ni mkoa tajiri kuliko Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Mheshimiwa Waziri amedanganywa kabisa kwani Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa maskini kabisa katika nchi hii pamoja na Mikoa yote ya Kusini. Labda kama kuna ajenda ya siri sisi watu wa Pwani tusiyoijua, basi tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze hizo ajenda ambazo sisi hatuzijui.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitazungumzia takwimu, ukurasa wa tano wa taarifa ya Mkurugenzi iliyokwenda kwa Mheshimiwa Waziri ambayo Mheshimiwa Waziri ameitumia katika Bunge lako hili Tukufu inaonesha kwamba Watanzania wa Rufiji wanaishi kwa kipato cha Sh. 25,000 kwa siku, huu ni udanganyifu wa hali ya juu. Niseme tu kwamba hakuna Mrufiji anayeishi kwa Sh. 25,000 na hii siyo kwa Rufiji tu hata kwa Mkoa mzima wa Pwani hilo suala ni la uongo wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu hizi zinaonesha kwamba wananchi wa Mkoa wa Pwani wanapata pato la zaidi ya Sh. 700,000 kwa mwaka, huu ni uongo wa hali ya juu. Mimi kama Mwanasheria niko tayari kula kiapo kuthibitisha kwamba uongo huu haukubaliki ndani ya Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kwamba Rufiji tuna zaidi ya square kilometers 500,000 ambazo hizi zilipaswa zitumike kwa ajili ya kilimo, eneo hili kubwa liko ndani ya bonde la Mto Rufiji. Takwimu pia zinaonesha kwamba ni asilimia 0.6 tu pekee ya wananchi wa Jimbo la Rufiji ambao wanajishughulisha na kilimo katika maeneo haya. Pia ikumbukwe kwamba zaidi ya asilimia 99 ya wananchi wa Jimbo la Rufiji wanategemea kilimo, lakini kilimo hiki hata pale wakati ambapo tuliona matrekta yanakwenda maeneo mbalimbali Rufiji hatujawahi kuona trekta hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu hizi nitaendelea kupingana nazo, kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi iliyokuja kwa Waziri wa Fedha, katika ukurasa wa 23 inaonesha kwamba hata vile Vyama vya Msingi vimeanguka na vinadaiwa na wananchi. Hata ukiangalia wananchi wangu ambao wanategemea korosho, korosho imekwama na imeanguka hata katika soko la dunia. Ukiangalia takwimu wananchi wanadai zaidi ya bilioni moja kwa Vyama hivi vya Msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi Mheshimiwa Waziri wa Fedha ana-rely kwenye information baada ya kutuma watu wake kwenda kutafiti na kupata takwimu za msingi kweli vinginevyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha atuambie agenda iliyopo ili kama wanataka kupeleka maendeleo sehemu fulani ijulikane, lakini siyo kutumia takwimu za uongo, nami niko tayari kula kiapo kutokana na suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia bajeti ya kilimo hakuna sehemu yoyote inayozungumzia Rufiji. Waziri wa Kilimo alikiri hilo na akaahidi kupeleka fedha, tunamshukuru kwamba ameahidi kuwasaidia vijana wa Jimbo langu la Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 35 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, inazungumzia kwamba zaidi ya 4.9 percent ya bajeti ya Serikali itakwenda kwenye kilimo lakini Rufiji haipo katika maeneo hayo. Kwa hiyo, hii inaonesha wazi kwamba takwimu zilizotolewa ni za uongo na tunamwomba Waziri wa Fedha sasa kujikita katika kusaidia wananchi wanyonge na maskini. Tunategemea sasa asilimia 40 ya pato hili la Taifa ikasaidie wananchi wanyonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, turudi katika suala zima la elimu. Tarehe 5 Machi, 1998, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:-
“Nobody is asking us to love others more than we love ourselves; but those of us who have been lucky enough to receive a good education have a duty also to help to improve the well-being of the community to which we belong; is part of loving ourselves!” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu alisisitiza akisema kwamba:-
“Education should be for service and not for selfishness”.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hili kwa sababu Rufiji tuna shule moja tu ya sekondari kidato cha tano na cha sita japokuwa Rufiji ilianzishwa miaka ile ya 1890. Mgawanyo wa pato la Taifa ni kikwazo kikubwa na tunaona kwamba asilimia 40 iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo haitawafikia wananchi wanyonge hususani wa Jimbo langu la Rufiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi majuzi niliuliza swali kuhusu wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji wa Tarafa ya Ikwiriri ambao wanapata maji kwa asilimia ndogo tu. Nilipokea majibu hapa kutoka kwa Waziri akituambia kwamba kiasi cha fedha tulichoomba kwa ajili ya ununuzi wa mota tusubiri bajeti ya 2017/2018, huu ni uonevu wa hali ya juu. Hawa ni wananchi wachache wasiopata maji safi na salama wanaambiwa wasubiri bajeti ya mwaka ujao ili kutoa shilingi milioni 36 tu. Ikumbukwe kwamba katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri kuna maeneo ambapo wametengewa zaidi ya shilingi bilioni 100 ya maji sisi Rufiji hakuna hata senti moja. Huu ni uonevu wa mgawanyo wa pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu hapa maneno ya Mwandishi Mashuhuri wa mashairi na mwanaharakati, Maya Angelou ambaye aliwahi kusema:-
“People will forget what you did, but people will never forget how you made them feel”.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema kwamba, maneno ya Mheshimiwa Waziri wa Maji yametufanya tusononeke na tuumie sana katika mioyo yetu kwa kuwa eneo hili la Rufiji ndiyo pekee lenye shida ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu Kanuni 21 za Uongozi, zinazozungumzia The Law of Solid Ground…

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Maxwell aliwahi kusisitiza neno moja la kuwataka...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa, nilifikiri unamalizia kwa kuunga mkono hoja, muda umekwisha.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Hapana siwezi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA YA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitambue michango ya Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako hili Tukufu waliochangia kuhusu taarifa ya Kamati yetu ya Katiba na Sheria. Waheshimiwa Wabunge 21 walichangia kwa kuzungumza lakini pia Wabunge watatu walichangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitambue michango ya Waheshimiwa Mawaziri waliosimama mbele ya Bunge lako hili hususani Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja. Nami nitajikita kwenye baadhi ya hoja ambazo ziliibuka na kuzitolea maelezo na pia kuliomba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo kwenye taarifa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema natoa shukrani za kipekee kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia taarifa yetu hii ya mwaka ambao ni 21. Naanza na hoja ya Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab, Kamati inakubaliana dhahiri kabisa na mapendekezo yake kwamba Bunge liazimie kuitaka Serikali kufanya jitihada za kutosha kupunguza misongamano magerezani, tatizo la ucheleweshwaji wa kesi Mahakamani zinazohusiana na makosa ya mauaji na madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kwamba Kamati ina uwezo wa kulazimisha mahakama na kubadilisha taratibu ili kesi zichukue muda mfupi, sina hakika sana na hoja hii. Niseme tu kwamba kwa kuwa nilipata fursa ya kutumikia mhimili wa Mahakama kwa muda mrefu kidogo nafahamu zipo taratibu za kimahakama ambazo zinafuatwa na Mahakama zetu ikiwa ni pamoja na Katiba na Sheria ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Judicial Administration Act ambayo ilipitishwa na Bunge lako hili Tukufu mwaka 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mchakato wa kunyongwa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa na kama Serikali inashindwa basi kifungu husika kibadilishwe kama ambavyo imezungumzwa na Mheshimiwa Adadi nitalitolea ufafanuzi hapo mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa Mheshimiwa Abdallah Mtolea kuhusu watu wenye ulemavu na kwamba Kamati iliombe Bunge liazimie kwamba bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iongezwe hasa kwa Fungu la 65 linalohusika na kazi na ajira ili kuwe na mazingira bora ya kutengeneza ajira kwa vijana. Kamati pia inapenda kuikumbusha Serikali kwamba kile kiasi cha asilimia 10 kilichotengwa kwa ajili ya vijana na wanawake basi kiasi hiki kisipunguzwe na ile asilimia 50 iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo pamoja na OC asilimia 40. Kwa hiyo, Kamati inaitaka Serikali kwamba kile kiwango cha asilimia 10 kilichotengwa kwa ajili ya akinamama na vijana kiwe ni kiwango asilia isipungue hata shilingi moja ili sasa vijana wetu pamoja na akinamama waweze kufaidika na kiasi hiki cha asilimia 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunatambua kwamba, nchi yetu inaongozwa na Chama cha Mapinduzi. Kwa mujibu wa ukurasa wa 110 wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ilitengwa kiasi cha Sh. 50,000,000 kwa ajili ya kila kijiji. Tunaiomba Serikali kuhakikisha kwamba kiasi hiki cha fedha sasa kimetolewa ili kwenda kusaidia vijiji vyetu katika maeneo yetu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia inakubaliana na mawazo ya Mheshimiwa Mtolea kwamba Serikali iweke msisitizo mkubwa katika kusimamia haki na maslahi ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu adhabu ya kifo, katika taarifa yetu ya Kamati kuhusu Muswada Na.4 wa mwaka 2016 iliishauri Serikali kupunguza misongamano magerezani na kufuata sheria ili adhabu ya kifo ambayo inatambulika kwa mujibu wa Kanuni za Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 iweze kutekelezwa. Adhabu hii ya kifo ipo katika kifungu cha 197 na kifungu cha 196 ambacho kina-establish kosa la kuua. Kamati iliishauri Serikali kwa kuwa kuna mrundikano mkubwa wa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa adhabu hii iweze kutekelezwa mara moja kwa sababu jukumu hili ni la kikatiba na la kisheria. Pia kama Serikali inaona adhabu hii haitekelezeki basi ni vyema ikawasilisha maoni ili iweze kuondolewa kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaendelea kuishauri Serikali utekelezaji wa adhabu hii uendelee kama ambavyo umeainishwa katika kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu, Sura 16. Tunafahamu ni mateso makubwa sana wanayapata wale waliohukumiwa kunyongwa wakisubiri adhabu ya kifo. Wao wenyewe wako tayari kupatiwa adhabu yao ya kifo iwapo itatekelezwa hata kama ni kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengine ni Mheshimiwa Taska Mbogo ambaye yeye amezungumzia suala la NSSF ambalo sitalizungumzia zaidi hapa kwa sababu tayari Mheshimiwa Waziri ameshalidokezea kuhusiana na mchango mkubwa wa hifadhi za jamii katika Taifa letu. Pia kama ilivyoagizwa katika taarifa za Kamati, Kamati inaendelea kusisitiza kwamba maagizo ya Bunge yatekelezwe na taasisi zote kama yalivyoelekezwa kuhusiana na uwasilishwaji wa mikataba ya uwekezaji unaofanywa na taasisi hii ya NSSF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taasisi za usimamizi wa haki, katika taarifa yake Kamati imesisitiza Mahakama na Tume ya Haki za Binadamu ziongezewe bajeti katika mwaka wa fedha ujao wa 2017/2018 ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo. Bajeti hiyo itasaidia utolewaji wa semina ili wadau wawe na uelewa wa kutosha wa sheria zinazopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lucia Michael alizungumzia kwamba jukumu la Polisi sasa limebadilika kutoka ulinzi wa amani na kuelekea kwenye ukusanyaji wa kodi. Kamati pia inaendelea kushauri Serikali kwamba siyo jukumu la Polisi kukusanya kodi kama ambavyo inafanyika leo hii Polisi wanakusanya kodi kwa makosa mbalimbali ya barabarani ambapo wanawakamata washtakiwa na wanakusanya kodi kama wao ni TRA. Kamati inaitaka Serikali jukumu la ukusanyaji kodi liendelee kubaki TRA na kulitaka Jeshi la Polisi kuacha mara moja kufanya kazi hizi ambazo hawawajibiki kwa mujibu wa taratibu na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota alizungumzia kuhusiana na fedha kutolewa chini ya kiwango kilichopitishwa. Msimamo wa Kamati ni kwamba fedha ziongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ucheleweshwaji wa kesi mahakamani ombi la Mheshimiwa Adadi, kama nilivyosema hapo awali jibu katika taarifa ya Kamati kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, tarehe 3 Mei, 2016, Kamati iliagiza Wizara na taasisi zake kuhakikisha kwamba Mahakama inapunguza wingi wa kesi yaani backload of cases mahakamani na kwamba haki itolewe kwa haraka na kwa mujibu wa sheria kwani justice delayed is justice denied.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nimpongeze Mheshimiwa Jaji Mkuu Msatafu Mohamed Chande Othman kwa jitihada zake kubwa alizofanya katika kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani ambapo naamini Kaimu Jaji Mkuu wa sasa hivi anaweza kuendeleza ile njia nzuri ambayo alianzisha Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taarifa ya Kamati kwa ujumla, Mheshimiwa Mtolea alisema kwamba taarifa imebeba maudhui mengi ya kikatiba na kisheria. Labda niseme tu kwamba Kamati ya Katiba na Sheria mpaka sasa imeshawasilisha Bungeni taarifa tisa, tatu za kibajeti na sita za Miswada ya Sheria. Kamati pia ilitoa maoni na mapendekezo ya jumla kuhusu Wizara na taasisi inazozisimamia, masuala ya kazi, ajira na watu wenye ulemavu yapo katika taarifa rasmi ya Kamati yaliyosomwa hapa Bungeni tarehe 19 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ngombale alizungumzia kuhusu Mabaraza ya Ardhi pamoja na uboreshwaji wa Kamati. Kamati pia inaishauri Serikali hususani Wizara ya Katiba na Sheria na tutaona uwezekano wa kukaa na Wizara hii ili kuweza kuzungumza na Mheshimiwa Waziri kuona uwezekano wa kesi za ardhi kurudishwa katika Mahakama ya Tanzania; kwa sababu tunafahamu kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107 inaitaja Mahakama kama ndiyo mhimili wa utoaji haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba upo mkinzano unaotokana na Mabaraza kuwa chini ya mihimili tofauti. Mfano, Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji yapo chini ya TAMISEMI, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya yapo chini ya Wizara ya Ardhi lakini pia ipo Mahakama Kuu ambayo inawajibika chini ya Mahakama. Hivyo, Kamati inaona kuna mwingiliano mkubwa wa haki katika Mahakama na Serikali na ipo sababu kubwa hapo baadaye kuwepo na kesi nyingi za kikatiba kupinga hukumu zilizotolewa katika Mabaraza ya Ardhi kwa kuwa jukumu la mwisho la utoaji haki lipo chini ya Mahakama ya Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Omary Mgumba amechangia kuhusiana na mgogoro wa wakulima na wafugaji. Jambo hili sina hakika kabisa kama limeelekezwa kwenye Kamati yangu au ile Kamati ya Utawala lakini nataka niseme tu kwamba ni kweli kabisa mgogoro wa ardhi ni mkubwa sana katika nchi yetu na tunaona kabisa kwamba ile misingi imara aliyotuachia Mwalimu Nyerere ya Watanzania kupendana inakwenda kuvunjika iwapo migogoro hii ya wakulima na wafugaji haitatatuliwa mara moja. Hivyo, tunaona kabisa kwamba Wizara ya Kilimo na Mifugo imeshindwa kutatua mgogoro huu na tunaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu sasa kuingilia kati ili kuweza kuondoa matatizo haya yaliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima itambulike kwamba hakuna mgogoro wa ardhi, mgogoro uliopo ni mwingiliano wa kijinai yaani criminal trespass kati ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, hatuna migogoro ya ardhi na naamini kabisa kwamba nchi yetu ina ardhi kubwa, mgogoro huu iwapo utatatuliwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa utaweza kwisha mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Frank Mwakajoka alizungumzia kuhusiana na watu kukata tamaa kupiga kura. Kamati yetu kwa kuwa inasimamia Tume ya Uchaguzi tunaiagiza Serikali kuongeza fungu kwa ajili ya Tume ya Uchaguzi ili kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wananchi kukamatwa kwa kutoa taarifa za njaa, tunaishauri pia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kuendelea kutoa taarifa kuhusiana na majanga na maafa ili iweze kuondoa kero kubwa ambayo inajitokeza hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Cecilia Paresso alizungumzia kuhusiana na ucheleweshwaji wa kesi kwamba viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakikamatwa na kesi zao hazichukui muda mrefu. Ni jukumu la utendaji haki kama ilivyo katika Katiba kwamba ni lazima haki iendelee kuonekana imetendeka. Naamini kabisa kwamba siyo jambo la busara kwa kiongozi kuendelea kubaki mahakamani kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tunaishauri Mahakama kuendelea kusikiliza kesi haraka hususani zinazowahusu viongozi wa vyama vya kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia itambulike kwamba zipo taratibu za rufaa ambazo zimeainishwa katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunawaomba wale wote ambao wana malalamiko kuhusiana na kesi basi wafuate taratibu za rufaa ambazo zimeainishwa katika Katiba, lakini pia katika sheria mbalimbali za nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la akinamama magerezani, Mheshimiwa Mbaruk alizungumzia suala hili. Kamati inakubalina na mawazo ya Mheshimiwa Mbunge kwamba maslahi ya watoto yazingatiwe yaani best interest of the child pale ambapo wafungwa wanajifungulia magerezani. Kamati inasisitiza kwamba watoto wanaozaliwa katika mazingira haya watazamwe kwa umakini kwa ajili ya haki zao kama watoto kwa mujibu wa Sheria ya Watoto ya mwaka 2009 lakini pia na Mkataba wa Haki za Watoto wa mwaka 1989. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Paresso pia aliendelea kusisitiza kuhusiana na mrundikano wa wafungwa gerezani na utawala wa sheria. Suala hili Kamati inalitambua na inaungana na maoni ya Mbunge kwamba Serikali na Mahakama zifanye jitihada za kutosha kupunguza mrundikano wa kesi na wafungwa magerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango iliyotolewa kwa ujumla ni kuhusu mrundikano wa wafungwa magerezani, wingi wa kesi mahakamani na kasi ndogo ya kumaliza kesi, haki za watu wenye ulemavu, suala la ajira na vijana, uongezaji wa bajeti katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ukaguzi wa miradi ya maendeleo, muda wa kikanuni uongezwe na jengo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali lipewe kipaumbele. Kamati inakubalina na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge na inaomba yawe sehemu ya mapendekezo ya Kamati na Bunge hili iyakubali kama maazimio ya Bunge yalivyotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba Bunge lako sasa lipokee na kuikubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo kwenye taarifa hiyo pamoja na yale mengine ambayo nimeyasoma katika Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mbunge na Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache sana. Jambo la kwanza, naipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ya kuwatumikia wanyonge; pili, nyongeza ya Wizara, hii Bajeti itaweza kuwasaidia Watanzania wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Jimbo langu la Rufiji. Kwa bajeti mbili sasa za Wizara hii, Serikali imesahau Wilaya ya Rufiji. Mwaka 2016 haikutengwa fedha yoyote kwa ajili ya Hospitali yetu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rufiji ni moja ya maeneo ambayo Serikali inapaswa kutoa kipaumbele sana. Hii ni kutokana na kwamba, kwa muda mrefu Jimbo la Rufiji limesahaulika. Kwa sasa tuna changamoto kubwa sana za kiusalama; kumewepo na ujambazi mkubwa na mauaji yanayoendelea; na kunahitajika mahitaji makubwa ya huduma bora za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ilijengwa mwaka 1960, lakini mpaka sasa haijawahi kukarabatiwa na majengo mengi ni mabovu yanayohitaji kubomolewa. Hakuna hata vitanda vya upasuaji; kilichopo kimoja ni cha miaka ya 1960; hali ya hospitali ni mbaya sana. Wakati wote yanapotokea matatizo makubwa kwa watu kudhuriwa kwa risasi, tunalazimika kusafirisha majeruhi kwenda Wilaya ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rufiji ilizaliwa kabla ya uhuru, lakini ndiyo Wilaya yenye matatizo makubwa. Umuhimu wa kuiboresha Hospitali ya Wilaya hauepukiki, kwa kuwa umbali uliopo kutoka Rufiji kwenda Hospitali ya Mkoa wa Pwani ni wa masaa zaidi ya sita kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Utete. Wagonjwa wengi hufia njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naipongeza Serikali kwa kutuletea Mganga Mkuu Mchapakazi. Naomba huruma ya Mheshimiwa Waziri, akisaidie Kituo cha Afya Ikwiriri kuongeza vifaa na ununuzi wa jenereta; Kituo cha Afya Moholo, kutuongezea fedha za ununuzi wa vifaa; na ujenzi katika Kituo cha Afya Mwaseni Mloka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akifika hapa azungumze kauli ya Wizara yake ili kuweza kusaidia Watanzania wanyonge walioko Rufiji ambao hukosa msaada wa matibabu kutokana na hali ya Hospitali yetu ya Wilaya iliyojengwa mwaka 1960; akinamama wanakufa kutokana na uhaba wa Watumishi, kuwahudumia majeruhi wanaoshambuliwa na majambazi, matatizo yanayoendelea kila wiki sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa fursa. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kwa kuendelea kuniombea dua hususani katika kipindi hiki ambacho ni kipindi kigumu kabisa kupata kutokea kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani hususani wakazi wa Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kufanya kazi nzuri kabisa katika Wizara hii ambayo ni moja ya Wizara ngumu kabisa katika nchi yetu hii. Mheshimiwa Waziri yeye pamoja na timu yake wamefanya kazi nzuri na mimi nawapongeza sana, sisi wananchi wa Rufiji wametusaidia kwa mambo kadhaa ambayo nitayazungumza hapo mbele lakini pia nimpongeze Mkurugenzi yule wa Misitu Ndugu Mohamed, nimpongeze Meneje wetu wa TFS kutoka kule Rufiji ambae marazote amekuwa akitatua kero za wananchi wangu na mimi namfananisha Profesa Maghembe na kanuni ya kwanza ya uongozi iliyowahi kutolewa na Dkt. John Maxwell ambae aliwahi kuandika kitabu chake The Laws of the Leadership akisema kwamba; “Personal and organizational effectiveness is proportional to the strength of a leadership” na mimi namuona yeye kama ni kiongozi ambaye ameweza kuimiliki Wizara hii na ninaamini Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati anakuteua aliamini wewe ni muadilifu na umechapa kazi. Wizara hii ina madudu mengi sana na kama ungekuwa umeyumba kidogo basi Wizara hii kwa kweli ingekushinda mapema sana.

Lakini nikupongeze kwa kusimamia Ibara ya 26 ya Katiba na kumtaka kila Mtanzania kusimamia na kufuata sheria za nchi yetu na hii nimeiona kwasababu wakati wa mijadala ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii tumeona hoja nyingi zinazoibuka ni hoja zilizopo kwenye Wizara ya Kilimo na Mifugo na ni wewe sasa umekuwa kama Waziri wa Kilimo na Mifugo lakini pia umekuwa kama Waziri wa Ardhi na umeendelea kuchapa kazi na mimi naomba niwakukmbushe Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakumbuke kwamba Ibara ya 26(2) inatupa mamlaka sisi Wabunge iwapo tunaona sheria yoyote ambayo inasimamiwa na Profesa Maghembe sheria ile inakinzana na matakwa ya nchi yetu tuliyonayo sasa basi ni vyema Wabunge sasa tukaleta sheria ile ndani ya Bunge lako hili tukufu kupitia Ibara ya 64 ya Katiba ili tuweze kubadilidha sheria ile na tusimlaumu Profesa Maghembe kwa kuwa anasimamia Ibara ya 26 ya Katiba ya kusimamia na kufuata sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magazeti mengi ya wiki hii yameandika mambo mengi kuhusu Rufiji, Kibiti na Mkuranga. Gazeti la leo la Citizen limeandika taarifa kwamba; “Why Rufiji residents are reluctant to cooperate over murders” lakini gazeti la jana ninalo hapa limeandika taarifa kwamba; “Rufiji families pain after losing their lovely ones.”

Jana mmoja wa wahanga aliyepigwa risasi siku tatu zilizopita amefariki jana alipigwa yeye na baba yake, yeye lipigwa risasi ya tumbo na jana amefariki na tunamshukuru Mbunge wa Kibiti kwa kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba mwili ule unafika Kibiti na shughuli za maziko zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie katika Bunge lako hili tukufu, unao Wabunge watatu ambao wanaishi katika maisha magumu sana kupata kutokea katika nchi hii; Mbunge wa Mkuranga, Mbunge wa Kibiti pamoja na Mbunge wa Rufiji. Tunaishi katika maisha magumu sana na siyo sisi tu hata katika familia zetu, lakini pia hata wapiga kura wetu wanaishi katika maisha magumu sana. Wananchi wamekonda sana hawawezi hata kushiriki katika shughuli za maendeleo hali ni mbaya sana na tunaiomba Serikali jambo hili kulifanyia kazi haraka kwasababu jambo hili linaendelea kutanuka na jambo hili siyo dogo kama ambavyo Wabunge wengine wanaweza kufikiria hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wamekuwa wakihoji maswali ni kwa nini Wabunge hawazungumzi ndani ya Bunge? Tunafanya hivi kwa makusudi kabisa lakini tunataka wananchi wetu wajue tunafanya kazi kubwa kuhusiana na jambo hili lakini yapo mambo sisi hatuwezi kuyazungumza kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani wananchi wangu wa Ikwiriri wanakushukuru sana kwa kufika, kujionea familia ambazo ziliathirika ambazo waume zao wamepigwa risasi na kufariki, wananchi wangu wanakushukuru sana. Lakini nataka niseme Serikali isikie na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ajue kwamba mambo haya yanayotokea hayatokei kwa bahati mbaya, mambo haya yana root cause, mambo haya yamepangwa, tunataka Serikali ijue hilo. Yapo mambo mengi, zipo chuki nyingi ambazo zimejengwa kwa wananchi, zipo chuki nyingi, yako mambo mengi ambayo yalifanyika yanatoa kero kubwa kwa wananchi ndiyo maana hata gazeti la leo lilipoandika taarifa hizi mimi siashangaa sana kwasababu ninajua kwamba yako mambo ambayo Serikali sasa inapaswa kuyafanya na inatakiwa iyafanye sasa wala isisubiri kwa sababu jambo hili ni kubwa na linaendelea kutanuka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi naomba katika miongoni mwa mambo ambayo sisi tunaendelea kumpongeza Rais wetu ni terehe 31.03.2017 Rais Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kufanya kikao chake na Waziri Mkuu wa Ethiopia alikubali kuwasaidia Watanzania kwa kuonyesha dhamira ya kujenga Stigler’s gauge iliyopo kule Rufiji ili wananchi wetu waweze kupata umeme wa uhakika kwani tunaamini kabisa miongoni mwa kero kubwa za wananchi wangu ni kutokuwa na umeme kwa takribani miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mwaka wa pili sasa wananchi hawana umeme wa uhakika sasaa hizi ni miongoni mwa kero kubwa ambazo wananchi wangu wanazo na leo nazungumza kwa uchungu kabisa, kero hizi muunganiko wa umeme ni kilometa nane tu lakini Waziri wa Nishati na Madini ameshindwa kutuunganishia umeme kwenye Gridi ya Taifa kwa miaka mwili wananchi wa Kibiti, wananchi wa Rufiji na wananchi wa kutoka kule Kilwa hawapati umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili na tunaamini kabisa kwamba uzalishaji wa umeme upo kwenye Stigler’s gauge utasaidia upatikanaji wa umeme katika maeneo mengine hiyo ni miongoni mwa kero kubwa tulizonazo kwasababu tatizo hili ni kero kama nilivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo tatizo la barabara ambalo Mheshimiwa Rais amekubali kutujengea barabara yetu ya Nyamwage kwenda Utete na mimi naomba nimpongeze na ninaomba wananchi watambue kwamba kero hii ya barabara imepatiwa ufumbuzi nasema haya kwa sababu ya kiini cha tatizo tulilonalo, wananchi wanalalamika sana na hatuna sababu ya kwa kweli kwa nini tuendelee kukaa kimya.

Nikuombe sasa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii nirejee kwako, zipo kero katika maeneo yetu. Kwa mfano, katika Kata ya Kipugira watu wako wanaweka GPS kwenye nyumba za wananchi wetu, lakini naomba niikumbusghe Wizara yako kwa kusimamia Katiba; Ibara ya 16 ya Katiba inatoa uhuru wa faragha, lakini swali hili nilimuuliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ni kwa nini Wizara yako inaweka GPS kwenye nyumba za wananchi wangu? Wanavunja ibara ya 16 ya Katiba ambayo inatoa haki ya faragha ambayo kila mwananchi anayo haki ya ku- enjoy haki ya faragha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimuombe Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa unipe majibu kuhusiana na jambo hili ni kwa nini Wizara yako sasa inakiuka Ibara ya 16 ya Katiba lakini pia nimuombe Mheshimiwa Waziri akisimama hapa atuelezee tarehe 9 Septemba Waziri Mkuu alifika Rufiji na katika maeneo aliyokwenda ni pale Utete na alijionea wananchi walikuwa na malalamiko mengi sana. Upo msitu wa Kale ambao wananchi wa Utete pamoja na Chemchem wamekuwa wakiutumia kwa kilimo kwa miaka mingi sana.

Mheshimiwa Waziri naomba nikukumbushe nafahamu kuna tamko la Waziri Mkuu la upimaji upya wa maeneo yetu, lakini tukumbuke kwamba michoro ya awali ambayo Wizara yako inatumia ni michoro iliyochorwa na wakoloni mwaka 1936. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utambue dhamira ya wakoloni ya kuchora michoro ile ni kwa sababu population ya Tanzania ilikuwa bado ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule wa mkoloni tulikuwa tunazungumzia population ya watu milioni nane mpaka milioni 10. Lakini leo hii Mheshimiwa Waziri tuna watu zaidi ya milioni 55 na Rufiji wakati ule tulikuwa kuna watu ambao walikuwa hawazidi hata 20,000; 30,000, lakini leo hii tunapozungumza tuna wananchi zaidi ya 200,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe ulisimamie hili, lakini hii ni pamoja na Kata yangu ya Mbwala katika vijiji vya Nambunju pamoja na Kitapi, maeneo haya yote Wizara yako imeanza kuyapima upya na Wizara sasa inachukua maeneo yote ambayo wananchi walikuwa wakiishi na kutaka kuyafanya maeneo yale ya misitu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri uzingatie hili kwani ukichukua maeneo haya wananchi hawatakuwa na pa kwenda kabisa. Nikuombe ulisimamie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine kuhusiana na hotel levy; kodi hii ya hotel levy ambayo imekuwa ikitolewa kwenye nyumba za kulala wageni, kodi hii ni kero kubwa sana. Tukuombe sasa Wizara yako iweze kulingalia kulipitia kwani wananchi wanaomiliki nyumba hizi za wageni wanalipa shilingi 100,000 ya leseni kwenye Halmashauri, lakini pia wanalipa hii hotel levy. Wakati huo huo wanalipa tena kodi ya mapato TRA shilingi 560,000, wakati huo huo wanalipa hotel levy, wanalipa tena leseni, wanalipa gharama kubwa sana. Wananchi wangu kuanzia Jaribu Mpakani kwenda moja kwa moja Kibiti mpaka kule Mkuranga na Rufiji wanalalamika sana kuhusiana na kodi hii. Na nikuombe Mheshimiwa Waziri basi muweze kuingalia na kuweza kuona namna gani mtaweza kuitatua suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija pia katika suala zima la mahusiano kati ya Wizara yako na wananchi wetu wanaozunguka vijiji, nikuomba Mheshimiwa Waziri sasa ukija kujibu hapa ueleze mkakati wako wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 4, mwezi wa Tano, mwaka huu, 2017, nilisimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu, nikitoa pole kwa familia ya ndugu Chanjale aliyepigwa risasi kule Ikwiriri Kata ya Umwe, na leo nimesimama kwenye Bunge hili Tukufu nikitoa pole kwa familia ya mmoja wa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM aliyepigwa risasi zaidi ya nane jana, Ndugu Alife Mtulia ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kutoka Rufiji pia ni mkazi wa Jimbo la Kibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio haya yanayoendelea katika eneo letu la Pwani yanadhamiria kutukwamisha kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo nami nataka niendelee kuwasihi wananchi wa Rufiji, Mkuranga na wakazi wa Kibiti kuendelea kuchapa kazi na kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi. Hapa nataka niwakumbushe tu kwamba hakika Mwenyezi Mungu amekadiria maisha ya kila mwanadamu, na tunaamini kabisa kwamba mwanadamu anapozaliwa miezi mitatu tu akiwa tumboni mwa mama yake tayari Mwenyezi Mungu anakuwa ameshamuandikia mambo yake yote katika dunia. Qurani inasema Kulla maagh yuswibana inna maagh katana llaahu lanah ikimaanisha kwamba hakika Mwenyezi Mungu ameshamkadiria mambo yake kila mwanadamu aliyezaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, kwanza kabisa wananchi wa Rufiji tunatambua sana umuhimu wa elimu na umuhimu wa elimu hii kwa sisi wenye imani ya kiislamu tunatambua kwamba wahyi wa kwanza kabisa Mtume wetu Muhammad kuupokea ilikuwa inahusu elimu. Katika Sura ile ya Iqra ambayo Mtume wetu alikabidhiwa na akiambiwa asome, niseme mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba umuhimu wa elimu umesikilizwa katika kila sehemu na wananchi wa Rufiji wamepata bahati kubwa ya kupata Mbunge ambaye ni msomi na ana uwezo wa kusaidia kuwapambania katika jambo hili la elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza sana Serikali, nimpongeze sana Waziri wa Elimu. Kwanza kabisa Waziri wa Elimu alivunja historia na rekodi kwa kufika Rufiji kwa mwaliko wa Mbunge, alifika Rufiji akajionea hali ya miundombinu ya shule zetu za Rufiji, wananchi wa Rufiji wamenituma nikuambie wanakupongeza sana na uchape kazi sana. Wako nyuma yako, lakini kwa namna ya kipekee kabisa wanakushukuru sana kwa kutoa shilingi milioni 259 kwa ajili ya ukarabati wa shule ya sekondari ya Utete. Wananchi wa Rufiji pia wanakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kukubali ombi la Mbunge la kutoa kibali cha shule ya sekondari Umwe ambacho kilikaa kwa zaidi ya miaka kumi kutosajiliwa. Wananchi wote wa Ikwiriri wanakupongeza sana na wanakukubali kweli, tunakuombea afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wamenituma, wameniambia kwamba walikupa maombi ya kukarabati shule yetu ya sekondari ya Muhoro pamoja na shule ya sekondari ya Ikwiriri. Hali ya miundombinu ya shule zetu umejionea Mheshimiwa Waziri, tunakuomba sasa utusaidie. Kwa sababu katika Mkoa wa Pwani, Rufiji umeweza kutupatia shilingi milioni 259 tu, tunakupongeza. Wananchi wa Kibiti pia kupitia kwa Mbunge wao, Mheshimiwa Ally Seif Ungando, wameniambia pia nikuambie wanakupongeza sana kwa kutoa kiasi cha shilingi 1,700,000,000 kwa kukarabati shule ya sekondari Kibiti, wanaomba pia uwasaidie kukarabati shule ya sekondari Zimbwini, shule ya sekondari Bungu, shule ya sekondari Mlanzi pamoja na shule ya sekondari Nyamisati ambayo umetoa shilingi milioni 260 pamoja na shukrani kwa kutoa shilingi milioni 253 kwa kukarabati shule ya sekondari Mtanga kule Delta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Rufiji umetoa kwa shule moja, nikuombe sasa utusaidie wananchi wa Rufiji, wapo wengi hapa wanaomba wapatiwe viatu kwa kuwa wana miguu, binafsi miguu sina.

Kwa hiyo, nikuombe lile tamko lililowahi kutolewa na Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Kwanza la miaka ya 1970 la kuboresha elimu katika maeneo ya watu ambao walikuwa hawajasoma sana, leo hii tumejionea Maprofesa hapa kama Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, ni miongoni mwa watu waliosoma wakati ule ambapo waliweza kusaidiwa na Mwalimu Nyerere na wakapata elimu kwa kuwa maeneo yao hayakuwa na mwamko wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba watu wa Rufiji sasa utusaidie, utuletee mwamko wa elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule zetu na wananchi wanaamini kabisa kwamba maombi yao haya utayachukua, utayapokea na kuyafanyia kazi. Pia kwa namna ya kipekee wanaomba utusaidie kwa kupitia Mfuko wa Elimu utuboreshee shule yetu ya msingi Umwe, shule ya msingi Mgomba, shule ya msingi Muhoro, shule ya msingi Ngarambe, na ninamuomba Waziri wa TAMISEMI pia alichukue hilo na aone umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaboresha suala zima la elimu katika maeneo yetu ya Mkoa wa Pwani, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa namna ya kipekee kabisa, tuwaangalie wananchi wa Pwani; kama ambavyo alifanya Mwalimu Nyerere, haitakuwa dhambi kufanya ili kuwapa manufaa wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao kwa kweli wameathirika kwa hali na mali kutokana na tatizo la kukosa elimu. Nikuombe wakati Mheshimiwa Waziri unahitimisha hapa utusaidie suala zima la mikopo, Bodi ya Mikopo iweze kuwaangalia wananchi wa Rufiji, watu wa Mkuranga, watu wa Kibiti na watu wa Kisarawe ambao wamekosa elimu, wakati wa mgao huu wa Bodi ya Mikopo basi waweze kufikiriwa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Rufiji wamenituma, wameniambia kwamba wanacho Chuo cha Maendeleo pale Ikwiriri (FDC), ulifika mwenyewe ukajionea, wanaomba chuo kile sasa kiwe ni Chuo cha VETA kwa sababu kutoka Rufiji kwenda Kibaha kufuata elimu hii ya VETA ni mbali sana kwa zaidi ya saa sita. Wanaomba sasa Chuo hiki cha FDC uje utuambie mtakiboresha ili kiwe ni Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mnaboresha elimu kwa watoto wetu, tunaomba muangalie, yapo maeneo Rufiji ambapo hakuna shule, ni umbali mrefu, kwa mfano kule Mtanange kijijini kwangu wapo watoto zaidi ya 500 ambao hawasomi kabisa, lakini yapo maeneo Kata ya Mgomba kule Mupi, wapo watoto wengi ambao hawasomi kabisa. Tukuombe Mheshimiwa Waziri tuletee wataalam wako waweze kuangalia ni namna gani wataboresha elimu. Ninaamini kabisa iwapo tutaboresha elimu tatizo hili ambalo linaendelea leo hii halitakuwepo tena kwa sababu tutakuwa na wasomi wengi eneo letu la Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, zipo shule ambazo tunahitaji kukarabati, tunakuomba kupitia Mfuko wa Elimu utusaidie. Kwa mfano, ipo shule ya msingi Mchengerwa iliyopo kule Miangalaya ambayo nimeanza ujenzi wa darasa moja lakini pia tunayo shule ya msingi Kilindi ambayo imetoa madaktari wengi lakini shule hii ni shule ya miti tu na watoto wetu wanapata taabu sana inaponyesha mvua na wakati mwingine jua linapokuwa kali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wakizungumzia suala zima la kuwaruhusu watoto wetu waliopata ujauzito kuendelea na masomo. Mimi ninaomba niwakumbushe sana Waheshimiwa Wabunge kwamba suala hili iwapo wataendelea kulisogeza mbele sana wakumbuke wanavunja Ibara ya Tano ya Katiba kwa kutaka kuwaruhusu watoto wetu kushiriki kwenye shughuli za ngono.

Mimi ni muislamu, nilisema hapa, nitashangaa sana kuona Wabunge waislamu wakishabikia suala hili na kutaka watoto wetu washiriki kwenye shughuli za ngono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Qurani inatuambia nilisema hapa, nataka nirudie inasema kwamba wallah takrabu zinah inah kanah taishatan wasahalan sabilah. Waislamu tumezuiwa kabisa, na jambo hili iwapo tutaendelea kuwasaidia watoto ambao wamepata ujauzito waendelee na masomo ni sawana kwenda kuongeza mafuta katika moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe, wakati ule ambapo Wazungu wanaondoa biashara ya utumwa, miaka ile ya 1800 ....

TAARIFA...

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa aliyoitoa ni sahihi, suala hili syo la udini lakini nataka niseme tu kwamba suala hili ni muhimu sana kwa Watanzania wakalitambua ni vema Watanzania sasa wakalea watoto wao kwa misingi ya elimu ya dunia na elimu ya ahera, ndiyo maana nikasisitiza hapa kwamba kuliweka jambo hili ni kusisitiza na kuwataka watoto wetu washiriki katika mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 2 Februari, 1835, Lord Maclay, mmoja wa Wabunge mashuhuri kule Uingereza aliwahi kusema kwamba Afrika hatuwezi kuitawala mpaka pale ambapo tutaweza kudhibiti elimu yao na kuhakikisha kwamba wanafanya mambo kutokana na tunayotaka kuyafanya. Ninaamini, nimeona Wazungu wakiwepo katika Bunge lako hili Tukufu na ninaamini… (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: …ninaamini suala hili wapo watu wana-engineer ambao wanalitaka jambo hili. Mheshimiwa Lord Maclay alisema maneno haya, naomba niwanukuu kwa kiingereza:

“I have travelled across the length and breadth of Africa and I have not seen one person who is a beggar, who is a thief such wealth I have seen in this country, such high moral values, people of such caliber, that I do not think we would ever conquer this country, unless we break the very backbone of this nation, which is her spiritual and cultural heritage and therefore, I propose that we replace her old and ancient education system, her culture, for if the Africans think that all that is foreign and English is good and greater than their own, they will lose their self esteem, their native culture and they will become what we want them, a truly dominated nation”

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya siyo ya kwangu ni maneno yaliyowahi kutolewa tarehe 2 Februari,1835. Ninaomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge iwapo wanasisitiza jambo hili wakumbuke Bunge lililopita tulifanya marekebisho ya sheria hapa, Sheria Na. 253. Kwa mujibu wa marekebisho haya ya Sheria Na. 353, kifungu cha 61 ambacho kilitoa mamlaka kwa Serikali kuhakikisha kwamba watoto wote wanaoshiriki katika masuala ya uasherati pamoja na ngono wadhibitiwe. Kuliruhusu jambo hili ina maana kwamba tunakinzana na kifungu hiki cha Sheria Na. 61 ambayo Bunge hili lilitunga kifungu hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa wa Sheria ya Elimu, kifungu cha 60(b) ambacho kimetoa mamlaka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwa niaba ya Wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji basi naomba nitoe mchangi wangu kuhusiana na bajeti hii iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako hili tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii nimpongeze sana Wazari wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kuja na bajeti nzuri ambayo imezingatia maoni ya wananchi, maoni ya Wabunge na maoni ya wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwasababu ukiiangalia bajeti hii na ukipitia takwimu zilizowahi kutolewa na Central Intelligence Agency (CIA) katika dondoo zao za World Fact Book ambazo waliwahi kuzitoa ambazo zimeelezea mipango mbalimbali ya bajeti ambazo zinatolewa na ambazo
zinatolewa na CIA katika takwimu zao zinazotolewa mara kwa mara ambazo zinachunguza nchi mablimbali zaidi ya
267. Katika takwimu zilizotolewa na World Fact Book zinaifanya bajeti yetu ya Tanzania kuwa ni miongoni mwa bajeti bora kabisa hapa Afrika na dunia na ukiangalia takwimu hizi zimegawanya bajeti katika maeneo matatu; yaani nchi zinazojitegemea, nchi tegemezi na nchi zingine zikijumuisha nchi za Ulaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, bajeti yetu ni dhahiri kabisa ni stimula to economic sector na imedhamiria ku- alleviate poverty katika nchi yetu hii ya Tanzania. Niipongeze Serikali sana kwa namna ya kipekee kabisa ambavyo imedhamiria sasa kutukwamua Wananchi wa Jimbo la Rufiji. Tukiangalia miradi mbalimbali ya Benki ya Dunia imefika Rufiji leo hii kutokana na maombi ya Mbunge wa Jimbo la Rufiji na tumeweza kupata miradi kadhaa ya kutoka Benki ya Dunia ambapo sasa wananachi wangu wa Kata ya Mbwala wataweza kupata maji ya kutosha katika maeneo ya Nambunju, Tawi, Kikobo lakini pia katika maeneo mbalimbali maeneo ya Miangalaya, Namakono, Tawi, Siasa kule Utete na pia Serikali imedhamiria kuchimba visima viwili katika Kata ya Chumbi na haya yote yalikuwa ni maoni yangu na maombi yangu kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imekubali kutuchimbia kisima katika shule ya sekondari ya Mkongo pamoja na kusambaza mabomba katika kata hii ya Mkongo lakini pia katika kata ya Ngarambe, Njawanje, Kingulwe na Namakono, Kipugila pamoja na maeneo ya Nyaminywili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema niipongeze Serikali kwasababu maeneo yetu mengi wakati Serikali inafikiria kumkwamua Mwanamke au Mwanamama kumtua ndoo kichwani sisi kule wananchi tulidhamiria kuondoa vipara kichwani kwa akina mama kwa sababu wananchi wetu wamekuwa wakibeba maji katika umbali mrefu zaidi ya kilometa saba na yako maeneo na baadhi ya vijiji ambavyo wananchi wamediriki kuhama vijiji vyao kwasbabu tu ya kutokupatikana kwa maji. Kwa hiyo, kwa namna ya kipekee kabisa naipongeza sana Serikali kwa kudhamiria sasa kutatua kero ya maji kwa wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija upande wa pili kuhusiana na suala zima la kilimo kama ambavyo Mwalimu Nyerere aliwahi kusisitiza katika kitabu chake cha Ujamaa kwamba “The hidden story of the sociallist village” kilichowahi kutolewa mwaka 2008 na kikarekebishwa tena mwaka 2014 na Bwana Ibott aliwahi kusisitiza kuhusiana na vijiji vya ujamaa katika kuboresha na kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchumi wa kujitegemea sisi wenyewe Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi Wananchi wa Jimbo la Rufiji tunayo ardhi iliyo nzuri yenye rutuba na tunaamini kabisa ardhi ya Rufiji inaweza kulisha Nchi yetu hii ya Tanzania lakini pia inaweza kulisha mpaka Afrika Mashariki, lakini tatizo kubwa tulilonalo ni watu wachache ambao wamejimilikisha ardhi yetu ya Rufiji na imesababisha kwamba wawekezaji wengi wanakosa ardhi wanapokwenda TIC kuomba kufanya uwekezaji katika maeneo yetu ya Rufiji, tunaonekana Rufiji hatuna ardhi kwa sababu tu kuna watu wachache ambao wamejimilikisha ardhi, ardhi ambayo hawaitumii kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo kwa kupitia Sheria ya ardhi sura ya 113 na Sheria ya ardhi sura ya 144, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Ardhi lakini pia Mheshimiwa Rais kunyang’anya Wawekezaj wote Matapeli walioingia Rufiji ambao wamejimilikisha ardhi na hawaitumii ardhi kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyopita Waziri wa Kilimo alisimama katika Bunge hili na kuwaambia Warufiji kwamba watapata Kiwanda cha Sukari. Leo hii wananchi wa Rufiji wananihoji, wanauliza hiki kiwanda kimekwenda wapi? Lakini tunajua kwamba yupo Muwekezaji aliyechukua ardhi katika Kata ya Chumbi, Muhoro na maeneo mengine ya Tawi katika Kata yetu ya Mbwala akidhamiria kujenga Kiwanda cha Sukari lakini sisi tunajua kwamba mwekezaji huyu ni tapeli na hana uwezo wa kujenga kiwanda hiki na tunaiomba Serikali kupitia Waziri wetu wa Kilimo, Waziri wetu wa Viwanda asimame hapa atuambie na tunamuomba Mheshimiwa Rais afute hati hizi zote na ikiwezekana hati hizi wakabidhiwe mashirika ya umma kwa mfano PSPF pamoja na Mashirika mengine NSSF na LAPF ili waje Rufiji kutujengea cha sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya Rufiji ni ardhi yenye rutuba sana, tunaamini tukipata Kiwanda cha Sukari wananchi wangu wataweza kulima miwa. Nikuombe Waziri wa Kilimo au Waziri wa Viwanda au Mheshimiwa Waziri wa Fedha usimame hapa utuambie. Lakini pia Waziri wa Ardhi usimame utuambie wale wawekezaji matapeli waliokuja Rufiji na kuchukua ardhi ni lini watanyang’anywa ardhi hiyo na ardhi hiyo irejeshwe Serikalini ili sasa wawekezaji wanapokwenda TIC waweze kupata ardhi ya kuja kuwekeza katika maeneo yetu ya Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayasema haya kwa sababu wananchi wengi wa Rufiji hawana shughuli za kufanya yaani economic activity kwa wananchi wa Rufiji ni ndogo sana. Na ndio maana leo hii baadhi ya wananchi wanajiingiza kaitka mambo yasiyofaa. Kwa hiyo, ili kulikwamua tatizo hili niombe Serikali sasa kuhakikisha kwamba inawasaidia Warufiji ili sasa wananchi wangu waweze kupata shughuli mbalimbali za kufanya katika uwekezaji ambao utafanywa na wawekezaji watakaoletwa na Serikali kupitia TIC pamoja na Wizara nyingine mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niseme hili kwa sababu ninaamini kabisa kilimo ndio kitaweza kumkomboa Mtanzania na kama tunavyofahamu kwamba asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, tunaiomba Serikali kuwa serious kabisa kwenye jambo hili la kilimo. Ninaamini kabisa kwamba iwapo tunahitaji kujitegemea ni lazima tuzingatie Kilimo hiki ambacho nimekizungumzia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine tulilonalo kwa wananchi wa Rufiji ambao ninaomba niishauri Serikali kama ambavyo imezungumzwa katika ukurasa wa tisa wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni tatizo la barabara. Tuna kila sababu ya Rufiji kuomba Serikali sasa itujengee barabara ambazo zitasaidia kuongeza shughuli za uchumi, na barabara hizi ambazo nazizungumzia hapa zimezungumzwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukisoma ukurasa wa 46 wa Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo inazungumzia uboreshaji wa Miundombinu. Niombe Serikali sasa, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kukubali kutujengea barabara yetu ya Nyamwage kwenda Utete, niiombe Serikali sasa ujenzi wa barabara hii uharakishwe na uanze sasa. Kwani wananchi wana kiu kubwa ya kusubiri ujenzi wa barabara hii yenye kilometa 33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia barabara ningine ya kutoka Ikwiriri kwenda Mwaseni kule Mloka, itasaidia kufungua shughuli za uchumi. Na ninaamini kabisa wa Rufiji watashiriki kwa hali na mali katika kushiriki katika shughuli za uchumi. Na barabara nyingine ni yakutoka Kibiti kuelekea Mkongo, barabara hii pia ni muhimu sana kwa shughuli za uchumi wa Rufiji. Na barabara ya kutoka Bungu kuelekea Nyamisati ni barabara muhimu sana iwapo barabara hii itajengwa itaweza kuwakomboa Warufiji na Warufiji wengi watashiriki katika shughuli za uchumi na itawaondoa katika fikira za kushiriki katika mambo yasiyofaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie dakika mbili tatu kushauri katika suala zima la madini. Nchi yetu imefika hapa kwa sababu ya kuwepo kwa mikataba mibovu kama ambavyo Wabunge wengi wamelizungumza jambo hili. Na mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kupambana na ukoloni mamboleo, mimi nauita ukoloni mamboleo kwa sababu hili limezungumzwa na watu wengi Duniani akiwepo Profesa Lumumba. Pia tumeona mfano wa yeye aliyofanya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, wameanza kuiga Marais wengi na viongozi wengi wa Dunia wameanza kuiga. Kwa mfano Rais wa Latin America hivi juzi amezuia kilo 1300 ya dhahabu, ni kwa sababu tu mikataba mingi ya dhahabu, mikataba mingi ya madini imekuwa ni mikataba mibovu ambayo inawakandamiza wananchi ambao wanamiliki madini yale. Na tunasema mikataba hii ni detrimental to public interest, mikataba hii ni mibovu na mikataba ambayo haifai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza naomba niishauri sana Serikali yangu, kabla hatujafikia hatua ya kurekebisha mikataba hii, basi tuanze kwa kurekebisha Sera ya Madini, sera hii ya mwaka 1997. Sera hii ya madini inayoiondoa Serikali katika umiliki wa madini yetu hapa nchini na kuyafanya madini kuwa chini ya wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kabisa kwamba Seneta Ndassa amenifilisi kidogo ni kama vile ameingia kwenye hotuba yangu ya siku ya leo, kwa sababu nami sikupendezwa na mijadala, hususan ya siku ya jana ambayo ilikiuka kabisa Ibara ya 28 ya Katiba, ambayo inatutaka sisi Waheshimiwa Wabunge, au Watanzania wote kuwa na Utaifa. Pia inakiuka Ibara kadhaa ambazo nitapenda kuzizungumza hapo mbele, lakini nitajaribu kuzungumza kitaalam zaidi ya vile ambavyo Mheshimiwa Mzee Ndassa amezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana wewe, tarehe 17, mwezi Oktoba, nilipata fursa ya kutembelea Lenin’s Mausoleum, ni kaburi la Vladmir Lenin, Baba wa Taifa la Kirusi na nilifanya hivyo kwa sababu mimi ni mmoja wa wapenzi sana wa siasa za ujamaa na nimesoma vitabu vyake vingi sana. Nilifanya hivyo pia kukumbuka dhima ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea lakini pia ya kuchapa kazi na kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi napenda kusema kwamba Mwalimu Nyerere ni Baba wa Taifa letu kama alivyo Vladmir Lenin ambaye amehifadhiwa pale Moscow Kremlin
- Russia na anapewa uangalizi mzuri na wananchi wa Kirusi. Pia kama Watanzania napenda kunukuu maneno ya William Shakespeare aliyewahi kusema katika Hamlet moja, mbili mpaka 187; alisema kwamba: “He was a man take him for all in all, I shall not look upon his like again”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda nimnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa sababu alituunganisha Watanzania bila kujali itikadi zetu pamoja na imani zetu za dini pamoja na ukanda na ukabila. Hayo yote nimeona niyaseme kwa sababu nami sikuridhika sana na mijadala hususan ya siku ya jana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania asiyeona kazi nzuri inayofanywa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli huyo ni mgonjwa. Nasema kwa sababu yuko Mwandishi mmoja wa vitabu anaitwa Said Nusi, mwaka 2016 alitoa kitabu chake kinachosema Ujumbe kwa Wagojwa. Said Nusi alisema kwamba Mwenyezi Mungu ameshusha magonjwa kwa wanadamu na ameweka dawa yake katika famasia za ardhi na akawateua wanadamu kuweza kuwatibu walio wagonjwa kwa kuwapa uwezo yeye mwenyewe japokuwa yeye Mwenyezi Mungu ndiyo anatoa maradhi na yeye mwenyewe ndiyo wa kuyaponywa maradhi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, uzalendo mkubwa anaoufanya wa kulinda rasilimali za Taifa hauwezi kupimwa na mtu yeyote katika nchi yetu hii na hauwezi kupingwa hata kidogo. Nami binafsi natambua maandiko yaliyowahi kutolewa na Shaaban Robert katika tenzi zake alizowahi kumsifu Siti Binti Saadi, kwa wale wasomaji wa vitabu watawiana na mimi. Itafika wakati Watanzania tutahitaji kuenzi mambo mazuri yanayofanywa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuja kutibu na akipigania rasilimali, kupambana na rushwa, ufisadi na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kikubwa zaidi nimpongeze sana Rais huyu kwa kupambana kuhakikisha kwamba Ibara za tatu na tisa za Katiba ya Ujamaa na Kujitegemea inalindwa katika nchi yetu. Binafsi napenda sana kuamini katika ujamaa na kujitegemea na Tanzania bado tupo katika ujamaa na kujitegemea, hakuna anayeweza kupinga jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme hili kwa sababu mwandishi wa vitabu Martin Harok aliwahi kusema na kunukuliwa kwamba siasa hizi za ujamaa na kujitegemea ambapo nchi yetu inafuata command economy ni moja ya siasa bora kabisa ambazo zinadhamiria kujenga dhamira moja ya Kitaifa yenye kutoa matokeo chanya, kuwa na National Goals na as a results of the National goals often defensive and generally ruthless commitment to a single goal, ambapo sasa hapa tunaona kuna viwanda, reli standard gauge pamoja na suala zima la Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya nane ya Katiba inazungumzia kwamba nchi ni ya wananchi na wananchi ndio wenye nchi hii ya Tanzania na Serikali ina mkataba na wananchi na tutapimwa 2020 wakati tunapokwenda tena kuomba kura kuelezea yale mambo mazuri tuliyoyafanya. Naomba ninukuu Ibara ya 9(g) ambayo inazuia Serikali na vyombo vyake vyote vya umma kwamba: “Kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vitatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu.”

Pia Ibara ya 13(4) pamoja na Ibara ya 13(5) pamoja na Ibara ya 28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimezuia ubaguzi na mijadala yote yenye dhamira ya kuwatenga au kuwabagua Watanzania kwa kufuata ukanda, ukabila au udini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mijadala hii kwa mujibu wa Ibara ya 28 ya Katiba inayotutaka Watanzania kulinda Utaifa, basi uizuie na iwapo Mheshimiwa Mbunge yeyote atazungumzia mambo haya ya ukanda basi azuiliwe na asiruhusiwe kuzungumza mbele ya Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya jana ilikuwepo mijadala mingi na mizito. Kwanza kabisa ni kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato. Binafsi kuna watu ninaowaamini sana ndani ya Bunge lako hili Tukufu, sijawahi kuhoji hata siku moja uwezo wa Mheshimiwa Dkt. Mukasa, namwita Dkt. kwa sababu naamini ni mtu mwenye uwezo mkubwa, lakini sijawahi kuhoji uwezo wa ndugu yangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa sababu naamini ni watu wenye uwezo mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo lazima asimame mtu wa Kanda ya Ziwa kutetea uwanja wa ndege wa Chato, wananchi wa Jimbo la Rufiji tunaweza tukasimama na tukatetea vema kwa sababu maandiko yanasema a good defender is the one who knows how to defend. Wanasheria tunaamini kabisa kwamba Mwanasheria bora ni yule anayejua wapi pa kuitafuta ile sheria, a good Lawyer is the one who knows where to find the law.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme hii kwa sababu ukisoma Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 55 mpaka 58 unazungumzia ujenzi wa viwanja vipya vya ndege, pia kuboresha viwanja tulivyonavyo. Hii ni Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, haihitaji mtu wa Kanda ya Ziwa kuitetea, ni Sera ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo Serikali inaelekeza mambo yake kutokana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vinavyojengwa ni vingi, siyo kiwanja cha Chato peke yake, tunacho Kiwanja cha Kigoma ambacho kitajengwa, kuna Kiwaja cha Mafia ambacho kitajengwa, kipo kiwanja cha Mtwara ambacho kitajengwa. Hii ni kwa mujibu wa Ilani lakini pia ni kwa mujibu wa mpango ambao umewasilishwa na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi wa reli, ujenzi huu unakwenda kusaidia uchumi kwa sababu dhamira ya Chama cha Mapinduzi ni kunyanyua njia kuu za uchumi ili kuwafanya Watanzania waweze kutoka kwenye uchumi wa kawaida na kwenda kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa mchakato wa ujenzi wa Bwawa la Stiegler’s Gorge, hii ni fikra ya Mwalimu mwaka 1956 Mwalimu Nyerere alidhamiria kwamba baada ya uhuru atajenga Bwawa la Stiegler’s Gorge ili kuweza kusaidia nchi yetu kuweza kupata umeme wa kutosha na kuweza kuuza nje ya nchi. Niwapongeze sana wananchi wa Jimbo la Rufiji, hususan wa Kata ya Mwaseni ambao wamelitunza bwawa hili kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 muda kama huu nilisimama mbele ya Bunge lako Tukufu na nikahoji ni kwa nini Wilaya yetu ya Rufiji, Kilwa pamoja na Kibiti tunakosa umeme kwa siku tunapata umeme kwa saa nne, wakati tunayo Stiegler’s Gorge. Mwaka 2016 nilihoji pia ndani ya Bunge lako hili Tukufu ni kwa nini nchi hii tunauza umeme ghali wakati tunayo Stiegler’s Gorge ambayo tunaweza kuzalisha umeme na tukasambaza nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunategemea kujenga reli ambayo inakwenda kutumia umeme, lakini pia tuna viwanda ambavyo vinajengwa kila siku. Nimpongeze ndugu yangu, Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo kwa kuzindua mchakato wa ujenzi wa viwanda, viwanda hivi vitahitaji umeme na umeme huu ni wa Stiegler’s.

Mheshimiwa Spika, ninachoiomba Wizara ya Nishati ni kuzingatia umeme huu wa Stiegler’s Gorge uweze kuwanufaisha pia na wananchi wa Rufiji. Nimwombe Waziri wa Nishati atakaposimama hapa aseme, baada ya ujenzi wa Stiegler’s Gorge mchakato mzima upitie katika Wilaya yetu ya Rufiji ili Kata ya Mwaseni iweze kunufaika, wananchi wa Mloka na maeneo mengine waweze kunufaika, wananchi wa Kata ya Kipugila waweze kunufaika,wananchi wa Kata ya Mkongo waweze kunufaika, wananchi wa Kata ya Ngorongo waweze kunufaika na wananchi wa Jimbo zima la Rufiji waweze kunufaika kutokana na mradi huu mkubwa wa umeme kwa sababu wananchi wa Rufiji ndio waliolitunza bwawa hili toka mwaka 1956 mpaka leo hii. Haya ni maneno ambayo nimeyazungumza kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu natambua dhamira ya Serikali ya kujenga miundombinu mbalimbali ili kuweza kuboresha njia kuu za uchumi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tarehe 3 Machi, aliwaahidi wananchi wa Tarafa ya Ikwiriri kwamba kabla ya mwaka 2020 atajenga barabara ya Nyamwage kuelekea Utete. Niombe sana, kila Mbunge anatamani kuacha legacy atakapoondoka, mwaka 2020 nitakaposimama kuomba kura na mimi nitaacha legacy yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Rufiji tunasema, labda pengine hakuna mwingine yeyote zaidi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iwapo barabara hii ya Nyamwage kuelekea Utete itajengwa, Makao Makuu ya Halmashauri yetu. Rufiji ilianzishwa wakati wa mkoloni ni Wilaya ya sita wakati huo, lakini hatuna hata nusu kilometa ya barabara ya lami.

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa Rais wetu akiijenga barabara hii ya Nyamwage – Utete aliyoahidi mwenyewe kwamba kabla ya mwaka 2020 barabara hii itakuwa imekamilika, lakini katika mpango sijaliona hili, kama kuna uwezekano walirekebishe ili wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji waweze kunufaika na uchumi huu ambao wanachangia kupitia maliasili na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara yetu ya Ikwiriri kuelekea Kata ya Mwaseni, naomba sana, kwa kuwa Serikali inakwenda kujenga bwawa la Stiegler’s Gorge, hakuna namna tutaepuka kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Serikali kutokana na makusanyo tunayoyapata, ianze kujenga barabara ya kutoka Nyamwage kueleka Utete ili wananchi waweze kupata barabara yao ya Halmashauri kwa mara ya kwanza toka tumepata uhuru. Pia barabara ya Ikwiriri kuelekea Mwaseni ni barabara muhimu sana, hali kadhalika barabara ya kutoka Bungu kuelekea Nyamisati katika Wilaya ya Kibiti ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali sana kwa kutuletea miradi mingi ya maji. Naipongeza Serikali na nampongeza Waziri wa Maji, baada ya kuteuliwa tu kuwa Waziri alifika Rufiji na kujionea miundombinu mbalimbali ya maji.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Maji ahakikishe kwamba ile miradi anayotuletea ambayo nilimwomba mwenyewe inayokwenda katika Kata za Mbwara, Chumbi, Utete, Mkongo, Ngarambe, Kipugira na nyingine, basi iweze kukamilika kwa wakati ili mwaka 2020 tuweze kutamba kwamba tumeweza kuwafanyia wananchi jambo fulani ambalo litakuwa na manufaa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, kilimo kimezungumzwa katika makaratasi, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, Rufiji tuna ardhi ya kutosha na wakati fulani tulipewa taarifa na Waziri wa Viwanda kwamba atatujengea kiwanda cha sukari katika Kata za Chumbi, Mbwara pamoja na Muhoro. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunatambua wapo wawekezaji mafisadi waliochukua ardhi yetu wananchi wa Rufiji na kuishikilia ili kutafuta wawekezaji wapate cha kwao cha juu.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na nimwombe Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa ukali anaoufanya katika kujenga uchumi wa nchi yetu, anyang’anye ardhi hii mara moja ili tuweze kupata kiwanda hiki cha sukari kwa mara ya kwanza katika nchi yetu na kwa mara ya kwanza katika eneo letu la Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, anyang’anye ardhi hii ambayo imechukuliwa na mwekezaji mmoja mfanyabiashara aliyeimiliki na hataki kujenga kiwanda, amezuia Serikali kuweza kupata mwekezaji wa kujenga kiwanda hiki, ardhi hii iweze kunyang’anywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niikumbushe Serikali, Rufiji tuna square kilometers 500,000 ambazo ziko ndani ya Bonde la Mto Rufiji. Naiomba sana Serikali kuona namna ya kuboresha kilimo katika maeneo yetu ili wananchi wa Rufiji pia tuweze kunufaika na Serikali yetu na tuseme kwamba tunatembea kifua mbele kwamba Serikali ya Awamu ya Tano sasa imedhamiria kuunyanyua uchumi wa wananchi wa Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee katika elimu. Sote kabisa tunatambua kilichotokea Rufiji na Kibiti kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tumeshindwa kufanya siasa, wananchi wameshindwa kushiriki katika kilimo lakini kitu kikubwa ambacho kinatukwamisha ni tatizo kubwa la elimu.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Elimu, kama ambavyo aliweza kutenga fedha za uboreshwaji wa shule za sekondari za Kibiti, Muhoro na sekondari ya Utete namwomba pia aone uwezekano wa kuboresha miundombinu ya shule zetu, hususan shule ya Sekondari ya Ikwiriri pamoja na miundombinu ya shule zetu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua, ukiangalia takwimu tulizonazo leo hii katika maeneo ambayo yameathirika sana na elimu ni eneo la Rufiji, Kibiti, Kisarawe na maeneo mengine ya Pwani. Leo hii tuna watoto zaidi ya 300,000 nchi nzima ambao wanaacha shule bila sababu maalum. Nimwombe Waziri wa Elimu akisimama hapa atuambie mpango mkakati ambao Serikali itakuja nao wa kudhibiti utoro katika shule na kuacha shule mara moja.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Elimu akisimama atuambie Serikali inafanya mchakato gani wa kubaini watoto ambao waliacha shule miaka kumi iliyopita na kuweza kujua wako wapi leo hii. Bila kufanya hivyo, watoto wengi leo hii wanaoacha shule, wanakwenda kujiunga katika vikundi mbalimbali vya kigaidi. Hii inatuletea shida kwa sababu vijana wetu wengi wanapotea na Serikali haielewi wamekwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza niweke kumbukumbu sawa kuhusu hili ambalo limezungumzwa na ndugu yangu Mheshimiwa Vedasto kwamba vita vya Majimaji vilianzia Rufiji katika Kata ya Mbwala, Kata ambayo inapakana na Vijiji vya Kilwa na eneo hili la Nandete ambalo amelisema ni Vijiji vilivyopo Rufiji, Nandete pamoja na Tawi. Lakini pia ikumbukwe hata huyo mpiganaji Kinjekitile Ngwale alinyongwa katika mti uliopo pale Muholo ambao umeng’oka hivi karibuni tu, kwa hiyo, vita hii ilianzia Rufiji haikuanzia Kilwa naomba niweke kumbukumbu sawa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, kuna mwangwi inanipa tabu kujua taarifa hii inatoka wapi!

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Kuchauka.

SPIKA: Aaaah! Mheshimwa Kuchauka Mbunge wa Liwale.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumzia vita ya Majimaji. Muasisi wa vita ya Majimaji ni Kinjekitile Ngwale, Mngindo, na wakati ile vita inaanza Kinjekitile Ngwale alikuwa Iringa anaendelea kukusanya majeshi huku nyuma wanakijiji wa Kijiji cha Nandete walikwenda badala ya kupalilia mashamba ya pamba walifyeka pamba zote ndipo Wajerumani wakaja na nguvu wakaanzisha ile vita wakati Kinjekitile Ngwale bado yupo Iringa. Kwa hiyo, nimpe taarifa kwamba ile vita ya Majimaji ilianza Kilwa na chanzo chake ni wakulima walipokwenda kufyeka pamba badala ya kupalilia. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimwa Spika, taarifa hii siipokei kwa sababu vita ya Majimaji ilishaanza mapema na Kinjekitile alitafutwa kwa kuwa alikuwa mganga tu wa kienyeji, lakini yeye hakuwa muasisi wa vita hii.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa, endelea Mheshimiwa Muhagama. (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpe taarifa babu yangu Mheshimiwa Mchengerwa kwamba Kinjekitile Ngwale alikuwa mganga wa kienyeji aliyewadanganya wapiganaji wa vita kwamba maji yanaweza kupunguza makali ya risasi na ndiye aliyesababisha tushindwe ile vita ahsante. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa. (Kicheko)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, taarifa hii naipokea imekaa vizuri. Pamoja na hotuba nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyosheheni matumaini na ujenzi wa Tanzania mpya, nina imani kubwa sana kwamba vipaumbele vya Taifa letu sasa vimeimarisha hali ya ujenzi si wa Taifa peke yake bali ya ujenzi wa wazalendo wapya. Vipaumbele hivi ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu amevitoa visingefanikiwa kama Taifa hili lisingelikuwa na Jemedari Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye yeye kwa uchapa kazi wake, uhodari wake amechangia kwa kiasi kikubwa sana Taifa letu sasa pengine kesho, keshokutwa linaweza likawa ni Taifa ambalo linajitegemea lenyewe.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imejikita katika mambo mengi hususani katika kilimo, afya, miundombinu, maji, umeme, mafuriko pamoja na eneo hili la Corona na mambo mengine mengi. Tuwaombe tu Watanzania kuhusu eneo hili la Corona kwamba ni vyema Watanzania wakafuata ushauri unaotolewa na Wizara ya Afya, lakini pia ushauri unaotolewa na Kamati zilizoundwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati za Maafa za Mikoa pamoja na zile za Wilaya. Kwa hiyo Watanzania waaache viburi, Watanzania waache ujuaji namna pekee ya kuwaokoa Watanzania ni kufuata maelekezo yanayotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, hakuna namna nyingine.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba imekuwa nzuri sana kama ambavyo nimesema Mheshimiwa Waziri Mkuu amegusia eneo hili la mafuriko. Ikumbukwe tu kwamba Rufiji hakuna mvua hata moja inayonyesha, mvua zinanyesha Nyanda za Juu Kusini, pia ikumbukwe tu kwamba eneo kubwa la Rufiji liko kwenye bonde, kwa hiyo maji yote ya mvua na maji ya kwenye mabwawa mbalimbali hapa nchini yanakuja Rufiji na hii imepelekea robo tatu ya Rufiji yote sasa iko kwenye maji. Mafuriko haya hayakuanza juzi japokuwa nitambue mchango mkubwa wa Ofisi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini lazima tukiri kwamba wataalam wetu walichelewa kutufikia Rufiji na hiki kwa kweli ni kilio cha wananchi wetu wa Jimbo la Rufiji.

Mheshimiwa Spika, tatizo ambalo naliona si lingine isipokuwa sababu kubwa ni Fungu 37 hatukutenga fedha kwenye hichi Kitengo cha Maafa hakuna fedha na badala yake tunategemea zile Ofisi za Maafa za Mikoa na Wilaya. Niiombe pengine Bunge kwa kuwa sasa eneo hili Mbunge wa Jimbo ndio anawajibika kuwahudumia wananchi na ikumbukwe nchi hii ni ya wananchi na mfariji namba moja kwa wananchi ni Serikali, hii ni kwa mujibu wa Ibara ya Nane ya Katiba ambayo inasema nchi ni ya wananchi. Basi, tuwaombe Wizara kuangalia uwezekano sasa wa kutenga fungu kwenye hili Fungu la maafa ili wataalaam wetu pale ambapo wanasikia taarifa za maafa iwe rahisi wato kutufikia.

Mheshimiwa Spika, japokuwa zaidi ya familia 20,000 zimekosa makazi, zimekosa vyakula, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ilituletea baadhi ya vitu ambavyo kwa kweli ni vichache hususan kwenye eneo hili ambalo lilikuwa eneo la maafa. Walituletea ndoo ambazo zilikuwa tupu nadhani unaweza kuona wananchi wa Rufiji wanachohitaji ni faraja hawahitaji ile huruma ambayo pengine wanapaswa wasifanye kazi hapana wanachohitaji ni faraja kidogo ambayo pengine Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inasema tunacho chakula cha kutosha kwa zaidi ya asilimia 110, hii haijapata kutokea toka nchi yetu imepata uhuru. Vyakula vilivyopo leo hii ni zaidi ya asilimia 110, naamini ofisi hii haishindwi kuja kutuletea hata kama vyakula vikikosekana, hata mbegu za msaada ili tuweze kupanda pale maji yanapokuwa yametulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba mafuriko yameleta maafa makubwa katika kila sekta kwa mfano vipo vituo vya afya ambavyo vimezingirwa na maji na vingine havifai kabisa. Eneo la maporomoko ya mto yamekikumba Kituo cha Afya cha Muhoro, tayari ofisi yetu ya Wilaya Ofisi ya Mkoa tumekwishaandika barua TAMISEMI kuweza kuomba fedha za dharura ili wananchi wetu waweze kujengewa kituo cha dharura kwa sababu eneo hili la Muhoro lina wakazi zaidi ya 25,000.

Kwa hiyo niombe Ofisi ya Rais TAMISEMI, watakapokuja kufunga hapa watuambie iwapo kama kuna fedha hizi za dharura ambazo tunatambua kwamba zipo waangalie uwezekano wa kuwasaidia wananchi hawa.

Mheshimiwa Spika, leo hii wananchi wa Muhoro wanakosa matibabu, japokuwa tunatambua kwamba maji yameanza kuondoka taratibu, japokuwa yapo mabwawa mengine ambayo yemefunguliwa hivi karibuni, maji haya yanaweza kuchukua muda mrefu kwa kuwa mafuriko ndio kwanza yataanza mwezi huu mwezi wa nne kule kwetu Rufiji. Kwa hiyo tuwaombe Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa fedha za dharura kuweza kuona uwezekano wa kuwaangalia wananchi wetu wa Kata ya Muhoro kwa kutoa fedha hizo ili tuweze kujenga kituo kuwahudumia wananchi zaidi ya 25,000 ambao kwa leo hawana hawapati huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, mafuriko yameathiri ikiwa ni pamoja na mradi wetu wa kuzalisha umeme mradi ule wa Mwalimu Nyerere. Tunapata kigugumizi wakati mwingine pale ambapo tunamtafuta Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kumweleza maafa ya mafuriko kwenye mradi huu Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi hajawahi kufika Rufiji kupitia barabara ambayo mradi huu unaelekea. Barabara kubwa inayotumika ni barabara ya Kibiti kuelekea Mroka lakini Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi hajawahi kufika Rufiji kupitia barabara hii, pengine anasubiri Mheshimiwa Rais akiwa anakwenda yeye ndio aje Rufiji kupitia barabara hii. Hata nilipozungumza naye alisema amewaagiza wataalam wake kupeleka vifaa kupitia Morogoro. Vifaa hivi vinatoka Mtwara Dangote, inawezekana vipi vitoke Dangote vipite Pwani, vipite Dar es Salaam viende kwenye mradi wa umeme.

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa umeme kama kweli Taifa letu limedhamiria ukamilike wakati Mheshimiwa Rais wetu Magufuli akiwa madarakani, basi ni vyema wataalam hawa wakafika maeneo haya, barabara hii…

SPIKA: Ni barabara unayoongelea Mheshimiwa?

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, ni barabara ya Kibiti - Mroka. Barabara ya Kibiti - Mroka imeharibika na magari makubwa yameharibu barabara hii hata mafuriko ya mwaka 62 barabara hii iliendelea kupitika lakini leo hii barabara hii haipitiki, inachukua masaa 10, barabara hii inahitaji tu utatuzi…

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa unapata taarifa toka kwa Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mbunge anayeongea Mheshimiwa Mchengerwa mjukuu wangu kwamba mvua zilizonyesha ni mvua za return period ya miaka 100. Wakati tunaanza mradi wa kujenga Bwawa la Nyerere mkandarasi alipewa barabara tatu; barabara ya kwanza ni hiyo Kibiti - Mroka, njia ya pili ilikuwa ni kwenda na TAZARA, anakwenda mpaka eneo la Fuga na tuliimarisha na ile barabara ya kutoka Fuga kwenda kule, nayo imeimarishwa vizuri, lakini barabara ya tatu ilikuwa ni ya upande wa Morogoro na yeye amekuwa anatumia zaidi ile barabara ya kule kwa Mheshimiwa Mchengerwa kwa sababu ni kweli ni fupi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mvua zilizonyesha kuna kipande cha mita 200 ambacho kuna bwawa lipo eneo lile, limeungana na mafuriko ya Mto Rufiji na kile kipande kina maji ya kina cha mita mbili, kwa hiyo hakuna namna yoyote gari linaweza likapita. Kwa hiyo, mkandarasi sasa hivi atapita Fuga au atapita njia iliyoko kule upande wa Morogoro. Kwa hiyo nilitaka kumpa taarifa kwamba hii ni nature ambayo hatuwezi kufanya chochote kwa akili ya kawaida ya mwanadamu. Naomba avumilie tu Mheshimiwa Mchengerwa baada ya mafuriko kupita na barabara ile kukauka basi hatua nyingine zitafanyika.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, tunachoomba Mheshimiwa Waziri apite kwenye hii barabara ajionee. Hii barabara miaka yote toka mafuriko ya 1962 mafuriko ya 1974, mafuriko ya 1998, 1988, 2018 barabara hii iliendelea kupitika, leo hii wananchi wangu wanatumia masaa 10 kupita barabara hii, mimi mwenyewe nimepita, yako matrekta yanapita pale kinachohitajika ni kifusi tu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la aibu kwenye mradi huu, mradi unatekelezwa Rufiji, waathirika wa kwanza watakuwa ni Warufiji, lakini cha kushangaza Mkurugenzi wa Kinondoni anaomba service levy ya utekelezaji wa mradi. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aeleze hapa, mradi huu uko Rufiji, unatengenezwa Rufiji, Warufiji ndio watu wa kwanza kuupokea kupitia Mbunge wao, lakini mpaka leo service levy haijalipwa Rufiji, watu wa Kinondoni wanaitaka service levy,. Angalia ajira 3,300 Warufiji waliajiriwa ni 200 kati ya ajira 3,300, tukiuliza ni upande wa nishati, hatupati majibu; tukimuuliza mkandarasi yeye ameweka watu tu, kwa hiyo athari zakwanza za mradi huu zitawakuta wananchi wa Rufiji na sisi ndio watu wa kwanza kuupokea mradi huu hatuna tatizo hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Hansard hotuba yangu ya mwaka mwezi Novemba, 2016, nilipambana na Mheshimiwa Waziri Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati ule kuomba utekelezaji wa mradi huu tunachoomba Warufiji wapate haki hata kama kidogo; hatuna nishati, hatuna madini, hatuna Tanzanite, tuna mradi huu, hiki ndio kitu pekee tulichonacho. Tunachoomba Wizara hizi mbili ziwaangalie Warufiji kwa sababu ndio watu wa kwanza utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kufikia mwisho wa mjadala wetu wa bajeti yetu hii wa ofisi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, namshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo aliyoyatoa siku ya jana kuhusu masuala yanayohusu ofisi yangu wakati akilihutubia Bunge lako Tukufu. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa maelekezo yake tumeyapokea, tumeyaelewa, tutayazingatia na kuyafanyia kazi kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia uniruhusu niwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kuunga mkono hoja niliyoiwasilisha jana katika Bunge lako Tukufu. Vilevile niwashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao hawakuweza kuchangia kwa sababu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha hoja, naomba kusisitiza kuwa ofisi yangu na taasisi zote zilizo chini yangu tumejipanga vizuri kutekeleza yale yote tunayoyapanga kuyafanyia kazi mwaka ujao wa fedha ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na ustawi wa Watanzania. Ninatambua umuhimu wa mchango wenu katika jitihada za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, lakini pia maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyonadiwa katika uchaguzi uliopita, lakini pia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022-2025/2026) na Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa siku ya jana katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vita dhidi ya rushwa, tumeendelea kujidhatiti na kukabiliana na vitendo vya rushwa nchini, hali ambayo imeongeza nidhamu, uadilifu na matumizi bora ya madaraka na fedha za umma. Mafanikio ya juhudi zetu yamedhihirishwa na taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Kazi iliyo mbele yetu ni kuhifadhi mafanikio hayo na kuongeza juhudi ili kutokomeza rushwa na ufisadi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo hayo tumejipanga vyema kuandaa na kutekeleza mkakati mpya wa mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini utakaozingatia changamoto zinazojitokeza sasa. Vilevile tunakusudia kuongeza ufahamu kwa wnanachi kuhusu masuala ya rushwa, kuboresha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa na kuimarisha utendaji wa Taasisi yetu hii ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wanyonge, ofisi yangu itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa MKURABITA ili manufaa yake yawafikie wananchi wengi zaidi. Wakati huo huo, tutaendelea kusimamia maadili na mwenendo wa watumishi wa umma, uwe ni mwema na uendane na miongozo mbalimbali ya watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka ujao wa fedha, tutaendelea kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao ili kuboresha na kuimarisha usalama wa mifumo ya Serikali ili iweze kubadilisha taarifa tunazozipata. Matumaini yetu ni kuwa hatua hii itaongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi yangu itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuimarisha utawala bora katika uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa kubuni sera, kanuni, na sheria za uendeshaji wa shughuli za utumishi wa umma na kuwajengea uwezo watumishi waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hilo tutaendelea kulinda haki za watumishi wa umma kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo. Aidha, tutahakikisha kuwa ngazi za mishahara na madaraja ya watumishi yanapandishwa kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais siku ya jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapenda kuona watumishi wanalipwa stahiki zao kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Stahiki za mtumishi ni haki yake mtumishi husika na siyo huruma, ni right, siyo privilege kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara. Tunataka kuondoa kero za kimaslahi zinazowakabili watumishi wa umma na uonevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nitaweka utaratibu wa kupokea malalamiko ya watumishi na nitachukua hatua kali za kinidhamu kwa wale wote watakaoshindwa kuwahudumia watumishi na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi yangu itaendelea kuratibu, kusimamia, na kukuza jitihada za Serikali, Serikali mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na viwango vya miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi zote za umma hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kumaliza naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa kutoa maoni yao na pengine lazima nikiri kwamba maoni tumeyapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hoja chache ambazo pengine ningependa kuzitolea ufafanuzi. Kuna hoja hii ambayo imezungumzwa sana kuhusu Idadi ya Wakurugenzi saba, Ma-DAS pamoja na Ma-RAS ambao walikwenda kwenye kugombea kwenye nafasi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii kama Wizara tumeipokea. Kama ambavyo nimesema Rais wetu amejikita katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa kila Mtanzania.

Kwa hiyo tutalichukua jambo hili tutakwenda kulifanyia kazi kama kutakuwa na mtumishi ambaye pengine alikuwa Mkurugenzi, alikuwa RAS au alikuwa DAS na alikwenda kugombea na kama alifuata taratibu zote ambazo zinatakiwa za kisheria na kikanuni zilizowekwa basi mtumishi yule kama haki yake itamtaka arejeshwe kazini, atarejeshwa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe kwa sababu tunatambua kwamba wapo watumishi ambao tayari walirejeshwa kazini na jukumu la Serikali hii kuhakikisha kwamba inafanya kazi zake kuondosha double standard, kwa hiyo tutalichukua jambo hili, tutakwenda kulifanyia kazi kwa wale watumishi ambao wana haki ya kurejeshwa kazini watarejeshwa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe na kama kuna Mbunge yeyote Mheshimiwa Mbunge yeyote anataarifa au watumishi hawa wapo basi wafike ofisini kwangu ili tuweze kupitia taarifa zao na yule mweye haki ya kurejeshwa kazini atarejeshwa kazini. Kwa sababu huu ndiyo msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba inatenda haki kwa wakati ili kila mmoja wetu aweze kupata haki zake stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuhusu suala hili la upandishwaji wa madaraja limezungumzwa kwa kina sana. Naomba niseme kwamba tumeziagiza Taasisi na Maafisa Utumishi wote nchini kuhakikisha kwamba wanatuletea taarifa za watumishi wote katika maeneo yao. Tayari wizara yangu imekwishatenga nafasi za upandishwaji wa madaraja. Kwa sasa tunao watumishi zaidi ya 91,841 ambao wataigharimu Serikali zaidi ya shilingi 73,402,166.926. Kwa hiyo, tumejipanga kuhakikisha kwamba tunawapandisha madaraja watumishi kwa mikakati ambayo tumejiwekea sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuhusu hili suala la ajira mpya tayari Wizara yangu imejipanga kuhakikisha kwamba tutatoa ajira mpya 40,737 ambazo zitawagawinyika katika kada mbalimbali za utumishi wa umma. Tunazo ajira za elimu ambazo tunategemea kuzingataza hivi karibuni, ajira 9,667 na katika sekta ya afya tunategemea kutangaza ajira 10,467 na hivi karibuni tutatangaza ajira 2,116 za afya tukisubiri taarifa ya bajeti ambayo tutatangaza ajira zitakazopungua kutokana na hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika sekta ya kilimo tutatangaza ajira 1,046 kulingana na bajeti tutakayoipata. Katika sekta ya mifugo ajira 758, katika uvuvi 175, katika polisi 1,346 na katika magereza ni ajira 427. Jeshi la Zimamoto ni ajira 510, uhamiaji ajira 404, hospitali na mashirika ya kidini na hiari 1,486 na ajira nyinginezo ni 13,192. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwatulize Waheshimiwa Wabunge watambue kwamba Serikali yao ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha kwamba tunakwenda kupunguza maeneo ambayo tunajua yanachangomoto nyingi za ajira katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mahusiano kati ya Ma-RC, Ma-DC, na Ma-DAS hili nimelizungumza kwa kina kabisa. Ni vyema kila mtumishi wa umma akatambua kwamba mtumishi yeyote wa umma hapa nchini yupo chini ya Wizara ya Ofisi yetu. Wizara hii ambayo inasimamia nidhamu za watumishi wote wa umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe Ma- RC, Ma-DC na Naibu Wakurugenzi na wale wote wanaoangukia kwenye Wizara hii kujikita katika kuhakikisha kwamba wanalinda viapo vyao ambavyo wamekula mbele ya Mheshimiwa Rais. Lakini pia nichukue fursa hii kuwataka viongozi wote wa Chuo cha Uongozi kujipanga vyema katika kuhakikisha kwamba wanatoa semina kwa viongozi wote wa umma ambao wanaangukia katika nafasi ya Naibu Wakurugenzi, Wakurugenzi, Ma-RC, Ma-DC na viongozi wengine wote wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili suala la utolewaji wa nyaraka, suala hili nimelizungumza kwa kina. Ofisi yangu itakwenda kujipanga, tutakwenda kupitia nyaraka zote, zile nyaraka ambazo tunaona zimetolewa na zinakiuka sheria nyaraka hizo zote hizo tutazifuta. Nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, lakini naamini kwa kipindi ambacho nimekaa katika ofisi hii binafsi sijaona nyaraka ambayo imetolewa imekiuka sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama kuna taarifa ya nyaraka yoyote ambayo imetolewa na inakiuka sheria tutakwenda kujipanga na kuhakikisha kwamba nyaraka hiyo tunaiondosha na kuifuta ili sasa kwa namna ile ile ya misingi ya tasfiri ya sheria tunakuwa na Katiba, tuna sheria, tuna kanuni pamoja na miongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafuu ya muda ninaomba sasa pamoja na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge iliyotolewa ninaomba kutoa hoja. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa naibu Spika, naafiki. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma alienijalia afya njema kusimama ndani ya hili Bunge lako hili Tukufu. Lakini pia nimtakie pole bibi yangu Nyankulu kutoka kule Mtanange, leo hii anapambana na vita ya kansa, namuombea apone haraka ili aendelee kuniombea.
Tatu niseme tu kwamba niwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Rufiji kwa namna ya kipekee kabisa kuniomba leo hii nibaki ndani ya Bunge kwa sababu siku ya leo ni siku ambayo Mwenge umefika katika Jimbo langu la Rufiji. Kwa kutambua kwamba Jimbo la Rufiji linabeba asilimia 50 ya Hifadhi ya Taifa letu, wakaniambia nibaki kwa ajili ya kuzungumza mambo ya msingi kabisa kwa ajili ya ustawi wa taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hii ni nchi yetu sote, nianze kwa kusisitiza kwamba nchi hii ni yetu sote. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua Brigedia Jenerali Gaudencia Milanzi. Tunatambua uteuzi wake una changamoto nyingi kwamba anapaswa kufanya kazi, kupambana na majangili ili ni kufuta aibu kubwa iliyotokea mwezi Januari ya kuuwawa kwa rubani wa ndege Bwana Roger Gower. Hakika jina la pilot huyu litakumbukwa katika nchi yetu na litaandikwa katika historia kwani alikuwa ni miongoni mwa wapambanaji wanaosaidia kupambana na ujangili katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia kwa undani sana taarifa za kwenye mitandao lakini pia nimefuatilia kwa umakini uwasilishwaji wa hoja mbalimbali ndani ya Bunge lako hili Tukufu. Pia nina fahamu zipo taarifa za wadau mbalimbali kutumiwa ili kujaribu kukwamisha bajeti ya Wizara hii; wadau mbalimbali wakiwemo na wanasiasa pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango mbalimbali iliyowasilishwa katika Bunge lako hili Tukufu imejikita kwa watu wengi kuzungumzia haki za wafugaji lakini wamesahau kwamba wakulima tunao na wana haki zao za msingi na wanachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa la nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere aliwahi kutukumbusha kuhusiana suala hili la kubagua au kubaguana, kuanza kuwabagua watu fulani kuwaona watu fulani wao ni muhimu kuliko watu wengine. Lakini naomba nisisitize Ibara ya 13(4) ambayo inafafanua kuhusu haki ya kutobagua watu au kundi fulani. Wakulima wamebaguliwa sana ndani ya hili Bunge lako Tukufu. Ninaomba niseme wakati wa uwasilishwaji wa Wizara ya Kilimo tuliona wafugaji wengi walifika hapa Dodoma, lakini pia wakati wa uwasilishwaji wa Wizara hii wafugaji wengi pia wapo ndani ya Dodoma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu Ibara ya 13(5) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayofafanua mambo kadhaa na emphasis is mine na nisisitize hili:- “Katika kutimiza haja ya haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, pahali wanapotoka, maono yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watendewe wao ili waweze kupewa fursa au faida katika nchi hii.” Ibara hii inasisitiza haki ya kutobagua watu fulani. Naomba msisitizo huu Waheshimiwa Wabunge wauchukue ili tunapokuwepo hapa tujadili haki za msingi za wananchi wetu wote wa Tanzania bila kubagua huyu ni mfugaji au huyu ni mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vurugu hizi kati ya wakulima na wafugaji nizungumze kidogo, hazikuanza zamani sana sisi kule Rufiji tulizoea kuamka unakutana na mpunga; lakini leo hii mifugo imeingia, lakini silaumu kilichotumika ni Ibara ya 14 ya Katiba yetu ambayo inaruhusu Mtanzania kuishi popote. Ibara hii ya 14 ilitumia baada ya Waziri Mkuu Fredrick Sumaye pamoja Lowassa kuendeleza mchakato huu wa kuhakikisha kwamba mifugo inasambaa ndani ya nchi yetu. Si tatizo baya kwa sababu huu ni utekelezaji wa Ibara hii ya 14. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapa nikumbushie Ibara hii ya 14 ambayo inakwenda sambamba na ukumbushwaji wa sheria mbalimbali. Ninaamini Wabunge wengi wanasahau kwamba tunazo sheria nyingi ambazo zinatuongoza katika nchi yetu hii, na iwapo tutawashauri wananchi wetu kufuata sheria hizi hakutakuwepo na mgogoro wowote kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushie Sheria ya Matumizi ya Ardhi Namba 6 ya mwaka 2007 ambayo inatoa mchakato mzima wa namna gani ardhi itatumika na wapi wakulima waweze kufanya kilimo chao na wafugaji waweze kufuga wapi mifugo yao. Pia tunayo Sheria ya Mpango wa Vijiji sheria ya mwaka 1999 lakini pia tunao Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi. Mpango huu ni wa mwaka 2013 mpaka 2033. Tunayo sheria ya kuhifadhi maliasili pamoja na miongozo mbalimbali ya viongozi isiyokinzana na Katiba. Tunayo Ibara ya 26 ya katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatusisitiza wananchi wetu kufuata sheria. Tatizo hapa ni wananchi kutotaka kufuata sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe tu kwamba sheria hizi zilitungwa na Bunge hili, kama tunaona sheria hizi ni mbovu ni jukumu la Bunge letu hili Tukufu kubadilisha sheria hizi.
Katika kubadilisha sheria hizi Ibara ya 26 inazungumza wazi sina sababu ya kuisistiza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nirudi kwenye hoja zangu za msingi, hoja ambazo wa Rufiji wamenituma nije niwawakilishe hapa. Nianze kuzungumzia kodi ya kitanda. Niende haraka haraka, kodi hii ya kitanda ambayo ilitoka shilingi 8,000 kwenda shilingi 120,000 kodi hii iliundwa ili kuwakandamiza Warufiji. Mimi nikuombe kodi hii ambayo hata kama Mrufiji umelalia kitanda miaka 30 unawajibika kukilipia kodi iwapo unatoka nacho Rufiji unakwenda Wilaya zinazofuata Kibiti na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kodi hii Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuiondoa kodi hii ambayo ni kodi kandamizi.
Kwa wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji. Nitaomba taarifa kuhusiana na kuondolewa kwa kodi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 30(3) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inanipa mamlaka mimi kupitia iwapo sheria au miongozo ya Serikali inakinzana na Katiba, mimi kama Mbunge na mwanasheria nguli nitakuwa na uwezo wa kufungua kesi ya Kikatiba ilikuweza kuomba Mahakama kutoa tafsiri fasaha ya kuondoa kodi hii ya kitanda ambayo ni kandamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa mbele ya Bunge lako hili Tukufu, baada tu ya kumaliza Bunge hili iwapo Waziri hataifuta kodi hii nitafungua kesi ya Kikatiba kwa sababu kodi hii ni kandamizi na ikinzana na Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hiyo nisiizungumzie kiundani zaidi lakini nirudi kwenye kodi ya mkaa. Kodi hii ya mkaa imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Niliwahi kufanya tafiti kuhusiana na kodi ya excise duty, kodi hizi ambazo zinakuwa zinatolewa na Serikali ili ku-discourage consumption. Kuongezeka kwa kodi ya mkaa kunasababisha ongezeko kubwa la maisha kwa wananchi wetu wa Jimbo la Rufiji ambao wanategemea biashara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende mbele, nikimbie haraka haraka kidogo, naomba nizungumzie kuhusiana na pesa ya upandaji wa miti. Wananchi wangu wamekuwa wakichangia wanapokuwa wanalipa kodi ya mkaa wanachangia kiasi cha shilingi 830 kwa gunia kwa ajili ya kupanda miti. Naomba nipate taarifa kutoka kwa Waziri miti ambayo imeshawahi kupandwa na watu wa TFS ili kuweza kujiridhisha kwamba miti hiikweli inapandwa na pesa hii inatumika inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka kutokana na muda nizungumzie suala la migogoro…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitoe shukrani zangu za dhati kwako kwa kuniona. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema kuweza kuzungumza kwa mara nyingine kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze kwa kusema kwamba maji ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa ambayo yameainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020. Ukisoma ukurasa wa 86 wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi unazungumzia mchakato huu wa kusogeza karibu huduma za kijamii, lakini pia tatizo la maji katika Jimbo langu la Rufiji ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda siku zote nimekuwa nikisimama nikizungumza kwa masikitiko, lakini pia hata katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri sijaona sehemu yoyote katika hotuba yake kuzungumzia Rufiji kwa ujumla. Tatizo la maji Jimbo la Rufiji ni kubwa sana. Labda niseme tu kwamba ni asilimia tano tu ya wananchi wa Jimbo la Rufiji ambao wanapata maji safi na salama na hata hii asilimia tano ambayo tunaizungumzia ni katika Kata ya Utete tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata tatizo la maji Tarafa ya Ikwiriri na tumepeleka maombi kwa Katibu Mkuu kuhusiana na ukarabati wa moter ambayo imeharibika kwa muda mrefu toka mwezi wa Kumi na Mbili, lakini mpaka hii leo tunavyozungumza tatizo la maji bado lipo. Shilingi milioni 36 ambayo tuliiomba Wilaya ya Rufiji kwa ajili ya ukarabati wa moter katika Kata hii, Tarafa hii ya Ikwiriri mpaka leo hatujapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia kiundani, Rufiji sisi hatukupaswa kuwa na tatizo la maji kwa sababu kwanza tuna Mto Rufiji ambao una uwezo wa kusogeza maji maeneo yote. Ni masikitiko makubwa, toka Adam na Hawa, mto huu haujawahi kutumika, siyo kwa kilimo wala siyo kwa maji tuweze kutumia wananchi wa Jimbo la Rufiji, lakini pia mto huu kama ungeweza kutumika vizuri, Wilaya ya Kibiti ingeweza kupata maji safi lakini pia Wilaya ya Mkuranga, Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Kisarawe zingeweza kupata maji safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko makubwa. Niliwahi kuzungumza na Waziri wa Wizara hii akaniambia kwamba kwa sasa hivi Mto Rufiji hautatumika kwa sababu wanategemea visima ambavyo vimechimbwa. Sasa unajiuliza; tunaeleka wapi? Tunategemea maji ya visima ambavyo vinaweza vikakauka wakati wowote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara hii, nina fahamu kwamba Serikali yangu inachapa kazi na siwezi kupingana na ndugu zangu hawa Wahandisi ambao Mheshimiwa Rais amewateua katika Wizara hii. Ninachokiomba kwa mwaka unaofuata, basi Wizara hii iweze kutufikiria sisi wananchi wa Pwani kwa sababu naamini iwapo Serikali itaweka mpango mzuri kwa ajili ya kusaidia wananchi hawa hususan kwenye jambo hili la maji, basi hata Dar es Salaam itapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua matatizo ya maji siyo Rufiji tu, ukienda Temeke leo hii maji hakuna; ukienda Mbagala maji hakuna; ukienda Kigamboni kwenyewe maji hakuna; maji kidogo ambayo yanapatikana yanasaidia maeneo ya Upanga, Oysterbay na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara hii itusaidie. Leo hii tunachukua maji kutoka Kanda ya Ziwa tunaleta mpaka Tabora, zaidi ya kilometa 500, lakini ukisema uchukue maji ya Mto Rufiji uyasambaze maeneo ya Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Kibiti na maeneo mengine ya Dar es Salaam haitagharimu zaidi ya kilometa 200 kwa sababu kutoka Dar es Salaam mpaka Rufiji ni kilomtea 160 tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara hii, ni kwa muda mrefu sasa sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji na Pwani tumenyanyasika kwa muda mrefu sana. Naamini ujio wangu Bungeni hapa basi itakuwa ni fursa kwa wananchi wangu waweze kufurahia usururu wangu, kwa sababu mimi najiita sururu kutokana na uchapakazi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii sasa itusaidie. Matatizo ya maji yako katika kata zangu zote, tukiondoa Kata moja tu ya Utete. Kata ya Ngarambe wananchi wangu wanakanyagwa na tembo kwa sababu tu ya kwenda kutafuta maji; Kata ya Mbwala wananchi wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa tano kufuata maji; lakini pia hata kata nyingine zote hakuna maji safi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia, tuingie katika mpango ili mradi mkubwa uweze kutokea pale katika Mto wa Rufiji tuweze kupata maji safi ambayo yataweza kusaidia wananchi wetu wa maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini iwapo tutatekeleza hili, tutakuwa tumetekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi na hii itatusaidia sana kuondoa kero kubwa ya wananchi ambayo imekuwa ni kilio cha muda mrefu. Masikitiko yangu kwa Rufiji nimekuwa nikiyazungumza kwa muda mrefu, inawezekana labda wenzangu walikuwa wakitoa malalamiko haya, hayafanyiwi kazi, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri, mimi na Naibu Waziri tumekaa kwa muda mrefu sana tumekuwa tukizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii kwa namna ambavyo amekuwa akichapa kazi. Namwomba apate muda ili aweze kufika Rufiji ajionee kero hizi za wananchi. Leo hii watoto wanashindwa kwenda shule ili waweze kufuata maji kwenye maeneo ambapo kuna mito. Katika maeneo hayo ambayo inabidi waende kufuata maji kuna hatari nyingi. Kuna wengine ambao wanaliwa na mamba, lakini pia inasababisha watoto washindwe kwenda shule kwa sababu ya kwenda kutafuta maji. Wanasafiri zaidi ya kilometa tano, kilometa sita kwenda kufuata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa leo hapa ni kumwomba Mheshimwa Waziri; nafahamu katika kitabu hiki, katika hotuba ya leo hajazungumza lolote kuhusiana na Rufiji. Hata kiasi cha fedha ambacho wamekitenga kwa ajili ya Rufiji, shilingi milioni 460 ni kiasi kidogo sana ambacho hakitaweza kutatua kero za maji katika Jimbo la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe tu, Jimbo la Rufiji na Wilaya ya Rufiji ni kubwa kuliko Mkoa wa Kilimanjaro. Eneo la Rufiji ni zaidi ya square kilometa 13,600 ambayo ni sawasawa na Mkoa wa Kilimanjaro; lakini utajionea kwamba Rufiji tunapata maji asilimia tano tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri, nafahamu wanachapa kazi sana, katika mpango unaokuja waweze kufikiria Rufiji ili kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kuondoa kero kubwa ya maji ambayo ni kilio na imekuwa ni aibu kwa muda mrefu. Kwa sababu ukianza kuzungumza matatizo ya maji Rufiji wakati tuna Mto Rufiji ambao leo hii wananchi hawawezi kusogea kutokana na hatari ya mamba, kwa kweli ni masikitiko makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yangu ni hayo. Naiomba Wizara ichape kazi kuweza kutusaidia wananchi wa Jimbo la Rufiji, Kibiti, Kilwa ambao tuko karibu; na naamini iwapo mradi huu utatekelezwa na Serikali basi tutaweza kutatua kero ya maji kwa maeneo yote ya Pwani mpaka Dar es Salaam ambako tunaamini kwamba hivi visima ambavyo leo hii Mheshimiwa Waziri anasema kwamba anachimba visima kwa ajili ya Dar es Salaam, ipo siku vitakauka. Sasa sioni sababu ni kwa nini tusichukue maji ya asili ambayo yapo; yalikuwepo toka Adamu na Hawa ambayo hata leo hayajawahi kutumika. Hayajatumika katika irrigation na hayajatumika katika maji safi ya kunywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba Wizara hii iweze kufikiria. Naamini kabisa hata kama utakuwa na PhD lakini unafikiria visima, ukashindwa kufikiria maji ya asili ya Mto Rufiji, kwa kweli naona kuna matatizo. Labda kama Wizara ituambie kuna mpango mkakati wa kuamua kuitenga Rufiji kwa sababu mambo haya nimekuwa nikiyazungumza kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara hii sasa kukaa na Wataalam kufikiria mradi mkubwa wa maji ambao utaweza kusaidia watu wa Pwani na maeneo mengine ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa, japokuwa nilidhani kwamba ningeweza kuchangia mchana lakini nakushukuru sana inawezekana mchana kutakuwa na wachangiaji walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia katika Taarifa zote za Kamati kama ambavyo zimewasilishwa na Wenyeviti. Kwa masikitiko makubwa sana, taarifa hii ya Kamati ya Mifugo na Maji iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu, ukurasa wa 12 unazungumzia migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana na taarifa hii ya Kamati ambayo kwa namna moja au nyingine wameshindwa kabisa kuona kwamba mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ni mgogoro mkubwa ambao unahitaji Serikali kuingilia kati kwa haraka. Nimesikitishwa sana kwa sababu ukisoma taarifa hii, mgogoro kati ya wakulima na wafugaji umeandikwa nusu page, kwa kweli ni masikitiko yangu makubwa na hiki ni kilio cha wakulima wote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maana kwamba hatuwapendi wafugaji, tunawapenda sana wafugaji, lakini kwa namna ambavyo Serikali imeshindwa kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji na ndiyo maana nasimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu na mara zote ambapo nasimama tunaona kabisa hatari kubwa; ile amani tuliyoachiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inakwenda kupotea kwa sababu tu ya mgogoro huu kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimelisema hili kwa muda mrefu sana na hata Waheshimiwa Mawaziri wanafahamu hilo. Mgogoro huu kati yetu, sisi Rufiji kule, hatuna mgogoro wa ardhi naomba Bunge lako Tukufu litambue, Rufiji hatuna mgogoro wa ardhi; tulichonacho ni criminal trespass, mwingiliano wa jinai ambao unafanywa na wafugaji katika maeneo ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa na mwezi wa 11 watu wawili wameuawa, mkulima alichinjwa na mfugaji alichomwa moto akiwa hai katika maeneo ya Kilimani. Cha kushangaza sana hakuna kiongozi yeyote wa Serikali au Wizara aliyefika katika maeneo husika ili kuweza kutoa pole na kuweza kuongea ili kuondoa mgogoro huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko yangu makubwa sana na Wanarufiji wote leo hii wananiangalia kwenye TV, nimesimama mbele hapa; si Tanzania tu, dunia nzima Wandengereko wote dunia nzima na Warufiji wote wanajua; mgogoro kati ya wakulima na wafugaji unapaswa utatuliwe haraka sana vinginevyo unakwenda kuligawa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mambo mazuri ambayo alituachia Rais wetu wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kupendana Watanzania tunaona kabisa kwamba tunaanza kubaguana. Mimi nasema wazi mbele ya Bunge lako Tukufu, mgogoro huu unakuwa mgumu kwa sababu viongozi wa Wizara hii wengi ni wafugaji na wanashindwa kutatua matatizo ya wakulima. Naomba niishie hapo, message sent and delivered kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tatizo kubwa la RUBADA. Tunayo hii Mamlaka ya RUBADA, Mamlaka ya kuendeleza Bonde la Mto Rufiji. RUBADA ilianzishwa mwaka 1978. Dhamira ya uanzishwaji wa RUBADA ilikuwa ni kuendeleza bonde pamoja na Mto Rufiji, lakini tunasikitika sana Warufiji baada ya Mamlaka hii kukabidhiwa Bonde la Mto Rufiji basi wananchi wa Rufiji wamekuwa maskini wa hali ya juu. RUBADA imeshindwa kuwasaidia Warufiji lakini pia RUBADA imeshindwa kuwasaidia wananchi wote wanaoishi na wanaopitiwa katika Bonde la Mto Rufiji kuanzia Morogoro na maeneo mengine yote ya Tanzania yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge liazimie sasa kuivunja RUBADA mara moja na Mamlaka yote ambayo inamilikiwa na RUBADA ibaki chini ya Halmashauri husika ikiwa ni pamoja na vijiji. Tunaamini kabisa Warufiji tukikabidhiwa bonde letu la Mto Rufiji tutaweza kuwatafuta wawekezaji watakaosaidia kilimo cha umwagiliaji. Naomba katika maazimio liingie azimio la kuifuta RUBADA, haina maslahi yoyote na hawana uwezo wa kuwasaidia Watanzania wanaoishi maeneo ya Rufiji zaidi ya kufanya udalali ambao hata sisi wenyewe tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushie jambo lingine la mwisho, ni kuhusu ujenzi wa nyumba zinazojengwa na National housing.Tukiangalia dhamira ya Mwalimu Nyerere, mimi ni mjamaa kweli kweli! Tukiangalia azimio la Mheshimiwa Rais wetu wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, uanzishwaji wa National Housing ulilenga kuwasaidia Watanzania wanyonge, Watanzania wadogo wasio na uwezo, wafanyakazi wa Serikali, lakini leo hii National Housing ipo kwa ajili ya matajiri tu. Hakuna Mtumishi wa Serikali wala Mtanzania mnyonge mwenye uwezo wa kwenda kupanga kwenye nyumba za National Housing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliombe Bunge lako Tukufu, ile dhamira ya uanzishwaji wa National Housing kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza alivyoanzisha, kuchukua nyumba za Mabepari na kumilikiwa na Serikali. Dhamira ile ilikuwa ni kwenda kuwasaidia Watanzania wanyonge pamoja na Watumishi wa Serikali, naomba Bunge lako pia liazimie, National Housing iweze kuchunguzwa na kuangaliwa sasa ni namna gani itaweza kuwasaidia Watanzania walio wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe maazimio haya yaingie na niombe Mwenyekiti wa Kamati atakaposimama hapa aweze kujibu hoja hizi kama ambavyo nimeweza kuzieleza. Mgogoro wa wakulima na wafugaji unahitaji kuingiliwa kwa haraka sana na Serikali ili uweze kutatuliwa. Ni jambo la aibu sana kwa Kamati kuandika nusu page mogogoro wa wakulima na wafugaji. Watanzania wanauawa, Watanzania wanauana, wamepoteza dhamira ya kupendana wenyewe kwa wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ile miiko ya Mwalimu Nyerere aliyoianzisha wakati ule wa kupigania uhuru na hata baada ya uhuru. Tunaomba Kamati iweze kujiuliza ni kwa nini wamefikia hatua hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma vizuri ukurasa wa 13 unasema kwamba viongozi wa Serikali ambao wanashiriki katika kutatua migogoro hii hawakuwashirikisha wafugaji. Hili ni jambo la aibu kabisa. Ni wakulima wangapi wameshirikishwa katika mgogoro huu? Hili ni jambo la aibu, lakini tunafahamu kwamba kwa sababu wakulima hawana pa kusemea, lakini sisi kama viongozi wao tunasimama hapa kwa ajili ya kuwatetea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wapiga kura walio wengi; lakini tunatambua kwamba katika pato la Taifa, kilimo kinachangia asilimia zaidi ya 70. Tuiombe Serikali itambue hilo. Pia hata Wizara ukiiangalia namna ambavyo inatupuuza wakulima. Ukiangalia katika bajeti iliyopita, Wilaya yetu ya Rufiji ambayo tuna ekari zaidi ya 13,000 ambapo kuna bonde zuri kwa ajili ya kilimo tungeweza kuuza Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ya Kati, lakini Wizara ya Kilimo imetenga sifuri kwenye bajeti yake ya kilimo kusaidia wananchi wa Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusaidia kilimo tunaamini kwamba hata hiyo Tanzania ya viwanda hatutafikia huko. Naomba kuwasilisha lakini naomba; katika maazimio niliyoyaomba ni pamoja na kuifuta RUBADA kwa sababu haina faida yoyote kwa Watanzania. RUBADA wamekuwa madalali na sisi hawatusaidii lolote. Tunaomba bonde libaki chini ya wananchi wanaomiliki bonde hilo na maeneo ya mto ili tuweze kuwatafuta watu watakaoweza kutusaidia katika kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wana Rufiji wote duniani, nasimama hapa nami kuwasilisha ya kwangu lakini kwa kuzingatia maelekezo yaliyowahi kutolewa katika kitabu chake Paul Flynn, mmoja wa Wabunge wazoefu nchini Uingereza kinachozungumzia how to be an MP. Pia Profesa Phillip Collin naye katika kitabu chake aliwahi kuzungumzia mambo ya msingi kabisa ambayo Mbunge anapaswa kuyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumshauri dada yangu Mheshimiwa Sabreena atambue kwamba BAKWATA sasa ina uongozi ulio imara na wachapakazi sana. (Makofi).
Shekhe Mkuu wa sasa, Shekhe Zuberi ni mchapakazi sana na mambo haya ya dini tusiyalete kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu mmoja anaitwa K. Sachiarith mmoja kati ya wa washindi wa Global Award, katika Mkutano wa 136 wa Bunge wa Dunia uliofanyika kule Bangladesh, aliwahi kuzungumza maneno ambayo napenda niyazungumze katika Bunge lako hili Tukufu. Ndugu Sachiarith aliwahi kusema kwamba kama akinamama wangewezeshwa miaka 50 iliyopita basi dunia tungekuwa na Taifa jema sana (if women were empowered in the last fifty years we could have a better world).
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliendelea kwa kusisitiza kwamba iwapo vijana wangezaliwa na akinamama waliowezeshwa miaka 50 iliyopita basi tungekuwa na vijana wazalendo wa Taifa, waadilifu na tungekuwa na Taifa lenye nguvu sana, Tanzania ingekuwa ni Taifa lenye nguvu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme maneno haya kwa sababu tunaona kabisa kwamba vijana waadilifu utawakuta upande huu tuliokaa wengi. Hapa nataka nimtofautishe ndugu yangu Bwana Tundu Lissu ni miongoni mwa ignorant pan-politician. Nimeona niseme hivi kwa sababu Tundu Lissu hana uzalendo wa Taifa hili, anaendekeza harakati, yeye ni mwanaharakati lakini si mwanasiasa. Kwa hiyo, tunawaomba Watanzania kumuepuka na kuepukana naye kwani dhamira yake ni kuligawa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 na 64 ni kutunga sheria na kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasheria wote duniani wanatambua kwamba nchi hii inaendeshwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa......
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naikataa kwa sababu Shekhe Zuberi ni Shekhe ambaye anatambua elimu ya dunia pamoja na ya akhera. Ni mtu muadilifu na mchapakazi sana na ameweza kui-transform BAKWATA kuwa ni chombo kizuri sana kwa Waislam. Niwaombe Waislam wote kuendelea kuiamini BAKWATA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasheria wote duniani wanatambua kwamba nchi inaongozwa na katiba, sheria, kanuni na taratibu. Vilevile inaongozwa na taratibu za Chama Tawala ambacho ndicho kimeiweka Serikali madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme hili kwa sababu upo upotoshaji mkubwa uliozungumzwa na Tundu Lindu kuhusu Rais kwamba haitaki Katiba Mpya. Naomba nikumbushe Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ambayo katika ukurasa wake wa nne (4) inazungumzia mambo yatakayotekelezwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Katika Sura ya Saba ya Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi pamoja na maneno mengine ukurasa 163 katika aya ya 144 inazungumzia mambo yafuatayo ambayo naomba niyanukuu hapa.
“Mchakato wa kutunga Katiba Mpya umeendeshwa na umefikia hatua ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba ambayo itapigiwa kura ya maoni”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo nchi hii inaongozwa kwa mujibu wa taratibu kama ambavyo nimezisema.
T A A R I F A...
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naikataa kutoka kwa layman huyu na naomba nimsaidie kwamba nchi inaongozwa na katiba, sheria na kanuni na taratibu ambazo Chama Tawala ndicho kilichosimamisha dola madarakani. Chama cha Mapinduzi kilikuwa na Ilani ya Uchaguzi ambayo wananchi walio wengi waliiona na kuisoma wenzetu walikuwa na tovuti ambayo ilikuwa ni vigumu kwa wananchi wa vijijini kuiona na kuisoma na kuikubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 118 ya Katiba ambayo Tundu Lissu amepotosha hapa jamii kwa kusema kwamba Mheshimiwa Rais amevunja Katiba kwa kutomchagua Jaji Mkuu wa Tanzania. Ibara ya 118 haimlazimisha Rais kuchagua Jaji Mkuu wa Tanzania. Ibara ya 118 iko wazi kabisa. Mheshimiwa Tundu Lissu anaifahamu sheria na anaijua Ibara hii imezungumza vizuri lakini anachofanya ni kupotosha Watanzania na kuleta taharuki katika nchi yetu hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa masuala mengi kuhusu demokrasia na utawala bora. Chama cha Mapinduzi kinaongozwa na Ilani na ukurasa wa 146 umezungumzia demokrasia na utawala bora. Nataka niseme hapa kwamba chama hiki kina demokrasia ya kutosha na unapomwona nyani anamtukana mwenzie ni vyema akajiangalia nyumani kwake. Chama hiki kimekuwa na Wenyeviti kadhaa kila baada ya miaka kumi wenzetu wamekuwa na Mwenyekiti amekaa madarakani zaidi ya miaka 20. Hauwezi kuzungumzia demokrasi wakati nyumbani kwako kunaungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii mwaka 1961 ilikuwa na Rais wa kwanza alikuwa Mzanaki, Mheshimiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Baada ya Mwalimu Nyerere wananchi walimchagua Rais wa Awamu ya Pili, Mzee wetu Mheshimiwa Ally Hassan Mwinyi, alikuwa Mzaramo wa kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1995 baada ya kupitishwa mfumo wa vyama vingi 1992 tulimchagua Mheshimiwa Benjamin Mkapa, huyu alikuwa Mmakonde kutoka kule Kusini. Mwaka 2005 tulimchagua Mheshimiwa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete huyu alikuwa Mkwere kutoka pale Pwani. Taifa letu leo hii tunashuhudia kuwa na Rais Msukuma kutoka Kanda ya Ziwa. Hii ni demokrasia ya hali ya juu ambayo wenzetu hawana.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema nyani akawa anaona kundule kuliko kutukana wenzio wakati wewe mwenye una matatizo.Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze katika kuishauri Serikali yangu njema ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianzie hapo kwenye uzalendo, miaka ya 90 Mwalimu Nyerere aliwahi kumthibitisha Kawawa katika moja ya mikutano yake pale Mnazi mmoja kusema kwamba Kawawa ni muadilifu sana na alikuwa tayari kutoa machozi kuthibitisha kwamba Kawawa alikuwa ni muadilifu. Nami ndani ya Bunge lako Tukufu naomba kuthibitisha kwamba iwapo siku moja Wabunge walio wengi wakasema kwamba mambo mazuri anayofanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa nchi hii si uzalendo, basi nitaliomba Bunge lako hili Tukufu kufuta hili neno uzalendo katika dictionary ya Kiswahili. Kwa sababu mambo makubwa anayoyafanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni uzalendo wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwa maneno mawili matatu ambayo nimeyaacha pembeni. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana wakati unahitimisha hoja yako hapa...
Nikukumbushe jambo moja, kwanza, tuiangalie kada ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ambao wamekuwa wakipata mishahara midogo. Zipo taarifa wako Mahakimu zaidi ya 118 ambao hawajapandishwa vyeo na hao ni Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa hali ya uchumi tuliyonayo ni vyema tukawaangalia Mahakimu pamoja na Wanasheria wa Serikali ili kuwawezesha fedha kidogo kwa ajili …
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa napenda niseme kwamba Taifa hili linategemea Bunge na uzalendo wetu ndio utakaoliweka Bunge hili katika…
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja na nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kila jambo alilolifanya katika Bunge hili.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dakika ni chache sana, nami nichukue fursa hii kuwatakia pole Watanzania wote ambao wamekubwa na majanga mbalimbali hususan ya watoto wetu kule Arusha; lakini pia Watanzania wote kule Rufiji ambao wamekumbwa na matatizo mbalimbali ya ujambazi ambayo niseme tu kwa hali ya kawaida, tatizo hilo la ujambazi limeacha wajane wengi na watoto wengi yatima. Naliomba Bunge lako wakati mwingine tunapochangia kwenye mambo ya sherehe, basi mnikumbuke kule Rufiji, mnifikirie kwani nina wajane wengi na watoto yatima wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kutoa pole kwa wale wote waliokumbwa na mafuriko makubwa kule Rufiji hususan Kata yangu hii ya Mohoro, kwa kina Chii kule mpaka kwa mzee Mikindo, Kata ya Mwasemi, Kipugila, Ikwiriri, Umwe, Mgomba, Ngarambe pamoja na Chemchem.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe watu wa Rufiji msemo mmoja katika Quran unaosema kwamba kullama yuswiibana, illamaa qataba Allah lana, ikimaanisha kwamba nothing will happen to us, except what Allah has decreed for us. Hakuna linaloweza kutokea mpaka pale ambapo Mwenyezi Mungu amelipanga litokee baina yetu. Mwenyezi Mungu ametuandikia kila jambo litakalotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwatia moyo wananchi wangu wa Rufiji wasibabaike na jambo linaloendelea na hili ni tatizo la amani, waendelee kuijenga nchi yao, kwani Tanzania hii ni ya kwetu sote nasi tutaendelea kuwapigania huku katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini pia wale ambao wamesoma vitabu mbalimbali watakumbuka kitabu cha “Comperative Government and Politics,” watatambua ni namna gani Mheshimiwa Rais ataweza kulisaidia Taifa hili hapo mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nampongeza sana na tuseme tu kwamba nchi hii inamhitaji sana. Mabadiliko makubwa katika nchi kama Bangladesh ambao wameweza kubadilika kwa kipindi cha miaka 10, tunaamini kabisa kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anaweza kuivusha Tanzania kutoka hapa ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ya kuzungumza, lakini niseme kwa uchache tu kwamba suala hili la maji limezungumzwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi. Ukiangalia Ilani yetu ya Uchaguzi; Serikali imeundwa na Chama cha Mapinduzi na utekelezaji ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Pia tunaongozwa na Kanuni za Uongozi wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mujibu wa Ilani, katika ukurasa wa nne wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, inasisitiza Serikali kufanya yale yote yanayoletwa ndani ya Serikali kwani ni yale ambayo yanaongozwa na Ilani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 66 wa Ilani yetu ya Uchaguzi inasisitiza katika kusogeza huduma za kijamii karibu na kwa wananchi. Suala la maji safi na salama limezungumzwa katika ukurasa wa 83 wa Ilani, nami nataka nijikite katika ukurasa wa 85 wa Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo imedhamiria kutua ndoo kichwani kwa mwanamke. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa ukurasa 85, Ilani imedhamiria kuongeza asilimia 53 ya maji vijijini mpaka kufikia asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, kule kwangu Rufiji niliwahi kufanya ziara katika kijiji kimoja pale Kikobo. Wananchi wa Kikobo wamehama kijiji kile kwa sababu ya tatizo la maji na walichonieleza ni kwamba kule Dar es Salaam ukiwa na pesa kidogo unaonekana unatoka kipara kichwani, lakini akinamama wa eneo la Kikobo wanatoka vipara kwa sababu ya kubeba ndoo kwa muda mrefu. Wanasafiri na maji kwa zaidi ya kilometa saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tatizo hili ni kubwa sana kwa nchi yetu, nami niseme tu kwamba sisi tulishaanza utekelezaji wa Ilani. Mimi binafsi nilishaanza uchimbaji wa visima mbalimbali katika eneo langu, yale maeneo korofi kabisa!

Mheshimiwa Naibu Spika, nimechimba visima katika Kata ya Mgomba Kusini, Mgomba Kati, Ikwiriri Kati, Nambanje, Mpalange, Mtanange tunakwenda kuchimba pamoja na Mpima; lakini pia Mpalange kwa Njiwa kote tunakwenda kupeleka visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo korofi ambayo tunaamini kabisa Serikali ikiweza kutusaidia, tutaweza kutatua kero ya maji. Hapa nazungumzia katika Kata ya Chumbi, hususan katika Kijiji cha Nyakipande, pamoja na Miangalaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa, napenda niwapongeze watani wangu hawa wawili kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja pamoja na marekebisho yatakayofanywa na Wizara. Ahsante.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua anazochukua kukabiliana na Upotevu wa Mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 25 Aprili, 2017 nilisimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu na nikasema kwamba nchi hii imepata Rais mzalendo namba moja. Niliposimama nililiomba Bunge lako Tukufu kufuta neno uzalendo katika Kamusi ya Kiswahili iwapo siku moja Wabunge walio wengi watasema kwamba mambo yanayofanywa na Dokta Pombe Magufuli siyo uzalendo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokifanya Dokta John Pombe Magufuli ni utekelezaji wa Kanuni ya 10 ya Uongozi (The Law of Connection) ambayo inasema kwamba, leaders touch the heart before they ask for the hand. Mambo haya yaliyofanywa hivi punde ni ya kizalendo na yamemgusa kila Mtanzania katika moyo wake, wale walio katika Vyama vya Upinzani lakini pia hata wale ambao tupo katika Chama Tawala hapa nchini na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni uwepo wa mikataba mibovu na nakumbuka wakati nasoma historia nilimsoma Carl Peters mwaka 1884 ambaye aliingia Afrika na kuwasainisha Mababu zetu mikataba ya hovyo kabisa. Leo hii tunajionea uwepo wa mikataba mibovu kabisa hapa nchi ambayo Rais wetu Dokta John Pombe Magufuli amedhamiria sasa kwa kupitia Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015-2025, ukisoma vyema ukurasa wa 28 na 29 wa Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, inazungumzia kuhusu usimamiaji wa madini yetu na kuhakikisha kwamba madini haya yanawanufaisha Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Azimio letu hili ambalo limetolewa siku ya leo lakini pia niiombe tu Serikali kufuata maelekezo yaliyowahi kutolewa na Keith Jefferis ambaye aliwahi kuwa Deputy Governor kule Botswana ambaye aliwahi kusema kwamba, the paradox of plenty inatokana na kwamba nchi nyingi zenye utajiri wa madini zimekuwa na umaskini wa hali ya juu. Sasa tuombe yale maelekezo yaliyotolewa na Keith Jefferis tuweze kuyafuata katika nchi yetu hii ili sasa madini haya yaweze kuwakomboa Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi aliyowahi kuyazungumza Keith Jefferis ni uwepo wa open and transparent katika mineral licensing pamoja na taxation regime. Tuombe uwazi uwepo katika mikataba hii ambayo tayari Rais amekubali kuileta kwenye Bunge hili, uwazi huu utaweza kuisadia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa sisi Watanzania hususani Jimbo langu la Rufiji wanaamini kabisa kwamba mambo haya yakitekelezwa vyema barabara zetu za kutoa Nyamwage - Utete zitajengwa kwa kiwango cha lami, mambo haya yakitekelezwa vyema basi hata leo hii tusingekuwa na deni la Taifa. Naamini kabisa mambo anayofanya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nimshukuru sana mzalendo namba moja nchini ambaye ni Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi nzuri sana siku tatu zilizopita za kusimamia rasilimali za nchi yetu hii Tanzania. Niliwahi kusema hapa kwamba, Dkt. John Pombe Magufuli ni mzalendo namba moja, na uzalendo wake tunauona hapa kwa namna ambavyo anawatetea watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi kwa Waheshimiwa Mawaziri wote wa Wizara hii, kwanza kwa Mheshimiwa Lukuvi, Naibu wake pamoja na Wasaidizi wao wote, kwa kweli Wizara hii ni ngumu lakini Mheshimiwa Lukuvi amefanya kazi nzuri sana kwa kipindi kifupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia umaskini uliopo katika Jimbo langu la Rufiji. Jimbo la Rufiji lina square kilometer 13,600 na eneo la Bonde la Mto Rufiji ambalo linafaa kwa ajili ya kilimo ni zaidi ya hekta 500,000. Kutokana na utapeli wa madalali na kutokana na wawekezaji matapeli ambao wameingia Rufiji, leo hii ukifika TIC hauwezi kupata eneo la uwekezaji Rufiji. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kuliangalia hili na kuangalia uwezekano wa kunyanganya maeneo yote ambayo wawekezaji matapeli wamechukua ardhi yetu ya Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaskini tulionao ni kwa sababu matapeli hawa wamehodhi maeneo haya na hawayafanyii shughuli yooyote. Leo hii Rufiji tusingekuwa maskini kwa sababu ardhi ndio utajiri wa hali ya juu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri sasa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali yetu ya Awamu ya Tano iweze kupambana na matapeli hawa. Yako maeneo yaliyochukuliwa na watu wa RUBADA, pia yako maeneo yaliyochukuliwa na watu wanaojifanya ni wawekezaji lakini siyo wawekezaji wa kweli. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri maeneo hayo uyarudishe ili sasa wale wawekezaji wanavyopita TIC waweze kuelekezwa na kufika Rufiji wapatiwe maeneo ya uwekezaji. Kwa sababu, maeneo tuliyonayo ni ya kutosha, ardhi ipo tupu, wananchi wanashindwa kushiriki kwenye shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namwomba Mheshimiwa Waziri, kama sio yeye au Waziri anayehusika, atakapofika hapa atupe taarifa ni kwa nini mwaka 2006 Serikali iliamua kuhamisha mifugo kutoka Bonde la Ihefu na kuleta mifugo katika Bonde la Mto Rufiji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tufahamu sababu ya kuhamisha mifugo Bonde la Ihefu. Tunafahamu kabisa kwamba uhamishwaji wa mifugo kutoka Bonde la Ihefu kupelekwa maeneo mbalimbali ya nchi ulitokana na uharibifu mkubwa wa Bonde la Ihefu. Sasa nataka nifahamu, je, Serikali ilidhamiria kuleta mifugo katika Bonde la Rufiji ili sasa na bonde hili liweze kuharibika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu hayo Mheshimiwa Waziri; kama sio yeye au Waziri yeyote anayehusika atakapofika hapa atupatie majibu haya, ili Warufiji waweze kufahamu kiini cha matatizo haya, kwa sababu wakulima leo hii wanashindwa kushiriki katika shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba Warufiji walikuwa na ndoto za kupatiwa kiwanda katika eneo la Muhoro pamoja na Chumbi. Mheshimiwa Waziri atakapofika hapa, naomba atuambie, je, ardhi ile ambayo ilitengwa kwa ajili ya mwekezaji, bado ipo? Je, mwekezaji huyu anaifanyia utaratibu gani ili sasa tuweze kupata majibu ya jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 3 Machi, 2017, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifika Rufiji na katika maeneo aliyofika, alifika Ikwiriri na katika kauli alizowahi kuzitoa Mheshimiwa Rais aliwaambia Watanzania wa Rufiji, hususan Wenyeviti wa Vijiji kutouza maeneo yao. Aliwaambia wawe makini sana na madalali na matapeli wanaotaka kuchukua ardhi yetu pale Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 9 Septemba, 2016 Waziri Mkuu pia alifika Rufiji, lakini pia katika maeneo ambayo yana mgogoro mkubwa wa ardhi ni eneo letu la Kata ya Chumbi. Tarehe 4 Mei, 2017 Waziri wa Ardhi aliniandikia barua ya kutatua mgogoro wa ardhi pale Chumbi. Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Waziri hakuweza kufika Chumbi, lakini wananchi wa Kata ya Chumbi wanaamini labda mimi ndio nimemzuia Mheshimiwa Waziri kufika Kata ya Chumbi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa, atoe majibu, ni kwa nini hakufika katika Kata ya Chumbi ambako kuna mgogoro mkubwa wa ardhi? Miongoni mwa malalamiko ya wananchi ni kwamba, Mwenyekiti wa Kijiji ameuza ardhi ambayo ina ukubwa wa takriban zaidi ya ekari 2,400 kwa Sh. 9,700/= kwa ekari moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Mheshimiwa Rais alishatoa tamko la Wenyeviti wa Vijiji kutouza maeneo yao, naomba Mheshimiwa Waziri akifanya majumuisho, basi atupe majibu ya jambo hili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikupongeze wewe kwa kuiunda Kamati hii ambayo tunafanya kazi nao kwa karibu sana chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Nyongo. Tunawashukuru Wajumbe wa Kamati kwa sababu wakati wote ambao tumekuwa tukipokea maoni ya Kamati hii tumekuwa tukifanyia kazi ipasavyo. Unaweza ukaona hakuna hoja nyingi kuhusu Wizara yetu. Zipo hoja tano ambazo Kamati imeibua na moja ambayo Mheshimiwa Festo Sanga ameizungumza mdau wa karibu sana katika sekta hii ya michezo na sisi tunamshukuru sana kwa ukaribu wake.

Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kwamba wakati Mheshimiwa Rais anaianzisha Wizara hii alizingatia yale maelezo ambayo Rais wa Awamu ya Kwanza aliyatoa wakati anaanzisha Wizara ya Vijana na Utamaduni. Tutahakikisha kwamba yale maono na fikra za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaziendeleza na tunatambua kwamba anguko la sekta zetu ambazo tunazisimamia hasa Sekta ya Utamaduni ni anguko la Taifa letu. Kwa hiyo tutapambana kuhakikisha kwamba yale maono ya wazee wetu, viongozi wetu waasisi wa Taifa hili tunayalinda na kuyasimamia ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwashukuru sana wadau katika sekta zetu hasa sekta za michezo, kwa kuona namna ambavyo Serikali inafanya kazi kubwa katika kuboresha sekta hii. Nawashukuru wadau kwa kukubali mapinduzi makubwa ambayo tunakwenda nayo katika Sekta ya Michezo, Sanaa na Utamaduni.

Mheshimiwa Spika, nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba, leo tumepokea taarifa kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi ambazo zinafanya vizuri sana hasa katika ligi bora Afrika na Tanzania. Kwa takwimu ambazo zimetolewa leo ni ligi namba tano katika ligi bora kabisa Afrika, kidunia Tanzania ni ligi namba 39 kwa ligi ambazo zinafanya vizuri kabisa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutahakikisha tunaendeleza yale ambayo viongozi wetu Mheshimiwa Rais anatamani yatokee katika sekta hii. Nikiri kwamba tuko katika mapinduzi makubwa kwenye sekta hii na tunatambua kwamba hii ndio sekta ambayo Serikali tunatumia kama nguvu shawishi yaani soft power ya nchi. Hivyo, tutahakikisha maelekezo ya viongozi, maelekezo ya Kamati na maelekezo yako tunayafanyia kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, tunayo mambo matano ambayo yameibuliwa, lakini nianze na hili suala la kuhusu Kiswahili (BAKITA) kama ambavyo wewe mwenyewe ulivyosema. Niseme tu kwamba maneno yote ambayo uliyazungumza yaliyowasilishwa ni maneno fasaha na sanifu kama ambavyo yamewasilishwa kwa mujibu wa sarufi ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, katika Kiswahili kuna kauli tano za msingi zinazoathiri maumbo ya vitenzi, kauli hizi ni kama ifuatavyo: -

(a) Kauli ya kutenda;

(b) Kutendwa;

(c) Kutendewa;

(d) Kutendana; na

(e) Kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sarufi za Kiswahili zina kanuni ya kubadilisha vitenzi kuwa nomino na katika kukamilisha mchakato huo, kiambishi “u” huwekwa mwanzoni na kiambishi “g” huwekwa mwishoni. Kwa hiyo yale ambayo yamezungumzwa ni Kiswahili fasaha na sanifu kama ambavyo naomba nielekeze hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Kamati iliibua mambo kadhaa, jambo la kwanza, ilikuwa ni msingi wa uibuaji wa vipaji; jambo la pili, ni ujenzi wa viwanja kwa ushirikishwaji wa wadau; jambo la tatu, ni kuhusu vazi la Taifa; jambo la nne ni kuhusu mdumdo wa Taifa (beats); na jambo la tano, ni kuhusu Chuo chetu cha Malya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Festo Sanga aliuliza kuhusu hatua ambayo Serikali imefikia katika ujenzi wa viwanja. Sisi kama Serikali tumefanya kazi kubwa sana ya kuwashirikisha wadau katika kuibua vipaji. Hata hivyo, nichukue fursa hii katika kushukuru Maafisa Utamaduni kote nchi nzima ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa na kazi nzuri sana ya kutambua vipaji katika maeneo yetu. Tunatambua katika vijiji, vitongoji, kata na wilaya kuna vijana wengi sana wenye uwezo na wenye vipaji vikubwa, lakini hawatufikii kwa ukaribu kwa sababu ya maeneo waliyopo. Tumekwishawaagiza na tumefanya vikao kadhaa na Maafisa Utamaduni ambao tumewekeana mikakati ya namna gani tunaweza kwenda kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaibua vipaji.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nitumie fursa hii kuwapongeza sana Watanzania ambao wanatumia vipaji vyao kama mtaji wao hasa wale Ramadhan Brothers ambao wamefanya kazi kubwa kutangaza nchi yetu, kutangaza utalii wa Tanzania, vile vile na wadau wengine wadau wengine ambao wamekuwa wakiibuka, akiwemo bwana Mandoga amekuwa akifanya kazi nzuri, nje ya mipaka ya Tanzania, anaitangaza vizuri Tanzania. Hata hivyo sisi kama wizara tunawapongeza sana kwa kazi kubwa na kazi nzuri ya kuendelea kuitangaza nchi yetu kupitia vipaji walivyo navyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwishaanzisha mchakato wa mtaa kwa mtaa. Tunatambua kwamba katika nyakati ambazo tulikuwa tunaanza mchakato huu hatukuwa na bajeti ya kutosha. Tunaishukuru Kamati kwa kuendelea kutupigania, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia. Basi tunaamini kabisa katika bajeti ijayo tutakuwa tumeweka kifungu maalum kuhakikisha kwamba tunakwenda kwa kasi sana kuhakikisha kwamba tunafika kila mtaa. Dhamira yetu na dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kwenda mtaa kwa mtaa kusaka vipaji, vipaji vya mpira lakini na vipaji vingine.

Mheshimiwa Spika, eneo hili la ujenzi wa viwanja, nichukue fursa hii kumshukuru sana Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa ushirikiano wa karibu ambao tumekuwa nao. Pia nichukue fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu, tunatambua kwamba inawezekana huko nyuma hatukuwa na mipango mizuri, inawezekana ndio sababu ya kwa nini tumechelewa kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa viwanja unaanza. Hata hivyo, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mipango imekamilika, michoro imekamilika na tunaishukuru Wizara ya Fedha kwa kuridhia sisi kuendelea kwa hatua ya kutafuta mkandarasi na hatua nyingine.

Mheshimiwa Spika, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba zabuni ya ujenzi wa uwanja wa Dodoma tayari imekwishatangazwa. Vile vile dhamira yetu sisi kama Serikali, kama Wizara ni kwenda kujenga uwanja wa kisasa ambao Afrika hakuna. Kwa hiyo tutajenga uwanja wa kisasa kweli kweli hapa Dodoma na Zabuni tumekwishaitangaza. Kwa hiyo mategemeo yetu mwezi wa tatu tutamkabidhi Mkandarasi site kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja wa mpira wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa viwanja vya sanaa, tayari zabuni tumeitangaza na hata Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuingia kwenye tovuti ya Serikali wakaweza kuona zabuni ya uwanja wa sanaa tayari imekwishatangazwa. Hata hivyo, Mkandarasi wa ujenzi wa viwanja changamani; vya Dodoma pamoja na Dar es Salaam tayari amekwishapatikana. Kwa hiyo, tunategemea wakati wowote mchakato wa ujenzi utaanza. Kwa hiyo, naomba niendelee kuwatia matumaini Watanzania. Sisi katika Wizara hii tumekwishakubaliana kufanya kazi kwa bidi, tumekubaliana mimi na wasaidizi wangu kufanya kazi usiku na mchana.

Mheshimiwa Spika, tutawathibitishia Watanzania kwamba yale mapinduzi ambayo wanatamani kuyaona yatatokea katika nyakati ambazo Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mabadiliko hayo.

SPIKA: Sekunde thelathini, kengele imeshagonga.

WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nitoe taarifa tu kwamba ule mchakato wa ujenzi wa shule 56 tayari umekwishaanza. Tumekwishaanza kule Tabora na tutakuwa na shule saba za mfano za kuanzia na naamini kufikia mwezi wa Machi au Aprili, Mkandarasi atakuwa amekwishapatikana kwa kuwa tayari wizara ya Fedha imekwishatupatia fedha za kuanzia. Tunamshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi kubwa na nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema tu kwamba, Watanzania wana matumaini makubwa sana na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi katika wizara tutahakikisha tunafanya kazi usiku na mchana katika kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta hii ya Michezo, Sanaa na Utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja ya Kamati iliyotolewa mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada usiku wa deni haukawii kukucha.” Baada ya siku mbili za michango mizuri sana ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge, nianze hitimisho langu kwa kuahidi kuwa ingawa hapa nitajibu kwa kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala yaliyoibuliwa, lakini nikuahidi kwamba michango mingi ina tija na tunaandaa utaratibu ili tuweze kuijibu kwa maandishi michango yote ambayo imeulizwa na Waheshimiwa Wabunge. Naomba nichukue pia fursa hii niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, nitajenga matumaini katika mioyo ya Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge waniruhusu niingie katika vifua vyao ili nipunguze mazito waliyoyabeba ya changamoto mbalimbali za migogoro ya aina mbalimbali inayohusu Wizara yetu. Natambua kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa amezungumza kuhusu changamoto, ndovu akataja kwa jina lingine watu wakacheka kidogo, lakini nikuthibitishie, nitaingia katika mioyo ya kila Mbunge, kwa sababu natambua kwamba Waheshimiwa Wabunge hawa wanafanya kazi kubwa ya kuzungumzia maslahi ya wananchi wetu katika maeneo yao. Kwa hiyo niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niseme tu mambo yafuatayo kwamba wananchi wetu waliotupa heshima ya kuwa katika Bunge hili Tukufu sisi pamoja na Chama chetu Tawala, yako mambo wanayoyahitaji sisi kama Serikali tuyafanye. Kwa muda mrefu Wizara yetu hii Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miongo mingi sana wamepita Waheshimiwa Mawaziri wengi sana na kila nyakati ambazo Waheshimiwa Mawaziri wakisimama nyakati hizi za bajeti mambo mengi yanayozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge imekuwa ni changamoto changamoto, changamoto kila siku ni changamoto katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, hata yale mambo ambayo yanatuletea tija katika Utalii Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyasahau hawayazungumzi kwa mapana yake, kwa sababu Wizara hii toka nyakati za Baba wa Taifa mwaka 1961 mpaka nyakati hizi za Rais wetu wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na changamoto, changamoto, changamoto. Sasa nadhani wakati umefika na lazima tuseme kwamba wakati ni sasa kuhakikisha kwamba sisi kama Wizara tunajipanga vizuri ili kuhakikisha kwamba tunazimaliza changamoto zote ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumza ili tutakapokutana hapa mwakani tusizungumze tena changamoto, tuzungumze namna tutakavyoweza kukuza utalii wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge nikushukuru sana wewe, niwashukuru Maafisa pamoja na Wenyeviti wote wa Kiti chako kwa kusimamia vyema mijadala hii kuhusu Wizara hii kwa siku hizi zote mbili. Niendelee kutoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, mdogo wangu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kuchambua na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, Wizara imepokea na kuchambua michango kutoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, lakini pia tumechambua michango ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia 57 na Mheshimiwa Mbunge mmoja amechangia kwa maandishi, jumla michango 58 tumeipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujielekeza kqwenye baadhi ya hoja, chambilecho wahenga, “mcheza kwao hutuzwa”. Napenda kusema hapa nakuunga mkono Watanzania wenzangu kuipongeza Timu ya Yanga, lakini vile vile nimpongeze sana Rais wa Yanga, Engineer Hersi Said kwa kuendelea kuitangaza vyema nchi yetu nje ya mipaka ya Tanzania na dunia kwa ujumla kwa kushika nafasi ya pili kwenye Fainali za Kombe la Shirikisho Barani Afrika sambamba na kutoa Mfungaji Bora na Golikipa Bora wa mashindano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua hii imeiwezesha brand ya Tanzania kuzidi kujulikana katika mataifa mbalimbali na hivyo kuchochea hamasa za watalii na kutoa mataifa mbalimbali kwenye vivutio vyetu Tanzania. Kwa ushindi huo Wizara yangu inatoa offer, inatoa offer kwa wachezaji na viongozi wa klabu ya Young African baada ya kazi hiyo ngumu tutaratibu pamoja na viongozi wao kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu tutaufanya watakapokuwa mapumziko. Sambamba na hilo, naomba nichukue fursa hii kuwakaribisha mashabiki wote wa Yanga kwenda kujumuika pamoja na wachezaji wao katika safari hiyo katika tarehe itakayotangazwa na utaratibu utakaowekwa ziara hiyo tunaomba ipendekezwe iitwe kwa jina la The CAf Finalist Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi na shukrani maalum ziende kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kujitoa kwake tumeeleza humu jinsi filamu ya Tanzania the Royal Tour ilivyoleta mafanikio lukuki hapa nchini, lakini siyo tu kwa watalii kuongezeka lakini pia nchi yetu sasa ni kivutio cha mastaa mbalimbali na watu mashuhuri duniani wamekuwa wakija hapa nchini na wanaendelea kujakutokana na juhudi hizi za Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wageni wetu hawa wanapenda faragha yao na tunazingatia hilo mara zote lakini wapo ambao wameridhia jamii yetu iweze kutambua Tanzania kutuunga mkono kwa kupitia filamu ya Royal Tour, hivi ninavyozungumza leo hii naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba hivi juzi tumepokea wageni kutoka nchini Marekani; mtoto wa aliyekuwa Rais wa Marekani, mtoto wake na familia yake wapo hapa nchini Tanzania, bwana Donald Trump Junior yupo hapa nchini Tanzania amekuja kuunga mkono jitihada za Serikali na atakuwepo nchini kwa mapumziko ya siku kadhaa na nitamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aridhie ili kesho niweze kukutana naye kuzungumza ni namna gani wanaweza kutuendeleza katika biashara hii ya utalii hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya hoja za Kamati na Wabunge; Kamati yako lakini na Wabunge wengi zaidi ya 14 wakiwemo Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Tecla Mohamedi Ungele, Jacqueline Ngonyani Msongozi, Jeremiah Mrimi Amsabi, Simon Songe, Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Deus Clement Sangu.

SPIKA: Samahani Mheshimiwa Waziri, hawa ni akina nani?

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, hawa ni Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwenye baadhi ya maeneo.

SPIKA: Kanuni zetu haziruhusu. Ahsante sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, tunao Wabunge wengi waliochangia kwenye baadhi ya hoja na wamechangia kwa hisia sana. Nichukue fursa hii kwanza kabisa kusema mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zetu, TANAPA, TAWA, Ngorongoro, pamoja na TFS zinaongozwa na Jeshi la Uhifadhi, Jeshi Usu. Jeshi hili la Uhifadhi ni Jeshi ambalo limepewa mafunzo ya kutosha, Jeshi hili la Uhifadhi ukiangalia utaratibu wa kijeshi na Waziri wa Ulinzi angekuwepo hapa angenisaidia, ni jeshi la pili baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kama sijakosea.

Mheshimiwa Spika, Jeshi hili lina mafunzo ya kutosha, kwanza niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao pengine wanaweza kujaribu ku-undermine uwezo wa jeshi hili basi watambue kwamba jeshi hili ni jeshi ambalo lina mafunzo ya kutosha na kwa kuwa jeshi hili lina mafunzo ya kutosha, kero za Wabunge hapa kila aliyekuwa anasimama anazungumzia kuhusu ndovu.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi kwamba kila panapotokea wafugaji wameingia ndani ya Hifadhi, wenzetu wa Jeshi la Uhifadhi wanachukua hatua za haraka sana na kila ambapo pengine wananchi wananingia kwenye Hifadhi, Jeshi la Uhifadhi linachukua hatua za haraka sana, lakini kelele zote za Waheshimiwa Wabunge hapa ndani ya Bunge kuhusu wanyama hawa wakali kuingia kwenye maeneo ya wananchi, lazima tukiri kwamba hatua za haraka zinachelewa kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa na kwa bahati nzuri sana Jeshi la Uhifadhi chini ya TANAPA, TAWA, Ngorongoro linaongozwa na Majenerali wa Jeshi ambao walifanya kazi kubwa sana kwenye Taifa hili, kazi nzito sana kwenye Taifa hili, tunatambua tuna kazi kubwa ya kufanya kuendelea kuliimarisha jeshi hili, lakini naomba nitoe maelekezo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, nimekwishakaa na Viongozi wa maeneo haya wa Ngorongoro TAWA, TANAPA na TFS lakini pia nimeshawakutanisha na viongozi mbalimbali wa Chama Tawala wanaotoka kwenye maeneo ya wananchi, tumekwishakubaliana kwamba Kiongozi yoyote wa Uhifadhi katika eneo lake iwapo Waheshimiwa Wabunge wataendelea kupiga kelele kwenye maeneo hayo na kiongozi huyo akaendelea kubaki ofisini, maana yake ni kwamba yule Kiongozi wa Taasisi ile mimi nitashughulika naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwishakubalina, kila mmoja wetu afanye kazi zake, kama tunaweza kuchukua hatua za haraka dhidi ya wafugaji wanaoingia ndani ya Hifadhi vilevile tuchukue hatua za haraka kuwaondoa wanyama wakali katika maeneo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo zone zetu za kila Hifadhi na tumekwisha kufanya kikao. Nikuthibitishie mimi ni tofauti kidogo na ninaposema namaanisha, kiongozi yoyote wa Uhifadhi ambaye yupo kwenye eneo lake na kunakuwepo na kelele za wananchi yeye kushindwa kushuka kwa wananchi kukaa na kuzungumza nao, maana yake huyo hanifai katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nichukue fursa hii kwanza kutoa pole kwa wananchi wote ambao wamepata madhara mbalimbali katika maeneo yote na ndio maana ningetamani sana hata kuwataja Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wamezungumza kwa uchungu sana, kila Mheshimiwa Mbunge kwa namna alivyozungumza na hatuna sababu ya kuwa na changamoto hizi hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tunavyo vitengo vyetu mbalimbali tunatambua panapokuwepo na changamoto mara nyingi Wizara ya Maliasili na Utalii ndio inayoguswa lakini tunajipanga vizuri na wenzetu wa TAMISEMI kwa sababu katika kila Wilaya nchi hii tunao Maafisa Wanyamapori, lakini swali la kujiuliza ni kwamba hawa Maafisa Wanyamapori kila wilaya wanafanya kazi gani? Kwa sababu hata tukiwauliza Waheshimiwa Wabunge hapa pengine hata hawawajui Maafisa Wanyamapori kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo misingi ambayo Baba wa Taifa aliianzisha. Katika nyakati za Uhuru tulikuwa na Afisa Wanyamapori kila Kata na kwenye vijiji, lakini hapo katikati mambo kidogo yakabadilika na leo hii hatuna Maafisa Wanyamapori kwenye vijiji na kwenye Kata na kwenye Tarafa, lakini hili tumekwishalizungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwishatuagiza ili tuandae mpango mkakati ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kupata Maafisa Wanyamapori katika meneo yetu hayo ya vijiji na maeneo ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosisitiza hapa, tutamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na wenzetu tutakaa ili tuweze kuzungumza, kuona uwezekano hawa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya warudishwe kwenye Wizara hii ili niweze kuwashughulikia vizuri katika maeneo yao. Tunatambua yako maeneo Maafisa Wanyamapori wanafanya kazi nzuri sana, kwa mfano kule Tunduru aliyekuwepo Afisa Wanyamapori akifanya kazi nzuri sana lakini baadaye wakamhamisha, Mbunge wa Tunduru analalamika, sababu za kumhamisha mambo tu ya hovyohovyo ambayo hayaeleweki. Tumemwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naye ameridhia kuhakikisha kwamba Afisa yule aliyehamishwa kutoka Tunduru, arudi Tunduru akafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba changamoto hii imeleta vilio kwa wananchi katika baadhi ya maeneo na hata leo tunapozungumza kule Bariadi kuna mwananchi amekanyagwa na tembo muda tunapozungumza kule Bariadi. Kwa hiyo tunatoa pole kwa wananchi, lakini pia tunatambua kwamba changamoto hii ya wanyama wakali inaleta changamoto pia hata mpaka kwetu. Hivi karibuni wiki mbili zilizopita askari wetu kule Ngorongoro amechomwa na ndovu na kufariki. Kwa hiyo ni changamoto ambayo ipo pande zote mbili, lakini tumeandaa mpango mkakati wa kuona ni namna gani tunakwenda kumaliza changamoto hizi, mpango wa miaka kumi (2020 mpaka 2024).

Mheshimiwa Spika, mpango huu mkakati umeainisha hatua za muda mfupi na hatua za muda mrefu ambazo tutakwenda kupambana ili kuweza kuhakikisha kwamba changamoto hizi tumezimaliza. Aidha nichukue fursa hii kama ambavyo nimesema kuwaomba wenzangu wakati huu utakuwa mgumu kidogo katika Wizara hii, tunataka kila mmoja wetu afanye kazi kwa uweledi. Kila mmoja wetu afanye kazi kwa uweledi huku tukitanguliza ubinadamu mbele, nadhani hii lugha imeeleweka vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe Maafisa wetu katika maeneo mbalimbali tufanye kazi kwa uweledi tufanye kazi usiku na mchana na kauli yangu hapa ni kwamba hawa ni Askari Jeshi, maana yake tunataka kuona wakifanya kazi usiku na mchana, wakifanya kazi wakati wa jua, wakifanya kazi wakati wa mvua kuhakikisha kwamba wamekwenda kumaliza tatizo na migogoro mbalimbali ya wanyama wakali kuingia katika maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, lipo eneo lingine lenye migogoro, kati ya maeneo ya Hifadhi. Suala hili pia limegusiwa na Kamati ya Bunge lako Tukufu pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumza jambo hili. Wewe mwenyewe ni shahidi kwamba Baraza la Mawaziri liliwateua Waheshimiwa Mawaziri Nane kwenda kuzunguka na kupita katika maeneo mbalimbali. Nakiri kabisa kwamba Waheshimiwa Wabunge hapa wamezungumza, yako maeneo ambapo pengine tunapaswa kuendelea kupita zaidi ili tuzungumze na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu, Baraza la Mawaziri ni kikao cha juu kabisa cha Serikali cha maamuzi. Sasa wapo Waheshimiwa Wabunge hapa wamelalamika kwamba yapo maeneo ambapo hakuna migogoro, wananchi wameridhia yale maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amekwishasema hapa, sasa kama maamuzi yamefanywa na Baraza la Mawaziri na kuna watendaji katika Serikali kule chini ambao walipaswa kutoa matamko na mpaka leo hii hawajatoa matamko, maana yake wanakinzana na maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Rais. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ni Mheshimiwa Rais mwenyewe, maamuzi haya yamekwishafanywa, yako maeneo ambapo hakuna migogoro, ni jukumu la wale watendaji waliokasimiwa mamlaka na Mheshimiwa Rais, kutoa matamko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tumetoa mpaka tarehe 28 Mwezi wa Sita ili Waheshimiwa wanaohusika kwenye maeneo yao, yale yasiokuwa na migogoro kutoa matamko mara moja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amekwishalizungumza hili. Yako maeneo ambapo Baraza la Mawaziri limerejesha maeneo kwa wananchi. Kwa hiyo, sababu hii tunawataka wale wanaohusika watoe maelekezo ili yale matamko yaende yakawasaidie wananchi kwa sababu Mheshimiwa Rais ameridhia kwenda kuwagawia maeneo yale wananchi. Kwa hiyo, niwaombe waliokasimiwa mamlaka maeneo hayo kuhakikisha kwamba wamelitekeleza eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni tuhuma za askari wa uhifadhi kutumia nguvu na ubabe na mabavu. Baadhi ya Wabunge walizungumza hili, wamechangia katika eneo hili, naomba nisiwataje kwa misingi ya kanuni, wameeleza malalamiko kuhusu eneo hili na niwathibitishie tumekubaliana kufanya kazi kwa uweledi.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri ngoja nikuweke huru, ukiorodhesha ndio kanuni inakatakaza, kama unamjibu Mbunge na hoja yake mahususi huyo uliyemchagua inaruhusiwa, yaani vile ulivyokuwa unaorodhesha Wabunge waliochangia ndio kanuni inakataza. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Wabunge wamezungumza hivi kwamba kuna matumizi ya mabavu lakini nichukue fursa hii kama ambavyo nimesema, ndani ya hifadhi zetu kuna mengi. Tunao pia wafugaji ambao wanaingia ndani ya hifadhi na silaha za moto, lakini pia tunao watu wanaoingia na silaha za moto ndani ya hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mambo mengine uridhie tu nisiyazungumze hapa, lakini nimepokea hoja hii ambayo imezungumzwa na Mheshimiwa Kasheku Musukuma pamoja na Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, akituomba twende kufanya mapitio ya Sheria ya Uanzishwaji la Jeshi la Uhifadhi na nimtaarifu kwamba Wizara yetu inaendelea kufanya reform kubwa sana. Tunaendelea kufanya mapinduzi makubwa sana kwenye sekta zetu zote na nimtaarifu tu kwamba hakuna mlango utakaobaki bila kufunguliwa katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwishaanza kufanya mapitio ya sheria mbalimbali, tumekwishaanza kufanya mapitio ya kanuni mbalimbali, zipo kanuni ambazo zinaingiliana, zipo kanuni ambazo zinakinzana, lakini zipo kanuni ambazo hazitoi tafsiri sahihi iliyotolewa na sheria. Kwa hiyo, niwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tutakwenda kulipitia na niko tayari baada ya Bunge hili nitakaa na Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi pamoja na Mheshimiwa Ally Juma Makoa pamoja na Mheshimiwa Festo Richard Sanga na Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah ili niweze kupata ushahidi wa yale mambo ambayo wameyazungumza kuhusu askari ambao wanafanya vitendo kinyume na utaratibu wa Jeshi la Uhifadhi na iwapo nitapokea ushahidi huo tutachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutachukua hatua pale ambapo tunaona kabisa kuna vitendo vya hovyo vya uonevu, tutachukua hatua dhidi ya askari wote ambao wanafanya vitendo hivyo. Pia nilitaarifu tu Bunge lako Tukufu kwamba tunaendelea na vikao na pengine tarehe 11, 12 tutafanya vikao na Wenyeviti wa Bodi TANAPA, Ngorongoro, TAWA pamoja na TFS; ili tuweze kujadiliana kwa pamoja kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa jeshi hili la uhifadhi. Ili tuweze kujiridhisha katika maeneo yenye mapungufu na tuweze kuyarekebisha katika maeneo hayo. Niwaahidi tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tutakapokutana hapa mwakani haya mapungufu yote itakuwa ni makofi tu na furaha kwa kweli. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango mingi katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mifugo kutaifishwa na kutozwa faini. Kwa hotuba yangu kuu nilinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akitoa hotuba ya Arusha Manifesto ambapo alisisitiza kwamba uhifadhi ni lazima tuamue. Sisi kama Taifa ni lazima tuamue na lazima tuseme ukweli kwamba kuna haja ya kulinda hifadhi zetu. Mheshimiwa Baba wa Taifa alisema kwamba, Taifa lolote bila uhifadhi si Taifa na akayaomba Mataifa mbalimbali kuhakikisha kwamba tunashirikiana nao katika uhifadhi. Hivyo, naomba nisisitize kwamba tuna kila sababu ya kulinda hifadhi zetu kwa ajili ya vizazi vya leo na vizazi vya kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutambue tu kwamba hifadhi zetu zinachangia katika pato la kigeni zaidi ya asilimia 25 pamoja na kwamba kiasi hiki ni kidogo sana lakini lazima tukiri kwamba kwenye mchango katika Pato la Taifa ni karibu asilimia 21 na kwenye fedha za kigeni ni asilimia 25 naomba nirekebishe hilo kidogo. Kwa hiyo, tuna kila sababu ni kwa nini tuzilinde hifadhi hizi na niwaombe Waheshimiwa Wabunge pale ambapo tunajadili kuhusu uhifadhi basi kila mmoja wetu arejee kwenye kauli ya Baba wa Taifa aliyoitoa wakati ule wa Arusha akitoa hotuba yake kwenye Arusha Manifesto.

Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize hapa tena, kama Taifa ni lazima tukubali kwamba tunazo sheria, tunazo kanuni na sheria hizi kwa mfano sheria kuhusu TANAPA zimetoa miongozo za kutaifisha mifugo baada ya maamuzi ya Mahakama na kama kuna ushahidi wowote kwamba kuna afisa yeyote anataifisha mifugo bila uamuzi wa Mahakama, basi nipewe taarifa hizo ili tuweze kuzifanyia kazi mara moja.

Mheshimiwa Spika, utaratibu uliopo ni kwamba Mahakama ndio hutoa maamuzi wakati wa utaifishaji wa mifugo kwa mujibu wa sheria hizi. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kama wana vielelezo vya ziada, basi waweze kunipatia ili tuweze kuona ni namna gani tutaweza kuchukua hatua katika maeneo ambapo watendaji wetu wamekuwa wakitenda mambo ambayo ni ya utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na sheria nyingine suala hili pia limechangiwa na Kamati pamoja na Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso. Nitoe tu taarifa kuwa marekebisho ya utungaji wa sheria mpya hizi za kuzipa mamlaka zaidi taasisi hizi, zimefika hatua nzuri. Tunaendelea kuwaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kuwa na subira kwa sababu tunaendelea kufanya mapitio na hivi karibuni tutawashirikisha wadau ili tuweze kukamilisha urekebishwaji wa sheria hizi ili kuweza kutoa mamlaka lakini pia sheria ambazo zitaenda kusaidia katika uhifadhi wa eneo letu la Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kukamilishwa kwa zoezi la Ngorongoro; nichukue fursa hii kuishukuru sana Kamati, lakini pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwenye eneo hili. Jukumu la Serikali kwa misingi ya Ibara ya nane ni ustawi wa wananchi lakini kama inavyofahamika kwamba Serikali inafanya kazi pia kwa kupita utekelezaji wa Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ibara ya 67 imezungumzia kwa kina sana kuhusu uhifadhi, lakini namna ambavyo tuna kazi kubwa ya kuustawisha ustawi wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba, suala la Ngorongoro limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge lakini nataka niwaahidi hapa kwamba wakati natoa hoja hapa Bungeni siku ya Ijumaa nilizungumza hili kwa kina kabisa na sisi kama Serikali hatutarudi nyuma, tunatambua kwamba tunao baadhi yetu wakishirikiana na vijana wengine wa Mataifa ya nje. Tena vijana hawa wa Mataifa ya nje ndio wamekuwa wengi sana. Wakienda huko wakizunguka zunguka kwenye baadhi ya maeneo mbalimbali, Mahakama za nje ya Nchi, Mahakama za Ulaya na maeneo mengine wakijaribu kututekenya. Nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu hatutarudi nyuma kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawashukuru sana Watanzania wa Ngorongoro ambao wameridhia wenyewe kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro na kwenda kwenye maeneo mengine. Sisi kama Wizara tutaendelea kupitia maelekezo ambayo Kamati imetoa. Tutaendelea kutekeleza maelekezo ambayo Waheshimiwa Wabunge wametushauri kwenye Bunge hili Tukufu ili tuhakikishe kwamba utekelezaji wa jambo hili unatekelezwa, lakini tunatambua kwamba tunaendelea kufanya mashauriano na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuhakikisha kwamba jambo hili tumelitekeleza kama ambavyo tumeahidi mbele ya Bunge Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni mikakati ya kutangaza utalii. Kamati ya Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza sana kwa kina jambo hili, lakini pia katika hotuba yangu ya awali niliweka hadharani mikakati 10 ya kutangaza utalii ikiwa ni pamoja na ubunifu na teknolojia, ambavyo vitaongoza katika mchakato huu wa kutangaza utalii.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumza sana kuhusu hifadhi, lakini hatujazungumzia sana kuhusu utalii. Nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe kwa kulianza jambo hili. Niwashukuru Watanzania, niwashukuru pia wadau mbalimbali wa utalii ambao kwa kipindi kirefu sana wamefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana ya kutangaza utalii nje ya mipaka ya Tanzania lakini sisi kama Serikali sasa tumekwishalianza jambo hili. Nichukue fursa hii kuwaomba wawakilishi, Mabalozi wetu waliopo katika maeneo mbalimbali kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, tunazipongeza Balozi mbalimbali ambazo zinafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. Balozi wetu kila Nchini, Balozi wetu Nchini Afrika ya Kusini na maeneo mengine wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa, kama jambo hili likishikwa na kila Mtanzania, kila mwananchi wa Tanzania akitoka akazungumza mazuri kuhusu utalii, kuzungumza mazuri kuhusu Nchi yetu, Baba wa Taifa ameturithisha mambo makubwa, mambo mazuri amani na utulivu, lakini Taifa letu lipo katika eneo jiografia ambayo hakuna popote Afrika. Tunaamini kabisa Mwenyezi Mungu ametupa akili, ametupa na uwezo wakati ni sasa, kila Mtanzania kutoka kuzungumzia mazuri kuhusu Taifa letu. Sisi kama Wizara pia tayari tumekwishaanza mazungumzo na wenzetu ta Tripadvisor tipo advisor wenzetu wa Expedia lakini pia tunaendelea na mazungumzo na wadau mbalimbali ambao wao wana mchango mkubwa sana katika Sekta hii ya Utalii. Pia tunaendelea kuwakaribisha wadau katika Sekta ya Utalii walioko kwenye Mataifa mbalimbali duniani ambao tayari wamekwishaanza kuja kutoka China na maeneo mengine duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nikuombe hotuba yangu hii iingie kwenye Hansard ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya vizazi vya leo na vizazi vya kesho.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ufafanuzi nilioutoa pamoja na maelezo mengi ambayo nimeyazungumza na kwa sababu ya muda, naomba sasa baadhi ya hoja nitaziwasilisha kwa ufafanuzi wa hoja nyingine kwa maandishi, lakini natambua hapa kwamba wapo Wabunge wakiwemo Wabunge wa Mbarali, Ngorongoro, Serengeti, Mheshimiwa Kakunda na wengine wote waliomba tufike kwenye maeneo yao na wengine ambao sijawataja kule Nachingwea kule kwa ndugu zangu Kusini na maeneo mengine, kote nitafika kwa ajili ya kupitia na kuzungumza na wananchi ili tuweze kufanya kazi hii ambayo tumekabidhiwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa ufafanuzi huo na majibu yote ya hoja niliyowasilisha na mengine nitakayowasilisha kwa maandishi, naomba yaingie kwenye Hansard ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya na uzima na kutuwezesha kukutana mbele ya Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ridhaa yake yeye mwenyewe kuona umuhimu wa utekelezaji wa maazimio yote haya mawili na haya ndio maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndio yanatoa muelekeo wa Serikali na kututaka sisi kama Serikali kuangalia maslahi ya Watanzania, hasa Watanzania wa kawaida kabisa. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe tu kwamba michakato hii hasa ya maazimio haya haikuanza chini ya utawala au uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, yalianza na viongozi waliomtangulia na sasa ni takribani zaidi ya miaka saba, tumehangaika tumekwenda na kurudi. Sisi kama Serikali tumejitahidi katika nyakati zote kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi hasa za wananchi wetu hawa wa kawaida, kuwapatia maeneo ambayo watakwenda kuyatumia kwa maslahi yao.

Mheshimiwa Spika, tatu, nikushukuru sana wewe na Kiti chako kwa kuendelea kutupatia miongozo mbalimbali, lazima nikiri mafanikio na leo sisi kama Serikali kuwepo hapa ni kwa sababu ya miongozo yako, jitihada zako, kuhakikisha kwamba unasimama vyema kusimamia yale yaliyoelekezwa katika Ibara ya 63 na Ibara ya 64 na mengine katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunakupongeza sana kwa sababu kuna wakati kulikuwa kuna giza kidogo lakini ukasema unataka kuona mwanga. Hayo yote uliyoyafanya kwa sababu ulizingatia maslahi ya wananchi ambao wao ndio wametuweka hapa Bungeni, tunakupongeza na tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba dhamira ya Serikali yoyote, Serikali yoyote halali, dhamira ya Serikali yoyote iliyo madarakani, Serikali yoyote makini, ni ustawi wa wananchi wake, ndio dhamira ya Serikali yoyote. Serikali imepewa mamlaka yake na wananchi kwa misingi ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali imepewa mamlaka na wananchi kwa sababu nchi hii ni ya wananchi na wananchi wameelekezwa moja kwa moja kwa misingi ya Katiba kushiriki katika maamuzi yanayofanywa na Serikali na wananchi wanashiriki katika maamuzi ya Serikali kwa misingi iliyoainishwa katika Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watanzania wanashiriki kwenye maamuzi ya moja kwa moja yanayoamuliwa na Serikali. Ibara ya 21 imetoa mwongozo wa namna gani wananchi watashiriki kwenye maamuzi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaipongeza Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, kwa sababu viongozi wa Mataifa mengine wangeweza kuamua wao wenyewe kama viongozi. Mheshimiwa Rais angeweza kuamua yeye mwenyewe, lakini akaona kwamba, Serikali ya Chama hiki ikaona kwamba ni muhimu wananchi wakashirikishwa moja kwa moja na ndio msingi ulioainishwa katika Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wanashiriki kwenye maamuzi katika mikataba, katika majadiliano, katika mambo kama haya ya kupandisha hadhi hifadhi na kuzishusha hadhi hifadhi. Ibara ya 21 imetoa maelekezo ni namna gani wananchi watashiriki kwenye maamuzi ya Serikali na namna ambavyo wananchi wanakwenda kushiriki kwenye maamuzi ya Serikali ni kupitia wawakilishi wa wananchi waliochaguliwa na wananchi wao na hao wawakilishi ndio hao tunaowazungumzia, Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wametoa maoni mengi sana katika maeneo yote haya mawili, eneo la Kigosi lakini pia eneo la Ruaha, nasi kama Serikali tumesikiliza maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Kwanza tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, katika maoni ya Waheshimiwa Wabunge, Wabunge takribani 10 wote wameunga mkono Maazimio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia taarifa ya Kamati imeunga mkono Maazimio lakini nikushukuru pale ambapo ulipoagiza Kamati hasa kwenye hoja moja ya eneo la Ruaha, ukatutaka tuende tukajiridhishe, tunakushukuru sana sana kwa sababu haukutoa mwongozo tu kwa Kamati lakini ulitoa mwongozo kwa sababu unalinda maslahi ya wananchi na hiki ndicho kilichotuleta hapa Bungeni, tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi na Kamati tulipata fursa ya kwenda kujionea kule Ruaha na yale ambayo hoja za Kamati kuhusu ni kwa nini Mwekezaji ameachwa na wananchi wameondolewa. Mimi nilipata fursa ya kujionea hali hii na Wajumbe wa Kamati, tulifanya vikao kadhaa na baadae tukaenda site kujionea hali halisi, niliporejea niliwaambia wenzangu kwamba sisi ni wawakilishi wa wananchi lakini pia kilichofanyika pamoja na jitihada kubwa na kazi nzuri ambayo imefanywa na Waheshimiwa Mawaziri Nane waliozunguka kuhakikisha kwamba wameyaangalia maeneo yale ambayo hayana hadhi wakapendekeza yaondolewe, ni lazima tuwapongeze kwa kazi kubwa na kazi nzuri sana ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakatoa takribani hekta 74,000 kwa wananchi kule eneo la Ruaha lakini baada ya kwenda kujionea eneo lile, mimi nilishawishika pia na niliporejea nikawaambia wenzangu hapa ni lazima tufanye jambo ili kulinda maslahi ya wananchi, kwa sababu hiki ndicho ambacho wananchi wametuweka hapa kwa sababu ya kulinda maslahi yao na kama ambavyo nimesema dhamira yetu sisi Serikali ni kulinda na kuendeleza ustawi wa wananchi wetu, kwa hiyo isingelikuwa na maana yoyote ya safari yetu kule Mbarali kama tusingeliweza kuliona hili na tukaona kwamba hili changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliporejea tulifanya kikao na nimshukuru Mwenyekiti wetu nae aliridhia kwa sababu mchakato huu unapita taratibu za kisheria, taratibu za kitathmini. Sisi kama Serikali baada ya kuwa tumefanya mapitio kwa viongozi wetu tukaona kwamba ipo haja ya kuwafikiria hawa wananchi katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa michakato hii ni michakato ya kisheria, kwa kuwa michakato hii ina taratibu zake za kufanya tathmini ili tuweze kujiridhisha ni eneo gani ambalo wananchi wataweza kulitumia kwa sababu kama mwekezaji amebakizwa kwenye eneo hilo hilo ambalo tunasema ni ardhi oevu wananchi walipoondolewa, basi ili kutenda haki, mwekezaji naye alipaswa kuondoka kwenye eneo lile, lakini kama Serikali tumeridhia tunasema kwamba mwekezaji ana miundombinu ya maji kwenye eneo hili, sisi kama Serikali ni lazima tujitathmini kwamba hapa kama tumemuacha mwekezaji, ni muhimu tukalinda maslahi ya wananchi pia katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili tuliliangalia na tukasema kwamba ipo haja ya kulifanyia tathmini hili na tunafanya commitment mbele ya Bunge lako Tukufu kwa sababu Kamati imetuagiza na inapoagiza Kamati maana yake imeagiza Bunge kwa misingi ya Kanuni. Sisi tunaliomba Bunge lako liridhie kupitisha Azimio hili lakini tunaomba tuliahidi Bunge kwamba tutarejea hapa mwezi Septemba ili kufanya marekebisho tuwaangalie wananchi wa eneo lile la Mbarali ambao wameondolewa, katika maono ambayo mimi nimejiridhisha kabisa kwamba kulikuwepo na haja ya kufanya tathmini ya kina ni kwa nini wananchi wameondolewa kwenye eneo lile. Kwa hiyo, tunaomba tuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tutarejea mwezi Septemba na kwa kuwa tumekwishampa taarifa Mheshimiwa Waziri Mkuu haja ya kufanya tathmini kuwaangalia wananchi katika eneo lile ambalo tutaleta mapendekezo iwapo Bunge litaridhia, basi eneo lile hatutalirejesha kwa wananchi kwa sababu tunajua tukilirejesha kwa wananchi watu wachache watanufaika na eneo hili. Kwa hiyo, tutalirejesha kwa Serikali pengine kupitia Mkoa au TAMISEMI au kupitia Wizara ya Kilimo ili liweke utaratibu wa kuandaa miundombinu ya maji na wananchi waweze kunufaika katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ina migogoro jumla karibu 836, na kama uliusikiliza maoni mengi ya Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, wapo wengi wamekuwa na imani na mimi. Mimi ni mtu wa field, naomba niwathibitishie katika kipimo ambacho nitaomba Wabunge wanipime ni kwenda kumaliza migogoro hii 836. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na Ndugu yangu Ole-Sendeka alikwenda nje kidogo ya hoja kuzungumza kule Jimboni kwake lakini nimpe taarifa kwamba nitafika huko Jimboni kwako. Mara nyingi huwa sipendi kuletewa taarifa mezani, ninapenda nifike kule field nijionee mimi mwenyewe ili pale tunapopeleka maoni au ushauri kwa Mheshimiwa Rais uwe ni ushauri ambao unakwenda kulinda maslahi ya wananchi hasa wanyonge kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo pamoja na migogoro hii 836 lakini tumeongezewa mgogoro mwingine jumla migogoro 837 wa kule Iringa kwa sababu ya simba ambao wameingia kwenye maeneo yetu tayari tumekwishapeleka helicopter, tumepeleka askari wetu zaidi ya 21 wapo kule wanaendelea kuwasaka wale simba, lakini migogoro hii mingine ninaomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge nitafika kila kona kuhakikisha kwamba tumetatua migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipopewa nafasi hizi tuliaminiwa na Mheshimiwa Rais lakini ukweli ni kwamba wapo Watanzania wana uwezo mkubwa huko nje pengine wangepewa nafasi hizi wangefanya vizuri zaidi. Kwa hiyo, tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba tunalinda na kutetea maslahi ya wananchi na hapa ndipo tunakiri kabisa kwamba kazi aliyofanya Rais wetu kurejesha maeneo haya kwa wananchi ni lazima tumpongeze na tumshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walijaribu wengi lakini Rais Dkt. Samia ameweza kurejesha maeneo haya kwa wananchi. Tulisimama hapa katika hotuba ya bajeti yetu tukaeleza Mheshimiwa Rais aliendeleza yale ambayo yalianzishwa na Rasi wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ya kwenda kufanya mapitio kwenye maeneo ya migogoro na wakati nahitimisha hotuba yangu ya bajeti tulisema, kufikia Tarehe 28 mwezi wa Sita, wale waliokasimiwa mamlaka ya kuhakikisha kwamba wanatatua migogoro kwenye maeneo yao wafanye hivyo, lakini pamoja na hilo tunatambua yako maeneo mengine bado kuna vuguvugu la migogoro. Nitafika huko ili nitakapokuja kwa wenzangu tutawashauri namna bora ya kwenda kumaliza migogoro tuliyonayo kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msingi wa hoja zetu zote mbili nimeona hapa kumekuwepo kidogo na hofu ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu kukabidhi eneo la Kigosi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Misitu chini ya TFS chini ya Sheria Namba 323. Wahifadhi wetu tulipowapa nafasi katika maeneo yao tuliwakabidhi majukumu katika misingi ya sheria ambayo nimeitaja hapa.

Mheshimiwa Spika, TFS itakwenda kuandaa mpango wa usimamizi wa misitu hasa Msitu wetu huu wa Kigosi ambao tumeuzungumza. Mpango huu utaandaliwa katika kutimiza matakwa ya Sheria ya Hifadhi ya Misitu sura Namba 323. Kwa hiyo, ninaomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, TFS hawa ni wahifadhi lakini hawa wote ni Askari Jeshi. Kwa hiyo, jukumu lao kubwa ni kulinda hifadhi ya misitu lakini pia ikumbukwe kwamba maeneo mengi yenye vyanzo vya maji wanaolinda ni hawa wahifadhi - TFS. Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu wale wote ambao walikuwa na hofu. Hili ni Jeshi kamili, wamepata mafunzo ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, katika eneo ambalo hatutakuwa na msamaha ni wale wahifadhi ambao tumewakabidhi mamlaka ya kwenda kufanya kazi na kusimamia kwenye maeneo yao na wao wakaenda kutuangusha kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, tutatoa kipindi cha maangalizo ili tumpime kila mmoja uwezo wake, kwa namna ambavyo anakwenda kutekeleza maelekezo ambayo ninyi Bunge mtatushauri katika Kikao hiki. Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba TFS ni Jeshi kama lilivyo Jeshi la TAWA, TFS ni Jeshi kama lilivyo Jeshi la TANAPA, wanapata mafunzo sehemu moja kwa hiyo hawa ni wanajeshi na kwa marekebisho ya sheria na kimuundo ambao tumekuwa tukiendelea kuyafanya tumeendelea kuwapandisha hadhi kuwa ni Jeshi USU. Kwa hiyo niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ushirikishwaji wa wananchi tumelipokea hili, na sisi tunakiri kabisa moja ya changamoto kubwa ambayo tumeikuta kwenye Wizara hii, maamuzi mengi yalikuwa yakifanyika bila kuwashirikisha wananchi. Hili tunalikubali kabisa, nilikwishatoa maelekezo kwa Wakuu wa Hifadhi katika maeneo yote kuhakikisha kwamba wanashuka kuzungumza na wananchi na kazi hii tumekwishaianza kwa TANAPA, TAWA na TFS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi tunapozungumza wanapita na kuzunguka katika kila Mkoa na wanavyopita katika kila Mkoa, wanakwenda kuzungumza na Viongozi wa Serikali katika kila Mkoa, Viongozi wa Chama Tawala katika kila Mkoa ili waweze kubeba maono ya wananchi kwenye maeneo yao. Tunaamini kabisa ushirikishwaji wa wananchi utatusaidia sisi kama Wizara kwenda kutatua migogoro hii ambayo nimeitaja zaidi ya 800 inayotukabili leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa hapa ni kuhusu uwekaji wa alama za mipaka. Kama ambavyo nimesema na kama ambavyo tayari tumekwisha waagiza wataalam wetu wahakikishe kwamba uwekaji wa alama za mipaka unakuwa shirikishi. Nimesema hapo awali, migogoro mingi imetengenezwa kwa sababu wananchi wengi wamekuwa hawashirikishwi kwenye maamuzi. Kwa hiyo, kwa kuwa tayari tumekwishatoa maelekezo na kwa kuwa tayari wataalam wetu wanaendelea kuhakikisha kwamba wanakwenda kuwashirikisha wananchi katika utatuzi wa migogoro kwenye maeneo mbalimbali, uwekaji wa alama za mipaka ni lazima wawashirikishe wananchi na haya tayari tumekwisha waagiza wataalam wetu, katika maeneo mengi tayari hili linaendelea kutekelezwa na niseme tu kwamba nimepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge wale ambao walikuwa na hofu na hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitahakikisha katika maeneo ambapo tunaendelea kufanya tathmini ya ardhi, katika maeneo ambapo tunaendelea kufanya tathmini ya hifadhi zetu tutaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wameshirikishwa moja kwa moja. Tunapozungumza kuhusu wananchi siyo tu viongozi wawakilishi, Wabunge na Madiwani, lakini pia mpaka chini kwenye vitongoji, kwenye vijiji na wananchi wenyewe washirikishwe kwenye vikao mbalimbali ili tunapofanya maamuzi yawe ni maamuzi ambayo hayataleta hitilafu na kuturejesha hapa katika mijadala ambayo tungeliweza kuitatua mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu utolewaji wa elimu. Tutaendelea kutoa elimu hasa katika maeneo ambayo tumeyarejesha kwa wananchi na kama ambavyo mwenzangu amezungumza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane amekwishalisema hilo kwamba tutaendelea kutoa elimu ili yale maeneo ambayo yamerejeshwa kwa wananchi yaweze kutumika katika minajili iliyokusudiwa na Serikali. Kwa hiyo, hili tutaendelea nalo na nikuthibitishie tu kwamba mimi na taasisi zangu zote tunaendelea kutoa elimu na kupitia TAWA, TANAPA, TFS tunaendelea kutoa elimu, hivi sasa wanaendelea kuzunguka kama ambavyo nimesema awali na tutaendelea kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji ili kuendelea kuhakikisha kwamba wanatatua baadhi ya changamoto za wanyama wakali kwenye baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili kwa kuwa Bunge hili tayari limekwishatupitishia bajeti, tutakwenda kuanza kulitekeleza baada ya kuahirishwa kwa Bunge letu hili Tukufu, lakini nikuthibitishie tu kwamba yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wametuletea hapa tutakwenda kuyafanyia kazi. Naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba maeneo mengi ambayo wameshauri, pamoja na kwamba wameunga mkono kwa asilimia 100 hoja zote zilizotolewa yale mengine machache ambayo tunaamini kabisa tuna haja ya kwenda kuyafanyia kazi ili kulinda maslahi ya wananchi wetu tutakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kimsingi hoja ambazo zimekwishazungumzwa tayari nimekwishazitolea ufafanuzi wa kina kabisa ili tuweze kuhakikisha kwamba Azimio hili linakuwa na msingi lakini Maazimio haya yanakuwa ni ya kulinda maslahi ya wananchi wetu tunaowawakilisha kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ya mwisho ambayo imezungumzwa hapa ni kuhusu mazoezi haya ambayo tumeyafanya hasa kwenye Hifadhi yetu ya Kigosi lakini Hifadhi yetu ya Ruaha yaweze kupita kwenye maeneo mengine. Zoezi hili halitaishia katika maeneo haya ya Ruaha na Kigosi, tutaendelea nayo. Hakuna sifa yoyote ya kuendelea kupata hasara kwenye maeneo wakati tunaweza kufanya jambo ambalo likasaidia Taifa letu. Kwa hiyo, tutaendelea kuyapitia kwenye baadhi ya maeneo kuhakikisha kwamba maeneo yetu yote yanakuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi ambayo yameshauriwa na Waheshimiwa Wabunge yamekuwa na tija na sisi tunasema tu kwamba kama Serikali tutakwenda kuyafanyia kazi. Nikiri tu kwamba kwa wale Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumza kuhusu eneo letu lile la Kigosi hasa kuhusu eneo la uzalishaji wa asali, nikuthibitishie kwamba sisi tumejipanga vyema kuhakikisha kwamba eneo hili tunaliandaa kwa ajili ya wafugaji wa asali na shughuli nyingine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe tu kwamba leo hii Serikali inaingiza karibu takribani dola milioni 14 peke yake katika sekta hii na hicho ni kiwango cha asilimia tano tu cha asali ambayo inauzwa nje ya nchi, lakini kwa zoezi hili ambalo tumelifanya hapa hasa la eneo la Kigosi itatusaidia kama Serikali kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji wa asali kutoka tani 38,000 mpaka tani 132,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwango hiki kitaisaidia Serikali kukusanya zaidi ya dola milioni 50. Kiwango hiki kitasaidia Serikali kukusanya takribani dola milioni 50 kwa asali ambayo itauzwa nje ya nchi. Nilitaarifu tu Bunge lako Tukufu kwa eneo ambalo tutalirejesha ukanda huu ndiyo ukanda ambao kwa Afrika unaongoza kuwa na asali nzuri. Tuseme kwa Afrika ni namba mbili, ukanda huu ambao tunarejesha eneo la Kigosi, kwa hiyo, tutaongeza jitihada.

Mheshimiwa Spika, na hivi karibuni tutazindua mpango tunaouita, “Ondoa shoka kamata mzinga.” Mpango huu utakwenda kuzihusisha Wilaya zote, mpango huu utakwenda kuhusisha Mikoa yote inayoguswa na Azimio hili hasa Azimio la Kigosi ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanashiriki moja kwa moja kwenye shughuli hii ili tuweze kuongeza mapato. Hatuna sababu hata kidogo ya kuwaambia Watanzania ni kwa nini leo hii mchango wetu kwenye Sekta ya Wizara ya Utalii ni asilimia 25 hasa kwenye fedha za kigeni, hatuna sababu ya kushindwa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuongeza jitihada na mpango wa Ondoa shoka kamata mzinga utakwenda kuongeza fedha za Serikali, fedha za kigeni lakini pia utatoa mchango kwenye Pato la Taifa ili tuweze kutoka kwenye asilimia 22 na sisi dhamira yetu tutoke asilimia 22 tuende mpaka asilimia 30 kama mchango kwenye Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, licha ya uamuzi wa Serikali wa kumega eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 478 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwenda kwa wananchi, Serikali itaendelea kufanyiakazi ushauri uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wa kufanya tathmini ya eneo lingine linalopakana na Shamba la Kapunga kwa upande wa Kusini Mashariki ili kujiridhisha kama eneo hilo bado lina hadhi.

Mheshimiwa Spika, nami nimesema inawezekana kwamba ni vema tukaangalia maslahi ya wananchi katika eneo hili, na nilithibitishie tu Bunge lako Tukufu kwamba tayari wataalam wamekwishaanza, wako uwandani na tayari wamekwishaanza kufanya tathmini ya kiwango gani tutarejesha kwa wananchi na baada ya hapo tutarejea kwa wenzetu chini ya Mwenyekiti wetu ili kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu na kushauri mamlaka waridhie kiwango ambacho tutaona kwamba ni muhimu kukitoa kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ninaomba sasa kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri ngoja, ili tuongozane vizuri umehitimisha hoja zote mbili kwa wakati mmoja. Sasa ili Bunge liweze kufanya maamuzi kwa maana ya wewe kutoa hoja, toa hoja moja moja. Kuhitimisha umehitimisha pamoja nilikuacha tu uendelee ili umalize hoja zako zote. Toa hoja moja moja unatoa moja unaenda zako kukaa Bunge linaulizwa lifanye maamuzi halafu utaleta hoja nyingine. Kwa hiyo, unaweza kuanza na mojawapo kati ya hizi mbili, yoyote tu ambayo iko karibu hapo.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja ili Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liridhie katika Mkutano huu wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha Nne cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa, Sura ya 282 inayoazimia kuridhia kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,760 kama ilivyoainishwa kwenye kiambatanisho ili iwe Hifadhi ya Misitu ya Kigosi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.


WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia manufaa ambayo Serikali imekwishazungumza kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na wananchi wa maeneo husika watayapata kutokana na marekebisho yaliyopendekezwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa Sura 282, inaazimia kuridhia marekebisho ya mipaka ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kumega kilomita za mraba 478 kutoka kwenye hifadhi hiyo na baadaye marekebisho hayo kufanyika. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha itakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 19,822 kama ilivyoainishwa kwenye kiambatanisho.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushukuru, kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini nimshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Lazima tukiri kwamba wakati fulani Taifa letu linahitaji kufanya maamuzi magumu sana ili tuweze kupiga hatua za maendeleo na sisi kizazi cha leo tunatambua waasisi wetu waliotangulia wa Taifa hili kuanzia kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuja kwa Rais wetu wa Awamu ya Sita yamefanyika maamuzi mengi magumu ambayo yamelifanya Taifa hili kuwa Taifa imara, yamelifanya Taifa hili kuwa Taifa lenye amani na utulivu na mambo mengi kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuchukua hatua muhimu kabisa za uchumi katika Taifa letu. Tunampongeza sana Rais wetu kwa kuendelea kuchukua maamuzi magumu ya kiuchumi na Baba wa Taifa aliwahi kusisitiza miaka ya 1961 wakati wa Arusha Manifesto. Sisi katika Sekta ya Utalii Baba wa Taifa aliyaondoa na kuyapandisha hadhi baadhi ya maeneo ili tuweze kuhifadhi na alisema kwamba tutafanya kila tuwezalo ili tuweze kuhifadhi, kwa sababu uhifadhi si tu kwa ajili ya kustaajabishwa na wale wanyama lakini bali tunahifadhi ili iwe mustakabali wa kizazi cha leo na kizazi cha kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema Hotuba ya Waziri wa Fedha, kwanza nimpongeze sana na sisi tunampongeza na kumtia moyo aendelee kufanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika eneo hili la fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu Dkt. Samia kwa mara ya kwanza kabisa alifanya maamuzi magumu ya kutoka ofisini na kwenda kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour na watu wengi walibeza. Watanzania wengi walizungumza maneno mengi sana kuhusu ni kwa nini Mheshimiwa Rais leo hii ametoka ofisini na kwenda kuitangaza Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha amezungumza kwa kina mapato yaliyopatikana kutokana na utalii ambayo yametokana na kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi tunasema tutaendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na wakati mwingine Taifa letu kama ambavyo nimesema tunahitaji kufanya maamuzi magumu na maamuzi haya aliyoyafanya, anayoendelea kuyafanya katika uchumi, katika sekta yetu ya utalii ni maamuzi ambayo yatalifanya Taifa hili kupiga hatua sana kwenye sekta hii ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi katika hoja walizozizungumza hapa kwa mara ya kwanza kabisa tumewaona Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana kuhusiana na utalii. Katika miaka mingi sana tumekuwa tukizungumza kuhusu hifadhi. Msingi wa uhifadhi ulianzia nyakati za Baba Taifa, utalii haukuzungumzwa kwa muda mrefu sana kwenye Bunge hili katika miaka mingi sana, lakini tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana kuhusu utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba maeneo mengi ambayo wametushauri, tutakwenda kuyafanyia kazi. Hoja nyingi ambazo zilikuwa zinakwama kwa sababu ya urasimu kwenye Sekta ya Utalii tutakwenda kuzikwamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukiri na kumshukuru Mheshimiwa Rais. Tulipoteuliwa kwenye nafasi hii mimi na Mtendaji Mkuu katika Wizara hii, tumeingia katika nyakati ambazo tumekuta kuna changamoto nyingi sana katika sekta ya uhifadhi. Tumekuta kuna changamoto nyingi za wanyama wakali, kuna changamoto nyingi za wanyama waharibifu na lazima nisimame hapa kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, toka tulipoanza kujadili Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, tukaja kujadili Bajeti hii Kuu kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa, alisema moja kwa moja. Katika misingi ya Ibara ya 21, wananchi wengi wanawakilishwa leo hii Bungeni na Wabunge waliochaguliwa na wananchi. Sauti za wananchi zimezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yao yote tukianzia kule kusini mpaka magharibi na maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitambue mchango wa Mheshimiwa Kuchauka, Mheshimiwa Kitandula ambaye pia amezungumza kwa uchungu sana kuhusiana na matatizo ya uhifadhi, matatizo ya ndovu katika eneo la kule Jimboni kwake. Sisi kama Serikali ni lazima tujitafakari sana kwenye eneo hili, kwa sababu michango mingi iliyozungumzwa nikiri kabisa kwamba kama Serikali tusipochukua hatua za haraka tatizo hili linaweza kuwa kubwa zaidi hata ile dhamira ya uhifadhi tunaweza tusiione. Dhamira ya Baba wa Taifa kuhusu uhifadhi tunaweza tusiione. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Serikali lazima tukajipange na nimewaambia wenzangu kila mmoja kwenye eneo lake tujipange hasa. Tunatambua kwamba eneo hili linahitaji fedha nyingi na Baba wa Taifa alisema kwamba pamoja na kwamba uhifadhi ni faida kwa Taifa letu lakini peke yetu hatutaweza ni lazima tupate msaada kutoka maeneo mbalimbali. Mashirika ya Kimataifa, lakini nilipotoka hapa asubuhi nilikuwa nateta na Waziri wa Fedha kumwomba zipo fedha ambazo zimetengwa kwa mujibu wa sheria na hizi kwa muda mrefu zimekuwa hazitufikii Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi ni gharama kubwa. Wahifadhi wetu wanafanyakazi kubwa na kazi nzuri sana, kazi ngumu sana pamoja na changamoto nyingi ambazo tunaendelea nazo lakini lazima tukiri kwamba changamoto la wanyama wakali ni janga ambalo tunahitaji kama Serikali kujipanga hasa ili tuweze kulimaliza. Inawezekana changamoto hizi zikawa zimesababishwa na pande nyingi; upande wa wananchi wanaweza wakawa na mchango wao, lakini sisi pia kama Serikali lazima tujipange hasa kwa sababu ipo mipango mingine ambayo inapangwa bila kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii wakati mwingine, ndiyo inapelekea leo hii tunajikuta kwamba tuna matatizo mengi ambayo tunahitaji kwenda kuyatatua na matatizo haya yanahitaji fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nateta pale na Waziri wa Fedha kuona ni namna gani wataweza kuendelea kutusaidia kwa sababu mchango wa sekta hii hauwezi kudharauliwa. Sekta hii inatoa mchango kwa asilimia karibu 25 fedha za kigeni na kwa fedha za ndani GDP mchango zaidi ya asilimia 22, lakini mchango huu ni mdogo. Tunaamini kabisa tukijipanga vizuri tukaweka mikakati mizuri ya uhifadhi na utalii tukaweza kudhibiti wanyama wakali, tukaweza kutengeneza sera nzuri, tukadhibiti ubadhirifu wa fedha, tukadhibiti rushwa katika uhifadhi, tukadhibiti rushwa katika uwekezaji wa uhifadhi. Naamini kiasi hiki ambacho leo hii tunakiona asilimia 25, asilimia 21 kwenye pato la Taifa, basi tunaamini kabisa tunaweza kuvuka lengo na kufika mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha amenithibitishia, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mwenyekiti wa Kamati, alipokuwa anazungumzia suala la retention na fedha nyingine za kisheria ambazo zinapaswa kuja kwenye Wizara. Waziri wa Fedha amenithibitishia na yeye ni msikivu sana, naamini tutakaa pamoja kuweza kuona ni namna gani tunawenda kumaliza changamoto hizi kwa kupata fedha ambazo ameniahidi kwamba Wizara itapata ili tuweze kuzimaliza hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na michango mingi ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika Bunge lako hili tukufu pamoja na mambo mazuri ambayo Waziri wa Fedha ameyazungumza. Sisi kama Wizara tutaendelea kujipanga vizuri. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, tunatambua Wizara yetu ina–cover karibu asilimia 50 ya nchi yetu, asilimia 50 ya nchi yetu ipo ndani ya hifadhi. Tuna kazi kubwa kila mmoja wetu na sisi tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge, wawakilishi wa wananchi, kama ambavyo wameweza kuzungumza kwa kina hapa kuhusu changamoto za wananchi kwenye maeneo yao, tutafika huko, tutakwenda tuweze kuona namna gani tunatatua changamoto ambazo zinawakabili katika maeneo ambayo Wabunge wanawawakilisha wananchi kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuwathibitishie Watanzania, changamoto hizi zimepata mwenyewe na mwenyewe si mwingine ni huyu Mndengereko. Tutakwenda kuhakikisha kwamba changamoto hizi tumezimaliza, tutafika kusini, tutafika magharibi, mashariki na kaskazini kuhakikisha kwamba mzigo huu tuliokabidhiwa tunautendea haki na Watanzania wawe na furaha na nchi yao katika nyakati zote za masika na kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mdogo nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninakushukuru tena, asubuhi nilipata fursa ya kukupongeza na kukushukuru kwa bahati mbaya ulikuwa kwenye majukumu mengine mazito ya Kitaifa.

Mheshimiwa Spika, ninachukua fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, ninaishukuru sana Kamati ya Bunge ambayo imekuwa ni mshauri mzuri wa Wizara hii, tumepokea maelekezo, tumepokea maoni yote ya Kamati na yale maeneo yenye mapungufu mawili, matatu tayari Naibu Waziri amekwisha yatolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, siku ya leo kumekuwepo na wachangiaji zaidi ya 20 na wachangiaji wengi toka asubuhi wamekuwa wakitupongeza Wizara, hivyo Wizara tunalichukua hilo kama deni ili tuende tukafanye vizuri zaidi. Ukiangalia maelezo yetu Wizara, hotuba yetu imejikita katika taarifa ambazo kwa kweli msingi wake ni Bunge, ndiyo maana tunaipongeza sana Bunge, tunawapongeza sana Wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Mwenyekiti mahiri kabisa Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwa kutushauri, kwa kutupa maoni na kimsingi naomba niwaambie Watanzania kwamba Wizara hii itaongozwa na ubunifu, Wizara hii itaongozwa na weledi pia Wizara hii itaongozwa na uchapakazi.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni Wizara ya wananchi kwa msingi wake kwa sababu wananchi wanaitegemea izara hii katika kuleta furaha na faraja, kwa mantiki nyingine Wizara hii ni Wizara ya furaha na faraja kwa Watanzania. Jukumu letu kubwa tutaiponya mioyo ya Wasanii. Ninaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tunakwenda kuponya mioyo ya wanamichezo pia tunakwenda kuimarisha utamaduni, hivyo haya naomba niweze kuyaweka vizuri kabisa katika Bunge lako Tukufu kwamba tutakwenda kuchapa kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba ile kazi ambayo tuliianza nayo tunakwenda nayo mbele ili Kwenda kuleta faraja kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja chache ambazo Naibu Waziri hakupata fursa ya kuzitolea ufafanuzi wa kina, hapa ninaomba nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja chache ambazo ninaamini Watanzania wanatamani kuzisikia. Imeibuka hoja hapa kuhusu suala la ZFF, FIFA, CAF na TFF. Eneo hili Wizara tunahitaji kuendelea kulifanyia kazi sana ili Watanzania waweze kuwa na furaha kwa pande zote mbili. Ninachukua fursa hii kulitangazia Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, tumekuwa na ushirikiano wa karibu kabisa baina ya Wizata yetu ya Michezo, Utamaduni na Sanaa pamoja na Wizara ya Michezo ya Zanzibar, tumeshirikiana na karibu sana, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Michezo Zanzibar, amefanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba timu yetu ya Serengeti Girls iliweka kambi Zanzibar toka tunaanza mashindano ya kulekea Kombe la Dunia, kwa hiyo ninawapongeza sana Viongozi wa Zanzibar, leo nafikiri tulikuwa nae Rais wa ZFF hapa Bungeni. Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia miongoni mwa Wajumbe ambao niliwateua kuingia katika Baraza la Michezo BMT, mmoja wa Wajumbe katika Baraza la Michezo anatoka Zanzibar. Pia tumewashirikisha wenzetu kutoka Zanzibar katika baadhi ya Kamati mbalimbali muhimu za nchi yetu katika kuendeleza michezo hapa nchini, hivyo Wizara tunashirikiana vizuri.

Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kazi kubwa inayofanya na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pia ni lazima tupongeze na tukiri kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar, ni kazi kubwa na nzuri. Tunaliahidi Bunge lako Tukufu kwamba eneo hili tutakwenda kulifanyia kazi, msemo ambao napenda niutumie hapa ni kwamba hakuna mkate mgumu mbele ya chai, hivyo katika Wizara hii hakutakuwa na jambo gumu, kila jambo tutahakikisha tumelifanyia kazi na kulitatua kwa mustakabali wa Taifa letu. Hivyo naomba niwashauri Waheshimiwa Wabunge wasiwe na wasiwasi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo lilizungumzwa hapa ni kuhusu Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA) kwamba kifanye uchaguzi. Watanzania wanataka mabadiliko, wanataka mabadiliko katika sekta ya michezo, eneo hili ninatambua Mheshimiwa Mbunge amelizungumza hapa, lakini kwa mujibu wa taratibu na kwa mujibu wa miongozo, utaratibu wangu ni kufuata utaratibu. Ninatambua Mheshimiwa Mbunge anaweza asiridhike na majibu haya lakini siwezi kuwa na majibu mazuri ya kumfurahisha zaidi ya haya ninayoyasema sasa.

Mheshimiwa Spika, inawezekana huko nyuma wenzangu hawakufuata taratibu lakini mimi nitanyooka kwenye taratibu. Ninawathibitishia kabisa kwamba TWFA haina wanachama katika baadhi ya Wilaya, haina wanchama walisajiliwa katika baadhi ya Mikoa, tayari nimeshawaagiza wenzangu katika Mikoa na Wilaya kuhakikisha kwamba wanaharakisha michakato ya kupata wanachama wa TWFA ili tuweze kuwapata Viongozi ambao wamechaguliwa katika misingi ambayo wanachama wao wenyewe wamewachagua. Kwa hiyo, inawezekana nisiwe na majibu mazuri hapa, lakini ninawathibitishia Waheshimiwa Wabunge, inawezekana tulikuwa hatufanyi vizuri kwa sababu tulikuwa hatufuati utaratibu.

Mheshimiwa Spika, nyakati zangu hizi tutahakikisha tumejikita katika misingi ya kufuata taratibu ili tuweze kufanya vizuri. Ninakuomba Mheshimiwa Mbunge ninatambua majibu haya hayawezi kukufanya ushindwe Ubunge lakini sitakuwa na majibu mazuri zaidi ya haya ninayokuambia kwamba watu wafuate taratibu nami nitajikita katika misingi ya taratibu. Hayo ndiyo majibu yangu kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Uwanja wa Dodoma, Serikali yetu ya Awamu ya Sita imedhamiria hakika katika kuhakikisha kwamba uwanja wa Dodoma unajengwa. Ninaomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba dhamira na ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba Tanzania tunaendesha mashindano ya Afrika ya mpira wa miguu ifikapo mwaka 2027, hizi ndizo ndoto za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Katika maeneo ambayo Wizara yetu imeyapa kipaumbele ni ujenzi wa uwanja wa Dodoma. Naomba niwathibitishie Wabunge kwamba Wizara hii itaongozwa na mikakati, itaongozwa na weledi na uchapakazi, hatutajikita katika sehemu ambayo tumefungwa na bajeti tu. Viongozi katika Wizara hii tumekubaliana kila mmojawepo kuhakikisha anachapa kazi, tunajiongeza tusifungwe na mipaka ya bajeti tuliyonayo, huu ndiyo msingi ambao nimeujenga katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika Wizara tayari tumeshafanya vikao kadhaa na wadau wa michezo. Naomba nilitaarifu Bunge lako kwamba tayari tumepokea wadau mbalimbali wa michezo zaidi ya Saba ambao wako tayari kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa uwanja wa Dodoma na tayari tumekwishaonesha michoro ya uwanja wa Dodoma, mchakato wetu ni kuhakikisha kwamba uwanja huu umejengwa ndani ya miezi 17, pengine baada ya kuahirishwa kwa Bunge hili Tukufu tutaendelea na michakato ya kumpata mdau ambae atashirikiana na Serikali katika ujenzi wa uwanja huu.

Mheshimiwa Spika, naomba niwathibitishie Watanzania wote kwamba Dodoma ndiyo Makao Makuu ya Nchi, tutahakikisha kwamba tunajenga uwanja wa kisasa, siyo uwanja tu wa kawaida, nimewaagiza wenzangu, tumepokea michoro ile ya awali lakini tumesema kwamba hatuwezi kuwa na uwanja ambao unatumika tu kwa ajili ya mpira wa miguu, tunataka tupate uwanja ambao utakwenda kutumika katika kuendesha mikutano mbalimbali, kuwepo na shopping mall ndani, maduka mbalimbali pia kuwepo na ofisi. Dhamira yetu ni kujenga uwanja wa kisasa kabisa, hii ndiyo ndoto ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba uwanja wa Dodoma umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu kodi kati ya timu ya Yanga na Simba ambalo limezungumzwa hapa, Wizara tayari tumekaa na Wizara ya Fedha nae neo hili ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wasiharakishe kwa sababu tayari Waziri wa Fedha amelichukua na pengine kwa kuwa tunae siku ya kesho hapa ataweza kulitolea ufafanuzi wa kina kabisa eneo hili la kodi kwa sababu linaangukia katika Wizara yake, lakini mimi Waziri mwenye dhamana kwenye eneo hili tutaendelea kushirikiana na Waziri wa Fedha kuona ni namna gani tunaleta nafuu kwa Watanzania ambao wamejitolea kuendesha michezo hapa nchini hasa timu hizi kubwa za Yanga na Simba. Tumelipokea suala hili na tutakwenda kulifanyia kazi, ninaamini kwamba kwa kuwa maandalizi ya Finance Bill yanaendelea Waziri wa Fedha atakuja kulitolea ufafanuzi wa kina kabisa eneo hili. Serikali tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi kwa maslahi na maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la ujenzi wa Arena, viwanja vya sanaa, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba tayari Wizara imeshakaa na Wadau mbalimbali ambao wamejitokeza kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa viwanja vya Sanaa. Tunakwenda kujenga viwanja ambavyo pengine kwa mara ya kwanza Afrika vitakuwa ni vizuri na bora kuliko viwanja vyote Afrika. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam tunategemea kujenga uwanja ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua na watu 16,000 mpaka 20,000 pia kwa Mkoa wa Dodoma tunakwenda kujenga uwanja utakaochukua watu takriban 15,000. Eneo hili michakato yote imekamilika, michakato ya maongezi na wadau imekamilika, hatua ambayo tumebakiza hivi sasa ni ya majadiliano baina yetu na wadau ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza Kwenda nalo na kulikamilisha eneo hili, lakini Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inayo dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tumejenga Sports and Arts Arena.

Mheshimiwa Spika, Rais wetu kwa mara ya kwanza ifikapo mwaka 2023 pengine anategemea ku-host mashindano ya kutafuta wanasanaa bora hapa Afrika, MTV Music Awards. Kwa mara ya kwanza kabisa Afrika ni dhamira ya Mheshimiwa Rais anataka kuona pengine mashindano ya kuwatafuta wanamziki bora yamefanyika katika viwanja vyetu vya Sanaa. Hili tunaenda kulifanyiakazi Pamoja na wadau kuhakikisha kwamba Serikali imetekeleza eneo hili.

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa hapa eneo la COSOTA kuhusu mirabaha. Wizara ni lazima tukiri mapungufu ambayo tumeyaona kwenye eneo hili la mirabaha. Tumeshauriwa na Kamati pia Waheshimiwa Wabunge hapa wamelizungumza suala hili kwa kina kabisa wakibeba maono na maoni ya Wasanii nchini. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kama ambavyo nimesema awali, yapo mambo makubwa ambayo tumekwishaanza kuyafanya, katika eneo hili naomba niwaambie wenzangu akiwemo Mheshimiwa Babu Tale, kwamba mkate mgumu utawezekana mbele ya chai. Eneo hili ni dogo sana, tutakwenda kulifanyia kazi. Mimi kama Waziri nimepata fursa ya kukaa na kuzungumza na Mameneja wa wanaoendesha kampuni ya Wazafi, nimezungumza nao. Nimezungumza na viongozi wao, Babu Tale mwenyewe, nimezungumza na Meneja Mkuu anayemsimamia Diamond Platnumz, pia nimezungumza na Diamond mwenyewe ili tuweze kwa pamoja kushikamana, tuzungumzie kero zetu na tuweze kuzitatua. Nimefanya mazungumzo hayo ili kwa pamoja tuweze kuleta manufaa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto hizi na tayari Mheshimiwa Rais amekwishatupa maelekezo tarehe 31 Mei, kwamba tuhakikishe tunakwenda kuzimaliza changamoto hizi. Nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba tayari nilikwishatoa maelekezo kwa COSOTA kuhakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali kutafuta mfumo mzuri ambao utatoa haki ili kila msanii mwenye haki aweze kupatiwa haki yake. Kwa hiyo hili tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, Mheshimiwa Sanga amelizungumzia hili eneo la ujenzi wa viwanja akitoa nukuu za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu, kwa mwaka huu wa fedha tunakwenda kukarabati uwekaji wa nyasi bandia na ujenzi wa viwanja vya kisasa kabisa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba nilitangazie Bunge lako tukufu kuwa, tunakwenda kuweka nyasi bandia na kukarabati Uwanja wetu wa Jamhuri wa Dodoma. Kwa mwaka huu wa fedha tunakwenda kukarabati, ukarabati mkubwa ikiwa ni pamoja na kuweka nyasi bandia katika Uwanja wetu wa Sokoine, Mbeya. Naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba tunakwenda kukarabati pamoja na kuweka nyasi bandia katika Uwanja wetu wa Sheikh Amri Abeid kule Arusha. Naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba tunakwenda kuweka nyasi bandia na kuboresha Uwanja wetu wa Mkwakwani uliopo kule Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba tunakwenda kuweka nyasi bandia na kukarabati Uwanja wetu wa Kirumba ulikoko kule Mwanza. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwa kiasi cha fedha ambacho Mheshimiwa Rais ametupatia kupitia Wizara ya Fedha tunakwenda kufanya ukarabati mkubwa katika Uwanja wetu wa Benjamin Mkapa pamoja na Uwanja wetu wa Uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndoto za Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kwamba Taifa letu linaendesha mashindano ya Afrika (AFCON) ifikapo mwaka 2027. Hii ndiyo sababu tumeanza kutenga kiasi cha bilioni kumi kwa ajili ya ukarabati mkubwa katika viwanja vyetu hivi. Tunakwenda kuweka nyasi bandia lakini pia tunakwenda kukarabati miundombinu ya ndani katika viwanja vyetu hivi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia kukutana hapa siku ya leo katika kujadili hoja hizi zote mbili. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuniamni na kuniteua katika nafasi hii kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, nichukue nafasi hii kukupongeza sana kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge ya Ulimwengu. Hongera sana. Pia, kwa kuwa niliwahi kuwa Mjumbe wa Mabunge haya natambua ugumu wa kupata nafasi hiyo. Kwa hiyo, nikupongeze sana pamoja na timu uliyokuwa nayo huko kwenye kampeni za ushindi.


Mheshimiwa Spika, lazima nikiri Wabunge wamefanya kazi kubwa katika misingi ya Katiba Ibara ya 61, 62 kuhusu kuisimamia Serikali. Kwa kila Kiongozi wa kuchaguliwa na kwa viongozi sisi wa kuteuliwa, Wabunge wanatutaka tufanye kazi zaidi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Mawaziri kila mmoja wetu katika eneo lake ameweza kutoa majibu ya hatua ambazo tumechukua. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kama Waziri ninayehusika na masuala ya Utawala, Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan iko imara sana leo kuliko jana.

Mheshimiwa Spika, hata leo tukisema tunakwenda kwenye chaguzi zetu hizo za kesho tutashinda kwa kishindo kwelikweli. Katika maeneo mengi ambako tumepita kazi kubwa imefanyika, lakini lazima nikiri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya LAAC imefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana, Mheshimiwa CAG amefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na ushirikiano ya karibu sana Wizara ya TAMISEMI na lazima nikiri kwamba mtu wa kwanza kuzungumza nae baada ya uteuzi wangu tukiachana na hawa wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, lazima tukiri taarifa hizi zinatusaidia kuboresha utendaji kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanya vizuri lugha ya kila mmoja wetu kwenda kuwajibika hakuna lugha nyingine kwenda kufanya kazi tu. Hakuna lugha nyingine na umewasikia kila Mheshimiwa Waziri akisimama hapa anazungumza ni namna gani tumewajibika tumeenda kufanya kazi katika maeneo yetu. Hakuna lugha nyepesi wasaidizi wetu na mimi nimekwisha waambia hata wasaidizi wangu Naibu Mawaziri, huu ni wakati wa kazi kama tunataka kupata ushindi wa kishindo miezi kumi ijayo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni lazima tufanye kazi hasa kwa kuzisoma taarifa hizi vizuri na kwenda kuzitendea haki kama ambavyo tumeshauriwa na Mwenyekiti wa Kamati pamoja na taarifa ya Mheshimiwa CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TAMISEMI hatuna muhali, hatuna muhali hata kidogo, tunachukua hatua kama ambavyo Waheshimiwa Mawaziri wengine wamekuwa wakifanya na sisi tunachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa hapa, taarifa ya utendaji usioridhisha kwenye baadhi ya Halmashauri tunachukua hatua, tunachukua kwelikweli na leo nitaendelea kuchukua hatua. Naomba nikuthibitishie utekelezaji wa taarifa hizi tumeendelea kutekeleza kwa kiwango cha hali ya juu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua, hata wakati fulani nilipokuwa nikiwaona Waheshimiwa Wabunge fulani wakizungumza hapa pengine wamesahau kwamba nimechukua hatua juzi tu katika maeneo yao. Mheshimiwa Kuchauka alizungumza, Mheshimiwa Mbunge wa Kigoma kule Ndugu yangu amezungumza lakini Mheshimiwa Kuchauka anafahamu hatua nilizochukua juzi tu hapa takribani kama mwezi mmoja tu uliopita tumewasimamisha kazi Watumishi ambao wameshiriki kwenye ubadhirifu wa fedha, lakini siyo kuwasimamisha tu…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nilichozungumza hapa nataka nimpe taarifa mzungumzaji anazungumza vizuri sana, mimi kwenye mchango wangu nilisema tatizo liko TAMISEMI, katika hao Saba aliowapunguza yeye juzi alipokuja, mimi nilishapeleka taarifa zao miaka miwili iliyopita, TAMISEMI wanalindana.

SPIKA: Sasa hiyo taarifa, Waheshimiwa Wabunge ukisema TAMISEMI wanalindana, Mheshimiwa Mchengerwa yumo ama hayumo, maana yeye anakuambia hapa kwamba kachukua hatua na wewe unakubali kwamba kachukua hatua lakini unachojaribu kusema ni kwamba hatua zimechelewa, sasa ukitumia, sema walikuwa labda, sema walikuwa wanalindana ili ndiyo tujue hizi hatua.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, walikuwa wanalindana na ndiyo maana nikasema nimetoa taarifa miaka miwili iliyopita.

SPIKA: Ahsante sana, sasa kusema wanalindana maana yake ni sasa wakati hatua zimechukuliwa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nilishawaripoti kwamba Fulani na Fulani wanatuharibia Halmashauri, hakuna kitu kilichoendelea mpaka alipokuja yeye, kwa hiyo tunaiambia Serikali kwa ujumla kwamba wanalindana.

SPIKA: Sawa, Mheshimiwa Kuchauka ukitumia lugha hiyo tena tutarudi kwenye Kanuni zetu hapa, ukisema walikuwa maana yake unakiri anachosema Waziri kwamba kachukua hatua, ukisema wanalindana maana yake ni sasa na hawajafanya chochote, wewe unataka kipi kati ya hicho?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, huko nyuma walikuwa wanalindana.

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Waziri unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, wakati tunachukua hatua kule Liwale nilichukua hatua mbele yake yeye akiwa pale pale, si kwa sababu mimi na yeye tulikuwa tumezungumza, yeye ni shahidi lakini kwa sababu ya vyanzo tulivyo navyo ndani ya Ofisi ya Rais, nilichukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa kuwasimamisha kazi na kutengua uteuzi wao na wengine kufikishwa Mahakamani, tumechukua hatua kwa waliokuwa Wakurugenzi wa Halmashauri ya Majiji, Jiji la Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam, Arusha na wengine wako ndani.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua katika Manispaa za Singida, Iringa, Mtwara na Sumbawanga na hata aliyekuwa Mkurugenzi wa Sumbawanga akahamishiwa kwingine tumemrejesha ili akajibu kesi iliyopo Mahakamani. Kwa hiyo, zile taarifa kwamba kuna watu wanahamishwa wanapelekwa sehemu zingine katika kipindi hiki chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mtumishi yeyote popote alipo, awe amehamishwa, awe amestaafu, atakayeshiriki kwenye ubadhirifu wa fedha za umma hatutasita kumchukulia hatua, popote alipo na huo ndio ujumbe ambao tumeutuma katika maeneo ambapo tumekwisha kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, pia tumechukua hatua katika Halmashauri mbalimbali kule Monduli, Muheza, Korogwe, Masasi, Kilosa, Uvinza, Buhigwe, Busega, Sengerema, Buchosa na Mvomero. Hivi tunapozungumza wataalam wangu wako uwandani wanaendelea kufanya uchunguzi kwa taarifa ambazo tumeendelea kuzipokea kutoka TAMISEMI, kutoka kwa watoa taarifa mbalimbali, naomba nitoe taarifa kwamba TAMISEMI inaendelea na uchunguzi katika Halmashauri za Wilaya ya Kibaha ambayo imezungumzwa kwenye taarifa ya LAAC, tunaendelea na uchunguzi kule Kigoma, tunaendelea na uchunguzi Uvinza, tunaendelea na uchunguzi Ileje pamoja na Ifakara.

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ole-Sendeka

TAARIFA

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, Wasomi wanasema “mnyonge mnyongeni haki yake mpeni”. Ni kweli kwamba Mheshimiwa Mchengerwa hufuata nyayo za Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu wa sasa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa katika kushughulikia mafisadi, natamani kama watu wote wangeungana na Mawaziri wako wengi tu waliochukua hatua, kwa kwenda kwa kasi hii ya muda mfupi uliokaa TAMISEMI tuna matumaini makubwa sana na ninahakika Waziri Mkuu amempata Msaidizi katika eneo hilo.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa ya ndugu yangu na rafiki yangu. Tunaendelea kuchukua hatua hata kwa Wakuu wa Idara, naomba nitoe taarifa kwamba Wakuu wa Idara ya Vitengo vya Ununuzi na Ugavi 23 tumekwisha waondoa, Waweka Hazina 16 tumekwisha waondoa, Wakuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Sita na Wakaguzi wa Ndani Wawili waliondolewa nafasi zao.

Mheshimiwa Spika, Waganga Wakuu 10 wa Mikoa wameondolewa nafasi zao, Waganga wa Wilaya 46 wameondolewa nafasi zao na mwingine tumemuondoa hivi karibuni kule Mbogwe, tumemuondoa hivi karibuni. Kwa hiyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan inachukua hatua madhubuti.

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa kuhusu….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nikiri Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa sana, sana, sana na ni lazima panapotokea mafanikio makubwa ni lazima credit tumpe Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na kazi nzuri anayoifanya kwenye maeneo yetu. Hatutaki tumpe taabu Mheshimiwa Rais 2024/2025, na ili tuweze kufanikiwa tusimpe taabu ni lazima tufanye kazi kwa bidii hakuna lugha nyingine! Hakuna lugha nyingine.

Mheshimiwa Spika, wale wote ambao wametajwa kwenye ripoti naomba niseme maneo yafuatayo; ole wake kiongozi yeyote mzembe na mbadhirifu, ole wake! Kiongozi yeyote mzembe kwenye Wizara yangu na asiye na nidhamu nitakaye mkuta huko na wabadhirifu, nataka niwaambie siku zao zinahesabika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri malizia mchango wako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kumuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuchukua hatua dhidi ya Mkurugenzi wa Igunga, aliyekuwa Mkurugenzi kule Kigoma Ndugu Athumani Francis Msabila, kumsimamisha kazi mara moja kwa sababu ya ushiriki wake wa fedha za mifumo akishirikiana na watendaji wa mifumo walioko TAMISEMI wawili walitajwa katika taarifa ya ripoti. Katibu Mkuu awasimaishe kazi mara moja na taarifa hizi za ripoti ya LAAC pamoja na hii ya CAG ni wakeup call kwa kila mmoja wetu kuwajibika kwenye eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutahakikisha tunawatendea haki Watanzania, Serikali inafanya kazi kubwa sana ni lazima tumtendee haki Mheshimiwa Rais, kwa sisi viongozi kufanya kazi kwa bidi, hakuna lugha nyingine ni lazima tufanya kazi kwa bidi kila mmoja wetu katika eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja ya Kamati ya LAAC pamoja na Kamati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ninakuomba uridhie majibu ya kila Mbunge kwa namna yalivyotolewa TAMISEMI tumekwishaandaa majibu ya kila hoja kwa namna ilivyotolewa na tutaiwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu ili tuweze kuwakabidhi Waheshimiwa Wabunge kila mmoja aweze kuipata na kuisoma, na wasisite wakati wowote pale popote kunapotokea changamoto TAMISEMI tutakuwa nanyi leo na kesho kuhakikisha kwamba tunafanya kazi kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naomba kuwasilisha. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenywekiti, na mimi nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara nyingine.

Pili niwashukuru Wajumbe na Wabunge wote wa Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamechangia kwa namna moja ama nyingine kufanikisha taarifa yetu hii ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenywekiti, tumepokea wachangiaji saba ambao wamezungumza mbele ya Bunge lako Tukufu, na wachangiaji wawili walituletea michango yao kwa maandishi. Kimsingi michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni michango ya kawaida ambayo binafsi ninaamini kabisa kwamba wanaunga mkono Taarifa ya Kamati. Nimshukuru sana Profesa Kabudi kwa niaba ya Serikali pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Ikupa na wote kimsingi wameunga mkono hoja za Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo baadhi ya mambo ambayo yameibuka nayo ni kuhusu watuhumiwa kutofikishwa katika Mhakama ya Mafisadi ambayo imezungumzwa na Mheshimiwa Taska Mbogo lakini pia ukiukwaji wa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa askari polisi kukusanya faini kwa kutoza faini na kuwalazimisha wale wanaowakamata kutokana na makosa mbalimbali ya traffic kulipa faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia makosa mbalimbali ambayo hayajaainishwa kwenye Sheria ya Makosa Barabarani kutozwa faini na polisi wa usalama wa barabarani ambayo inakiuka Ibara ya 107 kama ambavyo Mheshimiwa Amina Mollel ameizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Daniel Mutuka amempongeza Mheshimiwa Rais kusaini sheria mbalimbali ambazo zimetungwa na Bunge lako hili tukufu pamoja na Mheshimiwa Jaku ambaye yeye alizungumzia kuhusu kesi za mahabusu kukaa muda mrefu Mahakamani, vilevile pia kwamba inakuaje kosa linatendeka Zanzibar na mshitakiwa unaletwa Tanzania Bara kushtakiwa. Pia amezungumzia kuhusu Mahakama ya Kadhi pamoja na kuhusu kipengele cha mafuta na gesi ili kuridhia Zanzibar nao kuwa na haki katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mmasi pia amezungumzia kuhusu Ofisi ya CPD, Mheshimiwa Zacharia amezungumzia kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Barabara ambayo imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianzie Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama ya Mafisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Bunge lako hili Tukufu ambalo lilifanya marekebisho ya Sheria Namba Tatu ya mwaka 2016 na kutunga Sheria ya Mafisadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni jukumu la Mahakama kwa kuwa Mahakama ndiye mwamuzi wa mwisho kabisa katika utoaji haki kamati yangu inaendelea kuikumbusha Serikali kwamba wale wote waliotuhumiwa ni vyema wakafikishwa mbele ya mahakama. Kwa kuwa ni lengo la Serikali na lengo la Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupigania ufisadi pamoja na rushwa basi ni vema wale wote walishitakiwa kwa makosa mbalimbali ambao hawajafikishwa mahakamani waweze kufikishwa mahakamani ili Mahakama itoe tafsiri na kuamua kesi ambazo ziko mbele yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Susan Lyimo amezungumzia kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Ndoa. Labda niseme tu kwamba kwa kuwa kesi hii inayohusiana na masuala haya ipo Mahakamani na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nakumbuka siku moja, mbili zilizopita amelizungumza jambo hili naomba na mimi kwa kutumia Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge nisilizungumze kwa sababu nitakuwa nakiuka matakwa ya sheria husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Mary Muro Deo naye alituandikia akizungumzia kuhusu uchelewashaji wa kesi mahakamani. Kwa kuwa taarifa yangu imejieleza kwa kina kuhusu sababau za msingi za ucheleweshaji wa kesi mahakamani ninaomba Serikali ijielekeze katika utekelezaji wa maagizo ambayo Kamati yangu imetoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu suala la changamoto za Muungano kuhusu masuala ya mafuta na gesi, jambo hili kwa kuwa liliwahi kujadiliwa kwenye Kamati yangu, nimkumbushe tu Mheshimiwa Jaku kwamba jambo hili tayari lilishashughulikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunatambua kwamba hii ni sehemu ya changamoto kubwa zilizoibuka wakati wa mjadala wa Katiba Mpya, lakini tunatambua kwamba Serikali yetu kupitia Wizara ya Muungano tayari ilishatoa maelekezo kwa Wanasheria Wakuu wa Serikali wote kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kukaa na kutunga sheria kuona utaratibu mzuri wa kuweza kutatua jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Bunge lako tukufu kwani mwaka 2015 tayari imetunga Sheria ya Mafuta na Gesi. Sheria hii imekwenda kufuta sheria iliyokuwepo ya Mafuta na Gesi ya mwaka 1984 sheria ambayo ilikuwa haiitambui Zanzibar katika mchango wa kuchunguza lakini pia kushughulika na masuala ya mafuta na gesi. Kwa hiyo, jambo hili tayari limeshashghulikiwa kwa kutokana na changamoto iliyokuwepo na tayari mchakato huu umeshasha fanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini …….

T A A R I F A . . .

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuwa jambo ambalo ndugu yangu analizungumza lipo katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninatambua kwamba mabadiliko ya katiba ndiyo yatakayoweza kuliondoa jambo hilo katika sehemu ya Muungano, lakini kwa hatua iliyopo sasa Serikali tayari imeshalifanyia kazi na ndiyo maana Bunge lako hili tukufu lilitunga Sheria ya Mafuta na Gesi mwaka 2015 na kupitishwa mbele ya Bunge lako tukufu. Pia ninazo taarifa kwamba Zanzibar tayari pia wanayo Sheria ya Mafuta na Gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mchakato wa watuhumiwa kuhamishwa kutoka maeneo mbalimbali kule Zanzibar na kuletwa hapa Bara, nimuombe ndugu yangu ajielekeze katika Ibara ya nne ya Katiba ambayo inaizungumzia jambo hili. Pia sitaki kwenda mbele sana huko kwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria atayatolea ufafanuzi masuala haya iwapo utayaleta mbele yake, niombe tu kuhitimisha hoja yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza kwa kina shughuli zilizotekelezwa na Kamati, maoni na mapendekezo ya Kamati naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako sasa liipokee na kuikubali Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kama Maazimio ya Bunge hili. Naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Lakini niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi zake kubwa za kufanikisha utawala bora wa kujenga ustawi wa maendeleo ya uchumi jamii wa Taifa letu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi mazuri yamezungumzwa na mimi kwa niaba ya Warufiji na Wandengereko wote duniani niseme tu kwamba tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri iliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais wetu kwa kuchagua Mawaziri wa Nishati wazuri wachapa kazi ambao leo hii kuliwaka umeme eneo nusu la Rufiji, lakini hivi tunavyozungumza maeneo mengi ya Rufiji sasa yanakwenda kuwaka umeme, ikiwa ni pamoja na ahadi ya Waziri wa Nishati kwamba sasa kule Kata ya Ngarambe watapata umeme na nimeambiwa leo na kesho Kata ya Mwasenyi watawashiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi mazuri ya kuzungumza kuhusiana na sifa za Serikali ya Awamu ya Tano, lakini kwa uchache wa muda naomba nijielekeze katika hoja ambazo nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa awaeleze Watanzania. Kamati ya Katiba na Sheria ilimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutatua migogoro iliyopo katika vyama vya siasa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama kwenye Bunge lako hili Tukufu awaeleze Watanzania je, Serikali ina juhudi gani za kutatua migogoro ya vyama vya siasa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba, migogoro ya vyama vya siasa inakwenda kujenga taswira potofu kuhusu kuminywa uhuru wa siasa na demokrasia. Waziri Mkuu atueleze je, migogoro hii inasababishwa na mazalia ya mambo gani yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi? Je, ni historia ya nchi yetu? Je, ni uhuru wa Tanganyika? Je, ni Mapinduzi ya kule Zanzibar? Au ni sintofahamu ya elimu ya uraia? Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha masomo ya uzalendo na masomo ya umoja wa kitaifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba, uzalendo na utaifa unajengwa kama ambavyo ilivyo kwa Masheikh, Mapadri na Maaskofu wanajengwa na kuandaliwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta mapinduzi ya kifikra unaodhamiria kuzalisha elimu ya vyama vya siasa inayotokana na mawazo duni ya udumavu yasiyoendana sambamba na mageuzi ya dira ya Serikali ya Awamu ya Tano?

Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa basi atuelezee je, Serikali wakati tukiwa tunajielekeza katika suala zima la kuwaangalia Watanzania na kuangalia uzalendo uliopo pamoja na fikra za Watanzania, je, Serikali na ofisi yake inajipanga vipi kutoa elimu ya utaifa na kuondokana na msongo wa Taifa ili kuondokana na maporomoko ya miiko na maadili ya Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa pia awaeleze Watanzania yalikuwa ni mawazo yapi ya Baba wa Taifa wakati wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi? Lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu awaeleze Watanzania atakaposimama hapa makutano ya mawazo ya vyama vya siasa na ni kwenye ndoto gani ya Taifa letu? Na je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuondoa kusigana na huku kusigana kunasababishwa na ombwe la kitu gani linalosababisha kutofautiana kati ya wanasiasa, ili kuweza kujenga jamii nzuri ya Watanzania ambao kwa kweli wanailinda amani ya nchi yao na kuwa na umoja wa kitaifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa basi awaeleze Watanzania Ibara ya 8 ya Katiba inatambua kwamba, ustawi wa wananchi unajengwa na Serikali yao, lakini pia Ibara ya 26 ya Katiba inatambua na inakataza kuondoa mgawanyo au kufanya makosa ambayo ameainishwa katika Katiba au makosa yaliyoainishwa katika sheria tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa basi aelezee kuhusiana na mgawanyo wa pato la Taifa, yako manung’uniko mengi. Tunatambua wananchi wa Rufiji, wananchi wa Pwani, wananchi wa Kusini tunatambua kwamba, kipo kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kuendeleza Hifadhi ya Selous, lakini tunapata taarifa kwamba, kiasi kile cha fedha kimepelekwa kuendeleza Ruaha. Haya ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi wengi wa Rufiji, Kusini na maeneo mengine wanayalalamikia, basi Mheshimiwa Waziri Mkuu ukisimama hapa ni vyema ukawaeleza wananchi wakatambua ni namna gani na ni kwa nini mgawanyo wa pato la Taifa umekuwa ni kikwazo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atakaposimama hapa atambue kwamba, wananchi wa Rufiji wana imani na Serikali yao ya Awamu ya Tano, lakini pia, wamenituma nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, tarehe 02/03/2017 Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifika Ikwiriri na akaahidi ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nyamwage kuelekea Utete. Mheshimiwa Waziri Mkuu tukuombe wananchi wa Rufiji sasa jambo hili mpelekee Rais wetu na atambue kwamba wananchi wa Rufiji wana imani kubwa na Serikali yao na atambue kwamba tumebakiza miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ahadi hii ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami ilianza mwaka 2017 na Mheshimiwa Rais alisema itajengwa kabla ya mwaka 2020 basi, atambue kwamba ni kilometa 33 na kwamba tumebakiza miaka miwili tu. Na Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo kwa kweli, ni msingi wa wananchi wetu wa Rufiji na Pwani na maeneo mengine sisi tunampa hongera sana Rais wetu wa Awamu ya Tano kwa jitihada zake za dhati kabisa za ujenzi wa bwawa la Stiegler’s Gorge kama ambavyo nimetanguliza kusema. Na niseme tu mwenzangu amesema kwamba Stiegler’s Gorge ilianza miaka ya 1960, lakini mimi nataka kukataa niseme kwamba Stiegler’s Gorge kama sisi wa Rufiji tunauita STIGo, ilianza miaka ya 1956 wakati wa harakati za TANU, harakati za uhuru wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mwalimu Nyerere alidhamiria kujenga umeme huu kuweza kuikomboa nchi yetu. Na sisi tunaunga mkono na wananchi wa Rufiji tunaunga mkono sana, tunachoomba Serikali yetu ya Awamu ya Tano kama ilivyo madini katika maeneo mengine na wananchi wa Rufiji wanaomba kunufaika na Stiegler’s Gorge. Tuiombe Serikali kuhakikisha kwamba mradi huu wa Stiegler’s unakwenda kujenga barabara yetu ya kutoka Mwasenyi - Mloka kuelekea Ikwiriri, lakini pia, kutoka Mwasenyi - Mloka kuelekea Kibiti na maeneo mengine ya Morogoro yanayopakana na Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni ndoto za Mwalimu Nyerere hatuna haja wala hakuna sababu ya kuzibeza. Na kwa kweli, Rais Magufuli amefanya maamuzi magumu na ni miongoni mwa Marais ambao tuliwasubiri kwa muda mrefu sana. Na sisi tunampa pongezi sana kwa jitihada hizi. Na Warufiji tuko tayari kutambua mradi huu utakwenda kuinufaisha nchi, lakini utakwenda kuinufaisha Rufiji kwa mambo mengi mazuri yanayokuja; ujenzi wa barabara, ujenzi wa madaraja, Daraja la Utete litajengwa kuiunganisha Rufiji na maeneo mengine ya Kusini. Tunampongeza sana Rais wetu, lakini pia tunamtakia kila la heri katika kutekeleza mambo haya yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa rejea ya muda niseme tu kwamba pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Waziri, Profesa Mbarawa na Mawaziri wake wote naomba Serikali itambue kwamba siasa za Rufiji ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa za Rufiji ni ngumu sana kwa sababu wananchi wetu wengi wanaamini kwamba serikali imewaacha mkono. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa utambue kwamba boma la Rufiji lilijengwa mwaka 1800. Hii inamaanisha kwamba Rufiji ilikuwepo nyakati za mkoloni, ni Wilaya ya sita nyakati za mkoloni na ni Wilaya ya 21 nyakati za uhuru (tulivyopata uhuru). Historia yetu inamuweka Bibi Titi Mohamed kuwa ni Mbunge wa kwanza Rufiji aliyepigania barabara ya kutoka Dar es Salaam kuja Kibiti na barabara hii ilijengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Warufiji hawaamini ahadi aliyoiweka Mheshimiwa Rais ya tarehe 2 Machi, 2017 kwamba barabara ya Nyamwage - Utete sasa inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami. Nimuombe Waziri ukisimama hapa waambie Warufiji kwamba sasa barabara hii inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa bahati mbaya nimekagua kwenye kitabu chako sijaona ukurasa wowote unaozungumzia barabara ya Nyamwage - Utete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana, ukisoma ukurasa wa 228 imetengwa kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya upembuzi yakinifu barabara ya Nyamwage - Utete. Nikuombe Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa waeleze wananchi wa Rufiji namna ambavyo Serikali sasa inakwenda kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kuwa akina mama wengi wanafariki wakiwa wanalekea Utete kupata huduma za hospitali. Barabara hii ina kilometa 32 tu lakini inatumia masaa manne mpaka masaa matano kutembea kwenda Halmashauri ya Wilaya. Tangu mkoloni na baada ya uhuru, Rufiji ndiyo Wilaya pekee ambayo haiunganishwi na lami katika Halmashauri zote za awali, tangu nyakati za mkoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri, Warufiji sasa wamechoka, miaka 57 wamechoka, wamenituma niseme kwamba wamechoka. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakaposimama hapa uwaambie ahadi ya Dkt. John Pombe Magufuli ya tarehe 2 Machi, 2017; alisema mwenyewe pale Ikwiriri kwamba ataijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kabla ya mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, siasa za Rufiji ni ngumu sana, Warufiji wanabadilisha Wabunge kila baada ya miaka mitano. Nataka niiambie Serikali kwmaba iwapo barabara hii haitajengwa basi wajue na mimi watanikosa mwaka 2020. Niiombe Serikali, lazima niseme, niiombe Serikali hiki ni kilio cha muda mrefu Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana utuambie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukurasa wa 212 Mheshimiwa Waziri umezungumzia ukaratabati mdogo, nikuombe tupe ufafanuzi wa ukarabati mdogo wa barabara Nyamwage - Utete. Kama barabara hii tayari Mheshimiwa Rais aliashaahidi na ameeridhia ujengwe, sasa je, ni kwa nini ni kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati? Ni kwa nini fedha hizi zisiende kwenye mambo mengine na barabara hii ikajengwa kwa kiwango cha lami? Tumechoka Mheshimiwa Waziri. Nikuombe sana ukisimama hapa utueleze. Tumebakiza miaka miwili tu kwenda kwenye uchanguzi, sina sababu ya kukaa kimya, dhamira yangu ni kuizungumzia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti. lakini pia tunaomba Mheshimiwa Waziri tumeridhia ukurasa wa 196, ujenzi wa barabara ya kutoka Kibiti kuelekea Mwaseni - Mloka ambako inajegwa kwa kiwango cha lami, nikuombe Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa sasa utuelezee kuhusu Daraja la Utete kwa sababu halimo kwenye orodha ya mipango ya Serikali, na kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa nishati yeye alikwambia kwamba daraja hili litajengwa ili kuweza kuwaunganisha wananchi wa Rufiji na wananchi wa Kusini, tukuombe sasa utuelezee daraja hili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango wangu niliochangia katika Bunge lako Tukufu leo; nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Waziri wa Ujenzi Engineer Kamwelwe ambaye natambua uchapa kazi wake, akiwa Naibu Waziri wa Mji alifanya kazi kubwa sana na kuwasaidia sana wananchi wa Jimbo langu. Pamoja na kazi kubwa aliyoifanya, pamoja na mchango wangu wa kuongea Bungeni, nimwombe Waziri azingatie yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri kwa kukubali ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete kilomita 33, barabara hii ni ahadi ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya tarehe 4/3/2017 kuwa itakamilika kabla ya 2020. Nimwombe Mheshimiwa Waziri sasa kwa kuwa upembuzi yakinifu umekamilika, aje sasa kuweka jiwe la msingi mwezi Juni ili wananchi wapate imani kwani barabara hii imeondoa Wabunge wengi.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali inisaidie ili niweze kurudi 2020 – 2025. Nyamwage-Utete ni kiini cha anguko la kiuchumi Rufiji, ubovu wa miundombinu ni kero kubwa kwa wananchi, Mheshimiwa Waziri afike sasa Rufiji ili kuanza ujenzi wa barabara hii, pamoja na barabara ya Nyamwage Utete. Niombe Serikali ikubali ujenzi wa barabara ya Kibiti - Mloka ambayo inasaidia wakandarasi wanaojenga mradi wa umeme wa Rufiji (Stiegler’s). Barabara hii ni chafu sana na haifai. Mradi huu wa umeme utachelewa sana iwapo barabara hii haitajengwa kwa kiwango cha lami. Ipo barabara ya Ikwiriri – Mloka ambayo ni kioo cha uchumi wa Rufiji, tunaomba Serikali kuiweka katika mpango wa ujenzi wa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, ipo barabara ya Utete – Ngarambe, hii ni muhimu sana kufungua utalii wa Pwani ya Kusini. Ngarambe kuna Selou na pia kuna vipepeo vinavyoweza kuvutia watalii.

Mheshimiwa Spika, nyingine ni barabara ya Mloka - Kisarawe, Mloka - Kisaki, Bungu – Nyamisati – Kisiju - Mkuranga, Vikindu – Vianzi. Hizi ni barabara muhimu kwa kufungua uchumi wa Mkoa wa Pwani, ubovu wa miundombinu hii kumepelekea kudumaa kwa uchumi na ndiyo sababu kumekuwepo na wimbi kubwa la umaskini katika eneo la Pwani ya Kusini.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii na kwa niaba ya Wandengereko wote duniani tunakushukuru sana na tunakuombea dua kwa kuwa Mbunge wao sasa ameweza kusimama na kuzungumza mbele ya Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote ambao wamewasilisha taarifa zao, Mheshimiwa Suleiman Jafo kaka yangu pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwa kweli niseme tu kwamba wanafanya kazi nzuri. Hata hivyo, pamoja na kwamba wanafanya kazi nzuri Watanzania wanaendelea kuwaombea dua pamoja na kuiombea Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi iendelee kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Tunatambua kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano sasa imeridhia kuwarejesha baadhi ya watendaji wale ambao wana vigezo maalum kuweza kurejea kazini. Hii ni pongezi kubwa sana, kwa niaba ya watendaji wote nchi nzima wanaishukuru sana Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akumbuke kwamba miaka ya 2000 walikuwepo Watendaji wa Vijiji ambao walifanya kazi kwa kujitolea ambao kabla ya tamko la mwaka 2003 watendaji hawa mwaka 2004, Waziri wa Utumishi aliyekuwepo wakati ule, Brigedia Ngwilizi alitoa tamko la kutoa ajira kwa Watendaji wa Vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aweke kumbukumbu zake vizuri sana. Wakati wa tamko lile la mwaka 2004 ambalo lilipelekea kuajiriwa watendaji wengi wa vijiji hususani vijiji vyangu karibu vyote vya Wilaya ya Rufiji, watendaji wale hawakuwa na sifa ya kuwa na vyeti vya utumishi. Mwaka 2006 tamko lililofuata liliwataka watendaji waajiriwe kwa kuwa na vyeti vya utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tumshauri vyema Mheshimiwa Rais atambue kwamba wapo watendaji walioajiriwa mwaka 2004 bila ya kuwa na vyeti vya utumishi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu iwapo leo hii tunasema kwamba watendaji wale waondolewe kazini kwa kuwa hawakuwa na vyeti, lakini vigezo vya ajira mwaka 2004 havikuwataka wao wawe na vyeti vya utumishi.

Mheshimiwa Waziri iwapo tutaamua kuwaondoa kazini watendaji hawa tunavunja mambo mengi ya kisheria hususan Sheria za Kazi. Pia niwashauri watendaji wote nchini wale ambao wanaangukia kwenye tatizo hili; iwapo barua zao za ajira zinaonesha kabisa kwamba hawakupaswa kuwa na vyeti vya utumishi, basi wasilalamikie katika mioyo yao, wasisite kwenda kwenye Mahakama za kazi ili waweze kupata haki zao za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu watendaji hawa hawana makosa, kosa ni letu sisi wenyewe viongozi wa Serikali ambao tulitoa tamko la ajira kwa watumishi ambao hawakuwa na vyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Suleiman Jafo, nimshukuru sana kwa kazi nzuri aliyoifanya; lakini kipekee kabisa nimshukuru kwa kiasi cha fedha alichokitoa kwa ukarabati mkubwa wa Kituo chetu cha Afya cha Ikwiriri, tulipokea shilingi milioni mia saba. Hata hivyo nimwombe na nimkumbushe, aliwaambia wananchi wa Rufiji kwamba atawapatia kiasi cha shilingi milioni mia saba nyingine kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kule Mwaseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, nimwombe Katibu Mkuu kama maagizo haya anayo basi kuhakikisha kwamba kiasi hiki cha fedha kimekwenda; na wananchi wa Kata ya Mwaseni tayari walishaandaa mazingira ya ujenzi wa kituo cha afya kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba Kata ya Mwaseni ndipo tutakapozalisha umeme wa Stieglers’ Gorge. Kwa hiyo utoaji wa fedha hizi milioni mia saba ni muhimu sana, kwa sababu tunategemea kwamba population ya wananchi wa Kata ya Mwaseni itakuwa kubwa sana. Kwa kuwa sasa Mbunge wao amepambana kuhakikisha kwamba Stieglers’ Gorge sasa inarejea na sisi tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tumwombe sana Mheshimiwa Waziri, kiasi hiki cha fedha sasa kiweze kufika na wananchi wetu wa Kata ya Mwaseni waweze kupata kituo cha afya kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatambua kazi ya Waziri, Mheshimiwa Suleiman Jafo ni nzuri sana. Yeye ni mchapakazi kwa ajili ya wanyonge; wananchi wa Rufiji wanaomba nyongeza ya ambulance kwa ajili ya Kata hii ya Mwaseni pamoja na Tarafa nzima ya Mkongo, pia katika Kata ya Mbwala kuna uhitaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea katika elimu nimwombe Mheshimiwa Waziri atambue kwamba Rufiji tumetoka katika matatizo makubwa sana mwaka 2017, matatizo ambayo yalitisha nchi nzima katika maeneo ya Rufiji, Mkuranga pamoja na Kibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tutambue matatizo haya yalisababishwa na mambo mengi, lakini miongoni mwa mambo haya lazima tutambue kwamba wananchi wengi asilimia karibu 90 ya wananchi wa Rufiji, vijana wanaoanza darasa la kwanza hawaendelei kidato cha nne, hawaendelei kidato cha sita. Niseme zaidi ya asilimia 95 ya vijana wanaoanza darasa la kwanza hawaingii chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, yako mengi yanayosababisha vijana kushindwa kuendelea na shule, yako mambo mengi sana. Pia katikati ya mambo haya ni mazingira ya shule, umbali wa shule zenyewe tulizonazo na pia ziko baadhi ya kata ambazo hazina shule zetu za kata kwa mfano Kata ya Ngarambe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Ngarambe kuelekea Utete ni zaidi ya kilometa 68. Huwezi kuamini kwamba kijana anayefaulu kidato cha nne anapaswa kwenda kusoma Utete ambako anatakiwa atembee kwa kila siku kilometa 68. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, upendeleo na dhamira ya Serikali kuona umuhimu wa kunyanyua elimu katika maeneo ambapo mwamko wa elimu ni mdogo; si dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ipo hata katika Katiba ukiisoma ibara ya nane (8) ya Katiba inazungumzia umuhimu wa Serikali kunyanyua ustawi wa maisha ya wananchi wake. Tunapokwenda kunyanyua ustawi wa maisha wa wananchi tunazungumzia umuhimu wa maendeleo ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atambue kwamba nchi yetu hii ipo jamii ya tabaka la wananchi wenye maisha duni na dumavu. Tabaka hili ni miongoni mwa tabaka la wananchi wa Rufiji pamoja na maeneo mengine ya Kibiti. Pia yapo maeneo ya tabaka la wananchi wenye maisha endelevu, yako maeneo hayo, ameyazungumzia katika ukurasa wa 56 wa hotuba yake katika mchakato wa kuboresha miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tunapokwenda kuboresha miji tuangalie maeneo yenye matatizo makubwa, maeneo ambapo kumekuwepo na migogoro ya mara kwa mara. Kwa mfano, Rufiji mwaka 2007 yalitokea machafuko makubwa kati ya wakulima na wafugaji, lakini mwaka 2017 kumetokea matatizo makubwa ya amani kila mmoja anafahamu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati amedhamiria kwenda kutatua matatizo haya na tunaipongeza Serikali kwa kazi nzuri iliyofanya, tuangalie sasa uwezekano wa Serikali kwenda kubadilisha kabisa hali ya maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liliwahi kufanywa na Mwalimu Nyerere miaka ya 70 ambapo aliongeza mwamko wa kutoa elimu na kuwasaidia wananchi wenye matatizo makubwa ya elimu na ya kiuchumi. Miongoni mwa watu walionufaika tunaye Profesa Kabudi alinufaika na mpango wa Mwalimu Nyerere wa mwaka 1973 na niiombe Serikali sasa kipekee kabisa…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na naipongeza sana Wizara na Serikali kwa ujumla. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako hili tukufu, lakini nikushukuru sana wewe kwa kunipa fursa ya kuchangia katika mapendekezo haya ya mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba lengo kuu la Serikali ni ustawi wa Wananchi wake. Na Wananchi ndio msingi wa mamlaka na Serikali itapata madaraka na mamlaka yote kutoka kwa Wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya mpango yana mambo saba ambayo yamezingatiwa. Jambo la kwanza lililozingatiwa wakati Mheshimiwa Dkt. Mpango anaandaa mpango wake ni Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2025, lakini pia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017, 2020/2021, lakini pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzingatia kuyandaa haya mpango pia ni lazima uzingatie Katiba, lakini pia uzingatie sheria na maelekezo ya viongozi. Maelekezo ya viongozi ni sheria kama ambavyo leo hii tunapitia mpango na baadae mapitio yale yatakuwa ni sheria ambayo yatakwenda moja kwa moja katika kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nianze na hili na niseme tu kwa nia njema kabisa, kumekuwepo na sintofahamu ambayo baadhi ya Wabunge wamezungumzia kutoridhishwa na baadhi ya majibu ya Waziri wetu wa Ujenzi.

Sisi ni miongoni mwa watu ambao tulimpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi akiwa Waziri wa Maji, lakini amekuwa akitoa kauli ambazo wakati fulani haziridhishi na mimi nichukue nafasi hii kumuomba sana kwamba ile kazi nzuri aliyoifanya akiwa Waziri wa Maji basi aweze kuiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambapo Mheshimiwa Rais aliweka ahadi. Ahadi zile ni sheria ambazo zinahitaji kutekelezwa, lakini sasa wewe Mheshimiwa Waziri ukinijibu mimi kwamba yale uliyoachiwa na Mheshimiwa Profesa Mbarawa wewe hauhusiani nayo, ninapata taabu sana kuelewa ni namna gani sasa umeamua kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba sheria ya uongozi inatutaka viongozi kugusa mioyo ya wananchi wetu na kutugusa sisi wenyewe, leaders touch the heart before they ask for hands. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri arekebishe na arejee kwenye kasi yake nzuri aliyokuwanayo akiwa Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 9 ya Katiba inazungumzia namna ambavyo shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya Wananchi wetu wote, lakini Ibara ya 9(d) inasema kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa uangalifu na kwa pamoja. Mheshimiwa Dkt. Mpango amezungumza changamoto nyingi ambazo kimsingi ndio mijadala ya Bunge letu hili tukufu, amezungumzia ugumu wa ukusanji wa kodi, amezungumzia kushuka kwa biashara za Kimataifa, amezungumzia upungufu wa wafanyakazi (ajira), lakini pia amezungumzia kupungua kwa misaada na pia amezungumzia madai ya watumishi.

Mimi nimuombe sana Dkt. Mpango wakati sasa anakuja kujibu hapa hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, kwanza kabisa atambue kwamba lipo andiko liliwahi kutolewa na Tony Cliff katika kitabu chake alichowahi kuandika Building the Party ambacho kimetolewa mwaka 1975, akimnukuu Lenin.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa lolote ni vyema tukajiuliza tulichonacho na namna ambavyo tunataka tukitumie, mimi kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji na kwa Watanzania wote, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa nia yake thabiti katika ya kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme yaanai Stigler’s Gorge, mradi wa kuzalisha umeme kule Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kilio cha muda mrefu sana cha Watanzania, kwa kuwa historia inatuambia kwamba jambo hili lilianzia miaka ya 56.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mwalimu Nyerere yeye akiwa ni pioneer wa jambo hili, alisisitiza sana kwa mchakato huu wa uzalishaji wa umeme ambao utakwenda kuwasasidia Watanzania wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipongeze Serikali, lakini pia niwapongeze sana wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kwa kuwa jambo hili wao walinikabidhi mwaka 2015 na ilikuwa ni ahadi yetu sisi nyakati za kampeni, lakini pia mwaka 2016 niliingia nalo ndani ya Bunge lako hili tukufu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini pia nimpongeze sana Waziri wa Nishati atambue kwamba wananchi wetu wa Jimbo la Rufiji wanamuunga mkono sana, na kwa kuwa mradi huu upo Rufiji, asikate tamaa na sisi tunasema kwamba Serikali iendelee na mchakato wote wa kuandaa miundombinu ya ujenzi wa bwawa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo changamoto ambazo sisi wananchi tunaziona. Leo hii tunatambua kwamba hata tukiwauliza Mawaziri wetu wanaohusika suala la wakulima na wafugaji, halijazungumzwa sana katika vitabu vyetu hivi, hata Dkt. Mpango hajalizungumzia sana ambavyo ni namna gani Serikali itakwenda kuwasaidia wafugaji katika kuandaa maeneo ambayo wataweza kufanya mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais kutekeleza ujenzi huu wa uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Stigler’s Gorge pale Rufiji, lakini tunahofia sana wananchi wa Rufiji, kwa kuwa leo hii mifugo imeingia sana katika eneo la Bonde la Mto Rufiji na pengine tunalaumu sana Serikali wakati ule miaka ya 2005
walipoamua kuondoa mifugo katika Bonde la Ihefu na kuleta mifugo katika Bonde la Mto Rufiji wakijua kabisa kwamba dhamira ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1956 ilikuwa ni kulilinda Bonde la Mto Rufiji na ndio maana Mwalimu Nyerere mwaka 1978 alianzisha sheria maalum kabisa sheria ya kuanzisha RUBADA ili kuweza kulinda Bonde la Mto Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali na nimuombe sana Dkt. Mpango, atakapokuja kuhitimisha hapa basi aone changamoto hii kubwa ambayo Mheshimiwa Rais leo hii anakwenda kutekeleza mradi huu wa Stigler’s Gorge, mradi wa kuzalisha umeme Bonde la Mto Rufiji. Lakini leo hii tuna mifugo zaidi ya laki tano ndani ya Bonde la Mto Rufiji, tunafahamu Bonde la Ihefu lilikufa na uoto wa asili ukaharibika, mvua zilikuwa hazinyeshi na leo hii tunakwenda kuandaa Bonde la Mto Rufiji ambalo mifugo zaidi ya laki tano imeingia kwenye Bonde, hakuna jitihada zozote ambazo zimeandaliwa na Wizara yaK ilimo, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Ardhi na Wizara nyingine namna gani wanakwenda kutatua kero kubwa ya wakulima na wafugaji, ili sasa kumsaidia Mheshimiwa Rais wakati anakwenda kutekeleza mradi huu wa kuzalisha umeme, kuwepo na maji ya kutosha kwa sababu tunatambua kwamba mradi huu utahitaji uzalishaji wa maji yaani mvua za zaidi ya miaka miwili au miaka mitatu kuweza kujaza bonde lile katika uzalishaji umeme.

Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kuhitimisha aelezee mpango wa Serikali ni namna gani sasa Serikali itakwenda kutatua kero kati ya wakulima na wafugaji. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nitambue michango yote iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Idadi ya Wabunge waliochangia ni 18 na kwa nafuu ya muda sitawataja majina. Pia nitambue michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Mawaziri wote na katika baadhi ya hoja ambazo tayari Waheshimiwa Mawaziri wameshazijibu, sitakwenda huko tena kwa sababu ninaamini kama ni ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge basi utakuwa umechukuliwa na Waheshimiwa Mawaziri na pengine wataufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limezungumzwa kwa kina pengine napenda kulisisitiza sana ni kuomba Kiti chako kwamba hizi semina kwa Waheshimiwa Wabunge ni muhimu sana ili kila mmoja wetu aweze kutambua mipaka ya kuchangia hususan inapohusu mihimili hii mitatu inayounda Serikali. Kwa sababu ipo michango mingi ambayo imezungumzia kuhusu Mahakama na inatambulika kabisa kwamba Mahakimu au Majaji wana kinga na malalamiko yoyote dhidi ya Hakimu/Jaji mamlaka yake ya juu ni kukatia rufaa kutokana na maamuzi ambayo yametolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge walitambue hilo na pengine tutumie fursa ya uelewa wetu kuwaambia wananchi wetu umuhimu wa kuheshimu mihimili hii yote mitatu lakini hususan kabisa mhimili wa Mahakama ambao ndiyo umepewa mamlaka yote ya utoaji haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 ya Katiba. Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge watambue kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Jaji Mkuu lakini pia watendaji wa Mahakama wamefanya kazi nzuri sana kuboresha mifumo ya utoaji haki hapa nchini. Natambua hilo kwa kuwa mimi ni miongoni mwa vijana ambao tumekulia kule, najua hali ilivyokuwa huko nyuma na hali ilivyo sasa kwa kweli Mahakama imefanya kazi kubwa sana, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo yamezungumzwa kuhusu mamlaka ya utoaji haki na masuala ya dhamana. Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwamba ni vyema wakajikita kabisa katika kusoma vizuri Ibara ya 26 ya Katiba ambayo inamtaka kila Mtanzania kutii Katiba na sheria zetu za nchi ambazo zinatuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema tukaitambua mipaka ya utoaji haki na ni vizuri tukajikita kutafuta wataalam watusaidie katika maeneo ambapo tunaamini kabisa hatukutendewa haki. Ukisoma vizuri Katiba na sheria za nchi yetu zimetoa maelekezo mazuri kabisa ni namna gani ambapo mtu anapaswa kukata rufaa lakini ni namna gani ambapo Mahakama inapaswa kutoa dhamana na masuala mengine yote ambayo yamezungumzwa kwa kina hapa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nilivyosema Wabunge 18 ndiyo waliozungumza mambo mbalimbali na kwa kuwa tayari mengine yameshajibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na tunaamini mengine yamechukuliwa vizuri na Waheshimiwa Mawaziri, naomba nijikite tu kwenye baadhi ya masuala machache ya muhimu ili kuongeza msisitizo katika maeneo hayo. Kwa ujumla utendaji wa Wizara na taasisi zinazosimamiwa na Kamati yangu ya Katiba na Sheria ni wa kuridhisha sana ukiacha baadhi ya changamoto ambazo tayari Serikali imeshaanza kuzitafutia ufumbuzi. Hivyo, Kamati inaipongeza na kuishukuru Serikali kwa ushauri wao mzuri uliofanikisha utekelezaji wa shughuli za Kamati. Maeneo ambayo Kamati imebaini kuwa na changamoto, imetoa mapendekezo yake kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi kama yanavyoainishwa katika Sehemu ya Tatu ya taarifa ya Kamati kuanzia ukurasa wa 39 mpaka 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya maeneo hayo yaliyobainishwa na kutolewa mapendekezo ni pamoja na Serikali iongeze usimamizi na uratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu nchini na itangaze rasmi Wajumbe wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu. Jambo hili tayari Naibu Waziri wa Vijana ameshalizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo lingine mwingine ni Serikali ianzishe pia Mfuko wa Masuala ya Wenye Ulemavu na kuanzisha fungu dogo la kibajeti kwa kulitengea fedha kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020. Ushauri huu pia umezingatia maoni ya wadau wengi wa kundi hili muhimu katika jamii ambao wamechangia yetu kupitia vikao mbalimbali vya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo lingine ni Serikali pia iongeze usimamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuimarisha SACCOS zilizopo na kudhibiti SACCOS hewa za vijana ambazo hukopeshwa na kupokea fedha za Serikali. Pia Ofisi ya Waziri Mkuu iwe na ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao ndiyo wenye dhamana ya Halmashauri kwa lengo la kuhakikisha kila Halmashauri inawajibika na kuratibu fedha zinazotolewa na Mfuko wa Vijana na kusimamia marejesho yake kwa wakati. Maoni na mapendekezo ya Kamati ni kama ambavyo imefafanuliwa katika taarifa yangu ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza kwa kina shughuli zilizotekelezwa na Kamati kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2018 hadi Januari, 2019, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kukubali maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii ili yawe maazimio ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba amani na utulivu wa Taifa letu ni misingi iliyoachwa na Waasisi wa Taifa hili katika kuimarisha Serikali, Bunge kusimamia Serikali na Mahakama kuachwa kuwa huru katika kuamua mashauri mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere miaka ya themanini aliwahi kusema kwamba zipo kazi ambazo kila Mtanzania anaweza kufanya, lakini miongoni mwa kazi hizo, siyo kuwa Hakimu au kuwa Jaji. Mwalimu Nyerere alizingatia kwamba Katiba yetu ya mwaka 1977 lakini nyakati za upatikanaji wa uhuru, yako mambo mengi ambayo Watanzania pengine wangependa kuwa nayo. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameendelea kufanya uteuzi wa Majaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kifupi kilichopita, tumepata Waheshimiwa Majaji vijana kabisa na tunaipongeza Serikali kwa sababu Waheshimiwa Majaji hawa wataweza kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 na kupata uzoefu mrefu zaidi kuliko kuteua mtu ambaye amekuwa mtu mzima na anashindwa kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Msemaji ame-challenge mamlaka ya Mheshimiwa Rais kuteua Majaji akiishutumu Tume ya Utumishi wa Mahakama aki-cite Ibara ya 113 kwamba inashindwa kumshauri vyema Mheshimiwa Rais. Naomba nimkumbushe msemaji kwamba ajiongoze katika Ibara ya 109, ibara ndogo ya (7) pamoja na ibara ndogo ya (8). Mheshimiwa Rais hafungwi na masharti katika uteuzi wa Waheshimiwa Majaji. Mheshimiwa Rais ana uwezo wa kumteua Jaji yeyote, kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika ibara ndogo ya (7) au vile atakavyoona yeye mwenyewe inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa katika taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu demokrasia. Msemaji katika ukurasa wa 15 amesema kwamba Tanzania haifuati misingi ya demokrasia iliyoainishwa katika chapter mbalimbali za Umoja wa Mataifa pamoja na Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimkumbushe Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba demokrasia siyo Coca Cola. Niseme haya kwa kuwakumbusha Watanzania wote kwamba hotuba iliyotolewa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi, hotuba hii ilitolewa tarehe 18 mwezi Februari, 1992 naomba ninukuu baadhi ya maneno ambayo Mwalimu Nyerere aliwahi kuyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alisema kwa sauti yake kwamba “Utaratibu wa kidemokrasia uliobora kwa nchi yoyote, yaani utaratibu utakaofaa kwa nchi hiyo utatofautiana wakati wowote kati ya nchi moja na nchi nyingine na hata kati ya nchi moja, utaratibu utakaofaa utatofautiana kipindi kwa kipindi. Demokrasia si bidhaa kama Coca Cola ambayo nchi moja inaweza kuagiza kwa fedha za kigeni kutoka nchi nyingine na nchi zote duniani zikawa zinakunywa Coca Cola ile ile; na ole wake nchi yoyote ambayo haina fedha za kigeni.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maneno ya Julius Kambarage Nyerere aliyowahi kuyasema wakati huo. Naomba niwakumbushe tu wenzangu kwamba demokrasia zinatofautiana, nami napenda niishauri Serikali kutoridhia mikataba ya namna hiyo kwa sababu hatuwezi kufanana. Demokrasia iliyopo Tanzania haiwezi kufanana na demokrasia iliyopo Misri pamoja na nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe ushauri. Tanzania kuna Wilaya zaidi ya 169, lakini kati ya Wilaya hizo, Wilaya 27 tu pekee ndiyo zenye Mahakama za Wilaya ambazo ziko katika mamlaka ya usikilizwaji wa mashauri katika wilaya hizo. Wilaya zaidi ya 87 zinaazima majengo mbalimbali katika maeneo husika. Pia Wilaya zaidi ya 23 wanategemea kutoka kwenye mamlaka ya wilaya za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, kwa kuwa mamlaka ya uanzishwaji wa mikoa na wilaya ni mamlaka ya Serikali, naiomba Serikali, wakati inaandaa mpango mkakati wa kuanzishwa wilaya, basi pengine wafikirie ni namna gani wanaweza kuisaidia Mahakama kwa kuanzisha majengo ya Mahakama, lakini wakati fulani inakuwa ni aibu kwa Mahakama kwenda kununua ardhi au kutafuta ardhi ya kujenga Mahakama za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali wakati inafikiria kwenda kuanzisha Mamlaka za Wilaya na Mikoa, izingatie pia kwamba ipo Mahakama ambayo imetamkwa kwenye Ibara ya 107 kwamba ni muhimu kuwepo kwa Mahakama katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kushauri ambalo nimejaribu kulieleza katika taarifa yangu, ni marekebisho ya sheria Na. 2 ya mwaka 2018 ambayo yamempa mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Naiomba sana Serikali, namwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona uwezekano wa kuleta marekebisho ili Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, basi iweze kupata proceeds ya kiasi cha fedha ambayo inaokoa wakati wa uendeshwaji wa mashauri yale ya uhujumu uchumi na mashauri mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nimelizungumza vizuri sana kwenye taarifa yangu na naomba nisisitize kwa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona uwezekano wa kuleta marekebisho ya sheria au kwa kutumia kanuni ili mwongezea mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka kuweza kupata kiasi cha fedha kidogo ambacho kinaweza kusaidia. Eneo hili, siyo tu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, hata vyombo vingine vinanufaika na maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kusisitiza ni kuhusu mlundikano wa mahabusu. Wiki kadhaa zilizopita tulimsikia Mheshimiwa Rais akitoa maelekezo kuhusu moja ya kesi za jinai ambazo mtu mmoja alishitakiwa kwa kosa la mauaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, lakini pia tuiombe sana Mahakama. Sheria Na. 2 ya mwaka 2018 imetoa maelekezo fasaha kabisa kuhusu jukwaa la haki jinai. Nami niseme kwamba Mahakama imepata bahati kubwa sana kwa kumpata Jaji Kiongozi ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka, ana ufahamu mzuri sana kwenye eneo hili. Sheria hii imeelezea utaratibu wa haki jinai. Tumwombe Mkurugenzi wa Mashtaka atumie jukwaa hili ili kupunguza mlundikano wa mahabusu Magerezani na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imezungumzwa kuhusu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mchengerwa kwa mchango wako.

MBUNGE FULANI Mwongozo, mwongozo wa Spika.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, ni aibu kubwa sana kwa taifa hili kuwa na wanasheria ambao wanafanya negotiation kwa miaka saba. Hii inadhalilisha sana wanasheria hapa nchini au wale wote ambao wapo katika tume ya kufanya negotiation kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, uliunda Kamati ya Tanzanite hapa pamoja na Kamati ya Almasi. Wabunge walitumia miezi mitatu tu kuishauri Serikali na kufanya marekebisho katika mikataba ambayo ilikuwa ni mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kupitia matakwa ya Ibara ya 63 ya Katiba na marekebisho ya sheria tuliyoyafanya mwaka jana ambayo yanalipa mamlaka Bunge kupitia mikataba mbalimbali, nikuombe unda Kamati. Kama tatizo ni mkataba kwenye suala zima la Bandari ya Bagamoyo, unda Kamati, Wabunge wako vizuri, hatutatumia miaka saba. Tunahitaji miezi miwili, miezi mitatu na tutaishauri Serikali na pengine tutawaita wahusika. Kama mkandarasi anayejenga hana uwezo, basi tutafute mkandarasi mwingine ambaye atahusika na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ikizingatiwa kwamba bandari hii ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anguko kubwa la kiuchumi la watu wa Pwani limetokana na ubovu wa miundombinu. Wewe ni shahidi, Pwani ya Kusini, kuanzia Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Kilwa miaka 700 iliyopita walikuwa na uwezo wa kutengeneza coin yao. Juzi katika Pwani ya Australia wameokota coin ambayo ilitengenezwa Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, tumekwenda pamoja Russia, tumekutana na wananchi wa Fiji, wao wanasema walitokea Rufiji, Pwani ya Tanganyika ambako ndiko kunatokea Nyamisati na maeneo mengine. Wewe ni shahidi tulikuwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Pwani siyo goigoi bali tatizo kubwa tulilonalo ni miundombinu mibovu. Iwapo miundombinu itaboreshwa, Pwani ya Kusini tutaweza kulisha Tanzania hii.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi ulikuwa Kingupila na Ngarambe, Rufiji kuna viwanja vya ndege vitatu, ndiyo wilaya pekee hapa nchini ambayo ina viwanja vya ndege vya kutosha. Mkoloni asingejenga viwanja vya ndege kama eneo hili lilikuwa halifai kiuchumi. Kule Ngarambe kuna vipepeo mamilioni ambavyo duniani hakuna lakini watalii watafikaje Ngarambe, ubovu wa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya miundombinu imefanya Warufiji washindwe kuzalisha. Tunaona ni bora tulime vyakula vitakavyotufaa wenyewe kuliko kulima vyakula vingi ambavyo inatugharimu kusafirisha kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, tarehe 4 Machi, 2017, Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete. Sitakuwa na mchango wowote iwapo nitashindwa kutaja barabara ya Nyamwage – Utete ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi.

Mheshimiwa Spika, sisi wanasheria tunatambua, zipo ahadi wakati wa kampeni, ahadi hizi wakati mwingine zinaweza zisitekelezeke kwa sababu ni ahadi ambayo mtu anaahidi ili aweze kupata. Mheshimiwa Rais aliahidi 4 Machi 2017 kwamba barabara hii itajengwa. Mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, anakuwa Rais wa kwanza kujenga barabara hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kwa kuridhia barabara hii ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Warufiji wamechoka na maneno, tumebadilisha Wabunge zaidi ya tisa, mimi ni Mbunge wa tisa ukianzia Bibi Titi Mohamed, kule ni miaka mitano mitano na Wabunge wamehukumiwa kwa sababu ya barabara hii ya Nyamwage – Utete. Unaweza ukawa ni Mbunge mzuri sana, ukawa na mchango mzuri sana kama mimi lakini kama tutashindwa kujenga barabara ya Nyamwage – Utete, hatutoki. Katika sehemu ambayo kuna siasa, kule mtu hajasoma darasa hata moja lakini ni profesa kwenye siasa, anayajua tusiyoyajua. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimpongeze Waziri kwa kuridhia lakini kusema peke yake Warufiji wamechoka na maneno. Nimesema sana, Waziri anajua, nimekwenda sana ofisini kwake na yeye ameridhia barabara hii sasa inakwenda kujengwa, Warufiji wanaomba kuona vitendo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameridhia sasa kufungua Pwani ya Kusini, tunakwenda kwenye utalii wa picha, tunakwenda kwenye mradi wa umeme wa Stiegler’s lakini huko kote hatuwezi kufika kama barabara zetu hazitaboreshwa. Barabara ya kutoka Kibiti – Mloka kama haitajengwa kiwango cha lami mradi wa Stiegler’s utachelewa sana, pengine utachukua miaka kumi kukamilika. Kwa sababu ukarabati uliofanywa ambao Mheshimiwa Waziri ameuzungumzia kwenye kitabu chake hiki, ukurasa wa 15, ukarabati ule sasa hivi kutoka Kibiti - Mkongo unatumia saa nne, kilometa 15, niombe Serikali kukarabati barabara hii.

Mheshimiwa Spika, zipo barabara ambazo iwapo zitafunguliwa Pwani kutakuwa kuchele kwelikweli. Nikuombe barabara ya Kisiju – Mkuranga; Vikindu – Vianzi; Nyamwage – Utete nimeshaisema; Ikwiriri – Mloka, Mloka – Kisarawe, Mloka – Kisaki, Utete – Ngarambe, Kibiti - Mloka pamoja na Bungu – Nyamisati. Barabara hizi zikifunguliwa Pwani tutazalisha na tutailisha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna bonde kubwa lenye ekari zaidi ya laki tano ambazo hazijalimwa; watalimaje? Kutoa mazao kutoka shambani kupeleka sokoni tunatumia saa nane au kumi. Niiombe Serikali, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amedhamiria kuifungua pwani, tuifungue pwani kwa kuboresha miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, katika ukurasa wa 15 amezungumzia barabara ya Chalinze, express way. Mheshimiwa ndugu yangu, Mheshimiwa Serukamba, amesema sana, nimuombe Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mchengerwa. Nakushukuru sana kwa mchango wako, umenikumbusha mbali, kweli nayaelewa maeneo haya.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia taarifa yetu ya mwaka lakini kipekee kabisa niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri ambao kimsingi wamejibu hoja nyingi ambazo kamati yangu ya katiba na sheria imeziibua. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mzee Mkuchika kwa kutoa darasa zuri kwa Waheshimiwa Wabunge ambalo kwa kweli limeeleweka kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mahiga kwa majibu mazuri Mheshimiwa Kairuki ambaye ametoa ufafanuzi mzuri kuhusu suala nzima la uwekezaji lakini pia Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye amefafanua kwa kina kabisa kwa hiyo hoja nyingi ambazo, zimeongelewa na Waheshimiwa tayari zimeshajibiwa na waheshimiwa Mawaziri hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima niseme kwamba tatizo kubwa ambalo nimeligundua kwa baadhi ya waheshimiwa Wabunge si hoja ya kulalamika bali ni hoja ya kutofahamu sheria na taratibu ambazo zinaongoza Taifa letu. Ni kuombe sana wewe kupitia nafasi yako umshauri Mheshimiwa Spika basi pale ambapo Wabunge wapya wanakuja katika Bunge hili kwa kupitia legislative support programme awamu ya pili, atumie fursa hiyo kutoa elimu ya ufahamu wa Sheria kwa Wabunge eneo hili iwapo litatimia vizuri hoja nyingi zitakuwa zimejibiwa na hakutakuwa na malalamiko yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimegundua kwa mfano Mheshimiwa Lema analalamikia malaka ya mkurugenzi ya mashitaka na Waheshimiwa wengine ukiangalia, Bunge hili halina mamlaka kwa Bunge hili kwa taarifa halina mamlaka ya kuoji vipengele vya Katiba Bunge hili halina mamlaka nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tatizo kubwa tulilonalo ambalo nimeligundua ni waheshimiwa Wabunge wengi kutokuwa na ufahamu wa Sheria kutokuwa na knowledge ya sheria kwahiyo pengine Mheshimiwa Spika kwa kupitia legislative support programme awamu ya pili aweze kutoa elimu ya ufahamu na nina amini iwapo eneo hili likitekelezwa basi maswali kama yale ambayo yalikuwa yanaulizwa ambayo yalikuwa yanaulizwa na Mheshimiwa Lema hayataulizwa tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na eneo la pili unapo hoji mamlaka ya DPP Mkurugenzi wa Mashitaka maana yake unaoji ibara ya 59 ya katiba zipo taratibu za kuoji katiba, zipo taratibu za kuoji sheria ambazo Bunge hili imezitunga. Kwa hiyo, kwa kutumia utaalamu ule ule ambao Mheshimiwa Spika atatusaidia Waheshimiwa Wabunge itatusaidia san asana kufahamu ni kanuni zipi ambazo kama wabunge tunapaswa kuzitumia pale ambapo tunaona sheria fulani ina mapungufu au kipengele fulani kina itilafu kidogo namna gani Mbunge anapaswa kuja na hoja hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi kama nilivyosema yamejibiwa niendelee kukumbusha tu Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Kairuki basi kwa kuwa Serikali hii ni ya Viwanda kama ambavyo imesisitizwa sana kwenye Bunge lako hili tukufu tumuombe Mheshimiwa anayetekeleza eneo hili la uwekezaji basi kuharakisha mchakato wa utengenezaji wa mapendekezo ya sheria ya uwekezaji. Sheria ya uharakishwaji ya uwezeshaji ya biashara ili sasa iwe raisi kwa utekelezaji wa yale ambayo malengo ya ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi imekuwa ikiwa meendelea kusisitiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili Mheshimiwa Jitu Soni ameniandikia akioji kuhusu utekelezaji wa sheria ya Finance Art, ya mwaka 2019 ambayo imetoa exemption kwa baaadhi ya utekelezaji wa misamaha ya VAT katika eneo la Serikali Kuu na Serikali za Mitaa nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha basi eneo hili liweze kushughulikiwa kwa haraka ili kuondoa mapungufu yaliyopo kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu vibali vya kazi ambao kimsingi Mheshimiwa Jenistar Waziri wa Nchi ametoa ufafanunuzi wa kina kabisa. Lakini Mheshimiwa Ruth Mollel amesisitiza kwa kina sana kuhusu ucheleweshwaji wa mashauri, nimuombe Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwa jupo hapa kusisitiza mahakimu wetu wote nchini na kutumia kifungu cha 225 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ili kuweza kuharakisha katika mashauri ambayo yanachelewa ili mashauri yale ambayo yamevuka siku 60 basi kuona uwezekano wa mahakimu kuyaondoa mashauri yale ambayo iwapo Serikali basi itaona kwamba iko tayari kuendelea na mashitaka hayo inaweza kuleta kwa kupitia kifungu hicho hicho kifungu kidogo cha tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo limesisitizwa kwa kina ni kuhusu mamlaka ya mkurugenzi wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa niwaombe waheshimiwa Wabunge watambue kwamba katiba yetu lakini pia sheria ya kupambana na kuzuia rushwa sura ya 7 sheria hii inatoa ufafanuzi kifungu cha 7 kinatoa ufafanuzi wa kazi ambazo taasisi hii inafanya kwa kina kabisa sina haya ya kurudia niwaombe Waheshimiwa Wabunge tujielekeze pengine tukisoma sheria hii maswali kama haya ambayo ni mepesi yanaweza yasiulizwe kwenye Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo Mheshimiwa Lema alioji ni kuhusu mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuliondoa shitaka pale ambapo anapoona yeye anapendezwa nalo kuliondoa na kulirejesha wakati wowote niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba tukisoma mwenendo wa makosa ya jinai kifungu cha 91 kinampa mamlaka mkurugenzi wa mashitaka na mamlaka yake hayahojiwi sehemu yoyote ukisoma Ibara ya 59 ya katiba mamlaka ya mkurugenzi wa mashitaka haojiwi wakati wowote pale ambapo wataona inafaa anauwezo wa kuliondoa shitaka wakati wowote kabla ya hukumu kutolewa na mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili jukumu ni la mkurugenzi wa mashitaka na nijukumu la Bunge hili iwapo inaona kwamba kipengele hiki hakifai basi Bunge hili linaweza kujiongeza ili kuona uwezekano wa kurekebisha kifungu hiki. Lakini kwa sasa hatuna mamlaka ya kuhoji mamlaka ya mkurugenzi wa mashitaka ambaye yanapatikana katika ibara ya 59 ya katiba yetu lakini mamlaka ya kufuta shitaka wakati wowote kabla ya hukumu kutolewa yapo kwa mujibu ya kifungu 91 cha sheria hii kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge kujielekeza katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hoja nyingi zimejibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na mimi naomba kutoa hoja kwa taarifa yangu kama ambavyo nimesema hapo ahsante.

MHE. YAHAYA Y. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania atakubaliana nami kwamba Taifa hili kwa miaka mingi sana lilihitaji kuwa na Rais mwenye kufanya maamuzi, kutoa matamko ambayo kesho na kesho kutwa yatafanyiwa kazi na kuwa sheria. Kwa hiyo, sisi wananchi tunaotoka kwenye eneo la Pwani ya Kusini tunapendekeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa tamko la kuamua sasa eneo hili la Selous kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, huu ni utaratibu mzuri kabisa wa kizalendo wa kuwaenzi wapigania uhuru akina Mwalimu Nyerere, lakini pia ninaamini huko tunakokwenda mbele katika eneo letu la Rufiji, basi kutapatikana eneo ambalo pengine tutaliita Bibi Titi Mohamed ambaye yeye alikuwa ni Mbunge wetu wa kwanza kule Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi wananchi wa Pwani ya Kusini tunaamini kabisa kwamba kwa miaka mingi sana tulipuuzwa na hili lilitokana na mgawanyo hafifu wa pato la Taifa na ilisababisha kuwepo kwa umasikini wa hali ya juu, lakini Watanzania na wananchi wote wa Tanzania pamoja na dunia nzima inatambua uwepo wa utajiri mkubwa sana katika eneo la Pwani ya Kusini. Kwa hiyo, sisi wananchi wa Rufiji tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini lazima nichukue fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri wa Maliasili na Utalii anachapa kazi kweli kweli, kwa hiyo, sisi tunampongeza sana na maamuzi haya ni maamuzi sahihi, lakini tunatambua vipo vikwazo viwili pengine katika kuelekea uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere yako mambo ambayo pengine ni lazima tuyazingiatie na tuyatekeleze sasa.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba miaka ya 2006 Serikali iliamua kuhamisha mifugo kutoka Hifadhi ya Bonde la Ihefu na kupeleka katika eneo la Kusini pamoja na Pwani kule Rufiji na kuendelea Kilwa na Mtwara. Tatizo la uwepo wa mifugo katika eneo la Hifadhi hii ya Mwalimu Nyerere litakuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa kukua kwa eneo hili la hifadhi.

Mheshimiwa Spika, tuiombe Wizara sasa kufanya maamuzi magumu, maamuzi sahihi. Taifa hili lina eneo kubwa sana, Tanzania hatupaswi kugombana kati ya wakulima na wafugaji, lakini pia hata wafugaji wanapaswa kuwepo katika maeneo yaliyoidhinishwa na Serikali. Tuiombe Serikali kufanya maamuzi ya makusudi kabisa kuondoa mifugo kwenye eneo hili la Hifadhi ya Mwalimu Nyerere kuanzia Rufiji katika Kata za Mkongo, Ikwiriri na kuendelea; maeneo haya ni maeneo yote ambayo tunayategemea sasa baada ya kuanzishwa kwa Hifadhi hii ya Mwalimu Nyerere. Uwepo wa mifugo katika eneo letu kutaathiri hata uanzishwaji au ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme pale, Bwawa la mwalimu Nyerere.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi ya kuchangia siku ya leo na nilifanya tafiti za kutosha kuhusiana na marekebisho ya muswada huu hususani suala zima la tafsiri ambazo hazipatikani katika marekebisho ya sheria hii hata sheria mama hususani tafsiri kwa mfano local firms ambayo haipo katika sheria hii inayorekebishwa na hivyo wakati mwingine italeta tabu hapo baadae. Lakini pia nimeona Ibara ya 11 inayopendekeza marekebisho katika kifungu cha 31 ili kuondoa sharti la kubainisha katika kanuni la kusimamia ununuzi Halmashauri yaani Madiwani sasa kuondolewa katika usimamizi wa manunuzi yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia kwamba siku ya leo nina majonzi na kwamba kwa kuwa wananchi wangu wamekatizwa haki ya kuishi kwa mujibu wa Ibara ya 14 lakini pia kwa kuwa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatamka kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Ibara ya 9 kwamba lengo kuu la Serikali itakuwa ni ustawi kwa wananchi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, majonzi haya yamenifanya nishindwe kuchangia siku ya leo na nitaomba nichangie kwa maandishi ili nishirikiane na ndugu zangu wa Rufiji ambao wameuwawa ikizingatiwa kwamba mmoja wa mtu aliyefariki ni ndugu bwana Ngayonga.
Kwa hiyo, naomba kwamba yale mapendekezo yaliyoletwa na Serikali mimi niaafikiana nayo na kwa siku ya leo kwa kuwa nina majonzi nitashindwa kuchangia, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa mambo machache kusema kwamba, Tanzania is a sovereign state. Tanzania ni nchi huru na Taifa lolote kuwa huru kuna mambo mawili lazima yatimie, jambo la kwanza ni Taifa hilo kuwa huru kutunga sheria zake za ndani na kufanya maamuzi ya ndani bila kuingiliwa na Taifa lolote. Jambo la pili, Taifa lolote kuwa huru ni kuamua kufanya siasa za nje bila kuingiliwa na Taifa lolote. Ndiyo maana tunasema Tanzania is a sovereign state.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeamua nianze kusema haya kwa sababu miezi michache iliyopita tuliona clip iliyokuwa inasambaa kutoka kule Ujerumani ikiwaonesha Wabunge wa kutoka Ujerumani wakituambia Watanzania tusimamishe utekelezaji wa mradi wa Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni upungufu wa fikra tuseme na pengine wenzetu wanapaswa kutambua kwamba, Taifa lolote linapokuwa huru, linakuwa huru kutunga mambo yake na kufanya mambo yake bila kuingiliwa na Taifa lolote. Kwa namna hiyo katika clip ile inawaonesha Wabunge wa Ujerumani wakisema kwamba, wao ni koloni la Tanzania wakiamini kwamba bado ni koloni lao. Niiombe Serikali kufanya maamuzi yafuatayo:

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Serikali ifanye tathmini ya athari za ukoloni hapa nchini, ukoloni ulituathiri nchi yetu kwa kiwango gani? Wakati huo tunatambua kwamba Ulaya imejengwa na Afrika kupitia raw materials zilizotoka hapa Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Tuombe Serikali ifanye tathmini ya athari za ukoloni, lakini baada ya kufanya tathmini ya athari za ukoloni Serikali ifungue kesi katika Mahakama ya Kimataifa kudai fidia zinazotokana na ukoloni.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo, Kenya imefanya hivyo na Mahakama za Kimataifa zimeamuru wenzetu waweze kulipwa fidia kutokana na athari za ukoloni, niliona nianze hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vita ya Dunia Tanzania tuliachwa chini ya League of Nations, tuliachwa chini ya Waingereza, lakini tunatambua kwamba, Waingereza hawakufanya lolote kwa Taifa letu, walitufanya Tanzania tuendelee kudumaa kiuchumi. Serikali pia, ikiwezekana ifanye tathmini ya athari zozote zilizofanywa na Taifa la Uingereza ili tuweze kufungua mashtaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya kudai fidia zilizotokana na athari hizi za ukoloni ambazo zimefanywa na wenzetu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi lazima niipongeze sana Serikali lakini pili nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kudhamiria kutekeleza Mradi wa Stiegler’s Gorge. Mradi huu ni nembo (symbol) ya Taifa letu. Mwalimu Nyerere mwaka 1956 wakati wa kupigania uhuru, wakati ule alivyokuwa akija Rufiji alidhamiria kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa. Wamepita viongozi wengi wa nchi hii, Marais wengi wamepita, maamuzi yaliyofanywa na Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ni maamuzi magumu na ya kizalendo ya kwenda kutekeleza mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unakwenda kuongeza pato la Watanzania. Tukiweza kuzalisha umeme megawatts 2,100 inamaanisha kwamba viwanda vyetu vyote vitaweza kupata umeme wa kutosha. Tutambue kwamba umeme kutokana na mradi huu utakwenda kuuzwa kwa bei ya chini kabisa. Ni kiongozi gani ambaye anaweza kukubali kufanya maamuzi haya magumu, ni Rais peke yake aliyedhamiria kuwakomboa Watanzania. Kwa hyo, sisi tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami lazima niseme sisi watu wa Rufiji tumetunza vyanzo vile kwa muda mrefu sana. Kupitia kwa Mbunge wao Mchengerwa, mara kadhaa nimeleta hoja hapa kabla hata Serikali kuamua kufanya maamuzi haya. Lazima tukiri kwamba huu ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba wakati Serikali inakwenda kutekeleza mradi huu, tuwakumbuke watu wa Rufiji kwa sababu zipo kelele za wananchi wetu wa Rufiji kwamba kwenye ajira hawajachukuliwa wengi. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwamba wakati sasa tunakwenda kutekeleza mradi huu, kipaumbele cha kwanza kabisa cha ajira kiwe ni kwa wananchi wetu wa kutoka Rufiji kwa sababu ndiyo wameutunza mradi huu kwa miaka mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mradi huu kutengenezwa utaendelea kubaki Rufiji na ndiyo maana tunasema kwamba Warufiji tuwaangalie kwanza kwa sababu wao ndiyo wanautunza mradi huu lakini kupitia Mbunge wao, ndiyo tulileta hoja hapa kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa. Yako maeneo yatahitaji uboreshaji wa miundombinu kupitia kwenye mradi huu, tunaipongeza sana Serikali imejenga barabara na madaraja. Tunaomba sasa barabara hizi ambazo zimejengwa na Serikali zijengwe kwa kiwango cha lami. Ili mradi huu utekelezwe kwa miaka mitatu anayoitaka Mheshimiwa Rais, kipande cha kutoka Kibiti - Mkongo ni kibovu sana, tunaiomba Serikali kuhakikisha kwamba eneo hilo linaboreshwa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutoa mchango wa namna gani tunaweza kuongeza kodi, ipo kodi inasahaulika. Pengine Mheshimiwa Waziri wa Fedha akisimama hapa atuambie ipo kodi ambayo kimsingi inawekwa kwa ajili ya ku-discourage consumption. Kodi hii mara nyingi tunaita excise duty au sin tax. Kodi ambayo inatakiwa itozwe kwenye sigara na pombe lakini kodi hii imesahaulika kwa muda mrefu. Serikali inatumia mabilioni ya fedha kutibu watu TB lakini haijafanya nyongeza yoyote ya kodi kwenye sigara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuandika andiko moja 20 iliyopita kuhusiana na makusanyo ya kodi ya sin tax. Tuombe Mheshimiwa Waziri aangalie Watanzania wanaathirika sana na sigara, Serikali inapaswa ku-discourage consumption kwa kuongeza kodi hii ili Watanzania waache kutumia sigara. Pia hata kodi kwenye pombe Serikali iangalie uwezekano ili iweze kuongeza mapato lakini pia ku- discourage consumption ya vitu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tumekuwa tukiangalia sana madini ya dhahabu lakini yapo madini mengine ambayo yanatumika kwenye viwanda, Serikali imesahau sana. Tumuombe Waziri wa Fedha atakaposimama hapa atuambie Serikali imefikia hatua gani kuhusu kuimarisha na kuboresha mchakato wa matumizi ya madini ya soda ash ambayo yanapatikana kule Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya yana fedha nyingi sana kuliko hata dhahabu lakini Serikali imekaa kimya, haizungumzia jambo lolote kwenye eneo hili. Tunatambua kwamba Wajapan walitoa fedha nyingi sana na fedha hizi walipewa watu wa NDC. Waziri wa Fedha akisimama hapa atuambie fedha hizi zimekwenda wapi na kama kuna wanaohusika kuzila fedha hizi, basi Serikali ichukue hatua kali kwa wahusika wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua madini haya (industrial minerals) ndiyo yananufaisha nchi nyingi sana. Bajeti ya Marekani inategemea madini ya viwandani. Kwa hiyo, niombe Serikali kuzingatia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa huu ni mchango wangu wa mwisho kwa Wizara hii ya TAMISEMI, hususan kwa Bunge hili la Kumi na Moja, ninaomba nisajili mchango wangu wa ushawishi wa leo, ushawishi wa kesho mwezi Oktoba na kwa matumizi ya vijana wa karne hii na karne inayokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya ujenzi wa Tanzania mpya imefanywa na Mawaziri wengi. Lakini kipekee kabisa Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetimiza ndoto za ujenzi wa taifa jipya kifkra na kimtazamo. Wizara hii imefanikisha ujenzi wa Tanzania katika Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya, Sekta ya Miundombinu na katika maeneo mbalimbali. Wizara hii haikuijenga tu Tanzania, haikujenga tu Taifa, bali imejenga na imeimarisha mitazamo chanya ya kifikra na kimantiki ya wazalendo wapya hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuona Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kuwa ni kiongozi wa pili wa Taifa letu hili ambaye amefanikisha na anafanikiwa sasa kuzalisha wazalendo wapya hapa nchini. Na hii inajidhihirisha kwa mitazamo yake ya kielimu kama mwalimu, mitazamo yake ya kifkra kama mwanafalsafa wa Hapa Kazi Tu, na anatendea haki mitazamo yake hii ya Hapa Kazi Tu kwa kuwataka Watanzania wote kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu ni kiongozi mwenye misimamo isiyoyumba katika kufanya maamuzi. Na katika wazalendo ambao ninawaona Mheshimiwa Rais amefanikiwa kuwatengeneza, si mwingine bali ni wengi isipokuwa kipekee nimtaje Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Selemani Jafo. Amekuwa mkweli, hodari na mchapakazi mwenye kufika kila eneo, hasubiri Mheshimiwa Rais anapokwenda, yeye anatangulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunampongeza sana na kumtakia kila la heri katika wajibu wake. Na tunaamini wananchi wa Kisarawe watamchagua kwa wingi sana na pia hakutakuwa na ushindani katika jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, pamoja na mapambano tunayoendelea nayo ya Ugonjwa huu wa Corona, niombe sasa Ofisi hii ya Rais, TAMISEMI kutoa maelekezo ya makini kabisa kwa watendaji wote wa kata na vitongoji kutoa maelekezo kwa wenyeviti wote wa vijiji na vitongoji pamoja na wenyeviti wa mitaa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 9 ya Katiba yetu ambayo inatambua misingi ya uendeshaji wa nchi yetu kwamba ni misingi ya kijamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa viongozi wote hawa ofisi ya Rais TAMISEMI sasa itoe maelekezo kwa kuwataka viongozi hawa kufanya kazi kama mchwa ili kuweza kutambua katika maeneo yao wale wageni wanaoingia, wenyeji waliopo, wagonjwa waliopo, lakini pia kutambua wale wahalifu katika maeneo yao. Hii ni misingi ambayo tunaitambua nchi yetu inafuata iliyopo katika Ibara ya 9 ya Katiba yetu, misingi ya ujamaa na kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi na shukrani sana kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa namna ya kipekee kabisa Waziri wa TAMISEMI ametambua kwamba Rufiji ilizaliwa miaka 600 iliyopita, na kwa kutambua hilo amegundua kwamba wafanyakazi wa Halmashauri ya Rufiji wanafanya kazi katika jengo lililojengwa mwaka 1889, akaona ni bora wafanyakazi hawa awafikirie na kukubali kutoa fedha za ujenzi wa jengo jipya la Halmashari ya Wilaya ya Rufiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakupongeza sana na tukuombe Mheshimiwa Waziri sasa wataalam wako wanaoandaa michoro na BOQ kutuharakishia sana kwa sababu wananchi wa Rufiji wana kiu kubwa ya kupata jengo jipya kutokana na jengo lao hili kudumu zaidi ya miaka 100 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hiyo, niombe sasa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Rufiji kwa kuwa hospitali iliyopo ilijengwa mwaka 1960 ikihudumia Wilaya za Kilwa na Rufiji pamoja na wilaya ziliopo karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na athari za mafuriko ambayo Rufiji imepata nimuombe Mheshimiwa Waziri Jafo, miaka kadhaa iliyopita niliomba fedha za ununuzi wa boti, mafuriko yametuletea shida kiasi kwamba hatukuwa na boti katika maeneo yetu. Kwa hiyo, kuna fedha Mheshimiwa Waziri alishatoa shilingi milioni 200, kwa bahati mbaya sana fedha hizi zilirudishwa tena TAMISEMI. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufunga hapa watangazie wananchi wa Rufiji kwamba sasa ile milioni 200 umeirudisha Rufiji ili tuweze kununua boti kuwasaidia wananchi wetu ambao watapata maafa ya mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, athari za mafuriko zimekumba baadhi ya vituo vyetu vya afya ikiwa ni pamoja na Kituo cha Afya cha Muhoro. Muhoro kuna watu takribani 25,000 lakini sasa hivi wanakosa huduma za afya kutokana na athari kubwa ya mafuriko ambayo tumeipata. Nikuombe Mheshimiwa Waziri ukiwa unafunga hapa sasa utuambie zile fedha za dharura zilizopo katika Wizara yako muweze kuzitenga kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Muhoro pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ngorongo ambao leo hii hawawezi kwenda Kata ya Kipugira kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara ya TARURA, barabara ya kutoka Utete kwenda Ngarambe. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa kukarabati barabara hii. Barabara hii iwapo itakarabatiwa basi itawezesha mizigo inayotoka kule Dangote inayokwenda kwenye mradi wa Rufiji kwa kuwa mradi huu ni kipaumbele cha Mheshimiwa Rais namba mbili kabisa baada ya Mradi wa SGR, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kutambua kazi kubwa Mheshimiwa Waziri anayofanya, tunatambua leo hii anajenga Daraja la Mbuchi kule Muhoro. Lakini anapojenga Daraja la Mbuchi pale Muhoro mafuriko yamekomba Daraja la Muhoro kwa hiyo nimuombe kwa fedha zile anazoanza kule Mbuchi aanze sasa kujenga Daraja la Muhoro ili wananchi waweze kupita Muhoro waweze kwenda Mbuchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunatambua kiasi cha fedha nyingi ambacho Wizara yake imetoa katika eneo la elimu, eneo la afya, zaidi ya shilingi bilioni tano imeingia katika eneo la elimu na eneo la afya. Kwa Mtanzania asiyetambua mchango huu atakuwa na matatizo kichwani mwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili, nianze kwa kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Rufiji kwa kunichagua kwa kishindo na kukomboa Kata zote 13 na kupata ushindi ambao haujapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango tunaoujadili leo, una mambo makuu matatu. Jambo kubwa la kwanza ni utawala bora; ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; na uchapa kazi kufikia malengo ya Mpango uliokusudiwa. Hizi siyo ndoto pekee za Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, hizi zilikuwa ni ndoto za Mwasisi wa Taifa hili, Rais wetu wa Awamu ya Kwanza, ambapo yeye katika fikra zake aliamua kuziweka fikra zake katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma Ibara ya 9 ya Katiba, inazungumza misingi ya kwenda kuwasaidia Watanzania; kumsaidia mwananchi mmoja mmoja na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi. Kwa hiyo, haya yote yanayozungumzwa leo na Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, yana msingi wake katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwasisi wetu wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ibara ya 9(e) inazungumzia Watanzania kwenda kufanya kazi. Hili ndiyo jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais analisisitiza leo kuwataka Watanzania kufanya kazi ili kwenda kutimiza ndoto za Mpango wa Maendeleo ambao tunaukusudia. Haya pia siyo mageni. Mambo haya tayari yana msingi wake, yalianzishwa na Mwalimu Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Mpango wa Taifa wa Maendeleo baada ya uhuru uliotolewa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1964 mpaka mwaka 1969 na Mpango wa Pili wa Maendeleo uliosomwa mwaka 1969 mpaka mwaka 1974, haya yote yalidhamiria kwenda kukomboa Watanzania. Ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanda na mambo mengi makubwa, Mwalimu Nyerere dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha Tanzania yote inafikika. Wakati ule nchi yetu miundombinu ilikuwa ni square kilometa 86,000, wakati huo Tanzania ilikuwa na watu milioni 9 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujiulize, changamoto zilizopelekea ni kwa nini tulishindwa kufikia malengo ambayo Mwalimu aliyakusudia? Hapa tunajikita katika Watafiti wa kiuchumi wanavyosema. Tunaye mtafiti mmoja anaitwa Daron Acemoglu pamoja na James Robinson, katika kitabu chao cha tafiti kilichokuwa kinazungumza ni kwa nini mataifa yanashindwa kujiendeleza, waliwahi kusema: “Mataifa mengi yanashindwa kwa sababu hayana strong institutions and vigilance. Hayana taasisi zilizo imara, lakini siyo taasisi kuwa imara peke yake, taasisi ambazo zinaweza kujua changamoto tulizonazo na kesho tutafikia wapi? Kama tutashindwa katikati, ni jambo gani tutafanya ili tuweze kufika kule tunakotaka kufika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo tunapoiangalia bajeti ya Serikali na tunagundua kwamba Bajeti ya Serikali ya 2019/2020 tulikusanya asilimia 92.8, lakini mwaka 2020/2021 makusanyo ni asilimia 88. Ziko sababu nyingi ambazo wachumi wetu, tungekuwa na taasisi imara wangeweza kutuambia, ni kwa nini tumeshindwa kufikia malengo yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo lilijadiliwa na Bwana Acemoglu, alisema: “The quality of political and economic institutions.” Ni lazima tuwe na taasisi za kisiasa zinazozingatia uchumi, lakini pia tuwe na taasisi za kiuchumi ambazo ni imara, zinaweza ku-focus na kujua Tanzania tunataka kwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote lazima tuangalie, bajeti yetu leo hii, dhamira yetu ni kukusanya shilingi trilioni 26, je, Taifa letu tutaweza kukusanya shilingi trilioni 13? Kwa sababu tayari tumepanga shilingi trilioni 10 itumike katika miradi ya maendeleo na fedha hizi lazima zitokane na makusanyo ya ndani, tunawezaje kufika huko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimekuwepo kelele nyingi sana kuhusu chombo chetu cha TRA namna kinavyokusanya na namna kinavyoshindwa kuwa imara na kutumia taasisi nyingine. Ili tuweze kufanikiwa yapo mambo mawili lazima tuyafanye. Jambo la kwanza, ni lazima tuzipe immunity institutions zetu ili ziweze kujitosheleza, ziwe imara na ziweze kufanya maamuzi kwa niaba ya Watanzania ili tuifikie Tanzania mpya tunayoitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo Bunge linaweza kufanya ni kuitaka Serikali kuleta mbele ya Bunge lako Tukufu vipaumbele vya Taifa vikionyesha flagship projects. Zile project zote ambazo ni kubwa na za kimkakati, basi Bunge liiagize Serikali na litoe Azimio la Kibunge ambapo hatatokea mtu yeyote kuweza kubadilisha Maazimio ya Bunge ili tuweze kuainisha miradi ya kimkakati, vipaumbele vya Taifa letu na ni wapi tunataka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amefanya vizuri sana, amekuwa na mpango mzuri sana wa kuipeleka Tanzania mbele, lakini hatujui kesho atakuja nani? Kama Bunge likitoa Azimio na likiungwa mkono na Wabunge zaidi ya robo tatu, kwamba tunataka miradi ya maji ikamilike, tunataka miradi ya mwendokasi wa treni ikamilike, hakuna kiongozi mwingine atakayeweza kuja kubadilisha haya kwa sababu tayari Bunge limeshatoa Azimio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono hoja hii, lakini tuiombe Serikali kama siyo Bunge hili, Bunge linalokuja, ilete ndani ya Bunge vipaumbele, miradi ya kimkakati ili Bunge tuamue robo tatu ya Wabunge kuikubali. Asije Kiongozi yeyote baada ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli kwenda kuipinga miradi hii ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati kwa maoni na maelekezo ambayo wametupatia Wizara yetu ya TAMISEMI. Lazima nikiri kwamba lengo la Serikali yoyote duniani ni ustawi wa wananchi wake, na hii ndiyo sababu Wizara yetu ya TAMISEMI imedhamiria kuiweka Wizara mikononi mwa wananchi. Tunaposema tunaiweka Wizara mikononi mwa mwananchi, maana yake tunawapa wananchi mamlaka ya kutukagua na kuturekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi huu ni msingi ambao umepatikana katika Ibara ya 8 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 9 na kuendelea mpaka Ibara ya 21, ambayo imewazungumzia wawakilishi wa wananchi katika maeneo yetu. Sauti ya wananchi inawakilishwa na Madiwani na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Bunge hili, Kamati imepewa mamlaka ya kuwawakilisha Waheshimiwa Wabunge wengine. Kwa hiyo, sisi kama Wizara lazima nikiri kwamba tumepokea maelekezo ya Kamati. Inawezekana maelekezo mengi huko nyuma hayakufanyiwa kazi, lakini siyo wakati wangu. Naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba kazi hii kubwa ambayo Kamati imefanya, sisi Wizara tutahakikisha kwamba yale maelekozo ambayo Kamati imetoa, kwetu sisi Wizara tunakwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na wenzangu wote kwamba ule utendaji wa kimazoea sasa tunauacha (business as usual) tunauacha. Ili tuweze kuwawakilisha wananchi vyema kama ambavyo nimesema nchi ni ya wananchi, wawakilishi wa wananchi ndio hawa Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani kwa misingi ya Ibara ya 21 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, tutahakikisha sheria zetu, kanuni zetu zinaenda sambamba na tafsiri iliyotolewa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, tutahakikisha ile misingi na mifumo ya utungwaji wa kanuni ambayo pengine huko nyuma zilikuwa haziendi vizuri, tutakwenda kuziboresha ili kanuni zetu zote zinazotungwa ziwe ni zile ambazo zinaangalia maslahi ya wananchi wetu katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme mbele ya Bunge lako tukufu kwamba mapendekezo ya Kamati ambayo yametolewa yana msingi wake, kwa sababu Kamati hii ndiyo Kamati ambayo inatoa sauti ya Wabunge wote ndani ya Bunge hili Tukufu. Kwa hiyo, tutakwenda kuyafanyia kazi mapendekezo yote ya Kamati na niwaombe Waheshimiwa Wabunge wajenge matumaini. Tutakwenda kuboresha mifumo yetu ya utungwaji wa kanuni zetu, na pia tutaboresha mifumo yetu ya utungwaji wa sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshawaeleza watendaji katika Wizara hii, kila moja wetu kijipanga hasa kwa sababu ni lazima tulinde maslahi ya wananchi wetu. Ninaposema tunakwenda kulinda maslahi ya wananchi wetu, ni kwenda kutunga kanuni na sheria ambazo zinaangalia maslahi ya wananchi wetu katika maeneo yetu mbalilmbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba ninaipongeza Kamati na ninaunga mkono hoja ambazo Kamati imetoa na sisi kama Wizara tutakwenda kujipanga vizuri, mimi na wasaidizi wangu, kuhakikisha kwamba yale mapendekezo ya Kamati yaliyotolewa kwa Wizara yetu hii ya TAMISEMI, ambayo ni Wizara ya wananchi, na kwa kuwa tayari nimeshatoa maelekezo kuirejesha Wizara hii kwa wananchi, tutakwenda kulinda maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha kwamba kanuni zinazotungwa ni kanuni ambazo zinalenga kulinda na kutetea ustawi wa wananchi katika maeneo yetu yote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika misingi ya sheria, tutajikita katika kuhakikisha kwamba sheria zetu zinaendana na tafsiri ya Katiba kama ambavyo Katiba imefafanua.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja ya Kuazimia Kuwahamisha Maafisa Ushirika katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Maafisa Ugani chini ya Wizara ya Kilimo
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nitambue dhana iliyoibuliwa yenye dhamira ya kuchangamsha fikra za maamuzi mbalimbali katika Taifa letu na nikushukuru kwa kuridhi dhana hii kujadiliwa. Kama ambavyo kaka yangu aliyekaa muda huu amezungumza hapa. Nchi hii ni ya wananchi, msingi wa Serikali katika kuamua mambo yoyote ni lazima yaamuliwe na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Simbachawene amezungumzia Ibara ya 8 lakini ukienda Ibara ya 21 inazungumza misingi ya maamuzi mbalimbali ambayo inawashirikisha wananchi kupitia wawakilishi wa wananchi, Wabunge na Madiwani.

Mheshimiwa Spika, swali la kujiuliza hapa ni utekelezaji wa wajibu wa kila mmoja wetu. Hata ukiwasikiliza Waheshimiwa Wabunge, malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge ni namna gani wale walioko kule chini wanashindwa kutekeleza wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhana ya ugatuzi wa madaraka huu ni msingi ambao wa Baba wa Taifa ameturithisha kabla ya kuondoka kwake. Imeingizwa kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 145 ambayo Mheshimiwa Sendeka ameizungumza hapa. Huko tunakoelekea leo pengine tuna miezi 11 twende kwenye chaguzi na pengine baada ya mwaka mmoja tuna Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Spika, swali la kujiuliza hivi leo, maeneo mengi ambayo yameondolewa kutoka TAMISEMI, kutoka kwenye Serikali kule chini yanatuletea matatizo makubwa sana. Hasa ukiangalia kwa mfano tuna migogoro mingi sana ya ardhi eneo hili. Tumekwisha kaa tumezungumza na Waziri wa Ardhi tumekubaliana kwamba hili pia tulipitie na tuone uwezekano wa kuirudisha TAMISEMI. Leo hii… (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, leo hii…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Godwin Kunambi.

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante namuunga mkono Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Kimsingi sio tu kupoka madaraka kwa wananchi kinachokwenda kutokea ni failure ya hawa wanaopelekwa kwenye Wizara ya Kisekta, mfano mzuri Wizara ya Ardhi leo hii hatutatatua migogoro ya ardhi kamwe nchi hii kama hatujarejesha watumishi wa ardhi TAMISEMI, ahsante.

SPIKA: Sina uhakika nimesikia vizuri, umesema nchi hii hatutatatua?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nasema hivi, naomba kurejea; nchi hii kama kuna kosa tulifanya ni kutwaa watumishi wa ardhi kutoka TAMISEMI kwenda Wizara ya Ardhi ambayo ni ya Kisekta.

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mchengerwa unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa hii kwa mikono miwili, ni makosa makubwa yalifanyika katika eneo hili na tumekubaliana na Waziri wa Ardhi kwamba suala hili tunakwenda kulifanyia kazi ili hawa watu waje kwangu niwashughulikie vizuri. (Makofi)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunti Majala.

TAARIFA

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nataka nimpe mzungumzaji anyezungumza kwamba hawa maafisa ardhi walikuwa TAMISEMI tangu enzi hizo na migogoro ilikuwa imekithiri. Wakati huo kumbuka wewe ndiyo ulikuwa Wizara ni hiyo hiyo moja. Vijiji na vitongoji mnapanga ninyi lakini mkitoka hapo suala la ardhi wako kwako mkienda mnawaambia wananchi wamevamia na ninyi ndiyo mlikuwa mnapima mipaka. Kwa hiyo, hiyo haiwezekani kwamba hao watu kutolewa kupelekwa kwenye Wizara ya Kisekta eti mmepunguza migogoro. Hamjapunguza wala hamja… nakushukuru.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa unapokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakuomba unilindie muda, ni vema…

SPIKA: Mheshimiwa ngoja, muda wa taarifa ni sehemu ya muda wako kwa sababu anaboresha mchango wako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni vema Waheshimiwa Wabunge wakatofautisha masuala ya kiutawala na masuala ya kisera lazima tutofautishe. Lakini… (Makofi)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, taarifa niko hapa.

SPIKA: SPIKA: Hii ni taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Miraji Mtaturu.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba siku zote chakula ili kinoge ni lazima kiwe na chumvi. Kilimo kiko kwa wananchi wa chini kabisa kwenye kitongoji utakapokiondoa kilimo kwa maana ya afisa ushirika ukamtoa pale kijijini kilimo kitakufa. Kwa hiyo, naomba nimpe taarifa mtoa taarifa kwamba maafisa ushirika wabaki katika eneo la halmashauri ili wasimamie vizuri kilimo chetu. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa Sekunde 30 kengele ya pili imeshagongwa, samahani kengele imeshagongwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa lakini jambo hili ni kubwa na niwaombe pamoja na dhana njema ya kulileta hapa Bungeni watuachie Serikali tukalijadili kwa kina na tutaangalia sehemu yenye mapungufu tutakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, juzi tulichukua maamuzi ya kuwaondoa baadhi ya watendaji kule Mbeya Mjini walioshiriki kwenye ubadhilifu fulani baada ya maamuzi kutolewa na madiwani lakini kama hao pia wangeenda kwenye sekta husika.

SPIKA: Hapo nakuongezea sekunde 30, Waheshimiwa Wabunge humu ndani si huwa tunazungumzia watu wanaofanya kazi vibaya na vizuri? Sasa kama Mkurugenzi wangu wa jiji anafanya kazi vizuri msifie kidogo Mheshimiwa Waziri. (Kicheko/Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge pamoja na nia njema ya kuleta jambo hili. Tukumbuke kwamba tuna changuzi mbele yetu, siku chache tuna chaguzi mbele yetu. Nawaomba sana mridhie jambo hili mliache kama lilivyo ili tuweze kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba tunawasimamia hawa vema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana kabisa kwamba jambo la usimamizi lakini nichukue fursa hii kumpongeza mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kwa kazi kubwa na kazi nzuri na niwaombe wakurugenzi wengine kwenye maeneo mbalimbali wachukue maamuzi kama haya itatusaidia sana Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba miradi yetu inatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumuomba mtoa hoja aridhie jambo hili linbaki ndani ya Serikali na sisi tutakaa na Wizara ya Kilimo tuone ni namna gani tunaweza ku…

Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Muda wake umekwisha, Mheshimiwa Waziri weka nukta hapo. Muda umekwisha Mheshimiwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru ahsante.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wandengereko wote duniani pamoja na Warufiji wanaoishi kule Rufiji, naomba nichangie mambo machache. Nikiwa kama Mwenyekiti, tayari nilishawasilisha baadhi ya mambo ya msingi, lakini naona nitakuwa siwatendei haki Warufiji iwapo sitazungumza mambo kutokana na muswada huu na ni namna gani Muswada huu utawasaidia Wandengereko wa Rufiji pamoja na makabila mengine wakiwepo Wamakonde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kutoa pole kwa viongozi wa Serikali ambao wamepata ajali siku ya jana katika Jimbo langu la Rufiji akiwemo Mkuu wetu wa Wilaya Mheshimiwa Juma Njwayo pamoja na DAS wetu ambaye leo hii yupo pale Muhimbili anapata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu wa upatikanaji wa taarifa kama ambavyo umeelezewa na wenzangu, muswada huu ni muhimu sana kwa nchi yetu, ukizingatia kwamba ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa ikijaribu kupitia hili na lile ili muswada huu uweze kuwasilishwa kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba muswada huu uliwahi kuwasilishwa katika Bunge lililopita na tatizo kubwa la muswada huu wakati ule ni kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge na watu mbalimbali walidhani kwamba ni Muswada wa Habari badala ya Muswada wa Upatikanaji wa Taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwamba muswada huu unaleta sheria hii ya upatikanaji wa taarifa kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa zilizopo chini ya himaya ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake. Niseme tu kwamba muswada huu unatambua haki ya Watanzania ya kupata taarifa kutoka katika mamlaka mbalimbali, nikinukuu Ibara ya 8(1)(a) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua kwamba nchi hii ni ya wananchi na kwamba mamlaka ya nchi yapo chini ya wananchi; na kupitishwa kwa muswada huu kunatoa fursa kubwa kwa wananchi wetu kuweza kupata taarifa kuhusu miradi pamoja na mambo mbalimbali ya msingi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nirejee Ibara ya 18 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ambayo inatoa fursa kwa kila Mtanzania kuwa na haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa. Naomba pia ninukuu maneno ya Mheshimiwa Dkt. Dale McKinley kutoka kule Afrika ya Kusini. Katika chapisho lake aliwahi kusema kwamba; “the state of access to information in South Africa;” katika page ya pili alisisitiza kwamba “if there is one right contained in the constitution that symbolically connects all other rights, it is their right to access to information. The control of information and enforced secretely was at the heart of anti-democratic character of the apartheid system.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ninukuu maneno hayo ili Waheshimiwa Wabunge wafahamu kwamba muswada huu umuhimu wake siyo tu katika Bunge hili, bali kwa wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla. Upatikanaji wa taarifa utatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwamba Serikali hii ya kipindi hiki ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba wale wasimamizi, viongozi wa taasisi za umma na pamoja na Serikali wanatoa taarifa sahihi kwa wananchi wetu wanapozihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, demokrasia hii ni ya hali ya juu ukizingatia kwamba Tanzania katika Afrika itakuwa ni nchi ya tano kupitisha sheria ya namna hii. Ukiangalia idadi ya nchi tulizonazo Afrika lakini siyo tu Afrika, dunia nzima, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi ya 67 kupitisha sheria ya namna hii. Japokuwa tunasema kwamba katika dunia nchi ya kwanza kupitisha sheria hii ilikuwa New Zealand miaka ile ya 1766 lakini Tanzania tunaingia katika record ya dunia kwamba miongoni mwa nchi ambazo zinaweka uwajibikaji mbele kwa watendaji wetu wa Serikali pamoja na taasisi mbalimbali za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapa nijikite sana katika Jimbo langu la Rufiji. Upatikanaji wa taarifa utawasaidia Wandengereko wa Rufiji, Kibiti pamoja na wananchi mbalimbali waliopo kule maeneo ya Kilwa, Kibiti pamoja na Rufiji. Nimeona niseme hili kwa sababu kwa mfano, pale kwangu Rufiji kuna tatizo la umeme kwa takribani huu ni mwezi wa 11, lakini wananchi hawana taarifa sahihi ni kwa nini umeme haupatikani kipindi hiki chote? Upitishwaji wa sheria hii utamruhusu Mrufiji popote pale alipo kuweza kuhoji na kupata taarifa kutoka kwa viongozi wetu ambao watakuwa wameidhinishwa yaani information officer wa maeneo husika ili waweze kujua hasa tatizo kubwa la umeme ni nini katika Jimbo letu hili la Rufiji pamoja na Kibiti kwa Mwenyekiti wa Wandengereko pale Bwana Ally Seif Ungando. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kuhoji tu ni kwa nini kuna shida ya umeme, tunafahamu Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda na Rufiji tunategemea kuwa na viwanda kwa mujibu wa Waziri wetu ambaye ametuahidi, tutakuwa na kiwanda cha kwanza pale Chumbi. Kiwanda cha Sukari tutakuwa nacho pale Chumbi, lakini ukiangalia tatizo la umeme linalotukabili ambalo Serikali haijatoa taarifa ni kwa nini tuna tatizo la umeme, sheria hii itawawezesha wananchi kupata taarifa, lakini pia Serikali itaweza kuboresha tatizo tulilonalo pale katika Jimbo letu la Rufiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri kwamba sheria hii itawasaidia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo langu katika Kata ya Utete pamoja na maeneo mengine kuhoji miradi mbalimbali ambayo imekuwa ni kero kubwa. Upatikanaji wa taarifa kuhoji miradi kwa mfano; Mradi wa Nyamweke, Segeni pamoja na miradi mingine mikuwa ambayo iko ndani ya Jimbo langu la Rufiji, wananchi wangu wapiganaji wa kule maeneo mbalimbali wataweza kupata taarifa kujua miradi hii imeidhinishiwa fedha kiasi gani na ni kwa nini mradi huu haujakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii pia kuzungumzia, yupo mkandarasi mmoja aliwahi kukabidhiwa moja ya barabara pale Rufiji kuikarabati. Mkandarasi huyu wakati wa ukarabati wake alikuja na kitoroli pamoja na chepeo kukarabati barabara ambayo ni ndefu. Sasa wananchi wanahoji lakini hawawezi kupata taarifa ni kiasi gani kiliidhinishwa katika mradi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti sheria hii itawasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kuweza kuhoji mambo ya msingi ambayo yameidhinishiwa fedha katika vikao vyetu vya Madiwani lakini pia yameidhinishiwa fedha na Serikali yetu hii. Kama nilivyosema hapo awali, demokrasia hii ni kubwa kabisa kutokea katika nchi yetu na ni historia kubwa ambayo tutaifanya katika Bunge lako hili Tukufu. Waheshimiwa Wabunge wetu wataingia katika historia kwa kupitisha sheria hii ambayo itaifanya Serikali kuwajibika na kuwepo kwa uwazi (transparency) ili wananchi waweze kupata taarifa za msingi kuhusiana na jambo lolote lile isipokuwa tu yale ambayo yanagusa usalama wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo, naomba niwasilishe kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini nianze kama vile ambavyo Vladimir Lenin Mwasisi wa Taifa la Kirusi amekuwa akianza katika hotuba zake kabla ya Russian Revolution mwaka 1905 - 1907 kwa kumwomba Mwenyezi Mungu kuendelea kuipa hekima na busara Serikali yangu ya Awamu ya Tano na kumpa afya njema Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mjadala huu umesababisha kuibuka kwa hoja nyingi ambazo kwa namna moja au nyingine zinadhihirisha wazi kabisa kwamba kuna matabaka ya kikabila na ya kikanda ambayo yamekuwa yakiibuka kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nami naiomba sana Serikali kuzingatia Kanuni (The Law of Connection), zile Kanuni ambazo ziliwahi kutolewa na Dkt. Maxwell. Tuwashike mioyo wananchi wetu. Kabla hatujakwenda kuwaomba mikono, basi tuzingatie kuwashika sana mioyo wananchi wetu na tuwahurumie sana wananchi wa Mikoa ya Kusini na Pwani. Tunapozungumzia Pwani tunaanzia Kibiti, Rufiji pamoja na maeneo ya Kusini Lindi na Mtwara kwa kuwa mijadala ya korosho ni siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi hiki cha siku mbili, tatu mjadala huu umeibuka, tumetengeneza heroes wengi ndani ya Bunge lako hili Tukufu pengine bila Serikali kutambua jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 63 na Ibara ya 64 ya Katiba hii imeipa mamlaka Bunge kutunga sheria. Ibara ya 13(5) imeipa mamlaka Bunge kutunga sheria. Zipo sheria ambazo zinapaswa kutungwa na Bunge, sheria zile zikawa na element za kibaguzi.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa, Bunge linaweza kutunga sheria ambayo inaenda kubagua watu au sehemu fulani. Hayo aliyafanya hata Mwalimu Nyerere miaka ya 1970 pale alipotoa mwamko wa elimu kwa watu wa Kanda ya Kati na kutunga Kanuni za Elimu ambazo ziliwasaidia watu wa Kanda ya Kati ambao kwa kipindi kile walikuwa hawajapata mwamko mkubwa wa elimu.

Mheshimiwa Spika, hili tuliliona kwa sababu wapo maprofesa ambao walisoma nchi hii kwa kuwa Mwalimu Nyerere alitunga Kanuni za kiupendeleo wakati ule, lakini pia hata sheria hizi ambazo leo hii zimezungumzwa sana kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alitoa upendeleo kwa baadhi ya maeneo. Naomba nijikite katika Ibara ya 13(5), naomba niisome, inasema hivi:

“Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Ibara hii neno ‘kubagua’ maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia Utaifa wao, kabila, mahali walipotokea, maoneo ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali yao ya kimaisha.

Mheshimiwa Spika, inaendelea kusema kwamba, watu wa aina fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni, kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima. Isipokuwa kwamba neno kubagua halitafafanuliwa kwa mujibu wa Katiba hii, kwa maana hiyo, itazuia Serikali kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la kurekebisha matatizo mahsusi katika jamii.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba ipo mipango ambayo Serikali ilifanya, pengine siyo sheria wala siyo kanuni, naomba niondoe maneno hayo ambayo mipango au taratibu zile ziliweza kuwasaidia baadhi ya watu wakapata elimu ili kuweza kuondoa ile hali ambayo ilikuwepo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, msingi wa mjadala huu wa siku ya leo ninaomba nijikite katika Sura ya 203, Sura ya147 pamoja na Sura ya 123. Nchi yetu hii, Serikali imepata mamlaka kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba wananchi ndiyo msingi wa Serikali na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Serikali wakati wote liwe ni ustawi wa wananchi wake na mimi nianze kwa kusema kwamba ninaunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na kudhibiti matumizi mabaya. Naunga mkono kwa hali zote. Mjadala huu uliweza kumwibua Mwanasheria Mkuu wa Serikali na nimeona hapa Mheshimiwa Mwambe
amezungumzia kesi ambayo Wakili namba moja wa nchi yetu hii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliizungumza kesi hii.

Mheshimiwa Spika, sitaki kwenda ndani kwenye msingi wa kesi hii, japokuwa tunafahamu kwamba hukumu za Mahakama zinazingatia mambo makuu matatu; zinazingatia maelezo ya kina yaliyopo katika kesi husika, lakini pia zinazingatia analysis ya ushahidi pamoja na sheria zilizotumika katika kufanya maamuzi ya kesi husika na mwisho kabisa zinazingatia reason ya hukumu iliyotolewa na Mahakama.

Mheshimiwa Spika, msimamo wa Mahakama utaendelea kuwa kwamba fedha hizi ni za wakulima. Hii ni kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama. Hapo hapo natambua kwa dhati kabisa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kwenda kudhibiti matumizi mabaya. Nami nampongeza sana Rais wangu wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ya kipekee kabisa, baada ya kuona kwamba matumizi ya fedha hizi haziendi kuwasaidia wananchi au haziendi kusaidia lengo lililokusudiwa wakati wa kutungwa kwa sheria hii naomba kutoa mapendekezo yafuatayo Serikali iweze kuyapokea:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, kwa kuwa watu wa Pwani na Kusini wanaona kabisa kwamba kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiwaacha pembeni na pengine ndiyo sababu ya msingi ya kutungwa kwa sheria hii. Naiomba Serikali kuzingatia matakwa ya Ibara ya 9 ya Katiba.

Mheshimiwa Spika, kimsingi nilikuwa najikita kwenye maoni yaliyotolewa na Wabunge wengi kwenye Bunge lako Tukufu, hayo yalikuwa ni maoni ya Wabunge wengine wala siyo maoni yangu, naomba nirekebishe jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, niseme kabisa kwa dhati mimi binafsi natambua jitihada za Serikali hususan jitihada anazichukua Rais Dkt. John Pombe Magufuli kudhibiti matumizi ya fedha. Ndiyo maana katika moja ya mapendekezo yangu ninaiomba Serikali, kwa kuwa dhamira ya kuendeleza zao la korosho ni pamoja na kuwepo kwa tafiti na maendelo ya watu, niiombe Serikali sasa kwa namna ile ile kuangalia yale madeni yaliyopo kwa sasa na kuona uwezekano wa Serikali kudhibiti fedha zile yenyewe. Hayo ni baadhi ya maoni yangu.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa nukuu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliyowahi kuitoa mwaka 1962 na nukuu hii naomba nijielekeze moja kwa moja kwa kijana mwana-CCM Tegemeo Saambili ambaye aliwahi kuandika kuhusu maana halisi ya kiongozi akifanya reference ukurasa wa 50 wa hotuba ya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, kwa ridhaa yako naomba niisome hotuba hii. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:

“Uhuru tulioutaka haukuwa uhuru wa kuondokana na Wakoloni, tulitaka uhuru uwepo kwa kila mwananchi na
kushirikiana na mwenzake kuijenga nchi yetu mpya, nchi ambayo raia wote ni sawa bila kugawanyika baina ya watawala na watawaliwa, baina ya matajiri na masikini, wajinga na wenye elimu, wenye taabu na wenye raha. Tulitaka kujenga nchi ambayo raia wote wanayo furaha ile ile ya kupata heshima, elimu na riziki na wote wakiwa na nafasi ile ile ya kuitumikia nchi yao kwa kadri ya uwezo wao.”

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naridhia mapendekezo ya Serikali. Pia, naiomba Serikali sasa iende kudhibiti matumizi ya fedha hizi ili sasa yale matakwa ambayo yalikusudiwa katika matumizi ya fedha hizi yaende moja kwa moja kama ambavyo Serikali imedhamiria kufanya.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, baada ya Mzee Chenge (Mtemi) kuzungumza, sidhani kama nitakuwa na maneno mazuri sana ya kuzungumza kwenye Bunge lako Tukufu lakini nitaomba ni-respond kidogo kwenye baadhi ya mambo, nakushukuru sana kwa kunipa dakika tano.

Mheshimiwa Spika, ni vyema Wabunge wakajielekeza kwa mujibu wa Kanuni ambazo zinatuongoza katika Bunge letu hili Tukufu. Ukiisoma Kanuni ya 84(3), Kamati yangu baada ya kupokea maoni ya wadau ilikaa pamoja na Serikali na ikakubaliana hoja nyingi na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema, kwa mara ya kwanza tunaipongeza sana Serikali kwa kukubaliana na ushauri wote wa Kamati iliyoutoa na maamuzi ya mwisho ya Kamati kukubalina na Serikali ilikuwa ni tarehe 24 Januari, 2019, nimuombe mjumbe Mbunge aliyezungumza kwamba Serikali haikuja kukubaliana na Kamati maneno haya ni ya uongo na nia ya uongo kabisa kwamba Kamati ilikubaliana na Serikali na msingi wa sheria hii angalau kwa dakika moja yapo maeneo ambayo Mheshimiwa Mzee Chenge ameyagusa na niipongeze sana Serikali kwa sababu ukilisoma jedwali la marekebisho ukurasa wa pili umekwenda kutibu tatizo lile ambalo Mheshimiwa Mzee Chenge alikuwa analisema hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, isipokuwa tu Serikali kwa huruma yake baada ya neno by birth iongeze comer ili sasa sentensi hizi sasa ziwe mbili nikiwa na maana ya kwamba kifungu cha 6B ambacho Mheshimiwa Mzee Chenge amekizungumza tayari Serikali imeshakiandika na ukikisoma kifungu hiki ili tuweze kutibu tatizo ambalo Mheshimiwa Mzee Chenge amelisema basi tunaweza kuongeza comer baada ya by birth na sentensi hii ikasomeka kwamba; “that person is the citizen of United Republic by birth, and both parents of that person are citizen of United Republic” tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tayari tumetibu tatizo ambalo pengine ingetulazimu watu baadaye kwenda kukuomba tafsiri za Kikatiba.

Mheshimiwa Spika, lakini ni kwa nini sasa Muswada huu ni muhimu wakati huu, ukisoma Ibara ya 5(c) ambayo yanaainisha majukumu ya msajili ndiko jukumu la kwenda kusimamia chaguzi za ndani za vyama. Jukumu hili linasomeka sambamba na Ibara ya 7(6)(b) ambayo inazungumzia jenda na masuala mengine ya vijana na wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, mimi na wewe we are the living example tujifunze yalitokea mwaka mmoja uliopita kiko chama Mbunge wake alikuwa na ulemavu baada ya kufariki chama hicho kikaleta Mbunge ambaye haendani na matakwa yalikuwepo hapo awali. Kifungu hiki kinakwenda sasa kutibu tatizo lililokuwepo na kumpa msajili Mamlaka ya kuwataka wanachama wa chama chochote kuhakikisha kwamba wanazingatia eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia pia majukumu ya msajili, msajili sasa anakwenda kusimamia Katiba ya nchi kwamba anakwenda kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi ikiwa ni sambamba na Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wapo wanachama wa chama fulani walikwenda sehemu fulani wakatoa kauli ambazo zinakinzani na kanuni za adhabu sura ya 16 penal code sura ya 16 ukisoma kifungu cha (89) sheria inazuia mtu yoyote mtanzania kuvunja sheria kuzungumza maneno ambayo yanakwenda kuharibu amani.

Mheshimiwa Spika, yaani the penal code ukisoma sehemu ya tisa inazungumzia offences against public tan quality. Offence hizi siyo za mtanzania wa kawaida peke yake ni za watanzania wote sasa kwa kifungu hiki kinakwenda kumsaidia msajili kwenda kutibu matatizo ambayo yanajitokeza kwa mwanachama wa chama chochote ambaye anatoa kauli ambazo zinakwenda kuharibu amani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yupo Mbunge alitoa kauli kwamba kule Rufiji watu 700 wamefariki, kauli hii ni mbaya sana na pengine kwa kutumia kifungu cha 89 Serikali ione uwezekano wa kulifanyia kazi jambo hili. Kwa sababu unaposema watu 700 wamefariki inamaanisha kwamba asilimia moja ya wa Rufiji wamefariki wameuwawa kauli hii ni mbaya sana na pengine iwapo tutampa msajili mamlaka atakwenda kushughulika na eneo hili.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho kabisa ni uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi umezungumzwa katika Katiba sheria hii inakwenda kuzuia taasisi au mtu fulani kuanzisha kikundi cha ulinzi ambacho kinakwenda kuchukua mamlaka ya Jeshi la Polisi au Jeshi la Wananchi Tanzania, lakini vikundi vingine vya kawaida havijazuiliwa kwa mujibu wa sheria hii, lakini sisi sote watanzania ni mifano halisi. Ukiangalia kilichotokea tarehe 27 Januari, 2001 kule Pemba watu walianzisha vikundi vya ulinzi wakaenda wakamkamata Askari wakamchinja kama kuku mambo haya ni mambo mabaya na watu wa namna hiyo pia baada ya hapo hayakuishia hapo kikundi hiki cha ulinzi kilikwenda mbele zaidi na wakawa wanakunywa kwenye…

SPIKA: Ahsante sana nashukuru sana.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sikudhamiria kuchangia lakini…

MWENYEKITI: Basi kaa chini.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na baadhi ya hoja nimeona nizungumze kwa uchache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme msingi wa marekebisho Na. 4 mwaka 2019 ni utekelezaji wa hati idhini iliyotolewa na Mheshimiwa Rais, hati namba 48, 49 pamoja na 50 ya mwaka 2019. Marekebisho namba 2 ya mwaka 2018 ndio msingi wa marekebisho haya namba 4 mwaka 2019 ambayo yamekwenda kubadilisha mfumo wa kisheria, hususan wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zimekuwepo hoja nyingi ambazo hata ambaye pengine ningelikuwa sina ufahamu wa sheria ningelihoji hoja kama hizo ambazo baadhi ya Wabunge wamekuwa wakizihoji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo pengine linahitaji ufafanuzi, kwanza pengine Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwana kazi kubwa sana ya kuwaelimisha Wabunge kuhusiana na marekebisho ya sheria hizi zote 11 ambazo kimadhumini na kimantiki ilikuwa na maana kubwa sana ili kuweza kutekeleza Sheria Na. 2 ya mwaka 2018 lakini pia kuweza kuweka mfumo mzuri wa utoaji haki hususan katika hii Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwepo hoja ya ni kwanini Mkurugenzi wa Mashitaka anapewa mamlaka ya yeye kuidhinisha kesi kwenda mahakamani. Hii ni misingi ambayo imewekwa katika Sheria ya National Prosecution Service Act lakini pia ukisoma Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Prevention of Corruption) imewataka TAKUKURU kabla ya kuendelea na mashitaka basi kuwasilisha taarifa zao au uchunguzi wao kwa Mwendesha Mashitaka ili aweze kutoa kibali cha kushitaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamehoji ni kwa nini Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameleta kifungu hiki cha kumtaka Mkurugenzi wa Mashitaka kutoa kibali cha kushitaki. Pia kitu kikubwa ambacho pengine Wabunge wangejielekeza ni kwamba si Bunge tu hili kwa wakati huu au mtu yeyote mwingine mwenye mamlaka ya kufanya marekebisho yoyote hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa leo hataweza kufanya marekebisho tofauti na haya ambayo yamekuja kwa sababu msingi wa hoja hii ni Ibara ya 59(b) ambayo imempa Mamlaka wa Mashitaka wa kushitaki makosa yote ya kijinai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Kamati au mimi kama Mchengerwa pengine nimeona ni vyema kabisa iwapo tutakwenda katika misingi ile ambayo Mheshimiwa Rais aliisema ya kupunguza mashauri, tutawezaje kupunguza mashauri? Tunatambua kwamba kuna kesi nyingi ambazo zipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka lakini ili kuweza ku-qualify kifungu hiki, tuliona ni vyema sasa tukaongeza kifungu kingine ambacho kitampa mamlaka Waziri wa Katiba na Sheria ili kuongeza vitu viwili; kitu cha kwanza ni kuongeza wale wasaidizi wa Mkurugenzi wa Mashitaka wawe na mamlaka ya kutoa idhini ya kushitaki na ili tuweze kusaidia kwa sababu Taifa lolote ambalo linapambana na rushwa, msingi wake ni kuruhusu Mkurugenzi wa Kupambana na Rushwa kuruhusiwa kuingia mahakamani moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii ni practice ya nchi nyingi sana duniani, ukienda kule UK, Finland, Scotland na nchi nyingine Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa amepewa mamlaka sawa na Mkurugenzi wa Mashitaka lakini huku kwetu Katiba imezuia kwa mujibu wa Ibara ya 59 lakini ili tuweze ku-qualify eneo hilo ni vyema sasa kama ambavyo Serikali imekubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na pengine wajumbe wanaweza wakasoma jedwali la marekebisho ambalo Mwanasheria Mkuu wa Serikali amelileta ambalo tayari limeweka kifungu cha kusaidia katika kupambana na rushwa lakini pia katika kupunguza mashauri ambacho kitamtaka Waziri wa Katiba na Sheria kuongeza baadhi ya vifungu katika kanuni ambazo zitawataka Mawakili wote wa Serikali Wafawidhi wa Mikoa na Wilaya kuweza kusikiliza au kutoa idhini ya usikilizwaji wa kesi za jinai katika maeneo yao ambazo zitaangukia kwenye kiwango fulani cha fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuweza kupunguza tatizo hili la mrundikano wa mahabusu nimeona hili ni eneo zuri ambalo tumpongeze Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuridhia eneo hili kuingizwa kwenye sheria na tuwatoe hofu wale ambao wadau wa kupambana na rushwa kwamba Bunge hili kwa wakati huu halina mamlaka ya kurekebisha Katiba Ibara ya 59(b) na pengine marekebisho haya ambayo tayari yameletwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndio tiba ya eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo pengine limekuwa natafsiri ambayo kwa kweli si nzuri au baadhi ya watu wametoa tafsiri ambayo pengine haikueleweka vizuri na kutokana na hotuba yangu ya Kamati ni eneo lile la waendesha mashitaka yaani Mawakili wa Serikali kuzuiliwa kufanya kazi ambazo zinagongana na kazi za msingi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mapendekezo ambayo Kamati ya Katiba imeyatoa ni mapendekezo mazuri nitumie fursa hii kumpongeza sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuridhia marekebisho ambayo kamati ilikuwa imeyatoa na msingi wa marekebisho ambayo yametolewa kwenye jedwali la Serikali na ambalo limetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni hoja ambazo Kamati ya Katiba na Sheria imezitoa. Na ukisoma katika taarifa ya Kamati ya Katiba na Sheria imekwenda kutoa tafsiri ni namna gani Serikali itaweza kutibu tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa pengine Serikali ianzishe utaratibu wa kutoa posho ambazo zinakwenda kutibu lile tatizo la Mawakili wa Serikali kutoruhusiwa ku-practice. Pili, ikumbukwe pia kwamba kuwa wakili wa kujitegemea vipo vyeti viwili ambavyo Mwanasheria anapaswa kupata; cheti cha kwanza ni kile cha ku-practice kama Wakili lakini cheti cha pili ni kuruhusiwa kuwa kamishna wa viapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili Serikali iweze kutibu tatizo hili na kama kamati ilivyoshauri na tuipongeze Serikali kwa kukubali sasa kwamba wale Mawakili wa Serikali wataruhusiwa moja kwa moja kuwa Makamishna wa Viapo na kwa kulitibu hilo pengine linaondoa kelele nyingi ambazo Wabunge wamekuwa nazo hususan ni kwanini Mawakili wa Serikali hawataruhusiwa ku-practice.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; tuipongeze Serikali kwa kuongeza baadhi ya ibara katika marekebisho ya jedwali la Serikali lililowasilishwa hapa Bungeni ambalo sasa linamtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda kuweka utaratibu mzuri ambao utawaruhusu Wanasheria wa Serikali kuruhusiwa ku-practice kwenye kesi ambazo hazina mgongano na Serikali. Kwa hiyo, yule Mwanasheria wa Serikali ambaye pengine angetamani ku-practice kama Wakili wa kujitegemea atawekewa utaratibu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao utamruhusu yeye kuruhusiwa ku-practice kwa kuangalia tu kwamba jambo analokwenda kulifanya haligongani na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maeneo mawili ambayo pengine ningetamani kuyazungumza ili kuweza kuweka mambo vizuri. Baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)